Balaa Sehemu ya Tatu
KIJASUSI

Ep 03: Balaa

SIMULIZI Balaa
Balaa Sehemu ya Tatu

IMEANDIKWA NA: HALFANI SUDY

*********************************************************************************

Simulizi: Balaa

Sehemu Ya Tatu (3)

‘Auae kwa upanga siku zote huuwawa kwa upanga’ Iko hivyo, na wahenga walishasema zamani sana. Sita wa Six killers alikufa aina ya kifo sawa na aliyokufa yule askari. Na watu wengine wengi waliouwawa na kiti kile cha kifo! Sasa Dokta Yusha alikuwa huru tena lakini katika jumba hatari sana. Jumba ambalo hakuwa anajua linalindwa na walinzi wangapi, jumba ambalo hakujua ni aina gani ya ulinzi wanaoutimia. Ni mbwa ama binadamu? ‘Bora nife kwa bastola, bora nife kishujaa, kuliko kufa kwa njaa!” Dokta Yusha aliiokota ile bunduki iliyokuwa inatumiwa na Sita, SMG ambayo dokta Yusha alikuwa anajua kuitumia. Alifunzwa Kiwira Mbeya, katika Chuo cha Magereza, na alishawahi kuitumia mara kadhaa huko Mtwara, alikoajiriwa. Dokta Yusha alipiga hatua za taratibu kuelekea nje ya chumba kile. Chumba alichoambiwa ndio kaburi lake. Kwa maana hiyo Dokta Yusha sasa alikuwa anatoka katika kaburi lake! Nje kulikuwa na giza, ingawa si kubwa sana kama la mle ndani. Nje angalau kulikuwa na mbalamwezi, mbalamwezi ambayo ilimuwezesha kuona Dokta Yusha. Kwa mwendo wa kunyata Dokta Yusha alikuwa anatambaa na ukuta wa kile chumba

kuelekea upande wa mashariki, upande ambao lilikuwepo geti kubwa jeusi la nyumba ile. Aliishika imara ile bunduki iliyomdondoka Sita, tayari kupiga endapo atasikia ukelele wowote ule utakaotokea mbele yake. Dokta Yusha alikuwa tayari kwa lolote. Tayari kuuwa! Tayari kuuwawa! Aliambaa na ule ukuta wa bluu hadi akaumaliza, sasa ilimbidi apite sehemu ya wazi ili kulifikia geti. Sehemu hatari zaidi, sehemu ambayo ni rahisi sana kudunguliwa na risasi! Maana hakukuwa na kizuizi chochote. Alikwenda kwa haraka, kwa kusaidiwa na giza, au tunaweza sema kwa kudra za Mwenyezi Mungu, alilifikia geti. Dokta Yusha aliangalia pembeni ya geti, alimwona mlinzi, mlinzi ambaye alikuwa amelala huku akitoa sauti mbaya ya kukoroma. Mlinzi mzembe sana akiyelinda nyumba hatari sana! Dokta Yusha alimsogelea yule mlinzi taratibu akijua kwa vyovyote funguo ya geti atakuwa nayo yeye. Alimfikia. Kwa kutumia mkono wake wa kulia alimpiga karate moja ya nguvu katika chembe, mlinzi hakuweza kustahamili uzito wa karate ile, alikufa usingizini. Alimpekua haraka haraka yule mlinzi, alikipata alichokitaka…funguo. Dokta Yusha sasa alikuwa anafungua geti la kutoka nje ya nyumba ile hatari, nyumba ambayo hakuna mateka aliyewahi kutoka hai baada ya kuingia mle. Dokta yusha alifungua geti na kutokomea msituni akiwa na bunduki yake. Wakati Dokta Yusha, akitoroka kule kambini msituni. Kundi la Six killers walikuwa njiani wakirejea kambini kwao. Walikuwa wanatoka Kilwa Masoko mjini, walikoenda kufanya starehe zao. Wote walikuwa wamelewa ndani ya gari huku wanaimba nyimbo zisizoeleweka. Walikuwa na furaha sana baada ya kuona mipango yao inaenda kama ilivyopangwa, pia waliweza kumkamata mtu ambaye alikuwa anawasumbua sana, Dokta Yusha. ‘Laiti wangejua’ * Katika hospitali ya wilaya Kilwa Kivinje hali ya wagonjwa ilikuwa mbaya sana. Kulikuwa hakuna huduma kabisa kwa wagonjwa wa hospitali hiyo. Madaktari waliokuwa wanaaminiwa sana kwa kutoa huduma nzuri sasa walikuwa wamebadirika. Walidharau sana wagonjwa, hawakuwajari kabisa. Malalamiko mengi yalipelekwa katika uongozi wa wilaya, lakini malalamiko hayo hayakubadirisha kitu. Madaktari hawa sasa walikuwa na pesa nyingi sana, pesa za kumuhonga mtu yeyote yule atakayeonesha kutaka kuwaingilia au kukwamisha mipango yao. Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa alikuwa kimya, mkuu wa wilaya ya Kilwa alikuwa kimya, na mbunge pia alikuwa kimya, ingawa walipelekewa malalamiko mara kwa mara huku hali za wagonjwa waliolazwa hospitali zikiendelea kuwa mbaya! Upande wa hali za Nasra, Hasina nazo zilikuwa taabani. Nasra alikuwa anapumulia mashine katika hospitali ile iliyokuwa na huduma dhaifu sana kwa sasa, Nasra alikuwa amehamishwa wodi na kupelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi, ICU, hali yake ilikuwa mbaya sana. Huku Hasina na Mzee Mpaukha wakiwa bado wanapigania maisha katika wodi ileile aliowaacha Dokta Yusha. Mwili wa marehemu dereva Musa ulikuwa ushatolewa katika ile wodi na kupelekwa machinjioni. Katika chumba cha kuhifadhia maiti ambako ndipo kundi la Six killers walikuwa wanafanyia shughuli zao.

Kutoonekana kwa Dokta Yusha siku nzima, ilizua hofu kwa ndugu zake. Dokta Yusha alitafutwa ule usiku lakini hakupatikana, na kwa bahati mbaya zaidi alikuwa hapatikani kwa simu yake pia. Hali ilikuwa ngumu sana kwa familia zote mbili. Familia ya Mzee Mpaukha na familia ya Mzee Yusuph, baba yake na Dokta Yusha. Dokta Yusha alikuwa anahitajika sana wakati ule, pengine kuliko wakati wowote ule, alikuwa mtu muhimu sana, licha ya kutaka kujua usalama wake mwenyewe, lakini pia alihitajika sana kuwahudumia wagonjwa wa pale hospitali, hasa kumuhudumia mkewe Nasra na rafiki wa mkewe Hasina, ambao walikuwa na hali mbaya kupita kiasi. Ndugu walitafuta sana. Lakini hawakumuona! * Usiku huo Kundi la Six Killers nd’o walikuwa wanarudi kambini kwao, huko porini Ngome. Walishuka katika gari yao huku wakiwa na furaha kubwa sana. Furaha iliyotokana na pombe, furaha iliyotokana na mipango yao kwenda sawa. Taa za gari yao zilipomulika geti wote walipigwa na butwaa! Geti lao lilikuwa wazi, waliingia ndani moja kwa moja bila kusemeshana, walienda katika chumba cha mateka wao. Walimsahau hata kumwangalia mlinzi pale mlangoni. Mateka wao hakuwepo! Wakajaribu kumpigia simu Sita. Cha kushangaza hata Sita waliyemuacha kwa ajili ya kumlinda Dokta Yusha nae hakuwa anapatikana. Walirudi tena getini, ndipo walimkuta mlinzi akiwa amelala, walipomgusa ili kumuamsha, mlinzi alidondoka chini moja kwa moja. Macho yaliwatoka vibaya sana! Hakika Dokta Yusha alikuwa kawaweza sana, ilikuwa haijawahi tokea hata siku moja kutoka mtu salama katika nyumba ile. Ilikuwa ni mwiko, ilikuwa ni dhambi kubwa sana kwao kutoka mtu katika nyumba ile akiwa hai! Ile nyumba ilikuwa ni zaidi ya kaburi, kile kiti kilikuwa ni mithili ya Israel mtoa roho. Nyumba ile ilikuwa imeondoka na roho za watu wengi sana. Roho za watu mbalimbali wasio na hatia, roho za askari wengi, roho za wapelelezi wengi, roho za viongozi wengi na roho za watu wa kawaida zisizo na hesabu. Kile kiti kilikuwa kimewageuza rangi watu wengi sana. Kutoka rangi yao ya asili,

kuwapeleka rangi nyekundu kisha nyeusi tii, kisha kutoa harufu kali sana. Kile kiti hakikuwahi kukosea katu. “Natoa nusu saa, Dokta Yusha awe mbele yangu hapa, hapana siyo Dokta Yusha, natoa nusu saa maiti ya Dokta Yusha iwe mbele yangu hapa. Maana akija mzima hapa nitamfanya kitu kibaya sana, naona bora mniletee maiti tu inatosha” Don Genge aliunguruma kwa hasira. Dokta Yusha sasa aligeuka mwiba. mwiba mkali sana! Vijana wa Six Killers, ambao sasa walibaki wanne tu. Maana Tano alikuwa anauguza goti lake, na Sita alikuwa hajulikani alipo mpaka sasa waliingia kazini. Moyo wa Don Genge ulikuwa unafukuta moto, alikuwa na hasira isiyomithilika katika moyo wake. Ni kweli, Dokta Yusha angepelekwa hai pale, ingekuwa balaa! Walipotoka nje kundi la Six killers walijigawa. Wakati Moja na Nne wakielekea upande wa mashariki wa pori lile, Moja na Tatu walielekea upande wa magharibi. Kumsaka Dokta Yusha. Ilikuwa ni msake mpaka umpate! Wakati kundi la Six killers likijigawa namna hiyo kumsaka Dokta Yusha kwa kwenda upande wa mashariki na magharibi. Dokta Yusha alikuwa mbali kidogo na ile kambi ya wale makatili. Ilikuwa ni porini sana, Dokta Yusha alikuwa anasonga mbele akiwa hajui anaelekea wapi. Hadi sasa alikuwa hajui msitu ule upo sehemu gani nchini Tanzania. Alikuwa anaenda mbele tu ili kukiepuka kifo. Na bunduki yake mikononi. Saa kumi na mbili asubuhi ilimkuta Dokta Yusha akiwa katika ufukwe mwanana wa bahari ya hindi. Ulikuwa ufukwe mpya ambao hakuwahi kufika wala kuuona hapo kabla. Moja na Nne, waliokuwa wanaenda upande wa mashariki, upande sahihi alioelekea Dokta Yusha. Huu upande kulikuwa na ufukwe wa bahari ya hindi ambao watu wengi ndani ya Kilwa walikuwa hawaufahamu. Moja na Nne nao walifika katika ule ufukwe. Ingawa ilikuwa mbali na pale alipotokea Dokta Yusha. Jamaa wakaanza kutembea ufukweni kumsaka Dokta Yusha. Dokta Yusha alikuwa amechoka sana, alikuwa anatembea taratibu ufukweni huku akiangalia nyuma mara kwa mara. Ufukwe ulikuwa mrefu sana, kiasi kwamba ni ngumu kumuona mtu aliye mbele yake. Kundi la Six killers walipewa nusu saa kupeleka maiti ya Dokta Yusha. Na sasa ni masaa mawili hawakuwa na maiti ya Dokta Yusha wala harufu ya Dokta Yusha. Mara kwa mara Don Genge alikuwa anawapigia simu vijana wake, lakini jibu lilikuwa lilelile, hawakuwa wamemuona Dokta Yusha. Mwishowe Don Genge aliwaambia vijana warudi kambini, ili waende kujipanga upya. Hiyo ndio ilikuwa nusra ya Dokta Yusha kukamatwa kule ufukweni mwa bahari. Dokta Yusha aliendelea kuufata ule ufukwe. Bila kujua ufukwe ule utamfikisha wapi? Lakini aliufata. Kambini kundi la Six killers walikutana. Kilikuwa ni kikao tofauti na vikao vyote walivyowahi kufanya. Kikao hiki kilitawaliwa na hasira, hofu na chuki! Wote walikuwa na hasira kali kwenda kwa Dokta Yusha. Wote walikuwa na hofu ya kukamatwa na Polisi, maana yake walikuwa wanaamini Dokta Yusha alishaijua mahali ilipokuwa kambi yao, wote walikuwa na chuki, walikuwa wanamchukia sana Dokta Yusha. Ni yeye ndiye aliyeingilia kati mipango yao ambayo ingewawezesha kupata hela nyingi sana. Hela ambazo zingewawezesha kuwa matajiri milele. “Mambo yamebadilika haraka sana, sisi tulipanga hivi lakini mambo yanaenda vile. Sasa tumefikia katika hali mbaya sana, mipango yetu inaenda mrama, ndio…mipango yetu inaenda songombingo. Kidudu kidogo sana kinawasumbua. Kumbukeni nyinyi ni nusu makomando, mnashindwaje kumkamata mtu ambaye hajapita kozi yoyote. Tano na Sita nimewapoteza ilhali yule nyang’au hana hata jeraha letu. Yaani Tano anapambana na kale jamaa na kukishindwa, hizo ni dharau, dharau kubwa sana, dharau zisizo na mfano. Natoa oda mpya sasa, ukimuona Dokta Yusha popote pale muue kwanza kisha nd’o umhoji. Hatutakiwi kufanya mchezo kabisa! Kumtafuta Dokta Yusha kwende sambamba na kutoa mioyo kule hospitali. Leo usiku tumepanga na Dokta Sharifa tuwatoe mioyo wale majamaa zake, ili imuumize, tukimuuwa mkewe na kumtoa moyo lazima atajitokeza, hapo ndipo tutamuuwa kirahisi” Don Genge alitoa hotuba ndefu huku kila mtu akikubali kwa kutingisha kichwa. Kwa hakika, Kundi hatari la Six killers walikuwa wanataka kupiga pigo la mwisho! Baada ya maelezo hayo kila mmoja aliingia ndani kupumzika. Six killers walikuwa wamechoka sana. Wote pombe zilikuwa zimewaisha vichwani mwao. Ama hakika Six killers walikuwa wamepatikana, na kupata pigo kubwa sana, baada ya wapiganaji wao wawili kukutana na mkono wa Dokta Yusha! Wakati vijana wanne wa Six killers wakiwa wameenda kupumzika, Don Genge yeye hakwenda kupumzika kabisa. Yeye ndiye alikuwa mkuu wa misheni hii. Na ilimpasa kupeleka ripoti kwa wakuu wake, na sio ripoti tu, wakuu walikuwa wanataka ripoti nzuri ya kueleweka toka kwa Don Genge. Don Genge atapumzika vipi wakati hakuwa na ripoti ya kueleweka hadi sasa?
Don Genge yeye hakwenda kupumzika kabisa. Yeye ndiye alikuwa mkuu wa misheni hii. Na ilimpasa kupeleka ripoti kwa wakuu wake, na sio ripoti tu, wakuu walikuwa wanataka ripoti nzuri ya kueleweka toka kwa Don Genge. Don Genge atapumzika vipi wakati hakuwa na ripoti ya kueleweka hadi sasa? Pamoja na kupata idadi ya mioyo waliyoagizwa lakini Tano alikuwa mgonjwa, Sita alikuwa kapotea, adui yao namba moja duniani, Dokta Yusha alifanikiwa kuwatoroka. Ni ripoti mbaya zaidi tangu Don Genge apewe kazi hii. Hakika hakupaswa kupumzika, na hakupumzika kweli. Don Genge alienda sebuleni, aliwasha kompyuta yake na kuanza kuikagua, kila kitu kilikuwa sawa. Alifungua kabati kubwa lililopo pale sebuleni, namo kila kitu kilikuwa sawa. Don Genge akajua kwamba Dokta Yusha hakuwa ameingia mle ndani. Alirudi kwenye sofa kubwa lililopo pale sebuleni, alikaa kwa mtindo wa kujitupia sofani. Alianza kuwaza mustakabali wa kisanga kile kilichokuwa kinawaendesha mrama sasa.
Dokta Yusha aliendelea kuufuata ule ufukwe, cha ajabu ule ufukwe uliomfikisha katika kijiji cha Mpara, kijiji ambacho kipo ndani ya Kilwa Masoko. Alipofika hapo kijijini ndipo aligundua kumbe bado yupo ndani ya Kilwa. Porini Mpara Dokta Yusha alichimba shimo refu na kuifukia ile bunduki, huku akiweka alama kwa juu asiisahau sehemu ile. Alivyomaliza akaendelea kutembea na pori. Hakutaka kabisa kupita barabarani akiuhofia usalama wake. Lakini alitoka kule porini na kuikaribia vipori vidogo vilivyokuwa karibu na barabara kuu ya lami. Alivyogundua kama yupo Mpara, nia na madhumuni yake ni kwenda hospitali ya Kilwa Kivinje kwa miguu! Ilikuwa ni safari ngumu lakini na ndefu lakini ilikuwa ni lazima aende Kilwa Kivinje, alihisi hatari kubwa sana kumuacha mke wake na ndugu zake wengine katika hospitali ya wilaya Kilwa. Dokta Yusha alitembea kwa miguu, ilikuwa safari ngumu sana, lakini hakukuwa na namna nyingine. Ilikuwa ni lazima atembee. Alipofika hospitali ya Kivinje breki yake ya kwanza ilikuwa ni wodi aliyowaacha wakina Nasra. Alipofika mlangoni tu na kuangalia katika kitanda alipokuwa amelazwa mkewe, Nasra. Alipingwa na butwaa! Kitanda cha Nasra kilikuwa tupu. Hakukuwa na mtu. Akiwa kasimama palepale mlangoni chozi la uchungu liligusa sakafu ya hospitali. Dokta Yusha alikuwa analia. Kutumuona Nasra pale kitandani alijua kuna mawili, kama mkewe kipenzi hajafariki na kuhamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti basi kundi lile la wanaharamu itakuwa wamemteka. Lakini Dokta Yusha yote hayo mawili hakutaka kabisa yatokee. Alikuwa anampenda sana Nasra, na alikuwa anatamani sana kumuona Nasra anakuwa na siha njema kama zamani. Dokta Yusha alipiga hatua za taratibu kuingia ndani ya hospitali, huku akifuta machozi kwa kutumia kiganja chake, alikipita kitanda cha mkewe, Nasra akiwa anakiangalia sana, alifika katika kitanda alicholala Hasina, alipofika tu pale kitandani kilitokea kitu cha ajabu sana! Hasina alifungua macho! Dokta Yusha hakuamini alichokuwa anakitazama, ulikuwa ni ukweli ambao hakukubaliana nao. “Umeamka Hasina, niambie mke wangu Nasra yuko wapi, naomba uniambie hata kama wamemchukua wale washenzi, wewe nambie tu” Dokta Yusha alikuwa anaongea na Hasina lakini ilikuwa ni kama anaongea na sanamu, Hasina alimwangalia tu, bila kusema chochote. Maneno yale ya Dokta Yusha yalimuamsha Mzee Mpaukha toka usingizini. Naye alishangaa sana kumuona Dokta Yusha pale. Kwa sauti dhaifu aliongea. “Ulikuwa wapi Dokta, umeacha watu wanateseka sana hapa, hii sio hospitali kabisa, hapa ni wakala wa kifo!” Dokta Yusha alimwacha Hasina, alisogea taratibu kuelekea katika kitanda alicholala Mzee Mpaukha huku akiyasikiliza kwa umakini sana maneno akiyoyaongea Mzee yule. Yalimuingia kabisa akilini. “Nimekuelewa mzee wangu” Dokta Yusha aliongea kwa huzuni alipofika pale kitandani. Huku akijificha ili asijulikane kama alikuwa analia. “Katafute gari sasahivi Dokta, katafute gari kama unatujari, utuhamishe katika hospitali hii” “Nasra yupo wapi baba?” Aliuliza. “Nasra yupo ICU” “Tutaondoka vipi sasa baba na mke wangu yupo ICU?” “Ni kwa kudra ya Mwenyezi Mungu, hata huko ICU unafikiri anapewa huduma gani, amelazwa tu kama alivyolazwa hapa! Tuhamishe Dokta hii siyo hospitali!” Don Genge alikaa pale sofani muda mrefu kidogo. Baada ya kutafakari sana akapata wazo kichwani kwake, na akalifanyia kazi wazo lake muda huohuo. Aliitoa simu yake katika mfuko wa suruali yake, akatafuta namba fulani na kuzipiga. “Hallo Dokta Zaidi Kilumba” “Nambie Don wa madon” “Huyu jamaa katoroka huku, lakini kwa vyovyote vile lazima aje hospitali kuviangalia hivyo vikaragosi vyake, weka mtu makini wodini atuambie pindi tu atakapotia mguu wake hapo hospitali” “Sawa Don, natekeleza hilo sasahivi” Kwa bahati nzuri mtu aliyewekwa na Zaidi Kilumba alifika pale wodini wakati Dokta Yusha akiwa ameenda kutafuta gari kwa ajili ya kuwapakia wagonjwa wake na kuwatoa katika hospitali ile, iliyogeuka kuwa hatari sana sasa, au wakala wa kifo kama alivyoiita Mzee Mpaukha. Baada ya nusu saa Dokta Yusha alirejea, akiwa na gari aina ya Costa kwa ajili ya kuwapakia wagonjwa wake. Dokta Yusha alishuka garini, kwa mwendo wa kasi alielekea wodini. Alitembea kwa kasi kwa kuwa alijua hatari ya kukaa pale hospitali kwa muda mrefu. Uharaka wake lakini haukupunguza umakini wake, Dokta Yusha alikuwa makini pia. Alikuwa anamwangalia kila mtu , ili angalau ajue kama hatari ikiwa inamkaribia. Ghafla! Akiwa njiani Dokta Yusha alishikwa bega na mtu. Alistuka sana. Aligeuka kwa kasi na tahadhari kubwa sana. Tayari kwa lolote. Alikuwa Mwanasheria mlevi. “Mbona faster Dokta” Mwanasheria aliuliza. “Nataka nihamishe wagonjwa wangu Mwanasheria” “Nimetoroka Polisi kuja kukwambia hiko kitu kaka” “Umetoroka Polisi?” “Hatuna muda wa kuongea hapa, wewe ni hatari zaidi kuonekana hapa, rudi garini nakuletea wagonjwa wako wote garini” “Unajua Nasra alipo Mwanasheria, basi twende wote” “Rudi garini!” Mwanasheria mlevi alisema kwa hasira. Hakuongeza neno, aliondoka kuelekea wodini, akimwacha Dokta Yusha amehemewa. Hakuwa na jinsi, alirejea kwenye gari huku akishangaa akili za Mwanasheria mlevi. Sasa Dokta Yusha alianza kumhusudu Mwanasheria mlevi. Alianza kumwamini yule mlevi akiyemdharau sana kabla ya kisanga hiki. Mwanasheria mlevi aliingia wodini akiwa anaangaliwa na yule kijana, mlinzi aliyewekwa na kina Don Genge. Moja kwa moja alienda katika kitanda cha Mzee Mpaukha. Aliteta nae kidogo kisha akatoka nje. Mwanasheria mlevi alienda nyuma ya wodi ile, sehemu ambako kulikuwa na choo pia. “Mamaaa nakufaaaaaaa!” Mwanasheria mlevi alipiga makelele yasiyo na mfano kule nyuma ya wodi. Watu walichanganyikiwa. Na baadhi ya watu walikimbilia kule nyuma. Yule kijana aliyewekwa na Dokta Kilumba nae alivutwa na ukelele wa Mwanasheria. Naye alielekea kule nyuma ya wodi. Wakati yule kijana akikimbilia kwa kupita upande wa mashariki kuelekea nyuma ya wodi, Mwanasheria mlevi alipita upande wa magharibi kurudi mbele ya wodi. Yule kijana umbea ulimponza, watu wengi waliendelea kukusanyika kule nyuma ya wodi bila kuelewa kilitokea nini. Mwanasheria mlevi aliingia wodini harakaharaka, kwa kushirikiana na mzee Mpaukha wakamweka Hasina katika kiti chenye magurudumu manne, na kuanza kuondoka nae kwa kasi kuelekea garini, Mwanasheria mlevi ndiye aliyekuwa akisukuma kiti kile huku akifuatwa kwa nyuma na Mzee Mpaukha, aliyekuwa akifuata kwa mwendo wa taratibu. Walifika ilikopaki ile gari, kwa kushirikiana na Dokta Yusha walimuingiza Hasina garini. Mwanasheria mlevi alishuka katika gari harakaharaka ili akamchukue na Nasra, mkewe Dokta Yusha. “Unaenda wapi tena Mwanasheria?” “Kumchukua Nasra” “Nishamchukua tayari, ingia kwenye gari tuondoke” “Safi sana comrade” Mwanasheria mlevi alisema huku akimwangalia Nasra aliyekuwa amelala katika siti ndefu za nyuma ya ile gari. Safari ya kukimbia katika hospitali ile ya wilaya, ambayo sasa ilikuwa ni sawa na wakala wa kifo wa wilaya ilianza. Kule nyuma ya wodi watu walitafuta sana bila kumuona mtu aliyepiga kelele. Hawakuona kitu, watu walianza kuondoka kidogokidogo, huku wakionesha kukereka kwa kiasi kikubwa, na yule kijana nae alirejea katika lindo lake.

Kule nyuma ya wodi watu walitafuta sana bila kumuona mtu aliyepiga kelele. Hawakuona kitu, watu walianza kuondoka kidogokidogo, huku wakionesha kukereka kwa kiasi kikubwa, na yule kijana nae alirejea katika lindo lake. Alikaa palepale kwenye kiti akimsubiri Dokta Yusha afike pale, ili awape taarifa mabosi wake waliomtuma. Laiti angejuaaaaa… Alikuwa amechelewa sana. Hakujua kwamba Mwanasheria mlevi alimuona pale muda mwingi sana, na alimtilia shaka yule kijana pale kitini. Ndio akaamua kuucheza ule mchezo wa makelele. Mchezo uliomuokoa awali Dokta Yusha bila kujua kipindi anaelekea katika chumba cha kuhifadhia maiti alipokuwa amejificha Tano, na sasa mchezo uleule wa makelele unaookoa watu wengi zaidi lakini safari hii ukichezwa kwa kukusudia Don Genge alibaki masikio wazi kusubiri taarifa katika simu yake. Lakini simu haikupigwa. Baada ya kukaa kwa muda mrefu kidogo, Don Genge alinyanyuka pale sofani na kwenda katika chumba wanacholala Six killers, aliwaamsha kwa upole na kuanza kuongea. “Six Killers, mmelala vya kutosha vijana, nina maana yangu kuwaruhusu mje kulala wakati kama ambao hamkupaswa kulala kabisa. Kuanzia sasa hamtalala tena, mpaka mtakapomleta Dokta Yusha hapa! Kule wodini kuna kijana tumemweka endapo kama Dokta Yusha atawasili atujulishe kupitia kwa Dokta Kilumba. Lakini hadi sasa hakuna taarifa yoyote. Inamaana yule mwanaharamu hajafika pale hospitali. Sasa wote mnaenda wodini kumchukua yule mzee na yule dada na mtaenda kule ICU kumchukua yule mfu. Leo ndio siku yao ya kufa!. Vifo vibaya sana, ambavyo havijawahi kushuhudiwa na Dunia hii. Hakikisheni hamfanyi kosa lolote vijana ” “Sawa Bosi” Six Killers waliitikia kwa pamoja. Wakaondoka. Safari ya kuelekea hospitali Kilwa Kivinje ilianza. Six killers wakiwa na hasira sana na Dokta Yusha. Mtu ambaye anataka kuwakosesha usingizi. Wakati wao wanaelekea Kilwa Kivinje hospitali, Dokta Yusha akiwa na Mwanasheria mlevi na wagonjwa wao walikuwa nd’o wanakipita kijiji cha Mandawa wakielekea mkoani Lindi. Nia yao ni kuwapeleka wagonjwa wao katika hospitali misheni ya ndanda, Mtwara. Six killers walienda moja kwa moja katika wodi waliolazwa Mzee Mpaukha na Hasina. Waliingia kwa mbwembwe kubwa sana. Lengo ni kuwabeba wale wagonjwa na kwenda kuwaua vibaya sana, na kuwatoa moyo kule katika chumba cha kuhifadhia maiti. Walikuta wodi ipo tupu!. Hakukuwa na mgonjwa yeyote pale wodini. Moja alichukua simu yake na kumpigia Don Genge kumtaarifu habari hizo mbaya kabisa, habari ambazo ni chungu kutoka katika mdomo wa Moja, zilikuwa chungu kusikiwa na sikio la Don Genge. “Bosi hakuna mtu humu wodini” Moja alisema kwa fadhaha bila hata kumsalimia Bosi wake. “Unasemaje wewe!” Don Genge aliuliza kwa ghadhabu. “Hakuna mtu Bosi hapa wodini, jamaa itakuwa katuwahi” Moja aliongea kwa utulivu sasa. “Huyo kijana aliyepewa kazi ya kulinda hapo yupo?” “Tunae hapa” “Afe yeye leo, na moyo wake utolewe, afe kifo sawa na tulichopanga kuwaua wale mbwa!” Don Genge aling’aka simuni. Yule kijana alianza kutetemeka. Muda uleule Six killers walimgeukia. Hawakuwa na mas’hara hata kidogo. Walimsukasuka kwa nguvu, safari kuelekea katika chumba cha kuhifadhia maiti ilianza. Walikuwa wanaenda kumuua yule kijana! Wahenga waliwahi sema, siku zote mshahara wa dhambi ni mauti. Kijana aliponzwa na Mwanasheria mlevi, mlevi anayetumia akili sana katika mambo yake, mlevi ambaye watu wengi walikuwa wanamdharau, bila kujua uwezo wake wa juu wa akili aliokuwa nao. Kijana aliingia katika kesi asiyoijua mwanzo wala mwisho. Hakuwekea uzito maagizo aliyopewa na Dokta Zaidi Kilumba, hakujua kama kosa lolote la aina yoyote ile lingegharimu maisha yake. Hakupewa tahadhari hiyo na Dokta Kilumba, labda angepewa hiyo tahadhari angekuwa makini zaidi. Au labda angeikataa kabisa ile kazi ya kifo. Lakini ilikuwa bahati mbaya sana kwake, hakutahadharishwa awali pia hakupewa muda wa kujitetea, ili kuelezea kitu gani kilitokea, kwanza kundi la Six killers hawakuwa na muda huo, muda wa kumhoji yule kijana dhaifu, walikuwa na haraka isiyo na kifani. Ilikuwa lazima wamtafute Dokta Yusha, ilikuwa lazima wapate mioyo kumi na tano siku hiyo. Kumbuka walibaki wanne sasa, ukiondoa wale madaktari vibaraka na manesi wafata mkumbo. Kumbuka Tano alikuwa mgonjwa, Sita alienda kusikojulikana. Walikuwa lazima wajigawe vizuri ili kufanikisha mipango yao..ilikuwa lazima wawepo wa kuhakikisha zoezi la utoaji moyo linaendelea kama kawaida, pia wawepo wa kuhakikisha zoezi ambalo lilikuwa gumu sana kwa sasa, zoezi la kumtafuta Dokta Yusha na wenzake linafanikiwa. Yule kijana asiyekuwa makini, na kuzidiwa akili na mlevi, aliuawa kwa kunyongwa shingo na Moja wa Six Killers, na kutolewa moyo kikatili na Dokta Sharifa Juma. Tatu na Nne walibaki pale hospitali, kulinda usalama wa pale, Moja na mbili ndio walienda kuwasaka wakina Dokta Yusha, kuwasaka mahala pasipojulikana. Ghafla, simu ya Don Genge iliita. Aliangalia katika kioo cha simu yake, kilisomeka….. Kifo! Don Genge alipokea ile simu huku akiwa na hofu kuu. “Hallo Bosi” Don Genge aliita simuni kwa sauti yake yenye hofu. “Nipe maendeleo ya project yetu Don Genge” “Mambo yako sawa Boss, ingawa kuna kidudu mtu katuingilia kidogo katika mipango yetu” “Ni nani huyo Don Genge? na kaiingilia vipi hiyo project?” “Anaitwa Dokta Yusha, amegundua kila kitu tunachokifanya huyo jamaa ni mjanja sana aisee” “Na na bado anaendelea kupumua mpaka sasahivi?” “Ndio Bosi anapumua, ingawa naamini anamalizia pumzi zake za mwisho” “Six killers wanasemaji?” “Wanajaribu kupambana vijana, ila bado hali haijakaa sawa mpaka sasa, mmoja ni missing in action, na mmoja ni majeruhi” “Nani aliyepata majeruhi, na nani missing in action?” “Majeruhi Tano, missing in action Sita” “Lazima ufanye kitu Don, usiache hali ikawa namna hiyo, vipi kuhusu mzigo?” “Mzigo uko wa kutosha, tutausafirisha kesho asubuhi” “Fanya hivyo Don, mzigo umepungua sana huku, na tuna oda nyingi sana” “Nitafanya hivyo” “Sawa jamaa, huyo jamaa sijui Dokta nani anastahili kifo kabla hajatoa taarifa kwa jeshi la polisi au mahala popote ambako itakuwa si salama kwetu” “Nimekuelewa Bosi, nitahakikisha tunamziba mdomo” Simu ikakatwa. Kifo, alikuwa ndio Mkurugenzi mkuu wa mradi huu kitaifa. Mradi wa kutoa mioyo ya maiti. Mioyo ambayo ilikuwa inatumika katika utengenezaji wa sumu hatari na kali zaidi duniani, Sumu ya Proxine! Sumu ambayo, ukiigusa bila ya kuwa na kizuizi chochote kinachofuata ni kifo! Kifo baada ya dakika thelathini tu. Sumu ambayo ilikuwa inatengenezwa nchini Ujerumani, lakini malighafi za kutengeneza sumu hiyo zilikuwa zinatoka Tanzania. Sumu ya Proxine, sumu hatari iliyopigwa marufuku kutumika dunia mzima lakini vikundi vya kigaidi vilikuwa vinaitumia kwa siri, na huipata kwa gharama kubwa sana. Hiyo ndio kazi ya mioyo hii ikiyochukuliwa na kundi la Six killers likiongozwa na jasusi wa najasusi Don Genge. Unaweza ukasema utoaji wa mioyo wa maiti haukuwa na madhara sana kama asemavyo Don Genge, lakini je hivyo ndivyo wanavyopaswa kufanyiwa maiti, na je matumizi ya sumu ya Proxine, yalikuwa hayadhuru watu wasio na hatia? (Kumbuka riwaya ya Angamizo) Dokta Yusha na msafara wake uliingia katika hospitali ya misheni ya Ndanda, wote wakiwa hoi kwa uchovu wa safari. Moja kwa moja walienda kwenye hospitali hiyo kubwa ya misheni. Wagonjwa walichangamkiwa walipofika nje tu ya hospitali hiyo. Manesi wenye vitoroli waliwapokea haraka haraka na kuwapeleka wodini. Kwa umakini na kasi walipewa huduma zinazojitajika. Huduma zilizomridhisha sana Dokta Yusha. Alikuwa na furaha usoni, ingawa furaha yake ilisinyaa akikumbuka madhila ya watu wale wabaya aliowaacha huko Kilwa. * Baada ya wiki moja, Mzee Mpaukha alikuwa mzima kabisa. Nasra na Hasina

waliendelea kuwa wafu kitandani. Huku Hasina akifumba na kufumbua macho yake bila ya kuongea lolote. Akiba ya pesa aliyokuwa anaweka Dokta Yusha ilimsaidia sana katika kipindi kile kigumu kilichohitaji awe na pesa za kutosha. Huko Kilwa Masoko, kundi la Six killers lilikuwa katika hali ngumu sana. Wiki nzima walimsaka Dokta Yusha bila mafanikio yoyote. Six killers walianza kuingiwa na hofu labda Dokta Yusha amefichwa sehemu fulani baada ya kwenda kutoa taarifa Polisi na muda wowote watakuja kukamatwa na mipango yao kuwa hadharani, pamoja na kuwa na fikra hizo lakini hawakusumbuliwa kabisa na Polisi. Hali iliyowaaminisha kwamba askari Polisi hawakuwa wanajua lolote. Six killers waliendelea kufanya kazi zao, lakini wakiwa na wasiwasi mkubwa sana. Dokta Yusha alikuwa ameichukua furaha yao na kwenda kuificha mahali kusikojulikana. Walijua ipo siku isiyokuwa na jina mambo yatakuwa mabaya sana kwao. Upande wa Tano wa kundi la Six killers hali yake iliendelea vizuri. Sasa alianza kufanya mazoezi madogo madogo ishara kwamba goti lake lilianza kupata nafuu. Aliendelea kutibiwa kwa siri kwenye ile nyumba yao iliyopo kule porini Ngome. Sita wa Six killers walimtafuta sana, lakini hawakuweza kupata, na wala hawakupata fununu wapi amekwenda. Hawakuwa na hisia kabisa kwamba kiti cha kifo ndiyo sababu ya kifo cha Sita. Ukweli ni kwamba, kutoweka kwa Dokta Yusha kuliongeza hofu kwa kundi la Six killers. Sasa wakawa hawafanyi kazi kwa uhuru tena kama zamani. Iliwapasa kuhamisha mahala pa kufanyia operesheni zao zile za kikatili, sasa wakawa wanaiba maiti na kwenda kuzitoa moyo huko kambini kwao, kisha kuzitelekeza porini ngome. Kubadilisha mahali pa kufanyia mauaji kukazua jambo jipya katika hospitali ya wilaya ya Kilwa, kwa maana zilikuwa zinapotea maiti kumi na tano kila jua lilipokuwa linazama. Kupotea maiti kumi na tano kila siku ndiko kukazua jambo kuu. Tanzania nzima sasa ikapata habari juu ya upotevu huo wa maiti huko Kilwa. Wananchi wa Kilwa wakawa wanaishi kwa woga na wasiwasi mkubwa sana. Hakuna aliyekuwa anajua maiti za wapendwa wao zinapotea vipi. Wananchi wenye imani dhaifu wakahusianisha matukio hayo na imani za kishirikina. Wananchi wa Kilwa walijaribu kila njia kuzuia wizi wa maiti lakini hawakufanikiwa. Upotevu huo wa maiti ukawasogeza karibu wapelelezi mbalimbali nchini Tanzania na waandishi wengi kwenda Kilwa kufatilia sakata hilo. Kazi ilikuwa ngumu sana kwa wapelelezi hao, hii kazi ya kuiba maiti ilifanywa na watu makini, tena wakishirikiana na madaktari makini pia. Wapelelezi walipeleleza kwa siri sana lakini hawakupiga hatua yoyote. Laiti wangejua wapelelezi hao wangemtafuta Dokta Yusha ama Mwanasheria mlevi, hao ndio walikuwa wanajua kila kitu juu ya sakata hili.

Laiti wangejua wapelelezi hao wangemtafuta Dokta Yusha ama Mwanasheria mlevi, hao ndio walikuwa wanajua kila kitu juu ya sakata hili. Mmoja wa waandishi wa habari aliyekuja kuchunguza sakata hii alikuwa anaitwa Gabriel Rondo. Mwandishi wa habari mahiri toka gazeti la Chokochoko. Gabriel Rondo alikuwa Mwandishi wa habari mdadisi sana, mara nyingi akifatilia jambo hufatilia kwa undani kabisa, na huja na habari yenye kumridhisha kila msomaji wa gazeti la Chokochoko. Asubuhi moja Mwandishi wa habari Gabriel Rondo ilimkuta akiwa mlangoni kwa Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya Kilwa. Nia na madhumuni ni kwenda kupata maono ya Mganga huyo wa wilaya juu ya kupotea maiti maiti kumi na tano kila siku katika hospitali yake. Gabriel Rondo alifika katika ofisi ile mnamo saa mbili asubuhi, lakini mganga mkuu Dokta Zaidi Kilumba hakuwa amefika. Dokta Kilumba aliwasili ofisini kwake saa sita mchana, akiwa ananuka harufu mbaya ya pombe. Alifika ofisini kwake na kukuta msururu wa mkubwa watu ukimsubiri yeye, Dokta Zaidi Kilumba aliwapita watu wale kwa dharau kama hakukuwa na watu pale, Dokta Zaidi Kilumba hakuwajari, hakuwasalimia wala kuwaangalia usoni watu wale. Alijiinamia chini na kuingia ofisini kwake akiambatana na harufu yake ya pombe. Watu pale nje walianza minong’ono, minong’ono iliyotoka katika midomo ya wasemaji na kutua moja kwa moja katika masikio yote mawili ya Mwandishi wa habari Gabriel Rondo. Baada ya Dokta Zaidi Kilumba kuingia ofisini kwake, wateja waliokuwa katika foleni pale nje walianza kuingia ofisini kwa Dokta Kilumba, kulingana na foleni yao. Watu waliingia ofisini mpaka zamu ya Mwandishi wa habari, Gabriel Rondo ilifika. “Naitwa Gabriel Rondo, Mwandishi wa habari wa gazeti la Chokochoko” Gabriel Rondo alijitambulisha baada ya salamu. “Naitwa Dokta Kilumba, mganga mkuu hapa” Dokta Kilumba nae alijitambulisha. “Nina masuala machache ambayo nataka ufafanuzi toka kwako Dokta” “Sawa nakusiliza Ndugu Gabriel Rondo” “Hivi ni muda gani sahihi kwa mtumishi kufika kazini?” “Ni saa moja na nusu, ila leo nilikuwa na dharura kidogo” Dokta Kilumba alijibu swali la Mwandishi Gabriel Rondo huku akijibu swali asiloulizwa. “Jana ulifika kama leo, juzi ulifika kama jana, ulikuwa na dharura pia?” Mwandishi Gabriel aliuliza swali lililotokana na minong’ono aliyoisikia kule nje. Dokta Kilumba hakujibu, alikaa kimya. “Tuyaache hayo Dokta, labda itakuwa unadharura kweli kila siku, naomba unijibu swali hili sasa, je una taarifa za kupotea maiti kumi na tano kila siku katika hospitali yako?” “Taarifa hizo ninazo Mwandishi” “Kwahiyo ndani ya siku saba, maiti ngapi zimepotea Dokta?” “Maiti nyingi sana” Dokta Kilumba hakujishughulisha hata kuhesabu, alijibu tu. “Kwa fikra zako unadhani maiti zinapotelea wapi?” “Samahani Mwandishi, hilo swali siyo mahali sahihi hapa, mimi siyo mlinzi wa hospitali hii, mimi jukumu langu kuu ni kuhakikisha wagonjwa wanapona basi, wagonjwa wakifariki tu siyo jukumu langu tena, kwa bahati mbaya pia mimi sihusiki na chumba cha kuhifadhia maiti, kwa kifupi ninachoweza kukwambia, una maswali mazuri sana ndugu Mwandishi lakini umeyauliza kwa mtu asiye sahihi kabisa” “Wewe ni mtu sahihi Dokta! Dokta Kilumba wewe ni mganga mkuu wa hospitali hii. Una jukumu la kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa katika hospitali yako. Maiti zinapotea katika hospitali yako halafu unasema siyo jukumu lako, inaonesha kiasi gani usivyojua wajibu wako Dokta!” “Sina maelezo zaidi, nikichotaka kukwambia nishakwambia, siongozi neno hapa wala sipunguzi, kupotea kwa maiti siyo jukumu langu, nukta!” “Mbona kama hauoneshi kujari Dokta juu ya kupotea kwa maiti katika hospitali yako?” “Kujari kuhusu nini Mwandishi, watu wanaiba maiti zao wenyewe ili kuitia doa hospitali halafu nd’o nijari?” “Una uhakika na uyasemayo Dokta, inaingia akilini mtu kuiba maiti yake mwenyewe halafu alalamike kuibiwa?” “Hilo sio swali langu, kawaulize wenyewe wanaoiba” “Kama kuna mchezo mchafu wowote unaoendelea hapa hebu uacheni Dokta, unajua hamuwatendei haki wananchi” “Nakuomba toka nje!” “Hahaha natoka ila nakuahidi nitarudi tena Dokta!” Mwandishi wa habari, Gabriel Rondo alinyanyuka taratibu na kutoka nje. Alivyotoka nje tu, Dokta Kilumba alichukua simu yake na kumpigia Don Genge. “Hallo Don kuna Mwandishi anaitwa Gabriel Rondo hapaswi kuliona jua la magharibi. “Analeta chokochoko huyo Mwandishi kama jina la gazeti lake?”. Kabisa Don, kumuacha hai ni kulitafuta balaa, huyu Mwandishi Inaonesha kuna vitu anajua kuhusu sisi” “Usijari Dokta Kilumba, alasiri ataisikia kwenye bomba, kama ana fununu yoyote kuhusu sisi ataipeleka huko kuzimu” Baada ya kukatwa simu kundi la Don Genge walifanya walichopaswa kufanya. Na walichofanya kilileta matunda mazuri kwao, maana ni

kweli, saa kumi kamili jioni mwili wa Mwandishi wa habari, Gabriel Rondo uliokotwa katika ufukwe wa pwani ya Kilwa Kivinje. Mwili ulikuwa hauna macho, mwili uliojaa majeraha mengi sana, huku utumbo ukiwa unachungulia nje, ishara kuwa Gabriel Rondo alipitia mateso makali sana kabla ya kuuwawa! Nani angeweza kuutambua kuwa mwili ule ulikuwa wa Mwandishi Gabriel Rondo, hata ndugu zake wa karibu wasingeweza kuutambua. Ni kitambulisho kilichoning’inizwa kifuani kwake nd’o kilimtambulisha kuwa mwili ule ulikuwa wa Mwandishi Gabriel Rondo. Bila shaka kitambulisho hiko kiliwekwa makusudi na wauaji makatili wa Mwandishi huyo. Jeshi la polisi la Kilwa Masoko likishirikiana na polisi wa Kilwa Masoko waliingia kazini kumsaka muuaji wa Mwandishi wa habari wa gazeti la Chokochoko Gabriel Rondo. Vyombo vya kutetea haki za binadamu vikapaza sauti zao, kupinga mauaji ya kikatili aliyofanyiwa Mwandishi wa habari. Chama cha waandishi wa habari nao walilaani kifo cha Mwandishi mwenzao na kutoa maadhimio mazito Kwa Serikali. Tanzania nzima sasa ikageuzia jicho lake Kilwa, habari katika magazeti, televisheni zilihusu matukio ya ajabu yanayotokea Kilwa hasa katika hospitali ya wilaya ya Kilwa Kivinje. Taarifa hizo ziliruka moja kwa moja mpaka katika hospitali ya misheni ya Ndanda, hospitali aliyokuwepo Dokta Yusha na wagonjwa wake. Dokta Yusha aliyasoma yote kwa umakini mkubwa sana, akijua sasa mambo yamekuwa mabaya zaidi huko Kilwa. Hakushangazwa sana na taarifa za kupotea maiti kumi na na tano kila siku, ila alishangazwa na kuuwawa bila hatia kwa Mwandishi wa habari wa gazeti la Chokocho, Gabriel Rondo. “Lazima nirudi Kilwa kuuokoa jahazi” Wakati Dokta Yusha akiwa na mpango wa kurudi Kilwa. Kwenda kufichua uozo wa uongozi wa hospitali ya wilaya ya Kilwa, Kinyonga. Pamoja na kuweka hadharani ukatili wa kundi la Six killers. Huko Kilwa Kivinje mambo yalikuwa magumu sana. Mambo yalikuwa magumu kwa kundi hatari la Six killers, mambo yalikuwa magumu kwa jeshi la Polisi la Kilwa na wananchi wa Kilwa kwa ujumla. Kifo cha Mwandishi wa habari wa gazeti la Chokochoko, Gabriel Rondo hakikuwarudisha nyuma kabisa waandishi wa habari wengine. Waandishi wa habari hawakuweka chini kalamu zao. Waandishi wa habari sasa walipamba moto. Wakiushutumu uongozi wa hospitali ya wilaya ya Kilwa, Kinyonga chini ya uongozi wa Dokta Zaidi Kilumba kwa balaa kubwa waliolileta. Ziliandikwa habari kuhusu udhaifu wa uongozi wa hospitali ya Kinyonga, yaliandikwa makala kuhusu unyama wa uongozi wa hospital ya Kinyonga. Na chini ya habari zote hawakusahau kuandika maneno haya ‘upumzike salama Gabriel Rondo’ Taarifa za magazeti yale yalisambaa kwa kasi sana. Yalisambaa Tanzania yote, na baadhi ya nchi nje ya Tanzania. Kwa bahati au mzuri msambao wa habari hizo mbaya ukamfikia kijana mmoja….. Kijana shupavu sana, kijana mwerevu na mahiri katika sanaa ya mapambano.

Na chini ya habari zote hawakusahau kuandika maneno haya ‘upumzike salama Gabriel Rondo’ Taarifa za magazeti yale yalisambaa kwa kasi sana. Yalisambaa Tanzania yote, na baadhi ya nchi nje ya Tanzania. Kwa bahati au mzuri msambao wa habari hizo mbaya ukamfikia kijana mmoja….. Kijana shupavu sana, kijana mwerevu na mahiri katika sanaa ya mapambano.


Ilikuwa asubuhi tulivu sana na kijana huyo alikuwa amekaa katika sebuleni yake, katika nyumba ya kisasa iliyopo huko Mikocheni, Dar ea salaam. Asubuhi hiyo alikuwa anaangalia televesheni, ambapo kipindi cha kusoma magazeti kilimkuta akiwa ametulia kwenye sofa. Vichwa vingi sana vya habari vilisomwa katika magazeti hayo, lakini kichwa cha habari cha gazeti la Shupavu ndicho kilichomvutia zaidi. “Kilwa kuna balaa !” Kichwa cha habari hiko, kilichoandikwa kwa wino mwekundu, kuashiria uzito na uhatari wa habari hiyo, kulimnyanyua kijana huyo kutoka sofani, na miguu yake kumpeleka mtaani kutafuta gazeti la Shupavu ili aisome kwa makini habari hiyo. Hakupata shida sana kupata nakala ya gazeti la Shupavu. Baada ya dakika tano kijana huyo alirudi nyumbani kwake akiwa na gazeti la Shupavu mkononi. Alikaa tena palepale alipokaa awali, na kuanza kuisoma habari ile, ‘Kilwa kuna balaa!” Ilikuwa habari iliyoandikwa kwa umakini mkubwa sana, huku Mwandishi ikionekana alifanya utafiti wa kutosha kabla ya kushika kalamu yake na kuandika habari ile. Habari hiyo ilieleza kila kitu kuhusu Mpango wa utoaji mioyo ulivyo katika hospitali ya Kinyonga. Mwandishi pia akieleza uwepo wa kambi ya watoa mioyo huko porini, na kuweka hadharani udhaifu na ukatili wa uongozi wa hospitali ya wilaya Kilwa, Kinyonga. Habari ile ilimfanya yule kijana atafute jina la mwandishi wa habari ile. Hakukuwa na jina, maneno kutoka kwa ‘Na mwandishi wetu’ yalisomeka juu ya habari ile. Yule kijana akapiga hatua nyingine mbele, alifunua kurasa za ndani, kutafuta namba ya mhariri, aliipata. Aliziandika zile namba za mhariri katika kidaftari chake kidogo, kisha kuzinakili katika simu yake na kuzipiga. Simu iliita. “Hallo, habari yako?” Upande wa pili uliongea na kusalimia. “Bila shaka naongea na mhariri wa gazeti la Shupavu?” “Ndiye mwenyewe, nani mwenzangu?” “Naitwa Daniel Mwaseba” “Ahaa Daniel. Vipi kaka yangu” “Nina shida ndogo sana Mhariri naomba unisaidie” “Shida gani hiyo Daniel?” “Nataka unitajie jina la mwandishi wako mmoja na namba yake ya simu” “Yupi huyo?” “Aliyeandika habari yenye kichwa cha habari….. Kilwa kuna balaa” “Hiyo habari tumetumiwa na msomaji wetu, tena ilikuwa katika mtindo wa makala lakini sisi tukaamua tuiandike katika mfumo huo wa habari” “Mmeipataje sasa ile habari?” “Jamaa katutumia kwa email, na hatuna contact zake kabisa, zaidi ya hiyo email ambayo nayo kama imetelekezwa, maana tunajaribu kumuuliza vitu hamna majibu yoyote” “Sasa kwanini mmeiweka ile habari ilhali hamna hata uhakika nayo?” “Ile habari ina ukweli kwa asilimia mia moja, nenda Kilwa Daniel utayagundua makubwa kuliko hayo aliyoyaandika huyo jamaa” “Nataka mawasiliano na huyo jamaa kwanza, ndipo niende Kilwa, hatuishi kwa hisia” “Tutajitahidi kukutafutia kaka” Kwa wanaomjua Daniel Mwaseba hakuwa mtu wa kuombwa kuingia katika msako au misheni ya kuwasaka maadui wa nchi ya Tanzania. Alikuwa kashaingia rasmi katika kadhia hii tangu alivyoamua tu kwenda kununua lile gazeti. Daniel Mwaseba alitoka nje ya nyumba yake, akapanda gari lake na safari ya kuelekea Kilwa ilianza. Ndani ya kambi ya Don Genge hali ilikuwa mbaya sana. Watu wote mle ndani walikuwa na nakala ya gazeti la Shupavu mkononi, wakisoma habari ile mbaya sana iliyoandikwa na Mwandishi wetu. Wote walikuwa wamejiinamia chini, wamekuwa wadogo mithili ya piriton. Gazeti la Shupavu lilianika kila kitu kuhusu wao na mipango yao. “Kuna msaliti kati yetu” Moja wa six killers aliropoka kwa sauti kubwa. Wengine wote walikaa kimya, kama hawakuisikia ile kauli toka kwa Moja. Kilipita kimya cha dakika kama tano, Tano ambaye sasa alikuwa amepata nafuu kile kidonda cha goti alivunja ukimya. “Hakuna msaliti…” “Ilaaa….” Moja alidakia kabla Tano hajamalizia alichotaka kusema. “Mimi nina wasiwasi Sita ametekwa, na ni yeye ndiye aliyetoa siri zetu hizi” Tano aliongea kwa upole. Don Genge alimwangalia Tano kwa jicho Kali huku akitetemeka mikono kwa hasira. “Sasa kama Sita kakamatwa si muda wowote nasi tutakamatwa?” Dokta Sharifa aliuliza huku sauti yake ikionesha woga dhahiri. “Hatuwezi kukamatwa. Hata huyo Sita hapajui mahala hapa kwa usahihi wake, kama usivyopajua wewe, ila tatizo hatutofanya kazi yetu tena, maana pale, hospitalini kutakuwa na ulinzi mkali sana baada ya taarifa hii” Don Genge alifafanua. “Kipo tutakachofanya, jamaa wanataka mioyo ya

maiti kumi na tano kila siku, hawajari maiti ya mtoto mdogo au mkubwa. Itabidi twende mashuleni, tunawateka watoto, tunawauwa na kisha tunawatoa mioyo, zoezi la kutoa mioyo tutalifanyia hapa” Moja hakukubali kushindwa, alitoa wazo ambalo kila mmoja alilikubali kwa kichwa. Don Genge sasa akaelewa, kwanini jamaa amepewa namba moja katika kundi la six killers, alikuwa katili sana. Alikuwa na akili sana. Mpango wa kuwateka watoto wa shule ulibarikiwa na wote. Wakisubiri kesho yake waanze kuufanyia kazi mpango huo mpya. Sasa askari walijigawa kulinda shule zote za mjini Masoko. Na wazazi wengine waliingiwa na uwoga sana, hawakuruhusu watoto wao waende shule. Kuruhusu mtoto kwenda shule ilikuwa ni sawa na kumpoteza kabisa! Vilio ndani ya Kilwa vilizidi na kupaa zaidi, vikafika hadi nje ya mipaka ya Tanzania. Umoja wa mataifa kupitia shirika lake la watoto wakatoa kauli, na kuitaka Serikali ya Tanzania kuongeza nguvu katika kuwasaka wauaji hao. Marekani nayo ikatoa kauli, na kulaani pia vitendo hivyo vya kinyama. Hadi sasa watu wa Kilwa wakiwa hawajui chanzo cha mambo hayo kutokea. Mji ulipoa, watu wakiishi kwa woga mkuu. Watu wazima waliogopa, watoto wadogo waliogopa! Uwoga ulioathiri hadi shughuli za kiuchumi za Kilwa. Wakubwa waliogopa kwenda makazini, watoto waliogopa kwenda shuleni. Wakati ulinzi ukishamili katika shule zote za Msingi na Sekondari Kilwa. Polisi wakigeuka walinzi wa shule, kundi la Six Killers walibadirisha aina ya pigo sasa. Walevi saba walitoka majumbani kwao jioni lakini hawakurejea kwao usiku wa manane kama ilivyo ada yao. Walipokuwa wanarejea majumbani kwao usiku baada ya kulewa, njiani walidakwa na Six killers na kupelekwa porini ngome. Six Killers walikuwa wanahitaji mioyo, iwe ya watoto, iwe ya wakubwa, iwe ya walevi ama ya wazima. Kwa bahati mbaya kabisa, miongoni mwa walevi waliokamatwa usiku ule mbaya ni mama Kindumba, rafiki kipenzi wa Mwanasheria mlevi. * Ilikuwa ni wiki kadhaa tangu Mwanasheria mlevi kutoonekana katika kilinge chao cha ulevi. Ilikuwa huzuni kwa walevi wote kutoonekana kwa Mwanasheria mlevi. Huku lawama zote zikiienda kwa jeshi la polisi ambao ndio walimchukua kwa mara ya mwisho. Lakini pamoja na kutoonekana kwa Mwanasheria mlevi, walevi hawakuacha kunywa pombe. Waliendelea kunywa pombe huku wakimlilia Mwanasheria mlevi. Hakuna hata mlevi mmoja aliyewaza kwenda kituo cha polisi kujua hatma ya Mwanasheria mlevi. Wao wenyewe walikuwa wanajihisi wakosefu. Waende kituo cha polisi halafu…. Ndipo ulikuja usiku huu, usiku ambao walevi saba walipotea katika mazingira ya kutatanisha. Ukiwa ni muendelezo wa kupoteza kwa wanafunzi. Six killers walifanya kazi kwa umakini mkubwa sana, kila Mlevi alikamatwa kwa namna yake. Huku mama Kindumba akiwa mlevi wa mwisho kukamatwa usiku ule. Mama Kindumba alitoka kilabuni saa nane ya usiku. Alikuwa na furaha sana, alikuwa kalewa barabara, akiimba nyimbo yeye mwenyewe na kucheza yeye mwenyewe. Alikuwa anakata mitaa usiku wenye giza nene bila wasiwasi wowote. Watu husema pombe hupunguza uwoga kwa mlevi, inawezekana ikawa kweli maana mama Kindumba hakuwa na uwoga wowote usiku ule. Nyimbo zikizoimbwa kwa sauti ya kilevi na mbwembwe za kilevi zilikoma alipokutana na Bedui, Moja wa Six Killers. Pombe zote ziliishia hapo, nyimbo ziliishia hapo. Kwanza aliona Kivuli kirefu cheusi, kisha kivuli hiko kilirusha kofi moja la nguvu toka katika mkono ulioshiba wa Kivuli, mkono uliochanganyika na dawa za kulevya ulimlaza Mama Kindumba usingizi nzito. Mama Kindumba alilala katika mtaa wa Kariakoo pale karibu na ukumbi wa Hall fear na kuamka katika pori la Ngome. Na mama Kindumba kukamilisha idadi ya walevi saba waliotekwa siku hiyo. Mpelelezi Daniel Mwaseba ilikuwa ni sawa na askari Polisi wa kituo cha Polisi Masoko. Kila alipojaribu kuweka mtego wake kuwatega wahalifu kundi la Six killers waliutegeua mtego wake. Wakina Don Genge walikuwa wajanja sana walibadili aina ya watu wanaowateka mara kwa mara. Wakati wanawateka wanafunzi wa shule ya Msingi Masoko, siku ya pili yake Daniel Mwaseba alienda kulinda katika shule ya Msingi Mnazimmoja. Lakini Six killers hawakwenda kuteka tena wanafunzi wa shule ya msingi, walibadili mbinu, walienda kuteka wanafunzi wa shule ya Sekondari Kilwa. Wakati Daniel Mwaseba alienda kulinda shule ya Sekondari Mtanga, kundi la six Killers walibadili tena mtindo walienda kuwateka walevi. Daniel alikuwa anatabasamu kila tukio linavyotokea, ishara kwamba alikuwa anakasirika sana. Huyo ndiye Daniel Mwaseba hutabasamu kila mambo yanavyokuwa mazito. Kwa upande wa kundi la Six killers kwao ilikuwa ni furaha, vifijo na nderemo. Walikuwa na mateka wengi sana. Sasa walitulia katika kambi yao wakiwa na uhakika wa kupata mioyo kumi tano kwa siku kadhaa.

ITAENDELEA

Balaa Sehemu ya Nne

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment