SIMULIZI Pumbazo - Ep 1
SIMULIZI

Ep 1: Pumbazo

SIMULIZI Pumbazo - Ep 1
SIMULIZI Pumbazo – Ep 1

IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Simulizi : Pumbazo
Sehemu Ya Kwanza (1)

ILIKUWA yapata majira ya saa tatu na dakika zipatazo kumi na mbili kwa mujibu wa saa yangu ya mkononi.
Nilikuwa nimegida chupa za pombe zipatazo tatu na hapo nilikuwa nikikisikia kichwa changu walau kwa kiasi fulani kikiwa kimechangamka na ule mzigo wa mawazo ukiwa umepungua.
Ilikuwa ni kawaida yangu kila ninapotingwa sana na kazi ofisini basi hata kabla sijafika nyumbani ilikuwa ni kanuni moja lazima nipite baa kwa ajili ya kujiweka sawa. Si kwamba nilikuwa nikiiamini sana pombe la! Ulikuwa utaratibu tu…

Wahudumu wa pale walikuwa hawanichangamkii sana kwa sababu sikuwa aina ya yule mwanaume ambaye wao walitaka niwe, mwanaume wa kuwatongoza ama kama sitawatongoza basi niwe nawapa ofa ya kunywa bia walau moja moja. Au kama sifanyi yote hayo basi walau niwabughudhi kwa kuwashika maziwa na makalio yao ambayo yamenona.
Mimi sikuwa na ukaribu huo kwao hivyo hata katika meza yangu sikuwa nimezungukwa na wahudumu, nilikuwa nipo peke yangu. Na wala sikutarajia mgeni yoyote yule katika meza yangu……
Nikiwa katika kuianza chupa ya nne mara nikasikia sauti ya kike ikisema nyuma yangu, ilikuwa ikiniomba kuwa kama sitajali basi aketi pamoja nami.
Huyu hanijui vizuri! Niliwaza kimyakimya
Nikaitazama chupa yangu, na nilikuwa najikubali sana linapokuja suala la kunywa bia upesi. Nikaona si tatizo akiketi kwa sababu baada ya dakika tano ama sita hatakuwa na mimi tena bali yeye na chupa tupu nitakazoziacha pale.
Nikamkaribisha akaketi!
Akanisalimia nami nikamjibu huku nikipata muda wa kumtazama uso wake uliojawa na simanzi.
Sikujali lolote na wala sikumuuliza…..
Nikaendelea kugida pombe yangu hadi ilipokaribia kuisha… yeye alikuwa ana pombe yake lakini hakuwa ameinywa hata kidogo, alikuwa amejiinamia tu muda wote.
Anazuga! Nikajisemea huku nikichekea mbavuni
Nikazungusha macho yangu kiwiziwizi na kugundua kuwa licha ya kuinama binti yule alikuwa katika kilio.
Nikatamani kumuuliza lakini nikajizuia kwa sababu kwa kitendo cha kumuuliza basi sikuwa na namna nyingine zaidi ya kuyasubiri majibu yake.
Nikaitazama saa yangu ya mkononi tena, muda ulikuwa unakimbia haswa. Nikamkumbuka mama Jose. Huyu alikuwa ni mke wangu, kati ya wanawake wote niliowahi kukutana nao kabla sijaoa hadi kuja kukutana na mama Jose na kuzaa naye mtoto mmoja.
Sikuwahi hata siku moja kushuhudia siku ambayo mwanamama huyu alinizoea na kupunguza wivu.
Alikuwa na wivu mkali sana.
Ili kuepusha shari nikaona kuwa ni heri niende nyumbani. Nikamuita muhudumu na kumuulizia juu ya baki yangu katika ile pesa niliyokuwa nimempatia.
Muhudumu yule akauvuta mdomo wake kwa ghadhabu huku akionekana waziwazi kutawaliwa na chuki…
Labda alitaka niisahau ile pesa ili iwe baraka kwake.
Lakini ubaya mimi sikuwa mtu wa kusahau!!
Baada ya kupewa baki yangu, nikasimama niweze kuondoka. Nikamuaga yule dada ambaye muda wote alikuwa ameinama akilia kwa uchungu.
Hakunijibu badala yake alinyanyua uso wake na kunitazama.
Uso wake ulikuwa umevimba bila shaka ni kwa sababu ya kulia kwa muda mrefu, nilimtazama kwa uchache lakini nilimwona kama mtu aliyetingwa na jambo kubwa sana ambalo halipoozeki kwa kunywa bia za idadi yoyote ile.
Kuna mguso niliupata lakini hapohapo nikamkumbuka tena mama Jose. Nikaamua kuondoka.
Nyumbani hapakuwa mbali sana, ni kama mita mia tatu na nukta kadhaa hivyo nilitembea kwa miguu.
Nilifika getini na kuanza kubisha hodi lakini hakuna aliyekuja kufungua.
Nikabisha tena hodi bado mlango haukufunguliwa, nikatoa simu yangu ili niweze kumpigia mama Jose lakini nikakumbuka kuwa sikuwa na salio la kuweza kupiga simu.
Ni nini kimemlaza fofofo hivyo mama Jose……
Nikatambua kuwa sina namna nyingine zaidi ya kufanya zaidi ya kurejea nilipotoka ninunue muda wa maongezi na kisha kuwasiliana na mama Jose anifungulie geti.
Moyoni nilikuwa nimeghadhabika huku nikijiapiza kuwa kama mama Jose ameacha kunifungulia geti kwa sababu ya hasira zake za kipuuzi basi kwa mara ya kwanza ataijuwa ladha ya kupigwa na mumewe.
Wakati natafakari namna ambavyo nitamnyoosha mama Jose mara nikashtushwa na sauti ya kilio kwa mbali, bila shaka kilikuwa ni kilio cha mwanamke na alikuwa katika kuomba msaada.
Nikasikiliza kwa sekunde kadhaa ile sauti ikasikika tena….
Nikaipuuzia lakini nikakumbuka kuwa kabla sijawa na kazi yangu hii ya sasa iliyokuwa ikinipa msongo wa mawazo kila kukicha niliwahi kulitumikia jeshi la polisi.
Nikajisikia kuguswa sana na kilio kile lakini hapohapo nikihofia usalama wangu kwa sababu sikuwa polisi tena.
Nikapuuzia na kuendelea mbele kurejea kule baa ambapo kuna duka linalochelewa sana kufungwa. Hapo ningeweza kununua muda wa maongezi na kuwasiliana na mke wangu.
Wakati naendelea kupiga hatua mara nikasikia vishindo. Nikasita na kutulia tuli huku uoga nao ukiniingia kwa sababu sikuwa na silaha yoyote pale.
Ghafla mbele yangu akatokea mwanamke akiwa yu uchi wa mnyama, akaanza kukimbilia kuja upande niliokuwa hapa sasa nikataka kutimua mbio lakini nikajikaza. Akafika na kutaka kunikumbatia…. Nikapiga hatua kadhaa nyuma akaanguka chini huku akinililia kuwa nimsaidie.
Alipomaliza kunisihi vile hapohapo wakatokea wanaume wawili waliokuwa wanamkimbiza, hawakuonekana kuwa na silaha.
Wakasimama wakinitazama, wakaniambia niwaachie yule binti kwani ni dada yao anafanya umalaya wanataka kumrudisha nyumbani.
“Kaka usiwasikilize hao mimi sio dada yao… siwajui wanataka kuniua wanataka kuniua..” Alinisihi kwa sauti ya chini huku akiwa bado anahema juu juu.
“Mjomba eeh!Hili jambo halikuhusu tafadhali usinunue kesi usiyoijua haumjui huyo dada wala sisi hautujui… ila sisi kwa sisi tunajuana huyo ni dada yetu tunamuomba…..” sasa alizungumza mmoja aliyekuwa mrefu huku akinisogelea.

Hadi wakati huo sikuwa na uhakika kama nahitaji kumsaidia yule dada ama la.
“Kaka… nimekaa meza moja na wewe baa… sikuwa nafanya umalaya pale usiwaamini nakuomba wataniua….” Alizungumza tena kwa sauti ileile. Hapa sasa akanifanya nimtupie jicho mara moja na kugundua ni mwanadada yuleyule tuliyeketi naye pale baa….
Hapa sasa nikahisi anahitaji msaada…..
Nikiwa sijajua nitaondoka naye vipi, tayari mtu mrefu alinifikia na kunisukuma.
Pombe ilikuwa imenilegeza kidogo nikayumba lakini sikuanguka.
Nikamtazama bwana yule na kutambua kuwa mwili wake ni wa hovyo tu, mwili mkubwa lakini hana mbinu ambazo mimi nimepitia nikiwa jeshini.
Hapohapo nikaamua kukumbushia enzi nikafyatuka teke moja kali likamkumba katika mbavu zake akatokwa na mayowe makubwa.
Sikumpa nafasi ya kufikiria nikaokota jiwe na kumrushia yule aliyekuwa anakuja kutoa msaada likampata barabara kifuani.
Nafsini nilikuwa namlaumu sana mama Jose kwa kuacha kunifungulia mlango maana nilijiuliza ikiwa kweli wale ni kaka wa dada yule ni kesi gani hiyo nilikuwa nimeinunua…..
Licha ya hayo sikuacha kupambana… nikamfyatua tena yule mtu mrefu teke la ubavu wa pili.
Kisha upesi nikatoa kitambulisho changu cha kupigia kura kisha nikawatetemesha kwa kuwaonyesha kile kitambulisho ambacho niliamini kabisa kuwa hawatapata ujasiri wa kunilazimisha wakisome.
Nikajitambulisha kama mwanajeshi na kuwasihi waondoke pale mara moja kabla hawajalala pabaya.
Wakatimua mbio bila kusema neno lolote lile wakamwacha yule dada akiwa yu uchi wa mnyama mbele yangu.
“A….A….sa….nte…” maneno haya yakamtoka yakiwa ya mwisho kabisa kabla hajapoteza fahamu zake.
Hapa sasa nikajikuta katika kuchanganyikiwa.
Nitafanya nini na mwili wa mwanamke aliye uchi wa mnyama halafu hana fahamu zake na usiku ulikuwa umeenda.
Ilikuwa tayari saa tano kasoro dakika chache sana.
“Ramadhani mimi nimejinunulia kesi mbaya kabisa hapa….” Nilijisemea huku nikiwa sijapitisha maamuzi ya aina yoyote ile……

Nilibaki katika sintofahamu katika giza lile lisilotisha sana lakini lilibaki kuwa giza lililomaanisha ule ulikuwa usiku.
Nikawa najiuliza ni maamuzi yapi sahihi natakiwa kuyachukua.
Nikafikiria kumwacha pale yule binti aliye uchi wa mnyama nami niondoke zangu kwa sababu hata jina lake tu nilikuwa silifahamu.
Nikamtazama jinsi uso wake ulivyotazamika bada ya kupoteza fahamu, alinihitaji haswa kwa wakati ule.
Nikajiuliza ni vita kubwa kiasi gani nitaiibua nikisema nimbebe binti yule eti niende naye nyumbani kwa mama Jose mke wangu kisha nimueleze eti yule mwanamke asiyekuwa na mavazi nimemuokota huko na sasa nimekuja kumuhifadhi.
Walah! Mama Jose aidha angejiua ama la kesho yake angefungasha virago vyake na kuondoka.
Kuhusu hili la kumpeleka binti yule nyumbani nikalifuta kabisa katika kichwa changu.
Nikiwa bado katika kufikiria mara binti yule akachezesha mguu kisha akafumbua macho…..
Baada ya muda mchache alikuwa wima akijaribu kujificha kwa sababu alikuwa yu uchi wa mnyama.
Nikavua shati langu upesi na kumpatia akajifunga kiunoni halafu nikavua na fulana yangu ya ndani nikampatia akajistiri juu.
Nikaongozana naye huku nikimuuliza ni wapi nyumbani kwao ili nimpeleke, akakataa katakata akasema ni kweli ana kwao lakini hawezi kwenda kwa usiku ule na kwa siku inayofuata pia hataweza kwenda.
Nilitamani sana kumuuliza nini tatizo hadi ashindwe kwenda nyumbani kwao lakini nikaona huo haukuwa wakati muafaka.
“Nisikilize binti, chukua hii pesa nenda ukalale nyumba ile pale ya kulala wageni. Lipia siku mbili…. Huo ndo msaada wangu pekee kwa sasa, nimeoa na ninajua wakati huu mke wangu atakuwa ana mashaka makubwa sana, sijawahi kuchelewa kurudi nyumbani kwa kuchelewa kiasi hiki…..” nilimsihi huku nikimkabidhi kiasi kile cha pesa.
Alizipokea huku akinishukuru sana kwa kumwepusha na balaa lile la kubakwa na wale vijana wabaya.
Sikutaka kurefusha maongezi zaidi nikaondoka katika uelekeo wa kuelekea nyumbani kwangu, tayari nikiwa nimesahau kuwa kilichokuwa kinanipeleka kule nilipokutana na yule binti ni safari ya kwenda kununua muda wa maongezi niweze kumpigia mama Jose.
Nikaitazama saa yangu, muda ulikuwa umeenda haswa nadhani hata lile duka nililojiaminisha kuwa lilikuwa linachelewa sana kufungwa lingekuwa limefungwa tayari.
Nikaamua kuelekea nyumbani kwangu nikiwa kifua wazi.
Nilitembea upesiupesi huku uoga ukiniingia, niliwahofia wale wanaume huenda wameenda kukusanya wenzao na kisha kunivizia wanifanyie lolote la kunidhuru.
Baada ya kuitazama saa yangu niliificha simu katika pensi yangu niliyokuwa nimeivaa kwa ndani.
Sasa nilitembea upesiupesi sana huku kila mara nikigeuka nyuma…. Hadi nilipofika mlangoni kwangu.
Safari hii niligonga mara moja tu nikazisikia hatua zikisogea kuja mlangoni, sikuhitaji kufanya uhakiki nilishatambua kuwa zilikuwa hatua za mama Jose.
Aliuliza nikajitambulisha, akanifungulia mlango. Nikataka kuingia mara akajitanda mlangoni ili nisipite bila hiari yake.
“Mbona umechelewa sana kurudi?Mbona upo kifua wazi?Mbona unahema juu juu mume wangu?”aliniuliza maswali mfululizo.
Nikamsihi twende ndani, akanishika mkono tukaelekea ndani wakati huo nikijipanga nini cha kumweleza ili anielewe vizuri pasi na kutia mashaka yoyote yale.
Tulifika sebuleni, nikataka kuyumbisha maneno nikajikumbusha kuwa gharama ya kuutunza uongo ni kubwa sana.
Nikamfikiria mke wangu alivyokuwa mtu wa kukuza mambo, jambo dogo kulifanya kuwa kubwa kupita maelezo. Nikajipangia majibu ambayo anaweza kuyatoa, jibu la kwanza atakalotoa kwa maelezo yangu ni kwamba nimefumaniwa na mwanamke nimekimbia kutoka nyumba ya kulala wageni ndo maana sina shati.
Jibu la pili ambalo angefikiria ni kwamba nilikuwa na Malaya ama changudoa ambaye tulielewana bei lakini sikumpa sawa na alichohitaji hivyo tumeishia katika mgogoro mkubwa na akaamua kubaki na shati langu kama fidia.
Kwa mantiki ile nikapima katika mzani na kuona ni heri uongo utakaomuacha salama mke wangu huku nami nikiwa na amani kuliko ukweli ambao utazua mengi mabaya yanayokera.
Nikamweleza mke wangu kuwa nilikabwa na vibaka, nikatumia uzoefu wangu wa jeshi kuwatoroka.
Mama Jose akanipa pole lukuki huku akinipooza.
Akaniandalia maji bafuni nikaoga kisha tukala pamoja chakula.
Usiku huo ukapita.
Japokuwa nilikuwa nimechoka sikuwa mvivu katika kuamka, niliamka kwa wakati nikafanya mazoezi ya kukimbia kama ilivyokuwa kawaida yangu.
Niliporejea ndani nilitarajia kukuta mke wangu ameniwekea maji bafuni, kwa sababu hayo ndiyo yalikuwa maisha yetu ya kila siku nikimaliza kufanya mazoezi.
Ajabu haikuwa vile nikamkuta ameketi sebuleni akiwa yu katika utulivu wa hali ya juu sana katika maungo yake yote kasoro mdomo wake tu.

Mama Jose alikuwa amenuna na alikuwa ameuvuta mdomo wake kwa kiasi kikubwa!
Balaa! Nikajisemea, lakini nikajifanya kama sijaitambua hali ile ya mabadiliko ya ghafla kwa mke wangu.
Nikataka kumpita niendelee na utaratibu mwingine.
Mama Jose akaninyooshea mkono huku akinipatia simu yake ya mkononi.
“Ongea na Malaya wako.” Aliniambia.
Nikajisikia mapigo yangu ya moyo yakipiga kwa nguvu haswa, ndugu msikilizaji ni heri niwe wazi kuwa japokuwa nilikuwa nimemuoa mama Jose ndoa ya bomani na nilikuwa napendana naye haswa lakini kuna masalia kadhaa bado yalikuwa yameniganda.
Nikajiuliza atakuwa ni nani huyu aliyeisaka namba ya mke wangu na kumpigia simu.
“Malaya wangu….aah! Malaya wa nani?… hiyo simu nani kapiga….” Nilihoji huku nikiingiwa na kigugumizi kikali.
Mama Jose akanikata jicho la chuki, nikajikuta naipokea simu ile.
Kutazama sio kwamba kuna mtu alinipigia simu bali kuna ujumbe ulikuwa umetumwa.
Nikausoma kwa makini kabisa.
“SIJUI HATA NISEME NINI LAKINI ASANTE SANA KWA SIKU YA JANA, NIPO GESTI ILEILE ULIYONIACHA.SIIKUMBUKI HATA SURA YAKO LAKINI NINAPOTAZAMA SHATI LAKO NI KAMA NAKUONA. NIMETAMANI KUKUPIGIA SIMU LAKINI NIMEHOFIA KUWALETEA USUMBUFU USIKU HUU…. SIMU HII SIO YANGU NIMEAZIMA NITOE SHUKRANI.”
Niliingiwa na ubaridi baada ya kuusoma ujumbe ule, kwa maana halisi kabisa iliyotokea jana ulikuwa ujumbe safi kabisa kutoka kwa mwanadada anayetambua mana ya fadhila. Lakini kwa mazingira yale ya ujumbe kutumwa katika simu ya mke wangu nay eye kuwa wa kwanza kuusoma ilihali jana yake nilimwongopea kuwa nilikabwaa, hapo ndipo utata ulipoanzia.
Nilijikuta najutia ule uongo wangu wa siku iliyopita, laity kama ningeusema ukweli nadhani ujumbe huu ungezidi kuiimarisha kweli yangu.
Ubaya ni kwamba neno ninge huja wakati ule wa majuto.
“Rama….. yaani Rama…. Rama umempa mwanamke mwingine namba yangu ili aniumize hivi… Rama!!” Mama Jose alianza kulalamika huku akitetemeka sana na sekunde hiyohiyo akaanza kutokwa machozi.
Na kama ilivyokuwa kawaida yake akaanza kulalamika huku akikumbushia ni jinsi gani wazazi na ndugu zake walimtenga kwa sababu ya kuolewa na mtu asiyekuwa wa dini yake, japokuwa hakuna aliyebadili imani yake lakini hata ndugu zangu mimi hawakuridhika.
Lakini ile nguvu ya mapenzi nikamuoa Aneti ndoa ya bomani tukapata mtoto wa kwanza tukamuita Jose. Na sasa Aneti anaitwa mama Jose.
Mama Jose aliugulia pale kilio cha kwikwi na kila alipojaribu kuzungumza alikuwa akiishia kulia kwa sauti ya juu… niliumia sana kumtazama katika hali ile lakini nilimtambua vyema pale asingeweza kunisikiliza vyema.
Nikaketi katika kochi nikaanza kujipanga namna ya kumtuliza.
Lakini kabla akili aijapata mbinu za kumtuliza mara nikashambuliwa ghafla nawazo.
“Namba ya simu ya mke wangu yule binti ameitoa wapi?”
Nikasimama wima mdomo wazi mikono kiunoni.
Nikajikuta katika pumbaziko la namna yake!!
Nikatambua kuwa sio mke wangu tu aliyekuwa katika matatizo hata mimi nilikuwa katika tatizo jipya la kutafuta jawabu.
JIFUNZE.
UKWELI unayo thamani kubwa sana….. ukisema ukweli hauna haja ya kukumbuka kwa sababu hata usiku wa manane ukiamka utasema ukweli uleule.
Gharama ya kuutunza uongo ni kubwa sana.
ZINGATIA!!

Isikupite Hii: Geza Anasakwa Auwawe – Ep 01

KUKAA kimya wakati mke wangu analia juu yangu ilikuwa kuhalalisha hisia zake kuwa ni kweli mimi nimempatia mtu namba yake kwa ajili ya kumuumiza jambo ambalo si kweli kabisa.
Nikajikaza kisabuni hatimaye nikazungumza.
“Aneth mke wangu…..nisikilize.sikiliza sasa nikueleze ukweli ulivyo na ninaomba unisamehe sana kwa sababu jana nilikuongopea. Sikujua kama yatakuwa makubwa kiasi hiki…” nilianzia pale na sikumpa nafasi ya kuzungunmza nikaelezea tukio lote lilivyokuwa kwa msisitizo mkubwa sana.
Lakini mke wangu alinitazama kwa jicho la dharau iliyochanganyika na chuki. Ni kama hakuelewa wala kuamini nilichokuwa namueleza.
“Yaani wanaume… sijui mkoje yaani….eti alikuwa uchi wa mnyama ukampa shati lako. Rama nenda ukawadanganye mahawara zako huko sio mimi….kumbuka nimekuzalia mtoto Rama. Nimekataa kuwasikiliza wazazi wangu Rama…” Alinijibu mama Jose kwa malalamiko.
Sikuwa tayari kuona ndoa yangu ikiharibika mapema kiasi hiki, najua hili lingekuwa doa kubwa sana…. Kwa upande wangu baba aliyesema kuwa nimerukwa akili yaani sijaona wasichana warembo wa dini yangu nikamrukia Aneti, sasa angethibitisha kuwa kweli nilikuwa nimerukwa akili iwapo tungeachana. Kwa upande wa Aneti ingekuwa hali ngumu zaidi kwa sababu kwao walikuwa wamemtenga, sasa chuki ingezidi na wangemsimanga.
Ya nini ayapate haya mtoto wa watu?
Nilijiuliza na kuona kuwa bado ninayo nafasi.
“Mama Jose nakuomba simama…. Twende wote, shika simu zangu sipigi simu wala sifanyi kitu chochote naomba twende alipo huyo mwanamke mwenye nguo zangu…. Mama Jose simjui hata jina huyo dada… simjui na utakuwa shahidi… nilimsaidia tu.” Nilimsihi sasa mama Jose, lakini akakataa katakata akasema hayupo tayari kudhalilika mbele ya kadamnasi pale yule mwanamke wangu atakapoanza kumtukana na kumrushia makonde.
Maneno yale ya mke wangu yaliniumiza sana, na laiti kama ningesema niende peke yangu basi ningemwacha katika maumivu makali sana.
Hapo sasa nikalazimika kutumia amri, nikavaa fulana yangu bila hata kuoga. Nikamwambia mama Jose kuwa tunaenda kwa yule mwanamke ikiwa ni amri na si ombi.
Akatii amri japo kishingo upande!
Akajitanda upande wa kanga kustiri nywele zake, tukaondoka.
Kimya kilitanda njia nzima hakuna aliyemsemesha mwenzake. Hatua kwa hatua mimi nikiwa kiongozi hadi tukaifikia ile nyumba ya kulala wageni niliyomuelekeza aingie kulala pale.
Wakati tunataka kuingia niliwaona kwa mbali vijana watatu, mmoja kati yao sura yake haikuwa ngeni hata kidogo.
Nikamsemesha mke wangu kwa mara ya kwanza, nikimwambia kuwa wale vijana mmojawapo namfananisha kama wale waliotaka kumbaka binti yule usiku.
Mke wangu akanitazama kisha akatikisa kichwa kwa masikitiko ni kama alikuwa akiona namlaghai waziwazi.
Hali hiyo iliniumiza sana, ila sikuwa na la kufanya ili kumuaminisha.
Tukaingia ndani ya ile nyumba ya kulala wageni, hapo sasa ikawa mshikemshike nitauliza jina gani na muhudumu anielewe, maana wenye nyumba hizi kwa kutunza siri hawajambo. Mwanao wa kike anaweza akahifadhiwa na bwana ndani ya nyumba zao kwa siku tatu mfululizo, wanajua wazi ni mwanao lakini hawasemi kitu.
Wana roho ngumu! Nilijisemea.
Lakini sikuwalau maana kasheshe la fumanizi nilikuwa nalijua waziwazi, mafumanizi husababisha vurugu na kisha uharibifu wa mali.

Tulienda hadi mapokezi nikiwa bega kwa bega na mke wangu, nikajitambulisha pale mapokezi na kisha kumtambulisha mke wangu.
Na hapo nikaelezea juu ya ujio wa mwanadada aliyejifunga shati na kuvaa fulana nyeupe usiku uliokwishapita.
Ili kumfanya yule bwana aamini zaidi nikamweleza kuwa yule dada nilimpatia pesa mimi alipie siku mbili.
Hapo akatikisa kichwa kukubaliana na nilichosema.
Lakini hakuniruhusu kwenda kumwona badala yake akaniuliza ikiwa kuna mtu mwingine ambaye alitakiwa kuonana na yule dada tofauti na mimi.
Hapo sikuwa na jibu, nikamweleza bayana kuwa yule dada hata jina simjui bali nilimsaidia tu na hatujawasiliana hadi alipotuma ujumbe kwa mke wangu.
Nikamweleza yule muhudumu juu ya tatizo lililozuka na nimekuja hapo na mke wangu ili tu aamini kuwa mimi huyo binti simfahamu kabisa balini msaada tu ambao umenitokea puani mimi.
Maneno yangu yalimuingia lakini alikuwa anashindwa kusema jambo fulani ambalo sikulijua hata.
Baada ya muda akatueleza kuwa anaenda kumuuliza iwapo yupo tayari ili waingie.
“Aah! Nimwambie nani amekuja?” aliniuliza.Nikamwambia amweleze kuwa yule kaka aliyemsaidia usiku.
Yule bwana akaondoka zake akituacha pale na mke wangu.
Kwa jicho la kuibiaibia nikamwona mke wangu kidogo akianza kupata tumaini jipya kuwa nilichomwambia ni kweli tupu. Lakini hakuwa na imani ya asilimia mia.
Baada ya muda yule muhudumu alirejea, alikuwa mwenye mashaka kidogo.
Akatueleza kuwa anajaribu kugonga kile chumba na hakuna majibu lakini ndani kuna mtu. Hapo sasa akatueleza kuwa kuna mwanaume amekuja hapa akidai yeye ni mume wa yule binti na wana miadi ya kuonana, hivyo aliingia ndani na kutoka baada ya muda mchache akidai kuwa anaenda dukani kununua kinga.Tangu hapo hakurudi tena.
Muhudumu akashauri twende kuufungua mlango kwa kutumia funguo za ziada yumkini kuna tatizo.
Hapa sasa badala ya kuvuta mdomo, niliiona hofu machoni mwa mke wangu. Labda alihisi ninamzuga ama aliwaza lolote alilowaza la kumletea mashaka.
Muhudumu akatuongoza hadi katika kile chumba.
Tukajihakikishia wenyewe kwa kugonga kile chumba…. Kweli hapakuwa na majibu kabisa. Zaidi ya kusikia miguno ya kimahaba chumba cha jirani mwanamke akilalamika hapakuwa na sauti nyingine iliyojibu!
Hapo sasa muhudumu akaingiza funguo wa ziada na kuufungua mlango.
Lahaula!
Kitandani hapakuwa na mtu bali mashuka tupu….
Tukaangaza huku na kule na hapo muhudumu akabaini kuwa kuna mtu alitoka kwa njia ya dirishani.
Kwanini apitie dirishani wakati alikuwa hadaiwi chochote?
“Rama usitake kunichezea Rama, kama umenichoka Rama naomba uniache hata bila talaka hiki unachonionyesha ni talaka tosha.” Gatimaye mama Jose alizungumza kwa uchungu huku midomo yake ikitetema kwa hasira.
Muhudumu upesi akakagua mali zake, alikagua hadi kipande cha sabuni kilichokuwa bafuni.
Vyote vilikuwepo hakuna kitu kilichoondolewa.
Watu bwana! Yaani anajali mali zake kuliko usalama wa mteja mwenyewe.
“Mh! Labda ameondoka na kandambili maana aliingia bila viatu..” muhudumu akajisemea huku akiinama uvunguni mwa kitanda kutazama iwapo kandambili zipo ama la.
Alipoinama uvunguni, ghafla akaruka na kujibamiza ukutani.
Mke wangu akatokwa na yowe kubwa la uoga huku akinikumbatia….hii ni baada ya Yule muhudumu kumbabatiza aliporuka.
Macho yalikuwa yamemtoka pima muhudumu. Alizidi kujibanza ukutani huku akitetemeka sana.
Alitaka kusema neno lakini aliishia kuunguruma tu na kupepesa macho.
Hapo sasa niliingiwa na hofu pia.
Nikaamua kwa ujasiri na mimi niiname nione alichokiona muhudumu hadi kujikuta katika hali ile.

HAIKUWA mara yangu ya kwanza kuona tukio ama lile wakati nilipokuwa kazini kabla ya kuamua rasmi kuyavua magwanda na kuendelea na maisha nikiwa kama raia wa kawaida.
Lakini kwa wakati ule sikuwa natishika sana kwa sababu nilikuwa kazini…
Sasa sipo kazini!
Nilishuhudia mwili ukiwa umekunjwa katika namna ambayo mwanadamu wa kawaida ukikunjwa basi tamati yake ni mauti hata pasipo kuhesabu dakika tano.
Shingo yake iligeukia mgongoni huku miguu ikiwa imevunjwa!
Hivyo hata kwa kiumbe kile mvunguni mwa kitanda hapakuwa na haja ya kuusaka ushahidi wa kitabibu kuthibitisha kuwa mwili ule hauna uhai pale ulipo.
MSIMULIZI ANASIMULIA
Hili la kukosa uhai kiwiliwili kile hakukumwogopesha sana Rama. Kilichomwogopesha zaidi ni kwamba aliyeuwawa ni yule mwanadada ambaye usiku uliopita tu alitoka kumsaidia kwa kumpigania asibakwe na kisha kumpatia pesa ambazo zingemtosha kabisa kulala pale kwa siku mbili kabla hajaamua ni wapi aelekee.
Wivu wa mama Jose ulikuwa umetimka mbio na nafasi yake kuchukuliwa na na hofu kuu!
Hofu ya kuishi chumba kimoja na maiti.
Rama alijua hila za maafisa wa polisi, ikiwa watakutwa eneo lile basi watakamatwa kwa ajili ya kulisaidia jeshi la polisi upelelezi……
Upelelezi kwa kesi ya mauaji, ungeweza hata kuwagharimu mwezi mzima bila kuipata dhamana!
Rama akakikamata kiganja cha mkono cha mkewe na kisha akamvuta watoke nje… wakimwacha muhudumu akihaha kupiga simu popote alipojua!!
****
Rama na mkewe wakiwa wanashindana kutembea kwa kasi kubwa walielekea hadi lilipokuwa gari la abiria lililoelekea walipohitaji wao, mama Jose akapanda wa kwanza akifuatiwa na mumewe.
Ikawa bahati mbaya hawakuketi siti moja.
Hata hivyo hakuna aliyejishughulisha na hilo.
Safari ikaanza kwa ukimya wa hali ya juu kati ya wawili hawa…..
Baada ya vituo viwili gari lilisimama na abiria wengine wakapanda, hawa wa sasa hawakupata nafasi za kukaa.
Mama Jose alikuwa amejiinamia muda wote akiombea gari lifike waendapo amsikilize mumewe ataamua nini juu ya hili.
Sasa hakukumbuka kuwa wakati akiwa na wivu hakutaka hata kidogo kumwamini mumewe lakini sasa anahitaji kumwamini na kumtegemea kwa asilimia zote!!
Wanawake bwana!
Mama Jose kila alipoyafumba macho yake aliiona taswira ya kiumbe kile kilichonyongwa katika mtindo wa kutisha sana hadi kilipopoteaza maisha. Hali hii ikamfanya asitamani kufumba macho yake bali kuyaacha wazi kila muda.
Baada ya kuinama kwa muda mrefu, gari lilisimama tena kituo kingine, akaisikia sauti ya kondakta ikiamrisha abiria mwenye mtoto akalie siti ambayo kuna abiria mmoja alitakiwa kushuka.
Kweli gari liliposimama akashuka abiria akiacha pengo katika nafasi aliyokuwa amekaa Mama Jose.
Abiria wakampisha mama mtoto huyo akajibanabana hadi akafika eneo aliloachiwa wazi akaketi, akamsabahi mama Jose.

Mama Jose akajibu huku akiwa bado ameinama……
Mawazo yake hayakuwa hapo kabisa!!!
Gari lilipoanza kuondoka yule mama mtoto akamuomba mama Jose amshikie mtoto ili aweze kutoa nauli kabisa…… hapa sasa mama Jose aligeuka kumtazama yule abiria na hapa ndipo kilipozuka kizaazaa!!
*****
RAMA ANASIMULIA
Licha ya kujifanya kuwa sijatetemeshwa na tukio lililotokea lakini hakika nilikuwa katika hofu kuu, ila sikutaka mama Jose atambue kabisa kuwa nimeogopa.
Niliingia garini na kuketi huku nikishukuru kuwa sikukaa siti moja na mke wangu, nilimjua vyema mama J. Hana subira yule hata kidogo….
Angeanza kuniuliza maswali kedekede palepale garini na kunilazimisha nimjibu kama anavyotaka yeye, sikutaka jambo hilo litokee.
Kweli hatukukaa siti moja!
Nikiwa katika siti yangu, nilikuwa namuona vyema mama Jose. Nilimwona alivyokuwa akiumizwa na mawazo, alikuwa amejiinamia muda wote wa safari ile…. niliamini kuwa kuna haja ya kulisawazisha jambo hili mapema sana.
Nikafikiria pia juu ya ile maiti katika nyumba ile ya kulala wageni, nilijiuliza ni kitu gani kimemsibu dada yule hadi kujikuta katika dhahama ya kuuwawa kifo cha namna ile ya kutisha.
Hakika sikupata majibu, badala yake kichwa kikaanza kuniuma na mimi nikajiinamia kama mama Jose wangu.
Hazikupita hata dakika tano tangu niiname niliposikia makelele makubwa sana kutoka ndani ya ile gari, nikajikuta katika taharuki. Hapohapo nikaunyanyua uso wangu ili nijue ni kipi kinatoke.
La! Haula…..
Alikuwa ni mama J akipiga mayowe huku akimwachia mtoto aliyechukuliwa na mwanamke ambaye nilikuwa namwona mgongoni pekee.
Nikajiuliza kulikoni, huenda kila abiria alijiuliza kulikoni kama mimi.
“Baba Joseeee jiniiiiii….mzimuuuuuu!” sasa alinipigia kelele, sekunde moja akinigeukia huku sekunde nyingine akimtazama yule mwanamke aliyebeba mtoto……
Kelele za mama Jose ziliwatisha sana abiria na hadi dereva akalazimika kusimamisha gari na kuiweka kando.
Kitendo cha mama Jose kuniita kwa sauti kuu vile, hii ikasababisha yule mwanamke kugeuka na kutazama ni nani hasa huyo baba Jose.
Mungu wangu!!
Nikakutanisha macho yangu ana kwa ana na sura ya mwanamke ambaye alikuwa uvunguni mwa kitanda akiwa amenyongwa vibaya mno hadi kupoteza uhai wake kisha kutelekezwa palepale bila msaada wowote hadi tulipokuja kumgundua na sisi tukaondoka kimyakimya kuepuka kujiingiza katika mambo yasiyotuhusu.
Mapigo yangu ya moyo yalipiga kwa nguvu sana macho yetu yalipogongana… nilijiona nikitazamana na maiti aliyefumbua macho ghafla wakati anasafishwa tayari kwa kuzikwa.
Miguu ikaingiwa ganzi kali kisha nikawa natetemeka waziwazi.
Nilikuwa nayasikia tu haya mambo ya kishirikina hapo kabla, kwa mara ya kwanza niliyashuhudia kazini kwangu baada ya mfungwa mmoja kupotea katika mazingira ya kutatanisha yaliyoambatanisha nguvu za giza na kusababisha polisi watatu waliokuwa lindo kutupwa gerezani.
Hii ilikuwa sababu moja kuu sana iliyosababisha nifanye harakati za kuiacha kazi ile.
Sasa ninakutana na mkasa huu wa kutisha…. yaani dakika kadhaa nyuma niliona maiti sasa maiti hii inanitazama.
Mkojo ukabisha hodi, nikaugomea usipenye na kunidhalilisha!!!
Abiria wakaanza kuingiwa na mashaka sasa…na wao wakaingiwa na PUMBAZO
Ikazuka tafarani ya aina yake isiyosemekanika!

MKE wangu alizidi kupiga mayowe ya hofu huku akinisihi nimsaidie, sasa aliniita kwa majina yote aliyoweza na baada ya kuona msaada wa upesi haupatikaniki akaanza kumuita mama yake na Mungu wake kwa juhudu zote.
Yule mama mwenye mtoto alistaajabu, hakuonyesha dalili yoyote kuwa alikuwa na nia mbaya nasi.
Tatizo ni moja tu!
Inawezekana vipi maiti atokee ghafla ndani ya gari huku akiwa na mtoto halafu moja kwa moja akaenda kuketi pamoja na mke wangu.
“Nipisheni…. nipisheni…” nilianza kujitapa. Kisha nikajipuuza baada ya kugundua njia ya kwenda alipokuwa mke wangu ilikuwa wazi kabisa hapakuwa na haja ya mtu yeyote kunipisha, wakati huo wote abiria wengine walikuwa wameanza kuteremka garini kwa kugombea mlango wa kutoke.
Wanawake walisikika wakilia kwa hofu huku waklisemezana kuwa mzuka ulikuwa umevamia garini, wanaume nao hawakusogea karibu na lile songombingo!
Nilipiga hatua kadhaa na kumfikia yule mama mwenye mtoto. Hapa tena tukagonganisha macho.
E walaa!
Alikuwa ni yuleyule binti tuliyeonana siku iliyopita kisha nikamsaidia.
“Unataka nini we mwanamke?” nilimuuliza bila kujipanga vizuri.
“Niwaulize ninyi, mnataka nini kwangu? Maana siwaelewi asilani..” alijibu huku akionekana kustaajabu.
Kitendo cha kunigeukia kwa sekunde kadhaa, hapohapo mama Jose alipanda juu ya siti na kisha akaparamia kioo kabla hajarukia dirishani na kutua nje na kisha kilio kikuu kikasikika.
Kilio cha maumivu!
“Mna nini nyie?” aliniuliza yule mama akiwa na mtoto wake ambaye sasa alikuwa akilia kwa juhudi sana baada ya songombingo ile ya aina yake, watu barabarani walikimbilia mahali ambapo bila shaka ni Mama Jose alikuwa ametua baada ya kutokea dirishani.
Kitendo kile kikanivuta na mimi kutoka nje kwa sababu nilijua tayari mambo si mambo, nikampita yule mwanamke wa ajabu na kushuka chini.
Mama Jose alikuwa ametulia tuli akiwa ameikumbatia barabara ya lami.
Nikauchekecha umati ule hadi nikamfikia mama Jose.
“Mama Jose… we mama Jose….. Anetiii…Aneti hebu amka…” nilimsihi lakini alibaki katika utulivu uleule.
Nikiwa nazidi kupagawa mara nikasikia sauti za kinamama zikinipigia kelele, sikuwa nasikia walichokuwa wanasema badala yake niligeuka na kuona kuna mahali walikuwa wananyoosha vidole.
“Nyuma yako linakuja jiniiii…” mama mmoja alipaza sauti zaidi.
Ebwana ee! Ile nageuka nakutana na yule mama akiwa amebeba mtoto wake. Alikuwa anapiga hatua kujongea nilipokuwa nimeinama.
Upesi nikasimama wima, nilijidanganya kuwa nimesimama kiujasiri sana lakini haikuwa hivyo nilikuwa natetemeka sana.
“Samahani kaka yangu…. samahani sana nakuomba nizungumze nawe dakika moja tu!” alizungumza kwa utulivu huku akionekana pia kupagawa.
“Nini? Nani? Uzungumze na nani?” niliuliza kibwege.
“Kaka yangu sijui ni nini kimetokea hadi inakuwa hivi ilivyo…. naomba unieleze huenda kuna jambo mimi na wewe hatulijui!” alinisihi.
Kauli zake thabiti sana na bila kupepesa macho zilinifanya nikaanza kumuamini.
“Wewe ni nani?” nilimuuliza.

“Naitwa Nasra… Nasra binti Kombo. Mwanangu anaitwa Nusrati… naitwa mama Nusrati.” Alinijibu kwa kirefu… wakati huo tayari watu walikuwa wametuzunguka.
“Jana tulikuwa wote baa… baadaye ukakabwa na majambazi nikakufadhili nguo zangu na pesa… umenizushia kesi kubwa sana kwa mke wangu na asubuhi hii….. asubuhi hii dakika chache zilizopita…..” nilishindwa kusema neon nililotaka kumalizia kwa sababu halikuwa jambo jepesi…. kusema kuwa nilimkuta amepoteza uhai ilikuwa ni sawa na kujiopeleka polisi na kusaidia upelelezi wa kesi hiyo.
“Kaka yangu, si mimi niliyekuwa nawe, sinywi pombe wala si mtembezi wa usiku nitamuacha nani na mwanangu….. huenda umeonana na Hajrati”
“Hajrati… Hajrati ni nani?”
“Hata simfahamu…” alinijibu huku akionekana kupagawa, jibu lake likasababisha raia waanze kupiga kelele kumzonga kuwa ni mwongo.
“Hajrati…. Hajrati niliambiwa kuwa nilizaliwa pacha na kisha katika mazingira ambayo siyaelewi vizuri niliporejea kutoka Oman ambapo nilipelekwa tangu utoto wangu sijabahatika kumuona huyo Hajrati.” Alijibu kwa kirefu.
“Na niliambiwa kuwa tofauti kubwa kati yetu ni hiki kidoti puani, yeye hana mimi ninacho…” alimalizia utetezi wake huku akiwa bado mwenye hofu.
Kwa utetezi huo nilifumba macho mara moja na kutambua kuwa ni kweli kabisa nilikuwa nazungumza na mtu mwingine kabisa.
Bila shaka hata yeye alinisoma macho yangu na kugundua hilo.
“Kaka umemuona wapi Hajrati, nina shida naye sana tafadhali nakuomba unielekeze ulipomuona huyo ndugu yangu wa pekee katika ulimwengu huu.” Alinisihi. Sasa sikuwa na hofu kwa asilimia kubwa kama ilivyokuwa hapo awali.
Sikuwa na cha kumjibu kwa wakati ule, bali zilifuata hekaheka za kumsaidia mke wangu kumpandisha katika teksi tayari kwa kumpeleka hospitali.
MSIMULIZI ANAINGIA
ILE hali ya kusikia kuwa Ramadhani na mkewe wamewahi kwa namna moja ama nyingine kuonana na Hajrati kilimtie kimuhemuhe Nasra, kuna kitu kikubwa kilikuwa katika moyo wake. Hakutaka kumwacha Rama kwa sekunde. Alivunja ratiba zilizokuwa mbele yake na kuamua kuandamana na Rama kuelekea hospitali ambapo mkewe alipatiwa huduma ya kwanza, alikuwa ameteguka mguu wake hivyo walimchua kwa madawa mbalimbali kabla hajaruhusiwa kuondoka.
Rama hakumruhusu Nasra aonane na Aneth kwanza hadi hapo atakapokuwa ameuleza ni kitu gani kilichokuwa kinaendelea.
Kweli baada ya Rama kumweleza ukweli mama Jose, sasa aliweza kuonana na Nasra bila hofu kubwa.
Nasra alijiona kama mwenye donge zito haswa kifuani, alitamani kujua juu ya jambo ambalo aliliona kuwa ni la muhimu sana juu ya pacha wake.
Rama alishindwa kumweleza bayana kuwa Hajrati ni maiti katika chumba kimojawapo katika nyumba za kulala wageni. Alijizungusha na kumweleza kuwa alikutana na binti huyo katika baa na baadaye katika hekaheka za kumwokoa asibakwe….
“Atakuwa Vonso huyo… ni Vonso tu…” Nasra alisema kwa uchungu.
Rama akauliza Vonso ni nani… Nasra hakujibu badala yake alibaki kupambana na mawazo yake mwenyewe.
“Yaani inamaana haijatosha tu au?” alisema kama anayezungumza peke yake huku akijifuta machozi kwa kutumia kiganja cha mkono wake.
Rama alikuwa mchovu na aliyetawaliwa na mawazo sana juu ya vitu vilivyopita ndani ya muda mfupi, hata usikivu wake haukuwa mzuri sana kwa nasra.
Akaghairisha mazungumzo yale kwa kumpatia nambari za simu ili waweze kuwasiliana siku iliyofuata.
Nasra akaipokea huku akiwa na majonzi ya waziwazui, kuna kumbukumbu mbaya ilikuwa imetawala kichwa chake.
Si yeye tu hata Rama alitawaliwa na kumbukumbu ya kumwona pacha wa Nasra akiwa mfu. Ukweli ambao hakutaka kumshirikisha Nasra kwa kuhofia kuzua tafrani kubwa sana.
Wakaagana, Rama akiondoka na mkewe na Nasra naye kivyake!
________
MAMA JOSE alilala fofofo sana, lakini Rama hakukumbwa lau na lepe la usingizi. Alikuwa anawaza sana juu ya kila kitu ambacho kimetokea, awali alidhani kuwa ataweza kuikimbia kesi hii kwa kuwakimbia polisi upesi baada ya kumshika kiganja mkewe na kutoroka naye, lakini sasa amekutana na pacha wa marehemu…..
“Sina ujanja hapa hii kesi inazaa na mimi wazi wazi…” alijisemea kwa sauti ya juu kiasi iliyomfanya mkewe ageuke na kuendelea kufurahia usingizi wake.
Akajaribu kuutafuta usingizi lakini ikawa ngumu, akakiona kitanda kichungu. Akainuka na kuketi katika kochi lililokuwa pale ndani.
Dakika hazikupita sana akasikia hatua zikisogea kuelekea katika nyumba aliyokuwa anaishi. Akatega sikio vizuri hatua zikazidi kusogea.
Hatimaye mlango wake ukagongwa….
Ilikuwa yapata saa sita usiku…..
Rama akasikilizia kwa muda kama waliogonga hodi alikuwa anawafahamu, siko likaipokea sauti na ubongo ukamnong’oneza Rama kuwa aliyekuwa anagonga mlango ni bosi wake.
Usiku huu anataka nini? Alijiuliza hukua akisimama kuujongea mlango. Jibu la k2wanza alilojiwekea ni kwamba bosi wake amesikia juu ya majanga yaliyompata na sasa ameona usiku usipite bila kumpa pole.
Lakini upande wa pili aliikataa dhana ile, bosi wake hakuwa mtu anqayejali wafanyakazi wake kiasi kile.
“Nani?” aliuliza kibabe huku akiigiza kuwa anatokea usingizini.
“Rama eeh Martin hapa….. Martin wa ofisini.”
“Mkurugenzi nini tena usiku huu….”
“Aaah! Fungua bwana tuzungumze unataka niliwe mbu nje bwana…” alijibu kimzaha.
Rama akaufungua mlango, mlangoni hakuwa mkurugenzi peke yake, bali palikuwa na watu wanne, wawili kati ya hao aliwatambua kuwa mmoja ni bosi wake na yule wa pili alikuwa ni Nasra!
Pacha wa marehemu!
Sura yake ilijenga chuki kubwa sana na hakuwa na dalili yoyote ya kutabasamu wala kuunda urafiki na Rama.
“Dada unao uhakika kuwa ni huyu?” bwana mmoja alimuuliza Nasra, Nasra akatikisa kichwa kuthibitisha kuwa ni yeye.
“Bwana Ramadhani Said, una dakika tano za kujiandaa tunaondoka wote kuelekea kituo cha polisi, kuna jambo nyeti la kujadili nawe….” alizungumza yule bwana huku akitoa kitambulisho chake na kumpatia Rama.
Rama alipagawa!

Uisku wa saa sita Rama akiwa hajapitiwa na lepe la usingizi, mara anapata ugeni…. ugeni wa kushtukiza.
Anapotoka nje anakabiliana na Nasra pacha wa marehemu, mkurugenzi wake pamoja na askari wawili.
Anapewa dakika tano za kujiandaa ili waondoke naye!!

“Nani?” aliuliza kibabe huku akiigiza kuwa anatokea usingizini.
“Rama eeh Martin hapa….. Martin wa ofisini.”
“Mkurugenzi nini tena usiku huu….”
“Aaah! Fungua bwana tuzungumze unataka niliwe mbu nje bwana…” alijibu kimzaha.
Rama akaufungua mlango, mlangoni hakuwa mkurugenzi peke yake, bali palikuwa na watu wanne, wawili kati ya hao aliwatambua kuwa mmoja ni bosi wake na yule wa pili alikuwa ni Nasra!
Pacha wa marehemu!
Sura yake ilijenga chuki kubwa sana na hakuwa na dalili yoyote ya kutabasamu wala kuunda urafiki na Rama.
“Dada unao uhakika kuwa ni huyu?” bwana mmoja alimuuliza Nasra, Nasra akatikisa kichwa kuthibitisha kuwa ni yeye.
“Bwana Ramadhani Said, una dakika tano za kujiandaa tunaondoka wote kuelekea kituo cha polisi, kuna jambo nyeti la kujadili nawe….” alizungumza yule bwana huku akitoa kitambulisho chake na kumpatia Rama.
Rama alipagawa!
“Dakika nne zimesalia afande!” askari mwingine alimwambia Rama kwa sanifu.
Rama akaingia ndani na kuvaa suruali yake, kisha akabaki katika sintofahamu.
Alimjua vyema mama Jose!
Akisikia jambo kama hilo usingizi utapaa moja kwa moja huku akipagawa na kupiga simu kwa kila ndugu amjuaye usiku huo…..
Rama akajiuliza kuwa itakuwaje ikiwa jambo lenyewe litakuwa ni dogo la kumalizika usiku huohuo, Mama Jose aende kuhangaisha watu na kuwafanya wapagawe?
Pili, itakuwaje ikiwa mama Jose atadamka na kukuta kitanda kikiwa cheupe na yeye Rama hayupo, huo utakuwa mwanzo wa kumuhisi vibaya kuwa ameenda kwa kimada.
Rama alichanganyikiwa na dakika alizopewa zilikuwa zinayoyoma, akaamua kuchukua kalamu na karatasi akaandika ujumbe mfupi na kuuacha pale mezani.
Kisha akatoweka na wale maaskari, mkurugenzi wake pamoja na Nasra pacha wa marehemu.
“Yaani Rama umeichafua sana kampuni yetu…. kumbe uzushi mtupu ulivyotoa vigezo vya kuacha uaskari nasi tukakuamini…” mkurugenzi alikuwa wa kwanza kuvunja ukimya huu. Wale askari wakatikisa vichwa, Rama hakujua kama wanamsikitikia yeye ama wanamsikitikia anayetoa kauli hizo.
“Na utanilipa kwa kuniita mimi jinni mbele za watu….” Nasra naye akazungumza. Wale maaskari wakatikisa vichwa tena, rama akashindwa kuelewa wanamuunga mkono yule binti ama wanamsikitikia yeye.
“Jamani lakini….”
“Hakuna cha lakini Rama ni heri ukaendelea kuwa kimya kuliko kuzungumza utazua mengine…’ askari alimkatisha kwa ghadhabu.
“Sawa lakini…” akataka tena kuzungumza, sasa alikutana na kibao kikali shavuni. Kisha akashikwa mikono yake hna kufungwa pingu!
Ama! Rama alikuwa amekamatika pabaya, mbaya zaidi hakuijua sababu ya yote haya kutokea.
Gari ilisimama mbele ya kituo cha polisi, askari wasiopungua wanne wakiwa na mitutu walikuja kumpokea Rama huku wakimzonga huku na kule kana kwam,ba anaweza kutoroka muda wowote ule.
Rama alikosa la kusema hadi pale alipohifadhiwa katika chumba cha mahabusu, huku akiwa peke yake.
______
RAMA ANASIMULIA KILICHOJIRI.
SIKUTAMBUA nini maana ya tukio lile, ulikuwa ni mfululizo wa matukio mengi ndani ya masaa machache, mfululizo wa visa ambavyo sikuujua muunganiko wake. Kwanza kukyrtana na mwanamke baa akiwa ameketi na chupa yakle ya bia ikiwa imejaa na asiinywe hata kidogo badala yake akitokwa machozi tu, pili kukutana na mwanamke huyuhuyu akiwa anakimbia uchi huku akidai kuwa kuna watu wanataka kumuua, nikapambana nao na kumsaidia kisha nikampatia shati na fulana yangu…..
Kitendo hicho sikukiweka wazi mbele ya mke wangu, palipokucha nikaamkia katika lawama baada ya ujumbe kutoka nyumba ile ya kulala wageni… ujumbe ule ukazua kizaazaa na ili kutetea ndoa yangu ya bomani nikalazimika kuondoka na mke wangu hadi katika nyumba ile na hapo tukakutana na mwili ukiwa umekunjwa vibaya sana na kupoteza uhai.
Nikamshika kiganja mke wangu ili kuukimbia ule ushahidi… katika gari kama filamu vile tunakutana na kizaazaa. Kabla siku haijaisha vizri hata usingizi sijaupata vyema nakutana na hili la kudakwa nyumbani kwangu na kisha kulala mahabusu!
Hakika ulikuwa mlolongo usosemekana!
Chozi likanitoka!
Nikisema nililala mahabusu nitakuwa nimekosea kwa sababu hata sikulala, baada ya masaa kama mawili nikafunguliwa milango na kuchukuliwa kupelekwa katika chumba kilichotawaliwa na giza na mbu wakali walioikosa damu ya mwanadamu kwa muda mrefu.
Nilidhani kuwa nipo peke yangu katika chumba kile ambacho hata mbele sikuweza kuona.
Lakini mara nikasikia sauti ya mtu akijikohoza. Na kisha akazungumza.
“Rama yu wapi Vonso…. tupatie jibu upesi ili tukuache uende kulala na mkeo ama chelewa kujibu na uendelee kuwapa mbu hawa faida.”
Kulisikia jina Vonso kukanikumbusha kauli ya Nasra. Lakini hii ilikuwa mara ya pili kulisikia jina hili, hakuna mahali nimewahi kulikiskia zaidi ya hapa na hapo kabla kwa Nasra.
Sauti ile ilitulia kimya kabisa bila kunisisitiza kujibu.
“Simjui Vonso… sijawahi kulisikia jina hilo zaidi ya leo aliponiambia Nasra.” Nilijibu kwa kujiamini.
“Nasra ambaye muda si mrefu ulimuua dada yake ili asitoe siri zenu!” sauti ile ilinieleza kwa kejeli.
Hapo sasa niliusikia mwili wangu ukiingiwa ubaridi mkali, hata yale maumivu ya kung’atwa na mbu sikuyahisi tena.
“Sijaua na kamwe sijawahi kuua mkuu….” nilijikaza kiujasiri ili nisionyeshe namna yoyote ya kutetereka.
Hapohapo nikasikia mjeledi ukitambaa katika mgongo wangu. Maumivu yakasafiri katika mwili mzima na kujikuta nikipiga magoti bila kupenda.
“Rama utamtaja tu Vonso alipo na mtalipa madhambi yenu….” sauti ilinisihi kwa sauti ile ile iliyojaa fedheha.
Ndugu msikilizaji hapo sikuwa najua lolote la kufikirika wala lenye uhalisia. Nilikuwa katika pumbazo gizani!
Ile kauli ya rama utamtaja tu Vonso hakika ilinichanganya na nilijua maana ya kauli ile kwa jeshi la polisi, ikifikia hatua afisa anakueleza vile maana yake yupo tayari kutumia njia zozote zile ilimradi tu useme kile ulichokificha katika moyo wako.
Nilijua vyema kwa sababu hata mimi nilifundishwa namna ya kumuhoji muharifu.
Mwili wangu ukaingiwa hofu nikiwa bado katika giza lile nene la kutisha lililo chini ya utawala wa mbu wenye kiu ya damu kiasi cha kung’ata kana kwamba wanaondoka na nyama kabisa.
Baada ya hapo nikasikia hatua zikisogea kisha zikatulia, nikawa najiuliza mtu anayenihoji yu upande gani wa mwili wangu.
Hapohapo ghafla taa zenye mwanga mkali zikawashwa na kunimulika machoni.
Ile najaribu kujiziba macho yangu hapohapo nikawa nimefanya kosa kubwa kuuacha mgongo wangu wazi. Mjeledi ukapenya!

Nikapiga mayowe makubwa sana ya uchungu, mayowe yale yakawa kama yameuzima ule mwanga mkali.
Giza likarejea na mbu nao wakachukua utawala wao wa kunishambulia bila kupeana zamu ya kung’ata.
“Silijui jina hilo afande!” nililia huku nikimsihi mtu nisiyemuona.
Kwa sauti ya utaratibu kabisa kana kwamba hakuna kilichotokea mtu yule alinijibu.
“Rama… mimi sijakuuliza iwapo unalijua jina ama la… maana hata majambazi huwa hawajuani kwa majina bali matendo yao. Nahitaji tu unieleze ni wapi tutampata huyo shetwain muuaji mwenzako” alizungumzan huku akimalizia kwa kupiga kite cha ghadhabu.
Alipotaja jina ‘Shetwain’ akili yangu ikafanya kazi upesi na hapo nikagundua kuwa aliyekuwa akinihoji ni mtu niliyekuwa namfahamu.
Nasem,a nilikuwa namfahamu ila si kwamba tulikuwa tunafahamiana.
Huyu alikuwa ni mpelelezi ambaye alikuwa akihusika na kesi nzito nztito.
Ukisikia kesi imefikia hatua ya kukabidhiwa kwake basi utambue wazi kuwa muhusika akikamatwa ni lazima huyu bwana amalize hasira zake kwanza ndipo mambo mengine yaendelee.
Usoni alionekana mpole sana lakini hakuwa na utu katu!
Kwa muonekano wake huu maafande wenye vyeo vya kawaida wakambatiza jina lililoanza kimasihara akalikataa lakini baadaye akalikubali.
Walimuita sajini PILIPILI!
Wakimaanisha kuwa anawasha na kuumiza lakini haui!
Nilikuwa mikononi mwa sajini Pilipili!
Moyo wangu ulipiga kwa nguvu sana huku mwili ukiingiwa ubaridi!
Naam! Nini kinajiri katika mkasa huu… VONSO ni nani na kuna uhusiano gani katika haya yanayotokea…….

ITAENDELEA

SIMULIZI Pumbazo – Ep 2

Leave a Comment