Msaliti Asakwe Sehemu ya Kwanza
IMEANDIKWA NA: PATRICK J. MASSAWE
*********************************************************************************
Simulizi: Msaliti Asakwe
Sehemu ya Kwanza (1)
MAJIRA ya saa nane za mchana, walionekana vijana watatu, wakiwa wamekaa upande wa baa, ndani ya hoteli maarufu ya The Tropic Inn. Ni hoteli iliyojengwa juu ya kilima kidogo, kando ya barabara kuu, iendayo jijini Kigali na kwingineko.
Hali ya hewa ilikuwa ni ya baridi, ilifuatiwa na manyunyu pamoja na ukungu mzito mweupe, uliofunika milima yote iliyozunguka eneo maarufu la Nyakarambi, Mkoa wa Kibungo, ulioko eneo la mpakani, kati ya nchi ya Rwanda na Tanzania .
Muda wote vijana wale walikuwa wamekaa katika meza ya pembeni, wakila na kunywa, na pia kujadiliana mambo muhimu kwa sauti ya chini. Meza iliyokuwa mbele yao ilikuwa imesheheni vinywaji vya kila aina, bia pamoja pombe kali aina ya wiski, ili kuiondoa ile baridi iliyokuwa ikiwaingia barabara maungono mwao ingawa walikuwa wamevalia makoti mazito.
Baridi ilikuwa ni kitu cha kawaida katika maeneo yale yaliyokuwa yamezungukwa na milima nyingi. Ingawa wote walikuwa bado vijana, hawakuwa na haja ya kukaa na wanawake, ambao walikuwa wamejazana ndani ya baa ile wakiwa kama kivutio kikubwa kwa wateja! Ukweli ni kwamba walikuwa wamefika pale kupanga mikakati yao muhimu sana , ambayo hawakutaka mtu yeyote aisikie zaidi ya wao kama walivyo. Na ndiyo maana wakajichimbia kwenye kona ndani ya ukumbi ule wa baa.
Vijana wale walijulikana kwa majina ya Roman, Obale na Laurento, ambao kitaaluma walikuwa ni wanajeshi waliokuwa wamepitia mafunzo maalum ya kijeshi na kufuzu vizuri. Ni mafunzo ambayo yalikuwa yakifanyika katika misitu mikubwa iliofungamana ya Kibungo.
Vijana wote watatu, walikuwa na maumbile makubwa ya kimazoezi, kutokana na ile suluba ya kuishi msituni kwa muda mrefu. Pia, hawakutofautiana sana kiumri, kwani walikuwa na umri kati ya miaka ishirini na mitano, au zaidi kidogo. Hakika walikuwa vijana wabichi bado, ambapo walikuwa wamefika pale Nyakarambi kwa usafiri wa gari aina ya Toyota Land Cruiser, wakitokea katika makazi yao ya siri yaliyoko katika msitu wa Kibungo, palipokuwa na kambi maalum ya kijeshi iliyokuwa inamilikiwa na waasi.
Ni kundi la waasi lililokuwa linaongozwa na Ofisa Mwanajeshi, Kanali Fabio Rushengo, ambaye ni mhusika mkuu na mmoja wa askari waliohusika na mauaji ya kimbari, yaliyotokea nchini Rwanda mnamo mwaka 1994, ambayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya laki nane! Ni mauaji ambayo yaliutikisa ulimwengu mzima kwa jinsi walivyouawa watu wengi kwa mara moja!
Vijana, Roman, Teobale na Laurent walikuwa na sababu maalum iliyowafanya wafike pale Nyakarambi, ambayo ni juu ya kupanga mpango wa kumtoroka kiongozi wao, Kanali Fabio Rushengo, baada ya kuchoshwa na maisha ya kukaa msituni kama nyani, wakiwa na mawazo ya kuipindua serikali halali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.
Kwa upande wao waliona ni sawa na ndoto ya mwendawazimu anayeota asichokifahamu! Basi, ndipo walipoamua kukutana katika mji ule mdogo wa Nyakarambi, ulioko umbali wa kilometa 30 kutoka mpakani Rusumo, upande wa pili wa nchi ya Rwanda .
Sehemu ile palikuwa na kituo kikubwa, ambacho hapo awali kilitumika kupokea wakimbizi waliokuwa wanarudi nchini kwao kwa hiari yao mwenyewe, baada ya kuridhishwa na hali ya usalama wa maisha yao . Ni Kituo kilichosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) wakati ule kwa upande wa nchi ya Rwanda .
Vilevile mji ule ulikuwa na starehe za kila aina, hasa ukizingatia palikuwa na mkusanyiko wa watu wengi, wakiwa ni wafanyabiashara na madereva wa magari makubwa yanayosafirisha mizigo kati ya nchi za Tanzania , Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo.
Kijana Roman ndiye aliyekuwa kiongozi, alivuta pumzi ndefu na kuzishusha. Halafu akawaangalia Teobale na Laurent kwa zamu, jinsi walivyokuwa wanakunywa bia aina ya Primus ndani ya bilauri kubwa, ikiwa kama vile alikuwa anawakagua, nao, Teobale na Laurent wakawa wanamwangalia kwa kuashiria kwamba walimsubiri aanze kuzungumzia kilichowafanya wakutane muda ule.
Kiutaratibu wao ni kwamba walikuwa wanamheshimu sana kiasi ambacho walimpendekeza awe kiongozi wao kwa sababu alikuwa ni jasiri asiye na woga!
“Natumaini wote tu wazima…” Roman akawaambia kwa sauti ndogo.
“Sote tu wazima, ndiyo maana tumekutana hapa,” Teobale akasema kwa sauti ndogo.
“Na nyote mnaelewa kilichotuleta hapa Nyakarambi, na kukaa kikao hiki,” Roman akaendelea kusema
“Tunaelewa kilichotuleta,” akaongeza Laurent huku akimwangalia Roman.
“Vizuri kama mmenielewa,” Roman akasema na kuongeza. “Hapa tumekuja kuongelea suala la kiongozi wetu Kanali Fabio Rushengo!”
“Ndiyo. Ni suala hilo lililotuleta hapa!” Teobale alijibu kwa niaba yao wawili na Laurent.
“Basi, inabidi tuachane naye, na kujiondoa katika kundi lake; ambapo ni kama tunapoteza muda kwa kuishi msituni muda wote. Eti ni kuukwepa mkono wa serikali ya Rwanda , ambayo siyo rahisi kuiangusha!” Akaendelea kusema Roman. “Cha muhimu sasa ni kuondoka kabisa hapa nchini Rwanda , na kukimbilia sehemu nyingine na kujisalimisha kwa Maafisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi. Baada ya kujisalimisha kwao, tutawaeleza uovu wote wa Kanali Fabio Rushengo, bila shaka wao watatusaidia na kutupatia ufumbuzi, au wenzangu mnasemaje?”
Baada ya Roman kusema vile, Teobale na Laurent wakaangaliana. Halafu Laurent akavuta pumzi na kusema: “Ni wazo zuri sana Roman. Lakini kwa ninavyofahamu, kwa mtu katili kama Fabio, hawezi kutuacha hai baada ya kugundua kwamba sisi tumemsaliti? Ukizingatia yeye ana medani ya ukamandoo katika masuala ya kivita?”
“Kwani unafikiri anaweza kutufanya nini?” Roman akamuuliza Laurent.
“Ni lazima atusake popote pale tutakapokimbia, na hatimaye kutuangamiza! Fabio ana mtandao mkubwa sana hadi sehemu za mipakani!”
“Kweli, anaweza kufanya hivyo. Lakini kabla hajatumaliza sisi, tutakuwa tumemmaliza yeye!” Roman akasema kwa msisitizo na kujiamini.
“Hebu tupe mipango,” Teobale akasema na kuendelea. “Tummalize kivipi?”
“Kwa njia rahisi sana . Si mnajua kuwa Kanali Fabio alikuwa ni mtu wa kuhifadhi kumbukumbu zake nyingi zinazohusu mipango yake ya maovu?”
“Kweli. Fabio ni mtu makini sana , kwani huwa anahifadhi kumbukumbu zake kwa kuziweka ndani ya Diski ya Kompyuta (Kihifadhia vitu kama vile, Maandishi, picha, sauti nk.) ambayo huichapa mwenyewe kwenye kompyuta, na kuzificha anapojua ndani ya ofisi yake!” Laurent akasema kwa umakini.
“Naam!” Akadakia Roman. “Basi tutaondoka na Diski mbili zenye mpango mzima wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, kuanzia mwanzo mpaka mwisho!”
Wenzake hawakumwelewa kwamba wangeondoka nazo vipi angali Diski zilikuwa zimefichwa sehemu ya siri? Teobale na Laurent wakamwangalia Roman baada ya kusema vile.
“Umesema jambo la maana Roman. Sasa hizo Diski tutaipataje?” Teobale akauliza.
“Hiyo ni kazi rahisi sana . Mimi naifahamu vizuri ofisi ya Fabio, na sehemu anapohifadhi nyaraka zake nyeti. Ni ndani ya droo iliyoko katika kabati maalum la chuma, hivyo kazi hiyo niachieni mimi, kwani nitaichukuwa kirahisi!” Roman akasema akiwapa moyo wenzake.
“Lakini cha muhimu tujue kwamba baada ya kutekeleza mpango huo, tutakimbilia wapi, yaani sehemu ya kwenda kujisalimisha!” Akasema Laurento.
“Kazi rahisi tu…” akadakia Roman. “Tutakimbilia sehemu za Ngara, nchini Tanzania , ambapo kuna Ofisi za Umoja wa Mataifa. Baada ya kufika tutawaeleza yote kwamba tumemtoroka Kanali Fabio, kiongozi msaliti, aliyeko katika msitu wa Kibungo, hivyo sisi tuko tayari kuwa mashahidi dhidi ya maovu yake punde atakapokamatwa. Hilo ni wazo langu jamani, tuchangie!
“Nimekubaliana na huo mpango wako kama ulivyopanga!” Laurent akasema huku akitabasamu.
“Ama kweli hicho ni kichwa!” Teobale naye akasema na kuongeza. “Mia kwa mia nimekubaliana nao kama ulivyopanga. Cha muhimu sasa tupange ni siku gani gani ya kuondoka!”
“ Kama tutafanikiwa, basi hatutakuwa na muda wa kupoteza. Tutaondoka muda wowote kwa kupitia katika barabara yetu ya siri, eneo la Rusumo kwa kutumia usafiri wa pikipiki yetu kubwa, ambayo ina uwezo wa kutubeba wote watatu. Baada ya kufika katika mto Rusumo, tutakuta kuna walinzi wenzetu, ambao huwa wanalinda. Ili wasitushtukie, tutawadanganya kwamba tuko doria katika kuimarisha ulinzi sehemu ile ya Rusumo, mpakani. Bila shaka watakubali na kuturuhusu kuvuka ng’ambo ya pili ya mto…”
“Tutaipakia pikipiki yetu ndani ya boti na kuuvuka mto ule mpaka upande wa pili na kuendelea na safari yetu kuelekea Ngara , Tanzania . Ni matumaini yangu mpaka hapo tumeelewana wapiganaji wenzangu!” Roman akamaliza.
“Hakuna shaka…umeeleweka vizuri,” Teobale akasema huku akiungwa mkono na Laurent.
Ni kwamba waliridhika!
“Ok, kama ni hivyo, ni vyema tumalizie vinywaji vyetu, kasha tuondoke!” Roman akawaambia.
Walipomaliza vinywaji, ilikuwa imetimu saa kumi na mbili za jioni. Wakanyanyuka na kutoka nje ya hoteli ile ya The Tropic Inn, iliyokuwa juu ya kilima kidogo, kilichofanya mandhari ya pale ipendeze hasa ukizingatia ilikuwa imezungukwa na miti mingi, pamoja na miamba michache yam awe iliyokuwa imechongwa kwa ustadi wa hali ya juu.
Wakaliendea lile gari Toyota Land Cruicer walilofika nalo, ambalo lilikuwa katika sehemu ya maegesho. Wakapanda na kuondoka kuelekea katika Kambi yao kwa kuifuata barabara ya vumbi, iliyokuwa inakatiza katika makazi ya watu, na hata, na hata vijijini katikati ya milima mingi. Ni hadi walipofika katika kambi yao na kuonekana kama walikuwa wametoka katika matambezi yao ya kawaida. Kumbe walikuwa na agenda ya siri! Ni usaliti dhidi ya Kiongozi wao Kanali Fabio Rushengo!
Ukweli ni kwamba hawakuwa na njia nyingine zaidi ya hiyo!
Kanali Fabio Rushengo alikuwa ni mwanajeshi aliyefuzu katika medani ya kivita, na aliyepata cheo katika umri mdogo wa ujana tu kutokana na kujituma kwake, pamoja na elimu aliyokuwa nayo. Yeye alikuwa ni mmoja wa wahusika wa machafuko yaliyotokea nchini Rwanda , mwaka 1994.
Baada ya mauaji yale ndipo alipokimbilia eneo la Kibungo, akitokea jijini, Kigali , akiwa na wafuasi kadhaa waliomuunga mkono, ambao walijichimbia ndani ya msitu ule mzito ili wasiweze kukamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya mauaji yale ya Kimbari yaliyoutikisa Ulimwengu!
Hata hivyo, viongozi wengi wa Serikali ya Rwanda hawakujua kwamba Kanali Fabio alikuwa bado mzima, kwani walijua ameshakufa muda mrefu katika machafuko yale, baada ya gari aina ya Jeep, alilokuwepo kulipuliwa na kombora zito la ‘ RPG’ (Rocket Propeller Gun) kule jijini Kigali .
Ni kwamba gari lile kabla halijalipuka, aliwahi kuruka nje na kukimbia katika maficho, ukiwa ni mtego aliokuwa ameutega yeye, ili kuwalaghai watu wasiweze kujua. Na ndiye aliyekuwa akiendesha machafuko yale kwa baadhi ya Wahutu na Watusi wenye msimamo wa wastani ndani ya nchi ya Rwanda .
Ili asiweze kujulikana, baada ya kukimbilia ndani ya msitu wa Kibungo, Kanali Fabio alijibadili sura yake kwa kufanyiwa upasuaji (Plastic Surgery) na mtaalamu aliyemuagiza kutoka nje ya nchi, kwa malipo manono. Hivyo sura yake ikawa ni nyingine tofauti na ile ya mwanzo, na akawa anatembelea sehemu mbalimbali bila kujulikana, kiasi cha kumsaidia kuratibu mipango yake ya nyuma. Na ili wasiweze kujulikana, ndani ya msitu ule wa Kibungo, walianzisha kijiji kidogo, na kushughulika na kilimo ili kuficha maovu yao .
Pia, wasaliti hao, walikuwa wamekimbilia ndani ya msitu huo wakiwa na silaha nyingi za hatari, ambazo walikuwa wamezihifadhi ndani ya handaki chini ya ardhi. Ni handaki lililokuwa limechimbwa kwa ustadi wa hali ya juu, ambapo kwa nje palikuwa na mitambo ya kufua umeme-jua uliosaidia kuzalisha umeme ule katika eneo lile la nyumba za kambi. Umeme ule ulisaidia kuendesha mtambo wa mawasiliano ya siri, ambao ulikuwa siyo rahisi kwa mtu yeyote kugundua zaidi ya wao wenyewe!
Kwa ujumla kundi lile liliweza kuwasiliana na watu wa aina mbalimbali kwa kuendesha vitendo vyao vya kijasusi, kiasi cha kuweza kudumu kwa muda mrefu bila bughudha yoyote tokea mauaji yale ya kimbari yatokee. Wakawa wanapanga mipango ya kuihujumu Serikali wakiongozwa na kanali Fabio, aliyekuwa na nguvu za kutosha, hasa ukizingatia umri wake ulikuwa miaka 47 hivi, akiwa mtu shupavu mwenye mwili uliojengeka kutokana na mazoezi aliyokuwa anafanya kila siku ili kuuweka mwili wake imara!
Kielimu, Kanali Fabio alikuwa ni msomi wa elimu ya kidato cha sita, na pia Chuo Kikuu cha Kigali . Baada ya kuhitimu masomo yake ya Chuo Kikuu, ambapo alisomea Uhandisi wa Mitambo, alijiunga na Jeshi la Rwanda kabla machafuko yale hayajatokea, ikiwa ni kazi aliyoipenda, akiwa na ndoto ya kuja kuwa kiongozi mkubwa siku moja; tena kiongozi wa nchi!
Tuseme alipenda sana madaraka!
Ni hadi yalipotokea mauaji yale ya Kimbari, yaliyosababishwa na machafuko ya kikabila, ambapo Kanali Fabio alichangia kuhamasisha baadhi ya askari wa chini yake, kufanya mauaji yale! Yalikuwa ni mauaji ya Wahutu na Watusi wenye msimamo wa wastani, ambao hawakuwa na hatia yoyote!
Ni hatari!
Baada ya machafuko yale ndipo Kanali Fabio alipoamua kukimbilia ndani ya msitu wa Kibungo akiwa na wafuasi wengi vijana. Pia, walikuwa na silaha nyingi walizoiba katika maghala ya kuhifadhia silaha sehemu mbalimbali, kwani hakukuwa na udhibiti wowote, ni harufu ya damu ilikuwa inanukia kila pembe ya nchi!
Ni kuchinjana tu!
Roman alikuwa kijana mjanja sana , ambaye alijua anachofanya. Baada ta kupanga ule mpango wao wa kumtoroka mkuu wao, Kanali Fabio, kila sekunde, dakika na saa, alikuwa hachezi mbali sana naye, kwani walikuwa na ukaribu, tofauti na wapiganaji wengine. Nia yake ilikuwa ni juu ya kuweza kuzipata zile Diski mbili, zenye siri ya maovu, ambazo Fabio alikuwa amezihifadhi ndani ya ofisi yake iliyojitenga na makazi yao kwa umbali kiasi.
Kwa vile Kanali Fabio alikuwa anamwamini Roman, hakumtilia shaka kabisa. Lile lilikuwa ni kosa kubwa sana alilofanya, kwani siku ya tatu tu, tokea wapange mpango ule wa kumtoroka, Roman alipata mwanya wa kuingia ndani ya ofisi ya Kanali Fabio, baada ya yeye kutoka nje ya kambi ile kwa shughuli zake binafsi. Baada ya kuingia, Roman akaliendea kabati la chuma lililokuwa mle ofisini, akapekuwa ndani yake na kufanikiwa kuzipata Diski mbili walizokuwa wanazihitaji.
Alifanikiwa kuzipata ndani ya droo mojawapo, kati ya droo kama kumi hivi alizokuwa amehifadhi vitu mbalimbali vilivyoweza kuuendesha ule mtandao wao. Ukweli ni kwamba alikuwa amefanya kazi ya ziada sana , baada ya kupekuwa kwa uangalifu sana . Baada ya kufanikiwa, Roman akalifungua lile kabati kama lilivyokuwa mwanzo, kisha akatoka huku akiwa na matumaini. Akaenda kuwasiliana na vijana wenzake, Obale na Laurento, ambapo walipanga mpango wa kutoroka usiku uleule kabla Kanali Fabio hajawashtukia.
Ilipotimu saa mbili za usiku, wote watatu walikuwa wameshajiandaa vya kutosha, wakiwa wameiandaa ile pikipiki kubwa aina ya Kawasaki . Waliijaza mafuta ya kutosha, pamoja na ya akiba yatakayoweza kuwafikisha katika safari yao waliyodhamiria. Giza nene lilikuwa limetanda eneo zima la msitu wa kibungo.
Lakini ni giza ambalo halikuwazuia kutimimiza azma yao ya kutoroka kama walivyopanga. Ili isijulikane kama wameondoka ndani ya kambi ile usiku, wakatoka kimya kimya, huku wakiikokota ile pikipiki bila kuitia moto, hadi walipofilka mbali. Wote watatu wakaipanda na kuifuata barabara ya siri iliyokuwa inakatiza katikati ya msitu uliokuwa na milima na miteremko mikali sana . Roman akiwa mtaalam, ndiye alikuwa anaendesha ile pikipiki kubwa! Wakakata mbuga!
Kwa vile barabara ile ilikuwa mbaya, walitumia saa moja na nusu kufika eneo la Rusumo, ambapo palikuwa na ule mto mkubwa sana . Ni mto Rusumo uliokuwa na upana wa mita 120 hivi, na ili kuuvuka ilibidi kutumia mtumbwi au boti. Vilevile ni mto uliotumika kama mpaka wa nchi za Rwanda na Tanzania , ambapo walitegemea kuwakuta walinzi, vijana wawili ambao pia ni waendesha boti maalum inayotumika kuwavusha watu ng’ambo ya pili ya mto ule. Ni vijana waliojulikana kwa majina ya Ndayize na Wizimana.
Walinzi wale, walikuwa wameshauona mwanga wa pikipiki ile kuanzia mbali, ikiwa inaelekea pale walipokuwa. Hivyo wakaamua kubanisha juu ya kilima kidogo, sehemu iliyokuwa na kibanda chao cha ulinzi, kilichoezekwa kwa nyasi. Wakawa wanaangalia kwa makini watu wale walivyokuwa wanaelekea sehemu ile usiku ule, bila kutoa taarifa yoyote.
Ndayize na Wizimana walikuwa na bunduki zao aina ya Sub-Machine Gun ‘AK 47’ tayari kwa kufyatua risasi kama angetokea adui. Roman na Obale wakafika katika eneo lile na kusimamisha pikipiki. Hata hivyo walikuta pakiwa kimya, bila kuwaona wale walinzi. Wakashuka na kuamua na kuamua kutoa ishara zinazowafanya watambuane katika kundi lao, ambapo Roman alipoanza sauti kali iliyokipasua kile kimya cha usiku ule kwa kusema: “Chuiii!”
“Simbaa!” Wizimana aliitikia ishara ile wakiwa bado wamebanisha juu ya kilima kile.
Halafu walinzi wakashuka kuwafuata baada ya kugundua ni wenzao, ambapo baada ya kuwafikia, waliwakuta ni Romeo, Teobale na Laurent wakiwa wamesimama kando kidogo ya pikipiki yao , na pia wamevalia majaketi mazito ya kukabiliana na baridi.
“Oh, ni nyie?” Ndayize akasema huku akiiweka bunduki yake vizuri.
“Ni sisi watu wa kazi!” Akasema Roman.
“Karibuni jamani…” Ndayize akamwambia.
“Ahsante sana …”
“Vipi jamani, mbona usiku wote huu? Safari ya wapi?” Ndayize akauliza.
“Jamani sisi tuko safarini, kwetu ndiyo kumekucha!” Akasema Roman na kuendelea. “Si mnajua bosi, Fabio ametupangia kazi ya kufuatilia fununu za maadui ng’ambo ya pili ya mto huu. Hivyo sisi ndiyo tunavuka kwenda kufanya upelelezi juu ya fununu hizo!”
“Hakuna tatizo…mnaweza kuendelea na safari, ngoja tuwavushe…” Ndayize akasema huku akiuamini ule uongo!
Wote wakaiendea ile boti kubwa iliyokuwa imeegeshwa kando ya mto Rusumo. Ni boti iliyokuwa na injini ya Yamaha, na kwa kusaidiana, wakaibeba ile pikipiki na kuipandisha juu ya boti, halafu wakaisukuma ndani ya maji, kasha wakapanda.
Nahodha wa boti alikuwa ni kijana Ndayize, ambaye aliitia moto na kuondoka kwa mwendo wa kasi na kuelekea upande wa pili wa mti ule, ambao ni upande wa nchi ya Tanzania. Ni sehemu iliyokuwa na vichaka vilivyofungamana na kulizidisha giza lile la kutisha!
“Oh, tumefika jamani!” Roman akasema baada ya kufika upande wa pili, ambapo hawakuchukuwa muda mrefu.
“Na kweli…” akaongeza Teobale.
Baada ya kufika ukingoni, wote wakashuka ndani ya boti, kisha wakasaidiana kuitoa ile pikipiki, ambayo baadaye, vijana Roman, Teobale na Laurent waliipakia na kuwaaga, Ndayize na Wizimana. Hata hivyo walinzi wale waliendelea kuwaangalia nusu wakiwaamini nap engine kutowaamini! Lakini hawakuwa na la kufanya. Pikipiki ile ikaondolewa kwa mwendo wa kasi kulitoka eneo lile la Rusumo!
“Turudi zetu…” Wizimana akamwambia Ndayize huku akiirukia boti yao .
“Hakuna shida,” Ndayize akasema halafu akaendelea. “Hivi ni kweli unawaamini hawa jamaa, kwamba wametumwa kazi na bosi usiku huu?”
“Hata mimi sijui. Lakini si ndiyo walivyosema wao?”
“Tumefanya kosa sana kuwaamini.”
“Sasa ulitakaje?”
“Tungemuuliza kwanza bosi…”
“Basi, hakuna jinsi…twende zetu…”
Hatimaye, Ndayize na Wizimana wakarudi ng’ambo ya pili ya mto, upande wa Rwanda , kuendelea na kazi yao ya ulinzi. Lakini ukweli unabakia kwamba, vijana wale walikuwa wamewatoka kiaina! Walikuwa wanakwenda kumchoma kiongozi wao, Kanali Fabio.
Ama kweli ulikuwa ni ujasiri wa hali ya juu!
Safari iliendelea usiku ule, huku pikipiki ikichanja mbuga. Roman alikuwa akiiendesha huku akiifuata njia ya mkato isiyo rasmi, hadi walipofika katika barabara kuu ya lami inayotoka nchini Rwanda , kuelekea Tanzania , kupitia kituo cha ukaguzi, Uhamiaji na Ushuru wa Forodha mpakani Rusumo. Sehemu yote ilikuwa kimya kabisa, kukizungukwa na pori tu. Hakukuwa na dalili za kuishi kwa binadamu katika eneo lile zaidi ya wanyama wadogo wadogo tu.
Baada ya kuiacha barabara ile, wakaifuata hadi walipofika katika kitongoji cha Benaco, eneo la Ngara. Wakaiacha barabara ya lami na kuifuata ya vumbi hadi walipotokeza eneo la Kumunazi. Roman akiwa ni mwenyeji, aliiendesha ile pikipiki kuelekea katika makambi ya Wakimbizi ya Lukole, wakati ule yalikuwa yakihifadhi wakimbizi kutoka nchi za Burundi na Rwanda , ambao wengi wao walizikimbia nchi zao kutikana na machafuko na mapigano ya kikabila, kati ya Wahutu na Watutsi.
Hatimaye wakafika kwenye kizuizi cha upekuzi wa kuingia ndani ya makambi, ambapo palikuwa na walinzi maalum. Ni walinzi waliowekwa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, ambao huteuliwa kutoka katika makundi ya wakimbizi, hasa wale wanaojua lugha ya kiswahili kwa ufasaha. Katika kizuizi kile, palikuwa na kibanda kilichokuwa kando ya barabara upande wa kushoto. Mlinzi mmoja akatoa amri huku akimulika tochi.
“Simamaa!”
“Sawa!” Roman akasema na kusimamisha pikipiki.
“Zima taa na ujitambulishe!” Amri ikaendelea kutolewa.
Roman akazima taa.
“Jitambulisheni!” Wakaambiwa!
“Sisi ni Wakimbizi!” Roman akasema.
“Wakimbizi?” Mlinzi yule akauliza kana kwamba alikuwa hajamwelewa.
“Ndiyo…wakimbizi!” Akasistiza Roman.
“Wakimbizi kutoka wapi?”
“Tunatoka nchini Rwanda !”
“Mh, makubwa!” Mlinzi yule akasema, kisha akaenda kuwasiliana na mkuu wao.
Hatua iliyofuata ilikuwa ni kuwapeleka Roman, Laurent na Teobale katika Kituo cha Polisi kilichokuwa ndani ya kambi ya wakimbizi ya Lukole, Ngara. Ni kituo kilichokuwa umbali wa kilometa mbili hivi kutoka pale kwenye kizuizi. Nia yao ilikuwa ni kwenda kupata ufumbuzi, ukizingatia wale walikuwa ni wakimbizi kweli, waliokuwa na sababu za msingi, ingawa wakimbizi wa Kinyarwanda walikuwa wamesharudi nchini Rwanda muda mrefu, baada ya nchi yao kuwa katika hali ya usalama.
Mpaka muda ule vijana, Roman, Teobale na Laurent wanafikishwa kwenye Kituo cha Polisi, palikuwa pameshapambazuka. Askari waliokuwa pale walifanya mahojiano nao, na baada ya kuridhika nao, wakawakabidhi kwa Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ambapo ilikuwa mlemle kambini.
Maofisa wale wakawachukuwa na kuwasafirisha hadi mjini Ngara, katika Ofisi za Umoja wa Mataifa. Nao wakafanya mahojiano nao na kuona walikuwa wanafaa kuwa mashahidi muhimu dhidi ya Kanali Fabio, msaliti wa Serikali ya Rwanda .
Siku ileile jioni yake, vijana wale walitafutiwa makazi ya muda mjini Ngara, ili ufanyike utaratibu mwingine wa kuweza kuwasafirisha sehemu yoyote itakapopangwa. Hakika walijiona kuwa wamejikomboa kutoka mikonono mwa Kanali Fabio Rushengo. Wakataka kuyaanza maisha mapya kama wao, bila kutegemea kuishi msituni wakipokea amri ya mtu mmoja!
Asubuhi siku ya pili kulipambazuka vizuri. Kanali Fabio aliamka na kuendelea na utaratibu wake wa kila siku wa kujua mwenendo mzima wa shughuli za ulinzi wa kambi ile yao . Hata hivyo Fabio alishtuka baada ya kutowaona vijana wake watatu, Roman, Obale na Laurento, kwani ilikuwa ni lazima wapige ripoti kila asubuhi. Na hata baada ya muda aligundua kwamba walikuwa wamemkimbia, kwani waliondoka na vitu vyao muhimu, pamoja na ile pikipiki yao kubwa aina ya Kawasaki , ambayo haikuwepo katika gereji ya kuhifadhia vyombo vya moto.
Kanali Fabio akiwa amechanganyikiwa, akaingia ndani ya ofisi yake na kufanya upekuzi wa kina baada ya kuingiwa na wasiwasi, na ndipo alipogundua kuwa vijana wale walikuwa wameondoka na zile Diski mbili zilizokuwa na ule mpango mzima wa mauaji ya Rwanda ! Ukweli ni kwamba hakuwaelewa walikuwa na maana gani kumtoroka, tena wakiwa na ile siri kubwa ya mauaji aliyokuwa ameificha muda mrefu sana .
Basi hakutaka kupoteza muda, Fabio akaamua kumwita msaidizi wake wa karibu, aliyejulikana kwa jina la, Emmanuel Miburo, au kifupi Emma. Halafu akamwambia wakutane kwenye chumba cha mikutano, ambacho huwa wanafanyia mikutano mara kwa mara. Chumba kilikuwa kimejengwa kwa matofali ya kuchoma na kuezekwa juu kwa nyasi, ndani yake pakiwa na viti vilivyotengenezwa kwa miti iliyochimbiwa chini, na juu yake kuezekwa mabanzi.
Emma aliusikiliza ule wito wa mkuu wake, Kanali Fabio na kuingia mle ndani ya chumba na kumsubiri. Fabio akaingia mle ndani, ambapo hakukaa kitini kama kawaida yake, akawa amesimama huku ameshika kiuno chake na kutikisa kichwa!
Alikuwa akisonya ovyo!
“Nashindwa kuelewa!” Kanali Fabio akamwambia Emma.
“Kuelewa nini mkuu?” Emma akauliza huku akimshangaa kwa kumuoana akiwa katika hali kama ile!
“Nimechanganyikiwa!”
“Kwani vipi mkuu…umechanganyikiwa nini?” Emma akamuuliza baada ya kumwona akiwa katika hali kama ile! Ni kweli, amechanganyikiwa!
“Sijui ni kitu gani kinaendelea!”
“Hebu niambie mkuu…kuna nini?”
“Hivi una habari kuwa umetokea usaliti ndani ya kambi yetu?” Kanali Fabio akamwambia.
“Sina habari mkuu!”
“Basi elewa hilo! Hapa kambini usaliti umetokea! Na mpaka hivi sasa ninapoongea na wewe hapa ndani ya chumba hiki, wenzetu, Roman, Teobale na Laurent wametoroka hapa kambini na vitu vyao vyote!”
“Mungu wangu! Wametoroka?”
“Ndiyo!” Fabio akasema na kuendelea. “Na mbaya zaidi wameondoka na Diski zangu mbili, zenye taarifa zangu ya siri nilizohifadhi ndani yake!”
“Mh, makubwa! Mkuu unasema kwamba walitoroka jana usiku?”
“Ndiyo, lakini taarifa za kutoroka kwao nimezipata leo asubuhi, kutoka kwa walinzi waliokuwa zamu katika mto Rusumo. Ni Ndayize na Wizimaana, ambao waliwaona wakiwa na ile pikipiki kubwa ya hapa Kambini.”
“Sasa sijui watakuwa wameelekea wapi?” Emma akaendelea kuuliza.
“Ukweli ni kwamba sielewi…lakini nasikia walipovuka mto Rusumo, walielekea upande wa Tanzania , kwenye makambi ya wakimbizi yaliyoko Ngara!”
“Hata mimi nahisi watakuwa wamekimbilia huko. Lakini cha kujiuliza ni kwa nini wamechukuwa zile Diski?”
“ Hilo ndiyo la kujiuliza!” Fabio akasema na kuendelea. “Naona kwamba wana sababu zao, hasa ukizingatia kwamba hawakuacha ujumbe wowote!”
“Mh, hii kali!” Emma akasema huku ameinamisha kichwa chake chini!
“Sasa sijui tufanyeje Emma? Hebu naomba ushauri!”
“Ushauri wangu ni kuwafuatilia kama watakuwa wamekimbilia Ngara , Tanzania , ambapo sisi ni wenyeji!”
“Kwa hivyo unanishauri nitume mtu?”
“Ndiyo mkuu!”
“Itabidi nikutume wewe!”
“Usitie shaka mkuu! Nitakwenda mimi mwenyewe!”
“ Safi sana Emma…” Kanali Fabio akasema na kuendelea. “Ndiyo maana nakuamini!”
“Ni hivyo mkuu, kwa vile mimi ni mzoefu ndani ya makambi yale. Nitakwenda kupeleleza, kama itakuwa wamefika kule, tutajua la kufanya, ikiwa yote ni kusubiri maelekezo!”
“Basi, tutafanya hivyo…itabidi uwafuatilie huko, ambapo ukiwapata itakupasa uwalipue baada ya kuhakikisha umezipata zile Diski zangu. Mimi nakufahamu sana Emma, hakuna muda wa kupoteza…tupange safari!”
“Ndiyo mkuu… mimi ni mtu wa kazi. Napendelea nisafiri kesho, siku ya leo itakuwa ni kwa ajili ya maandalizi!”
“Hakuna tatizo…kajiandae!”
Kanali Fabio na Emma Miburo wakamaliza kupanga mikakati yao ya kuwasaka wale wenzao waliowasaliti na kuikimbia kambi ile. Baada ya kumaliza kila mmoja akaendelea na shughuli zake, ambapo Emma alikwenda kujiandaa kwa ajili ya safari ile ya mtafutano, ambapo hakujua kama angefanikisha kuwapata.
Ukweli ni kwamba alijua kuwa vijana wale, walikuwa ni watu wenye medani za kivita, hivyo siyo rahisi watoroke, halafu waje kupatikana tena! Walijua walichokuwa wanafanya!Emma Miburo alikuwa ni mmoja wa wale watu makatili sana .
Hapo mwanzoni alikuwa askari katika Jeshi la Rwanda , ambapo alijiunga pindi alipomaliza elimu ya Sekondari, kidato cha nne, ikiwa ni kazi aliyoipenda tokea mwanzoni akiwa mdogo, hasa ukizingatia baba yake alikuwa Mwanajeshi. Ndiyo kusema alikuwa ametokea katika familia ya kijeshi na kuishi katika Kambi za Kijeshi!
Baada ya machafuko yale yaliyotokea nchini Rwanda , ndipo Emma alipojiunga na kundi la Kanali Fabio, baada ya kuhamasishwa kwamba angefaidika. Na kweli, akapewa cheo cha msaidizi wake.
Akiwa na umri wa miaka 35 tu, Emma alikuwa jasusi wa hali ya juu, na mjuzi wa kutumia silaha za aina mbalimbali, ambazo alijifunza kutokana na kuipenda kazi ile ya jeshi. Hakika alikamilika kila idara!
Vilevile Emma hakuwa mgeni nchini Tanzania , kwani alikuwa ameshatembelea sehemu mbalimbali, kama mkoa wa Kagera, hasa katika makambi ya wakimbizi ya Benaco, Wilayani Ngara. Pia, aliwahi kutembelea mikoa ya Mwanza, Kigoma na Arusha katika mizunguko yake. Ndani ya jiji la Arusha, Emma aliwahi kukaa akiwa ni mwenyeji wa mfanyabiashara mmoja maarufu, aliyeitwa, Paul Rugoye, aliyekuwa anamiliki kampuni ya kuhudumia watalii, na nyinginezo.
Emma aliweza kuishi vizuri bila kubughudhiwa na mtu yeyote, kwani hakuna aliyejua kwamba alikuwa raia wa nchi jirani ya Rwanda .
Basi, huyo ndiye mtu hatari na jasusi, Emmanuel Miburo!
Mjini Ngara, nchini Tanzania , Maafisa wa Umoja wa Mataifa, walikuwa wameshaomba kibali kwa Wizara ya Mambo ya Ndani, kwa ajili ya kuwasafirisha vijana, Roman, Teobale na Laurent, mpaka mkoani Arusha, ilipo Mahakama ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Rwanda yaliyotokea Mwaka 1994. Na ile ilikuwa ni baada ya taratibu zote kukamilika siku ile ya pili yake tu tokea watoroke nchini Rwanda . Ili waweze kuwahishwa Arusha, na pia kuepuka mtego wa kuwadhuru,walikodiwa ndege ndogo, ambayo ingewafikisha mapema.
Majira ya saa moja za asubuhi, wote watatu walichukuliwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser hadi katika uwanja mdogo wa ndege, ulioko katika vilima vya Ngara, nje kidogo ya mji, sehemu yenye miteremko mikali. Ingawa uwanja ule ulikuwa umejengwa mlimani, lakini sehemu yenyewe ilikuwa tambarare, hasa ukizingatia maeneo yote yalikuwa na milima na mabonde mengi. Baada ya kufika pale uwanjani, wakaikuta ndege ndogo aina ya Cessna Caravan ya kampuni ya kukodi.
Wote wakapanda wakiongozwa na Maafisa wawili wa Umoja wa Mataifa, waliokuwa wasindikizaji. Na dakika mbili baadaye rubani akaiwasha ndege na kuiondoa kuelekea katika njia yake ya kurukia, hatimaye akaitoa kwa mwendo wa kasi na kuirusha kuelekea upande wa Mashariki. Ilikuwa ni safari ndefu, lakini baadaye ndege ile ilifika Arusha na kutua kwenye uwanja wa ndege ulioko Kisongo, jijini Arusha.
Wote wakashuka na kupokewa tena na Maafisa wa Umoja wa Mataifa, waliofika na magari yao . Roman, Teobale, na Laurent wakapanda ndani ya gari mojawapo na kuondoka pale uwanjani, kuelekea sehemu waliyotafutiwa makazi ya muda. Walikuwa wametafutiwa nyumba nzuri ya kuishi iliyojengwa kwa ajili ya mashahidi muhimu wa kesi za watuhumiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda.aa
Makazi yao yalikuwa eneo la Njiro, lililoko nje kidogo ya jiji la Arusha, ikiwa ni sehemu iliyotulia, zilipojengwa nyumba nyingi zinazomilikiwa na wafanyakazi wa mahakama ile, wengi wao wakiwa raia wa nje ya Tanzania . Ni nyumba iliyokuwa inalindwa kwa muda wa saa 24 na walinzi maalum, ili wasiweze kudhurika na watu waovu, wengi wao wakiwa ni wale waliohusika kwa njia moja ama nyingine katika kufanikisha mauaji yale, walioukwepa mkono wa sheria.
Baada ya kuhakikisha usalama wao, vijana, Roman, Teobale na Laurent, walijichimbia ndani ya nyumba ile huku wakipanga mikakati yao juu ya kutoa ushahidi ule wa Diski, na jinsi ya kuweza kuwasiliana na Maafisa wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo wakaona kuwa ni busara wangezitoa punde zitakapohitajika. Wakazichimbia sehemu za siri huku wakimwazia kiongozi wao, Kanali Fabio atakavyochanganyikiwa!
Nchini Rwanda , ndani ya msitu wa Kibungo, katika kambi ya waasi, Emmanuel Miburo, msaidizi wa Kanali Fabio alikuwa ameshajiandaa vya kutosha, punde tu alipopanga safari ile ya kuwafuatilia vijana, Roman, Teobale na Laurent, Ngara, nchini Tanzania , ambapo alihisi kuwa wamekimbilia huko. Hakika alikuwa ameandaa baadhi ya zana zake za kazi kama, bastola, visu maalum, na dawa za aina mbalimbali zikiwa ni pamoja na za sumu pamoja na za usingizi, ambazo zingemsaidia sana katika kazi ile ya kijasusi!
Alipomaliza, Emmanuel akaondoka kwa kupitia njia ya halali, kwani alikuwa na Hati ya kusafiria iliyomtambulisha kama ni mfanyabiashara anayesafiri nchi mbalimbali za ukanda wa Maziwa Makuu, kama vile, Burundi , Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo , Uganda na Tanzania . Hivyo alipitia ‘Boda’ ya Rusumo na kuvuka mpaka upande wa Tanzania , halafu akachukuwa usafiri wa gari dogo hadi katika kitongoji kidogo cha Benaco.
Pale akashuka na kufanya utaratibu wa kutafuta chumba cha kupanga katka nyumba ya kulala wageni, na kwa sababu alikuwa amezoeleka na watu wengi, hakuwa na wasiwasi wa kufichuka kwa mpango wake mwovu wa kufanya upelelezi!
Emmanuel alipanga nyumba ya wageni ya Kivulini Gesti, iliyokuwa maarufu sana katika kitongoji kile, ikiwa inatumiwa na watu wengi, hasa madereva wa magari makubwa ya mizigo yanayolala pale usiku wakati wakiwa safarini kuelekea nchini Rwanda na kwingineko.
Ilipotimu saa sita za mchana, Emmanuel aliamua kuelekea katika makambi ya wakimbizi ya Lukole, yaliyokuwa umbali wa kilometa kumi na tano kutoka katika kitongoji kile cha Benaco. Akachukuwa usafiri wa teksi, ambayo ilimfikisha ndani ya kambi na kumshushia eneo la Sokoni, palipokuwa na pilikapilika nyingi za watu.
Akiwa ni mtu mzoefu ndani ya kambi ile, Emmanuel alizunguka kutwa nzima na kujichanganya na wakimbizi wengine. Akawa anapeleleza kwa kila anayefahamiana naye, ambapo alifanikiwa kupata taarifa zile kuhusu vijana, Roman, Teobale na Laurent. Akaambiwa kuwa ni kweli walifika kujisalimisha kwa polisi wanaolinda usalama, na kisha kupelekwa kwa Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani, pamoja na wale wa Umoja wa Mataifa na kufanya mahojiano nao!
Ni hatari!
Pia, Emmanuel aliambiwa kwamba vijana wale walikuwa wameondoka kwa ndege asubuhi ile, kuelekea Arusha, tayari kuwa Mashahidi Muhimu, baada ya kuwa na ile siri nzito. Baada ya kuzipata habari zile, Emmanuel akaondoka ndani ya kambi ile ya wakimbizi, na kurudi Benaco alikopanga chumba. hakika alirudi akiwa amechanganyikiwa sana , kwani hakutegemea kabisa kama vijana wale walikuwa wameamua kufanya vile.
Akakodi teksi iliyomfikisha na haraka akaingia chumbani na kumharibarisha Kanali Fabio Rushengo, kwa kutumia simu ya mkononi, ambayo mtandao wake ulitumika katika nchi mbalimbali duniani.
“Emma Miburo hapa mkuu!” Emma alijitambulisha baada
ya kumpata kwenye laini.
“Ndiyo Emma…habari za huko…”
“Habari za huku siyo nzuri mkuu!”
“Una maana gani?”
“Nimefanikiwa kufika hadi ndani ya kambi ya wakimbizi ya Lukole, Ngara. Nimefanya upelelezi wangu na kugundua kuwa vijana wale ni kweli walikuwa wamefika kujisalimisha kwa Maafisa wa Umoja wa Mataifa!”
“Mh!” Fabio akaguna. “Baada ya kujisalimisha?”
“Wakawaelewa shida yao iliyowapeleka nchini Tanzania , ambayo siyo nyingine zaidi ya kukukimbia wewe!”
“Kunikimbia mimi?”
“Ndiyo mkuu!” Emma akasema na kuendelea. “Tena mbaya zaidi, wamesema kwamba wana siri nzito dhidi yako ambayo hata mimi sijaijua!”
“Mungu wangu! Ni zile Diski zangu tu, zenye mambo yangu ya siri!” Kanali Fabio akadakia.
“Na kingine zaidi ya hapo mkuu, ni kwamba wameshasafirishwa kwenda Arusha, katika Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya Mauaji ya Rwanda !”
“Oh, basi Emma!”
“Basi nini bosi?”
“Basi…basi…rudi haraka tupange mipango mingine kabla mambo hayajaharibika!” Kanali Fabio akamwambia.
“Sawa Mkuu…nitafanya hivyo!”
Baada ya Emmanuel kupewa maagizo yale, akaamua kuwa ni lazima afunge safari ya kurudi Kibungo, nchini Rwanda punde patakapopambazuka tu. Na kweli palipokucha Emma aliondoka kwa njia ile aliyokuja nayo hadi nchini Rwanda katika kambi ya waasi!
Kazi ilikuwa bado!
Paul Rugoye alikuwa ni mfanyabiashara maarufu jijini Arusha , Tanzania , ambaye alikuwa anamiliki kampuni ya kuhudumia watalii, iliyojulikana kwa jina la Rugo safaris, ambayo makao yake yalikuwa Arusha. Ni kampuni iliyokuwa na wateja wengi sana kutokana na zile huduma nzuri walizotoa.
Basi, Paul Rugoye ndiye aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, akifuatiwa na wasaidizi wake, kama vile, Meneja, Mhasibu na wengineo, ambao walikamilisha safu ya uongozi wa kampuni ya Rugo Safaris.
Ingawa Paul Rugoye alikuwa mfanyabiashara, pia alikuwa ni jasusi hatari sana . Alikuwa kishirikiana na Kanali Fabio Rushengo kwa njia moja ama nyingine. Akiwa na umri wa miaka ipatayo hamsini hivi, Paul alikuwa ni mzaliwa wa Mkoa wa kibungo, nchini Rwanda .
Lakini kwa kipindi chote alijifanya ni mzaliwa wa Wilaya ya Ngara, Mkoani Kagera, na kabila lake ni Mhangaza, ingawa ni kweli kwamba alizaliwa upande wa Tanzania . Ndiyo tuseme kuwa ndugu zake wengi walikuwa nchini Rwanda , ambao idadi kubwa wakiwa wahanga wa mauaji ya kimbari.
Akiwa jijini Arusha, Paul Rugoye alikuwa akifanya upelelezi, chini ya kivuli cha kumiliki ile kampuni ya kuhudumia watalii, akimsaidia Kanali Fabio. Nia yake ilikuwa ni kuweza kugundua watu waliotegemea kutoa ushahidi katika Mahakama ile ya mauaji ya Rwanda , inayoendeshwa na Umoja wa Mataifa. Halafu kinachofuata ni wao kumaliza kwa njia za kijasusi wanazozijua wenyewe. Hakika walikuwa ni watu hatari sana !
Ndipo Kanali Fabio akiwa nchini Rwanda , alipoamua kumpigia simu Paul Rugoye, na kumweleza lile tatizo la kusalitiwa na wale vijana watatu, Roman, Teobale na Laurent, ambao walikuwa wameshawasili jijini Arusha. Baada ya kumaliza kumweleza yote, akamalizia kwa kusema:
“Sasa naomba ushauri wako…”
“Aisee…kuna kazi…lakini, sisi tukiwa watu wa kazi, hatushindwi kitu!” Kanali Fabio akamwambia kwa sauti ya kujiamini na kusisitiza!
“Unayosema ni kweli…” Paul alisema na kuendelea.
“Sasa usihofu. Mimi nitapanga mipango kambambe. Tuma vijana wako wa kazi, kama watatu hivi, waje hapa jijini Arusha, ambao tutafanya nao kazi na kuwasambaratisha wasaliti hao kabla hawajaleta madhara yoyote kwa upande wetu!”
“Kuhusu vijana wa kazi, hakuna tatizo, nitawachagua leo hii hii. Lakini tatizo jingine ni namna ya kuwasafirisha kutoka hapa nchini Rwanda hadi huko Arusha.”
“ Hilo lisikutie hofu. Mipango yote nitaipanga mimi, na jinsi ya kuwachukuwa vijana hao kutoka huko mpaka Arusha.”
“Sawa Paul…nakutegemea wewe!”
“Usihofu…tutawasiliana zaidi.”
Kanali Fabio na Paul wakakubaliana katika mpango ule, ambapo alikubaliana katika mpango ule, ambapo alikubali kuratibu mpango mzima wa safari ile ile, kuanzia Rusumo, Ngara, hadi jijini Mwanza , Tanzania .
Fabio akapanga kuwachagua vijana wake shupavu, aliokuwa anawaamini sana , ambao ni Jean Rutaga, France Bizimana na Pierre Bisamo.
Ni vijana waliokuwa na taaluma ya kijasusi wa hali ya juu!
MAJIRA ya saa tatu za usiku, Kanali Fabio alikuwa amekaa ndani ya chumba cha mikutano. Alikuwa anawasubiri vijana wake, Jean , France na Pierre, ambao alikuwa ameshawaeleza juu ya kukutana kwao kwa ajili ya kazi ile ya kukata na shoka. Ingawa yeye alitakiwa awe mtu wa mwisho kufika, lakini alijikuta ametangulia kwa ajili ya wasiwasi uliokuwa unamtawala. Muda wote aliokuwa amekaa pale, Fabio alikuwa akiangalia saa yake na kuendelea kuwaza juu ya zile Diski mbili, na mpango mzima wa mauaji ya Rwanda aliyokuwa ameyapanga.
Kama Diski zile zikiwafikia wahusika, basi angehusishwa na mauaji yale, kitu ambacho hakupendelea. Tuseme vijana wake waliomtoroka, wangekuwa mashahidi muhimu, ambao wangewezesha kukamatwa kwake, ingawa alikuwa amesahaulika muda mrefu sana , na pia alishabadilisha sura yake kwa kuwekewa ya bandia!
Sasa iweje wamharibie mipango yake?
Haiwezekani!
Ni lazima wafuatwe kule walipo!
Wafutwe katika uso wa dunia!
Wakati Kanali Fabio akiwa katika lindi la mawazo, vijana maalum, Jean, Pierre na France wakaingia ndani ya chumba kile cha mikutano walichoahidiana kukutana usiku ule.
“Mkuu tumefika!” Pierre akasema kwa niaba ya wenzake, wakiwa bado wamesimama.
“Oh, karibuni na mkae…” Fabio akasema huku akivuta pumzi ndefu.
“Ahsante mkuu!” Wote wakasema na kukaa vitini.
“Vizuri sana !” Kanali Fabio akasema huku akiwaangalia vijana wake, na kukubali kweli walikuwa ni watu wa kazi!
Baada ya kukaa, wakaendelea kumwangalia Kanali Fabio aweze kuwapa majukumu aliyokuwa amewaitia usiku ule. Ukweli ni kwamba walijua kuwa kulikuwa na kazi muhimu, hasa ukizingatia haikuwa kawaida ya kiongozi wao kutangulia katika chumba cha mikutano kabla yao , kama alivyofanya siku ile. Kwa vyovyote kuna jambo kubwa lilikuwa limemkwaza!
Kimaumbile, kijana wa kwanza, Jean alikuwa mrefu, mwenye umbile la miraba minne liliojengeka vyema. Alikuwa na umri wa miaka 30 hivi, akiwa Jasusi tegemeo kwa Kanali Fabio. Kijana wa pili, France , naye alikuwa amefuzu kama Jean, na tatu ni Pierre, ambaye naye alikuwa na taaluma kama wenzake wawili.
Wote walijazia miili mithili yua wabeba vyuma! Hakupoteza muda, Kanali Fabio akawaeleza madhumuni mazima ya ile safari yao ya kuwafuatilia wenzao waliowasaliti, Roman, Teobale na Laurent, waliokimbilia jijini Arusha, nchini Tanzania . Halafu akamalizia kwa kusema: “Ni matumaini yangu kuwa nyote mko tayari kwa kazi!”
“Ndiyo, sisi tuko tayari kwa kazi!”
“Tuko timamu mkuu!” Pierre akasema.
“Tuko tayari mkuu!” Akaongeza France .
“Vizuri sana kama mko tayari,” Kanali Fabio akawaambia na kuendelea. “Nimeshafanya mawasiliano yote na Paul Rugoye, aliyeko Arusha , Tanzania , ambaye ataratibu safari yenu nzima. Mtatoka hapa kambini kwa usafiri wa gari mpaka Rusumo kwa kutumia barabara yetu ya siri inayokatiza msituni, hadi kwenye mto Rusumo. Baada ya kufika pale mtoni, mtavushwa na boti mpaka ng’ambo ya pili, upande wa Tanzania . Mkishavushwa tu, mtatembea kwa miguu umbali wa kilometa tatu hivi, mpaka mtakapofika katika barabara kuu iendayo Benaco kutoka Rusumo.
“Pale mtakuta gari moja aina ya Mitsubishi Fuso, la mizigo, likiwa limeegeshwa kwa kuwasaidia nyie. Dereva wake ameshapewa maelekezo yote kuwa awachukuwe hadi Mwanza, na baada ya kufika jijini Mwanza, mtakuta usafiri mwingine uliotayarishwa na Paul Rugoye, wa kuwafikisha Arusha…sijui mmemnielewa?” akamaliza Fabio.
“Tumekuelewa mkuu…” wakasema kwa pamoja.
“Ok, kama mmenielewa, nifuateni…” Kanali Fabio akawaambia.
“Sawa mkuu…” vijana wale wakasema huku wakinyanyuka na kumfuata nyuma.
Walielekea na kuingia ndani ya handaki maalum, ambamo ndani yake kulikuwa na silaha za kila aina. Baada ya kuingia ndipo alipowapangia majukumu mengine, pamoja na kuwapatia zana za kazi, na mavazi yaliyoweza kuficha silaha za hatari, zikiwemo bunduki fupi fupi aina ya ‘Uzi,’ bastola za kijeshi, na mabomu ya kutupa kwa mkono. Pia, akawapa dawa maalum za vidonge, ambazo zilikuwa sumu kali iliyoweza kuua mara moja, ambavyo hutumiwa na majasusi wanapokuwa wamezidiwa ili wasiweze kutoa siri kwa jinsi walivyokula kiapo!
Mbali ya silaha hizo, pia walikabidhiwa vifaa vya mawasiliano, ambavyo vingewasaidia kuwasiliana watakapokuwa Arusha. Baada ya kuchukuwa vifaa vyao vyote, wakatoka ndani ya lile handaki hadi nje, ambapo walikuta gari aina ya Toyota Land Cruiser likiwasubiri tayari kwa safari ile kuelekea Rusumo mpakani!
“Jamani, usafiri ndiyo huu hapa!” Kanali Fabio akawaambia.
“Ni sawa mkuu!” Wote wakasema na kujiandaa kuingia ndani ya gari.
“Haya, nawatakia safari njema. Lakini kumbukeni kuwa mawasiliano ni muhimu sana !”
“Tutafanya hivyo mkuu!”
Wakamalizana.
Hatimaye wote wakapanda ndani ya lile gari, ambapo dereva alikuwa ndani yake akiwasubiri. Akalitia moto na kuliondoa eneo lile la kambi. Ulikuwa ni usiku wa saa tano, na sehemu yote ilikuwa giza tupu. Hata hivyo baada ya saa moja na nusu wakawa wamefika Rusumo, mbali kidogo na ule mto. Dereva akalisimamisha gari kando ya msitu mzito, na vijana, Jean, Pierre na France wakashuka wakiwa na ile mizigo yao midogo, kisha wakamruhusu aondoke kurudi Kambini.
Baada ya dereva kuondoka, vijana wale wakabaki wakijadiliana jambo fulani harakaharaka, halafu wakapanda ile boti iliyowavusha hadi nga,ambo ya pili ya mto na kushuka. Boti ikarudi ilipotokea ikiendeshwa na walinzi. Vijana wale wakaanza kutembea kwa mwendo wa kasi kuelekea sehemu waliyoelekezwa, huku wakishindana na lile giza la usiku. Baada ya kutembea umbali wa kilometa tatu wakaifikia barabara kuu ya lami iliyopita katikati ya mabonde na milima, ambapo waliahidiwa kulikuta lile gari likiwasubiri wao.
Kazi nzito!
Katikati ya kiza kizito, gari moja, lori, aina ya Mitsubishi Fuso, lilikuwa limesimamishwa kando ya barabara, kama vile lilikuwa limeharibika. Kwa muda ule lilikuwa limefunikwa turubai nyuma, wakati dereva na utingo wake wakiwa wamejifungia ndani sehemu ya mbele. Hakika sehemu ile ilitisha sana hasa ukizingatia usalama wake ulikuwa mdogo, kutokana na majambazi waliokuwa wakiteka magari yaliyokuwa yanasafiri katika barabara ile, na kupora chochote walichoona kinawafaa. Wengi wa majambazi yale, ni wakimbizi waliowahi kuwa wanajeshi nchini mwao.
Hata hivyo dereva wa gari lile aliyeitwa Antoni Mjivumi, hakuwa na wasiwasi wowote baada ya kuhakikishiwa usalama wake na Paul Rugoye, aliyemkodi kwa gharama kubwa sana . Na ni kwa ajili ya kuwabeba vijana wale, Jean , France na Pierre, kwa siri kuwasafirisha hadi jijini Mwanza, kukwepa wasiweze kushtukiwa katika mipango yao waliyopanga.
Wakiwa ndani ya gari, dereva Antoni Mjivumi, na utingo wake, Cosmas Kishoka, waliweza kusikia vishindo vya miguu ya watu waliokuwa wanatembea kama wanalijongelea gari lao. Kwa vile sehemu yote ilikuwa kimya kabisa, sauti iliweza kusikia, hata ya wadudu wadogo waliokuwa wakilia kule porini. Utingo Cosmas akanyanyua kichwa chake na kuangalia kule nje kulipokuwa na kiza kizito, halafu akamwambia dereva:
“Haloo, Mjivumi eee!”
“Eee…unasemaje Cosmas?”
“Nasikia mchakacho huko nje, kama vile watu wanatembea…”
“Labda ni wale watu tulioambiwa kuwa tuwasubiri!” Dereva akasema huku naye akinyanyua kichwa chake.
“Naona kuna watu watatu…” Cosmas akasema baada ya kuwaona wale watu watatu, Jean , France na Pierre.
“Basi ndiyo wenyewe…”
Baada ya sekunde kadhaa watu wale wakalifikia gari na kusimama. Dereva akaufungua mlango na kuwaangalia watu wale waliokuwa wamevalia makoti makubwa yaliyofanya watishe katika kiza kile!
“Usalama uko?” Dereva akauliza.
“Hakuna shaka, usalama upo!” Jean akasema huku akiwasha tochi yake kubwa.
“Karibuni jamani…”
“Ahsante sana …hamjambo?”
“Sisi hatujambo.”
“Tumeelekezwa kuwa tutaukuta usafiri wa gari hapa.”
“Hamkukosea…ndiyo hapa…” Anton Mjivumi akasema na kuendelea. “Na ndiyo tunawasubiri, hivyo pandeni garini!”
Utingo Cosmas akawafungulia mlango wa upande wake, nao wakaingia ndani ya gari lile, sehemu ya nyuma ambapo palikuwa na uwazi mkubwa wa kuweza kukaa watu wale. Kwa kawaida magari mengi ya safari huwa yana sehemu ya ziada, ambayo huwa na kitanda cha kupumzikia, au hata kulala. Basi sehemu hiyo ndiyo waliyotumia vijana wale hatari kujichimbia kwa ustadi mkubwa pamoja na mizigo yao . Pia, walikuwa wamefunikwa na pazia zito, kiasi kwamba siyo rahisi kwa mtu kugundua palikuwa na watu waliojificha zaidi ya utingo na dereva.
Kusema kweli dereva yule, Anton Mjivumi, hakujua lolote kuhusu watu wale’ kama walikuwa hatari. Baada ya kupanda garini, akalitia moto na kuliondoa kwa mwendo wa kawaida na wote wakiwa kimya kabisa, hakuna aliyezungumza na mwenzake. Lakini kwa upande wa utingo Cosmas hakuwa na amani na watu wale waliojificha baada ya kupanda ndani ya gari lile? Hata hivyo hakusema kitu hadi walipofika katika kitongoji cha Benaco, penye njia panda ya kwenda Karagwe na Mtukula. Wakati huo ilikuwa imeshatimu saa 12 za alfajiri, kukiwa kumeshapambazuka.
Dereva akalipaki gari wakajipatia kifungua kinywa na walipomaliza wakaendelea na safari yao kuifuata barabara inayoelekea maeneo ya Nyakaura, Runzewe, Biharamulo na Kahama. Kwa bahati nzuri hawakukutana na kizuizi chochote hadi walipofika Biharamulo, ambapo kwa muda wote Cosmas alikuwa na wasiwasi na watu wale waliokuwa wanaongea lugha ya Kinyarwanda na kifaransa! Na mara nyingi wakiliongelea jiji la Arusha, na pia kuwa na kipeperushi kilichokuwa na ramani ya jiji hilo .
Baada ya kutoka Biharamulo, wakaendelea na safari kuelekea Mwanza. Vijana, Jean, Pierre na France wakawa wanawasiliana kwa simu zao za mkononi na Bw. Paul Rugoye, aliyekuwa jijini Mwanza, kuwapokea. Hakika yote yalizidi kumchanganya utingo Cosmas! Akayaweka rohoni! Lakini akipanga kuwa ni lazima aje kuyalipua baadaye itakapobidi.
Dereva akaendelea kuendesha gari huku akipangua gea moja baada ya nyingine. Hakuwa na mawazo mengine zaidi ya kuwazia safari yake afike salama akiwa na wale watu alioambiwa awachukue, na mara nyingine alikuwa akivuta sigara na kupulizia moshi nje ya dirisha.
ITAENDELEA
Msaliti Asakwe Sehemu ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;