Mwajuma Utamu Sehemu ya Tano
CHOMBEZO

Ep 05: Mwajuma Utamu

SIMULIZI Mwajuma Utamu
Mwajuma Utamu Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA: JUMA HIZA

*********************************************************************************

Chombezo: Mwajuma Utamu

Sehemu ya Tano (5)

Damian alikuwa ni muuza magari show room, japokuwa nilijitahidi kumpamba lakini bado alionekana kuwa wakawaida, hakumfikia Martin kwa utajiri aliyokuwa nao.

“Martin anakupenda tatizo wewe unaichezea bahati,” aliniambia.

“Simpendi,” nilimwambia.

“Kwanini usingemwambia ukweli akajua kuliko hivyo unavyompotezea muda wake?”

“Suzie hivi upo tayari kweli kuacha fuko la hela likupite?”

“Hapana lakini.”

“Sasa ndiyo ujue nilikuwa sina jinsi, acha nitumie pesa zake, moyo wangu haupo kwake, kwasasa moyo wangu unaishi kwa mwanaume mwingine ambaye ni Damian,” nilimwambia Suzie pasipo kujua kuwa baadae ningeweza kuumia na kumwaga machozi kwasababu ya mapenzi.

Usiku wa siku hiyo nilienda kukutana na Damian nyumbani kwake Mbezi Beach, siku hiyo niliacha mambo yangu yote, nilijua nitautumia usiku mzima kuwa naye hivyo nilijipanga kwa mechi ya usiku huo.

Nilipofika nyumbani kwake alinikaribisha huku akinitolea tabasamu pana, nilijihisi kuwa na furaha mno kila nilipokuwa nikimtazama Damian, alikuwa ni mwanaume aliyejua kuiteka akili yangu kisawasawa.

Baada ya stori za muda mfupi Damian aliandaa chakula kwani kilikuwa tayari, tulikula kwa pamoja huku furaha ikionekana kututawala, tulipomaliza kula tuliendelea kupiga stori mpaka pale ulipofika muda ambapo tulikuwa chumbani, wote tulikuwa kama tulivyozaliwa, kilichoendelea wakati huo hakifai kusimuliwa hapa ila wewe fahamu kuwa tulifanya mapenzi usiku huo.

Tulipomaliza kufanya mapenzi Damian aliniambia twende tukaoge ili tuondoe uchovu uliyokuwa umetutawala, nilifanya kama alivyonitaka nifanye, tulipomaliza kuoga tulirudi kitandani kwa ajili ya kulala.

Muda wote huo Damian alionekana kuwa mwenye furaha, nilihisi labda kwa mapenzi niliyompa siku hiyo ndiyo yalimfanya kuwa katika wakati huo.

Kipindi ambapo nilikuwa nimejilaza kitandani, nilianza kuhisi kichwa kikiniuma, maumivu yaliendelea kuongezeka mpaka ukafikia wakati maumivu yakawa yametawala kichwa kizima.

Nilipomwambia Damian kuhusu maumivu hayo ya kichwa haraka akaenda kuniletea maji kwenye glass, aliniambia niyanywe kwani yangeweza kuniponya. Nikafanya kama alivyoniambia.

Maumivu bado yaliendelea kuongezeka, nikaanza kuhisi kizunguzungu wakati huo kichwa kiliendelea kunigonga. Nilishindwa kuyavumilia maumivu hayo mwisho nikaanza kupiga kelele, Damian akaoneka kupagawa. Ni hapo ambapo nilijikuta nikilala usingizi wa nusu kifo, sikujua ni kitu gani kiliendelea tena mahali hapo.


Nilipata fahamu na kujikuta nipo katika chumba kimoja kilichoonekana kuwa kama gofu, mazingira ya chumba hicho yalitisha mno, hakukuwa kuna harufu nzuri iliyotoka eneo hilo, ndani ya chumba hicho palitawala harufu ya kinyesi pamoja na ya mizoga ya binadamu iliyoonekana kuoza na kisha kubaki mifupa tu.

Mazingira niliyoyaona ndani ya chumba hicho yalinitisha mno, nikatamani kuinuka na kukimbia lakini sikuweza kufanya hivyo kwani nilikuwa nimefungwa kamba miguuni na mikononi lakini pia mdomoni nilikuwa nimezibwa kwa gundi ya karatasi.

Kila nilichokuwa nikitamani kukifanya kwa muda huo nilishindwa, mwisho ilibidi nitulie kwani hata pale nilipojaribu kupiga kelele, sauti yangu haikuweza kutoka kwasababu ya ile gundi niliyozibwa nayo.

Nilikumbuka mara ya mwisho nilikuwa kitandani na Damian, sikujua ni nini kilitokea mpaka kikasababisha kunileta ndani ya chumba hicho. Bado niliendelea kujiuliza maswali ambayo kiukweli yalikosa majibu, sikujua mpaka kufikia muda huo nilikuwa eneo hilo kwasababu gani.

Baada ya kupita dakika kadhaa mara mlango wa chumba hicho ukafunguliwa kisha akaingia mwanaume mmoja ambaye alivalia mavazi meusi pamoja na mask iliyonifanya nishindwe kuitambua sura yake.

Alipoingia moja kwa moja akaja kunitoa gundi mdomoni, nikatoa pumzi ndefu kisha nikaanza kukohoa. Mwanaume huyo hakuonekana kujali lolote, alionekana kuwepo mahali hapo kwa ajili ya kukamilisha kazi yake, alichoamua kukifanya aliingiza mkono wake upande wa nyuma ya suruali kisha akatoa bastola halafu akanielekezea usoni kuashiria kuwa alidhamiria kunipiga risasi kwa muda huo.

Niliamini huo ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yangu, nilikuwa nikitetemeka, japokuwa sikujua nilifanya kosa gani mpaka kufikia hatua ya kutekwa lakini mwanaume huyo alioenakana kudhamiria kuniua.

“Nimekukosea nini?” nilimuuliza mwanaume huyo kwa kujiamini, swali langu likaonekana kuwa kituko, akaitoa bastola kwenye paji la uso wangu kisha akaanza kucheka kama mwendawazimu.

“Nipo hapa kwa ajili ya kukuuwa kama nilivyowaua malaya wenzako,” alinijibu mwanaume huyo.

“Kivipi na nimekukosea nini?” nilimuuliza.

Maswali yangu yalianza kuonekana kuwa kero kwa mwanaume huyo, alichokifanya ni kuitoa ile mask aliyokuwa ameivaa, ni hapo ambapo nikaiona sura yake, haikuwa ngeni machoni mwangu.

“Damian!” niliita kwa mshangao mkubwa.

“Yeah..” aliitika kisha akawa anaibusu bastola aliyokuwa ameishika.

Nilihisi kuchanganyikiwa baada ya kumuona Damian mbele ya macho yangu, kwa maana hiyo yeye ndiye aliyehusika kuniteka, sikutaka kuamini hata kidogo.

“Huu ni mpango wa kukuangamiza kama nilivyowaangamiza malaya wenzako,” aliniambia kisha akaikoki bastola yake tayari kwa kunimiminia risasi.

“Unataka kuniua?”

“Ndiyo tena sasa hivi.”

Majibu ya Damian pamoja na muonekanao aliyokuwa nao uliitosha kuelezea kuwa yeye ndiye alikuwa jini mweusi ambaye jeshi la polisi lilikuwa likimtafuta usiku na machana, aliua machangudoa wengi sana na siku hiyo alikuwa katika mpango wa kuniua na mimi pia.

Sikutaka kuamini kama nilinasa kama mtego huo na nilichokuwa nikikisubiri ni kupigwa risasi kisha uwe ndiyo mwisho wa maisha yangu. Kumbukumbu za Savela zilianza kunijia pamoja na kifo chake cha kikatili alichouwawa, ile mizoga iliyokuwa imezagaa ya binadamu ilitosha kuniambia kuwa muuaji alikuwa ni Damian. Nilimchukia sana, nilimuona kuwa binadamu mwenye roho ya kinyama.

“Sali sala zako za mwisho,” aliniambia Damian wakati huo alikuwa ameninyooshea bastola.

Kiukweli niliamini huo ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yangu, kimoyomoyo nilianza kusali sala zangu za mwisho, nilifahamu hata iwe vipi ni lazima ningetoka ndani ya chumba hicho nikiwa maiti.

Machozi yalianza kunitoka, kila nilipokuwa nikimtazama Damian nilihisi kukiona kifo changu ambacho muda wowote kilikuwa kinakwenda kutokea.

“Kabla hujaniua tafadhali naomba nitubu dhambi zangu ili hata nikifa huko niendapo mbinguni niende sehemu salama,” nilimwambia huku machozi yakiendelea kunitoka.

Alichokuwa akikisubiri Damian ni mimi kutubu dhambi zangu kisha anifyatulie risasi kama alivyokuwa amedhamiria, nilifumba macho yangu kisha nikaanza kumuomba Mungu anisamehe madhambi yangu kwani muda mfupi ningekuwa katika safari ya kwenda mbinguni.

Paa… paa …paa…

Nilichokisikia wakati nilipokuwa nimefumba macho yangu ni milio ya risasi, niliamini risasi hizo nilipigwa mimi, nilipoyafungua macho yangu kwa mara nyingine sikutaka kuamini kile nilichokuwa nikikishuhudia. Niliuona mwili wa Damian ukiwa chini huku ukitapatapa, damu zilikuwa zikimtoka kutokana na risasi alizokuwa amepigwa.

Ghafla! niliwaona polisi wakiwa ndani ya chumba hicho, sikutaka kuamini kile kilichokuwa kimetokea katika maisha yangu, yaani kama sio kutokea polisi ningeshakuwa maiti siku nyingi.

Polisi walinisaidia kunifungua kamba nilizokuwa nimefungwa nazo miguuni na mikononi, siku hiyo ndiyo ilikuwa mwanzo wa kuokoka na kifo nilichokuwa nimekikaribia.

Polisi walionekana kufanikiwa kazi yao kwa asilimia mia moja kwani muuaji huyo aliwasumbua mno, siku hiyo ndiyo walifanikiwa kumkamata na baada ya kumpiga risasi alifariki dunia hapohapo.


Baada ya kunisurika kifo na Damian au jini mweusi kama alivyokuwa akijulikana niliachana na biashara ya uchangudoa, sio mimi tu bali hata Suzie na yeye alichana na biashara hiyo.

Jambo la kushangaza baada ya Martin kurudi kutoka Dubai, Suzie aliitumia nafasi hiyo kumueleza kila kitu ambacho kilitokea katika maisha yangu.

Martin alinichukia baada ya kuambiwa hayo na kama haitoshi aliamua kuhamisha mapenzi kwa Suzie ambapo walifanikiwa kufunga ndoa na kubahatika kuzaa watoto mapacha, Gracious na Precious.

Niliumia sana baada ya tukio hilo kutokea hata hivyo sikuwa na wa kumlaumu, maisha yangu niliyachezea mwenyewe.

Baada ya kupita miezi mitatu niliamua kwenda kupima, majibu yalionyesha kuwa nilipata maambukizi ya virusi vya ukimwi hivyo nilitakiwa kuanza kutumia vidonge vya ARV kwa ajili ya kuongeza siku za kuishi.

Ni pigo kubwa katika maisha yangu, kiukweli najutia mambo mengi tena machafu niliyoyafanya katika maisha yangu, idadi ya wanaume niliyotembea nao inafika mia tatu.

Maisha ya mjini yalinishinda, niliuza kila kitu nilichoachiwa na Martin kama zawadi katika maisha yangu. Japokuwa ni miaka mingi sana imepita tangu nilipoondoka nyumbani kwetu Mtwara lakini niliamua kurudi.

Sikuwa ni Mwajuma yule wa zamani tena ambaye nilionekana kuwa mrembo wa sura mpaka umbo la kumvutia mwanaume yoyoye rijali, huyu wa sasa nilikuwa naishi na virusi vya ukimwi na muda wowote Mungu anaweza kunichukua kwani afya yangu imezidi kudhoofika.

FUNZO: Katika maisha wakati mwingine jifunze kutokana na makosa ya mtu mwingine, nimeamua kukusimulia kumbukumbu za maisha yangu ili na wewe ujifunze kutokana na makosa niliyoyafanya.

Naomba ukimaliza kuisoma kumbukumbu hii uyachukue yale yote mazuri kisha uyafanyie kazi na yale yote mabaya tafadhali naomba usiyachukue. Narudia tena katika maisha wakati mwingine jifunze kutokana na makosa aliyoyafanya mtu mwingine.

MWISHO.

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment