Magnum 22 Sehemu ya Pili
KIJASUSI

Ep 02: Magnum 22

SIMULIZI Magnum 22
Magnum 22 Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA: RICHARD MWAMBE

*********************************************************************************

Simulizi: Magnum 22

Sehemu ya Pili (2)

SHAMBA

“Nina habari ya kushangaza kidogo!” Chiba akarudia sentensi hiyo kwa sauti ya chini kisha akaendelea kucheza na kompyuta yake kwa hili na lile.

“Yes!” akashangailia na kuvuta kijitabu chake, akachukua kalamu na kuandika maneno mawili.

Kariakoo, Mtaa wa Sikukuu…

Kisha akaandika maneno hayo kwenye meseji na kuituma kwa Amata. Chiba alikuwa akifuatilia simu nyingi sana siku hiyo, ni hii iliyopigwa saa tano kasoro robo iliyomshtua kidogo kwa mambo mawili.

Kwa nini afiche habari hiyo? Ina maana ni siri, na simu hiyo yaani namba hiyo haijawahi kupigwa hapo kabla, haina historia kwenye mtandao ikiwa na maana ni namba mpya. Chiba akajishika nywele zake na kuzikuma nyuma mbele.

Hapa ni pazuri kuanzia! Akawaza.

Nahitaji kuwajua hawa, tema wameongea kiingereza tu, wazungu, ni akina nani? Akajiuliza. Chiba huwa hana mzaa akiamua kumfuatilia mtu kidijitali. Akainua simu yake na kupiga katika kampuni ya simu na baadae ikapokelewa na mtu aliyemtegemea.

“Asee! Kuna namba hii….” Akamtajia “…. Nataka kujua imesajiliwa lini na kwa jina gani” akauliza.

“Subiri kidogo niitazame!” akajibiwa, “usikate simu,” Chiba akaambiwa naye akatii kie alichoambiwa.

Hizi kazi hizi za kubahatisha hizi, majanga! Akajiwazia na wakati huo akasikia simu ikimwita… “Braza! Braza!”

“Sema!”

“Hiyo namba imesajiliwa siku nne zilizopita na mwanamama mwenye jina Elizabeth Mc Qued, katika ofisi yetu ya Mnazi Mmoja,” yule kijana akajibu, Chiba akaiandika pembeni na kumshukuru mtu huyo.

“Yes!” akajisemea. Huku akiinua simu na kumpigia Amata.

“Heee braza, wapi sasa?” akamuuliza.

“Nipo mitaa ya Msasani,”

“Kuna mzigo nahitaji uufatilie tujue ndani nje!” akamwambia.

“Sawa! Nasubiri….” Amata akajibu na kumpa ishara Gina kuegesha gari mahala pazuri. Kishs akachukua simu yake, haikupita hata sekunde kumi ujumbe ukaingia, akausoma kwa makini na kumpa simu Gina, naye akausoma pia.

“Kwa hiyo!”

“Twende Mnazi Mmoja sasa hivi,” Amata akamwambia Gina na ye’ akaingiza gari barabarani na kurudi mjini. Kutokana na foleni za barabarani hawakuweza kufika haraka, hivyo ilimpasa Gina kupita njia za vichochoroni na kufanikiwa kutumia kama saa moja na robo hivi kuwasili eneo husika.

Ndani ya ofisi hiyo kulikuwa na watu wengi sana, wao hawakujali, walichokifanya ni kuingia kwa meneja na kujieleza hasa ni nini wanachokifuata. Na baada ya kuonesha vitambulisho haikuwa tabu kupewa huduma. Yule meneja akaingia kwenye mtandao wao na kupekua hapa na pale na kuprinti fomu ambayo ina maelezo yote. Kamanda Amata akaitazama ile karatasi na maelezo yote kabisa, kisha akaitazama picha iliyokuwa katika karatasi hiyo.

“Elizabeth Mc Qued,” akatamka jina lake na kuitazama picha ya mwanamke huyo mwenye nywele ndefu zilizomwagika mabegani mwake. Macho yake yaliyoingia ndani kidogo yalimfanya aonekane kama mwanamke mwenye hasira. Akampa picha ile Gina kisha yeye akaagana na meneja huyo na kutoka nje tayari kwa safari. Wakiwa ndani ya gari, Amata akachukua ile karatasi na kuipiga picha kisha akamtumia Chiba.

“Ifanyie kazi!” akamwandikia kwenye meseji.


Chiba akiwa Shamba, akapokea taarifa ile kutoka kwa Amata na Gina, akaitazama kwa kina kisha akaingiza zile data katika kompyuta yake na kuiskani ile picha. Akajaribu kumtafuta mtu huyo kama anaweza kumpata kwenye mitandao ya kiusalama. Picha nyingi zikazunguka kwenye kompyuta ya Chiba kama dakika tano hivi na baadae ikasimama picha ya mwanamke anayefanana na yule kwa mambo mengi sana.

Angela Queen! Akasoma jina lililojitokeza kiooni, kisha akajaribu kuoanisha na picha ile aliyotumiwa na Amata. Jina la mwanamke huyo likawa linamjia kichwani mara kwa mara. Ijapokuwa mambo mengi hayakuonesha kushahabiana lakini Chiba alikuwa na shauku kubwa sana ya kumjua mwanamke huyo. Akainua simu yake na kumpa maelekezo ya wapi alipo mwanamke huyo.

Kutoka Mnazi mmoja Gina akawasha gari na kurudi mjini mpaka katikati ya Mtaa wa Azikiwe karibu na Mnara wa saa.

“Yupo hapo hapo, ningekuwa naweza kumwona ningewaambia, lakini hapa GPS yangu inanionesha kuwa anaelekea upande wa Posta Mpya,” Chiba akamwelekeza Amata na Gina. Amata akaangaza huku na huku asione mtu wa kumfananaisha, Gina naye vivyo hivyo.

“Hatumwoni!”

“Tazama vizuri!” Chiba akamwambia Amata, msako ukaendelea. Baada ya kuchunguza kwa makini, Amata akamshika Gina begani na kumpa ishara kuwa atazame upande wa jengo la posta. Mwanadada mmoja wa kizungu alikuwa akitembea harakaharaka, akiwapita watu huku akiwahi katika maegesho ya taksi pembezoni mwa benki ya CRDB. Macho ya Amata hayakubanduka kwa mwanamke huyo mwenye nywele ndefu, nyeupe.

“NI huyu kweli?” Gina akauliza.

“Ndo’ namwangalia” Amata akajibu huku akitoa simu yake.

“Unataka kufanya nini?” Gina akauliza huku akimtazama Amata nini anachotaka kufanya. Mara akamwona yule mzungu akiinua simu yake na kuiweka sikioni, mara akaitoa na kuirudisha katika mkoba wake.

“Ingia kwenye gari, uifuate ile taksi,” Amata akamwambia Gina. Wakaingia garini na kuondoka taratibu wakiifuata ile taksi. Baada ya kuzunguka picha askari wakachukua mtaa wa Makunganya, huko mbele wakapita mitaa kadhaa na kuivuka barabara ya Lumumba, wakachukua Mtaa wa Libya kuja upande wa Kariakoo. Wakati Gina akitaka kuvuka barabara ile tayari askari akasimamisha magari yanayotoka upande wa Mnazi Mmoja.

“Aaaaaaa shit!” Gina akapiga ukelele na kukanyaga breki kwa nguvu. Baada ya dakika kama tano hivi, yule askari akaruhusu magari ya upande wa Gina yapite. Kwa mwendo wa taratibu akaendesha katika Mtaa wa Libya na kuteremka kama anakuja Barabara ya Msimbazi, akakunja kushoto na kuangalia pembezoni kama ataliona lile gari, halipo. Baada ya kuufuata mtaa huo, mita kadhaa kabla ya Soko la Kariakoo akaliona limeegeshwa katika maegesho ya Hoteli ya Al Uruba.

“Egesha hapa!” Amata akamwambia huku tayari kafungua mlango wa gari. Wakatika Gina anaegesha yeye keshashuka, “nisubiri hapa!” akamwambia huku akikatisha barabara kuielekea hoteli hiyo. Tayari Kamanda Amata alikwishamuaona mwanamke yule kasimama kaunta hivyo hakutaka kupoteza nafasi hiyo. Akazikwea ngazi na alipofika mlangoni na yule mwanamke akawa anatoka akiwa na kijana mwingine wa Kizungu, wakapishana na Amata akafika kaunta na kusimama akitazamana na mhudumu wa kaunta hiyo.

“Nikuhudumie nini?” yule mhudumu akauliza.

Kamanda Amata hakujibu kwanza, akageuka nyuma kuwatazama watu wale, mara akasikia muungurumo wa gari na kuliona likipita kasi. Sekunde chache akamuona Gina naye katoka kasi kuwafuata, hakujali. Akageuka na kumtazama tena yule mhudumu, aliyekuwa akimalizia kufunga kitabu cha leja.

“Nahitaji kufika chumba namba 221,” akamwambia mwanadada huyo. Amata tayari alikwishapiga jicho na kuona chumba hicho kimepangwa na mwanamke, akajua kwa kuomba huko ni rahisi kupata ruhusa ya kuingia ndani yake. Lakini lengo lake hasa lilikuwa ni kufika chumba namba 119 ambacho ndicho alichofikia mzungu yule, na hili alilijua baada ya kuona funguo ya mwisho aliyoweka yule mwanadada kwenye shelfu yake. Amata akaruhusiwa, akazikwea ngazi mpaka ghorofa ya kwanza chumba namba kumi na tisa. Akasimama kwa muda na kuingia funguo yake isiyoshindwa kitu, akiwa tayari kavaa glovu mikononi, akauchezea ule ufunguo na mlango haukuleta kiburi. Amata akakaribishwa na chumba kipana chenye kitanda kimoja na kiti kimoja, begi kubwa lilikuwa ndani ya kabati ambalo mlango wake haukufungwa. Akaliendea na kutupa jicho ndani yake pasi na kugusa chochote. Macho yake tu yalitosha kukagua kila kionekanacho, hakukuwa na kibaya zaidi ya nguo tu. Zaidi ya hillo hakukuwa na kitu kingine katika chumba kile, Amata akageuka huku na huko, hakuona cha maana.

“Mh! Ni huyu au tumechanganya?” akajiuliza kwa sauti ndogo, kisha akausogelea mlango wa bafuni na kuusukuma taratibu, naaaam ni huku alipoikuta ile kanzu imefuliwa na kuanikwa.

“Yes! Nitakuwa mgeni wako usiku huu, humuhumu tutajua mbivu na mbichi!” akasema na kujitoa taratibu ndani ya chumba hicho, akatokomea nje.


Gina akajikuta anashindwa aende wapi, gari alilokuwa analifuatilia lilimpotea kwenye mataa ya makutano ya Barabara ya Bibi Titi, Ohio na Ally Hassan Mwinyi. Akatoa gari nje ya barabara na kuegesha kando ya jengo la Msalaba Mwekundu, akateremka na kuvuta hatua mpaka kwa askari wa usalama barabarani na kumuuliza kama ameliona gari hilo. Jibu alilolipata ni kuwa gari hilo limeelekea Mtaa wa Ohio. Akaingia tena garini na kuifuata barabar hiyo mpaka Mtaa wa Samora, hakuliona. Akachukua simu yake na kumpigia Amata.

“Vipi?”

“Wamenipotea!” Gina akajibu.

“Isiwe wamekugundua tu… maana kama ndivyo tutakuwa tumewagutusha…” Kamanda akamwambia Gina kwa simu hiyo.

“Hapana hawajanigundua,” akajibu.

“Ok usicheze mbali na mitaa hiyo, mgeni wetu wa jana ni yeye huyo, na lazima usiku huu tumfungie kazi,” Amata akamwambia Gina.

“Sawa Boss!” Gina akajibu na simu ile ikakatika.


Martin Gupter na Amanda Keller wakateremka na kuachana na taksi ile, wakavuka barabara na kupita kama mitaa mitatu hivi wakaingia kwenye Lexus Jeusi, humo wakamkuta Fredy akiwasubiri.

“Vipi? Kila kitu level?” Martin akauliza.

“Bila shaka, tutapata kila kinachoendelea katika mkutano huo, na hilo hapo mbele ndilo jingo letu la kulengea shabaha,” akamwambia Martin. Kijana huyo akalitazama kwa makini sana, “inabidi kujua njia za kuingilia bila kujulikana na mtu,” akasema.

“Usijali, nimepanda mpaka juu kabisa na picha nilizopiga ni hizi hapa!” akamwambia na kumpa simu yake kubwa atazame pande mbalimbali zinavyoonekana kutoka juu. Alipojiridhisha na picha hizo, akamrudishia Fredy simu yake.

“Nimeona!” akamwambia.

“Inachobidi kufanyika ni wewe kusubiri mpaka dakika ya tukio ikikaribia ndipo ujitokeze,” Amanda akaongeza kusema huku Fredy akiondosha lile gari mpaka barabara nyingine upande wa pili wa eneo la tukio. Akaegesha gari karibu na jengo lingine ambalo kwalo Fredy alijua kuwa halitakuwa na kash kash za ulinzi.

“Huku hawafiki, hivyo nitaweka gari hapa, mara tu baada ya tukio fika hapa haraka na ndipo tutakapoondokea, hakikisheni hamuachi alama yoyote nyuma kama tulivyofanya Angola na Ivory Coast.

“Nimekupata!” Martin akajibu na kujiegemeza kitini tena. Kwenye dashboard ya gari hilo saa ilisoma saa nane mchana.

“Sasa ni hivi, inabidi kuingia shimoni kwa sasa mpaka kesho saa nne asubuhi ndo awamu ya pili ya kazi yetu itafanyika. Baada ya mazungumzo hayo, Fredy akawasha gari na kuondoka.

VII

OFISI NDOGO

JIONI HIYO MADAM S alikutana na vijana wake ili kukusanya taarifa na tafutishi za siku nzima, kilichomfurahisha ni kwamba, vijana wake tayari walikuwa wamefanya kazi kubwa kuliko idara nyingine yoyote ya usalama katika ziara hii.

“Nawakubali!” akawaambia, “kwa hiyo huyu mnamhisi?” akaongeza swali.

“Kinachtufanya tumhisi ni kwa nini atumie jina la marehemu? Unajua wauaji wengi hupenda kutumia majina ya marehemu tena uhakikisha wamejua kila kitu kuhusu huyo mtu kisha utwaa jinale na kulifanyia kazi. Mpaka sasa huyu yupo kwenye tageti lakini kiuhalisia hatujui analengo gani la kufanya hivyo kwa sababu mpaka sasa hakitukia chochote…”

“Ndicho ninachodauti….” Madam S akaikata kauli ya Amata.

“Ila hatuwezi kumwacha!” Amata akasema.

“Siyo tu hatuwezi bali pia hatutakiwi kumwacha, ila naomba msimkamate kwa kuwa si kazi yenu, nataka mumfuatilie nyendo zake mjue hasa ni nini anafanya, ila msimwache kwa kuwa asije akaleta madhara….” Madam S akawaambia.

“Kesho ndiyo haswa siku ya kikao, sijui niwagawanye vipi, lakini naomba tu msiwe mbali na ukumbi wa mkutano kwani hatujui kipi ni kipi,” akaongeza kusema na kuwatzama viajana wake kwa zamu. Safari hii TSA haikuwa imekamilika kwani Scoba na Jasmini hawakuwepo kwatika timu kwa sababu za kikazi. Mara baada ya kikao hicho wakapeana mikakati ya nini cha kufanya usiku huo ikiwamo kumsaka yule anayejiita ‘Abdulah El Marik’.

USIKU WA SIKU HIYO

GINA aliegesha gari mtaa wa Pemba, nyuma tu ya hoteli ya Al – Uruba, “Here we are!” akamwambia Kamandal Amata aliyekuwa ameketi katika siti ya mbele.

“Yes! Kazi moja!” Amata akajibu huku akijiweka tayari, akapacjika bastola moja kiunoni huku akiweka silaha kadhaa sehemu tofauti za mwili wake. Shati lake jeusi na suruali ya rangi hiyo vilimkaa vyema kabisa, akachukua kofia aina ya ‘capello’ nyeupe akaiweka kichwani pake, tai ya rangi hiyohiyo nayo akaipachika shingoni.

“Nitakukuta haa baadae kidogo,” akamuaga Gina na kumpa busu zito la kinywani. Kisha akaondoka zake. Kwa hatua za harakaharaka akapita katikati ya maghorofa ya Wahindi na kujikuta kaibukia nyuma ya hoteli hiyo. Jukumu lililokuwa hapo ni kupanda kwa nje na kuibukia katika chumba hicho ambacho tayari alikuwa amekikariri jinsi kilivyokaa na upande kilichopo. Haikumuwia vigumu kwani alijua vyema jinsi ya kuifanya kazi hiyo. Akaikamata tai yake na kuvuta, akaitoa shingoni na kuitia mfukoni, akaivua kofia na kuigeuza ndani nje – nje ndani kisha akaivaa tena ikiwa ya rangi nyeusi. Kamanda Amata alitulia kimya kabisa kwenye kiambaza cha ukuta akisikiliza moyo na hisia zake kama kuna chochote ambacho kitamletea taabu muda huo, hakuna. Taratibu, akakamata ruva za kibaraza cha kwanza na kudanda kama nyani akihakikisha hafanyi kishindo cha aina yoyote ile kitakachosababisha watu kugutuka na kumharibia misheni yake. Dakika moja ilikuwa kubwa sana, tayari alikuwa amefika pale anapopahitaji, akatua kibarazani na kutulia akimya akiwa amepiga goti moja na sikio lake likisikiliza kwa makini kama ndani kuna mtu. Naam, sikio la Amata likafikiwa na sauti za watu wawili zikilalamika.

Muda muafaka! Akajisemea huku akiitoa bastola yake kiunoni na kuiweka tayari, akainuka taratibu na kusimama mkabala na mlango, mkono mwingine ukakamata funguo Malaya na kuitia tunduni polepole, akaizungusha kiasi kwamba hata watu walio ndani wasijue kama kuna kiumbe kinaingia ndani ya chumba hicho.

Kitendo cha mlango kufunguka ghafla ndicho kilichowafanya wawili wale wakatishe starehe yao na kukurpuka wakitaka kupiga kelele.

“Shhhhhhhh!!!!!!!!!” akawaaambi huku akiwa kawanyooshea bastola yake, “Mmepanga chumba hiki saa ngapi?” akawauliza.

“Sa- sa- a kumi jioni!” mwanaume akajibu huku akimeza mate.

“Shiit!” akang’aka na kuiweka bastola yake kiunoni, “samahani kuwavurugia starehe, kuna mtu niliyekuwa namtegemea kumkuta, sorry!” akawaomba msamaha na kutoka nje, akadanda kwenye ukuta wa kijibaraza na kuruka kwa ustadi mpaka chini, akatua bila kufanya ukulele, kisha akapenya kwenye njia zile zile na kulifikia gari. Akafungua mlango na kuingia ndani, akaketi huku akimtazama Gina.

“Go! Go! Go!!!!!!” akamwamuru na mwanamke huyo akaondoa gari kuufuata Mtaa wa Pemba mpaka Lumumba, akakunja kushoto na kurudi kama anakuja Umoja wa Vijana, kabla ya kufika makutano ya Barabara ya Lumumba na Morogoro akasimama na kutazama nyuma na kisha pande nyingine, usalama upo.

“Vipi?” akamuuliza Amata.

“Hayupo…”

“Hayupo?” akauliza kwa shauku ya kutaka kujua.

“Si ungemsubiri arudi….” Gina akasisitiza.

“Amehama chumba na si ajabu hata hoteli yenyewe,” Amata akajibu kwa kirefu.

“Oh come on!!!” Gina akahuzunika, “katuzidi akili, alijua kama tutamfuata au kahisi tu?” akauliza.

“Kujua kama tutamfuata labda kama ulimwambia wewe, lakini hivi hivi sijui kama anaweza kujua…” Amata akajibu na kutumbukiza utani humo humo. Gina akaamua kuliingiza gari barabarani na kuondoka zake. Muda huo Kamanda Amata akachukua simu ya upepo na kumpigia Chiba kumtaka afuatilie namba ile iko wapi kwa muda huo. Jibu alilopewa na Chiba lilimkatisha tamaa kabisa baada ya kuambiwa kuwa namba ile haisomi tangu saa saba mchana.

Saa saba mchana! Amata akawaza. Akili yake ikazunguka huku na huko lakini hakupata jibu la kuiridhisha roho yake. Akainua simu yake nyingine akapiga namba fulani na kuiweka sikioni.

“Yes, mtu wetu kapotea kwenye sight tangu saa saba!” akamwambia Madam S.

“Ok cha muhimu ni kuimarisha ulinzi wa nje, na tuombe kukuche salama, kama ana nia mbaya na kikao hiki basi na’ hakika tutamtia mkononi,” akamjibu na kukata simu.

Amata akaiweka simu ile mahala pake na kutulia kitini, akamtaka Gina kuendelea na safari mpaka nyumbani kwa Chiba, Msasani kwa Nyerere, wakaiacha Barabara ya Old Bagamoyo na kuingia kulia upande wa baharini mpaka kwenye jumba hilo.

“Karibuni wapendanao,” Chiba akawakaribisha Amata na Gina. Badala ya kujibu Gina akatabasamu na kumtazama Amata.

“Umesikia Amata….”

“Umeanza!” Amata akamjibu kisha wote wakaingia ndani.

Ndani ya sebule pana, Amata, Gina na Chiba waliketi kwa mazungumzo mafupi.

“Kwa nini atoroke?” Amata akauliza.

“Ndiyo hapo ninapokuwa na shaka na watu hawa, sasa tunao wawili, yule mwanamke na yule kijana aliyemchukua pale Al Uruba,” Amata akasema.

“Ndiyo, tunaunganisha mambo tu na moja na moja itakuwa mbili tu… uwanja wandege tulimshuku huyu kijana, nje ya uwanja wa ndege alilakiwa na huyu mwanamke, na sasa tumeona mchana huu akimchukua pale Al Uruba na kumpeleka sijui wapi… nafikiri sasa tuangalie ni wapi mwanamke huyu anaishi…” Amata akasema.

“Hilo ndo la mzingi kwa sasa,” Gina akaongezea.

“Anhaaaaa mawazo yamegongana, huyu mwanamke simu yake imewahi kuongea mara kadhaa Golden Tulip, nikiwa Shamba nimejaribu kufuatilia mazungumzo yale, nimegundua kuwa watu hawa hawaongei mambo yao kwa uwazi simuni bali hupanga kukutana ndipo huzunguza mipango yao… kwa nini wafiche? Hilo la pili, lakini lingine ni kuwa hawako wawili, hawa jamaa wapo watatu na ninahisi kuwa kwa sasa wapo pamoja ndiyo maana wameweza kuzima simu,” Chiba akaeleza.

“Watatu!” Gina akashangaa.

“Ndiyo, wapo watatu…”

“Haijalishi, twende Golden Tulip sasa,” Amata akawaambia wenzake huku akiitazama saa yake, saa saba usiku. Gina na Amata wakaingia garini na kuanza safari wakimuCha Chiba nyumbani kwake akiwa anawafuatilia kwa vifaa vyake vinavyoongozwa kwa satellite.

GOLDEN TULIP

SAA NANE USIKU, hoteli ya Kimataifa iliyojengwa kando kando ya Barabara ya Toure ilikuwa kwenye hali ya utulivu. Magari mengi yalikuwa maegeshoni na ni walinzi tu walikuwa wakipita huku na huko kuhakikisha usalama wa vyombo hivyo. Gina akaongoza gari mpaka katika maegesho ya hoteli hiyo.

“Tunawapataje?” Gina akamuuliza Amata huku akizima injini ya gari hilo.

“Tutatumia Soviet Method, kwani picha ya yule mwanamke huna?” Amata akamtupia swali Gina.

“Ipo!” Gina akajibu.

“Sawa, ichukue twende nayo,” Amata akamwambia Gina huku tayari keshafungua mlango na kuteremka nje. Gina naye akateremka na kumfuata, hatua zao zikawafikisha katika meza ya mapokezi ya hoteli hiyo. Katika ofisi hiyo kulikuwa na wanadada wawili waliovalia nadhifu na kupendeza kwelikweli.

“Karibu sana Golden Tulip, nikusaidie nini?” mmoja wa wale wadada ambaye beji juu ya kifua chake ilimtambulisha kama Esther Kwimba akawakaribisha.

“Asante sana, sisi ni maafisa uhamiaji tumekuja hapa tunamtafuta mtu huyu… je mmewahi kumuona? Akamwambia mrembo yule huku akimwonesha kitambulisho cha kazi hiyo. Mwanadada yule akachukua kitabu cha leja na kukiweka tena mezani.

“Alikuwapo hapa, lakini amecheck out, likizo yake imekwisha!” akajibu. Amata akamkazia jicho kana kwamba bado hajarizika na jibu hilo, “huamini au?” akaongeza swali.

“Si kwamba siamini, ila nataka unambie ni saa ngapi ametoka na nani?” Amata akampiga swali mwanadada yule. Akafunua kitabu cha wageni na kutazama mpaka kwenye jina lile, Angela Queen.

“Angela Queen, amecheck out saa 11 jioni ya leo,” akajibu mwanadada yule.

Kamanda Amata akamtazama Gina, “tumemkosa?” mwanamke huyo akauliza huku akiweka mkono wake shavuni kwa masikitiko.

“No!” Amata akajibu, kisha akaaga na kutoka na Gina mpaka kwenye gari.

“Hatuwezi kumkosa, kama ametoka saa kumi na moja ina maana kwamba ndege yake ni saa moja usiku au saa kumi na mbili jioni ….”

“Ikizidi sana saa mbili usiku,”

“Yes! Kwa maana hiyo hatuna budi kutazama kama kuna ndege ya kutoka nje ya Tanzania mida hiyo,” Amata akamwambia Gina. Gina hakutaka kuchelewa akainua simu na kupiga kwa Lulu kutaka kujua kama kuna ndege yoyote ya kutoka nje ya Tanzania, jibu ambalo alilipata ni kuwa ‘hakuna’. Akamtazama Amata kwa nukta kadhaa kisha akamwambia, “Atakuwa humuhumu nchini”.

“Usiseme nchini, kwa kusema hivyo ndiyo unazidi kumpoteza, sema humuhumu jijini…”Amata akaongezea.

“Wapi sasa?”

“Sijui!” akamjibu huku akijiegemeza kitini na mkono wake ukishikwa kichwa, ukimya ukatawala kwa nukta kadhaa kati ya wawili hawa.

“Gina!”akaita, “sasa naweka nguvu zangu kwa asilimia tisini kwa mwanamke huyu na hao wenzake, mchezo wanaufanya unanitia mashaka, naihisi hatari mbaya sana siku ya kesho,” akamwambia.

“Yaani…. Kama sijakuelewa flani hivi,” Gina akaonesha mashaka katika hilo.

“Nasema, hawa jamaa sasa inabidi tuwafungie kazi, naanza kuhisi hatari siku ya kesho,” akarudia kusema.

“Kwa hiyo!”

“Yaani hapa tulipofikia yatupasa kutoa taarifa panapohusika ili kuanzia asubuhi ulinzi uwe mkali kila kona. Akamwambia Gina huku akifunga mkanda wa gari lake. Tayari jogoo wa kwanza alikwishawika, huyu kwenye mila zetu tungemchinja kwa sababu kafanya hivyo kabla ya wakati.

“Kumekucha, twende tukalale,”

“Unataka cha asubuhi?” Amata akamtania.

“Toka hapa!!!!” akamwambia huku akiwasha gari na kuyaacha maegesho hayo taratibu.


SIKU ILIYOFUATA

PAMABAZUKO LA SIKU HII lilimkuta Kamanda Amata na Gina kitandani, ni sauti ya kengele ya mlango ndiyo iliyowakurupusha katika usingizi wao.

“Aaaaaaaahhhhhhhh!” Gina akainuka na kutwaa koti lake lililoshonwa kwa kitambaa kizito cha taulo. Akavuta droo na kuchukua bastola yake ndogo akaifutika katika mfuko wa ndani huku mkono wake ukiwa huko, akatoka chumbani na kuelekea sebuleni. Akafika na kuufungua mlango macho yakagongana na kijana muuza maziwa ambaye anamfahamu, daima huja kumletea bidhaa hiyo.

“Leo mbona umewahi sana?” akamwuliza.

“Nina safari saa tatu asubuhi ndo maana nimekuetea mapema, hata hivyo nilijua kuwa umetoka maana niliona gari inageuza hapa getini,” yule kijana akamwambia.

“Gari?”

“Eee gari moja ya bei mbaya sana, nyeusi hivi… lakini ilivyonipita kwa mbele nikaona kuna wazungu watatu…”

Gina akatahayari kwa maneno hayo, akajiuliza juu ya gari hilo, hakulijua.

“Ok! Labda walipotea njia!” akamwambia na kumshukuru, kisha akamwambia asubiri kidogo, akaingia ndani na kumletea shilingi elfu ishirini kama nauli kwa safari kwa kuwa kijana huyu huwa anamsaidia mara nyingi hata kazi za hapo nyumbani. Mara baada ya kurudi ndani akamkuta Kamanda Amata akiwa tayari ndani ya suti safi.

“Vipi baba?” akamuuliza.

“Vipi?! Kazi mama, unajua leo ni siku ngumu sana, by the way kijana anasema ni gari gani lilikuja?

“Ee mwanaume hupitwi, wivu tu, yaani ushakuja kusikiliza…”

“Ndiyo, lazima nijue nini kinazungumzwa,” Amata akajibu huku akifunga vifungo vya mikono ya shati lake.

“Ninapata wasiwasi, anasema kuna gari jeusi lilikuwa na Wazungu watatu ndani yake, nina wasiwasi kwa sababu huyu tunayemsaka hata pale uwanja wa ndege alitumia gari jeusi…”

“Hata Chiba alituambia kuwa anahisi wapo watatu,” Amata akamwambia, “kwa hiyo wamekuja mpaka nyumbani, wamepajuaje? Walikuwa wanatufuatilia?” akaongeza maswali yaliokosa majibu.

“Vaa tuondoke! Haraka!” Kamanda akamwambia Gina na ni nukta hiyo hiyo simu yake ikaita kwa fujo, akaichuku na kuitazama, Chiba.

“Ndiyo kaka!” akaitikia.

“Jiangalieni nahisi mpo hatarini, kwa usalama tokeeni mlango wa nyuma,” akamwambia kupiti asimu hiyo. Dakika ishirini baadae, Gina naye akawa tayari, safari ikaiva.

“Tutokee mlango wa nyuma!” Amata akamwambia Gina, naye hakubisha, wakatumia njia hiyo kutoka nje, wakakodi taksi na haraka wakaingia katikati ya jiji. Breki ya kwanza ilikuwa ofisi ndogo. Madam S alikuwa tayari ndani ya ofisi hiyo, zaidi ya yeye safari hii kulikuwa na mgeni mwingine zaidi, Inspekta Simbeye.

“Nilijua tu kuwa muda huu mtaingia, haya hatuna muda wa kupteza…” akawaambia huku akiwataka kuketi.

“Kumekucha na siku yetu ni hii, kwa ushirikiano wetu tutaweza kuzuia jaribio la mauaji ambalo lina tetesi ya kutokea,” Madam S akasema.

“Mauaji?” Amata akauliza.

“Ndiyo, Simbeye alikuwa hapa,”

Inspekta Simbeye, akiwa ndani ya nguo za kiraia, lakini mkononi mwake kukiwa na simu ya upepo, alikuwa ofisini hapo dakika chache tu zilizopita. Ni mara chache sana ya Inspekta huyu wa kudumu kuja katika ofisi hii, kazi zao daima hufanyika mahala popote wanapochagua.

“Amepata hii meseji…” akampa simu Amata.

“Tunajua, mnatufuatilia,

lakini mjue kuwa tumejipanga na

tutatekeleza azma yetu,

lazima Somali Land iwe huru.

Tunahitaji Ardhi ya mama zetu,”

Ni sisi Freedomfighter!”

Kamanda Amata, akairudisha simu ile kwa Madam S, “ndiyo tunawafuatilia, na leo hii tutawatia mkononi,” akamalizia kusema.

“Mh! Wajitangaza sasa,” Gina akasema.

“Wameona tayari mmegundua nyayo zao,” akajibu, “sasa nataka niwape mpango kazi wa kufanya,” akaongeza.

Madam S akajikohoza kusafisha koo, “tatizo hatujui ni wakati na saa ngapi na ni njia gani watu hao watatekeleza mpango wao,” akawaambia.

“Yes!!” wakajibu kwa pamoja.

“Good sasa mpango wa kwanza ni kuzuia mkutano kuanza saa tatu, tukague ukumbi mzima kama kuna mlipuko au kitu chochote ambacho kitahatarisha uhai wa mtu. Pili tukiruhusu mkutano ufanyike tuhakikishe tumekagua gari zote za viongozi hao kabla hawajapanda kuja ukumbini, na ukaguzi wa kila mtu anayeingia ukumbini, asiruhusiwe mtu kuingia na simu, saa, wala chochote kile cha mawasiliano au chuma. Naongeza kuwa viongozi wote wasile chakula wala kunywa maji kutoka katika hoteli hiyo…” Madam S akatoa muongozo wa kwanza, akamgeukia Simbeye.

“Inspekta nimemwambia kuwa ninathitaji vijana wake wa kikosi maalumu kuanza kuweka ulinzi kwenye ukumbi huo sasa, ili kuzuia mtu yeyote kuingia ndani ya eneo la ukumbi huo,” akawaambia. Baada ya hapo akachukua simu maalumu ya ofisi na kupiga mahala fulani pa siri, akatoa angalisho la kuzuia mkutano huo kwa muda. Hakutaja muda gani ila alieleza hilo na kutaka kuonana na Mkuu wa Itifaki ya mkutano huo haraka iwekanzvyo.

“Kamanda Amata, hakikisha unategua kitendawili hikl ndani ya dakika chache zijazo kwa kombat ya aina yoyote, Chiba utakuwa na Amata, lakini wewe unajua ni nini cha kufanya, fuatilia hii meseji ujue imetoka wapi nahitaji ndani ya dakika chache tu uwe umenipa jibu. Gina nataka ufanye kazi ndani ya ukumbi wa mkutano kwa siri, hakikisha hutambuliki kwa yeyote, najua unajua nini cha kufanya.


Madam S alikutana na Mkuu wa Itifaki katika ofisi yake ndani ya jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani. Hakikuwa kikao bali ni kupeana maagizo juu ya nini cha kufanya katikma mkutano huo.

“Unajua kuzuia mkutano kwa muda usiojulikana tunajenga picha mbaya sana katika uso wa kimataifa, kuna wajumbe wa Commoniwealth na UN na jumuia nyingine kubwa ambazo kwazo sisi hutegemea mengi. Sasa wanajua saa mbili tunatakiwa ukumbini then mnachelewesha mambo, Wazungu hawa watatasusa mkutano…” akazungumza bwana yule aliyetuna kitini kama chatu aliyemeza mbwa.

“Achana na Wazungu, mambo ya Afrika lazima yaamuliwe na yafanywe kiafrika, mkutano umeahirishwa kwa sababu za kiusalama, kuna tetesi za umwagikaji wa damu katika mkutano huu, inaonekana wewe wapenda litokee siyo?” madam S akamwambia huku akiwa tayari kainuka kitini.

“Si napenda litokee, bali mambo ya kiitifaki hayaendi hivyo mama,” akamwambia.

“Sasa ni hivi, kikao kitaanza itakapotangazwa, na ikiwezekana, hakitakuwepo kwa kabisa au tutabadilisha ukumbi,” Madam S akamwambia.

“Kubadilisha ukumbi?” akauliza huku naye akijitahidi kusimama kuonesha msisitizo lakini tumbo lake likamzuia kufanya hivyo. Wakati huo Madam S tayari alikuwa keshafungua mlango anaondoka.

Katika mahoteli yote ambayo wageni wale walifikia kulikuwa na ulinzi mkali sana, askari wenye sare na wasio na nazo walikuwepo, kila mmoja akiwa ametingwa na kile anachotakiwa kufanya. Hali ilikuwa tete, vijana wa Usalama wa Taifa walikuwa hai hai kujaribu kugundua mpango huo kila eneo muhimu ambalo walilihisi, lakini kazi ilikuwa ngumu.

Asubuhi hiyo hiyo, Gina alitinga katika ukumbi wa mkutano kama alivyotakiwa kufika, katika lango kuu la kuingia katika eneo la ukumbi huo, aishuhudia askari wa FFU na baadhi wa JW wakiwa wameweka ulinzi mkali, waandishi wa habari na watu wengine ambao tayari walikuwa wamewasili, wakatakiwa kukaa mbali kidogo na eneo kwa kuwa kuna kazi iliyokuwa ikifanyika.

“Akuna cha bomu wala nini,” akasikika mtu mmoja akisema.

“Basi tu, tunataka kuonekana tuko makini na usalama hamna chochote, walishindwa Angola na Ivori Coast kuzuia mauaji ya viongozi itakuwa sisi….” Mwingine aisikika, huyu ni kati ya wale Watanzania wanajidharau na kutokujiamini. Barabara kadhaa zilifungwa tayari kuruhusu wageni wa mkutano huo kuwasili muda wowote.

Kati ya watu waliokuwa katika kundi la waandishi wa habari, alikuwapo Amanda Keller akifuatilia kila kitu kwa ukaribu kabisa. Na taarifa zote ambazo zilipatikana hapo, zilifika kwa Martin na Fredy moja kwa moja. Hakuna mtu ambaye alimjua mwanamke huyo kuwa ni ‘kidudu mtu’ kati ya watu hao, na kutokana na mchanganyiko wa waandishi Wazungu kwa Waafrika haikuwa rahisi kumjua.


Ndani ya hoteli ndogo ya Kunduchi Beach huko Kunduchi, Martin na Fredy walikuwa wakipata kifungua kinywa huku wakisika mengi kutoka kwa Amanda.

“Wanafikiri sisi ni wajinga kufanya kazi yetu kwa wazi hivyo?” Fredy akamuuliza Martin.

“Sisi ni profesheno, yani nitamtungua huyo jamaa mpaka wenyewe watashangaa, salama yao ni kuachia ambacho tajiri wetu anataka,” Martin akamjibu Fredy huku akiweka kikombe cha kahawa kinywani na kupiga funda moja kwa mruzi.

“Wanafanya ukaguzi kama kuna mlipuko wowote….”

“Hah! Hah! Hah! Hah! Waache wafanye mazoezi maana hakuna watakachopata…” Martin akazungumza, “ni risasi moja tu basi ambayo wanatakiwa kuitafuta na si bomu au kemikali au sumu ya kwenye chakula, na risasi hii ninayo mimi peke yangu tu, na ndiye ninayejua ni wakati gani wa kuiruhusu ifanye kazi yake, na wasipoangalia watakufa wao, tena kifo kibaya,” akamwambia Fredi huku mkononi akiirusharusha risasi moja kubwa.

Upande wa pili, Chiba alikuwa ndani ya gari lake akiendesha taratibu huku akijaribu kufuata mawasiliano fulani ambayo aiyahisi si ya usalama sana. Kutoka ndani ya gari hilo aliweza kusikia sauti ya Amanda ikipeleka taarifa mahali fulani. Alichokuwa anafanya yeye ni kufuata wapi mawimbi hayo yanaelekea kwa kuangalia nguvu yake kawenye chombo hicho. Sasa alikuwa tayari maeneo ya Tangi Bovu na signal ilimwonesha kuwa upande huo wa Bagamoyo ndiko mawimbi hayo yanakwenda.

“Nina uhakika wa kuwatia mkononi muda si mrefu, huyu mwanamke yupo huko mjini ila sijajua ni eneo gani, na inaonekana anajua information zote,” Chiba akamwambia Amata kwa kifaa chake maalumu ambacho hakiingiliani na mawasiliano yoyote ya huko duniani.

“Ngoja nijaribu kumgundua kama nitafanikiwa maana inaonekana anajua sana kujibadili,” Amata akamjibu Chiba, “na ukigundua ni wapi walipo, naomba unijulishe usifanye kitu, ili tuje tuwatie displin na wajue kuwa sisi si watu wa mchezo mchezo,” akaongeza kusema huku akiwa mita chache kutoka Hoteli ya Kepinski Kilimanjaro ambapo Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye ni Rais wa Ganbia pamoja na marais wengine walifikia mahala hapo. Ulinzi wa hapo haukuwa wa kawaida, kila aliyeingia alikaguliwa mpaka maeneo nyeti kabisa ya mwili wake.


Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa akakutana kwa siri na Mkuu wa Itifaki, mara hii ndani ya Ikulu, yaani makao makuu ya Rais wa nchi.

“Mheshimiwa, sasa tunaweza kuruhusu shughuli ziendelee, vijana wanasema usalama upo mwingi tu, hakuna walichokigundua kibaya,” yule Mkurugenzi akamwambia Mkuu wan chi huku mwanaitifaki yule akitikisa kichwa kuafikia hayo.

Baada ya kutafakari kwa sekunde kadhaa, akawataka kusubiri, akawaacha sebuleni na kuingia ndani katika chumba chake cha siri, akainua simu yake na kupiga namba fulani, akampata Madam S ambaye yeye ndiye aliyekuwa na usemi wa mwisho wa Rais huyo.

“Hali ikoje huko?” akamuuiza.

“Vijana hawajagundua chochote kibaya, nimewapa taarifa watu wa usalama na itifaki kuwa sasa shughuli inaweza kuendelea lakini ulinzi ndiyo kitu cha muhimu sana,” akamjibu.

“Sawa! Asante, nategemea hautakuwa mbali na eneo,” akamwambia.

“Bila shaka, na nitaongeza minzi wa siri kwa mgeni wetu kwa kuwa siamini mtu zaidi ya viajan wangu tu,” Madam S akamwambia.

“Fanya hivyo,” Rais akamwambia na kukata simu.

Saa nne kamili, waandishi wakaruhusiwa kuingia ukumbini na wageni wengine, wakapangwa mahala pao tayari kwa mkutano huo. Dakika kama ishirini baadae, ving’ora vikasikika na gari za bei mbaya sana zikaingia mfululizo katika eneo la ukumbi huo na kuegeshwa mahala salama kabla vingozi kuruhusiwa kushuka. Walinzi maalumu kutoka nchi ambazo marais wao walikuwapo waizingira magari hayo pande zote, huku masikioni mwao wakiwa na vifaa maalumu vya mawasiliano. Hakuna aliyejua ni nani wanayewasiliana naye, ilikuwa siri yao. Saa nne na nusu wote kwa pamoja wakafungua milango na kuwateremsha viongozi hao kisha kuwaingiza ukumbini humo, lakini kati ya wote hao, rais wa Gambia ambaye ndiye haswa mwendesha mkutano hakuwapo. Yote haya Amanda alikuwa akiyaona yote na kuwapa taarifa watu wake.

Kule Kunduchi, tayari vijana wale walikuwa wakijiandaa kuondoka kuelekea mjini tayari kwa kazi waliyotumwa. Martin akiwa chumbani kwake, akafunga kila kilicho chake tayari kwa safari na Fredy vivyo hivyo. Baada ya kila kitu kukamilisha wakaweka kila kitu ndani ya gari na wao kujipakia tayari kwa safari.

Chiba alifika katika hoteli hiyo na kupishana na gari lile getini pasi na kulichunguza sana, akaingia na kuegesha la kwake ndani kisha akateremka mpaka mapokezi. Alikuwa na uhakika kabisa kwamba mawasiliano hayo yametoka hapo.

“Karibu Kunduchi Beach Resort!” akakaribishwa na kijana mmoja mrefu mwenye asili kama ya Kisomai hivi.

“Asante sana, ninauliza mwenyeji wangu kama nimemkuta,” Chiba akamwambia huku akitoa picha na kumwonesha. Yule kijana akaichukua na kuingalia mara moja tu, akamrudishia kisha akatikisa kichwa kushoto kulia.

“Vipi?” Chiba akauliza.

“Dah! Kaka umejipatia dodo nini…. Maana wanawake hawa Wakizungu ni wagonjwa sana wa mapenzi ya kiafrika….” akasema.

“Kajilengesha mwenyewe mi nifanye nini, kuna mwanaume anayekataa mwanamke wa Kizungu, kwa mfano wewe angeamua kukupa, ungekataa?”

“Aaaaa brazaaa si unajua tena, bahati za wachache hizo, nikiipata siiachi,”

“Sasa je! Chumba chake kiko wapi?”

“Namba 50, Impala!” akamjibu. Chiba akavuta hatua mpaka upande wa vyumba na kukagua mpaka akakipata hicho akitakacho. Akapiga jicho katika tundu la ufunguo, hakuna ufunguo, akili ya kwanza ikamwambia kuwa ndani humo hakuna mtu. Akatazama huku na kule yuko peke yake eneo hilo, akachukua funguo yake na kuipachika, akanyonga mara mbili kitasa kikakubali tekenyo hilo, ukafunguka. Chiba akakaribishwa katika chumba kipana cha mviringo kilichobeba samani za thamani.

Bila shaka hii ni suit! Akawaza na kuingia ndani taratibu kisha akaufunga mlango nyuma yake. Akaitazama saa yake na kuizungusha kwenye pete ya juu, akasubiri kama sekunde kumi hivi hakuna chochote. Akachukua kifaa chake cha mawasiliano na kuwasiliana na Amata, akampa taarifa kuwa yupo chumbani kwa mwanmke huyo. Kamanda Amata akampa ‘go ahead’. Chiba akapekua hapa na pale, akainua hiki na kile, katika meza moja akakutana na kadi sakima ndogo kabisa ‘micro chip’ akaitazama kwa mahaba na kuichukua kwa uangalifu mkubwa, akaipachka katika simu yake na kuhamisha mafaili yote katika simu hiyo, kisha akaichomoa na kuirudisha mahala palepale. Akafungua moja baada ya jingine kusoma japo vichwa vya mafaili hayo. Lakini wingi wake haikuwa rahisi kumaliza yote hayo. Akaendelea kupekua hapa na pale na ndipo akakutana na begi moja dogo, alipolifungua, akakutana na nwele bandia kama sita hivi za aina tofauti na midomo bandia, nyusi, kope mpaka mboni za macho.

Mshenzi huyu, ndo maana anatusumbua si ajabu hata wanaume wake nao hujibadili! Akawaza na kuviacha kama alivyovikuta. Katika kuendelea kupekua pekua hakukuta kitu zaidi, akaamua kutoka ndani ya chumba kile akakifunga na kurudi kaunta.

“Ah mara hii?” yule kijana akauliza.

“Hapana, nitarudi muda si mrefu kuna vitu nachukua nje hapo,” Chiba akajibu huku akielekea garini, akawasha na kuondoka. Akiwa njiani akaegesha mahala na kuchukua simu yake.

Inawezekana kuna faili za kushughulikia haraka kabla sijafika mjini! Akawaza, kisha akafungua ile simu na kupekua mafaili mengi mengi, lakini haya hakuwa na mvuto nayo ijapokuwa yalikuwa ni ya mipango mingi mingi tu. Katika karibu na kukata tama akakutana na faili moja lililoandikwa Magnum 22, kwanza akalipuuza, lakini baadae, akaamua kutazama nini kilichopo ndani yake. Hakuamini macho yake, taarifa za mipango yote ya mauaji zilikuwa humo, ijapokuwa hazikueleza mengi yaliyopita, ila zilieleza mpango mkakati wa mauaji ya Dar es salaam, na wakati gani wa kufanya mauaji hayo. Chiba alihisi jasho likimtiririka kwapani, lakini kilichompa faraja ni kuwa wauaji wanasubiri hatima ya mktano huo ndipo wauae endapo ombi lao litakuwa limekataliwa. Akaitupa simu yake kitini na murudisha gari barabarani kisha akaondoka kwa kasi sana kuelekea mjini. Akatazama saa yake, tayari ilitimu saa sita kasoro robo, akainua simu yake na kumpigia Amata.

“Nakupata Chiba!” Amata akaipokea.

“Mkutano umefikia ratiba gani sasa?” akamuuliza.

“Wapo kwenye speech ya mwisho, Mkuu wa Nchi anashukuru ugeni huo…” Amata akajibu kwa kuwa hata yeye alikuwa akisikiliza kupiti chombo maalumu, na hakuwa mbali na eneo hilo.

“Agenda ya Somali Land, imetengwa au la?”

“Chiba mbona unaniuliza maswali ambayo yananitatanisha?” Amata akaongea kwa ukali.

“Just nijibu…”

“Imekataliwa, na wamesema haiwezekani kuwa hivyo!” Amata akajibu.

“Sasa….”

“Chiba kikao kimeisha, ngoja nicheki nini kinaendelea…”

“TSA 1 muuaji atatumia Magnum 22 mpango wao ni kumdungua Rais wa Gambia kutokea juu ya ghorofa la TPSA, wakati wa kupiga picha ya pamoja,”

“What? Chiba!” Amata akaita huku akifungua mlango wa gari na kuubamiza, akainua macho kutazama ghorofa lile, hapo ndipo akagundua kuwa ni kweli kutoka juu ya jingo hilo unaweza kumpata kirahisi mtu akiwa katika mlango mkuu wa ukumbi ule.


Kwenye gari ambalo ndani yake kulikuwa na Fredy na Martin, walikuwa wakipata kila kitu kutoka katika mkutano huo. Amanda kutoka ndani ya ukumbi wa mkutano alikuwa akiwapeperushia mawasiliano yote, kila kilichokuwa kikizungumzwa na kuamuliwa. Mara baada ya agenda za mkutano kwisha, ikafuata hotuba fupi ya shukrani kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama mwenyeji kuwashukuru wageni hao. Ni wakati huo Gina alipokuwa tayari kamhisi mwanamke yule aliyejipachika katikati ya wanahabari wa kimataifa, aliporudisha macho tena, hakumwona. Gina akahisi kupata ganzi na tayari viongozi walikwishamaliza mkutano, sasa walikuwa wakipeana mikono tayari kwenda nje kwa ajili ya picha ya pamoja.

“Wamekataa, hatuna budi kutekeleza tunalopaswa,” Fredy akamwambia Martin.

“Umeona mwenyewe jinsi jamaa wanavyotuandama, wamegundua nyayo zetu, tunapotoa mguu nao wanakanyaga…”

“Sekunde tano mbele yao tupo salama, na hakika hizo tano tutakamilisha kila kitu…”

“Amanda!”

“Nimeshamwambia jinsi ya kutoroka…” Fredy bakajibu.

Martin akateremka garini na mkoba wake, akavuka barabara na kulipita jingo la kwanza kisha akaingia lile la pili la TPSA, akaingia kwenye lifti na kwenda juu kabisa, huko akakiendea kibanda kidogo ambacho kilikuwa na mitambo yote ya kuongozea lifti hiyo, akaiharibu na kuzima umeme ndani ya jingo hilo. Harakaharaka akafungua mkoba wake na kuchomoa vipande vitatu vya bunduki, akaviunganisha kwa haraka na kuiweka tayari, risasi moja akipachika ndani ya bunduki hiyo, Magnum 22 riffle, akafyatua miguu yake na kulala chini kimya huku akijifunika tambara ambalo lilifanana rangi na sakafu ya eneo hilo na kuruhusu mdomo tu wa buduki kutokeza nje. Jicho lake likiwa tayari kwenye lensi yenye nguvu kabisa alikuwa akiwaona viongozi wale wakitoka nje huku ulinzi maduhubuti ukiwa umewazunguka. Kila alipojaribu kumuweka kwenye shabaha yule anayemtaka watu walikuwa wakipita hapa na pale na kumpoteza shabaha.

“Shabaha ngumu Fredy!” Martin akamwambia Fredy kwa chombo chao cha mawasiliano.

“Five seconds Martin,” Fredy akamjibu.

Mikikimikiki ilikuwa kwa watu sita tu kwa muda huu, hakuna mwingine aliyejua nini kinaendelea kaetika eneo hilo. Gina alikuwa akizungusha macho huku na kule kujua ni wapi mwanamke yule wa kizungu kapotelea, Chiba alikuwa akifanya juu chini kutafuta mawasiliano mengine ambayo aliyanasa yakiwaunganisha watu hao, Kamanda Amata akitaka kuhakikisha muuaji hafanikishi azma yake yeye akiwepo hapo. Upande wa pili, Martin Gupter akiwa anahaha kutafuta shabaha maridhawa kummaliza mtu wake, Fredy akiwa anajaribu kumpa tumaini Martin kumaliza kazi huku akijipanga ni jinsi gani ya kumuokoa mtu huyo, Amanda akiwa tayari katoweka ukumbini na kupotea kusikojulikana, ilikuwa ni shida. Wanausalama wengine wakiwa wanaendelea kufanya kazi zao za kiusalama wakiwa wanajua hali ni shwari kama walivyo hakikishiwa.

Kamanda Amata akaingia ndani ya jingo lile, akaifiki lifti na kujaribu kuibonyeza hapa na pale.

“Steppppssss!!!!” sauti ya Chiba akamfikia kutoka nyuma. Watu katika jingo hilo hawakuelewa kinachoendelea, wakaona ni kama moja ya muvi za Hollywood. Amata akakamata ngazi na kuanza kupanda kwa kasi huku akikimbia kuelekea juu, nyuma yake akifuatiwa na Chiba.

“Wana sekunde tano tu,” Chiba akamwambia Amata.

“Twendeeeee!!!!” Amata akapiga kelele na kuendelea kukimbilia kule juu.


Wakati picha ikiwa tayari kupigwa pale mbele ya jengo la mkutano, mabodigadi walikuwa makini kabisa kuangalia kila mtu na kila mpiga picha maana walikuwa wakijua kuwa aina ya budnuki huwa kama kamera. Gina akiwa anajua nini alichotumwa, akaivaa miwani yake na kuangaza huku na huko, miwani ile iliweza kusogeza taswira ya kila mtu anayekuwa mbele yake. Ni hapo alipoinua uso wake juu kutaza lile jingo baada ya kusikia mazungumzo ya Amata na Chiba. Kitu cha kung’aa kilimulika usoni mara moja akili yake ikamwonesha hatari, hakusubiri nini wala nini. Kutoka yeye mpaka pale waliposimama Rais wa Gambia na wa Tanzania ilikuwa ni kama mita nne hivi, na walinzi wengine walikuwa wamezunguka huku na huko. Alichosikia sikioni mwake ni jina lake.

“Dowwwwwwnnnnn!!!!!” akapiga kelele huku akijirusha mzima mzima na kuitawanya miguu yake hewani. Mguu mmoja ukatua kifuani mwa Rais wa Gambia na mwingine kifuani mwa Rais wa Tanzania, kutokana na nguvu ya kiki hiyo maraisa wale wte wakaenda chini. Mmoja wa walinzi wa Rais wa Gambia alikuwa makinia sana, wakati Gina akijichota kujiinua huku akipiga kelele, tayari alikwishachomoa bastola na kumlenga sawia, akaachia risasi mbili na zikamwishia Gina mgongoni. Gina akaenda chini pamoja na marais wale. Kingine kilichoshuhudiwa ni Aide de Camp wa Rais wa Gambia aliyesimama nyuma ya bosi wake akipigizwa mlangoni na damu nyingi zikimvuja shingoni, akaanguka akiwa hana uhai. Walinzi wa maraisa wakavamia eneo haraka na bundukia zikawa nje waziwazi, wanajeshi na polisi tayari wakazingira eneo na marais pamoja na wageni wakaondosha haraka katika eneo lile.

Madam S hakuwa mbali sana, alijishika kichwa alipomwona mlinzi yule akiinua bastola kumlenga Gina, hakuweza kufanya chochote lakini alitamani kuwahi au kumkataza, akachelewa.

Masikini binti yangu!!!! Akajisemea moyoni huku akijisika kichwani na mara baada ya viongozi wale kuondolewa, alishuhudia Gina akiwekwa kitandani huku akivuja damu mgongoni na kinywani, akiingizwa kwenye gari la wagonjwa pamoja na yule ADC wa Gambia.


Kamanda Amata alifika juu ya kabisa ya ghorofa, kwa mguu wake akaupiga mlango kwa nguvu nao ukafunguka na kujipigiza upande wa pili. Martin aliposikia kishindo hicho akageuka na kumwona jamaa huyo akimjia kasi, hakutaka kuipoteza nafasi. Akarudisha jicho kwenye lensi na kuweka shabaha, akapachika dole lake la shahada na kuvuta trigger, bunduki ile ikatema, na risasi ikahama kwa kasi kuelekea kule ilikoagizwa. Martin aliinuliwa na teke moja la nguvu lililotua ubavuni mwake, akabingirika na kusimama kabla hajakaa sawa, akajikuta akipata shambulizi la ghafla, akapepesuka na kushindwa kujielewa, kamanda Amata akaenda hewani na kumpa double kiki za kifua, zikamsumkuma na Martini akajigonga kwa nyuma kwenye ukingo wa ghorofa akayumba na kujirusha kwenda chini.

“Amejiuaaa!!!” Chiba akapiga kelele akiwa tayari kafika kwenye ule ukingo na bastola mkononi.

Martini alidaka waya wa umeme, akauachia na kudaka nyaya za simu, zikakatika, akashuka nazo mpaka kwenye jengo la pili, akaruka sarakasi maridadi kabisa na kujikuta chini. Dakika hiyo hiyo, gari lililokuwa likiendeshwa na Fredy likafunga breki kali na mlango wa ubavuni ukafunguka, Martini akajitoma ndani huku rsasi ya askari mmoja ikifumua kiatu chake. Fredy akapiga norinda na kuweka gari sawa, akabadili gia na kuondoka kwa kasi. Akafuata barabara ya kuelekea ikulu, na kisha kukamata ile ya Agha Khan kwa kasi ya ajabu, akanyoosha na kupitiliaza mpaka kwenye barabara ya Ocean na kupitiliza bila kukunja kutoka kwenye ukingo wa bahari gari lile likapaa hewani na kutua majini.

Askari waliokuwa wakilifukuza kwa pikipiki na gari ,ahiri za polisi, wakasihia hapo na kushuhudia gari lile likizama taratibu majini na kupoteleamo.

“Wamechagua kifo chao!” askari mmoja akasikika huku akipanda pikipiki lake tayari kwa safari ya kurudi.

Kamanda Amata na Chiba wakawasili eneo hilo na kukuta askari wale wakiwa wamezubaa kutazama majini.

“Vipi?” akauliza.

“Gari limetumbukia baharini na kuzama!”

“Wamechagua kifo chao!” mwingine akadakia.

Kamanda Amata akajua wazi kuwa upeo wao wa kufikiri umeishia hapo, akainua simu na kupiga kwa Inspekata Simbeye.

“Ee Kijana!” Inspekta akaitikia.

“Nahitaji boti na wazamiaji kama sita hivi wafike eneo lote la bahari ya Dar Es Salaam hususan Ocean Road mpaka Msasani na Kunduchi haraka nataka wajlitafute gari la jamaa wametumbukiza baharini,” akamwambia.

“Clear!” akajibu na kukata.

Amata na Chiba wakaingia garini na kurudi, hawakubakia eneo lile kwani tayari walikwishawapa kazi vijana.

“Dah! Washenzi wametuzidi kete!” Amata akasema huku akiendesha gari kwa kasi ya ajabu.

“Yule mwanamke atakuwa karudi Kunduchi, kwa sababu mizigo yake bado ipo pale…” Chiba akasema.

“Sasa ili kumuwahi, inabidi kutumia pikipiki,” Amata akamwambia wakati akisimamisha gari mbele ya ukumbi ule uliokuwa ukifanyika mkutano. Chiba akatelemka na moja kwa moja akaliendea pikipiki kubwa la polisi na kulipanda, baada ya mazungumzo mafupi na askari huyo, akaliwasha na kutokomea. Kamanda Amata akageuza gari na kurudi moja kwa moja mpaka Ofisi Ndogo ambako huko alikutana na Madam S akiwa kasawajika uso wote. Akaingia na kujitupa kitini mara moja, akiwa amechoka vibaya mno.

“Wapo salama?” akamuuliza Madam S.

“Yes, Gina amefanya kazi kubwa sana kuwasevu, alijitoa mhanga kiukweli,” Madam S akamsimulia Amata kilichojiri huku chini. Amata akabaki kustaajabu mambo yaliyofanywa na mwanamke huyo, “kwa hiyo mzima au amekufa?” akauliza kwa hamaniko kubwa.

“No ni mzima, bullet proof ilimsaidia sana, ila kama mlengaji angepiga kichwa hatungekuwa na Gina tena,” Madam S akamwambia, “Hata hivyo risasi ya muuaji imeondokana na maisha ya mtu…”

“Nani?”

“ADC wa Gambia…” akamjibu. Kamanda Amata akabaki kimya kwa sekunde kadhaa.

“Muuaji ametoroka, ni mwanaume wa Kizungu, bunduki yake ipo garini na risasi aliyotumia tuna ganda lake pia,” akamwambia.

“Lazima asakwe, popote duniani, na atiwe mkononi, endelea na Chiba mi ninaelekea Ikulu mara moja lakini tukutane hapa jioni nitawatumia taarifa” akamwambia na kuagana naye. Kamanda Amata akatoka na kuingia garini mwake akawasha na kuelekea Kunduchi ambako Chiba alikuwa ametangulia kwanza.

Huko Kunduchi Chiba aliwasili na kuweka pikipiki yake vizuri, hakusubiri kuuliza wa kusabahi mtu, mbio zake zikaishia katika mlango ule ule aliyoingia mwanzo, akanyonga kitasa bastola mkononi, akaingia, peupe, hakuna mtu. Akatazama kile chumba, hakuna mzigo hata mmoja. Akashusha bastola yake na kuiweka kiunoni mara akasikia vishindo vya watu nyuma yake alipotazama ni walinzi wa hoteli ile.

“Hamjamwona huyu mwanamke akitoka?” akauliza.

“Alitoka asubuhi sana hapa, na hajarudi,” mmoja akajibu huku mwingine akitazama huku na huko.

“Shit!” akachukua simu yake na kupiga namba fulani akaiweka sikioni.

“Hayupo, na kila kitu chake hakipo,” akamwambia Kamanda Amata.

“Ok rudi tukutane Hospitali ya Lugalo, Gina yuko pale” akamwambia.

“Yupo hospitali? Mzima au?” Chiba akauliza.

“Mzima kabisa,” Amata akamjibu lakini ilionekana wazi kuwa hakuridhika au kuamini jibu hilo.


Ndani ya Hospitali ya Lugalo jeshini, Gina alihifadhiwa ndani ya chumba cha peke yake, macho yake alikuwa ameyafumba na kubaki kimya kabisa. Kilichomgutusha ni mlango uliofunguliwa taratibu na watu wawili wakaingia ndani yake. Akafumbua macho yake taratibu na kutazama, aliwajua, Amata na Chiba.

Chiba alikuwa wa kwanza kukifikia kitanda cha mwanamke huyo na kumwacha Amata nyuma.

“Uko sawa?” akamwuliza.

“Ndiyo niko sawa, hakika ililikuwa ni pumzi yangu ya mwisho, nisingeweza kuwaona tena ndugu zangu na wapenzi wangu kama nyie,” Gina akasema huku akimkumbatia kwa nguvu Chiba na kisha Amata.

“Hauna majeraha yoyote? Au maumivu?” Amata akauliza.

“Ni hapa tu kwenye kiungo cha paja na kiuno kwa sababu nilianguka vibaya, ile risasi ilipoteza taiming yangu… vipi mmepata mshenzi yule?” akawauliza.

“Ah wapi! Wametoroka, wale jamaa wanaiujua kazi yao vyema sana, hawabahatishi,” Amata akajibu.

“Dah! Tunafanyaje?”

“Aluta continua, yaani mapambano yanaendelea. Kama hakuna la ziada wakuruhusu…” Amata akamwambia Gina huku akiketi juu ya kitanda kile.

“Wangeniruhusu mapema tu, ila niliwaomba wasubiri kidogo,” Gina akajibu huku akitoka kitandani na kuketi juu yake.

“Umekuwa shujaa Gina,”

“Ilibidi, kama ningechelewa kidogo tu basi rais wa gambia angekuwa hana uhai, nilijua wazi kuwa risasi ile ingenipata mimi na kutoniletea madhara, lakini yule mlinzi wa rais aliponifyatulia risasi ndipo akanipotezea malengo na badala yake ile risasi ikamwaribu vibaya ADC, amekufa, hana uhai,” Gina akajibu huku akiangusha machozi.

“Usilie Gina, hii ndiyo kazi yetu, uhai wetu u mkononi na tunauweka rehani siku zote, kumbuka kiapo chetu daima, for my people, for my nation,” Amata akamwambia.


Katika kilindi cha bahari, Martin, Fredy na Amanda walikuwa wakiendelea na safari yao. Chombo ambacho walikuwa wakikitumia ardhini kama gari la kisasa aina ya Lexus mara hii kilikuwa nyambizi ndogo ya kisasa aina ya Violina. Kama ni teknolojia, basi hapa ilitendewa haki kwani chombo kimoja kiliweza kubadilika mara tatu.

Mara baada ya kulitumbukiza gari hilo majini pale Ocean Road hakikuchukua hata dakika moja kumezwa na maji na kutoonekana tena. Kikiwa chini ya maji kiligeuka na kuwa nyambizi ndogo yenye kasi ya ajabu. Fredy alikiongoza na kwenda kukiweka katika pwani ya Kunduchi kama Boti ya kawaida mara baada ya kukiibua majini. Hawakukaa sana Amanda ambaye alitoroka katika ukumbi wa mikutano aliungana nao na safari ya kutoroka nchi ikaanza rasmi. Chombo kile kikazama tena majini na kusafiri chini kwa chini huku kikiongozwa kwa satelaiti ambayo iliwajulisha mahali walipo na upande gani wanaelekea.

“Asante sana Fredy,” Martin akashukuru.

“Asante ya nini?

“Ya nini? Fredy, kiukweli nilijua leo niko matatani, sijamwelewa yule jamaa…”

“Jamaa gani?” Amanda akadakiza swali.

“Kule ghorofani, nimepambana na mtu mmoja mwepesi sana wa mapigano, sikumjibu chochote kwa sababu nilijua wazi kuwa nikionesha umahiri wangu, nitapoteza muda na kuongeza nafasi ya kukamatwa, nikakubalia anipige name nilipopata upenyo ni kajirusha chini, si kwamba nilimkimbia bali wakati mwingine hata kukimbia ni silaha,” Akaeleza, “Nilikuwa nawaza nikifika chini nitawatoroka vipi askari na watu waliopo huko, bahati nzuri na wewe unafika, hakika ni pona yangu…” Kamalizia.

“Sasa tumefanikiwa kuua au?” Amanda akauliza.

“Sidhani, nilichokishuhudia ni mtu aliyeruka kuwaokoa wale marais, nafikiri kama ni kuua atakuwa amekufa mtu mwingine ila si mlengwa…” akamjibu.

“Safari hii tumekutana na wajuvi,” Fredy akawaambia, “sehemu zote tulizopita hatukuwa kujulikana wala nini lakini hapa nashangaa, yaani wana intelijensia ya hali ya juu, na hata bomu tulilotega kule nyumbani sidhani kama litafanya tuliyokusudia,” akamaliza kusema na kuhamishia macho yake katika luninga iliyokuwa mbele yake ikimwonesha ni wapi wanapita. Chombo hiki kilikuwa kikisafiri kilomita moja tu kutoka nchi kavu hivyo kamera yake ndogo ambayo huwa juu inaweza kupata picha nzuri na vizuri ya wapi wanapita.

“Tunakaribia kufika mpaka wa Tanzania na Kenya,” Fredy akawaambia.

“Oh asante Mungu, siitaki kabisa hii nchi…” Martin akawaambia, “tukivuka mpaka nambie,” akamwambia Fredy.

“Ili iweje?” Amanda akauliza.

“Ili ninywe pombe,” akajibu na kujilaza kitini.

“Mmmmm hapo sawa, jamani mkumbuke tunapiga nanga Mombasa, tajiri anatusubiri katika Hoteli ya Likoni High Class,” Amanda akawaambia wenzake nao wakaitikia.


HOTELI YA LIKONI HIGH CLASS

NDANI YA HOTELI hii, katika apatimenti inayojitegemea na yenye kila kitu cha thamani, watu watatu walikuwa wameketi kimya wakitazama matangazo ya luninga kutoka vituo vya Tanzania. Habari iliyokuwa ikitawala ni juu ya tukio la mchana wa siku hiyo la kukoswakoswa kuuawawa kwa marais wa Gambia na Tanzania kwa kuwa haikujulikana rasmi ni yupi aliyekusudiwa.

Sasa ilikuwa ni hotuba ya Rais wa Tanzania akihutubia taifa mubashara kupitia kituo hicho kutoka Ikulu ya Dodoma ambako yeye na mgeni wake walipelekwa kwa siri siku hiyo hiyo.

“…ni tukio ambalo hatukulitegemea, ni magaidi waliojaribu ama kuniua mimi au mwenzngu Rais wa Gambia na mwenyekiti wa Umoja wa nchi za Afrika.

Kwa maneno haya, nawahakikishia Watanzania na Wagambia na Waafrika wote kwa ujumla kuwa, Mwenyekiti wetu wa Umoja wa Afrika yupo salama, na mimi kama mnavyoniona, isipokuwa tumepoteza watu wawili; msaidizi wa Rais wa Gambia na mwanausalama kutoka Tanzania, Mwenyezi Mungu awalaze pema peponi.

Kwa kumalizia napenda kuwaambia wale waliojaribu kutekeleza ugaidi huu, kuwa sasa nawatangazia vita, popote walipo duniani, nitawakamta na tutawashughulikia ipasavyo. Kama wanasikia hotuba hii basi wasubiri kiama chao au wajiue kabla hatujawafikia, asanteni. Mungu ibariki Afrika Mungu ibariki Tanzania.”

Jaffer Bakhari, akavua miwani yake na kuzima luninga hiyo, akawatazama wasaidizi wake kwa zamu kisha akarudisha macho yake mbele.

“We have missed him!” (tumemkosa) akawaambia.

“I cannot believe, I know Martin Gupter, never miss the range…” (siwezi kuamini, namjua Martin Gupter hawezi kukosa shabaha) akajibu mmoja wao.

“Hawa watu wanacheza sana na sisi, kwa nini wanang’ng’ania ile ardhi? Hawataki kutuachia?” Jaffer akalalama, huku wafuasi wake wakiwa kimya kabisa, “Ok, kesho tutaondoka kwenda Dubai, pale tutakutana Embriyo nzima tutajua nini tunafanya,” akawaambia.

“Na hawa je? Martin na wenzake,” kijana mmoja akauliza.

“Kazi yao itaendelea, ila nitawaficha kwa muda na maelekezo yote nimeshawapa ya wapi wanatakiwa kwenda kujificha. Mambo yakitulia tutaanza tulipoishia… ninyi si mmesikia huyu Rais wa Tanzania anachosema, haya maneno si ya kupuuzia hata kidogo, hah hah hah nevey atafurukuta tu na kina Gupter lakini kamwe hawezi kuigusa Embriyo… san asana nayeye namweka kwenye hesabu, anatakiwa auawe!” Jaffer akawaambia navijana hao wakamkazia macho kumtazama kana kwamba ni mara ya kwanza kumwona. Tajiri huyu akampa ishara mmoja wa vijana hao naye akamkabidhi bahasha kubwa, akaiweka mezani. Dakika hiyo hiyo wanadada warembo wa Kiarabu wakaingia katika sebule hiyo na kutoa huduma za vinywaji na vitafunwa kwa watatu hao.

Simu ya Jaffer ikapiga kengele mara tatu, akaiinua na kutazama kwenye kioo, “wamekaribia, dakika kumi zijazo watakuwa hapa,” akawaambia akimaanisha Martin na wenzake.

VIII

Jioni hii, Kamanda Amata, Chiba, Gina na Madam S walikutana Ofisi ndogo kwa majadiiano mafupi juu ya siku nzima ilivyokwenda.

“Mmefanya kazi kubwa sana nyie vijana!” Madam akawaambia viajana wake, “lakini kazi ndiyo kwanzaaaaa inaanza, mheshimiwa Rais amesema anawataka hao watu ama wawe marehemu au wazima,” akawaambia.

“Kasema hivyo?” Chiba akauliza.

“Ndiyo! Tena kasisitiza sana kabla ya kuondoka kuelekea Dodoma,” akawajibu.

“Sawa! Ni wajibu wetu daima kuweka rehani maisha yetu, kama atakavyo atawapata ama wafu au wazima,” Amata akajibu. Muda wote huo, Gina alikuwa kimya kabisa, hakutaka kuongea wala kujibu swali. Saa kama mbili hivi zilifuata za mkutano mzito wa kupanga kazi.

“Kutokana na hili, mkutano wa dharula umeamua kuunda kikosi cha wapelelezi kwa ajili ya kuwaska wauaji au magaidi hawa,” Madam akawaeleza, “Lakini hata hivyo ofisi ya muda ya usalama ya AU itakuwa hapa Dar es salaam na wamesema wanataka idara ya usalama ya Tanzania ilifanyie kazi hili,” akawaambia.

“Sisi?” Chiba akauliza.

“Ndiyo, sisi, ukiona hivyo, wametuamini… wameona kazi yetu leo tu, wamekubali…” Madam S akawaambia na kutabasamu.

“Tunaanzia wapi kuwatafuta hawa watu?” Gina akasema kwa mara ya kwanza.

“Wewe wajua,”

“Wala usijali, tutapata tu pakuanzia, kama tumegundua target yao tutashindwaje kujua pa kuwapata?” Chiba akauliza.

“Mnajua, Mwenyekiti wa AU ambaye ndiye Rais wa Gambia ameridhia sisi kuingia kazini kwa siri, na tayari ametenga fungu la kutosha hata kabla hiyo ofisi haijaanzishwa rasmi… Amata you are the leader! Tunasubiri tu idhini ya wengine hasa Baraza la Usalama, ” akasema na kumtazama kijana huyu mtanashati mwenye sura ya upole iliyoficha ujasiri wa hali ya juu.

“Tena nimefurahi kwa hili, nina uchungu sana, naomba tu walibariki, watu wachache hawawezi kutuletea uumbavu wao nyumbani kwetu,” Amata akazungumza.

“Ok, zaidi ya hayo, tukapumzike, nitakuiteni kama kuna taarifa nyingine ila kwa sasa endeleeni na shughuli zenu za kawaida za kujenga Taifa,” Madam S akamaliza kuwaambia na kuagana nao.


Siku iliyofuata, Martin na wenzake waliabiri katika ndege ya shirika la Kenya na kuiacha ardhi ya Afrika Mashariki kuelekea mafichoni.

“Wakitupata wakatambike!” Fredy akamwambia Martin aliyekuwa kimya muda wote.

“Ni kweli,” akafungua kinywa chake kusema, “ lakini Tanzania wameitia doa kazi yangu kwa mara ya kwanza, mpaka sasa bado nawaza wamewezaje kugundua nyayo na mbinu zetu,” akaongeza kusema, “bunduki yangu nimeiacha nah ii inaweza ikaleta shida kwenye mipango mingine,” akamaliza na kuinua bia yake aina ya Heineken iliyokuwa katika kijimeza kidogo na kuimiminia tumboni mwake yote kama ilivyo.

“Afrika haina utundu wala teknolojia ya kugundua sisi ni nani na wapi tulipo, mi naona wazi kuwa hakuna kazi rahisi tuliyowahi kuipata kama hii ya safari hii,” Amanda akaongeza.

“Hapana, kazi nyepesi haiwezi kuingia doa kama hii, hii kwangu ndiyo kazi ngumu sana, na inaendelea kuniumiza kichwa,” akaeleza.

“Tulia The hunter!” Amanda akamwambia.

Muda mfupi baadae wakatangaziwa kuwa wanatua katika Uwanja wa Ndege wa Lungi jijini Free Town, Sierra Leone. Mara baada ya kutoka na kuuacha uwanja huo walichukua gari na moja kwa moja wakaelekea katika mji mdogo wa Waterloo ambako kulikuwa na nyumba moja ya mashambani waliyoitumia kujificha mara wamalizapo matukio yao.

SIKU TATU BAADAE

KAMANDA AMATA alisimama mbele ya bosi wake, wima kabisa, kwa ukakamavu wa kiaskari. Pembeni yake yaani upande huu na mwingine kulikuwa na Gina na Chiba, kati yao na Madam S kulikuwa na meza kubwa yenye vitendea kazi vya kiofisi.

“Nimewaita rasmi, hii hapa mbele yangu ni barua kutoka ofisi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Nchi za Afrika kitengo cha usalama. Kimeiomba Tanzania ifanye kazi ya kuwasaka watu hawa waliojaribu kufanya mauaji ya marais, wakamatwe popote walipo duniani.

Niliitwa Ikulu, nikapewa barua hii, ikiwa na maana kuwa kazi hii imeletwa rasmi katika kitengo nyeti cha huduma hatari na za siri TSA, ifanyie kazi. Name nimesimama hapa kuwatuma kazi hiyo. TSA 1 !” akaita.

“HOT”

“Nakupa jukumu sasa, kiofisi ufike popote inapohisiwa watu hawa wapo, kimwili na kiroho kwa njia yoyote ile wakamatwe, ikibidi lolote lifanyike, clear?” Madam akamwambia.

“For my people, For my Nation … nipo tayari!” akajibu.

Madam S akainua kabrasha lililokuwa mezani kwake na kumkabidhi mikononi, naye akapokea kwa mikono miwili. Kabrasha lile lilikuwa limefungwa kwa karatasi laini inayoweza kuonesha mpaka upande wa pili. Kilichofungwa ndani ni faili moja lenye karatasi kama hamsini hivi na juu yake kulikuwa na maandishi makubwa yaliyosomeka, ‘MAGNUM 22’.

“Najua unajua nini unapaswa kutenda,” Madam S akamwambia na kuketi tena kitini, kasha vijana wake nao wakaketi katika viti vyao, “kama mnavyojua hii ni kazi nyingine nzito, kumsaka muuaji ni sawa na kuwinda, maana hata yeye anajua kuwa anasakwa na anajua ni nini afanye ili asikamatwe, lazima ujue hesabu za magazijuto, lakini ninaamini kuwa mtaweza. TSA 2 utabaki hapa utamsaidia kaka yako kwa kila anachohitaji kiteknolojia, hakikisha umpotezi kwenye rada yako. TSA 5 utakuwa tayari kwa usaidizi wowote utakaohitajika,” akamalizia kwa kuwaambia.

Baada ya hapo Kamanda Amata na Chiba wakainuka tayari kuondoka, wakaagana na Madam S na kutoka nje y ofisi hio huku lile kabrasha likiwa katika mfuko wa karatasi. Safari yao iliishia Gezaulole, Shamba, huku ndiko mambo yote hupikwa.


Katika meza yenye umbo la yai, vijana hawa wawili waliketi kwa kutazamana, Amata akaweka kabrasha lile mezani na kulichana ili kujua nini kipo ndani yake. Ni karatasi kadhaa zenye maelezo mengi yanayohusiana na kile kinachodhaniwa kuwa ni kisa cha watu hao kutaka kumdhuru Rais, zaidi ya hapo kulikuwa na taarifa fupi ya mauaji ya Angola na Ivory Coast. Kwa ujumla ndani ya bahasha hiyo kulikuwa na kazi mbili kubwa, moja ni kufanya uchunguzi kama mauaji ya Angola, Ivory Coast na shambulio la Dar e salaam vina mahusiano na muuaji ni mmoja? La pili ni kuwa kama ndiyo, basi askew na atiwe mbaroni kwa gharama yoyote ile na kama siyo basi huyu aliyehusika na shambulio la Dar es salaam atafutwe. Sambamba na hayo yote palikuwa na picha za maeneo ambako matukio hayo yalifanyika katika nchi zote tatu na tafutishi chache ambazo zilipatikana tayari ziliwekwa vielelezo vyake.

Kamanda Amata akashusha pumzi na kujiegemeza kitini.

“Vipi?” Chiba akamuuliza huku akilivuta lile kabrasha na kuanza kulipekua. Kamanda hakujibu swali lake bali alibaki kimya akitafakari hili na lile.

“Nafikiri nianzie wapi, Angola, Ivory Coast au wapi!” akajisemea.

“Hapa, anzia hapa na kutoka hapa utakwenda huko kote,” Chiba akamwambia, naye akatikisa kichwa juu chini.

“Kuna mengi unayotakiwa kuanza nayo hapa nyumbani,” akamwekea picha moja mezani, iliyomwonesha kijana mmoja mrefu mwenye shingo nyembaba na nywele kama za Kisomali hivi.

“Huyu ni nani?” Amata akauliza.

“Huyu ni mhudumu wa mapokezi katika hoteli ya Kunduchi, alinipokea kwa furaha sana na kwake nimepata jambo moja tu…”

“Lipi?”

“Alinambia kuwa mwanamke huyu ana wanaume wengi… sasa inabidi kujua wanaume hao labda tutapata picha Fulani ya kuwasaka…” Chiba akasema.

“Good! Huyu lazima nimuone leo hii, najua kutoka hapa nitaweza kujua nini kinafuata…”

“Sawa! Hilo la kwanza, hapa kuna mpango wa siri ambao uliniwezesha kukujuza kuwa tageti ya jamaa ipo wapi, na mara moja katika faii hili nililolifuma chumbani mwa yule mwanamke limeeleza kila kitu ,mpango mzima,”

“Unasema?!” Amata akahamaki.

Chiba hakujibu, akachukua simu yake na kumpa Kamanda Amata, naye akaipokea na kuanza kuperuzi faili lile, kila alipozidi kwenda zaidi alijikuta akipigwa na bumbuwazi.

Kumbe mpango upo hivi! Akawaza huku akiendelea kuchambua na vya chini, “kwa hiyo ina maana sasa watakuwa safarini kuelekea Sierra?” akauliza.

“Kama wamefanikiwa kutoka nchini, basi watakuwa tayari wamefika nchini humo, lakini mpaka sasa sijapata habari yoyote iwe kutoka Uwanja wa ndege au bandarini au Ubungo, hamna kitu, ina maana wapo ndani ya nchi hii,” Chiba akasema.

“Hapana Chiba, hawa jamaa nakuhakikishia wameshatoka nchini, unakumbuka lile gari lao walivyolitumbukiza baharini? Na polisi wanamaji wamesemaje, ‘hatujaona gari wala nini’ nahisi sasa lile gari lina uwezo wa kutembea majini tena chini kwa chini…”

“Aaaaa Amata kaka, kwani hapa tupo kwenye muvi za James Bond?” Chiba akatania.

“Habari ndo hiyo, watu kama hawa kutokana na wanachokifanya lazima wajipange sana katika kutoroka, tungelipata gari sawa, halipo baharini, liko wapi? Washasepa. Haya umeenda Kunduchi kwa yule mwanamke umepata nini, ameondoka saa ngapi na kwa vipi, kuna uwezekano kabisa kuwa lile gari limesafiri kutoka hapa na kumchukua yule mwanamke kisha wakatokomea kwa njia hiyohiyo na kuvuka mpaka…. Na ukiangali kama wametoroka kwa njia hiyo, basi watakuwa Kenya,” Amata

Amata akazungumza kwa makini sana.

“Umenena Amata, wanaweza kuwa Kenya tena Mombasa…”

“Yeah! Chiba nakuamini sana, ihifadhi hii info, mi naenda kwanza Kunduchi nikaanzie kazi huko,” Amata akamwambia swahiba wake huku akiinuka tayari kwa safari.

KUNDUCHI RESORT

Kamanda Ama akawasili katika hoteli hiyo na kuegesha gari mahala pake. Hatua zake ndefu ndefu zikamfikisha katika kaunta ya hoteli hiyo nzuri nay a kisasa. Mapokezi hapo akakaribishwa na wahudumu wa wili wa kike wenye tabasamu la bashasha. Akawasabahi na moja kwa moja akamuulizia kijana yule anayemtaka. Haikuchukua muda kuitiwa kwani alikuwa upande mwingine wa hoteli hiyo. Kijana huyu mwembaba, mrefu mwenye tabasamu na maneno ya kuvutia na utani uso kifani alikutana uso kwa uso na Amata.

“Naitwa Justus!” amata akajitambulisha, “tunaweza kuongea kidogo?” akamuuliza.

“Bila shaka kaka yangu, kwanza kabisa mi naitwa Umar,” akajitambulisha kwa jina moja tu. Kisha wakavuta hatua hadi karibu na bwawa kubwa la kuogelea.

“Mr Umar, mimi ni mgeni hapa kwenu, na shida yangu kubwa ni kuwa namtafuta mtu huyu, je umewahi kumuona hapa?” akamwonesha picha ya Amanda.

“Aaaaaaahhhhhh!!!! Huyu?” Umar kama kawaida yake akachanusha tabasamu pana usoni pake.

“Huyu mwanamke kanishinda, na wewe upo kwenye listi?” Umar akauliza. Kamanda Amata akabaki na kigugumizi kwa sekunde kadhaa akijiuliza kichwani mwake.

“Listi ya nini?”

“Aaaaaa yule mzungu ni mtalii wa ngono, mpaka vigogo hapa wamekuja sana kumgonga,” akaeleza.

“Vigogo?”

“Ee yule nani yule alikuwa balozi huko Emirate huko…”

“Aaaa Balozi Bailhani?”

“Yes!”

“ Achana na hayo, mi nataka nijue huyu mwanamke yuko wapi?” akamuuliza.

“Alikaa hapa kama siku tatu hivi…”

“ Sikia Umar, yule mwanamke kaingia nchini bila kibali, tunamtafuta…”

“Ah mzee we kumbe ni imigresheni?”

Mazungumzo kati ya wawili hawa yakachukua kama nusu saa hivi, Umar akaeleza mengi anayoyajua juu ya mwanamke huyo, nyendo zake na watu kadhaa aliokuwa nao karibu. Kwa namna moja kwa Amata mazungumzo haya yalimpa faida lakini pia yakamwachia maswali; je ni kweli alikuwa akifanya mapenzi na watu hao aliyotajiwa au kulikuwa na jambo lingine, hakupata jibu mara moja kwa kuwa huko chumbani waikuwa wao wawili tu yaani mwanamke huyo na mgeni wake.

Hata Balozi Bailhan? Akajiuliza.

“Kwa hiyo amecheck out lini?”

“Mh huyu katoroka, hajatuaga wala nini yaani hata sisi hapa hatuelewi kaondoka ondoka vipi,” Umar akaeleza.

“Asante kwa maelezo yako, umenisaidia sana, nitakutafuta wakati mwingine hata tupate kinywaji kidogo,” akamtania.

“Usijali kaka, hata wewe unakaribishwa hapa kupumzika na shemella wetu,” naye akamtania, wakaagana wakipeana mikono kisha Amata akampa kadi kazi yake.

“Kwa lolote, waweza kunipigia,” akamwambia.

“Asante,” akashukuru kisha kila mmoja akachukua njia yake.

Ndani ya gari lake kamanda Amata akachukua kijitabu chake kidogo na kuandika jina Bailhani akapiga mstari na kuunganisha na jina bandia la mwanamke yule ambaye mpaka dakika hiyo hawakupata jina halisi. Kisha akaondosha gari lake na kurudi mjini.


Amata alikutana na Chiba na Gina mchana huo kwa chakula cha mchana katika hoteli ya Double Tree. Pamoja na chakula hicho mazungumzo ya hapa na pale yalikuwa yakiendelea mahala hapo.

“Hujanipa mchapo wa Kunduchi,” Chiba akamwambia Amata.

“Huko poa tu, yule kijana kanipa umbeya wa kutosha, lakini katika mazungumzo yetu na yeye nimeweka akilini jina moja tu na nataka nilifanyie kazi…”

“Jina gani asee?” Chiba akauliza.

“Balozi Bailhani. Inasemekana alikuwa akimwona mara kadhaa akija pale na mwenyeji wake ni huyu mwanamke, jamaa anasema kuwa balozi huyo alikuwa anakula mzigo,” Amata akasema.

“Mmmm labda, lakini swali ni kwamba walikutana vipi au walifahamiana wapi?” Chiba akamalizia.

“Siyo la kuliacha hilo ee, Gina mama, kazi yako hiyo!” Amata akasema.

“Eeeee muda wa kula bwana, ngoja nimalize ndo unipe kazi,” Gina akalalama.

“Haya Malkia!” Amata akajibu na chakula kikaendelea kuliwa huku mazungumzo mengine yakiendelea.

“Nahitaji kwenda Angola,” akawaambia.

“Kumekucha….” Gina akadakia.

“Na makucha yake…” Chiba naye akamalizia.

“Ee lazima tujue ulinganifu wa mambo haya ili nijue kama naingia kazini kumsaka mshenzi huyu basi nimsake kwa nguvu zote,” akawaambia.

“Sure!” Chiba akaunga mkono.

“Kuna vitu nahitaji kuvijua kutoka Angola, nikivipata hivyo nikioanisha na Ivory Coast kazi imeisha… hayawani hawa…. Umesema wapo watatu ee…”

“Ee ni watatu,”

“Lazima wapatikane iwe kwa jasho au machozi…” Amata akawaambia wakti akimalizia chakula chake.

“Safari lini?” Gina akauliza.

“Ikiwezekana kesho niwe Luanda na Mungu akipenda kesho hiyo hiyo nigeuke kurudi Dar…” akawaambia.

“Amata, ukiingia Luanda nakuhakikishia hutopenda kurudi Dar badala yake utaendelea kwenda Ivory Coast,” Chiba akamwambia.

“Ikibidi, itakuwa hivyo,”

“Basi kabla hujaondoka twende shamba nikakufanyie identification, sina imani sana na kazi ya safari hii maana tunamuwinda muwindaji,” Chiba akamwambia. Wote wakatoka na kuingia garini, safari ikaanza kuelekea Shamba huku wakimuacha Gina akifanya utaratibu wa usafiri wa Kamanda wa usiku huo.

SHAMBA

Wakiwa katika Safe House au Shamba kama inavyojulikana, Kamanda Amata na Chiba walikuwa katika chumba maalum chenya mitambo anuai.

“Natakiwa kukuwekea identification Chip, ili kila utakapokwenda nikuone na iwe rahisi kukufuatilia…” Chiba akamwambia Amata.

“Aaaa ila haka kadude kanauma asee,”

“Ni kweli lakini hatuna jinsi, safari hii nitakuweka pajani,” China akamwambia Amata huku akifungua mkoba maaumu wenye mashine ya kubeba kifaa hicho. Ni kitu kama bunduki au sijui tuite bastola, kazi yake kubwa ni kuweka mwilini mwa mwanadamu micro chip inayowasiliwana kwa satelite na kuonesha ni wapi mtu huyo alipo kwa wakati huo. Kamanda Amata akatulia na Chiba akafanya hivyo kama ambavyo anafanya siku zote.

“Assssss ah! Shit!” Amata akapiga kite cha maumivu wakati chip hiyo ikisukumwa ndani kwa nguvu na mashine ile.

“Weka mkono wako hapa,” Chiba akamwambia. Naye akaweka mkono katika kitu kama bangili kubwa kilichounganishwa na mashine hiyo, kisha Chiba akatazama kwenye kompyuta yake na kujaribu kuviunganisha vitu hivyo viwili.

“Aaaaaa hapo sawa, sasa nakuona mubashara, upo Gezaulole, Kigamboni,” Chiba akasema na kuanza kufunga mkoba wake. Si kwamba alikuwa anamwona kama alivyo, bali alimwona kwa alama ya dot nyekundu inayowakawaka katika ramani na kuonesha ulipo.

LUANDA – ANGOLA

KATIKA UWANJA wa ndege wa kimataifa wa Quatro de Fevereiro, Kusini kabisa mwa Mji Mkuu wa Angola, Luanda, Kamanda Amata aliwasili na ndege ya shirika la Kenya ‘Kenya Airways’. Akainua uso wake na kutazama anga la nchi hiyo, moyo wake ukamkaribisha katika jiji hilo, la kupendeza kwa macho na fahari zake.

“Boa noite senhor!” (habari za jioni mheshimiwa) akasikia salamu kutoka nyuma yake, Amata akageuka na kugongana macho na mtu mmoja, mwembaba wa wastani, ana nywele nyingi zilizochanganika na mvi, ndevu za wastani zilikipendezesha kidevu chake.

“Boa noite, como você está?” (nzuri hujambo?) akamjibu salamu yake, kisha wakapeana mikono kama kawaida ya Waafrika kunesha kwamaba sisi ni kitu kimoja.

“Bem-vindo em Luanda, você precisa de um imposto?” (Karibu Luanda, unahitaji huduma ya taksi?) yule mzee akamkaribisha Amata na kumtupia swali. Kwa haraka haraka Kamanda Amata akamsoma machoni na kumwelewa mara moja mzee huyo, hakuwa na mawaa yoyote.

“Sim! Preciso de um imposto, você pode me levar para o hotel Alvalade?” (Ndiyo, ninahitaji taksi, unaweza kunipeleka Hoteli ya Alvalade?) akakubali na kumuuliza huku tayari wakianza kunyayua mguu kwa hatua ya kwanza kuelekea kwneye maegesho ya uwanja huo.

“Claro que eu posso!” (Bila shaka ninaweza!) yule mzee akajibu na wote wakaendelea kutembea bila kuongea chochote mpaka katika gari hilo. Lilikuwa gari la kawaida sana, si zuri la kutisha bali tunaweza kuliita la kawaida.

“Dakika ngapi tutakuwa pale?” akamuuliza kwa Kireno cha kubabaisha.

“Kama kumi au chini ya hapo kama hakutakuwa na msongamano barabarani…”

“Na hapa ni kama kwetu Dar es salaam?” Amata akamuuliza.

“Oh unatokea Dar es salaam, Tanzania? Ninapenda sana nchi hiyo na ninapenda kufika kabla sijafa…” yule mzee akaongea kwa furaha sana baada ya kujua kuwa mwenyeji wake anaipenda nchi yake. Gari lile likawashwa kwa shida kidogo likagoma kuwaka.

“Ossshhhh!!! Matatizo yameanza!” akalalama.

“Vipi, bovu?” Amata akauliza.

“Aaaaa vijana hapa wanatumia sana uchawi, hawataki mimi nipate pesa,” akaendelea kulalamika.

“Usiamini uchawi, gari lako ni bovu, mi nasukuma we uliwashe!” Amata akamwambia na kutelemka chini, akaenda nyuma ya gari hilo na kulisukuma peke yake, sekunde chache likawaka, akarudi na kuketi kwenye kiti cha abiria.

“Tunaweza kwenda!” akamwambia na yule mzee akatia gia ya kwanza na kuondoka zake kupitia Barabara ya Revolução de Outubro na kunyoosha moja kwa moja mpaka kwenye mzunguko na kuchukua ile Barabara ya Cmte Gika. Dakika chahe tu kweli waliingia katika hoteli hiyo kubwa ya nyote tano. Kamanda Amata akachomo noti mbili za Kwanza 5000 kila moja. Mzee yule badala ya kuzipokea akabaki akitetema mikono.

“No, ninyingi sana hizi kwa sfari ya kilomiti tatu,” akasema.

“Najua, ninakupa kwa sababu nataka umpelekee chakula kizuri mama yangu leo, usijali kwani kesho nitakuhitaji asubuhi hapa,” Amata akamwambia ma mzee yule akampatia mgeni wake kadi kazi yake kwa minajiri ya mawasiliano.

Kamanda Amata akavuta kijibegi chake na kuingia ndani ya hoteli hiyo ya kisasa inayoonesha kuwa na starehe zote za msingi ambazo mwanadamu angehitaji.

“Karibu Alvalade Hotel, karibu Luanda!” mwanadada mrembo aliyekuwa ndani ya suti nadhifu kabisa alimkaribisha kijana huyu mtanashati, mwenye siha ya kiume na mwili uliojengeka kimazoezi kwa wastani. Kwa kumtupia jicho alihisi kama amekutana na kijana wa ndoto zake, akajikuta akikosa neno na kubaki kumwemwesa midomo yake.

“Signorita!” Amata akaita huku mezani akiwa tayari ameweka karatasi inayoonesha booking yake na kadipesa yake aina ya MasterCard.

“Oooh! Ulikwsihaweka booking,” akasema mwanadada yule huku akichukua ile karatasi na kugeukia upande wa kompyuta yake. Dakika kama mbili baadae tayari akawa na kadifungushi kwa ajili kufungua mlango wa chumba chake.

“Twende nikuoneshe chumba chako!” yule mwanadada akamwambia Amata na kutoka upande wa pili, kisha wakafuatana na kuingia kwenye lifti na kupanda mpaka ghorofa ya saba, wakatoka kwenye lifti na kuingia chumba namba 11A.

“Hiki ni chumba chako Mr Spark!” akamwambia Amata.

“Aaaanh hutaki kunionesha zaidi?”

“Kukuonesha nini?” yule mwanadada akajibu huku akiondoka zake na kumwachia Amata mtikisiko wa nyama za nyuma. Kama kuumbwa aliumbwa, mfupi, mwenye unene wa wastani, aliyebinuka kiunoni kuja chini, na fundi aliyeishona nguo aliyoivaa unaweza kusema kuwa kazaliwa nayo. Kabla hajaingia katika lifti akageuka nyuma na kutazama alipotoka, akagongana macho na Amata ambaye bado alikuwa kasimama nje ya mlango huo akimsindikiza kwa macho. Kamanda Amata akachukua mfukoni kadi kazi na kuiangusha sakafuni, kisha akapachika kadifungushi yake katika ushoroba mdogo wa kitasa cha mlango huo, kisha akabonyeza namba fulani na kufungua. Akaingia ndani kuufunga mlango nyuma yake, mara baada ya kuhakikisha usalama wa chumba hicho akavua nguo zake na kutwaa vazi la kuvalia na kujibwaga kitandani, haikuchukua muda akapitiwa na usingizi. Ni mara chache sana kwa Kamanda Amata kuingia hotelini na kupatwa na usingizi haraka kwa kuwa daima alikuwa akija kwa shari hivyo ama ulala kitini kwa tahadhari au kwa mang’amung’amu kwa kuwa hujiweka tayari kwa lolote. Lakini safari hii kwake iikuwa kama picnic tu ambayo hata mwili wake ulijikuta unataka kupumzika zaidi.


Asubuhi ya siku iliyofuata ilimkuta Amata katika gym ndani hoteli hiyo. Alikuwa akifanya mazoezi makali mpaka wengine walikuwa wakimshangaa lakini yeye hakujali bali aliendelea na mazoezi yake na kuhakikisha mwili umetona jasho la kutosha. Akaschukua taulo lake na kujifutafuta taratibu huku akimshukuru kiongozi wa darasa hilo la mazoezi.

Ndani ya chumba chake, aliingia maliwato na kujimwagia maji kisha akarudi kuvaa nguo zake maalumu za kazi, yaani suti safi aliyoinunua mara tu alipofika uwanja wa ndege wa Luanda. Akajitazama kwenye kioo na kugeuka huku na huko, waaaaaoh, amependeza mno. Akauvuta mkoba wake na kufungua vijifuko vya siri, akatoa baadhi ya silaha zake anazozijua yeye na kuzipachika katika mwilia wake, bastola yake aina ya PPK na kuipachika mahala pake. Akahakikisha yupo tayari kuondoka, akiwa anamalizia kuiweka sawa tai yake akasikia mlango ukigongwa kisha ukasukumwa na mtu ambaye hakumtegemea akaingia ndani akiwa na toroli yenye kifungua kinywa juu yake. Alipogeuka kumtazama akamtambua mwanadada yule yule aliyempokea jana na kumwongoza chumbani.

“Wewe ni Waitress au receptionist?” akamtupia swali lakini macho yake yote yalikuwa yakiangali kifua kizuri cha mwanadada huyo kilichopambwa kwa matiti ya saizi ya kati.

“Yote mawili, vipi kwani?”

“Nashangaa unaleta kifungua kinywa, isitoshe sikuagiza room service!” Amata akamwambia mrembo yule.

“Nimeamua nikuletee maana jana nilikuona umechoka sana, au hupendi?” akamwambi huku aking’atang’ata ulimi wake. Kamanda Amata akamtazama kwa jicho la kiu, kiu ya penzi.

“Sina muda wa kunywa chai!” akamwambia muhudumu yule.

“Ila una muda wa nini?”

“Wa kuondoka!” alipojibu hayo tayari mwanamke yule alikuwa amemaliza kazi ya kuandaa kifungua kinywa mezani. Akafungua mlango na kuondoka zake huku akimwacha Amata anatoa macho tu. Mara baada ya kuondoka mwanamke yule, Amata akatoka chumbani na kuchukua njia nyingine, akatelemka hadi chini huku tayari simu yake ikiwa sikioni kwa mawasiliano. Ijapokuwa hata yeye alimhusudu sana mwanamke huyo kwa siku ya kwanza tu kama ilivyokuwa kwa mhudumu yule lakini Amata hakutaka kuonesha udhaifu bali alitumia uanaume wake kuamua kuondoka huku roho ikitamani na kuijutia nafasi hiyo.

Katika maegesho tayari yule mzee wa siku ya jana alikuwa keshafika na kuegesha gari lake vizuri akilifutafuta ili ling’ae.

“Mzee!” Amata akaita kwa kutumia lugha ya Kireno. Alipolifikia gari akafungua mlango wa abiria na kuketi tayari kwa safari.

“Wapi asubuhi hii?”

“Condominio Bela Vista!” akamtajia mahala anapotaka kufika. Mzee yule akawasha gari, bila shida safari hii likakubali na kuondoka eneo hilo. Iliwachukua dakika kama arobaini hivi kufika katika jingo hilo la kifahari sana ambalo kila mtu alikuwa akijua na kutambua kuwa ni sehemu ya biashara hasa ya matajiri kuja kupumzika ama kuzungumzia biashara zao au kuja na vimwana kupunguza mawazo ilhali wake zao wamewaaacha nyumbani.

“Nisubiri hapa, nakuja!” Amata akamwambia yule mzee na kulifuata jingo hilo. Suti aliyovaa na mkoba aliyoubeba vilishabihiana haswa na mahali anapongia.

“Karibu sana, tunaweza kukusaidia!?” akaulizwa na kijana mmoja aliyekuwa nyuma ya dawati hilo la maulizo.

“Ndiyo, naweza kuonana na Bwana Fernades Pereira?” akauliza.

“Una miadi naye?”

“Bila shaka!” akawajibu na kuwapa kikadi kidogo ambacho Madam S alimpatia kwa siri.

Dakika tatu baadae, akachukuliwa na msichana mrembo, kwa kumtazama tu mavazi yake akajua kuwa ni katibu muhtasi wa mtu huyo. Wakaongozana pasi na kuongea mpaka katika ofisi fulani kubwa sana. Ofisi hii iliyokuwa tupu kabisa isipokuwa meza kubwa na viti viwili tu, na juu ya meza hiyo kulikuwa na simu moja ya kizamanai sana lakini ilioneka bado mpya kabisa.

“Você precisa esperar aqui, o Sr. Pereira vai se juntar a você em breve!” (subiri hapa, Mr Pereira ataungana nawe muda si mrefu) mwanadada yule akamwambia. Na Kamanda Amata akasubiri kama alivyoamuriwa, yule msichana wa kadiri ya miaka ishirini na tano au thelathini hivi akapotelea katika moja ya milango mingi iliyozunguka ukumbi huo. Sekunde hiyo hiyo akasikia mlango wa nyuma yake ukifunguka, alipogeuka akakutana uso kwa uso na mtu mmoja mwenye umbo kubwa, Mwafrika aliyevali suti ya kawaida tu, kwa huku kwetu tungeiita Kaunda Suit.

“Karibu sana Mr. Spark!” yule jamaa akamkaribisha Amata huku akiketi kitini na kumtaka Amata naye afanye hivyo.

“Yes! Tuna dakika chache sana za mazungumzo kama kumi na tano hivi, karibu…” yule jamaa akamwambia Amata huku akimkazia macho usoni.

“Nami nina jambo moja la kuzungumza nawe…”

“Ndiyo!”

“Nimetumwa kutoka Tanzania…”

“Najua!”

“Mkoba huu…” akauweka mezani “unatakiwa unatakiwa ndani yake ikae taarifa ya mauaji ya Rais wa Angola yaliyotokea miezi kama minne iliyopita,” akamwambia.

“Kwani mimi ndo’ nilimuua?” Perreira akauliza.

“Siyo wewe!”

“Ila…”

“Inajulikana kwamba tafutishi yote ya mauaji hayo wewe unayo, na hata jengo lililotumika ni lako, hivyo bila shaka una kimojawapo ama taarifa ya mauaji au mpango wa mauaji…”

Perreira akashusha pumzi ndefu na kumtazama kijana huyu ambaye hakuwa anaonesha hata tabasamu usoni mwake.

“Nani kakutuma hizo habari za kipumbavu?” akamuuliza Amata.

“Haina haja kujua ni mambo mawili tu yanayotakiwa kuwamo ndani ya mkoba huu,” Amata akajibu. Yule bwana akajifikicha macho na kisha kuyarudisha kwa Amata na ndipo alipojikuta akitazamana na domo la bastola aina ya PPK.

“Katika jumba hili, mtu huwa haingii na bunduki, wewe umewezaje?” Perreira akamuuliza Amata.

“Ndiyo ujue kwamba jumba lako halina ulinzi kama unavyofikiria,” Amata akajibu.

“Ok, ukinambi nani kakutuma, mimi nitakupa utakacho, huwa sina shida na watu wa serikali ila nataka nijue nani kakutuma…”

“Nimetumwa na AU…”

“Addis Ababba…”

“Yes!”

“Ok, nifuate, ila bunduki yako ihifadhi vizuri,” Perreira akamwambia kisha

akainuka na kuuendea mlango mmoja wapo huku nyuma akifuatwa na Amata, wakaingia mahali pengine tofauti na ile ofisi ya kwanza. Huku kulikuwa na watu wachache wake kwa waume waliokuwa kwenye mazungumzo, tunaweza ita ya falagha kwa maana usingeweza kusikia wanachoongea ila ungewaona wanaongea. Mlango mwingine ukawafikisha nje kabisa kwenye bustani nzuri na ya kupendeza, yenye maua aina aina na vitu vizuri vya kuvutia.

“Sikiliza,” Perreira akamwambia Amata na nukta hiyo hiyo mwanadada mmoja aliyevalia bikini akafika mahala pale akiwa na kitunga mkononi mwake, hakuwa Mhindi wala Mwarabu ila alikuwa na nywele ndefu mpaka makalioni, akafungua kile kitunga na Perreira akachukua sigara moja kubwa na kuiwasha kisha akaipachika kinywani na kuibana kwa midomo yake miwili. Baada ya kupiga pafu tatu kubwa na kuutoa moshi hewani akamtazama Amata kwa mara nyingine.

“Mimi ni mtu mwema sana, huwa nasaidia serikali nyingi kwa mambo mengi, nasaidia makundi mengi ya huduma za kibinadamu kwa mambo mengi, ila kwa hilo ulilotumwa, Mr. Spark nina wasiwasi sana… Mimi sina mpango wa mauaji, ila nina taarifa ya mauaji, lakini sikai nayo hapa taarifa nyeti kama hiyo. Tazama kuleeeeee, unaona kile kisiwa?” akamwambia. Amata akatazama na kukiona vyema kabisa.

“Pale panaitwa Ilha da Canzaga, itakupasa uende utamkuta mtu mmoja anaitwa Oliviera, mwambie nimekutuma akupe hiyo kitu, na ukiishaipata kwa sababu wengi wanaitafuta, utatakiwa ufanye juu chini uondoke katika jiji hili kabla hujang’anywa. Maana kuna watu wengi wako hapa Luanda wanataka kitu hicho hicho,” Perreira akamwambia. Na mara ukasikika mlio wa boti, ikasimama mbele kidogo baharini, na opareta wa chombo hicho alikuwa ni yule mwanamke aliyeleta sigara kwa Perreira.

“Tutaonana baadae, all the best!” Fernandes akamuaga Amata. Kamanda alipotaka kumpa mkono, yeye akachukua sigara yake nakuendelea kuvuta huku akigeuza kurudi ndani ya jumba lile.

Amata akatembea harakaharaka na kuingia ndani ya boti lile na safari ikaanza. Kamanda alijiegemeza katika kiti cha nyuma huku mwanamke yule akiwa kwenye usukani mbele yake akiedesha chombo hicho kwa kasi huku amesimama na kumfanya kijana huyu kusisimkwa mwili kila alipomtazama. Kiu kilimshika, akasimama na kumwendea pasi nay eye kujua, akafika nyumayake na kumkamata kiuno.

“What!!!” yule mwanamke akapiga ukelele mara baada ya kuhisi kuwa ameshikwa bila ridhaa yake.

“Mh mhhhhh, endelea na kazi, u mrembo sana bibie!” Amata akamwambia huku kidevu chake akiwa kakiegesha begani kwa mwanamke huyo.

“Kaa kitini tafadhali,” akasema yule mwanamke.

“Nitakaaje wakati wewe umesimama?” akamuuliza.

“Kwa hiyo?”

“Tukae wote,” akamwambia huku akimbusu nyuma ya shingo. Yule mwanadada akajikuta kwenye wakati mgumu sana.

KISIWA CHA ILHA DA CANZAGA

Kijana mmoja akaondoa jicho katika lensi kubwa ya bunduki ndani ya jengo moja la ghorofa mbili katika kisiwa hicho.

“Vipi?” mwingine akauliza.

“Huyu jamaa inaonekana anajua nini kinampata!”

“Kwa nini?”

“Si amemkumbatia Alegria, sasa nakosa shabahsa sahihi,” yule kijana akamwambia mwenzake, naye akaja na kuweka jicho kuangalia.

“Mh!” akaguna.

“Vipi?”

“Mwache afike, tutafanya kazi hiyo hapa hapa,” akasema.

Wale jamaa wakaendelea kuiangalia ile boti ikizidi kuja katika jumba hilo.

Katika boti lile, Amata bado alikuwa nyuma ya Alegria, akimpapasa kimahaba sehemu za kiunoni na juu kidogo ambapo panatengeneza umbo halisi la mwanamke.

“Sipendi kushikwa namna hiyo tafadhali,” Alegria akamwambia Amata huku mikono yake bado ikikamata usukani mdogo wa chombo hicho.

“Katika jingo hilo ndipo tunakwenda?” akamuuliza.

“Ndiyo!” mwanake yule akajibu. Amata akamwacha mwanamke huyo na kuketi tena kitini, akachukua miwani yake maalumu na kuivaa. Miwani hii ilikuwa na uwezo mkubwa wa kukuza vitu vilivyo kilomita moja kwa umbali na kumfanya mvaaji avitambue kwa urahisi. Alipohakikisha imemkaa vyema, akazungusha vijinobu viwili vilivyo upande huu na mwingine. Kamanda Amata macho yake yakagongana na mtu anyeshusha darubini na pembeni yake kuna bunduki kubwa ya kudungulia. Tayari walikuwa kama mita mia mbili hivi kufika katika ghorofa hilo, Akili ya Amata ikafanya kazi haraka na kuamua kwa kasi ya ajabu, akainuka kutoka kwenye kiti na kukanyaga batani ya mwendokasi na kuifanya ile boti iongeze kasi kwa ghafla kiasi kwamba Alegria alishindwa kuiongoza na kumuangukia Amata. Kijana huyo akamdaka na kumkumbatia huku mguu wake bado ukiwa kwenye ile batani.

“Unafanya nini wewe?” yule mwanamke akapiga kelele na kumpiga kipepsi Amata. Maumivu aliyoyasikia hayakuwa ya kawaida katika moja ya mbavu zake.

“Tuliaaa mwanamke!” Amata akamwambia na kumtupia upande wa pili, mwanamke yule akajiinua na kumtandika pigo moja matata, Amata akaona asiwe mjinga kwa tayari aliijua azma ya wenyeji wake, akatoa mguu kwenye ile batani na kumpiga ngwala Alegria, akaanguka vibaya na kujikuta akitumbukia baharini. Kamanda akarudisha mguu kwenye batani na injini ya boti ikavuma na kunyanyua chombo hicho mara baada ya kugusa mchanga. Boti ile ilipaa na kutua kwenye dirisha moja la kioo, ikaingia nusu na kuning’inia. Amata akaruka haraka nje na kutua sakafuni, mara risasi chache zikapiga sentimita chache kutoka pale alipokuwa ameangukia, lakini tayari alikwishabingirita na kuhama eneo kusudiwa. Alipotulia tayari bastola ilikuwa mkononi na alipofyatua shabaha yake haikupotea bure. Mtu mmoja akaanguka kama mzigo, na Amata akamuwahi na kummalizia kwa guu moja zito la shingo.

“To the ground floor!!!!” sauti kutoka ghorofa ya juu ikasikika, Amata akajiweka tayari, bastola mkononi, akajibana sehemu akisubiri kuona hao wanaoamriwa kuja upande wake. Punde tu akamwona kijana mmoja akiteremka kupiti ngazi ya mzunguko inayounganisha ghorofa ya juu na ile ya chini. Kamanda Amata akajua mara hii ameingia kwenye domo la mamba, akainua bastola yake na kufyatua risasi moja, shabaha maridhawa. Kijana yule akapiga yowe moja na kuanguka vibaya sakafuni. Amata akahama kutoka pale na kwenda upande mwingine kulikokuwa na maboksi makubwa ambayo hata hakujua nini kipo ndani yake, akatulia kimya kabisa.

ITAENDELEA

Magnum 22 Sehemu ya Tatu

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment