Fedheha Sehemu ya Tano
IMEANDIKWA NA: AHMED MNIACHI
Simulizi: Fedheha
Sehemu ya Tano (5)
Taisamo alikaa dakika kadhaa akisubiri nakala ya risiti ya manunuzi ya gari ambalo lilisababisha ajali ya makamu wa Raisi. Alikuwa kwenye fikra nzito muda huo alishindwa kuelewa kwa nini ilikuwa ni lazima kwa makamu wa Raisi, yaani mtu mmoja anashambuliwa kutoka pande tatu tofauti? Alikuna kichwa kwa kidole chake cha shahada. Mara mlango ukafunguliwa badala ya yule aliyemtarajia akaingia Msichana mrembo.
“Unaitwa na mkurugenzi.”
Taisamo akainuka bila kuongea lolote na kumfuata yule dada.
Akapandisha ngazi hadi ghorofa ya kwanza wakaifuata korido ndefu hadi ofisi ya mwisho kabisa ambayo ilikuwa imeandikwa mlangoni DIRECTOR.
Hakumuona tena yule Afisa mauzo na badala yake alimkuta mzee mnene mwenye nywele nyingi nyeupe. Mzee huyo alikuwa na rangi ya maji ya kunde, uso mpana na pua bapa. Alikuwa amevaa suti ya rangi ya kijivu.
Alimtulizia macho yake yule mzee huku akistaajabu ule mzunguko ambao ulikuwa umeanza.
“Habari kijana.” Alisalimia yule mzee kwa sauti nene yenye mikwaruzo bila ikionesha kuathirika kwa pombe.
“Nzuri, shikamoo mzee.”
“Mh, ahsante. Nimelipata ombi lako lakini utaratibu ulioutumia sio utaratibu wetu wa ofisi kwani ilibidi uandike barua kisha ungejibiwa baada ya siku tatu sawa?” alimtazama huku akisubiri jibu la kukubaliana na kauli yake hiyo.
“Mzee, kuna mambo mengine ni ya dharura hivyo subira haifai tena.”
“hilo sio ombi na kwa kawaida hakuna ninachozungumza kikarudi nyumba.”
“Ni kweli lakini nasikitika kukufahamisha kuwa nalazimika kuvunja utaratibu wako, na nitakulazimisha kufuata taratibu zangu kwa nguvu.”
“Kijana, naona umekosa adabu ondoka ofisini kwangu.”
Wakati anamaliza kauli hiyo tayari alikuwa anatazamana na mdomo wa bastola ambayo ilikuwa imeshaondolewa kitunza usalama.
“dakika mbili zinatosa kuchagua kati ya kifo au kutoa risiti ninayoihitaji.”
“Sijawahi kuona mtu anayefanya mambo ya kipumbavu kama wewe, unafikiri ni jambo rahisi kiasi hicho wakati kuna kamera maalumu za usalama zinakumulika, na unanichekesha zaidi kwa kutofahamu kuwa umezungukwa na askari wenye silaha nzito.” Kauli hiyo ilimalizika ikifuatiwa na kauli nyingine nzito kutoka nyuma yake.
“Weka silaha yako mezani halafu urudi nyuma hatua kadhaa, kabla hatujasambaratisha kichwa chako.”
Haikuwa sauti ngeni katika masikio ya Taisamo, alikumbuka moja kwa moja kuwa ni sauti ambayo aliisikia nyumbani kwa dokta Kilonzo.
“Umemuua dokta, umemuua nesi na sasa unakuja kunimaliza mimi?”
Alihoji Taisamo akiwa amenyanyua mikono juu.
“Leo jua linawaka usitegemee kuwa litazimika ghafla kama ulivyozimika umeme nyumbani kwa dokta.”
“ni kweli lakini leo ni wewe ndiye utakayezimika.”
“Unachekesha sana na hii inathibitisha kuwa kweli mfa maji haachi kutapatapa, yaani unafikiri unaweza kunusurika katika kibano kama hiki?”
Taisamo aligeuka taratibu na kukutana na sura kavu za watu wanne wenye bastola.
“Bado unaweza kuendelea na jeuri mbele ya wanaume kama hawa?”
“Wanaume waoga ambao wanamfuata mtu mmoja tena wote wakiwa na bastola.”
“Mzee tunafanyaje sasa?” Aliuliza yule muuaji wa dokta.
“Nimepewa agizo kuwa anatakiwa afikishwe kunakohusika na kama hatatoa ushirikiano ndani ya siku mbili……”
“Achinjwe?” alidakia muuaji wa dokta.
Taisamo alikamatwa kwa nguvu na kuishuhudia sindano ikididimia begani kwake. Dakika chache baadae alihisi kizunguzungu na hatimaye akapoteza fahamu.
Hakujua tena kilichoendelea hadi pale alipozinduka na kujikuta kwenye chumba kipana chenye dirisha kubwa la kioo. Hakuwa peke yake kulikuwa na mwanamke ambaye alifungwa kwenye kiti kama alivyofungwa, tofauti na yeye huyu alionekana kujeruhiwa sehemu kadhaa za mwili wake kwa kipigo.
Taisamo alikuwa anakiona kifo chake waziwazi, hakuona kama kuna dalili ya kunusurika mbele ya mikono ile ya madhalimu.
Kilichokuwa kinamsikitisha ni kuwa mpaka muda ule alikuwa hajafumbua mafumbo kadhaa juu ya mauaji yale, alitaka angalau kwa hisia kujua ni nani anaweza kuhusika na mauaji yale, si hivyo tu kwanini mzunguko ule ni mkubwa na unawahusisha watu kadhaa. Kuna nini kinaendelea?
Mara mlango ukafungulia na kumfanya aondoke kwenye dimbwi la mawazo. Mtu aliyeingia alikuwa na umbo la wastani kiasi ilikuwa ni vigumu kuelezea iwapo alikuwa ni mrefu au mfupi, alikuwa amevaa shati jeupe na tai nyeusi, chini alimalizia kwa suruali nyeusi na viatu vya rangi ya kahawia.
“Habari yako bwana Taisamo.”
“Nzuri.”
Alijibu Taisamo kwa mkato huku akimtolea macho ya shauku yule mtu.
“Una nafasi nzuri tu ya kujiokoa kwenye madhila haya nayo ni kutoa ushirikiano kwa kujibu maswali nitakayokuuliza, uko tayari?”
Taisamo hakujibu chochote akabaki kumkodolea macho tu yule mtu.
“Kwanza nataka kujua umetumwa na nani na mpaka sasa umefikia wapi, pili nataka kujua familia ya marehemu Ole Nunga umeipeleka wapi na nani alikutuma kwenda kuiondoa?”
“Ningefurahi sana kama ungeweza kunifahamisaha wewe ni nani na umetumwa na nani ili tuweze kufahamiana maana njia uliyotumia kunialika kwenye huu usaili wako inanitia shaka.”
“Sitaki nikulazimishe kuzungumza naomba unijibu maswali yangu.”
“Nami sitaki unilazimishe kujibu.”
Jibu hilo likafuatiwa na teke kali la kifuani ambalo lilimfanya akohoe mfululizo.
“Nimekwambia nataka majibu la sivyo……”
“Mutaniua kama mulivyomuua muheshimiwa?”
“Nini wewe? John njooni mumshugulikie huyu kiumbe.”
Dakika chache baadae zilikuwa ni za kipigo kikali kwa Taisamo, akapoteza fahamu huku shati lake jeupe likiwa limetapakaa damu.
Alipozinduka alishangaa kukuta nyongeza ya mtu mwingine huyu akiwa mwanaume naye akiwa kwenye mateso kama yake. Akatulia huku akishangazwa na mambo yale ambayo yalikuwa yanatokea kama ndoto katika maisha yake.
“Huyu naye ni nani?” Lilimpitia swali kichwani mwake huku akishuhudia kipigo kikali kikiendelea kwa Yule mgeni.
“James Makabi nafikiri ulistahili sana kuitwa Makapi, badala ya makabi…” Alitulia Yule mtu na kumwangalia kwa Dharau James huku Taisamo akiyatazama yale mambo kwa kustaajabu.
“Ndiyo lazima niwe makapi si ndio mlivyopanga nimuue muheshimiwe makamu wa…..” Hakumaliza kauli yake kali likamsukuma tena sakafuni safari hii akifikia uso na kuchanika kidogo eneo la kidevuni.
“Kama hatutapata majibu ya kuridhisha wewe, na hao mbwa wenzio leo mnatandikwa risasi, hivi ninavyokueleza zimebaki dakika arobaini tu.”
Taarifa hiyo ilimfikia Taisamo na kumshtua sana, alijua wazi kuwa jamaa hawana utani na ni lazima watatandikwa risasi lakini alikuwa na shauku kubwa ya kumfahamu Makabi na uhusiano wake na kifo cha makamu wa Raisi. Kufa akiwa hajategua kitendawili kile ilikuwa karaha nyingine kubwa sana kwake.
Wakati Inspekta Tunu anaingia kwenye gari ndipo akashikwa bega, alipogeuka macho yake yakakutana na Mrakibu mwandamizi wa jeshi la Polisi Benard Kagasheki.
“Vipi Inspekta mbona umetoroka hospitali?”
“Ooh, habari afande.”
“Salama, nimetoka hospitali sasa hivi nilikuwa nakuja kuuliza kituoni kwako kama wana taarifa zako baada ya kukukosa.”
“Duh, mbona ulikuja mapema sana?”
“Ni kweli, nilikuwa nataka kujua hali yako na kama inawezekana pale ulipofikia kwani jukumu anataka kupangiwa mtu mwingine na wewe unahamishwa kutoka makao makuu kwenda mkoa wa Rukwa.”
“Eti…….!!!!” Aliduwaa Inspekta Tunu huku akiwa haamini anachokisikia.
“Ndivyo jopo la wakuu lilivyopanga”
“Yaani napangiwa haya mambo nikiwa mahututi kitandani…… afande hebu nielezeni nini kinaendelea hapa mbona sielewi?”
“Si vema kujadili mambo haya huku barabarani kama, utanifuata ofisini kwangu saa mbili na nusu.” Alitamka mrakibu kasha akatembea kwa haraka kuliendea gari ambalo lilikuwa limeegeshwa upande wa pili wa kituo kile cha teksii.
Zilipita dakika kadhaa huku Inspkta Tunu akiwa ameganda pale akishangaa jinsi mambo yanavyobadilika katika namna ya kushangaza, kikubwa kilichomshangaza ni kuona kuwa Mrakibu alikuwa akimfuatilia hatua kwa hatua. Angeweza kutuma askari wa cheo cha chini kumfuatilia lakini kitendo cha kuja mwenyewe tena katika namna ile ya kushtusha kilimpa wakati mgumu sana.
“Vipi tunaondoka ?” Aliuliza dereva teksi huku akishindwa kujua ni lipi sahihi kati ya kumwita afande au dokta kwani aliyasikiliza maongezi ya Inspekta na mkuu wake mwanzo hadi mwisho.
“Hapana, nahitaji kurudi ofisini kwanza.”
“Poa.”
“Hawajatoa ushirikiano bosi….” Aliongea kwenye simu mmoja kati ya watu wane ambao walikuwa kwenye chumba alichofungiwa Taisamo.
“Kwa hiyo tuwauwe wote au ….”
“Sawa.” Alisikika akijibu Yule mtu.
Bosi kasema wapigwe risasi wote.
Watu watatu wakaondoka na kumwacha mmoja ambaye alikuwa na bunduki aina ya SMG.
“Maliza kazi Kiongozi… sisi tuko huku nje.” Aliongea Yule ambaye muda mfupi alikuwa anaonge na simu na kumwacha jamaa akiikoki bunduki kwa furaha kubwa. Taisamo alimtazama jamaa kwa huzuni na kutaka kumbembeleza lakini akasita.
“Naanza na huyu mwanamke, umesikia Makabi? Nataka usikie uchungu kama niliyousikia siku uliyomuua mshikaji wangu Moyo.”
Alimlenga vizuri usawa wa kichwa huku akitabasamu kwa furaha kubwa kabisa.
“Pwaaaaaa……… Kishindo kikubwa kilisikika huku kikifuatiwa na mtawanyiko wa vitu.
Taisamo alitoa macho ya hofu huku akijaribu kujitoa kwenye kiti bila mafanikio. Damu zilitapakaa sakafuni, kishindo kilicholeta mshtuko kilimkuta kila mmoja mle ndani, ilikuwa ni patashika.
Inspekta Tunu alijiinamia alichanganyikiwa huku akiwa hajui nini alitakiwa kufanya muda huo. Akashikanisha vidole vyake kwa nguvu na kubana meno kwa hasira.
Nini kinaendea? Swali lilipita kichwani mwake na kumfanya aingiwe na ghadhabu zaidi.
“Hii nchi ina utawala wa sheria kweli au nimazingaombwe tu?”
Alivuta saraka lililokuwa pale mezani kisha akachomoa karatasi na peni na kuziweka pale mezani. Alitumia muda wa dakika chache kutafuna kizibo cha peni kabla ya kuanza kuandika .
YAHUSU KUACHA KAZI…………. Ndivyo alivyoanza baada ya kutanguliza anwani zote muhimu ambazo zinatakiwa kwenye barua za kikazi. Hasira zilikuwa zimemtawala na alihisi kuwa yuko sahihi kwa hatua hiyo ambayo alitaka kuichukua.
Ilimchukua dakika kumi kukamilisha barua ile. Akaegeme kiti na kujikuta akipitiwa na usingizi kwani bado dawa zilikuwa zinamlewesha.
Kelele za askari ambao walikuwa wanaingia kazini ndizo zilizomshutua kutoka usingizini. Akachukua ile barua na kuipitia upya huku akitikisa kichwa kuonesha kuridhika na kile alichoandika.
Akatoka mle ofisi huku akipishana na askari kadhaa ambao hawakuficha mshangao kutokana na Inspekta kuja na mavazi ya kidaktari.
“He, ina maana kaja mara moja tu kutoka hospitali?” Askari mmoja alimuuliza mwenzake.
“Hata mimi sielewi, halafu kwanini kavaa mavazi ya kidaktari?”
“Jamani, si bora tungemuuliza?” Mwingine alitoa hoja.
“wee, mimi nilikuwa wa kwanza kutaka kumuuliza lakini jinsi sura yake ilivyo inaonesha kuna jambo. Askari ambao walikuwa wanaingia zamu asubuhi ile walikuwa wanaendelea kuulizana maswali ambayo majibu yake alikuwa nayo Inspekta Tunu.
Alitembea kwa haraka safari hii akivuka kituo cha magomeni cha usalama na kuelekea Mikumi, alikuwa anayafanya hayo akiwa katika akili ambayo si ya kawaida, alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa. Kamishana, mrakibu… sijui na nani mwingine hawa wote wanahusika. Aliwaza huku akiwa ameshavuka barabara na kuelekea upande wa pili ambako kulikuwa na hospitali ya Magomeni.
Ghafla, akakumbuka kitu akajikuta anasita kuendelea na safari.
“Yaa, siku mbili kabla ya kuhamia kituo kipya nitakuwa nimepiga hatua kubwa sana.” Aliwaza huku akirudi na kuelekea tena kituo cha teksi cha mikumi.
“Yaa, lazima niikamilishe hii kazi haraka iwezekanavyo !” Alijisemea kwa sauti ndogo wakati akiwa karibu kabisa na kituo kile ambacho alifika hapo kabla.
“Wapi mama.” Aliuliza dereva teksi.
“Nipeleke kawe, lakini kwanza tupitie CRDB nataka kutoa pesa kwenye ATM.”
“Usijali mama.” Alijibu huku akijitoma kwenye gari.
Taisamo alikuwa anatarajia kuiona risasi ikisambaratisha kichwa cha Tamasha ambaye hakumfahamu jina. Lakini katika hali ambayo hakuitarajia akashtushwa na kishindo cha risasi ambayo ilipasua dirisha lile la kioo.na kumfikia kichwani Yule adui ambaye alikuwa amedhamiria kuwaua. Kisha likafuatia tukio lingine ambalo lilimpa maswali mengi kuliko majibu.
Dirishani alipenya msichana mrembo ambaye hakuwa mgeni katika macho ya Taisamo.
“Suzan…. Teacher Suzy….” Alibwabwaja kama mtu anayeweweseka.
“Hapana… ah no nitambue kama teacher Suzy halafu baadae utanitambua kama Kapteni Rose kutoka makao makuu ya jeshi la wananchi Tanzania.
Taisamo aliduwaa na kuacha mdomo wazi.
“Kumbe wewe ndiye Rose”
“Hatuna muda wa kupoteza Luteni naona umeumia sana, hii inaitwa Rescue mission na ni dakika saba tu natakiwa kukamilisha hii kazi.
“Rose, teacher Suzan……. “ Alizidi kubwabwaja lakini Yule mwanamke aliyejitambulisha kama Kapteni Rose hakujishugulisha kumjibu badala yake alikuwa anahangaika kumfungua Tamasha ambaye alikuwa kwenye hali mbaya zaidi.
Vishindo vya watu waliokuwa wanakuja kasi havikumshtua kapteni ambaye alionesha kufanya kazi yake bila wasiwasi. Dakika chache baadae zilisikika sauti za kitasa wakati kinafunguliwa na mtu aliyeko nje. Kapteni Rose aliruka dimbwi la damu na kusimama upande wa kulia wa mlango. Watu wawili waliingia ndani kwa kasi huku mmoja akiwa na bastola mkononi. Walikuwa ni wale mapandikizi ya watu ‘mabaunsa’ kama wanavyojulikana mtaani.
Ulikuwa ni wakati wa ajabu zaidi kwa Taisamo kwani alishuhudia ile bastola ikielea hewani baada ya kupanguswa kwa teke kali na Rose au Suzy mpangaji mwenzie kama alivyo mfahamu hapo kabla.
Haikuishia hapo pale alipofungwa alikuwa akishuhudia staili kali za Goju-ryu hii ni aina ya kareti ya kijapani ambayo inachanganya staili nyepesi na ngumu kwenye makabiliano. Go inamaanisha ngumu huku ikihusisha makabiliano ya moja kwa moja kama urushaji wa mateke na mikono ile Ru ni laini au nyepesi ambayo inahusisha zaidi minyumbuliko na mitembeo rahisi anayoifanya mtu wakati wa pambano. Hivyo goju-ryu inahusisha mbinu zote hizi ikiwa ni pamoja na kuepa,kuzuia na kupangua makonde na mateke.
Aliziangalia staili hizi kutoka kwa mwanamke mrembo mwenye cheo cha kapteni ambaye alikuwa akimsumbua mara kadhaa kwa simu kumbe akiishi naye nyumba moja bila kumfahamu. Dakika chache zilizofuata alishuhudia vijana wale wawili wakiwa sakafuni bila fahamu. Ni aina ya upigaji ambao alikuwa hajawahi kuuona kokote. Hili lilimshangaza sana Taisamo na kujikuta akihusudu aina ile ya upigaji.
“Dah, Jeshi halikukosea kukupa cheo hiki Rose.” Alitamka Luteni Taisamo huku akimkazia macho kapteni Rose ambaye alikuwa anamfungua kamba alizofungiwa pale kwenye kiti. Rose hakujibu kitu badala yake aliendelea kufungua alipomaliza akaenda kumfungua Makabi.
“Hatuna muda wa kujadili, nimebakiwa na dakika moja tu ya kukamilisha mpango wangu sote tutapitia hapa dirishani, wewe (huku akimuoneshea kidole Makabi ) Kwa kuwa hujaumia sana utamnyanyua huyu mwanamke kisha mimi nitampokea kwa nje. Luteni najua uko vibaya lakini jitahidi tuondoke hili eneo kwa sasa sio eneo zuri.
Taisamo huku akichechemea nae alikua akijivuta kuelekea pale dirishani, wote wakapita pale Dirishani salama bila kupata purukushani.
Usiku wa manane ndani ya ukumbi uleule. Mkuu aliinua kichwa akawatazama wajumbe waliohudhuria mkutano kwa dakika kadhaa na kwa macho makavu huku akijilamba kingo za midomo yake ambazo zilianza kukauka. Alinyanyua glasi ya maji ambayo ilikuwa pale mezani akajimiminia funda tatu za haraka kabla ya kuyarudisha macho yake kwa wajumbe. Wajumbe walikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua nini kimejiri mpaka kufikia hapo.
“Mambo hayajakaa sawa.” Alianza Mkuu na kutulia kwa dakika kadhaa kana kwamba alikuwa amemaliza kongea.
Bwana Wahuva Kilale alikuwa miongoni mwa wajumbe wa mkutano huo, naye alikuwa anasubiri kwa shauku kubwa nini ataongea mkuu.
“Tumefanya kazi ya ziada ya kumuondoa mtu ambaye angetuletea matatizo lakini tumeharibu sana kwani jahazi sasa linaenda mrama na kama hatutakuwa makini tunaelekea kuanguka kabisa kisiasa”
Akatulia na kuwaangalia wajumbe ambao waliganda kwenye viti kama barafu ndani ya jokofu, kila mmoja alikuwa ametoa macho ya hofu kumuelekea mwenyekiti.
“Wengi mlikuwa hamfahamu, lakini kwa taarifa ni kwamba kuna watu walijaribu kunusa kuhusu kifo cha makamu wa Raisi lakini tukawadhibiti huku tukitoa uhamisho kwa wengine ili kuvuruga utaratibu wao, kimsingi hatukuwaogopa wao kama wao na wala hakuna mamlaka inayoweza kututikisa zaidi ya habari hizi kufika kwenye vyombo vya habari na masikio ya wananchi.” Akatulia na kuwatazama tena wajumbe huku akitafunatafuna meno yake. Nafikiri nyote mtakuwa mashuhuda jinsi tulivyoweza kuwafunga mdomo waandishi kadhaa wa habari huku wengine tukiwapa warning kwa kuwang’oa kucha na meno, ni zoezi ambalo limetusaidia sana kwani wameacha kusema na wale waliotaka kusema wameogopaUtaratibu huu utatumika kwa yeyote atakayeonekana kutishia maslahi yetu. Lakini bado kuna tatizo inaonekana kuna watu nje system wamelivalia njuga suala letu, tulishafanikiwa kuwaweka mikononi wale ambao walionekana kuwa kikwazo lakini taarifa zilizopo ni kuwa hao watu wametoroka na wameokolewa na mtu au watu wanaodhaniwa kuwa na ujuzi wa hali ya juu. Sasa kinachonishangaza ni kuwa watu wote muhimu tunao hapa nani tena anahusika na sakata hili?”
Taisamo aliendelea kumkazia macho Suzy kwa kustaajabia mambo aliyoyafanya.
“Wewe mwanamke ni balaa, yaani siamini kama kuna mrembo mwingine kama wewe ambaye badala ya kukaa mbele ya kioo akihangaikia uso wake kwa kuuremba kwa mainjofesi….. Dah yaani sijui niseme nini.”
“Ha ha ha umefanya kazi nzuri Taisamo wewe ni mwanaume wa shoka, tulikuwa tunakufuatilia hatua kwa hatua Jenerali kakusifia sana.”
“Ha! Ina maana mlikuwa manafahamu kuwa sihusiki na yale matukio?”
“Mwanzo tulikutilia Mashaka lakini kilichokusaidia ni kutoa taarifa kwa Meja ingawa ilikuwa vema taarifa ile ungeipeleka moja kwa moja kwa Jenereli lakini hakijaharibika kitu kwani ulikuwa katika mazingira ambayo yalikufanya ushindwe kujiamini.”
“Kwani Meja anahusikaje na kitengo wakati alishastaafu siku nyingi?”
“Kitengo ni zaidi ya unavyofikiri, Meja amestaafu katika majukumu ya kawaida lakini bado tuko naye kwenye M.I tena ni mshauri mkuu wa mambo ya silaha.”
“Kwa hiyo nanyi mmegundua nini upande wenu?”
“Uchu.”
“Uchu kivipi?”
“Tumegundua kuwa muheshimiwa anaondoka madarakani huku bado akiyapenda madaraka hivyo ili kuendelea kutawala nje ya madaraka ni lazima awaweke watu ambao watakuwa kama rimoti yake huku yeye akitawala nyuma ya mgongo.”
“Sasa kama muheshimiwa ndio Muhusika mkuu unafikiri sisi tutawezaje kutatua hili?”
“Ziko njia tatu tu, leo wakuu watakaa kuamua ni njia ipi itumike, Kwanza ni kumuua muheshimiwa na kuuvunja mtandao wake ambao unahatarisha amani na uchumi wan chi, pili ni kumlazimisha muheshimiwa kujiuzulu na tatu ni jeshi kuchukua nchi na kudhibiti kila kitu.”
“Sawa na wale wawili ambao tulikuwa nao umewafahamu?”
“Ndiyo ni Jemsi Makabi na mchumba wake Tamasha, Makabi katueleza kitu kuanzia jinsi alivyolazimishwa kusababisha ile ajali na hatimaye kufanikiwa kunusurika.”
“Dah, kwa hiyo ni yeye ndiye kasababisha ile ajali! Mh… ajabu kweli, sasa huyu ni mtuhumiwa au inakuwaje?”
“Kutokana na mazingira ya ajali tumekubaliana nae kuwa hakutaka kumuua muheshimiwa kwani iwapo angekuwa na nia hiyo basi lilikuwa jambo rahisi sana kwake kummaliza kwa ajali ile.”
“Kwa hiyo mmemrudisha kwake?”
“Hapana yeye ni shahidi muhimu sana kwetu na kwa mujibu wa maelezo yake tumebaini kuwa anayehusika ni afisa mwandamizi wa idara ya usalama wa Taifa ambaye anajulikana kama Othmani Geresha huku akitumia jina la bandia la Mjomba Masharubu ambalo amekuwa akilitumia sana kwenye kupanga mikakati yake ya mauaji pia tunasubiri kumweka katika himaya y.”
“Hapana ni mtu hatari sana ambaye kwa pamoja tunatakiwa kumtia mikononi mwetu kwa umakini mkubwa kwani vinginevyo itakuwa ni hatari kubwa na kwa kutambua hilo mkuu katuongezea nguvu, Tutaongezewa watu wengine wawili ambao ni Sajenti Jesca Mpangala na Staff sajent Mariam Goza.”
“Duh, kwanini nimeletewa wanawake watupu?”
“Ha ha ha ha Othmani Geresha ni mtu hatari sana na ana akili na mbinu nyingi lakini udhaifu wake tumegundua uko kwa wanawake.”
“Lini tutaanza hiyo kazi maana nina hasira sana na hao jamaa.”
“Ni baada ya kupata ripoti kamili kutoka kwa Inspekta Tunu wa jeshi la polisi………”
“Ni Inspekta ambaye aliamua kuacha kazi wakati yeye ndiye alikuwa ameshikilia upelelezi wa tukio hili tulipofuatilia tukagundua kuwa kuna tatizo hivyo leo tutapokea maelezo yake kisha tutayaunganisha katika misheni yetu.”
“Kwa nini tusianze na Yule mkuu wa kampuni ya uuzaji magari maana anaonekana kuwa mshirika mkubwa wa uovu huu!”
“Ni wazo zuri lakini yote hayo ni baada ya kupata taarifa kutoka kwa Inspekta ambaye mpaka sasa yupo kwenye mahojiano maalumu na Jenerali.”
“Dah, kwa hiyo hii kazi nitaifanya na warembo watupu.”
“Ha ha ha mimi basi tena.”
“Wewe ni zaidi ya warembo Suzy ah… no Rose dah halafu sitasahau yaani we unanipigia simu kumbe uko ndani mlemle.”
“Ok, sasa wacha nikamsikilize Jenerali anasemaje maana nahisi atakuwa amemaliza kuongea na Inspekta.”
Saa 4.30 usiku, Othman Geresha alikuwa amekilaza kichwa chake kwenye kona ya moja ya sofa ghali. Macho yake alikuwa ameyaelekeza kwenye Tv ambayo muda huo alikuwa ameizima. Hakuwa anaona chochote kilichokuwa mle ndani, fikra zake zilikuwa nje kabisa kwa mara ya kwanza alijihisi kuwa kwenye hatari kuliko wakati wowote ule, alihisi kuwa alitakiwa kufanya mauaji kuliko wakati wowote ule ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kunusurika na mikono ya maadui zake.
Alijaribu kutafakari namna maficho yale yalivyoweza kubainika na hatimaye kuokolewa kwa Taisamo na wenzake. Akiwa kwenye tafakuri hiyo mara simu yake ya mkononi ikaanza kuita.
“Ndiyo mkuu.”
“Tuonane hapa namba tatu.” Aliskia sauti kutoka upande wa pili.
“Sawa mkuu.” Akakata simu na kuuendea mlango kwa haraka.
Aliendesha gari huku akiwa na mawazo mengi sana, hakujua kwanini mambo yameharibika kuliko wakati wowote ule.
Ndani ya dakika ishirini na mbili alikuwa katika viunga vya ofisi hiyo nyeti. Ambapo sekunde sitini baadae alikuwa ana kwa ana akikabiliana na mkuu wa idara ya usalama wa Taifa nchini.
“Geresha, hatuna muda wa kupoteza kwa sasa kwani tukifanya mchezo sio watu wetu tu watakaoanguka bali hata chama kinaweza kuanguka kuna hatari ya kuingia watu wanaoitwa Wazalendo madarakani, wakishaingia wao watu wengi watapoteza heshima zao, nataka ufahamu mambo ambayo ulikuwa huyafahamu, Kwanza kuna akaunti zetu ziko nje ambazo baadhi ya wapinzani wameanza kunusa nusa huko, haya yote yanahitaji kuzimwa tena wakati mwingine kwa kuwaondoa hata wenzetu ambao tunaona wanaweza kuwa kikwazo pia.” Akatulia kidogo Mzee huyo ambaye alionekana kutokuwa katika hali ya kawaida siku hiyo.
“Sijakupa nafasi ya kuongea kwa sababu hata wewe mwenyewe unafahamu kuwa hali ni mbaya na inahitaji kurekebishwa haraka iwezekanavyo, hivyo kuna majina ya watu ambayo tumekuwekea ndani ya bahasha hii, wanatakiwa kuondolewa haraka sana kabla mambo hayajazidi kubadilika na mara hii tunatumia Plan B hatutatumia tena Plan A, hivyo ni kuua bila kuhoji.”
“Nimekueewa mkuu nakuhakikishia kuifanya kazi hii kwa umakini zaidi kwani hata mimi nimeona jinsi mambo yalivyoharibika.” Alisikika Makabi huku akichukua ile bahasha yenye majina hayo. Kisha akanyanyuka pale kitini na kuelekea nje moja kwa moja tayari kwa maandalizi ya kazi hiyo aliyopangiwa.
Ndani ya nyumba ile ya kisasa ambayo ilikuwa inamilikiwa na Jeshi la wananchi Maafisa wanne wenye vyeo tofauti walikuwa kwenye mjadala mkali jinsi yakuanza kazi yao.
“Kwa hiyo tutaanza pale kampuni ya magari, sajenti Jesca utatangulia ofisi ya mkurugenzi halafu sisi tutafuata dakika tano baadae sawa?” Aliuliza kapteni Rose.
“Sawa mkuu, lakini natakiwa kufanya nini nikishafika?”
“Wewe ni askari tumia mbinu yoyote ya kumchelewesha, tumeweka hizo dakika tano ili kama ataleta watu kukuvamia tuwatie nguvuni kwa pamoja.”
“Unafikiri anaweza kufanya kama alivyonifanyia mimi.” Alihoji Taisamo.
“Inawezekana pia, lakini tunahakikisha kifaa chake cha mawasiliano kiko hewani ili kama kuna dharura yoyote tuweze kufahamu.”
“Hakuna shida.” Alijibu sajenti Jesca kwa kujiamini.
“Tunaondoka dakika ishirini kutoka sasa, nafikiri kila mmoja yuko tayari kwa kazi, kama kuna swali au hoja anipatie sasa hivi”
Taisamo akakohoa kabla ya kuzungumza.
“Naomba nisaidiwe kitu kimoja Kapteni, nataka kujua mmiliki wa gari lenye nambari za usajili TKD 2341.”
“Unaweza kutudokeza anahusika vipi na hili sakata letu.”
“Ndiyo, ile siku ambayo aliuwawa dokta, muuaji alitoroka kwa gari lenye namba hizo kwa bahati mbaya sikuwahi kufuatilia zaidi kutokana na muingiliano wa mambo kama ulivyoona.”
“ok, hilo tutamwachia Inspekta Tunu atalifanyia kazi kupitia kwa watendaji wenzake.”
“Si mlisema ameacha kazi?”
“Ni kweli, lakini bado anaweza kuwa msaada mkubwa sana kwetu kupitia kwa watendaji ambao alikuwa nao hapo awali.”
“Ok itakuwa vema.”
Sajent wa jeshi la wananchi kutoka kitengo maalum cha MI alikuwa anapandisha taratibu ngazi zinazoelekea kwenye ofisi ya mkuu wa kampuni ile ya uwakala wa magari aina ya NISSAN PATROL, nyuma alifuatiwa na wanajeshi watatu wenye vyeo vya kapteni, Luteni na Staff sajenti.
Macho ya kawaida yasingeweza kufahamu kuwa walikuwa safari moja.
Akagonga mlango wa osfisi na kisha kuingia ndani.
“Karibu Aunt.” Sauti nyororo ya kike ndiyo iliyompokea tofauti na matarajio yake.
“Ahsante naweza kuonana na bosi?”
“Hapana…ah sina uhakika atakuja muda gani maana si kawida yake mpaka saa nne hii awe hajafika kazini.”
“Ok.Nitarudi tena baadae kidogo.” Alimaliza kauli yake hiyo kwa kuubamiza mlango wa ofisi ile.
Nje wale maafisa wengine wa jeshi walikuwa wameshafika usawa wa lango la kutokea nje kwani kila mmoja alikuwa amevaa kisikilizio maalum ambacho kilimwezesha kujua kilichokuwa kinajiri ndani kati ya sajenti Jesca na yeyote yule.
Baada ya kulifikia gari lao aina ya Landrover 110, Taisamo alimgeukia Rose.
“Wapi sasa au kwa Kamishna?”
“Hapana, tutafika nyumbani kwa huyu jamaa (huku akinyooshea mkono majengo ya ile kampuni ya magari) kisha tutafika nyumbani kwa kamishna halafu tunamalizana na Geresha ambaye atatuonesha njia jinsi ya kumpata mkuu wa kampeni hii.”
“Mpango nzuri.” Hatimaye ilisikika sauti ya Staf sajent Mariam Goza dereva wao ambaye mara nyingi alikuwa anapenda ukimya jambo ambalo lilimshangaza sana Taisamo.
“Unakufahamu nyumbani kwake?” Aliuliza Taisamo.
“Ndiyo tunazo details zake zote, anaishi Upanga karibu na kituo cha zamani cha polisi, nyumba namba 54K”
“Duh, uko makini sana kapteni.”
“Lakini si zaidi yako na nahisi hii ni mara ya mission ya mwisho kwangu kuwa juu yako baada ya hapa tutakuwa nafasi sawa au utakuwa zaidi yangu.”
Baada ya dakika Arobaini gari lilikuwa katika eneo lililokusudiwa, kama ilivyokuwa mwanzo safari hii pia chambo alikuwa Sajenti Jesca.
Alipolifikia lango akabonyeza kitufe cha kengele ambacho kilikuwa upande wa kulia wa lango. Ilimchukua sekunde chache kushuhudia lango likifunguliwa.
“habari za kazi”
“Nzuri sijui nikusaidie nini?”
“naomba kuonana na Mr. Kairuki”
“Ulikuwa na ahadi naye?”
“Hapana.”
“Basi ngoja niongee nae kwanza.” Alisikika yule mlinzi huku akiliacha lango likiwa wazi na kuelekea ndani.
Mariam Goza alitumia fursa hiyo kulisogeza gari pale langoni. Kisha Taisamo akawapa ishara wenzake ya kuingia moja kwa moja kule ndani.
Dakika mbili zilikuwa zimepita bila yule mlinzi kutoka nje, Taisamo akausukuma mlango na kuingia ndani huku akifuatiwa na maafisa wengine wa jeshi.
Yule mlinzi alikuwa ametumbua macho huku mikono ikiwa kiunoni akistaajabia kile alichokuwa anakiona. Maafisa wale wa jeshi walijumuika katika mduwao ule kwa sekunde chache.
“Vipi ndugu nini kimetokea hapa.”
“Dah, sielewi ndugu zangu mimi ni kama ninyi tu ingawa nimetangulia kuikuta hii hali.” Alijibu Mlinzi huku akiushangaa mwili wabosi yule wa kampuni ya uwakala wa magari ambaye alikuwa amepigwa risasi kifuani na kufanya kidimbwi cha damu pale sakafuni ulipolala mwili ule.
“Ni nani alikuwa na marehemu mara ya mwisho.”
“Nafikiri ni vema maswali hayo nikiwajibu polisi.”
“Sisi ni zaidi ya hao polisi.” Alijibu Kapteni huku akitoa kitambulisho chake na kumkabidhi.
“Mlinzi alikitazama kile kitambulisho na kujikuta akitumbua macho kwa mara nyingine kumshangaa dada yule mrembo kupewa cheo kikubwa cha kijeshi.
“Nafikiri ni vema ukitujibu maswali yetu.”
“Mtu wa mwisho kuja hapa ni rafiki yake mkubwa ambaye sidhani kama anaweza kuwa yeye.”
“Unaweza kutuelezea jinsi alivyo huyo mtu?”
“Ni mrefu, mweusi, pua yake ni pana na hupendelea sana kuvaa suti nyeusi na kofia ya pama.”
“Oh, huyo atakuwa Geresha.” Aliongea kapteni Rose.
“Ni kweli kapteni, nafikiri sasa tubadilishe huu mpango, badala ya kuanza na hao wengine ni bora tuanze na huyu Geresha la sivyo atasababisha madhara makubwa sana.
*
Saa 4.30 usiku, Geresha a.k.a Mjomba Masharubu alikuwa anaondoka nyumbani kwake kwa pikipiki aina ya Boxer. Hakufahamu kuwa alikuwa ameongozana na kikosi maalum cha kijeshi chenye watu wanne. Mwendo wake ulikuwa wa wastani hivyo ilikuwa ni fursa nzuri kwa wawindaji wake kumfuatilia kwa umakini zaidi.
Safari yake ilimfikisha kwenye Baa maarufu ya SIMBA KAPAKATWA iliyopo maeneo ya Ilala boma. Kama kawaida yake aliingia hapo akiwa na lengo la kuondoka na mrembo ambaye angemvutia usiku huo.
“Jesca nafasi yako hiyo.”
“Yap, ngoja nimuwahi.” Alisikika Sajenti huku akiwa nje ya gari.
Kwa mwendo wa madaha aliingia mle ndani na kutafuta meza ambayo ilikuwa karibu kabisa na pale alipokaa Geresha. Geresha hakujishugulisha na Jesca badala yake muda mwingi alikuwa anabofyabofya simu yake kana kwamba kuna mtu alikuwa anawasiliana naye jambo ambalo lilimtia mashaka Sajenti Jesca.
Kwa sifa alizozisikia kuhusu Othman Geresha hii haikuwa tabia ya kawaida. Kwanza mtu mwenyewe alikuwa anakunywa soda tofauti na matarajio yake kuwa ni mnywaji mzuri wa pombe na huwa hana tabia ya kulewa kijinga.
Ghafla akamuona Othman Geresha akiondoka kwa kasi kuelekea upande wa vyooni. Sekunde chache baadae likafuata tukio jingine la aina yake.
Taa za mle ndani zilizimika ghafla na kisha ikafuata milipuko ya bastola ambayo ilileta taharuki kubwa na kuwafanya watu waache viti vyao na kuanza kutawanyika huku kila mmoja akipiga kelele anazozijua kutokana na hofu.
“Msaada kapteni nimevamiwa….. oooh..aaaaah.”
Sauti ya mtu aliyekuwa kwenye matatizo iliwafikia kapteni,Luteni na Staf Sajenti ambao walikuwa wanasubiri wakiwa kwenye gari.
Hakukuwa na mashauriano tena kila mmoja alishika vema bastola yake na kukimbia akielekea eneo la tukio.
“Kuweni makini si mmesikia hizo bastola zinavyopigwa kiufundi na mpigaji si mmoja tena inaonekana wamedhamiria kuua na si kutisha watu.” Alisikika taisamo kwa sauti iliyojaa ghadhabu.
Jesca alikuwa hasikiki tena badala yake zilikuwa ni sauti za watu waliokuwa wanakimbizana tena zikielekea kupungua. Mtafaruku pale ndani ulikuwa mkubwa kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu kwa maafisa wale wa jeshi kupenya kirahisi kutokana na uwingi wa watu waliokuwa wanatoka eneo lile.
“Anatoroka, mtafuteni sajenti mimi namfuatilia.” Alisikika Taisamo huku akiikimbilia ile pikipiki aina ya boxer ambayo ilikuwa imewashwa tayari kwa kuondoka. Alifanikiwa kwenda hatua kadhaa ndipo bastola ya Luteni ilipofanya kazi na kumpata bega la kushoto kwa nyuma.
“Shiiiiiiit……….” Aliropoka Geresha huku akimalizia kwa tusi zito la hifadhini. Akajitupa chini huku bastola ikiwa mkononi. Taisamo alikuwa makini na hakutaka kuruhusu kosa lolote wakati huo. Akamfyatulia risasi nyingine mkono wa kulia na kumfanya adondoshe ile bastola.
Ghafla akasikia milipuko mingine ya bastola kutoka mle Baa.
Yalikuwa ni majibizano makali baina ya Maafisa wale wawili na watu wanne waliokuwa na silaha. Taisamo hakutaka kupoteza muda medani ya kivita ilimtuma kuwa wakati ule alitakiwa kutoa msaada kwa wenzake.
Huku akiwa katika mbio kalindipo kwa mshtuko mkubwa alipogongana na mtu aliyekuwa anakimbia kutoka ndani. Kwa msaada wa taa za jengo la jirani alimtambua! Walikutanisha macho yao huku kila mmoja akihema.
“Tumekutana tena rafiki, umenikumbuka.”
“nakukumbuka sana, sasa unasemaje?”
“Ulikatisha maswali ambayo nilikuwa namuuliza dokta sasa leo nataka kufahamu huyu Mkuu ni nani na bila shaka jibu unalo wewe.”
“Unafikiri ni rahisi kiasi hicho kupata jibu?”
“Ni rahisi sana Mr.Majogo, kumbe jeshi linaamini kuwa lina watu mahiri wakati watu wenyewe ni wasaliti tena tumekuamini na kukuweka kitendo muhimu cha MI nawe unatuangusha kiasi hiki? “ Ilikuwa ni sauti ya Rose ambaye alikuwa nyuma ya yule jamaa huku akiwa na bastola mkononi machozi yakiwa yanamtiririka mashavuni mwake, hiyo ilikuwa ni ishara tosha kwa Taisamo kuwa Sajenti Jesca amepoteza maisha.
“Dondosha bastola yako chini kabla hatujakulipua.” Sajini mtumishi ‘staff sajent’ Mariam Goza alifoka baada ya kufika eneo lile.
“Kumbe unamfahamu huyu?” aliuliza Taisamo.
“Huyu ni Elias Majogo ana cheo cha Meja na ni kiongozi wa Unit nyeusi, sasa nashangaa kiongozi anakuwa hivi sijui anaowaongoza watakuwaje!”
“Meja tafadhali mtaje mkuu kwa usalama wako.”
“Bado si rahisi kapteni siwezi kujibu maswali yako wala ya Luteni, nyote ni wadogo sana kwangu ingawa mmebahatika kuniweka katika himaya yenu.”
“Utajibu tu hapa huna ujanja Meja.”
“Nikiwa kaburini labda…” alijibu huku akilamba mikono yake.
“Anajiua mzuie…..” Alipiga kelele Rose akimwamrisha Taisamo kumzuia Meja lakinini alikuwa amechelewa.
“Duh, jamaa alikula kiapo kibaya sana yaani alikuwa na sumu mkononi!” Alistaajabu Staff Sajent Goza.
“Vipi hali ya Jesca?”
“Jesca ameuwawa na nimeshatoa taarifa anakuja kuchukuliwa, Vipi umemkosa Geresha?” Alimaliza kwa kuuliza.
“Geresha nimempiga risasi na kwa jinsi alivyo hawezi kutoroka inabidi naye achukuliwe kwani atakuwa msaada mkubwa sana kwetu.”
“ Ok inatakiwa abanwe usiku huuhuu.”
Mazishi ya Sajenti Jane yalifanyika kwa heshima zote za kijeshi huku akiwa amepandishwa cheo na kuwa Warrant officer class one. Mazishi yake yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kijeshi huku taarifa ya kifo chake ikiahidiwa kutolewa baada ya wiki mbili.
“Enhe sasa nini kinafuata?”
“Tunatakiwa kumaliza kazi iliyobaki.”
“Tunaanzia wapi?”
“Tutaanza na ripoti tuliyoletewa na Inspekta.”
“Mbona kama ile ripoti itakuwa inaturudisha kwa watu waliokufa?”
“Hapana, bado hatujafahamu chochote kutoka kwa kamishna wa kanda ya Dar es salaam.”
“Wazo zuri kwa hiyo tunatakiwa kwenda ofisini kwake?”
“nafikiri ni vema ikiwa hivyo.”
Wakachukua gari la jeshi ambalo lilikuwa na namba za kiraia, safari hii wakiwa peke yao bila kumshirikisha Goza.
“Bado unanipenda Luteni!” Aliuliza Rose huku wakiendelea kukata mitaa kuelekea kwenye jengo la makao makuu ya Polisi kanda ya Dar es salaam.s
“Kwanini usingeniuliza swali hilo bila kutaja cheo changu”
“Ha ha ha ha vizuri, nafikiri tutaongea zaidi tukikamilisha hii kazi.”
“Sawa, tutaongea na nitakuonesha jinsi ninavyokupenda.”
“Sasa mbona unaendeleza hii mada.”
“Ok, I’m sory dear.”
“ha ha ha ha nani Rose au Suzy?”
“Teacher Suzy.” Waliendeleza utani wakati wanakaribia majengo ya Polisi makao makuu kanda ya Dar es salaam.
“Mimi nitabaki kwenye gari.”
“Kwanini tusiende wote.”
“hii ni mission yako mimi nilipewa mission ya kuja kukuokoa tu.”
“Ok.” Alijibu huku akiubamiza mlango wa mbele na kuanza kutembea kuelekea kule ziliko ofisi.”
“Habari yako Dada!” Alimsalimu mmoja wa askari ambao aliwakuta pale kaunta.
“Nzuri, nhe eleza shida yako….” Alisikika yule dada kwa sauti iliyojaa dharau.
“Nahitaji kuonana na Kamishna.”
“Kamishna yupi, hapa makamishna ni wengi.”
“Kamishna wa kanda maalum.”
“Eh, kwani una shida gani maana mkuu yuko bize sana leo mara aende ikulu mara arudi sasa sio ugomvi na mkeo ndio uende kwa kamishna.”
“Ni muhimu nahitaji kumuona!” Mara hii aliongea akiwa ametoa kitambulisho chake.
“Ok, pita huku kulia pandisha hizo ngazi floor ya kwanza mlango wa tatu upande wa kushoto, utaona hapo mlangoni kumeandikwa kamishna lakini sina uhakika kama bado yupo ofisini.”
Akapita kimlango kidogo cha pale kaunta na kuelekea upande aliolekezwa.
“Karibu.” Dada aliyekuwa nyuma ya kompyuta kubwa aina ya Fujitsu siemens alimkaribisha Taisamo.
Taisamo alitumia muda mfupi kuisanifu ofisi ile ambao ilikuwa ni ndogo kabla ya kuifikia ofisi kuu ya Kamishna. Alijua moja kwa moja kuwa anaongea na katibu muhtasi wa mkuu huyo.
“Ahsante, habari yako.”
“Nzuri, sijui nikusaidi nini?”
“Nahitaji kuonana na Kamishna.”
“leo yuko bize sana na ametoa agizo kuwa hahitaji kuonana na mtu yeyote yule.”
“Ok, Vema lakini mimi sio mtu yeyote.”
Aliongea Taisamo huku akiwa ameshafungua mlango wa ofisi ya kamishna. Hata hivyo hakukuwa na yeyote ofisini.
“Yuko wapi?”
“Wewe sio mtu yeyote, unashindwaje kujua aliko?”
“Ok, kzi njema.”
Aliongea Taisamo huku akimwacha yule mwanamke mwenye cheo cha koplo akiwa amebinua midomo yake kwa hasira.
“Vipi?”
“Aliuliza kapteni Grace wakati Taisamo akiwasha gari.”
“Huyu tumuibukie nyumbani kwake tena usiku.”
“Kwanini?”
“Nahisi upatikanaji wake siku hizi ni mgumu kidogo.”
“Ok, Twenzetu.”
Aliyainua macho yake juu, akatazama jinsi Pangaboi lilivyokuwa linazunguka, upepo wa feni ulimpunguzia adha ya joto na mbu. Aliitazama tena barua ya Mrakibu mwandamizi wa jeshi la polisi ndugu Benard Kagasheki akatikisa kichwa kwa masikitiko. Barua ilikuwa inamtaka kutoa sababu za msingi zilizomfanya aandike barua ya kuacha kazi.
“Nitamjibu, lakini nafahamu fika kuwa anajua kwanini naacha kazi, hili jeshi limejaa dhulma, unafiki, usaliti, wizi na ujambazi. Yaani liko kinyume kabisa na yale linayoyapigania.” Aliwaza huku akiwa ameishika mkononi ile bahasha ambayo ilikuwa na muhuri pale juu ambao ulikuwa umeandikwa CONFIDENTIAL.
Ghafla kama aliyekumbuka jambo akainuka pale kitandani. Akaangalia saa ya ukutani ilikuwa ni saa 4.10.
“Muda unaruhusu.” Alijisemea kwa sauti ndogo huku akijizoazoa pale kitandani.
“Kuna kitu nilikuwa sijakamilisha na siwezi kukiachia njiani.” Aliwaza huku akifunga mlango wa chumba chake.
“Leo nikuandalie nini mama mkubwa.” Leticia mtoto wa mdogo wake alimuuliza wakati anavuka kizingiti cha nyumba.
“Sina uhakika kama nitarudi mapema lakini ningependa sana nipate ugali na samaki.” Alijibu huku akiiacha nyumba ile ambayo aliishi yeye na huyo mtoto wa mdogo wake ambaye.
Alitembea hatua kadhaa hadi barabarani ambako alikodi pikipiki iliyomfikisha kariakoo mtaa wa Muheza.
“Asante.” Alisikika dereva bodaboda baada ya kupewa pesa yake.
Aliiendea nyumba aliyoihitaji kisha akabisha mlango kama mara tatu hivi.
“Kariiibu.” Sauti ya kike ilisikika kutoka ndani.
Sekunde chache baadae mlango ukafunguliwa na mwanamke wa makamo.
“Karibu.”
“Asante, habari yako.”
“Samahani sijui naweza kumuona mwenye nyumba?”
“Hapana baba amesafiri lakini majukumu yote katuachia sisi.”
“Wewe ni mwanawe?”
“Ndiyo.”
:Unaitwa nani?”
“Mwamtumu.” Alijibu huku akionesha wasiwasi kwa mbali.
“Ok, kuna maswali mawili matatu ambayo ningehitaji majibu kutoka kwako.”
“Sawa, karibu ndani.” Inspekta akasimama huku yule dada akifunga mlango.
Akaongozana na yule dada hadi kwenye chumba kidogo ambacho kilikuwa na kitanda, viti na vyombo mbalimbali.
“Karibu.”
“Asante.” Alijibu huku akichomoa kitambulisho chake.
Mwamtumu alikiangalia kile kitambulisho kwa haraka.
“Sijui utakunywa nini!”
“Hapana nashukuru, sihitaji chochote kwa sasa.”
“Enhe, bila shaka ni kuhusu John.”
“Ndiyo umejuaje?”
“Toka ameuwawa John hapa huwa hawaishi watu wanaokuja kuuliza hili na lile kuhusu John. Tena wengine wameacha na namba zao za simu hapa .”
“wanataka nini hao walioacha namba za simu?”
“Kuna huyu mmoja ambaye amejitambulisha kuwa ni Kamishna yeye ametoa maagizo ya kupelekewa taarifa kama kuna askari yeyote atafika hapa kuulizia lolote juu ya kifo cha John.”
“Nawe umekuwa unafanya hivyo?”
“Ningekuwa nafanya hivyo iwapo ningeachiwa hela ya vocha.”
“Vizuri, kuna kitu chochote cha marehemu ambacho kilikuja kuchukuliwa na ndugu zake au yeyote yule?”
“Hapana, waliwahi kuja baadhi ya ndugu zke hapa lakini hawajachukua chochote walisema mpaka familia itakapokaa na kuamua nini kifanyike.”
“Sawa, sasa nitaomba kuingia huko chumbani kwa marehemu”
“Hakuna tatizo funguo ziko hapa, na utaongozana nami.”
Ilikuwa ni mara ya pili kwa Inspekta kuingia ndani ya chumba hiki ambacho alijikuta akiambulia kipigo kilichomsababishia kulazwa.
Alizunguka hapa na pale huku kwa umakini mkubwa akitazama mpangilio wa kila kitu mle ndani. Hakuchelewa kukiona alichohitaji. Ilikuwa ni Laptop ambayo ilivunjwavunjwa. Na kubaki ikiwa kama takataka fulani. Kwa umakini mkubwa Inspekta aliipindua ile Kompyuta pakato. Akatabasamu baada ya kukiona alichokihitaji ingawa hakuwa na uhakika na uzima wake. Hardisk ndogo ilikuwa inaning’inia nyuma ya ile kompyuta.
“Mwamtumu!”
“Abee!”
“Kuna mtu yeyote ulimuona akitoka na kamera humu ndani?”
“Hapana, isipokuwa yule anayeitwa sijui kamishna alikuja na watu fulani waliichezea ile kamera kisha kuna kitu walikichomoa humo ndani halafu wakaihifadhi kamera kwenye begi.”
“Ok, nashukuru sasa mimi naondoka na hiki (huku akionesha Harddisk) tafadhali naomba usimwambie yeyote kuwa nilikuja hapa kama kuna lolote utanifahamisha namba yangu ni hii hapa” Akampa kikaratasi kidogo ambacho kilikuwa na namba yake.
“Mh. Haya “ Alijibu Tunu ambaye kiumri hawakupishana sana na Inspekta.
Safari hii hakutokea mlango wa sebuleni badala yake alipitia mlango wa uani. Akatembea taratibu huku akiangaza macho yake huku na huko kuangalia kama anaweza kupata usafiri. Alilazimika kutembea mita mia moja ndipo alipokutana na pikipiki.
“Boda boda?”
“Ndiyo shangazi, wapi unaenda?”
“Nifikishe Kawe.”
“Ok. Usijali.”
Alipofika nyumbani kwake haraka haraka akaelekea chumbani kwake, akachuchumaa na kufungua kabati ndogo la kitandani ambalo alikuwa anahifadhi vitu vyake muhimu. Hakuchelewa kukipata alichokihitaji. Ilikuwa ni harddisk ya nje ambayo alikuwa anaitumia kuhifadhia taarifa zake nyeti. Alichokifanya ni kuiondoa ile harddisk ndani ya jumba lake na badala yake akaiweka ile harddisk aliyoichukua nyumbani kwa marehemu John Oscar.
Kisha akaiwasha kompyuta yake ya mezani ambayo ilikuwa mle chumbani.
Kwa kutumia program ya Ava find akatafuta faili la picha akalipata. John alikuwa anayapanga mafolda yake kwa tarehe na Mwezi, hivyo likawa zoezi rahisi kwa Inspekta.
Akawa anafungua picha moja baada ya nyingine nyingi zikiwa ni za lile tukio la kuuwawa kwa makamu wa Raisi. Baada ya kutembeza picha kwa dakika kadhaa ndipo alipoiona picha ambayo ilimshitua. Aliitizama kwa makini na kujikuta akitokwa na jasho kisha hofu ikamtawala.
Akainua simu yake na kupiga namba fulani.
“Shikamoo mkuu!” Baada ya kujibiwa akaanza kutoa maelezo.
Saa 11.23 Gari lililomchukua Kapteni Rose na Luteni Taisamo lilikuwa katika viunga vya nyumba ya Inspekta Tunu. Walipiga honi mara mbili kisha Inspekta Tunu akatoka na kusimama mlangoni.
“Karibuni sana.”
“asante.” Alijibu Taisamo.
“Karibuni ndani.”
“Ahsante sana.” Safari hii alijibu kapteni.
Wakamfuta hadi chumbani huku wakiwa na hamu kubwa ya kujua alichowaitia. Alikuwa hajaizima ile kompyuta hivyo macho yote yalihamia kwenye kioo hicho. Wote kwa pamoja wakazidisha umakini.
Picha hiyo ilikuwa inaonesha gari la makamu wa raisi likiwa limepinduka kwa upande mmoja huku kwa upande mwingine kukiwa na watu wawili siti ya nyuma ya gari ndogo la polisi.
Mtu mmoja alikuwa ameshika bastola ambayo alikuwa ameilenga gari ya makamu wa Raisi wakati yule mwingine alikuwa atazama tukio lile.
“Dah, huyu si kamishna?”
“Ndiye haswa.” Alijibu Inspekta na kuwafanya Taisamo na Rose watazamane.
“Ok kazi kwenu, huu ndio ulikuwa msaada wangu kwenu kama nilivyoombwa na Jenerali.”
Saa 4.33 nyumba ya kamishna ilikuwa imezungukwa na wanajeshi kumi waliopewa kazi maalum ya kuchunga nyendo za Kamishna kuanzia nyumbani kwane.
Wanajeshi wakiwa wamekata tamaa ghafla wakamuona mkuu huyo akiingia lakini safari hii ikiwa ni msafara wa magari matano. Taisamo na Rose walikuwa kwenye kundi hili .
“Ah, no… kuna tatizo kapteni.”
“Nini tena?”
“Msafara huu naona kama Rais naye yumo.”
“Kivipi, naliona gari lake binafsi.”
“sasa tufanyeje?”
“Mfahamishe Jenerali nafikiri kazi itakuwa imeishia hapa.”
Rose hakufanya ajizi akapiga simu kwa Jenerali ambaye mara moja alimfahamisha Rose kuwa yuko njiani.
“Ndo ninachompendea huyu mzee, muda wote yuko tayari kwa lolote.”
“Hawakukosea waliompendekeza kushika nafasi hii.”
Utulivu ulikuwa umetawala nyumbani kwa kamishna, kikao kama hiki kilikuwa kikifanyika hapa kwa mara ya kwanza kabisa. Kama kawaida muheshimiwa Rais au Mkuu kama alivyojulikana kwenye vikao hivi vya siri alikuwa ndiye mwenyekiti wa mkutano huu wa siri.
“Ndugu wajumbe, nafikiri hii ni mara yetu ya kwanza kukutana kwenye eneo hili baada ya wenzetu kadhaa kupoteza maisha, tulikuwa na mtandao mzuri ambao tayari umeshaanza kuvurugwa. Lakini napenda mfahamu kuwa huu sio mwisho wetu kwani kuna makosa machache ambayo yalisababisha hali hii ijitokeze, hata hivyo hatua tuliyopiga ni kubwa na ni ya ushindi kwani Muheshimiwa OLE NUNGA alikuwa kikwazo kikubwa cha mipango yetu. Leo tumekutana hapa baada ya siku mbili za majonzi ya vifo vya wapendwa wetu…………………………..” Akatulia kidogo na kumeza funda mbili za maji ya baridi kisha akaendelea. “………………..Leo nina jambo muhimu sana nataka kuwaeleza, safari hii tumeamua kijiti ashike ndugu Tobias Tambo. Huyu amekuwa na ushirikiano nzuri sana nasi na si mtu mropokaji kama mlivyomuona wakati alipokuwa waziri wa mambo ya ndani, naamini ni mtu ambaye atatulinda sisi na familia zetu, ni mtu ambaye baada ya kuambiwa kuhusu nafasi hii ameahidi kuwa atapambana na yeyote atakayejaribu kugusa zile akaunti zetu zilizoko nje ya nchi…(yakasikika makofi) hivyo nawaomba musiwe na wasiwasi bado tutaendelea kuwa na sauti na nchi hii hata kama tutakuwa nje ya madaraka (Yakapigwa makofi mengine safari hii ikiwa ni pamoja na sauti ya minong’ono)….. Nafikiri naondoka madarakani nikiwa nimefanya mambo makubwa sana kwenu mfano ni IGP hapo … ndugu zako watano wako Benki kuu hawa tu wanatosha kusaidia ukoo wenu ukiacha wale wengine ambao wako kwenye mashirika makubwa, Tumeendelea kuhakikisha kuwa tunashika nafasi katika makampuni, mashirika na taasisi muhimu….. Ni kazi kubwa nimeifanya ya kuleta mapinduzi haya ambayo yametufanya tuzishinde sera za Josi Mkulu ambaye alikuwa na mifumo ambayo ilitufanya viongozi tufanane na raia wengine. Tumejaza nafasi zote muhimu kama kuna zilizosalia basi hizo wataambulia wale wengine ambao si wenzetu, nawashukuruni nyote na nitahakikisha kama mwenyekiti wa chama mgombea wetu anashinda.” Alimaliza na kupigiwa makofi.
Ghafla, mlango wa sebule ulifunguliwa. Kikosi cha wanajeshi watano kikaibukia pale kikaoni kikiongozwa na Jenerali Nalinga.
“Muheshimiwa, tumebahatika kusikia hotuba yako yote na jambo zuri zaidi ni kuwa imerekodiwa. Kwa maslahi ya nchi na usalama wa Taifa nyote mtachukuliwa kambini, ili kuhitimisha jambo hili kistaarabu utatakiwa kufuata maelezo ambayo utapewa na jeshi, vinginevyo ni kukubali jeshi lichukue nchi nawe ushtakiwe na mahakama maalumu ya kijeshi…….” Alitulia Jenerali ambaye hakuwa na masihara. Rais muheshimiwa Herman Makwaya alikuwa anatetemeka huku jasho likimvuja. Wote wakajikuta wakiwa chini ya ulinzi na kuondoka na kikosi kile cha wanajeshi.
*
James Makabi na Tamasha walikuwa wamepumzika katika moja ya baa za maeneo ya kiwalani wakipata kinywaji baada ya kuachiwa huru kutoka chini ya uangalizi wa jeshi.
Wakati huo Runinga iliyokuwa imefungwa pale baa ilikuwa inarusha taarifa ya habari. Habari ya kwanza ndiyo ambayo iliwasisimua wengi mle ndani.
“Dar es salaam, Muheshimiwa Rais Herman Makwaya amefanya mabadiliko makubwa katika ngazi mbalimbali za uongozi hapa nchini, mabadiliko hayo ameyafanya akiwa amebakiza miezi sita tu ya kuondoka rasmi madarakani, katika mabadiliko hayo amewaachisha kazi wakuu wote wa vyombo vya ulinzi isipokuwa jeshi la wananchi na nafasi zao zitachukuliwa na watu wengine mapema mwezi ujao. Pia amemteua Inspekta Tunu Nzowa kuwa Kamishna wa makosa ya jinai, huku akiwapandisha vyeo Luteni Alex Taisamo na Kapteni Rose Mwingira ambao wote wanafikia ngazi ya Meja. Aidha muheshimiwa ametangaza kuachia nafasi ya uenyekiti wa chama, amesema kuwa kutokana na umri na hali yake ya kiafya anahitaji kupumzika sasa hivyo hatajihusisha tena na siasa katika maisha yaliyobaki…….”
“Mh, Afrika!” Aliguna huku akimshika mkono Tamasha na kuinuka pale alipokaa.
MWISHO
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;