Hekaheka Msituni Sehemu ya Pili
KIJASUSI

Ep 02: Hekaheka Msituni

SIMULIZI Hekaheka Msituni
Hekaheka Msituni Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA : KALMAS KONZO 

********************************************************************************

Simulizi : Hekaheka Msituni 

Sehemu Ya Pili (2)

“Sasa katika wiki hili nitafanya mchakato wa kuacha kazi. Kuacha kazi kwangu hakutakuwa katika mfumo wa kawaida. Kutakuwa ni kwa kutoweka tu kazini. Naamini jeshi litanisaka lakini halitanipata. Na pia ndani ya wiki hili litafanya ziara ya kuangalia ni mahali gani katika nchi hii ambapo patatufaa kuweka kambi ya jeshi letu” Kanali Edson Makoko aliongea.

“Basi sawa. Nadhani tutawasiliana kwa kila hatua” bwana Shukuru Kizibo aliongea.

SASA ENDELEA

“Jambo la msingi unatakiwa uandae magari kama matano hivi ambayo tutaanza nayo katika matumizi hapo kambini” Kanali Edson Makoko aliongea.

“Hilo ni jambo dogo sana kwangu. Idadi yoyote ya magari ambayo unayataka, utayapata” bwana Shukuru Kizibo aliongea.

Baada ya hapo wawili hawa waliendelea na mazungumzo yao ambayo yalichukua muda mrefu sana. Mazungumzo yao yalikuwa ni katika kuimarisha na kuboresha mikakati kuelekea jambo lile la uundwaji wa jeshi mpaka mapinduzi ya kijeshi ambayo watayafanya hapo siku za mbeleni.

Bwana Shukuru Kizibo alionekana ni mtu mwenye furaha sana kukutana na Kanali Edson Makoko na kufanya naye mazungumzo. Aliona kama mipango yake inaelekea kutimia kwa urahisi kabisa tofauti na vile ambavyo alidhani hapo awali. Hii ilimpa chachu ya kuendelea kusonga mbele na michakato ya uundwaji wa jeshi.

********

BAADA YA MIAKA MIWILI

Kikundi cha waasi Cha Bantu Military Movement (BMM) kwa sasa kilikuwa kimekuwa. Kilikuwa ni kikundi ambacho kilikuwa na jeshi kubwa sana kwa sasa. Kilikuwa kikiendesha jharakati zake za uasi kutoka katika misitu ya Masolo misitu mikubwa ambayo ilikuwa ikipatikana kusini mwa nchi ya Bantu.

Serikali ya Bantu chini ya Rais Ditrick Mazimba ilikuwa ikijaribu kupambana na kikosi hiki pasi mafanikio ya kukiangamiza. Kilikiwa ni kikundi ambacho kilikuwa na nguvu sana. Kilikuwa kimejiimarisha kila mahali kuanzia silaha, chakula mpaka huduma za afya. Kikundi hiki kilizidi kuwa tishio kadri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele.

Kanali Edson Makoko alizidi kupata umaarufu mkubwa sana kwani ilisemekana ndiye aliyekianzisha kikundi hiki mara baada ya kulisaliti jeshi la wananchi wa Bantu kuacha kazi na kuacha kazi na kutorokea katika misitu ya Masolo.

Lakini iliaminika kwamba mbali na Kanali Edson kuwa kiongozi wa kikundi hiki, lakini kulikuwa na mkono wa mtu mkubwa mwenye pesa ambaye alikuwa akikifadhili kikundi hiki. Lakini hakuna mtu yeyote ambaye alikuwa akifahamu mfadhili wa kikundi hiki. Watu wengine walifika mbali kwa kuwaza.

Walihisi huenda kulikuwa na nchi fulani huko Ulaya ambayo ilikuwa ikikifadhili kikundi hiki kwa silaha na huduma mbalimbali. Hakuna hata mmoja aliyefahamu kwamba bwana Shukuru Kizibo ndiye ambaye alikuwa mfadhili mkuu wa kikundi hiki.

Bwana Shukuru Kizibo alikuwa na furaha muda wote kadri alivyokuwa akiyaona maendeleo na mafanikio ya kikundi hiki. Aliona kama ndoto zake za kuwa Rais wa Bantu zilikuwa jirani sana kutimia. Aliamini kwamba alikuwa jirani kabisa katika kuishangaza dunia na kuifanya isiamini kile ambacho itakuwa ikikishuhudia.

Kwa upande wake Kanali Edson Makoko alikuwa na furaha kubwa sana pengine kumpita hata bwana Kizibo. Hii hasa ni kwa sababu ndoto zake za kuwa na pesa pamoja na nguvu zilikuwa zimetimia. Mpaka sasa alikuwa amekwishamchota bwana Shukuru Kizibo pesa nyingi sana.

Bwana Shukuru Kizibo yeye kwa upande wake hakuwa akifahamu kwamba alikuwa akihujumiwa na Kanali Edson Makoko. Yeye alimwamini mwanajeshi huyu muasi kwa kiwango chote cha uaminifu. Alikwishausahau ule usemi wa wahenga usemao ‘Kikulacho ki nguoni mwako’

Yalikuwa ni majira ya usiku bwana Shukuru Kizibo alikuwa amejaa tele nyumbani kwake. Alikuwa ametulia yeye na familia yake wakiyafurahia maisha. Bwana Kizibo alikuwa na familia ya mke na watoto watatu.

Bwana Shukuru Kizibo aliipenda sana familia yake. Alitaka muda wote iishi maisha ya raha mustarehe. Hakutaka ipate shida hata kidogo. Jambo hili ndilo ambalo lilimfanya kila uchao azidi kupambana katika miradi yake ili aweze kuingiza pesa nyingi sana.

Bwana Shukuru Kizibo alipata ugeni ambao hakuutaraji. Ugeni huu ulikuwa ni wa Kanali Edson Makoko. Nasema ugeni huu hakuutaraji kwa sababu, kwa siku ile hakuwa na miadi kabisa ya kukutana na Kanali Edson Makoko. Alichofahamu ni kwamba Kanali Edson Makoko alikuwa msituni akiendelea na shughuli zake za kijeshi.

“Karibu sana bwana Makoko!” bwana Shukuru Kizibo alimkaribisha Kanali Edson Makoko katika chumba chake cha mazungumzo kwa kumpa mkono na kasha kumwonyesha mahali pa kuketi.

“Nashukuru sana bwana Kizibo. Vipi hali yako pamoja na familia?” Kanali Edson Makoko alijibu na kusabahi.

“Sisi tuko salama kabisa. Mungu anazidi kutupigania” bwana Shukuru Kizibo alijibu.

“Vipi, naona leo umenitembelea kwa ghafla pasi miadi. Vipi kwema kweli huko kambini?” bwana Shukuru Kizibo aliongea akiuliza.

“Huko kwema kabisa bwana Kizibo. Ondoa shaka kabisa kwani kila kitu kipo salama kabisa” Kanali Edson Makoko alijibu.

“Nafurahi kusikia hivyo. Haya nipe maneno rafiki yangu. Shughuli zinaendaje huko?” bwana Shukuru Kizibo aliuliza.

“Shughuli zinaenda vema kabisa. Jeshi linazidi kuwa imara na tishio kabisa kwa serikali. Yaani kwa sasa serikali inakosa kabisa usingizi kwa kutuhofia. Na hili ni jambo jema kabisa katika kuelekea mafanikio ya adhma yetu” Kanali Edson Makoko aliongea.

“Sawasawa, hizo ni habari njema kabisa kuzisikia” bwana Shukuru Kizibo aliongea.

“Sasa bwana Shukuru Kizibo, mimi na wewe tumetoka mbali sana. Tumeshirikiana mambo mengi sana katika michakato yetu. Umekuwa msaada mkubwa sana mpaka hapa tulipofikia. Ninapaswa kukushukuru sana kwa hilo” Kanali Makoko aliongea na kumtazama bwana Shukuru Kizibo usoni.

“Usijali bwana Makoko kwani jambo hili ni la kwetu sote” bwana Shukuru Kizibo alijibu.

“Sasa bwana Kizibo, mimi nimekuja kukuaga na kukutakia safari njema” Kanali Edson Makoko aliongea maneno ambayo yalikuwa ni magumu sana kwa bwana Shukuru Kizibo kuyaelewa.

“Una maana gani bwana Makoko? Umepata wapi taarifa kwamba mimi nasafiri? Mbona mimi sina ratiba ya kusafiri kwa sasa?” bwana Shukuru Kizibo aliuliza kwa mshangao.

“Ni kweli bwana Kizibo lakini ratiba yaw ewe kusafiri nimeitengeneza mimi. Na nimekuja hapa kwako kwa ajili ya kukusafirisha!” Kanali Edson Makoko aliongea.

“Unasemaje bwana Makoko?” bwana Shukuru Kizibo aliuliza.

Bwana Shukuru Kizibo hakulipata jibu la swali lake kwani alijikuta akitazamana na mtutu wa bastola ambao ulikuwa umeelekezwa katika paji lake la uso.

“Unasemaje bwana Makoko?” bwana Shukuru Kizibo aliuliza.

Bwana Shukuru Kizibo hakulipata jibu la swali lake kwani alijikuta akitazamana na mtutu wa bastola ambao ulikuwa umeelekezwa katika paji lake la uso.

SASA ENDELEA

“Hapana bwana Makoko, huwezi nifanyia hivi” bwana Shukuru Kizibo aliongea.

“Pole sana bwana Shukuru Kizibo. Ninahitaji sana pesa, mali, umaarufu pamoja na cheo. Uwepo wako utakuwa ni kikwazo katika kufanikisha adhma yangu. Uliyoyafanya mpaka sasa kwa nafasi yako yanatosha. Sasa unapaswa kusafiri na uniache mimi hapa duniani nikiendelea kuyafaidi maisha” Kanali Edson Makoko aliongea kwa tambo.

“Hapana bwana Edson. Usifanye hivyo tafadhali. Kama wataka pesa mimi nitakupa kiasi chochote ukitakacho!” bwana Shukuru Kizibo aliongea.

“Hapana bwana Shukuru. It’s too late to decide. Maamuzi na mipango hii nilikwishaipanga muda mrefu sana!” Kanali Edson Makoko alijibu.

Bwana Shukuru Kizibo alibaki ameyatumbua macho yake. Hakuamini kile ambacho kilikuwa kikitokea. Alijihisi kama yuko ndotoni. Alijilaumu sana kwa kumwamini mwanajeshi huyu ambaye alikuwa ni hatari kama nyoka.

Alichobaki kukifanya kwa muda ule ni kumwomba mwenyezi Mungu amwepushe na kikombe kile ambacho kilikuwa ni kigumu sana kukinywa. Hakufahamu kama alikuwa na uwezo zaidi wa kumshawishi Kanali Edson Makoko kuyabatilisha mawazo yake.

Risasi moja ambayo ilitoka katika bastola ile yenye kiwambo cha kuzuia sauti ya Kanali Edson Makoko ilipenya katika paji la uso la bwana Shukuru Kizibo. Risasi ile ilitokeza nyuma ya kichwa na kukifumua kabisa kisogo cha bwana Shukuru Kizibo. Mwili wa bwana Shukuru Kizibo ulidondokea juu ya meza.

Baada ya hapo Kanali Edson Makoko alikichomoa kisu chake kikali kutoka katika ala yake na kuikatakata shingo ya bwana Shukuru Kizibo.

Alipotoka hapo Kanali Edson Makoko alienda mpaka sebuleni ambako familia ya bwana Shukuru Kizibo ilikuwa imetulia ikitazama televisheni. Huko nako Kanali Edson Makoko alifanya mauaji ya kutisha nay a kinyama sana. Aliikatakata miili ya wanafamilia wale na kuitenganisha vichwa na viwiliwili vyake. Hakika hali ilikuwa inatisha sana katika jumba la tajiri Shukuru Kizibo.

Baada ya kuridhishwa na mauaji ambayo alikuwa ameyafanya, Kanali Edson Makoko alitoweka kutoka katika eneo lile huku akiwa ameyabeba mabegi kadhaa ambayo yalikuwa yamejaa fedha. Pesa hizi zilikuwa ndani ya jumba lile la marehebu Shukuru Kizibo.

******

Mauaji ya bwana Shukuru Kizibo na familia yake yaliishtua nmchi nzima ya Bantu. Watu wengi walishangaa kwa mauaji ya kikatili kama yale kufanywa na binadamu. Mauaji yale yalivihangaisha sana vyombo mbalimbali vya usalama mchini Bantu kujua sababu hasa ya mauaji yale.

Iliaminika huenda ulikuwa ni uhasimu wa kisiasa ndiyo ambao ulipelekea mauaji yale. Lakini wengine waliamini kwamba bwana Shukuru Kizibo kama mfanyabiashara mkubwa wa kimataifa, alikuwa na maadui wengi katika biashara zake. Huenda alikuwa amedhulumiana na mfanyabiashara mwenzake ambaye aliamua kulipa kisasi kwa kutekeleza mauaji yale.

Lakini zote hizo zilikuwa ni hisi tu. Hakuna upande hata mmoja ambao ulikuwa na jibu sahihi. Siri ya vifo vile alibaki nayo marehemu Shukuru Kizibo pamoja na Kanali Edson Makoko.

Msiba ule ulilitingisha Taifa zima la Bantu kwa sababu bwana Shukuru Kizibo alikuwa ni mtu mkubwa sana katika medani za siasa. Pia alikuwa na umaarufu mkubwa sana katika sekta ya biashara. Hivyo umaarufu wake ulikuwa umetapakaa Bantu nzima na kuvuka mipaka yake.

Wafuasi wa chama chake cha siasa waliomboleza sana. Waliona kama wamepata pengo kubwa sana ambalo lilikuwa ni vigumu sana kuzibika. Bwana Shukuru Kizibo alibaki kuwa ni mtu wa kukumbukwa katika historia ya chama chake.

Serikali ya Bantu nayo iliumizwa na vifo vile kwa sababu bwana Shukuru Kizibo alikwua na umuhim mkubwa sana katika medani za siasa ya Bantu. Pia Taifa lilikuwa limepoteza nguvu kazi kwani bwana Shukuru Kizibo alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa sana ambapo biashara zake zilikuwa zikiingizia nchi kipato kikubwa sana. Hivyo msiba huu ulikuwa umegusa kila kona miongoni mwa wananchi na nchi nzima ya Bantu kwa ujumla.

*******

“BMM oyeeee!” Kanali Edson Makoko aliongea kwa nguvu.

“Oyeeeeee!” wanajeshi walijibu wakizinyanyua bunduki zao juu.

Hii ilikuwa ni katika paredi ambayo ilikuwa imeitishwa katika kambi ya BMM huko katika misitu ya Masolo.

“Kama ambavyo mmesikia ni kwamba, mzee wetu bwana Shukuru Kizibo pamoja na familia yake wameuawa kikatili sana. Hili ni pigo kubwa sana kwetu kwani mzee yule alikuwa ndiye mfadhili wetu mkubwa!” Kanali Edson Makoko alitulia na kuwatazama wanajeshi wake ambao walikuwa wamejawa na nyuso za huzuni.

“Ninaamini na ninafahamu kwamba mauaji haya yamepangwa na kutekelezwa na Rais Ditrick Mazimba kwa sababu ndiye alikuwa hasimu wake mkubwa. Nadhani leo ndiyo mmeuona unyama ambao Rais huyu anao!”

Kanali Edson alizidi kutema cheche akimchafua Rais Ditrick Mazimba ndani ya fikra za wanajeshi wale. Kwa kifupi wanajeshi wale walikuwa wakilishwa sumu mbaya nay a hatari sana ya kuichukia serikali yao. Kanali Edson Makoko alikuwa anajua sana kucheza na saikolojia ya wanajeshi wale.

“Sasa je, kuuawa kwa bwana Shukuru Kizibo ndiyo iwe mwisho wa harakati zetu za kuhakikisha tunaichukua dola?” Kanali Edson Makoko aliuliza kwa mzuka mkubwa.

“Hapanaaaa! Haiwezekani kabisaaaaaa!” wanajeshi wale walijibu kwa umoja kwa jazba kubwa sana.

“Nami nawaunga mkono kwa kusema haiwezekani. Nitawaongoza nma nitahakikisha tunampindua Rais mnyama na shetani Ditrick Mazimba. Kifo cha mlezi na mfadhili wetu ni lazima kilipwe!” Kanali Edson Makoko alifoka kwa jazba huku wanajeshi wakishangilia kwa kuzinyanyua silaha zao juu.

“Hatuna sababu ya kuendelea kumwacha shetani huyu akivuta hewa ya dunia hii kwa raha mustarehe wakati ndani yake amejaa ushetani kwa kutokomeza roho za watu wasio na hatia!” Kanali Edson aliongea.

“Lazima auawe! Tunataka Bantu mpyaaaa!” wanajeshi wale walipiga kelele wakimshangilia sana Kanali Edson Makoko.

Wanajeshi wale hawakuifahamu siri ambayo ilikuwa nyuma ya pazia. Hawakufahamu kwamba kiongozi wao huyu ambaye alikuwa mbele yao ndiye ambaye alikuwa anahusika na mauaji yale. Laiti wangelifahamu hilo, kamwe wasingebaki pale kumsikiliza mahubiri yake. Ni lazima wangeanzisha vurugu kubwa sana.

Lakini Kanali Edson Makoko alikuwa na akili kubwa sana. Alikuwa amesajili watoto katika jeshi lake ili iwe rahisi kwake kuuteka ufahamu wao. Alichofanya ni kuupandikiza ukatili ndani ya vichwa na mioyo yao. Aliwalisha sumu ya ukatili dhidi ya binadamu. Kadri walivyozidi kuwa wakubwa basi walizidi kuwa ni watu wa hatari sana ambao walikuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yoyote ya kikatili pasi kusita.

******

Lakini Kanali Edson Makoko alikuwa na akili kubwa sana. Alikuwa amesajili watoto katika jeshi lake ili iwe rahisi kwake kuuteka ufahamu wao. Alichofanya ni kuupandikiza ukatili ndani ya vichwa na mioyo yao. Aliwalisha sumu ya ukatili dhidi ya binadamu. Kadri walivyozidi kuwa wakubwa basi walizidi kuwa ni watu wa hatari sana ambao walikuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yoyote ya kikatili pasi kusita.

SASA ENDELEA

Rais Ditrick Mazimba alikuwa ni Rais kipenzi cha watu wengi sana nchini Bantu. Alikuwa ni Rais ambaye alifanikiwa kuwaunganisha wanabantu na kuwafanya kuwa kitu kimoja. Alikuwa ni Rais ambaye alikuwa ameleta upendo, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi. Rais Ditric Mazimba alikuwa ni Rais ambaye alipinga sana ufisadi na aliapa kupambana nao mpaka tone lake la mwisho la jasho lake.

Pia Rais Ditrick Mazimba aliwawajibisha viongozi na watumishi wote wa serikali ambao walikiuka katiba ya nchi na kuamua kwenda kinyume nayo. Jambo hili lilisababisha Bantu kuanza kufikia mapinduzi makubwa sana ya kiuchumi ambayo haikuwahi kufikia hapo awali.

Rais Ditrick Mazimba alikuwa ametenga miezi miwili ya kufanya ziara katika nchi nzima ya Bantu. Katika kipindi hicho cha miezi miwili aliamini kwamba atakuwa ametembelea kila eneo katika nchi ya Bantu. Na kwa sasa alikuwa amekwishaianza ziara yake.

Katika ziara hii alikuwa akiwatembelea wananchi wa Bantu na kusikiliza kero zao ambazo zilikuwa zikiwakabili. Hii ilikuwa ni kawaida kabisa kwa mheshimiwa Rais Ditrick Mazimba kufanya hivi kila baada ya kipindi fulani. Jambo hili lilimuongezea thamani Rais huyu mbele ya wananchi. wananchi waliona kwamba alikuwa ni Rais ambaye alikuwa akiwajali sana.

“Eneo hili la Matutu halina mahali pazuri penye hadhi na usalama wa kulala Rais. Labda mpaka katika eneo la Soweni mji unaofuata kutoka mji huu” mkuu wa Wilaya ya Soweni alikuwa akiongea na maafisa usalama ambao walikuwa katika msafara ule wa Rais.

“Pana umbali gani kutoka hapa?” afisa usalama mmoja aliuliza.

“Ni takribani kama saa moja na nusu!” mkuu wa wilaya alijibu.

“Tutafika usiku” afisa mwingine alichangia. :Hakika, lakini hii si nzuri” afisa mwingine naye aliongea.

“Basi tunaomba ufanyike utaratibu wa kuhakikisha kwamba mahali salama panaandaliwa” afisa usalama mmoja aliongea.

“Usijali. Mahali pako salama na pia pako tayari muda wote!” mkuu wa wilaya aliongea.

Kwa wakati ule yalikuwa ni majira ya saa kumi na mbili za jioni. Magari ya msafara wa Rais yalikuwa yakizidi kutimua vumbi kwa mwendo wa kasi sana. Walitaka wahakikishe kwamba wamefika Soweni kabla masaa hayajaenda sana na giza halijawa zito sana. Madereva ambao walikuwa wakiyaendesha magari yale walikuwa ni mafundi hasa katika udereva. Walikuwa wakijua kuyamudu magari yao ambayo yalikuwa yakirindima vilivyo juu ya barabara.

*******

Msafara ule ulifika salama katika mji wa Soweni. Mji huu ulikuwa umechangamka na ndiyo yalikuwa makao makuu ya wilaya ya Soweni.moja kwa moja mkuu wa wilaya aliuongoza msafara ule mpaka katika ikulu ndogo mahali ambapo mheshimiwa Rais angelala.

Ulinzi ambao ulikuwa mahali hapa ulikuwa ni mzito sana. Maafisa usalama na walinzi mbalimbali walikuwa wametapakaa kila kona ya ikulu hii ndogo mjini Soweni. Hii yote ilikuwa ni katika kuhakikisha suala zima la usalama linaratibiwa na kutekelezwa vema kabisa.

Inchaji wa ulinzi na usalama katika alikuwa akitembelea kila kona ya ikulu ile kuhakikisha kwamba mambo yalikuwa yanakwenda sawa sawia. Askari huyu alikuwa makini sana katika utendaji wa kazi yake.

Nje ya chumba ambacho alikuwemo Rais palikuwa na walinzi wawili. Ndani ya chumba ambacho Rais alikuwemo kulikuwa na mlinzi mmoja ambaye alikuwa akihakikisha usalama kwa kiongozi huyu wan chi unakuwa sawa.

Yalikuwa ni majira ya kuelekea saa nne za usiku, askari walinzi pale nje ya chumba alimokuwemo mheshimiwa Rais Ditrick Mazimba walitazamana na kukonyezana.

ITAENDELEA

Hekaheka Msituni Sehemu ya Tatu

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment