Msako wa Mwanaharamu Sehemu ya Pili
KIJASUSI

Ep 02: Msako wa Mwanaharamu

Msako wa Mwanaharamu Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE

*********************************************************************************

Silimulizi : Msako Wa Mwanaharamu

Sehemu Ya Pili (2)

“Gina, twende mbele zaidi,” akamwambia Gina, na ile gari ikaondolewa mahala pale mpaka kwenye njia panda ya kuwenda kwenye magofu ya Kaole na ile ya kwenda Bagamoyo mjini.

“Subiri!” Chiba alimwambia, kisha akamwambia aelekee kulia. Gina moja kwa moja akachukua barabara hiyo na kupita magofu ya Kaole akaendelea mbele mpaka alikokuta njia inaishia na kukutana na mkondo wa maji uliokatisha eneo hilo.

“Tunafanyaje?” akauliza.

“Tuache gari hapa, twende kwa miguu tufuate hii signal inawezekana ni Amata au Scoba, ila mmoja kati yao signal yake imepotea kabisa sijui tutampataje,” Chiba alijibu huku akiwa tayari kakanyaga ardhi ya eneo hilo akichukua hiki na kile ndani ya begi lake kabla hajaliweka mgongoni. Wakiwa bado wanaendele kutafuta hapa na pale katika vichaka hivyo, saa moja baadaye ndipo Jasmine alipoungana nao na kuweka nguvu pamoja jioni hiyo kufanya mtafuto huo mgumu.

Rejea sasa…

KURASINI

MARA BAADA YA KUMALIZA SHUGHULI za Shamba, Madam S alirudi katika afisi ile ya siri iliyotengenezwa ndani ya meli mbovu katika bahari ya Kurasini, wapiga mbizi waliotumwa kuutafuta mwili wa Amata walirejea na boti yao ‘KINYAMKERA’. Inspekta Simbeye na Madam S walikuwa wakisubiri kwa hamu huku wakiwa hawana mazungumzo mengi. Taarifa hiyo haikutangazwa na mtu yoyote wala hakuna chombo cha habari kilichothubutu kuvunja amri hiyo ya usalama wa taifa.

“Hatujapata mwili wa mtu yeyote kule majini!” kijana mmoja kati ya wale watatu waliokwenda kuchunguza yale mabaki ya ndege, ikiwezekana na kuupata mwili wa Amata walifikisha taarifa hiyo kwa Inspekta Simbeye na Madam S waliyekuwa ndani ya lile meli bovu.

“Isipokuwa tumepata hiki kiboksi cha kurekodi mwenendo wa ndege, taarifa ambazo tumezipata kutoka humu ni kuwa ndege hii ilipoteza mawasiliano angani kwa ghafla kwa kitu kama mlipuko. Baada ya uchunguzi kule chini ya maji, tumegundua kuwa ile ndege imedunguliwa, na kombora lililotumika ni RPG Rocket kwa kuwa tumefanikiwa kuona mabaki yake,” kijana mwingine akaelelzea kwa ufasha zaidi na kuwasilisha vyuma vya kombora hilo.

“RPG Rocket?” Madam S akadakia kwa kuuliza.“Unataka kunambia kuwa ndani ya nchi hii kuna watu wanamiliki silaha nzito za kivita kama jeshi, hii ni hatari, ni hatari sana,” Madam S alizungumza huku akionekana wazi kukosa utulivu wa mwili na roho kwa swala hilo.

Oh! Shit, atakuwa wapi Amata? Madam akajiuliza pasi na kupata jibu sahihi ndani mwake.

“Sawa naomba hiyo taarifa yote katika nakala laini tafadhali,” Madam S aliomba huku akilielekea dirisha dogo na kutazama nje kwa nukta kadhaa kabla ya kugutuliwa na sauti ya kijana yule akiwa tayari na taarifa ile mkononi mwake ikiwa ndani ya CD. Akaipokea na kuondoka katika ofisi ile ya ajabu.

Baada ya kujiridhisha na kila kitu, akaagana na Simbeye na kutolewa katika ile afisi mpaka eneo maalumu la nchi kavu upande wa Kigamboni, kutoka hapo akatembea hatua chache na kuchukua gari yake aliyoiacha kwenye afisi moja ya chama na kuelekea tena Shamba.

  • * *

Madam s aliwasili katika jumba hilo kwa njia anayoijua mwenyewe, shughuli za ndani humo zilikuwa zikiendelea kama kawaida. Ni Chiba tu aliyekuwa anajua ujio huo kwani kila anayeingia ndani ya jumba hili huweza kumwona kupitia kamera ndogo za usalama ambazo si rahisi kugundulika na mtu wa kawaida. Ndani ya sebule kubwa alipomwacha Scoba alimkuta palepale akifunua funua gazeti na kusoma hapa na pale.

“Kweli, tulifanya kosa kuwakabidhi wale askari lindo la mtu hatari kama yule, lakini tungefanyaje wakati hao ndiyo wenye jukumu la kulinda wahalifu?” Madam S akauliza huku akitembea na kujitupia kochini. Sauti hiyo ilimgutua Scoba, kwa sababu hakusikia hata kelele ya wayo wa mwanamama huyo.

“Yeah, ni sahihi sana kwa hilo lakini yule mtu uhatari wake ni wa kimataifa zaidi, tazama jinsi walivyo muokoa hao majahiri wake, ile ni mbinu ya kivita Madam,” Scoba aliongea.

“Kiukweli walidhamiria, maana hata kumkamata kwake yule bwana hakukuwa rahisi, tulipata tabu sana pale Bombay, lakini tulimleta. Halafu kumuona anatutoka mikononi kirahisi namna ile, lo, nina uhakika Amata huko aliko si ajabu bado anamsaka, na akimpata hawezi kumleta na roho yake,” Scoba akazungumza.

Ukimya ukatawala kati ya hao watu wawili, kila mmoja akiwaza lake. Scoba akarudisha mawazo yake kwenye mtanange wa Bombay.

Miezi mitatu nyuma

SAFARI YA BOMBAY – INDIA

“Una uhakika utamleta?” Madam S akamwuliza Amata.

“Tumeanza kudharauliana siyo?” Amata akajibu swali kwa swali.

“Siyo kudharauliana, maana wewe nakujua, mi nikikwambia umlete hai we utaleta viatu vyake tu nikiwa na maana utakuwa ushanyofoa roho yake,”

“Inategemeana, daima nikiona mtu mbishi kufika mzima lazima nimgawanye mara mbili, yaani nimtenganishe mwili na roho na hapo ndipo nambeba kirahisi,” wote wakacheka kwa maneno hayo.

“Sawa, serikali iko tayari kukupa msaada wowote utakaouhitaji, maana waziri mkuu kaagiza mtu huyo aletwe hapa,” Madam akamwambia Amata kwa msisitizo.

“Tawile, zimefika na ataletwa,” kisha akapiga saluti na kugeuka kulitazama jengo la Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.

“Kamanda Amata, Pancho Panchilio ana mtandao mkubwa sana ndani na nje ya nchi, uwe makini, timu ya utafiti ipo huko siku nne zilizopita na wameshafanya kazi kubwa sana wanakusubiri wewe ukamalizie,” Madam S aliendelea kutoa rai yake kwa kijana huyo shupavu.

“See you soon!” (Tutaonana punde tu) akamuaga Madam na kuondoka zake.

  • * *

“Wapi tena? Maana mwenzetu huishiwi safari weye,” Mhudumu wa ukaguzi wa Swissport akamtania kwa kuwa alikuwa akimfahamu hasa kwa kumwona mara nyingi uwanjani hapo.

“Umeanza Lulu, naenda Uhindini mara moja,”

“Uje na zawadi tu,”

“Usijali, kacholi zenye pilipili utapata,” Kamanda akajibu na kuishia kwenye chumba cha kupumzikia wasafiri. Baada ya nusu saa kupita aliondoka na ndege ya Shirika la Air India.

UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA

CHHATRAPATI SHIVAJI – BOMBAY

KAMANDA AMATA aliingia katika jiji hilo usiku wa manane, moja kwa moja alitoka nje ya jengo hilo. Kando tu ya maegesho ya uwanja huo, aliweka begi lake chini, akaingiza mkono mfukoni na kutoa sigara akaibana kwa midomo yake miwili huku kichungi cha sigara hiyo kikiwa ndani ya kinywa chake. Mkono mwingine ukatoa kiberiti cha gesi na kukiwasha. Mara baada ya kuiwasha akavuta kavuta pafu mbili kisha akaizima na kuisigina na kiatu chake.

Mbele yake akapita mzee mmoja na kujikoholesha, umbali wa sentimeta kama mia hivi akaonesha ishara ya mkono ya kumtaka Amata amfuate. Kamanda Amata akaona ishara ile na kumfuata mpaka kwenye gari moja ya kizamani, Ford Anglia.

“Mr. Spark!” akaita kwa sauti yake nzito.

“Mavalanka,” Kamanda naye akajibu. Yule mzee akachukua lile begi na kulitupia ndani, kisha akaingia mlango wa dereva na kumwacha Amata akiufungua ule wa abiria.

“Karibu sana Bombay. Ni mara yako ya kwanza kufika?”

“Ndiyo, sijawahi kuja Bombay wala India kwa ujumla,”

“Ha! ha! ha! ha! Hakika utafurahia maisha katika kila nukta ambayo utapata nafasi ya mapumziko, wasichana wazuri wenye maumbo ya kuvutia watakuburudisha sana kwenye maklabu ya usiku na kadhalika, ila uwe mwanagalifu wengine wanakuwa kazini,” Yule mzee alimwambia Amata.

“Mi najua hii nchi ya kidini bwana, inakuwaje kuna klabu za usiku?”

“Akh! Klabu za usiku zipo duniani kote…”

“Ila sina tabia hiyo,” kamanda akajibu kwa mkato.

“Ah weeeeeeee! Nakujua vyema kijana. Ok, tuyaache hayo, Hoteli ya Grand Hyatt inakufaa sana,” alimwambia huku akikunja kona na kuingia katika lango kuu la hoteli hiyo na kuegesha gari yake.

“Unaona?” akauliza.

“Nini?”

“Hoteli kubwa nzuri ya kisasa ina bwawa la kuogelea kule juu na casino nzuri kabisa,” Yule mzee akamwambia huku akimsaidia kushusha lile begi.

“Asante sana, tutaonana tena,” Kamanda akamuaga huku akivuta hatua kuelkea ile hoteli lakini kabla hajafika lango kuu la kuingilia mapokezi akapokelewa na vijana waliondaliwa kwa kazi hiyo kwa kila msafiri anayekuja.

Akafanya itifaki zote za mapokezi na kuingia katika chumba chake. Mara baada ya kuufunga mlango alikitazama chumba hicho kikubwa jinsi kilivyo na kilivyopangwa samani zake kwa mtindo wa kuvutia. Akainua saa yake ya mkono na kuifyatua upande wa juu, lile eneo lenye mishale ya saa likafunuka kama kifuniko na kuacha sehemu ya chini ikiwa na kitu fulani chenye uwezo wa kutambua aina yoyote ya mlipuko na kuonesha kama kuna mitambo ya kunasa sauti lakini akakuta kuna usalama wa kutosha. Akairudisha saa yake kisha akaliendea dirisha kubwa na kusogeza pazia pembeni. Majengo marefu kwa mafupi yalimkaribisha, taa za kupendeza za barabarani na majumba ya starehe zilionekana wazi zinavyopishana angani.

“Bombay!” akasema kwa suti ndogo.

Akiwa bado dirishani hapo akagutushwa na hodi iliyobishwa mlangoni, akauendea taratibu na kuufungua kwa hadhari kubwa. Sura ya mwanadada mrembo wa Kihindi ilimpokea kwa tabasamu lenye bashasha lililojaa na kuufanya uso wa mwanadada huyo kuwa wa mviringo, vishimo vilivyojitokeza katika mashavu yake vikawa kama vidimbwi vya maji katika jangwa.

“Samahani kuna mzigo wako hapa, tulisahau kukupatia pale kaunta,” yule msichana aliyekadiriwa kuwa na miaka ishirini hivi alimwambia Amata kwa sauti tamu iliyozitikisa kwa upole ngoma za masikio yake. Akainua mkono na kuipokea bahasha iliyokuwa mkononi mwa dada huyu huku akiking’ang’ania kiganja cha mkono huo.

“Mmm asante, unaitwa nani?” Kamanda akaanza ubembe wake.

Yule binti hakujibu kwanza, akamtazama Amata juu mpaka chini, akameza mate.

“Sukaina!” akajibu.

“Oh! Sukaina, jina zuri sana, asante kwa mzigo au kuna lingiine?”

“Hapana!” akajibu na kuanza kuondoka.

“Sukaina!” Kamanda akaita na yule binti akageuka.

“Napenda kuonana nawe ukimaliza kazi leo,”

“Mmmmm! Bwana wangu anakuja kunichukua, kwaheri,” akajibu na kuondoka zake.

Kamanda Amata akabaki katumbua macho akimwangalia yule mrembo akipotelea kwenye lifti huku vazi lake zuri lenye kumetameta likimfanya kuonekana mrembo zaidi. Macho yaliposhiba akarudi ndani na kuifungua ile bahasha.

Bastola moja ndogo ililala ndani yake ‘Beretta 92FS 99mm’, Kamanda Amata akaichukua na kuigeuzageuza, bado ilionekana mpya na haijatumika kabisa. Pembeni yake kulikuwa na kasha iliyojaa risasi, akaichukua na kuichana kisha akazijaza katika ile bastola na kuipima kidogo kama inafiti mkononi mwake. Bastola kama hii aliitumia zamani kidogo hivyo alishaanza kuipoteza ufanisi wake, kifaa chake cha kuzuia sauti nacho kilikuwa pamoja nayo. Akavuta memo ndogo na kuisoma.

‘Mgahawa wa Dinasty saa 2:15 asubuhi, meza namba 5’

Alipomaliza kuisoma akainkunja na kuitia kwenye begi lake kisha akaliendea bafu. Baada ya kuoga na kujiweka vizuri aliutafuta usingizi usiku huo na kuupata kwa tabu.

MGAHAWA WA DINASTY – saa 2:10 asubuhi

Akiwa ndani ya suti safi Amata aliteremka katika taksi na kuingia ndani ya mgahawa ule, mlangoni alipokelewa na mwanadada wa Kihindi aliyevalia vazi la kitamaduni, akamkaribisha na kumwonesha ukumbi wenye ukubwa wa wastani ambao ndani yake kulikuwa na watu walioketi wakipata ama kahawa au chai kila mmoja na kile alichopenda. Harufu ya vyakula na marashi ya Kihindu viliikinaisha pua ya Amata kwa sekunde chache, moja kwa moja akaiendea meza namba tano ambayo haikuwa na mtu yeyote aliyeketi hapo.

Pembeni mwa meza hiyo dirisha kubwa la kioo liliruhusu mtu yeyote kuona mandhari safi ya jiji la Bombay, na pia ungeweza kuwaona kwa uzuri watu waliokuwa wakipita huku na kule kwa shughuli mbalimbali. Katika usawa kabisa wa meza ile lakini upande wa nje kulikuwa na barabara kubwa iliyokuja kuungana na hiyo iliyo hapo. Amata aliitazama ile barabara iliyokwenda asikokujua.

N Ave Road! Amata alisoma kibao kikubwa cha rangi ya kijani kilichoonekana kupitia dirisha hilo kikiitambulisha barabara hiyo iliyonyooka kiasi kwamba mtazamaji aliweza kuona mpaka mwisho wake kama sio mbovu wa macho. Akiwa katika kushangaa huko akahisi kama mtu anaketi katika kiti cha mbele yake, akageuka taratibu na kugongana macho na Chiba aliyekuwa kajigeuza kidogo sura yake kwa kujiweka vichunusi vya hapa na pale na uvimbe wa bandia katika paji lake la uso.

“Karibu Bombay!” aliongea kwa sauti iliyoonesha kuwa na kikohozi kikali kwani mara kwa mara alikuwa akikohoa.

“Nimeshakaribia komredi,” akajibu na kujiweka sawa huku kifungua kinywa kikiteremshwa mezani taratibu na mhudumu aliyeijua kazi yake, wakasitisha mazungumzo yao kusubiri zoezi hilo lifanyike.

“Hapa kazi iliyopo ni ndogo tu lakini ni ngumu,” akaongea huku akiangalia huku na huko.

“Mbona unaongea kama una wasiwasi na jambo?”

“Lazima kuwa na wasiwasi kwani jamaa wamenishuku tangu juzi wakati nafuatilia nyendo za mwanaharamu, lakini niliwatoka hawakunipata tena”.

“Ningeshangaa!” Amata akaongezea.

“Sasa Kamanda, mpango upo hivi, Pancho Panchilio ana makazi yake ndani ya Hekalu Hanuman. Hili ni hekalu la Kihindu. Geuka kulia, tazama hiyo barabara,”

“N Ave Road,” akasoma tena yale maandishi kwenye lila bango.

“Barabara hii moja kwa moja mbele inakutana na barabara ya SB Patil na kufanya njia panda,”

“Enhe!”

“Hapo sasa ndipo penye hilo hekalu, nimemwona kwa macho yangu japo ilikuwa kazi ngumu sana, sijui tutamchukuaje,” Chiba alimweleza Amata aliyekuwa kanyamaza kimya akisikiliza huku akili yake ikizunguka kwa kasi ya ajabu.

“Kuna ulinzi mkali au vipi?” akauliza.

“Kuna kamera sabini na nne nje, na ndani zisizopungua thelethini, pale wanaingia Wahindu tu, mtu mweusi huna nafasi, kuna walinzi pande zote ndani na nje wenye vifaa vinavyoweza kumtambua yeyote mwenye nia mbaya na eneo hilo. Isitoshe ni eneo la hekalu ambalo hata viongozi wengi hupenda kuabudia hapo,” Chiba aliuliza.

“Nakusikiliza,” Kamanda alimwambia.

“Inabidi tumchukue akiwa hai,”

“Na tukimchukua tunampeleka wapi?”

“Bahrain House, pembezoni mwa Bombay karibu na bahari, jengo hilo halitumiki, limetelekezwa, tutafanya shughuli yetu humo na kuondoka naye.”

“Safi sana Chiba, nitahitaji kutembelea hekalu hilo ili nilione kwa ukaribu,” Kamanda akasema.

“Haina haja,” akaingiza mkono mfukoni na kuchomoa kipande cha karatasi, akakikunjua na kukiweka mezani.

“Hii hapa ni ramani ya jengo hilo,” akamwonesha.

Wakatazama pamoja, Chiba akamwonesha Amata kila kona yenye kamera na ulinzi wa binadamu, walipojiridhisha, akairudisha mfukoni ramani ile.

“Sawa Chiba, nimeona, lakini bado mi na wewe hatujui hasa huyu mtu anaishi kona gani pale au anakuja na kutoka,” Kamanda akazungumza..

“Aaaa aisee halafu kweli, hapo sikutumia umakini,” akakiri.

“Usiwe na shaka, huyu mtu atakamatika tu hata awe na mizizi mingi kama mnazi, atang’oka tu,” Kamanda alisema.

“Nakuamini kamanda, Madam S atakuwa hapa muda si mrefu,” Chiba akazungumza.

“Safi, sasa fanya hivi kama inawezekana Madam aombe usafiri binafsi, aje na ndege ili tukimtia mkononi huyu jamaa tuondoke naye kiurahisi, kumbuka kwenye ndege ya abiria akileta vurugu ni hatari kwa mamia ya watu,” Kamanda alimpa maagizo Chiba.

  • * *

Kama kawaida ya Jiji la Bombay, watu walikuwa wengi barabarani, pikipiki za magurudumu matatu, usiseme, zilikuwa zikisafirisha watu huku na kule. Kwa ujumla kulikuwa na magari machache sana lakini pikipiki zilitawala kila kona. Kamanda Amata alikuwa ndani ya moja ya ‘Bajaj’ hizo akielekea upande mwingine wa jiji.

“Mwenyeji wetu hapa ni Sha Kapur, yeye ni mwanausalama mstahafu, anajua mengi na Madam S alinishauri kukutana naye,” Chiba aliendelea kuongea huku akiwa katika bajaj nyingine tofauti na ile aliyopanda Amata. Lakini kwa kutumia kifaa kidogo kabisa cha mawasiliano aliweza kusikilizana vyema na swahiba wake huyo,

“Lazima tumuone, lakini kwanza ngoja nilione hilo hekalu hata kwa nje,” Amata akajibu.

“Yote heri,”

Kamanda Amata aliteremka na kumlipa yule dereva, alipoinua uso wake mbele akaona lile hekalu kubwa linalopendeza kwa macho. Hekalu la Hanuman.

Ilikuwa mchana wa saa saba watu wakipishana kuingia na kutoka ndani ya hekalu lile huku ibada zikisikika kwenye vipaza sauti, watu waliopendeza kwa mavazi mbalimbali ya tamaduni za Kihindi walikuwa eneo hilo akina mama kwa akina baba, watoto kwa vijana. Umbali kama wa mita ishirini kutoka katika lango kuu la hekalu hilo kulikuwa na kundi la watu waliokuwa wakinunua vitu fulani ambavyo hakuvijua vizuri ni vitu gani. Akavuta hatua mpaka eneo lile. Amata alikuwa tofauti kwa mavazi, hakuna aliyevaa suti eneo lile, kila jicho lilimtazama yeye.

Karimati, kachori na vyakula mbalimbali vya Kihindi vilikuwa hapo, Kamanda Amata akasogelea mahala pale na kuinama kutazama kwa ndani kumuona muuzaji.

“Svagata,” (Karibu) sauti nyororo ya kike ikapenya masikioni mwa Amata.

“Dhan’yavada,” (Asante sana) akajibu kawa lugha hiyo ya Kihindi na kumtazama mwanadada huyo, macho yao yalipogongana kila mmoja akabaki kakodoa. Amata hakuamini anayemwona na wala mwanadada huyo hakuamini aliye mbele yake.

“Amata!” akabaki kama aliyepigwa shoti ya umeme.

“Hapa si salama, njoo huku, nifuate,” Yule msichana akaondoka na kumwachia kijana wake aendelee na kazi hiyo.

  • * *

Chiba alitikisa kichwa na kumtazama Amata akiondoka na Yule mwanamke.

“Hili ndilo tatizo la huyu jamaa, keshanasa,” Chiba alinung’unika. Akajitoa pale aliposimama na kusogea upande wa pili ili amwone vizuri Kamanda anaelekea wapi, akasimama mahali penye kiduka, akaagiza kinywaji na kuendelea kumtazama swahiba wake akipotelea ndani ya nyumba mojawapo katika eneo hilo, hatua kama mia mbili kutoka katika lile hekalu. Naye taratibu akaachana na kinywaji chake na kuendelea kutembea huku akipiga mruzi kuelekea eneo lile, alipofika hakuwaona kabisa isipokuwa lango lililofungwa na kubaki bila mlinzi. Akatazama huku na huku hakuna mtu; akavuka na kuliendea lile lango, alipolisukuma, likasukumika; akajipenyeza ndani taratibu na kusimama wima huku lile lango likijifunga nyuma yake.

Ukimya wa eneo lile ulimtia wasiwasi Chiba, akapepesa macho yake huku na kule hakuona mtu wala kiumbe hai chochote chenye uwezo wa kujongea. Mimea mirefu ilikuwa ikiyumbayumba kwa upepo wa taratibu. Kati ya mimea mingi iliyoshikana na kushonana kulionekana nyumba moja ndogo iliyonakshiwa kwa nakshi za kiajemi.

Hapa hakuna usalama! akawaza na kuichomoa bastola yake kutoka mafichoni na kuiweka kiganjani tayari kwa lolote. Mwendo wake wa minyato ulifanya aonekane kama mvamizi wa eneo hilo.

  • * *

“Amata! Nini kimekuleta India?”

“Sikutegemea kabisa kukuona SaSha,”

“Hapa ni nyumbani vyovyote ujavyo tegemea kuniona,” SaSha alimwambia Amata huku akiwa amekumbatiwa na kuegemea ukuta, nyuso zao zikitazamana na pumzi kupishana kwa kasi. Taratibu vinywa vya wawili hawa vikaanza kukaribiana huku mihemo ikiongezeka.

Mlio wa kengele ulimshtua SaSha na kumsukuma Amata pembeni, akasogea dirishani na kuvuta pazia taratibu; kutoka ndani aliweza kumwona Chiba. Lakini Chiba hakuweza kumwona SaSha kutokana na dirisha lile kufichwa na mimea iliyotambaa kwa nje.

SaSha akachomoa bastola na kuiweka tayari akiulelekea mlango. Kamanda Amata taratibu akavuta pazia kutazama kilicho nje.

“SaSha!” akaita kwa sauti ndogo. SaSha akageuka kumtazama akampa ishara ya kurudi.

“Kijana wangu huyo, ananilinda, anaitwa Chiba”. SaSha akarudisha bastola yake na kufungua mlango huku akinyosha mikono yake juu kuonesha ishara ya amani.

“Karibu Chiba, tafadhali hapa ni mahala salama,” SaSha akamwambia Chiba na wakati huo Chiba akashusha bastola yake na kuiweka katika kikoba chake.

“Karibu ndani,” akamwambia huku akiingia ndani ya ile nyumba. SaSha akaweka vinywaji mezani na wote wakaendelea kunywa taratibu huku wakibadilishana mawazo.

“Amata, kuna nini Bombay? Maana wewe huwezi kuja sehemu kama hii kwa likizo,” SaSha akauliza tena.

“Nimemfuata mwanaharamu,”

“Nani na yuko wapi?”

“Mwanamke! Hutakiwi kumjua we endelea na kazi yako hili halikuhusu, nimeshakujibu,” Amata akajibu kwa ukali kidogo. Akamgeukia Chiba na kumtambulisha.

“Anaitwa Sasha, ni agent wa shirika la kijasusi la CBI hapa India, alikuwa Tanzania miaka kadhaa nyuma katika sakata lileee la yule gaidi, kama unakumbuka,”

“Nakumbuka, sakata la Jegan Grashan?” Chiba akauliza.

“Ndiyo,” akajibiwa na kisha ukimya ukatawala. Kamanda Amata akanyanyuka na kuliendea dirisha la upande wa nyuma akatazama na kuona shughuli mbalimbali zikiendelea, hakuweza kujua kama ni za uvuvi au ni kitu gani, akampa ishara Chiba asogee pale dirishani. Nukta chache, Chiba alikuwa pamoja na Amata huku mkono akiwa na darubini ndogo lakini yenye nguvu kubwa, inayoweza kupima na kukuandikia umbali wa hicho kitu kilipo kutoka uliposimama wewe. Amata akiweka machoni na kutazama, kwa mbali kulikuwa na boti iliyoonekana ikija upande huo.

“Tazama hiyo boti,” akamwambia Chiba huku akimpa ile darubini na yeye akaiweka machoni na kutazama.

“Amata!” akaita baada ya kutazama kwa sekunde kadhaa.

Ile boti ilifika karibu na pwani lakini ilishindwa kusogea kutokana na kupwa kwa maji, watu kama nane walisogea kule baharini na kumbeba mtu mmoja kwenye kiti maalumu kama mfalme wa kikoloni. Huku watu wengine wakirusha maua na kuonekana kama wanampa heshima mtu huyo.

“Shiit!” Chiba aling’aka na kumpa ile darubini Amata.

“Vipi?”

“Pancho Panchilio,” akajibu Chiba, “laiti ingekuwa tummalize, basi hapa ndipo tungeiushangaza Dunia,” akaongeza.

“Bibi yako anataka amnase kofi kabla hajafungwa,” Amata akasema na wote wakacheka. SaSha akafika hapo dirishani na kumnyang’anya darubini Amata kisha akaanza kuangalia yeye.

“Waoh! Chief anarudi,” SaSha akajisemea kwa sauti huku akirudisha darubini kwa Amata.

“Ni nani Yule?” Chiba akahoji baada ya kugundua kuwa mwanamke huyo anamjua Pancho kama Chfu.

“Yule ni Chief wa ukoo fulani ambao unamiliki hilo hekalu hapo, ni mtu mwema sana kiasi kwamba watu wa ukoo wake umtukuza kama mfalme,” SaSha akawaeleza Chiba na Amata wakati huo Chiba alikuwa akinasa mazungumzo yale kwa kutumia pete aliyokuwa ameivaa kidoleni mwake.

“Kwa hiyo anakuja kuwasalimu watu wake?” Kamanda akauliza lakini swali lake lilikuwani la kutaka tu uhakika wa jambo ambalo Chiba hakulichunguza sawasawa.

“No! hapo ndipo anapoishi,” SaSha akajibu huku akimtazama Amata.

“Nitakwenda kumsalimu au vipi Chiba?” Amata akapendekeza.

“Oh! No! hamuwezi kumuona, huwa haonekani kwa urahisi hivyo hususan kwa ninyi watu weusi. Watu wake humuona kwa nadra sana, kupata muda wa kuzungumza naye labda ni dakika tano tu na ni mara moja kwa mwezi,” SaSha akaendelea kueleza.

“Anaitwa nani?” Chiba akauliza.

“Premji Kanoon,” SaSha akajibu; Chiba na Amata wakatazamana na kubaniana macho. Amata akarudisha darubini machoni na kutazama ule msafara. Wale vijana waliombeba waliendele kutembea na kuiacha pwani kisha wakaingia kwenye ngome kubwa ambayo ndani yake ndiko kuna hilo hekalu. Walipopotelea ndani yake, akashusha ile darubini na kumrudishia Chiba ambaye aliificha ndani ya koti lake. Amata akamwangalia SaSha.

“Anaishi wapi?” akauliza.

“Humo humo ndani, chini ya hilo hekalu kuna kasri kubwa sana ambalo ndilo anloishi siku zote. Kesho ni sikukuu ya Diware, watu wengi kuliko hapo unapoona watakuja, nafikiri utaweza kumwona vizuri kwani baada ya ibada kuna sherehe kubwa kwenye uwanja huko nyuma zinazoambatana na michezo mbalimbali,” SaSha akaeleza.

“Ok, natamani kuhudhuria,”

“Bila shaka, jioni ni kwa kila mtu,” SaSha akamaliza kuongea na kuwapa vinywaji wawili hao.

  • * *

Premji Kanoon aliteremshwa kutoka katika kile kiti akakanyaga chini kwa miguu yake na moja kwa moja akaingia kwenye kijimlango kidogo na kujifungia. Akateremshwa chini ya ardhi ambako kulikuwa na kasri lake lisilo na bugudha. Alipofika tu akapewa huduma zote zilizomstahili ikiwa pamoja na kukandwakandwa mabegani, kuoshwa miguu kupakwa mafuta ya kunukia katika nyayo zake na mambo mengine mengi. Chumba chote kilinukia udi, aliinuka na kusogea karibu na sanamu moja lenye ukubwa wa wastani, akainamisha kichwa chake huku akiwa kabana viganja vya mikono yake kifuani kwa uchaji wa hali ya juu. Sekunde kadhaa akamaliza na kutoka eneo hilo huku akimwagiwa maua mazuri ya kunukia naye akakanyaga juu yake.

Hatua chache akalifikia sanamu lingine, akasimama mbele yake na lile sanamu likasogea pembeni taratibu, akapita na likarudi mahala pake. Kilikuwa chumba kidogo chenye giza, kikamteremsha chini zaidi na huko akaingia kwenye ukumbi wa wastani uliokuwa uking’azwa kwa taa zinazobadilisha rangi. Akaketi kwenye kiti kimoja kikubwa kilichokuwa nyuma ya meza yenye nakshi za kupendeza. Mbele yake kulikuwa na watu wanne, vijana wakakamavu wenye miili ya wastani, vichwani mwao walivaa vilemba ambavyo viliwatambulisha kuwa wao ni Singasinga.

Akajikohoza kidogo na wale vijana waliendelea kusimama pale wakiwa kimya kabisa. Pancho Panchilio au wao wanamwita Premji Kanoon.

“Sina lingine, nataka auawe au wauawe,” akasema.

Wale jamaa wakaitikia kwa vichwa tu, hawakuongea lolote; pembeni yao kukatokea picha kubwa ya Amata.

“Mnamwona huyu?” akawauliza, wote wakageuka na kuitikia kwa vichwa.

“Mna uhakika ndiye mliyemwona uwanja wa ndege?”

Wakajibu tena kwa kutikisa vichwa.

“Vizuri, sasa nataka auawe mara moja yeye na yule wa mwanzo, watu wa jamii kama hii hawafai kuishi kwa sababu huaribu mipango ya watu. Sikilizeni, huyu mnayemwona kwenye picha ni mtu hatari sana, mnapokwenda kumshambulia hakikisheni mmejipanga vizuri, mnanielewa?” akawauliza.

“Ndiyo, tunakuhakikishia jua la kesho hawezi kuliona kamwe!” mmoja aliyesimama mbele ya wenzake akajibu kwa ushupavu. Zile taa zikazimika na Pancho akapotea kwenye milango yake ya siri.

MKESHA WA DIWALI

“Kamanda Amata!” SaSha akaita kwa sauti ya chini.

“Niambie mtoto mzuri,” Amata akajibu.

“Unalala hapa siyo?”

“No! natoka sasa maana usiku huu tuna kazi ya kufanya. Kesho uje pale Grand Hyatt Hoteli, utanikuta,” kamanda akamwelekeza.

“Mmmmm! Nikikufumania maana wewe huwezi kulala bila mwanamke,”

“Acha uongo,” akamjibu huku akijinasua kutoka katika mikono ya SaSha iliyokuwa imembana pale kitandani, akaingia bafuni na kujiweka sawa, alipojitumbukiza ndani ya suti yake na kutokomea nje ya jengo lile.

“Swiiiiiiiiiih!” sauti ya mruzi ilimshtua Amata akasimama na ghafla gari moja ikatokea mbele yake na kusimama.

“Twenzetu kumekucha!” Ilikuwa sauti ya Chiba, akajipakia garini na wakaondoka kwa kasi.

“Kamanda tuko matatani, jamaa wamejipanga wanajua kama upo hapa, nilichofurahia ni kuwa wanakuzungumzia wewe na hawajui kama mimi niko hapa,” Chiba akaeleza huku akiongeza kasi ya gari yake kumbe hakuwa akijua kuwa wenzake walishammaizi muda mrefu.

“Asee, watakuwa wamejuaje kama niko hapa?”

“Ah hapo ni sehemu mbili tu ama uwanja wa ndege au hotelini, watu kama hawa huwa na macho mengi na masikio kila mahali,” Chiba akaongea harakaharaka.

“Sasa Chiba na sisi tugeuze kibao, kazi yetu tuifanye leo hii hii usiku tukichelewa kitanuka, maana wanaweza kusali wale tukageuka panya kwenye nchi ya watu,” Kamanda akaongea huku akijiweka vizuri kitini,

“Twende hotelini, nikachukue begi langu niliweke humu garini maana kuanzia sasa kambi popote”.

Chiba akakunja kona kali na kujikuta kapita katika taa nyekundu, honi za magari zikasikika kila upande, lakini hakusimama akakanyaga mafuta na ile gari ikazidi kuunguruma kwa nguvu.

HOTELI YA GRAND HYATT

GIZA LILIKUWA likishindana na taa za umeme zilizopendezesha jengo hilo la hoteli. Siku hiyo ambayo ilikuwa ni usiku wa kuamkia sherehe kubwa sana kwa dini za Kihindi ulijawa na watu wengi. Wale waliopenda ibada walienda mahekaluni na wale waliopenda starehe walienda kwenye makasino.

Gari moja, dogo, jeusi likaegesha katika maegesho na vijana wawili wakateremka, vijana hao wenye mandevu na maviremba vichwani mwao hawakuwa na la kuongea wala kusalimiana na yeyote waliomuona. Mmoja wao akainua simu na kupiga, akaongea maneno machache na kuiweka mfukoni ile simu kisha akauendea mlango mkubwa wa ile hoteli. Moja kwa moja alisimama mbele ya kaunta na kubadilishana maneno kadhaa na mhudumu aliyekuwa hapo na kutoka kuelekea kunako lifti za kupanda juu.Yule mwenzake alibaki kwenye makochi ya mapokezi akivuta gazeti hili na lile, mtego.

  • * *

“Chiba wewe nisubiri upande uleeee, mi naingia kutoa begi tu napitia mlango wa nyuma kisha tunaondoka bila kuaga,” Amata akamwambia Chiba wakati akiufunga mlango wa gari hiyo na kumwacha Chiba akiondoka taratibu kuelekea upande wa pili wa ofisi hiyo. Amata akavuta hatua za nusu kukimbia na nusu kutembea, akazikwea ngazi na moja kwa moja akaifuata kaunta na kukaribishwa na yule binti wa jana yake, Sukaina.

“Ndiyo mrembo! Ujumbe wangu wowote?” akauliza.

“Ujumbe wako nimekupelekea chumbani tayari,”

“Sasa mbona hukusubiri hukohuko unikabidhi?” Amata akaanza maneno yake ya ubembe.

“Mmmm na wewe, tangulia nakuja,”

“Waja kweli au ndiyo kunipaka mafuta kwa mgongo wa chupa?”

“Naja kweli we tangulia dakika kumi nitakuwa nimefika maana ndiyo nafunga ofisi natoka. Nikukute kitandani sawa bebi?” Sukaina akarusha maneno ya kumlegeza Amata huku akijuwa wazi kuwa ni kitu gani kitakachomtokea kijana huyo. Yule jamaa aliyekaa pale kwenye kochi akamwoneshea ishara ya dole gumba Sukaina na kunyanyuka taratibu kuelekea kule ndani alikoenda Amata.

Kamanda Amata alibofya kitufe cha kuiita lifti lakini alihisi vinyweleo vyake vikisimama na mwili ukisisimka, akarusdi nyuma hatua mbili na kugeuka akapanda kwa ngazi za kawaida mpaka ghorofa ya nne kulikokuwa na chumba chake. Alipoufikia mlango, akautazama juu hadi chini, kisha akatupa jicho pale kwenye kitasa kile cha kielektroniki ambacho kufungua ulipaswa ku-chanja kwa ‘smart card’ kisha mlango ungefunguka. Moyo wake ukawa mzito kufanya jambo hilo, jicho lake lilipotua kwenye ile sehemu akagundua uwa mlango ule umefunguliwa kwa maana alama yake ya kiuzi alichokitengeneza kama kifundo fulani na kukipachika katika ule mfereji wa kuchanjia kadi haukuwepo. Akachomoa bastola yake ‘Berreta’ na kupachika kile chombo cha kupoteza sauti kisha akachomoa kadi yake nyingine na kuchanja, mara mlango ukajinasua loki zake. Akaufungua ule mlango kwa kasi na kubamiza kwa nyuma, kumbe yule mjinga alijificha upande huo. Akajikuta akipigwa na mlango usoni, akatoka pale huku bastola ikimwanguka chini na mkono kajishika pua.

Amata alirudisha bastola yake kikobani na yule bwana alipogeuka, alikutana na makonde mawili ya maana yaliyopita yote usoni, akayumba na kujibamiza mezani kabla hajaenda chini ambako hata hakufika kwani teke kali la Amata lilitua usoni na kumtupia upande wa pili wa kitanda. Kamanda Amata akaweka tai yake vizuri na kufunga upya saa yake, kisha akaruka kitanda na kutua upande wa yule bwege ambaye alikuwa akijiandaa kunyanyuka ilhali hali yake tayari ilikuwa tete. Alipotua sakafuni alihisi mlango ukifunguka tena nyuma yake, bila kuuliza, alichomo bastola na kujirusha chini huku tayari keshafyatu risasi mbili zilizoishia tumboni mwa yule mjinga wa pili na kumbwaga chini huku akigombania roho yake isimwache.

Amata akageuka haraka na kumrudia yule wa kwanza ambaye tayari alikuwa amesimama na kujiandaa kwa mapambano.

“Umemuua Rajiv! Sasa zamu yako,” akaunguruma huku shati lake likiendelea kulowa kwa damu zilizokuwa zikichirizika kutoka puani mwake.

“Tulia mpumbavu wewe,” Amata alimjibu kwa lugha hiyo ya Kihindi aliyokuwa akijarobu kumwemwesa japo maneno mawili.

“Tupa bastola tupambane, hujui kama nchi hii ndiko alikozaliwa Amitah na Mithun?” lile jamaa likamwambia Amata.

“Hamna tabu,” Amata akaipachika kwenye kikoba chake. Wakati akifanya hilo Yule jamaa alitua kifuani mwa Amata kwa miguu yake miwili. Amata akapepesuka na kujibamiza ukutani huku akimwona jamaa akitua sakafuni kwa miguu yake ileile. Kabla hajatulia, Amata alijizungusha huku akiwa amebonyea na kuwa mdogo kama mbuzi, mguu wake wa kulia uliozunguka kwa kasi ulimchota ngwala yule bwana aliyekuwa akijaribu kuruka ili akwepe pigo hilo, lakini haikuwa hivo kwani alichotwa vibaya na kubamiza kisogo chini huku kiwiliwili kikimfuatia juu yake. Alijitahidi kunyanyuka lakini guu la Amata likatua kwa nguvu kifuani na kumafanya ateme damu.

“Unamjua Premji Kanoon?” akamwuliza.

“Husilitaje bure jina la mtu huyo,”

Kamanda Amata akamwinamia na kumchapa kofi moja kali lililomwacha taabani.

“Nani mshirika wenu hapa?”

“Hatuna mshirika,” akajibu kwa taabu. Kamanda Amata akachomoa kisu cha kukunja na kukifyatua hewani, ile ncha yake ikachachamaa juu, alipokishusha kilitua kwenye nyama ya paja.

“Aaaaaiiiiiggghhhh! Sukaina wa mapokezi,” akajibu huku akifumba macho na kubana meno.

“Shenzi kabisa wewe,”

Akakichomo na kukifuta damu kwa nguo za yule jamaa huku akisimama na kukipachika mahala pake. Damu ilikuwa ikimbubujika pale chini. Amata akafungua kabati na kutupia vitu vyake ndani ya begi lake.

‘Haina haja ya kupoteza muda’ akawaza na kuivuta bastola yake.

“We mjinga salamu hii umpe mungu wako Premji Kanoon, mwambie Kamanda Amata yuko hapa,” akafytaua risasi na kuvunja goti la mguu wake mmoja, kisha akasonya na kupotea akiacha maumivu, kifo na kilio ndani ya chumba hicho.

  • * *

Amata akatupi begi lake katika kiti cha nyuma na kujiweka kiti cha mbele.

“Vipi?” Chiba akauliza.

“Mmoja kafa, mwingine atakuwa kiwete milele na wengine tunawafuata leo hii hii,” Kamanda akajibu huku Chiba akiondoka eneo lile na kutokomea gizani.

“Itawezekana kufunga kazi usiku huu? Maana nilikadiri saa sabini na mbili,” Chiba akauliza huku akiiacha barabara kubwa na kuingia kwenye barabara ya vumbi iliyopita katika miti mingi ambayo moja kwa moja ilikuwa ikielekea Bahrain House.

“Usijali, hapa kazi tu, ndani ya saa hizi arobaini na nane tayari huyu mtu atakuwa mikononi mwetu. Naamini Madam atafanya ulivyomwambia,” Kamanda akaeleza huku akiweka bastola yake na silaha nyingine tayari tayari.

“Usihofu juu ya Madam, ameona jua kabla yetu”.

Chiba akaegesha gari ndani ya jengo hilo na kuteremka kisha akaingia mahala fulani na kuchukua silaha mbili tatu na mavazi ya kutumia katika hali halisi itakayowakumba, mabomu ya machozi na vinyago vya kuzuia sumu hiyo, mavazi ya kuogelea na mitungi ya hewa mine. Sehemu nyingine ya jengo hilo akafungua boti ndogo iliyokuwa kwenye kitoroli na kuivuta kwa mikono yake mpaka, ndani yake akatupia vile vitu na kuisukuma mpaka majini. Bahari haikuwa mbali na jengo hilo kuukuu: Kamanda Amata na Chiba wakaingia kwenye boti na kuiwasha, safari ikaanza.

“Watatusubiri kwa njia ya barabara, sisi tutaingia kwa njia ya maji!” Chiba akasema.

ITAENDELEA

Msako wa Mwanaharamu Sehemu ya Tatu

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment