Noti Bandia Sehemu ya Tano
KIJASUSI

Ep 05: Noti Bandia

SIMULIZI Noti Bandia
Noti Bandia Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA: BEN R. MTOBWA

*********************************************************************************

Simulizi: Noti Bandia

Sehemu ya Tano (5)

Mahakama ilifulika watu, kila mmoja akiwaza hili na lile. Ilikuwa imeahilishwa jana kutokana na hoja mbalimbali zilizowasilishwa mahakamani hapo, kufuatia malumbano ya kisheria na leo ilikuwa siku rasmi ya kutoa hukumu. baada ya taratibu zote za kimahakama, kama kawaida, askari maalum alipaza sauti kuashiria kuingia kwa mheshimiwa Hakimu, watu wote alisimama.

Kanali Benny Emilly, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi, alikuwa mmoja wa watu waliofika hapa, Mzee huyu alikuja kusikiliza hukumu ya kesi hii akiwa na baadhi ya wasaidizi wake kadhaa. Kabla ya kufika mahakamani hapa alifanya kila njia kuwasiliana na Teacher, hakubahatika kupata mawasiliano yake. Baada ya Hakimu kuingia na kuketi katika kiti chake, alichukua baadhi ya mafaili yaliyokuwa mezani hapo na kuyapitia moja baada ya jingine, baadhi aliyaweka kando, hatmaye akabakiwa na faili moja mkononi.

“Kutokana na umuhimu wa kesi ya uhujumu uchumi iliyo mbele yangu, nimelazimika kuahilisha kesi zingine zote zilizokuwa zitajwe leo, wahusika katika kesi hizo wafike chumba cha kumbukumbu kwa ajili ya maelekezo zaidi ikiwa pamoja na kupangiwa tarehe nyingine ya kesi, nitasikiliza kesi ya kuhujumu uchumi inayowahusu Hawa Msimbazi nana Tony Sime, bila shaka wapo?”, Hakimu alihoji baada ya kueleza.

“Naam mheshimiwa, wateja wangu wako mbele yako”, alieleza Kyaruzi, ambaye ni mwanasheria upande wa utetezi. akaandika maelezo, baada ya kujiweka sawa, akasema.

“Mwendesha mashitaka”.

“Mheshimiwa Hakimu, kesi iliyoko mbele yako ni Kesi namba 208 ya mwaka huu, kama ilivyosomwa hapo awali, washitakiwa Hawa Msimbazi na Tony Sime, wanashitakiwa kwa pamoja kuwa mnamo tarehe 15 ya mwezi huu, huko Uwanja wa Ndega wa Dar es Salaam, walikamatwa na askari wakijaribu kuingiza dawa za kulevya aina ya heroine, ambalo ni kosa la kuhujumu uchumi”, akageuka.

“Mheshimiwa, baada ya watuhumiwa hawa kukamatwa kwanza walikaidi amri halali waliyopewa na askari, wakidai kuwa mzigo wao si dawa za kulevya isipokuwa ni malighafi kwa ajili ya kiwanda chao cha kutengeneza tembe za kutibu malaria. Ili kujiridhisha, malighafi hizo zilipelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali. Ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa mzigo uliokamatwa ukiingizwa nchini ni dawa hatari za kulevya aina ya heroin ambazo zimepigwa marufuku na Serikali ya Tanzania kuingizwa hapa hapa nchini”.

Haraka mwanasheria wa utetezi akasimama na kugonga meza, “Mheshimiwa Hakimu, suala la dawa za kulevya si jambo la kufanyia mchezo, kama wateja wangu walivyoieleza mahakama yako tukufu jana kuwa hawahusiki kabisa na dawa za kulevya, inashangaza sana mwendesha mashitaka wa Serikali kung’ang’ania kuwa ripoti ya mkemia mkuu wa Serikali imethibitisha wateja wangu walibeba dawa za kulevya jambo ambalo si kweli”.

Mwendesha mashitaka wa Serikali akasimama tena. “Kama si dawa za kulevya… naomba uieleze mahakama, wewe unadhani watuhumiwa hawa waliingiza nini hapa nchini?. Mheshimiwa kama ishu ni kuagiza mizgo kwanini wasitumie cargo kusafirisha mizigo yao?”.

“Mheshimiwa Hakimu, maelezo ya wateja wangu yako wazi kabisa, wameieleza mahakama yako tukufu kuwa mzigo wao ni maalum kwa ajili ya kutengeneza tembe za kutibu malaria. Tena wakasisitiza kuwa kama mzigo huo ni dawa za kulevya si wao, inawezekana wamefanyiwa njama za kibishara mambo haya yapo. Mheshimiwa, kinachoshangaza ni kwamba mzigo uliokamatwa umepelekwa kwa mkemia mkuu wa Serikali bila wateja wangu kuhusishwa hii haikubaliki. Inawezekana wakafanyiwa hujuma, ndivyo inavyoonekana. Mheshimiwa, mahakama ni chombo cha haki, kisitumike kuwaonea wateja wangu”, mwanasheria wa utetezi alieleza.

“Mheshimiwa, kama nilivyoileza mahakama yako tukufu jana. Narudia, haiwezekani watu hawa wasafiri kutoka hapa nchini, waende nje ya nchi, watumie pesa nyingi kwa ajili ya kufuata malighafi za kutengeneza tembe za malaria. Mheshimiwa, mzigo uliokamatwa ni mali ya washitakiwa hawa. naamini hata wewe unasafiri nje ya nchi, lakini huwezi kuchukua mzigo usioujuwa, hawa ni wafanyabiashara wazoefu wa bishara chafu, wakiachiwa wanaweza kuligharimu taifa”, aliketi baada ya kusisitiza.

“Mheshimiwa, inawezekana kabisa mwendesha mashitaka wa Serikali ana sababu zake binafsi kwa wateja wangu, jambo hili lisichukuliwe kijuujuu, taratibu ziko wazi mheshimiwa, tusitumike vibaya kwa sababu mkemia mkuu wa Serikali, mwendesha mashitaka wa Serikali ndiyo iwe njia ya kuwaumiza wateja wangu, haitawezekana mheshimiwa, kwanza walipaswa kuitwa ili washuhudie vipimo husika, lakini hili limefanyika bila wateja wangu kuhusishwa”, mwanasheria wa utetezi alilalama kwa mara nyingine.

Hakimu aligonga meza, ukimya ukatawala kwa dakika kadhaa. “Hukumu. Nimesikiliza hoja za pande zote mbili kwa makini na kupitia maelezo ya pande zote kwa umakini mkubwa. Hivi niwaulize, inawezekanaje mtu ubebe mzigo usioujuwa kutoka huko nje, ukibadili ndege hii na hii hadi unaingia nchini, mzigo huo huo ukaubeba kwenye magari kuelekea nyumbani bila kujua umebeba nini?”, Hakimu alihoji.

“Kama umefanyiwa njama au watu wanataka kuharibu biashara yako ama sifa yako, inawezekana kabisa mheshimiwa, wengi wamekutwa na kashfa za aina hii, naiomba mahakama yako tukufu iwatendee haki wateja wangu”, mwanasheria wa utetezi alirudia kusihi.

Dakika kadhaa zilipita kukiwa kimya, hakimu akiichezea kalamu yake kwa meno, …”Usinifundishe kazi. Naam, Mwendesha mashitaka wa Serikali ameieleza mahakama hii kuwa mnamo tarehe 15 mwezi huu, watuhumiwa wawili, Hawa Msimbazi na Tony Sime, mlikamatwa huko Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere, mkiwa na mzigo ambao ripoti ya mkemia mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin. Jambo hili ni zito, bila shaka unajuwa kuwa dunia nzima imepiga marufuku matumizi ya dawa hizi, sijui hata mmewezaje kutoka huko nchi za mbali, mkavuka ukaguzi pale Uwanja wa ndege, hatmaye mkaingia nchini na kutiwa mbaroni na vijana waaminifu katika taifa hili”, Hakimu alieleza huku wengine wakitazamana.

“Mmmh wamekwenda na maji hawa”, kijana mmoja aliyekuwa mahakamani hapo alimnong’oneza mwenzake.

“Mwanasheria wa utetezi anasema inawezekana wateja wake walibeba mzigo wasioujuwa, lakini wamekiri kuwa walisafiri kwa ajili ya kuingiza malighafi za kutengeneza tembe za malaria, walipoulizwa na mwendesha mashitaka inawezekanaje watu watumie gharama kubwa kusafiri nje ya nchi ili kuingia mzigo wa gharama ndogo ambao haukidhi matumizi, hawakutoa jibu. Walipoulizwa tena kwanini wasitumie njia ya cargo kusafirisha mizigo yao hawakutoa majibu. Hii inaonyesha kabisa watuhumiwa hawa walikusudia kuingiza dawa za kulevya hapa nchini”, Hakimu alieleza.

“Baada ya kusikiliza kesi hii na kupitia vingu mbalimbali vya sheria, nimethibitisha bila kutia shaka kuwa watuhumiwa hawa wana kesi ya kujibu. Kabla sijatoa hukumu, mnaweza kujitetea.

“Mheshimiwa Hakimu, tunaomba huruma yako, kwa upande wangu nina jukumu la kuwalea wazazi wangu ambao ni wazee sana, nina watoto wadogo wanahitaji msaada wangu mheshimiwa, wakinikosa wataathirika sana, naomba huruma unifikirie kwa hilo mheshimiwa, pia nasumbuliwa na tatizo la kifua”, Hawa Msimbazi alijitetea.

“Tunaomba msaada wako mheshimiwa, kimsingi hili ni kosa la kwanza, tunaomba mahakama yako itupunguzie adhabu”, Tony Sime alieleza huku hakimu akiandika maelezo yao kwa makini.

“Kuwa na wazazi wazee, watoto wanakutegemea haikupi tiketi ya kukufanya utende makosa, mbona wewe hukuwaonea huruma watoto wa wenzio, dawa za kulevya ni hatari kubwa. Naam ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye mawazo na tabia kama yenu, nawahukumu kwenda jela kila mmoja miaka kumi na mitano”, wote wakaanguka chini wakati hakimu akitoka mahakamani.

Taarifa za kufungwa jela kwa watuhumiwa wawili wa dawa za kulevya, Hawa Msimbazi na mwenzake Tony Sime, zilisambaa haraka kwenye mitandao ya kijamii. Blog ziliripoti habari hii kwa mbwembwe, waandishi wa mitandao wakipishana kwa vichwa cha habari na maelezo yaliyosisimua wengi.

Blog ya MPIGANAJI iliandika. Breaking News, halafu mwandishi akaweka maneno haya. WAFANYABIASHARA WA DAWA ZA KULEVYA WAKIONA CHA MOTO, WATUPWA JELA MIAKA. 15. Blog ya KAMANDA WA MATUKIO iliruka na kichwa cha habari, DAWA ZA KULEVYA ZAWAPELEKA JELA MIAKA 15, MICHUZI wakaandika, MAHAKAMA YATOA ADHABU NDOGO KWA WAUZA DAWA ZA KULEVYA. Redio zikatangaza habari hii, waliosikia walishangilia.

Shamla shamla ziliendelea mitaani. ulikuwa ushindi mkubwa kwa Serikali. Lakini ghafla habari hii ikagauka msiba. Masaa kadhaa baada ya hukumu, taarifa zikaenea kuwa Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo na kutoa hukumu amepigwa risasi na kuuawa ofisini kwake. Hofu ikatawala. Wakati viongozi wakitafakari kuhusu tukio hili. Habari nyingine inasambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa, askari kadhaa wameuawa na wengine kujeruhiwa vibaya baada ya kutokea mapigano makali wakati wakisindikiza wafungwa.

Taarifa hii ilieleza kuwa wafungwa wawili waliotuhumiwa kuingiza dawa za kulevya nchini, Hawa Msimbazi na Tony Sime, waliokuwa wakipelekwa katika gereza moja Jijini Dar es Salaam wametoroshwa wakiwa wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi. Wananchi wakapatwa na masikitiko, Mzee mmoja wa makamo aliposikia taarifa hizi kwenye vyombo vya habari alitoa machozi.

Habari zinamfikia Kanali Beny Emilly, anashindwa kuyaamini masikio yake, anasimama sekunde kadhaa mbele ya kiti chake, hofu inamwingia, anajaribu kwa mara nyingine kuinua simu yake ya kiganjani kuwasiliana na Teacher. Bahati mbaya simu hiyo haipatikani anaelekea kuchanganyikiwa, furaha yake inageuka kalaha, machozi yanamlengalenga.

“Nini hii?”, Kanali Emilly anajiuliza wakati akielekea nje ya ofisi yake.

Taarifa hii inawafikia wakubwa wa nchi, vikao vya dharura vinakaa. “Nini kumetokea”, anahoji mkuu wa nchi. “Hili haliwezekani katika nchi hii”, anasisitiza bila kupata majibu. Wasaidizi wake wanajaribu kueleza msimamo.

Simu zinapigwa huku na huko bila mafanikio, “Nani hasa wameshiriki katika tukio hili”, Kanali Emilly anajiuliza kwa mara nyingine.


Nilijaribu bila mafanikio kutambua wapi tulipofichwa. Tulikuwa tumesimamishwa mbele ya watu hawa huku mikono na miguu yetu ikiwa imefungwa barabara kwa kamba ngumu. Pamoja na mazoezi makali ninayofanya karibu kila siku, lakini hapa niliyasikia maumivu kutokana na staili iliyotumika kutufunga hizi kamba. Ukweli hata uwe na mazoezi kiasi gani kwa mtindo huu lazima utasikia maumivu.

Wote watatu tulifungwa kwa mtindo mmoja, yaani miguu yetu ikiwa imefungwa kamba, mikono nayo ikiwa imefungwa vizuri kwa nyuma halafu kamba hizo zimevutwa na kufungwa sehemu ya juu. Kwa maana hiyo mikono yetu ilivutwa nyuma ikaangalia juu na kutusababishia maumivu makali sana.

Kelele za mashine na baadhi ya watu zilisikika, hali hii ilinifanya nikabaini kuwa eneo hili lilikuwa la viwanda. Niliwaza na kujiuliza mambo mengi, nilimuomba mungu angalao awanusuru wenzangu Julius Nyawaminza na Claud Mwita ili mimi nichukue nafasi yao.

Nilijilaumu kwa kuweka tahadhali ndogo wakati naingia pale hotelini, hata hivyo sikupaswa kulaumu sana maana tayari nilikuwa katika mikono ya mauti. Hasira na chuki kwa watu hawa zilinijia, nikatamani kufanya miujiza lakini sikuweza tena.

Mlango ulifunguliwa mtu mmoja mnene ambaye sikuwahi kumuona katika historia ya maisha yangu akaingia ndani, alikuwa mtu makamo, mwenye umri kati ya miaka hamsini na sitini, alivaa mavazi yaliyomkaa vizuri na miwani ya jua, mtemba ukiwa kinywani mwake. Alionekana mtu mwenye busara kiasi, lakini kwa uzoefu wangu nikabaini mtu ni mmoja wa watu washenzi pengine zaidi ya Carlos Dimera.

“Karibu Mzee Mtemba”, sauti nzito ya Jackina ilisikika, Mzee huyo alipita taratibu akituangalia kwa tabasam na bashasha, baada ya kushikana mikono na Carlos akaketi.

“Nimekuita ushuhudie vifo vya mbwa hawa. Mzee Mtemba bila shaka unatambua jinsi mtandao wetu ulivyotikiswa, chanzo ni hawa washenzi wanaoamini biashara ya dawa ya kulevya itakomeshwa, ni ndoto ya mchana”. Akainua macho. “Poleni sana, ujinga wenu umewakosti, mimi ni mtu mwenye huruma sana lakini kwenu sintakuwa na huruma kamwe”, Carlos akasisitiza.

“Wewe ndiye unaona hivyo Carlos, lakini pia tambua kuwa mjinga wa leo ndiye mwelevu wa kesho, kufa ni jambo la kawaida katika maisha ya mwanadamu, sisi hatuogopi kufa, naamini siku moja utakufa pia, adhabu yako mbele za Mungu itakuliza milele”, nilimwambia.

“Mwangalie mpumbavu huyu, wakati wewe unakufa leo mimi nataendelea kula maisha, nitatanua kwa raha zangu, pole sana Teacher, wewe ni miongoni mwa watu waliochelewa sana katika maisha. Hebu mtieni adabu mbwa huyu”, Carlos aliagiza. Vijana wawili wakanijia tena na kuanza kunitwanga.

Wakati wote huo Mama Feka alikuwa akichezea simu yake ya kiganjani, sikujua alichokuwa akifanya nadhani alikuwa akiwasiliana na watu wake fulani. Vijana hawa walinivamia na kunipiga ngumi kadhaa tumboni na kunisabanishia maumivu makali zaidi.

“Utalipa, iko siku utalipa”, nilieleza wakati nakaribia kupoteza fahamu.

“Teacher, kama nilivyokwambia hapo awali mtandao wetu ni mkubwa mno, umesambaa dunia nzima, mijini na vijijini, tunao viongozi wakubwa katika Serikali. Huyu Mzee wa Mtemba ndiye Mkuu wa Operesheni ya wizi wa kutumia noti bandia, ambazo nafikiri ulionyeshwa na bosi wako, wengi wameuza majumba yao kupitia mzee huyu”, Carlos alidokeza, sasa nikaelewa sababu za mtu huyu kufika mbele yetu maana niliwahi kumsikia lakini kwa jina la Benny.

Mzee Mtemba akasimama. “Asanteni sana vijana wangu, kama ulivyoelezwa, mimi ndiye kigogo wa opereshani ya noti bandia. Lakini kabla sijaongea nanyi, binafsi nichukue nafasi hii kutoa hongera kwa kazi yenu nzuri, mmejaribu kututia matumbo joto. Mimi ni mfuatiliaji wa siasa za nchi hii, miaka zaidi ya kumi niliyoishi humu, nimegundua kuwa nchi hii haina mwenyewe, ndiyo maana tumeweza kuishi hata bila kufuata taratibu za uhamiaji, nawasikitikia sana vijana hawa ambao umri wenu bado mdogo sana, lakini mtakufa leo, mimi ni mtu wa imani na huruma sana, sipendi kuona mtu akiuawa, lakini nyie mmekitafuta kifo wenyewe, ndiyo maana nimekuja mnijuwe pia nishuhudie vifo vyenu”, alieleza mtu huyu halafu akaketi.

“Mzee Mtemba, binafsi nimekuwa nikieleza habari hizi kwa mifano ili adui zangu watambue mimi ni mtu wa aina gani, lakini vijana hawa hawakunisikia eti kwa sababu tu wamekunywa maji ya bendera. Kikosi ninachokiongoza kina nguvu kubwa kushinda dola ya nchi hii, Hawa na Tony wako huru, hebu ingieni ndani”, Carlos Dimera alieleza. Mlango ukafunguliwa Hawa na Tony tuliowakamata na dawa za kulevya na kisha kuwafikisha mahakamani wakaingia wakiwa na nyuso za hasira.

“Asante sana bosi. Tuko huru sasa”, alieleza Hawa huku akionyesha hasira alizokuwa nazo kwangu. “Ulijisikia jasiri kwa kutukamata, lakini ujasiri wako leo umekwisha”, aliongeza.

“Ni kweli, lakini amini utakamatwa tena”, nilimwambia kwa mkato.

“Mpaka itokee. Naamini kifo chako kitawaogopesha wengi, hata mashujaa waliokuwa wakijipanga kujiingiza katika suala hili watakaposikia mwili wako umeokotwa kando ya bahari, mmmh watarudi nyuma”, Hawa aliongeza.

“Hii ni kuwaonyesheni kuwa hatushindwi kitu, kama mzee Mtemba alivyosema, leo ndiyo mwisho wenu kuishi duniani, tulitaka mhakikishe kuwa Hawa na Tony hawafungwi jela, sasa ni wakati mzuri kwenu kupeleka habari hii huko kuzimu, poleni sana”, carlos aliongea kwa kujiamini.

“Tuko tayari kwa lolote, lakini mtambue kuwa hakuna mwenye nguvu zaidi ya dola, sisi tutakufa leo, lakini wapo ambao wataendeleza hapa tulipofika, wengine wamezaliwa tayari, wengine wako katika matumbo ya mama zao”, niliwaambia kwa sauti ya kutetemesha na hasira.

“Yawezekana wewe una mapungufu katika kichwa chako, mtu gani wewe usiyeogopa kifo, mbona wengine wamenyamaza”, alisema Carlos.

“Kunyamaza kwao si kwamba wanakuogopa kufa, wamekudharau sana, nikwambie ukweli, kabla hamjatoka hapa leo mtakuwa mmekamatwa wote, hii ni nchi ya watanzania, hata hawa vibaraka wako pia ni watanzania lakini wasarti wa nchi iko siku yao”, niliwaambia.

“Ombeni Mungu wenu azipokee roho zenu kwa mara ya mwisho, sihitaji kuumizwa kichwa cha…. Carlos alikatishwa na kelele za vishindo na risasi zikasikika kutoka nje. Risasi zikaendelea kulindima, wote tukaingiwa na hofu, ghafla umeme ndani ya chumba hiki ukazimika, kukawa giza.

Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa hivi kupita, risasi zikarindima tena huku nafsi zetu zikiwa zimejawa na hofu kubwa. Ghafla taa ndani ya chumba hiki ziliwashwa, vijana wawili nadhifu sana waliingia ndani ya chumba hiki kwa kasi ya ajabu, silaha zao zikiwa mikononi wakazikata kamba zilizofungwa kwenye miguu na mikono yetu kwa visu vikali. Ukweli ni kwamba Vijana hawa sikuwahi kuwajua kabisa.

“Poleni sana bosi, tutaongea baadaye”, alisema mmoja wa vijana hawa baada ya kuzikata kamba tulizofungwa kwa kisu chake imara.

“Usijali”, niliwaambia huku zikinyoosha viungo vya mikono yangu. Risasi zikasikika tena nje, mmoja wa vijana hawa akatufahamisha kuwa tusihofu ilikuwa kazi ya Peter Twite, ambaye alikuwa nje ya chumba hiki kuimarisha ulinzi wetu.

Bahati mbaya ni kwamba, hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa katika vurumai hiyo, Carlos Dimera, Mzee wa Mtemba na vijana wao kadhaa walifanikiwa kutoroka salama kutoka katika eneo hilo. Kazi nzuri iliyofanywa na Mama Feka ilikuwa imenusuru maisha yetu.

Ilikaribia kuwa saa tano za mchana, Wakati wote sikujuwa tulikuwa sehemu gani, baada ya kutoka ndani ya chumba hiki, nilishangazwa kuona kumbe tulikuwa kwenye ofisi za karakana ya Tazara, kando ya barabara ya Nyerere. “Mmmh inakuwaje”, nilijiuliza kwa sauti baada ya kumuona Peter Twite akinijia.

“Pole sana mkuu, tuondoke haraka eneo hili, watu wengi sana wameuawa hapa, tuondoke kabla polisi hawajafika, wanaweza kutuleta nongwa, tukacheelewa”, alisema huku akinishika mkono kunisabahi.

“Ni kweli kabisa Petet, hii inaweza kutuchelewesha pia”, nilimwambia, sisi tukaingia ndani ya gari alilokuwa akiendesha Twite, tukaondoka kuelekea sehemu za Vingunguti. “Wapi Fred?” Niliuliza.

“Fred, tuliwasiliana saa tatu hivi, akaniuliza kama nimesikia taarifa za mauaji ya Hakimu aliyehukumu kesi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, nikamwambia nimesikia, akaniuliza kuhusu kutoroka kwa watuhumiwa hao mikononi mwa polisi, nikamjulisha kuwa taarifa hizo ni kweli, mwisho akanifahamisha anawatafuta lakini hawapati, baada ya hapo sijamsikia tena na simu yake haipatikani”, alieleza Twite wakati anavuka kwenye njia ya reli ya Vingunguti.

“Twende Green Pub, nadhani patafaa kwa mazungumzo kidogo wakati tukifikiri na kutafakari tuwafanye nini watu hawa”, nilisema, wakati Peter Twite akizungusha usukani wa gari tukaingia Barabara ya Nyerere na kuelekea eneo la Vingunguti.

“Watu hawa wamejipanga vizuri kutenda uhalifu”, Nyawaminza alisema baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu.

“Inaonyesha hivyo. Lakini tuwe makini sasa, maana jana tu nimekamatwa mara mbili, naamini wanatumia mawasiliano ya mitandao kujua mahali tulipo, sasa tusiamini mtu yeyote”, niliwaasa.

“Hakika. Mimi bado najiuliza ilikuwaje wakaingia kwenye ofisi za umma pale karakana na kuzitumi kama sehemu zao, ingekuwa siku za mapumziko kama sikukuu ama Jumamosi, Jumapili nisingehofu, lakini leo siku ya kazi?” alihoji Twite.

“Tutajua baadae. Hawa ni wahalifu wakubwa, wanachofanya ni kuvamia na kuua wahusika, wanatumia eneo hilo kwa muda halafu wanasepa. Wengine hutumia maeneo hayo nyakati za usiku, lakini hawa wako vizuri mpaka wakati huu mchana kweupe?” nilisema wakati Twite amesimama kwenye taa za kuongoza magari za Jeti.

Tulikuwa na magari matatu, ambayo hayakufauatana kwa karibu kutokana na hali ya usalama. Peter alichepuka tukaingia kwenye barabara mbovu ya vumbi, baada ya kuvuka kizuizi cha reli ya kati, akaingia kulia kama tunarudi katikati ya Jiji. Tukazipitka ofisi za Kiwanda cha BECO, Nilikuwa makini kuangalia kila gari lililokuwa mbele au nyuma yetu, hatmaye tukaingia Green Pub.

“Ipo njia ya mkato hapa, lakini nilipita Jeti kwa sababu za usalama”, Twite alidokeza.

“Nilikusoma, ndiyo maana nikawa kimya”, nilijibu wakati tukitafuta sehemu nzuri ya kuketi. Bahati nzuri mwenye sehemu hii rafiki yangu Kinyami Mwitazi ananifahamu, alipotuona alituelekeza sehemu nzuri tukaketi. Bada ya kila mmoja kuagiza kinywaji chake, tukagawanyika, wale vijana wakatafuta sehemu yao mbali kidogo tofauti na sisi.

“Peter, najiuliza sijui hata nikushukru kwa maneno gani. Maana sijui hata ilikuwaje ukajuwa kuwa tumefungiwa pale Karakana?” nilianzisha mazungumzo.

“Ni hadithi ndefu, lakini tumshukru sana Mama Feka, nadhani atafika hapa muda si mrefu. Bosi ulicheza sana kumuingia dada huyu katika kazi hii, bila yeye sijui ingekuwaje?” Peter alidokeza.

Mara Pikipiki kubwa aina ya Honda XL CC 250 ikasimama upande wa pili wa Reli, juu ya pikipiki hiyo kulikuwa na vijana wawili nadhifu, mmoja wa kiume na mwingine mwanamke wote wakiwa wamevalia miwani ya tinted usoni. Msichana mrembo sana alishuka, baada ya kuangalia huku na kule akatembea kuelekea mahali tulipoketi.

“Unamfahamu huyo?” Peter aliniuliza.

“Bila shaka ni Mama Feka, ama kweli ametakata”, nilisema. Yule kijana aliyemleta aliinua mikono, akatupungia halafu akaondoka.

“Na huyo?”.

“Huyo ni kjana wetu, miongoni wale ulioagiza wakae kwenye pointi wakiwa na Pikipiki, vijana hawa hawajalala toka tuanze kazi hii, kama tukiimaliza salama, tusiwasahau, utazani wamewahi kufanya kazi hizi”, Peter alishauri.

“Ni kweli kabisa Peter”.

Baada ya kutushika mikono, Mama Feka alivuta kiti karibu yangu akaketi. “Poleni sana Teacher, nasikia usingizi sana lakini usijali, karibu tutashinda vita nitapata wasaa mzuri wa kulala”, alieleza.

Akaanza kutueleza habari zote, toka nilipokamatwa kule Hoteli Bela Vista Kinyerezi, alivyoniwezesha kutoroka pale kiwanda cha Blanket Keko, kutekwa kwa Julius Nyawaminza, Claud Mwita na hatimaye mimi.

“Shemeji yangu Teacher, kazi hii ni ngumu, lakini nakiri kuwa baada ya wewe kuniingiza katika jambo hili imesaidia kujua mambo mengi, sasa nazijua sababu za watu kuniita Cthia Rothrock, nimewiva sana, angalieni saa zenu”, alisema wote tukainamisha vichwa kuziangalia saa zetu, ilikaribia kuwa saa saba mchana.

“Inakaribia saa saba mchana. Binafsi nimsifu na kumpongeza sana Peter, baada ya kutambua kuwa simu zenu zimeingizwa kwenye mtandao wa mawasiliano na kila mlichofanya pale pale kilionekana, sikuona sababu ya kuwasiliana na simu zenu, nilitengeneza laini yangu ya siri, ambayo nimeitumia kwa ajili ya kuwasiliana na Peter tu. Na kweli imesidia kuokoa maisha yenu, nilichanganyikiwa sana nilipomuona Mzee wa Mitemba, yule Mzee akiitwa maeneo kama yale, mmmh usitehgemee kutoka salama, tumshukru sana Mungu”, alisema.

“Ilikuwaje wakatoroka wakati tulikuwa tumeizingira ofisi ile?, tena ajabu ni kwamba tumeua watu ambao hawahusiki kabisa”, Peter alihoji.

“Pale ndani ya ofisi ile, chini kuna milango miwili ya siri, ukibonyeza kitufe inafunguka unazama na kuna njia ya kutokea sehemu nyingine kabisa, tumepita huko”, alieleza Mama Feka.

“Hawajakushtukia?”, niliuliza.

“Wee, siyo rahisi, unajuwa wakati nawasiliana na Peter, kidogo Carlos anishtukie, lakini nilikuwa nimefanya ujanja fulani, nilifungua sehemu ya game, nikawa nacheza huku natuma ujumbe, kwa kuwa simu yangu niliitoa sauti, basi ilikuwa kazi rahisi kujibu kila swali Peter aliloniuliza”.

Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, akaanza kutueleza tena habari za kutisha na kusikitisha sana, “Watu wengi sana wamepotea, nimeona mambo mengi ya kutisha sana, namshukru Teacher alinijenga kisaokolojia kabla sijaingia huko. wale watu ni hatari sana. Naomba mnisikilize kwa makini sana”, tukajiweka tayari kumsikia huku nywele zikinisiimka kichwani, sikuamini kama Mama Feka angetusaidia kiasi hiki. Kimya kimya nilituma ujumbe wa maandishi kwa Kanali Benny Emilly ili naye afike sehemu hii maana tulikuwa tunajiandaa kuingia vitani.

“Mkishindwa kuwakamata leo, itakuwa ndiyo salama yao, hawatakamatwa tena, wamepanga kutokomea leo, hivi tunavyongea hapa kuna meli ndogo iko ufukweni mwa Bahari, itaondoka nadhani itakuwa saa kumi Alasiri, wana kikosi kizuri sana, wanao vijana mahiri katika mapigano, ili kazi yetu iwe rahisi lazima tujipange sawasawa”, alishauri.

“Tumekusikia”, nilimwambia, halafu nikawageukia wenzangu, “bila shaka wote tumemsikia Mama Feka?”.

“Naam”, walijibu huku tukiendelea na vinywaji. Mara simu yangu iliita nikapokea. Ilikuwa simu kutoka kwa Kanali Emilly.

“Angalia upande wako wa kuume ulipoketi, kuna Pick Up single cabine rangi ya kijani, ina kiturubai nyuma, njoo ingia tuzungumze”.

“Nakuja bosi”, nilisema huku nikisimama. “Jamani, ngoja nimsikilize kigogo, nendeleeni nakuja”, nikawaacha na kuelekea kwenye gari lililokuwa limeegeshwa mbali na eneo tulipoketi. Nilipokaribia dereva wa gari hilo alishuka na kunielekeza niingie upande wake.

“Jambo Mkuu”, nilimsalimia Kanali Emilly baada ya kuongia ndani ya gari hii.

“Jambo, habari ya kupotea Teacher?. Mpaka nikapatwa na hofu kubwa. Ulipatwa na nini Kapteni?”

Nikaanza kumweleza kilichonitokea hata nikatekwa na kutoroka kule Kiwanda cha Blanketi. Nikaeleza jinsi tulivyoponea chupchup kuuawa kwenye ofisi za Karakana ya Tazara, maelezo haya kiasi fulani yalionekana kumuumiza rohoni.

“Poleni sana vijana wangu. Siku zote Mungu humsaidia asiye na hatia, yule anayeonewa. Teacher mwanangu, mpaka sasa adui anaelekea kuchanganyikiwa, cha msingi tusilegeza kamba, au unasemaje?”

“Hakika”.

“Mmekwama wapi?”.

Nikaanza kumweleza kuhusu mpango ulio mbele, “Hatujakwama Mkuu, tunachofanya sasa ni kujadili plani B, kuvamia eneo fulani ufukweni mwa Bahari. Taarifa zilizopo ni kwamba wamepanga kutoroka leo jioni wakitumia Meli ndogo ambayo tayari imejazwa shehena ya dawa za kulevya kwa ajili ya kuelekea Mombasa. Na sisi hatutawapa nafasi hiyo, Leo ndiyo mwisho ama wao ama sisi”, nilisema.

“Amina”, Kanali Emilly alisema kwa ishala huku akiangalia juu.

“Samahani, Afande nakuomba shuka kwenye gari twende uongee na vijana, uwape hamasa, vita si lelemama, habari kutoka kwenye vyanzo vyetu ni kwamba adui ana nguvu na vifaa vya kisasa kama silaha na mitambo”, nilimwambia akahamasika, akafungua mlango tukashuka kuelekea kwa wapiganaji. Wote wakasimama, machozi ya furaha yakamtoka.

Mchana huu sehemu nyingi za starehe zilikuwa zimefungwa, hii ni kutokana na agizo la Serikali kuwataka watu wafanye kazi kwanza na kustarehe baadaye, kutokana na hali hii tulipata wasaa mzuri wa kukaa hapa Green Pub kumsikiliza Kanali huyu wa Jeshi, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Upelelezi, Benny Emilly. Alikuwa Mzee wa makamo na nywele zake zilikuwa zimebadilika rangi kuwa nyeupe kabisa. Baada ya kufuta machozi ya uchungu yaliyomtoka akiwa mbele yetu, alivuta kiti kilichokuwa karibu akaketi. Tukasogeza viti ili kumsikia atasema nini.

“Wapiganaji wangu shupavu, nyie ndiyo hazina ya nchi yetu, sisi wazee tumechoka, tunaelekea ukingoni, jukumu lenu sasa ni kulinda heshima ya nchi yenu. Mimi sina kawaida ya kutoa machozi mbele ya watoto, lakini leo yamenitoka. Mnajua kwanini yametoka. Nimefurahi sana kuwaona katika hali hii ya umoja, bila umoja hakuna ushindi. Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema Umoja ni nguvu, Mzee Kenyatta naye akasema Harambee, maana ni lilelile. Watanzania wanasubiri ushindi kutoka kwenu. Kabla ya kuja mbele yenu nimeongea na Teacher pale ndani ya gari, amenieleza misukosuko na hatari zilizowakuta, nafurahi kusikia mko salama na hakuna aliyekata tamaa. Ndiyo maana nikatoa machozi baada ya kuwaona mkiwa salama. Teacher amenijulisha pia kuwa leo ni siku ya kufa ama kupona kati yetu na vibaraka wa taifa letu. Pia amenifahamisha kuhusu mama huyu jasiri, ambaye kwa kiasi kikubwa amesaidia kuoko maisha yetu. Asante sana mama”, Kanali Emilly alieleza huku akimshika mkono.

“Hakika, bila Mama Feka pengine taarifa za habari za ndani na nje ya nchi wakati huu zingekuwa zinasimulia habari nyingine kabisa”, Julius Nyawaminza alieleza.

“True. Unachosema ni kweli kabisa”, Claud alirukia.

“Mimi sikutegemea kama mama huyu ataimudu kazi niliyomuomba atusaidie, lakini nilitokwa na hofu aliponidokeza kuwa alipitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa Operesheni Ushindi. Kweli anastahiri kuitwa mshindi”, nilieleza.

“Anastahiri kabisa”, alieleza Kanali Emilly, halafu akaendelea kwa msisitizo. “WAPIGANAJI. Naomba mnisikilize kwa makini sana. Teacher, Julius, Claud, Peter, Mama Feka kama ambavyo Teacher anakuita na Fred ambaye simuoni hapa, Teacher unazo taarifa zozote kuhusu Fred?.” aliuliza kabla ya kuendelea.

“Naam, tunawasiliana, hatuwezi kuwa hapa wote kama wajinga, amenijulisha kuwa yuko pamoja nasi hapahapa karibu kabisa anaangalia usalama wetu, tuko salama bosi”, nilimwambia.

“Oh, vizuri sana. Hii ni mesheni ya aina yake, tujitahidi kwa njia yoyote wahalifu hawa wakamatwe na ushahidi, tusifanye makosa kabisa, sheria za nchi hii zinataka mtu akutwe na ushahidi, ili tushinde vita hii lazima adui akamatwe na kielelezo, yaani hayo madawa ya kulevya yapatikane, vingine tutakuwa tumefanya kazi bure, tutawafikisha mahakamani bila kielelezo?”, Kanali Emilly alihoji baada ya kushauri.

“Tutajitahidi kufanya hivyo. Lakini Afande, kazi kubwa imefanywa na mama huyu shemeji yangu, leo tunaingia vitani wakati yeye hana kumbukumbu za aina yoyote katika kumsaidia endapo itatokea bahati mbaya. Mkuu vita si lelemama, lolote laweza kumpata na muda huu hakuna nafasi tena. Naomba Mama Feka aingizwe katika kumbukumbu zako”, nilimshauri Kanali Emilly akatingisha kichwa kukubaliana na mawazo yangu.

“Hilo halina tatizo kabisa Teacher, kama ulivyotangulia kusema vita si lelemama, tuombe Mungu awasaidie kwa mapenzi yake naamini mtarudi salama, nitafurahi sana kuwaona. Viongozi wote wa serikali wako pamoja nanyi, niwahakikishie tuko pamoja nanyi, niwatakie kila la heri wote”.

“Amina”, tulijibu kwa pamoja.

“Naomba muwe makini na waangalifu sana, Mama Feka?” Kanali Emilly aliita.

“Naam baba”.

“Nimeambiwa wewe ndiye unalifahamu vizuri eneo walilopanga kwa ajili ya kutoroka, saidia tafadhali, msiwape nafasi hata kidogo. Kwa vile muda unakwenda sana sasa niwaache mjipange. Mheshimiwa Rais ameahidi kutoa zawadi nono kwenu”.

“Ni kweli baba, mimi si mwenyeji sana katika Jiji hili, hata hivyo nitajitahidi kuwapeleka. Bahati nzuri ni kwamba huyu mzungu Carlos ananiamini sana, niko kwenye orodha ya wanaosafiri. Naweza hata kuwachelewesha ili tufanikiwe”, alisema.

“Tutajitahidi huku tukimuomba Mungu”, nilisema kwa niaba ya wenzangu wote. Kanali Emilly akasimama baada ya kutushika mikono, akaondoka.

Nilitumia nafasi hiyo kuwajenga vijana wangu kisaikolojia. Baada ya kujiweka vizuri tukajigawa katika makundi mawili tofauti, Peter kama ilivyo ada alianza kuondoka na Mama Feka, akawachukua na vijana wetu kutoka Lugalo, wakaondoka kuelekea eneo la Kunduchi Beach. Mimi Claud Mwita na Julius Nyawaminza tukampitia Fred, tukaanza tukaelekea Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Baada ya kufanikiwa kuuruka mtego wa kukamatwa na vijana shupavu wa Peter Twite pale karakana ya Reli ya Tazara, Carlos Dimera na kundi lake walikimbia na kufanya harakati za kuihama Dar es Salaam. Wakijua mambo sasa yametibuka.

Haraka, Carlos aliwasiliana na Emilio Pablo, kiongozi wa vikundi vya wasambazaji wa dawa za kulevya duniani, bila kupepesa maneno Carlos alimfahamisha kigogo huyo kuwa hali ya hewa ya Dar es Salaam, imegeuka. Akaeleza jinsi walivyopata ushindani kutoka kwa vijana ambao mpaka sasa hawajafahamika.

“Huo ni uzembe wako Carlos, sharti letu unapomkamata adui yako hana budi kuishi hata kwa sekunde moja, maneno gani umefanya. Ok, sasa unahitaji msaada gani zaidi?”, Emilio alihoji.

“Kama nilivyojulisha awali, vijana walifanikiwa kuiba shehena yote ya dawa iliyokuwa imekamatwa na kupelekwa kwa mkemia, mzigo uko salama na sasa tuko katika maandalizi ya kuondoka Dar es Salaam leo mchana kwa boti kubwa sana ambayo tayari iko ufukweni mwa bahari ikisubiri safari.

“Safi, niwapongeze hao vijana kwa kufanikiwa kuufikisha mzigo ndani ya boti salama, lakini unawapeleka wapi, huo ni mzigo kwetu, una hakika mzigo uko salama?’.

“Naam bosi, hilo halina shaka, mzigo uko salama kabisa. kuhusu hao maisha yao yatakoma baada ya kuondoka, Tunaondoka Dar es Salaam mchana tukabiliwa na changamoto moja, Tunaelekea wapi baada ya Dar es Salaam?”. Carlos alihoji. Baada ya kuelezana hili na lile, alikata simu.

Madawa mbali mbali ya kulevya, vifaa kadhaa vya kutengeneza noti bandia, silaha na dhana nyingine zilihamishwa na kuhifadhiwa ndani ya boti kubwa iendayo kasi sana. Boti hii iliyoandaliwa kwa ajili ya safari, kuelekea mahali kusikojulikana. Carlos mwenyewe alipanga kwenda ama Stontown ya Unguja, Visiwani Zanzibar ama Malindi ya Mombasa, nchini Kenya. Lakini pia alijiuliza Zanzibar ni sehemu ya Tanzania, itakuwaje.

Hakuwa tayari kuwaacha vijana wake, lakini agizo la Pablo Emilio ni lazima wateketee, alionekana kuwathamini, kuanzia wasambaza dawa za kulevya na kundi la watakatishaji wa noti bandia. Ukweli ni kwamba aliagizwa na wakubwa kuwatosa katikati ya bahari na kutokomea kabisa.

“Tumefanya makosa makubwa kuruhusu hali hii. Kutoroka kwa Teacher na wenzake ni changammoto kubwa kwetu, niseme kuwa kazi kubwa iko mbele yetu, nani kati yetu amewahi kumuona nyati aliyejeruhiwa?” Carlos alihoji.

“Ni hatari, nyati anapojeruhiwa haangalii Simba wala Chui, usicheze kabisa na Nyati aliyejeruhiwa, anatwanga kila kilicho mbele yake, miti, mawe”, Jakina alieleza.

“Sasa hiyo ndiyo changamoto iliyo mbele yetu. Nyati aliyejeruhiwa ni hatari zaidi ya Chui, ndiyo maana nimeamua tuhame Dar es Salaam kwa muda, upepo mbaya ukipita tutarudi, sawa jamani”, Carlos alieleza.

“Sawa bosi, kama tunaihama Dar es Salaam, tunakwenda wapi?” Hawa Msimbazi alihoji.

“Tunakwenda kuanzisha makazi mapya na maisha mapya kwa muda. Kuhama sehemu moja kwenda sehemu nyingine ni jambo la kawaida. Ndiyo maana nikasema tunaanzisha makazi mapya na maisha mapya, nawaahidi kuishi maisha mazuri zaidi huko. Kama nilivyosema huu ni upepo, ukipita tutarejea”, Carlos alieleza.

“Tuko pamoja nawe bosi Carlos, kila neno lako kwetu ni sheria. hiki ni kikosi chenye nguvu kubwa zaidi ya vikosi vya jeshi. Hata majeshi ya Marekani huhamisha kambi, kama ni silaha tunazo za kisasa na kila aina”. alisema Jakina kwa kujiamini.

Carlos akainua simu yake ya mkononi. “Hallo Sweety wangu, uko wapi baby?. Wakati wa safari umewadia”, Carlos aliuliza.

“Oh baby, bado niko saloon baby wangu, natengeneza nywele, si umesema tunaihama Dar es Salaam leo?. Nipendeze kwanza”, Sweety alijibu kwa sauti ya nyepesi ya mahaba.

“Tumebakiwa na nusu saa tu kuihama Dar es Salaam, mwambie huyo msusi aongeze bidii, usiniangushe Sweety wangu”. Carlos aliagiza.

“Nimemwambia ajitahidi baby”.

“Uko pande zipi?”

“Maeneo ya Riverside saloon ya rafiki yangu”.

“Ok, sasa nisikilize Sweety wangu, ukimaliza tafuta taksi, mwambie dereva akulete Kunduchi Beach Hoteli, ukifika hapo nijulishe nitakupa maelekezo, usiingie ndani ya hoteli”.

“Asante baby, nitajitahidi kuwahi”.

“Ok”, akamaliza.


Ilikuwa saa nane na dakika ishirini hivi nilipoegesha gari kwenye maegesho ya kituo cha mafuta cha GAPCO kando ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi huku tukiangalia barabara iendayo nyumbani kwa Carlos Dimera, Peter na Mama Feka walikuwa wametudokeza kuwa Carlos alikuwa akifanya maandalizi mwisho kwa ajili ya kutoroka. Tulisubiri waanze safari hapo saa nane na nusu kama tulivyoelezwa. Gari la Carlos aina ya BMW nyeusi lilikuwa nje kabisa ya geti na kutufanya tuamini kuwa yupo.

Magari kwenye barabara hii yalikuwa mengi kiasi. Kwenye kituo cha Mafuta cha GAPCO, niliegesha gari sehemu ambayo tuliweza kuona vizuri mwanzo na mwisho mwa barabara hii.

Ilipofika saa sane na nusu kamili, lango la nyumba hiyo lifunguliwa, gari moja ndogo rangi nyekundu Pick Up aina ya Isuzu Deep ilitoka ndani taratibu na kuegeshwa mbele ya gari lililokuwa nje. Jakina alikuwa wa kwanza kutoka ndani akiwa amevalia suti nyeusi. Roho yangu ilianza kuingiwa na hofu, nikajua mapambano na vibaraka hawa yameanza. Dakika chache zikapita, Carlos naye akiwa amevalia suti ya aina kama ile alitoka, wote wawili waliingia ndani ya gari iliyokuwa nje. Jakina aliingia upande wa dereva. Carlos akakaa kwenye viti vya nyuma.

Niliinua simu yangu ya mkononi kuwasiliana na Kanali Emilly, “Kamanda, ndiyo tunaelekea kwenye uwanja wa mapambano, uwe tayari tukikuhitaji ufike kwa wakati, ukituona tena ujuwe tumerudi na ushindi, usipotuone basi, ujuwe makubwa yametupata”.

“”Nimeacha kazi zote kwa ajili ya jambo hili, Teacher kama nilivyosema tulipokutana, Mungu yuko upande wetu, unajua kwa nini?. Kwa sababu tunapigania haki ya wengi”. Kanali Emilly alieleza, kabla hajaendelea nikakata simu.

Magari haya mawili yaliondoka taratibu, gari la mbele lilipokuwa hatua chache kabla ya kufika kwenye barabara kubwa ya Ali Hassan Mwinyi lilisimama na kulifanya gari la nyuma pia kusimama. Vijana wawili walioshiba sawa sawa walishuka juu ya miti wakaingia ndani ya gari la mbele safari ikaanza.

Watu waliokuwa eneo hilo walishangazwa na tukio hilo, lakini sisi tulijua hiyo ni mojawapo ya kazi za majasusi. Tulisubiri mpaka wafike kwenye makutano ya Ali Hassan Mwinyi ama Old Bagamoyo na Kawawa, tukaanza kuwafuata kwa nyuma. Unapowafuata watu wa aina hii lazima ujipange sawasawa, vinginevyo itakula kwako. Tuliwafuata kwa siri, walipofika kwenye taa za usalama barabarani za Morocco walichepuka na kuingia barabara iendayo Kawe.

Mchana huu magari yalikuwa mengi kwenye barabara hii, kiasi kwamba haikuwa rahisi mtu kubaini kama anafuatwa. Baada ya mwendo wa kilomita nne ama tano hivi wakaufikia mzunguko unaogawa barabara zinachepuka moja kwenda Kawe na ile ya Mbezi Beach, gari lao lilipunguza mwendo sana, nadhani walifanya hivi kwa kusudi maalum. Walipovuka kwenye mzunguko huu mbele kidogo walisimama. Mtu mmoja aliibuka akitokea kwenye uchochoro, akazungumza na Carlos. Mimi niliwapita kama siwajui nikasimama mbele ya mtu anayeuza mamatunda kwenye baiskeli. Dakika chache baadaye magari hayo yalitupita tukasubiri kidogo halafu tukaanza kuyafuatana tena.

Tuliendelea kuwafuata kwa makini hadi walipofika kwenye mzunguko mwingine unaogawa barabara tatu, iendayo White Sends Hoteli na Africana. Magari bado yalikuwa mengi kwenye barabara hii, wakati huo mimi nilikuwa nikiendesha gari ndogo aina ya Golf VW Combi iliyoonekana kuchoka kidogo, waliiacha barabara ya kulia inayokwenda White Sends hoteli, wakaifuata inayokwenda Afrikana.

Tuliendelea kuyafuata magari haya kwa umakini wa hali ya juu sana, walipofika njia panda ya Africana waliingia kulia, wakaendelea na barabara ya Tegeta. Tuliendelea kuwafuata hivyo hivyo. Walipofika kwenye makutano ya barabara iendayo Kunduchi, Salasala na Tegeta, eneo la Mtongani, walipunguza mwendo halafu yakachepuka na kuingia tena barabara ya kulia, nami pia nikaingia kwenye barabara hiyo. Baada ya mwendo wa dakika chache, dereva wa gari la mbele alionyesha ishala ya taa kuwa wanaingia kulia.

“Sasa nimeelewa, wanakwenda Kunduchi Beach hawa. hakuna sababu ya kuwafuata tena”, niliwajulisha wenzangu ambao waliokuwa kimya wakijitafakari. Halafu nikawasiliana na Twite. “Mko wapi Peter na vipi hali ya usalama huko?”.

“Mipango inakwenda vizuri bosi, kama tulivyokujulisha Carlos amepiga simu kwa mara nyingine akimwambia Mama Feka ajitahidi kuwahi ili safari yao ianze, sisi tuko sehemu tunasubiri mjipange kwanza, halafu Mama Feka anachukua taksi kama alivyoelekezwa na Carlos, bahati nzuri ni kwamba eneo hilo nalifahamu kiasi, ukiiacha Kunduchi Beach Hoteli, mbele kidogo kuna wafanyabiashara wa samaki wengi sana”, Twite alinijulisha.

“Mwambie Mama Feka avae ile fulana ya bletprof niliyompa, wakati wowote kazi inaanza, mwambie karibu tunaingia kwenye hatari kubwa zaidi, kuna magari mawili yanaelekea hapo, sisi sasa tunasubiri taarifa kutoka kwako”.

“Taarifa kama nilivyokudokeza kuwa eneo hilo kuna wavuvi, vijana wetu Wilson na Edger tayari wako huko kama wachuuzi wa samaki, wanasema ulinzi ni mkali sana kila gari ama mtu anayeelekea huko anachunguzwa, bahati nzuri leo wageni wengi wanaokwenda Kunduchi Beach Hoteli, Wilson anasema mnaweza kuegesha gari kwenye maegesho ya hoteli halafu mkajua cha kufanya.”

“Umesomeka Peter,” nilisema halafu nikawageukia wenzangu, “Jamani, Peter anasema Wilson na Edger wako kwenye pointi. Vijana hawa wanasema ulinzi ni mkali sana eneo hilo, Sisi tutaingia Kunduchi Beach Hoteli, halafu tutatafuta njia zandani kwa ndani, hata ikibidi kuvunja milango na madirisha vita si mchezo”, niliwajulisha wenzangu.

“Iwe isiwe, leo lazima kieleweke, Teacher tusiwape nafasi tena watu hawa ama zao ama zetu”, Claud alisema.

“Nina usongo na watu hawa, walivyotutesa pale Karakana ya Tazara, ole wao waingie kwenye anga zetu”, Nyawaminza nae alisema.

“Sikilizeni, tunakwenda kuuza roho zetu, lolote laweza kutokea, lazima tujipange sawasawa kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. Fred utabaki sehemu hii kama akiba yetu, ukiona kimya utajua cha kufanya, pia wasiliana na Kanali Emilly, mwambie asogee eneo hili. Nyingi wengine twendeni kwenye uwanja wa vita”, niliagiza.

“Tuko pamoja”, Fred alisema.

Baada ya kujipanga vizuri, tulikubaliana na wenzangu kuwa tuliache gari letu kwenye maegesho ya magari ya Chuo cha Maofisa wa jeshi pale Kunduchi, tulikubaliana nianze kuondoka, ili wao wafuate. nilitafuta taksi iliyoniacha Kubnduchi Hoteli. Mkoba wangu mdogo uliosheheni vifaa vyangu muhimu vya kazi ukiwa begani nilitembea taratibu nikitafuta sehemu ya vyoo vya upande wa mashariki, nilipovipata niliingia na kujimwagia maji kiasi, halafu nikafumua sehemu ndogo ya juu ya paa nikapanda na kuangalia eneo lote la bahari.

Hali ya eneo hili ilikuwa tulivu kabisa, kwa mbali ndani ya bahari kulikuwa na meli kubwa na ndogo zimeegeshwa katikati ya bahari, bila shaka zinazosubiri kushusha mizigo bandarini, baada ya kujuiridhisha kuwa hali ni salama nilipenya kwenye tundu hili na kushuka upande wa pili kwa tahadhali kubwa. Claud na Nyawaminza nao wakitumia njia hiyo, wote watatu tukafanikiwa kuruka kiunzi hiki salama.

Ndani ya dakika kumi, tayari tulikuwa tumelizunguka eneo lote la bahari. Boti iendayo kasi ilikuwa imeegeshwa ufukweni ikisubiri kuondoka, ilikuwa boti kubwa ya injini mbili, yele magari na mengine kadhaa yalikuwa yameegeshwa kwa mbali kidogo na boti, “Mwambie Mama Feka anaweza kuja sasa”, nilimwambia Peter.

“Kuko salama?”.

“Ndiyo maana nikasema anaweza kuja”, nilimwambia.

“Nafikiri wote tumeona ulinzi ulivyo. Kitu ninachotaka ni kufanya mashambulizi kimya kwanza mpaka tutakapolazimika kuwashambuliwa walioko ndani ya boti. Walinzi sita wanaonekana upande huu. Mimi nitapita kushoto, Nyinyi mtashambulia upande wa kulia. Nawatakia heri”.

Tulipeana mikono kimya kimya kwani hatukujua nini kitatokea. Mimi nilikuwa wa kwanza kujitokeza kwenye kimsitu nikabana kama hatua tatu hivi kulikuwa na mlinzi anavuta sigara, mikononi ameshika bunduki kubwa aina ya AKA 47 huku akiangalia kwenye magari. Sikuona sababu ya kutoa silaha, nilimsogelea kimya kimya nikitembelea tumbo. Nilipokuwa karibu kabisa niliibukia na kuziba midomo, akataka kupiga kelele lakini mimi nilikuwa mwepesi zaidi nikazima kelele zake kwa kumnyonga.

Tulikuwa tumekwenda haraka sana, Claud alinyoosha mkono wake wa kulia na kunionyesha ishala kuwa hali ilikuwa shwari. wao walipita wakajibanza kwenye mapango ya mawe ya bahari, mimi nikaendelea kutumia miti kuwasogelea tukiona kila kinachotendeka.

Mlinzi mwingine alikuwa hatua kumi hivi lakini hakujua nini kimetokea. Kwa vile nilikuwa nimevaa mavazi ya mtu niliyemuua mwanzo alifikiri mimi ni mwenzao hivyo nilimfuata nikiangalia chini kama mmoja wao mpaka nilipomfikia.

“Vipi kuna wasiwasi wote?”, nilimwuliza.

Aliinua kichwa.

“Hakuna…..”

Kabla hajamaliza nilimkata karate ya katikati ya kichwa akafa palepale. Nilimwegemeza vizuri kwenye mti nikamwacha kama mtu aliyekaa hai. Claud na Nyawaminza nao walikuwa wamekwenda kasi wakiwa wameua walinzi kadhaa.

Tulikuwa tumefanikiwa kuizingira boti hii kutoka kila upande. Mara nikamuona Mama Feka anawasili katika eneo hili, akitembea taratibu kuelekea kwenye boti. Kama ilivyo kawaida Jakina alitoka ndani ya boti ili kumpokea.

Karibu yangu niliweza kuaona walinzi wawili wakilanda huku na huku, nikaanza kuwanyatia. Kabla sijawafikia nilisikia mlio wa risasi upande wa akina Nyawaminza. Nikajua mambo yametibuka. Nami nikainua bunduki AK 47 niliyoichukua kwao na kuanza kuwateketeza walinzi waliokuwa karibu yangu. Kwa kuwa vita vilikuwa vimeanza rasmi nilikimbia nikirusha risasi bila mpangilio.

Hali ya hewa katika eneo hili ilikuwa imechafuka, kumbe kulikuwa na askari wengi ufukweni, sijui hata walitokea wapi tukaanza kupambana, milio ya risasi iliendelea kusikika. Hali hii ilimfanya Mama Feka akimbie kurudi upande wa magari.

Tuliendelea kupambana na watu hawa kishujaa. Mara nikaona askari wawili wakianguka kutoka juu ya miti, bunduki zao zikiwa mikononi. Kumbe walikusudia kunirushia risasi, wakati wanajiandaa kufanya hivyo Claud, alikwisha kuwaona hivyo akawaua kabla hawajanimaliza.

Nilisikia injini za boti zikiwashwa, nikajuwa wanataka kuondoka, nikamfanyia ishara Claud akaiona na yeye akanifanyia ishara ya kuonyesha kuwa Nyawaminza alikuwa chini ya maji anajaribu kuingia ndani boti. Kuona hivyo nilimfanyia ishara kuwa na mimi nakwenda ndani ya boti hivyo atuchunge wote. Tulikuwa tumeuwa idadi kubwa ya askari waliokuwa wamebaki ni wachache tu.

Niliruka chini huku nikiachia risasi ovyo nikafika kwenye boti. Nilikajitupa kwenye mlango na kujiviringisha mpaka ndani, kama umeme nikarukia na kumpiga risasi nahodha wa boti hii aliyekwa kwenye injini akaanguka ndani ya maji. Huko nje nilisikia bado Claud anaendelea kumimina risasi ili kuwazuia walioko ndani wasitoke nje.

Nilipoinuka niliona kama wamebaki kumi tu ndani; wengine wote tulikuwa tumewateketeza. Nilimwona Nyawaminza nae anaviringisha na kuingia ndani. Wale watu walimwona na kabla hawajapiga risasi niliwahi wawili, wengine wote wakarudi kujificha nyuma.

Nyawaminza aliruka mpaka nilipokuwa.

“Asante bosi umeniponya”,

“Usinishukru ndio sababu tuko wote. Kwanza kazi uliyoifanya wewe na Claud sikuitegemea. Kazi imekuwa rahis kabisa”.

“Kuna watu kama wangapi humu ndani?”.

“Hawazidi kumi, na wote wako upande huu wamejificha. Nafikiri wanamlinda Carlos Dimera”.

Huko nje kulikuwa kimya; Tukajua Claud anasubiri sasa kashi kashi kutoka kwetu.

“Sikiliza Nyawaminza, lazima tuwafanyie ujanja ili tuwapunguze. Mimi nitasimama juu ili niwadanganye. Walivyo wajinga watainuka ili wanipige risasi. Mimi nikiita jina kaa tayari na silaha yako kisha anza kumimina risasi. Mimi nitaruka kitambo, hivyo utawapata kama mchezo. usiogope”.

Niliinuka kama umeme nikawaona wote mara moja.

Nikaita

“Carlos Dimera?”.

Hapo hapo kama umeme nikaruka nyuma ya upande mwingine. Walinzi wanne wainuka ili kunitupia risasi huku wakiwa wamejitokeza hadi vifua. Nyawaminza aliwamiminia risasi na kuwashindilia wote risasi katikati ya vifua vyao wakafa pale pale. Nilimwonyesha ya vidole kuwa wamebaki watatu, kwani nilipokuwa nimeruka niliona wako saba.

“Teacher, nilisikia sauti ya Carlos anaita.

“Unasemaje?”, nilimwuliza.

“Naomba tuzungumze”.

“Kuhusu nini tena Carlos, lazima ujuwe kuwa Tanzania haiko tayari kuchezewa, biashara ya dawa za kulevya peleka huko kwenu kusiko na maadili mema katika jamii, watu wanavaa nguo fupi, wanaume wanaoana, hizo imani zibaki kwenu”, nilimwambia.

“Tafadhali tuzungumze?”, aliomba kwa mara nyingine.

“Umechelewa sana Carlos, maana umeigharimu nchi hii, hivyo tutakupeleka mbele ya vyombo vya sheria ndivyo vitakavyo kuhukumu, umeua ndugu zetu wengi, umesababisha vijana wetu kujiingiza katika matumizi ya dawa haramu za kulevya, hufai kuonewa huruma”.

“Huwezi kunichukua hapa nikiwa hai”.

Kumbe wakati huu tunajibishana Mzee wa Mtemba naye na askari wao mwingine nao walikuwa wamejivuta karibu kabisa na mimi. Ghafla nikahisi kuna kitu karibu nami.

“Teacher”, Nyawaminza aliita ambaye pia alikuwa amewaona.

Kusikia tu hivyo, niliruka pale nilipokuwa na wakati huo nikawaona Mzee wa Mtemba na yule kijana mwingine karibu kabisa na mimi wameinua bastola tayari kufyatua. Nilijiviringisha hewani namna ambayo hata wao walishangaa risasi zao zote zikanikosa, wakati ule ule nikaachia za kwangu nikawapata wote nao wakaanguka chini.

Carlos aliinuka akasimama juu, akachukua bastola akataka kujipiga risasi. Bunduki tatu zililia kwa wakati mmoja na kuupiga mkono wake. Kumbe Claud nae alikuwa amefika mlangoni na kuona kitendo alichotaka kukifanya akakizuia. Nyawaminza nae aliona akazuia wakati na mimi niliona nikazuia asijipige risasi.

“Bado tunakutaka ukiwa hai ili ukajibu maswali ya watanzania”, nilimwambia huku bado anashangaa jinsi risasi tatu zikitoka pande tofauti zilivyoweza kupiga kiganja chake tu.

Mara tunasikia kelele za milio ya magari ya polisi.

“Kanali Emilly yuko njiani”, niliwaambia wenzangu ambao sasa tulikuwa tumemzunguka Carlos.

Baada ya mapigano makali yaliyodumu kwa saa kadhaa, tukibishana kwa risasi na watu hawa, hatmaye tulifanikiwa kuiteka boti hii, Carlos Dimera, Hawa Msimbazi, Jakina, Mzee wa Mtemba na baadhi ya masalia ya askari wao walijisalimisha mbele yetu.

Mama Feka alikuja na kunikumbatia, “Hongera sana Teacher, kazi yenu mliyonituma nimeimaliza”, alisema huku akinibusu na kujiegemeza kwenye kifua changu, nikambusu pia. carlos Dimera na wenzake wakabaki wameduwaa.

“Mnamfahamu malkia huyu, anaitwa Sweety, bila huyu kazi ya kuwakamata ingekuwa ngumu, asante sana Mama Feka”, nilisema.

Kanali Emilly alifika akiwa na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu Serikalini, Mawaziri wa Ulinzi na Mambo ya Ndani, pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo. Kanali Emilly alitushika mikono na kutuangalia sehemu mbali mbali za miili yetu kama tumepatwa na majeraha. Tulikuwa salama kabisa.

“Wakuu, boti hiyo imebeba vifaa vyote vya hujuma, kuanzia dawa za kulevya, vifaa vilivyotumika kutengeneza noti bandia na baadhi ya silaha za vita ambazo hatujui ziliingiaje hapa nchini”, nilieleza kwa uchungu.

Baada ya taratibu zote kufanyika, askari kutoka idara zote tuliwaacha wazee waendelee na mambo yao sisi tukaondoka kishujaa.

MWISHO

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment