Red Butterfly Sehemu ya Tano
IMEANDIKWA NA: HALFANI SUDY
*********************************************************************************
Simulizi: Red Butterfly
Sehemu ya Tano (5)
“Hajataka tu kuniua. Alikuwa na uwezo wa kutudungua wote wawili. Amefikaje hapa ikiwa kuna ulinzi wa gari zima la Polisi wenye silaha? Sasa hao askari wanaonilinda nje wanafanya kazi gani ikiwa mtu anamfikia na kumuuwa shahidi muhimu kama huyu. Huyu mwanamke kuna kitu alikuwa anakijua kuhusu kipepeo mwekundu au pengine anamjua kabisa huyo mwanamke kichaa. Nitafanya nini sasa iwapo ushahidi wote umepotea….” Adrian alikuwa anawaza peke yake.
“Kama ninataka kushinda katika vita hii ninahitaji mtu makini wa kunisaidia. Hawa Polisi wamedhihirisha kwamba hawaiwezi kabisa kazi hii hata kidogo. Lazima nitafute mtu mwengine nitakayekuwa nae pamoja huku tukilindana. Sitaki awe askari, mwanajeshi wala mtu wa usalama wa Taifa. Nitaenda kuongea na Daniel ili anisaidie kumpata huyo mtu” Adrian alikuwa anawaza peke yake. Alitoka nje na kumpigia IGP John Rondo, alimwambia kila kitu kilichotokea huku askari wakiwa hawajamuona kabisa muuaji. Akaomba ulinzi ule usitishwe kwakuwa hauna faida kwake. Baada ya Adrian kumuelezea vizuri mpango wake IGP John Rondo akakubali. Na Adrian alikuwa anaelekea katika hospitali ya Kairuki kuonana na Daniel Mwaseba. Akiwa njiani simu yake iliita, alikuwa yule mtu wa kule China, Maxi Lee.
“Hallo habari za sahivi” Adrian alisalimia.
“Nzuri Adrian, vipi Tanzania?” Maxi Lee aliuliza.
“Huku kila kitu kinaenda sawa. Nakusikiliza wewe vipi yule mtu wetu anasemaje?” Adrian aliuliza.
“Yule mwanamke amekuwa mgumu kueleza. Tumemtesa sana lakini hana hata Dalili ya kusema chochote. Tumejaribu kumchunguza yeye mwenyewe. Tumegundua kwamba jamaa alishapitia mafunzo ya kijeshi huko Cuba. Tumetuma taarifa kwa watu wetu huko Cuba ndo tunasubiri watasemaje kuhusu huyu mtu” Maxi Lee alisema.
“Nimekuelewa, nasubiri taarifa za huko Cuba zitakuwa zinasemaje. Na nashukuru sana kwa msaada wako”
“Usijari. Serikali yenu na yetu zimekuwa zikisaidiana katika mambo kadhaa, hivyo wala usijari”
“Sawa nashukuru sana. Na tutauendeleza uhusiano huu”
Simu ikakatwa.
“Elizabeth Nevvile atakuwa yupo wapi? Alipotelea kwenye ndege au hakusafiri kabisa. Hilo swala la Elizabeth Neville nalo linaniumiza sana kichwa. Nashukuru sana Maxi Lee kwa kunipigia simu na kunieleza walipofikia, maana lazima Daniel angeniuliza” Adrian alikuwa anawaza akiwa juu ya pikipiki yake.
“Lakini huyo mwanamke ana maana gani kulijumuisha jina la Elizabeth Neville wakati hakusafiri. Bila shaka kuna mchezo fulani unachezwa ngoja nisubiri hayo majibu ya Cuba”
Adrian alikuwa anakata kona sheli kuingia kushoto katika lami iliyokuwa inaelekea katika hospitali ya Kairuki. Alipaki pikipiki yake na moja kwa moja aliingia katika wodi aliyolazwa Daniel, hiyo ilikuwa saa tatu na robo usiku. Haukuwa muda wa kuangalia wagonjwa lakini Adrian aliingia kwa urahisi kwakuwa alikuwa askari. Alipofika wodini Adrian alipigwa na butwaa!
Alimkuta Daniel Mwaseba akifanya mazoezi mepesi.
“Daniel mbona mapema sana. Ungepumzika kwanza ili kidonda kipone vizuri” Adrian alisema.
“Hata kama ninaumwa lakini siwezi kuacha kufanya mazoezi hii ni kwa afya yangu” Daniel alisema huku akitembea kwa kuchechemea akielekea kitandani. Akakaa.
“Eeeh nambie habari za huko Adrian?” Daniel aliuliza. Leo alikuwa mchangamfu zaidi.
“Mambo bado magumu kaka Daniel. Red butterfly bado amekuwa mwiba mkali sana kwangu. Ni sawa na mwiba wa mchongoma. Yaani unachoma utakavyo na unaumiza vibaya sana. Ukiuchomoa unauma, ukiuacha unauma. Red butterfly ni mwiba wa mchongoma..” Baadae Adrian alimulezea kila kitu Daniel, akamueleza pia kuhusu habari za Elizabeth Neville.
“Nimekuelewa Adrian. Sasa una mpango gani mana Red butterfly amewauwa mashahidi wote ambao wangetufikisha kwenye jibu” Daniel Mwaseba alisema.
“Kuna mtu mmoja tu pengine anaweza kutupa majibu. Mtu huyo ni yule mzee tuliyemkosa kule Tandika Foma”
“Utampataje sasa? Bila shaka amechukuliwa na Red butterfly?” Daniel aliuliza.
“Hilo linawezekana, lakini katika kufatilia nyendo za Red butterfly. Na katika kufatilia hizo nyendo ninahitaji mtu makini wa kunisaidia. Ninahitaji mtu anayejielewa kabisa. Naomba unisaidie Daniel kumpata huyo mtu” Adrian alisema.
“Hii kazi inahitaji mtu makini sana. Kwakuwa wewe hauhitaji kijana kutoka jeshi letu la Polisi lazima nikutafutie kijana mwaminifu wa kufanya naye kazi. Kuna vijana watatu walikuwa makini sana katika kazi kama hizi. Pamoja ya kwamba sio askari polisi lakini siku zote husimama upande wa haki. Kwa bahati mbaya vijana wawili wamefariki wakijitolea kutetea nchi hii. Richard aliuwawa katika misheni ambayo kuna mwandishi ameiweka katika kitabu na kuiita Biashara ya kifo na Binunu pia aliuwawa katika mkasa ambao ulikutanisha na mke wangu ambao pia kuna mwandishi aliuandikia kitabu na kukiita Elizabeth Neville. Sasa amebaki kijana mmoja tu, anaitwa Martin Hisia. Ni kijana makini sana ambaye bila shaka ukiwa nae mtasaidiana vizuri na kumshinda Red butterfly” Daniel alisema kwa kirefu.
“Nashukuru sana Daniel, kwakuwa huyo mtu umempendekeza wewe bila shaka ni mtu makini sana. Naomba uniunganishe nae ili tuimalize hii kazi. Nimechoshwa sasa na mauaji ya kinyama yanayofanywa na Red butterfly” Adrian alisema kwa hasira.
Daniel aliitoa simu yake chini ya mtu na kuanza kuitafuta namba ya Martin. Aliipata na kuiweka sikioni.
“Vipi kaka Daniel leo umenikumbuka” Martin alisema kwa nguvu simuni.
“Kama kawaida yako upo klabu Martin, nawe huachi tu maisha hayo?” Daniel alisema.
“Nikiwa sina misheni yoyote haya ndo maisha yangu. Naamka klabu, nashinda klabu nalala klabu, maisha yenyewe mafupi haya” Martin alisema kwa mbwembwe.
“Upo klabu gani sasa Martin? Nina shida na wewe muhimu sana” Daniel alisema.
“Nipo maisha basement hapa. Kuna wazee wa Ngwasuma hawa” Martin alisema.
“Achana na muziki, njoo katika hospitali ya Kairuki sasahivi. Nje utapokelewa na mtu na kukuleta nilipo. Kuna kazi ya haraka ya kufanya” Daniel alisema.
“Nakuja sasahivi kaka. Nilivyosikia neno kazi tu mwili wote umenisisimka, si unajua sijafanya hizi kazi siku nyingi tangu ile kazi ya kule Mafinga” Martin Hisia alisema kwa hisia.
“Sawa nakusubiri” Daniel akasema.
Ilimchukua dakika saba tu Martin kufika Mikocheni katika hospitali ya Kairuki. Hakukuwa mbali sana na Maisha basement alipokuwa. Alipofika moja kwa moja alipelekwa katika wodi ya alipo Daniel Mwaseba.
“Ofisini ni wodini bro, una misheni gani?” Martin aliuliza kwa utani.
“Nilipigwa bastola ya mguu na mwanamke mmoja anaitwa Red butterfly, ndio huyo amenifanya nikuite hapa” Daniel alisema.
“Nipe kazi nikakulipie. Kama yeye ni Red butterfly mimi ni Green Chameleon” Martin alisema. Na kufanya wote wacheke.
“Martin, huyu ni mwenzangu anaitwa Adrian Kaanan. Huyu ndiye askari anayechunguza kifo cha Mheshimiwa Elisha Ngwena na wale watu saba waliouwawa. Sasa uchunguzi wake umekuwa mgumu kidogo kwakuwa yupo peke yake. Nataka umpe kampani” Daniel akasema.
“Hesabu ombi lako limekubaliwa. Nina hamu sana ya kufanya kazi. Si unajua ni muda sana sijaingia kazini” Martin alijibu.
“Naifurahia sana ari yako ya kufanya kazi Martin. Najua itasababisha uifanye kazi hii kwa haraka na umakini mkubwa. Maelezo mengine kuhusu hii kazi atakupa Adrian” Kisha Daniel akamgeukia Adrian ” Adrian kutana na Martin Hisia. Binadamu mwenye Hisia kuliko yeyote yule duniani. Ingawa Martin si askari Polisi lakini ni mzoefu sana kwa misheni kama hizi. Utamueleza kila kitu Martin bila shaka mtafanikiwa kumkamata Red butterfly ” Daniel alimaliza.
Adrian na Martin walipeana mkono tayari kufanya kazi pamoja. Moyoni mwake Adrian alifurahi sana kupata mtu wa kufanya nae kazi pamoja. Alimwamini Martin kwakuwa alichaguliwa na mtu aliyemwamini sana. Alimweleza jinsi uchunguzi wake ulipofikia na kupanga mipango mipya mbele ya Daniel Mwaseba, waliamini ule ndio ulikuwa mwisho wa Red butterfly. Hadi wanaondoka katika hospitali ya Kairuki ilikuwa ni saa sita na robo usiku.
SURA YA TANO
Asubuhi na mapema, Adrian na Martin walikuwa katika hoteli ya Ocafona inn iliyopo Posta. Walikuwa nyuma ya meza iliyojaa vitu mbalimbali. Kulikuwa na mabakuli makubwa mawili ya supu, chupa ya chai na vikombe viwili vilivyojaa chai. Kulikuwa na sahani moja yenye chapati nane na vyupa vya maji viwili vilivyojaa maji ya baridi. Wanaume walikuwa kimya wakikishambulia kile chakula.
Iliwachukua dakika saba. Vitu vyote vilivyokuwepo pale mezani vilikuwa vimeisha, sasa waliagiza juisi ya matunda kushushia. Hapo ndipo Adrian aliongea.
“Kama nilivyokueleza jana Martin, Red butterfly ni hatari sana hivyo yatupaswa kuwa makini sana. Bila hivyo anaweza kutuua muda wowote autakao”
“Usiwe na hofu Adrian. Huyo Red butterfly mwisho wake umefika. Kuhusu hatari mimi nishapitia hatari nyingi sana. Hii ya red butterfly itakuwa inaongeza tu idadi ya hatari nilizopitia” Martin alisema kwa kujiamini.
“Nafurahi sana kukutana na mtu anayejiamini kama wewe. Unanifanya nami nizidi kujiamini” Adrian alisema.
“Sasa Adrian yatupasa kwenda kwa mjane wa marehemu Elisha Ngwena. Bila shaka kule tutapata kitu baada ya kuwahiwa kwa mjane wa mzee Fuga Tondo. Wewe utaingia ndani na kwenda kumuhoji mjane, mimi nitakuwa nakulinda. Najua Red butterfly anazifatilia nyendo zetu lakini safari hii nakuapia hatoki salama” Martin alisema.
“Ok mpango mzuri, twende tukaufanyie kazi” Adrian alisema.
Martin na Adrian walinyanyuka vitini na kwenda nyumbani kwa marehemu waziri wa mambo ya ndani, hayati Elisha Ngwena.
Saa moja kasoro dakika kumi walikuwa mbele ya nyumba ya hayati Elisha Ngwena.
“Adrian utaenda kumuhoji mke wa Elisha. Tutawasiliana hatua kwa hatua. Jiamini, unalindwa na Martin Hisia” Martin alisema.
“Sawa Martin, tumia hisia zako vizuri kwa kila utakayemuhisi vibaya, Red butterfly hatujui atakuja katika ngozi ipi leo” Adrian alisema huku akivaa earphone za mawasiliano.
“Nimekuelewa vizuri Adrian” Martin akajibu.
Adrian alielekea katika nyumba ya marehemu Elisha huku akiangaliwa na macho ya Martin Hisia. Alifika ndani, alikaribishwa na nyumba iliyojaa huzuni na simanzi. Macho ya watu yalikuwa mekundu, ishara kwamba walikuwa wamelia vya kutosha. Adrian aliulizia mahali alipo mke wa marehemu, akaenda kuitiwa. Alienda mwanamke aliyekuwa amevaa gauni refu jeusi na kitambaa cheusi kichwani sebuleni. Macho yake yalikuwa yamevimba yakimaanisha yalikuwa yamelia sana.
“Lazima nimweleze kila kitu. Nimsimulie mwanzo hadi mwisho, ili nione kwa namna gani atatupa msaada” Adrian alikuwa anawaza.
Adrian alijitambulisha. Akamsimulia kila kitu kuhusu Red butterfly na mauaji ya viongozi wa kiwanda cha nguo cha urafiki wa mwaka 1955 hadi 1957. Mke wa marehemu Elisha alikuwa anamwangalia tu. Hata lilipotajwa jina la Red butterfly hakuonesha mstuko wowote ule katika macho ya Adrian. Kabla hajajibu kitu Adrian alijua kwamba wameenda sehemu isiyo sahihi.
“Kiukweli mimi ndo nalisikia leo jina la Red butterfly. Sijawahi kumsikia marehemu mume wangu akilitaja wala yeyote yule” Mke wa marehemu Elisha alijibu baada ya kuulizwa na Adrian kama anamjua Red butterfly.
Baada ya maongezi yaliyodumu kwa dakika kumi Adrian aliondoka, huku akiwa hajapata chochote kile. Walikuwa katika nafasi ileile ya awali. Bado fumbo la Red butterfly lilikuwa gumu kufunguka.
Wakati akitoka nje mara simu yake iliita. Aliitoa mfukoni na kuipokea. Ilikuwa namba ngeni.
“Haloo habari yako?” Adrian alisalimu.
“Safi Adrian. Nimesikia wewe ndio unahusika na kesi ya Red butterfly, naomba tukutane katika hoteli ya the Atrium sasahivi. Nina vitu vya kukusaidia katika uchunguzi wako” Sauti ya kike ilisema simuni.
“Ni nani wewe?” Adrian alilipata swali.
“Adrian, jina litakusaidia nini wakati ukija unanikuta mwenyewe. Mfano nikikwambia ninaitwa Janet na usiponikuta the Atrium utafanya nini? Njoo the Atrium boy nina vitu vya kukusaidia katika uchunguzi wako unaoufanya” Sauti ya kike simuni ilisema kwa kujiamini sana.
Simu ikakatwa.
“Ni nani wewe?” Adrian alilipata swali.
“Adrian, jina litakusaidia nini wakati ukija unanikuta mwenyewe. Mfano nikikwambia ninaitwa Janet na usiponikuta the Atrium utafanya nini? Njoo the Atrium boy nina vitu vya kukusaidia katika uchunguzi wako unaoufanya” Sauti ya kike simuni ilisema kwa kujiamini sana.
Simu ikakatwa.
Adrian alienda hadi katika gari alilomuacha Martin. Cha ajabu Martin Hisia hakuwepo. Aliangazaaagaza lakini hakumuona Martin. Hali ya uwoga ikaanza kumshika.
“Martin yupo wapi? Yatupasa tuwahi the Atrium tukamsikilize huyo mwanamke” Adrian aliwaza.
Adrian alisimama mbele ya gari akimsubiri Martin.
“Kuna kitu nimekihisi hapa. Ninakifanyia uchunguzi” Kile kifaa alichovaa sikioni kiliongea. Ilikuwa sauti ya Martin.
“Sawa Martin. Mimi ninaenda the Atrium mara moja, nitarudi hapa sio muda mrefu” Adrian alijiibu ile sauti.
“Unaenda kwa jambo hilihili?” Martin akauliza.
“Ndio” Adrian akajibu “Nitakuja kukusimulia vizuri nikirudi”
“Ok, poa, take care” Martin alitahadharisha.
“Nawe pia take care” Adrian alijibu.
Adrian akapanda gari na kuelekea the Atrium hoteli, Sinza kumfata mwanamke aliyemwambia kuwa ana ushahidi wa sababu ya mauaji anayoyafanya Red butterfly. Adrian alikuwa askari Polisi, alifundishwa kutoidharau taarifa yoyote ile, maana huwezi jua ipo itakupelekea kufumbua fumbo lako. Adrian aliongeza mwendokasi wa gari ili awahi the Atrium hoteli.
“Martin Hisia itakuwa kahisi nini? Ninaomba hisia zake ziwe kweli na zisaidie kufumbua fumbo gumu la Red butterfly” Adrian aliwaza akiwa njiani.
Akachukua simu yake na kumpigia Daniel Mwaseba.
Martin Hisia alikuwa uwani katika nyumba ya marehemu Elisha Ngwena. Pale uwani waombolezaji wengi walikuwa wamejaa wakijadili hili na lile. Hasa kuhusu tabia za ajabu za mjane wa marehemu.
Pale mwanzo, pindi Adrian aliposhuka tu ndani ya gari Martin alikuwa nyuma yake. Lakini hakuwa Martin Hisia aliyeachwa na Adrian. Martin huyu alikuwa katika mavazi ya kike. Alikuwa katika baibui jeusi huku akiificha sura kwa mtindo wa ninja. Hisia zake zilimwambia awe hivyo, na kama ilivyo ada Martin hapingani na Hisia zake. Wakati Adrian yupo sebuleni akisubiri kuitiwa mjane wa marehemu, Martin alipiga hatua mbele, alikuwa katika korido ndefu iliyokuwa inaelekea uwani. Alifika uwani mahali ambapo kulikuwa na wanawake wengi wakiandaa mapishi. Ndipo aliposikia mjane wa marehemu akiitwa kwenda kukutana na mgeni wake. Martin akajua mgeni anayezungumziwa ni Adrian, Martin alimwangalia mjane wa marehemu alipopewa taarifa zile. Alikuwa ni mwanamke mwembamba ambaye alikuwa amevaa suruali ya kitambaa huku juu akivaa blauzi nyekundu. Martin Hisia alishangaa, ile haikuwa namna ya uvaaji ya mwanamke aliyefiwa na mumewe. Hisia zake zilimwambia kuna kitu.
Kitu kingine kilichotekenya hisia za Martin ni uso uliotahayari na uwoga aliposikia kuwa anaitwa na mgeni, kwanini atahayari?, kwanini ajawe na uwoga?. Martin Hisia alimfata nyumanyuma yule mwanamke, ndipo alipomuona baada ya kuelekea sebuleni alielekea chumbani kwake. Na haikuzidi dakika moja alitoka mwanamke mwenye nguo nyeusi na ushungi mweusi kichwani. Ilihitaji umakini mkubwa sana kugundua kwamba yule mwanamke aliyeingia awali ndio huyu aliyetoka. Sio kwa umbo, ni ule uharaka wa kuingia chumbani, kubadili nguo na kutoka. Sio tu haukuwa uharaka sahihi kwa mtoto wa kike avaapo nguo, bali hata kwa mtoto wa kiume. Ulikuwa uharaka wa ajabu sana!
“Kwanini mjane wa marehemu Elisha avae nguo nyingine na wakija wageni abadili? Kwanini mke wa marehemu Elisha awe na furaha akiwa mwenyewe lakini aingiwe na uwoga wa ajabu pindi apatapo taarifa za mgeni? Lakini uharaka wa kubadili nguo na kutoka nje ni uharaka wa ajabu sana” Hisia za Martin Hisia zilikuwa hisiani.
“Lazima nibaki hapa ili kuchunguza matendo ya mjane wa marehemu” Martin Hisia akiwa katika vazi la baibui na nikabu aliwaza.
Alivyotoka kuongea na Adrian mjane wa marehemu alirudi tena chumbani kwake. Kwa haraka ileile alibadili zile nguo za maombelezo na kuvaa nguo zake za awali. Hali hiyo ilikuwa ni utata kwa Martin Hisia. Ndipo alipomgia simu Adrian amwache pale ili aendelee na uchunguzi.
Adrian alitumia nusu saa kufika katika hoteli ya The Atrium iliyopo Sinza Africasana. Alishuka ndani ya gari yake na harakaharaka alikwenda katika hoteli ya the Atrium kwenda kukutana na huyo aliyemwita. Alipofika tu mlangoni simu yake iliita. Aliitoa simu mfukoni na kumwangalia aliyepiga, ilikuwa ni namba ileile iliyomfanya awe pale.
“Nimekuona Adrian. Njoo moja kwa moja kama unaelekea msalani, nipo meza ya tatu kama unatoka msalani. Nimevaa nguo nyeusi na miwani nyeusi” Simu ilisema pale tu Adrian alivyoipokea. Hakupata hata nafasi ya kujibu yake maelezo. Simu yake ilikatika.
Adrian alifata kama maelezo yalivyosema. Alimuuliza muhudumu mmoja tu mahali vyoo vilipo. Alielekea baada ya kuelekezwa. Na kweli, meza ya tatu kutoka chooni kulikuwa na mwanamke aliyekuwa amevaa suruali nyeusi na tshirt nyeusi akiwa amekaa juu ya kiti, mbele ya meza yake kulikuwa na soda aina ya sprite.
Adrian aliisogelea ile meza huku akiwa amechukua tahadhari zote. Mkono wake haukuwa mbali na mahali alipoweka bastola yake.
“Karibu sana Adrian” Yule mwanamke alisema kwa bahshasha.
“Ahsante sana Elizabeth Neville..” Adrian alisema bila wasiwasi wowote ule.
Mshangao mkuu ulimpata yule mwanamke.
Hebu leo niambie…Tufanye wewe ni Martin Hisia, je kwa hisia zako Red butterfly ni nani?
MWISHO
Also, read other stories from SIMULIZI;