Msako wa Mwanaharamu Sehemu ya Kwanza
KIJASUSI

Ep 01: Msako wa Mwanaharamu

Msako wa Mwanaharamu Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE

*********************************************************************************

Silimulizi : Msako Wa Mwanaharamu

Sehemu Ya Kwanza (1)

Katika Pori fulani huko BAGAMOYO

PORI LILIONEKANA TUPU, hakukuwa na kipya zaidi ya miti ileile ya kila siku, kila mmoja ukiwa mahala pake. Kutokana na miti hiyo kuwa mbalimbali kiasi, iliwezekana kiumbe chochote kutembea katika pori hilo bila kupata shida. Mvumo wa upepo wa wastani kutoka baharini vilipiga mruzi kila mara, ukipanda na kushuka. Ndege wa porini kama dudumizi na tetere na wengine wengi walikuwa wakitoa sauti zao kuashiria Magharibi imekaribia huku wengine wakionekana angani wakirudi kwenye viota vyao wakiwa makundimakundi. Ndani ya pori hili lenye miti mikubwa na midogo na mimea yenye mfano wa kamba kamba ambazo zingetoa upinzani kwa binadamu kutembea kwa kuwa si mazingira yake kulikuwamo na watu watatu wakitafuta kitu, mwanaume mmoja na wanawake wawili.

“Una uhakika Chiba kuwa ni eneo hili?” Gina akauliza.

“Ndio ni eneo hili, maana kila nikiangalia kwenye rada yangu hapa, ishara inaishia hapa,” Chiba akajibu wakati huo Jasmine akiwa ameketi juu ya mzizi wa mti mkubwa. Gina akachukua ile rada kutoka katika mkono wa Chiba na kuitazama; juu katika kioo chake kulionekana mchoro kama wa ramani iliyopigwa picha kwa satellite na kitu kama doti nyekundu ilikuwa ikiwakawaka kwa kufifia.

“Mbona hii signal kama inafifia?”

“Betri inakwisha muda si mrefu, kumbuka tangu asubuhi inafanya kazi na sijaichaji ina wiki sasa,” Chiba akajibu na kufungua chupa yake ya maji. Jasho lilikuwa likimtiririka bila mafanikio ya kile anachokitafuta. Jasmine akiwa na begi lake mgongoni lenye vifaa vyake vya kazi alikuwa akisikiliza tu hakujua nini cha kuongea.

“Lakini Chiba, uelekeo ndio huu, tuko sahihi?” Jasmine aliuliza kwa taabu kidogo kutokana na uchovu uliomkabili. Watu hawa watatu walikuwa katika pori hilo katikati ya Bagamoyo na Mbegani kwa operesheni maalum ambayo ilikwishawachukua siku mbili katika eneo hilo na isioneshe mafanikio.

“Yaani kiukweli kabisa eneo hasa ni hili, tatizo ni wapi kwa maana signal yangu inaishia hapa na haiendelei kuonesha kama kuna eneo lingine, hatuna budi kupiga kambi hapa na kulala usiku huu,” Chiba aliwaeleza wenzake.

“Ha, nani alale hapa porini?” Jasmine aling’aka huku akiwa kapata nguvu ya kusimama.

“Wote lazima tulale hapa,” Chiba akasisitiza.

“Hakuna kulala hapa ni mpaka tupate jibu ndiyo itakuwa njia ya kutoka ndani ya pori hili,” Gina naye akasisitiza kwa kuongezea sentensi nyingine.

“Enhe! Hilo ndilo nilikuwa nalisubiri kwa muda mrefu sana, nilifikiri mmechoka kumbe bado mna nguvu,” Chiba aliwaeleza. Wakapeana moyo na kuendelea kutafuta humo porini kwenye vichaka na juu ya miti huku jua likichwea na kagiza kuanza kuingia taratibu.

  • * *

Dakika chache baadae giza lilikuwa juu ya uso wa nchi wakati Gina, Jasmine na Chiba wakiwa wametawanyika kila mtu upande wake, wakiendelea kuwasiliana kwa walk talk zao ambazo ziliunganishwa kwa mtambo mdogo uliobebwa katika begi la Gina. Majira kama ya saa nne usiku hivi ndipo Gina alipoona kitu kilichomshtua.

“Shiiit!” akang’aka na kuwaita wenzake kwa kutumia chombo hicho. Dakika nne baadae wote waliungana wakimulika eneo hilo na tochi zilizofungwa vichwani na kuwekwa katika paji la uso wa kila mmoja wao, zote tatu zikamulika mahala pale.

“Hii ni simu ya Scoba!” Chiba akawaambia kisha akasimama wima na kuwa kama anayeangalia kitu katika vichaka hivyo huku akihema kwa nguvu.

“Vipi?” Gina akauliza.

“Kwa vyovyote hapa ni eneo la tukio”.

Jasmine akaiokota ile simu kwa mkono wenye gloves na kuiweka ndani ya mfuko wa plastiki kisha wakaanza kupita vichakani polepole huku wakiangalia kwa makini. Saa moja baadae Gina akakutana na kitu kingine, mkufu, wakauokota na kuuweka kwenye mfuko mwingine wa plastiki. Wakati msako huo ukiendelea Gina alikuwa akijawa na machozi lakini alijaribu kujibana asilie kwa sauti, moyo wake ulipoteza matumaini.

Saa sita usiku, ukimya ukiwa mkubwa katika mapori hayo, Jasmine alijikwaa vibaya na kuangukia kitu kama binadamu.

“Oh, Shiit!” akapiga kite huku akijiinua kutoka pale alipoanguka. Kurunzi yake ikamulika mwili wa binadamu uliolala kimya ukiwa na damu iliyoganda katika nguo yake iliyofanana na ovaroli la kijani cha mgomba.

“Scoba! Aiyaaaa!!!” Chiba alijikuta akichanganyikiwa alipouona mwili wa Scoba na kuutambua kwa ile beji yake iliyobanwa katika mkanda wake wa kiunoni. Alikuwa amelala kimya akiwa katapakaa nyasi kila mahali na parachute lake likiwa kando juu ya miti midogo midogo.

Daktari Jasmine harakaharaka, akashusha begi lake na kutoa kifaa cha kupima mapigo ya moyo ‘Stethoscope’ na kuipachika masikioni mwake huku tayari Chiba amekwishafungua jaketi la juu la Scoba na kumwacha kifua wazi. Jasmine baada ya kupachika masikioni mwake kile chombo, upande wa pili akauweka juu ya kifua cha Scoba upande wa kushoto na kutulia kimya huku akikihamisha hamisha lakini eneo lile lile.

Wote walibaki kimya wakiweka matumaini yao kwa mwanadada huyo daktari. Baada ya kusikiliza kwa makini mkubwa huku akifinya sura na kuiachia akachukua kitu kingine na kumfunga katia kiungo cha sehemu ya juu ya mkono na ile ya chini, kile chombo kilikuwa kama mpira Fulani wenye kitu kama saa upande mmoja, kisha akapachika kile kidubwasha cha kwanza pale upande wa juu wa kiwiko na kufanya kama anajaza upepo kwa kuminyaminya kitufe kingine na mara ule mpira ukajaa upepo na kubana sawia mkono wa Scoba, Jasmine akawa akiangalia kile kitu kama saa huku akiusoma ule mshale wake uliokuwa ukitikisikatikisika huku ukirudi chini. Aliporidhika akauachia ule upepo na kutoa ile mashine.

“Vipi?” Chiba akawahi kuuliza.

“Mzima, ila mapigo ya moyo yako chini sana,” Jasmine akajibu huku akichukua kitu kingine ndani ya begi lake, akatoa chupa ya maji ‘drip’ na kumpa Chiba aishike kwa juu kwa mtindo wa kuinging’iniza kisha akachukua sindano na kutoboa moja ya mishipa ya Scoba katika mkono wake na kupachika ule mpira, akachezea kidubwasha fulani na kisha akasimama akiwa kajishika kiuno. Akitazama huku na huko.

“Tumsogeze hapo kwenye hako kamti,” akasema na kisha Chiba akampa Gina ile chupa aendelee kuishika wakati yeye na Jasmine wakimsogeza Scoba mpaka walipopataka na kumuweka vizuri.

“Piga kambi mwanaume, tufungue zahanati,” Jasmine akamwambia Chiba ambaye tayari alitoa katika begi lake aina ya kitambaa kigumu kisichopitisha maji, akakibana kwa vyuma Fulani alivyovito humohumo na kisha akafyatua kitu kama mwamvuli mkubwa na kufunika mahali hapo, wote wakawa ndani ya kijumba kidogo kilichoweza kuwahifadhi dhidi ya wadudu sumbufu.

“Atapona?” Chiba aliuliza.

“Bila shaka,” akajibiwa na Jasmine.

“Sasa Amata atakuwa wapi? Au inawezekana akawa jirani hapa hapa?” Gina aliuliza kwa dukuduku.

“Nafikiri ni maeneo haya haya kama alifanikiwa kuruka kama mwenzake, maana Scoba inaonekana aliruka na hapa anaonekana ameumia sehemu ya nyuma ya shingo kwa kuwa ndiyo inayoonesha uvimbe,” Jasmine alieleza.

“Tuendelee kumtafuta maana bibi yake huko aliko kila dakika anapiga simu mpaka kero,” Chiba aliwaambia wenzake.

“Na anavyompenda, yaani leo halali, na bila kumzuia angekuja huku porini,” Gina akaongeza.

“Eeh jamani huko mbali, kwani sisi hatupendi?” Jasmine akauliza kwa shaka.

“Sijasema hivyo, wote anatupenda kama watoto wake, ni jambo zuri sana”. Wakiwa katika kuongea mara wakasikia michakacho ya watu au wanyama, hawakujua ni kitu gani, Chiba akanyanyuka na kukamata shotgun yake mkononi tayari kwa lolote na wakati huohuo Gina naye alikuwa tayari upande wa pili wa kibanda kile naye shotgun ikiwa mkononi inasubiri amri tu.

Ndani ya kile kibanda Jasmine naye alikuwa tayari na bastola mkononi.

Kutoka katika kile kichaka wakaibuka vijana wanne wakiwa na mbwa watatu, mikononi mwao walikuwa wameshikilia mavisu makubwa na mikono yao ikiwa imelowa damu.

“Amani jamani!” mmoja wa wale vijana akasema.

“Amani kwa wote,” Chiba akajibu wakati huo Gina alikwishasimama pembeni na bunduki yake ilikuwa ikwaelekea vijana hao.

“Vipi porini hapa na usiku huu? Hamuogopi? Hili pori sio zuri kabisa ndugu zangu, fanyeni hima muondoke,” mmoja wa wale vijana aliyekuwa kifua wazi aliwaeleza Chiba na wenzake.

“Tupo kazini kaka,” Chiba akajibu.

“Najua lakini hili eneo lina mambo ya ajabu, watu wengi hupotea humu na hawajulikani wanakokwenda, vitu vya ajabu hunekana na kukipambazuka huwa tunashuhudia mabaki ya miili ya binadamu,” mwingine akaeleza.

“Hapa ndio Mlingotini, wakiwakamata watawatoa sadaka,” Yule wa kwanza akaeleza.

“Nimewaelewa, nisikilizeni, mnamwona huyu?” Chiba akawafunulia kile kihema na wale jamaa wakamwona Scoba aliyekuwa amelala kimya na ile drip ya maji ikiendelea kushuka na kuingia mwilini mwake.Wale jamaa wakatazamana na kisha kurudisha macho kwa Chiba.

“Huyu ni nani?” wakauliza.

“Rafiki yangu, nimekuja kumtafuta huku tangu jana asubuhi haonekani,” Chiba akaeleza.

“Hamjaona mwingine kama huyu?” Gina akadakia swali.

“Hapana ila jana kuna kitu cha ajabu kimetokea huko baharini, tuliona kama ndege sijui ikiwaka moto anagani kisha ikaanguka baharini nafikiri, kwani tulipokuja kutazama hatukuona chochote,” wakeleza. Ikawa zamu ya Gina na Chiba kuangaliana.

“Eneo gani mlipoona huo moto au mlipuko?”

“Huku, usawa wa baharini, halafu ule moto ukaangukia huko huko,” wakajibu huku wakionesha uelekeo wa tukio lile kwa vidole vyao. Chiba akamtazama Gina kisha wote wakatikisa vichwa vyao kuashiria wameelewa jambo.

“Tunafanyaje?” Gina akauliza. Chiba akabaki kimya akifikiri jambo.

“Jamani twendeni kijijini hapa mahala si pazuri hata kidogo,” mmoja wa wale watu akatoa ombi na kisha msafara ukaanza kwa kumbeba Scoba huku na huku kwa kutumia miti iliyofanywa kama machela.

“Tukiwa kijijini tutawaonesha vizuri kule ambako tuliona tukio hilo,” mwingine akaeleza huku msafara ukiendelea katika mapori na usiku wa giza nene.

  • * *

Siku iliyofuata…

MADAM S aliweka sawa pazia la dirisha ofisini kwake kisha kurudi kitini kukaa kama mwanzo huku kichwa chake kikiwa hakijatulia hata kidogo. Aliitazama saa yake ya ukutani na kurudisha macho yake mezani kwa mara nyingine kabla hajagutuliwa na mlio mkali wa kengele ya simu. Akainyakua kwa shauku na kuiweka sikioni, akashusha pumzi kwa nguvu huku mkono mmoja akiwa kajishika moyoni.

“Ndiyo, Chiba…” akaitikia namna hiyo huku uso wake ukijawa na shauku ya kujua kilichojiri.

“Operesheni imefanikiwa kwa asilimia hamsini, tumempata Scoba katika hali mbaya lakini sasa anaendelea vyema…”

“…Endelea…”

“…bado hatujampata Kamanda Amata na pia hatuna fununu yoyote juu yake,” Chiba akajibu na kutulia kimya.

“kwa hiyo nini kimewakuta hasa kwa maelezo ya Scoba?”

“Scoba bado hawezi kuongea, ila tunafanya utaratibu wa kumfikisha hospitalini kwa matibabu zaidi, ila kwa haraka haraka tumegundua kuwa ndege waliyokuwa wakitumia ama imepata hitilafu na kuanguka au imetunguliwa…”

“Mungu wangu! Mmeona mabaki yoyote ya ndege au imekuwaje?”

“Hapana Madam, hakuna mabaki ya ndege tuliyoyaona ila kwa uchunguzi tulioufanya inaonekana ndege hiyo imeangukia baharini…”

“Sawa, kwa hiyo tunahitajika kugeuka samaki sivyo?” Madam akauliza kwa lugha tata.

“Ndiyo Madam, inabidi iwe hivyo,” Chiba akajibu.

“Sawa, aaaaaaa… nipe dakika kadhaa kisha nitakupigia,”

“Copy!” Chiba akakata simu.

Madam S alitulia na kutuliza akili yake huku akiizungusha huku na kule, kisha akapiga ngumi mezani na kuinua simu yake akaiweka sikioni na kubofya tarakimu kadhaa. Upande wa pili ukaitikia.

“Hello!” sauti nzito ikalipenya sikio la mwanamama huyo.

“Msaada wa haraka tafadhali…”

“Wapi?” ile sauti ikauliza.

“Nyumba ya samaki,”

“Copy!” ile simu ikakatwa. Madam S akatoka ofisini na kuvaa koti lake la suti alilokuwa amelitundika kwenye kining’inizio kilichochongwa kwa fimbo ya mpingo, akatoka na kuubana mlango nyuma yake.

  • * *

KURASINI…

Ndani ya meli mbovu iliyotelekezwa kwa miaka mingi katika eneo hilo watu wawili walikutana kwa mazungumzo ya dakika zisizozidi tano. Madam S alikuwa akitazamana na Inspekta Simbeye katika mkutano huo wa dharula.

“Ndiyo Madam!” Simbeye alianza namna hiyo mara tu baada ya kuingia katika meli hiyo chakavu iliyozama nusu na kubaki nje nusu ilihali ndani yake kuna mitambo ya kuchunguza usalama wa baharini kama rada ambazo huweza kuona kitu chochote kisicho samaki kikiwa zaidi ya maili mia moja chini ya maji. Vijana wanaoijua kazi hiyo wa Jeshi la Polisi na lile la Wananchi walikuwa wakifanya kazi humo usiku na mchana; hakuna aliyewaona wakiingia wala wakitoka, na hakuna aliyewahi kujua kama meli hilo linalozidi kuoza kwa nje kwa nini lilikuwa halihamishwi mahala hapo.

“Njiwa wangu amepigwa manati, kadondoka majini, alikuwa na mayai mawili, moja nimelipata lakini lingiine mpaka sasa sijalipata wala kuliona…” Madam alimwambia Simbeye.

“Oh, pole sana, nilipata taarifa ila sikujua mayai ya nani! Sasa unatakaje?” akauliza Simbeye.

“Nahitaji samaki, japo wawili tu wakaangalie kule chini?”

“Umesomeka Madam,” Simbeye akajibu kisha akaagana na Madam S na kuondoka zake kutoka ndani ya meli hilo.

Dakika mbili baadae, boti iendayo kasi inayojulikana kwa jina la ‘KINYAMKERA’ inayoweza kupita juu na chini ya maji ilichomoka ndani ya meli hiyo ikiwa na vijana watatu waliovalia tayari kwa kuendesha maisha majini. Safari kuelekea katika bahari ya Bagamoyo ilikuwa imewiva.

  • * *

Simu ya Chiba akafurukuta mfukoni akainyanyua na kiuiweka sikioni.

“Tuko njiani!”

“Copy!” kisha ile simu ikakatwa. Chiba akawatazama wenzake.

“Madam yuko njiani!” akawaambia.

Wakaitikia kwa vichwa huku wakiwa tuli wakiangalia huku na kule kwa vifaa vyao maalum, pia wakitumia kompyuta kumtafuta Kamanda Amata kwa picha za satellite wakijaribu ku-ping tarakimu za utambulisho wake lakini haikuonekana hata dalili za mtu huyo kuonekana. Chiba alimtazama Jasmine aliyekuwa na Gina muda huo.

“Dokta, vipi mgonjwa?” akamuuliza.

“Yuko poa, naona sasa anaweza kuongea japo si kwa ufanisi sana,” Jasmine akajibu na kisha wote wakarudi kwenye ile hema yao ambayo sasa walikuwa wameijenga tena kijijini pembezoni kidogo. Nukta hiyo hiyo kifaa cha mawasiliano mgongoni mwa Gina kikakoroma, akaukwanyua mkonga wa chombo hicho na kuupachika sikioni.

“Unasomeka,” akitikia.

“Nipe uelekeo tafadhali…”

“ Nyuzi 278 Kaskazini kwa kipimo wima na 120.56 Mashariki kwa kipimo ulalo,” Gina akajaribu kujibu kwa kutumia vipimo vya ardhini kuielekeza helkopta hiyo ya polisi kufika eneo lile bila tabu. Haikuchukua muda lile helkopta liliwasili eneo hilo na kutafuta uwazi ili litue. Lilipopata nafasi ya kufanya hivyo likatua katika uwanja wa shule. Chiba, Gina na Jasmine sasa wakisaidiwa na vijana wa pale kijijini walimbeba Scoba hadi kwenye dege hilo na kumpakia kisha wakaondoka zao bila kuchelewa.

“Poleni kwa kazi vijana,” madam aliwapa pole.

“Asante lakini kazi haijaisha,” Gina akawa wa kwanza kujibu.

“Najua msijali, mnaweza kutazma chini?” akawauliza. Kisha wote wakajaribu kuangalia kwa kupiti kioo kikubwa kilicho chini ya dege hilo.

“Nini kile?” Gina akauliza.

“Vijana washafika wanajaribu kutazama kama Kamanda atakuwa kabaki huko au vipi, wamekuja na boti inayopita ndani ya maji,”

“Waoh!” Gina akashangaa

“Lakini sina uhakika kama Amata atakuwa huko kwenye maji, maana kama yuko huko basi amekwishakufa,” Jasmine akaeleza dukuduku lake.

“Usiseme hivo Jasmine,” Chiba alimkata kauli.

“Kamanda hawezi kufa kijinga hivyo!” Scoba alijibu kwa tabu kidogo, wote wakageuka kumtazama kutoka pale alipolala.

“Naona ana nguvu sasa, anaweza kuongea” Dkt. Jasmine alimweleza Madam S.

“Yeah, ila ngoja tufike mahala salama,” akaeleza Madam na wote wakahafiki.

  • * *

Wale vijana watatu wakiwa chini ya maji waliweza kufika eneo ambalo ndege ile iliangukia, vilikuwa vipande vichache vilivyonasa katika miamba na mapango ya baharini, haikuwa ndege kamili au vile vipande havikukamilika. Waliendelea kuchunguza hapa na pale ndipo wakagundua kuwa ndege ile ilidunguliwa kutokana na alama kubwa nyuma kabisa upande wa chini, kipande hiko hakikuathiriwa na mlipuko ule.

Walifanya juu chini na kufanikiwa kupata kisanduku cheusi (black box) ambacho kazi yake ni kurekodi mwenendo mzima wa ndege ikiwa angani. Walipokipata na kukihifadhi kazi iliyobaki ilikuwa ni kutafuta binadamu wa pili kama ataonekana. Saa nzima ilipita hawakufanikiwa, walipekuwa kila kona ya mwamba na pango lakini hakukuwamo mtu yeyote wala mabaki yake. Walipokamilisha awamu hiyo ya zoezi wakaondoka zao na kurudi kwenye boti yao. Wakiwa ndani ya boti hiyo ya kisasa walitoa taarifa kwa Simbeye na wakatakiwa kurudi mara moja.

  • * *

SHAMBA (Safe HOUSE)

Scoba aliketi kimya juu ya kiti cha vono, mbele yake kulikuwa na Madam S na Jasmine.

“Nina uhakika Kamanda hajafa, ama ameangukia mbali au yuko mahala, kwa sababu yeye alikuwa wa kwanza kutoka kwa parachute,” Scoba alieleza.

“Kwani nini hasa kimewatokea?” Madam alisaili.

“Tumedunguliwa, lakini hatujui hata kombola limetokea upande gani, sasa inakuwa ngumu kueleza, mi nilmestuka kitu kimeshafika mkiani, kilichofuatia sikuwa na jinsi zaidi yaku – evacuate. Mwamvuli wa Amata ulikuwa wa kwanza kufyatuka na kumtoa nje na mimi ulifuatia,” akaeleza. Madam S akabaki kimya kabisa akiwa hajui la kusema, baadae akarudisha uso kwa Gina.

“Mwanaharamu aliyefanya hivi lazima apatikane,” Madam S akasema kisha akamgeukia Scoba.

“Lakini kuna mlichogundua?”

“Kiukweli bado, pale tulikuwa tunakiona kijiji cha Kaole na vile vya pembezoni zaidi ni mapori mpaka Mbegani”.

“Sasa nani kawatungua?”

“Inawezekana kabisa ni wanajeshi wa kambi ya Mlingotini kwani tulipita pande hizo hatukuwa na ruhusa yoyote,” Scoba akaeleza na Madam S akatikisa kichwa. Kisha akatoka na kuwaacha Jasmine na Scoba yeye akatokomea katika chumba kingine.

Dakika kama tano baadae akarudi na taarifa nyingine kwa Scoba kuwa kambi ya jeshi ya Mlingotini hawajadungua ndege yoyote eneo hilo kwani wao hawawezi kudungua ndege bila idhini ya mkuu wa kikosi.

“Basi, kutakuwa na kambi ya siri eneo hilo, hili ndio tatizo la serikali kuuza viwanja kiholela, hata mnayemuuzia hamumjui wengine magaidi hawa,” Scoba akazungumza huku akisimama.

Madam S alimtazama Scoba kwa tuo na kisha akamtupia swali.

“Hatujamuona kamanda kabisa hata kwenye mitambo yetu haonekani, kama hajafa atakuwa wapi?”

“Kamanda hawezi kufa, tuendelee kumtafuta,” Scoba akajibu.

Rudi siku tatu nyuma… ‘siku ya tukio’

SHAMBA

KAMA NI SURA YA HASIRA basi ilionekana wazi kwa Madam S alipokutana na vijana wake ndani ya nyumba yao ya siri huko Gezaulole. Kikao hiki kiliitishwa haraka sana baada ya tukio lisilotegemewa kutokea eneo la Darajani katika Barabara ya Nyerere, saa sita mchana kweupe.

Kamanda Amata alikuwa kajiinamia kama awazae jambo wakati wengine wakijaribu kuchanganya akili kwa hili na lile juu ya hilo.

“Lakini mi nilisema kuwa mtu yule asilindwe na askari wa kawaida kwani ana mbinu nyingi za kujiokoa,” Chiba akaeleza.

“Yeah ni kweli lakini kumbuka pia sisi si kazi yaetu kulinda watuhumiwa,” Madam akamjibu. Ukimya mwingine ukatawala.

“OK!” sauti ya Madam S ikawazindua vijana wale watano waliokuwa katika lindi la mawazo ya sintofahamu.

“Lazima tumsake na tumtie mkononi, mtu mmoja hawezi kutunyanyasa sisi tena wanataaluma wa kazi hii. Tutamsaka na kumleta tena hapa, Chiba jaribu kufuatilia wapi anaweza kuwa ameelekea ili tuone la kufanya,” Madam akatoa amri na Chiba akaondoka eneo hilo kuelekea kati kachumba chake maalum.

“Usione niko kimya yaani huyu bwana ananiumiza kichwa, nikikumbuka jinsi nilivyompata kwa shida, we acha tu!” Kamanda Amata alimwambia Madam S huku akitoka eneo hilo.

“Najua lakini naamini tutampata tena,”

“Ndiyo tutampata lakini kwa jinsi ile ina maana huyu jamaa bado ana nguvu sana na hatujui kajipanga namna gani,”

“Unalosema ni kweli, kwani hata mbinu iliyotumika kutekwa kwake mbele ya mikono ya polisi haijawahi kutokea na wala hatukutegemea, imekuwa kama filamu ya Hollywood, aisee!” Madam alimweleza Amata huku wote wakitembea kwenye ujia mrefu ndani ya jengo hilo.

“Yatupasa tuwe makini sana, hatujui mara hii ataibukia wapi. Na tukimpata safari hii atajuta kuzaliwa dume,” Amata akaongea kwa uchungu.

Madam S akasimama na kumtazama kijana huyo aliyekuwa amekwishasonga mbele kwa hastua kama tatu hivi, naye akasimama baada ya kumwona bosi wake kafanya hivyo, wakatazamana.

“Utamfanya nini?” Madam akauliza.

“Nitamtoa korodani!”

“Na we’ unaweza!”

Kisha wakaendelea na safari yao katika jingo hilo.

  • * *

CHIBA alikuwa ametingwa kwenye mitambo yake, kompyuta kadhaa zilimzunguka na mashine nyingine mbalimbali. Ndani ya chumba hicho aliweza kuikusanya dunia yote na kuiweka ndani ya kioo kimoja cha kompyuta. Msako wake aliuanzia palepale eneo la tukio, Darajani, akijaribu kufuatilia uelekeo wa chopa iliyombeba mtuhumiwa wao mara tu baada ya kukombolewa kutoka katika mikono ya polisi, ndani ya gari ya chuma alipofungwa minyororo miguuni na mikononi na kuacha askari sita wakiwa hawana uhai.

Chombo chake kilimuonesha uelekeo wa Kaskazini Mashariki, yaani maeneo ya Mbweni mpaka Bagamoyo, lakini alishangaa kila akifika eneo fulani la Mbegeni ule mtambo ulikiuwa unashindwa kueleza uelekeo sahihi wa kile chombo, akajaribu na kujaribu lakini alishindwa. Akashusha pumzi ndefu na kujiegemeza kitini kabla ya kunyanyua simu na kumjulisha Madam S juu ya hilo. Ilichukua dakika moja tu mwanamama huyo kuwasili ndani ya chumba hicho maalum cha mawasiliano. Baada ya kuongea mawili matatu na Chiba walifikia azimio la kumsaka mtu huyo iwe angani au ardhini. Kikao kikaitishwa tena na wote wakakutana.

Meza hii ndiyo daima hufanyiwa maamuzi mazito na mepesi, ya kukata au kuua, kutesa au kutekenya, vyote huamuliwa hapa. Ukiitazama utaiona tu, kwanza inaviti sita kwa idadi yao, kila mtu hukaa kiti hicho hicho kila wakati, ni sawa na kusema ndicho ‘afisi’ yake kwa hapo, meza ya duara.

Mara tu baada ya kukutana, kikao kikaanza kwa kumsikiliza Chiba akieleza kile alichokigundua katika mtafuto wake wa kimtandao.

“Haya kama alivyotueleza Chiba, sasa hapa tunakwenda kimakundi, kundi moja na la kwanza litakuwa angani hili ni Scoba na Amata, kundi la pili Gina na Chiba mtakuwa ardhini mkifuatilia kwa chini na la tatu ni mimi (Madam S) na Jasmine tutakuwa katika uokoaji. Hivyo basi sasa tuingie kazini”. Madam S alipanga kikosi chake, hakuna aliyekuwa na mashaka katika hilo kwani walijua kuwa mwanamama huyo huwa hakosei kwenye kupanga. Kila kitu kikawekwa sawa, kila mmoja na mwenzake wakajipanga ni wapi pa kuanzia, kazi ikaanza.

JESHI LA WANAMAJI KIGAMBONI

KAMANDA AMATA NA CHIBA waliwasili katika kambi hiyo majira ya saa tisa alasiri wakiwa tayari kwa shughuli hiyo ngumu. Wakati huohuo Chiba na Gina walikuwa tayari katika gari wakielekea Tegeta mpaka Mbweni kuendeleza msako.

Baada ya Kamanda na Chiba kusaini kabrasha fulani fulani pale jeshini tayari kuchukua ndege ndogo inayoweza kutua na kuruka majini, walikabidhiwa kofia ngumu za kuvaa na kupewa maelekezo machache na rubani wa jeshi kisha wakaingia katika ndege hiyo ndogo yenye uwezo wa kubeba watu watatu tu. WAkaketi na kufunga mikanda, Scoba kama kawaida yake ndiye alikuwa rubani mkuu wa kuirusha ndege hiyo.

“Hivi wewe kuna kitu hujawahi kuendesha?” Amata akauliza kwa utani.

“Kipo,”

“Kipi?”

“Ungo”.

Wote wakaangua kicheko na wakati huo tayari injini ilikuwa ikizunguka na Scoba akiitoa ndege hiyo mahala pake kuelekea katikati ya bahari tayari kuruka na kuanza safari ya msako.

Dakika tano baadae walianza kuliona jiji la Dar es salaam kutoka juu jinsi linavyopendeza. Muda wote walikuwa wakiwasiliana na Chiba na Gina waliokuwa wakisafiri kwa gari kuelekea upande huo. Walipofika eneo ambalo walihisi ndipo hasa wanapopataka, juu kabisa ya anga la Bagamoyo, pande za Mbegani kuja Kaole walikuwa wakitumia darubini maalumu yenye nguvu kutazama chini kama wanaweza kuona chochote chenye maana kwao huku picha zile moja kwa moja zikirushwa mpaka kwenye kompyuta ya Chiba ambayo alikuwa nayo ndani ya gari hiyo iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi na mwanadada Gina.

“Mpaka sasa hatuoni chochote zaidi ya misitu na nyumba za wenyeji,” Kamanda alimwambia Chiba.

“Scoba Scoba, shusha ndege chini zaidi angalau futi elfu mbili tuone kama twaweza kugundua chochote,” Chiba akatoa maagizo na Scoba akateremsha ndege hiyo kama alivyoagizwa, wakaanza tena kutazama kwa kile chombo huku ndege hiyo ikizunguka huku na huko bila kutua chini. Baada ya mzunguko wa muda mrefu, wakaingia na upande wa bahari na kwenda mbali karibu na pwani ya Zanzibar, kisha wakarudi tena upande wa Pumbuji.

“Hey! Amata, hebu cheki pale!” Scoba akamshtua Amata, naye akatazama kwa ile darubini.

“Shiit, kile ni kisiwa sivyo?” Amata akauliza.

“Hiki kisiwa nakijua, kulikuwa na kitu pale cheupe kinang’aa kama paa jipya lakini kimepotea na kuchukua rangi ya uoto uliopo,” Scoba aliongeza.

Kamanda Amata akamwonesha ishara ya kidole ya kwamba aizungushe ndege hiyo na kukizunguka kile kisiwa ikiwa ni pamoja na kuteremka chini zaidi.

“Scoba unaanza kuzeeka, lile ni pori tu!” Amata akamwambia Scoba huku akigeuza ile darubini upande mwingine wa Kaole. Bado ndege ilikuwa haijamaliza kuzunguka kile kisiwa, Scoba aliendelea kutazama kwa makini sana.

“Kwa hiyo tunafanyaje?” Scoba akauliza.

“Tucheki na upande ule kuleeeee,”

“Ok!” Scoba akajibu na kuiweka sawa ile ndege kisha akainyanyua juu ili kuendelea mbele.

  • * *

Scoba hakuwa amekosea kwa kile aichokiona, na Amata vilevile hakuwa amekosea kwa kile alichokisema, hivyo basi kila mmoja alikuwa sawa kwa wakati wake. Katika eneo hilo kulikuwa na kisiwa kikubwa kilichozungikwa na mikoko na uoto mwingi wa baharini.

Hiyo kama haitoshi, ndani ya kisiwa hiki kulijengwa jingo kubwa lenye vitu vingi sana, na ujenzi wa jingo hili ulikuwa ukifanyika kwa siri sana, hakuna mwananchi aliyejua wala kiongozi wa serikali. Walichokiona wao ni nyumba moja tu ya kawaida sana iliyojengwa juu ya kisiwa hicho, lakini kumbe chini yake kulikuwa na ngome kubwa iliyojengwa kwa ustadi sana. Na kati ya vyumba vingi vilivyopo, kimojawapo kilikuwa na mitambo ya rada, inayoweza kuona chombo chochote kinachopita angani usawa wa kisiwa hicho au kinachokuja majini usawa wa kisiwa hicho. Ndani ya chumba hicho kulikuwa na wataalam wanaofanya kazi kwa siri na zamu kila siku kwa saa ishirini na nne.

Siku hii, watu watatu walikuwa ndani ya chumba hicho wamejifungia, walikuwa wametingwa kusoma kitu kikubwa kama saa lakini hiki hakikuwa na tarakimu yoyote isipokuwa kilikuwa na mistari ya duara kadhaa na mstari mmoja wa rangi ulikuwa unazunguka huku na kule.

Mlio wa kitu kama bip ukaanza kusikika ndani ya chumba kile. Mlio huo ulianza kusikika kwa mbali sana lakini baadae ukawa na sauti kubwa.

“Vipi?” mmoja akauliza.

“Kuna kitu kama ndege hapa naiona inaelekea upande huu wetu,” akajibiwa. Yule bwana akasogea karibu na kile chombo na kuangalia.

“Mmmhh! Ni ndege hii hebu washa ile camera kubwa tuone,”

Nukta hiyo hiyo, kitu kama antenna kikaibuka kutoka katikati ya mapori na kusimama wima kati ya miti. Ndani ya chumba hicho waliweza kuona picha halisi ya ndege ile.

“Nani hawa?” mwingine akauliza huku akiwa katumbua macho.

“Sijui, hebu toa taarifa kwa mkuu wa kikosi,”

Yule kijana akatoka na kuelekea pembeni kisha akachukua simu na kukoroga tarakimu fulani.

“Mkuu, kuna ndege tunaiona kwenye rada inaelekea upande huu, hatua gani tuchukue?” Yule kijana akaongea huku akitweta.

“Subiri nakuja hukohuko,” akajibiwa.

Sekunde kumi hazikupita mlango ukafunguliwa na mtu mmoja mwenye tambo kubwa la kimazoezi akaingia; moja kwa moja akaiendea ile meza na kutazama ile picha iliyopigwa kwa kamera ya siri.

“Shiit! Hii ni ndege ya jeshi, fanyeni hivi, ikifika mbali jaribuni kuona nini kinaendelea ndani kisha mitumie hizo picha afisini kwangu,”akawaambia. Wale jamaa wakaendelea kuisoma kila inavyozunguka, na baada ya kukaa kwenye kona nzuri waliweza kuipiga picha na kuona nini kipo ndani ya ndege hiyo. Wakapeleka taarifa kuwa kuna watu wawili wanaoonekana kupiga picha fulani. Kutoka kwa Yule jamaa akawaamuru wajaribu kunasa mawasiliano yao ili kusikia nini kinazungumzwa.

Zoezi hilo halikuchukua hata dakika mbili, kutoka katika kile chumba, wakaweza kunasa mawasiliano kati ya Amata na Chiba. Baada ya kujua kuwa ni wao wanaowindwa amri tu ikatolewa na mkuu wa kikosi.

“Ilipue,” akawaamuru.

“Haiwezi kutuletea matatizo tukiilipua?” kijana mmoja akauliza.

“Nimesema lipua tena haraka!”

Hakukuwa na lingine, missile equipment ikafunguliwa na kujitokeza juu kidogo ya ardhi lakini ndani ya msitu huo wa mikoko kisha ikafyatuliwa na moja kwa moja ikafuata ndege ile iliyokuwa na Amata na Scoba ndani. Mlipuko haukuwa wa kutisha sana lakini ndege ile ilikatikavipande na kuangukia baharini.

  • * *

Ndani ya ile ndege, Scoba alisikia kengele iliyopiga kwa nguvu, akatazama kwenye dashboard yake na kuona ishara kuwa wapo kwenye shabaha

“Amataaaaaa!” akapiga kelele baada ya kuona kwenye kuwa wamedunguliwa. Kitendo bila kuchelewa, Kamanda Amata akabonyeza kidubwasha kilicho chini ya kiti chake na vyuma vilivyoshika kiti hicho vikaachiana wakati huo tayari Scoba keshabinya kinobu kilichoandikwa neno ‘Evacuate’. Ile ndege ikafunguka juu na kiti cha Amata kikatolewa nje na kuiacha ile ndege.

Hakuna alichokishuhudia zaidi ya mlipuko mkubwa angani na ile ndege kupasuka vipandevipande.

“Scoobbbaaaaa!!!!!” Kamanda Amata alipiga kelele akiwa hewani lakini hakumwona Scoba. Vyuma vilivyoruka kimojawapo kikampiga kichwani Amata akapoteza fahamu akiwa anaelea angani huku parachute lililokuwa tayari limefunguka likimbeba na kumteremsha taratibu.

Scoba, mara tu baada ya Amata kutupwa nje alifyatua kiti chake lakini alichelewa nukta kadhaa, wakati kile kiti kikimrusha nje lile kombora likawa tayari limeshaipiga ile ndege eneo la kati kati, akajikuta ananasa kwenye vyuma vya ndege hiyo. Akajitahidi na kujifyatua lakini parachute lake liliharibika vibaya, akajitahidi kuliongoza ili adondokee nchi kavu akafanikiwa. Kutokana na kuchanika kwa parachute hilo alifika chini kama mzigo na kujipiga vibaya akatulia kimya kwa sekunde kadhaa, macho yake yakiwa bado yanatazama anga la dhahabu jioni hiyo na taratibu akaanza kuhisi giza huku sauti za ndege zikipote kwa mbali, akazirai.

Amata akiwa hana fahamu alidondokea baharini na kupigwa pigwa na mawimbi mpaka kando kidogo. Jua la jioni lilikuwa tayari linang’aza sehemu hiyo na misafara ya ndege nayo ilikuwa ikirudi viotani.

  • *

Huku chini kwenye gari, kioo cha kompyuta ya Chiba kikawa cheusi ghafla, hakuna chochote kilichoonekana.

“Vipi tena?” akajiuliza.

“Vipi kwani?” Gina akauliza.

“Nahisi hatari, maana sauti ya mwisho nilioisikia ni ya Scoba akimwita Amata, hebu weka gari pembeni kwanza,” Chiba akamwambia Gina. Naye akafanya hivyo, ile gari ikasimama kando mwa barabara katika eneo la Zinga. Chiba akajaribu kucheza na kompyuta yake lakini hakuna alichoweza kuona zaidi ya ujumbe wa ‘Error 706’ uliokuwa ukijitokeza mara kwa mara, akaifunga ile kompyuta na kumgeukia Gina.

“Vipi?” Gina akauliza, lakini kutoka katika macho ya Chiba aliweza kuuona mshangao uliokosa mwelekeo.

“Huko hali si shwari, siwapati Amata na Scoba,” Chiba akajibu huku akijiweka sawa kitini na kuinua simu ndogo iliyofungwa ndani ya gari hiyo.

“Unataka kuniambia nini?” Gina akauliza huku mikono yake iliyokuwa imeshika usukani sasa ilianza kutetemeka na alionekana kubana meno yake ama akizuia kilio au akinyima uchungu nafasi ya kujiweka hadharani.

“Mawili, ama ndege ina hitilafu au wamedondoka,” Chiba akajibu na wakati huo tayari simu iko sikioni akimwitikia Madam S.

“Nakusoma Chiba!” Madam S akaitikia

“Kuna hali isiyoeleweka, Simpati ndege angani, mawasiliano yamekatika,” Chiba akamwambia.

“Unataka kusema nini?”

“Sauti ya mwisho niliyoisikia inaashiria hatari, Scoba alimwita Amata kwa nguvu kisha nikasikia kishindo na ukimya kwa asilimia 101,” akaeleza.

Kupitia simu hiyo ya upepo, Chiba aliweza kumsikia Madam S akishusha pumzi kwanguvu.

“So?” Madam S akarudi hewani mara hii sauti yake haikuwa kama kwanza, ilikuwa imejaa kitetemeshi.

“Probably, men down!!” Chiba akamaliza hhuku macho yake yakitona machozi.

Akatulia kumsikiliza bosi wake akimpa maelekezo kadhaa kisha huku akiitikia tu kwa kuguna pasi na kusema neno lolote.

“Clear and out!” akaitikia na kukata simu kisha akaipachka mahala pake na kumtazama Gina.

“Madam anasemaje?”

“Anasema tuwahi na Dkt. Jasmine anakuja na vitendea kazi vya kutosha kwa msaada wa haraka. Gina akaingiza gari barabarani na kutimua mbio kama kichaa, akageuza na kurudi nyuma kidogo kisha akaikamata Mapinga aliiacha barabara ya kwenda Dar es salaam na kupinda kushoto kuchukua nyingine kuelekea Mbegani.

“Shiiit!” Gina aliendelea kugugumia huku akikanyaga mafuta kama kichaa, mshale wa mwendo kasi ulikuwa katika namba 110 na vumbi lililoachwa nyuma halikuwa la kawaida. Baada ya mwendo wa takribani dakika arobaini na tano, Gina alisimamisha gari karibu na kijiji fulani, Chiba akajitokeza juu ya gari na darubini yake na kuangalia kwa darubini katika uwanda wa nyasi fupifupi. Darubini hii ilikuwa ni ya kisasa sana, yenye madini yanayiwezesha kuona hata katikati ya giza, na kupambanua kila inachokiona na kukupa maelekezo kuwa kitu hicho kipo kilomita ngapi. Baada ya dakika kadhaa akaingia ndani, na kuchukua kifaa kingine kama simu lakini kilikuwa kikubwa zaidi, akakiwasha na kubonya vitu fulani fulani kisha akaanza kuangalia, rangi na michoro mbalimbali inayotokea katika kile kioo, baada ya sekunde kadhaa kukawa na kijitaa kinachowaka eneo Fulani la kioo cha kile kidubwasha.

ITAENDELEA

Msako wa Mwanaharamu Sehemu ya Pili

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment