Roman Abramovich – Utajili wa Damu, Risasi na Umafia Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA : THE BOLD
*********************************************************************************
Simulizi : Roman Abramovich: Utajiri Wa Damu, Risasi Na Umafia
Sehemu Ya Tatu (3)
Siku nyingine wako kweye halaiki ya kitaifa… wakati wimbo wa taifa unaimbwa Yeltsin akainuka na kwenda kumpokonya kipaza sauti mwendesha shughuli na kuanza yeye kuongoza kuimba wimbo wa taifa huku akiimba hovyo hovyo na kwa sauti ya ulevi.
Yeltsin alikuwa na tatizo na alikuwa anatakiwa kuondolewa madarakani haraka iwezekanavyo. Kama wakifanya uzembe na bunge likamuondoa madarakani Yeltsin na kumuweka mtu wao kuna kila dalili kwamba mali zao zote zitataifishwa na hata wao wenyewe kuishia jela maana wanasiasa wengi ndani ya Moscow walikuwa na hasira na namna ambavyo ma-oligarch wanaitafuna nchi kwa kukingiwa kifua na Yeltsin.
Lilikuwa linahitajika suluhisho la haraka kabla mambo hayajaaribika. Ma-oligarch wote walimtazama Abramovich, tumaini lao lilikuwa kwake atoe wazo wapate suluhu wa nini kifanyike.
Kwenye sehemu iliyopita nilieleza kwamba afya ya mwili na akili ya Rais Boris Yeltsin haikuwa imara mwishoni mwa miaka ya 1995 mpaka mwanzoni mwa 1996. Yeltsin alikuwa kiroja kila ambapo alikuwa mbele ya umma. Ma-oligarch wakaanza kukuna vichwa kutafuta mrithi wake kabla ya bunge la Urusi kumuondoa Yeltsin kwa lazima na kumweka mtu wao. Lakini katika juhudi hizi ma-oligarch macho yao yote yalikuwa kwa Roman Abramovich.
Sasa, nianze kwa kusema hiv…
Kuna suala moja la kushangaza sana kuhusu Putin. Kama ni mfuatiliaji wa mambo utakuwa umeshuhudia kwa mara kadhaa na kwa miaka kadhaa amekuwa na migogoro karibia na kila Oligarch nchini Urusi isipokuwa Roman Abramovich pekee. Tena ajabu ni kwamba Abramovich ikitokea anashambuliwa labda na vyombo vya habari vya magharibi, Putin huwa ni moja ya watu wa kwanza kumtetea.
Kwa nini? Kwa sababu mwaka 1996 tofauti na mategemeo ya watu wote juu ya mrithi wa Boris Yeltsin, katika kikao cha ile inner circle ya Rais, Roman Abramovich alipendekeza jina la Vladmir Putin kuwa mrithi wa kiti cha Urais wa Urusi. Katika ulimwengu wa siasa za Urusi kipindi hicho Putin hakuwa lolote wala chochote na hata wananchi wengi hawakuwa wanamjua. Putin hakuwahi hata kuwa ‘balozi wa nyumba kumi’. Lakini Abramovich alimtaka Putin amrithi Yeltsin.
Kwa nini? Kuna sababu kadhaa… sababu za wazi ambazo ‘alishea’ na wenzake lakini pia kulikuwa na sababu binafsi ambazo wengine hawakuzijua. Ma-oligarch kama ambavyo ilikuwa kwa warusi wengine walikuwa wanataka kuijenga upya ‘image’ ya kiti cha rais wa Russia. Kwa kiasi fulani ‘image’ ya kiti cha urais wa Russia ilikuwa imechafuka kutokana na vimbwanga ambavyo Yeltsin alikuwa anavifanya. Ma-oligarch na warusi walikuwa wanataka Rais ambaye ataakisi ukakamavu, weledi na msimamo thabiti kuitetea Russia dhidi ya mabeberu ya magharibi. Vladmir Vladmirovich Putin alikuwa na sifa hizi zote.
Lakini kulikuwa na sifa nyingine ambayo wengine hawakuijua… sifa ambayo ni Vladmir na Abramovich pekee waliifahamu.
Nitakuwa sijatenda haki nikizungumzia historia kamili ya Vladmir katika makala hii kwa maana binadamu huyu haswa anastahili nitulie nimuandikie makala yake kabisa kumuhusu yeye mahususi na wala sio kuchomekea tu historia yake ndani ya makala yenye kuhusu jambo lingine. Na kwa hakika hata makala tu tutakuwa hatujatenda haki… twapaswa kumwandikia kitabu kabisa binadamu huyu ambaye kwa mwaka wa tano huu sasa Jarida la Forbes linamuorodhesha kama mtu mwenye ushawishi zaidi ulimwenguni akimpiku Obama kwenye miaka ya mwisho ya uongozi wake na akiendelea kumburuza hata Rais wa sasa Donald Trump na pia kuwapiku miamba mingine kama Rais Xi jiping na baba mtakatifu Papa Francis. Yako mengi sana ya kuyaandika kuhusu kiongozi huyu mahiri, viko visa vingi vya kusisimua ambavyo bado wengi hawavifahamu. Yako mengi ya kujifunza na iko mikasa mingi ya kuburudisha kuhusu maisha yake.
Lakini ili niweke msingi mzuri wa hoja ya kile ambacho nakusudia kukisema kuhusu yeye na Abramovich, nitachomekea kijipande kiduchu tu walau cha historia yake.
Mwaka 1975 miezi michache baada ya kumaliza elimu ya chuo kikuu Putin alijiunga na shirika la kijasusi la KGB. Mwanzoni alipojiunga na KGB alifanyakazi ndani ya Second Chief Directorate lakini baadae kidogo akahamishiwa First Chief Directorate ambayo hasa ilihusika ushushushu pamoja na ujasusi nje ya Urusi. Jukumu lake la kwanza baada ya kuhamishiwa kwenye idara hii ilikuwa ni kufatilia nyendo za raia wa kigeni na maafisa balozi mbalimbali ambazo zilikuwa katika mji wa Leningrad ambako ndiko alizaliwa, kukulia na kusoma. Baadae kidogo alihamishwa na kupelekwa Ujerumani ya Mashariki enzi zile kabla ya taifa la ujeremani kuungana. Akiwa huko alifanya kazi yake ya ushushushu kwa kutumia ‘cover’ ya mtafasiri mbobezi wa lugha ya kirusi kutoka kingereza na kijerumani ambapo huduma hii alikuwa anaitoa kwa wafanyabiashara na watumishi wa serikali. Hapa ufahamu kwamba Putin anaongea lugha ya kijerumani kwa ufahasa wa hali ya juu. Kazi yake kule ujerumani ilikuwa nzito kidogo… kwanza alikuwa akikusanya taarifa juu ya serikalli lakini pia alikuwa anafanya kukusanya intelijensia za ‘open source’. Intelijensia ya open source ni ile inayopatikana kutoka kwenye vyanzo vya habari ambavyo umma una ‘access’ navyo kwa mfano magazeti, internet, televisheni, redio na kadhalika. Ukusanyaji wa intelijensia ya namna hii inaweza kuonekana kama rahisi kulinganisha na intelijensia inayokusanywa ‘covertly’. Lakini kwa maoni yangu binafsi hii ni moja kazi nzito zaidi katika ukusanyaji wa intelijensia. Hebu vuta picha kwa mfano wewe ni afisa usalama hapa nchini na kazi yako ni kukusanya intelijensia ya open source. Maana yake ni kwamba muda wote usiku na mchana unatakiwa ku-monitor habari ambazo kwenye televisheni zote nchini, radio zote muhimu, usome magazeti yote ya kila siku, ufuatilie kila habari inayo-trend jamii forums, facebook, instagram na twitter. Sasa hapa ugumu sio kufuatilia tu habari bali unapaswa kuchambu ‘pumba na mchele’. Ni lazima u-prioritize habari gani inaweza kuwa na value kwa idara na habari gani ya kuipuuza na kuachana nayo. Habari hizi ambazo zinaonekana kuwa na value kuna mfumo maalumu ambao Analysts wanaziingiza kwenye database ya idara ambapo siku yoyote inaweza kuhitajika kama ikionekana inakuwa complemented na intelijensia fulani ambayo imekusanywa covertly.
Hii ndio ilikuwa kazi ya Putin kule Ujerumani Mshariki.
Baada ya ukuta wa Berlin kudondoka Putin pamoja na maafisa wengine iliwabidi kukimbia Ujerumani na kuchoma moto nyumba ambayo walikuwa wanakaa ili kupoteza ushahidi wa mafaili ya ujasusi na intelijensia waliyokuwa wanakusanya. Kuna visa vya kusisimua sana vilitokea wakati huu ambao siku nikipata fursa ya kuandika kuhusu Putin nitavieleza.
Baada ya kuondoka Ujerumani, Putin alirejea Russia kwenye mji aliozaliwa wa Leningrad ambapo KGB walimpangia jukumu jipya katika chuo kikuu cha Leningrad kitengo cha masuala ya nchi za nje. Jukumu lake hasa hapo chuo kikuu lilikuwa ni kutathimini wanafunzi ambao wana ‘potential’ ya kujiunga na KGB. Ni katika kipindi hiki ambacho Vladmiri Putin alipanda cheo ndani ya KGB kufikia kuwa Kanali.
Nilieleza pale juu kwamba Putin alisoma pia kwenye chuo hiki. Kipindi hicho alichosomaga alijenga urafiki mkubwa na mwalimu wake aliyeitwa Profesa Anatoly Sobchak. Kwa hiyo Putin aliporejea tena chuoni hapa japo safari hii kwa kazi maalumu alifufua upya urafiki wake na Profesa Sobchak. Kwa maoni yangu pasipo urafiki huu kamwe Putin asingekuja kuwa rais wa Russia. Nikirejea baadae kidogo nitaeleza ni kwa namna gani urafiki wake na Profesa Sobchak ulimfungulia njia za siasa ndani ya Moscow na hatimaye kuwa noticed na Abramovich na kwa sababu gani hasa zilimvutia Abramovich…
Yule mwalimu wake wa chuo kikuu Profesa Anatoly Sobchak ambaye Putin aliporejea kutoka Ujerumani na kupangiwa jukumu la kishushushu chuo kikuu cha Leningrad alifufua upya urafiki naye, mwaka 1990 Profesa Sobchak aligombea kiti cha Umeya wa mji wa Leningrad na kushinda. Baada ya kushinda kiti cha Umeya alimteua Putin kuwa mshauri wake wa masuala ya Kimataifa.
Mwaka uliofuata Putin alijiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya KGB kutokana na kutoridhishwa na msimamo mpya wa idara hiyo na utendaji wake. Nikiwa mahususi zaidi, kujiuzulu huku kwa Putin kulikuwa ni siku ya tarehe 20 August mwaka 1991. Kama unafahamu vyema historia ya Urusi unaweza kuona kwamba hiyo ilikuwa ni siku mbili tu baada ya jaribio la kumpindua rais Michail Gorbachev. Hii ilikuwa ni namna yake Putin kuonyesha kwamba hakukubaliana na kile ambacho kilikuwa kimetokea. Uamuzi huu wa kujiuzulu kutoka shirika la kijasusi la KGB ulikuwa ni mgumu sana kwa Putin kwani maisha yake yote ya ukubwa aliyaishi kama jasusi ndani ya shirika hili.
Nchini Urusi katika ofisi ya Meya shughuli zinaendeshwa kupitia kamati mbalimbali ambazo zinakuwa chini ya ofisi ya Meya. Mwaka huo huo 1991, Putin ‘akaula’ tena… akateuliwa kuongoza kamati ambayo inashughulika na Mahusiano ya kimtaifa, uwekezaji kutoka nje na usajili wa makampuni (tusichanganye na kile cheo chake cha awali, “Mshauri wa Meya juu ya Masuala ya Kimatifa”). Hapa ndipo ambapo nataka hasa kupawekea mkazo zaidi.
Eneo la Leningrad lina utajiri mkubwa sana wa migodi ya chuma na uzalishaji aluminium. Kwa hiyo cheo hiki kipya cha kuongoza kamati ya kushughulikia uwekezaji, usajili wa makampuni na mahusiano ya nchi za nje kilikuwa ulaji mkubwa. Siku nikiandika kuhusu Putin nitaeleza kisanga ambacho kilitokea mwaka wake wa kwanza tu baada ya kuteuliwa kuongoza kitengo hiki mpaka kupelekea kuchunguzwa na Baraza la Bunge la Mji wa Leningrad.
Niwape kwa muhtasari tu… ni kwamba katika kipindi hiki Urusi ndio ilikuwa ina-recover kutoka kwenye mdororo wa kiuchumi. Jamii nyingi zilikuwa zinaishi kwenye umasikini wa kupitiliza. Kwenye baadhi ya miji walikuwa wanaweza masharti nafuu ya uwekezaji kama vile misamaha au unafuu wa kodi.
Sasa kuna makampuni kutoka nje ya Russia ambayo kwa maelekezo ya Putin kama mwenyekiti wa kamati ya uwekezaji ya Leningrad yaliuziwa kiasi cha ‘metals’ zenye thamani ya dola milioni 93 kwa makubaliano kwamba walete chakula cha msaada. Chakula hiki cha msaada hakikuonekana Leningrad. Ikazuka minong’ono kwamba kuna watu Putin alikula nao dili kwenye mchezo huu. Ndipo hapa ikaundwa tume ikiongozwa na mwanamama machachali Marina Salye……. Kuchunguza kisanga hiki. Kuna vimbwanga vingi sana ndani ya skandali hii ambavyo sitaviongelea leo hii, lakini mwisho wa uchunguzi wa kamati wakatoa pendekezo kwamba Putin afutwe kazi na pia afunguliwe mashtaka.
Lakini hakuna lolote kati ya hayo mapendekezo ambayo kilitekelezwa ambalo lilitekelezwa. Kwa nini?
Ukiwa porini, ukila nyama hakikisha unakula na simba… hakuna ambaye atathubutu kukusogolea kupoka mnofu wako.
Habari za ndani zinasema kwamba kuna uwezekano mkubwa Putin alifanya dili hii kwa kushirikiana na Oligarch Berezovsky ambaye kwa kipindi kile alikuwa na ushawishi mkubwa sana ndani ya Moscow. Tunakumbuka kwamba Borozovksy pia ndiye kwa kipindi hicho alikuwa ‘mentor’ wa Roman Abramovich.
Skandali hii ndio kwa mara ya kwanza ilimfanya Abramovich kumfahamu Putin na kuvutiwa naye kutokana na historia yake ya kutumikia kwenye shirika la ujasusi,uimara wa misimamo yake na pia haiba yake ya kutaka mabadiliko ya kimfumo ndani ya Russia. Putin alikuwa anajulikana mjini Leningrad kutokuung mkono sera za kijamaa ambazo zilikuwa zinatumika huko nyuma kuendesha nchi.
Wanasema ukiona vyaelea ujue vimeundwa. Ni nandra mno mno kwa mtu yeyote yule kwenye ulimwengu wa sasa kupanda mpaka nafasi ya juu kabisa ya utumishi wa nchi kama vile Urais kwa bahati mbaya. Kuna watu watasema “vipi kuhusu Trump.” No, it wasn’t an accident. Kuna wengine wanahisi hata rais fulani hapa Afrika Mashariki mwaka 2015 aliukwaa Urais kwa bahati mbaya bila kujua historia yake ndani ya Idara ya Ujasusi wa nchi hiyo na bila kujua kikao cha kimkakati cha April 23, 2015 kilichofanyika nje kidogo ya mji wa Morogoro kati ya maafisa waandamizi wa idara ya ujasusi wa nchi hiyo na viongozi watatu wakubwa wastaafu. Too bad siwezi kuandikia hayo mambo…
Ninachotaka kusema ni kwamba ukiona vyaelea ujue vimeundwa… ni nadra mno katika ulimwengu wa leo mtu kuinuka mpaka kufikia uongozi wa juu wa nchi kwa bahati mbaya. Kila kiongozi anaundwa na kufinyangwa na mtu fulani.
Nimeeleza kwamba skandali ya uuzaji wa ‘metals’ zenye thamani ya dola milioni 93 ndizo ambazo zilimfanya Abramovich kumfahamu Putin na hatimaye kuvutiwa naye… sasa taratibu Abramovich akaanza kumfinyanga Putin. Huko nyuma nilishaeleza ni namna gani ambavyo Abramovich aliweza kujijenga kiushawishi na mpaka hatimaye kuwa kati ya wale wajulikanao kama “The Family” ndani ya Moscow na hata baadae ushawishi wake kupitiliza kuwa pengine mtu mwenye kusikilizwa zaidi na Rais Boris Yeltsin.
Ni katika kipindi hiki ambacho Roman Abramovich akaanza kumjenga Putin. Nitaeleza namna ambavyo Putin alikuwa anapanda ngazi kwa kasi ya ajabu mara baada ya kwenda Moscow.
Sasa,
Katika uchaguzi ambao ulifuata yaani uchaguzi wa mwaka 1995 yule Profesa rafiki wa Putin alipoteza kiti chake cha Umeya. Hii ilimlazimu Putin kuhamia Moscow kuangalia fursa nyingine. Baada ya kuwasili tu Moscow kwa ushawishi wa Abramovich Putin aliteuliwa kuwa deputy Chief wa Idara ya Presidential Property Management. Idara hii ilikuwa inahusika na menejiment ya mali za Urusi nje ya mipaka yao (kama vile uwekezaji) lakini pia Idara hii ilihusika na kuhamisha mali za nchi ambazo awali zilikuwa chini ya Shirikisho la Urusi kabla ya kuvunjika na kuzihamishia kwenye umiliki wa Urusi ya sasa. Unaweza kuona ni kwa kiasi gani jukumu huli lilikuwa ni nyeti.
Mwaka mmoja baaadae, kwa mara nyingine tena kwa ushawishi wa Abramovich Putin aliteuliwa kuwa Naibu katibu mkuu Kiongozi. Wakati anateuliwa katika nfasi hii, ile ya ile nafasi ya kwanza pia bado alikuwa anaendelea nayo (nafasi ya Deputy Chief of Presidential Property Management Department). Miezi michache baadae ile nafasi ya kwanza ambayo aliteuiwa kama Deputy chief, akapandishwa cheo kuwa Chief. Kwa hiyo kwa wakati mmoja Putin alikuwa ni Naibu katibu Mkuu kiongozi na pia alikuwa Chief of Presidential Property Management Department.
Kila baada ya miezi kadhaa Putin alikuwa anapanda cheo kwa kasi ya ajabu na kuna mahala maalumu ambako Abramovich alikuwa anataka Putin afike.
Siku ya tarehe 25, July mwaka 1998 kwa nguvu na ushawishi wa muda mrefu wa Oligarch Roman Abramovich… Putin aliteuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa Federal Security Services (FSB). Hii FSB ndio idara ambayo iliundwa kurithi kazi za kijasusi za KGB ambayo ilivunjwa. Kwa hiyo kwa muda wa miaka miwili tu tangu aingie Moscow Putin alikiwa amepanda vyeo kwa kasi na sasa alikiwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa wa Russia.
Usione vyaelea, vimeundwa.
Tunarejea pale ambapo ma-oligarch walimfuata Abramovich kumuomba mawazo… ni nani anafaa kumrithi rais Boris Yeltsin??
Wao walikiwa wanauliza leo… lakini mwenzao alijiandaa kuwajibu swali hili miaka minne nyuma. Tayari alikuwa na mtu kichwani kabla hata hawajauliza au kwa usahihi zaidi, alikuwa na jibu la swalo lao kabla hata hawajaanza kuwaza kuhusu swali hilo.
Maana halisi kabisa ya mtu anayeishi kimkakati na Kuwaza kimkakati. A natural born tactician.
Hakuna kitu kizuri kama kiongozi ambaye anaweza kujitathimini na kukubali mapungufu yake na kukubali kukaa pembeni kupisha wengine. Mtu wa namna hii hata kama kuna madudu aliyafanya unajikuta unapata nafasi ya kumsamehe moyoni.
Licha ya mapungufu yake yote na vituko juu ya vimbwnga alivyovifanya kuidharaulisha Russia, lakini ulipofika wakati na kuelezwa ukweli kwamba ni muda muafaka akae pembeni kupisha mtu mwingine, Boris Yeltsin hakuifanya shingo yake kuwa ngumu.
Roman Abramovich akakutana na ma-oligarch wenzake. Akawapa pendekezo lake la nani anadhani anafaa kuwa rais mpya wa Russia. Akaweka sababu zake mezani… ma-oligarch wakakubaliana naye.
Nilieleza kwamba wale wanaojiita ‘The Family’ ambao ni ma-oligarch na wanafamilia ya Yeltsin kimsingi ndio ambao walikuwa wanaendsha nchi. Na ndani ya The Family kulikuwa na ule ‘Utatu Mtakatifu’… Abramovich, Tatyana na Yumachev. Na katika kipindi hiki Abramovich alikuwa na nguvu ya ushawishi kwa Yeltsin kuwazidi wote hata ndani ya The Family na Utatu Mtakatifu.
Kwa hiyo ulipofika wakati wa kuzungumza suala hili zito na Yeltsin… ni Abramovich pekee yake… yeye na Yeltsin pekee walijifungia ofisini na ‘kuyajenga’.
Kwanza Abramovich alimueleza Yeltsin kwa nini huu ni muda muafaka yeye kukaa pembeni na kumpisha kiongozi mpya. Baada ya Yeltsin kuukubaliana na hili, Abramovich akamueleza kuhusu pendekezo la mrithi wake. Abramovich akamueleza kwamba anapendekeza Vladimir Vladimirovich Putin, Mkurugenzi Mkuu wa FSB aanze kuandaliwa kurithi kiti hicho cha Urais. Kama ambavyo aliwafafanulia ma-oligarch ndivyo pia ambavyo alimfafanulia Rais Boris Yeltsin.
Tarehe 9 August mwaka 1999 Rais Boris Yeltsin alimteua Vladimir Putin kuwa Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu. Yaani kipindi hicho ilikuwa kunakuwa na Waziri Mkuu alafu anakuwa na Manaibu watatu au wawili. Yaani mfano mzuri kama Zanzibar walivyo na ‘Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wa Rais’. Kwa hiyo Putin aliteuliwa kuwa Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu wa Russia. Nimeeleza kwamba kipindi hiki Russia ilikuwa kwenye mparaganyiko fulani hivi wa kimfumo. Wakati Putin alikuwa anateuliwa kuwa Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu lakini nafasi ya Waziri Mkuu ilikuwa wazi. Ndani ya muda wa chini ya miezi kumi na tatu, walikuwa wameteuliwa Mawaziri Wakuu wane tofauti na kufukuzwa. Uteuzi huu wa Putin kuwa Naibu wa Kwanza wa Waziri mkuu ulitangazwa asubuhi ya tarehe hiyo 9… lakini ajabu sana ilipofika majira ya jioni siku hiyo hiyo Putin aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Russia.
Mkakati… Abramovich… Abracadabra…
Uteuzi wa Putin kuwa Waziri Mkuu mwanzoni haukushitua sana watu japokuwa hakuwa na umaarufu kwa wanasiasa wala wananchi kwa sababu kama ambavyo nimeeleza kuwa kwa muda wa kama miezi kumi na tatu tu tayari kulikuwa na Mawaziri Wakuu wane walioteuliwa na kufutwa kazi. Kwa hiyo watu walikuwa wanamuhesabia siku tu Putin kabla yay eye pia ‘kutumbuliwa’… ni kama vile hapa kwetu nchini, ukiteuliwa kuongoza Wizara ya Maliasili na Utalii au Wizara ya Nishati na Madini… watu wanakuhesabia miezi tu.
Lakini siku tatu tu baada ya uteuzi wa Putin, Rais Boris Yeltsin alifanya kitu cha tofauti kulinganisha na Mawaziri Wakuu waliopita ambao aliwahi kuwateua. Katika hotuba yake kwa wananchi alitamka kwamba anatamani Putin awe mrithi wake wa kiti cha Urais siku akiondoka kwenye cheo hicho… wenye kusoma alama za nyakati wakaelewa nini kilikuwa kinaendelea. Hii haikuwa ile ‘teau kisha fukuza’. Putin alikuwa anaandaliwa kuchukua nchi.
ITAENDELEA
Roman Abramovich – Utajili wa Damu, Risasi na Umafia Sehemu ya Nne
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;