Mifereji Ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA THE BOLD
************************************************************************
Simulizi : Mifereji Ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili
Sehemu ya Tatu (3)
Makaratasi yale yalionyesha ramani na mpango mji wa jiji la Nice. Kuna makaratasi yalionyesha nyumba kwa nyumba na jengo kwa jengo kwa jiji lote la Nice. Makaratasi mengine yalionyesha juu ya mifumo ya barabara ya jiji zima. Makaratasi mengine yalionyesha juu ya mfumo ya maji taka ya jiji zima na hapa katika karatasi hizi za mifumo ya maji taka ndipo hasa Spaggiari aliwataka awaeleze kuhusu mpango wake anao ufikiria. Katika karatasi hiyo inayoonyesha mfumo wa maji taka, Spaggiari akawaonyesha mahali ambapo benki ilipo na akaweka alama kwenye karatasi kisha akawaonyesha mfereji wa maji taka wa chini kwa chini ( Sewer) ambao unapita karibu kabisa na benki hiyo na pia akaweka alama kwenye mfereji huo kisha akawafafanulia zaidi. Akawaeleza kuwa upande ambapo mfereji huo unapita na kupakana na benki ni takribani mita 5 tu kutoka kwenye mfereji mpaka kwenye Kuba (Vault) ya benki. Hivyo basi kama wataweza kuchimba shimo la chini kwa chini (tunnel) lenye urefu wa mita 8 kutoka kwenye mtaro huo wa maji taka kuelekea upande wa benki basi watakuwa wamefika katikati ya sakafu ya vault ya benki ya Société Générale na kitu pekee kitakachobaki ni kutoboa tundu dogo kwa kwenda juu na watakalolitumia kuingilia ndani ya vault kutoka kwenye tunnel walilochimba kutoka mtaroni. Huo ndio ulikuwa mkakati wake.
Spaggiari aliwaangalia nyuso za wale waliokuwepo kwenye hicho kikao na alikuwa na uhakika kuwa wamevutiwa na mkakati huo ingawa walikuwa na maswali kadhaa.
Spaggiari akatoa fursa waulize maswali na swali la kwanza lililokuwepo kwenye vichwa vya wengi lilikuwa je, watakapokuwa chini wanachimba hilo shimo (tunnel) hawatashtukiwa kutokana na makelele na mitetemo watakayo sababisha. Spaggiari akawajibu kuwa japokuwa tunnel la urefu wa mita 8 wanaume kama wao 15 wana uwezo wa kulichimba ndani ya siku hata 3 lakini ili kuzuia kusababisha kelele na mitetemo amepanga kuwa shimo hilo litachimbwa taratibu kana kwamba wanakula chakula kwenye sahani kwa kutumia kijiko. Haijalishi itachukua wiki au miezi mingapi.
Swali lingine lilikuwa je itakuwaje kama vault ina ‘sensors’ za kuhisi mitetemo au sauti? Spaggiari akawajibu kuwa kuhusu hilo wampe kama siku tatu atafahamu hiyo vault ina ‘sensors’ zipi na ni namna gani watakavyo jiahami nazo.
Spaggiari akauliza kama kuna swali lingine. Hakukuwa na swali. Kisha akawaukiza, “who is in?” (“Nani atashiriki nami kwenye hili?”) wote 15 waliobakia kwenye kikao hicho walikubali kushiriki katika tukio hilo.
Spaggiari akawaeleza kuwa anawapa wiki moja kila mtu akamalize ratiba zake alizokuwa nazo, mwenye familia akaage na kudanganya anavyoweza kwani wakikutana baada ya hiyo wiki moja watakuwa na wiki kadhaa au pengine miezi kadhaa ya kutekeleza tukio hilo ambalo halijawahi kufanyika kabla.
Wakaagana, wakatawanyika.
SPAGGIARI NA GENGE LAKE WANAINGIA ‘KAZINI’
Wakati wenzake wakiwa wamerudi makwao kuaga familia zao ili warejee baada ya wiki moja kwa ajili ya ‘kazi’, yeye Spaggiari kesho yake alifika mpaka kwenye benki ya Société Générale na akaomba kuwa mteja afunguliwe sanduki jipya kwa ajili ya kuhifadhi vitu vyake vya faragha/siri ( safe deposit box) katika vault. Baada ya kukamilisha taratibu zote za kujaza nyaraka za maandishi na kulipia gharama za huduma hiyo hatimaye akapelekwa na muhudumu wa benki mpaka kwenye vault na kuonyeshwa kisanduku ambacho kitakuwa chake. Kisha muhudumu akatoka nje ya mlango ili kumpa faragha Spaggiari ahifadhi vitu vyake. Baada ya kuachwa peke yake Spaggiari akatoa saa kubwa ya muito (alarm clock) ambayo ilikuwa kwenye kibegi kidogo alichokuja nacho. Saa hii ilikuwa na ukubwa wa kufanana kabisa na saa kubwa ya ukutani. Lakini ilikuwa nzito zaidi. Na ilitengenezwa kuwa saa ya muito ambayo muda uliotegeshwa ukifika Saa inaita na kutetema (vibration). Spaggiari akaitegesha saa hiyo iwe inaita usiku wa manane. Kisha akaiweka kwenye kisanduku chake alichoonyeshwa. Kisha akakifunga kisanduku, akatoka nje akakabidhi funguo ya kisanduku kwa muhudumu na kurudi nyumbani.
Baada ya wiki moja kupita na wenzake kurudi kwa ajili yakuanza kazi, kwanza kabisa Spaggiari akawapa muhtasari juu ya alichofanikisha mpaka mda huo. Akawaeleza kuwa hawahitaji kuhofu kuhusu ‘sensor’ za mitetemo au sauti kwakuwa ameng’amua kuwa vault hiyo haina ‘sensor’ zozote zile. Walipo muuliza amejuaje, akawaeleza kuhusu Saa ya muito aliyoiweka kwenye hiyo vault na kuitegesha iwe inaita muda wa usiku. Na akawaeleza kuwa kwa siku kadhaa amekuwa akichunguza na hajaona taharuki yoyote kutoka kwa walinzi au alarm za ulinzi za benki zikilia hivyo ana uhakika kabisa hakuna ‘sensors’ zozote kwenye hiyo vault.
Spaggiari alikuwa sahihi kabisa kwani vault hiyo ni kweli haikuwa na sensor zozote, wenyewe wenye benki waliamini kuwa vault hiyo ilikuwa haiingiliki kwa namna yoyote (utterly impregnable) kwasababu mlango wake wa chuma ulikuwa mnene zaidi ya kuta tatu za nyumba ya tofali zikiunganishwa pamoja na mtu alihitajika kuingiza namba maalumu (combination) na kutumia funguo kubwa mbili maalumu ili aweze kuufungua. Pia kuta za hiyo vault zilikuwa haiwezekani hata mtu kuzigusa akiwa nje kwani vault ilikuwa kati kati ya jengo la benki na kuta zake zilikuwa nene kiasi kwamba zinazidi hata unene wa kuta tatu za nyumba ya kawaida.
Baada ya Spaggiari kuwapa wenzake muhtasari huo, kawaeleza kuwa hivyo basi saa hiyo ya muito watakuwa wanaitumia kama muongozo wa ziada ili wawe wanachimba kwa usahihi zaidi kuekekea chini ya sakafu ya vault (pinpointing). Baada ya kupeana muhtasari, Spaggiari akaondoka na wenzake ili akawaonyeshe eneo la kazi.
Mifereji Ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki Wala Ukatili Sehemu ya Nne
Also, read other stories from SIMULIZI;