La Ultima Letra Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA: THE BOLD
*********************************************************************************
Simulizi: La Ultima Letra
Sehemu ya Nne (4)
Nidhamu na Ufanisi wa Kijeshi
Ili kupanua zaidi ushawishi wao, Los Zetas wakaanzisha oparesheni maalumu ya kudhibiti eneo la mpaka kati ya Mexico na Guatemala.
Ieleweke kwamba Cocaine ya nchini Mexico kiasi kikubwa kinaingizwa kutoka nchi za Bolivia, Colombia na Peru. Na kutoka kwenye nchi hizo ili uingie nchini Mexico ni lazima upite nchini Guatemala.
Serikali ya nchi ya Guatemala ni Moja ya serikali dhaifu zaidi kutokana na rushwa na ukosefu wa rasilimali fedha za kutosha. Hii ni sababu nyingine kuifanya kama ‘transit’ ya kupitisha biashara haramu.
Kitendo cha Los Zetas kudhibiti mpaka wa Mexico na Guatemala hii ilimaanisha kuwa walikuwa na uwezo wa kudhibiti mizigo ya mabosi wao pekee ndiyo inayopita mpakani na hivyo kufanya magenge mengine yatetereke kibiashara kutokana na kukosa ‘mizigo’.
Licha ya oparesheni za kikatili zilizokuwa zikifanywa na Los Zetas, lakini wanachama wa kikundi hiki walikuwa na nidhamu ya hali ya juu inayoakisi weledi wao wa kijeshi.
Los Zetas walikuwa hawajihusishi na vitendo vya wizi au ujambazi au kuua ama kuteka watu wasio na hatia.
Siku zote wenyewe wanajitanabaisha kuwa wnafanya matukio kwa watu maalumu ambao ni wapinzani wao kibiashara na kama hutaki kukutwa na madhira yao basi usijihusishe na biashara haramu.
Pia makamanda wa juu wa Los Zetas waliandaa nishani maalumu za kijeshi ambazo waliwatunuku wapiganaji wao ambao walitumikia Los Zetas kwa mafanikio makubwa.
Kutokana na ufanisi wa hali ya juu wa oparesheni za Los Zetas walifanikiwa kurudisha miji mingi kwenye himaya ya Gulf Cartel na kuonesha dalili kuwa Gulf Cartel wanaelekea kuwa vinara wa biashara ya mihadarati ndani ya America ya kusini wakiwapiku Sinaloa Cartel.
Katika miaka miwili ya mwanzo ya oparesheni za Los Zetas zilisaidia kurejesha zaidi ya miji 10 katika himaya ya kibiashara ya Gulf Cartel.
Ushindi wa Los Zetas katika Vita kuu II ya Magenge ya mihadarati.
Katika ulimwengu wa habari za kipelelezi hasa kuhusu magenge ya mihadarati, inaelezwa kwamba “vita kuu ya kwanza” ya magenge ya mihadarati ilitokea miaka ya 1980 kati ya Medellin Cartel na Cali Cartel.
“Vita kuu ya pili” ya magenge ya Mihadarati ilianza mwaka 2009 na ilikuwa kati ya Loz Zetas dhidi ya Gulf Cartel (mwajiri wa los zetas)
Walifikiaje katika vita hii???
Mwaka 2003 takribani miaka mitatu baada ya kuundwa kwa Los Zetas kikundi maalumu cha ulinzi ndani Gulf Cartel lilitokea tukio muhimu sana ambalo kilikuja kuwa na athari kubwa hapo baadae.
Maafisa wawili wa Kimarejani ambao mmoja aliitwa Dubois ambaye alikuwa ni afisa wa kitengo cha kudhibiti madawa ya kulevya cha Marekanj (DEA) na mwenzake aliitwa Fuentes ambaye alikuwa ni afisa wa shirika la upelelezi la marekani (FBI) wote wawili walikuwa ndani ya gari lenye namba za usajili za kidiplomasia lilikuwa linakatiza mitaa ya mji wa Tamaulipas ambao ndio makao makuu ya genge la Gulf Cartel.
Ndani ya gari hilo lenye vioo visivyoonyesha (tinted) kwenye siti ya nyuma walikuwa wamempakia mtoa taarifa wao (informant) ambaye walikuwa wanakatiza nae mitaa ya mji wa Tamaulipas akiwaekekeza namna ambavyo biashara ya madawa ya kulevya inavyofanyika na inavyopitishwa kwenda marekani.
Wakiwa wanaendelea kukatiza mitaa ghafla ikatokea gari nyingine ikaanza kuwafuatilia kwa nyuma. Wakataka kuongeza mwendo ili kuiepuka gari hiyo lakini ikatokea gari ya Polisi ikaziba njia mbele yao.
Kufumba na kufumbua zikatokea gari nyingine tatu na kuwazunguka kila upande.
Kisha watu wenye silaha nzito za moto wakashuka kwenye magari hayo na kuwaamuru maafisa hao washuke kwenye gari. Dakika chache baadae ilikuja gari ya kifahafi aina ya Jeep ambayo alishuka Boss wa Gulf Cartel Bwa. Cardenas.
Cardenas alikuwa ameshikilia bunduki aina ya AK47 ambayo kitako chake kilitengenezwa kwa dhahabu.
Kwa utulivu na kujiamini Cardenas akawaeleza kuwa hana shida na wao maafisa wa serikali bali ana shida na mtu waliyemficha kwenye siti ya nyuma ya gari (yule informant).
Maafisa wakakataa kuwa kuna mtu yuko siti ya nyuma! Cardenas akawaamuru wasogee pembeni alipekue gari ili ahakikishe kama kweli hakuna mtu siti ya nyuma. lakini maafisa wakakataa kwa kumueleza kuwa gari hiyo ni mali ya serikali ya marekani hivyo hawawezi kumruhusu raia wa kigeni kulipekua.
Cardenas akashikwa na hasira na kuwaambia kuwa anawapa nafasi ya mwisho wamsalimishe mtu waliye mficha siti ya nyuma lakini maafisa hao wakaendela kukaidi.
Cardenas akaamuru vijana wake wawamiminie risasi maafisa hao. Vijana wake wakawaua maafisa wa marekani papo hapo mchana kweupe tena mita chache kutoka makao makuu ya polisi wa mji wa Tamaulipas na hakuna askari aliyethubutu kuingilia.
Kisha wakamteka informant aliyekuwa ameficha siti ya nyuma na kuondoka naye. Mwili wake ulikuja kuokotwa siku mbili baadae akiwa amekatwa kichwa.
Kitendo hiki cha maafisa wa marekani kuuawa kinyama kiliamsha hasira za serikali ya marekani na wakaanzisha oparesheni maalumu ya kumsaka.
Hatimaye mwaka 2007 walifanikiwa kumkamata Cardenas na akashitakiwa na kuhukumiwa miaka 25 gerezani.
Lakini licha ya kuwa gerezani Cardenas aliendeleza biashara zake za madawa ya kulevya akiwatumia washirika wake wa Gulf Cartel na kuwaangamiza maadui zake kwa kutumia kikundi cha Los Zetas.
Mwaka 2009 kulikuwa na sherehe zijulikanazo kama ‘Day of The Child’ (siku ya mtoto) huko nchini Mexico.
Katika siku hiyo kwenye mji wa Tamaulipas kuliandaliwa sherehe kubwa ya kifahari ambapo watoto zaidi ya 2000 pamoja na wazazi wao walialikwa. Mwishoni mwa sherehe hiyo ikatangazwa kuwa sherehe hiyo imedhaminiwa na Cardenas.
Kitendo hiki kiliwaudhi sana serikali ya Marekani kwani ilikuwa kana kwamba Cardenas alikuwa anawadhihirishia kuwa licha ya kumfunga gerezani yeye bado alibakia “mfalme” nchini Mexico.
Hivyo basi Marekani ikawapasa watumie Sheria maalumu ya ‘Kingpins Act’ kuomba serikali ya Mexico kumuhamishia Cardenas kwenye magereza ya Marekani.
Mexico wakakubali na Cardenas akahamishiwa nchini Marekani.
ITAENDELEA
La Ultima Letra Sehemu ya Tano
Also, read other stories from SIMULIZI;