Operation Entebe Sehemu ya Tatu
MEANDIKWA NA : THE BOLD
*********************************************************************************
Simulizi : Operation Entebbe
Sehemu ya Tatu (3)
Baada ya kuwatenganisha raia wote wa Israel na kuwaweka kwenye chumba kingine peke yao hapo hapo kwenye terminal, kuna mwanadada raia wa Ufaransa aliyeitwa Jocelyne Monier yeye jina lake halikuitwa kwenye ile list ya wanaotakiwa kutengwa kwenye chumba kingine (Waisrael na Wayahudi). Lakini ‘boyfriend’ wake alikuwa ni Muisrael na aliitwa jina na kutengwa na wengine katika kile chumba kingine. Mwanadada huyu ili kuonyesha kumtia moyo mpenzi wake na kupinga huu ubaguzi uliokuwa unafanywa na hawa magaidi, kwa hiari yake alijipeleka kwenye chumba cha mateka wa Kiisrael. Si mwanadada huyu pekee ambaye alifanya kitendo hiki cha ushujaa, lakini pia kulikuwa na mwanamama mwingine aliitwa Janet Almog (rai wa Marekani) na mateka mwingine aliyeitwa Jean-Jacques Mimouni (raia wa Ufaransa) nao kwenye kuonyesha hali ya kuwaunga mkono wenzao waliotengwa kwenye chumba kingine na kupinga ubaguzi uliokuwa unafanywa na maharamia hawa, nao walijipeleka kwa hiari yao kwenye chumba ambacho mateka hao walikibatiza jina “Chumba cha Waisrael”, ambacho mateka wote walijua fika kwamba kuna jambo baya maharamia hao walikuwa wamepanga kulifanya.
Licha ya maharamia kwa kushirikiana na jeshi la Uganda kufanya uchambuzi huu wa kina kuhusu uraia wa kila mateka waliye naye, lakini walifanya kosa kubwa sana ambalo lilkuja kuwagharimu sana hapo baadae. Kwenye uchambuzi wao wote huu walioufanya walishindwa kumng’amua mateka mmoja mwanajeshi wa Israel ambaye alikuwa ana uraia pacha na siku hiyo alikuwa anatumia passport ambayo sio ya Israel. Mateka huyu alikuja kuwa muhimu sana huko mbeleni kuwapatia Mossad Intelijensia mujarabu kabisa kuhusu watekaji, jengo wanaloshikilia mateka, na namana wanavyoshirikiana na jeshi la Uganda.
Siku iliyofuata yaani June 30, maharamia haya wakawaachia mkupuo wa kwanza wa mateka wasio raia wa Israel au wayahudi. Katika mkupuo huu wa kwanza waliachia mateka 48 ambao walikuwa ni wazee, watoto na akina mama wenye watoto wadogo.
Baada ya mkupuo huu wa kwanza wa kuwaachia mateka hawa wachache, maharamia wakaweka wazi matakwa yao ili waweze kuachia mateka wengine. Kwanza kabisa walitaka walipwe fedha kiasi cha dola za Kimarekani milioni 5. Na pili walitakakuachiwa kwa wafungwa 53 wenye asili ya kipalestina wanaotuhumiwa kwa ugaidi, ambao kati yao 40 walikuwa kwenye jela za Israel na 13 katika nchi nyingine za Ulaya. Watekaji hawa wakatoa ‘ultimutum’ kwamba kama matakwa yao hayatatekelezwa ndani ya masaa ishirini na nne yajayo (mpaka tarehe 1 July saa 8 mchana) basi wataanza kuua raia wa Israel mmoja baada ya mwingine.
Dunia nzima ni kama ilisimama kwa masaa kadhaa kutokana na sintofahamu iliyogubika kila mahali. Sintofahamu hii ililetwa na ukweli kwamba, ilikuwa inajulikana wazi kwa miaka yote kwamba Israel wana sera ya kutofanya mazungumzo au makubaliano na Magaidi. Kwahiyo kila mtu alikuwa nafahamu kuwa kuna uwezekano mkubwa ndani ya masaa 24 yajayo ulimwengu ukashuhidia watu zaidi ya 200 wakichinjwa kama kuku.
amin-aiport-jpg.524097
Rais Idd Amin akiwa uwanja wa ndege “kuwasalimu” mateka
NCHINI ISRAEL: KIKAO CHA BARAZA LA MAWAZIRI
Nchini Israel kikao cha dharura cha baraza la mawaziri kilikuwa kimeitishwa na waziri Mkuu Yitzhak Rabin kujadili kuhusu hatua za kuchukua kuokoa raia wake ambao wameshikiliwa mateka huko uwanja wa ndege wa Entebbe, Uganda.
Hali ya kikao ilikuwa tete sana kutokana na kila dakika waliyokuwa wanaitumia kujadili ndivyo ambavyo walikuwa wanaikaribia saa 8 mchana ya tarehe 1 July. Walipowasilana na Ujerumani na Ufaransa ambao nao walikuwa na baadhi ya wafungwa wa Kipalestina ambao watekaji walitaka waachiwe… walipowaomba ushirikiano wao kuhusu kukabali kuachia hao wafungwa, Ujerumani na Ufaransa walikataa katakata kuachia hata mfungwa mmoja wa Kipalestina ambaye alikuwa kwenye magereza zao.
Sintofahamu ilizidi kuongezeka. Masaa yalizidi kuyoyoma. Saa 8 mchana ya tarehe 1 July ilizidi kukaribia. Harufu ya damu ilikuwa inabisha hodi mlangoni kwao. Licha ya weledi wao wote walionao lakini mbele yao waliona giza.
Inapaswa kukumbukwa kwamba Idd Amin aliwahi kupatiwa mafunzo ya weledi wa kijeshi nchini Isarel (Special Force Training). Kwa hiyo baraza la mawaziri likamuagiza Baruch Bar-Lev, kamanda mstaafu wa IDF ambaye alihusika kumpatia mafunzo ya kijeshi Amin kipindi yuko Israel na kufanikiwa kujenga naye ukaribu. Baraza la Mawaziri likamuagiza Baruck (marafiki zake humuita “Burka”) kufanya mawasiliano na Rais huyo wa Uganda ili kujaribu kumuomba awashawishi magaidi wanaoshikilia mateka kwenye uwanja wake wa ndege wa Entebbe wawaachie mateka hao bila masharti magumu.
Kupitia kwa Burka, Israel ilifikia mpaka hatua ya kumuahidi Idd Amin kuwa kama atafanikisha kuachiwa kwa mateka hao basi watatumia ushawishi walionao kuhakikisha kuwa Amin anatunukiwa tuzo ya amani ya Nobel.
Lakini Amin hakulegeza msimamo, akaendelea kuwasisitiza kuwa hakuna namna nyingine yeyote ambayo mateka hao wataachiwa bila masharti yaliyotolewa na watekaji kutimizwa.
Baada ya juhudi hii ya kumuhonga ‘tuzo’ kugonga mwamba, Waziri Mkuu wa Israel akawasiliana na serikali ya Marekani na kuwaomba wamshawishi Rais wa Misri Anwar Sadat ambaye alikuwa anaheshimiana sana na Amin ili amshawishi kuwaamuru magaidi yaliyoko uwanjani kwake Entebbe waachiemateka bila masharti magumu.
Amin bado akashikilia msimamo kwamba hakuna mateka atakayeachiwa pasipo masharti yaliyotolewa kutimizwa.
Juhudi hizi za kumshawishi Amin zilikula muda mwingi sana na hatimaye wakajikuta tayari kulikuwa kumekucha asubuhi. Mbele yao kulikuwa kumebakia masaa chini ya manane kabla ya damu ya zaidi ya watu 200 kumwagika.
ITAENDELEA
Operation Entebe Sehemu ya Nne
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;