Malaika wa Shetani Sehemu ya Tano
KIJASUSI

Ep 05: Malaika wa Shetani

SIMULIZI Malaika wa Shetani
Malaika wa Shetani Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA: BEN R. MTOBWA

*********************************************************************************

Simulizi: Malaika wa Shetani

Sehemu ya Tano (5)

“Ndiyo.”

“Wapi?” “Ndotoni.”

Wakacheka. Ulikuwa mwanzo mzuri kwa Nuru. Baada ya mwendo mfupi, kuyaruhusu mapaja yake yaonekane, kuruhusu mkono wa mroho huyo uyaguse, kazi ilikuwa imekwisha.

“Ndege inaondoka saa nane mchana. Sasa hivi ni saa moja na robo. Kwa nini usipumzike kwangu kidogo?”

“Kupumzika! Huwezi kuongea kinaganaga?”

Dereva alicheka na kugeuza gari. Likapenya mitaa mitatu na kusimama mbele ya nyumba mpyampya. “Naishi na mdogo wangu wa kiume. Bila shaka kasha kwenda zake shule. Tutakuwa mimi na wewe tu.”

***

Nyumba ilikuwa nzuri, chumba pia kilivutia. Nuru alichagua kuketi juu ya kitanda, jambo ambalo lilimfurahisha sana mwenyeji wake. Alipotoka kuendea vinywaji Nuru alimzuia. Hakuwa na muda wa kutosha. Alieleza. Wala haikuwa uongo. Kijana huyo aliposhuka kitandani ili amkumbatie Nuru, alipokelewa kwa pigo kali ambalo hakulitegemea. Akaangukia zulia. Nuru alimwongeza pigo jingine. Kisha, akamfunga kamba za miguu na mikono. Baada ya hapo aliipapasa mifuko yake. Kama alivyotegemea, kijana huyo hakuwa dereva wa kawaida. Katika moja ya mifuko yake ya koti Nuru alipata bastola. Na ilikuwa na kiwambo cha kupotezea sauti. Kwa furaha Nuru aliifungia mapajani, kisha

akachukua ufunguo wa gari na kutoka harakaharaka.

Gari lilimfikisha mbele ya jumba lilelile alilolihitaji.

Alipokelewa na mbwa yuleyule kwa dalili za mjuano. Hata hivyo, alikuwa akitembea kwa dhiki kubwa. Kiuno chake kilikuwa kimeteguka au kuvunjika. Alipomfikia Nuru miguuni alianza kumlamba miguu katika hali ya mjuano. Ni hapo alipomfumua kichwa kwa risasi tatu. Akakata roho na kuanguka kama mzigo. Ndipo Nuru alipoanza safari ya kuingia ndani, bastola ikiwa imemtangulia.

Alitembea kimya kama kivuli, akipiga kila hatua kwa adhari na uangalifu. Alichungulia kila chumba kwa makini kabla hajakiendea cha pili. Alikuwa na kila hakika ya kumfumania adui yake akiwa kajisahau.

Haikutokea kuwa hivyo. Alikuwa akikaribia chumba cha mateso aliposhangaa kusikia sauti toka nyuma yake ikimwamuru kusimama. Aligeuka kwa haraka. Lakini hakuwa mwepesi zaidi ya adui yake ambaye alimdaka na kumtia kabari huku akimpokonya silaha kwa urahisi kama vita vya paka na panya.

“Nilijua utarudi,” alisema kwa kebehi. “Nilijua wewe pia ungependa kufia humu kama wengine.” Likacheka kabla ya kukebehi kwa sauti mbaya zaidi likisema, “Usijali. Dakika chache baadaye utakuwa marehemu. Na nilikuwa na hamu kubwa sana ya kukuua kwa jinsi ulivyokivunja kiuno cha mbwa wangu. Au hukujua kuwa wanawake wenzako watamlilia kwa jinsi anavyojua mapenzi?”

***

Uwanja wa Ndege haukuwa na watu wengi kama ilivyo kawaida. Joram alihisi kuwa hakukuwa na ndege za kuondoka wala kutua muda huo, jambo ambalo lingewafanya wasubiri sana kupatiwa usafiri wa binafsi.

Aliyatupa macho yake huku na huko kwa haja ya kumwona Nuru. Hakumwona. Akawageukia askari hao na kuwatupia swali hilo. Kiasi wakiwa wameshangaa walitazamana na kisha mmoja wao kusema kwa ukali, “Utamsubiri hapa. Atafika muda wowote kuanzia sasa.”

Joram aliitazama saa yake. Hakuwa na muda mrefu wa kusubiri. Hivyo, aliwatazama askari hao kwa kuwapima. Hakuona kama wangemsumbua. Mmoja akiwa binadamu wa kawaida,

asingeukosa udhaifu wa kibinadamu. Na yule aliyefanana na samaki, huyu hakosi kasoro kichwani. Akawageukia wafanyakazi wa kawaida. Kila mmoja alikuwa na shughuli zake. Hakuna ambaye angemsumbua kwani wakati wakijiandaa yeye angekuwa kilomita nyingi toka kiwanjani hapo. Hata hivyo, nje ya kiwanja hicho kulikuwa na kundi la askari ambao walisimama kwa mistari kama wanaomsubiri mgeni rasmi. Joram alijua kuwa wao pia walikuwa kazini, kwa niaba yake. Wasingemsumbu… akageuka kumtazmaa yule anayetumia uso wa samaki.

“Choo kiko wapi hapa?” “Huruhusiwi kwenda chooni.”

Joram akamkazia macho na kuuliza, “Yaani, una maana ninayo ruksa ya kujisaidia hadharani?”

Askari hao walitazamana.

“Sema. Kwangu sio tatizo,” Joram aliwahimiza huku akiibana miguu yake na kurukaruka kidogo kama anayeteseka kwa haja ndogo. “Lazima muwe kama binadamu. Mnajua kabisa mimi si mhalifu na…”

Wakalazimika kumwongoza, mtutu wa yule aina ya samaki ukiugusa mgongo wa Joram. Mbele ya mlango wa choo, mmoja alibaki, wa pili akaingia naye. Alikuwa samaki mtu. Joram hakuwa na muda wa kutosha. Hivyo, badala ya kupoteza muda wake alifungua zipu na kuukanda mkojo. Ulipoanza kutoka mtu samaki alitulia na kuulegeza mtutu wake toka mgongoni mwa Joram. Hakujua kilichotokea kwani sekunde hiyohiyo alipokea pigo kali ambalo hakulitegemea. Teke la kifaransa lilimtoka Joram bila kugeuka. Kabla askari huyo hajajua afanye nini alijikuta kajaa tele katika kabari la Joram. Hakufanya ubishi wowote wa haja zaidi ya kutapatapa huku akimkwaruza Joram kwa kucha zake. Haikumsaidia. Dakika iliyofuata alikuwa chali, juu ya sakafu. Joram alifanya haraka kumvua mavazi yake na kuanza kuyavaa. Shati lilikuwa kubwa na suruali fupi, inayobana. Hakuwa na muda wa kusumbukia hilo. Alijikamilisha kwa viatu na kofia, kisha akaufungua mlango.

Yule askari wa pili alikuwa hatua kumi nje ya chumba hicho akivuta sigara. Joram alimwita kwa mkono. Askari huyo, bila kuangalia kwa makini alikuja haraka akidhani anaitwa na mwenzake. Alipofika mlangoni ndipo alipojua kosa alilolifanya. Alijikuta akitazamana uso kwa uso na bastola ya Joram. Hakuwa

na nafasi ya kuelekeza yake. Akaitazama ikipokonywa toka mikononi mwake na kupotelea katika mfuko wa Joram. Kisha, alisukumizwa chooni humo. Kitako cha bastola kilichotua ghafla kando ya sikio lake kilimfanya apoteze fahamu na kuanguka juu ya mwenzake, kando ya shimo la choo.

Gari lililowaleta, Landlover lenye mabakamabaka, lilikuwa bado liko palepale walipoliacha. Joram aliliendea na kuingia. Akalitia moto na kuondoka taratibu, bastola mbili alizowapokonya askari hao zikiwa mwilini mwake, mavazi ya kijeshi na tepe za cheo cha Captain zikiwa begani alipita katika kikundi cha askari waliomzunguka bila wasiwasi wowote. Wawili watatu walimpigia saluti. Aliitikia huku akitabasamu. Alipouacha uwanja alikanyaga mafuta kwa nguvu zake zote. Gari nusura lipae. Lilipenya katika mitaa na kuingia mjini.

Joram alikuwa na muda wa saa moja na robo kabla ya kuwadia wakati wa ahadi yake na bi Tunu, muda ambao ungemtosha sana kulipa deni alilokuwa akidaiwa, deni la damu. Ni kweli, bado alikuwa gizani; hamjui nani rafiki nani adui katika mkasa huu. Hata hivyo, lile jitu, ambalo lilimtesa na kumdhihaki kama mtoto mdogo, jitu ambalo bila shaka limemnasa Nuru na kumtesa lipendavyo, kwa kila hali lilihusika kwa njia hii au ile katika kuyaangamiza maisha ya akina Betty. Joram alikuwa ameapa kuwa asingeondoka katika nchi hii na kuliacha likipumua. Hivyo, muda huu uliosalia aliamua kuutumia kwa ajili hiyo; alitafute na kulishughulikia. Hakuwa na hakika, lakini aliamini kuwa angelipata katika jengo lilelile, la mateso. Hisia pia zilimnong’oneza kuwa angempata Nuru katika jengo hilohilo. Ni huko gari lilipokuwa likielekea.

Mbele ya jumba hilo Joram alilisimamisha gari kama kawaida na kuanza safari ya kuingia ndani. Akiwa katika mavazi ya kijeshi, tepe nzito begani, bastola mbili mgongoni, alitembea katika kila hali ya kujiamini. Alitoa pakiti yake ya sigara toka mfukoni na kuchambua moja ya zile sigara zake na kuiweka tayari. Akiwa mwenyeji tosha katika jengo hilo hakujisumbua kuchungulia kila chumba. Alikwenda moja kwa moja hadi alipoufikia mlango wa chumba cha mateso. Aliugonga mara mbili. Alipoona kimya akaufungua na kuingia.

Alitegemea kumkuta adui yake, lakini hakutegemea kumkuta akiwa na Nuru, na hasa akimtesa kwa umeme. Hilo peke yake

lilitosha kumfanya Joram asahau kila alichopanga kichwani na badala yake, kwa wepesi wa ajabu, alizichomoa bastola zake zote mbili na kuzielekeza usoni mwa jitu hilo. Jitu lilicheka kwa hasira baada ya kugundua makosa lililoyafanya. Lilikuwa limemsikia mtu akizima gari na kuingia. Lilisikiliza na kupima vishindo vya mtu huyo, likawa na hakika kuwa alikuwa mtu ambaye hakuhitaji kutiliwa mashaka. Zaidi lilimtegemea mtu ambaye angemtembelea mida hiyo.

“Zima umeme mara moja,” Joram aliamuru.

Sauti yake ilimzindua Nuru ambaye alilazwa chali juu ya meza, nusu uchi, umeme mkali ukimtesa kupitia mgongoni. Alikuwa amepiga kelele nyingi kwa maumivu, jambo ambalo lilimfanya ashindwe kusikia chochote alichotamka. Kwa udhaifu mkubwa akainuka ili akiache kikao hicho cha mateso.

“Zima, na mikono uiweke juu,” Joram aliamuru tena.

Dude hilo lilimshangaza Joram. Pamoja na ukatili bado lilikuwa jeuri. Lilimcheka Joram kwa kicheko chake kibaya, huku likimsogelea kujiandaa kumvamia. Jambo moja halikufahamu. Halikufahamu kuwa Joram hakuwa na muda wa kutosha. Hivyo, badala ya kulisamehe tena aliifyatua bastola zake zote mbili. Ghafla, mikono ya kiumbe huyo ikawa imevunjika. Damu nyingi ilivuja toka katika mikono hiyo. Jitu liliguna kwa maumivu ambayo yalilifanya lifikie kiwango cha mwisho cha hasira zake. Huku likipiga ukelele wa ajabu lilifanya jambo ambalo si Joram wala Nuru aliyelitegemea. Liliruka angani na kujibinua mara mbili. Wakati huohuo Joram alipokea mateke kumi ambayo yalitua barabara katika bega la mkono wake wa kushoto na kuutegua. Bastola ikamtoka mkononi na kuanguka chini. Lakini mkono wa pili wa Joram ulikua makini. Toka hapo chini alipoanguka akaachia risasi nne ambazo ziliivunja miguu ya adui yake na kumfanya alazimike kulala chini huku akitukana, “Shenzi.”

“Mshenzi zaidi yako?” Joram aliliuliza kwa kebehi huku akilitazama. Alimgeukia Nuru na kumwendea. “Pole sana mpenzi,” alimwambia huku akimkumbatia. “Mbwa aliyelala hapa alikuwa mtu pekee wa kumwogopa katika nchi hii. Bila shaka kazi yetu imefikia ukingoni leo.”

Nuru hakuwa na sauti. Kila alichojaribu kutamka bado hakikutamkika. Alichofanya ilikuwa ni kulia tu, huku kalalia

kifua cha Joram Kiango. Alilia kuliko alivyotegemea, akisikia uchungu mkali na aibu kubwa kwa yote yale ambayo alitendewa, hasa na mbwa. Hakuwa na habari kuwa teke lake la mwisho lilimvunja mbwa yule kiuno hata akashindwa kufanya chochote alichokusudia.

Joram alimtoa Nuru kifuani na kuidaka mikono yake yote miwili ambayo aliitazama mara moja na kisha kuibusu huku akicheka. “Nilijua wasingethubutu.”

“Wamethubutu. Wame… Nime…” alinong’ona kwa jitihada kubwa.

“Wasingethubutu. Vidole walivyovileta niligundua kuwa si vyako mara nilipovitazama. Pengine walivinunua toka katika majumba ya maiti au waliviokota tu hospitali. Walitegemea kunitisha.”

“Vidole ga-gani?” Nuru aliuliza.

“Ni haithi ndegu. Hatuna muda wa kutosha,” alisema akilisogelea jitu hilo na kulisokomeza domo la bastola mdomoni. “Sikia. Sina hamu ya kuua. Lakini usipoyajibu maswali yangu yote, sio kwamba nitakuua tu, bali utakufa baada ya mateso makubwa sana.”

Ukatili katika roho mbaya ya jitu hilo ulikuwa hai bado. Lilimcheka Joram kifedhuli huku likisema, “Usijisumbue. Siwezi kukujibu lolote. U kinda tu katika dunia hii. Umenipata kwa bahati tu. Hawakukosea waliposema ndege mjanja hunaswa na tundu bovu.”

Joram alikasirika. Jitu hili lenye kila haki ya kunyongwa hadharani lina haki gani ya kumsumbua? “Kufa, huna budi ndugu yangu. Lakini itakuwa baada ya kuyajibu maswali yangu yote,” alifoka akijitutumua kuliinua ili alilaze juu ya kijimeza cha mateso. Alikuwa na hakika zote kuwa umeme ungeumaliza ukatili wa kiumbe huyo. Haikuwa kazi ndogo kutokana na uzito wa jitu lenyewe na maumivu ya mkono wake. Lakini kwa msaada wa Nuru, walilifikisha juu na kuliacha kama lilivyozaliwa baada ya kuyatatua mavazi yake yaliyoloa damu. Kilicholala hapo kilikuwa kipande cha nyama kilichotisha na kuchukiza. Nuru alikimbilia swichi ya umeme na kuiwasha. Mkondo wenye voti nyingi za umeme ulipita katika mwili huo mkubwa na kumfanya aangue kilio. Sauti yake, pindi likilia ilikuwa kubwa, mbaya inayochekesha zaidi ya kusikitisha.

“Sasa utajibu kila swali langu,” Joram alisema baada ya kumwamuru Nuru kuzima.

“Sisemi.”

Ikawashwa tena, likalia tena; kwa nguvu kuliko awali huku likisema, “Acha nitasema. Tafadhali, nitase…” lilipokaribia kuzirai umeme ulizimwa.

“Nadhani sasa utasema,” Joram alifokaa. “Nani aliyekuajiri kufanya unyama kama huu?” aliulza. “Sema upesi kabla sijaongeza umeme.”

“Simjui,” lilijibu. Joram alipotishia kuwasha umeme lilidakia, “Sikia. Usinitese zaidi. Nitasema…”

Ghafla mlio wa bastola ulisikika toka juu ya paa. Mateka wao alikoroma kwa maumivu mapya. Risasi ya pili ilimfanya anyamaze. Joram, ambaye alikuwa amejiviringisha mara mbili na kumfikia Nuru, bastola yake ikiwa tayari; alitazama zilikotokea risasi. Hakuiona haja ya kujibu shambulio hilo. Risasi zilitokea juu, katika kijitundu kidogo sana. Zaidi masikio yake makali yalikwisha sikia vishindo vya mtu akikimbia. Akafanya haraka kuukimbilia mlango. Ulikuwa umefungwa kwa nje. Akarudi mezani na kumtazama mateka wao. Alikuwa marehemu, roho imemtoka kitambo. Asingejibu swali lolote tena.

“Shit” ilimtoka Joram. Upuuzi ulioje huu! Vipi akayaruhusu masikio yake kulala mchana hata afungiwe kijinga. Na ni nani huyu ambaye anaendelea kumchezea wakati aliamini ameufikia mwisho wa mchezo huu hatari? Alijiuliza. Kisha, aliitazama saa yake. Zilisalia dakika chache sana kabla ya miadi yake na bi Tunu. Akageuka kuutazama mlango. Ulikuwa imara, ukimcheka kwa lolote ambalo angethubutu kuutendea. Lakini ilikuwa lazima atoke chumbani humo, tena haraka. Akamgeukia Nuru kama anayemtaka msaada.

“Tutatokaje?” ulikuwa msaada pekee alioupata toka kwa Nuru.

sAA nne kamili iliukuta ukumbi wa mikutano wa makao makuu ukiwa tayari umejaa. Ni kiti kimoja tu, cha mwenyekiti wa kamati ambaye pia ni Rais wa nchi hii, ndugu Abdul Shangwe, ambacho kilikuwa wazi. Angeweza kuingia wakati wowote. Hivyo, wanakamati walikuwa wakizungumza kwa sauti za chinichini, baadhi wakicheka; baadhi wakinong’ona

au kutaniana katika hali ya kawaida.

Lakini ilikuwa dhahiri katika macho na sauti ya kila mmoja kuwa hiki hakikuwa kimoja kati ya vikao vya kawaida. Hiki kilikuwa kikao chenye moto, ingawa moshi ulikuwa haufuki. Halikuwa jambo la kawaida, machoni na masikioni mwao kusikika mtu mzito katika serikali yao akitangaza ghafla kujiuzulu, mtu kama Shubiri Makinda; Waziri Mkuu na makamu wa kwanza wa Rais. Zaidi ya mtu ambaye ujana wake wote ameupoteza kwa ajili ya nchi hii, mtu ambaye ameiweka roho yake mashakani siku nenda siku rudi kwa ajili ya nchi. Na hasa mtu ambaye ni chanda na pete kwa Rais. ‘Kitu gani hasa kinachoweza kumfanya achukue uamuzi kama huo?’ Kila mmoja aliendelea kujiuliza swali ambalo alijaribu kumwuliza Shubiri, lakini hakuna aliyepata jibu zaidi ya “Nataka kujipumzisha.”

Kupumzika! Shubiri ambaye hufanya kazi usiku na mchana! Shubiri ambaye mara nyingi kila kauli yake katika mikutano huungwa mkono mara moja kwa jinsi alivyo na hekima! Si

amewahi hata kusikia minong’ono kuwa bila fikra zake nchi isingefika hapa ilipo! Si kuna wakati hata mwanakamati mmoja aliwahi kupendekeza Shubiri aongoze nchi! Na si Shubiri mwenyewe aliyekuwa wa kwanza kupinga wazo hilo! Vipi leo ajiuzulu ghafla, katika hali ya kushitisha!

Waliendelea kujiuliza hilo na mengine mengi, wakimtazama kiwiziwizi.

Shubiri alikuwa akiusoma mshangao katika macho yao. Zaidi ya mshangao aliona dalili za majonzi katika macho ya baadhi yao. Angefanya nini? Alijiuliza, akijihurumia pamoja na kuwahurumia wao. ‘Hawawezi uelewa,’ alfajiri kimoyomoyo. Ingemchukua miaka mingi kujieleza hata aeleweke kwani hata yeye binafsi alikuwa hajaelewa. Na ingemwingia vigumu sana kuelewa, kama Joram Kiango asingetokea…

Aliendelea kutulia juu ya kiti chake, akiitupia jicho la wizi saa yake mara kwa mara. Kiti cha Rais kilichokuwa wazi kilimkera sana. Alihitaji atokee haraka ili athibitishe kauli yake ya kujiuzulu mbele ya umati huu, awe huru.

Ndiyo, roho yake ilikuwa nzito sana kutengana na umati huu ambao amekuwa miongoni mwao siku nenda siku rudi. Ilikuwa sawa na kushiriki katika kikao ambacho kinakuzika hai, toka katika dunia halisi, dunia ambayo si kwamba uliipenda tu, bali ushiriki katika kuiumba hata ikawa kama ilivyo. Kwa namna moja Shubiri alijiona kama msaliti, kwa namna nyingine alihisi anasalitiwa. Laiti wangeelewa. Lakini kuelewa katika suala hili halikuwa neno jepesi kama lilivyo. Lilikuwa zito, gumu na linalotatanisha. Lingeweza kuwa kisu ambacho kingeipasua nchi na kusababisha mto wa damu ambao mafuriko yake yangewakumba wengi. Kuelewa lingeweza kuwa jembe ambalo lingeijaza nchi makaburi mapya na vilio katika kila nyumba. Shubri hakuwa tayari kuyashuhudia hayo. Heri wasielewe. Kujiuzulu ilikuwa dawa pekee.

Tazama wasivyomwelewa! Tazama wanavyosikitika!

Ni hapo chozi lilipomtoka na kuteleza juu ya shavu lake, chozi jeupe ambalo kwa ajili ya nuru lilionekana kama la dhahabu. Alijaribu kulifuta, lakini haikuwa kabla ya watu wengi kuliona, jambo ambalo lilisababisha machozi mengi zaidi kuanza kuteleza toka katika macho ya watu mbalimbali, machozi ambayo

yalifuatwa na vilio vilivyosikika kwa minong’ono toka hapa na pale.

“Kwa nini umepania kujiuzulu?” mtu mmoja alimwuliza kwa majonzi.

“Huwezi kuelewa,” alijibiwa kwa sauti ya minong’ono.

***

Saa nne kamili ilimkuta Joram Kiango mbele ya nyumba namba arobaini katika mtaa wa Lolongo. Ulikuwa mmoja kati ya mitaa ile iliyofichika na kusahaulika japo inasomeka katika ramani za mji. Kusahaulika kwake ndiko kulikoufanya uwe mtaa mchafu, wenye harufu mbaya, itokanayo na mchanganyiko wa maji, matope na takataka zote zinazofurika katika mitaro na mabomba ya maji machafu. Ni ajabu kwamba mtaa ulikuwa na umeme ambao ulikuwa ukifanya kazi! Pengine huu umeme pia ulisahauliwa mara baada ya kuwekwa? Joram alijiuliza.

Kufika kwake hapa kwa wakati uliopangwa ilikuwa baada ya jitihada kubwa. Alipojikuta mfungwa katika chumba kile cha mateso matumaini yake ya kutoka hai yalianza kufifia. Lakini wazo lilimjia mara moja. Umeme una nguvu za ajabu. Hufanya kazi nyingi. Kwa msaada wa Nuru, aliunga hiki na kile, akitumia vifaa vya mateso chumbani humo na hata kupata mashine ambayo ilitafuna komeo za mlango huo baada ya dakika chache tu za kutoka jasho. Alikuwa amemshawishi Nuru kumsubiri katika hoteli moja, lakini hakuwa Nuru mbaye angeafikina na wazo hilo. Lakini Nuru alisisitiza afuatane naye. Akijua kuwa sumu ya mwanamke ni mwanamke Joram alisita sana kabla ya kuafiki kuandamana naye. Hata hivyo, alitumia hila ya kumwomba amsubiri katika kijimgahawa walichokiona upande wa pili wa mtaa huo kwa dakika kumi. “Baada ya hapo nifuate ukiwa na bastola yako tayari!” Ni hilo lililomaliza ubishi wa Nuru. Nuru, ambaye alimshangaza Joram kwa kutokubali kuliacha jengo lile kabla ya kupekua kila chumba hata alipoipata kamera ya picha za video ambayo aliifungua na kutoa mkanda, aliutazama mkanda huo harakaharaka na kisha kuuharibu kwa moto huku akipambana na Joram aione. Hilo lilimshangaza Joram, lakini hakuwa na muda wa kulisumbukia. Wangelijadili

baadaye. Safari yake hii ilikuwa na umuhimu wa kwanza. “Hodi! Alitamka akigonga tena mlango huu. Ni hodi yake

ya sita ambayo ilijibiwa kwa mlango kufunguka polepole na kuruhsu sura ya mwanamke kuchungulia. Haikuwa sura ngeni kwa Joram. Ilikuwa ileile, nzuri inayovutia, sura ya Tunu, mkewe Rais.

Mara tu mlango ulipofunguka Joram alijipenyeza ndani na kumkumbatia mwanamke huyu, busu likafuata. Ilimshangaza Joram aliposoma mshangao na hofu katika macho ya mama huyu kana kwamba hakutaka wala kutaraji Joram amkabili kimapenzi. Kwa nini ilhali ni jana tu waliposheherekea mapenzi usiku kucha juu ya kitanda? Haya hizi zimetokea wapi kwa mwanamke ambaye saa chache zilizopita hakuzijua? Joram akaamua kumwongezea busu la pili. Hili halikupokelewa kwa mshangao. Lilisafiri na kuwasili katika kila hali ambayo Joram aliitaraji kwani lilipokelewa katika kila hali ambayo ilionyesha kuwa mwanamke huyo alikuwa na njaa na kiu ileile ya mapenzi na mahaba. Alimkumbatia Joram kwa muda kama anayefarijika mwili na roho. Hata hivyo, mshangao ulimrudia Joram mara moja, ghafla, aliposukumwa kando na kuulizwa, “Wewe ni nani, na unataka nini hapa?”

“Vipi mpenzi…”

“Mimi sio mpenzi wako!” sauti kali, ya kike ilimkatiza. “Kama umepotea nyumba rudi nje ukaitafute upya.”

Joram hakuyaamini masikio yake. Na kama hayaaminiki, macho pia hayaaminiki? Kwani aliyesimama mbele yake hakuwa mwingine zaidi ya Tunu yuleyule ambaye wamefurahi naye usiku wa jana. Na alikuwa na hakika kuwa alimridhisha kwa kiwango ambacho kisingefutika katika akili yake mapema kiasi hicho, kiasi cha kufukuzwa! Au usiku wa jana haukuwahi kutokea? Yawezekana kuwa yote yale ilikuwa ndoto tu? Ndoto tamu kiasi kile! La! Haikuwa ndoto. Hilo Joram alikuwa na uhakika nalo. Ndoto isingemwongoza hadi nyumba hii na kumkuta mwanamke yuleyule. ‘Pengine akili za mama huyu zina kasoro?’ Alijiuliza. ‘Rais ana mke mwenye akili hafifu?’ Hilo Joram alielekea kuliamini. Vinginevyo angeweza kuwa na nyumba yake, binafsi katika mtaa uliofichka kama huu? Na vipi Rais amruhusu?

Joram akageuka kukitazama chumba hicho. Ilikuwa sebule pana iliyojitosheleza kwa karibu kila kitu kinachostahili kuwemo katika chumba cha mwanamke aliyeendelea na mwenye uwezo ki-uchumi; makochi ya thamani, meza za bei, zulia maridadi.

Kabati maridhawa, na kadhalika. Hata hewa chumbani humo haikuwa ya kubahatisha. Ilikuwa ikitoka katika mashine ya kurekebisha hewa. Kwa kila hali chumba hiki kilitofautiana sana na mazingira ya mtaa huu, kama ambavyo kilitofautiana na sura ya nyumba hii kwa nje. Joram akayarejesha macho yake juu ya uso wa mwenyeji wake. “Unajua nina muda mfupi sana, mpenzi? Tafadhali tuzungumze harakaharaka.”

“Tuzungumze nini?” “Ile siri uliyoniitia.” “Siri gani?”

Hasira zikaanza kukinyemelea kichwa cha Joram. “Sikia Tunu. Kama ulivyosema jana, siri hii ni ya hatari, siri ambayo itaifanya nchi irudiwe na amani. Vinginevyo, utabeba lawama hapo damu itakapoanza kumwagika na watu kuteketea. Au ulikuwa umeleweshwa na mapenzi hata ukaanza kutapatapa kiasi cha kusema uongo bila haya?”

Ilikuwa dhahiri katika macho ya mwenyeji wake kuwa alikuwa haelewi neno lolote. Kwa sauti isiyo na hakika alinong’ona, “Kama sikosei nadhani unahitaji kuonana na daktari wa magonjwa ya akili. Ebu toka nje ya nyumba yangu tafadhali. Toka.” Sasa alikuwa akifoka.

Joram akaduwaa. Kwa mara nyingine tena alijikuta kapiga kichwa ukutani katika mkasa huu. Akaitazama saa yake. Saa nne na dakika kumi! Bila shaka kamati kuu tayari ilikuwa imeketi kama ilivyotangazwa. Kwa kila hali Joram alijua kuwa msukosuko uliokuwa ukiendelea katika kamati hiyo, na hata kujiuzulu kwa Waziri Mkuu kulihusiana na mikasa pamoja na maafa ambayo yaliwatokea watu wasio na hatia. Siri aliyoahidiwa, iliyokuwa itoke katika kinywa cha mke pekee wa rais, isingekosa kuhusiana na swala hilo. Jambo hilo lingemsaidia Joram kuunga hapa na pale apate anachokihitaji. Vipi basi mwanamke huyo ambaye alfajiri tu alikuwa mkweli alipoahidi kutoa siri, mara anaonekana mkweli kabisa kuwa hajui chochote, pamoja na kumjua Joram? ‘Alazimishwe kuutapika ukweli?’ alijiuliza.

Joram aliusikia mlango ukifunguka polepole na kisha kufungwa. Hatua nyepesi za kike zilinyata kuwajia. Joram hakuhitaji kugeuka. “Karibu Nuru,” alisema akimtazama Tunu. Baada ya kuirudisha kibindoni bastola yake kwa kutoisikia harufu ya maafa, Nuru aliwaendea na kusimama kando ya

Joram, “Karibu.” Joram alisema tena. “Bi Tunu, huyu hapa ni mwenzangu ambaye nadhani unamfahamu sana habari zake japo hamjapata kukutana ana kwa ana. Anaitwa Nuru,” akamgeukia Nuru na kuendelea “Kutana na Bi Tunu.”

“Kwa nini umekazana kuniita Tunu? Nani aliyekwambia kuwa naitwa Tunu?” mwenyeji wao alifoka. “Ninawaomba kwa mara ya mwisho kutoka nje ya nyumba yangu. Na mkichelewa dakika moja zaidi nitawaitieni polisi.” Mzaha ulikuwa mbali na sauti yake. Hata macho yake sasa yalikuwa yakiitazama saa iliyokuwa ikining’inia ukutani. “Nitahesabu mpaka tatu.”

“Tunu, tafadhali…” “Moja!”

“Tunu…” “Mbili!” “Tunu…”

Ghafla mwenyeji wao alipiga ukelele wa maumivu makali huku akianguka chini. Damu nyingi ilimwagika toka katika tundu moja katika paji la uso na jingine kifuani.

Joram na Nuru walitoa bastola zao huku wakigeuka mlangoni. Walikuwa wamechelewa. Adui yao alikuwa akiwasubiri, mkononi akiwa na bastola mbili zenye viwambo vya kupotezea sauti ambazo zilielekezwa vifuani wao. “Dondosheni silaha zenu chini, mara moja,” alifoka kwa sauti ndogo ambayo ilitetemeka kiasi.

Joram hakuwa na njia zaidi ya kutii. Huku akijilaani tena kwa uzembe, aliiachia bastola yake. Nuru pia akafanya hivyohivyo.

Adui yao alikuwa mwanaume ambaye aliificha sura yake kwa miwani ya jua na kofia pana iliyoumeza uso wake. Alikuwa kavaa mavazi yaliyochakaa. Kidevu chake kilimezwa na ndevu ambazo Joram hakuhitaji kuambiwa kuwa zilikuwa za bandia. “Joram Kiango,” alisema. “Kumbe ni tabia yako kutowaheshimu wake za watu? Nilikuheshimu sana, lakini siwezi kukuvulilia zaidi. Una haki ya kufa kama huyo Malaya mwenzako aliyelala hapo. Na utakufa sasa hivi.” Sauti yake haikuwa ngeni masikioni wa Joram Kiango.

Ilikuwa sauti ya Rais Abdul Shangwe mwenyewe.

***

Naam, Shangwe ambaye wanakamati wenzake waliendelea kumsubiri katika chumba cha mikutano, mshangao ukianza

kuonekana wazi machoni mwao, kwani kati yao hakuna aliyejua kuuthamini muda zaidi yake. ‘kitu gani ambacho kinaweza kumchelewesha muda wote huu katika kikao muhimu kama hiki?’ Shubiri alijiuliza kwa mara nyingine. Kama kuna jambo ambalo lilimfanya Shubiri amuheshimu sana Rais Shangwe, jambo hilo ni wajibu. Tangu utoto wake, hakupata kumuona mtu mwingine ambaye aliuheshimu wajibu wake zaidi ya Shangwe. Daima alikuwa mstari wa mbele katika kutekeleza chochote ambacho alitakiwa kufanya, na alikitekeleza kwa moyo mmoja. Katika michezo, masomo , sanaa, katika mijadala na katika kila suala. Shangwe hakuwa na mzaha: jambo ambalo lilimfanya awe kiongozi hapa na pale. Wala hakujipendekeza bali alipendekezwa. Tangu utotoni, kila mtoto alipenda kuwa katika kundi lililoongozwa naye: Shubiri akiwatangulia wote. Ni yeye ambaye daima alikuwa wa kwanza kulitaja jina lake. Na angeweza kulitaja tena na tena. Kama ingekuwepo shule ya Urais Shubiri aliamini kuwa Shangwe angeteuliwa kuwa kiranja mkuu. Iwapo ungekuwepo Umoja wa Marais Shangwe angeweza kabisa kuwa mwenyekiti, au Rais wao, Rais wa Marais.

Hiyo ilikuwa imani ya Shubiri, imani ambayo ilimtia ari na ujasiri mwingi kuwa pamoja naye, na kuchapa naye kazi; akiwa na moyo uliojaa furaha na roho iliyofurika ufahari kwa kuwa mwenzi na mpenzi wa mtu huyu, mtu ambaye kwake haikuwa kawaida kwa maneno na vitendo, mtu ambaye angeweza kuumba mlima kwa maneno na kubomoa mlima kwa neno, mtu ambaye angeweza kuushawishi umati, kumfanya mwenye hasira acheke na mwenye furaha alie. Naam, mtu jasiri katika maneno na hodari katika vitendo.

Umakini wake huo ndio uliomvutia Shubiri hata akamtaka

urafiki, tangu utotoni.

Asingeisahau siku ile ambayo alianza shule na kujiunga na wenzake katika mchezo wa mpira. Alitokea mtoto huyu ambaye alijiunga katika michezo, akiwa golikipa. Shubiri ni mchezaji pekee aliyefaulu kumfunga magoli matatu, jambo ambalo halikumfurahisha golikipa huyo, hata akamchezea rafu. Ndipo walipopigana, ugomvi ambao baadaye ulizaa urafiki wa kudumu; urafiki uliowashangaza walimu na wazazi wao kiasi cha kuwafanya wajione wenye dhambi sana kuthubutu kuwatenganisha.

Wakasoma sana, juhudi zao zikiwa wazi katika kila somo; lakini historia ikiongoza. Walipenda sana kusoma habari za mashujaa ambao walifanya mengi yaliyodumisha majina yao milele. Zaidi walifurahishwa na watu weusi walioshinda utawala wa watu weupe na kuziongoza nchi zao.

Tahamaki ikafika ile siku ambayo shubiri alimtazama Shangwe

kwa makini na kisha kusema, “Kwa nini tusiombe uhuru pia?” “Uhuru! Nani atatuongoza?”

“Wewe!”

Shangwe alicheka. “Unatania,” baadaye alisema. “Vita vya uhuru sio mchezo.”

“Unaweza kuongoza vita hiyo… na nina hakika utaiongoza hadi ushindi… Utakuwa Rais wa nchi hii.”

“Mimi! Kwa nini?”

“Una vipaji vyote vya uongozi. Kila mtu anakusikia na kukuelewa. Kila mtu anakuwa nyuma yako.”

Wakati huo walikuwa likizoni toka ng’ambo ambako walikuwa wakimalizia masomo na shahada za pili. Shangwe alikwishakuwa kiongozi katika idara mbalimbali za vyuoni na alifanya vizuri. Hivyo, madai ya Shubiri hayakuwa ndoto tupu. Taratibu ndoto ikaanza kuwa kweli. Wakaanzisha mijadala. Wakaanzisha chama. Wakapata wanachama. Wakaongoza vita. Kama ndoto nyingine, uhuru ukapatika. Shagwe kiti cha kwanza, Shubiri cha pili yake.

Shubiri aliendelea kuwaza faraja aliyokuwa nayo baada ya kuona ndoto yao ikitokea kuwa kweli. Alifarijika zaidi kujiona akiwa bega kwa bega na mtu huyu mwenye nguvu na uwezo wa pekee. Hasa ilimpendeza zaidi kufahamu kuwa alikuwa mshauri wake mkuu. Shangwe hakufanya mengi ya haja bila ushauri wa Shubiri. Na hayo machache aliyoyafanya yalisababisha migogoro kiasi cha kuiyumbisha nchi. Ni vile tu wananchi wengi walikuwa kama vipofu wanaosafiri baharini katika jahazi, hivyo utokeapo upepo wasikujue kuwa upepo huu ni kusi au kaskazini. Lakini tena, daima Shangwe alijitokeza kama naodha mzuri, akalielekeza jahazi vyema akipambana na mawimbi na hata kulifikisha pwani salama. Shida na misukosuko hiyo ilitokana na uamuzi wa watu, watu waliichukulia kama sehemu ya maisha. Hakuna aliyeona. Hakuna aliyepinga. Shangwe aliendelea kuwa Shangwe, nuru na nguzo ya taifa.

Jina lake liliendelea kuwaka. Na kwa dhamira ya kuliongezea nuru Shubiri aliendelea kumshauri na kumkosoa. Kuna wakati ambao Shangwe aliupinga ushauri wa Shubiri, jambo ambalo lilimfanya Shubiri ashangae sana. ‘Shangwe anaanza kuishiwa na uwezo wa kuona mbali?’ alijiuliza kwa mashaka kwani suala hilo lilikuwa wazi kabisa. Ukazuka ubishi. Siku chache baadaye

, Shubiri, kama adhabu alihamishiwa Wizara nyingine, ndogo sana. Alipouliza kisa aliambiwa ili akaiokoe Wizara ambayo inalegalega. Alijua anadanganywa. Lakini aliiokoa Wizara. Ikapata uhai na mafanikio makubwa. Kama shukrani zake Shangwe alimpa Wizara nyingine. Hiyo pia aliiokoa. Akaendelea kuchezewa kama mpira, mara hapa mara pale hadi majuzi alipojikuta kakirudia tena kiti cha uwaziri mkuu.

Ni wakati huu Shubiri alipoanza kuona dalili za magonjwa katika macho na sauti ya Shangwe, magonjwa ya kujiamini na hofu. Alianza kuzungumza kama anayetoa amri, bila mashaka wala matumaini ya kupingwa. Na alipopingwa badala ya kushawishi ili aeleweke yeye alifoka. Na, kama kawaida, aliungwa mkono; katika kamati na mikutano yake.

Nayo hofu ilijitokeza katika tabia kwa jinsi alivyokuwa hana imani hata kwa wapenzi wake. Alimshuku kila mmoja na kutomwamini mtu. Aliuongeza ulinzi wake na kupoteza fedha nyingi kwa silaha za kisiasa. Hata kulikuwa na fununu ambazo zilienea kuwa, alianzisha kikosi chake cha siri ambacho kilikuwa cha watu wa nje ambao walielimishwa sana mbinu zote za kuua, kwamba kikosi hicho kilikuwa kinatumiwa kuua mtu yeyote, ambaye angeweza kuleta mashaka kwake. Madai hayo yalipata mizizi wakati mbunge mmoja aliyekuwa akidai kuwa ili kura ya kugombea urais iwe ya haki lazima kuwa na wagombeaji wawili badala ya mmoja kama ilivyo kwa wabunge. Kesho yake mbunge huyo alitangaza bungeni kuwa ametishiwa kuchinjwa iwapo asingeacha madai hayo. Akadai kuwa asingeacha. Siku mbili baadaye aliteuliwa kwenda nchi moja ya nje kushika nafasi ya balozi mmoja ambaye aliugua ghafla. Mbunge mwingine ambaye aliendeleza madai ya mwenzake alipata ajali ya gari na kufa, yeye na familia yake yote. Fununu zikaenea kuwa ni kazi ya jeshi la siri la Rais.

Shubiri hakupenda kuziamini fununu hizo. Hivyo, alipata wasaa wa kuongea na Shangwe na kumsaili hayo. “Na wewe

unaweza kuamini upuuzi huo?” aliulizwa.

“Ni vigumu kuamini. Lakini naelekea kuamini maana umebadilika, Shangwe. Kwa nini unaua? Alimjibu.

Ni hapo alipotazamwa kwa lile jicho ambalo halikupata kumtoka akilini, jicho ambalo liliujaza hofu moyo wake. Naam, jicho ambalo Shubiri hakuamini kuwa Shangwe angeweza kuwa nalo kwani halikuwa jicho la kibinadamu.

***

“Utakufa na huyo bibie, japo hastahili kufa,” Shangwe alikuwa akiendelea kuwasimanga. Dalili zote za mauaji zilikuwa katika macho yake. Zaidi, maiti moja, ya mwanamke mzuri, ilikuwa chali miguuni mwao, damu mbichi ikiendelea kumvuja. Maiti nyingine mbili nyingine moja ikiwa ya Nuru na ile ya Joram ni vitu ambavyo vilikuwa wazi kabisa katika sauti yake alipoongeza kwa ukali “Umenilazimisha kuua. Nimefanya kila njia kuyahifadhi maisha yako, nikizingatia hadhi yako na mchango wako katika kuilinda Afrika. Kwa bahati mbaya, hukupenda kunisikia. Hivyo, sina lawama,” alimaliza akiiandaa bastola yake.

Joram alijua maisha yake yako hatarini. Alijua kabisa kuwa Shangwe sasa alikuwa kama simba aliyejeruhiwa, asingesita kuyatimiza matakwa yake. Hata hivyo, hilo halikumzuia kujisikia faraja… Pamoja na maisha yake kuwa mashakani bado alihisi roho yake ikifika kivulini baada ya safari ndefu ya msitu wa jangwa. Huku akicheka, alimgeukia Nuru na kusema, “Hatimaye kobe kajitokeza nje ya gamba lake. Au sio mpenzi?” Nuru alipochelewa kujibu Joram alimgeukia Shangwe na kumcheka tena. “Rais mtukufu, laiti dunia ingekuona unavyopendeza katika madevu hayo bandia, kofia pana, na bastola mkononi kama jambazi halisi! Nadhani hakuna ambaye angeamini. Unasemaje?”

Kejeli katika kicheko na sauti ya Joram pamoja na kebehi katika maswali yake, vilimfanya Shangwe, ambaye hasira zake ziko sirini sana; zijitokeze katika macho yake. Alinong’ona neno ambalo halikutamkika vizuri. Kisha, akailenga bastola katika kifua cha Joram, kidole chake kikijiandaa kuifyatua.

“Sijui itakusaidia vipi kutuua,” Joram aliendelea kueleza kwa utulivu. “Ndiyo pengine itakusaidia. Itakufanya upate sifa nyingi zaidi ya mwuaji mzuri. Na kama unadhani kutuua ni kuyasafisha au kuyafunika madhambi yako, unajidanganya. Mara tu baada

ya kifo changu dunia nzima itafahamu madhambi yako yote.”

Kwa mara ya kwanza Joram alisoma kitu zaidi ya hasira katika macho hayo, hofu. Kwa kwa sauti ya hofu vilevile, japo alijaribu kuikaza, Shangwe alifoka, “Mwongo.”

“Mwongo?” Joram aliuliza akitabasamu. “Niue basi, uone nilivyo mwongo. Unangoja nini? Niue mara moja.”

“Mwongo!” Shangwe alifoka tena. “Unajua nini juu yangu?” “Najua kila kitu,” alimjibu. “Najua kuwa wewe si binadamu

bali mnyama. Machoni mwa watu daima umejifanya mwema kama malaika. Lakini nadhani utaniwia radhi nikikuita malaika wa shetani, vinginevyo ungewezaje kuwa na roho ya kinyama kiasi cha kuua watu wengi wasio na hatia? Kwa kweli, umetia aibu; mtukufu Shangwe.”

“Nani mwenzangu?” UlikuwamkondoambaoJoramaliuhitaji,mkondowamaongezi.

Alijua ni maongezi peke yake ambayo yangemwezesha kuahirisha mauti yao, ambayo yalikuwa wazi mbele yao; yakiwamezea mate. Kuua, ulikuwa wokovu pekee wa Shangwe. Awaue awazike na atakuwa ameuzika ukweli mzima; naye kubakia mtakatifu kuliko watakatifu… Ni hilo ambalo lililomfanya Joram aamue kuununua wakati, kwani siku zote wakati hutenda maajabu nyakati za mwisho kama hizi.

Shutuma zake kwa Shangwe hazikuwa uongo mtupu. Moja kati ya tabia za mpelelezi zikiwa kutomwamini mtu na kumshuku kila mmoja kuitwa kwake na Shangwe kupeleleza mkasa huu hakukumfanya ashindwe kutazama kwa jicho lenye mashakamashaka ambayo yaliota mizizi pindi vitisho na ajali zilipoanza kuwatukia na hasa Shangwe alipoanza kumlazimisha afanye kazi kinyume cha tabia yake. Ilikuwa wazi kuwa kuna mtu ambaye alifahamu jukumu la harakati zao zote, naye akawa akiarifu kwa mtu au watu ambao waliwatendea ukatili uliodhamiriwa kuwatisha. Nani ambaye angekuwa na fursa nzuri ya kuzifahamu nyendo zote ziadi ya Shangwe?

“Nani amemwua?” alimwuliza. “Aliyelala hapo chini ni hayati mkeo. Umemwua kwa mkono wako, mbele yangu. Hilo halikutoshi kukufanya ujione ulivyo mnyama?”

Kwa mara ya kwanza, Shangwe alicheka. “Kumwua huyo malaya! Ana haki ya kufa. Mwanaume gani ambaye anaweza kustahimili kuishi na mwanamke anayejiuza hovyo? Wewe tu

jana ulikuwa naye, unahitaji ushahidi gani zaidi?”

“Ni wewe uliyemshawishi kunifuata. Kama angefahamu kuwa ulimtuma kwangu ili umwue kamwe asingenijia.”

“Ndivyo alivyokuambia? Basi alikulaghai.” Alipumua na kuongeza, “Nilimtuma ili akuonye kwa mara ya mwisho, urudi kwenu baada ya maisha yenu kuwa hatarini. Nikamlaghai kuwa ningesafiri. Taarifa hiyo ikamfanya aamue kulala nawe. Wapelelezi wangu waliniarifu kila kitu. Ningeweza kuwafumania, lakini sikupenda aibu. Ningeweza kuamuru muuawe palepale kitandani, bado nikailinda heshima yako. Niliposikia ahadi yenu ya kukutana hapa tena, ndipo hasira zikanishika. Nikaamua kumwua. Na kwa ajili hiyo nakuua na wewe pia.”

Shangwe alivuta pumzi kwa nguzu na kuongeza, “Kifo chako ni halali kabisa, Joram. Kila mtu ataafiki hatua niliyoichukua ya kukuua kwa kitendo chako cha kishenzi. Kwa bahati mbaya, si kila mtu ambaye atasikia habari hii ya aibu. Itakuwa siri. Ni Rais wako tu ambaye ataarifiwa. Na kwa kuisikia kanda iliyonasa sauti zenu pindi mkifanya mapenzi hatashangaa wala kukionea uchungu kifo chako. Sasa kaa vizuri nikutie risasi katika kichwa chako. Nina mkutano muhimu sana ambao unanisubiri.”

‘Hadithi nzuri iliyoje!’ hadithi isiyopingika,’ Joram aliwaza huku akitabasamu kwa hasira. Afrika ina balaa gani hata kuwa na kiongozi mwongo na mnafiki kama huyu? Kama atawaua na kuondoka hapa na hadithi kama hii nani ambaye asingemwamini? Nani ambaye angejisumbua kuupata ukweli halisi na mzito ambao uko nje kabisa ya uongo huu uliopikwa ukapikika?

“Nilikuambia u nani vile, Shangwe? Malaika wa Shetani? Nadhani nimekupendelea sana. Labda ningekuita mdogo wake shetani, kama si mwanae. Zaidi ya ukatili u kiumbe mwongo kuliko waongo wengi sana. Kwa taarifa yako, nakufahamisha kuwa dunia haitaendelea kuwa na binadamu hatari kama ulivyo. Uliponiita toka nyumbani na kuja hapa kwako kwa visingizio, bila kujua ulikuwa ukiita hukumu yako mwenyewe. Makosa yako yalikuwa yamekuchosha wewe mwenyewe bila kujifahamu. Na kwa makosa hayohayo ukaniita. Umejihukumu mwenyewe. Adhabu yako inayokustahii ni kitanzi. Hata hivyo, Afrika haina historia ya kuwahukumu viongozi, japo waovu kiasi gani. Hivyo, tutaifadhi aibu yako na kukupa adhabu ndogo sana;

ya kukuomba ujiuzulu.” Joram akasita kidogo. Kisha, akaongeza kwa sauti ya amri, “Na sasa itue bastola yako chini na uondoke mara moja kurudi mkutanoni, ukaiandike barua ya kujiuzulu kwako.”

Ilikuwa sauti yenye uhakika, sauti ambayo pamoja na kushawishi, ililazimisha. Nusura itimize wajibu. Kwa muda, Shangwe aliduwaa kana kwamba alikuwa tayari kuitii amri ya Joram. Kisha, kama aliyejikumbuka, alijikaza na kuiweka sawa bastola yake, tayari kuua. Kwa sauti ambayo ilitetemeka kidogo, alinong’ona, “Nadhani una wazimu. Sielewi chochote unachosema. Jiandaeni kufa. Mngependa kusali kabla?”

“Nina wazimu?” Joram aliuliza akimcheka. “Huelewi chochote nnachosema, sio? Huelewi kuwa ni wewe uliyemtuma hayati Patauli nchini Tanzania baada ya kumpa sumu ambayo ingemwua polepole kwa hila? Huelewei kuwa ni wewe pia uliyewatuma watu wako kwa hila kumwandaa Betty ili ajifanye hawara yake Patauli na kunipa fununu ambazo ulikusudia kuzifanya kishawishi ambacho kingefanya nimshuku waziri mkuu wako ili aweze kuhalalisha kifo chake ambacho ulikusudia kwa msaada wa wauaji wako? Huelewi? Nini ambacho huelewi Shangwe?”

“Bado sikuelewi.” Shangwe alimjibu.

“Bado hunielewi! Vizuri sana. Nitakufahamisha kwa tuo.” Joram alikohoa kidogo. “Nitakufahamisha kwa marefu na mapana.” Akaongeza, “Ulipoupata uongozi wa nchi hii. Kwa msaada wa hekima na ushauri mwingi wa rafiki yako Shubiri ulijikuta ukiwa na mawazo yasiyo na hakika kwa kazi yako. Ndipo ukajenga tabia ya hofu, ukimwogopa rafiki yako. Hofu yako ilikuwa kwamba ingetokea siku ambayo angeweza kuchukua madaraka ya kuongoza nchi badala yako. Hofu yako ilitokana na jinsi ulivyomwona akiwa mtu mwenye hekima na vipaji vyote vya uongozi kiasi cha kuungwa mkono mara kwa mara katika vikao vingi. Ni hapo ulipoanzisha kampeni za sirisiri na kumpaka matope, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wachapishaji magazeti wakitumia sana picha zake, pindi anapokuwa amenuna tu; ili watu wamwogope na kumchukia. Hukufanikiwa sana. Katika mabaraza yenu na, kutokana na taarifa zote ambazo ulizipokea toka kwa wapelelezi wako Shubiri aliendelea kuwa mtu mashuhuri wa kutumainiwa. Moyo wa shetani ukazidi kukushika. Ukabuni mbinu mbaya zaidi, za kumwangamiza.

Kwa bahati mbaya sana kwako, mtoto wa watu, ambaye hana hatia alinusurika toka mikononi mwa jeshi lako la siri mara kwa mara. Kila walipomfuata nyumbani kwake usiku hawakumkuta. Ni hapo ulipobuni uovu mbaya zaidi; kwa kunifikria mimi.”

“Nia na matumaini yako ilikuwa kunilazimisha kwa hila niamini kuwa Shubiri ni mtu hatari na mwuaji. Ili nitoe taarifa hiyo ambayo ungeitumia kuwashawishi viongozi wenzako, ambao wanamwamini sana Shubiri, waafikiane na matakwa yako, hivyo ulimtuma kwangu. Akiwa mtu aliyekuamini na kukuthamini sana, hakushuku chochote hata alipopewa dawa ambazo zingemwua mara moja baada ya siku kadhaa. Bahati ilikuwa upande wako kwani japo ulitegemea afe siku mbili au tatu baada ya kuniona kwake alichelewa sana kuniona hata akafia mikononi mwangu, jambo ambalo lilinitia kiu ya kuja nchini humo kuona kulikoni. Na nilipofika ulijifanya hufahamu chochote juu ya suala hilo, hali ukiwa umemwandaa Betty anishawishi zaidi pamoja na mwuaji wako ili amwangamize. Uliendelea kunitisha kwa ajali nyingi za watu wasio na hatia pamoja na kunishawishi nirudi kwetu. Vitisho vyako vilianza kugeuka ukweli, na kuwa hofu moyoni mwako baada ya kuona nikifanya shughuli zangu bila nia ya kukujulisha ninalofanya. Hofu yako ilikuwa kwamba ningeweza kuonana na Shubiri ana kwa ana na kupata ukweli wa mambo.

“Na kwa taarifa yako nimemwona Shubiri. Usiku wa jana tulizungumza naye. Kule kumwona tu, kumenifanya niondoe mashaka yote niliyokuwa nayo juu yake. Japo hatukuongea naye, nadhani tulielewana. Matokeo ya kuelewana kwetu ndio ile barua aliyokuletea ya kuomba kujiuzulu. Akiwa mtu mwaminifu rohoni, mkamilifu akilini, hakuiona haja ya kuendelea kuwa katika serikali hii ambayo haimwelewi wala kumthamini. Wala hayuko tayari kuruhusu damu ya watu wengi, wasio na hatia imwagike kwa ajili yake au yako. Kama mwungana ameamua kuacha kiungwana. Nawe, baada ya kutaabika sana kwa kutokujua ninalofanya, kiasi cha kumtuma mkeo kwangu ili apeleleze na kunishawishi kuondoka, ulipoipata barua ya Shubiri uliona kama umefika mwisho wa matatizo yako. Ukawa huitaji tena msaada wangu usiotabirika. Ndipo ukaamua kulitumia jeshi lako kututoa nje ya nchi hii, hasa baada ya kumwua asubuhi hii, mwuaji na msiri wako mkuu, ambaye ulimpa mafunzo makali ya

kininja.”

Joram alisita kidogo kabla hajaongeza kwa sauti ya hasira zaidi. “Huna aibu Shangwe. Ushenzi na unyama wote ambao umewatendea watu wasio na hatia, pamoja na mateso yote aliyoyapata dada yangu, Nuru hapa, ni mambo ambayo kamwe hayasemeki. Ninayo masikitiko makubwa kukwambia kuwa sitauondoa mguu wangu katika nchi hii kabla ya kuhakikisha dunia inafumbua macho na kuiona ngozi ya kondoo uliyoivaa juu ya ngozi yako halisi ya fisi mroho,” alipoendelea alikuwa mkali zaidi. “Na sasa nitakuomba, kwa mara ya mwisho, itue bastola yako chini na kuiweka mikono yako juu kama inavyomstahili kila mhalifu.

Amri hiyo, ambayo ilitamkwa kwa uhakika, nusura imfanye Shangwe atii, kwa jinsi ambavyo hakuitegemea. Kwa muda aliduwaa, kajisahau na kuzisahau bastola zake. Ilikuwa fursa ambayo Joram alikuwa akiisubiri sana. Alijiandaa kuchupa angani ili azibetue silaha hizo. Hata hivyo, alisita kidogo kwa kuyahofia maisha ya Nuru. Akaamua kusubiri fursa nzuri zaidi. Lilikuwa kosa ambalo Joram alilijutia sekunde iliyofuata tu kwani Shangwe alijikusanya mara moja, na kuwalenga vizuri bastola zote mbili, huku akisema, “Ndiyo. U mpelelezi mzuri sana. Sikukutegemea kung’amua chochote katika siri hiyo ambayo tuliificha kwa gharama zote, pamoja na damu. Hata hivyo, uhodari wako huo unakupa sifa moja tu; ya kukifanya kifo chako kiwe na umuhimu mkubwa na wa haraka zaidi; ingawa hujui yote…”

‘Hujui, na utajuaje uchungu wa binadamu anayeheshimiwa na kila mtu duniani, matajiri kwa masikini, waoga kwa mashujaa, wema kwa waovu, kudharauliwa na mtu mmoja tu ambaye ni mkeo? Utajuaje msiba wa mwanaume alalaye na mkewe huku kamnunia kila siku? Zaidi utaijuaje aibu ya mume, kulala na mke kama huyo, na inapotokea moja ya zile siku haba sana za mapenzi, mara yanapomkolea, aanze kulalamika kwa kulitaja jina la mwanaume mwingine? Na ambaye ni Waziri Mkuu wako? Hapana. Huwezi kuelewa, Joram. Huwezi kuelewa kuwa Shubiri kwangu amekuwa kama mwiba katika chembe ya moyo. Au punje ya mchanga katika jicho. Kila wazo la hekima “Shubiri,” serikali ni “Shubiri” Mkutanoni “Shubiri.” Hata nyumbani juu ya kitanda chako! Hapana. Kifo tu ndiyo ilikuwa haki pekee ya Shubiri. Afe

kama alivyokufa huyu malaya wake. Bahati imekuwa upande wake. Amenusurika katika “ajali” na mitego mingi. Lakini iko siku. Pamoja na kujiuzulu kwake, iko siku. Pamoja naye Joram Kiango!’

Shagwe alitamani kuyatamka hayo kwa sauti, amwambie Joram ili afe akiyafahamu. Lakini hakuyatamka. Yasingeweza kutamkika. Badala yake aliwatazama kwa ukali zaidi, tayari kuua.

Ile sura nzuri, inayofahamika sana katika vyombo vya habari na mikutanoni, sura ya Shangwe, isiyokosa shangwe na tabasamu, sura ya mwungwana na mstaarabu ilitoweka ghafla. Badala yake, mbele yao ilisimama sura ya kutisha na kuogofya, sura ya mauti, sura ya mwuaji ambaye alikuwa tayari kuua tena. Joram alijua kuwa wako katika hatari kubwa kuliko zote katika maisha yao. Wakati wowote risasi zingefyatuka na wao kuwa maiti. Akayatazama maiti ya Tunu, ambayo yaliendelea kulala miguuni mwao, kwa amani na utulivu. Ilikuwa dhahiri kuwa dakika yoyote wao pia wangekuwa marehemu. Joram, akiwa mtu ambaye hakati tamaa haraka, alijikaza kisabuni na kuuchekea uso huo kwa sauti huku akiutupia swali hili na lile kwa nia ya kununua muda. Shangwe hakujibu lolote. Alilenga

shabaha vizuri zaidi na kujiandaa kuua.

Kuua si kazi rahisi, hasa kuwaua watu wasio na hatia wala wasiwasi; ambao wametulia mbele yako wakikutazama. Ni hilo tu ambalo lilikichelewesha kifo chao. Shangwe alikuwa akibabaika na bastola, roho ikiwa tayari kuifyatua hali vidole vikisita. Kana kwamba waliusoma upinzani huo katika fikara zake, Joram na Nuru waliendelea kumkazia macho yanayomcheka, tabasamu la dhihaka katika nyuso zao. Ni hiyo tu iliyokuwa silaha yao pekee; na iliwasaidia kwani, mara, kama ndoto, mlango ulifunguka taratibu na kuruhusu umbo zuri la mwanamke kuingia.

Wote waligeuka kumtazama.

Wote walitokwa na macho ya mshangao.

Kama enzi ya maajabu na miujiza ilikuwa imepita kitambo, hii ilikuwa enzi gani? Kwani aliyeingia alikuwa mwujiza au zaidi. Alikuwa yuleyule Tunu, mkewe Shangwe, ambaye muda huohuo alikuwa chali sakafuni, akiwa maiti yaliyokauka kitambo. Waliinama na kumtazama alivyosimama akiwa hai, akiwatazama. Hakuna aliyeamini macho yake. Hakuna aliyekumbuka mahali

ulipokuwepo ulimi wake. Wote wakabaki kimya wakimtazama kama wanaitamza ndoto ya mchana, na kisha wakatazamana.

Naye alikuwa akiwatazama, mshangao ukiwa wazi machoni mwake. Alianza kwa kumtazama Shangwe aliyeduwaa na bastola zake. Akawageukia Joram na Nuru ambao walisimama mbele ya bastola hizo. Kisha, akayahamisha macho yake na kuyateremsha chini ambapo yaliushuhudia mwili uliolala hapo chini. Ilikuwa kama sinema ya mazingaombwe, ambayo ilimtoa mtu yuleyule, katika jukwaa moja, hapa akiwa kalala, hapa kasimama; akijitazama. Tofauti pekee ilikuwa mavazi tu. Huyu aliyesimama alikuwa katika mavazi ya kileo zaidi, suruali na T-shirt nyepesi, macho kayafunika miwani, kichwa kikiwa kimemezwa na kofia ileile ambayo aliivaa alfajiri ya leo. Alionekana kama mtu aliyekuwa ndotoni, hayaamini macho yake. Na mara alipoelekea kuyaamini alitokwa na ukelele wa ghafla. Machozi mengi yalimtoka, akamsogelea marehemu na kumwangukia akimkumbatia, huku akilia kwa sauti maneno ambayo hayakusikika. Kisha, akainuka na kumsogelea Joram. “Ni huyu aliyemwua?” aliuliza akiulekeza mkono wake kwa Shangwe. Hakuhitaji jibu. Aligeuka mara moja na kumwendea. Alisimama mbele yake na kumkazia macho yake yaliyojaa machozi. “Wewe… kwa nini umefanya unyama huu? Umeua nusu ya uhai wangu. Hustahili kuishi,” alifoka akizipokonya bastola zote mbili toka katika mikono ya Shangwe ambaye aliduwaa na kuzielekeza kifuani mwake. “Hustahili kuishi,” alifoka tena akifumba macho.

AMA ilivyokuwa kwa wanakamati wengine, Shubiri pia alichoka kuitazama saa yake. Saa moja na nusu ilikuwa imepita bila Rais kuonekana. La kushangaza zaidi ni ile taarifa iliyowafikia baada ya kupiga simu, kwamba Shangwe alikuwa ameondoka nyumbani hapo kwa siri bila kuwaaga hata

walinzi wake maalumu.

Kutoweka nyumbani na ofisini, mara kwa mara, halikuwa jambo geni kwa yeyote aliyemfahamu Shangwe. Mara moja aliwahi kuvaa mavazi ya kimasikini na kutembea barabarani kama fukara yeyote, anayetafuta kazi. Safari yake hiyo iliishia katika ofisi ya bwana mkubwa mmoja ambaye alikuwa na sifa nyingi za ulaji rushwa na unyanyasaji. Inasemekana kuwa bwana mkubwa huyo alimfukuza Shangwe kama mbwa mara alipotia mguu katika ofisi yake. Hakujua kuwa alikuwa akimkemea nani hadi kesho yake alipojikuta hana kazi kwa amri ya Rais. Matokeo ya kitendo hicho yakawa ile kampeni ya kuwafukuza viongozi wengi waliokuwa wakiyatumia vibaya madaraka yao. Wala si hilo tu. Zilikuwepo fununu nyingi za Shangwe kuonekana hapa au kujitokeza pale ghafla, katika hali na mazingira ambayo hayakutegemewa.

Ndiyo, kutoweka kwake hakukuwa mwujiza. Hata hivyo, kutoweka huku kwa leo, mbele ya kikao muhimu kama hiki, kulimshangaza kila mtu; Shubiri zaidi ya wote. Akiwa mtu

aliyemfahamu fika, alijua kabisa kuwa kulikuwa na sababu nzuri sana iliyomchelewesha. ‘Sababu gani? Uoga?’ Hilo alilitupilia mbali mara moja. Shangwe angeweza kwenda hata mbele ya umati wa simba wenye njaa kulitetea jina lake, akiwa na imani kubwa ya silaha zake; suti inayoshawishi na maneno yanayosisimua. ‘Aibu? Shangwe alimwonea nani aibu! Macho yake yalikwisha poteza aibu na haya zote.’ Zaidi hii I fursa ambayo Shangwe amekuwa akiililia kwa muda mrefu. Kuamua kwake kujiuzulu Shubiri aliamini fika kuwa alikuwa akimpa Shangwe zawadi ya pekee na ya mwisho ambayo alihitaji sana toka kwake.

‘Vipi basi anachelewa?’ Shubiri alijiuliza akiitupia jicho jingine saa yake. ‘Kitu gani kinamchelewesha?’

Mara chumba kizima kikamezwa na ukimya wa ghafla Shubiri akainua uso kutazama. Macho yote yalikuwa yameelekezwa mlangoni katika hali ya mshangao. Akayafuata macho hayo. Yeye pia alimezwa na mshangao mkubwa wa kumwona mtu aliyesimama hapo mlangoni. Alikuwa Tunu, mkewe Rais! Alikuwa katika mavazi yaliyochakaa kwa vumbi na damu. Uso wake ulijaa machozi.

Tunu alikuwa akitazama huko na huko. Mara alipomwona Shubiri aliondoka mbio na kumkimbilia. Walinzi walijaribu kumzuia. Lakini akawa mwepesi zaidi yao. Aliwakwepa na kumfikia Shubiri ambaye alikuwa amesimama kwa mshangao. Alipotanabahi Tunu alikuwa amemkumbatia kwa nguvu huku akilia. Kwa sauti ya mnong’ono alisikika akisema, “Nimemwua… Nimemwua…”

“Nani?”

“Shangwe Ame… Amekufaa”

Waliobahatika kuusikia mnong’ono huo walitahayari vinywa wazi. Ambao hawakusikia waliduwaa kwa kuuona mshangao na hofu katika macho ya wenzao.

Shubiri aliduwaa zaidi yao. Hakujua wapi alipoupata uwezo wa kuamuru mkutano uhairishwe kwa nusu saa, naye kumwongoza Tunu katika chumba cha faragha ambako alimfariji na kisha kumwomba aeleze kwa tuo chochote alichotaka kueleza.

***

Peke yao chumbani, juu ya kochi kubwa, bado Tunu

hakukubali kumwachia Shubiri. Alimkumbatia, kichwa kakilaza juu ya kifua chake, machozi yakiendelea kumtoka. Pamoja na hofu, pamoja na mshituko, dalili za kitu kama mapenzi zilikuwemo katika sauti ya Tunu pindi akipumua taratibu kifuani hapo.

Mapenzi! Na mke wa Rais wa nchi na rafikie mpenzi! Shubiri aliwaza kwa mshangao. Mwanamke huyu ana wazimu! Upo wazimu wa kupenda?

Asingeweza kusahau, tangu enzi za ujana wao mwanamke huyu alivyowahi kumpenda. Akiwa yeye na hayati nduguye walimpenda kupindukia. Hayo alikuwa akiyaona na kuwasikia wakisema. Kila alipoonana nao peke yake walidai kuwa wangependa kuolewa naye peke yake, kwamba hawakumtaka Shangwe. Lakini hawakujua kuwa mapenzi yake kwao hayakuzidi yale aliyokuwa nayo kwa rafikiye, Shangwe. Ni hilo ambalo lilimfanya akubali hata kumpoteza huyu Tunu, kumwachia Shangwe amwoe mara ilipotokea ile ajali ambayo ilimchukua Lulu na kumwacha Tunu. Machozi ya Tunu nusura yamtie wazimu kwani ni hapo alipoonja uchungu wa mapenzi kwa mara ya kwanza maishani mwake. Kumwacha umpendaye- akupendaye aende kwa mwanaume mwingine milele. Hata hivyo, bado mapenzi yake kwa Shangwe, na hasa kwa nchi ambayo aliamini ingeyumba endapo akili za Shangwe zingeathiriwa na jambo hili; akamshawishi Tunu; akaafiki kuolewa naye.

Tatizo kubwa lilijitokeza baada ya arusi yao. Kila mara, nyakati za usiku, Shubiri alishitushwa sana kwa kutembelewa ghafla na huyu mwanamke. Alipofika aliongea mengi ambayo hayaeleweki wala kukubalika. Zaidi, akimtaka mapenzi. Iko siku hata alithubutu kutamka kuwa yeye si Tunu bali ni Lulu, kwamba hakufa kama ilivyoaminika bali alikuwa amejificha mahala, humo mjini, akisubiri siku ambayo wangefunga ndoa. Hata aliomba kuwa kama Shubiri anaogopa amruhusu akabadili sura kwa plastic surgery ili awe kama mtu mpya, waoane. Shubiri hakumsikiliza wala kumruhusu kukaa. Alimpuuza kwa kila alichosema kwa kumtoa nje harakaharaka.

Angewezaje kuketi na mke wa Rais wake! Usiku wa manane, chumbani na kuzungumza kwa utulivu? Kwa ujumla, alimchukulia kama mwanamke mwenye wazimu wa mapenzi. Wazimu huo ulipoendelea ndipo alipoanza tabia ya kutolala nyumbani kwake, badala yake alijificha kijijini kwa mwalimu

Puta ambako alilala kwa utulivu na kufaidika sana kwa maongezi yake yenye hekima. Shubiri angeweza kuushukuru wazimu wa bi Tunu kwani, pindi akilala huko ndipo aliipata ile taarifa kuwa roho yake ilikuwa ikiwindwa usiku kucha kwa kosa ambalo hakulifahamu.

Naam, wazimu wa mapenzi, ambao wakati huo aliuchukulia kama mchezo au upuuzi ambao hakuhitaji kutiliwa maanani. Sasa sio mzaha tena. Tunu anadai tayari ameua. Amemwua Rais wa nchi na mume wake mwenyewe. Aweza kuwa amefanya hilo kwa ajili ya kumpenda? Alitamani kuuliza. Hakuthubutu kwani alilihofia jibu. Badala ya kuuliza aliishia kumtumbulia Tunu macho yenye swali hilo na mengi mengine.

Kwa sauti ya kilio, Tunu alilijibu swali hilo bila kuulizwa. “Nimemwua. Alikuwa na kila haki ya kufa. Unajua kuwa ameua watu wengi wasio na hatia? Unajua kuwa alitaka kukuua wewe zaidi ya kila mtu?” akasita. “Sikia, Shubiri,” aliendelea. “Niko radhi kunyongwa. Lakini sina budi kutangaza hadharani, dunia inisikie, kuwa ninayo furaha kubwa sana kumwua mtu huyu kwa mkono wangu.”

“Tunu,” hatimaye Shubiri aliupata ulimi wake. “Unajua kuwa umati mzima hapo nje umeshitushwa na madai yako? Unajua kuwa umma wa nchi yote hii unaisubiri kauli yako si kwa ajili ya kujua tu kilichotokea bali kwa ajili ya usalama na uhai wao? Unajua kuwa dunia nzima ya nje imeelekeza macho na masikio yake hapa kwako ikilisubiri tamko lako? Natumaini hayo unayajua kabisa. Hivyo, mpenzi, nakuomba unieleze kwa tuo kila kitu. Unaonaje ukianza kwa kunieleza sababu hasa ya kumwua Shagwe?” hatimaye lile swali lilimtoka.

Tunu alishusha pumzi kwa nguvu. Akamtumbulia Shubiri macho yake mazuri, macho ambayo yaliamsha kitu fulani katika tumbo la Shubiri, kitu kama kilekile alichokisikia siku ile alipoyaona machozi yake mara baada ya kumtaka aolewe na Shangwe. ‘Mapenzi?’ alijiuliza. Ameguswa na penzi la Tunu? Yeye! Ambaye hakuwahi kuyaonja tena tangu alipowahi kujihusisha na msichana huyu enzi za utoto? Hapana, nafasi ya mapenzi katika nafsi yake ilikuwa imemezwa kabisa na utumwa wake kwa nchi na wanachi wake. Mapenzi katika umri huu ilikuwa ndoto ya kipuuzi.

“Ndiyo. Nitaeleza yote,” Tunu alimjibu. “Kama nilivyosema

nimemwua kwa haki kabisa. Kitendo kilichonikera kuliko vyote ni kile ambacho amekitenda leo. Amemwua ndugu yangu, Lulu.”

“Amemwua au alimwua?” Shubiri aliuliza.

“Amemwua… leo hiihii. Tena hadharani, mbele ya Joram Kiango.”

Shubiri hakuelekea kumwelewa. “Unajua usemalo Tunu? Unajua kuwa Lulu alifariki miaka nenda rudi iliyopita? Nadhani ukajipumzishe nyumbani ili kesho uwe katika hali nzuri zaidi.”

“Sivyo, Shubiri. Nadhani huelewi. Labda nianze kwa kukutaka radhi kwa kosa kubwa ambalo tulikuetendea.” Akavuta tena pumzi na kisha kuendelea, “Unajua kuwa dadangu Lulu hakufa katika ajali ya mto kama ilivyoeleweka? Ni hila ya kitoto ambayo tuliipanga bila ya kujua matokeo yake, kwa ajili ya kukupenda…”

“Kunipenda!”

“Ndiyo. Unajua tulikupenda sana? Tulikuwa hatuna hali kabisa kwa ajili yako. Inashangaza kuwa hukutuamini. Hata hivyo, tulikula yamini kuwa tungeolewa wote pamoja na mtu mmoja tu, anayeitwa Shubiri. Wewe na wazazi wetu wote mlipotupuuza ndipo tukabuni mpango ule wa kitoto wa ‘kumwua’ Lulu ili miye ambaye nilikuwa mchumba wako wa halali niolewe nawe, kisha Lulu angetokeza, baada ya Shangwe kupata mke mwingine. Kwamba, tungekushawishi umchukue na Lulu pia. Hivyo, Lulu alijificha mjini, kwa mavazi na majina bandia. Kwa bahati mbaya, hata baada ya kile ‘kifo’ chake bandia bado hamkubadilika. Ilisikitisha sana hata miye mchumba wako halali nikalazimishwa kuolewa na Shangwe. Juhudi zetu zikawa hazina matunda. Lulu hakuiona tena haja ya kujitokeza, hasa baada ya kila alipokutembelea na kujaribu kukufafanulia yeye ni nani hukumwamini, wala kumsikiliza. Ikabidi atulie katika kijumba chake tulichokinunua, katika hali ya usiri huku akisafiri mara kwa mara. Mara mbili tatu aliamua kujiua, kwa kuona juhudi zake zikimletea dhiki badala ya faraja aliyotarajia. Lakini nilijitahidi kumshawishi aache mawazo hayo. Namshukuru Mungu kuwa alinisikia. Miaka yote hii amevumilia akiishi kama mkimbizi katika nchi yake mwenyewe.”

“Angeweza kuishi katika hali hiyo kwa miaka yote iliyosalia katika maisha yake kama Shangwe asingejitokeza leo hii na kumwangamiza kikatili akidhani kuwa ananiua miye…” Tunu alisita na kuanza tena kulia. “Amekufa kwa ajili yangu,”

alinong’ona akimkumbatia tena Shubiri. “Ni miye niliyekusudiwa kufa. Yawezekana kabisa kuwa alikubali kufa kwa ajili ya kuniokoa miye. Vinginevyo, angeweza kuitoa siri hiyo kwa Shangwe na kuiokoa roho yake.” Alisita tena. Alipoendelea alikuwa kama aliyemsahau Shubiri na kujisimulia mwenyewe. “Kifo cha Lulu ni kifo cha nusu ya uhai wangu. Nadhani adhabu aliyoipata mwuaji wake haimtoshi kabisa. Kama kweli uko moto ulioandaliwa kuwachoma shetani na wafuasi wake milele, ningeomba uongezwe mara mbili hapo utakapoichoma roho ya Shangwe.”

Kana kwamba ndio kwanza anamkumbuka Shubiri, alijikwanyua toka mikononi mwake na kumtupia macho makali, tofauti kabisa na yale aliyoyazoea Shubiri, macho yenye hasira, kisasi na ujasiri usiokadirika. “Ndiyo, nimemwua,” alifoka. “Rafikio nimemwua kwa haki kabisa. Maisha na vitendo vyake ni kama hadithi ndefu inayotisha na kusikitisha, hadithi ambayo haistahili kuyafikia masikio ya raia wake, ambao wengi walimtukuza na kumpenda sana. Si bado una hamu ya kuisikia hadithi hiyo? Haya, jiandae kusikia moja kati ya hadithi chafu, zinazonuka, zilizopata kutokea duniani.”

***

Kutwa nzima Joram na Nuru walishinda mbele ya televisheni katika chumba chao kipya walichokikodi. Macho yao yalitazama kwa makini kila habari iliyotangazwa. Ilielekea kuwa habari zote walizozisikia hawakuzifurahia. Ilikuwepo habari waliyoitaraji. Waliisubiri kwa hamu, si kwa ajili ya kuihitaji bali kwa ajili ya kuona itawasilishwa vipi, na wananchi wataipokeaje.

Ni wao waliomshawishi Tunu kwenda katika kikao kile muhimu na kueleza kila kitu kinaganaga. Joram alimshawishi hivyo Tunu baada ya kulikataa ombi lake la kufuatana nao huko. Alijitetea kwa kumweleza kuwa kwenda kwao ‘kungepunguza’ uzito wa suala zima.

Macho katika kioo cha televisheni, nyuso zikiwa zimechoshwa kwa matangazo yote yaliyokuwa yakiendelea. Walianza kushangazwa na ukimya huo wa ajabu. Saa zao zilisema kuwa ilikuwa yakaribia saa nane na nusu za mchana. Wakati wakitamani kuondoka ndipo matangazo yaliyokuwa yakiendelea yalikatizwa ghafla. Wimbo wa taifa wa Pololo ukapigwa. Baada

ya wimbo huo, sauti nzito, yenye majonzi na msiba mkubwa, ya Katibu Mkuu wa chama na Kamati ya nchi, ilifata ikisema:

…Kwa masikitiko makubwa, serikali ya Pololo inatangaza kifo cha kiongozi wake shupavu mtukufu, Abdul Shangwe. Kifo chake kimesababishwa na shambulizi la ghafla lililofanywa na maadui wa mapinduzi wa nchi hii nyumbani kwake. Hayati Rais amekufa baada ya kupambana nao kwa muda na kumjeruhi mmoja wao. Mkewe Rais, bi Tunu, pia amejeruhiwa kidogo katika shambulio hilo. Hata hivyo, hali yake si mbaya sana, yuko hospitali ambako amepumzishwa.

…Kwa mujibu wa Katiba ya Serikali na kwa maombi mengi ya wanakamati ndugu Shubiri Makinda, Waziri Mkuu ambaye leo hii aliomba kujiuzulu, ameombwa ashike wadhifa wa Rais hadi hapo uchaguzi mkuu utakapofanywa. Ndugu Shubiri akiwa mtu ambaye ameitumikia serikali kwa heshima na uaminifu mkubwa tangu utoto wake, amewaomba wananchi kuwa watulivu na wamkumbuke hayati Rais katika sala zao ili alazwe pema huko peponi.

…Taarifa hii ya tukio hili la kusikitisha litatangazwa baadaye…”

Joram na Nuru walitazamana. Mara wakaangua kicheko. “Afrika!” Joram alinong’ona katikati ya kicheko hicho.

Watu waliokuwa pembeni wakiisikiliza habari hiyo kwa hofu na mshangao walitazamana kwa chuki huku wakijiuliza; lipi la kuchekesha katika habari mbaya kama hiyo?

MWISHO

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment