Operation Gothic Serpent Sehemu ya Nne
MEANDIKWA NA: THE BOLD
*********************************************************************************
Simulizi: Operation Gothic Serpent
Sehemu ya Nne (4)
Nilieleza kwamba mtindo wa ushukaji kwenye chopa ulikuwa ni fast roping. Stadi hii ya fast roping niliieleza kwa uzuri sana nilipoandika makala kuhusu Operation Barras iliyotekelezwa na SAS ya Uingereza kuokoa wanajeshi wao nchini Sierra Leon.
Ni kwamba… katika stadi hii, chopa ya kijeshi inaruka chini chini kabisa karibu na ardhi au paa la jengo (mara nyingi umbali wa futi 70 (mita 21) kwenda juu) na kisha kamba zinaning’inizwa kutoka kwenye chopa na kisha makomando wanatumia kama hizi kushuka kwenye chopa na kutua ardhini au juu ya paa. Lakini ushukaji wake ni wa kasi kubwa, kana kwamba wanateleza kwenye ile kamba. Hiyo ndio fast roping.
Sasa chopa hii ambayo rubani alikosea na kwenda kwenye jengo lingine kaskazini mwa jengo husika… wakati chopa ya Black Hawk iko futi 70 kutoka ardhini na makomando wakiwa wana-fast rope… kwa bahati mbaya, komando mmoja, Todd Blackburn hakushika kamba sawa sawa wakati anashuka na akajikuta amedondoka chini ardhini umbali wa futi 70 kutoka angani. Ajali hii ilisababisha Todd kuumia vibaya kichwani na kuvunja shingo.
Wakati makomando wakijaribu kumpa huduma ya kwanza mwenzao, rubani aligundua kwamba amewashusha kwenye jengo ambalo si sahihi… ikabidi awaambie hili makomando kwa kutumia vinasa sauti masikioni mwao… kwamba ashushe chopa chini ili awapakie na kuwapeleka kwenye jengo husika na kumrudisha Todd kambini kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kidaktari.
Lakini makomando wakakataa pendekezo hili la rubani kushusha chopa kwa kuhisi kwamba huo mlolongo wa chopa kutua chini, wapande, wampakie Todd na kisha chopa iruke tena itachukua dakika nyingi na watakuwa exposed kwa muda mwingi kuliko kawaida na wanaweza kushambuliwa. Kwa hiyo wakamruhusu rubani wa Black Hawk aondoke wakisema kwamba watambeba mwenzao na kurudi nyuma kwa weledi mpaka kwenye jengo husika na ule msafara wa magari ukiwasili watampakia mwenzao.
Rubani akaondoa chopa yake hewani akiwaacha ‘Chalk Four’ pale chini kwenye jengo ambalo si sahihi. Makomando wa Chalk Four wakanza kujiandaa kuanza kurudi nyuma kwa tahadhali na weledi kuelekea jengo husika wanakotakiwa kuwa.
Lakini ghafla walisikia mfululizo wa mvua za risasi kuja upande wao… risasi mfululizo kana kwamba kuna watu wanajaribu ‘kuwa-pin’ wasielekee kule wanakotaka kwenda.
Walibakia wameduwaa wasijue nini kilikuwa kinatokea. Hawakutegemea hili… hawakuelewa nini kinatokea… mvua za risasi zilirindima mfululizo bila kukoma. Walijaribu kujibu mapigo… lakini kadiri walivyokuwa wanajibu mapigo ndivyo ambavyo walikuwa wanazidi kuchelewa kuwepo kwenye eneo wanalotakiwa kuwa, kutengeneza perimeter kwenye jengo walilomo washirika wa Aidid.
Bundi alikuwa ametua kwenye oparesheni… walikuwa wanatakiwa kufikiri haraka na kutumia weledi wao wote kujinasua hapa na pia kuwahi kwenye jengo wanalotakiwa kuwemo kwa sababu kuchelewa kwao kulikuwa kuna hatarisha maisha ya wenzao makomando wa Delta Force walioko kule ndani ya jengo ambako wanawakamata washirika wa Aidid.
Nitarejea… stay here!
OPERATION GOTHIC SERPENT; NGUVU YA IMANI, ITIKADI NA USHUJAA ULIOTUKUKA
SEHEMU YA NNE
Baada ya chopa kushusha makoamndo wa ranger ilianza safari kurejea kwenye base kama ambavyo nilieleza kwenye sehemu iliyopita. Nilieleza pia kwamba makoamndo wa ‘chalk four’ walishushwa kwa makosa majengo kadhaa kaskazini mwa jengo husika. Pia wakiwa wanashuka kutoka kwenye chopa mwenzao mmoja alidondoka wakati wa kushuka ardhini kwa kamba na kuumia vibaya. Wakiwa wanajaribu kurudi nyuma kwenda kwenye jengo husika ghafla walianza kushambuliwa mfululizo.
Hii ilisababisha chopa ambayo iliwashusha kutorudi kambini moja kwa moja badala yake watumie muda mchache kutoa ‘fire support’ dhidi ya maadui ambao walikuwa wanashambulia makoamndo wao pale chini. Wakati chopa hii ya Super 61 (inatamkwa super-six-one) ikifanya mashambulizi dhidi ya adui ili kuwawezesha makoando wa chalk four warudi kwenye jengo husika, ghafla chopa hii ilidunguliwa na bomu la RPG.
Ndani yake ilikuwa na makomando wane, wawili wakiwa marubani na wawili ‘snipers’ wa Delta ambao ndio walikuwa wanashambulia adui kule chini. Marubani wale wawili walipoteza maisha pale pale baada ya chopa kudondoka lakini wale makoamndo wadunguaji wawili walisalimika licha ya kupata majereha makubwa. Baada ya chopa kudondoka tu, wapiganaji wa Kisomali walianza kusogelea wakiwa katika makundi. Iliwabidi makomando ambao walisalimika kuendelea na mapambano ya kujibizana kwa risasi licha ya kuwa katika hali mbaya kutokana na ajali kudondoka na chopa.
Taarifa hii ilitumwa haraka kwenye chopa nyingine ambazo zilikuwa karibu na eneo hili la tukio. Mara moja chopa aina ya MH-6, Star 41 ikiwa na makomando wawili CW3 Karl Meir na CW5 Keith Jones ilitua karibu na eneo ambalo chopa ya Super 61 ilidondoka kwa ajili ya kutoa usaidizi. Moja ya vitu ambavyo ni tunu ya jeshi lolote duniani ni utii, lakini kuna wakati ambao mwanajeshi ili aweze kutimiza azma yake na kufanya ushujaa kwa nchi yake pengine anapaswa kuvunja tamaduni huu wa utii. Hiki ndicho ambacho kiliwasibu makomando Jones na Meir baada ya kutua na chopa yao eneo ambalo super 61 ilidondoka. Kwanza kabisa kamanda wao alikuwa anawapa amri kwenye radio kwamba wasitue chini hapo na hiyo chopa. Lakini iliwabidi kukaidi na kutua chini. Baada ya kutua tu Jones aliruka kutoka kwenye chopa na kwenda kuwahamisha wale makomando wawili wa super 61 ambao walikuwa wamejeruhiwa vibaya na kuwasogeza sehemu salama. CW3 Meir alibakia pale ambapo chopa yao ilitua akijibizana mapambano ya risasi na wasomali ambao walikuwa wanamiminika kwa kasi eneo hilo.
Juu angani kulikuwa na ‘surveillance helicopter’ ambayo ilikuwa inafuatilia utekelezaji wa oparesheni nzima. Wakiwa huko juu waliweza kuona makundi ya wasomali kwa mbali wakimiminika kuelekea eneo ambalo super 61 ilidondoka. Ndipo hapa ambapo ilitolewa amri kwa CW3 Meir kuwa arushe chopa kutoka pale walipo kwani muda mchache ujao kuna uwezekano wakazidiwa nguvu kutokana na wingi wa wasomali ambao walikuwa wanakuja eneo hilo. Lakini kama ambavyo nilieleza kuwa Meir ndiye pekee ambaye alibaki chopa ilipo, mwenzake CW5 Jones alikuwa anawahamisha makoamndo walionusurika kwenye Super 61 na kuwaweka eneo salama. Kwa hiyo baada ya Meir kupewa amari hii kuwa arushe chopa angani mara moja, alikaidi amri hiyo kwa hoja kwamba hawezi kurusha chopa na kumuacha mwenzake pale chini.
Majibizano ya risasi yaliendelea pale chini, Meir akijitahidi kupambana na wasomali walikuwa wanawasili eneo hilo huku Jones akiwaficha makoamndo wa super 61 na kuwapatia huduma ya kwanza.
Ramani ya mji wa Mogadishu kuonesha sehemu ambayo operation ilifanyika na mahala ambapo Super 61 na Super 64 zilidondoka
Wakati vurumai hili likiendelea ukatokea uzembe wa hali ya juu sana. Nilieleza kwamba katika mkakati huu, makomando walikuwa wanapaswa kufikishwa kwenye jengo lengwa kwa kutumia chopa na baadae msafara wa magari ya kijeshi utawachukua wakiisha kumaliza oparesheni na kuwarejesha kambini.
Lakini baada ya kutokea ajali hii ya chopa ya Super 61 kila mtu alikuwa ameshikwa na taharuki akili zote wakiwa wamezielekeza kwenye namna gani wanaweza kufanya uokozi wa wenzao hao ambao walikuwa wameanguka na chopa.
Hii ilisababisha kutokea kwa mkanganyiko wa mawasiliano. Kuna wale makomando ambao walifanikiwa kushushwa kwenye jengo sahihi lengwa na kuingia ndani na kukamalisha oparesheni, walijikuta wanasubiria mawasiliano kutoka kwa makomando walioko kwenye msafara wa magari ili waweze kuondoka wakati huo huo kumbe wale makoamndo walioko kwenye msafara wa magari nao walikuwa wanasubiri wasikie neno kutoka kwa makomando walioko ndani ya majengo ili waweze kuchukua hatua.
Kwa hiyo kwa namna fulani oparesheni ilikuwa kwenye mkwamo wa ghafla pasipo wenyewe kujua.
Makundi ya wapiganaji wa Kisomali walikuwa yanazidi kujongea kuelekea mahala ambako chopa ya Super 61 ilikuwa imedondoka.
Katika muda huu huu kulikuwa na chopa nyingine ya Super Six Four ambayo nayo ilitumika kushusha makomando eneo lile la awali la jengo lengwa. Kwa muda huu Super 64 ilikuwa upande wa kaskazini mwa mji wa Mogadishu ikijiandaa kurejea kambini. Lakini kabla hajafanya hivyo walipokea mawasiliano kwenye radio kuhusu kudondoka kwa Super 61 ikiwa na makomando wanne ambao wawili walifariki pale pale na wawili ndio wale ambao walibakia. Pia walipewa taarifa juu ya kutua kwa chopa ya MH-6, Star 41 ikiwa na makoamndo CW3 Karl Meir na CW5 Keith Jones ambao walienda kutoa usaidizi.
Pia makomando hao ambao walikuwa ndani ya Super 64 walisikia taarifa juu ya makundi ya wapiganaji wa kisomali ambao walikuwa wanamiminika kwa kasi kwenye eneo la tukio ambalo Super 61 ilikuwa imedondoka.
Mara moja pasipo kujiuliza au kufikiria mara mbili mbili, Super 64 ndani yake ikiwa na makomando wane, Tommy Field, Bill Cleveland, Ray Frank ambaye alikuwa rubani msaidizi na Mike Durant ambaye alikuwa rubani mkuu.
Kwa hiyo chopa ya Super 64 ikageuza na kuelekea kwenye eneo ambalo Super 61 ilikuwa imedondoka. Tukumbuke kwamba mpaka muda huu pale chini kulikuwa na jumla ya makomando wanne wa Kimarekani, wawili ambao walisalimika kwenye ajali na wawili ambao walikuja kuwaokoa. Lakini pia kwenye eneo la karibu yao kulikuwa na makundi ya wasomali ambao walikuwa wanajitahidi kuwasogelea wale makoamndo pale chini ambako Chopa ilikuwa imedondoka. Kwa hiyo kule juu angani ambako Super 64 ilikuwa imewasili ilikuwa inawawia vigumu sana kutofautisha na kuwachambua kwa usahihi zaidi mahali ambako adui wapo na namna ambavyo wanaweza kufanya shambulizi bila kuwadhuru makomando wao ambao nao wako kule chini.
Kwenye chopa makomando walikuwa na ‘mini-guns’ ambazo zina uwezo wa kufanya shambulio zito la risasi elfu nne ndani ya dakika moja. Kwa hiyo walitakiwa kuwa makini haswa kabla hawajafanya uamuzi wowote wa kuanza kufyatua risasi. Kwa dakika kadhaa chopa ya Super 64 ilifanya mzunguko kule juu kujaribu kutenganisha walipo adui na walipo makomando wao. Wakiwa kwenye mizunguko hii ya kulizunguka eneo ili waweze kufanya uamuzi sahihi wa kushambulia, ghafla walisikia mtikisiko mkubwa kana kwamba unaendesha gari kwa kasi kubwa na kugonga tuta bila kujua… helikopta ilisukumwa juu kwa nguvu. Kuna kitu kizito kiligonga kwenye mkia wa chopa na kulipua ‘tail rotor’ na ‘gear box’ papo hapo kwa haraka.
Japo bomu lilipuka baada ya kugonga mkia wa chopa, lakini mkia haukukatika moja kwa moja badala yake baada tu ya kulipuka ilianza kufanya chopa kupoteza uelekeo na kuanza kuzunguka kwa kasi huku ikishuka chini. Rubani Mike Durant aalifanya uamuzi wa haraka wa kuzima injini zote labda kusaidia chopa isizunguke kwa kasi na labda aweze kutua chini salama, lakini ilikuwa ni kana kwamba ametia mafuta ya taa kwenye moto wa kifuu, chopa ilianza kushuka chini kwa kasi kubwa na kujipigiza chini ardhini. Bahata nzuri tu ni kwamba… mfano chopa inavyoshambuliwa kama hivi na kupoteza muelekeo, ukizima injini walau unkuwa na uwezo wa kudhibiti uelekeo wake japo unakuwa bado hauna uwezo wa kuifanya isidondoke… hii ilisaidia chopa ya Super 64 kudondoka chini kwa muelekeo mzuri (matairi chini kama inatua kawaida) badala ya kudondoka kiubavu uvavu au juu chini.
ITAENDELEA
Operation Barras Sehemu Sehemu ya Tano
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;