Sikuachi Baby Sehemu ya Pili
CHOMBEZO

Ep 02: Sikuachi Baby

SIMULIZI Sikuachi Baby
Sikuachi Baby Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA: JUMA HIZA

*********************************************************************************

Chombezo: Sikuachi Baby

Sehemu ya Pili (2)

Ingawa Sesilia aliendelea kunitumia ujumbe mfupi na kunipigia simu kila wakati lakini sikutaka kujali hilo, nilikuwa nimepanga kuyapeleka majeshi kwa Samira ambaye alikuwa akinichanganya kwa wakati huo.

“Mbona hujibu lolote Metu?” alinitumia ujumbe Sesilia.

“Nipo bize,” nilimjibu.

“Upo bize unafanya nini?”

“Sitaki maswali mengi wewe elewa kuwa nipo bize.”

“Metu.”

“Nini?”

“Mbona unanijibu hivyo lakini?”

“Ulitaka nikujibu vipi sasa?”

“Basi mpenzi ukishamaliza huo ubize utaniambia.”

“Poa,” nilimjibu.

Niliendelea kumfikiria Samira pale kitandani nilipokuwa nimejilaza, akili yangu ilikuwa imetawala jina lake, nilipokuwa nikiitazama picha yake aliyokuwa ameiweka Profile WhatsApp ukichanganya na baridi kali iliyokuwa ikinitafuna nilizidi kumtamani vilivyo.

Kuendelea kuishi na ndoto au mawazo ambayo hutaki kuyafanyia kazi kamwe ni vigumu kubadilika na kuwa kama unavyowaza. Sikutaka kubaki kuishi na ndoto za kumpata Samira ambazo sikutaka kuzifanyia kazi, niliamua kumtumia ujumbe mfupi WhatsApp na kama bahati alikuwa online kwa muda huo.

“Mrembo,” nilimtumia.

“Abee Metu niambie,” alinijibu.

“Picha yako nzuri sana.”

“Ipi hiyo.”

“Hiyo uliyoiweka Profile.”

“Asante mwaya.”

“Usijali unafanyaje?”

“Nimelala, nahisi baridi ya hatari.”

“Pole ila umevaa sweta?”

“Ndiyo nimevaa lakini bado nahisi baridi.”

“Pole vipi nije?”

“Uje wapi?”

“Hapo ulipo?”

“Weee naogopaa.”

“Unaogopa nini sasa?”

“Tuachane na hizo habari niambie mambo mengine.”

“Mambo yako poa kabisa.”

“Nisamehe kwa kukusumbua leo.”

“Usijali hiyo ni kazi yangu wala usijali mrembo.”

“Sawa,” alinijibu.

Nilishindwa kumuingizia mada za kimapenzi kwasababu tayari alionekana kuzikwepa, hakutaka kuwasiliana na mimi kwa njia hiyo, sijui ni kwanini ila hakutaka kufanya hivyo.

Nikajikuta nikikosa maneno ya kumuandikia baada ya kunijibu ujumbe wake wa mwisho aliyouambatanisha na emoji ya mikono miwili iliyojikunja kuashiria kushukuru.

Nikaendelea kubaki online huku nisiwe na cha kumuandikia Samira.

“Nakupenda,” niliandika maneno haya kisha nikawahi kuyafuta, nilihisi kukosea kumuandikia.

“Sawa,” nilimuandikia na kumtumia kisha hapo hapo zikatiki tiki mbili za rangi ya blue kuashiria ujumbe tayari umeshapokelewa na kusomwa.

Nikamuona akiniandikia, nikasubiri jibu lake, wakati huo Sesilia alikuwa ameshaanza tena kunipigia simu, nikawa namkatia simu yake maana nilihisi usumbufu.

“Usiku mwema ila usisahau kesho mapema kuja kunichukua kuna sehemu nataka unipeleke,” alinitumia Samira.

“Sawa haina tatizo,” nilimjibu kisha hazikupita sekunde akawa tayari ameshatoka online.

Kama walivyosema wahenga kuwa siku zote pole pole ndiyo mwendo, sikutaka kuwapinga hata kidogo, niliamini katika msemo huo na ndiyo nilikuwa nikiutumia katika kumfukuzia Samira, sikutaka kuweka papara nyingi maana mwisho wa siku ningeweza kumpoteza.

Sesilia hakuchoka kunipigia simu, aliendelea kunipigia simu mfululizo, mwisho nikaamua kupokea.

“Mpenzi wangu kwanini unanifanyia hivi lakini?”

“Kitu gani kibaya nilichokufanyia?”

“Hupokei simu yangu.”

“ Nilikuambiaje?”

“Hata kama yani ndiyo uko bize muda wote huo halafu nakuona online WhatsApp kwani unafanyaje?”

“Sifanyi kitu.”

“Mmmh! Kweli Metu?”

“Sasa mbona unaguna au unataka nikudanganye?”

“Sio hivyo lakini unavyonifanyia sio vizuri, naumia mwenzako sina amani.”

“Umemaliza?”

“Unasemaje Metu?”

“Nakuuliza umemaliza kuongea?”

“Metusela una nini lakini mpenzi wangu mbona umebadilika sana?”

“Sesilia wewe ni mtu mzima halafu tena ni msomi hivi hata picha unayoiona bado tu hujui ni nini kinachoendelea au unataka mpaka uambiwe kuwa umechokwa hupendwi tena ndiyo utaelewa?”

“Unasemaje?”

“Sikupendi nimekuchoka,” nilimjibu kisha nikakata simu.

Yalikuwa ni maneno machache niliyomwambia Sesilia ambayo niliamini yangeweza kumuumiza sana huko alipo lakini sikutaka kuyawazia sana, kwanza niliamini alikuwa ni msichana na muda wowote angeweza kupendwa na kunisahau katika maisha yake.

“Kwanini umenifanyia hivyo Metu kwanini hukuniambia mapema kwamba hilo ndiyo lilikuwa lengo lako. Ziko wapi zile ahadi zako za kwamba utanioa na kunithamini kama mwanamke wako. Umenichoka baada ya kukupa mapenzi sawa Metu nashukuru sana ila sitaki kuamini kama kweli nimeachana na wewe,” alinitumia ujumbe mfupi Sesilia.

Niliusoma ujumbe huo kisha nikaufuta, sikutaka kuvishughulisha vidole vyangu kumuandikia ujumbe wa kumjibu. Kwa hasira nilizokuwa nazo nilifuta na namba zake huku nikiamini nilikuwa nimezikariri kichwani na kama angeweza kunitafuta siku na muda wowote basi namba yake niliifahamu. Siku hiyo ilipita huku nikiwa nimempa maumivu Sesilia asiyoyatarajia.

                                              ****

Niliamka katika siku nyingine ya jumapili ya mihangaiko kama ilivyokuwa kawaida yangu, nilijiandaa na kujiweka vyema tayari kwa kuichukua bodaboda yangu kwa ajili ya kwenda kumchukua Samira ambaye alipanga siku hiyo kutoka.

Sikuwa nafahamu alipanga kwenda wapi mapema yote ile hata hivyo sikutaka kujifanya mpekenyuzi sana, niliamua kumfuata nyumbani kwake ambapo hapakuwa na umbali kutoka pale nilipokuwa nikiishi.

Nilipofika nilipigia honi kisha akatoka nje, alikuwa amevalia mavazi yaliyompendeza sana, nilimtazama kwa jicho la kimatamanio kisha nikamfia kuwa alikuwa amependeza sana.

“Asante Metu vipi uko poa?” aliniuliza huku tabasamu likiwa bado limetawala usoni mwake.

“Niko poa,” nilimjibu kisha nikaendelea kumtazama jinsi alivyokuwa amependeza.

“Bila shaka shemeji anafanya kazi yake ipasavyo,” nilimwambia maneno ya kumtega huku nikitaka kufahamu kama alikuwa na mwanaume.

“Ndiyo tena anafanya kazi kubwa sana,” alinijibu jibu ambalo kimoyomoyo lilinichoma kwa kiasi fulani.

“Kwahiyo nakupeleka wapi leo asubuhi asubuhi usiyetulie mwanamke wewe,” nilimwambia kisha akacheka.

“Unacheka tena?” nilimuuliza.

“Nimefurahi,” alijibu huku akijaribu kukizuia kicheko chake.

“Haya niambie sasa leo wapi?”

“Nataka unipeleke Magomeni kwa wifi yangu.”

“Magomeni ipi?”

“Mapipa.”

“Sawa hakuna tatizo,” nilimwambia kisha akafunga mlango wa nyumba yake tukaondoka.

Bado niliendelea kuteswa na hisia za kimapenzi nilizokuwa nazo kwa Samira, nilihisi kumpenda sana na iliniwia ugumu kumueleza ukweli. Tulipokuwa barabarani kuna muda nilikuwa nikifunga breki za ghafla! hali ambayo ilimfanya anilalie mgongoni kwa kutumia kifua chache kilichobarikiwa chuchu za kusimama, nilisikia raha sana, mchezo huo ulikuwa endelevu mpaka pale nilipomfisha Magomeni Mapipa nyumbani kwa huyo wifi yake.

“Tumefika,” nilimwambia nilipokuwa nimepaki bodaboda nje ya nyumba ya huyo wifi yake aliyoniambia.

“Ndiyo asante sana,” aliniambia baada ya kushuka kisha nikamuona akiifugua zipu ya pochi yake. Nilifahamu alikuwa akitaka kunilipa lakini nilimsihi asifanye hivyo kitendo ambacho kilimshangaza sana.

“Wewe Metu,” aliniita.

“Nini?” nilimjibu huku nikimtazama usoni, nilikuwa nikitabasamu kwa wakati huo.

“Eti nisikulipe?” aliniuliza huku akionekana kushangaa.

“Ndiyo usifanye hivyo leo acha nikupe ofa Mrembo,” nilimwambia huku nikiendelea kumtazama.

“Ofa gani hii ya kutoka Tandika mpaka Magomeni hivi hayo mafuta huyaonei huruma?” aliniuliza kisha akazidi kuifungua zipu ya pochi yake.

“Nimekuambia usinilipe bana mbona hunielewi?” nilimwambia huku nikijifanya kuikataa ile hela aliyokuwa akitaka kuitoa. Nilikuwa nikimaanisha wala sikutamka kiutaniutani.

“Acha utani Metu,” aliniambia huku akionekana kutoniamini.

“Sikutanii kweli namaanisha,” nilimwambia.

Hiki ndiyo kitu ambacho najilaumu sana na nitaendelea kujilaumu mpaka kesho. Nilikuwa nikipenda sana kuwapa ofa wasichana, sikujali kupata hasara ya mafuta niliyokuwa nikitumia kutoka umbali mrefu, nilichokuwa nikikihitaji ni kuona msichana huyo ambaye nampa ofa mwisho wa siku anakuwa mpenzi wangu na ninafanikiwa kufanya naye mapenzi.

Kuna muda nilikuwa nikipata hasara na yote sababu kubwa ilikuwa ni wasichana lakini sikutaka kujali, niliendelea na mchezo huo ambao tayari ulikuwa umeniingia damuni. Kwa kuwa bodaboda ilikuwa ni mali yangu, nilijiajiri mwenyewe hivyo sikuona tabu yoyote.

“Samira kuna kitu nataka kukuambia,” nilimwambia kabla sijaagana naye.

‘Kitu gani?” aliniuliuza.

“Au basi nitakuambia siku nyingine.”

“Niambie Metu usiogope.”

“Hapana Samira nitakwambia siku nyingine usijali.”

“Kweli?”

“Niamini,” nilimwambia kisha nikaagana naye na kuondoka eneo lile, wakati huo sikuwa nimechukua hata senti moja yake.

Kiukweli nilitamani kumwambia ukweli kuwa nilimpenda na nilikuwa nipo tayari kufanya lolote kwa ajili yake lakini nilisita, kila nilipokuwa nikimtazama nilimuona kuwa msichana mrembo sana, msomi tena alikuwa na kazi yake ambayo ilimfanya aishi maisha ya kujiamini, hakuwa na shida yoyote katika maisha yake.

Urembo wake ulinichanganya mpaka nikawa nimeshaanza kumsahau Sesilia maana nilipoamua kuwalinganisha kwa urembo Sesilia hakuingia ndani hata mara moja kutokana na uzuri aliyokuwa nao Samira.

                                                   ****

Mapenzi yalichukua nafasi kubwa sana katika maisha yangu japokuwa watu wengi waliyokuwa wakinitazama waliamini kuwa mimi ni kijana mpole niliyekuwa na tabia nzuri ambayo vijana wenzangu walitakiwa kuziiga. Upole wangu na ukairimu wa njenje ndiyo uliyofanya nikazidi kuwa na wateja wengi sana ambao waliniamini kupita kawaida.

Wapo ambao waliniamini kuwa mimi ni mchaMungu, nililelewa katika mazingira ya kumjua Mungu hivyo nisingeweza kuwatapeli hata pale ambapo walinipa pesa nikawachukulia mizigo yao sehemu mbalimbali.

Kila mtu alinichukulia vile ambavyo alikuwa akinitazama, hakukuwa na mtu ambaye alinichukulia kuwa kama muhuni, mtu wa kupenda wanawake zaidi ya washikaji wenzangu ambao nilikuwa nikifanya nao kazi hii ya bodaboda. Wao ndiyo walikuwa wakifahamu yale yaliyokuwa yakiendelea katika maisha yangu japo siyo yote, kuna mambo pia walikuwa hawayafahamu.

“Vipi yule demu ulifanikiwa kumchukua?” lilikuwa ni swali la Amani dereva bodaboda mwenzangu ambaye aliniuliza tulipokuwa kijiweni Tandika Azimio, tulikuwa madereva wengi tukipiga soga za hapa na pale.

“Demu gani?” nilimuuliza huku nikionekana kusahau. Wale madereva wengine wakaanza kunicheka.

“Yule wa chuo,” aliniambia.

“Nani Sesilia?”

“Ndiyo huyohuyo.”

“Dah! mbona huyo demu nimeshambwaga siku nyingi sana.”

“Umeshambwaga?”

“Sasa niweke kambi ili iweje?”

“Mwanangu unazingua yule mtoto alikuwa anakuelewa sana yani mara hii umeshambwaga?”

“Kuna demu mmoja hivi ananichanganya sana akili yangu.”

“Demu gani tena?”

“Samira.”

“Nilijua tu! yani wewe mwaka huu tutakuzika.”

“Hahahaha! usiogope yani huyu nikifanikiwa kumpata moyo wangu utajisikia furaha sana,” nilimwambia maneno ambayo yalimuacha kinywa wazi, akabaki akinitazama muda wote huku asiwe na neno la kuniambia.

Hakukuwa na habari nyingine nilizozizungumza zaidi ya Samira, nilikuwa nikimuongelea na mara zote nilimsifia, hilo liliwafanya madereva wenzangu baadhi waanze kunichukia. Mmoja alikuwa ni Jamal ambaye alionekana kuchukizwa sana na maneno yangu ya kumsifia Samira.

“Hivi hakuna habari nyingine za kuzungumza?” aliniuliza.

“Sasa unataka nizungumze nini tena kama sio wanawake ambao wameumbwa kwa ajili yetu au hupendi jinsi ninavyomsifia?” nilimuuliza huku nikitabasamu.

“Tatizo sio kumsifia yani umezidi kuongelea sana kuhusu wanawake kwani hakuna habari nyingine za kuzungumza?”

“Jamal kwani bifu liko wapi?”

“Sio swala la bifu umezidi bana,” alinijibu Jamal huku akionekana kuchukia kwa kiasi fulani. Nikazidi kushangazwa na tukio hilo, msichana nimpende mimi, nimsifie mimi halafu mtu mwingine achukie hivi hii imekaa vipi. Niliona ni ujinga kuendelea kubishana, nikaamua kukaa kimya.

                                      ****

Sikupanga kuishia kumtazama usoni au kuzungumza naye lugha ya kibiashara kila siku, nilitamani siku moja mambo yabadilike na kitu ambacho nilikuwa nataka kitawale ni mapenzi. Nilitamani sana aniite mpenzi wake na mimi nimuite jina zuri la kimapenzi, nilitamani kwa kuwa niliamini nyota yangu na yake ziliendana maana niliutumia muda wangu mwingi sana katika kumfikiria na hiyo ndiyo sababu niliyoichukulia kama imani yangu.

Zilipita siku mbili huku desturi yangu ikiwa ni ile ile asubuhi kumpeleka Samira kazini na jioni kumrudisha. Kila nilipokuwa nikimtazama kiukweli nilihisi kupata msisimko wa kimapenzi, nilihitaji kushiriki tendo na msichana ambaye nilitamani kufanya naye alikuwa ni yeye.

Tatizo lilikuwa ni sehemu moja tu! kumwambia ukweli maana tulishaanza kuwa na ukaribu ule wa kaka na dada, iliniwia vigumu sana kumueleza neno nakupenda hasa katika mazingira yale.

“Mbona kama unaonekana haupo sawa?”aliniuliza siku moja jioni nilipokuwa nimemrudisha nyumbani kwake, nilijiwekamithili ya mtu ambaye hakuwa sawa kana kwamba kuna kitu kilikuwa kikinitatiza.

“Nipo sawa,” nilimjibu.

“Hapana nakufahamu Metu unaonekana haupo sawa,” aliniambia huku akionekana kuingiwa na wasiwasi.

“Nipo sawa usijali,” nilimwambia huku nikimtoa ule wasiwasi uliyokuwa umemuingia.

“Una nini lakini?” aliniuliza kwa sauti iliyojawa na mashaka mno.

“Aaghh! acha tu usijali,” niling’aka kisha nikamwambia.

“Niache wakati haupo?” aliniuliza.

“Samira usijali kuhusu mimi,” nilimjibu.

“No, siwezi embu niambie ni kitu gani kinachokusumbua Metu au kuna mtu umegombana naye?”

“Hapana.”

“Hapana nini sasa?”

“Nitakuambia siku nyingine.”

“Siku gani hiyo halafu hii ni mara ya pili unaniambia hivi kwani kuna kitu gani unanificha?”

“Samira sidhani hata kama nikikuambia utaweza kunielewa.”

“Una maanisha nini?”

“Nina shida kubwa sana na ninahitaji msaada wa haraka iwezekanavyo.”

“Shida gani hiyo?”

“Najua huwezi kunisaidia.”

“Niambie huwezi kujua labda nitakusaidia.”

“Hapana acha niondoke tutaongea siku nyingine.”

“No, Metu naomba usiondoke mpaka uniambie.”

“Kwanza muda huu umechoka nenda kajiandae upumzike halafu baadae tutachat, nitakuambia usijali.”

“Kweli?”

“Niamini mimi,” nilimwambia kisha nikageuza pikipiki yangu nikamuaga na kuondoka eneo lile.

Nilifahamu nilimuacha kichwani na maswali lukuki, alitamani kufahamu ni kitu gani kilichokuwa kinanisumbua, sauti yake ya huruma ikanifanya niamini lengo langu lilikuwa linaenda kufanikiwa na siku hiyo nilipanga uwe mwanzo wa kutupia gia zangu za kumpata kimapenzi.

Siku hiyo nilifanya kazi mpaka muda wa saa tano za usiku, nilipitia katika moja ya mgahawa niliyouzoea, nikala nilipomaliza nilirudi ghetto. Nilipofika nikaenda kuoga na baada ya kumaliza nikajilaza kitandani, muda huo Samira alikuwa tayari amenitumia ujumbe mfupi.

“Naweza kukupigia Metu?” alinitumia.

“Ndiyo kama hutojali,” nilimjibu kisha akaweza kunipigia, nikapokea.

“Hallo Metu vipi uko salama?” aliniuliza.

“Ndiyo,” nilimjibu.

“Una uhakika?” aliniuliza tena kwa sauti iliyokuwa na utulivu wa hali ya juu.

“Ndiyo kwani vipi?” nilimjibu kisha nikamuuliza.

“Hapana unajua leo jioni nilikuona haupo sawa ndiyo maana nimekuuliza hivyo,” aliniambia.

“Samira,” nilimuita.

“Abee,” akaitika.

“Upo na nani hapo?”

“Niko peke yangu kwanini umeniuliza hivyo?”

“Hapana nahisi hiki ninachokwenda kukueleza nitakuvunjia heshima ila utanisamehe,” nilimwambia kisha nikavuta pumzi ndefu na kuziachia.

“Wewe niambie usiogope lolote,” aliniambia.

“Samira,” nilimuita tena kisha nikanyamaza kwa muda.

“Abee Metu niambie basi,” aliniambia, wakati huo nilikuwa nikijipanga kumwambia yale yaliyokuwa yananisibu moyoni na sababu kubwa alikuwa ni yeye.

“Najitahidi kukaa nacho moyoni, nisikiseme lakini kuna muda nashindwa, nahisi nahitajika kukisema ila nitakisemea wapi wakati mazingira sio rafiki na licha ya mazingira muhusika mwenyewe anaonekana kutokuwa sawa na mimi,” nilimwambia maneno ya kuuzunguka mmbuyu.

“Sasa unavyoendelea kuzunguka na kunifumba unadhani nitafahamu ni nini kinachokusumbua?” aliniuliza.

“Samira wewe ni mtu mzima najua una akili ya kufikiria baya na zuri. Sitaki kuamini kuwa lugha ya Kiswahili imekutupa mkono na wenda asili yako ni ya Ughaibuni. Sitaki kuamini hilo kabisa,” nilimwambia huku nikiamini bado hajang’amua lolote nililokuwa namaanisha.

“Metusela hutaki kuniambia au?” aliniuliza kwa sautiya kukata tamaa, alitamani kusikia kile kilichokuwa kikinisumbua lakini kwa muda ule ni kama vile nilikuwa namficha.

“Samira nimetokea kukupenda halafu hata sielewi hisia hizi zimetokea wapi yani nashindwa kuelezea,” nilimwambia huku nikiwa nimejikaza mwili mzima, nilihisi baada ya kumwambia maneno hayo labda angeweza kunitukana nikajipanga kuyakoga matusi kisawasawa.

Nilimsikia akivuta pumzi ndefu na kuziachia, akabaki kuwa kimya cha muda wa sekunde kadhaa, nikahisi labda atakuwa amekata simu, nikaitazama bado alikuwa hewani.

“Samira,” nilimuita.

“Niambie.”

“Mbona umekaa kimya tena huongei?”

“Hapana Metu hivi nikuulize kitu.”

“Yeah! niulize.”

“Hivi umefikiria nini mpaka ukaniambia hivyo.”

“Hakuna nilichokifikiria zaidi ya mapenzi ya dhati niliyokuwa nayo kwako, nimejikuta nikitamani kuwa na wewe, uwe mwanamke wangu wa maisha na nitakupenda siku zote za uhai wa maisha yangu.”

“Metusela.”

“Naam!”

“Sidhani kama itawezekana.”

“Kwanini?”

“Mimi na wewe ni kama dada na kaka halafu isitoshe nina mpenzi wangu japo siishi naye lakini nampenda sitaki kumuumiza.”

“Nahisi nimekukosea nisamehe sana.”

“Usijali Metusela nafahamu kila kitu kuhusu mapenzi, naelewa jinsi hisia zinavyomuingia mtu kwa haraka. Wala hujanikosea, najua ni hisia zimekutuma uniambie hivyo, unastahili kuniambia lolote ila kwa wakati huu umechelewa mimi nina mpenzi wangu tayari.”

“Mpenzi wako ni yupi?”

“Mbona umeniuliza hivyo au unataka kumfahamu?”

“Ndiyo lakini kama itawezekana maana tangu nilipokufahamu sijawahi kukuona ukiwa na mwanaume labda wa kuniambia kila siku mdomoni.”

“Kwa sasa hayupo nchini amesafiri yupo Marekani kikazi.”

“Anafanya kazi gani?”

“Mbona unataka umfahamu sana wewe elewa kuwa yupo kikazi.”

“Sawa nimekuelewa Samira basi acha nilale, nahisi sipo sawa kabisa.”

“Una nini?”

“Nahisi homa halafu natetemeka.”

“Umemeza dawa?”

“Hapana.’

“Kwanini?”

“Sijanunua mpaka kesho Mungu akipenda.”

“Metu ujue unahatari wewe yani unaumwa halafu hununui dawa kweli?”

“Ningefanya nini wakati Muda wote niliutumia kwa ajili yako.”

“Kwa ajili yangu?”

“Ndiyo ila usijali nitakuwa sawa, acha nilale pia nikutakie usiku mwema,” nilimwambia kisha nikakata simu.

Licha ya maumivu niliyoyapata ghafla! baada ya Samira kuniambia alikuwa na mpenzi wake ambaye alikuwa nchini Marekani lakini sikutaka kuamini kama kweli nilimkosa, niliona kushindwa kumfuata kesho yake kwa ajili ya kumpeleka kazini kama ilivyokuwa kawaida yangu, niliutumia uongo wa kuumwa homa ili siku inayofuata nisiende kumchukua. Niliona haya kukutana naye.

Nikamkumbuka Sesilia ambaye ni siku chache zilipita tangu nilipomtukana na kumpa maumivu makali ya mapenzi, nilimkosea sana na kwa kitendo kile kilichokuwa kimenitokea cha kushindwa kumpata Samira nikaanza kumkumbuka.

Akili ikaniambia nichukue simu kisha nimuandikie ujumbe mfupi wa kumuomba msamaha lakini nilishindwa kufanya hivyo. Ni kama vile kulikuwa kuna nafsi inakuja na kuniambia ‘aliyepita amepita mtazame mwingine.’ Nikaghairi na sikutaka kuishika simu tena nikaamua kulala.

   ****

Niliamka asubuhi ya siku nyingine, nikakutana na ujumbe wa Samira aliyoniandikia kuwa siku hiyo nipumzike, nisiende kumchukua kutokana na kuumwa kwangu, hakuacha kunikumbusha katika ujumbe huohuo aliyonitumia kuwa nisisahau kwenda hospitali kupima kujua ni nini kilichokuwa kikinisumbua. Nilitabasamu baada ya kuusoma ujumbe wake aliyoumalizia na maneno ASUBUHI NJEMA.

Nilishindwa kuelewa kulikuwa kuna kitu gani kilichokuwa kikiendelea, ghafla! Samira alitokea kuwa mtu wa kunijali sana kitendo ambacho sikukitegemea kabisa.

“Unatumia usafiri gani?” nilimtumia ujumbe wa kumuuliza.

“Nitachukua bajaji usijali.”

“Leo unapanda bajaji?”

“Ndiyo sina jinsi itabidi nipande, sitaki nikusumbue Metu unaumwa.”

“Lakini sijazidiwa.”

“Hata kama lakini inabidi upumzike Metu.”

“Sawa.”

“Jioni nikirudi nitakuja kukusalimia ili nijue kama kweli umeenda hospitali na dawa unionyeshe.”

“Sawa karibu,” nilimjibu.

Sikutaka kuumiza kichwa juu ya vipimo na dawa za kumzugia Samira, nilichoamua kukifanya nilimpigia simu rafiki yangu ambaye alikuwa ni daktari, nilimueleza shida yangu na aliahidi kunisaidia.

Nilipomaliza kuweka mambo sawa nilienda kufanya kazi yangu ya bodaboda huku nikiwa makini kutazama muda ambao Samira alikuwa akitoka kazini.

Ilipofika majira ya saa tisa nilirudi nyumbani kwangu, sikupika wala kuandaa chochote zaidi ya kufikiria jinsi ya kumdanganya pindi atakapokuja kuniona. Nikajilaza kitandani.

Baada ya kupita lisaa limoja ghafla! nilisikia mtu akibisha hodi, nilitabasamu baada ya kuisikia sauti ya Samira.

“Karibu,” nilisema kisha nikaenda kufungua mlango.

ITAENDELEA

Sikuachi Baby Sehemu ya Tatu

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment