Mtambo Wa Mauti Sehemu ya Pili
KIJASUSI

Ep 02: Mtambo Wa Mauti

SIMULIZI Mtambo Wa Mauti
Mtambo Wa Mauti Sehemu ya Pili

Simulizi: Mtambo Wa Mauti

Mwandishi: BEN R. MTOBWA

Sehemu Ya Pili (2)

Maradhi hayo yanaweza kumfanya mtu kuwa na nafsi mbili au tatu zenye majina na tabia tofauti. Anaweza kuwa Amina, Asha au Aisha kivitendo na kitabia kwa nyakati tofauti. Wakati mwingine Amina au Asha huyo anaweza kuchukiana au hata kuoneana wivu na Aisha, kwa kutegemea wakati huo mgonjwa yuko katika taswira ipi.

Zipo kesi kadhaa za aina hiyo, baadhi zikihusisha hata mauaji, lakini watuhumiwa wakaachiwa huru na mahakama baada ya kuthibitisha kuwa wanaugua ugonjwa huo.

Joram aliamini kuwa Mona Lisa alikuwa na tatizo hilo. Aliamini kuwa alipomfuata jana na kunywa, ambako anaapa kuwa hajawahi kunywa maishani, alikuwa katika taswira yake mpya ambayo yeye binafsi haifahamu, taswira ya msichana wa kileo, sister doo, asiye na haya na mwingi wa mbwembwe. Ni hilo lililomfanya aamue kumfariji na hata pale Mona Lisa alipoomba kuondoka Joram alikataa katakata kwa maelezo

kuwa asingemruhusu kuondoka katika hali hiyo.

“Joram, mara hii naona unafanya jambo ambalo hujui hatma yake. Laiti ungenisikiliza…” Mona alimtahadharisha.

“Najua… Usijali…”

Wakiwa katika hali hiyohiyo ndipo usingizi ulipowapitia. Na ndipo Joram Kiango alipozinduka alfajiri na kujikuta akiwa

amekumbatia maiti ya aliyekuwa Mona Lisa huku tundu la risasi katika kifua chake likiendelea kuvuja damu.

Ndivyo ilivyokuwa.

W 4 X

ATIKA nchi hii iliyokumbwa ghafla na ubepari wa kutisha, kwa kisingizio cha ‘utandawazi’; katika nchi ambayo rushwa imekuwa maarufu kama dini, kiasi

cha kuwafanya wachache mamia yao waendelee kuneemeka huku wengi kwa mamilioni yao wazidi kudidimia katika lindi la ufukara, njaa na kukata tamaa; katika nchi ambayo serikali yenyewe haioni soo kumpa mtumishi wake mshahara wa shilingi 40,000 kwa mwezi huku ikijua fika kuwa maafisa wake wa ngazi za kati peke yake fedha hizo haziwatoshi hata kwa kutwa moja; vifo vya hapa na pale vimeondokea kuwa jambo la kawaida kabisa.

Redio, televisheni na magazeti siku zote yamekuwa yakitoa habari ambazo zamani kidogo zingeonekana kuwa za ajabu machoni mwa watu: Ajinyonga kwa deni la shilingi elfu tano; Mama amuua mwanae kwa kumuibia shilingi mia mbili; Mpiga debe amuua mwenzake kwa kugombea senti hamsini; Kibaka achomwa moto hadi kufa kwa kukwapua simu ya mkononi; na kadhalika na kadhalika.

Kama Mtanzania mwingine yeyote, Inspekta Haroub Kambambaya, alikuwa akizisikia, au kuzisoma habari hizo siku zote na kuishia kujiuliza maswali yaleyale ambayo kila mmoja alijiuliza, “Tunaelekea wapi?” au “Hatma ya nchi hii ni ipi kwa kasi hii ya maisha?”

Lakini Haroub Kambambaya hakuwa Mtanzania wa kawaida. Alikuwa afisa mzito, katika kitengo kizito, chenye dhamana maalumu katika masuala ya Usalama wa Taifa. Awali, kitengo hicho kiliongozwa na Inspekta Kombora ambaye sasa amestaafu na kuanzisha shughuli za kilimo katika wilaya moja ya mkoa wa Tanga. Huu ulikuwa mwaka wa pili toka Kambambaya alipoteuliwa kukikalia kiti hicho, ambacho awali hakujua kuwa kilikuwa ‘kiti cha moto’ kiasi hicho, kiti ambacho kilihusiana na kudokezwa juu ya kila tukio nyeti linalotokea nchini, ambalo kwa namna moja au nyingine linahusiana na Usalama wa Taifa. Macho yake yalitakiwa kuuona kila mkataba nyeti wa kibiashara baina ya mtu na mtu, mtu na asasi au serikali kwa serikali. Dawati lake lilitakiwa kupokea taarifa zote za nani anatoka na nani anaingia nchini kulingana na uzito wa majina au nafasi zao. Kuingia na kutoka kwa idadi kubwa ya pesa katika mabenki nchini, pia ni miongoni mwa mambo ambayo yalitakiwa kuifikia meza yake kwa ajili ya tathmini. Si hayo tu, hata mambo ambayo yalionekana ya kawaida, kama masuala ya kujiua, kuua, kutoweka au hata kutishia kujiua yalipitishwa mbele ya macho yake; mengi yakiwa yale ambayo hayakupata kuyafikia masikio ya wanahabari.

Ni mengi yaliyomfikia, mengi kati ya mengi hayo yalikuwa ya kusisimua. Lakini ni machache sana yaliyohitaji kufanyiwa kazi. Aidha, kati ya machache hayo, mengi yalirejeshwa mikononi mwa asasi za kawaida, ama polisi, au Usalama wa Taifa.

Ni katika mlolongo huo, Kambambaya alipolipokea jalada jipya lenye tuhuma dhidi ya Joram Kiango ‘kuua’ mtu na kisha kutoweka.

Kambambaya hakuwa mgeni wa jina la Joram Kiango. Alilisikia mara nyingi likitajwa katika mifereji na vichochoro vya ugaidi, ujambazi au uhaini. Hali kadhalika, alikuwa amesoma majarida na vitabu vingi vilivyochapishwa juu ya harakati za mtu huyo anayeitwa au kujiita Joram Kiango.

Alipitia jalada hilo harakaharaka kabla ya kuinua uso wake kumtazama msaidizi wake aliyeketi mbele yake akimsubiri.

“Kwa nini limeletwa hapa?” alimuuliza baadaye.

“Linaonekana kama tukio la kawaida kabisa la mauaji. Polisi yeyote aliyehitimu hatashindwa kujua aanzie wapi, aishie wapi katika kesi kama hii.”

“Ni kweli kabisa afande,” kijana huyo mkakamavu, mtanashati, anayeitwa Chaku Chikaya, alimjibu akitabasamu kidogo. “Lakini,” aliongeza. “Nadhani wameleta jalada hili hapa harakaharaka kwa kuwa wanafahamu jinsi ambavyo ofisi hii imekuwa ikishirikiana na Joram Kiango kwa njia moja au nyingine katika pilikapilika zake.

“Kushirikiana!” Kambambaya alimuuliza. “Kushirikiana, Sajenti!” alihoji tena. “Hapa tuna msichana asiye na hatia aliyeuawa kinyama. Hapahapa tunaye mtuhumiwa ambaye kutoweka kwake ni ushahidi wa kwanza wa kuwa kwake na hatia. Alama za vidole kwenye mwili wa marehemu na sehemu mbalimbali chumbani humo ni zake. Isitoshe ni yeye aliyekodi chumba hicho kwa jina lake na amekiacha bila kutoa taarifa yoyote mapokezi. Wewe, afisa hali kama hiyo unaichukulia kuwa ni ushirikiano?”

Sajini Chikaya alitamani kutabasamu. Alisita kwa jinsi alivyoyaona macho ya bosi wake yalivyokuwa hayana mzaha, jambo ambalo lilimfanya ashangae badala ya kucheka. Chikaya amekuwa na kikosi hiki kwa zaidi ya miaka kumi. Katika kipindi chote hicho amekuwa akishuhudia au kuhusika kwa namna moja au nyingine na harakati za Joram Kiango, harakati ambazo huanza kwa kumfanya Joram aonekane kama mhalifu na kuishia katika hali ya kumfanya aonekane shujaa wa Taifa. Kwa ufupi, Chikaya alikuwa mshabiki wa Joram Kiango.

Kitu ambacho hakufahamu ni kuwa bosi wake hakuwa mshabiki wa Joram Kiango. Kinyume na Mkuu wa Idara hii zamani, mzee Kombora, Kambambaya alimchukia Joram Kiango. Ni kweli, alihusudu mtindo wake wa kupambana na majanga mazito, ambayo yangeweza kuhatarisha usalama wa nchi na bara zima kwa namna anazojua mwenyewe. Hata hivyo, namna zake hizo, ambazo siku zote ziliishia kuvifanya vyombo vyote vya usalama vilivyofundishwa na kuhitimu, vionekane mbumbumbu visivyojua kazi zao, ndilo lililomfanya Kambambaya ajikute akijenga chuki dhidi ya Joram Kiango.

Siku zote alikuwa akiomba itokee siku, Joram ateleze na aangukie mikononi mwake ili amfunze adabu na baadaye kumpeleka chuoni. Aliiona siku hiyo kama inayokaribia.

“Sikiliza Sajini. Ushirikiano au ushoga katika suala hili ni ndoto. Hapa tunazungumzia kifo cha mtu. Tunazungumzia mtuhumiwa ambaye anafahamika, ambaye anaweza kuua tena. Ni wajibu wetu kushirikiana na polisi, kwa hali na mali ili tumpate. Mengine yatafuata baadaye.” Alisita kidogo kuitazama saa yake. Kisha, akauinua tena uso wake kumkazia macho Chikaya kabla ya kumuuliza, “Unadhani anaweza kuwa amejichimbia wapi?”

***

Supa D na maiti alikuwa kama bata na maji. Maiti zilikuwa sehemu ya maisha yake. Hakuna siku iendayo kwa Mungu ambayo hakupata kuhusika na maiti, kwa njia moja au nyingine. Mwaka wa kumi na sita sasa toka alipoingia katika kazi hii ambayo si kwamba ilimlazimisha tu bali pia ilimfanya aichukulie miili ya binadamu wenzake, ambao tayari uhai ulikuwa umewatoka, kwao awe kama fundi mwashi anayelichukulia tofali.

Supa D alikuwa mtendaji mkubwa wa chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, ajira ambayo awali aliichukulia kama kupelekwa jehanamu, lakini sasa aliiona kama pepo.

Kama ilivyo kwa maelfu ya watu wengine, Supa D alizaliwa kijiji fulani huko wilaya ya Mpwapwa. Aliona milango ya neema isingemfungukia bila kuja Dar es Salaam, kwani wote waliomtangulia toka kijijini hapo na kupotelea Dar es Saam walirudi miaka kadhaa wakiwa wamebadilika kiuchumi. Wanawake walinona na kupendeza, wanaume walinawiri na kuvutia. Ni hawa waliovaa vizuri, kula vizuri na kuwajengea wazazi wao nyumba nzuri. Ni wao waliowachukua wadogo zao na kuwapeleka mjini ambako walipata elimu nzuri.

Supa D alikuwa mtoto mkubwa katika familia yenye watoto tisa, akiwa mwanaume pekee. Akiwa amemaliza darasa la nne, ambalo wakati huo lilikuwa la juu zaidi katika elimu ya msingi, alijichukulia kama msomi aliyekosa kazi. Hivyo,

alifanya kila jitihada hadi alipopata nauli ambayo ilimfikisha

Dar es Salaam.

Kama kawaida, jiji la Dar es Salaam lilimpokea kwa kila aina ya dhiki na dhihaka. Hakuwa na ndugu, hakuwa na mahala pa kulala. Kwa zaidi ya wiki mbili alilala katika vituo vya mabasi, katika magofu na mara nyingine shimoni Kariakoo. Kutokana na idadi kubwa ya watu jijini Supa D hakupata kuulizwa na mtu yeyote ‘Wewe ni nani’, ‘Unafanya nini hapa’ au ‘Kwenu wapi.’ Hata kufungwa yeye alisikia juujuu tu.

Nyota yake ya jaa ilianza kufunguka asubuhi ile alipokutana na kijana mmoja wa kijijini kwao ambaye alikuwa ametoroka nyumbani kwao miezi kadhaa kabla yake.

“Uko huku?” “Wewe pia?” “Ulikuja lini?” “Wewe ulikuja lini?” “Unakaa wapi?”

Baada ya kipindi cha maswali na majibu mwenyeji alijitolea kumpeleka Supa D kwa mwajiri wake kwa ahadi ya kumpatia ajira na mahala pa kulala.

Mwajiri wake aliondokea kuwa mama mmoja mnene, wa Kimanyema, aliyekuwa na nyumba katika mtaa mmoja Mchikichini, Kariakoo. Alikuwa mwajiri wa vijana wengine wasiopungua kumi. Kazi yao ilikuwa kumuuzia kahawa, toka asubuhi hadi usiku wa manane, katika mitaa yote ya Kariakoo, ujira ukiwa chakula, mahala pa kulala na senti chache zilizotokana na faida iliyopatikana. Malazi yenyewe hayakuwa na gharama yoyote kwa mama huyo. Wote walilala uwani, ambako kila mmoja alitandika ama gunia au kirago sakafuni na kuubembeleza usingizi. Kunguni, mbu na viroboto pia walikuwa wapangaji wa nyumba hiyo na kwa ajili ya ugeni wake, walimlaki Supa D juujuu.

Kwa Supa D, ambaye wakati huo bado alikuwa akiitwa Charles Matonya, hiyo ilikuwa hatua kubwa katika maisha yake. Alifanya kazi ya mama huyo kwa moyo wake wote na juhudi zake zote, hali iliyofanya aondokee kuwa kipenzi cha mama. Lakini alikuwa pia kipenzi cha takribani wateja wake wote. Kila aliyeionja kahawa yake aliondokea kuwa mteja

wake wa kudumu. Uchamgamfu wake na ari yake ya kujifunza zaidi na zaidi kwa wateja hao vikamfanya awe zaidi ya ‘kijana muuza kahawa.’

Ni katika mlolongo huo mzee mmoja aliyekuwa akifanya kazi ya uhasibu hapo Muhimbili alimdokeza kuwa zilikuwepo nafasi nzuri za utunzaji wa usafi katika wodi ya wagonjwa. Matonya hakusita kuandika barua ya maombi. Na aliposhauriwa ‘kuongeza’ uzito wa barua yake kwa kutoa ‘kitu kidogo,’ hakushindwa kutokana na akiba ndogo aliyokuwa amejiwekea.

Wiki chache baadaye akawa mtumishi wa wakati huo lililokuwa likiitwa Shirika la Afya Muhimbili.

Kama ilivyo ada, enzi hizo kupata kazi Dar es Salaam ilikuwa rahisi kuliko kupata chumba cha kuishi. Supa D alihangaika kwa takribani mwaka mmoja, akichangia chumba na marafiki hadi alipobahatika kupata chumba huko Magomeni Mikumi, mitaa ya bondeni.

Aliendelea kuwa mchapakazi mzuri. Hata yule bosi mkorofi

kiasi gani hakuwahi kupata kigezo cha kumshutumu Supa

D. Aliwahi kuliko mtunza ufunguo, alichelewa kutoka hadi mtunza ufunguo alipomfukuza. Mara mbili aliwahi kufungiwa stoo akifanya usafi, kumbe muda wa kazi umekwisha! Hali kadhalika, alikuwa akijisomea, pamoja na kuzingatia mafunzo ya kazini na, hivyo, kujikuta akipanda ngazi kidogokidogo.

Ikaja siku ambayo alipokea barua ya uhamisho wa kuwa msaidizi wa mtunzaji chumba cha maiti, kazi ngumu iliyoambatana na nyongeza kwenye mshahara wake.

Kati ya yote aliyotarajia maishani, Supa D, au Matonya, hakupata kufikiria kuwa angeweza kufanya kazi katika chumba cha maiti. Alisoma barua ile mara mbilimbili huku akitafakari la kufanya. Kwa mara ya kwanza alifikiria kuacha kazi. Lakini kwa kuwa hakujua angeweza kupata wapi kazi nyingine, aidha kwa jinsi hisia zake zilivyomtuma kuwa kuacha kazi itakuwa sawa na kushindwa kazi akaamua kufanya; kwani si inafanywa miaka yote na wanaume kama yeye? Alijifariji.

Lakini pamoja na kujifariji huko bado alichokutana nacho chumbani humo hakukitegemea. Siku ya kwanza tu ya ajira

yake alilazimika kupokea maiti tatu za watu waliokufa kwa ajali. Walikuwa wanatisha kwa jinsi walivyoharibika na kutapakaa damu. Mmoja alikuwa amepasuka kichwa na, hivyo, kuufanya ubongo wake ambao ulichanganyika na damu kuzagaa mwilini mwake kama uji. Mmoja alikatika kabisa miguu yote miwili na kuwa kipande tu cha mtu. Mwingine hakuwa na jeraha lolote mwilini lakini kwa jinsi alivyotoa macho na kuacha kinywa wazi kama anayezomea, alitisha kuliko wenzake.

Ilikuwa ni wajibu wa Matonya kuwaosha, kuwarekebisha kwa kurudishia kichwa cha yule aliyepasuka, kumfumba mdomo na macho yule aliyeuacha wazi na kumtengeneza yule aliyekatika miguu, tayari kwa kuhifadhiwa katika majokofu ili ndugu zao watakapokuja wawakute katika hali inayotazamika. Pamoja na ujabali wake wote Matonya alishindwa kuifanya kazi hiyo. Alitetemeka mwili mzima, alitapika zaidi ya mara tatu na kujikuta akiweweseka ovyo. Wenzake waliokwishaizowea hali hiyo walicheka sana na kuendelea na kazi yao. Mmoja hata alikuwa akinywa chai huku kikombe kakiweka juu ya

maiti mmojawapo.

Jioni hiyo Matonya aliporudi nyumbani alishindwa kabisa kula. Usiku pia alishindwa kulala. Kila alipotaka kulala alimwona yule maiti aliyetoa macho akimkodolea huku wale wengine wakiwa kando. Hadi saa sita za usiku alikuwa hajapata hata lepe la usingizi. Ndipo lilipomjia wazo. Akakurupuka toka kitandani, akavaa na kuiendea baa moja ya jirani ambayo ilikuwa haijafungwa. Kwa mara ya kwanza maishani mwake akatoa hela yake na kununua bia. Kwa mara ya kwanza akanywa pombe. Akalewa. Alipokwenda kulala alipata usingizi.

Kwa mbali, moyoni mwake, ile hofu juu ya maiti ilikuwa palepale. Hata hivyo aliifukuza hofu iyo kwa kujizamisha katika mitungi ya pombe kali na kuogelea katika mabwawa ya bia. Kila alipokuja kazini alikuwa tayari amelewa na alipotoka kituo chake cha kwanza kilikuwa baa. Ulevi ambao uliambatana na ukarimu na hivyo kumfanya azidi kuwa maarufu mtaani.

Taratibu, hatimaye Supa D alijikuta amekizowea chumba cha maiti hadi nazo zikamzowea. Kupitia mapenzi yake kwa kazi yake alijikuta amezipenda maiti. Alizishika, hata baadhi

alizikumbatia. Si hilo tu, alianza hata kuzungumza na baadhi ya marehemu. Wako ambao alicheka nao na hata kuna wale ambao aliteta nao.

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa jina lake la Charles Matonya kutoweka na lile la Supa D kuchukua nafasi yake. Ni watu wachache sana waliokijua kirefu cha jina la Supa D kuwa lilimaanisha Super Drunker, kwa maana ya ‘Mlevi’ mashuhuri. Kiuchumi haikuwa ajira mbaya hata kidogo. Kwa jinsi binadamu wengi wanavyowaogopa wenzao mara uhai unapowatoka, kila mara alikuwa na fedha za ziada toka kwa ndugu, jamaa na marafiki waliohitaji msaada wa ziada wa kuandaliwa maiti wao. Wale bahili aliwatia hofu kwa kuwaonyesha maiti mbalimbali za kutisha kwa kisingizio cha

kumtafuta mtu wao hadi walipotokwa na ‘kitu kidogo.’

Siku hizi ambazo binadamu walikuwa wakiteketea kama nzige kutokana na maradhi mbalimbali, yakiongozwa na UKIMWI, wateja walikuwa wengi sana kwa Supa D. walitoka na kuingia, kila mmoja akitaka huduma ya haraka. Hivyo, senti za matumizi hazikuwahi kumpiga chenga.

Si hivyo tu, senti nyingine zilimjia kwa njia ambazo hakutegemea. Wako wateja waliomfuata kwa minajili ya kununua viungo mbalimbali vya maiti. Wako waliotaka sehemu za siri, wako waliotaka ubongo, wako waliotaka hata maiti nzima ya mtoto mchanga. Yote haya Supa D aliyatekeleza kwa hila sana, hasa kwa kutumia miili ya marehemu wa ajali na wale ambao hawakuwa na wenyewe.

Fedha ziliendelea kumiminika. Kinywaji kikaendelea kutiririka katika koo lake.

Lakini kila siku si Jumapili. Ziko siku ambazo wateja waliadimika bila sababu za msingi. Siku hizo Supa D alitumia mbinu za ziada kuhakikisha mfuko wake unajaa. Kwa mfano, iko siku… Supa D aliwahi kuwachekesha watu baa, wakati akimwaga ofa za bia. Baada ya muda aliuliza ghafla, “Mnadhani fedha hii ninayoinywa nimeipata wapi?” hakuna aliyejibu. “Hii ya leo nimeitolea jasho,” aliongeza. Kwamba jioni hiyo alikuwa hana pesa za kunywea. Na ‘wateja’ walikuwa adimu. Zilipofika dakika za majeruhi ndipo alitokea Mpemba mmoja bahili aliyetaka kumshughulikia marehemu ndugu yake ili

amsafirishe. “Nilijitahidi kumshawishi anipe angalao shilingi elfu thelathini ili aniachie kazi ya kumwandaa marehemu, alikataa katakata na kushikilia kuifanya mwenyewe. Nikamwachia na kukaa pembeni nikichora mbinu. Ikatokea wakati fulani nilimwona kageuka upande. Kwa hila, bila yeye kujua niliinua mkono wa marehemu na kuutumia kumpiga kofi la kisogo ambalo lilimshtua sana. Alipogeuka aliuona mkono wa marehemu ukianguka kurudia sehemu yake ya kawaida, huku mimi nikijifanya sikuuona. Pamoja na ubahili wake mpemba huyo alinipa zile elfu thelathini harakaharaka na kuniomba kuifanya kazi ile aliyoikatalia awali. Moyoni mwake aliamini kabisa kuwa amepigwa na marehemu kwa ajili ya ubahili.”

Huyo ndiye Supa D, Supa D ambaye jioni ya leo alikuwa akiushughulikia mwili wa msichana ambaye katika uhai wake alijulikana kama Mona Lisa.

Toka awali kabisa Supa D alibaini kuwa ama marehemu hakuwa mtu wa kawaida ama kifo chake hakikuwa cha kawaida. Maiti ilikuwa imeletwa hapo hospitalini toka saa tano na robo asubuhi hiyo, ikiwa imepakiwa katika gari la wagonjwa lililosheheni pia takribani polisi wanane, watatu kati yao wakiwa na mavazi ya kiraia. Mwili wa marehemu ulipelekwa chumba maalumu cha uchunguzi ambako daktari wa zamu alikaa nao zaidi ya saa nne. Alipomaliza kuufanyia uchunguzi na kuandika taarifa ya uchunguzi wake ambao aliwapa polisi nakala ndipo alipokabidhiwa Supa D kwa matayarisho zaidi na hifadhi.

Mara tu alipomfunua marehemu na kukutana na sura yake Supa D alipata hisia kuwa marehemu hakuwa mtu wa kawaida. Pamoja na kupokea maiti wa aina mbalimbali, wakiwemo wabaya na wazuri wa sura, Supa D hakupata kukutana na maiti ya mrembo kama huyu. Huyu alikuwa mzuri kuliko wazuri wote waliowahi kupita chumbani humo. Tazama sura yake inavyovutia! Tazama anavyotabasamu, hata baada ya roho yake kutoweka!

Kwa mara ya kwanza Supa D alijikuta amesahau lipi la kufanya kwa maiti huyo. Badala yake, kwa takribani dakika tano nzima, alikuwa bado kamkodolea macho; bado haamini

kama anatazama maiti au binadamu hai, kama anamtazama binadamu au malaika.

Baadaye aliukumbuka wajibu wake. Akauinua mwili huo na kuulaza juu ya meza maalumu. Akauvua nguo na kuuacha kama ulivyozaliwa. Pigo lingine likakipasua kichwa cha Supa

D. Haukuwa mwili wa kawaida! Kilikuwa kipande cha sanaa, iliyochorwa, ikachongwa na kisha kupuliziwa uhai! Uhai ambao sasa ulitoweka kutokana na jeraha kubwa la risasi ambayo ilikitoboa kifua hicho kizuri!

Zaidi ya pombe na pesa Supa D hakupata kupenda kitu chochote kingine, wanawake ikiwa sehemu ya vitu hivyo. Ndiyo, alipata kutamani, walio hai na maiti. Lakini ilikuwa kutamani tu. Huyu alimpenda! Alitamani afufuke, amwambie jinsi alivyompenda.

“Mpenzi, yeyote aliyekuua ni mnyama, mnyama aliyelaaniwa,” alijikuta akizungumza naye. “Ni mtu ambaye hafai kuishi. Wewe sio mtu wa kufa hata kidogo.” Alitulia kidogo akimwangalia. “Lakini mpenzi,” aliendelea. “Ilikuwaje hadi Mungu akakupendelea kimaumbile kiasi hiki? Unajua kuwa ni binadamu wachache sana wanaoukaribia uzuri wako?” Halafu akatulia tena kabla ya kuongeza, “Halafu mpenzi, nimeshakwambia kuwa nakupenda? Naomba ufahamu hivyo, tafadhali.”

Wakati Supa D akizungumza hayo alikuwa akiendelea na kazi yake. Mikono yake ilikuwa ikitambaa na kuteleza juu ya mwili huo mzuri kuusafisha, huku akifarijika vilivyo na mguso huo. Alifanya kazi kwa uangalifu mkubwa na mapenzi makubwa huku akiendelea kumnong’oneza marehemu hili na lile. Aliosha masikio, macho, pua na shingo. Alisafisha damu ambayo ilianza kuganda kwenye kifua chake na kuliosha vizuri tundu la risasi, ambalo baadaye aliliziba kwa pamba. Aliuacha mkono wake uteleze juu ya tumbo hilo laini na kuishia katikati ya miguu yake. Hapo mkono wake ulitulia kwa muda na kuviachia kazi vidole vyake. “Samahani,” alimnong’oneza. “Si unajua kuwa nakupenda?” Kisha alitabasamu ghafla. “Wewe ni bikira!” alisema. “Nilijua wewe ni bikira. Nilijua kuwa usingemruhusu mwanaume yeyote mwingine zaidi yangu. Nilijua…”

Ghafla, Supa D alipata hisia kuwa alikuwa anatazamwa. Akageuka. Watu wawili walikuwa wamesimama nyuma yake, kimya kama vivuli, wakimtazama. Walikuwa wanaume warefu, waliovaa suti nyeusi na miwani ya jua. Kwa kiasi fulani walimtisha Supa D, hasa kwa kutojua waliingia chumbani humo muda upi na waliingia vipi. Kama anakumbuka vizuri alikuwa amejifungia kwa ndani kabla hajaanza kazi ya kumwandaa marehemu.

Supa D akasimama na kuwakodolea macho ya hofu na aibu yanayouliza bila kutoa sauti “Sijui niwasaidie nini?”

“Endelea na kazi yako,” Mmojawao alijibu baada ya kusoma maswali katika macho ya Supa D. “Huyo mrembo si mtu wa kukaa chumba cha maiti. Wala si mtu wa kukaa kaburini. Muda mfupi baadaye atafufuka na kupaa angani. Endelea kumwandaa.”

Supa D aliduwaa. “Nyie ni nani na mmeingiaje humu?”

W 5 X

WA Insepkta Haroub Kambambaya alfajiri hiyo ilikuwa mbaya, ya kutisha na inayosikitisha kuliko alfajiri nyingine zote alizowahi kuishi katika uhai wake. Labda angeweza kuifananisha alfajiri hii na ile ya miaka kumi na sita iliyopita, wakati huo akiwa mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya Mzumbe, mkoani Dodoma. Alikuwa katika likizo fupi, akijiandaa kwa mtihani wake wa mwisho, likizo ambayo aliitumia kukaa na mama yake mzee katika kimojawapo cha vijiji vya Shinyanga. Akiwa mtoto wa mwisho, asiye na ndugu, baada ya dada zake wawili na kaka zake wanne kufa kwa maradhi mbalimbali utotoni, baba yake pia akiwa marehemu tangu yeye anatambaa; mama yake, binti Kaundime, alikuwa kila kitu kwake. Alikuwa bibi, babu, mama, kaka, dada na zaidi ya yote rafiki. Waliishi kwa mapenzi makubwa na kuridhika kwa chochote walichokipata kutokana na jasho la

mama huyu katika kijishamba chake cha mahindi.

Binti Kaundime alijinyima kila kitu na kujidhiki kwa kila hali ili kumpatia mwanae huyo wa pekee elimu. Kwa upande wake, Haroub hakuwa kipofu wa hali hiyo. Alifanya kila jitihada katika masomo yake ili apate elimu ya kutosha, ambayo ingempelekea kupata mshahara wa kutosha, ili aweze kuchukua jukumu la kumlea mama huyu.

Hivyo, alfajiri ile, wakati akiwa na hakika kuwa safari

ya kutafuta uhakika wa maisha ilikuwa inafikia ukingoni, aligutushwa toka usingizini na kelele za watu walioizingira nyumba yao. Baadhi walikuwa wakiimba nyimbo za kuwalaani wanga, baadhi wakitukana kwa sauti huku wengine wakipiga milango na madirisha yao kwa miguu, mawe na magongo. “Toka nje mchawi wewe. Toka upesi, zako zimefika leo,” mtu mmoja alisikika akisema.

Kwanza Haroub hakuelewa kinachoendelea. Alipotoka chumbani kwake na kumfuata mama yake kwake alimkuta amejiinamia akilia kwa kwikwi.

“Kuna nini mama?” aliuliza.

Mama yake alipomtazama alizidi kulia. Akainuka na kumkumbatia mwanae huku akisema kwa sauti ya dhiki, “kwa heri mwanangu. Nimekulea, nilitegemea unilee. Shetani ametushinda nguvu. Kwa heri ya kuonana.”

“Kwani kuna nini mama?” Haroub aliuliza.

Mama yake alimtazama kwa mshangao. “Kwani hujaelewa tu?” alimuuliza. “Hao watu wanakuja kuniua.”

Haroub hakuyaamini masikio yake. “Unasemaje?… Kwa nini?” alihoji.

“Siku zote wamekuwa wakidai kuwa mimi ni mchawi. Wanadai kuwa mimi ndiye niliyemuua baba yako na wanangu wote waliotangulia. Majuzi amefariki mtoto wa jirani yetu yetu mmoja ambaye tuliwahi kugombea mpaka wa shamba. Naamini ni yeye aliyewatuma kwa kudhani kuwa nimehisika na kifo cha mtoto wake. Haroub baba, ningekuwa mchawi kweli ningeshindwa kukuarifu wewe mwanangu?”

Kabla Haroub hajaua afanye nini, ajibu nini mlango wa mbele ulipigwa jiwe kubwa lililofanya ufunguke. Ulifuatiwa na moshi mkubwa ulioashiriwa kuwa nyumba yao tayari ilikuwa imechomwa moto. Wakati huohuo kundi kubwa la watu waliofunika nyuso zao kwa matambara liliingia ndani na kuwatenganisha yeye na mama yake. Alijaribu kupigania roho ya mama yake kwa nguvu zake zote, lakini mikono yake ilikuwa dhaifu sana mbele ya umati huo wenye mikono iliyokakamaa kwa uhalifu. Aliburuzwa nje na kutupwa chini, ambako alishuhudia mama yake kipenzi akipigwa kwa michi, mawe na magogo hata akakata roho. Alishuhudia pia mama

yake akimwagiwa mafuta ya taa na kuchomwa moto kabla ya watoa hukumu hao kuondoka zao huku wakiimba nyimbo za kujisifia.

Baada ya watu hao kuondoka ndipo majirani walipofungua milango yao na kumzoa Haroub ambaye alikuwa ameteguka mkono na kuumia mbavu kwa purukushani. Baadhi ya majirani walikimbilia polisi kutoa taarifa, taarifa ambayo haikuzaa matunda yoyote zaidi ya kuruhusu mwili wa marehemu uzikwe na ahadi ya “Upelelezi unaendelea.”

Ni tukio hilo lililomfanya Haroub Kambambaya afikie uamuzi wa; Nitakuwa polisi. Daima nitapambana na wahalifu wa aina zote na kuwatokomeza.

Alirejea shule na kufaulu vizuri masomo yake. Alijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam na kusomea shahada ya sheria. Alipohitimu alikuwa miongoni mwa wasomi wachache wa awali walioona umuhimu wa kujiunga na jeshi la polisi.

Akiwa askari shupavu, mkakamavu na mwadilifu alijikuta akipanda cheo baada ya cheo hadi majuzi alipoteuliwa kukalia kiti hiki, ambacho uteuzi wake ulifanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, cheo ambacho madaraka yake yanawiana na yale ya Kamishna Mwandamizi wa Polisi au Mkuu wa Majeshi, ingawa kinafichwa kwa pazia la uinspekta. Naam, cheo ambacho kilimfanya akalie kiti hiki “Cha moto,” ambacho alfajiri hii alianza kuuonja.

Kufuatilia kwake nyendo za Joram Kiango ili aweze kuelewa kilichotokea pale hoteli ya Comfort na kusababisha kifo cha yule msichana mrembo, Mona Lisa, Kambambaya alichukua hatua kadhaa madhubuti kwa lengo la kumtia mikononi Joram Kiango.

Akiwa kingunge wa kitengo, Kambambaya alikuwa na siri nyingi ambazo wasaidizi wake wa karibu hawakuzifahamu. Moja ya siri hizo ni ile ya kujua namba ya simu na jina la bandia ambalo Joram Kiango alikuwa akitumia katika simu zake za mkononi. Akiwa na namba mbalimbali katika makampuni AIRTEL, TIGO na VODACOM, huku akizungumza au kuandika ujumbe wa maandishi kwa namna ya mafumbo, haikuwa kazi rahisi kuzinasa simu zao. Hata hivyo, wataalamu wa sauti waliwahi kushirikishwa kuthibitisha kuwa huyo hakuwa

mwingine zaidi ya Joram Kiango.

Hivyo, lilipotokea hili, na Joram kutoweka Kambambaya aliitega mitego yake yote. Mmoja wa mitego hiyo ilifyatuka na kuinasa sauti yake pale alipotuma ujumbe wa maandishi kwenye namba fulani ambayo bila shaka iliorodheshwa kwa jina jingine la bandia. Kambambaya isingemchukua muda mrefu kumjua mtu huyo, lakini maadamu kwa sasa alichohitaji ni kumpata Joram Kiango mwenyewe, alichofanya ni kuwasiliana na kampuni ya simu iliyotumiwa ili kujua eneo ambalo ujumbe huo ulitokea.

Lilikuwa eneo la Manzese, lenye maelfu ya watu, maelfu ya majumba na maelfu ya vichochoro visivyo na mpangilio, eneo ambalo halina jina la mtaa wala namba za nyumba. Lakini hayo hayakumkatisha tamaa Kambambaya. Alitumia timu ya vijana wake sita, kuungana na polisi wa kawaida sitini, kulizingira eneo hilo usiku kucha na kumhoji kila atakayetiliwa mashaka hadi Joram Kiango atakapopatikana, operesheni ambayo aliichukulia kuwa ndogo sana na ya kawaida kabisa, hadi pale alipoamshwa usingizini na kupewa taarifa ya kuuawa kwa polisi wanne waliokuwa katika jukumu hilo.

Hakuyaamini masikio yake. “Wameuawa!” alinguruma katika simu yake ya mkononi, “Wameuawa vipi?… Nani kauawa?”

“Haijafahamika, afande. Ndio kwanza nafika katika eneo la tukio. Tuko katika vichochoro fulani, hatua kama mia moja hivi toka darajani. Inaonyesha…”

“Nakuja!” Kambambaya alisema akichupa toka kitandani. Alivaa shati na suruali ya karibu juu ya mavazi yake ya ndani, akaichukua bastola yake na kuitupia mfukoni. Dakika mbili baadaye gari lake lilikuwa likitafuna lami, toka Masaki kuelekea Manzese.

Alimkuta msaidizi wake, Chaku Chikaya, akimsubiri chini ya daraja, akiwa miongoni mwa askari wa kawaida wanne, wenye silaha. Chikaya akiwa mtu aliyekabidhiwa operesheni hii alimweleza Inspekta kwa tuo tukio zima lilivyokuwa.

“Marehemu hawa walikuwa na jukumu la kulinda vichochoro vyote vilivyotokea katika barabara kuu. Walikuwa wakitembea wawiliwawili. Inaonekana kama walioingia kwa

bahati mbaya katika mtego wa adui. Askari waliokuwa mbali kidogo ya eneo hili walisikia milio ya risasi ikilipuka ghafla tu. Walipokuja eneo la tukio walikuta miili ya wenzao ikiwa imedondoka chini. Hawakumwona mtu wala kusikia mtu akikimbia.

“Ni wazi kuwa yeyote aliyefanya mauaji haya bado yuko katika eneo hilihili. Kwa ajili hiyo nimeongeza ulinzi na kupanua wigo.” Chaku alisema.

Kambambaya alitikisa kichwa na kuunga mkono hatua hiyo, “Walisikia mlio wa bunduki aina gani?” alihoji.

“AK-47, mzee.”

AK! Kambambaya alishangaa. Ile bunduki hatari iliyogunduliwa na Mrusi, Kalashnikov, kwenye vita kuu ya pili ya dunia! Basi hii ni vita! Aliwaza.

Chikaya alimwongoza hadi mahala ilipokuwepo miili ya marehemu. Walilaliana wawiliwawili, baadhi wakiwa wameziangukia silaha zao, mmoja silaha yake ikiwa mkononi kama anayejiandaa kufyatua. Haikuhitaji utaalamu wowote kubaini kuwa kifo kiliwakuta marehemu hawa bila ya wao kutegemea. Ama walivamiwa ghafla, au waliingia katika mtego wa mauti.

Kuiona miili ya vijana hao wasio na hatia, wakiwa hawapo tena duniani, kuliamsha hasira katika nafsi ya Kambambaya. Nani aliyewaua? Kwa nini amewaua? Afanye nini kuwapata haraka wahalifu hawa ili wafikishwe mikononi mwa sheria? Alijiuliza harakaharaka, swali baada ya swali, maswali ambayo yeye binafsi hakutegemea majibu yake yawe karibu kiasi hicho, jambo lililozidi kumpandisha hasira.

Kiasi fulani hasira hizo ziliambatana na hofu, si hofu ya kujua kuwa mahala fulani, katika mtaa fulani, kuna mtu au watu hatari, wenye silaha hatari, ambao wanaweza kuwaua polisi wanne bila ya kigugumizi chochote. Ndiyo, hilo lilimtisha, lakini hofu nyingine ilikuwa juu yake binafsi. Hatua yake ya kuamua kumwinda Joram Kiango kwa nguvu nyingi kiasi hiki ilionyesha kuwashangaza na kutoungwa mkono na wasaidizi wake. Wanavyomjua Joram hawakuona kama ni mtu wa hatari kiasi hicho, wengine hawakuona umuhimu. Lakini maadamu yeye alikuwa na madaraka, alilotaka liwe, likawa.

Hivyo, sasa ilimtisha kwa kutojua atauambia nini umma wa Watanzania umwelewe; kwamba Joram Kiango alishukiwa kuua msichana hotelini! Kwamba kwa ajili hiyo alituma kikosi kikubwa cha askari kumtafuta! Kwamba katika purukushani hizo askari wanne wameuawa kinyama! Nani atamwelewa? Nani atamsikiliza?

Wakati akiwaza hayo Kambambaya alikuwa akiendelea na uchunguzi wa eneo hilo. Akiongozana na Chikaya, na askari wengine wawili, walipita uchochoro hadi uchochoro, wakiikagua nyumba baada ya nyumba. Ikiwa alfajiri ya siku ya kazi, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walianza kuamka. Walishangazwa kuona mitaa yao ikiwa ‘imevamiwa’ na polisi wenye dalili za madaraka makubwa. Kambambaya hakutaka kuwabugudhi raia kwa wakati huo. Aliwahoji wawili watatu, maswali mawili matatu, lakini wote walionekana kama wanaoulizwa, “Wewe ni mwanamume?” wakati anajiona ni mwanamume au “Wewe ni mwanamke?” wakati kila mtu anaona kuwa ni mwanamke. Kambambaya aliachana nao na kuendelea na uchunguzi wake.

Uchochoro mmoja uliwafanya watokee kwenye hospitali ya Daktari Omari. Alishangazwa na umati wa watu walioukuta umezingira hospitali hiyo, kila mmoja akiwa anatokwa na machozi ya hofu.

“Kuna nini hapa?” alihoji.

“Daktari ameuawa,” mmoja wa majirani alimjibu. “Daktari yupi?”

“Dokta Omari, mwenye hospitali hii. Wagonjwa waliokuja kupata sindano za masaa wamemkuta akiwa amelala kifudifudi, tundu kubwa likivuja damu toka kisogoni mwake.” Kambambaya hakusikiliza zaidi. Alipenya umati huo wa watu hadi ndani. Mwili wa Daktari Omari ulikuwa bado umelala sakafuni, katikati ya mlango wa kutokea ofisini kwake kuelekea wodini. Risasi iliyomuua ilikuwa imemfumua kisogo na kupotelea katika ubongo wake ilikuwa tayari imeganda na

kufanya kichwa chake kiungane na sakafu.

Kambambaya alitupia macho mezani. Majalada, vitabu, magazeti na vikorokoro vingine vya kiganga vilikuwa katika hali ya mpangilio mzuri. Viti na meza pia vilikuwa katika

utaratibu wake maalumu, hali ambayo ilimfanya apate hisia kuwa kifo kilimkuta marehemu bila purukushani yoyote.

“Mzee unaona pale?” msaidizi wake mmoja alimzindua.

Kambambaya akamtazama. Kisha akayafuata macho ya askari huyo yalikoelekea. Yalikuwa yakitazama ukuta mmoja uliokuwa na tundu dogo ambalo lisingekuwa limesababishwa na kitu kingine zaidi ya risasi. Kambambaya alitoa kisu chake na kukipenyeza ndani ya tundu hilo. Baada ya kuchokonoa kwa muda risasi kubwa ilidondoka. Akaiokota na kuitazama. Kama alivyotegemea, ilikuwa ya bastola aina ya AK.45, ambayo mara nyingi hutumiwa na maafisa wa polisi na jeshi pekee.

Risasi ukutani! Kambambaya aliwaza. Ilikuwa ya onyo au mpigaji alikosa shabaha? Kwa jinsi mwili wa marehemu ulivyokuwa, Kambambaya hakuona kama muuaji alihitaji kumtisha au kukosea shabaha!

Aliirudia meza na kuanza kupekua majalada hadi alipopata lile ambalo alikuwa akilitafuta, jalada lenye kumbukumbu ya wagonjwa wote walioingia na kutoka siku hiyo. Alilipitia jina kwa jina, akitazama aina ya maradhi yaliyowaleta, umri na taarifa nyinginezo. Wengi hawakuwa watu wa kutilia shaka. Majina yalikuwa ya kawaida, magonjwa ya kawaida. Lakini alipochukua jalada la wagonjwa waliolezwa na kukutana na mgonjwa mmoja tu mwenye jina la ajabuajabu mara moja alijikuta akisisimkwa na mwili wake:

Sheriff Mkono wa Birika! Miaka sitini na mitano! Maradhi yasiyoeleweka! Vipimo baadaye!

Kambambaya alipiga hatua za harakaharaka kukiendea chumba cha wagonjwa waliolazwa. Kama alivyotegemea alikuta chumba hicho kikiwa kitupu.

“Joram alikuwa hapa,” alinong’ona akimwelekea Chaku Chikaya. “Amelala katika chumba hiki. Tumechelewa sana. Tayari ametoweka tena.”

Chikaya hakumwelewa bosi wake. “Umesema Joram, afande? Una hakika?” alimuuliza.

“Bila shaka!” Kambambaya alimjibu. “Na kwa namna moja au nyingine anahusika na mauaji haya. Sasa umuhimu

wa kumpata ni mkubwa zaidi na wa haraka zaidi. Lazima apatikane katika saa ishirini na nne zijazo,” aliamrisha.

Wakati huo ikikaribia saa kumi na mbili za asubuhi, uwanja wa hospitali hiyo ulikwishafurika watu. Minong’ono ya hapa na pale iliendelea na, hivyo, kuzidi kuvuta watu wengine. Kambambaya alitoa maelekezo kwa wasaidizi wake, “Eneo hilo lifungwe; taratibu za kawaida, ikiwa pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na ripoti ya daktari zifuatwe.”

Kisha alilirudia gari lake ambalo lilimpeleka nyumbani kwake ambako alioga, akavaa mavazi yake rasmi, akanywa kikombe chake cha kahawa chungu, kisha akarejea ofisini kwake.

Kwa muda fulani Kambambaya aliduwaa ofisini, akiwa ameiinamia meza yake. Hakujua aanzie wapi, aishie wapi katika kulitafakari suala hili lililojaa utata, suala ambalo lilianza na kifo cha msichana mmoja tu hotelini, likafuatiwa na kutoweka kwa mtuhumiwa nambari moja na sasa tayari askari wanne na daktari mmoja ni marehemu.

Msaidizi wa ofisi yake alimletea kahawa nyingine ambayo aliinywa. Alipoingia tena alimletea jalada lililokuwa na taarifa ya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu aliyeuawa hoteli ya Comfort.

Kambambaya alikuwa na mzigo mzito kichwani mwake zaidi ya jalada hili. Alikuwa na jukumu zito la ‘kuhalalisha’ vifo vya askari wale wanne na daktari wa Manzese. Ulikuwa wajibu wake, tena wa haraka, kupata ufumbuzi au kiini cha mauaji hayo. Aidha, jukumu la kumnasa au kuwanasa wahalifu kwa kiasi kikubwa lilikuwa mabegani mwake. Kila dakika iliyopotea, kabla ya kupiga hatua yoyote katika hayo, ilimtisha zaidi. Hata hivyo, kutokana na ukweli kuwa msichana yule, ambaye hata jina lake lilikuwa halijafahamika, alikuwa wa kwanza katika mlolongo huo wa vifo, Kambambaya alijikuta hana jinsi, isipokuwa kulisoma jalada hilo kwa tuo.

Taarifa ya daktari ilikuwa na kurasa tatu zilizoandikwa kwa mtindo wa kitabibu. Juu ya ripoti hizo ziliambatanishwa picha kadhaa za marehemu zilizopigwa na polisi. Mojawapo ya picha ilimvutia Kambambaya kiasi cha kufanya aamue kuiweka chini taarifa ya maandishi na kuzikodolea macho.

Alikuwa amewasikia wasaidizi wake wakizungumza uzuri wa msichana huyo aliyeuawa. Hakuwa amefikiria kuwa alikuwa mzuri kiasi hiki! Picha hii ikiwa imeandaliwa katika hali ya kumfanya msichana huyo asionekane kuwa amekufa, marehemu alikuwa amevalishwa nguo na kuketishwa kwenye kochi, macho yakiwa yamefumbuka. Alionekana msichana mzuri sana, ambaye hakustahili kufa kifo cha kinyama kiasi kile. Picha nyingine zilipigwa kabla hajaguswa, zikionyesha alivyolala chali kitandani, tundu la risasi kifuani, kitu kama tabasamu mdomoni. Nyingine, bila shaka ilipigwa Muhimbili, ilimwonyesha akiwa mtupu kama alivyozaliwa. Isipokuwa kwa tundu la risasi lililoutia dosari mwili huo ulikuwa mwili pekee, ambao Kambambaya hakupata kufikiria kama binadamu wa kawaida angeweza kuwa nao.

Baada ya kuzitazama kwa makini picha hizo Kambambaya aliirudia taarifa ya daktari. Kwanza aliisoma harakaharaka. Baadaye aliirudia taratibu, akiitafakari kipengele baada ya kipengele.

JINA: Halijafahamika

UMRI: kati ya miaka ishirini hadi ishirini na mitatu.

JINSIA: Mwanamke.

MUDA WA KIFO: kati ya saa saba hadi saa tisa usiku.

SABABU YA KIFO: kutokwa na damu nyingi katika tundu lililotoboa moyo.

MAELEZO MENGINE: Marehemu alikuwa mtu mwenye afya nzuri kabla ya kifo chake. Isipokuwa kwa harufu ya lotion na pafyumu mwilini mwake, marehemu alikuwa msafi. Hakuwa amefanya mapenzi na mtu yeyote. Kwa ujumla, alikuwa bado bikira.

Taarifa hiyo ya mwisho ilimchanganya Kambambaya. Marehemu alikuwa bikira! Marehemu, ambaye taarifa alizonazo zinaonyesha kuwa alikuwa na mpenzi wake, Joram Kiango, wakinywa, kula na kulala zaidi ya mara moja! Haikumwingia akilini. Kama wanamtafuta Joram Kiango, kwa tuhuma za kumuua mpenzi au hawara yake, vipi hawara huyu awe safi kiasi hicho!

Kambambaya akaichukua tena picha ile ya marehemu aliyeketishwa kwenye kiti. Akaitazama kwa makini kana

kwamba alitarajia imwambie chochote. Haikumwambia. Alirejea katika jalada na kuendelea kufikiri. Mara akashikwa na hamu ya kumwona marehemu kwa macho yake mwenyewe. Akainuka na kutoka nje ya ofisi.

“Muhimbili,” alimwelekeza dereva wake wakati akiingia kwenye gari.

Dakika chachee baadaye alikuwa katika ofisi ya daktari wa uchunguzi wa maiti. “Naomba kumwona marehemu,” alisema baada ya kujitambulisha. Kambambaya alimwona daktari akibabaika kidogo kwa rai hiyo. “Vipi docta, mbona unawaza sana. Au kuna taratibu ambazo sijazifuata?”

“Hapana,” daktari alijibu.

Hakuona kama alihitaji kumwambia askari huyo tatizo lake. Ukweli ni kwamba pamoja na udaktari wake bado hakuwa mzoefu sana wa chumba cha maiti. Mara nyingi aliwategemea wahudumu wa chumba hicho, hasa Supa D ambaye alitekeleza majukumu yake kwa uhakika zaidi. Tatizo ni kwamba toka jioni jana Supa D alikuwa hajaonekana, jambo ambalo halikuwa la kawaida kwake.

“Twende,” alijikongoja daktari huyo baada ya kusitasita. Chumba cha maiti kiliwalaki kwa ile harufu isiyoelezeka,

harufu ambayo siku zote Kambambaya alishindwa kufahamu iwapo ilitokana na kuharibika kwa maiti, mchanganyiko wa madawa au yote kwa pamoja, harufu ambayo haizoeleki.

Alistahimili harufu hiyo kwa kusimama nyuma ya daktari alipovuta jokofu lililokuwa na taarifa za marehemu huyo. Mara Kambambaya alimsikia daktari huyo akitoa sauti ya mshangao, iliyofuatiwa na kutokwa na macho ya mshangao kama mtu aliyegusa waya wa umeme. Kambambaya akayafuata macho ya daktari huyo humo ndani ya jokofu. Yeye pia alipigwa na butwaa.

Badala ya msichana mrembo jokofu hilo lilikuwa na maiti ya mzee wa kiume, yenye ndevu nyingi zilizoachwa ovyoovyo. Ulimi wa marehemu huyo ulikuwa nje, shingo upande kama iliyovunjika huku damu ikiwa imeganda mdomoni, puani na masikioni.

Hatimaye, daktari alitokwa na sauti, “Supa D!” alisema kwa mshangao. “Jesus, kitu gani kimetokea hapa?”

Kambambaya hakumwelewa. “Ina maana umekosea na kufungua jokofu la maiti nyingine?” alimuuliza daktari huyo. “Hapana, Inspekta. Jokofu hilihili ndilo lililohifadhi maiti ya yule msichana. Na huyu ambaye yumo sasa ni mfanyakazi wetu wa chumba hiki ambaye alikuwa akihudumia mwili huo. Toka jana jioni Supa D hajaonekana. Ametafutwa kila mahali bila mafanikio. Nashangaa kumkuta humu, tena akiwa maiti.” Ndio kwanza ikampambazukia Kambambaya. “Yaani…” alitaka kumuuliza jambo, akasita. Badala yake aliuliza, “Kwa

hiyo maiti tunayoyatafuta yatakuwa wapi?” “Sijui.”

Kwa ushawishi wa Kambambaya daktari huyo alifungua majokofu yote. Kila maiti ilikuwemo, isipokuwa maiti moja tu, ya marehemu Mona Lisa.

Baada ya dakika nyingi za kuirudia tena na tena kazi hiyo na baada ya kupitia kumbukumbu za mapokezi mara mbilimbili, ilikuwa dhahiri Mona Lisa alikuwa ametoweka!

***

Mlipuko wa bomu uliotokea hotelini ulimpa Joram Kiango fursa nzuri sana. Hata kabla kishindo hicho hakijapoa yeye tayari alikuwa amechupa angani na kumfanya atue juu ya mgongo wa mtu aliyeiinamia injini ya gari kwa miguu yote miwili, huku wa pili akiwa amepokea kichwa kilichomfanya aangukie barabarani. Hakuinuka tena.

Mtu wa pili alikuwa mbishi zaidi. Alimtazama Joram kwa mshangao uliochukua sekunde moja tu, sekunde ya pili nafasi ya mshangao huo ilichukuliwa na hasira kali. Huku akivujwa na damu mdomoni alipangua pigo la pili la Joram kwa kukinga mkono huku akiachia teke farasi ambalo Joram Kiango hakulitegemea. Lilimpata barabara kifuani na kumfanya apepesuke. Teke la pili aliliona. Akalidaka kwa kuachia lake lililompata jamaa huyo katikati ya miguu yake, akaanguka akigugumia kwa maumivu.

Joram alimzoa na kumtupa ndani ya gari, kiti cha dereva. Alitaka kumchukua yule wa pili, lakini wakati huo watu walianza kufurika eneo hilo, huku magari yakiwa tayari yameweka msururu. Joram alifanya haraka kufunika boneti

na kisha kuingia kiti cha abiria, bastola mkononi. “Endesha gari,” alimwamuru mtu huyo ambaye bado alikuwa akiugulia, huku akimkuna utosi kwa mtutu wa bastola.

Si kwamba mtu huyo aliwasha na kuliondoa gari peke yake, aliliondoa kwa kasi ambayo Joram hakuitegemea, kuelekea ufukoni akiteremka na barabara ya Maktaba.

“Wewe!” Joram alimfokea, akimpiga kwa domo la bastola.

Ndio kwanza mtu huyo alikanyanga mafuta kwa nguvu zake zote. Akiwa na hakika kuwa mtu huyu alikusudia kuliendesha gari hilo hadi ndani ya Bahari ya Hindi, ambayo ilikuwa hatua chache tu mbele yao, Joram alimsukuma kwa nguvu kwa lengo la kumpokonya usukani. Hakuwahi. Lori lililosheheni masanduku ya bia, ambalo lilikuwa likiingia katika barabara hiyo, kutokea Barabara ya Sokoine, lilikutana nao uso kwa uso. Joram aliliona sekunde moja kabla alijawafikia. Aliwahi kufungua mlango na kuchupa nje ambako alibiringika mara kadhaa kabla ya kusimama na kuitazama ajali hiyo. Gari lile dogo, Toyota Mark II, sasa lilikuwa kama chapati mbele ya scania tani arobaini lililowagonga. Bado akiwa ameng’ang’ania usukani, mateka wake alikuwa sehemu ya chapati hiyo chochote ambacho Joram alikitegemea toka kwake asingekipata tena.

Huku akifuatwa na macho ya watu wenye mshangao kwa kunusurika kwake, Joram alipiga hatua mbili tatu kurudi New Africa, lengo likiwa kumpata yule mtu wa pili ili ajaribu kumdodosa na, hatimaye, kujua kitu gani kinaendelea. Haikuwezekana. Eneo zima lilikwisha zungukwa na polisi. Ving’ora vya magari ya polisi na zima moto pamoja na kelele za raia waliokuwa wakipambana na polisi eneo hilo vilipafanya pawe mahala palipojaa purukushani.

Akiwa hakujiandaa, huku mwanga ukizidi kuongezeka, Joram alijua kuwa ingekuwa hatari kwake kuendelea kukaa katika eneo hilo. Hivyo, alipenya taratibu hadi vichochoroni ambako alitembea taratibu, mkono mfukoni, sigara mdomoni, hadi nje kabisa ya eneo hilo.

Kichwa chake kikiwa kimejaa maswali, vitendawili na mafumbo tele ya kutatanisha, Joram alijua wazi kuwa alihitaji wasaa wa kutulia ili afikiri. Hata hivyo, hakuona kama

alikuwa na wasaa huo. Roho yake ilikuwa ikitafutwa kwa udi na uvumba huku jitihada zake za kujificha zikiwa zimegeuka mzaha. Zaidi, kuna huyu Mona Lisa ambaye anakufa na kufufuka kama mchezo wa kuigiza. Hapana, hakuwa na nafasi kabisa ya kuketi mahala popote ili afikiri. Ili kuinusuru roho yake na ili aweze kuipa chakula roho hiyo iliyokuwa na njaa kali ya kukitegua kitendawili hicho kinachoendelea, Joram aliamini kuwa ilimpasa kulala huku akiwa amefumba jicho moja na kutembea huku jicho moja likiangalia mbele na la pili likiangalia nyuma; wakati huohuo akiituma akili yake kufikiri harakaharaka kama kompyuta.

Ni hilo alilolifanya. Wakati akipiga hatua moja baada ya nyingine alijiuliza kilichowawezesha polisi na yeyote yule anayejiita au kuitwa Mona Lisa kumfikia kwa urahisi na haraka kiasi hicho. Kwamba alikuwa amefuatwa toka pale hotelini hadi hospitali alikojificha kamwe hakuhafikiana nalo. Kwamba daktari yule alikuwa ‘amemuuza’ kwa kutoa siri ya maficho yake hilo hakuliafiki vilevile, kwani alikuwa na hakika kwa asilimia mia moja kwamba daktari yule alikuwa hamfahamu na alidanganyika zaidi kwa mavazi, sura na majina yake ya bandia.

Kitu gani basi kilifanya maficho yake yabainike mara moja? Alijiuliza akiutia mkono mfukoni na kuangalia vitu alivyokuwa navyo. Isipokuwa kwa simu yake ndogo ya mkononi na pesa chache alizochukua benki, mifuko yake ilikuwa mitupu. Mzunguko wa pesa ni jambo mojawapo ambalo hufichua maficho ya watu wengi. Mara nyingi polisi wazoefu, hasa wale wa INTERPOL, hufuata mkondo wa pesa hata kubaini wapi alikojichimbia mtuhumiwa, hasa anayetuhumiwa kuiba pesa nyingi. Joram alijua wazi kuwa hilo halikufanya maficho yake yagundulike haraka kiasi kile, kwani hakuwa ametumia fedha nyingi na hizo chache alizotumia mzunguko wake usingeweza kuwa wa haraka kiasi kile. Hivyo, wazo hilo alilitupa kando.

Simu! Akakumbuka. Akiwa pale kitandani aliitumia simu yake kutuma ujumbe wa maandishi. Pamoja na ukweli kuwa aliinunua simu hiyo kwa jina la bandia lakini kwa jinsi alivyokaa nayo muda mrefu siku zote alishuku kuwa polisi walikwishainasa namba hiyo na wanamfuatilia. Hakuwa na

shaka tena kuwa ujio wa haraka wa polisi katika eneo lile la Manzese ulitokana na ujumbe ule. Isingekuwa kazi kubwa kwao kwenda kwa kampuni inayoendesha simu hizo na kujua eneo ambalo simu hiyo ilitumiwa. Sitaitumia tena, aliwaza.

Joram aliamini kuwa alikuwa ametegua kitendawili kimoja. Hata hivyo, alijua fika kuwa kitendawili hicho kilikuwa kimoja tu kati ya vingi vilivyomtinga. Bado alihitaji kufahamu kwa nini polisi watumie nguvu nyingi kiasi kile. Zaidi ya wao, alijua kuwa zaidi ya polisi walikuwapo watu au kikundi cha watu ambao, kwa njia moja au nyingine, walikuwamo katika kasi ya kuisaka roho yake. Hakuona kuwa watu aliojaribu kuwateka pale New Africa ni polisi. Hali kadhalika, mwanamke anayejiita Mona Lisa na mwenye sauti ya Mona Lisa hakuonekana kuwa polisi. Aidha, hakuona vipi kifo cha msichana mmoja tu kiwe kisa cha purukushani kali na nzito kiasi hiki. Juu ya yote hayo hakuona uwezekano wowote wa simu ile kumwezesha binadamu yeyote kubaini jina la bandia aliloandikisha kwa daktari na kulitaja kwa ufasaha jina la hayati Mona Lisa, huku sauti ikiwa imefanana vilivyo na ile ya marehemu yule.

Vitendawili au mafumbo hayo vilifanya kitu fulani kiamke katika nafsi yake taratibu, kitu kisichoelezeka, kitu kilichokuwa katika usingizi wa pono. Naam, kitu ambacho kilianza kumpa hamu na shahuku kubwa ya kulikabili jambo hili badala ya kuwa mkimbizi anayekimbiza ubawa wake kama kunguru mwoga.

Wakati akiwaza hayo, alikuwa katika Mtaa wa Samora, ambao tayari ulianza kufurika watu wenye shughuli zao. Joram aliuendea mmoja wa migahawa michache mtaani hapo na kujipatia kahawa ya moto na sambusa mbili. Toka hapo akaingia duka moja la nguo ambamo aliagiza mavazi ambayo hakupata kuyavaa kwa muda mrefu; suruali nyeusi ya jeans na jaketi lake. Pia, alinunua kofia pana ambayo alipoivaa ilifunika sehemu kubwa ya sura yake. Vitu vyote hivyo alivivaa papo hapo dukani. Hivyo, alipotoka alikuwa mtu mpya, tofauti kabisa na yule mzee mchafumchafu aliyeingia dakika tano zilizopita.

Toka hapo Joram aliifuata tena Samora, safari hii akielekea magharibi. Kwenye makutano ya mtaa huo na Barabara ya

Morogoro lilipo jengo kubwa la watoza ushuru, TRA. Kando ya jengo hilo kuna moja kati ya maduka mapya ya silaha yalioanzishwa karibuni. Kwa kuachia ‘kitu kidogo’ aliweza kuushinda urasimu uliowekwa kwenye biashara hiyo na kuruhusiwa kununua bastola mpya, kopo moja la pilipili za kujihami na baada ya kuwaza sana; pingu.

Alijaza kijanja fomu zote zilizohitajika na kuahidi kumalizia hatua zilizobakia, za kuipeleka bastola hiyo polisi hadi kamati ya Silaha ya Mkoa itakapoketi, kamati ambayo Joram alifahamu kuwa kutokana na wingi wa vigogo waliomo na uzito wa shughuli zao, inaweza kukutana baada ya miezi sita! Akajiona kuwa kiasi amekamilika. Joram alianza safari yake nyingine. Safari hii alielekea Mnazi Mmoja, katika bustani ya Jiji, ambako aliingia. Kati ya vivutio vya bustani hiyo ipo sanamu ya mzee mmoja anayepiga ngoma, sanamu ambayo kwa namna fulani imejengewa katika kitu kama pango, ambalo enzi za neema liliongeza uzuri wa mandhari kwa kujazwa maji. Kwa sasa, likiwa kavu, shimo hilo lilimfaa sana Joram Kiango, kwani mmoja wa wasiri wake alikuwa akilitumia kumletea taarifa alizohitaji toka ndani ya Jeshi la

Polisi.

Ujumbe ule alioutuma, ambapo uliandikwa kwa maneno machache, ndani ya fumbo ambalo mtu yeyote asiyekusudiwa asingeweza kuuelewa; alivyomfahamu ‘rafiki’ yake huyo alijua, ungekuwa umefika.

Ndani ya bustani hiyo Joram Kiango aliketi kwa takribani dakika ishirini hivi, katikati ya kundi la vijana wa mjini watatu, ambao hawakuchelewa kum’bom’ sigara na kisha kumshirikisha katika maongezi yao. Walikuwa wakijadili uwezo wa wachezaji wa timu za Uingereza, Manchester United na Liverpool. Pamoja na ukweli kuwa Joram hakuwa mjuzi sana wa masuala ya soka, bado hakushindwa kutia neno hapa na pale, jambo lililofanya akubalike.

Laiti vijana hao wangejua jinsi macho ya Joram yalivyokuwa makini, yakitazama huko na huko kuona kama kulikuwa na mtu yeyote wa kumtilia shaka. Hakuwepo. Hali ilikuwa ya kawaida kabisa. Polisi mmoja pale, muuza kahawa mmoja pale, wamachinga wawili kule, kila mmoja akiwa na hamsini

zake. Hivyo, hakuna aliyeona pindi Joram alipo ‘teleza’ na kwenda chini ya sanamu ile ya mpiga ngoma na kuchokonoa chini ya kigoda alichokalia ambapo aliokota karatasi iliyokunjwakunjwa, yenye harufu ya shombo la samaki, ambayo alilitia mfukoni na kwenda sehemu yenye usalama zaidi, ambako aliifungua.

Ulikuwa ujumbe mfupi, ulioandikwa katika mafumbo vilevile. Joram aliutafasiri. Ulisema;

Unatafutwa kwa udi na uvumba. Vikosi vyote vya usalama vimewekwa katika hali ya hadhari.

Marehemu aliyefariki hotelini ametoweka Muhimbili. Maiti yake yanasakwa huku na huko.

Watu wanakufa hapa na pale. Polisi wanne, daktari mmoja, Manzese. Wahudumu watatu New Africa. Hali inatisha…

Habari, ambayo Joram aliiona katika taarifa hiyo ilikuwa ya kutoweka kwa mwili wa Mona Lisa Muhimbili! Kwa nini maiti yaibiwe? Nani ameyaiba? Kwa faida ya nani? Na kutoweka kwa maiti hayo kunahusiana vipi na mwanamke ambaye amekuwa akimtokea kila anakotorokea na kujiita Mona Lisa? Au ni kweli kuwa Mona Lisa aliyekufa amefufuka?

Joram hakuwa mtu wa kuamini katika miujiza. Hivyo, asingependa kuamini hilo pia. Hata hivyo, kwa kila hali habari hiyo ilikuwa juu ya furushi kubwa la utata, furushi ambalo alihisi likizidi kumwelemea. Furushi ambalo ilikuwa lazima alitue haraka, kwa bei yoyote ile.

W 6 X

EJA Beka Mfumue alikuwa amelitumikia jeshi la polisi kwa takribani miaka ishirini sasa. Tangu alipomaliza masomo yake ya sekondari na kuchaguliwa kujiunga

na polisi hajapata si kuacha kazi pekee, bali kufikiria kuacha kazi. Ndiyo, mshahara ulikuwa hauridhishi kama ilivyo kwa watumishi wengine, hasa walio katika sekta binafsi. Ndiyo, kazi zilikuwa nyingi na shukrani haba. Lakini, pamoja na hayo yote, Mfumue aliipenda kazi yake, aliipenda sana kwani si kila kazi iwezayo kukupa hadhi na mamlaka mitaani kama ya polisi.

Hivyo, alipojikuta kasimama mbele ya Insepkta Haroub Kambambaya, akihisi macho yake makali yanapenya hadi ndani ya moyo wake, hakuwa na shaka kuwa mwisho wa uhai wake katika jeshi hilo ulikuwa umetimia.

“Unajua kuwa kama hutatoa ushirikiano tuna haki ya kukuhukumu kijeshi? Na hata tukikushitaki kiraia unajua kuwa tutakushitaki chini ya sheria mpya ya ugaidi? Kambambaya alikuwa akiendelea, nusu akizungumza katika hali ya kawaida, nusu akifoka.

“Najua,” Mfumue alijibu.

“Kama unajua sasa utatuambia ukweli. Yuko wapi Joram Kiango?” alihoji, macho yake bado yamekazwa barabara kumtazama Mfumue.

Katika hali ya kawaida Beka asingestahili kusimamishwa mbele ya mtu huyu ambaye zaidi ya kuitwa Inspekta cheo chake halisi hakikufahamika, mtu ambaye mara kwa mara anaitwa Inspekta tu, ingawa vikao vyake vingi humuweka pamoja na majeruhi wakuu wa majeshi yote, mtu ambaye mara nyingi huwa mwenyekiti wa vikao hivyo. Hivyo, meja Beka alijua kuwa ili kuuvuka mtihani huu mkubwa wa uhai wake alihitaji kuituliza vizuri akili yake. Jikaze, alijinong’oneza. Kukubali kiasi fulani cha ukweli siku zote huwa ni dawa katika hali kama hii.

“Natumaini sauti yangu inasikika vizuri Meja,” Kambambaya alirudia. “Yuko wapi Joram Kiango?”

“Sijui,” Mfumue alijibu. Lilikuwa jibu la kweli.

“Toka alipokupigia simu ile hamjapata kuwasiliana tena?” “Bado,” jibu jingine la kweli.

Kambambaya alimkazia macho kabla hajauliza, “Una hakika?”

“Ndiyo.”

“Ujumbe aliokutumia uliandikwa katika hali ya fumbo.

Alitaka nini?” Kambambaya alihoji ghafla.

Mtego, Beka aliwaza. “Alitaka msaada,” akamjibu. “Msaada gani?”

“Habari.” “Habari gani?”

“Alitaka kujua kama kuna habari au tukio lolote la kusisimua, lililotokea karibuni, ambalo linafuatiliwa na polisi,” nusu lilikuwa ukweli nusu uongo.

Kambambaya pia alihisi hivyo. Alimkazia Beka macho kwa muda kabla ya kuuliza taratibu, “ Kama tukio lipi?”

“Kama mauaji, wizi wa fedha nyingi, ugaidi na mambo kama hayo. Joram ni mshabiki mkubwa wa mambo hayo…”

“Ulimjibu nini?” Kambambaya aliuliza ghafla.

Mtego. Meja Mfumue aliwaza. Akaamua kutoa uongo wake wa kwanza, “Bado sijamjibu.”

“Kwa nini?”

“Sijapata nafasi,” uongo mwingine. “Vilevile,” aliongeza. “Sijawa na jambo lolote ambalo linaweza kumsisimua.”

Sasa Kambambaya alikuwa na hakika kuwa Meja Beka

ITAENDELEA

Mtambo Wa Mauti Sehemu ya Tatu

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment