Operation Gothic Serpent Sehemu ya Kwanza
MEANDIKWA NA: THE BOLD
*********************************************************************************
Simulizi: Operation Gothic Serpent
Tarehe fulani isiyojulikana mwaka 1993 – Sudan
“…ndugu zangu nyote katika imani, popote mlipo dunia. Wote tumeshuhudia udhaifu wa adui yetu. Wote tumeshuhudia kudhalilika kwa Marekani. Hili ni onyo, na huu ni ujumbe kwao. Kwamba tutawapiga tena, na tena na tena mpaka siku tutakapowafuta juu ya uso wa dunia au siku watakapo ongoka na kumuamini Mwenyezi Mungu. Huu ni ushindi kwetu sote na ishara ya kwamba adui yetu ni dhaifu. Nawataka wapigania imani wote, popote mlipo duniani, endeleeni kuwa na moyo mkuu. Adui yetu ni dhaifu, tumpige tena na tena na tena..”
– Sauti ya Osama Bin Laden katika moja ya rekodi zilizokuwa zinasambazwa kwa vikundi vya wapiganaji wenye msimamo mkali.
Nchini Marekani mwaka huo huo 1993
Wananchi wa Marekani walikua wamemka na habari ya kushtua. Vyombo vyote vya habari vilikuwa vimetawaliwa na habari juu ya kujiuzulu kwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani Bw. Les Aspin.
Ilikuwa ni habari ya kushitusha kuzingatia kwamba nchi bado ilikuwa imefunikwa na giza kutokana na kifo cha idadi kubwa ya wanajeshi wake barani Afrika.
Wakati huo huo rais Bill Clinton alikuwa kwenye mvutano mkubwa na Umoja wa Mataifa juu ya muelekea wa hali ya amani nchini Somalia. Bill Clinton akitaka kuondoa wanajeshi wake haraka huku Umoja wa Mataifa wakitaka Marekani kusubiri kidogo ili kuongoza oparesheni ya kuondoa wanajeshi wengine wote wa UN waliopo nchini humo.
Mogadishu, Somalia – Pembe ya Afrika
Mamia ya wananchi walikuwa wameandamana. Si kwamba walikuwa wameandamana kupinga jambo fulani au kuhamasisha suala fulani, la hasha… maandamano haya yalikuwa ni ya kusheherekea. Walikuwa wanasheherekea huku wakiwa na ‘trophy’ mbele yao. Mwili wa binadamu aliyekufa ambao walikuwa wameufunga kamba wakiuburuza mitaani wakiwa wameuvua nguo zote mwili huo. Tofauti na muonekano wa waandamanaji hawa ambao wengi walikuwa wembamba na weusi na sura za kuchongoka, mwili huu waliokuwa wanauburuza ulikuwa ni wa mtu mweupe, mzungu. Ulikuwa ni mwili wa mwanajeshi wa Marekani, mmoja wa mwanajeshi wa weledi ambaye alikuwa kwenye chopa ya kivita ya ‘Super Six Four’.
Ulimwengu wote ulikuwa kana kwamba umesimama na macho na masikio yote yalikuwa yameelekezwa nchini Somalia. Hakuna ambaye alikuwa anaamini kilichotokea. Hata Marekani wenyewe hawakutegemea kutokea kitu ambacho walikuwa wanakishuhudia.
Siku hii imeingia katika historia ya jeshi la Marekani kama moja ya siku chungu zaidi ambazo waliwahi kupitia. Ni siku ambayo kwa mara ya kwanza tangu kuisha kwa vita ya Vietnam, wanajeshi wa Marekani ndipo walipokabiliwa na mapigano mazito ya ana kwa ana na adui.
Lakini pia siku hii itufundisha kitu adhimu sana… kwamba hasira, imani na itikadi inauwezo wa kupambana dhidi ya weledi na ushujaa wa hali ya juu na ikashinda.
Genesis
Katika miaka ya 1986 Rais wa Somalia wa kipindi hicho, Mohammed Siad Barre alipata ajali ya gari katikati ya mji wa Mogadishu. Ajali hii ilitokana na upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa ambao ulisababisha gari ambayo ilikuwa inatumika kumsafirisha kwenda kujibamiza nyuma ya gari kubwa la usafiri wa umma. Rais Barre alipata majeraha makubwa sana, hasa hasa kichwani na pia alivunjika mbavu kadhaa. Ilibidi asafirishwe kwenda kutibiwa nchini Saudi Arabia kwa ajili ya matibabu.
Kwa miezi kadhaa ambayo Rais Barre alikuwa kwenye matibabu nchini Saudi Arabia, Jenerali Mohamed Ali Samatar ambaye alikuwa makamu wa Rais ilibidi akaimu nafasi yake na kuongoza nchi kama Rais wa Somalia.
Katika nyanja za siasa na masuala ya madaraka nchini humo kukaanza kuibuka minong’ono ya kutaka apatikane mrithi wa Urais wa Somalia. Barre alikuwa ameitawala Somalia kwa kipindi kirefu sana, umri wake ulikuwa umeenda mno na pia watu walikuwa na shaka na uimara wa afya yake.
Hata kipindi ambacho Rais Barre alitibiwa na kurejea kwenye afya njema na kurudi nyumbani Somalia, bado minong’ono iliendelea ya kutaka apatikane mrithi wake.
Ili kuonyesha kwamba yuko ngangari, Rais Barre aligombea tena Urais mwaka 1986, Mwezi desemba na kushinda ikimaakisha kwamba alipata muhula mwingine wa miaka saba wa kuendelea kuwa Rais wa somalia.
Lakini minong’ono haikuisha. Watu walitaka mrithi apatikane. Walitaka sura mpya kwenye uongozi wa nchi.
Na katika minong’ono hii kuliibuka majina mawili ambayo yalikuwa yanatajwa tajwa sana. Jina la kwanza lilikuwa la Jenerali Mohamed Ali Samatar, makamu wake wa Rais. Jina la pili lilikuwa la waziri wa Mambo ya Ndani Jenerali Ahmed Suleiman Abdille ambaye alikuwa ni mkwewe Rais Barre aliyemuoa moja ya binti yake.
Lakini kama ilivyo kwa madikteata wote duniani, kunapotokea tishio la madaraka yao kupokwa ni kana kwamba wanapata wehu. Rais Barre alianza kuwa dikteta katili akiwafunga na kuua wapinzani wake na wote ambao walikuwa wanaonekana kuwa na mwelekeo wa kumpinga.
Rais Barre woga wa madaraka kumponyoka ulioanda kwenye akili yake. Aliacha mpaka kusikiliza ushauri wa baraza lake la Mawaziri na badala yake aliongoza nchi kwa kuhusisha watu wachache sana ambao alikuwa anawaamini.
Kama ilivyo ada, watawala wakizidisha ukatili ndivyo navyo moto wa upinzani dhidi yao unavyozidi kukolea. Kwa hiyo Rais Barre sasa alikuwa anapingwa wazi wazi, ndani na nje ya Somalia.
Lakini kama tujuavyo kwamba nchi ya Somalia ina mgawanyiko mkubwa sana wa koo. Kwamba kuna uadui wa miaka mingi sana baina ya koo tofauti nchini humo. Rais Barre alianza kutumia mwanya huu wa uadui wa koo ili kuwaweka baadhi ya koo upande wake na wengine akiwapambanua kama koo adui kwa Taifa la Somalia.
Tunafahamu kwamba katika kipindi hiki ‘Derg’ ilikuwa na ushawishi mkubwa sana katika nchi zilizoko kwenye pembe ya Afrika. Derg ni kamati ya uongozi wa kijeshi ambao walisimamia kuondolewa madarakani kwa Mfalme Haile Selassie. Wao ndio waliokomesha utawala wa Kifalme nchini Ethiopia.
Japokuwa Rais Barre alikuwa anafanya uovu nchini kwake Somalia, lakini Mengistu Haile Mariam, kiongozi wa Derg huko Ethiopia alichukizwa mno. Ndipo hapa akaanza kuunga mkono vikundi vya wapiganaji wa kisomali ambao walikuwa wanataka Rais Barre aondoke madarakani.
Rais Barre hakuwa na simile… alitumua jeshi na silaha nzito kupambana na adui zake. Kufumba na kufumbua maeneo ya kaskazini mwa Somalia ambao ndiko hasa upinzani dhidi yake ulikuwa mkubwa, kuligeuka uwanja wa vita.
Hali hii ya nchi kuingia kwenye machafuko iliwahuzunisha sana watu wengi wazalendo na wenye ushawishi ndani ya Somalia akiwemo Rais wa kwanza wa nchi hiyo Aden Abdullah Osman Daar. Osman Daar aliongoza wanasiasa wengine wapatao mia moja wenye ushawishi mkubwa nchini humo kusaini waraka maalumu wenye kumtaka Rais Barre afanye suluhu na vikundi vya wapiganaji.
Kama wasemavyo kwamba sikio la kufa halisikii dawa. Rais Barre hakutaka kusikiliza rai hii ya wanasiasa wenzake wakongwe. Aliendeleza ukatili dhidi ya wote ambao walikuwa wanampinga na mapambano dhidi ya vikundi vya wapiganaji yalipamba moto.
Mapambano haya kati ya majeshi ya serikali na vikundi vya waasi yalidumu kwa miaka kadhaa.
Kadiri muda ulivyokuwa unaendelea ndivyo ambavyo majeshi ya Rais Barre yalikuwa yanazidiwa nguvu.
Mpaka kufikia katikati ya mwaka 1990 majeshi ya serikali yalikuwa yamezidiwa nguvu kwa kiasi kikubwa sana. Waasi walikuwa wametwaa sehemu kubwa ya vijiji na mitaa inayozunguka mji mkuu wa Mogadishu. Ndipo hapa ambapo watu walimbatiza jina la utani Rais Barre kwamba ni ‘Meya wa Mogadishu’, wakimanisha kwamba ni eneo la Mogadishu ndilo pekee ambalo Barre alikuwa na mamlaka nalo na maamuzi kutokana na vikundi vya waasi kutawala maeneo mengine yote ya nchi na Raias alikuwa hawezi hata kutoka nje ya mji huo.
Mwezi desemmba mwaka huo 1990 waasi wa USC (United Somali Congress) waliingia ndani ya mji wa Mogadishu wakiingozwa na Jenerali Mohamed Farah Aidid. Baada ya kuingia zilifuata wiki nne za mapigano makali kati ya USC na jeshi la rais Barre.
Mpaka kufikia mwezi January, wapiganaji wa USC walikuwa wamefanikiwa kuyashinda majeshi ya Rais Barre na hatimaye kumuondoa Barre mwenyewe madarakani.
Shida nyingine ikaibuka…
Nilieleza hapo nyuma kidogo kwamba Somalia wana mgawanyiko mkubwa na uadui wa koo. Kwa hiyo hata baada ya vikosi vya USC kumshinda Rais Barre na kumuondoa madarakani, koo nyingine zilikataa kumtambua Jenerali Farah Aidid kama kiongozi mpya wa Somalia. Matokeo yake vikundi hivi vya waasi vikaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe. Kila kikundi kikipigania kutawala eneo fulani.
ITAENDELEA
Operation Barras Sehemu Sehemu ya Pili
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;