Kitisho Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE
Simulizi : Kitisho
Sehemu ya Nne (4)
OFISI ZA USALAMA WA TAIFA- Saa 3:20 asubuhi
KIKAO KIZITO CHA IDARA ya Usalama wa Taifa kilikuwa kikiendelea ndani ya ofisi hizo, kila mtu alipigwa na butwaa kwa taarifa alizokuwa akizipata kutoka kwa Hosea. Ilikuwa ni asubuhi na mapema tu walipoitwa kutoka kwenye kona zao tofauti za kazi zao na kukutana hapo. Mara hii Scoba aliungana nao katika kikao hicho.
“Mpaka sasa ni huyu ambaye anaweza kutujuza juu ya watu hao! Kamanda Amata alikuwa hapa lakini na yeye haelewi watu hawa ni akina nani, anajaribu kupambana kiume kutegua kitendawili hiki, labda Scoba mwenyewe atueleze kilichompata kwa kifupi, kisha tuchukue hatua ya haraka,” Hosea akalieleza jopo.
Scoba akajikohoza kusafisha koo kisha akafungua kinywa kueleza mkasa uliomkuta.
SAA 16 ZILIZOPITA – Mtaa wa SHABAN ROBERT
Scoba aliegesha gari yake kandokando ya barabara hiyo mahala ambapo Tax nyingi huegeshwa, akateremka na kuliendea benchi ambalo madereva wa kijiwe hicho hukaa kusubiria wateja huku wakinywa kahawa na kupiga soga kama kawaida yao.
Akiwa ametingwa na mchezo wa draft aliyokuwa akiucheza na mwenzake huku wengine wakishangilia. Mara karibu kabisa ya mguu wake aliona mguu mwingine uliovikwa kiatu cha kike ukisimama na kumkanyaga kidogo, linguine lililomshtua ni ukimya uliofika ghafla.
“Aaa mrembo huyo! Karibu bibie,” sauti ya mmoja wa madereva ilisikika. Scoba akainua uso wake na kukutana na uso wa mwanadada, uso laini husio na chunusi, akashusha jicho mpaka kifuani, lo; kifua kilijaa sawia, matiti madogo yaliyobanwa na sidiria ya kisasa yaliongeza utamu na kusisimua mwanaume yeyote rijali.
“Twende!” Yule mrembo akamwambia Scoba.
“Na mimi?” Scoba akauliza.
“Ndiyo na wewe, nataka gari yako mie, maana we wajua kuendesha vile nitakavyo,” Yule mrembo akamwambia.
Scuba akanyanyuka na kujipukuta vumbi katika makalio yake,
“Haya mama twende kama wanitaka mimi,” wakaondoka na kuingia kwenye gari.
“Waitwa nani mrembo?” Scoba akaanza uchokozi.
“Naima,”
“Waoh, una jina zuri sana,”
“Kwa nini?” Naima akauliza.
“We huoni? Hata maana yake tu, mtu mwenye nguvu na uwezo mkubwa wa fikra ndiyo maana ya jina Naima, so sweet!” Scoba aliendelea kuonge huku akiingiza gari barabarani.
“Asante; twende Magomeni kuna watu wangu pale kisha utupeleke Kijiwe Samli tuna shughuli kule, leo nitakukodi siku nzima, shing’ ngapi?” Naima akauliza huku akiuvuta mkoba wake na kufungua zipu, maburungutu ya noti yalikuwa yamelala kimya.
“Kwa wewe mrembo sikuumizi, nipe Laki moja tu,” akamwambia.
“Haina tabu, nitakuongezea na hamsini,”
Wakakamata barabara ya Samora mpaka kwenye mzunguko wa Picha ya Askari, moja kwa moja wakapita Maktaba na kuikamata ile ya Morogoro mpaka Magomeni.
“Ingia Mapipa, mtaa wa tatu!” Naima akamwelekeza, Scoba akafanya hivyo, mbele ya nyumba moja iliyokwisha kwisha hivi akaegesha gari, Naima akateremka na kumwacha Scoba, akaingia kwenye ile nyumba. Baada ya dakika kama tano hivi akatoka yeye na vijana watatu, wakaingia garini, wale vijana wakaketi nyuma na Naima akaketi mbele.
“Kijiwe Samli,” akamwambia Scoba. Scoba aliwatazama kwenye kioo cha ndani wale vijana ambao hata kusalimia hawakusalimia, nywele zikamsisimka, akaihisi hatari mbele yake, akawasha gari na kuondoka zake. Wakiwa barabara ya Nyerere kuelekea maeneo ya Vingunguti mmoja wa wale vijana akawaambia wenzake kuwa kabla ya kwenda kwenye shughuli yao basi wapiti japo wapate mbili mbili, wakafanya hivyo, wakakunja kulia na kuchukua barabara ya Kiembe Mbuzi.
Kizota Pub.
“Egesha gari hapo,” mmoja wao akaamuru na Scoba akafanya hivyo. wakateremka na kuingia kwenye Pub hiyo, wakachagua viti na kuketi.
“Mwambie Angel kama kawaida,” kijana mwingine akamwagiza Mhudumu wa Bar na baada ya hapo vinywaji vikaletwa wakaanza kuburudika.
Iiwachukua dakika kama kumi natano hivi na kilamtu alikuwa kapata mbili, wakanyanyuka kuondoka.
Scuba alipokuwa katika usukani aliana kuahisi macho mazito, alijaribu kuyafungua lakini yalimuwia mazito, akaanza kupoteza umakini barabarani, aliendelea kupambana na hali ile lakini ikawa ngumu, akaegesha gari pembeni.
“Vipi?” Naima akamwuliza.
“Mmenipa nini nyie? Nyie majambazi ee?” akaongea kwa shida sana kwani kinywa chote kilimuwia kizito. Mlango wa nyuma ukafunguliwa, kijana mmoja akashuka na kumtoa Scoba kwenye usukani akaketi yeye, Scoba akawekwa nyuma mtu kati.
“Tueleze Madam S anaishi wapi?” swali hilo lilimrudishia akili Scoba ghafla, akawatazama wale vijana huyu kisha Yule.
“Ninyi mnamjua Madam S?” akawauliza.
“Hatuna muda wa kujibu swali lako, jibu swali letu,” Sauti ya mwingine ikasisitiza.
“Siwezi kuwajibu swali lenu,” Scoba alijibu kwa dharau.
“Unajifanya nunda siyo, kumbuka tuko wane hapa, tutakumaliza,”
“Hata mkiwa kumi au ishirini, siwezi kuwaambia,” akaendelea kuwadindia zaidi. Tayari ile gari ilikuwa ikiuwacha mji na kuelekea Gongo la Mboto. Domo la bastola likatua kwenye ubavu wa Scoba.
“Tulia, ukileta ujeuri wako tu nakumaliza,” akaambiwa. Scoba hakusubiri, alimshindilia kichwa Yule mwenye bastola, akamtindika ngumi huyu wa pili, vurugu ikaamka kwenye gari. Yule jamaa aliinua bastola lakini kabla hajafanya lolote mkono wake ukadakwa na bastola ilipofyatuka ikapita sentimeta chache kutoka kwa Naima ambaye ilibidi alalie upande wa dirisha, na ile risasi ikapasua kioo cha mbele. Dereva akayumba barabarani na kuitoa gari nje akasimama.
Naima aliachia pigo moja kali la ‘pigo la kifo’ lililotua sawia katika uso wa Scoba, akageuka huku akipiga yowe la uchungu, pigo la pili likatua shingoni na kumfanya Scoba kutepeta. Yule mwenye bastola alamshindilia pigo la kisogoni kwa bastola yake Scoba akazimika.
Kila mmoja alikuwa anathema kwa shughuli hiyo ya sekunde chache.
“Amekufa?” mmoja aliuliza.
“Akaongee na babu zake, mtupeni vichakani huko,” Naima akaamuru na Scoba akashushwa na kutupwa katika chaka.
§§§§§
SCOBA alimaliza kusimulia mkasa uliyompata, kila mmoja alisikitika sana na hali hiyo, minong’ono ikachukua nafasi kati yao.
Hosea akajikohoza na kurudisha ukimya kwa namna hiyo, “Ok, sasa nataka tuingie kazini ili kuwapata hao watu laeo kabla jua halijazama,” akatoa amri. Wakiwa bado katika kikao icho mara simu ya mezani katika chumba cha mikutano ikachukua uhai. Hosea akaipokea na kuiweka sikioni.
“Mkuu, katika barabara ya Ocean kuelekea Ikulu – Magogoni kuna gari zinafanya fujo,” ilikuwa sauti ya Avanti aliyekuwa katika chumba cha mawasiliano cha Teknohama. Baada tu ya taarifa hiyo jopo zaima likanyanyuka likimfuata Bwana Hosea na kuelekea kwenye chumba hicho kutazma hicho walichoambiwa.
Katika luninga kubwa kulikuwa kukionesha ramani ya jiji la Dar es salaam na kuonesha maeneo yote muhimu kwa ajili ya usalama wa Taifa. Zilionekana gari mbili zikielekea Upande wa Ikulu kutokea Hospitali ya Ocean Road.
“Zuia haraka, point namba mbili ifanye kazi tafadhali!” Hosea aling’aka na muda huo huo Avant aliinua kitu kama simu na kukiweka sikioni kisha akaboinyeza tufe Fulani na kuongea maneno machache, akatulia.
Bado macho hayo yote yalikodoa bila kufumba yakiangalia tukio hilo, hakuna aliyejua ni nini kinaendelea. Scoba alitulia akitazama kwa makini, akapenya katikati ya watu na kusogea karibu na Avant.
“Naomba nione picha inayowezekana tafadhari,” akamwambia Avant, naye akafanya manuva Fulani kwenye mashine yake wakaweza kuona vipande vya picha za magari hayo, Scoba alitazama kwa makini.
“Unaitambua hiyo gari?” Hosea akamwuliza.
“Yeah, kama sikosei hii Toyota Duet ni ya dada mmoja hivi ana uhusiano na Kamanda Amata, huyu dada ni daktari pale Agha Khan na huwa wakati mwingine tunamtumia kwa hili na lile, anaishi Upanga Sea View,” Scoba alieleza.
“Kamanda Amata,” Hosea akanong’ona, kisha akawaangalia watu wake, “Namtaka huyo anayefukuzana na Amata sasa hivi!!” akatoa amri na kuondoka mle ndani huku akiweka sawa miwani yake. Maafisa wale wakatazamana kisha mmoja akawapa ishara ya kutoka katika chumba kile.
“Ili tufike haraka eneo lile kwa foleni za Dar lazima tutumie njia ya anga, Chopa tafadhali, Scoba twende zetu,” afisa mmoja aliyeonekana kuwa na cheo cha juu kati yao alitoa amri hiyo, Scoba akakabidhiwa nafasi ya kuliongoza dude hilo, pamoja naye watu wengine wawili walikwea ndani yake wakiwa wamekamilika, bunduki ndogo na kubwa zilihusika, mashine ikanyanyuka.
§§§§§
Barabara ya Ocean ilikuwa imekumbwa na taharuki, Kamanda Amata, mwili wake ukiwa unavuja damu hapa na pale alikuwa akiendesha Toyota Duet kwa mwendo wa hatari akiifukuza gari ya mbele yake ambayo ilionekana wazi kuendeshwa na mtu anayeijua kazi yake. Ovateki zilizokuwa zikifanywa na huyo jamaa ni za hatari mpaka kila mtu alikuwa akishika kichwa kuhofia maisha ya hao walio ndani ya vyombo hivyo.
Walipokaribia njia panda ya Gymkhana na Ocean Road; Kamanda Amata akazipita gari mbili na kuingia upande wa kulia, baada ya kuisoma akili ya adui yake kuwa atapinda upande huo, hakuwa mbali na mawazo ya mtu huyo, gari zile zikakutana katikati ya njia panda na kusababisha ajali mbaya iliyohusisha gari kama nne hivi. Gari ya Kamanda Amata kutokana na udogo wake ilijifinya chini ya Land Cruiser Hard Top.
Gari aliyokuwa akiitumia Yule jamaa baada ya kukutana na ile ya Amata, alijaribu kuikwepa akajikuta akiingia katika ukuta wa Hospitali na ukuta ule kuvunjika vibaya. Mguu wake ulikuwa umenasa chini kwenye pedo, alijitahidi kuutoa na kufanikiwa. Akajivuta na kutoka nje kwa kupitia dirishani.
Kamanda Amata naye akajitoa taratibu huku mwili wake ukivuja damu. Kama kawaida ya Watanzania kama kawaida yao wakaanza kujazana, vibaka nao wakitafuta bahati yao, Kamanda Amata alijitupa nje na kudondokea barabarani.
Yule bwana alitazama huku na kule na kuona kundi la watu likija kwenye eneo la tukio, sura yote ilijaa damu, nguo alizovaa hazikutamanika. Mngurumo wa helkopta ndiyo uliomfanya aamue aliloamua, alitazama juu na kuona helkopta hiyo ikisogea eneo hilo, katika mlango wake mtu mmoja aliyevalia suti nyeusi akiwa kakamata bunduki yenye nguvu,
“Nimekwisha!” akajiwazia. Kitendo bila kuchelewa alichomoa bastola yake na kupiga tanko ya mafuta ile gari yake.
Mlipuko mkubwa ukatokea na gari kadhaa zilizokuwa eneo hilo zilishika moto, moshi ulitanda eneo lote, kelele za watu zikasikika huku na kule. Kamanda Amata akaenda pembeni kabisa na kuanza kutazama wapi adui yake alipo. Haikumchukua muda kumwona mtu huyo akiwa anatoroka kwa kujichanganya na watu.
“Shabash! Huwezi kunitoroka,” akasema kwa sauti ndogo, akavuta hatua na kuyapita magari matatu yaliyokuwa yamejibana hapo, akatokea upande wa pili na kumwona adui yake akipotelea katika kundi la watu. Kutokana na wingi wa watu ilikuwa ngumu kupenya eneo lile, akafikiri kwa haraka kuwa hapo ni kutumia plan B ili kumpata, lakini kabla hajatekeleza hilo. Gari ya polisi ilifika eneo hilo kwa mbwembwe na walipofika tu waliteremka haraka wakiwa na bunduki zao mikononi, mara moja walimwona Yule mtu aliyekuwa akijichanganya na watu.
Inspekta Simbeye akiwa na bastola yake mkononi, akatoa amri mtu huyo akamatwe mara moja, lakini mtu Yule naye hakuwa tayari kukamatwa namna hiyo, alichomoa bastola yake na kupiga risasi mbili hewani na kufanya hali ya taharuki mahala pale, baada ya kupiga hewani ile risasi, akashusha mkono na kufyatua tena, risasi ile ilimkosa mlengwa ikampata mmoja wa raia aliyekuwa eneo lile na kumjeruhi, hapo ndipo hasira za wananchi zilipopanda, walimvamia Yule bwana bila hata kujali polisi waliopo, walipiga na kupiga mpaka mtu Yule akapoteza uhai.
Ile Chopa ikateremka taratibu na kujiegesha pembezoni mwa ufukwe wa bahari, vijana watatu Smart Guys wakateremka na kuifikia ile maiti iliyopigwa vibaya na wananchi, Scoba aliteremka pia huku akiacha dude lile likiunguruma kwa hasira, Inspekta Simbeye na vijana wake wakawasili.
“Shiit!” akafoka Simbeye, “Siyo Mtanzania huyu!” akamalizia.
Akainua uso na kuangaza huku na kule wakatia huo tayari utepe wa polisi ulikuwa umezunguka eneo hilo na kuzuia Wananchi kufika hapo. Gari za zima moto tayari zilikuwa zikizima moto uliounguza gari takribani tano eneo hilo.
Kamanda Amata akatazama hali iliyokuwa hapo, akafikiria kama ajitokeze au la, lakini hiyo huwa si kawaida yake, alipigwa na bumbuwazi alipomuona Scoba, “Ni yeye au nimechanganyikiwa?” akajiuliza, kisha taratibu akaondoka eneo hilo huku akijiweka sawa uso wake. Akapotea eneo hilo.
6
CHIBA alimtambua mara moja Yule mtu pale mbele, ni mtu a;iyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu, kutoweka kwake kulisababisha maandamano makubwa ya waandishi wa habari, alikuwa mwandishi nguli wa habari nchini. Wananchi waliongea, katuni zikachorwa ikasemekana watu wa Usalama wa Taifa wamemteka na siku yoyote angeonekana akiwa hana macho, au meno. Au kucha.
“Kwa nini? Kwa nini walimteka na kumleta huku?” akajiuliza bila majibu.
“Unamjua huyu?” JoKi akamuuliza.
“Ndiyo namjua, na kwa nini mmemfanya hivi?” akamuuliza.
“Aaaaa ha ha ha ha, hii ni serikali kaka, ina Rais, Mawaziri, Wabunge, Wanausalam kama sisi na kadhalika, na ina maadui kama wewe. Nusu saa ijayo nawe nitakufanya hivi,” alipomaliza kusema hayo, risasi moja ilikipasua kichwa cha Yule mwandishi na kutawanya damu iliyonganyika na ubongo. Chiba alitetemeka kwa hasira.
“Jiandae, nitawapanga wote hapa na kuwa fumua mmoja mmoja huku nikitengeneza filamu ya kumbukumbu kama za wadi ya kusherehekea miaka mingapi sijui ya uhuru wa nchi yako,” akaongea kwa kebehi.
“Hicho ni kitisho!” Chiba akaunguruma kwa hasira.
“Kitisho! Kitisho ee,” JoKi alipomaliza hiyo sentensi, aliinua mkono kwa minajiri ya kumchapa kofi Chiba. Chiba aliigundua hiyo dhamira yake akasubiri kitendo hicho, kiganja cha mkono wa JoKi kilipolifikia shavu Chiba aligeuka ghafla na kukidaka kidole kimoja kwa kinywa chake, akakibana barabara kwa meno yake imara.
“Aaaaaaiiiigggghhh!” JoKi alipiga kelele za maumivu, alijitahidi kuuchomoa mkono wake kinywani mwa Chiba lakini ilikuwa kazi bure, alitumia mkono mwingine kumpiga ngumi za tumboni na kwingine lakini Chiba hakukiacha. Wenzake walijaribu kumnasua lakini wapi.
“Mwache au la nakupiga risasi,” mmoja wao alimwambia Chiba. Lakini Chiba hakujali alizidi kung’ata na kung’ata, mishipa ya hasira ikiwa imedinda usoni na shingoni. Yule mlinzi alitumia kitako cha bunduki kumpiga Chiba mbavuni lakini Chiba hakuachia. Wakati JoKi akijitutumua kujinasua alimpiga kichwa kizito Chiba, Chiba akayumba na kuanguka chini kama mzigo kutokana na kamba alizofungwa.
JoKi akamtazama Chiba kinywani akona damu zikitiririka, mara chiba akatema kidole kutoka kinywani mwake, JoKi akajitazama mkono wake, hakuna kidole kimoja, hasira ikawaka huku akipiga kelele kama mtoto.
“Na bado ukiniua mimi wapo watakaokata miguu yako kwa meno!” Chiba akazungumza kwa gadhabu.
“Jeuri sana wewe, si ndiyo?” mlinzi mwingine akauliza huku akimpa bunduki mwenzake ili amwadhibu.
“Mtieni adabu Mwanaharamu huyo nakuja sasa hivi,” JoKi aliagiza kisha yeye akatoka huku damu zikimmwagika. Yule mlinzi alivuta teke kali kumpiga Chiba pale chini, Chiba akajizungusha na kumchota ngwala ya maana, Yule mlinzi alipiga mweleka na kudondoka chini akitanguliza kisogo, akatoa yowe la uchungu, Chiba akainua miguu yake iliyofungwa na kuitua kwa nguvu katika koromeo la mtu huyo.
“We mwache mwenzio! Mi nakuua!” mlinzi wa pili alimpiga Chiba kwa kitako cha bunduki aina ya Rifle na Chiba akatulia kimya, huku akimwacha Yule mlinzi akiwa hana uhai.
§§§§§§
Hali ya Gina ilibadilika baada ya jeraha lake kumwaga damu nyingi, Dkt. Khadrai alijitahidi kuona namna ya kumsaidia, hakuna na damu ya akiba nyumbani kwake kwani ni ni kinyume cha sheria. Akiwa bado hajui la kufanya, mlango ukafunguliwa, Kamanda Amata akaingia ndani, moja kwa moja akafikia katika chumba hicho cha matibabu na kumkuta Gina akiwa tena kitandani.
“Vipi dokta?” akauliza.
“Hali imebadilika, damu nyingi imetoka katika jeraha lake,” akajibu.
“Oh Come on Gina. Sasa tunafanyaje?”
“Hapa nikupata damu nyingine kumwongezea, haraka,” Khadrai akajibu huku bado akiwa hai hai kumsaidia Gina.
“Ita gari yenu ya wagonjwa!”
“Oh, nilisahau kabisa, asant kunikumbusha,” akachukua simu yake ya upepo ambayo madaktari wote wanazo kwa ajaili ya mawasiliano ya karibu kama inahitajika. Akaita gari na na kuagiza ije na damu kabisa.
Dakika kumi hazikupita gari ya wagonjwa ilifika eneo hilo, Gina na Dr. Khadrai waliingia na safari ya kuelekea Agha Khan ilianza kwa mbwembwe kama kawaida ya madereva wa gari hizo.
Gina alilazwa katika hospitali hiyo chumba maalum ambacho hakuruhusiwa mtu yeyote kuingia zaidi ya Dr. Khadrai tu na baadae alimjuza Amata kuwa Gina yuko mahala hapo.
§§§§§§
Kamanda Amata aliiacha hospitali ya Agha Khan na kuingia mtaani, akatembea mpaka barabara ya Ally Hassan Mwinyi, alipoona hali ya hewa ni ya utulivu, akachukua simu yake na kupiga namba ya Mkuu wa Usalama wa Taifa, Bwana Hosea na kumwuliza juu ya Scoba, akajibiwa kuwa Scoba yupo salama na anaendelea vyema.
“Ok, ninamwitaji sasa tuingie kazini kwa nguvu zote,” akamwambia Hosea.
“Haina tabu kwani huyu ni wa kwenu, mkutano wapi?” Hosea akauliza.
“Kanisa kuu la Mtakatifu Joseph dakika kumi baadae,” kisha simu ikakatika. Amata aliingia kwenye tax iliyoegeshwa jirani kabisa, na kuitaka impeleke mpaka JM Mall ilipo ofisi yake ya siri au tuiite ofisi binafsi.
Aliwasili katika jengo hilo mida ya kama saa sita hivi, moja kwa moja akaiendea mbao ya magazeti na kutazama nini kilichoandikwa. Habari zilikuwa zile zile za jana yake ila zilikolezwa wino tu. Akapita taratibu na kuuendea mlango mkubwa wa jengo hilo. Akasimama kidogo karibu na mashine za kutolea pesa, akatzama huku na kule, kila mtu alikuwa akiendelea na hamsini zake, akasogea pembeni na kubonya kidubwasha cha lifti, ilipofika akaingia na kuiamuru imfikishe ghorofa ya nne.
Alipofika ghorofa ya nne aliteremka na kwa kutumia ngazi alipanda kwenda ghorofa ya sita ambako ofisi yake ndipo ilipo. Akaufikia mlango na kusita kidogo, jicho lake likatua chini ya mlango, kulikuwa na ncha ya bahasha ikichungulia nje, akaivuta kwa vidole vyake na kuitazama. Ilikuwa bahasha nyeupe, ndani ilikuwa na kitu kama kadi ya kibiashara, akaitazama kwa makini sana, akataka kuichana, akasita, akafungua mlango wake na kuucha wazi, akatulia kidogo, kisha akaingia ndani na kutembea taratibu. Kila kitu kilikuwa kama alivyokiacha mara ya mwisho, hakuna kilichoguswa wala kusogezwa. Moja kwa moja akaiendea jokofu ndogo iliyokuwa hapo akafungua, akatazama chupa zake za kinywaji, akacheka kidogo kisha akafunga, ijapokuwa alikuwa na kiu lakini hakuchukua chochote baada ya kuona mpangilio wa zile chupa umegeuzwa kwani yeye na Gina walikuwa na mpangilio wao maalum.
“Kama mmeweka sumu mtakunywa wenyewe,” akawaza kisha akavuta droo yake na kupekua hapa na pale, akachukua saa yake ya mkononi na kuivaa, akachukua miwani yake yenye uwezo wa kurekodi picha mjongeo, kuona nyuma bila kugeuka, bastola yake ndogo kuliko zote inayotosha kwenye kiganja cha mkono akaipachika mahala pake.
Akalivua koti lake na kulitupia huko, akavua shati na kuvaa fulana nyeupe inayobana mwili kisha akarudishia kila kinachohitajika, akafungua kijikabati kidogo na kutoa kikoti cha Kodroy akakivaa juu yake, pesa kama shilingi za Kitanzania laki tano akazitia kibindoni. Akaiinua bastola yake na kuisukuma slide mbele nyuma, “Iko fiti,” akawaza na kuikubali, kisha akafyatua magazine na kuiweka mezani, akapanga risasi zake nane na kuirudishia mahala pake, akaislide tena na risasi moja ikatumbukia chemba, akailoki na kuitia mkandani.
Akatulia kwa sekunde kadhaa kisha akaamua kutoka kwa nguvu zote kwenda kumsaka mbaya wake ambaye mpaka nukta hiyo hakujua yuko wapi. Alitoka na kuufunga mlango nyuma yake, akaingia kwenye lifti kwa minajiri ya kuteremka chini, kabla mlango haujajifunga, kijana mwingine akawahi kuingia na kusimama jirani na Amata lakini kwa nyuma. Kamanda Amata aliichomo miwani yake na kuivaa kisha kumtasama kupita vioo vidogo vilivyo kwenye miimo ya miwani hiyo.
Yule kijana alikuwa ametulia tuli hasemi lolote lakini kwa jinsi macho yake yalivyokuwa yakipepesa, Amata akajua kuwa huyo si mtu mwema, akajiweka tayari kwa lolote kwani mwili wake kw muda huo ulikuwa ukichemka damu ukizingatia bado ndugu zake hakujua wako wapi, kitendawili.
Aiendelea kumtizama huku akiangalia tarakimu zinazobadilika kutoka kumi na tano na kuteremka chini kwenda G, akamwona mtu huyo akiingiza mikono ndani ya kijaketi chake, akajua nini kinataka kutokea, akajiweka sawa.
Lakini alikuwa anatamani kucheka kila akimtazama kijana huyo aliyeonekana kujawa na wasiwasi. Ilionekana katika kazi hizo huyu atakuwa ni mwanafunzi tu kwa jinsi asivyojiamini, Amata akanyoosha mkono na kubofya tarakimu zile kwa kuingiza namba kama sita hivi na lifti ikasimama ghafla. Yule kijana alitoa waya kwenye koti lake na kutaka kumkaba Amata.
Kamanda Amata hakupoteza muda, alimjifanya anaudaka ule waya kumbe ilikuwa ni danganya toto, alipiga kiwiko cha mbavu dogo akalegea, alimnyanyua kwa kumshika mikono yake na kupigiza upande wa pili, akambwaga chini hoi. Kisha akapiga goti moja na kuondo amiwani yake usoni.
“We ni nani?” akamuuliza.
“Mi-mi-mi ni-metu-mwa,” akajibu huku akijikinga mikono yake usoni.
“Najua umetumwa, wewe ni nani?”
“Jose,” akajibu.
“Nani aliyekutuma?” akamchapa swali linguine.
“Mdada mmoja, yuko hapo nje,”
“Kavaaje na anaitwa nani?” Yule kijana hakujibu hilo swali, akabaki akimwemwesa mwemwesa midomo, Amata akamwinua kichwa na kumpigiza chini kwa nguvu.
“Nasemaaaa!” akalia kwa uchungu.
“Haya sema!” akamlazimisha kusema, mara hii bastola ikiwa mkononi.
“Simjui jina, alinipa hiki, akaniahidi pesa,” akatoa kadi ya kibiashara na kumpatia.
Kamanda Amata akaitazama na kusoma jina na namba za simu zilizopo, lakini alishangaa kuona jina la mwenye kadi ni la kiume. “Haijalishi, ndiyo njia zao hizi,” akawaza, akamtazama Yule kijana, yuko hoi pale chini, akamwacha na kufyatua zile namba kisha akaiamuru ile lifti iende juu kabisa. Huko akatoka na kuiacha akatumia ngazi kuteremka mpaka ghorofa ya sita ilipo ofisi yake, akaichukua ile kadi, na kuandika zile tarakimu katika mashine maalumu ambayo ina uwezo wa kukupigia simu ukajua unaongea na binadamu kumbe kompyuta, unachokifanya ni kulisha maneno kisha kuyaoanisha na yale ya upande wa pili, kwamba huyu akisema hivi yenyewe iseme vile, kisha akaunganisha ile mashine na simu yake ndogo aliyoipachika kwa mkono huku kisikilizio chake kikiwa masikioni, akatoka na kuondoka zake.
§§§§§
NAIMA akiwa ndani ya gari yake pamoja na wenzake wawili, aliipachika darubini yake machoni na kutazama kwa makini kwenye lango kuu la JM Mall, alichokiona sicho alichokitegemea, alimwona Kamanda Amata akitokea pale mlangoni na kuivaa miwani yake, kisha akatembea kuielekea gari moja aina ya Toyota Carina Ti, Kafungua buti na kujifanya anatazama vitu Fulani Fulani.
Naima na kijana wake mmoja wakatoka na kuwahi pale kwenye ile gari, Yule jamaa akamwona bado Amata ameinama akifanya shughuli zake kwenye ile gari iliyokuwa katika maegesho pweke upande wa pili wa lile jingo.
Kamanda Amata akahisi tayari kuna hatari, akatazama kwenye kioo chake cha siri kwenye ile miwani na kuona watu wawili wakimsogelea kwa mwendo wa Mamba awindapo, akataka kufanya makeke lakini akilini akawaza kutumia Art of War, jifanye mnyonge unapokuwa una nguvu, akaendele na shughuli yake.
“Usilete makeke yako ya kitoto, bunduko mbili zenye nguvu ziko nyuma yako na nkyingine kubwa ipo ghorofa ya pili, tulia hivyohivyo,” sauti ya Naima ikaunguruma.
Kamanda Amata alishalitegemea hilo na alijua kuwa ahadi yake na Scoba ilikuwa imetimia kwani wanapoahidiana kukutana Kanisa kuu la St Joseph, basi ujue hapo JM Mall ndiyo Kanisa Kuu.
“Simama!” akamwamuru.
Kamanda akafanya hivyo, kisha lile jitu la miraba minne likaja na kumpekuwa likachukua bastola tu bila kuona silaha nyingine zilizotapakaa mwilini mwa Amata. Naima akiwa mkononi na Shot Gun akamwongoza Kamanda Amata ndani ya gari hiyohiyo, Yule jitu akaketi kwenye usukani, Amata akawekwa nyuma huku Naima akiwa kampachika domo la Shot Gun katika ubavu wake.
Kamanda Amata alipotoka pale nyuma ya gari aliacha buti bila kufunga ila alilipachika kwa namna anayoijua yeye. Scoba alikuwa akiona mambo yote hayo, alipoingia tu garini na kuiwasha, alinyata taratibu na kufungua buti kisha akaingia ndani yake na kujiweka humo, akarudisha lile funiko na kuliegesha kwa namna ya ajabu, ile gari ikaondoshwa mahala pale na kuelekea kusikojulikana.
§§§§§
Simu ya kukamatwa kwa Kamanda Amata ilipokelewa kwa furaha sana na JoKi, naye muda huo huo akaingia katika chumba cha mawasiliano na Boss wake asiyeonekana sura na kumpa habari hiyo njema.
Pancho Panchilio alitamani aruke angani lakini hakuweza, aliinua simu yakena kuwapa ujumbe huo wenzi wake na kuwa wakutane huko kwenye kasri lao ili wamalize kazi waliyoidhamiria.
Ilimchukua dakika kadhaa tu Pancho Panchilio kuingia katika kasri lake huko Kerege kwa njia ya siri ambayo ni yeye tu aiyekuwa akiijua na kuitumia, na kila Mjumbe wake naye alikuwa na njia tofauti ya kuingilia, wao walikutana tu ndani ya jengo hilo.
Haikupita muda Mjumbe mmoja mmoja aliingia katika kasri hilo na kukutana kwenye chumba chao ambacho kwacho siku zote hufanyia mazungumzo na mipango yao.
7
ZANZIBAR
NURU MUSABAHA alitulia tuli kwenye kochi kubwa huku jicho lake likiwa kwenye luninga kupata habari mbalimbali kutoka Bara, mara kwa mara moyo wake ulikuwa ukilipuka na kujawa hofu lakini baadae alitulia tena, hata aliposikia unyayo wa paka yeye alihisi kama sijui kitu gani, alijua kila kinachoendelea huko Bara na kusudi kitekelezeke, alitakiwa kutoroka namna hiyo na kusubiri hali itulie na mumewe Mahmoud Zebaki awe na matumaini ya kurudi uraiani.
Asubuhi hiyo majira kama ya saa nne hivi, kila alipojaribu kuwasiliana na Ravi, simu hakupatikana, nah ii ndiyo ilimfanya achanganyikiwe zaidi, “Kwa nini hapatikani?” alijiuliza pa si na majibu. Kabla ya kuja Zanzibar alimshauri Ravi waondoke pamoja baada ya kuusuka mpango huo na mtu wasiyemjua, lakini Ravi yeye alikataa katakata kuondoka, akiamini kuwa maadam watu hao watakamatwa kwa siri yeye watamjuaje ilhali ni raia wa kawaida tu.
Alikuwa akisoma gazeti juu ya habari ya marehemu Mbunge lakini alihisi haelewi akalitupa huko, akazima TV na kujinyanyua kitini akasimama wima. Akavuta hatua fupi kukielekea chumba cha kulala lakini akiwa humo bado akili yake haikumkaa sawa, akaamua kubadilisha nguo alizokuwa amevaa, akavalia suruali ya jeans nyeusi, fulana moja yenye picha ya Madonna na kubebwa na neno Holyday , akajiangalia kwenye kioo na kujiona yuko fiti ukizingatia na shepu aliyonayo ya mchanganyiko wa Kimanyema na Kipemba basi utamu mtupu.
Alipojiweka vizuri akachukua pesa kidogo na kujaza mfukoni,
“Nikalale hotelini,” akawaza kisha akavuta juba lake na kujifunika mwilini akaacha macho tu kisha akanyanyua kijimkoba chake na kuanza safari ya kuondoka eneo hilo.
Alipoukaribia mlango tu, akasikia hodi ikibishwa, akasita kuuendea mlango, “Nani atanifuata huku?” akajipa moyo na kuuendea mlango, akaufungua.
“Karibu sana, nikusaidie nini?” Nuru akamwuliza huyo aliyegonga mlango.
§§§§§
Alikuwa kijana mtanashati, aliyeva suti yake nyeusi, miwani nyeusi akitazamana na Nuru pale mlangoni, Yule kijana alimwangalia Nuru chini mpaka juu na kulistaajabu umbo la mwanamke huyo, “Tangu lini Mpemba akawa na shepu ya maana kama hii?” akajiuliza.
“Mimi ni polisi Detective,” akajitambulisha na kumwonesha kitambulisho.
“Kwa hiyo mi nifanyeje, nikupandishe cheo au?” Nuru akauliza kijeuri lakini moyoni mwake alikuwa hoi, alihisi kijimkojo kwa mbali lakini akajikaza kikike.
“Hii ni barua ya wito wa kufika kituo cha polisi cha kati mara moja,” Yule kijana akamweleza. Nuru akaisoma pasi na kuishika kwai hakutakiwa kufanya hivyo. macho yake yakaonekana wazi kuwa na machozi.
“Nimefanya nini mimi mpaka michukue?” kauliza.
“Swali gumu mama, mi natekeleza wajibu, ukifika kituoni ndipo watakueleza yote,” akajibu Yule kijana.
“Ok, ngoja nijiandae,” Nuru akaomba.
“Hapana, hivyo hvyo ulivyo, mbona utarudi sasa hivi tu!” Yule kijana akamwambia na mara hiyo akaja mwenzake mwanamke WP aliyevaa kiraia na kumchukua Nuru mpaka kwenye gari. Safari ikaanza mpaka kituoni. Alipofika pale danadana ilikuwa ile.
“Na sisi pia tumepewa oda hiyo kutoka juu, hivyo madai yako yote utapewa majibu kutoka Dar es salaam,” akajibiwa hivyo na mkuu wa kituo.
Nuru aliishiwa nguvu, mapigo ya moyo yakashuka, akawa wa kupepewa tu, wakamvua viatu, wakamlegeza mkanda, wakambeba kwenye gari ya polisi mpaka hospitali ya Mnazi Mmoja.
Nuru alijua linalomkabiri, akashindwa kuvumilia.
§§§§§
Baada ya kujiganga na kupata unafuu wa maumivu alisonya huku akijiangalia kidole chake na kushikwa na hasira kali juu ya Chiba, “Atanikoma huyu mshenzi!” aliongea mwenyewe: Akainuka na kwenda huko kunakoitwa kuzimu alipofika katika chumba kile, alishamgaa kukuta mwili wa mlinzi umelala bila uhai, alipopepesa macho pembeni hakuona mtu mwingine.
“Shiit!” akang’aka kwa hasira na kuugeuza ule mwili, “Shetani huyu, kamuuaje huyu jamaa ilhali alikuwa na silaha mkononi?” akajiuliza kisha akaondoka kuelekea chumba kile alichomfungia kwanza. Akiwa njiani akakutana na Yule mlinzi wa pili.
“JoKi, huyu mateka ni hatari, kamuua Ngwabi kwa miguu yake,” Yule mlinzi akaeleza.
“Sasa yuko wapi?” JoKi akauliza.
“Nimemtupa huko kwenye chumba, sijui kafa au mzima maana nimempa kipigo cha maana,” akaendelea kueleza. Kisha wote wawili wakafuatana kwenda kumwangalia Chiba. Kweli hali yake ilikuwa mbaya, alilala mithili ya mfu, damu zikimvuja kichwani baada ya kupigwa sana kwa kitako cha bunduki.
“Safi sana! Sasa njoo nikupe maagizo mengine,” wakafuatana mpaka chumba walichomwacha Madam S.
“Unamwona huyu Kibibi, huyu atauawa kwa kukatwa na msumeno wa umeme nusu saa ijayo, yule mrembo ambaye hatujamfanya chochote kibaya, tutafanya naye ngono mbele ya wenzake kabla ya kumuua, yeye lazima afe kwa kuingiliwa, huyo mpumbavu huko uliyemwka vibaya kwa kipigo, tutamchinja na huyo anayekuja anayejifanya ndiye mjuaji yeye atakufa kwa kulowekwa kwenye tindikali, ni hivyo tu. Kwa hiyo waambie wenzako muandae hivyo yote, nusu saa jopo lote litakuwa hapa kwa kazi hiyo,” akamaliza JoKi huku akicheka na ubaya wa sura yake kuonekana wazi mbele ya kila anayemtazama.
Sonyo kali likamtoka Madam S, “Mnajisumbua tu!” akaongea kwa shida sana huku akiwa bado kafungwa na ile minyororo.
“Unasemaje we Kibibi?” JoKi akamuuliza Madam S. kisa akatoka na kuufunga ule mlango nyuma yake huku akiwaacha wale walinzi wawili pale langoni wakiwa wamesimama kwa ukakamavu.
§§§§§
Scoba bado alitulia kimya ndani ya buti la gari, akichungulia mara kwa mara kujua ni wapi wanaelekea, mpaka wakati huo alishaanza kujua maana tayari waliiacha Bunju A na kuelekea mbele.
“Kumbe ishu zote Bagamoyo!” alijisemea na kuendelea kutulia ndani ya lile buti kuona mwisho wa safari ni wapi na vipi ataweza kuanzisha msinambe.
“Lazima wajue kama sisi ni T.S.A,” akajisemea huku bado akifungua kidogo lile buti ili kuona wapi wapo.
Scoba alifikiria kwanza kuanzisha msinambe huo kabla hawajafika katika ngome yao, lakini baadae akaona wazi kuwa siyo vyema kwani kuna wenzao ambao hawajui walipo, hivyo ni bora kufika katika ngome ya watu hao kisha kwa pamoja waweze kufanya kazi hiyo. Akiwa amezama katika mawazo hayo akahisi ile gari inakata kona, akafungua buti kidogo na kutazama nje.
“Tumekata kushoto,” akajisemea, kisha akatulia tena.
Ndani ya gari hiyo hakuna aliyeonge wote walitulia kimya kana kwamba hakukuwa na mtu ndani yake. Ile gari ikasimama mahala Fulani, Scoba akajiweka tayari, akatega sikio kusikia nini kinaongelewa huko nje.
“Mpo wenyewe tu?” akasikia sauti kutoka nje ikiuliza.
“Kama unavyotuona,” Naima akajibu.
“Ok, ingizeni gari mpaka egesho namba sita mtakuta maagizo yenu,” ile sauti ikasema na kisha ile gari ikaingia taratibu na mara ikasimama tena.
“Vipi?” sauti ya Naima ikamfikia Scoba ndani ya buti.
“Hamjafunga buti, na mna bahati polisi hawakuwaona,” ile sauti ya mwanzo ikasema. Scoba akaona mtu kasimama nyuma ya buti, akatoa bastola yake na kuiweka tayari kwa lolote. Yule mtu akashika lile funiko la buti akalifunga kwa kulisukuma.
“Aiyaaa!” Scoba alinung’unika kimoyomoyo akajaribu kulitikisa lile funiko lo, limefungwa, akatulia na kusukuti kuona nini cha kufanya na atatoka vipi. Ijapokuwa hilo kwake alikuwa tatizo lakini tatizo lilikuwa ni muda. Ile gari ikatoka pale na kuingia ndani kwa ni alihisi baada ya kusikia mlio wa geti lililokuwa likijitembeza kuruhusu gari hilo liingine ndani, kisha likasimama mahali.
Scoba alijua kutika getini mpaka hapo walipo ni kama mita ishirini na kwa jinsi mlio wa gari ulivyobadilika akajua wameingia ndani ya kitu au jingo. Akatulia kusikia kinachoendelea nje.
“Ha ha ha ha, Umekamatika paka wewe!” sauti ya JoKi ilisikika,
“Naomba mumshushe kwa umakini sana, na silaha zenu ziwe tayari akileta ujanja muueni tu, hawezi kutusumbua akili sisi, kwanza mfikisheni Golgotha mkamtie adabu ila hakikisheni mmemfunga vizuri,” JoKi aliasa. Scoba alitulia kimya akisubiri kujua nini kitajiri, mpaka hapo alijua wazi kuwa ni yeye tu mwenye uwezo wa kuwakomboa wengine wote.
§§§§§
Naima aliwaomba wale jamaa kumtoa Kamanda ndani ya gari,
“Hana fahamu huyo amenusa Mandrax kwa wingi sana,” akawaambia. Vijana wane wakasogea na kuweka bunduki zao migongoni kisha wakamteremsha Amata na kumsimamisha chini.
“Hana ujanja huyo!” JoKi akawaambia.
“Mpelekeni ndani nakuja mwenyewe kumpa adabu,” Naima akawaambia, na wale vijana wakamburuza mpaka mpaka ndani ya kile chumba walichoagizwa na kuanza utaratibu wa kumfunga.
Muda wote huo Kamanda Amata alijifanya kalala fo fo fo kutokana nay ale madawa kumbe la, alikuwa akiwavunga na kusubiri muda kuafaka wa kuwaonesha kama yeye ni T.S.A 1.
§§§§§
Scoba alipoona tayari utulivu umerejea na kuna lango limefungwa akaona sasa ni wakati wa kufanya makeke yake. Akafyatua mkanda wake wa kiuno na kuchomoa kitu kama pini hivi, akaipachika sehemu Fulani katika kile kitasa kwa upande wa ndani, kisha kwenye kiatu chake akachomoa kitu kama chipio na kukipachika upande wa pili wa ile loki, akajaribu kufanya anayojua na sekunde tatu zilikuwa nyingi, kikaachia.
“Waohhh!!” akapumua kwa nguvu kisha aakachungulia nje na kuona giza tupu.
Akaichukua miwani yake na kuivaa akaibana vyema kabisa ili isije kuanguka akiwa kwenye harakati, miwani hii ilimpa uwezo wa kuona gizani. Alipoivaa tu akaanza kuona vyema ndani ya giza lililomo katika jengo lile. Akaangaza na kuona kuna kamera moja ya usalama upande ule ambao yeye anapaswa kutokea, kutokana na giza hilo hakujali, akafungua buti taratibu na kutoka akitanguliza mguu mmoja bila kufanya kelele yoyote. Akarudishia buti na kulibana tena. Alipokwisha kulibana akashtuka na kujishika kinywa,
“Shit! Mi mpumbavu sana!” alijisemea maneno hayo alipogundua kuwa amesahau bastola kwenye buti. Sasa hakuwa na silaha yoyote, hakuna jinsi. Akajibana ukutani, kisha akajivuta taratibu mpaka karibu na mlango ambao bila shaka ndipo walipoingilia na Kamanda Amata, akashika kitasa na kukivuta chini taratibu, kisha akausukuma, ulikuwa wazi,
“Missing in action!” akajisemea kisha akaingia ndani ya korido ndefu, akaivua miwani na kuruhusu ining’inie shingoni mwake.
Ndani ya korido hii kulikuwa na mwanga wa kutosha, hakukuwa na mlango wowote isipokuwa mbele yake umbali wa kama mita mia moja aliona kuna kingo za chuma akajua kwa vyovyote kuna ngazi za kuteremka chini. Kikwazo kimoja kikawa mbele yake, katikati ya korido kulikuwa na kamera nyingine ya usalama, na ujia ule ulikuwa mwembamba kiasi kwamba huwezi kupita mbali na kamera hiyo,
“Walijenga makusudi hivi,” akajisemea na kuanza kufikiri jinsi ya kuipita kamera ile.
ITAENDELEA
Kitisho Sehemu ya Tano
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;