Hisoria ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda Sehemu ya Tatu
KIJASUSI

Ep 03: Hisoria ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda

SIMULIZI Hisoria ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda
Hisoria ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda Sehemu ya Tatu

IMEANDIKWA NA: THE BOLD

*********************************************************************************

Simulizi: Hisoria ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda

Sehemu ya Tatu (3)

Ndipo hapa ambapo Paul Kagame akaona fursa. Kwamba ‘vita ya panzi, furaha ya kunguru’.

Yoweri Museveni yeye hatokei Kusini wala Kaskazini mwa Uganda… yeye amezaliwa na kukulia eneo la magharibi mwa nchi linalopakana na Rwanda sehemu inaitwa Ntungamo. (Hii ni moja ya sababu ya baadhi ya watu kuamini ana asili ya Kitusi).

Kwa hiyo huu ugomvi wa watu wa kaskazini na wa kusini haukuwa na mslahi nao kabisa. Ndipo hapa kwa kushauriana na Paul Kagame wakaanza michakato ya siri pembeni ya kujitenga na NCC na UNLA japokuwa Museveni alikuwa na ushawishi kwenye vyombo vyote hivyo.

Hatimaye mwaka 1980 Milton Obote alirejea Uganda na kushiriki kwenye uchaguzi mkuu mwaka huo na “kushinda”. Matokeo ya uchaguzi yalipingwa vikali na watu wengi akiwemo Yoweri Museveni.

Ndipo hapa ambapo Yoweri Museveni, Pual Kagame na Fred Rwigyema pamoja na Waganda wengine thelathini na saba tu walianzisha kikundi chao cha kijeshi walichokiita National Resistance Army (NRA) lengo kuu likiwa ni kumuondoa madarakani Rais mpya Milton Obote.

Kikundi hiki kiliendesha mapigano ya msituni dhidi ya majesho ya serikali kwa karibia miaka sita.

Licha ya udogo wake kwa idadi ya watu (japo baadae waliongezeka kuzidi watu arobaini wa awali) lakini ufanisi wao kwenye kushambulia kwa uhodar na kulichosha jeshi la serikali ulikuwa wa hali ya juu. Miaka hii sita ya kupambana na majeshi ya serikali yalidhihirisha namna ambavyo Paul Kagame alikuwa ni nguli wa ‘psychological warfare’ ambayo pia ilikuja kudhihirika kipindi cha mauaji ya kimbari (tutaongelea zaidi tukifika hapo).

Katika kipindi hiki cha vita kwa masuala ya kijeshi Paul Kagame alikuwa mtu muhimu na mwenye kuheshimika zaidi na wapiganaji wa NRA kuzidi hata Museveni mwenyewe. Nyadhifa zao ndani ya NRA zilikuwa karibia kwenye usawa mmoja.

Kwa upande wa jeshi la serikali hali ilianza kuwa tete. Kukaanza kutokea mifarakano ya kikabila kati ya wenyewe kwa wenyewe. Kaskazini mwa Uganda kuna makabila makuu mawili, Walangi (kabila wanalotokea Obote na Ojok) na Waacholi (kabila la Tito Okello ambaye kwa kipindi hicho alikuwa kamanda wa jeshi).

Askari wengi wa miguu walikuwa ni Waacholi na ndio ambao walikuwa wanakufa zaidi kwenye vita hiyo dhidi ya NRA. Walangi wengi walikuwa ni maafisa wa jeshi na ‘Special Forces’. Kwa hiyo askari wa miguu wakaanza kushinikiza serikali ifanye mazungumzo na NRA na kumaliza vita.

Jeneralu David Oyite Ojok

Yoweri Museveni na wapiganaji wa NRA msituni

Serikali ikafanya shingo ngumu na kukataa.

Wanasema lakuvunda halina ubani, mwezi Desemba 1983 Oyite Ojok alifariki kwa ajali ya ndege ambayo kuna kila dalili ya mkono wa Kagame. Kwa kipindi hicho Ojok ndiye alikiwa mkuu wa jeshi la Uganda. Ilikuwa inategemewa Obote amteue Tito Okello au mwenzake mwingine aliyeitwa Bazilio Olara-Okello (hakuna undugu wa damu kati yao licha ya kufanana ubini japo wanatokea kabila moja la Waacholi) ambaye naye alishiriki vita ya kumuondoa Idd Amin. Lakini ajabu Obote alimteua afisa wa chini kabisa wa jeshi aliyeitwa Smith Apon-Achak ambaye anatoka kabila lake la Walangi kuchukua nafasi ya Oyite Ojok.

Hii iliwafanya wanajeshi wenye asili ya kabila la Waacholi kumchukia Obote na serikali yake na hatimaye miaka miwili baadae kumpindua kutoka madarakani.

Baada ya Miltob Obote kupinduliwa na jeshi kutoka madarakani kukaanza mapigano baina ya vikundi vya msituni kila kimoja kikitaka kushika usukani wa kuongoza nchi. Ndipo hapa yalifanyika maongezi ya pamoja baina ya vikundi vyote vya msituni nchini Kenya chini ya Rais Daniel Arap Moi ili kuleta suluhu na kuweka muelekeo mpya wa nchi ya Uganda.

Tarehe 29 January mwaka 1986 Yoweri Kaguta Museveni akaapishwa kuwa Rais mpya wa Uganda.

Paul Kagame akateuliwa na Rais kuwa Chief of Millitary Intelligence.

Swahiba wake Fred Rwigyema akateuliwa kwenye wadhifa wa Waziri wa Ulinzi.

Pia baraza la mawaziri lilikuwa limejaa watusi kibao.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa Paul Kagame alikuwa ameiweka Uganda kwenye kiganja chake cha mkono japo hakuwa Rais. Lakini mtandao wa ushawishi ambao alikuwa ameujenga ndani ya serikali ya Uganda, baraza la mawaziri na kwenye jeshi ulikuwa ni mkubwa na una nguvu zaidi hata ya Yoweri Museveni ambaye aliapishwa kuwa Rais. Uzuri ni kwamba Museveni anafahamu umahiri wa Paul Kagame na hakutaka kutengeneza mvutano wowote naye kwa kuwa alikiwa anajua lengo kuu la Kagame lilikuwa ni lipi. Kagame hakuwa na nia yoyote ile ya kuwa Rais wa Uganda au kuendelea kuliendesha jeshi la Uganda. Ndoto yake ilikuwa ni moja tu, ndoto ambayo aliipata mwaka 1978 alipotembelea kwa siri nchi yake ya Rwanda, kwamba siku moja anataka kuwaokoa ndugu zake watusi kutoka kwenye unyanyasaji, kuuwawa, kudhalilishwa na mateso ambayo walikuwa wanapitia katika nchi yao.

Na sasa alikuwa amekamilika kwa kila kitu. Alikuwa na uzoefu wa kutosha. Alikuwa na weledi wa kutosha, tunaweza kuthubutu kusema kwamba katika kipindi hiki hakuna ambaye alikuwa anaweza kufikia daraja la umahiri wa Kagame katika masuala ya Ujasusi Afika Mashariki yote.

Lakini pia alikiwa na ushawishi katika nchi za kimakakati ambazo zinapakana na Rwanda, kwa maana ya Congo (huku aliwapeleka wapiganaji wa NRA kupata mafunzo ya siri ya Special Forces kipindi cha mapigano ya miaka 6 msituni dhidi ya majeshi ya serikali ya Milton Obote). Lakini pia alikuwa na ushawishi nchini Tanzania (mtoto wetu tuliyemfunza wenyewe ujasusi na alitusaidia sana kwenye vita ya Kagera). Na hakuna haja hata ya kusema kiwango cha ushawishi ambacho alikuwa nacho nchini Uganda.

Mbele yake kulikuwa na jambo moja tu la mwisho ambalo alikuwa anatamani litimie kabla hajaondoka juu ya uso wa dunia. Kuiweka nchi ya Rwanda mkononi mwake.

ad22e730eeb86328bc2ed0aa239bf97a.jpg

Siku ya kuapishwa Yoweri Kaguta Museveni kuwa Raia mpya wa Uganda Tarehe 29, January 1986

Fred Rwigyema

Paul Kagame

Itaendelea….

SEHEMU YA SITA

Katika sehemu iliyopoita nilieleza namna ambavyo Watusi, Paul Kagame, Fred Rwigyema na wenzake walivyoingia kwenye vikundi vya kijeshi chini ya Museveni na kushiriki vita ya Kagera na baadae kushiriki katika kumuondoa madarakani Rais Milton Obote.

Katika sehemu hii ya sita nataka tuangalie namna ambavyo moto wa mauaji ya Kimbari ulivyowaka na hatimaye tuangalie namna ambavyo Paul Kagame ameibuka kuwa mtu mwenye nguvu zaidi kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Ukanda wa maziwa makuu.

Ili kuelewa namna ambavyo mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yalivyoanza ni vyema kwanza kuelewa namna ambavyo RPF (chama tawala cha sasa nchini Rwanda chini ya Paul Kagame) ilizaliwa na kubadilika kutoka kuwa umoja wa wanaharakati na baadae kuwa kikindi cha kijeshi na sasa chama cha siasa

Turudi nyuma kidogo….

Baada tu ya Milton Obote kushika nchi kupitia uchaguzi ambao ulikuwa na utata mkubwa mwaka 1980 na hatimaye Yoweri Museveni kujitenga naye akishutumu uchaguzi kutokuwa wa haki na kuanzisha kikundi chake cha National Resistance Army, Milton Obote mara moja alianzisha kampeni ya kukipiga vita kikundi hicho kwa nguvu ya jeshi lakini pia kwa propaganda akishutumu kuwa kikundi hicho kiko chini ya “Banyarwanda” (watu wa Rwanda) na si raia wa Uganda.

Hii ilipelekea mwaka 1982 serikali ya Milton Obote kulazimisha Watusi wote waliopo nchini Uganda kuwa wanapaswa kuishi kwenye kambi za wakimbizi pekee na si mitaani kama raia.

Ikumbukwe kwamba Watusi wamekuwa wakiikimbia Rwanda tangu miaka ya 1960s, hivyo wengi wao walikuwa wamelowea Uganda, Congo na hata Tanzania na kufikia hatua ya kuishi maisha ya kawaida uraiani kama raia wengine wa nchi hizo. Kwa hiyo kitendo cha Milton Obote kutangaza kwa hakuna Mtusi anayeruhusiwa kuishi uraiani isipokuwa kwenye kambi za wakimbizi pekee ilizua taharuki kubwa sana.

Watusi wote ambao walikuwa bado wanajificha na kuendelea kuishi uraiani, walikamatwa na kufungwa na wengine kuuwawa.

Hata kwenye kambi za wakimbizi zenyewe nako Obote aliweka mashushushu ambao waliwakamata Watusi ambao walionekana kuwa na misimamo mikali kupinga serikali yake au kumuunga mkono Museveni na kikundi chake cha NRA na kisha kuwatia jela na wengi wakipotezwa kusikojulikana.

Hii ilipelekea kuibuka kwa wimbi la wakimbizi wa Kitusi wapatao 40,000 kukimbia Uganda na kurudi Rwanda. Ubaya zaidi walipofika Rwanda kutokana na wakimbizi hawa kiwa Watusi serikali ya Rais Juvenile Habyarimana ilitangaza kuwatambua watu 4000 pekee kati ya wote 40,000 waliorejea.

Kati ya hao waliobaki na kukataliwa kurejea Rwanda, serikali ya Uganda chini ya Milton Obote ikatangaza kwamba itawachukua wakimbizi 1000 tu.

Kwa maana hiyo walisalia watu 35,000 katikati ya mpaka wa Rwanda na Uganda wakiwa hawana kwa kwenda. Rwanda nyumbani kwao serikali ilisema haiwatambui, na Uganda ambako waliishi kwa miaka kadhaa nako serikali ilisema haiwataki tena na haiko tayari kuwaruhusu kuingia. Kwa hiyo wakabaki kwenye ombwe la sintofahamu kubwa.

Kama nilivyoeleza huko nyuma kwamba Paul Kagame ni ‘born tactician’ anajua ku-capitalise katika mazingira yote. Yaani anajua kuona fursa katika kila mazingira na muda mwingine hata kushawishi mazingira yatengeneze fursa.

Wanyarwanda hawa 35,000 ambao walisalia mpakani wakikataliwa na nchi yao ya Rwanda na ugenini Uganda walikaa mpakani kwa kipindi kirefu sana. Ndipo hapa Paul Kagame akaanzisha programu maalumu za propaganda na kushawishi vijana wa Kitusi walioko pale mpakani (kati ya wale 35,000) kujiunga na NRA ya Museveni ambaye yeye na Fred Rwigyema walikuwa ni waanzilishi wake wakishirikiana na Museveni.

Nieleze pia jambo lingine muhimu…

Wakati haya yote yanaendelea, ikumbukwe kwamba tangu mwaka 1979 baada tu ya Idi Amin kupinduliwa kutoka madarakani, Watusi wote walioko Uganda walianzisha taasisi yao iliyoitwa Rwandese Alliance For National Unity (RANU). Hii ilikuwa ni taasisi ya kwanza ya kisiasa kuwa chini ya ‘wakimbizi’ Afrika Mashariki. Lengo kuu la Taasisi hii ilikiwa ni kuratibu mipango ya kurejesha watusi wote nchini Rwanda kwa amani.

Turejee tena kwenye kile nilichokuwa naeleza…

Vijana wa Kitusi ambao walikuwa mpakani pamoja na wale wengine 35,000 wakashawishiwa kujiunga na NRA ya akina Museveni, Rwigyema na Kagame.

Nilieleza kwa uzuri kabisa namna ambavyo Milton Obote aliondolewa madarakani na NRA… sasa mpaka mwaka 1986 ambapo Milton Obote alitolewa madarakani, NRA ililuwa na wapiganaji wapatao 16,000 na nusu yao walikuwa ni Watusi.!

NRA ikashika nchi, Museveni akawa Rais, Fred Rwigyema Waziri wa Ulinzi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu, na Paul Kagame Mkuu wa Intelijensia ya Jeshi na Watusi wengi kupata nyadhifa za juu na nyeti katika jeshi na serikali ya Uganda.

Paul Kagame na Fred Rwigyema walitumia ushawishi wao na kuifanya serikali ya Museveni kutangaza kuwapokea tena Watusi wote ambao walisalia pale mpakani kutokana na kukataliwa na Rwanda na serikali ya Milton Obote. Lakini pia serikali ya Uganda ilitangaza kwamba Watusi wote ambao wamekaa Uganda kwa miaka 10 au zaidi watapatiwa uraia.

Huu ulikuwa ni moja kati ya wakati wa raha zaidi kwa Watusi. Ilikuwa ni neema kubwa. Shukrani zao japo zilikwenda kwa serikali la Uganda lakini shukrani za dhati na zaidi zilikwenda kwa vijana wao Paul Kagame na Fred Rwigyema kwa kufanikisha kuileta Neema hii.

Fred Rwigyema na Paul Kagame wakageuka kuwa mashujaa katika jamii ya Watusi.

Sasa basi…

Ile RANU ambayo nimeeleza hapo awali huwa ilikuwa inafanya Kongamano kuu kila mwaka kujadili uratibu wa mikakati ya kurejea tena Rwanda.

December mwaka 1987 likafanyika Kongamano kuu la saba la RANU jijini Kampala. Katika Kongamano hilo Fred Rwigyema akachaguliwa kiongozi wa taasisi hiyo na Paul Kagame akiwa Makamu wake.

Nafasi nyingine zote za uongozi na nafasi za kiutendaji waliwekwa maveterani ambao walipigana katika vita za kumng’oa Idi Amin na kumng’oa Milton Obote.

Kwa hiyo kufumba na kufumbua RANU ilibadilishwa kutoka kuwa taasisi ya kisiasa na kuwa chombo cha kijeshi. Na Rwigyema na Kagame hawakuishi hapo tu bali waliibadilisha jina RANU na kuwa Rwanda Patriotric Front (RPF).

Kwa hiyo ilikuwa rasmi sasa kwamba Paul Kagame na Fred Rwigyema walikuwa na misuli ya kijeshi kufanya kile ambacho walikuwa wanakiota tangu wangali watoto.

Walikuwa na maelfu ya vijana wa kitusi mikononi mwao ambao walikuwa na weledi wa kutosha wa kijeshi kutoka NRA ya Museveni na kwa sasa waliwasajili chini ya kikundi chao kipya cha RPF.

Sasa ulikuwa muda sahihi kabisa wa kwenda kuiweka Rwanda kwenye kiganja cha mikono yao na kuisuka upya vile ambavyo walihisi ni sahihi.

Fred Gisa Rwigyema

Yoweri Museveni

Jaribio la Kwanza – Octoba, 1990

Mwanzoni mwa mwezi huu octoba, Rais Juvenile Hibyarimana alikuwa amesafiri kwenda Marekani Kuhudhuiria Kongamano la Kimataifa kuhusu watoto ambalo liliandaliwa na Umoja wa Mataifa.

Rais Yoweri Museveni naye pia alikuwa Marekani kuhudhuria Kongamano hilo hilo.

Pual Kagame naye alikuwa Marekani kwa miezi kadhaa sasa kwa ajili ya kozi maalumu ya kijeshi katika chuo cha kijeshi cha Command and General Staff Collage kilichopo kambi ya Leavenwortg huko Kansas.

Kwa miezi kadhaa Kagame na Rwigyema walikuwa wakiwasiliana kwa simu kupanga mikakati ya kumuondoa madarakani Rais Juvenile Hibyarimana na serikali yake ya Kihutu.

Fursa hii ya Rais Hibyarimana kutowepo ndani ya nchi ilikuwa ni fursa adhimu kwao kutekeleza azma yao.

Kwa hiyo mpango ambao walikuwa wakiupanga kwa miezi kadhaa ulikuwa umefika muda wake wa kuutekeleza.

Kwa hiyo siku ya tarehe 1, october 1990 majira ya saa mbili na nusu usiku.… wanajeshi wa weledi wa juu (Special Forces) wenye asili ya Kitusi wapatao 50 waliondoka kutoka kwenye kambi zao za jeshi la Uganda kuufuata mpaka wa Rwanda na Uganda.

Walieleke moja kwa moja mpaka eneo la mpakani la Kagitumba ambako waliwatandika risasi walinzi wa mpaka mahali hapo na kusonga mbele kuingia Rwanda. Kama muda wa saa moja baadae walifuatiwa na maelfu mengine ya wanajeshi ambao walikuwa wamevalia sare za jeshi la Uganda.

Hawa waliluwa ni wanajeshi Uganda sawia kabisa lakini wenye asili ya Kitusi.

Walikuwa na silaha nzito nzito kama vile mashine guns, autocannons, vifaru, pamoja na rocket lauchers aina ya BM-21, vyote hivi vilitoka kwenye jeshi la Uganda.

Jeshi la serikali ya Rwanda walikuwa na wanajeshi wengi zaidi pamoja na vifaa bora zaidi kama vile magari ya kivita pamoja na helikopta ambazo walikiwa wamezipokea kama msaada kutoka kwa nchi ya Ufaransa miezi michache iliyopita. Lakini walikuwa wamezidiwa kete moja adhimu kwenye medani ya vita… hawakujiandaa!!

Shambulio hili lilikiwa ni la kushitukiza kwao na hawakuliona likija kwa hiyo vijana wa RPF walikuwa wamejiandaa kiakili na kimkakati kuzidi jeshi la Rwanda. Na zaidi ya yote walikuwa na ‘mbabe wa vita’ Fred Rwigyema akiwaongoza kwenye oparesheni hiyo ya kushtukiza.

Vijana wa RPF walienda kwa kasi mno na walikuwa wanafanikiwa kwa haraka mno kutimiza lengo. Ndani ya masaa machache walikuwa wameingia zaidi ya kilomita 60 ndani ya Rwanda waliuweka mji wa Gabiro mikononi mwao.

Ndani ya siku moja tu RPF walikuwa wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana na ilikuwa dhahiri kwamba majeshi ya serikali yalikuwa yamezidiwa nguvu na RPF. Kulikuwa na kila dalili kwamba muda wowote kuanzia siku ya pili ya uvamizi huo wa RPF mji wa Kigali ulikuwa unaelekea kuwekwa chini ya Himaya ya RPF na huo ndio unaweza kuwa ndilo anguko la serikali ya Rais Juvenile Hibyarimana.

Lakini kuna jambo la ajabu kabisa likatokea. Jambo ambalo kwa kufikiria kwa haraka haraka lilikuwa haliwezekani kabisa. Katika siku ya pili vikosi vya RPF vikiwa vimewazidi nguvu majeshi ya serikali na wakielekea kuiweka kigali mikononi mwao… katika mzingira ya kutatanisha sana, mwanajeshi na jasusi mbobezi wa uwanja wa vita kuwahi kutokea ukanda huu wa Afrika Mashariki, Fred Rwigyema aliuwawa kwa kupigwa risasi.

Nasema ilikuwa ni jambo la ajabu kwa kuwa vijana wa RPF walikuwa wamewazidi nguvu majeshi ya serikali na walikuwa wanaelekea kuiweka mikononi mwao mji wa Kigali. Lakini jambo la ajabu zaidi Rwigyema aliuwawa akiwa kwenye base (kambini) sio akiwa ‘front line’ au kwenye mapambano.

Kila mtu kuanzia wapiganaji wa RPF na mpaka viongozi wa jeshi la Rwanda walibakiwa na bumbuwazi wasielewe ni nini ambacho kilikuwa kimetokea. Inawezakanaje Rwigyema auwawe kirahisi hivi tena akiwa kwenye base sio ‘front line’? Kulikuwa na kila harufu ya hila kuhusika kwenye kifo hiki. Na mtu pekee mwenye uwezo wa weledi na uthubutu kumfanyia hila ya namna hii komando na jasusi mbobezi wa kaliba ya Fred Rwigyema ni mtu ambaye naye ni mwenye weledi na ubobezi wa kufanana na Rwigyema au kumzidi na si vinginevyo.

Ndipo hapa ambapo unadhihirika msemo wa kwamba kwenye maisha hakuna rafiki au adui wa kudumu… bali kitu pekee ambacho ni cha kudumu ni maslahi.

Yoweri Museveni ambaye nyuma ya pazia alikuwa anajua kila kitu kuhusu uvamizi huu na huku akisaidia kwa siri waasi wa RPF baada ya kupewa taarifa hii ya kuwawa kwa Rwigyema naye alipatwa na mshtuko mkubwa asielewe nini ambacho kilikuwa kimetokea.

Wote wawili, yeye na Kagame walikuwa nchini Marekani, Kagame akiwa Kansas na yeye Museveni akiwa New York. Moja kwa moja akainua simu kumpigia kagame akiwa na swali moja tu la kuuliza… “qu’est-ce qui s’est passé?” (Nini kimetokea?)

Alihisi kabisa… na pengine alijua kabisa kuwa Paul Kagame anajua cha zaidi kuhusi kifo cha Fred Rwigyema.

Itaendelea…

SEHEMU YA SABA

Katika sehemu ya sita nilieleza namna ambavyo RPF iliundwa na jinsi ambavyo jaribio la kwanza la kupindua serikali ya Rwanda likiongozwa na Fred Rwigyema lilikuwa na mafanikio makubwa katika siku ya kwanza tu lakini Fred aliuwawa katika mazingira ya kutatanisha sana kwenye siku ya pili tu ya jaribip hilo la mapinduzi huku tayari wakiwa wamedhibiti mji Kigali kutoka kwa majeshi ya serikali ya Kihutu.

Tuendelee…

KAGAME ANASHIKA USUKANI

Kifo cha Fred Rwigyema kilimshitua kila mtu na hasa hasa Rais Yoweri Museveni. Pasipo kuchelewa alipiga simu nyumbani Uganda (alikuwa bado hajarejea kutoka kwenye mkutano wa UN nchini Marekani) na akamuagiza mtu anayemuamini kwenye jeshi, kaka yake Salim Salehe kwenda Rwanda haraka kuchunguza tukio hili.

Nchini Rwanda mpaka leo hii moja ya mijadala ambayo ni ‘mwiko’ kuizungumza ni kifo cha Fred Rwigyema. Kama wewe ni mwandishi na ukajitoa ufahamu kuandika ‘mawazo’ yako kuhusu kifo cha Fred Rwigyema basi ndani ya siku chache jiandae kutembelewa na ‘watu wasiojulikana’.

Hii ni kwasababu Fred Rwigyema mpaka leo hii anahesabika kama moja ya mashujaa wa nchi hiyo na anaheshimika zaidi na Watusi kama shujaa ambaye ana mchango mkubwa katika kufanikisha kuwatoa watusi kwenye mateso na manyanyaso ya Wahutu. Kwa hiyo hoja yoyote yenye mlengo wa kumbebesha lawama hizo mtu fulani aliye hai kwamba alihusika na kifo hicho zinazimwa ili kuepuka mtu huyo kuchukiwa na watusi wenzake.

Suala la kuuwawa kwa Fred Rwigyema limezua nadharia nyingi sana. Mwanzoni ilianza kuenezwa propaganda kwamba Fred Rwigyema ameuwawa na risasi ambayo ilipigwa kwenda kwingine lakini ikagonga mahala fulani na kubadili uelekeo na kwenda kumpata Rwigyema Kichwani. Nadharia hii imepigiwa upatu kwa muda mrefu sana na serikali ya Kagame. Lakini mwanzoni mwa miaka ya 2000s kuna ukweli ambao ulibainika na kufanya nadharia hii kugeuzwa tena.

Nimesema kwamba Rais Yoweri Museveni alimtuma kaka yake Salim Salehe ili kwenda kuchunguza tukio la kuuwawa kwa Fred Rwigyema. Mwanzoni mwa miaka ya 2000s iligundulika kwamba Salim Salehe na kikosi chake alipofika Rwanda aliondoka na makamanda wawili wa RPF ambao baadae waliuwawa walipofika mpakani mwa Rwanda na Uganda. Makamanda hawa walikuwa ni Peter Bayingana na Chris Bunyezi. Hawa walikuwa ni makamanda wasaidizi wa Fred Rwigyema.

Baada ya taarifa hii kuvuja mwanzoni mwa miaka ya 2000s serikali ya Rwanda ikaja na nadharia/propaganda kwamba Fred Rwigyema alipigwa risasi na mojawapo wa makamda hao baada ya kutokea mabishano wakiwa kambini. Kwamba Fred Rwigyema alitaka waweke mkakati wa kijeshi ambao utawafanya kusonga mbele taratibu lakini kwa hakika na hatimaye kuidhibiti Kigali yote sawa sawa na kuwadhibiti wapiganaji wa Kihutu. Lakini Bayingana na Bunyezi wao walitaka wasonge mbele kwa haraka na kwa nguvu kubwa ya kijeshi.

Serikali ya Rwanda inasema kwamba baada ya mabishano makali Bayingana alipandwa na hasira na kumtolea bastola Rwigyema na kumtandika risasi ya kichwa.

Huu ndio msimamo wa serikali ya Rwanda mpaka leo hii juu ya kifo cha Fred Rigyema.

Maelezo haya yana ukakasi katika viwango kadhaa.

Kwanza kabisa, heshima ambayo Fred Rwigyema alikuwa nayo kwa wapiganaji wa RPF si jambo rahisi kwa mwanajeshi yeyote kuthubutu kumnyooshea bunduli Fred Rwigyema.

Lakini pia Bayingana si mtu mwenye haiba ya hasira za haraka na paniki mpaka kufikia hatua ya kumuua ghafla kwa hasira kamanda wake katika uwanja wa vita.

Ukakasi zaidi unaletwa na ushahidi wa afisa mwingine wa ngazi za juu wa RPF ambaye alishuhudia Rwigyema akipigwa risasi, afisa huyu anaitwa Stephen Nduguta. Nduguta anasema kwamba hakumbuki wala hakushuhudia watu hao watatu wakibishana, kitu ambacho anakumbuka ni kwamba Bayingana ghafla tu alichomoa bastola kutoka kiunoni na kumfuata Rwigyema pale ambapo alikuwa amekaa na kumtandika risasi kichwani. Hii inaonyesha dalili kabisa kwamba alikuwa na dhamira ya kumuua… kana kwamba alipewa maagizo kutoka kwa mtu wa juu zaidi kufanya hivyo.

Maagizo hayo yalitoka kwa nani?? Kagame? Najaribu tu kufikiro kwa sauti…

Hii ni moja ya mijadala ambayo mpaka leo inahitaji uchunguzi zaidi na tafakuri ya kina. Ni bahati mbaya vile ambavyo serikali ya Rwanda inazuia kabisa mjadala huru juu ya kifo cha Fred Rwigyema.

[16/01, 02:40] The Bold: Baada ya taarifa hii ya kifo cha Fred Rwigyema kumfikia Kagame kule nchini Marekani kwenye chuo cha kijeshi cha Fort Leavenworth, Kansas, mara moja alitoa taarifa kwenye uongozi wa chuo kwamba anahitaji kuondoka mara moja kurejea Africa. Uongozi wa chuo ulimkubalia ombi lake hilo na pia kumruhusu kuondoka na vitabu kadhaa ambavyo huko baadae Paul Kagame alivitumia sana kupanga mikakati ya kijeshi.

Kagame aliruka kwa ndege mpaka London, na kisha Addis Ababa, na hatimaye kutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe ambako alipokelewa na watu wa ‘Usalama wa Taifa’ wa Uganda na walimsafirisha mpaka mpakani na Rwanda.

Kagame alivuka mpaka na kuingia Rwanda siku ya tarehe 15 Octoba, 1990.

Kagame aliwakuta wapiganaji wa RPF wakiwa kwenye hali mbaya kweli kweli kinidhamu na morali. Kagame anaeleza kwamba kipindi hiki cha kwanza cha kuchukua mikoba kuiongoza RPF ni moja ya nyakati zake mbaya zaidi kwenye maisha yake. Wanajeshi hawakuwa na nidhamu na hawakuwa na kiwango cha kuridhisha cha morali. Kwa hiyo ilikuwa inamlazimu Kagame aanze kuwajenga upya wanajeshi wake kisaikolojia na kisha awajenge kwa uwezo wa kijeshi/kivita.

Jambo la kwanza kabisa ambalo Kagame alilifanya ni uamuzi wa kurudisha majeshi ya RPF nyuma. Hakuona busara au akili yoyote kuendelea kupeleka majeshi mbele vitani kwa hali mbaya ambayo aliwakuta nayo.

Kwa hiyo kwa wiki kadhaa baada ya kuchukua mikoba ya kuiongoza RPF Kagame pamoja na viongozi wengine wa juu wa RPF waliitumia muda huo kukusanya Intelijensia. Pia waliondoa vikosi vyao kutoka eneo la kaskazini mashariki mwa Uganda na kwenda kuweka makazi mapya kwenye eneo la milima ya Virunga. Nyuma waliacha wapiganaji wachache tu ambao walikuwa wanafanya mashambulizi madogo madogo ya kushitukiza dhidi ya vikosi vya serikali ambavyo walikuwa hawajui kwamba RPF wamehamishia makazi yao kwenye milima ya Virunga.

Kagame alichagua eneo hili la milima ya Virunga kutokana na ugumu wake wa kufikika. Kama ikitokea vikosi vya serikali wakigundua kuwa RPF wanajificha hapo kwa sasa itakuwa ni ngumu kuwavamia au kwafanyianshambulio la kusbitukiza. Kwa mfano ili kufika kileleni ambako wao walikuwa wameweka kambi ilikuwa ni safari ya wiki nzima kutoka vikosi vya serikali vilipo.

Lakini pia wakiteremka na milima hiyo kwa upande wa magharibi walikuwa wanashuka moja kwa moja na kuingia Uganda bila usumbufu wowote kutokana na ruhusa ya Rais Museveni.

Japokuwa milima ya Virunga ilikuwa ni sehemu mujaribu kabisa kuweka kambi kutokana na kuwapa faida ya kujilinda na kujihami lakini hali ya hewa ya eneo hili haikuwa rafiki. Milima ya Virunga iko mita 5,000 kutoka usawa wa bahari. Hakukuwa na vyakula wala miti ya matunda au mazao asili.

Mwanzoni wanajeshi wengi walikufa kwa baridi katika eneo hili. Lakini baada ya wiki kadhaa waliweza kuimudu sehemu hii na kuishi vyema.

Kagame alitumia miezi kadhaa akilijenga upya jeshi lake pasipo kuanzisha mashambulizi yeyote yale dhidi ya serikali ya Rwanda.

Paul Kagame ni ‘born-tactician’ na mtu mwenye akili nyingi sana. Na ni katika kipindi hiki ambacho sifa yake hii ilijidhihirisha kwa kiwango kikubwa zaidi.

Kuna bwana mmoja anaitwa Alexis Kanyarengwe. Huyu alikuwa ni mhutu na Kanali kwenye jeshi la Rwanda na mtu wa karibu sana na Rais Juvenile Habyarimana. Ilifika kipindi alitofautiana sana na Rais Habyarimana na ikabidi akimbie nchi ya Rwanda.

Kagame alimtafuta Alexis Kanyarengwe na kumshawishi ajiunge na RPF.

Kagame alifanya hivi makusudi ili kitendo hiki cha mhutu wa hadhi na kaliba ya Kanyarengwe kujiunga na RPF kutoa picha kwamba RPF ilikiwa ‘inclusive’, yaani ni kikundi chenye kujumuisha watu wa namna zote (Watusi na Wahutu) japokuwa uhalisia ni kwamba RPF ilikuwa ni kikundi cha watusi tena watusi waliozaliwa au kukulia Uganda.

Eneo la Milima ya Virunga

Ili kuonyesha zaidi ‘nia yake njema’ Kagame alimteua Kanyarengwe kuwa mwenyekiti wa kamati ya uratibu wa jeshi la RPF.

Kagame alianzisha ratiba kali ya mazoezi kwa wanajeshi wake kila siku. Na pia aliweka sheria kali ambazo wanajeshi wake walipaswa kuzifuata na kuziheshimu. Kwa mfano alitaka wanajeshi RPF wakienda kwenye vijiji vya karibu wanunue kile ambacho wanahitaji badala ya kuchukua kwa mabavu kama ambavyo imezoeleka kwa vikundi vya wapiganaji wa msituni. Pia wanajeshi wote wa RPF walipigwa marufuku kutumia pombe au dawa za kulevya na pia walitakiwa kuhakikisha wanakuwa watu wa mfano wa kuigwa wakiwa kwenye jamii za vijiji vya jirani.

Wanajeshi ambao walifanya makosa kama vile kuua, kubaka au kuasi RPF waliadhibiwa kwa kifo cha kupigwa risasi.

Hali hii ya nidhamu ya hali ya juu ya wanajeshi wa RPF iliwajengea sifa njema ambayo ilivuma kila mahala. Ghafla kulitokea idadi kubwa ya vijana hasa vijana wa kitusi kutoka Burundi, Zaire, Tanzania na Uganda ambao walijitolea kujiunga na RPF.

Kagame pia akaanzisha ofisi jijini Kampala ambayo ilikuwa na jukumu la kukusanya michango kutoka kwa watusi wenzao duniani kote ambao walikuwa tayari kuichangia RPF. Aloisia Inyumba ndiye alikuwa kamishna wa fedha kwenye ofisi hii ya Kampala.

Michango ilitolewa kutoka kwenye kila pembe ya dunia na hata kutoka ndani ya Rwanda kwa wafamyabiashara ambao walikuwa wamechoshwa na utawala wa kimabavu wa Rais Habyarimana.

Sifa njema ya RPF ambayo Kagame alifanikiwa kuijenga ndani ya muda mfupi ilifanya RPF nje ya medani ya vita, huko mitaani ionekane kama harakati fulani hivi za ‘kibinadamu’ ambazo zilikuwa zinapswa kuungwa mkono kwa nguvu zote.

Japokuwa fedha za michango walizopokea hazikuwa nyingi sana, lakini Kagame alikuwa ametengeneza utaratibu wa kuishi kwa kujinyima sana. Inajulikana namna ambavyo wanajeshi wa vikundi vya waasi na wapiganaji wa msituni namna ambavyo wanapenda kuishi maisha ya anasa iliyopindukia, starehe kila usiku na wakilala na kundi la makahaba au watumwa wa ngono. Lakini hii ilikuwa tofauti kabisa kwa Kagame yeye mwenyewe aliishi kwa mfano kabisa kwa kujinyima mno japo alikuwa ndiye kiongozi wao mkuu. Wapiganaji wake wote nao walifuata mfano huu. Waliishi maisha ya kujibana na kuepuka gharama ambazo hazikuwa na lazima. Kwa hiyo walifanikiwa kuokoa fedha nyingi ambazo walizitumia kununulia silaha.

Ikumbukwe kwamba katika kipindi hiki ndicho kipindi ambacho pia vita baridi kati ya Marekani na washirika wake na Urusi na washirika wake iliisha. Kwa hiyo kwenye soko la duniani kulikuwa kumefurika silaha ambazo zilikuwa zinauzwa kwa bei chee kabisa. Kwa hiyo Kagame alitumia vyema fursa hii kununua silaha za kisasa kabisa kwa kutumia kiasi kidogo cha fedha ambazo walikuwa wanafanikiwa kukipata kutoka kwenye michango wanayopokea.

Lakini pia jeshi la Uganda walikuwa wanapenyeza kwa siri kubwa silaha mpakani kwenda kwa RPF.

Ilipita karibia miezi mitatu tangu Kagame achukue uongozi mkuu wa RPF bila kufanya shambulio lolote au tukio lolote la kijeshi. Muda wote huu alikuwa analijenga upya jeshi lake na kwa hakika alifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana.

Kwa hiyo baada ya miezi hiyo mitatu alihisi kwamba ulikuwa umefika wakati sahihi kwa wao kuanza tena mashambulizi ya kijeshi dhidi ya majeshi ya serikali ya Rwanda.

Na kwa makusudi kabisa alichagua jiji la Ruhengeri kama sehemu ya kwanza ambayo wanapaswa kuzindua oparesheni zao za kijeshi.

Mji wa Ruhengeri… tazama milima Virunga kule nyuma kwenye ‘background’

Huko nyuma kwenye shehemu zulizopita nilieleza kwamba Kagame ni gwiji wa ‘psychological warfare’.

Hii inadhihirishwa na sababu ya kuuchagua mji huu lakini pia na namna ambavyo walikuwa wanaushambulia.

Tuanze na sababu za uchaguzi wa mji huu.

Sababu ya kwanza ya kuchagua mji huu ilikuwa ni kutaka ushindi wa haraka na kuingiza hofu kwa vikosi vya serikali. Kwa namna gani au kwa nini?

ITAENDELEA

Hisoria ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda Sehemu ya Nne

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment