Mikononi Mwa Nunda Sehemu ya Tano
IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA
*********************************************************************************
Simulizi: Mikononi Mwa Nunda
Sehemu Ya Tano (5)
Joram alibaki palepale sakafuni, akiwa amelala kifudifudi. Angetamani acheke, lakini soksi haikumruhusu. Isingekuwa vigumu kwake kujifungua kamba hizo. Ni hila ndogo tu ambayo huitumia wakati wa kufungwa, pamoja na mazoezi ya vidole ya muda mrefu. Hata hivyo, hakupenda kufanya hivyo mapema. Aliamua kusubiri kwani alikijua anachokihitaji. Kumpata mkubwa wao. Lazima mche uzaao matunda ya sumu ung’olewe badala ya tunda mojamoja. Hivyo, akaendelea kusubiri. Akajipumzisha kwa kulala chali, kiubavuubavu ama kukaa. Macho yake yalifanya kazi ya kukagua nyumba nzima kwa ujumla. Dirisha lilikuwa dogo kiasi cha kutoruhusu hata kichwa. Lakini endapo angehitaji kutoroka mlango usingemchukua dakika tano kumtii. Hakufanya hivyo bali aliendelea kusubiri.
Subira, subira! Hatimaye, kiza kikaumeza mchana. Usiku ukatawala; usiku ukakomaa. Sauti za watu waliokuwa wakipitapita mitaani zikapungua. Subira ikaanza kumchosha Joram, nafasi yake ikachukuliwa na hasira. Usiku wote huu? Vipi wasiporudi? Akajiuliza kimoyomoyo. Alijaribu kuipoteza hasira yake kwa kuusikiliza muziki wa bendi fulani ambayo ilikuwa ikitumbuiza katika jumba mojawapo la starehe mtaa wa pili toka hapo.
Usiku wa manane hasira za Joram zilitoweka ghafla pindi mlango ulipofunguliwa na adui zake wawili kujipenyeza ndani. Waliiwasha taa ya umeme ambayo ilitoa nuru kali iliyoyafanya macho yao wote kushindwa kuona vizuri. Macho ya Joram yalipooana na nuru hiyo aliweza kuwaona vyema adui zake. Macho yao yalionyesha, walikuwa wamelewa kiasi. Bastola zao zilezile zilikuwa mikononi.
“Wakati wako umekwisha,” Tom alisema akimsogelea Joram na kumkanyaga kichwa. “Dakika chache baadaye utakuwa marehemu ukizungumza na babu zako,”
“Na ni hapo utakapojua kuwa mchezo na kiumbe kama NUNDA ni wa hatari kwako,” Brown aliongeza. Walipoona kuwa Joram anashindwa kujibu walikikumbuka kitambaa kilichoufunga mdomo wake. “Mfungue tusikie atavyolia pindi roho ikimtoka. Sijui atalia kwa lugha gani,” Brown alishauri.
Tom akaifanya kazi hiyo. Soksi ambayo sasa ililowa udenda ikang’olewa toka kinywani na kutupwa kando.
“Namtaka mkubwa wenu. Namtaka Nunda,” lilikuwa ombi la kwanza la Joram Kiango mara tu alipopata uwezo wa kusema, ombi ambalo kama kawaida yake alilitoa kwa sauti ya amri isiyo na daliliyoyote ya hofu.
“Msikie! Eti anamtaka Nunda! Unamjua Nunda wewe? Unamweza Nunda wewe? Nunda! Usifanye mchezo naye. Jiji lote hili analitawala. Kuikana amri yake kunamfanya aamue kukuua. Wewe unakufa kwa kujaribu kumjua tu…” msemaji alikuwa Brown.
Joram alikatiza kwa kuuliza, “Unachotaka kuniambia ni kwamba humjui Nunda? Wote hamumjui? Wapumbavu basi ninyi. Mnawezaje kupokea jukumu la kuua mtu kwa ajili ya kuamriwa naye tu. Hamna lolote mtakalopata kwa kifo changu!”
“Kwa taarifa yako bwana Joram hamna yeyote anayemfahamu Nunda kati yetu. Ni gaidi mwenye kikundi kikubwa cha siri za ajabu. Sasa hivi aweza kuwa yuko dirishani akitusikiliza, tayari kutuua endapo tutasita kutimiza matakwa yake,” Brown alieleza.
“Uoga wa kuku. Mwanaume hatakiwi kuwa mwoga kiasi hicho. Mnaijua thamani ya maisha hata mkubali kuua bila ya kupata chochote? Mnajua kuwa kitanzi kinawasubiri mara tu mkitoka hapa? Msiwe wapumbavu. Niacheni niende zangu, nanyi muende zenu kama hamumfahamu Nunda. Sina kisa nanyi. Nilichofuata ni huyo Nunda tu,” sauti ya Joram ilikuwa na kejeli ilipoyaeleza hayo.
“Asitutishe huyu mtu, Bwana Brown,” Tom alisema akimgeukia mwenzake. “Hana budi kufa. Vinginevyo, ni sisi tutakaochinjwa na Nunda hadharani.”
“Kabisa. Tena nadhani tufanye haraka kwani mapambazuko yanakaribia,” mwenzake aliunga mkono. “Ondoka hapo, nimlenge shabaha. Nitapenda kumwua mwenyewe. Kesho asubuhi azolewe na gari la taka mitaani.”
Kicheko cha ghafla kilichomtoka Joram kikawafanya wote wasite na kuduwaa. “Mnajidanganya ndugu zangu. Hakuna yeyote kati yenu awezaye kuniua. Kwa taarifa yenu mimi ni Joram Kiango mwenyewe. Kamwe sifi kwa mkono wa mtu mwoga kama wewe. Nifungueni niende zangu kabla sijabadili mawazo na kuwachukulieni hatua za kisheria.”
Kwa muda waliduwaa kwa kutoamini vipi mtu ambaye yu mikononi mwa kifo aongee katika hali hii, Joram aliwatazama kwa macho ya kejeli, tabasamu la dharau likiwa wazi usoni kwake, tabasamu ambalo liliwaongezea hofu hata wakasita wakitazamana kama watu ambao hawakuyaamini masikio yao. “Tusidanganywe Brown,” Tom alikumbuka kusema baada ya kitambo hicho cha mshangao.” Hana lolote awezalo kufanya. Amefungwa wala hana silaha…” alilazimika kusita tena alipomsikia Joram akiangua kicheko kingine.
“Kufungwa!” aliwauliza “Yaani mnadhani kamba hizi hafifu zina uwezo wowote kwa Joram Kiango? Hivi hamjawahi kusikia watu wenye uwezo wa kukata kamba kwa mikono? Bila shaka mmewasikia. Labda tu nadhani hamfahamu kuwa mimi ni mmoja wao. Ninao uwezo huo na ninaweza kufanya hivyo wakati wowote.”
Adui zake wakatazamana tena. “Anawazimu. Sikujua, kumbe ana wazimu,” Brown alisema, “Kama si wazimu ni hila zake hafifu ambazo leo hazifui dafu. Ondoka Tom nimlipue kabla hajaupoteza zaidi muda wetu.”
“Usijisumbue kutikisika Tom. Iangalie bastola ambayo inakielekea kichwa chako.” Sauti ya Joram ilikuwa ileile yenye mzaha. Lakini safari hii iliwashtua zaidi kwani ilikuwa ikitokea juu badala ya chini alipokuwa amelala. Hivyo, wakageuka ghafla na kukutana na bastola yake ndogo ikikitazama kichwa cha Tom kikamilifu. Dakika hiyohiyo ile bastola iliyokuwa mikononi mwa Tom ilidondoshwa kwa judo na kutua katika mkono wa pili wa Joram. “Idondoshe bastola yako bwana Brown,” Joram alifoka. Safari hii sauti yake ikiwa kali pasi ya mzaha wowote kama awali. “Hima, vinginevyo nitawalipueni nyote kwa mpigo.” Bastola mbili mikononi mwake, zikiwatazama kikamilifu, zikamfanya Brown atii na kuiangusha miguuni mwake. “Rudi nyuma hatua nne,” akamwamuru. Brown alipofanya hivyo Joram alisogea na kuiokota bastola hiyo, akaitia mfukoni na kisha kuwageukia maadui zake kwa tabasamu.
“Wapumbavu nyie. Ni kweli kuwa hamumfahamu Nunda?” aliwahoji tena.
Wakatikisa vichwa kukubali.
“Basi mu wapumbavu wazuri sana. Mnajidhania werevu sana kujiita majambazi. Nitawakabidhi kwa polisi ambao ndio wanaojua la kukufanyeni. Msingenipinga nilipokushaurini kuniacha niende zangu ningekuacheni kwa amani.”
Ndipo alipowafungia kwa nje na kwenda mitaani ambako aliwapigia simu polisi. Aliporejea alifungua mlango kwa hadhari na kurukia ndani. Kinyume cha tegemeo lake la kuvamiwa aliwakuta mateka wake bado wameduwaa wakimtazama.
“Tuambie Joram, tafadhali,” Brown alisema mara tu alipoingia akiielekeza bastola kikamilifu mbele yao. “Hukuwa umefungwa kamba wewe?”
“Na silaha hakuwa nayo. Nimemsachi mwenyewe, kwa hadhari na uangalifu. Alichokuwa nacho ni pesa ambazo tumetoka kuzilewea. Mpaka sasa siyaamini macho yangu,” Tom aliongeza.
Joram akacheka. “Nilikuonyeni kitambo kuwa mnajidanganya,” aliwajibu kwa sauti yake tulivu.
“Mimi si mtu wa kuzuiliwa na kamba hafifu kama zile, wala bastola yangu hamwezi kufahamu nahifadhi wapi.”
“Yaani… yaani,” hawakujua waseme nini.
Polisi watano, wakiongozwa na Mkwaju Kombora mwenyewe, waliingia ghafla chumbani humo na kushangaa kumkuta Joram Kiango akicheka na majambazi wawili, mateka wake. Joram ambaye waliamini kuwa dakika hii alikuwa marehemu; maiti yake yakiwa mahali fulani jijini.
“Joram! Siamini!” Kombora alifoka.
“Amini usiamini mzee, zawadi niliyokuitia ni hii hapa. Watu wawili waliotumwa na Nunda kuniua. Usisumbuke kuwahoji hawamjuhi Nunda wala chochote juu yake,” alisema akitoa silaha zao na kumkabidhi Kombora. “Nadhani wote wana rekodi polisi. Bila hivyo, Nunda asingewafikiria kuwa wanafaa kuniua.” Akageuka na kutaka kuondoka.
“Usiondoke kijana,” Kombora aliita.
“Unajua kuwa unahitajika kueleza mengi juu ya watu hawa.”
Joram aligeuka na kumtupia tabasamu pana lililofuatiwa na sauti yake nyepesi isiyopingika.
“Nasikitika, mzee. Sitakuwa na nafasi ya kufanya hivyo. Hivi sasa kumekucha, bado ninayo kazi ndogo ya mwisho katika juhudi zangu za kumpata Nunda. Ninaye mpenzi wa kike, msichana mrembo ambaye ametishiwa na Nunda na kuniomba msaada wa kumwokoa. Nilimwahidi kumpata huyo Nunda kama zawadi ya arusi yetu. Leo ni siku ya kufanya hivyo. Lazima nimkabidhi Nunda kwake amfanye apendavyo,” alimaliza na kutoka haraka.
“Joram,” sauti ya Kombora ilimfuata.
Hakugeuka kumsikiliza.
***SURA YA SABA***
Alfajiri hii Adela Msufi ilimkuta bado kaduwaa chali kitandani bila ya angalau lepe la usingizi kumpitia. Macho yake yalikuwa yamevimba kwa machozi ambayo yalimtoka usiku kucha. Ingawa alijikaza sana akijipinduapindua kitandani, kwa nia ya kuyakausha machozi hayo, bado hayakukauka. Yaliendelea kububujika kama yatokayo katika chemchemi nzuri ya kupendeza.
Kilichokuwa kikimliza, mwenyewe kilimshangaza. Kwa kweli, hakujua wala kukiamini. Mapenzi! Ni kweli mapenzi yaweza kumliza mtu? Hasa mtu kama yeye? Alijiuliza. Kilichomshangaza zaidi ni swali lilelile alilokuwa akijiuliza tangu alipomwona, ni kweli kuwa ametukia kumpenda? Inawezekana akampenda mtu? Yeye! Yeye, ambaye tangu alipozaliwa hakuwai kumtazama mtu yeyote kwa jicho la mapenzi! Yeye ambaye alitukia kuamini kuwa kamwe asingempenda mwanaume yeyote katika dunia hii! Alijiuliza sana maswali hayo.
Hakupata jibu. Naam, hakulipata hadi leo baada ya kuona machozi yakimtiririka ovyo bila ya yote ayafanyayo kuyakomesha, kuzaa matunda. Leo, baada ya mtu mwenyewe kutoweka? Kwa nini asilifahamu hilo mapema? Angefanya lolote awezalo kuzuia maafa hayo. Lolote kwa bei yoyote. Hata kama ingemgharimu roho na damu. Angekuwa radhi kutoa. Naam, kwani amekwishagundua kuwa maisha yake hayana bei wala thamani yoyote bila ya yeye. Yeye tu. Yeye peke yake. Alikuwa kila kitu katika mwili na uhai wake. Alikuwa heri na fanaka yake.
Kwanini hakugundua kabla? Alijiuliza tena kwa uchungu. Machozi mengine yakaufuata mkondo wa yaliyotangulia na kudidimia katika mto ambao tayari ulilowa na kulipokeza godoro. ‘Kwa nini? Kwa nini? Kwa nini?…’ aliendelea kulalamika akijigeuza kifudifudi. Kwa ni…
Mara akasikia mlango wa chumba chake ukigongwa na kufunguliwa taratibu. Kwa uchovu mwingi akajigeuza polepole kutazama mlangoni. Mawazoni alitegemea kumwona mtumishi wa hoteli hiyo, akiwa na hili ama lile. Lakini hakitokea kuwa hivyo. Aliyeingia alikuwa mtu mwingine kabisa. Mtu yuleyule ambaye Adela hakutegemea kumwona tena duniani. Yuleyule ambaye alikuwa akiitesa nafsi yake kutwa kucha kiasi cha kukosa usingizi. Naam, yuleyule ambaye kwake alikuwa afya na uhai.
“Joram!” alifoka akiruka toka kitandani na kumkimbilia mlangoni ambako alimkumbatia kwa furaha. Akahisi uchungu wote uliokuwa ukimkereketa moyoni ukitoweka ghafla na nafsi yake kupokonywa na furaha, furaha kubwa isiyo kifani. Mara akajihisi akiipenda tena dunia na kuyathamini maisha, kinyume kabisa na maoni yake ya siku zilizopita. “Joram! Joram wangu. Furaha iliyoje kukuona tena? Oh… Joram,” alilalamika kwa sauti ya mnong’ono, sauti ambayo ilifuatwa na machozi mengi ambayo sasa yalikuwa faraja, si maombolezo.
Hali hiyo ya huba ilidumu kwa dakika moja tu. Dakika iliyofuata Adela alikwishakiepuka kifua cha Joram na kusimama mbele yake akimtazama kwa namna ya hofu na mshangao. “Joram, uko salama?” aliuliza.
Joram, ambaye muda wote huo alikuwa bado kasimama katikati ya chumba akitabasamu, alicheka kidogo. Kisha alimsogelea Adela na kuutua mkono wake juu ya bega lake. “Kurudi? Kurudi kutoka wapi mpenzi?”
“Ah! Joram usinifiche tafadhali. Nili… Nilikuja jana ofisini kwako nikiwa nimeleta shilingi elfu thelathini za malipo ya kazi hii niliyokupa, pamoja na kukuomba ukome kumsaka Nunda. Sikukukuta. Nikamkabidhi yule msichana wako. Lakini kabla sijaondoka niliwaona polisi wakifika na kuanza kuulizauliza juu yako. Walichosema kilinitoa machozi. Kwamba… kwamba umetekwa nyara na Nunda.” Kimya kifupi kikafuata. Adela alipoona Joram hajibu kitu akaongeza, “Ni kweli mpenzi? Niambie tafadhali. Sema ulivyookoka toka katika mikono ya mtu hatari kama huyo.”
“Haikuwa kutekwa nyara,” Joram akamjibu. “Nilijua kuwa naenda katika ziara fupi tu. Niliwadhiria kuandamana nao nikiwa na matumaini ya kuongeza chochote cha muhimu juu ya shughuli zangu za kumpata Nunda. Ziara hiyo haikuwa na mafanikio yoyote. Yote yale n’nayoyafahamu juu yake ndiyo hayohayo. Sina haja nyingine ya kupeleleza zaidi. Iliyobaki ni kuimaliza kazi uliyonituma. Leo hii.”
Machozi ambayo yalikuwa yakimtiririka Adela yalinyauka hima, kama ambayo yalimezwa na maelezo ya Joram. Badala yake kwa macho makavu, yenye dalili za hofu, alimtazama Joram kimya, kilichofuatwa na sauti fulani ambayo haikumfikia Joram kikamilifu. Sauti kama ya maumivu au maombolezo.
“Joram,” baadaye aliita. “Sijui mara ngapi nikuombe kuachana na harakati hizo. Tazama unavyotaabika na kuteseka. Tazama unavyoponea chupuchupu mara kwa mara. Joram, sikia mpenzi. Nitasema kwa mara nyingine kwamba maisha yako yanathamani kubwa kwangu. Kuwa kwako hai ndio uzima wangu. Vinginevyo, sina heri, Joram. Hivyo tafadhali mara elfu, acha tangu leo kumsaka huyo Nunda wako. Sawa, mpenzi?”
Badala ya jibu fupi, kama alivyotaka Adela, Joram alicheka kwanza na kisha kumjibu, “Nami mpenzi sijui nikuambie mara ngapi kuwa nimezoea kutimiza matakwa yangu. Maadamu niliwahi kukuahidi zawadi ya Nunda nitaitoa kwako leo na sasa. Sasa hivi…”
“Joram!” ilikuwa sauti kali. Sauti tofauti kabisa na ile ya Adela ambayo Joram aliizoea. “Joram!” alifoka tena. “Yaani maombi yangu yote kwako ni bure?”
“Bure kabisa.”
“Bure! Kwa nini, Joram?”
“Kwa kuwa Nunda ninaye sasa mikononi mwangu. Sina lolote jingine la kumfanya zaidi ya kukukabidhi kama nilivyokuahidi.”
“Joram!” sasa kilikuwa kama kilio badala ya maongezi. “Una… unachotaka kusema ni kipi Joram?… kwa… kwamba umemfahamu huyo Nunda?”
“Naam,” Joram alimjibu kamkazia macho.
Adela alitetemeka, nusura ashindwe kusema. Hata hivyo, alijikaza kisabuni na kuuliza kwa sauti hafifu yenye dalili za majonzi. “Una… unamfahamu? Ni nani basi? Nieleze, tafadhali.”
“Ni wewe mwenyewe, mpenzi wangu,” alimjibu kamkazia macho.
“Ni… nini?” Adela alifoka akitetemeka sauti na mwili. “Sijakuelewa Joram! Yaani!!!”
“Huna la kunielewa. Wewe mwenyewe ndiye Nunda Mla Watu ambaye ametaabisha na kutetemesha jiji hili kwa muda mrefu. Wewe peke yako! Wewe!”
“Joram!”
***
Kilifuata kitambo cha kimya, Joram akimtazama Adela kwa macho yake yanayocheka na uso wenye tabasamu. Adela aliduwaa kimya katikati ya chumba, domo likiwa limesahauliwa wazi kwa namna ya mtu aliyejikuta amesahau lugha zote duniani. Mwili wake uliendelea kutetemeka kiasi cha kuifanya kanga moja aliyokuwa ameivaa ilegee na kuanguka sakafuni na kumwacha na vazi laini la ndani ambalo halikuuficha mwili wake mzuri kikamilifu. Hivyo, umbo lake dogo, jembamba, lilikuwa dhahiri na kamili katika macho ya Joram, likiudhihirisha uzuri wake; uzuri mzuri; uzuri ambao macho hupenda kuuona daima; na mikono kutamani kuugusa na roho ikihitaji kumiliki.
“Pamoja na umbo zuri ulilojaliwa,” Joram alitamka alipomwona Adela akikosa la kusema. “Pamoja na kwamba u mtu, mtoto wa mtu, ambaye alikutegemea kuwa na utu kama yeye, bado umejigeuza mnyama, adui mkubwa wa watu na kuangamiza watu wengi wasio na hatia. Uzuri wako ni bure kabisa Adela. U mfano wa kaburi ambalo juu limepambwa vizuri hali ndani limejaa uozo. Ndivyo ulivyo wewe, mwuaji; adui; mwenye roho chafu kama shetani. Wewe u mwuaji mwanamke balaa asiyefaa kuwa hai…”
“Joram!” Adela alimkatiza kwa kufoka. Unajua umesema mengi sana hali mimi sijasema lolote? Unawezaje kuniita Nunda mimi? Mimi nawezaje kuwa Nunda? Watu waliwahi kuniambia kuwa una wazimu. Kumbe hawakukosea. Ni kweli, una wazimu. Unajiita mpelelezi hodari kumbe huna lolote ulijualo zaidi ya kubahatisha mambo yasiyofikirika wala kusadikika. Mimi… mimi niwe nani? Nunda?”
Haikuwa mara ya kwanza Joram kuitwa mwendawazimu. Hivyo, badala ya kukasirika alicheka. “Haikusaidii dada yangu,” alisema baada ya kicheko hicho kurejea katika hali ya tabasamu. “Kwa kweli, haitakusaidia chochote kukana. Ninao ushahidi tosha ambao unakutia katika hatia ya kujiita Nunda. Tangu awali nilikushuku: lakini sikudhani kuwa ungeweza kuwa Nunda mwenyewe. Nilidhani u mmoja wa watu wa mtu huyo ajiitaye Nunda. Hivyo, pindi nikikuacha huru na kufanya uchunguzi wangu nilikuwa nikiwatafuta watu unaoshirikiana nao na yeyote mwingine zaidi ya yale majambazi machache uliyoyajaza hofu na kuyalazimisha kukutii. Usitegemee kamwe kuwa damu isiyo na hatia uliyoimwaga ingeweza kukufikisha popote. Bei ya damu ni damu tu,” alisema kwa sauti ya kikazi, sauti iliyokuwa mbali na mzaha.
Adela alitulia kimya akimsikiliza. Kisha aliropoka ghafla akisema, “Koma! Sioni kwa nini uendelee kunihubiri mambo yako yasiyo na ukweli wowote. Una hakika gani kuwa mimi ni Nunda?”
“Hakika zote ninazo, zote ambazo mahakama ingezihitaji.” Akasema, “Nitazitaja na kukuomba uzikane endapo ni uongo. Tega sikio.” Akaanza kumweleza, “La kwanza ni kwamba wewe si Adela kama unavyojiita. Jina lako halisi ni Suzana. Suzana Msufi. Sio?”
Adela au Suzana kama alivyodai Joram, hakujibu lolote. Hivyo, Joram akaendelea, “Nilikushuku tangu ulipoingia katika ofisi yangu na kudai msaada wa kunusuriwa na Nunda. Haja yako haikuwa msaada bali upelelezi. Ulidhani kuwa nina uhusiano na polisi. Hivyo, ukataka kujua polisi wanafanya nini na wamefikia wapi. Ulilolifanya lilikuwa kosa lako kubwa la kwanza katika harakati zako za kiendawazimu. Hukujua kama ulikuwa ukijiingiza mwenyewe mkononi mwa Joram Kiango, badala ya Joram kuwa mikononi mwako kama ulivyodai katika waraka ulionitumia.
“Shaka yangu juu yako ilizidi mara nilipokuambia kuwa niliwahi kukuona West Bar nawe ukagutuka na kukana sana. Hukujua kuwa macho ya Joram yakishamwona mtu hayamtoi akilini kamwe. Kukataa kwako kulionyesha kuwa kuna jambo unaloficha, jambo la kutisha, vinginevyo usingekana kwa nguvu namna ile. Ndipo nilipojizamisha kupekua yote ambayo yangeweza kupatikana juu yako. Naam, niligundua mengi. Mengi mno. Yote hayo yakiwa machafu na yanayotisha mno, la kwanza likiwa lile la kufahamu kuwa ni wewe uliyemwua Ukeke Maulana kwa mkono wako mwenyewe. Ulimwua baada ya kumshawishi mahaba hata akaridhia kukupeleka ufukoni. Hilo niligundua baada ya kujiuliza ni kipi ambacho kinaweza kumwelekeza mwanaume yeyote sehemu kama ile saa kama zile za usiku. Majambazi? Kwamba alitekwa nyara? Hilo nililikanusha mara moja baada ya kuwasikia polisi wakizungumza walivyoyakuta maiti yake yakiwa yamelalia usukani. Ilikuwa kinyume kabisa cha mwanaume ambaye alikuwa mikononi mwa majambazi, akijua kabisa kifo chake kimewadia. Sijui ulipata nini katika mifuko ya marehemu yule. Lakini uchunguzi wangu umenionyesha kuwa injini ya gari lake na matairi viliibiwa na wapita njia tu. Pengine wavuvi waliokuwa wakienda au kutoka kazini kwao. Kweli, au uongo?”
Hakumjibu. Aliendelea kuduwaa wima mfano wa sanamu iliyosimamishwa katikati ya chumba.
Joram akaendelea kueleza, “Kifo cha mzee Matoke hakikutofautiana na cha Ukeke. Naye pia ulimwua kwa mkono wako mwenyewe. Nina hakika, kwani kisu kilichotumika kumwua Ukeke ndicho kilekile kilichomwua Matoke. Naye pia alikutwa katika hali ya mtu aliyekufa kirahisi akisubiri kisu hicho kimchome kama mwanaume yeyote anayesubiri busu. Ulimshawishi mahaba, aliposhawishika ukaichukua nafasi hiyo kumwangamiza. Mbinu hizohizo ulizitumia kwa lile jambazi hatari Makonko. Alikuwa hodari kwa wanaume wenzake lakini kwako akaanguka kirahisi. Sivyo dada yangu?”
“Tangu hapo ukaupenda mchezo wako wa kutisha na kuangamiza. Uliwatisha matajiri na wakakupa chochote ulichodai. Ukayatisha majambazi hata yakazitii amri zako na kuua wakati wowote ulipotaka. Umechuma mengi, fedha na sifa, sifa za kuitwa Nunda; jiji zima likikuogopa na kudhani kuwa u jitu moja kubwa; lenye kikundi kikubwa cha wafuasi hodari wa kuua. Itakuwa kichekesho kwa jamii kugundua kuwa wewe msichana mdogo kiasi hicho, mzuri kiasi hicho; ndiye tishio ambalo kila mtu aliliogopa; hatari zaidi ya mnyama mwenye kichaa.” Sauti ya Joram ilibadilika na kuwa yenye huzuni sana alipoongeza, “Dada yangu, mpenzi; mtoto mzuri kama wewe unawezaje kutenda unyama mzito kiasi hicho?”
Sauti ya Joram ilikuwa na nguvu fulani ya ajabu kwa Adela au Suzana, msichana huyo alilainika mwili mzima na kujikuta akianguka sakafuni. Kwa juhudi kubwa akajizoa toka hapo chini na kujivuta hadi kitandani ambako aliketi kwa kujibwaga. Machozi, ambayo yalinyauka kitambo, yakaanzisha mkondo mwingine toka machoni mwake na kuyaendea mashavu.
Joram alimtazama kimya, kwa muda. Kisha aliliendea kochi lililokielekea kitanda hicho na kuketi. Muda mrefu ulikuwa umepita kabla hajavuta. Hivyo, alipoketi alijiwashia moja ya sigara zake na kuanza kuivuta kwa utulivu. Macho yake yalifuata fundo la kwanza la moshi hadi lilipotoweka angani. Fundo la pili alilifanya kuwa mkondo mrefu ambao ulipaa katika mstari mnyoofu hadi darini.
Baada ya dakika moja ya mchezo huo aliyasafirisha macho yake hadi kitandani ambako kilio cha sauti ndogo ya kike kilikuwa kikitokea. “Joram!” sauti ya kike iliita mara macho yao yalipokutana. “Nimeona na kuamini kuwa u mpelelezi mzuri na mwenye busara kuliko nilivyokutegemea. Siku zote nilikuwa nikidhani kuwa wapelelezi hodari ni wale wa hadithini tu, kumbe nilikosea.”
Akameza kitu kilichomkaba koo kuizuia sauti yake isitoke kikamilifu. Kisha akaendelea, “Hata hivyo, Joram. Tuseme mimi ni Nunda, unadhani ndio mimi? Bado mimi ni msichana mzuri, akupendaye; msichana mwenye mali nyingi iliyofichwa mahali penye usalama; msichana akupendaye kwa moyo wake wote na roho yake yote. Na ninaamini ni wewe tu ambaye umeweza kugundua kuwa mimi ndio Nunda. Unaonaje tukisahau yote yaliyopita na kwenda zetu kuishi nchi yoyote yenye anasa na starehe? Ulaya ya Magharibi au popote pengine upaonapo. Unasemaje, Joram?” Joram alipotaka kumjibu alikatizwa kwa, “Usijibu harakaharaka, tafadhali. Fikiria kwanza utakavyokuwa mume wa msichana mzuri sana ambaye wengi wamemlilia kwa jasho na damu. Na…”
“Siuhitaji uzuri wako wa nje. Ndani u shetani anayetisha zaidi ya shetani mwenyewe,” Joram alifoka.
“Na… na kuwa mume wa mke tajiri sana. Fedha yote itakuwa mikononi mwako uitumie upendavyo.”
“Wala sihitaji pesa yako hata kidogo. Ni fedha chafu, nuksi inayonuka.”
Kikafuata kimya kifupi, kimya ambacho kilitumiwa kwa msichana huyu na mvulana wake kutazamana. Hakuna aliyejua aseme nini. Ghafla msichana alikivunja kimya hicho kwa kuinukia ghafla akisema, “Nina hakika, Joram huifahamu thamani ya mwili wangu ambao nautoa kwako. Hujui kuwa nina chochote ambacho mwanaume wa umri wako anahitaji. Nadhani wewe u mmoja wa wale wanaume wachache ambao hawaioni thamani ya mwanamke hadi anapokuwa uchi. Nitakuonyesha Joram, uone nilivyo. Naamini umbo langu la ndani litakushawishi.”
Alipomaliza maneno hayo tu alilivuta juu vazi lake na kubaki na lile la ndani tu. Hilo pia aliliteremsha ghafla. Sasa alisimama mbele ya Joram akiwa mtupu kama alivyozaliwa. Mwili wake mwekundu, wenye kiuno kilichokatika kike kabisa, mapaja yanayomeremeta na matiti ambayo hayakuonyesha dalili yoyote ya kuinama, ulisimama mbele ya Joram; ukimtazama. Macho yake yalilainika, sauti yake ikiwa na huba pindi aliponong’ona, “Nitazame, mpenzi Joram. Ona nilivyo kamili. Ni wengi waliokuwa wakiulilia mwili huu. Kwako nautoa bure.”
Kwa mara ya kwanza katika maisha yake Joram akujua afanye nini mbele ya mtu kama huyo. Ingekuwa rahisi kwake kumkabili adui mkubwa mwenye bastola zaidi ya msichana huyo mzuri ambaye hakuwa na chochote mwilini wala mkononi. Bila ya kujua alifanyalo alijikuta kainuka na kurudi nyuma hatua mbili huku jasho jembamba likimtoka.
“Joram, Joram wangu. Siku zote nilikupenda Joram. Unajua kuwa nilikupenda. Njoo tafadhali,” aliita kwa sauti ambayo ilimtesa Joram zaidi ya maumivu ya konde. Kisha alitulia kwa muda akimtazama Joram kwa makini. Halafu, kama aliyepata wazo jema zaidi alikirudia kitanda na kujilaza chali juu yake. Miguu akaifungua na macho kuyaelekeza kwa Joram. “Njoo mpenzi wangu. Njoo. Mimi ni wako, kwa ajili yako. Unahitaji kuujua ubora wangu, pengine. Njoo.”
Joram hakuinua mguu toka aliposimama. Zaidi ya dakika mbili zilizopita msichana huyo aliruka ghafla toka kitandani na kusimama mbele ya Joram. Alikuwa bado mtupu, lakini hakuwa tena mikono mitupu. Badala yake mkononi alishikilia jisu kubwa, refu, ambalo lingemeremeta kama si kwa ajili ya damu kavu iliyogandamana juu yake kwa kutofutwa kikamilifu baada ya kazi iliyotangulia.
“Hiki ni kisu kilichowaua wote waliokufa kwa kisu,” ilisema sauti ya kike, sauti katili yenye majivuno; tofauti kabisa na ile yenye huba aliyokuwa akiitumia dakika chache zilizopita. “Hupendeki Joram. Hilo nimeliona baada ya kujaribu kila ambacho ningeweza kufanya. Sina lawama. Umeyataka mwenyewe. Hupendwi ukapendeka. Utakufa kwa kisu hiki leo na sasa.”
Ndio kwanza tabasamu pevu likachomoza katika uso wa Joram Kiango.
***
“Alaa! Hatimaye umeamua kupambana nami ana kwa ana baada ya kuona hila zako ambazo ulizitumia kuwaua akina Ukeke kwangu hazifai?” Joram aliuliza akiwa amesimama kikamilifu mbele ya umbo hilo tupu, lenye kisu mkononi. “Yaani umeridhika na hoja hizo chache nilizozitoa juu ya kuwa kwako Nunda?” alicheka kwa sauti ndogo kabla hajaongeza, “Angalia kisu hicho. Kitakukata mwenyewe badala yangu. Kwangu, ni mchezo wa kawaida kushughulika na mtu mwenye kisu. Nakushauri uwe msichana mtii, ukitue, uvae mavazi yako na kuwasubiri polisi ambao watawasili hapa wakati wowote.”
“Polisi!” alifoka kike akipiga hatua nyingine kumwendea Joram. “Wataikuta maiti yako na yangu. Nisingependa kuua Joram. Nimelazimika baada ya kuona hutaki kunielewa. Nimekutaka hutakiki, nimekupenda hupendeki. Sasa hivi ndio kwanza nimegundua kuwa nilikosea kudhani kuwa nakupenda. Haiwezekani nikupende kwani wewe u mmoja wa wanaume wenzako. Nyote mu wakatili wenye mioyo ya kinyama. Sasa hivi umenitukana sana ukiniita shetani na matusi mengine chungu mbovu. Lakini kama wanaume wenzako wote hukujishughulisha kuuliza kwa nini niliamua kuwa mnyama kiasi hicho. Kama wote wengine unadhani na kuamini kuwa yote niliyoyafanya ni kwa ajili ya fedha. Sivyo, Joram. Maadamu nilikosea na kudhani kuwa nakupenda, bado nitakosea kwa mara ya mwisho nikuelekeze kwa nini nilifanya vile. Ndivyo, mimi ni Nunda. Nunda mwenyewe, mla watu, aliyekula watu akakinai. Kwa jina halisi ni Suzana Msufi, kama ulivyogundua. Nitakusimulia yote kabla sijakuua, ufe ukijua kisa cha ununda wangu.”
Suzana akakirejea kitanda ambako alivuta kanga moja iliyokaa ovyoovyo na kuifunga kifuani. Hakujali kuvaa vizuri. Hivyo, sehemu kubwa ya mwili wake ilikuwa hadharani, paja moja nje, nusu ya titi moja wazi.
Joram aliitumia nafasi hiyo kwa kuiwasha sigara nyingine. Suzana alipoketi kitandani naye alirejea kochi alilokuwa kalikalia na kujistarehesha tena juu yake. Akavuta mafundo kadhaa ya moshi na kuyasukuma hewani kwa nguvu. Kisha alimwelekea Suzana kikamilifu na kuanza kumsikiliza.
“Ni hadithi ndefu sana Joram. Nitajitahidi niwezavyo kuifanya fupi. Hadithi hii ilianza kijijini. Kijiji cha Kurio ambacho kiko katika Tarafa ya Kwamtoro, wilayani Kondoa. Ni huko ambako alizaliwa msichana huyu aliyetukia kuwa Nunda, tishio la wanadamu.”
“Wakati huo alikuwa msichana mdogo bado. Alicheza na wenzake kwa furaha daima. Wote walimpenda, naye aliwapenda. Akijua kuwa anapendwa alitenda yote aliyodhani mema na kuyaepuka yale maovu. Ulipofika umri wa mtoto huyo kwenda shule alijiunga kwa furaha na kusoma kwa juhudi. Mapenzi yake kwa masomo yakamfanya atokee kuwa mwanafunzi mwenye hekima ambazo ziliwashangaza walimu na kuwatisha wenzake.”
“Mara msichana huyo alijikuta yatima, hana mama. Kisa? Baba yake mzazi katika ulevi wake alimpiga mama yake usiku kucha hata akamvunja mgongo. Mama mtu alipelekwa hospitali ambako alikata roho baada ya kuteseka kwa maumivu makubwa kwa siku kadhaa. Baba mtu akaoa mke wa pili ambaye alimgeuza msichana huyu kijakazi ambaye mshahara wake ulikuwa matusi na kupigwa mara kwa mara. Akawa mnyonge asiye na hamu ya maisha. Daima aliomba kifo kimtwae na kumpeleka aliko mama yake. Kifo hakikutokea.”
“Akiwa bado kinda katika malimwengu yote hakujua lolote zaidi ya mema peke yake. Lakini ilimshangaza kuona wanaume walivyokuwa wakimtazama kwa tamaa. Ilimshangaza zaidi siku moja alipovutwa katika kona moja yenye kiza na mvulana mmoja mkubwa ambaye alimvua nguo na kumtia mweleka. Mweleka huo ulifuatiwa na kitendo ambacho kwanza kilimshangaza na kisha kikamwumiza, maumivu makali mfano wa jeraha bichi lililotiwa msumari wa moto juu yake. Maumivu hayo yalipopungua alishuhudia damu nyingi iliyotapakaa mapajani mwake. Kwa mwendo wa kujikongoja akajikokota hadi nyumbani kwao. Ingawa kitendo hicho alikisahau lakini ulikuwa mwazo wa mashaka yake juu ya utu wa mwanaume.”
“Aliendelea na masomo yake kwa moyo uleule. Kaka yake, ambaye alikuwa darasa la saba, akafeli mtihani lakini baba yake alimsafirisha hadi Dodoma mjini ambako alimwingiza katika shule za kulipia. Yeye alipofika darasa la saba na kuukalia mtihani alipita kama mzaha. Akachaguliwa kuingia shule ya sekondari ya Wasichana ya Msalato. Lakini, kwa mashangao, alimsikia baba yake akidai kuwa hangekwenda huko shuleni ili asubiri kuolewa. Hakuwa tayari kuolewa. Hivyo, ulipofika wakati wa kuingia shule aliondoka bila ya kuaga, akiwa hana vitu alivyohitajiwa kuwa navyo. Alisoma kwa bahatibahati akijisaidia kwa vibarua alivyofanya wakati wa likizo. Akili zake shuleni zingeweza kumvusha kwa matatizo ya kiuchumi na kimawazo ambayo yalikuwa yakimkabili usiku na mchana.”
“Katika kipindi hicho cha dhiki alizidi kuushuku utu wa wanaume kwa wanawake. Wote aliokutana nao walikuwa wakimtamani na kuisifu sura na umbo lake kwa nia moja tu; ya kujistarehesha kwa kile ambacho hakuelewa maana yake. Kilekile ambacho alikuwa hajasahau maumivu yake. Yale maumivu ambayo kila alipoyakumbuka alitetemeka. Hivyo, aliyaepuka maneno na vitendo vyote ambavyo vilikusudiwa kumwelekeza katika mweleka mwingine. Kuepuka kwake kukawafanya wanaume kunong’ona lile na hili juu yake. Kwa mshangao wake, baadhi ya wanawake wenzake walijiunga na minong’ono hiyo. Hakuelewa kwa nini wanawake hao wasiwe upande wake. Ndipo alipofahamu asili ya unyonge wa mwanamke, asili ya kukubali kwao kuwa watumwa wa wanaume wakiwapikia; kuwafulia; kuwalimia; kuwabebea kuni na maji vichwani; kuwabebea watoto wao miongoni kutwa; kushinda nyumbani wakiwasubiri na mambo mengine mengi yasiyoorodheka huku wakilazimika kustahimili kashfa na vipigo vya mara kwa mara. Akang’amua kuwa asili ya yote hayo ni unyonge wa mwanamke kuridhika na yote yamtokeayo, hasa mwanamke wa kijijini.”
“Hakuwa tayari kuifuata asili hiyo, kuwa mnyonge! Hivyo alipokitia mkononi cheti chake cha kufuzu kidato cha nne alikataa kwenda kijijini kwao, badala yake akaelekea Dar es Salaam ambako alitegemea kupata kazi ya kuajiriwa; aanze maisha ya kujitegemea. Ofisi ya kwanza aliyofikia alikuwa bwana mkubwa mmoja aliyejiita Ukeke Maulana. Huyu alimwahidi kazi mara moja na kumtaka wakutane mahala fulani usiku huo, mahala ambapo palitokea kuwa sirini. Na kilichofuata kilikuwa kile kitendo ambacho msichana huyu hakukitaka. Alilazimika kuanguka tena chali, mweleka ambao ulifuatiwa na kitendo kilekile. Lakini ilishangaza alipoona badala ya maumivu alipatwa na aina fulani ya faraja ambayo hakuwahi kuionja maishani mwake. Hata hivyo, hakukubali kumwona tena mtu huyo ingawa aliahidiwa kazi nzuri ofisini.”
“Siku chache tu baada ya kitendo hicho alijikuta akiwa mjamzito. Dhiki mpya ikaingia katika maisha ya msichana huyo. Hakujua aupeleke wapi mzigo huo. Unyama mwingine wa mwanaume kwa mwanamke! Kwa mara nyingine akayatupia jicho jingine maisha yake ya nyuma. Tangu alivyoonewa na baba yake, alivyofanywa yatima; alivyoteswa na yule mvulana utotoni; alivyotumbukizwa kwenye janga la dhiki na ulikuwa kama mkondo ambao siku zote ulimlazimisha kuelekea katika kwato katili za kiume ambazo zilimkanyaga tangu mwilini, akili hadi matumaini na huku zikiwa na kiu ya kuendelea kumkanyaga. Afanye nini kujitoa katika mkondo huo? Alijiuliza kwa machozi. Hakuona njia ya kutokea. Kazi asingeipata tena akiwa mjamzito. Mahala pa kuishi hakuwa napo baada ya kufukuzwa toka katika nyumba aliyofikia kwa kukosa pesa za kulipia.”
“Ndipo alipofikia hatua ya kufanya kile ambacho kamwe hakupenda kukifanya, kujikabidhi mikononi mwa wanaume ambao waliuchezea mwili wake kama mzoga kwa malipo hafifu ambayo yaliandamana na kashfa. Ulikuwa wakati mgumu kuliko nyakati zote alizowahi kupitia, kulazimika kumkumbatia mwanaume yeyote; mbaya kwa mzuri; anayetisha kwa anayechekesha; anayetesa kwa anayesimanga; anayependeka kwa asiyependeka. Yeyote, mradi ana chochote ambacho kingemwezesha kuishi. Wote waliomfikia ingawa aliwalaki kwa tabasamu, lakini moyoni aliwachukia zaidi ya sumu. Alijua ni mbwa mwitu katika ngozi ya kondoo, haja yao si zaidi ya kuburudisha nafsi zao zenye kiu isiyokatika. Na alimchukia zaidi yeyote ambaye alijitia kumpenda na kusisitiza ndoa. Mtu wa aina hiyo alimwona kama chui ambaye alitaka kuwa na zizi la mbuzi mwituni. Aliona kheri aendelee kuwa jamvi la wote badala ya kigoda cha mmoja wao.”
“Wakati ulipotimu alijifungua mtoto mzuri wa kiume. Usiku uleule ambao alimzaa akafanya kile ambacho wasichana wote waliopotoka hufanya mara wapatapo mtoto asiyehitajika. Alimnyonga na kuutumbukiza mzoga chooni.”
“Hakumtupa mtoto huyo kwa ajili ya upotovu kama wasichana wengine ili aendelee kuitwa msichana badala ya mama, la. Wala haikuwa kwa hofu ya kushindwa kumlea ipasavyo. Kilichomfanya amtupe hasa ilikuwa kule kuona kuwa kazaa kiumbe mwingine wa kiume, kiumbe mwingine ambaye angeendeleza kanuni ileile ya kuwafanya wanawake watwana au vyombo ambavyo vililetwa duniani kumstarehesha mwanaume. Yeye ambaye anahitaji kuiondoa kanuni hiyo, yeye ambaye ameteseka kwa ajili ya kanuni hiyo, vipi akubali kutunza kiumbe mwingine wa kiume? Ni hilo ambalo lilimshawishi kuangamiza damu yake mwenyewe.”
“Kitendo chake kilifahamika kwa jirani ambao waliiarifu polisi. Msichana huyo alikamatwa na kufikishwa mahakamani ambako alikiri kosa lake lakini hakuruhusiwa kueleza hoja zake. Akahukumiwa kifungo cha miaka mitatu na kazi ngumu. Huko gerezani aliteseka sana. Alipofunguliwa alirejea mtaani, katika vichochoro vilevile vya Buguruni, Magomeni, Kariakoo na kwingineko. Hali ikiwa ngumu kiuchumi, wanaume waliadimika mno. Ikawa vigumu kuwaona wakimfuata kama awali. Hivyo, akawajibika kuomba kazi ya kuuza pombe kwenye mabaa mengi, akikutana na watu wengi. Kati yao alifahamiana na majambazi, wafanya magendo na wagongaji, kama ambavyo alikutana na mahakimu, walimu na wakulima. Wote hao walimshirikisha katika harakati zao za maisha na siri zao bila ya kujijua. Ndipo akapata fursa ya kuwafahamu majambazi wengi na mienendo yao.”
“Ni wakati ambao alikuwa ameajiriwa West Bar alipokutana na mtu ambaye kamwe asingeweza kumsahau, mtu ambaye alikuwa kisa hasa cha kuanguka kwake kimaisha, adui yake mkubwa, Ukeke Maulana. Hasira zikampanda ghafla na njaa ya kulipiza kisasi kumteka hata akamwendea na kumshawishi mapenzi. Alipolaghaika badala ya kupokea mahaba aliyoyategemea alijikuta akipokea pigo la kisu, pigo lililomtoa duniani.”
***
Joram aliisikiliza hadithi hiyo kwa makini sana, macho yake yakimtazama Suzana hali mikono yake ikishughulikia sigara moja baada ya nyingine. Msichana huyo aliposita na kuvuta pumzi kwa nguvu, Joram alijirekebisha juu ya kiti na kunong’ona jambo ambalo halikumfikia Suzana.
“Msichana huyo ni mimi, Joram. Mimi hapa. Na hiyo ni hadithi ya kweli inayohusu maisha yangu.” Baadaye alisema kwa sauti ndogo, iliyotofautiana na ile aliyotumia kueleza habari nzima.
“Ndiyo,” Joram alimjibu. “Toka hapo naweza kueleza. Toka ulipotoka ufukoni ambako ulimwua Ukeke ndipo ulipomkuta Mohamed Matoke akibarizi nje ya nyumba yake, kama ilivyokuwa kawaida yake. Ukiwa bado na hamu ya kuua ukamwendea na kumshawishi mapenzi hata mkafuatana chumbani ambako ulimwangamiza. Siyo?”
“Kidogo umekosea,” Suzana akamwelekeza. “Kwa kweli, mara baada ya kumwua Ukeke nilichanganyikiwa nikiwa sijui la kufanya. Nilipokuwa nikienda zangu nisipokujua mzee huyo aliniita na kuanza kunitongoza. Hasira zilinipanda hasa nilipowaza kuwa huyu ni mwanaume mwingine ambaye alikuwa na njaa ileile ya kumfanya mwanamke kuwa chombo chake cha starehe. Anichezee kwa muda na kisha kunitupa! Ndipo nikaamua naye afe. Uoga wake pindi akifa ukamfanya aanze kunionyesha alikoficha fedha yake, fedha ambayo, kwa kweli, sikuhitaji wakati huo. Akawa amenipa wazo jipya. Wazo la kujipatia fedha nyingi. Hivyo, nilipomwacha nilifikiria namna ya kuipata fedha hiyo, ingawa sikujua namna ya kuitumia. Ndipo liliponijia wazo la kuyatumia majambazi yote niliyoyajua kuendelea kuua huku na huko hali mimi nikipita na kukusanya faida. Hakuna hata mmoja wao aliyenijua wala kunidhania kuwa ningeweza kuwa Nunda. Wote waliniona kama kila mwanaume amwonavyo mwanamke; mnyonge asiye na uwezo wa kufanya lolote.” Akacheka kidogo kabla hajasema, “Sijui ningeendelea mpaka lini kama usingetokea na kuharibu mkondo wangu wa kulipiza kisasi.”
Joram naye alicheka kidogo na kumjibu, “Ungeweza kuua jiji zima na bado usiibadili kanuni uliyokuwa ukipambana nayo. Kisasi siyo dawa ya kuondoa maradhi hayo ya ubinafsi ambayo yanaitesa jamii na dunia nzima. Sasa vaa vizuri, tupa kisu hicho tujadili hali yako ya baadaye.”
“Hapana. Bado nina kazi moja ya mwisho,” Suzana alimjibu akiinuka. “Nitakuua wewe, kisha nijiue na kuisahau dunia hii na maovu yake.”
“Usijidanganye, mpenzi wangu,” Joram alijibu akiwa amejituliza kitini, “Kuniua huwezi, wala sitapenda kukuona msichana mzuri kama wewe ukijiua. Hivyo, keti pale tuzungumze suala lako.”
“Joram!” sauti ya Suzana ilikuwa na mshangao. “Yaani hujanichukia kiasi cha kuniona mtu anayestahili kufa? Tuseme hukukusudia kunipeleka mahakamani nikanyongwe?”
Joram akatikisa kichwa kukataa. “Ndiyo, wewe ni mwuaji mkubwa, shetani mdogo ambaye amemwaga damu nyingi isiyo na hatia. Lakini bado u msichana mzuri kuliko wazuri wengi niwajuao.”
“Joram!” akafoka kwa mshangao uliochanganyika na hofu. “Sikujua kama wanipenda. Nilidhani haja yako ni kuniangamiza kama wanaume wenzako. Kumbe hatimaye ametokea mtu mmoja tu duniani ambaye ananipenda. Ni wewe peke yako,” akasita. “Kwa ajili hiyo sitakuua. Nitakufa peke yangu. Nife nikijua kuwa nimemwacha duniani mtu anipendaye,” alimaliza kusema akijiweka sawa na kukielekeza kisu ubavuni mwake.
Joram aliinuka hima akisema, “Usifanye hivyo Suzana!”
“Usiniguse mpenzi.”
Dakika hiyohiyo mlango ulifunguliwa na kuwaruhusu askari wanne wakiongozwa na Inspekta Mkwaju Kombora ambaye bastola yake ilimtangulia wazi mkononi.
“Usithubutu,” Kombora alifoka kwa sauti yake
Haikusaidia. Dakika hiyohiyo kisu kilikuwa kikizama katika moyo wa Suzana. Kikamlainisha na kumfanya aanguke chali kitandani. Kombora alimkimbilia na kuambulia damu nyingi ambayo ilibubujika toka katika jeraha kubwa la jisu hilo. Juhudi zake za kuizuia damu hiyo isiendelee kutoka zilikuwa kazi bure kwani macho ya Suzana yalianza kuelekea katika dalili ya kifo. Baada ya muda akawa mzoga uliolala nusu uchi. Ilikuwa baada ya kuliita polepole jina la Joram na kushindwa kusema chochote alichokusudia kusema.
“Umechelewa sana Inspekta,” Joram alisema akiyatoa macho juu ya maiti na kumtazama Kombora.
“Nimechelewa! Ulijuaje kuwa nilikuwa nikija?”
“Nilijua wazi kuwa ungenifuata tangu nilipokugusia kumtia Nunda mikononi leo. Naamini ulikuwa nyuma ya mlango ukisikiliza maongezi yetu kwani nilisikia minong’ono yenu. Hivyo, sitakuwa na haja ya kueleza chochote zaidi.”
*****MWISHO*****MWISHO****MWISHO****
Also, read other stories from SIMULIZI;