Kitanzi cha Mwisho Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE
*********************************************************************************
Sehemu ya Tatu (3)
Ni pale walipofika eneo la Vingunguti na kukuta lundo la watu, magari yalikuwa foleni, kamanda Amata akashindwa kujua kunani eneo hilo, kati ya vijana waliokuwa wakipitapita mmoja aliitwa na Kamanda Amata akasogea dirishani, “Vipi dogo kuna nini hapo, ajali?” akamuuliza.
“Yaani braza hapo palikuwa na mtanange wa polisi na majambazi, wengine wanasema sijui majambazi walikuwa wanataka kuteka gari, wengine wanasema ile gari ilikuwa na hela sasa walishindwa kufungua mlango, ns polisi wakawa wamefika,” Yule kijana akawa anaeleza.
“Kwa hiyo wamefanikiwa au ?” Amata akauliza.\
“Hapana, wameshindwa, jamabazi mmoja ameuawa palepale, wengine wamekimbia, na ile gari iliyokuwa inawindwa imeondoka mudfa si mrefu,” Yule kijana akajibu huku akianza kuondoka. Kamanda Amata akashusha pumzi, “Lo, nchi imekuwa kama Somalia hii, watu hawaogopi Serikali,”….
Akatoa gari yake upande wa kushoto kama wanavyosema vijana akatanua na kupita ‘service road’ kuelekea Tazara, akiacha eneo hilo bado watu wamejezana wakishangaa kinachoendelea.
“Amata mpenzi, kwani wewe hii kesi ya huyu mwanadada unaichukuliaje?” Gina aliuliza.
“Gina, mara ya tano unauliza swali hilohilo na mara zote nimekujibu, we inaonekana hata huko chuoni maprofesa wanapata tabu kukufundisha sio?” kamanda Amata aliongea kwa hasira kidogo huku akibadilisha gia na kuiacha barabara ya Nyerere na kupinda kushoto kuelekea Magomeni kupitia barabara ya kuelekea huko. Kamanda Amata alimtazama Gina kisha akaangalia mbele wakati huo alikuwa akiyavuka mataa ya Ilala Boma kuelekea Kigogo, “Gina, hili sakata la huyu mwanamke lazima lina mambo mengi ndani yake, kesi kama kesi ya mauaji kwa nini iwe katika mtindo huu? Wangapi wameua na wakanyongwa au kufungwa maisha mambo yakaisha lakini huyu kaua, sawa, ila ukweli anaujua yeye na Mungu wake, mimi na wewe hatujui. Sasa kwa nini matukio mengi yenye mkanganyiko yatendelee kuiandama au kumuandama mwanamke huyu? Lazima twende nyuma ya mapazia tuone kilichojificha, siifurahii hali hii lazima nifuatilie, kama ACP Chonde ameuawa kwa sababu ya sakata hili basi afande Magreth yupo hatarini, kwa nini wamuue Chonde na wamtafute kwa nguvu Yaumi, kuna jambo na jambo lenyewe sio dogo, lakini ukweli utajulikana nitahakikisha Yaumi hafungwi maisha wala hanyongwi, mimi ndio Kamanda Amata TSA 1,” aliongea kwa majigambo, huku akitabasamu na kumtazama Gina. “Haya mama umefika nyumbani kwako, au unataka name nishuke?” Amata akamwambia Gina wakati akiegesha gari yake vizuri pale mbele ya nyumba aliyopanga Gina, alipotaka kushuka Amata akashika mkono wa Gina, “Sikiliza, ni hatari sana na ni salama sana kwa wewe kuishi nyumba ya Kupanga, tafuta nyumba kubwa mbili, kampuni itazinunua moja yako na moja yangu,” kamanda akamuachia mkono baada ya kumwambia maneno hayo, Gina akabaki kumtumbulia macho kijana huyo shababi ambaye ukimuona sura yake ya upole hutoweza kujua kama ana purukushani za ajabu akiwa katika mapambano, labda utamuogopa tu kwa jinsi mwili wake ulivyojengeka kimazoezi.
“Mi nilijua unasema nitafute nyumba moja tuishi wote kumbe unataka mbili? Basi nitaishi hapahapa,” Gina alijibu hoja hiyo huku akiondoka zake, kamanda Amata alimsindikiza kwa macho mwanadada huyu ambaye kila mtu alimpenda kwa ucheshi wake na maneno mengi aliyonayonayo, shepu yake iliyojiumba sawia iliwafanya wanaume wengi wenye pesa zao za ukware kumsololea lakini waliondoka patupu, kutokana na kukaa muda mrefu uraiani tangu alipohitimu masomo yake ya sheria katika chuo kikuu cha Dar es salaam, Gina binti Komba Zingazinga hakujulikana kama ni WP. Ukichanganya na tabia yake ya kujichanganya ndio kabisa. Ni yeye na Kamanda Amata walilificha hilo mioyoni mwao pamoja na viongozi wake katika jeshin la polisi. Mwamvuli wa kampuni bubu ya AGI Int’ ilimfungia ndani na kuonekana ni mfanyakazi wa kawaida tu, ni Madam S alieomba mwanadada huyu machachari abaki na Kamanda Amata ofisini huku wakimtazama kama naye anaweza kuingian katika idara nyeti ya usalama wa Taifa, hata yeye mwenyewe hakulijua hilo, ni nyakati Fulani Fulani alikuwa akishangaa anapopewa majukumu nje ya ofisi yake kuyafanya na amri ikitoka kwa madam S. Gina alimuogopa na kumheshimu sana Madam S au mkwe kama alivyokuwa akimwita wawapo katika kutaniana. Madam S alimuona Gina kama mwanae, alimpenda kwa jinsi alivyo na hasa alipokuwa akimsaidia Kamanda Amata katika shuruba mbalimbali, akionesha umakini na uhakika kwa analolifanya, akiwamudu wale wanaomletea kashkash za maisha yake na pia jinsi alivyo mkakamavu, hakuwa na linguine, alikubalika machoni na moyoni mwa Madam S.
§§§§§
GEREZA LA KEKO
YAUMI alifikishwa katika gereza la Keko majira ya saa tisa alasiri akiwa chini ya ulinzi mkali, alifunguliwa pinmgu na ule mnyororo kwenye miguu yake akaingizwa katika selo ya peke yake. Hakuna askari aliyemuongelesha, kila kitu kilienda kimya kimya tu utafikiri wamelazimishwa kufanya hilo wakati ni wajibu wao. Yaumi alikuwa amechoka sana bado mwili wake ukiwa na maumivu ya kipigo alichokuwa akikipata toka kwa polisi kule Kampala, kila aliyemtzama Yaumi alimuonea huruma sana, alitamani aiambie serikali ‘muachieni huru lakini haikuwa hivyo’ sheria ilikamata mkondo wake. Yaumi alikiendea kigodoro kilichokuwa kwenye moja ya kona ya chumba hicho kidogo, akajilaza huku amejikunyata kana kwamba kuna baridi au mtoto mkiwa. Mawazo mengi yalikuwa kichwani mwake, alijua nwazi kuwa sasa hawezi tena kutimiza azma yake, alikiona kitanzi kilicho mbele yake, akajua mwisho wake umefika, hakuna msaada tena labda ule utokao kwa Mungu tu ambao wakati mwingine hata kifo huwa ni msaada kutoka kwake japo tunakuwa na mdioyo migumu kuelewa hilo. Ulinzi mkali ulikuwa kwa Yaumi, nje kidogo ya mlango wa chuma wa kuingiulia katika selo yake kulikuwa na askari wawili wa kike waliotakiwa kulinda hapo bila kuchoka wala kutoka hasa walipoambiwa kuwa, mwanamke huyo ‘ninja’ alikuwa anatoroka ulinzi na ngome ya Segerea na kuingia mtaani kufanya aliyoyafanya. Waliaswa na kuaswa, kuanzia ndani ya gereza hilo mpaka nje kuimarisha ulinzi. Siku hiyo eneo Keko lilikuwa na hali mbaya, kila kona ni polisi na askari magereza wakitembea kuzungukazunguka kuona kama kuna lolote.
Yaumi alikuwa akiiwazia kesho yake ambayo ndio ilipangwa hukumu ya kesi yake, alijua kwa vyovyote hana pa kuponyoka.
“Usiogope mke wangu Malaika mlinzi yupo anakulinda na atakuwa pamoja nawe, azma yako itatimia lakini si kwa mkono wako bali macho yako yatashuhudia na moyo wako utaridhia hayo yote, ukweli utadhihirika na wote waliohusika sherian itachukua mkondo wake,”
Ilikuwa ni sauti ya Bwana Kajiba iliyomjia katika ndoto usiku huo. Yaumi alikurupuka kama mtu anayekimbizwa, alihema kupita kiasi mpaka walinzi wa mlangoni walishtuka kwa mhemo huo, wakafungua kadirisha kadogo kumtazama, Yaumi akajilaza tena.
§§§§§
MAJIRA ya saa tatu usiku yalimkuta Kamanda Amata maeneo ya Barakuda bar katika njia panda ya barabara ya kutoka Tabata Bima kwenda Segerea na ile itokayo Vingunguti kwenda Tabata Chang’ombe, alichagua meza moja iliyokuwa peke yake na kuketi katika moja ya kona iliyomruhusu kuona kila aingiae na atokae. Akiwa ankunywa bia yake aina ya Safari Lager kwa utulivu wa hali ya juu, hakika hakujua anayemsubiri ni nani na atafika wakati gani, aliendelea kung’aa macho tu, akifanya mchezo wa kupiga ngumi hizani.
“Kaka jamani humalizi tu?” Kamanda Amata alishtuliwa na sauti laini yha mwanadada mhudumu wa bar hiyo, alipokuwa kainua chupa na kuitikisa, akaituta bado sana.
“Unataka kunipa nyingine?” Kamanda akauliza.
“Ndiyo maana yake,” Yule dada akajibu.
“Sawa lete nyingine pamoja na yako kisha ukae hapa name au unasemaje?” Kamanda alilianzisha, Yule mhudumun hakuwa na la kujibu aliona kapata bahati ya mtende, ukizingatia siku hiyo bar haikuwa na watu wengi hivyo ‘keep change’ hazikuwapo. Dakika tano baadae Yule dada aliungana na Amata pale mezani wakigonga cheers na kuendelea kupata kinywaji.
“Naona leo mnakula shush tu maana sioni watu leo,” Kamanda alianzisha mazungumzo na dada huyo.
“Ah leo pamekuwa hamna watu kutokana na zoazoa ya jana na juzi,” Yule dada akajibu.
“Umesema zoazoa ya jana na juzi? Ukimaanisha nini?” Kamanda Amata tayari alinasa kitu kwenye jibu hili nae hakutaka kupoteza nafasi aliendelea kumchimba dada huyo. “Ee kaka yangu we acha tu, maana juzi na jana wamesomba vijana hapa na kupelekwa Tabata polisi, si kulikuwa na mauaji yametokea juzi ilee usiku sasa ikasemekana waliomuua wanapatikana sana mitaa hii,” Yule dada alizidi kueleza huku akiwa hajui ni nani anayeongea nae muda huo. “Mh, sijasikia hiyo, nani ameuawa?” Amata aluliza kwa kunong’ona. “Kuna afande mmoja alikuwa huko Kimanga anaishi huku juu Vingunguti, walimkamata na kumuua hapo bondeni kisha maiti wakaenda kuitupa Ukonga sijui mto Msimbazi,” wakati Yule dada akijibu swali hilo aliingia mteja mwingine ambapo ikabidi ainuke kwenda kumhudumia, “Narudi kaka usijisikie mpweke,” akaaga na kuondoka. Kamanda Amata akajua hapahapa lazima apate kile anachokitaka, akatulia kimya akisubiri kujua nini ni nini kutoka kwa Yule dada. Punde tu Yule dada akawa anarudi kutoka kaunta akipita kwenye kijia kinachokuja mlango mkubwa ili afike kwa Amata. Pikipiki moja aina ya Kawasaki ikaegeshwa hapo nje kelele zake kila mtu alikerwa lakini alishindwa kumwambia huyo mwenye pikipiki hilo kuwa anawapigia makelele. Akashuka bwana mmoja mfupi aliyeshupaa alikuwa amevaa jeans nyeusi na Fulani kaba shingo nyeusi ikifunikwa na jaketi la ngozi ya rangi hiyo hiyo, aliingia kibabe akisindikizwa na mwenzake walioshuka katika pikipiki moja, akakutana na Yule mhudumu pale kwenye kile kijia, Yule bwana akambana kidevu Yule mhudumu kwa kiganja chake cha mkono na kumwambia kitu Fulani kama mtu anayemuonya mwingine, akamuachia na yeye kuelekea upande mwingine kuketi. Ilionekana wazi Yule dada alikerwa na kitendo kile alichofanyiwa na huyo jamaa, akatoa sonyo refu na kuelekea alikoketi Kamanda. “Vipi, mbona jamaa anaonekana mkorofi sana?” Kamanda aliuliza wakati Yule mwanadada akiketi katika nafasi yake. “Achana nalo hilo, siku mbili halikuwepo hapa tulikaa kwa amani, leo limekuja tena,” akalalama.
“Ni nani?” kamanda akauliza. “Ha, we kaka, hulijui hilo, linaitwa Chilungu, watu wanasemaga ni lijambazi, na lingekuwepo juzi lingesombwa,” jibu hilo kutoka kwa Yule mhudumu, liliushtua moyo wa Kamanda Amata, akaona kumbe aliyekuwa akimtaka kaja. Akajiuliza mara kadhaa ataanzia wapi kumtia nguvuni, hakupenda aonekane kuwa yeye ni mmoja wa makachero, hii ingemletea sifa mbaya mbele ya wanaomfahamu. Akafikiri kidogo na kupata jibu la haraka, akainua simu yake na kuchambua majina, la kwanza, la pili na la tatu, akaendele na macho yake yatua kwenye jina WP Magreth, akaandika meseji ya kumuuliza yuko wapi mida hiyo, sekunde chache akajibiwa
“… nipo maeneo ya Kisukulu kuna jambo tunalifuatilia,…”
Kamanda Amata akamuandikia kumuuliza kama yuko peke yake au na wengine, akajibiwa kuwa
“…Nikon a kampani kama watano hivi, kikazi zaidi,”
Hapo Amata akaona kuwa mambo si mabaya kwa maana kama yuko kikazi na wengine basi ina maana yupo kamili akiwa na silaha pamoja na vifaa vingine. Akatabasamu kidogo, akaandika meseji nyingine ya kufunga kazi.
“…Nipo barracuda bar hapa njia panda ya Segerea na Tabata Chang’ombe, kuna ndege unawahusu, njoo na kamba ya kufungia mabawa pamoja na manati ya kulengea kama ataruka, ukifika maeneo haya kabla hujaingia nishtue nikupe maelekezo…”
Ilikuwa meseji ya Kamanda Amata kwa afande Mgreth. Kamanda Amata akatulia pale mezani huku akiendelea kunywa bia yake. Meseji nyingine ikaingia kwa Kamanda Amata,
“…umesomeka na kueleweka, tuko njiani,…”
Mazungumzo kati ya Amata na Yule dada yaliendelea pa sin a Yule dada kujua lolote linaloendelea mahala hapo.
Zikaagizwa bia nyingine, wawili hao wakaendelea kunywa, Kamanda Amata alikuwa akihakikisha hawapotezi watu hao aliotaka wakamatike usiku huo, “Samahani nakuja,” alimwambia Yule dada kisha akanyanyuka na kutoka nje, baada ya muda akarudi na kuketi palepale. Alijua kitkachotokea hapo muda si mrefu hivyo akamwambia Yule dada akamtafutie sigara, akamtajia sigara ambayo anajua kabisa kwamba kwa hapo haipatikani, Yule dada alipoaga kaunta akatoka nje kuelekea madukani.
§§§§§
MAGRETH aliingia kama mteja mwingine katika bar ile akitanguliwa na Jamaa ambaye alienda moja kwamoja kaunta, kwa jinsi tu alivyo Kamanda Amata alijua kuwa kazi itakuwepo mahala hapo. Nje kulizungukwa na askari polisi wane wenye silaha zilizoshiba vizuri. Wakiwa wanajua wazi kuwa mbaya wao yupo hapo hawakutaka kuchezea hata nukta moja.
Yule jamaa wa kaunta akaagiza juisi ndogo ya boksi, akainywa polepole huku akimtazama Magreth aliyekwenda kuanzisha uchokozi wa makusudi, Kamanda Amata aliwaambia wawakusanye wote wawili katika meza ile.
“Habari yenu wakaka,” Magreth alisalimia. Chilungu al;ipoinua uso kumtazama mwanamke huyo akabaki katoa macho pima, alimfahamu WP huyu vizuri sana naye tayari alikuwa kwenye orodha yake ya watu aliyopewa kuwaondoa kwa donge nono, Chilungu akanyanyuka na kumkazia macho afande Magreth. “We mwanamke unafuata nini hapa, usiniletee usiku!!” akiwa katika kusema hayo aliingiza mkono kiunoni mwake na kutoa bastola alipomuoneshea Magreth tayari alikuta Magreth nae bastola mkononi, wakabaki wakitazamana kila mmoja bastola kwa mwenzake….
Ilikuwa kama sinema Fulani inayorekodiwa huko Hollywood, Kamanda Amata alikuwa bado ametulia pale kitini akishusha bia yake taribu kinywani huku nakitazama mchezo huo utaishia wapi, tayari bastola yake ilikuwa imeshawekwa kikazi, haikuwa mbali bali tayari ilikuwa mkono wa kulia ikiwa imebanwa na kiganja imara, kiganja kisicho na masihara katika kazi, ikiwa imeshaondolewa usalama na risasi tayari imedumbukia chemba.
“Shusha bastola yako wewe, kabla sijaamu vinginevyo,” Sauti ya Magreth ambayo daima ilikuwa nyororo leo ilibadilika na kuwa kavu kabisa ikionesha kutokuwa na masihara.
“Sishushi, huwezi kuniamulia, mwanamke Malaya wewe,” Chilungu alijibu kauli ya Magreth. Kosa alilofanya Magreth ni kuwa bado bastola yake haikuwa kikazi, bado alikuwa hatua moja nyuma, kidole chake kilicheza pale katika lock ya usalama, ilikuwa ni nafasi ya Yule jamaa mwingine pale chini, alipourusha mguu wake kwa ustadi mkubwa na kuupiga mkono wa Magreth ambao uliondoka katika shabaha na kwenda pembeni, Chilungu alijirusha mzima mzima na kutua juu ya meza, Magreth alifyatua risasi iliyopita jirani kabisa na kanyagio la mguu wa Chilungu na kutoboa meza kabla ya kuchimba chini, shabaha hiyo ilimkosa Chilungu wakati alipokuwa hewani akipiga samasoti kali na kutoka nje ya wigo wa bar hiyo, lakini akiwa juu alipiga yowe la maumivu, risasi kutoka kwa jamaa aliyekaa pale kaunta ilitua sawia kwenye kiganja cha Chilungu, akaanguka chini na Yule mwenzake alipotoka eneo lile baada ya kufanya lile la kumkosesha shabaha Magreth, alitoka eneo lile kwa kasi kuelekea kule alikoegesha pikipiki yao, akafika na kujitupia juu yake, akapiga kick moja likawaka, alipotaka kuondoka kwa manjonjo ambapo nia yake ilkuwa ni kumuendea Chilungu kumbeba na kuondoka eneo lile alikuta injini ya pikipiki ikizunguka peke yake, alipocheki cini, mnyororo haupo, upo chini, umekatwa au umekatika, akawaka hasira na kujitoa kwenye ile pikipiki, akajaribu bahati yake kwa kukimbia, “Simama kwa usalama wako!” ilikuwa sauti ya polisi mmoja aliyekuwa nje ya bar hiyo kulinda usalama, Yule jamaa hakusimama alitaka kujiokoa lakini nalisahau kuwa anacheza na mtu mwenye silaha, risasi mbili zilizotoka kwenye Sub Machine Gun (SMG) zilimsukuma na kumuongea mwendo wakati zikipenya mgongoni na kutokea kifuani, akajibwaga juu ya lundo la mchanga na kugalagala akiipigania roho yake.
Chilungu kabla hajanyanyuka eneo lile, afande Magreth alikuwa amefika, akiwa anajaribu kunyanyuka, teke kali lilitua tumboni mwake na kumrudisha chini, hajakaa sawa buti aliyovaa Magreth aina ya caterpillar ilikanyaga shingoni mwa Chilungu na kumnyima pumzi, “Afande unaniua afande,” Chilungu aliongea kwa tabu, “Usijali, hata ukifa hauna thamani kwa jamii san asana unaongeza mawazo na mateso kwa mwanamke mwenzangu aliyekuzaa,” afande Magreth aliongea maneno hayo huku akiuma meno kwa hasira, bastola ikiwa mkononi ikikilenga kichwa cha Chilungu.
Ilikuwa ni kelele eneo lote hilo, wananchi wakipiga makelele “Majambazi, majambazi,” huku wakirundikana katika eneo hilo kama kawaida ya Watanzania, watu waliokuwa kwenye bar ile, pombe ziliwatoka, wengine wakiwa wejikojolea kwa milio ile ya risasi, ilimradi tu kila kitu kilivurugika kwa dakika chache. Ni mtu mmoja tu alikuwa bado ameketi akiedelea kupata kinywaji chake pale mezani, Kamanda Amata, ambaye daima kwake mambo hayo ni kawaida sana, tena makubwa kuliko hayo, alitabasamu alipojuwa kuwa mpango umekamilika, yeye ni kama katumia rimoti kukamilisha swala lile, hakupenda kujionesha waziwazi. Mpaka dakika hiyo hata Magreth hakujua Amata ameketi wapi.
Land Cruiser ya buluu yenye namba za usajili zinazotanguliwa na PT iliingia kwa mbwembwe eneo na kuegeshwa jirani kabisa na mlango nwa bar hiyo, Chilungu alikokotwa akiwa na pingu mkononi huku mkono wake ukiwa unavuja damu, alipofikishwa pale katika gari kwanza kabla ya kupakiwa ndani alipata kipigo kitakatifu kutoka kwa maafande waliobakia garini, “Unatufanya watu tusistarehe na wake zetu tukeshe kukutafuta wewe hanithi,” alisikika mmoja aliyekuwa akimpa kipigo kikali, Chilungu alikuwa hoi hajiwezi chini, akiwa amelala nusu mfu. “Afande Godi,” Magreth aliita, “Muache huyo anatakiwa akahojiwe,” aliongezea kusema alipomuona Godi kaacha kumpiga Chilungu, “Haina haja Magreth, huyu ndiye aliyeua huyu,” alijibu huku wakimbeba na kumtupia nyuma ya gari hiyo, wakachukua na mwili wa Yule mwingine naye akatupiwa humohumo. Kisha wale polisi wote wakadandia nyuma tayari kwa safari, Magreth ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa msafara, akachukua nafasi ya mbele na safari ikaanza kuelekea kituo cha Polisi cha Tabata. Walichukua barabara ya kuja bima kwa mwendo wa kasi, walipofika katika zahanati ya Tabata karibu na shule wakakunja kulia na kuingia moja kwa moja kituoni.
BUGURUNI KWA MNYAMANI
FASENDY akiwa anawahudumia wateja wake katika chumba maalum ndani ya nyumba yake hakuwa na wasiwasi wowote wa maisha. Akiwa anajua wazi kuwa shoga yake Yaumi hayupo lakini alikuwa na uhakika kuwa siku yoyote atarudi tu kwani yeye alipenda kumwita mwanamke huyo ‘Ninja’.
“Mama mama kuna mgeni,” ilikuwa ni sauti ya motto wake aliyempa taarifa hiyo. Fasendy akanyanyuka na kuelekea huko kwenye huo wito, alifika mlangoni na kukutana na mwanaume mmoja akiwa ameongozana na mwanamke. Fasendy aliitambua sura ya huyo mwanamke mara moja ila ya mwanaume hakuitambua.
“Karibuni ndani,” akawakaribisha kwa kutumia lugha ya ishara wakati yeye akitangulia. Katika mtaa wote huo Fasendy alikuwa akitumia lugha ya viziwi kuwasiliana na watu, hakuna aliyekuwa akijua kuwa Fasendy hakuwa kiziwi isipokuwa Yaumi peke yake, alipowakaribisha watu hao, wakatazamana kisha wakamfuata, walijua kuwa wanayemtaka ndiye. Walipofika katikati ya korido ndefu, ukimya mkubwa ulikuwa umetawala nyumba hiyo, akasimama akawageukia na kuwaonesha karatasi lililofanyiwa lamination safi. Yule mwanamke akalichukua na kulisoma, akabaki kapigwa na bumbuwazi. Liliwekwa aina ya huduma au bidhaa zilizopo au zinazopatikana humo ndani. Bangi, Cocaine/Heroin/Mandrax etc, Gongo, Ngono za jinsi moja/jinsia tofauti; pamoja na hayo palikuwa na bei na kila kitu kiliainishwa vyema. “Mh!” Yule mwanamke aliguna, kisha wakamwambia japo kwa tabu kidogo kuwa wanataka kuzunguma nay eye, akawakaribisha katika chumba kimoja kikubwa ambacho ndani yake kulikuwa na samani za kisasa na kila aina ya vitu vya bei mbaya, akawakaribisha kochi moja na yeye akaketi katika kiti kingine, “Bila shaka wewe ndiye Fasendy,” aliongea Yule mwanaume, akatoa picha mfukoni na kumpa, Fasendy akaingalia kisha akavuta droo ya kabati lililo jirani naye akaitumbukiza ile picha na kufunga ile droo. “Sijakwambia uitumbukize kwenye droo, nataka unambie unamfahamu huyo mwanamke?” Yule mwanaume alisema kwa hasira huku akinyanyuka kumueleka Fasendy, kabla hajafika alijikuta anatazamana na domo la bastola iliyofungwa kiwambo cha sauti, akapewa ishara ya kurudi kitini, akatii na kujitupa kwenye kochi huku kijacho kikimtoka. Fasendy akafyatua pini iliyobana hijab yake na kuacha kichwa wazi kabisa, “Sikilizeni nyie,” akawaambia wale wageni huku akiwa anaongea kwa lugha na sauti ya kawaida, “Msifikiri duniani hapa binadamu tunaishi kwa shida tunataka, ni hali ya maisha hii, Yaumi kawakosea nini ninyi, mmh? Kwa nini mnamfuatafuata sana mtoto wa watu, kuua mmeua ninyi halafu mnamsingizia yeye, wanaharamu wakubwa nyie, utafikiri ninyi mmezaliwa na miti,” Fasendy alilalama huku bastola ile akiwa ameiweka mezani bila woga.
“Fasendy, kwa nini unamiliki silaha kama hii nyumbani, wewe ni nani?” ilikuwa sauti ya mwanamke mara hii. “Nyama kuku wa kike wewe, unafikiri uliyotufanyia kule gerezani Segerea na hapa? Hii himaya yangu, kumiliki silaha nchi hii si tatizo, na kuipata kwangu haiana tabu, mi ni Msomali, Napata silaha muda wowote ninaotaka, unasikia afande Marina, ila unachomfanyia Yaumi mwanamke mwenzio sio kizuri, nendeni mkamwambie Matinya, mpeni na salamu zangu kwamba jeshi la mtu mmoja linakuja kumkomboa Yaumi, namtaona kazi.” Wakati anasema hayo Yule mwanaume akainyakuwa ile bastola na kuiandaa kumfyatua Fasendy, lo, kabla hatimiza azma yake, chuma cha baridi kilipenya begani mwa Yule mwanaume na kuparanganya mifupa ya bega hilo. Marina alibaki akitetemeka huku akishuhudia bunduki aina ya Short Gun ikiwa imetulia mikononi mwa mwanamke huyo, hakuona hata ni wakati gani Fasendy aliichukua bunduki hiyo. “siwaui, nendeni mkamwambie Matinya niliyowaeleza, na msirudi hapa tena, nina uwezo wa kwenda kumchukua Yaumi Keko muda wowote nikimua.” Aliongea kwa kujigamba huku akiwataka watu hao kuondoka.
§§§§§
Ulikuwa ni wakati mgumu sana kwa Matinya, uzee ulikuja kwa kasi ya ajabu siku hiyo, asubuhi yake alikuwa kijana mtanashati lakini wakati huu alikuwa mzee kwelikweli tena mwenye kuchanganyikiwa mara kwa mara. Aliona wazi bila kificho kuwa mwisho wa udhalimu umefika. Akiwa kamaliza kugida Konyagi kubwa sasa alikuwa na chupa ya GIN mkononi mwake, mara mlango ukafunguliwa na Marina akaingia na kumkuta Matinya katika hali hiyo, “Vipi mpenzi?” akamuuliza Matinya. “Chukua bastola uniue,” ndilo jibu fupi lililotoka kinywani mwa bwana huyo. “Lakini na wewe ujiue kwani utapata shida sana baada ya kitendo hicho,” akamalizia kauli yake.
Muda huohuo Scogon na Simbila nao waliingia mle ndani, wakaketi.
“Sina lingine la kusema, tunakoelekea ni kubaya sana sana sana, Chilungu amekamatwa na jamaa yake ameuawa leo huko Baracuda bar, akitamka siri tu tumekwisha, Yaumi anapandishwa kizimbani kesho kwa hukumu, haya na wewe Marina nilikutuma wapi na mwenzako yuko wapi?” Matinya aliuliza kwa sauti ya kilevi.
“Mpenzi Yule mwanamke kasema usimfatefate, Yule mwanamke ni komandoo, anamiliki silaha mle ndani sijapata kuona, mwenzangu niliyekwenda naye kapigwa risasi ya began a nimemuacha kwa daktari wetu akimtibia,” Marina alieleza kwa uchungu. Matinya alibaki kimya akiwa hajui cha kufanya, aliona wazi jinsi wingu zito likiwa limetanda mbele yake.
SIKU ILIYOFUATA
MAHAKAMA KUU KISUTU
JAJI RAMSON SEMINDU alikuwa na wakati mgumu sana katika kesi hiyo, alikuwa amejiinamia katika meza yake kubwa iliyoa eneo la mbele la chumba hicho kikubwa cha mahakama hiyo, watu wakiwa wamejazana kila upande wakitega masikio kujua nini kitajiri katika hilo. Waandishi wa habari kama kawaida wakiwa wamepewa eneo lao maalumu katika kupata kila kinachoendelea katika mahakama hiyo.
Utulivu wa hali ya juu ulikuwapo kama unavyojua heshima ya mahakama, ilisikika sauti ya mwendesha mashitaka tu na baadae ilikifuatiwa na wakili wa serikali, kila kitu kilikuwa tayari, ushahidi ulikuwa wazi na Yaumi alikutwa na kesi zaidi ya kujibu ukiachana nay a kumuua mumewe, alipewa kesi ya kuuwa watu wengine wawili, uharibifu wa mali, na kutuhumiwa pia na lile kosa la kuua huko Kampala na uharibifu wa jengo la posta huko Kampala, tafutishi zote ziliwasilishwa kwa Jaji Ramson, siku moja kabla ili aweze kafanya yale aloiyotakiwa kufanya.
Katika waliokuwapo mahakamani hapo, Gina alikuwa miongoni mwa watu waliojazana mahakamani hapo, Dr Omongwe pia alikuwapo, afande Magreth alikuwapo pamoja na wengine wengi. Ulinzi mkali ndani na nje ulikuwa umeimarishwa na askari wa kikosi maalumu cha Magereza kutoka Ukonga KM.
Baada ya mawasilisho yote yaliyotolewa, ilikuwa ni zamu ya jaji kutoa hukumu dhidi ya mwanamke huyo, aliyeitwa ‘Hatari’
Hukumu ilisomwa kwa lisaa limoja na nusu, katika hukumu hiyo jaji Ramson Semindu alisema upande wa mashitaka ulioongozwa na wakili wa serikali umethibitisha mashtaka hayo pasipo na shaka yoyote, pia ushahidi wa watu wanne zaidi umethibitisha kuwa Yaumi alimuua mumewe na watu wengine watatu zaidi akiwemo Yule wa Kampala ambapo ushahidi wake uliwasilishwa mahakamani na polisi kutoka Kampala.
Yaumi akiwa kainamisha kichwa chake chini ndani ya kizimba kilichojengwa kwa mbao safi zinazong’aa, alikuwa akifuatilia neon moja moja la jaji huyo kijana. Jaji Ramson akiwa katika sauti iliyojaa uchungu ndipo alipomhukumu Yaumi kunyongwa hadi kufa. Hiyo ilikuwa ndiyo hatima ya binti huyo, Yaumi.
Baada ya hukumu hiyo mahakama ilikwisha, jaji Ramson aliinua kinyundo chake na kugonga kwenye kitako chake pale mezani, akafunga kabrasha lake na kutoka huku watu wote mahakamani wakiwa wamesimama kwa heshima, alifika mlangoni na kugeuka nyuma akamtazama Yaumi kwa huruma sana, kisha akaingia katika chumba kingine.
Askari Magereza wa kike alimchukua Yaumi, pingu mikononi na mnyororo mmoja miguuni mwake, akaondolewa na kupakiwa katika Defender ya magereza, safari hii hakupelekwa Keko, bali alifikishwa katika Gereza kuu la Ukonga kusubiri tekelezo la hukumu hiyo.
§§§§§
MADAM S alimtzama kijana wake, Kamanda Amata, aliyekuwa ameketi kitini kwa mtindo wa kutazamana, huku glass mbili za kinywaji zikiwa kati yao zikisubiria mashambulizi.
“Kamanda najua wewe huwa ni mtu wa kunusa, una pua zenye nguvu ya kudaka harufu kama mbwa wa polisi,” Madam S alimwambia Amata kwa kumtania.
“Ndiyo kazi yangu Madam, na ndiyo maana leo nipo hapa kwa swala hili,” kamanda aliongea kwa utulivu.
“Nimekuelewa, unahisi kuna jambo zito, sawa, inawezekana, lakini sasa mtu huyo ameshahukumiwa kunyongwa unafikiri tutampataje kwa ajili ya mahojiano na hana nafasi tena ya kukata rufaa, angekuwa amefungwa sawa, lakini ananyongwa,” Madam S alionekana kuumiza kichwa kwa hilo, maelezo kutoka kwa Kamanda Amata mpaka hapo yalikuwa yamemuingia vyema mwana mama huyu hakuwa na shaka hata kidogo kwa lile analoambiwa na kijana wake, alimuamini sana kuliko mtu mwingine yoyote katika kazi zao za kiusalama.
“Ok, nafikiri fanya unachojua na mi nitafuatilia nijue kama tayari hati ya kunyongwa imesainiwa au la, kama bado tunaweza kufanya kitu na kama tayari basi hatuna la kufanya.
“Ok, nafikiri fanya unachojua na mi nitafuatilia nijue kama tayari hati ya kunyongwa imesainiwa au la, kama bado tunaweza kufanya kitu na kama tayari basi hatuna la kufanya,” Madam S alimaliza kauli yake na kujiegemeza kitini.
“Sawa mheshimiwa, nimekuelewa,” kamanda Amata alijibu kiutani kama kawaida yake awapo na Madam S. akakiacha kiti chake na kutoka taratibu, “Kamanda!” Madam S akaita, Amata akageuka kuonesha kuwa ameitikia wito, “Uwe mwangalifu sana, kila unalolipata unipe taarifa ili nijue tunafanya nini, sawa, usifanye uamuazi wowote bila kunishirikisha ili tuamue pamoja, sasa fanya utafiti wako lakini subiri amri yangu” Madam S alimuasa Kamanda Amata.
Kamanda Amata alipotoka alinyanyua simu na kupiga namba ya Jaji Ramson ambayo alikuwa ameipata kutoka katika vyanzo vyake.
“Hallo! Yeah, naongea na nani?” Ilikuwa sauti tulivu ya Ramson.
“Upo ofisini? (…) naomba nisubiri hapohapo nakuja muda si mrefu,” Madam S alimwambia Jaji Ramson. Alipokata simu hiyo akatoka ofisini na kumuachia maagizo Fulani katibu wake kisha yeye akaondoka na gari yake ya kazini, pembeni akiwa na dereva wake ambaye naye ni mwanamke. Dakika kumi na moja tu tayari gari hiyo aina ya BMW yenye rangi nyeusi iliegeshwa katika maegesho ya Mahakama ya Kisutu, kila mtu aligeuka kulitazama gari hilo maana walilijua kuwa ni gari la watu wa usalama. Madam S alishuka na kuwaendea walinzi waliopo eneo hilo, muda huo hakukuwa na vurugu ya watu kwa sababu kesi zilikuwa zimekwisha hivyo ni shughuli za kawaida tu zilikuwa zikiendelea, akaongozwa hadi katika mlango ulioandikwa kwa maandishi ya kujinyonganyonga RAMSON SEMINDU, aligonga na kukaribishwa ndani.
Jaji Ramson alimkaribisha Madam S katika kiti cha wageni huku yeye mwenyewe akiwa juu ya kiti chake cha kunesanesa, usoni hakuonekana kuwa na furaha sana lakini alijionesha kuwa yupo kawaida. Madam S ambaye amepitia mafunzo maalum ya kumjua mtu yuko katika hali gani na wakati gani alilitambua hilo.
“Jaji Ramson, naitwa Madam S, kutoka idara ya usalama wa Taifa,” Madam S alijitambulisha huku akimpa mkono.
“Ndiyo madam, karibu sana, mimi ni Jaji Ramson,” naye akajitambulisha ijapokuwa Madam S alikuwa akimfahamu siku nyingi, kama ilivyo kazi yao kufahamu watu nyeti kama hawa na kuwatumia inapobidi.
“Nakusikiliza madam,” Ramson alianzisha mazungumzo huku akimtazama madam S aliyejaa kitini kakunja nne huku sura yake ikiwa tulivu lakini isiyo na tabasamu lolote.
“Nimekuja kwa mazungumzo mafupi mheshimiwa, unakumbuka kesi uliyoihukumu leo asubuhi?” Madam S alienda ,moja kwa moja kwenye kiini cha habari.
“Yeah, nakumbuka, maana nimehukumu kesi moja tu leo iliyomhusu Yaumi,” Ramson akajibu.
“Yaumi amefanya nini?” madam S aliuliza ili kujua wapi pa kuanzishia mazungumzo yake vizuri.
“Yaumi alishtakiwa kwa kumuu mumewe na zaidi ya hapo ameua watu watatu zaidi na kufanya tukio la kigaidi huko Kampala,” Ramson alieleza kwa lugha ya kawaida.
“Lakini mheshimiwa, hujawahi kujiuliza kwa nini kesi hii ya mauaji imekwenda haraka sana na mtu kuhukumiwa kuliko kesi nyingine za namna hii?” Madam S alimkazia macho Jaji Ramson.
“Ni kweli, lakini kuwahi au kuchelewa si tatizo, kinachotazamwa ni ushahidi umekamilika na anahukumiwa kwa mujibu wa sheria, kama ilivyokuwa kwa Yaumi, upande wa mshtakiwa hakukuwa na mtetezi, hivyo moja kwa moja kesi haiwezi kuchelewa,” Ramson akajibu kwa ufasaha na kumwacha Madam S akitafakari.
“Unalosema sawa, kwa kuwa wewe ni mwanasheria, lakini kuna kitu nataka kukijua, ila nimechelewa kutambua hilo, ila nina wasiwasi sana na uwendeshaji wa kesi hii…” Madam S akaktishwa na Ramson, “Kwa nini unasema hivyo?” akauliza Ramson, “Jiulize mheshimiwa, Yaumi kaua mumewe, Yaumi kaua watu wengine watatu, kwa nini yaumi afanye hivi? Ana ujasiri gani? Lazima kuna kitu, je tazama mazingira aliyoua halafu utanipa jibu,” Madam S alimuachia kazi jaji Ramson, “Ok, Madam, kwa hiyo ulikuwa unasemaje labda? Maana hukumu kama ile haiwezi kutenguka,” ramson alimwuliza Madam S.
“Ah, mi nilijua kuwa labda kuna shinikizo nyuma yake lililokufanya uiendeshe kwa haraka hivi au ushahidi utafutwe kwa haraka namna hii,” Madam S alimweleza jaji Ramson. Akiwa bado anamwangalia usoni jaji Ramson, madam S aliona jinsi alivyo na aligundua lazima kuna kitu nyuma yake, “Hamna kitu madam, wala hamna shinikizo mama yangu, ni mambo tu yamekwenda harakaharaka basi…” kabla Ramson ahajamaliza kusema mlango ulifunguliwa na mtu mmoja mwenye mwili mnene uliojaa mafuta, mtu mzima aliingia nkatika ofisi hiyo bila ya hodi, labda kwa sababi ya cheo chake au ubabe alonao, akagongana macho na Madam S, kila mmoja alimtambua mwenzake kwa kuwa mara nyingi hukutana katika vikao vyao vya kiusalama, wakapeana mikono na kusalimiana.
Gabriel Matinya, alimkazia macho Madam S kisha akamtazama jaji Ramson, “Sasa mheshimiwa, mi si mkaaji maana naona mna mazungumzo,” lakini akaktishwa na madam S, “Hapana kiongozi, mimi nimeshamaliza yangu na sasa naondoka, pata nafasi ya mazungumzo tu,” Madam S alisimama na kuaga akaondoka mahali pale, aliteremka ngazi na kuingia katika gari yake, akatulia. Sekunde tatu baadae akafungua kijidroo cha gari yake na kuvuta kwa nje kitu kama kijiredio chenye uwezo wa kunasa sauti, akachomoa na kidubwasha kingine akakitumbukiza sikioni mwake akabofya sehemu Fulani na kile kijiredio kikawa kinawaka na kuzima taa ya kijani, huku nje ya gari antenna ilikuwa ikichomoka taratibu. “Ondoa gari,” alimwamuru dereva wake, ile gari ikatoka pale na kufika nje ya geti, ikakunja kushoto kama inaelekea Nyumba ya sanaa, ilipofika jirani na ofisi za Unicef akamwambia aegeshe pembeni, Yule mwanadada dereva akafanya hivyo.
“Huyu bibi alifuata nini hapa?” ilikuwa sauti ya Matinya katika kile chombo sikioni mwa Madam S.
“Ah, alikuja alikuwa ana wasiwasi na hukumu ya Yaumi, lakini nimemwelewesha kuwa amehukumiwa kwa mujibu wa sheria,” Ramson alimjibu Matinya.
“Ok, sawa, maana hawa ndio wambea wenyewe hawa, wakishalishika jambo au kuhisi harufu Fulani ni wafuatiliaji wa kimyakimya, mwishowe unakuta tu mambo yameharib ika,” Matinya alieleza na Madam S alisikia kupitia kile chombo.
Madam S alipoingia ofisini kwa jaji Ramson alikuwa na kidubwasha hicho ambacho alikishika mkononi mwake, si rahisi kwa mtu wa kawaida kukigundua, kina uwezo wa kunasasauti na kurusha sauti hiyo katika mfumo wa kidigitali umbali wa mita mia tano za mraba, ni kidubwasha kidogo kama kifungo kinachotumiwa sana na watu kama hawa ili kupata mazungumzo wanayoyahisi yana jambo Fulani la siri. Mazungumzo yalipokuwa yakiendelea Madam S alibaini kuwa kuna jambo zito kati ya jaji Ramson na Mheshimiwa Matinya, kwani mazungumzo yao yalikuwa ni mazungumzo ya mwisho kwa muonekano wake. Aliposikia matinya anaaga na kuwa ameweka ahadi na jaji huyo kukutana katika mgahawa wa Steers, Madam S aliridhika kwa hilo na akaona lazima alifanyie kazi. “Ondoa gari, nirudishe ofisini,” alimwambia dereva wake huku akitoa kile kidubwasha masikioni mwake na kukirudisha sehemu yake, akajiegemeza vyema katika kiti cha mbele cha abiria wakati ile gari ikiwa inaumaliza mtaa wa Ohio kabla haijazungukia barabara ya garden.
Madam S aliingia ofisini mwake na kuketi katika kiti chake kirefu kama kawaida, akavuta kitabu chake cha kumbukumbu na kukiweka jirani, akafunguan kurasa yenye tarehe na mwezi huo, hakuandika kitu kingine zaidi ya majina matatu, Yaumi lilikuwa juu kisha akaweka kamstari kuelekea chini akaandika Jaji Ramson kisha kamsatari kengine kutoka kwenye jina la jaji Ramson kikaelekea kulia akaandika Matinya, akafunga kitabu chake na kukiweka pembeni kisha akavuta gazeti la siku hiyo na kuendelea kusoma akisubiri habari nyingine kutoka kwa Kamanda Amata.
§§§§§
Toyota Land Cruiser ilisogea taratibu ikitafuta maegesho katika maeneo ya karibu kabisa na mgahawa wa Steers, ndani yake alionekana mwanadada aliyekua amenyoa upara akiliendesha gari hilo, utamjua kuwa ni mwanamke kutokana na rangi nyekundu iliyokolea mdomoni, viajana wa maegesho walimuongoza hadi mahali alipoona panafaa akalipachika hapo, akafungua mlango na kukanyaga chini taratibu kwa madaha akaufunga mlango nyuma yake. Kila mtu alimshangaa mwanadada huyu aliyeonekana kutokujali lolote, alikuwa mrefu, mwili wa wastani, hakika angefaa kuwa miss, matiti madogo yalishikwa na kifua bapa kisicho na tumbo uzembe, kichwa chake kidogo kilipendezeshwa na upara wa haja, fulana nyekundu yenye maandishi ya kijapani ilimsitiri upande wa juu wakati chini alikuwa katika jeans nyeusi aina ya HOLIFIGER, raba kali za SAUCON ziliupendezesha na kuufanya mguu wake usikutane na mchanga wa Bongo. Aliingia katika mgahawa huo na kuelekea katika meza iliyokuwa katika kona kabisa ikiwa imekaliwa na mtu mmoja tu. Muda huohuo mtu mwingine aliongezeka, sasa wakawa watu watatu walioweza kutambulika bila hiana. Gabriel Matinya ambaye kwa hadhi yake hakuwa mtu wakuwepo eneo hilo, jioni hiyo alikuwako hapo, pembeni yake jaji Ramson aliketi kwa utulivu na Yule mwanamke ambaye kwa vyovyote unapenda kufahamu ni nani.
“Ramson amefanya kazi niliyokuwa naitaka, na sasa nimefurahi kidogo kwa kuwa kuna aina ya kero ambayo imepungua upande wangu, nilimhusisha Ramson kwa sababu alikuwa na rungu katika mhimili mmoja wa serikali, ameshamaliza kazi yake na hapa nilikwambia uje umpe haki yake ya mwisho ili sasa atoke kwenye hili swala tubaki wenyewe,” Matinya alimwambia Yule mwanamke, “Lakini hujanitambulisha kwa undani,” Yule mwanamke akamwambia Matinya. “Oh samahani, uzee sasa unakuja kwa kasi, huyu ni Ramson yeye ni jaji katika mahakama kuu ila kama unavyomuona ni kijana sana hivyo unaweza kumkirimia atakalo. Bwana Ramson huyu ni rafiki yangu wa kibiashara anitwa Fasendy yeye ni Msomali, lakini huwa anakuja na kuondoka nchini kutokana na biashara zake, anaishi Masaki kama unapenda kumtembelea,” baada ya utambulisho huo, Fasendy aliifungua pochi yake na kutoa kijitabu kirefu hivi, kitabu cha hundi, akamuandikia hundi ya pesa taslimu shilingi za Kitanzania milioni moja na kumpatia, kisha Ramsoni akaaga na kuondoka, akawaacha Matinya na Fasendy.
“Niambie sasa kazi tunaanza lini?” Fasendy akmuuliza Matinya. “Sasa tunataka kushughulikia kontena la vifaa limeshafika, likitoka tu wewe utaongozana nalo mpaka mahali salama ambapo utakagua vifaa vyote, kama viko sawa, tutafanya utaratibu utaingia navyo msituni, kule vijana wako tayari wanakusubiri wewe tu ukaanze kazi ya kuwapa mafunzo makali kwa muda wa miezi mitatu, na pesa yako utalipwa kwa awamu tatu, mwanzo, kati na mwishoni. Sasa nina ahuweni kidogo kwa kuwa mtu ambaye alikuwa ni kikwazo tayari amehukumiwa kunyongwa na nina uhakika kama si kesho basi keshokutwa atapata kitanzi kwani njia yote tumekwishaitengeneza,” Matinya alifunguka kueleza mpango ulivyo. Fasendy alimsikiliza mtu huyu kwa makini sana, aliposikia swala la hukumu ya mtu kunyongwa, akashtuka kidogo, lakini alijitahidi asioneshe hali hiyo, “Nani ananyongwa na kwa nini?” Fasendy aliuliza, Matinya akamuelezea hali yote ilivyo kisa cha Yaumi mpaka dakika hiyo, Fasendy akabaki kapigwa na mshangao, ndio kwanza alikuwa akijua kuwa sakata la Yaumi linahusiana na biashara Fulani ya watu hawa ambao wamemwita yeye kutoka Somalia kuja kuwasaidia upande Fulani wa mpango wao. Fasendy alibaki kimya akimtazama Matinya bila kummaliza, alimkumbuka Yaumi, shoga yake, akajiwazia moyoni na kupata maumivu yasiyo kipimo, Fasendy akaanza kulia.
“Mmenyonga Yaumi?” akauliza.
“Ndiyo, we yaumi unamfahamu?” Matinya akauliza. “Hapana simfahamu, ila nimesoma sana habari zake katika magazeti, kesi yake ilikuwa inanipa shida sana, nilikuwa namuonea huruma sana, lakini wanawake wengine wana roho mbaya kumuua mumewe!” Fasendy alimwambia Matinya akijifanya kuwa hayupo kabisa katika hilo. “Ndiyo hivyo, na sisi tukatumia mwanya huohuo kwa kuwa mumewe alikuwa mshirika wetu sasa aliamua kutusaliti, tukaona Yaumi atakuwa kikwazo,” Matinya alimalizia mazungumzo huku akinyanyuka na kufuatiwa na Fasendy, “Sasa twende kwa bwana mkubwa la hapa tumelimaliza,” akasema Matinya na wawili hao wakaondoka na kuingia kwenye Nissan Patrol yenye namba za serikali wakatokomea mitaani.
Madam S akatikisa kichwa kuonesha kuwa kuna kitu kingine ameking’amua, akavuta droo ya dashboard ya gari na kutoa kitabu chake kilekile cha kumbukumbu akaongeza jina chini ya lile la Matinya, akaandika ‘msichana mwenye upara’ kwa kuwa hakujua jina lake. Akawasha gari na kuifuatilia ile gari waliyopanda Matinya na Yule mwanamke ili ajue safari yao inaelekea wapI.
KITUO CHA POLISI – TABATA
KAMANDA Amata alifika kituo cha polisi Tabata mchana wa siku hiyo, nje alikutana na afande Magreth akiwa pale, wakasalimiana na kusogea pembeni.
“Nipe ripoti amesema nini baada ya kumbana,” Amata alimuuliza Magreth.
“Tumembana sana usiku kucha, amesema tu kuwa yeye alipewa kazi hii kwa malipo maalumu, lakini boss kabisa wa kazi hiyo hamjui, kwa kuwa aliikuta bahasha mezani ikiwa na pesa na ujumbe wenye kazi ya kufanya, hivyo akatekeleza.” Magreth alijibu lakini alijikuta akiwa kwenye himaya ya macho makali ya kamanda Amata.
“Hayo tu? Unafikiri ni ukweli anaoueleza? Ina maana hiyo meza huwa anaitumia peke yake?” Kamanda akauliza. Magreth akajikuta anashindwa kujibu swali hilo.
“Hilo hatukuuliza,” akamwambia Amata. Kasha Kamanda Amata akaomba kuonana na mtu aliyekuwa akifanya mahojiano na Chilungu, akapelekwa ofisi ya CID na kumkuta kijana mmoja mchangamfu sana aliyevali suti nadhifu kama anakwenda harusini, Magreth akamtambulisha Kamanda Amata (ACP Jaffari) kwa kijana huyo. Kasha mazungumzo yakaendelea.
“Kwa kweli afande, huyu mtuhumiwa Chilungu kaeleza hayo tu, hata hivyo kuna kitu cha ziada katika majibu yake, inaonekana ana uhusiano na watu wa karibu wa Kizota Bar pale Segerea ama mmiliki au wafanyakazi, amesema leo hii aliahidiwa kupewa kazi nyingine na mtu huyohuyo ambaye alimpa kazi ya kwanza,” Yule kijana alieleza kifupi lakini kwa mtindo ambao majibu yalijitosheleza.
“Ok, nimekuelewa, sasa nafikiri inabidi twende hapo Kizota Bar sasa hivi tukamnase mtu huyo tukishakuwa naye mkononi kazi itakuwa nyepesi,” kamanda Amata aliwaeleza.
“Sawa afande,” Yule kijana akajibu na kusimama kutoka pale kwenye kiti, akavuta motto wa meza na kutoa pingu mbili, akazitia katika mfuko wa koti, akanyanyua redio call yake, kisha wakatoka pamoja na afande Magreth na kamanda Amata (ACP Jaffari). Kwa kutumia gari ya Kamanda Amata waliondoka eneo la Tabata na kuelekea Segerea katika bar ya Kizota iliyopo katika kona ya kuingilia Segerea makaburini.
Kamanda Amata akaegesha gari karibu na watu wa bodaboda. Wakashuka na kuingia katika bar hiyo, Magreth na Yule kijana CID wakaketi meza moja wakati Kamanda Amata akenda kaunta na kuagiza kinywaji pamoja na vya wenzake, wakaendelea kunywa wakati wakisubiri windo lake.
Waliendelea kusubiri kama lisaa limoja hivi, Kamanda Amata aliiona Lexus moja nyeusi ikiingia mahali hapo, ikiwa na muziki mnene kiasi kwamba ilikuwa kero kwa waliopo eneo hilo. Hakuna aliyelitilia maanani gari hilo, kijana mmoja akashuka na kuingia katika bar hiyo, alikuwa ni wa kawaida tu, motto wa mtaani, alionekana hivyo kutokana na mavazi aliyokuwa amevalia na minyororo aliyoning’iniza shingoni. Akaisogelea kaunta na kumbusu mhudumu kwa mbali, na Yule mhudumu bila hiyana huku akitabasamu akarudishia busu lile kwa mbali vilevile. Yule kijana akatoa bahasha ya kaki na kumpa Yule mhudumu, “Kama kawaida basi, mpigie halafu mtegeshee,” aliposema hayo Yule kijana akaondoka na kutoka nje ya bar ile. Kamanda Amata akagundua mchezo huo unaochezwa mahali hapo, akamuona Yule mhudumu akitoa simu yake na kubonyeza namba fulani, kwa kuwa waliondoka na simu ya Chilungu, Amata akamuonesha ishara Yule CID aipokee simu hiyo. Yule kijana kwa haraka akatoka pale mezani na kuelekea nje, akaipokea ile simu, “We vipi! Utapitwa na gari ya mshahara,” ndiyo lugha laiyotumia Yule mhudumu huku asijue anaongea na nani. Yule CID kule nje akajifanya kukohoa kwa kuwa alijua sauti yake haitofanana na ya mlengwa. “Vipi kwani tayari?” aliuliza, “Ah muda tu, nakuwekea palepale,” akamwambia, “Poa fanya hivyo nipo tu hapa nje si mbali,” Yule CID akajibu.
Muda huohuo Yule msichana akatoka na ile bahasha na kuiweka katika meza fualani pamoja na bia ya Kilimanjaro akatumia kuikandamiza isipeperuke, akaiacha na kuondoka. Wakati Kamanda akishangaa tukio hilo akamkumbuka Yule kijana aliyeleta ile bahasha, akageuka kumtazama, akakuta ile gari haipo, akabaki mdomo wazi, akashuka pale katika stuli ndefu na kuelekea nje, hakuiona hata ilikoendea. Akarudi ndani na kumuona Yule CID akiingia kutoka nje, mara hii alikuwa akiielekea ile meza iliyokuwa na bahasha, alipofika akaisogeza bia pembeni na kuinyakua bahasha, Yule mhudumu akaja mpaka pale, “Samahani kaka sio ustaarbu, kuna mteja nimemuwekea hiyo bahasha yake na bia akija atalalamika wewe kuichukua, mbona watu hamjiheshimu ee?!” Yule mhudumu alikuwa akiongea Kiswahili cha waswahili kanakwamba anakusuta. Kamanda Amata akasogea mpaka pale, na kusikiliza mzozo huo, “Kwani we unamjua mwenye bahasha hii?” Yule askari akauliza.
“Ndiyo namjua na nimempigia simu sasa hivi!” yue mhudumu akaeleza.
“Mpigie tena basi,” Yule aksri amwambia na Yule mhudumu bila kujali akachomoa simu yake na kupiga zile namba, simu ikaita mkononi mwa Yule CID. Kwa kitendo hicho Yule mhudumu akabaki hana la kusema.
“Dada mimi ni afisa wa polisi, kuanzi sasa upo chini ya ulinzi,” Yule askari akamwambia. Magreth akafika na kuchukua pingu kwa Yule CID akamvesha na kuondoka naye mpaka kawenye gari waliyokuja nayo, pamoja na malalamikop yote aliambiwa tu atajua hiyo kesi polisi.
Wakiwa ndani ya gari kamanda Amata akaichana ile bahasha na kuifungua ndani, kulikua na hundi ya shilingi million mbili na kijikaratasi kidogo kilichosomeka ‘Dr Omongwe Shabani, Magereza Segerea, zahanati, zamu ya usiku leo,’ akaingiza mkono katika kijidroo cha gari akatoa kitu kama mkebe wa kompasi lakini mwembaba wa plastiki akaufungua na kuilaza ile hundi ndani yake, akafunga vizuri, kisha akabonyeza kitufe Fulani, na kitu kama mwanga kikaonekana kikitembea ndani ya kimkebe, alipokamilisha zoezi hilo Amata akarudishia kama vilivyo na kumpa Yule CID, “Hii ni kwa ushahidi wako wa kesi.”
Kutoka kwenye kile kimkebe akafungua kwa chini na kutoa hundi nyingine ya mfano uleule akaikunja na kuitia mfukoni, alikuwa ameitoa kivuli chake ‘photocopy’.
§§§§§
Wigo mkubwa wa ukuta ambao juu yake uliwekwa vipande vya chupa ulilificha jumba la kisasa ndani yake, lango lake lililoonekana kujifungua lenyewe liliruhusu gari ya Matinya na Fasendy kupotelea ndani kasha nalo likafichwa humo. Madam S alipita taratibu na gari yake na kuelekea mbele zaidi, alipoona panamfaa akaegesha gari pembeni na kuchukua simu yake, akabonya namba Fulani ambayo iliita moja kwa moja katika ofisi za ardhi kitengo cha mipango miji, akamuulizia mtu anayemfahamu na mara moja akampata, akamtajia namba za lile lango la ile nyumba zilizokuwa zikiashiria namba ya kiwanja, akahitaji kuambiwa ni nyumba inayomilikiwa na nani au kampuni gani, kasha akasubiri jibu. Hakuchukua muda mrefu, akatumiwa meseji kuwa ni nyumba inayomilikiwa na idara ya ushuru na forodha ya serikali, akamshukuru sana huyo aliyempa jibu na kukata simu kasha akapiga namba nyingine kwa rafiki yake ambaye ni mmoja wa waajiriwa katika idara hiyo, akauliza kama anamjua mtu anayeishi katika jumba hilo, akajibiwa ni meneja wa idara hiyo kanda ya Dar es salaam, Madam S akaona kuwa mpaka hapo alikuwa amefanya kazi kubwa ambayo hakupaswa kuifanya, akarudi ofisini huku akiwa amemwambia Chiba wakutane hapo ofisini kuna kazi ya ziada.
Majira ya saa tisa walikutana ofisini kwake katikati ya mji karibu kabisa jumba la mkuu wa nchi.
Madam S akiwa kitini kwake alionekana kuchoka sana. “Bibi ustahafu sasa, utakufa kwa mawazo!” Chiba alimtania wakati akiingia ofisini kwa Madam S.
“Na we usianze maneno kama kaka yako Amata, na leo mpaka sasa yupo kimya hajanipa lolote,” Madam S alikuwa akimwambia Chiba maneno hayo huku akichukua kinywaji kwenye glass na kumpatia.
Akachukua kamera yake ndogo na kuweka picha ya Yule mwanamke mwenye kipara, “Chiba, hebu mtambue huyu mwanamke,” Madam alimwambia huku akiwa anamkabidhi ile kamera. Chiba aliichukua na kuiangalia ile picha kwa makini sana, kasha akaihamishia kwenye kompyuta yake ndogo na kasha kuiingiza kwenye mtandao wa kiusalama na kusubiri pale mtandao huo ulipomwambia loading, mara ile picha ikarudi pale kwenye kioo na nyingine kama ishirini hivi, kati ya hizo picha tisa zilioana na kumuelezea Yule mwanamke kama mwanamke hatari katika medani za kijeshi, mzaliwa wa Somalia, aliyepitisha maisha yake kwa miaka mingi katika magenge ya wahuni na waasi, alilitumikia jeshi la Somalia kwa miaka minne na kisha kutoroka ambako mpaka sasa anatafutwa, taarifa zile zilionesha mpaka hati yake ya kusafiria pamoja na alama za vidole. Chiba akamjulisha majibu hayo Madam S. kwa taarifa hizo akashtuka sana na kung’amua jambo zito la mbeleni.
“Vipi Madam, unamhisi?” Chiba akauliza.
“Yeah, Chiba, hapa kuna jambo zito lazima tuwe tayari kwa kazi ngumu, mwitw Amata tafadhali, tuifanye kazi hii kiofisi zaidi” Madam S akamwambia Chiba.
§§§§§
Matinya, Fasendy na mtu mwingine mkubwa katika idara cha ushuru wa forodha walikuwa bandarini mida ya jioni ya siku hiyo. Huko katika gati namba tano ambako meli kubwa ya LINEA MESSINA ilikuwa ikipakua makontena mengi yaliyojazwa kama viberiti, lilikuwamo kontena moja la futi arobaini mali ya kampuni ya MG investment lilikuwa tayari limeteremshwa na kuwekwa pembeni tofauti na mengine. Likafunguliwa vifungo vyake na milango yake kubaki wazi. Fasendy akaingia ndani ya kontena hilo na kupepesa macho haraka haraka, akatoka na kumfanyia Matinya ishara ya dole gumba.
Matinya akanyanyua simu yake na kupiga anapopajua yeye kutoa taarifa kuwa mzigo umefika.
“Kwa hiyo mheshimiwa!” Matinya alimwuliza Yule kibosile wa idara ya ushuru.
“Yaani hapo kajipangeni mi mnitoe milioni ishirini tu huu mzigo kesho mnauchukua na hakuna atakayewakagua njiani, hii nchi yetu bwana.” Yule mkuu wa idara akamjibu Matinya.
Baada ya mazungumzo yao wakaagana na kila mmoja akaondoka eneo hilo. Fasendy na Matinya wakaingia kwenye ila gari ya serikali na kuondoka eneo hilo.
“Fasendy, nataka ndani ya mwezi mmoja wale jamaa kule chaka wawe kamili, maana shughuli yetu lazima ifanyike miezi miwili mbele kwa ufanisi wa hali ya juu. Leo usiku tutakuwa na kikao pale Paradise Hotel Bagamoyo, nakualika uwepo ili ujue mikakati yote jinsi ilivyo,” Matinya akamwambia Fasendy.
“Hamna shaka, ukiwa na mimi amini hakuna lisilowezekana, hili ni jeshi la mtu mmoja, waulize al shabab watakwambia mimi ni nani,” Fasendy alijigamba mbele ya Matinya.
OFISI KUU T.S.A
MADAM S alikutana na vijana wake makini wawili, Kamanda Amata TSA 1, Chiba Chibila TSA 2.
Kilikuwa ni kikao cha dharula siku hiyo jioni, wakichanganya mawazo ili kupata picha kamili ya lile wanalolizungumzia.
“Kamanda Amata, nieleze umefikia wapi katika jitihada zako?” Madam S alimuuliza Amata. Baada ya kutafakari kama sekunde thelethini hivi, Kamanda Amata akafungua kinywa chake na kueleza kuanzi pale alipoanza kuhisi kitu katika kesi ya Yaumi mpaka kifo cha Chonde na kumalizia juu ya mkakati wa kumsaka muuaji na waliomtuma. Lakini habari iliyomgusa sana Madam S ni juu ya ile hundi ambayo Kamanda Amata aliitoa kivuli kuwa ameifuatilia katika benki husika na kugundua ni nani mmiliki wa kitabu hicho cha hundi, na jina alilopewa hakuweza kuamini hata kidogo, jina la mtu mkubwa serikalini, Madam S alibaki midomo wazi, hakuamini anachokisikia, alimtazama Kamanda Amata na kuamini huyo jamaa ni kiboko na kweli anastahili kuwa namba moja katika idara yao nyeti, idara isiyo na mipaka, yenye kibali cha kuua au kumlinda mtu yeyote, yenye kuzuia au kuruhusu jambo lolote litokee ili mradi azma na lengo la kazi litimie.
“Kazi nzuri Kamanda Amata,” madam S alimpongeza kwa hilo, kisha nae akaanza kuwaelezea juu ya safari yake kwa jaji Ramson na mazungumzo yao, kisha akampa Chiba kile kifaa kilichonasa sauti ya mazungumzo ya Matinya na jajai Ramson, baada ya hapo akawaelezea alivyomfatilia Matinya na Fasendy mpaka kwenye lile jumba la meneja wa idara ya ushuru na forodha kule Masaki.
“Madam, nafikiri umeona nililokuwa nakwambia, nyuma yah ii kesi kuna mpango mzito,” Kamanda Amata alililieleza jopo.
“Sasa Kamanda na Chiba kwa kuwa kazi hii inayowahusu baadhi ya vigogo wa serikali, naomba ifanyike kwa siri sana, ila itakapofikia siku ya kufanya hivyo ndipo umma wa Watanzania utakapojua uovu wa wale wanaowapigia kura ili siku nyingine wajue nani ni nani,” madam S aliwaeleza Chiba na Amata.
“Sasa Madam, mi nafikiri ili tuujue ukweli wa hili lazima tumpate Yaumi,” Chiba alieleza.
“Lakini Yaumi ananyongwa, na kwa taarifa ambayo ninayo Yaumi ananyongwa kesho mchana wa saa saba katika gereza la Ukonga na mheshimiwa ameshasaini hati yake ya kunyongwa, tutafanyaje?” Madam S aliwaeleza.
“Hapo tuna mtihani mgumu, tungejua mapema tungefanya utekeji palepale atokapo mahakamani, sasa tutafanya nini?” Chiba aliuliza kwa wasiwasi.
“Yaumi atapatikana tu, Chiba kesho tunaenda kumtoa Yaumi gerezani, jipange,” Kamanda Amata akamwambia Chiba.
“Aaaa maadam umesema wewe Kamanda, hakuna kitakachoshindikana,” Chiba aliitikia.
“Mtafanyaje kumpata?” Madam S aliuliza.
“Madam S, mi na Chiba, we tuachie hiyo kazi, ikifika kesho saa tano chukua gari yetu ile prado isogeze karibu na gereza, Yaumi kesho tunamtoa, na hiyo itaitwa ‘mpango wa ukombozi’ tutakapompata tu ni moja kwa moja shamba, tunamficha dunia isimuone mpaka ukweli utakapodhihirika” Kamanda Amata akamweleza madam S.
Madam S aliwatazama vijana hawa kwa dhamu na kutabasamu kwa kuelewa kuwa kazi inawezekana. Madam S akamuomba Chiba amuonesha Amata ile picha ya Fasendy.
Amata aliitazamaile picha kwa makini sana, “Vipi, unamjua?” Chiba aliuliza. “Hapana simjui,” Kamanda Amata alijibu. Chiba alimpa Kamanda maelezo yaliyopatikana juu ya mwanamke huyo hatari kuliko hatari yenyewe, akayasoma kwa makini sana, “Ujue kabisa ipo siku ya kupambana nae,” Chiba alimweleza Kamanda.
Baada ya kikao hicho kilichodumu kwa takribani masaa matatu, mwisho mkakati ukapangwa wa jinsi ya kumtoa Yaumi gerezani kwa mbinu ambazo hazielezeki. Jambo kubwa la kwanza ilikuwa ni kutafuta ramani ya gereza ilo ambalo limejengwa na wakoloni wa Kiingereza miaka mingi nyuma kabla ya uhuru, lakini je ramani hiyo itapatikana wapi, si ajabu hata haipo nchini. “Sasa kutafuta ramani hiyo itakuwa ni sawa na kutafuta maiti ya kumi katika kisa cha Gharama ya damu kilichoandikwa na Richard Mwambe,” Madam S akawaeleza kwa kuwatatnia, wote wakacheka na kuanza kukumbushana juu ya kisa hicho kilichovuta hisia za watu wengi duniani.
§§§§§
Kama kuna siku ambayo matinya na washirika wake walikuwa na furaha basi usiku wa siku hiyo ambayo Yaumi alihukumiwa kunyongwa. Walikutana katika hoteli ya Paradise huko Bagamoyo na kupongezana kwa hatua hiyo kubwa. Wakisherehekea kumaliza awamu ya kwanza na sasa kuanza awamu ya pili ya mkakati wao. Miongoni mwao alikuwa Gabriel Matinya mwenyewe, Fasendy (mwanamke mwenye upara), OCD Kambale, meneja wa idara ya Ushuru na forodha, mtu mmoja mwenye asili ya kiarabu aliyejulikana kwa jina moja tu la Salim, tajiri mkubwa sana kutoka Oman, pia kulikuwa na mtu mwingine mkubwa tu kicheo katika jopo la watu wa karibu na mkuu wa nchi. Vyakula viliteketea na makumi ya chupa za pombe zaaina mbalimbali kumiminiwa katika matumbo hayo yasiyo na shukrani. Pamoja na hayo kulikuwa na mazungumzo ya hapa na pale kati ya hao.
Matinya alionekana ndiyo mwenyeji zaidi wa tafrija hiyo isiyo rasmi, wakiwa wameketi katika meza zilizounganishwa kwa mtindo wa duara, walikuwa ni wao tu katika ukumbi huo mdogo ambao mlango wake umepambwa kwa maandishi yaliyosomeka VIP Lounge
Katikati ya shughuli hiyo alisimama bwana Gabriel Matinya na kuzungumza machache na wenzi wake hao.
“Napenda kuchukua nafasi hii kukushukuruni nyote kujumuika jioni hii hapa Paradise, nafikiri si wote tunafahamiana, lakini si mbaya wakati huu ukawa ni wakati muafaka wa kusalaimiana, kwanza kabisa tunae mtu wa juu kabisa ambaye ndiyo namba moja wetu katika mpango huu, yeye anaishi nje ya nchi lakini atakuja nchini hapa usiku huu kwa ajili ya kuanza rasmi mkakati wetu, tunaye namba mbili wetu ambaye ni mimi ninayeongea, namba tatu yeye tupo nae hapa,” akatulia kidogo na kumtazama bwana mkubwa mmoja aliyeketi huku mikono yake kaikutanisha juu ya tumbo kubwa lililojazwa na ufisadi uliokithiri, kisha akaendelea, “Hao niliowataja kwa namba ndiyo walioshika hatamu katika mkakati huu, zaidi yao tuna mkufunzi wetu wa mafunzo haya nyeti bi Fasendy kutoka Somalia, ndiye mkufunzi wa mafunzo yetu, hapa tuna Bwana Salim, millionea kutoka Oman, ndiye anayefadhili mkakati wetu huu na kuhakikisha lazima ufanikiwe, zaidi ya hapo tuna rafiki wa karibu Bwana Gomegwa ambaye ni meneja wa idara nyeti ambayo tunaihitaji kuitumia kwa sasa, idara ya ushuru na forodha, tukiachana na jopo hili la juu, tuna kikosi kazi ambacho kinatekeleza kila linalotakiwa ili kuhakikisha mkakati wasioujua unafikia lengo lake, hwa wako nje ya hapa na hata sasa wako kazini kuhakikisha mambo hayaharibiki. Ijapokuwa tulikwamishwa na mtu mmoja lakini kwa sasa tayari hatma yake imekamilika na hivi ninavyoongea jua la saa nne kesho litakuwa ni la mwisho kwake, na mi nitakuwa pale kushuhudia tukio hilo. Tuendelee kula na kunywa bila shaka yoyote na kazi inaendelea kama tulivyopanga,” Matinya alizingumza mengi katika hafla hiyo lakini hakutaja kabisa ni mkakati gani unaozungumziwa hapo, wala hakutaja namba moja wa mpango huo ni nani. Katika hafla hiyo kulikuwa na namba mbili tu na namba tatu pamoja na hao waliotajwa.
Wakati wa hafla hiyo Fasendy alionekana wazi kutokuwa na furaha, alizama katika lindi la fikra na mawazo, hakuna aliyejua mwanamke huyo anawaza nini, Matinya alimgutusha mara kwa mara na alipomuuliza anawaza nini, jibu lilikuwa ni ‘Napanga mkakati wa kazi,’ lakini kiukweli Fasendy alikuwa anafikiri jinsi gani rafiki yake Yaumi waliyekutana mahabusu atanyongwa kwa ajili ya kuhakikisha mkakati huo unafaulu nay eye akiwa mmoja wa watu wanaounda au kuhakikisha lengo linafikiwa, akiwa analipwa pesa nyingi tena za kigeni. Fasendy alionekana wazi kuumia kwa kitendo hicho, alifikiri kuwa kama angelijua mapema basi angeshamtorosha Yaumi na kumhifadhi mbali na watu hao au angemsaidia kwa namna moja ama nyingine kufanikisha lengo lake la kulipiza kisasi cha kifo cha mumewe, hakika ilikuwa ni mapigano makali katika nafsi yake, ‘Nitamsaidiaje Yaumi? Nimechelewa, bado masaa machache atakula kitanzi, kitanzi ambacho si haki yake,’ Fasendy alijiwazia na alikuwa akiumia tangu ndani ya moyo wake.
§§§§§
Wakati wengine walikuwa wamelala usiku huo, wengine wakisherehekea kufanikisha mipango yao, mwingine akiwa gerezani akisubiri kunyongwa, ni watu watatu ambao walikuwa hawajalala, walikuwa wakifanya kazi ya ziada kuhakikisha mmoja anapona na wengine wanaangamia.
Kamanda Amata, Chiba na Madam S walikuwa katika ofisi nyeti au ‘Shamba’ kama wanavyoiita iliyopo huko Gezaulole, ng’ambo ya bahari, pande za mbali za Kigamboni, ni moja kati yab majengo mkongwe ya wakoloni wa kiarabu, lakini lilifanywa kuwa ofisi nyeti kwa kazi za kitengo hiki muhimu katika serikali. Ukilitazama kwa nje jengo hilo ambalo ni gofu, lilikuwa halina matunzo kabisa, hakuna mtu aliyejua kama humo ndani huwa kuna watu wanashughulika na kazi mbalimbali, na ukizingatia lilikuwa mbali kidogo na makazi ya watu, hali hiyo ilisaidia kuficha siri nyingi zilizopo hapo ndani, wengi waliamini kuna mashetani yanaishi ukizingatia nyakati Fulani wanaona taa ya ndani ikiwaka na wakati mwingine ikizimwa.
“Sasa hii ni ramani ya zamani sana, si unaona jinsi ilivyochakaa,” Chiba aliwaonesha Madam S na Kamanda Amata, “Unaona hapa ni lango kuu, linatazama kaskazini, huku mbele ndiyo barabara ya Pugu, upande wa mashariki wa gereza hili kuna makaburi ya zamani sana, inasemekana walikuwa wanazika wafungwa hasa waliokuwa wakinyongwa enzi hizo, na hizi ni nyumba za staff, kusini mwa gereza kuna uwanja wa mpira, ukiwa umezungukwa na nyumba za askari, upande wa Maghalibi kuna barabara inayoelekea chuo cha maafisa wa magereza. Hili gereza lina milango mikubwa miwili ya kuingilia ndani, kuna lango kuu upande wa Kaskazini unaotumika na wafungwa pamoja na askari pia raia wanaokuja kuwatembelea ndugu zao, mlango huu upo karibu na lango kuu la kupitia magari yote yanayoingia katika eneo hilo na linalindwa na askari watata kabisa wa KM, lango la pili lipo kusini, huku linatazamana na nyumba za askari, lango hili hutumika kuingilia mahabusu kwa kuwa mahabusu iko upande huu, watuhumiwa wote wanaotoka mahakamani huifadhiwa upande huu. Gereza hili lina vilinge sita vya walinzi juu kabisa ya ukuta huu mrefu ambao umezungukwa na zao la mkonge kwa mita mbili kutoka katika ukuta,” Chiba alikuwa akiichambua ramani ya gereza hilo kwa nje, ramani iliyochorwa miaka mingi nyuma, enzi za wakoloni.
“Aisee, hapa kibarua kipo,” Madam alisema kuonesha kuwa bado alikuwa hajui nini kitafanyika katika mpango huo. Kamanda Amata aliitazama tena ramani ile kwa umakini wa hali ya juu sana, kwa jinsi ulinzi ulivyokuwa umetanda nje kadiri ya maelezo ya Chiba ilikuwa ngumu kwa wao kuingia kwa njia ya kawaida.
“Ok, Chiba, sasa hapa kitanzi kipo wapi?” Kamanda aliuliza.
“Hapa kitanzi kipo upande huu wa Kaskazini mashariki, kwenye hiki chumba kikubwa, ambapo mlango wa kuingilia ni huu,” Chiba alikuwa akionesha kwa uhakika kupitia ramani hiyo.
“Na hiki kilichopita hapa ni nini?” Madam S alimuuliza Chiba.
“Kwa maelezo yalioyoandikwa ni kuwa hili ni bomba la maji taka ambalo hutpitisha maji kutoka gerezani na kumwaga huko mchafukoge,” akawaeleza.
Ramani ile ikageuzwa upande wa pili kulikokuwa na michoro mingine kama mine hivi iliyoonesha hasa muundo ya ndani na nje ya gereza hilo.
“Hapa kwenye hii point ni ghorofa au kitu gani?” Kamanda aliuliza.
“Ndiyo, hapa kwenye chumba cha kitanzi ambacho kimejengwa kwa chini kikitanguliwa na kitu kama shimo, juu yake kumejengwa jengo lenye urefu wa ghorofa sita, unaweza kupitia kwa ndani kutoka katika chumba cha kitanzi na kuibukia katika ghorofa hilo,” Chiba aliendelea kujibu maswali ya maswahiba wenzake.
“Ok, kazi imekwisha, Mimi na Chiba tutafanya kazi hiyo, Madam utakuwa katika kikosi cha ukombozi,” kamanda Amata alikuwa keshapata wazo la nini cha kufanya ili kuweza kufikia hapo anapotaka. Waliangalia saa ya ukutani, ilikuwa tayari imetimu saa nane za usiku, wakachukua vifaa vya muhimu kwa kazi hiyo, kwa maana waliona wazi kuwa hakuna nafasi nzuri ya kuingia katika gereza hilo isipokuwa ni muda huo wa usiku ili asubuhi iwakute katika maficho ndani ya gereza hilo, walichofikiri wao ni kupata nafasi tu ya kuona kile ambacho kitatukia kwa Yaumi na kujua ni jinsi gani wataondoka nae pale endapo watafanikiwa azma hiyo. Kamanda Amata akiwa ndani ya suti yake nadhifu ya kijivu, juu yake akatupia suruali ya jeans na jacket refu jeusi kabla hajaweka ile ninja yake na kujificha sura yake. Chiba na Amata walikuwa tayari, Madam S aliwachukua katika gari yao na kuja nao pande za Ukonga…
UKONGA
ALFAJIRI
SIKU ILIYOFUATA
ALFAJIRI ya siku hiyo ilimkuta Kamanda Amata na Chiba ndani ya kona tata ya Gereza la Ukonga, katika chumba maalum cha kitanzi, juu ya chumba hicho kulijengwa kighorofa kirefu ambcho kilikuwa na mlinzi upande wa juu kabisa. Chiba na Kamanda Amata waliingia ndani ya ngome hiyo usiku wa saa tisa kwa kupitia tundu lenye ukubwa wa mdomo wa ndoo, tundu hilo linalotumika kupitisha maji machafu ya jikoni na kuyatiririsha nje ya ukuta wa ngome hiyo. Baada ya kujipenyeza kwenye njia hiyo bila kuonekana walitokea jikoni na kisha wakapita kwenye dirisha dogo la kupitishia chakula cha wafungwa na kujikuta wapo katika tundu kubwa la mlango ambalo linakuwezesha kuona eneo kubwa la ngoome hiyo kwa ndani, taa kali zilikuwa zikimulika eneo hilo kiasi kwamba kila kinachopita lazima kionekane bila kujificha.
Mpango huo ulikuwa ni mpango salama, haikutakiwa hata tone la damu liguse ardhi, hiyo ndiyo tahadhari waliyopewa na mkuu wao wa kazi, Madam S, nao walihakikisha wanaitii. Hakukuwa na njia nyingine zaidi korido ndefu inayopita pembezoni mwa stoo iliyofungwa kwa milango madhubuti ya chuma, na korido hiyo ilikuwa iking’azwa kwa mwanga mkali wa zile taa kubwa zilizofungwa juu ya ukuta na zingine kwenye nguzo za chuma zilizogeukia pande zote. Hakukuonekana mtu katika eneo hilo, hiyo ilikuwa ni hatari zaidi, kwa maana Chiba na Amata hawakujua zaidi ya taa ni kitu gani kingine kinaongeza ulinzi eneo hilo kama hakukuwa na askari anayezungukazunguka. Kwa kutumia vifaa maalumu, TSA 1 aliweza kuwasiliana na TSA 2 bila kutoa sauti, kwa kunong’ona tu, kijipande kidogo chenye waya mwembamba kilitumbukizwa sikioni mwa mhusika na kisha waya wake kufichwa kwa kuzunguka shingo ndani ya vazi la mtumiaji na huo ndio unaopokea na kurusha mawimbi, kifaa hicho kinachounganishwa na simu ya mkononi ambayo imewekwa mahali pengine ikiwa imewashwa hurusha na kupokea mawimbi ya sauti kwa kutumia Bluetooth, kina uwezo wa kunasa mawimbi kutoka umbali mrefu. Simu iliyokuwa ikiwaunganisha ilfichwa katika moja ya vichaka vilivyo nje ya eneo hilo. Madam S aliweza kunasa mawasiliano hayo akiwa maenso ya Banana, kaegesha gari yake kama wateja wengine wa klabu ya usiku waliojazana katika moja ya klabu hiyo wakivinjari na wenzi wao kwa kula na kunywa. Katika gari yake akiwa na kopo tatu za redbull alikuwa aksikiliza muziki laini sana uliokuwa ukitoka katika spika za gari hiyo.
Kamanda Amata ilibidi achukue muda wa ziada kujaribu kuona atafanya nini juu ya zile taa ili aweze kupita yeye na pamoja na Chiba, alijaribu kukagua eneo hilo walilojificha, hakuona cha maana sana zaidi ya makorokoro yaliyojazana bila mpango. Akisaidiwa na miwani inayoweza kuona gizani ‘night goggles’ Chiba aliona waya mnene uliopita eneo hilo kuelekea mahali Fulani. Akajadiliana na kamanda lakini wakaona si vyema kutumia waya huo kuondosha mwanga katika eneo hilo. Katikati ya uwanja wa gereza kulikuwa na mti mkubwa sana, wakati wakiwa katika majadiliano ya kuwa wafanye nini kuweza kupita katika eneo hilo bila kujulikana, walijaribu kuangalia vilinge vya walinzi walio jirani kuona kama wamesinzia au la, walitumia darubini yenye nguvu kwa kazi hiyo. Lakini walinzi makini, hakuna aliyeonesha kulala wala nini, wote walikuwa makini na bunduki zao SMG zilizoshiba risasi. Kamanda Amata akasikia mlio wa kunguru kutoka kwenye ule mti, akampa ishara Chiba kuwa inawezekana kutumia mbinu hiyo ya Kunguru. Daima Kunguru hakai mmoja katika mti, hukusanyana familia nzima au tungeita ukoo.
Amata akampa maelekezo machache Chiba kwa majaribio kama mbinu itafanikiwa. Akachukua short gun akachomoa magazine iliyojaa risasi za moto na kupachika nyingine iliyokuwa na risasi za mipira, kisha akalenga ule mti, huku akiwa kafunga kifaa maalum cha kuzuia sauti ya bunduki ile, akafyatua risasi kama kumi hivi juu ya ule mti, muda huohuo, kundi la kunguru lilitimka kwenye ule mti, Kamanda Amata akmpa ishara Chiba na kwa kasi wakapita kwenye le korido mpaka wakaufikia mlango walioukusudia, wakati bado wale Kunguru wakipiga makelele na kuruka huku na kule, tayari Kamanda Amata alishacheza na mlango wa chuma ulioweka nkizuizi cha kuingia chini ya ghorofa hiyo iliyo katika kona ya kaskazini mashariki mwa gereza hilo, wakaurudishia mlango nyuma yao na kuufunga wa ndani kisha wakatulia bila kufanya mjongeo wowote wakikisoma chumba hicho kiko vipi.
Chumba kilikuwa giza kabisa, lakini waliweza kuona vizuri kabisa kila kilichomo, viti vichache na mbele kabisa palikuwa na kitu kama jukwaa dogo ambapo kama ni mtu akisimama basi wote mliokaa vitini mtamuona kwa juu kidogo. Kamanda Amata akashusha pumzi na kutazama vizuri, kwa haraka haraka akajua kuwa hicho ni chumba maalumu kwa kazi ile wanayoitarajia, mbele yake kulikuwa na ngazi inayopanda juu kidogo ambako viti vile vilipangwa, na ngazi nyingine ilikuwa ikielekea chini ambako palikuwa na mlango wa mbao. Akashuka mpaka kwenye ule mlango na kuufungua kwa hadhari kubwa, naam, palikuwa na kaveranda kadogo juu yake hapakuwa na dari bali uwazi mkubwa ulioweza kuonesha juu kulikokuwa na kamba nene iliyofungwa vizuri kwa umadhubuti kabisa. ‘Hapa huponi’ Chiba alijiwazia huku akiwa anapanda ngazi zinazoelekea juu, akaingia kwenye korido Fulani na kutafuta mahali pazuri na kujificha, wakati huo aliweza kuona eneo la tukio kwa uzuri kabisa. Kama si mtaalam wa mambo ya kijasusi huwezi kumgundua Chiba kwa jinsi alivyojichanganya na vitu vingine katika eneo alilojificha, vivyo hivyo kwa Kamanda Amata ambaye naye alikuwa kajificha katika upande mwingine.
§§§§§§
Tafrija ya akina Matinya na washirika wake ilifikia tamati mishale yaa saa nane usiku, kwa ujumla mipango yote ilikuwa ipo sawa. Baada ya tafrija hiyo waalikwa waliondoka kujiandaa kwa majukumu yanayomkabili asubuhi ya siku hiyo.
Gabriel Matinya alitoka hotelini hapo majira ya saa kumi alfajiri, kwenye gari yake alikuwa pamoja na OCD Kambale na Fasendy. Moja kwa moja walifika katika jumba la Fasendy huko Oysterbay na kumuacha wakikubaliana kukutana nae jioni ya siku hiyo ikiwa tayari mzigo wao umekwishatoka bandarini, meneja wa idara ya Ushuru na forodha alikuwa tayari ameshashikishwa hundi yake ya milioni ishirini ili kufaulisha mzigo huo kwa njia zisizo rasmi.
Asubuhi hiyohiyo ilimkuta afande Marina kazini, katika gereza la Segerea. Akiwa amesimama nje huku akionekana kama mtu anayesubiria jambo Fulani, alishtuka alipoona gari ya Dr Omongwe ikimfungia breki miguuni mwake, “Afande vipi, unaota jua?” lilikuwa swali la Omongwe ambalo kwa Marina lilikuwa kama mkuki wa moto moyoni, alishindwa kujibu, ukizingatia alishaambiwa na Matinya kuwa baada ya kifo cha Chonde kitafuata kifo cha Omongwe kwani yeye ndiye aliyejua japo kwa kidogo juu ya sakata la Yaumi na pia ni mtu wa karibu sana na Yaumi. Marina hakuamini kama anayemuona mbele yake ni Omongwe au mzimu wake. “Nipo Dr, si unajua huku kwetu asubuhi ni kabaridi Fulani hivi,” alijibu, na ile gari ikaendelea mbele kwa mwendo wa polepole mpaka ilipoegeshwa mbele ya zahanati ya magereza.
Marina alinyanyua simu yake na kupiga namba Fulani, akaweka sikioni kusikiliza upande wa pili.
“Hello, beibi hivi upo siriasi na mambo yako au la?” ilikuwa sauti ya Marina kwa Matinya kupitia simu hiyo.
“Kwa nini wasema hivyo?” Matinya akauliza.
“Ulinambia kuwa baada ya kupotea namba moja atapotea namba mbili,” Marina alizungumza kwa lugha ngumu kidogo.
“Ndiyo kwani vipi?” Matinya akauliza tena.
“Huyu hapa, mzima wa afya, ina maana mpango umefeli,” Marina alimpa taarifa kisha akakata simu.
Mheshimiwa Gabriel Matinya, mtu mkubwa katika idara za usalama ndani ya wizara nyeti ya mambo ya ndani na usalama wa raia, alihisi baridi kali likipita katikati ya mwili wake na kuishia miguuni. Akiwa tayari ndani ya sare yake ya kazi, safari ya asubuhi hiyo ilikuwa ni kuelekea katika Gereza la Ukonga ambako Yaumi alikuwa kwenye orodha ya kunyongwa baada ya adhabu hiyo kusitishwa kwa miaka mingi. Matinya alishindwa kuchanganyikiwa kwa habari hiyo, akarudi kitini akatafakari kwa kina, akainua simu na kumwita Scogon, akampa ujumbe afuatilie kujua imekuwaje Dr Omongwe hajauawa wakati ilipangwa asubuhi hiyo awe marehemu. Hali ilikuwa hivyohivyo kwa Scogon, alipatwa na kigugumizi cha maamuzi, kazi ngumu. Scogon akawaweka sawa vijana wake na kuanza kufanya uchunguzi kwa mtu waliyempa kazi hiyo, ambaye hakutakiwa kuwahusisha vijana hao, majibu waliyoyapata hayakuwaridhisha, walimpata Yule aliyepewa kazi, nay eye akawaambia kama ilivyokuwa mwanzo ujumbe ulifika kwa mhusika anayehusika kwa utekelezaji, na ujumbe ulifika kwa njia ileile kama ya mwanzo. Scogon akamuamuru afuatilie na ampe jibu hilo mara moja kwa njia ya simu. Ilikuwa ni utata juu ya utata, kila mmoja alikuwa amechanganyikiwa kwa upande wake.
SAA 3:30 ASUBUHI
VIONGOZI mbalimbali walikuwa katika eneo la Gereza la Ukonga, mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, kiongozi wa juu kutoka Jeshi la wananchi, kamishna wa Magereza, mkuu wa wilaya pamoja na kiongozi wa jeshi la polisi bwana Gabriel Matinya. Kutokana na kibali cha mkuu wa nchi, viongozi hao wa juu katika idara ya usalama nchini walijumuika kushuhudia kunyongwa kwa mwanadada Yaumi. Wote walikuwa tayari ndani ya eneo husika walilotakiwa kuwapo, ni miaka mingi ilipita adhabu hiyo haikutekelezwa na taifa hili lakini siku hiyo ilikuwa itekelezwe. Pamoja na kuwa mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yamepinga adhabu hiyo kutekelezwa, bado baadhi ya mataifa huko Asia na kwingineko yalikuwa yakiendelea kunyonga kama kawaida.
Kelele zilipigwa, maandamano yalifanyika, redio zilizungumza na televisheni zilionesha mambo mbalimbali yanayopinga adhabu hiyo, wanaharakati wakisimama kwenye majukwaa na kupigia kelele adhabu hiyo kuwa ‘ifutwe’ lakini bado baadhi ya mataifa yalifumba macho yakaziba masikio na kuendelea kuning’iniza watu mpaka vitanzi vinakwisha. Lakini yapo mataifa kama yetu ya nchi zinazoendelea, yanayojali utu wa mtu, yalisikia vilio, yakasikiliza maoni na kutii sauti ya watu, kwani yaliamini kuwa sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Tanzania ikiwa moja ya nchi zilizoacha kabisa kutekeleza adhabu hiyo labda kama kuna sababu hasa ya kufanya hivyo lakini haikuwahi kutokea kwa kipindi kirefu sana mpaka sasa mwanadada Yaumi anapohukumiwa kwa kosa hilo analodaiwa kutenda, wakiachwa wale wakubwa ambao kila kukicha wanaifilisi nchi kwa kuiba mapesa ambayo yangenunua madawa mahospitalini na kuokoa maisha ya wengi lakini je ni vifo vingapi vinatokea kwa wizi huo? Mahakama haziwaoni, sheria zinapishana nao, amini usiamini, sheria inauzwa na haki inanunuliwa.
Dakika chache baadae katika chumba hicho Yaumi aliingizwa akiwa kafunikwa mfuko mweusi usoni ili asione kile kinachoendelea didi yake. Baada ya itifaki zinazotakiwa kufanyika, alipandishwa juu ya kile kijukwaa na kamba kubwa likatoka kwa juu, lenye kitanzi chenye uchu wa kuibana shingo ya binadamu. Askari magereza mwenye dhamana alimvika kitanzi kile shingoni mwake tayari kwa kazi hiyo. Yaumi aliyefungwa kamba mikono yake kwa nyuma, hakuwa na la kujitetea, alisimama wima akisubiri adhabu hiyo, katika miguu yake tayari alikuwa amelowa kwa hofu na woga wa kifo hicho alichokuwa ama akikisikia au kuona kwenye vitabu, lakini siku hiyo ni yeye aliyetakiwa kuandikwa magazetini na wengine wasome.
Kila mtu alikuwa kimya kabisa katika chumba hicho, ilisikika sauti ya rola tu lililokuwa linaloshusha ile kamba kabla ya kupachikwa shingoni mwa binti huyo mrembo. Gabriel Matinya alikuwa ametulia katika mstari wa mbele, akiangalia kila hatua inayochukuliwa, kwa mara ya kwanza Matinya aliingiwa na huruma kwa Yaumi, alitamani kama angesema wamuache lakini hakuwa na uwezo huo tena. Mnyongaji alikwishweka kila kitu tayari kwa kazi hiyo, akasogea paembeni ili aweze kufyatua tu mtambo wake na Yaumi aning’inie katika kamba hiyo mpaka roho itakapoacha mwili, ni kitufe tu kinachofungua eneo la chini ambalo Yule aliyewekwa kitanzi hukosa pa kukanyaga na kujikuta akining’inia.
Kamanda Amata kutoka pale alipojificha aliweka tayari kiupinde chake kilichobeba kishale chenye makali huku na huku, akiwa kaminya jicho lake akilenga fundo la kamba ile huku akimwangalia Yule mnyongaji, akimsubiri aminye tu kile kitufe na yeye aitume shabaha hiyo. Wakati huo Chiba alishaweka tayari mabomu yake matatu ya machozi, tayari kuvuruga chumba hicho pindi tu Kamanda akifanya yake.
Ilikuwa ni sekunde tu ambayo matukio yote matatu yalifanyika kwa mara moja, kitufe kilipominywa tu, na kufungua na kusababisha pale alipokanyaga Yaumi kufunguka ili aning’inie na kitanzi kimalize kazi yake, ni nukta hiyo hiyo, Kamanda Amata alipofyatua ule upinde wake, kile kimshale kikapita sawia katika fundo la kitanzi lililokuwa nyuma ya shingo ya Yaumi na kukata sehemu ya kamba ambayo mara hiyo ilifunguka yote kwa kuwa haikuwa na nguvu ya kubeba ule uzito. Jopo la mashuhuda lilishuhudia Yaumi akianguka na kutumbukia kwenye kitu kama shimo huku kitanzi kile kikabakia si kitanzi tena. Kabla hawajapata kujua nini kimetukia, kila mtu akiwa katika mshangao uliojalizwa na butwaa, moshi mzito ulikitawala kile chumba na kila mtu alianza kukohoa na kupiga chafya, huku macho yakikosa nuru na kutapatapa kutafuta mlngo wa kutokea. Chiba alitua kwenye sakafgu na kukutana na Yule mnyongaji akiwa kwenye harakati za kuuendea mlango, alimpa pigo moja la judo lilompeleka chini na kumpotezea fahamu, alipogeuka upande ule alikokuwa Yaumi, hakumuona.
Mara moja Yaumi alipodondoka, alikuwa kama aliyepigwa shoti ya umeme, alijua tayari yeye ni marehemu lakini bado alijiona anahisi maumivu ya kudondoka, usoni hakuwa na lile tambara jeusi, kutahamaki akamuona mbele yake mtu kama shetani, aliyevaa dude la kutisha usoni, hakumuona sura ila alimuona akitua sakafuni kando yake, Yule mtu wa kutisha akamfungua kamba ya mikono kwa haraka ya ajabu kisha Yaumi akashuhudia Yule mtu akimpa lile pigo Yule askari. Ilikuwa kama sinema vile, akili ziliporudi kwa Yaumi, alijiinua na kuingia kwenye mlango mmoja aliouona mbele yake uko wazi, huko akakuta ngazi zinazopanda juu ya jengo lile, hakuwa na budi, Yaumi alijua ni mikasa ileile inayomuandama bado inamuandama, akaamu liwalo na liwe, wacha akajiue mwenyewe, alilivuta gauni lake alilokuwa amelivaa, akalipandisha mpaka mabegani na kuacha miguu huru, kisha kwa hatua za haraka akaanza kupanda zile ngazi kuelekea juu. Kamanda Amata, kijana nadhifu, alipoona moshi ule mzito hauna madhara kwake, alilivua lile guo alilolivaa maana lilimnyima wepesi katika utendaji wake, sekunde thelathini zilimtosha, akabaki na suti yake ya kijivu, akajiweka tai yake vizuri na dakika zilizobaki alizitumia kushuka hadi kwenye sakafu ya chini wakati wengine wakihangaika huku na kule kujinusuru na hali hiyo ya ghafla, mlangoni alikumbana na Yaumi, akapitwa palepale, kisha nay eye akageuza na kuanza kupanda ngazi akimkimbiza Yaumi huku akimuamuru kusimama.
ilipoanzia episode 1
1
DAR ES SALAAM
GEREZA LA UKONGA
KELELE za miguu za watu waliokuwa wakikimbizana huku wakipanda ngazi za jengo fulani zilisikika. Alikuwa ni mwanamke mmoja aliyevalia gauni tepe, refu lakini alilishika kwa mikono yake na kuifanya miguu yake kuwa huru, alionekana ni mwanadada aliyepitia kama si JKT basi mgambo maana alipanda ngazi kwa kukimbia huku nyuna yake akifuatiwa na kijana akiyevalia suti nadhifu ya kijivu akiwa na bastola mkononi. Mbio zile ziliendendelea huku yule kijana akisikika akisema
“Binti, simama tafadhali!” lakini yule mwanamke hakusimama aliendelea kupanda ngazi kwa kasi ileile, lakini mbio za sakafuni huishia ukingoni. Ilikuwa ni juu kabisa ya ghorofa ambako mwanamke yule alisimama akijiandaa kujirusha chini.
“Tulia hivyo hivyo tafadhali!” yule kijana alimwambia huku akiwa kamuoneshea bastola , Yule mwanmke alikuwa akitweta kama mbwa aliyekuwa akikimbizwa, aligeuka nyuma yake na kukutana macho na yule kijana.
“Nimechoka, nimechoka kuandamwa nanyi kila wakati, sioni haja ya kuishi, nimehukumiwa kifo lakini mnanitesa tu, bora nijiue mwenyewe” alifoka kwa hasira.
Akiwa bado na bastola yake mkononi, ikiwa imemuelekea Yule mwanamke, Kamanda Amata alishusha pumzi na akatulia, kwa sauti ya upole akamwambia Yule aliyekuwa akimkimbiza.
“Sikia mrembo, hapa upo kwenye mikono salama, sitaki kukudhuru, na kitendo cha kile kitanzi kukatika ni mimi niliyefanya hivyo, nakuhitaji wewe kwa shughuli za kiusalama, hakuna atakayekugusa, naitwa Kamanda Amata kutoka idara ya usalama wa Taifa kitengo kisicho na mipaka” akajitambulisha na kumuonesha kitambulisho ambacho si rahisi kwa mtu wa kawaida kukiona, mwanamke akashusha punzi na kuliachia lile gauni lake limfunike sehemu kubwa ya chini iliyokuwa wazi. Kamanda Amata alirekebisha tai yake na kuirudisha bastola mahala pake ndani ya koti. Akamsogelea yule mwanamke
“Unaitwa nani?” alimwuliza
“Yaumi” yule mwanamke alijibu kwa utulivu sana, hamu yake ya kujiua ilipotea ghafla na hamu ya kutimiza azma yake ilipata matumaini mapya, Kamanda Amata alimshika mkono na kuteremka nae ngazi za upande wa nje baada ya kusikia kuna watu wakipandisha juu kwa mgazi za ndani wakibishana kuwa mwanamke huyo lazima atakuwa juu ya jengo hilo.
ITAENDELEA
Kitanzi cha Mwisho Sehemu ya Nne
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;