Magnum 22 Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA: RICHARD MWAMBE
*********************************************************************************
Simulizi: Magnum 22
Sehemu ya Tatu (3)
Oliviera, kijana mshupavu wa mwili anayeaminiwa na mkuu wake Pereira, aliteremka taratibu huku mkononi mwake akiwa Shot Gun matata sana. Akaangaza angaza macho yake huku na kule akitembea hapa na pale kwa hadhari kubwa, fulana aliyoubana mwili wake ilionesha jinsi gani alikuwa ‘baunsa’. Kamanda Amata akaendelea kusubiri ili kijana huyo afike kwenye ‘kumi na nane’ zake.
Simpigi kwa risasi! Akasema moyoni huku akijiandaa kumpa shambulizi la dharula. Oliviera, akatazama na kutazama, hakuna mtu! Akaiweka sawa bunduki yake na kupiga ‘burst’, risasi mfululizo zikamwagika na kumua maboksi yale, kisha ukimya ukatawala.
“Vieira! Vieira!” sauti ya mwanamke ikaita kutoka nje.
“Alegria, ingia ndani, mshenzi huyu ametufanya vibaya…” Olivieira akamwambia mwanamke huyo.
“Amejificha humu ndani au amekimbilia wapi, sijui….”
“Shiiiit! Kamuua Joao!” Alegria akiwa na vazi lile lile la bikini, akamwendea marehemu pale chini na kumtikisa tikisa.
“Keshakufa,” Olivieira akasema.
“Kwa nini hamkumuua tangu tunakuja kama kawaida?” Alegria akamuuliza Olivieira.
“Huyu mshenzi ni mjanja, alijificha nyuma yako…”
“Hakikisha tunaitoa roho yake, maana kama akipata anachotaka ataharibu mambo!” mwanamke huyo akasema huku akichukua Shot Gun ya yule marehemu na kuikamata vyema. Muda wote huo, kamanda Amata alikuwa akiwatazama kutoka nyuma ya maboksi, pale alipo ni risasi kadhaa zilimpita karibu sana, kilichomuokoa ni kuwahi kulala chini. Kwa wakati huu alikuwa akisikiliza mazungumzo yote ya wawili hao, akajua kuwa marehemu anaitwa Joao, na pia kuwa anachokitaka kipo hapa.
Kumbe! Akawaza na kujiweka tayari kutoa shambulizi la dharula.
Hapa lazima mmoja afe na mwingine apate kipigo kitakachomlazimu kunipa kila kitu, shenzi sana! Akajisemea moyoni kisha akaanza kuchagua nani afe na nani abaki. Akimtaza Alegria, jinsi alivyoumbika hakutamani kabisa kumuua, lakini akajiuliza kama akibaki hai je aianajua kila kitu kilipo? Hakuoma haja ya kujiuliza hilo. Akaigiza mkono mfukoni na kutoa goroli tatu, akazirusha mja upande huu nyingine ule na nyingine katikati kwaribu kabisa na miguu yao, kisha yeye akahama haraka na kuelekea upande mwingine.
“Aaaaaaaaaaaaaiaiiiiiiiiiihhhhhhgggggghhhhh!!!!!” Oliviera akapiga kelele huku akimiminia risasi upande ule kwa minajiri ya kuua tu. Mwanamke yule naye akaungana naye kwa kufyatua risasi vilevile. Baada ya kama sekunde ishirini hivi, Olivieira akanyosha mkono na risasi zikakoma, kilichobaki ni harufu ya baruti tu. Oliviera akampa ishara ya mkono Alegria akimtaka kupita upande wa pili huku yeye akipita upande huu waibukie nyuma ya mabaoksi hayo. Kamanda Amata akajua wakitawanyika tu pale waliposimama itakuwa ngumu kuwashambulia. Akatumia nguvu zake zote na kuruka kutoka juu ya maboksi yale huku miguu yake ikimchangua mmoja baada ya mwingine. Oliviera alishtuliwa na kishindo cha Amata kuanda maboksi akatazama juu na kujikuta akikanyagwa na guu la uso, akayumba na kwenda kando wakati Alegria akienda chini na bunduki kumtoka mikononi.
Mara alipotua chini, Oliviera tayari alikwishajiweka imara, akamshushia konde moja zito, Amata akayumba kwa nyuma na kujikwaa kwenye mwili wa Joao na kuajikuta akitaka kuanguka kinyumenyume lakini akajiwahi. Oliviera alikuwa akimfuata Amata kwa kasi lakini alipomfikia tayari alijikuta kapoteza, kwani pigo moja la pili la tatu, yote ya karate yakamwacha hana hali. Jamaa huyo akainua pipa lililo karibu na kulirusha kwa nguvu, Amata akaruka sarakasi na kuliacha likipita chini. Alegria alijiokota kutoka pale chini kuokota ile bunduki, hata hakufanikiwa kuishika kwani alijikuta akiangukiwa na mtu juu yake.
“Tulia! Kahaba wewe!” Amata akaunguruma huku bastola ikiwa mkononi tayari ilikwshammaliza Oliviera.
“Nipe ninachohitaji haraka!” akamwamuru.
Alegria akarembua macho yake ili kumteka mwanaume huyo. Kama alifikiri Amata hudanganywa na wanawake kirahisi basi alikosea, risasi moja ikachimba milimita kama tatu hivi kutoka mguuni mwa mwanamke huyo.
“Nipe ninachotaka haraka kisha unirudishe kwa bosi wako,” akamwambia huku akimfuata taratibu. Mwanamke huyo mwenye bikini akajikuta hana kingine cha kumlaghai jamaa huyu.
Huyu ni nani? Akajiuliza.
“Huku, nifuate!” Alegria akamwambia Kamanda, kisha wakafuatana na Alegria akamzungusha mpaka upande wa nyuma.
“Inabidi twende bondeni,” akamwambia Amata.
“Bondeni wapi?” akamuuliza.
“Hicho unachokitaka, kipo bondeni,”
“Sitaki maneno, nipe ninachotaka,” Amata akasisitiza.
Pale aliposimama Alegria, pakafunguka na kuacha uwazi katikati, wakateremka na katika chumba walichopita, Amata akashtuka kukuta kuna mtu kafungwa minyororo miguuni na mikononi akining’inia.
“Shiit! Mfungue huyu!” akamwambia Alegria.
“Sina funguo, hiyo loki hufungwa kwa namba na namba hiyo anaijua Oliviera pekee, sasa si umeshamuua, kwa hiyo no way!” Alegria akajibu kwa dharau, Amata akavuta hatua moja na kumpiga kwa kitako cha bastola katikati ya paji la uso na kumpasua.
“Mfungue!!!” akamwambia. Alegria akajipapasa katika paji la uso, akashika damu inayotiririka, kisha akamtazama Amata.
Kama kuna kitu ambacho Kamanda Amata hakuwa anakipenda ni kuoneshwa dharau na mtoto wa kike. Akairudisha bastola mahala pake, kumfuata mwanamke huyo. Lakini kabla hajafanya atakalo, yule mwanamke akaliamsha dude kwa mapigo ya kutosha ya karate. Amata akayapangua yote kisha akamshushia moja la kilo nyingi na kumpeelka sakafuni. Kamanda akamuwahi huku tayari mkononi ana kisu kidogo amekwishakikunjua, akakididimiza kwenye nyama ya paja.
“Aaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaahhhhhh!!!!” Alegria akatoa yowe lililomstua yule mateka.
“Mfungue!!!” akamwambia na wakati huo tayari mkononi ana kisu kingine. Alegria akainuka kwa taabu na kutembea kwa kuushika ukuta huku damu ikimwagika kwenye paja lake, akaingia kwenye kile kuwazi na kubonya namba fulani kwenye kifaa maalumu, ile minyororo ikalegea na yule bwana akawa huru.
“Huyu ni nani?” akamuuliza.
“Mpumbavu kama wewe!” Alegria akajibu.
“Sawa, nioneshe ninachotaka,” akamwambia tena na mwanamke yule akaendelea kujikongoja mpaka kwenye mlango mwingine wenye kufuri.
“Hapa!” akamwambia Amata, naye hakufanya ajizi, akachukua bastola yake na kuifumua kisha mlango ukawa wazi. Kulikuwa na shelfu ya vitabu na kabrasha kadhaa. Amata akaingia ndani na kijichumba hicho na kuvuta hili na lile.
‘SECRET ASSASSINATION’ moja ya makabrasha lilikuwa limeandikwa hivyo.
“Thank you very much!” Amata akamwambia Alegria kisha akamwongoza kutoka nje wakampitia na yule bwana mwingine, Amata akamsaidia kumkokota mpaka pale kwenye boti lililonasa dirishani. Amata akalisukuma kutoka upande wa ndani nalo likajikita chini kwa upande wa nyuma, akatoka na kulivuta kwa nje, akalisukuma mpaka majini kwani hapakuwa mbali, kisha akamtaka mwanamke yule kushika usukani. Watatu hao wakaondoka taratibu na kutokomea baharini kurudi Condominio Bela Vista.
Palepale alipopandia boti ndipo liliposimama tena na Bwana Pereira akatoka nje kuwalaki. Mkononi mwa Amata kulikuwa na ule mkoba ambao ndani yake kuna lile kabrasha, akashuka nalo na kusimama wima. Kisha akageuka kwa Alegria na kuchomo kile kisu kutoka pajani. Pereira akaendeela kutazama Amata anavyomchomo kile kisu. Akakipangusa na kwa kitambaa kutoka mfukoni mwake na kukirudisha ndani ya koti la suti aliyoivaa.
“Umefanya nini?” Pereira akamwuulia Amata.
“Nashukuru kwa wema wako nimepata ninachokitaka, na nimempata rafiki yangu pia, good bye and see you soon!” Amata akamuaga na kuondoka na yule jamaa aliyechoka ambaye kwa mateso alibaki na nguvu aliyopewa na Mungu tu.
Kamanda Amata moja kwa moja alikwenda na mtu wake katika kliniki moja maarufu sana ambayo mzee yule, dereva wa taksi alikuwa anaijua na ndiye aliwapeleka. Katika kliniki hiyo, Amata akakutana na daktari mwanamama mtu mzima mwenye asili ya Kihindi, akamkabidhi mgonjwa huyo huku akimtaka asiruhusu kuonekana na mtu yeyote.
“Wala usiondoke, subiri hapahapa, ni masaa kama mawili au matatu tutakupa jibu na utaweza kwenda na mtu wako,” yule daktari akasema.
Kamanda Amata akasubiri. Baada ya saa mbili, kweli mtu yule alikuwa sawa, akitembea mwenyewe bila kushikiliwa, aliyeonekana kuwa na nguvu haswa.
“Na hizi ni dawa ambazo atatakiwa kunywa kwa wiki moja,” muuguzi akamwambia Amata kisha akazilipia na kuchukua majibu ya vipimo mbalimbali. Mtu huyo akatakiwa kurudi siku ya pili kwa matibabu zaidi au tuseme ya kina. Baada ya kutoka hapo, Amata na mtu wake wakaelekea mpaka Hoteli ya Alvalade ambako alimpangia chumba na kumpatia huduma zote ikiwamo mavazi na nyingine za kukandwa na kadhalika ili kumrudisha katika hali ya ubinadamu.
Baada ya saa mbili kupita, yule mtu akawa mwingine kabisa si yule aliyemwokoa kule kisiwani. Hakuwa kijana bali mtu wa makamo, mwenye mvi chache kichwani na ndevu zilizonyolewa kiufundi sana. Suti safi ya gharama ilitulia mwilini mwake, yote haya yalifanywa na Kamanda Amata lakini mpaka dakika dakika hii hakuna aliyemjua mwenzake, ni mtu huyu tu ambaye aliisikia japo sauti ya Amata lakini mwenzake hakusikia chochotebkutoka kwa mtu huyo.
Katika chumba namba 720, ndani ya Hoteli ya Alvalde, mtu huyu alisimama mbele ya kioo kikubwa akijitazama mwili wake uliositiriwa kwa suti ya gaharama.
“Ni nani huyu aliyeniokoa?” akajiuliza kwa sauti ndogo. Hakukuwa na wa kumjibu, akajitazama vidole vyake na kugundua kuwa kimoja kimekatika, hakipo kabisa, akatikisa kichwa.
“Walinikata kidole!” akajisemea tena. Akajaribu kutikisa mguu, unaweza kidogo japo bado una uzito au tuite ganzi.
“Miezi mine chini ya himaya ya washenzi hawa, bila Mungu wangeshaniua…” akajisemea.
Maneno yote haya aliyazungumza peke yake akiwa kasimama mbele ya kile kioo, mtu huyu aligundua udhaifu mkubwa wa mwili wake katika utendaji kazi. Jamaa hawa walimweka katika himaya yao kwa takribani miezi mine ilhali alikotoka walikuwa wakimtafuta na kusaidki kuwa kapotea au kafa kabisa. Akajaribu kuvuta kumbukumbu ya jinsi alivyoingia katika himaya ya washenzi hao hakukumbuka. Ubongo wake ulikuwa ukimleta mpaka anaingia kwenye gari, zaidi ya hapo ni giza na ukiwa.
Ngoh! Ngoh! Ngoh! Mbisho wa hodi ukamshtua kutoka katika mawazo yake. Akautazama mlango huo kwa chati huku kichwani mwake akijiuliza kama afungue au la.
Liwalo na liwe! Akajisemea na kuuendea mlango, akaufugua na macho yake yakagongana nay a Amata. Hakuongea kitu akajikuta akigwaya tu kwani hakumwona mtu huyo kutabasamu tangu alipomwokoa.
“Tunatakiwa kuondoka! Haraka!” Amata akamwambia.
Yule mtu hakujali kujiuliza imani yake yote ililala kwa kijana huyu ambaye ukiwaweka pamoja inaoneka wazi kuwa huyu ni mkubwa kama miaka mine au mitano kwa Kamanda. Akatoka na kumfuata Amata katika njia ya ngazi, kisha wakaachana na ngazi na kuchukua ukorido mrefu uliowatoa upande wa kumbi za mikutano huko wakateremka kwa ngazi nyingine mpaka chini kabisa, wakajikuta nyuma ya hoteli. Hawakujisumbua kuzunguka mbele, wakapita kwenye kijimlango kilichjengwa katika wigo wa hoteli hiyo na kuibukia barabarani, Amata akafungua mlango wa gari na kuingia ndani huku yule mtu akifuatia kisha wakaondoka kwa kasi.
Taksi ya akina Amata, ikawasili katika Nyumba ya Wageni ya Chicala iliyojengwa katika ghuba ya Total Angola.
“Hapa patatufaa!” akasema huku akitangulia kushuka na kuchukua mkoba wake kutoka katika siti ya nyuma. Hakujali kama mtu wake huyo anaelewa au haelewi. Kisha akamtazama yule mzee mwenye taksi ambaye mpaka dakika huyo hata yeye alikuwa akipelekwa pelekwa tu hajui nini kinaendelea.
“Sasa, we waweza kwenda, mimi nikikuhitaji nitakwambia, bado nina siku kama tatu hapa Luanda. Mtu yeyote akikuuliza kama niko wapi usimpe habari zangu sanasana nitumie meseji kwa siri na meseji hiyo aundike K.A, mi nitaelewa kuwa kuna mtu anakuuliza juu yangu. Akampa pes iliyotakata na kuagana naye.
Haikuwa Gesti ya hadhi kubwa ila si mbaya sana, wakapata chumba kiimoja chenye vitanda viwili na choo ndani. Ukikaa ndani ya chumba hiki na kutazama diridhani unakutana na Bahari ya Atlantiki na Kisiwa cha Ilha Da Canzaga unakiona kwa mbali sana ila kwa chombo kama darubini unaweza kukiona uzuri kabisa. Kamanda Amata akafunga mlango na kutupia mkoba wake kitandani kisha akaketi na yule mtu naye akaketi upande wa pili, yaani kwenye kitanda kingine. Kutoka katika meza ndogo pembeni yake, akanyakua simu iliyowekwa hapo na kuzungusha namba kadhaa kisha akaiweka sikioni. Baada ya kupokelewa upande wa pili, akaagiza whisky na bilauri mbili na kigudulia cha barafu. Haikupita muda mlango ukagongwa, akaufungua na mwanadada mfupi kibonge akaingia na kuweka kinywaji kile mezani kisha akaondoka zake. Amata akafunga mlango na kuketi huku akifungua kile kinywaji, moja ya bilauri akajimiminia na ile nyingine akampa rafiki yake ambaye hajawahi hata kusikia sauti yake.
Baada ya nusu saa ya kila mtu kupiga kama bilauli tatu hivi, Amata akafungua kinywa na kumuuliza, “ Wewe ni nani?”
Yule jamaa akamtazama Amata kana kwamba haelewi anachoambiwa.
“Naitwa Costantine!” akajibu kwa sauti ya kukwaruza sana kiasi kwamba Amata akajua wazi kuwa huyo jamaa ana shida kwenye mfumo wake wa sauti hasa kooni.
“Costantine?” Amata akarudia kwa kuuliza.
Mara hii kabla hajajibu akakohoa kwanza na kutikisa kichwa chake, “Yes! Costantine,” akajibu. Ukimya ukapita tena kwa jozi la sekunde, mara hii Amata akajua kwa nini mtu huyo hapendi kuongea kwani alihisi ana maumivu sana kwenye koo.
“Mimi naitwa Mr Spark kutoka Zambia…”
“Oooh Mr. Spark!”
Koh! Koh! Koh! Akakohoa mfululizo kisha akaendelea kusema, “Happy to know you… mimi nilikuwa nakufa polepole,” koh! Koh! Koh! “…lakini nashukuru umenileta tena duniani, umenipa nafasi ya pili ya kuishi,” akaongea kwa kirefu.
“Obrigado!” akamshukuru.
Costantine akainuka na kuelekea dirishani, akasimama na kuangalia upande wa baharini, kisha akachukua darubini ya Amata iliyokuwa juu ya meza, akatazama tena baharini.
“Ilha Da Canzaga!” akatamka. Kamanda Amata akainuka alipoketi na kumwendea pale dirishani, wakasimama pamoja.
“Unapaona vizuri?” akamuuliza.
“Yes!”
Kishapo, Amata akachukua simu yake na kufungua program fulani katika hiyo, wakati wote Costantino alikuwa akimwangalia anachofanya. Na mara mlipuko mkubwa ukaonekana kule kisiwani.
“Kila kitu kimeanguka!” Amata akasema. Costantine akatazama kisini na kushuhudia moto na moshi mzito, akageuka kwa Amata na kumtazama, akamwona akiirussha ile simu kitandani na kisha ye mwenyewe kujibwaga hapo na kujimiminia kinywaji.
“Who are you?” Costa’ akamuuliza.
“Mr. Spark… mwokozi wa wanyonge,” akamjibu.
“Kazi yako ni nini hasa hapa Angol?” Costa akaanza kumhoji Amata.
“Nilikuja kuiangusha Ilha Da Canzaga, bahati nzuri nimekuokoa na wewe lakini pia nilikuwa nahitaji hii…” akachomoa kabrasha lake mkobani na kumwonesha kwa mbali.
“A secret assassination!” akasoma.
“Yes! Sasa sikiliza, mimi nimemaliza na hatuna budi kuagana, lakini marafiki lazima wajuane kwa kina….”
“…Ndiyo, bila shaka…”
“Ulikuja kufanya nini Angola?” akamuuliza.
“Nilikuja kumsaka mtu mmoja muuaji anayetafutwa kila kona ulimwenguni, lakini mtandao wake ukahi kunitambua na wakaniteka na kujikuta nipo kule, hata sikuwa najua kama ni kisiwani mpaka nilivyoona tulipokuwa tunatoka,” Costa akasema.
“Muuaji?” Amata akauliza.
“Yes, muuaji mmoja profesheno… katika kumtafuta nikagundua kuwa ana misheni ya kufanya hapa Angola …”
“Lini ilikuwa atekeleze misheni hiyo….?” Amata akamkatiza kwa swali.
“Aaaaannnhhh huu ni mwezi gani, samahani!” Costa akauliza, kumbe hata hakuwahi kujua tarehe na miezi inakwendaje.
“September!” akajibiwa
“September?” khooo – kho! Akakohoa, “ina maana nimekaa miezi mine mateka?” akasema.
“Ni miezi mine iliyopita… huyu bwege anaitwa Martin Gupter ila hutumia majina mengi sana na sura nyingi za bandia kujificha, yeye hutumiwa na mitandao mikubwa ya mauaji ijapokuwa naye anatimu yake ya watu wawili wenye weledi mkubwa wa mbinu za kigaidi na mauaji, hayawajawahi kukamatwa wala kujulikana kwa majina halisi,” akamwambia Amata.
Akili ya Kamanda ikaanza kuunganisha matukio, akachekecha na kuchekecha, akaona kwa vyovyote vile kuna uwezekano mkubwa wa misheni yao kuwa moja ila ikatofautiana maudhui.
“Miezi mine ilopita, aliuawa rais wa Angola,” Amata akasema.
“Come on! Walifanikiwa? Hawa ni washenzi…” Costa akaongea kwa hasira kidogo.
Ina maana huyu jamaa anajua mengi juu ya hili! Amata akawaza na kubaki kimya kwa sekunde kadhaa akimtazama mtu huyo. Baada ya muda kidogo, Costantine akainua uso na kumtazama Amata.
“Martin Gupter ni muuaji hatarai sana, yeye amebobea katika assassination iwe ya moto au ya baridi. Anatafutwa, natafutwa na watu wengi ikiwamo mimi, nilipata siri ya kuwa wanakuja huku Angola ili kutekeleza mauaji ambayo wenyewe waliyaita ‘Mauaji ya Kihistoria’, nikiwa hapa nikawafuatilia sana mpaka nikajua ni wapi watafanyia shabaha yao, siku nilipokuwa nimepanga kumaliza mchezo nikajikuta matatani, nilikuwa nachukua gari kwenda eneo la tukio, ghafla nikapigwa na kitu kama bomba la chuma kichani, nikapoteza fahamu na kujikuta ndani ya chumba kile. Wao nao wakanitesa na kunipiga sana ili niwaambie ni nani kanituma…”
“Kwa hiyo ni hicho tu kilichokuleta Angola?” Amata akamuuliza.
“Hicho tu! Namhitaji Gupter nimtoe roho yake, nilishahesabu nimeshindwa lakini wewe umenipa nafasi nyingine na kwa nafasi hii lazima nimmalize,” akasema, “na wewe huna haja na huyu shetani?”
“Sina, ila ninachotaka sasa ni kukamilisha uchunguzi kama mtu aliyetaka kufanya mauaji Dar es salaam ni huyo huyo au la…”
“Tena?”
“Ee ila hakufanikiwa na risasi ikamuua mtu mwingine, sasa nataka kuhakikisha je muuaji huyu wa Angola na yule wa Dar es salaam ni mmoja? Amata akamwambia huyu mtu bila kumzungusha.
“Hiyo kazi ndogo, nitakupeleka kwa mtu mmoja ambaye anaweza kukusaidia kujibu maswali ya shida yako, kwa vyovyote atakuwa anajua nini kinaendelea”.
“Twende hata sasa!” Amata akasema huku akiwa tayari amekwishainuka.
Wakatoka nje na kufunga mlango kisha wakachukua taksi mpaka mtaa mmoja wa kimya sana, ni majumba makubwa na machache yaejipanga upande huu na ule.
“Tuache hapa!” Costantine akasema na lile gari likaingia pembeni, wakashuka na kulipa kisha likaondoka, wakalitazama kwa kulisindikiza mpaka lilipoishia kwenye upeo wa macho yao.
Kutoka hapo wakavuka barabara, na Costantine akaongoza njia mpaka katika jumba moja la kifahari. Muda wote huu, Costantini ndiye alikuwa mbele huku Amata akifuatia kwa karibu maana hakujua hata ni wapi kiukweli alikuwa akipelekwa.
Kelele za mbwa akibweka zilisikika ndani ya wigo wa jumba hilo, na kabla hata hawajabonyeza kitufe cha kengele, mlango ukafunguliwa na mtu mmoja wa makamo aiyevalia jinzi na fulana mchinjo akatoka na kulifuata geti hilo kwa mwendo wa haraka kidogo. Bila kuongea neno lolote akafungua geti na kuwapa ishara ya kuingia, wakafanya hivyo na bwana huyo akawaongoza mpaka sebuleni wakaketi.
“Yes! Nashindwa niseme nini, ni wewe au?” yule bwana akamuuliza Costantine, wala hakuwa na muda na Amata.
“Yes! Ni mimi, nilikuwa mikononi mwa mbwa kwa miezi karibu mine kwa mujibu wa kalenda,” Costa’ akaeleza.
“Nilijua umekufa, tumekutafuta sana, mpaka kwa waganga tumeenda, mwisho tukakubali kushindwa…”
“Mlikubali tu kushindwa, ila sikufa…” akamjibu kwa kumkatiza kile alichokuwa akiongea. Yule jamaa akampa ishara ya kumwita pembeni ili wazungumze machache.
“Hamna shida, ongea hapahapa!” Costa akasema huku akimtazama Amata, “Najua sijakutambulisha, huyu ni rafiki yangu, anaitwa Spark!” akamtambulisha Kamanda kwa mwenyeji wake kisha akafanya hivyo kwa Kamanda Amata, wakafahamiana na kupeana mikono.
“Nasikia mzee katunguliwa,” akaanzia hapo na Amata akawa kimya akaisikiliza tu.
“Yes! Tumeshasahau ila bado tuna kazi ngumu kwani baada ya kufanya uchunguzi na kuweka tafutishi zote pamoja lile kabrasha likaibwa, mpaka sasa badala ya kumsaka muuaji tunatafuta kabrasha,” akaeleza.
“Oh shit! Hamjapata chochote? Ni Gupter au ni nani?” Costa akauliza.
“Hatujang’amua ni nani mpaka sasa tumemwita jina ‘sweet killer’ kwa sababu anaua na hapendi kuacha chochote nyuma yake, bahati nzuri tu niliokote kitu hiki…” akainuka na kuiendea droo, akafungua na kuchukua kijimfuko cha plastiki akaenda nacho mezani na kukifungua ndani, akamwaga vitu viwili … “ganda la risasi lakini ni mita kama mia tatu kutoka eneo tunalolihisi muuaji alikuwako,” akaeleza.
“Naweza kulishika?” Amata akauliza.
“Yes, ila usitumie mkono tupu,”
“Sawa!” Amata akajibu na kutoa soksi za mikononi kutoka katika suti yake akavaa na kuinua lile ganda, akaligeuza kwa nyuma na kujikuta anapigwa na bumbuwazi.
Magnum 22 riffle! Akasoma kilichoandikwa kisha akampasia Costantine, naye akalipokea na kuatazama vizuri.
“Martin Gupter! Huyu ni Gupter, siri ya jamaa huyu ni kutumia aina moja ya bunduki, Magnum 22 riffle, nimepita kwenye kesi zake kama tatu hivi kati ya hizo wachunguzi wamegundua aina hii ya bunduki kutumika,” Costa akaeleza.
“Ungekuwa umefanikiwa kumpata, ungetusaidia sana, sasa utafanya nini, kwa ujumla si kwamab tumemkosa ila ni kazi sana kumpata,” yule jamaa akasema.
“Mh!” Costa akaguna, “Jerry! Huyu bwana naye anamtafuta Gupter naweza kusema hivyo,” akamwambia.
“Huyu? Mr Spark?” akauliza. Ni mara hii Jerry alimtazama Amata, akaondoa miwani yake na kuiweka kitini, akatikisa kichwa, “Unamtafuta Gupter, the sweet killer?” akamuuliza.
“Si kwamba namtafuta Gupter, kwa sababu mpaka sasa inabidi nijiridhishe kama ndiye ninayemtafuta. Si unajua kilichotokea Tanzania siku nne zilizopita!”
“Yes! Najua, na ninafuatilia kujua nini Tanzania inafanya kwa sababu tunaiamini sana kwenye maswala ya kijasusi, ila hatujasikia chochote,” Jerry akasema.
“Ninaanza kuona kuwa ni huyu aliyetaka kutekeleza mauaji ya Dar es salaam…”
“Kwa nini??” hii ‘kwa nini’ ikatoka kwa Jerry na Costa’ kwa mara moja. Kamanda Amata akaingiza mkono mfukoni na kutoa kijimfuko cha plastiki na kuweka mezani ganda la risasi kama lile lile.
“Shiiiiit!” Jerry akang’aka kwa kulitazama tu, kisha akamtazama Amata na kisha Costa.
Sasa nahitaji msaada wa jambo moja tu kutoka kwako…” akamwambia Jerry.
“Sema, na tutasaidiana kumtia mkononi mshenzi huyu!”
Kamanda Amata akatoa picha ya mwanamke wa Kizungu, akaiweka mezani, “katika tukio hilo, ulimwona mtu huyu ama anayefanana au mwanamke tu yoyote wa kizungu kama si akipita basi akitazama kinachoendelea au chochote kile?” Amata akauliza.
Jerry hakujibu, akaitazama ile picha kwa makini sana, kisha akamtazama tena Amata, wakatazamana, “ninamkumbuka hata kama ni miezi mine imepita, huyu mwanamke asubuhi ile, alikuwa akipita anafanya mazoezi ya jogging, nikamzuia na kumtaka apite upande mwingine, akatii wala hakuwa na ubishi, ndiyo ni huyu ama pacha wake, ila wanashahabiana,” akamwambia.
Kamanda Amata akachukua ile picha na kile kijimfuko akavirudisha kotini mwake.
“Spark! Vipi?” Costa akauliza.
Amata hakujibu, akamtazama Jerry, “Jerry, you people, mnafuga magaidi ilhali mnakaa na kunywa nayo,” akasema. Jerry akajikuta hana cha kusema akaendelea kumkodolea macho Amata.
“Kivipi?” Costa akauliza.
“Jerry, unamjua huyu?” akamuuliza akimaanisha kama anamjua Costantine.
“Yes, Costantine ni rafiki sana na mimi, tumefanya kazi hizi pamoja mara nyingi ila yeye sasa ni mpelelezi wa kujitegemea huko Costa Rica, alikuja hapa kwa minajiri ya kumsaka huyu mshenzi, na ni yeye aliyenigutusha mimi kuwa kuna uwezekano wa kutukia tukio la mauaji ya kiongozi hapa. Mara baada ya kunijuza nikalifikisha kunakohusika tukaanza kulifanyia kazi. Siku mbili kabla ya tukio sikumwona Costa, nikamtafuta sana pasi na mafanikio, nimeshtuka sana kumwona leo kwani nilikwishajua kuwa amekufa,” akaeleza.
“Washa TV,” Amata akamwambia Jerry, naye akafanya hivyo na habari waliyoikuta ni kuhusu Kisiwa cha Ilha Da Canzaga.
“What?” Jerry akajikuta anapigwa na butwaa baada kushuhudia moto mkubwa huko kisiwani huku jitihada za kuuzima zikiendelea.
“Samahani, naweza kwenda toilet?” Amata akaomba na kuoneshwa ni wapi choo kilipo. Akainuka na kuwaacha wawili hao wakiwa wamekodolea macho luninga, akafungua mlango na kuufunga.
Nusu saa ikapita, Amata hakurudi sebuleni, “hey! Mr Spark!?” akamuuliza Costa. Costa yeye hakujibu ila aliinuka na kuelekea chooni, akatikisa mlango, uko wazi, akausukuma huku akiita, hakuna mtu, kwenye tanki la maji ya kuflashi kuliandikwa kwa maka peni nyekundu.
Fernandes Perreira ndiye anayewasaliti! Costa akamwita Jerry naye akaja na kushuhudia maneno hayo.
“Ameondoka!” Jerry akasema.
MSAKO MKALI wa kumtia mkononi Amata ukaanzishwa ndani ya Jiji la Luanda, Fernandes Perreira mara baada ya jingo lake kule katika Kisiwa cha Ilha Da Canzaga kulipuliwa akajua tu hakuna mwingine zaidi ya mgeni wake aliyemtembelea na kutaka kupatiwa kabrasha la ‘SECRET ASSASSINATION’. Taarifa ikafika kwenye vyombo vya usalama na kazi ikaanza, akamatwe afikishwe panapohusika.
Fernandes Perreira alikuwa akizunguka huku na kule, nywele zimemsimama, hataki kungea na yoyote zaidi ya kufuta jasho tu, alichanganyikiwa, simu zilipigwa, akapokea, akaongea maneno machache tu, akakata. Wageni wengi, matajiri kwa viongozi wa serikali walimiminika kumpa pole kwa tukio hilo na baadhi yao ndiyo wakapata jazba ya kutaka mtu huyo asakwe mara moja.
Wakati yote hayo yakijiri, Kamanda Amata alikuwa akimlipa pesa dereva taksi wake, tayari kwa safari ya kurudi Tanzania, alijua kwa vyovyote lazima atakuwa hatarini tu, wakaagana na yule mzee huku akiwa amemwachia pesa nyingi tu. Kamanda Amata, akaingia katika ofisi ya ndege binafsi, bahati nzuri akapata ndege na kukodi, nusu saa baadae akaiacha Angola na kurejea Tanzania akiwa tayari keshapata jibu la moja na moja ni ngapi.
SHAMBA
MADAM S akarudi tena mezani alipowaacha Amata na Chiba, akatua lile kabrasha na kuvuta kiti, akaketi na kusogeza kabrasha lile kwake.
“Vipi?” Kamanda akauliza.
“Umefanya kazi kubwa sana mwanangu, ndani ya kabrasha hili kuna kila kitu, mpango mzima wa mauaji na mpango mzima wa uchunguzi, sasa swali ni kwamba ina maana hawa jamaa wanajuana na pande nzote?” akauliza.
“Nafikiri hivyo kwa maana wangepataje taarifa ya uchunguzi uliofanywa na wapelelezi wa serikali? Na wamepataje mpango mzima waq mauaji ya siri ambayo Gupter na wenzake wameupanga? Huyu ni nyoka mwenye vichwa viwili…”
“Ndumi la kuwili,” Chiba akamkatisha Amata.
“Nimesoma ndani ya kabrasha hili, nimegundua kitu kingine ambacho wala hatuna budi kuumiza kichwa…”
“Kipi hicho? Maana mimi sijasoma chochote,” Amata akadakiza.
“Mauaji ya Waziri Mkuu wa Ivory Coast ni wao pia waliohusika, maana nimeona mpango mzima hapa ndani na hakika wametekeleza isipokuwa si kwa mbinu ambayo wameianisha humu, mpango wa tat undo ulikuwa hapa kwetu ambao kwa hakika umefeli kwa asilimia themanini na tano,” Madam S akawaeleza vijana wake.
“Enhe!”
“Sasa hapa kuna mpango wan ne ambao maelezo yake hayapo sawasawa yaani hayajakamilika, inaonekana watu hawa huweka hizi karatasi hatua baada ya hatua…” akaeelza.
“Kwa hiyo walipanga mauaji ya watu wane?” Chiba akauliza.
“Yes! Na wane hao ni ndani ya miezi sita, wakiwa na maana kuwa Afrika itashtuka na kuwasikiliza kila wasemacho,” Madam akawaambia.
“Sawa, nani wa nne?” Amata akarusha swali.
“Enheeee hicho sasa ndicho kitendawili ambacho yatupasa kukitegua, na huyu wan ne anatakiwa kuuawa katika miezi hii miwili, ni nani na ni wapi, kazi ipo!” Madam S akafunga lile kabrasha na kuliweka kando.
“Tupo kazini,” akawaambia, “Na safari hii mkubali tu kuifanya peke yenu sijui kama Jasmine na Scoba watawahi maana wana kibarua kizito kule Haiti,” akawaambia.
Ukimya ukatawala kwa sekunde chache, hakuna aliyemwongelesha mwenzake wala kumshtua, Amata akavuta kwake lile kabrasha na kufungua kurasa ya mwisho kabisa. Huko akakutana na maneno machache tu ya kuhusu mpango huo wa nne.
“Watakamilishaje mpango wan ne kama wa tatu wamefeli?” Amata akauliza.
“Mi na wewe hatujui, sisi cha kufanya ni kuhakikisha mpango huo haufanikiwi kabisa kama ambavyo tumeweza hapa,” Madam akasema.
“Siri ya mpango wa nne wanayo wao wenyewe, yatupasa kuwatia mkononi,” Kamanda akawaambia.
“Naam, hivyo mwanangu huna mapumziko, anza kujiandaa safari ya Sierra Leone kama Chiba alivyosema imewadia, nataka kwanza ukahakikishe umewapata na kutibua mipango yao kisha hakikisha unapata kujua ni nani anayewatuma, yuko wapi na wapo wangapi,” akamwambia.
“Bila shaka, nitahakikisha hilo linafanyika,” akajibu
“Asante sana!”
Kikao kikafungwa ikiwa tayari TSA 1 anakabiliwa na mtihani mwingine wa kuwasaka hawa jamaa wauaji. Ni tafutishi za Chiba ambazo aizipata kwenye ile micro chip chumbani kwa Amanda kule Kunduchi ailiyomhakikishia kuwa watu hao mara baada ya kila mauaji huenda kujificha huko Sierra Leone, katika mji mdogo wa Waterloo.
“Comrade!” Chiba akaita. Amata akamtazama swahiba wake, mwenye renki inayofuata chini yake yaani TSA 2, mbobezi wa ujasusi wa kimtandao, mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Mlimani katika kitengo cha TEHAMA.
“Nambie comrade!”
“Una kazi ngumu kaka,” akamwambia.
“Sure, ila kama wewe upon a Gina pia naamini haitakuwa ngumu,”
“Unategemea kuondoka lini?”
“Hatutakiwi kuwapa muda mrefu washenzi wale, kwanza naamini mpaka sasa watakuwa wameshanganyikiwa kama wamepata habari ya Angola,” akamwambia Chiba.
“Na umewatetemesha haswa!”
“Na bado nitawasambaratisha kabisa…” Amata akasema huku akiinuaka na kuiendea moja ya kompyuta iliyo jirani naye ndani ya chumba hicho cha mawasiliano.
Jioni hiyo Kamanda Amata alifanikiwa kupata ndege ya shirika la Ethipian Airline ambayo ilimtaka kuondoka mchana wa saa sita wa siku inayofuata. Haikuwa mbaya sana kwake, cha muhimu tu ni kuwa alitakiwa kufika katika nchi hiyo na kumsaka Martin Gupter na watu wake.
“Naomba uendelee kuwachunguza watu hawa unipatie majina kamili, kama ingewezekana basi tungeweza kujua hata ni wapi katika huo mji wapo maana inawezekana wasiwepo kabisa hata Sierra Leone…”
“Kivipi?”
“Kwa sababu kama wao ni wajuvi wa mambo haya ya assassination, kwa kuwa wamefeli kwenye jaribio lao basi wanatakiwa wabadili mbinu zote zinazofuata, kwa maana ukikosa kutimiza lengo maana yake ni kuwa umeongeza uwezekano wa kukamatwa hivyo lazima ujifiche mahala pengine…” Amata akamwambia Chiba.
“Aaaaaaa mi sitaki wafanye hilo!”
SIERRA LEONE
KATIKA MJI MDOGO wa Waterloo, kando ya mto mkubwa wa Lofa, kulikuwa na jumba kubwa sana la ghorofa tatu ambalo lilijengwa katika ubavu wa mlima. Jumba hili kama ungelitazama ukiwa juu yam lima ungeliona ni la kawaida yaani si ghorofa, na kama ungekaa mtoni, maana yake bondeni ndipo ungeona kuwa ni ghorofa. Wakazi wa jumba hili walionekana mara chache sana, zaidi nji wafanya kazi wa bustani, shamba na mambo mengine, hawa ndo haswa ungewaona kuanzi asubuhi mpaka saa tisa alasiri, zaidi ya hapo huwa kimya na upweke wake.
Hakuna aliyemjua haswa mmilikiwa jumba hili, wala kumwona, japo tu walipata tetesitetesi kuwa ni malia ya tajiri mmoja wa Kiarabu ambaye yupo nchini humo kama mfanyabiashara mkubwa mwenye utajiri wa mafuta huko Saudia na sasa alikuwa tayari ameanza kuchimba mafuta katika Bahari ya Atlantiki.
Katika miezi sita hii wafanyakazi walishuhudia wageni wapya watatu; wanaume wawili na mwanamke mmoja, hawakuhoji kwa sababu hayakuwa yakiwahusu. Walikuwa wakikaa katika jumba hilo na kuondoka kisha wangekuja tena, vivyo hivyo.
Martin Gupter, Amanda Keller na Frederick waliweka kambi katika mjengo huu, wakipanga mambo yao ya siri na kuweka mipango yao ya kufichika ndani yake. Mkataba mnono wa tajiri Jaffery Bakhari uliwataka wajitenge na dunia kwa miezi takribani nane hivi ili wakamilishe misheni hiyo ambayo waliita ‘Secret Assasination’.
Mara tu baada ya kuikamilisha kazi ambayo almanusura iwagharimu maisha yao na kutibua kila kitu, walikuja tena katika jumba hilo ambalo Kamanda Amata alimwambia Chiba kuwa watakuwa wamefanya kosa kubwa kama watarudi Waterloo, na ndivyo walivyofanya.
Katika sebure kubwa yenye kila samani ya thamani watatu hawa waliketi wakijimiminia vinywaji vikali kwenye matumbo yao na kuzungumza hili na lile
“Nyie hamjanielewa,” Martin akawaambia wenzake.
“Si kwamba hatujakuelewa, ipo hivi, kushindwa kumuua Rais wa Gambia ni kupunguza usalama wetu, huwezi kujua ni nguvu gani watachukua kututafuta, hatukupaswa kurudi hapa,” Fredy akamwambia Martin.
“Ndo maana nimesema hamjanielewa, nilitaka turudi hapa makusudi kwa sababu kama watatuma mtu au watu kutuchunguza tulipo, na kama wamepata information yoyote juu yetu basi watakuja hapa na sisi itabaki kuwazika mmoja baada ya mwingine ndani ya kaburi letu. Cha kufanya ni kuweka tayari watu wetu katika maeneo myeti,” akawaambia.
“Umesomeka!” Amanda akajibu, “Na nina wasiwasi sana na Tanzania, hawa wanaweza kuamua kulivalia njuga…” akaongeza kusema.
“Of course, sasa inabidi tuwapate watu wote hatari wa Tanzania, inawezekana wakatuma mmoja wa hao, Fredy fanya hiyo kazi mara moja,” Martin akatoa amri na Frederick akaingia kazi na kuanza kuusaka mtandao wa serikali ili tu aweze kupenye ndani na kuufikia idara ya usalama. Mara simu ya Martin ikaanza kuita, akainyakua na kutazama, namba haikujionesha, hivyo hakujua ni nani anayepiga, akaifyatua na kuiweka sikioni. Akazungumza na mtu wa upande wa pili kama dakika kumi hivi, ni sura yake tu iliyokuwa ikibadilika badilika iliyowapa ishara Amanda na Fredy kuwa taarifa anayoipokea ni hatari. Baada ya mazungumzo hayo akakata simu na kuitupia kochini.
“Vipi?” Amanda akawa wa kwanza kuuliza huku Fredy akaiachana na ile laptop na kuwa tayari kusikiliza.
“Habari mbaya, yatupasa kuwa tayari na makini, tunaweza kuvamiwa any time…”
“…mbona sikuelewi…”
“Mambo yameanza Angola, Joao ameuawa, Oliviera ameuawa, yule mshenzi Costa ametoroshwa, na kisiwa cha Ilha kimeteketezwa kwa moto. Aliyeyafanya hayo inasemekana ni spy kutoka Tanzania, na kabrasha la S.A amelichukua…” Martin akaeleza.
“Mama yangu!” Amanda akang’aka, “inabidi tupange mbinu mpy a ya kujikinga haraka sana,” akasema na kabla hajamaliza mashine ya nukushi ikaanza kutoa ukulele wa kuashiri kuwa kuna jumbe unaoingia. Kweli, picha kubwa ya A4 ikajitokeza, Amanad akainyakua na kuitazama kisha akampa Martin na kisha Fredy, kila mmoja akaitazama kwa dakika au sekunde anazoona yeye zinamfaa.
“Huyu, huyu, huyu, nataka afie kwenye hili kaburi hapa,” Martin akasema.
Amanda akazidi kuitazama ile picha ya kijna arijali mtanashati aliyevalia suti na macho yake yakiwa yamefichwa kwa miwani.
“Amejitambulisha kwa Pereira kama Mr. Spark…” Martin akasema.
“Haina tabu tunamkaribisha Waterloo,” Fredy akajibu kauli ya Gupter na kuendelea kazi yake mtandaoni, safari hii badaal ya kuuchunguza ule mtandao wa serikali, sasa akawa anatafuta data zaidi za Mr Spark kama angeweza kupata.
“Ana bunduki yangu huyu,” Martin akasema, “ndiye binadamu wa kwanza aliyeumbwa na Mungu kufanikiwa kupata bunduki yangu, haiwezekani, unafikiri nitafanyaje kazi bila mtoto wangu? Tuna miezi miwili tu iliyobaki tukamilishe mkataba na Jaffery tukamate pesa nzuri ya kutuwezesha kumiliki Dreamliner, ila huyu anataka kutuharibia, ni nani huyu? Nitamzika akiwa hai hapa chini ya nyumba hii akakutane na wajomba zake,” Martin akasema huku akionekana wazi kuwa tayari kilevi kimeshaanza kumchukua.
“Naenda kulala, nikiamka tutapanga kazi ya siku tano tu ya kumuua mshenzi huyu!” akasema na kuipiga bilauri ukutani kisha akaingia zake vyumbani. Amata na Fredy wakabaki wakimtazama tu, hawakuwa na la kufanya juu ya hili. Mwanamke huyu wa kizungu, akajitupa kitini na kujiegemeza akionekana kusawajika uso kwa mawazo ya dharula yaliyomkuta.
SOMALIA
Katika Jiji la Mogadishu, ndani ya hoteli kubwa ya kisasa, Jaffery Bakhari alikuwa na kikao kizito kilichojumuisha watu wengine kama watatu hivi ukiachana na vijana wake watiifu. Dhumuni la kikao hiki lilikuwa ni kujadili musatakabali mzima wa kampeni yao.
“Tumekwama! Labda niseme hivyo,” Jaffer akawaambia wenzake.
“Gupter alituhakikishia kuwa kila kitu kitakwenda sawa, sasa nini kimetokea?” Mjumbe mwingine akauliza swali lakini hakuna aliyetoa jibu.
“Anyway, kampeni yetu haiwezi kusitishwa, itaendelea, cha muhimu ni kuiongezea muda. Kwa kuwa tulishawaangusha wawili, wakabaki wawili, nimeongeza mwingine na huyu ndiye hasa amekuwa mwiba kuliko nilivyotegemea,” Jaffer akasema.
“Nani?”
“Rais wa Tanzania. Mambo yote yameanza kuharibikia kwake, nimemweka kwenye orodha na kumpa kazi Gupter mwenyewe,” akawaambia swahiba zake nao wakabaki kutikisa vichwa juu chini.
“Kwa hiyo kutangaza uhuru wa Somalia ya Kusini hakutaweza kuwa kama tulivyopanga, sivyo?” akauliza mzee mmoja mwenye nywele nyeupe kuanzia kichwani mpaka kidevuni. Afya yake ilionekana njema kipesa ijapokuwa alikuwa akitembezwa katika kitimwendo.
“Tunahitaji uhuru wa Somalia ya Kusini haraka iwezekanavyo,” mjumbe mwingine akaongeza, “hatuwezi kubadili taratibu zet bali tuwaambie tuliowapa kazi kuwa tunahitaji mpaka kufiikia tarehe hii iwekama tulivyopanga hata kama ni kuwaua wote kwa siku moja sawa tu, wataomboleza na baadae watatulia sisi tutaipata nchi yetu,” akasema tena.
Kikao kilikuwa kirefu lakini mwisho wa yote walifikia muafaka na kukubaliana kumuondoa kwenye orodha yule wa Tanzania.
“Wakikataa kutupatia nchi yetu kikatiba basi jeshi letu litaingia katika mapambano mpaka tutakapoikomboa,” Yule mzee akasema tena na wote wakaafiki.
“Lakini hawa Watanzania lazima tuwatazame kwa jicho la pekee maana wametuharibia kabisa mpango…”
Baada ya saa kama tano hivi kupita, kikao kikamalizika na kupangwa tena pindi kazi ikikamilika. Watu hawa watatu wenye unasaba fulani walijiunga na kuwekeza pesa nyingi kwa minajiri ya kuikomboa ardhi ya Somalia ya Kusini kwa madai kuwa ni mali ya babu zao. Kutokana na hilo walipanda mbegu miongoni mwa watu wazawa wa upande huo kuwatenga na kuwanyanyasa wale wenye asili ya Kaskazini. Hali hii ikaleta mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mpaka Umoja wa Nchi za Afrika ukaamua kuingilia kati. Viongozi wengi wakapiga kelele juu ya hali hiyo hasa walipogundua kuwa wa-Kusini hao wanataka ardhi yao na kujitenga na Kaskazini.
Tangu waanze harakati hizi, wajumbe hawa wa juu kabisa wamekutana mara tatu tu, na wao ndiyo huwa na maamuzi ya mwisho, hiki kifanyike na hiki kisifanyike. Mara hii walikataa kabisa kubadili muda wa kutangaza uhuru wa nchi yao mpya. Kama pesa kwao hazikuwa tatizo, waliwekeza na kuwekeza, tayari walikwishapanga serikali, wakaunda jeshi na kubakisha tu kutangaza uhuru, hata maboksi yaliyojaa bendera mpya yalikwishawasili.
“Kumbukeni, tuna miezi mitatu tu, wakatae au wakubali, na wakitaka usalama wakubali, wakitaka damu imwagike wakatae,” Jaffer akamaliza na kuagana na wenzake na kujihakikishia kuimaliza kazi iliyobaki kwa miezi hiyo miwili.
DAR ES SALAAM
USIKU huo huo, Kamanda Amata alikuwa bize kitandani na mpenzi wake Gina, kilichokuwa kikiendelea hapo sina haja ya kukwambia. Hata kama ungesikia miguno ungeelewa maana yake ni nini. Kila mmoja alikuwa akimwonesha ufundi na utundu mwenzi wake. Baada ya muda wa kutosha wa burudani hiyo kila mmoja akabaki hoi.
“Hapo sasa tumeagana,” Gina akamwambia Amata.
“Umefurahi?”
“Siyo kufurahi tu, nimeridhika pia, yaani hata ukikaa huko mwaka mmoja mi sina hamu kabisa,” akasema.
“Haya bwana!” Amata akajibu na kukurupuka kitandani, akaketi na kuegemea besela la kitanda.
“Gina, unamwamini Mungu?”
“Yes!”
“Uniombee, maana kila nikifikiria hii safari yangu moyo wangu unazizima kwa woga,”
“Usihofu Amata, utakwenda na utarudi ninaamini hivyo…” Gina akamweleza.
“Aaaaa sijui, nahisi kama hii ni safari yangu ya mwisho….”
“Usiseme hivyo dear, hatari ngapi umepona, itakuwa hii? Si mimi tu wala Madam S, ila Watanzania wote wanakuombea, wanajua kuwa u mtetezi wao hata kama hawajawahi kukuona,” Gina akamfariji kwa maneno matamu.
Kamanda, akanyanyuka na kuliendea kabati kubwa la vipodozi ambalo katikati lilikuwa na kioo kirefu.
“This is Kamanda Amata, Amata Ric, TSA 1, nahisi kabisa kuwa muda si mrefu nitakiacha cheo hichi…”
“We unaongea maneno gani leo?” Gina akang’aka na kuinuka kumfuata Amata pale pale aliposimama.
“Usiwaze, go and kill them all… nauamini mkono wako,” akampet-pet na kisha kumrudisha kitandani na kuendelea na burudani zao.
SAA SITA MCHANA
Siku iliyofuata
Gina aliegesha gari nje ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, kutoka ndani ya gari hilo akashuka Kamanda Amata na kufuatiwa na Chiba. Gina alipotoka garini, wote watatu wakaongozana na kuingia ndani uwanja huo sehemu ya kuondokea na kuhakikisha wamemwacha Amata akiwa tayari ameshauvuka mlango wa ndege na kuingia ndani. Mara baada ya kuupunga mkono wa kwaheri, Gina akajikuta akiangusha machozi.
“Unalia nini?” Chiba akamuuliza.
“Ingependeza ningekwenda na Amata…” akajibu
“Hapana, hiyo kazi si levo yako mwache yeye aende na wewe utabaki hapa,” Chiba akamwambia huku akimshika mkono na kutoka naye nje mpaka kwenye gari lao. Ndani ya gari Chiba akaketi nyuma ya usukani kwa maana alijua wazi kuwa mwanadada huyo hawezi tena kufanya kazi hiyo kwani bado alikuwa akilia kwa vikwifukwifu.
IKULU YA TANZANIA
Wakati yote hayo yakiendelea, Madam S alikuwa na mazungumzo ya falagha na Mkuu wan chi ndani ya jingo tukufu la Ikulu ya Tanzania ambapo ndipo ofisi na makazi ya Rais. Hakukuwa na na lingine linalozungumzwa zaidi ya mkakati wa kuwasaka Gupter na wenzake kama ambavyo Mwenyekiti wa AU amewataka kufanya hivyo.
“Unaamini peke yake anaweza?” Rais akamuuliza Madam S.
“Kwani ni mara yakwanza kwa yeye kufanya kazi kama hii?” Madam naye akauliza swali.
“Aaaa noh! Ni wewe unayewaju vijana wako vyema, si mimi…”
“Mpaka sasa, kazi imeshaanza, kitendo cha kuwapotezea malengo yao na kushindwa kumuua mlengwa, tayari ni kazi kubwa, kwa vyovyote watakuwa wameshtuka na wanahitaji kujipanga upya,” Madam akasema, “kwa upande wa Angola keshagundua mpaka ni nani anayemtilia shaka kuwa amehusika kwa namna moja au nyingine kutimiza mauaji yale…”
“…alikwenda Angola?”
“Ndiyo, mbona karudi jana tu!” akajibu
“Na huko unasema – wapi sijui wapi…”
“Sierra Leone…”
“Yes!”
“Yaani tunavyoongea tayari yupo hewani…”
“Good ndiyo maana nakupenda, yaani unajua kupanga mambo yako mwenyewe…”
Mazungumzo, mikakati, vikapangwa ndani ya jengo hilo, Mkuu wa Nchi akakubaliana na Madam S juu ya maswala mengi ya kusalama nchini. Akapokea mapendekezo ya mabadiliko na mambo mengine mengi. Saa tisa mchana wakamaliza kikao hicho ‘nyeti’ na kila mmoja kurudi katika majukumu yake.
WATERLOO
MARTIN Gupter alizinduka usingizini, akaketi kitandani kwa dakika kadhaa kasha akachukua simu yake iliyokuwa juu ya mezxa ndogo na kuiangalia kama kuna ujumbe au mwito wowote uliofika. Hakuwa mbali na hisia zake kwani alama ya bahasha ilikuwa ikiwakawaka juu ya kioo cha simu hiyo kubwa. Akaifungua na kuusoma ujumbe huo, mara baada ya hapo akahisi ubaridi ukimpenya kuanzia utosini mpaka unyayoni, akainuka na kuelekea sebuleni ambako aliwakuta Fredy na Amanda wameketi sebuleni wakiangalia TV.
“Jamani, kumekucha!” Martin akawaambia.
Amanda na Fredy wakashtuka na kumtazama Martin, “Nini tena?” akauliza mwanamke huyo.
“Kuna mgeni anaingia usiku huu…”
“Sure?”
“Yes, nimepata ujumbe kutoka Dar, hivyo hatuna budi kutrace, hatutakiwi kumpa nafasi kabisa, maadam kaja, nataka afie kwenye kaburi la pamoja,” Martin akasema, Fredy na Amanda wakatazamana kwa sekunde kadhaa.
“Hakikisheni mnamtia mkononi kabla hajapumua katika Jiji la Free Town,” akaongeza na kuwaonesha picha katika simu yake.
“Ni huyu!?”
“Shenzi sana huyu, huyu ndiye kaharibu mpango wetu kule Tanzania, shetani mkubwa, naenda mwenyewe…” Fredy akasema huku akinyanyuka tayari kuondoka, Amanda naye akafuatia.
“Yaani we tulia, tunaenda kumleta, ndege gani wanasema?”
“Ethiopian Airline, inaingia saa sita usiku huu, mna saa kama mbili hivi,” Martin akawaambia.
“Usijali tunamuwahi na tunakuja naye hapa!” Amanda akaongeza kusema wakati akijiweka sawa kwa safari. Nusu saa iliyofuatia, Amanda na Fredy walikuwa tayari barabarani kuelekea Jijini Free Town, m
UWANJA WA NDEGE WA LUNGI
FREETOWN
Saa sita usiku, ndege iliyombeba Kamanda Amata ikakanyaga ardhi ya jiji hilo, na baada ya hpo ikaegeshwa vyema kabisa mahala pake na abiria wakaanza kuteremka mmoja mmoja. Watu kama hawa, wanaintelijensia daima hisia kali au hupenda kuita mlango wa sita wa fahamu huwaongoza katika mambo mengi, akiwa bado ameketi kitini na abiria wengine wamekwishaanza kuteremka, Kamanda Amata alihisi kwa vyovyote kuna wenyeji wanaomsubiri.
Ili wanione vizuri ngoja niwe wa mwisho! Akawaza huku akinyayuka na kushusha mkoba wake kutoka kwenye keria ya ndani, akaupachika begani na kuvuta hatua akiwa kama mtu wan ne hivi kutoka mwisho. Mataa ya kupendeza ya jiji hilo yakamlaki, kana kwamba yanamwambia ‘karibu katika jiji la dhahabu’.
Akiwa katika foleni ya ukaguzi wa vibali vya kuingilia nchini humo, Amata akawa akiangaza huku na huko kuangalia kupitia vyoo vikubwa kabisa, kama kuna anayemhisi kumsubiri. Naam macho yake yakagongana na Amanda, japo hakuwahi kumwona viozuri huko nyuma zaidi ya picha tu ambayo alikuwa ameiweka akilini, tayari nywele zake zilisisimka akajua, tayari.
Nimeshapata mrembo! Akajisemea huku akimkabidhi pasipoti yake mwanadada wa uhamiaji.
“Karibu sana Sierra Leone!” Yule mwanadada akamwambia huku akimkabidhi pasi’ yake.
“Asante kwa ukarimu wako, nimekaribia,” Amata akajibu na kuitia mfukoni pasipoti yake, akainua macho kuitazama tena pale alipo Yule mwanamke, hayupo. Kwa kitendo hicho akajua sasa kazi imeanza kwa maana hakujua hata ni wapi mwanamke huyo kaenda, hivyo ni ngumu kujua atatokea upande gani. Akameza funda la mate, na kuvuta hatua ndogo ndogo kuelekea nje, hatua mbili tatu hivi kabla hajafika katika mlango huo, akamwona mtu ambaye akamhisi vibaya. Amata akaingia upande wa kushoto, akapita kando ya maboksio mengi yaliyolundikwa hapo, akavuta hatua za haraka haraka na kuliacha lile eneo, akajikuta kwenye bohari kubwa ya cargo. Kutoka kule akatafuta wapi panaweza kuwa na mlango wa kuendea nje, kwa bahati akauona, akenda na kuufungua, ulikuwa umerudishiwa tu, akaingia na kukutana na ngazi zikiteremka chini. Hakuuliza wala kufikiri, akashuka nazo mpaka chini kabisa, huko akatembea kwa hadhari kubwa sana akihofia kamaera za uslama kumnasa na kumletea shida kwa walinzi. Bahati mbaya au nzuri hakukuwa na hata moja.
‘Emergecy Exit’. Akaona kibao kimeabndikwa hivyo.
Ningeshangaa! Akajisemea moyoni na kuingia hapo palipowekwa mshakle wa uelekeo, milango miwili mitatu akajikuta nje, upande mwingine kabisa wa uwanja.
Mtanitafuta kwa gharama! Akasema tena na kuendelea na safari, bahati nzuri hakukutana na mtu yeyote mpaka alipofikia seng’enge zilizotenganisha eneo ambalo watu wanaruhusiwa, yaani maegesho na shughuli nyingine muhimu na lile ambalo hairuhusiwi kwa mtu mwingine kuingia. Akatazama huku na huko, akaona walinzi tu wakiwa mbali kabisa, akaendelea kutalii kwa macho hakuona kitakachomzuia kufanya atakalo. Kutoka katika mkoba wake akachukua mkasi mdogo lakini wenye uwezo wa kukata waya, akafanya hivyo na kutengeneza tundu kubwa tu, akapita na kupotelea kwenye magari mengi yaliyojipanga hapo na kujaribu kutafuta kama anaweza kumuona yule mwanamke.
Kwa upande wa Amanda na Fredy walijikuta bado wanasubiri mgeni wao atoke lakini haikuwa hivyo.
“Mbona hatoki?” Fredy akauliza.
“Mh! Sijui ila nilimuona kwenye foleni na aliyekuwa mbele na nyuma yake wameshatoka nje,” Amanda akajibu.
“Ametupiga chenga, keshagundua kuwa tupo!” Fredy akasema.
“Come on!” Amanda akatamka huku akitoka eneo lile na kuchukua simu yake, akampigia Martin na kumpa taarifa hiyo.
“Yupo hapo hapo, hakikisheni mnampata au mnamuona, hata tukijua tu ni wapi anafikia kwetu irakuwa sawa,” Martin akawaambia nao wakaendelea kusaka hapa na pale kwa kutazama.
Mara baada ya simu hiyo, Fredy na Amanda wakatawanyika na kuendelea kuangalia hapa na pale labda wangeweza kumuona lakini haikuwa hivyo.
“Tunafanyaje?” Amanda akamuuliza Fredy mara walipokutana baada ya kutafuta kila mtu upande wake.
“Huyu mtata, sasa tukisema tuondoke, itakuwa haina maana ya kuja, tukisema tukae pia tunaweza kupoteza muda,” Fredy akamwambia Amanda.
“Anyway twende kwenye gari, tukaone cha kufanya….”
“Aaaaaaa nimepata mbinu ya kumnasa kama yupo hapa bado,” Fredy akamwambia Amanda.
“Enhe…”
“Twende kwenye gari kisha tuondoke, kama yupo na katugundua, atatufuata ndipo tutampata…” Fredy akatoa wazo, likaafikiwa na wote wakaingia garini.
Kamanda Amata akatamani kucheka lakini akajikaza akiwa sambamba na ua kubwa lililowekwa kama urembo katika eneo hilo, vivuli vya vichaka vya ua hilo vilimfanya asionekane kirahisi na jinsi alivyojiweka. Michezo hii ya kujificha au kujipoteza asionekane alijifunza huko Japan wakati akichukua mafunzo ya Ninjutsu.
Lazima nitumie mbinu za hali ya juu kuwakwepa hawa jamaa! Akajisemea moyoni wakati akiwatazama Fredy na Amanda wakiingia maegeshoni na kuingia ndani ya gari mojawapo ambao Amata alikuwa akiliona vyema. Kutoka waiposimama wakati wakiongea mpaka alipokuwa Amata ni kama mita nne hivi, ni ua kubwa tu lililowatenganisha, hawakuweza kumwona Amata kutokana na kutumia kivuli kujificha.
Baada ya jamaa hao kutulia garini, Amata akatoka pale na kutembea kwa mwendo wa paka mpaka kwenye magari mengine ya nyuma, akachukua kifaa chake cha kufyatulia vitasa vya gari, hakuchukua hata dakika, tayari alikuwa ameketi kwenye gari asiyeijua hata mmiliki wake, akafunga mkanda huku macho yake yakiwa yanalitazama lile analolilenga.
Fredy akawasha gari na kuliondoa, Amata akasubiri kama dakika hivi nay eye akawasha na kuwafuata.
“Nitafanya kama mlivyofikiri!” akasema kwa sauti kana kwamba kuna mtu anayeongea naye. Baada ya kuicha barabara itokayo uwanja wa ndege na kukunja kushoto kuifuata ile ya Airport Ferry. Kutoka yeye na ‘kina Fredy kulikuwa na gari kama tano hivi katikati.
Amanda akatazama kwenye kioo kisha akakaa sawa kitini, Fredy naye muda wote alikuwa akitazama kioo cha ndani na kile cha upande wake.
“Vipi?” Amanda akauliza.
“Sioni kama anatufuata!” akajibu.
“Sasa atakuwa kaenda wapi mshenzi huyu?” Amanda akauliza.
“Huyu si wa kuchezea, anaonekana na mjuzi sana wa mambo,” Fredy akajibu.
Wakiwa wamezama kwenye mazungumzo, gari aliyokuwa anaendesha Amata, ilikuwa ikipita kwenye upande mwingine wa barabara hiyohiyo, taratibu alikuwa akiyaovateki magari ya upande ule mwingine ambao Fredy alikuwa akiendeshea. Alipolifikia gari la akina Amanda, akaweka la kwake sambamba kabisa, wakawa wakienda pamoja.
Ghafla macho ya Amanda yakagongana na mgeni wao.
“Shiiiit!!!!” akapiga ukulele na Fredy akageuka kutazama.
“Come on!” naye akajikuta akitamka kabla hawajatahamaki, Amata akayumbisha gari lake na kulipigiza kwa nguvu kwenye lile la akina Amanda. Akahakikisha analisukuma mpaka nje ya barabara na kugonga ukingo wake. Baada ya ukingo ule kuvunjika, Gari walilopanda Fredy na yule mawanamke likaacha barabara na kutoka nje likagonga nguzo ya taa na kuanguka vibaya. l
“Fredy! Fredy!” Amanda akaita kwa shida, Fredy akatoka kwa kutumia kioo cha mbele, akamtoa Amanda ambaye alikuwa na michaniko ya kutosha usoni mwake. Haraka sana, Fredy akamwacha Amanda chini, akachomoa bastola na kuliwahi gari la Kamanda ambalo nalo liliishi kugongo kizuizi imara cha barabara hiyo kubwa na kusababisha ajali kubwa. Fredy akalifikia na kuweka bastola yake tayari huku usoni mwake akitiririkwa na damu. Kutahamaki, Amata hayupo garini, akatazama huku na kule hakumwona zaidi ya madereva wa magari mwngine waliokuwa wakitukana ovyo.
Kamanda Amata tayari alikuwa upande wa pili wa barabara, akajibana karibu na ukuta wa kutenga barabara ya magari na watembea kwa miguu, akachungulia kwa chati na kumwona Fredy akaihangaika na yule mwanamke anavyomwacha na kuja kwenye gari alilokuwamo yeye, anavyoshangaa shangaa mpaka anaamua kurudi garini.
Ningeamua kuwaua ningewaua sasa wote wawili au hata kuwakamata, lakini wakati wenu bado nyau nyinyi! Amata akaongea mwenyewe moyoni mwake wakati akiwashuhudia wawili hao wakakokotana na kuingia kwenye taksi moja iliyosimama hapo. Baada ya wao kuondoka, Amata akaruka ule ukuta na kuliendea lile gari kabla askari hawajafika, akalifikia na kupekua haraka haraka hapa na pale. Hakupata vingi ni kadi ya gari na kadikazi moja ikiwa juu ya kiti. Mara akasikia ving’ora vya magari ya polisi vikija upande huo. Akaingiza mkono katika mkoba wake akatoa kijichupa kidogo mithili ya cha dawa ya minyoo akakirushia ndani ya gari lile kisha yeye akaanza kutembea taratibu kuelekea upande mwingine. Baada ya hatua kama mia hivi akachukua simu yake na kuwasha tab maalum akaminya ‘kitufe tepe’ kilichoandikwa ‘Fire’, mlipuko mkubwa ukatokea na lile gari likapaishwa juu juu na kutupwa chini likiendelea kuwaka.
HOTEL YA SWISS SPIRIT
HOTELI YA KAWAIDA kabisa iliyojengwa katika jiji la Freetown, ndiyo ambayo kijana huyu aliichagua kama sehemu yake ya mapumziko kwa usiku huo kiwezekana na siku nyingine ambazo atakuwa mjini hapo. Bahati pekee aliyokuwa nayo ni kwamba kila anapoingia hukaribishwa na mwanamke mrembo katika meza ya mapokezi.
“Chumba kipo, tena kimebaki kimoja nafikiri kilikuwa kwa ajili yako,” mwanadada huyu akamwambia huku akiweka vizuri kipanya cha kompyuta yake, “Pasipoti tafadhali…” akamwambia. Amata akaingiza mkono katika mfuko wa koti lake na kuchomoa pasipoti akampatia. Yule mwanadada akaifanyia kazi kisha akachukua na kadipesa yake akaichanja kwenye kifaa maalum, Amata akaingiza namba zake za siri na kisha akarudishiwa vitu vyake.
“Karibu Swiss Spirit Mr. Maturin!” akakaribiswa na mwanadada yule na sekunde hiyohiyo akaja kijana mwingine akachukua mizigo na kutangulia nayo.
“Asante sana, nafurahi kukaribishwa na kiumbe mrembo kama wewe, hakika Mungu bado hajachoka kuumba na isitoshe ana sampuli mpya ya udongo…”Amata akamjibu huku akimpa lile tabasamu lake hadimu sana ambalo hulitoa kwa nadra sana. Macho ya wawili hawa yakagongana na kushikana kama sekunde tano hivi. Yule mwanadada akashusha pumzi ndefu na kuinama chini kidogo.
“203!” akatamka.
“Asante sana, lunch kesho…” Amata akaanza ubembe.
“Saa saba kamili….”
“A aaaa najua, wapi? Ikiwezekana mi na wewe!” akamwambia huku akijivuta tayari kwa kuondoka.
“Mmmmm wewe! Wacha nihudumie wageni kwanza…”
“Halafu…”
“Nenda bwana!” yule mwanamke akamwambia Amata naye akaondoka mezani hapo taratibu kuelekea katika chumba alichokwishaelekezwa.
Mlangoni mwa chumba hicho, akamkuta kijana yule aliyempokea na kutangulia akiwa amesimama nje, Amata akafika na kufungua mlango, kisha akamwacha yule kijana amsaidie kuweka begi lake na baadae yeye mwenyewe akaingia ndani na kusimama katikati ya chumba hicho. Hakikuwa kidogo wala kikubwa bali cha wastani chenye kitanda kikubwa, kiti cha vono na kijimeza kidogo, pembeni mwa kiti hicho kwenye kona kuna nguzo ya taa hafifu iliyokuwa ikiwaka. Akatazama kila kona kwa macho tu, kisha akainua mkono na kuizungusha saa yake kwa namna fulani na kusubiri kwa sekumde kadhaa, kimya. Alipohakikisha usalama wa chumba upo akavuta kiti kingine ambacho kiikuwa kwenye dressing table na kukivuta mpaka mlangoni, pale akakiweka na upande wa mgongo akauweka chini ya kitasa kana kwamba kimepimwa urefu, kikakaa sawasawa n kukizuia kitasa kisiweze kufunguka. Kisha akavua koti lake na kulitupia kitandani, akachomoa ile kadi ya gari na kusoma ilikuwa imeandikwa kifaransa tu. Hakuona shida, akachukua jina la mmiliki na anwani yake kisha akahamia kwenye simu yake na kuanza kutafuta mtu huyo anaweza kumpata wapi.
Laurent Yonibana, Western Province 25, Domatou Road! Akaandika kwenye kijikaratasi kisha akachukua ile kadikazi aliyoiokota mle garini akaigeuzageuza na kuisoma maelezo.
Jean de Pierre! Akasoma na kutazama namba za simu na ofisi gani anapatikana.
“Nitakuwa wageni wenu kesho,” akasema na kujiweka tayari kwa kuoga na kupumzika.
WATERLOO
Martin Gupter alikuwa akiendelea kupiga maji tu huku akusubiri simu yoyote kutoka kwa washirika wake huku akilini mwake akifikiria tu ni jinsi gani ambavyo atamwadhibu adui yake pindi tu akiletewa. Akiwa katika mawazo hayo simu yake ikaitwa kwa fujo, akainyakuwa na kutazama, Fredy, akajikuta moyo ukimwenda mbiyo.
“Safi sana Fredy! Umemtia mkononi?” akamuuliza kwa jazba kuu.
“Kumtia mkononi, siyo rahisi namna hiyo, keshatuumiza vibaya hivi hapa tupo, 5 Point Clinic kwa matibabu,” akamwambia. Martin akarukaruka kwa hasira, akasimama wima na kuongea na Fredy akitaka kujua kulikoni mpaka mtu huyo awazidi ujanja. Akatoka nje ya nyumba hiyo na kuingia garini, akawasha na kuondoka kuelekea Freetown ili kuwaona wenza wake.
Fredy na Amanda walikwishapata matibabu, alfajiri ya siku hiyo Martin aliingia kwenye Clinic hiyo akiwa kafura kwa hasira.
“Que c’est il passé?” (kumetokea nini?) akamuuliza Amanda, na mwanamke huyo akamweleza kila kitu. Martin alishikwa na hasira zaidi, akatembea huku na huko kisha akatulia huku mishipa ya kichwa ikiwa imemdinda kwa hasira.
“Je vais le tuer!” (nitamuua!) akasema huku akiwa ameshika tama na kukalia kitanda cha mgonjwa. Kisha akamtazama Fredy, “washa kamera zote za siri!” akamwambia kisha akasimama na kutoka nje huku akifuatiwa na vijana hao, wakaingia garini na kuondoka zao. Martin hakwenda mbali, breki ya kwanza ni eneo ajali ambako hakukuta gari lolote mahali hapo zaidi ya majivu tu. Akaendelea mpaka kituo cha polisi na kuripoti juu ya ajali hiyo ndipo akaambiwa hata gari lenyewe limekwishateketea kwa moto. Martin akafikiri kwa nukta kadhaa kisha akatazamana na askari huyo macho kwa macho. Maswali yake yote akajibiwa na alipowaambia kuwa walikuwa wakifunkuzwa na jambazi akakubaliwa hivyo polisi wakaingia katika kazi ya kumsaka jambazi huyo, haya yote ylifanyika tu kwa sababu mlalamikaji ni Mzungu na si vinginevyo.
Baada ya kukiacha kituo hicho, Martin akagesha katika amgahawa mmoja mjini hapo kwa kupata kifungua kinywa na mazungumzo machache.
“Lazima afe taratibu, cha kufanya sasa ni kujua vipi tutampata!” akawaambia Fredy na Amata.
“Sawasawa, ila inabidi tujiweke vyama huyu jamaa anaonekana ni mjanja sana,” Fredy akasema.
“Atakamatika tu, nakwambia atakamatika tu sasa nimeamua, hawezi kufanya sisi watotot wadogo!” Amanda akalalamika huku akifunga nywele zake vizuri.
“Yeyote anayefuata nyayo hizi, yupo hatarini, tumpate huyu tumchanganye na yule bwege mwingiene kisha tuwazike wazima,” Martin akawaambia.
“Ndiyo dawa yao!” wakamjibu.
Martin akaondoa gari taratibu na kuingia barabarani, lakini ghafla simu yake ikapata uhai, akaiinua na kuitazama, akampa Fredy aasome ujumbe huo.
“Swiss Spirit Hotel!” akasema.
“Basi mchezo umeisha, mpigie simu Imlan Marikante, mwambie tuonane Sea Port leo saa nne!” Martin akatoa maagizo na Fredy akafanya hivyo.
Saa nne asubuhi hiyo Martin alikutana na Imlan Marikante katika mgahawa wa Sea Port kwa mazungumzo mafupi huku akiwa kawaacha Fredy na Amata garini wakajadilialiana hili na lile.
“Namhitaji huyu mgeni kwa pesa yoyote ile!” Martina akamwambia Imlan.
Martin Gupter na Imlan Marikante walikuwa marafiki wa muda mrefu hasa kwenye kazi nyeti kama hii. Haikuwa mara ya kwanza ila tofauti tu ni kuwa huyu aikuwa akimtaka hai mara zote alitekeleza mauaji tu kwa njia mbalimbali kwa kumtumia kijana huyu huyu kwenye hoteli mbalimbali jijini hapo na pembezoni.
“Kwa nini unamtaka hai?” Imlan akamuuliza.
“Ana mengi ya kulipa, na ninataka afe kwa kuonja uchungu wa kaburi,” akamwambia.
“Sawa, kumpata utaweza, tena leo hii hii, nilimwona akiongez kimahaba sana na mhudumu wa mapokezi pale Swiss Spirit, tunaweza kumtumia yeye akamtia penzini kisha tukamnasa,” Imlan akapendekeza mbinu ambayo Martin hakuifikiria kabla.
“Unafikiri ataweza kumtia mkononi? Maana huyu jamaa nimeshaanza kumsoma, si wa kumkamata kijinga…”
“Martin! Hakuna mkate mgumu mbele ya chai, atakamatika, anda fungu la maana nimsuke yule mwanamke, tena ni vyema akimtoa pale na kwenda naye mahala pengine,” Imlan akasema.
“Sawa!” Martin akakubali na kuondoka na jamaa huyo mpaka benki, akachukua pesa iliyotakata na kumpatia.
“Nakuamini!” akamwambia Imlan.
Wakati huo huo, Kamanda Amata saa nne hiyo alikuwa mbali kidogo na Jiji katika eneo linalojuikana kama Western Province katika Barabara ya Domatou. Mbele yake alismama mzee wa makamo kadiri ya miaka sitini au sabini hivi, aliyechakaa kwa jua la Afrika.
“Unazungumzia gari, Renault Station Wagon?” yule mzee akauliza.
“Ndiyo, kabisa, hili gari bado ni mali yako au?” akamuuliza.
“Hapana hili gari kwangu lilishapotea miaka mingi sana, nimebaki na risiti za manunusi tu basi, we umeliona wapi?” akauliza yule mzee.
“Siyo tu kuliona, limepata ajali nikafikiri waliokufa ni kati ya wanao maana walikuwa wawili,” akamwambia kwa Kifaransa safi. Katika ya ugha chache ambazo Kamanda Amata alizijua kwa ufasaha, nah ii ni mojawapo.
“Ooooo, nashukuru sana kwa taarifa hili gari nilishaibiwa, polisi wamelitafuta sana laki hawakulipa, basi nikanunu jingine!” yule mzee akasema. Baada ya mazungumzo kama ya dakika arobaini na tano hivi, wakaagana na Kamanda Amata akawasha gari lake la kukodi na kurudi mjini.
Saa saba mchana alikuwa mbele ya Clinic ya 5 Point, akaingia kwa hatua fupifupi mpaka mapokezi, akamuulizia anayetaka kuonana naye, akapelekwa. Huyu hakuwa mzee, kijana mshupavu daktari kutokana na jinsi alivyovaa. Baada ya maamkiano, Amata akaiweka ile kadikazi mezani.
“Kadi hii imeokotwa kwenye eneo la ajali jana usiku, tunapenda kujua kama marehemu ni ndugu zako au marafiki!” Amata akamwambia na yule daktari akaichukua na kuitia mfukoni huku akimwangalia kwa makini sana.
“No labda ni wateja tu, maana kuna wateja wangu walikuja hapa jana usiku kutibiwa, wakanambia wamepata ajali mbaya jana usiku, na wao najua kuwa nimewapa hii kadi muda mrefu tu, sasa sijui hiyo ni ajali nyingine au! Maana kama ni vifo hakuna kifo katika ajali hiyo,” yule daktari akamwambia Amata.
“Ooooh Good! Naweza kuwaona?”
“Hawapo wameshaondoka kwani ni mikwaruzo tu hawakuumia sana!” akamjibu. Mara hii Amata akajikuta amekosea kwa jinsi alivyomwingia mtu huyo. Hakuwa na budi kuaga lakini tayari alikwishajua kuwa adui wake watajua ndani ya sekunde chache kuwa alikuwa hapo.
Baada ya hapa wameenda wapi washenzi hawa? Akajiuliza mwenyewe huku akiwasha gari na kuingia barabarani kurudi hotelini. Nusu saa ilimchukua barabarani, akawasili hotelini na kuegesha gari, akashuka na kuingia ndani. Kabla hajazikwea ngazi kwenda ghorofa ya pili ambako chumba chake kilikuwapo, akakutana na yule mwanamke wa jana, mfupi mwenye nyama zilizonona katika mwili wake.
Huwa napenda shepu za mtindo huu! Akawaza huku akizidi kukaribiana naye na kumwona akitabasamu.
“Ndiyo unatoka?” akamuuliza.
“Yes! Nitakuwa off siku mbili kisha nitaingia kazini tena,” yule mwanamke akajibu.
“Kwa hiyo siku mbili zote sintokuona? Mbona utakuta nimekonda mwenzio,” Amata akamwambia.
“Njoo nyumbani kwangu!”
“Namwogopa shemeji,” akamjibu.
“Mbona jana ulizungumzia chakula cha mchana nyumbani kwangu? Hukujuan kama kuna shemeji yako?” yule mwanamke akamwambia, “Bahati yako ni leo tu, ukiikosa utajutia,” akangeza kumwambia huku akivuta hatua kama anaondoka.
“So?” Amata akamtupia swali.
“Kama una mambo mengi basi wakati mwingine,”
“Kwa leo nimemaliza, na hata hivyo nilikuwa nafikiri kupata mwenyeji wa kwenda kuspenda naye jioni hii ili kesho niwe na akili mpya,” Amata akamwambia huyo mwanamke.
“Ndiyo umempata!” akajibiwa. Kamanda Amata akatoa tena lile tabasamu lake la nadra, akampa funguo ya gari na kumtaka amsubiri garini, naye akafanya hivyo. TSA 1 akazikwea ngazi kuelekea chumbani kwake, akafungua na kuingia ndani kwa tahadhari kubwa, baada ya hatu kama tatu nne hivi zilizomfikisha katikati mwa chumba hicho jicho lake likanasa kwenye kile anachokiona kitandani. Akabaki na mbung’ao, ua, waridi jekundu lilikuwa juu ya shuka jeupe kitandani hapo.
“Nini hiki?” akajiuliza huku akiendelea kutazama kitandani, akachukua simu yake
na kupiga picha. Kisha akalichukua na kuliweka kwenye chupa ya maua, akaingia maliwato na kujiweka sawa kisha akabadili nguo na kutoka ndani humo akiwa amechukua mkoba wake. Katika kazi kama hizi hupenda kutumia mkoba huu ambao hata akitoka katika chumba alichopanga huondoka nao akiwa na maana kwamba kuna kurudi au hakuna.
Ndani ya gari alimkuta yule mwanamke akisikiliza muziki wa Richard Bona uliokuwa ukirindima ndani ya redio. Safari ikaanza ikisindikizwa na mazungumzo machache kati ya wawili hao huku wakipigana vikofi vya kimahaba. Mara tu walipowasili nyumbani kwa mwanamke huyo walijibwaga sebuleni kwenye busati la pesa nyingi, mabusu motomoto yakachukua nafasi, dakika kumi, kumi na tano tayari vifua zilikuwa wazi, miili ikakutana na mahaba mazito yakachukua nafasi.
Saa kumi na mbili jioni, Martin Gupter, Fredy na Amanda wakawasili katika nyumba hiyo wakiongozwa na Imlan ambaye alikuwa akipajua vyema kabisa. Wakaegesha gari mbali kidogo na kuteremka wakiwa na silaha mbalimbali, kila mmoja alibeba ile aliyoona inafaa. Hakuna aliyekuwa akiongea na mwenzake, kimya kimya, walizipita nyumba kadhaa na kuielea ile ya yule mwanamke.
Mita chache kabla ya kuifikia, Martin akawasimamisha na kuwapa maneno machache, “Tunatakiwa kuizunguka nyumba, tutavamia na hakuna kuuliza, piga yaani piga mpaka awe unconfotable, kisha tutambeba kuondoka naye. Kama akiwa mkaidi zaidi hatuna budi kumuua tu hapo hapo,” akawaambia kisha wakaendelea kwenda na kugawana; Fredy na Imlan wakazunguka mbele, Amanda na Martin wakazunguka nyuma tayari kwa shambulizi la ghafla.
NDANI YA NYUMBA…
Amata akamaliza kazi pale sakafuni na kumwacha mwanamke yule akiwa vipandevipande kwa mapenzi mazito aliyopewa, macho yalimlegea kiasi kwamba hata hakuweza kuona vizuri kinachoendelea zaidi ya kukumbuka tu burudani aliyopewa na mwanaume huyo, moyoni akakiri kuwa hajawahi kuipata tangua azaliwe.
Amenikuna vilivyo! Akawaza na kuanza kujiokota tayari kuinuka. Kamanda Amata akalifikia jokofu na kufungua ndani, hakuna kinywaji kikali zaidi ya sharubati na vinywaji vitamu. Akapita na kuingia maliwato akajiweka sawa na kutoka.
“Vipi mbona kama unaondoka? Hapa ni kwako vaa taulo tu, kila nikihitaji unanipa maana lleo kwangu ni neema au hujui?” yule mwanamke akamwambia Amata na nukta hiyo hiyo, mlango wa mbele ukafunguliwa kwa kupigwa kwa nguvu nao ukatii na wa nyuma nao vivyo hivyo. Wanaume watatu na mwanamke mmoja wakaingia ndani ya nyumba hiyo. Kamanda akawatazama kwa zamu, akamtambua haraka Imlan na wale Wazungu akawatambua kwa kuwa alikwishawaona picha zao isipokuwa Martin huyu alimkumbuka kwani alimsulubu kidogo pale Dar es salaam.
Yule mwanamke akasimama kando akitetemeka huku akiwa kajisitiri matiti yake kwa kipande cha nguo na huku chini alibaki na nguo ya ndani tu. Fredy akamsukuma kando, naye akaangukia kwenye kochi, akamfuata Amata huku akiwa na mnyororo mkononi mwake, akauinua na kumtandika, Amata akauepa na wakati huohuo akamona Amanda akija kasi, akainua jagi la maji na kumtishia kama anarusha, Amanda akaepa lakini hakujua hila za adui yake. Lile jagi likatua usoni mwa mwanamke huyo na kumchana vibaya. Fredy alijaribu tena pigo lile lile lakini kabla hajafanikiwa Kamanda aliruka kwa ustadi na kumtandika teke la uso, akmbwaga upande mwingine wa chumba. Akaokota ule mnyororo na kukumbana na gongo zito kutoka kwa Martin, akalinasa na mnyororo ule, akauachia upande mmoja na kulifunga. Akamvuta kwake na kumpa kichwa kilichompepesua, akamwendea na kumkamata barabara. Pigo moja toka kwa Imlan likampotezea lengo Amata alipomwacha Martin akachomoka na kisu kutoka kiunoni mwa Martin, alipogeuka akamdidimizia Imlan tumboni kisha akamsindikiza kwa teke zito na kumwacha akienda kufia chini.
Akaruka hewani na kumtandika Amanda teke la shavu, akamng’oa jino moja, Martin akamwahi na gongo lake, Amata akainua kiti na kukinga, kikavunjika katikati. Akajikuta akipigwa pigo moja matata zana ambalo likamshtua pingili za mgongo, akageuka kumtazama Fredi akajikuta akipokea gongo la kisogoni liliompelekea kwenda chini. Amata akatowa yowe la uchungu, akapigwa tena gongo lingine lililomzima chini.
Akajaribu kuinua kichwa, hakuwesa, damu zikaanza kumvuja kisogoni, mchaniko ulionekana wazi kabisa. Amata akafunikwa na giza kuu, akajikuta akihama ulimwengu mmoja kwenda mwingine.
Giza kama giza nene lilinifunika na kuniacha hivyo nilivyo. Siwezi kuelezea nini hasa nilikuwa nakiona katika ulimwengu mpya zaidi ya kelele za watoto wachanga, watu wakiimba nyimbo wakati mwingine nilikuwa nasikia sauti za ndege zikiimba mara mvumo wa upepo na wakati mwingine maji yatirirkayo.
Nikajaribu kuita laziki sauti haikutoka, nikajaribu kuinua mkono lakini haikuwezekana, kando yangu kulikuwa kuna wanyama wane wakubwa tena wanyama wakali wakiwa wamenizunguka huku ndimi zao zikiwa nje kwa kuchoka zikionesha uchu wa nyama ya mwanadamu. Ni ngumu kukwambia ni wanyama gani ila niligundua kuwa ni wakali kutokana na macho yao na meno marefu.
“Kkaaffaa aauu bbaaddoo mmzziimmaa!!??” nikasikia sauti ya mnyama mmoja ikiuliza. Kisha mnyama mwingine akaanza kuninusa na kunilambalamba kwa ulimi wake mchafu unaonuka.
“Hhannaa mmaaiisshhaa mmaarreeffuu,, ttuukkaammttiiee kkaabbuurriinnii,” yule mnyama akanambia. Nikachukuliwa mahali nisipopajua, ambako niliona mambo mengi ya kutisha, pia niliona viumbe kama watu vikitembea kando yangu vikicheka na vingine vikilia. Nikaingizwa ndani ya kitu kama chumba na kufungikwa, huku sikuona chochote zaidi ya sauti ya giza kuu.
WATERLOO
Martin alibonyeza kitufe fulani ukutani na sehemu moja ya sakafu ikafunguka, kisha akawapa vijana wake ishara ya kichwa kuwa wawatumbukize hao watu ndani yake. Mwili wa Imlan ukatupiwa ndani ya shimo hilo, kisha mwili wa Amata nao ukatupiwa humo humo.
“Mwanadamu u mavumbi, na mavumbini utarudi na sijui kama bwana atakufufua siku ya mwisho!” Marini akasema huku akicheka.
“Hash to hash!” Amanda akasema na ile sakafu ikajifunga tena kama mwanzo na zuri la kisasa likafunika juu yake. Kilichofuata hapo ni kugangana kila mmoja alipoumia. Martin akatoa chip mfukoni mwake na kuiweka mezani.
“Hii ilikuwa inawapa taarifa Tanzani mahala alipo,” akawaambia wenzake na kuitia kwenye moto, “sasa watatafuta mpaka wakome!” akasema.
“What’s next?” Fredy akauliza huku akijishikashika mbavu zake.
“Tunaanza mipango ya kutekeleza mpango wetu wa mwisho, mara hii ni two in one,” Martin akawaambia.
Martin na wenzake walitoa taarifa hiyo kwa tajiri wao, nayo ikapokelewa kwa furaha, sasa kilichobaki ilikuwa ni kumaliza misheni yao ambayo iliingia doa siku za nyuma.
DAR ES SALAAM
…REJEA KWA CHIBA NA AMATA…
SAA KUMI NA MOJA jioni ndege ya Ethiopia ilitua katika Uwanja wa Julius Kambarage Nyerere, Chiba na Amata walikuwa ndani ya dege hilo. Machozi yakamtoka Amata alipotazama majengo na uoto wa asili wa nchi yake.
“Home sweet home!” Amata akasema na kujifuta machozi, akainuka kitini na taratibu wakatoka katika ndege hiyo. Badala ya kupitia njia ambayo wageni wengine wanapita, wawilia hawa wakafungua kijimlango kimoja na kushuka moja kwa moja uwanjani na kutembea mpaka chumba cha VIP. Gina alishindwa kuvumilia aliinuka kitini na kumkumbatia kwa nguvu Kamanda Amata hukua akilia kwa uchungu. Madam S akasabahiana na kijana wake, wakajuliana hali, lakini aligundua wazi kuwa Amata hayuko sawa. Mbele yao kulikuwa na Scoba na Dkt. Jasmine.
“Tusichelewe, tuondoke!” Madam S akawaambia, wakatoka na kufika katika magari ambayo yalikuwa yameandaliwa.
Dkt. Jasmine alimchukua Kamanda Amata na kuingia naye kwenye gari la wagonjwa, “lala hapa!” akamwambia naye akapanda juu ya kitanda na kujilaza, Jasmine akamchoma sindano na kumlaza usingizi.
SHAMBA
Madam S alitaka kujua kila jambo analolifanya Jasmine kwa Amata, siku hii yeye ndiye alikuwa msaidizi wa daktari katika procedure zote.
“Yaani kwa hili jeraha lake, tumshukuru Mungu tu alipona, maana tungeshamkosa,” Jasmine akamwambia Madam S.
“Kwa nini?”
“Kuna damu nyingi sana hapa, ena nahisi imeingia hata sehemu fulani fulani za mfupa wa kichwa,” akamwambia.
“Oh shit, don’t say that!!!” Madam S hakutaka hata kusikia habari hizo. Baada kama ya saa nzima kupita wakiwa nd.ani ya chumba hiki kidogo chenye vifaa tiba vilivyokamilika, kazi aliyokuwa akiifanya Daktari Jasmine ikakamilika.
“Ataamka baada ya muda gani?” Madam akauliza.
“Si muda mrefu kama nusu saa au dakika ishirini hivi,”
“Ok!” Madam akaitika na kuitazama saa yake, “lakini hatoweza kufanya kazi za mikikimikiki kwa muda gani?” akaongeza swali
“Inabidi apumzike kwa muda kama wa mwezi mmoja hivi…”
“Mwezi mmoja!… atakubai mwenyewe huyu, na hapo alipo akiamka tu atataka kumtafuta mbaya wake, kama alimpasua kichwani basi na yeye atataka kufanya hivyo hivyo…”
“Kwa nini unasema hivyo?” Jasmine akauliza.
“Namjua huyu, we ngoja aamke utaniambia,”
“Ok tumwache apumzike!”
Madam S na Jasmine wakatoka ndani ya kile chumba na kuja katika chumba kingine cha mazungumzo, ni sebule ndogo yenye viti kama sita hivi vya kisasa, luninga kubwa ukutani na redio yenye muziki mnene, mahali hapa hupatumia tu kama sehemu ya mapumziko. Katika sebule hiyo, walimkuta Chiba, Gina na Scoba wakiangalia mpira wa miguu katika luninga hiyo.
Mara tu baada ya kuingia sebuleni hapo, Gina alikuwa wa kwanza kumuuliza Madam S kuhusu maendeleo ya Amata, akajibiwa na kidogo roho yake ikatulia.
“Ulimkuta wapi?” Madam S akamuuliza Chiba.
“Inaonekana aliokotwa tu, nimemkuta katika mji mdogo wa Waterloo, yaani hata hakumbukii vitu vyake viko wapi,” Chiba akaeleza.
“Sasa hii ni hatari maana anaweza akasahau hata mambo muhimu ya kazi,” Madam akaongeza kusema.
“Ila tu asinisahau mimi?” Gina akadakia na watu wote wakaangua kicheko.
Daktari Jasmine alikuwa kimya muda wote huo, akisikiliza wanayoyaongea, alionekana wazi kuwa kuna kitu kinachomsumbua akilini mwake.
“Jasmine vipi?” Chiba akamuuliza.
“Safi tu!”
“Naona umetekwa na mawazo, sijui umezama wapi, tuambie ukweli bwana, au TSA 1 ni wa kufunga minyororo? Maana kama akipata kichaa atagonga watu ngumi humu mpaka tukimbiane,” akamtania.
“Hamna, jamaa yuko poa, na ataamka muda si mrefu,” akawapa moyo.
“Kwa hiyo Madam S, kazi tunaisitisha au vipi?” Chiba akamuuliza swali bosi wake.
“Sisi tumeondolewa, yaani ninyi hamuhusiki kabisa kabisa, wamekuja wapelelezi wengine kama nilivyokwambia, na tayari wameanza kazi, hapa Tanzania yupo mmoja, Angola kaenda mmoja, Ivory Coast kaenda pia na Somalia, kisha watakutana Addis Ababa kwa majumuisho ya kazi na kutoa uamuzi mmoja wa nini cha kufanya!” akajibu.
“Basi sisi wacha tule bata!” Chiba akasema na wengine wakaunga mkono.
“Of coz, kuleni mpaka kunguru ila mjue kuwa kazi hii sisi tutaifanya kama Tanzania kwa sababu hapa kwetu kumetokea shambulizi kwa hiyo lazima tukusanye information,” Madam S akawaambia.
SOMALIA
KATIKA HOTELI kubwa ya kisasa, Fadicky Al Habib alikuwa ametulia kimya huku vijana wake kama kumi hivi wakiwa wamemzunguka. Kama ungemwona ni kama anatafakari jambo hivi, maana mikono yake miwili ilikuwa kichwani huku viwiko vikiwa vimejitegemeza kwenye magoti yake. Baada ya muda kidogo akainua uso wake na kuwatazama hao vijana.
“Mna uhakika?” akawauliza.
“Ndiyo, sisi huwa hatufanyi kazi kwa kubahatisha!” kijana aliyeonekana kama kiongozi wao akajibu kwa niaba, “nilipigiwa simu, nikafuatilia, nikamwona, na hakika hata mimi nimeona yule ni kama mpelelezi fulani hivi,” akaeleza zaidi.
“Ok, si mnajua kiapo chetu?” akauliza.
“Ndiyo! Aliye kinyume chetu na akatwe shingo!” akajibu yule kijana kiongozi.
“Yatupasa kuzuia njia zote za kutunyima ardhi ya mama zetu, damu itamwagika kama kaka yangu Jaffery anavyosema na tutahakikisha tutaikomboa Somali yetum,” akawaambia nao wakaitikia.
“Hatutakiwi kuua mtu asiye na hatia, kwa hiyo mumpeleleze, mkimgundua kuwa anatutafuta sisi basi haina budi akatwe shingo, nimemaliza,” akaongeza kusema na wale jamaa wakatawanyika na kubaki mmoja tu aliyekuwa kama kiongozi wao.
“Kuna hatihati ya kuingiza vikosi mjini maana hawa wanaojiita AU wamegoma kuaichia ardhi yetu,” akamwambia yule kijana.
“Ni sawa tu, si unaona sasa wametawanya wapelelezi wao kila kona na ofisi yao wameiweka Dar es salaam!” yule kijana akasema.
“Nina mpango mmoja kichwani…”
“Upi?”
“Chunguza ujue lini wanafanya kikao kisha tunalipua wote wakiwa mkutanoni…” Fadicky akasema.
“Yesssss!!!! Nipe kazi nianze kuandaa mpango wa siri,” yule kijana akamwambia Fadicky.
“Bila shaka, ni wewe nimekuteua, hakikisha unafanya hilo, nitakuwezesha kila kinachotakiwa,” Fadicky akamwambia.
Mkakati huo ukaanza kusukwa kati ya wawili hawa, lengo ni kukomesha kabisa mikutano ya baraza la usalama.
DAR ES SALAAM
Kamanda Amata alirudiwa na fahamu na kuamka kama saa moja baadae, akajikuta chumbani peke yake, akapepesa macho yake mazito na kutazama huku na huko, akajaribu kuvuta kumbukumbu ya wapi alipo na baadae akakumbuka.
“Shamba!” akajisemea na kuinuka taratibu kwani hakuwa amefungwa popote, akaketi katika kitanda hiki kidogo. Akajishika jeraha lake kisogoni na kugundua kuwa amefungwa kitu kama plasta hivi, akajiminya kwa nguvu na kuhisi maumivu kwa mbali tofauti na mwanzoni. Dakika hiyo hiyo, mlango ukafunguliwa, Jasmin akaingia ndani.
“Anhaaaaa!!!! Umeamka ee, safi sana na sasa nilikuwa nakuja kukutazama,” Jasmine akamwambia.
“Aaaaa nimeamka, nilikuwa na usingizi mzito kidogo usio na ndoto…” Amata akaeleza.
“Ndiyo, unajisikiaje sasa?”
“Najisikia ok, nahitaji mazoezi zaidi ya kuuweka mwili fresh!” akasema.
“Hapana, unahitaji mapumziko Kamanda!” Jasmine akamwambia.
Kamanda Amata akamwita Daktari huyo karibu na kumnong’oneza, “Sina muda, nitapumzika tu nikimtia kwenye Martin Gupter kwenye mkono wa sheria,” akamwambia.
“Martin Gupter?”
“Yes!”
Jasmin akatulia kimya kwa nukta kadhaa huku mikono yake ikiwa kiunoni, “No!”
“Never say no!” Amata akamwambia na kusimama sakafuni wima, kwanza akayumba kidogo na baadae akasimama.
“Pole!” Jasmine akamwambia Amata.
“Asante! Asante sana…” akajibu huku akitembea kutoka upande huu kwenda mwingine, “Kule Sierra walinipa dawa za kienyeji, zilinisaidia sana kwani mara tu baada ya kupaka nikapata nafuu kubwa sana!” akamwambia Jasmine.
“Unakumbuka nini kilikupata?”
“Yeah! Ila siwezi kukieleza nitakiandika kama kitabu,” Amata akasema huku akiendelea kutembeatembea.
“Kitaitwaje?” Jasmine akauliza.
“Magnum 22,” Amata akajibu.
“Magnum 22?”
“Ndiyo, na jalada lake litakuwa na vitu viwili…”
“Vipi?”
“Ua Waridi jekundu na bunduki ya Magnum 22 rifle,” Amata akaeleza huku akifungua mlango kutoka na Jasmine akamfuata nyuma.
“Hizo picha zina maana gani?” Jasmine akazidi kumuuliza, si kwamba alikuwa akimuuzi ila alijaribu kuna uwezo wa ubongo wake kama unachokifanya unakikumbuka na bado una uwezo wa kufikiri.
“Yaani kifo na mapenzi. Mapenzi ndiyo yaliyonifanya nife!”
“Kwani ulikufa?”
“Kabisa kabisa, ndo maana nakwambia kuwa sitaki kupumzika mpaka nimvunje shingo Martin Gupter anayejificha nyuma ya sura tofauti na kuihadaa dunia, anayetafutwa kona mbalimbali kwa kutekeleza mauaji mepesi na magumu akitumia zaidi ya pasipoti na vitambulisho 100,” akaeleza. Wakati wakizungumza hivyo Madam S akaungana nao.
“TSA 1!” akaita.
“HOT” akajibu.
Madam S akatikisa kichwa na kumtazama Jasmine, “Unamwonaje?”
“Yupo sawa kabisa!”
“Good!”
Wakati wao wakizungumza Amata tayari alikuwa ndani ya chumba maalumu cha kulega shabaha, akachukua bastola na kujaza risasi zilizokuwa hapo mezani, akapachika magazine na kuanza kufyatua kulenga shabaha. Kati ya risasi kumi na mbili ni mbili tu zilikosa tena sentimita moja kutoka tundu la shabaha.
Kutoka nyuma yake, Amata akasikia watu wakipiga makofi, akageuka nyuma na kukutana na timu yake yote ikiwa imekamilika. Gina alikuwa wa kwanza kumkumbati na kumbusu kisha wengine wakapata muda wa kusalimiana naye. Si kwamba hawakumsalimia mwanzoni bali salamu hii ilikuwa maalumu sana. Nusu saa baadae alikuwa kwenye chumba cha mazoezi akipigana na punch bag kwa nguvu zote, jasho likimtiririka.
“Nani uliyempania hivyo?” Madam akamuuliza, mara hii wakiwa wawili tu ndani ya chumba hicho.
“Martin Gupter, Fredy na Amanda, haya ndiyo majina yao halisi,” akajibu na kuendelea kucheza na punch bag lake.
“Ujue kuwa misheni imekuwa aborted,” Madam S akamwambia Amata.
“Kwa nini?” akajibu huku sasa akiwa kaacha kupiga lile begi, akageuka kumtazama bosi wake.
“Baraza la usalama la AU limeamua kuhamisha misheni hiyo kutoka kwetu na kuwapatia kikosi maalum cha wapelelezi kilichoundwa na wao!” akasema.
“Kwa kuwa si hatuwezi kazi au?” akauliza.
“Wanasema tumekiuka makubaliano..” Madam S akamwambia Amata kila kitu kilichoamriwa katika kikao chao ijapokuwa hakutakiwa kumwambia mtu yeyote.
“Kawaambie, hicho wanachojaribu au kutaka kufanya kitawagharimu kwa sababu hawa jamaa wana mtandao wa hatari, yaani si ajabu wanatoka tu katika milango ya afisi zenu wameshaonwa… Gupter si wa kumfuata kama unavyomfuata paka wako, yule jamaa ni hatari, ana mtanda wa kutisha na sasa anafanya kazi na wanamtandao wengine nao wana masikio marefu kama yeye,” akatulia kidogo na kunywa maji, “mimi nilipoishia ndipo nitapoanzia,” akamwambia Madam.
“No! alzima uheshimu maamuzi ya kamati…”
“Siendi kwa ajili ya kamati, naenda kumsaka Gupter personally nina miadi naye,” akaanza kupiga tena begi lake mara hii kwa nguvu zaidi ya mwanzo.
ITAENDELEA
Magnum 22 Sehemu ya Nne
Also, read other stories from SIMULIZI;