Utata wa 9/12 Sehemu ya Kwanza
KIJASUSI

Ep 01: Utata wa 9/12

SIMULIZI Utata wa 9/12
Utata wa 9/12 Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA: HUSSEIN ISSA TUWA

*********************************************************************************

Simulizi: Utata Wa 9/12

Sehemu ya Kwanza (1)

Mwaka 1961

Kijiji cha Kazimzumbwi, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani.

Watu saba, au labda ni sahihi zaidi kusema viumbe saba, walikuwa wakisubiri kwa hofu kubwa ujio wa mtu, au kiumbe, atakayewaletea nafasi nyingine ya kuishi katika dunia hii ya binadamu waliyolazimika kuishi miongoni mwao, wakifuata taratibu zao na kuchukua mila na desturi zao; na wao wakionekana kuwa ni wenzao, binadamu kama wengine,ingawa kwa hakika wao hawakuwa binadamu hata kidogo. Pamoja na ukweli huu, bado walionekana kuwa ni binadamu halisi, na hakuna binadamu yeyote aliyekuwa na sababu ya kutowaona hivyo, kwani mbele ya macho ya watu wote, nao walikuwa ni binadamu kama wengine. Lakini ukweli ni kwamba,watu saba hawa na jamii yao ndogo sana iliyopo hapa duniani walikuwa na siri kubwa sana;siri ambayo hakuna binadamu,yeyote anayeweza kuifichua isipokuwa kwa msaada wa kiumbe kingine kutoka kwenye sayari ya mbali. Kiumbe asiyekuwa bindamu…kiumbe wa aina yao.

Wenyewe walikuwa wakijiita wazawa, na walikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya mambo ambayo binadamu wa kawaida hakuweza kabisa kuyafanya.Walikuwa na nguvu za ajabu zilizowawezesha kuwatawala binadamu wa ulimwengu huu kwa kadiri walivyopenda na hakuna lolote ambalo binadamu hawa, ambao wao wamejiingiza miongoni mwao na kuchukua muonekano na taratibu zao, wangeweza kulifanya kubadilisha hali hiyo, isipokuwa kwa msaada wa mmoja kati ya watu wa jamii yao…mzawa mwenzao.

“Wazawa” hawa walikuwa na nguvu ya kufanya mambo mengi ya kuwashangaza na hata kuwaangamiza binadamu waliokuwa wakiishi miongoni mwao iwapo walitaka au iliwalazimu kufanya hivyo. Na hawakusita hata kidogo kufanya hivyo pale ilipobidi. Lakini walikuwa wanawahitaji sana binadamu na hasa ulimwengu waliokuwa wakiishi. Kwao ulimwengu huu wa binadamu ilikuwa ni sehemu muhimu sana…lakini kwa muda maalumuu.

Walikuwa wamekaa kwenye sakafu ya pango kubwa lililokuwa chini ya mlima Kazimzumbwi, wakiendelea kusubiri kwa ukimya ulioficha hisia zao za hofu .Wote walikuwa wazee; watatu wanawake, wanne wanaume, baina yao hakuna aliyepungua umri wa miaka sabini na mitano. Na wote walikuwa uchi wa mnyama.

Katika hali ya kawaida, hawa walikuwa ni vikongwe wasioweza tena kufanya mambo yao muhimu wala kufikiri sawasawa .Lakini sio kwa hawa wazawa. Kwao vilivyochakaa ni ile miili ya kibinadamu tu waliyoivaa, lakini umakini, akili, nguvu na uwezo wao wa ajabu bado vilikuwa palepale. Tatizo ni kwamba sasa ulikuwa umefika muda wa wao kubadilisha ile miili ya binadamu iliyochoka na kuchukua miili mingine ili waendelee kuishi hapa duniani kama binadamu wengine mpaka pale muda wa wao kuendelea kuwepo hapa duniani utakapoisha na kuwapa nafasi ya kurejea walipotoka, kwenye sayari ya mbali, ambako huko ndiko haswa uzawa wao ulipotokea…wakiwa viumbe huru.

Iwapo hawatagundulika na kuangamizwa na watu, viumbe wa jinsi yao, ambao hata sasa walijua kuwa walikuwa wanawasaka, kabla ya muda huo kufika. Na leo ilikuwa ni siku iliyobeba usiku muhimu sana kwao. Ni siku ambayo ilikuwa inabeba hatima ya kuendelea au kutoendelea kuwepo kwao hapa duniani kwa muda mwingine mrefu, na hivyo kuendelea kupunguza idadi ya siku walizotakiwa kuendelea kuwepo katika dunia hii ya binadamu na kurudi kwao. Leo hii iliwazimu wajumuishe nguvu zao zote na kuziweka katika mwili wa msichana wa kibinadamu ambaye hajanajisiwa na mbegu zozote za kiume, msichana bikira, na wao watakufa kwa muda wa siku saba. Ndani ya siku saba hizo, nguvu zao zitakuwa zikijirudisha upya.Ndani ya siku saba hizo yule msichana bikira wa kibinadamu atakuwa katika hali ya nusu fahamu, hali ambayo binadamu huwa wakiita “undondocha”, mpaka siku ya nane ambapo ataingiliwa kimwili na kijana mzawa na kuitoa ile bikira yake. Hapo nguvu zao zitakuwa zimejirudisha maradufu, nao watarudi tena duniani katika sura ya binadamu wengine, ilihali ile miili ya awali waliyokuwa wameitumia ikizikwa na binadamu kwa mila na desturi zote za kibinadamu. Hakutakuwa na tatizo wala wasiwasi wowote juu ya vifo vyao, kwani si ni kawaida kuwa binadamu wakitimiza umri mkubwa kama ule huwa wanakufa! Binadamu watalia na kuombeleza juu vifo vya wazee wao wale bila ya kujua undani hasa wa mazingira ya vifo vile. Ama kwa yule bikira wa kibinadamu, yeye hatoonekana tena. Na hata ikitokea mazingira akaonekana, basi ndio atakuwa katika hali ile ya undondocha, na hatoweza kujua wala kueleza, ni nini kilimtokea. Ni wale “wazawa” pekee ndio watakaojua juu ya undani huo, na hivyo ndivyo itakavyokuwa daima…

Katikati ya jiji la Dar es Salaam, usiku ule ule…

Sherehe kubwa zilikuwa zikiendelea, watu wengi walikuwa wamejaa kwenye uwanja mkubwa wa michezo, na wengi wengine walikuwa wakiendelea kumiminika kiwanjani pale kama kwamba ilikuwa ni mchana na si usiku. Mataa yenye mwanga mkali yaliyotapaka kila pembe ya kiwanja kile na maeneo yaliyokizunguka, yalileta mwanga wa kutosha. Kote kulikuwa kuking’aa, na hivyo kuzidi kuleta ile hisia kuwa hakika ule haukuwa usiku bali ni mchana. Ilikuwa ni saa tano za usiku. Vikundi kadhaa vya ngoma vilikuwa vikitumbuiza kila upande wa uwanja ule, na vyote vilipata watazamaji na washangiliaji. Vifijo, hoihoi, nderemo na vigeregere vilitawala ndani ya uwanja ule, na, wakati huko nje mayowe ya furaha, mbinja na honi za magari vilitawala kwa mbali muziki wa dansi ulisikika, huu ulikuwa ukipigwa kwenye ukumbi wa starehe nje ya uwanja ule, wakati kutokea sehemu mbalimbali ndani ya uwanja ule, na maeneo kadhaa ya jiji, fataki zililipuliwa na kutupa miale ya moto yenye rangi za kuvutia na kufurahisha, ziliruka juu na kutawanyika hewani katika mapande mengi yenye cheche za rangi mchanganyiko zikiambatana na vishindo hafifu kwa kila mpasuko wa miale ile yenye kupendeza. Viongozi wa kitaifa, wazungu kwa waafrika, walikuwa wameketi kwenye viti maalumuu vilivyotengengwa kwa ajili yao pale uwanjani, na wengine walikuwa wakiendelea kuingia pale uwanjani kila baada ya muda uliopangwa wakiwa ndani ya magari mazuri na ya kifahari. Lilikuwa ni tukio kubwa, muhimu na la kihistoria. Kila mtu alikuwa na sababu ya kushereheka. Isipokuwa wazungu wachache, ambao hata hivyo, hawakuwa wazawa wa nchi hii, hivyo hakuna aliyejali juu ya hilo. Ilikuwa ni shangwe kila upande…

Barabara ya Pugu–Kazimzumbwi, usiku ule ule…

Gari aina ya Ford Anglia lilikuwa likisafiri kwa mwendo wa kasi katika barabara pweke ya lami likitokea kijiji cha Mzenga, Wilaya ya Kisarawe, kuelekea mjini Dar es salaam. Ndani yake lilikuwa na wasafiri watatu ambao safari yao kuelekea jijini iliwalazimu wapite kijiji cha Kazimzumbwi, kufuata barabara ile, waingie Kisarawe, Minaki, kisha wakate kushoto na kukamata barabara ya Pugu, Gongo la mboto na hatimaye katikati ya mji. Wawili kati ya vijana watatu waliokuwa ndani ya gari lile walikuwa wamelewa, kila mmoja akiimba wimbo wake, na wakati huo huo redio ya kwenye gari lile ikiwa imefunguliwa na wimbo Heart-brek Hotel wa Elvis Presley ukisikika kwa sauti ya juu.

“Banchikichaa…! Banchikichaaa-nchikichaa-nchikicha! Nii-likwenda…niilikwendaa-kwendaa-kwendaa…” Uwesu bin Shaame, aliyekuwa akiendesha gari lile alikuwa akiimba kwa kelele bila ya kujali kuwa lile gari lilikuwa likiyumba huku na huko katika barabara ile pweke huku likiwa kwenye mwendo wa kasi.

“Kelele Uwesu! Angalia mbele huko!” Sauti ilifoka kutoka kwenye kiti cha nyuma cha lile gari, lakini muda huo, Esmund Bwaira aliyekewa kule mbele pamoja na Uwesu aliachia mbinja kubwa ya kishabiki na hapo hapo akaanza kuangusha wimbo wa kihindi kwa sauti lake zito la kilevi. Na Elvis Presley naye alizidi kulalama kutokea kwenye redio ya lile gari na Heart-break Hotel yake. Basi ilimradi ilikuwa ni zogo mtindo mmoja ndani ya gari, na yule kijana wa tatu aliyekuwa kwenye kiti cha nyuma alizidi kuchukia.

“Hebu acheni kelele bwana! Hamuoni kuwa huu ni usiku? Na tuko katikati ya mapori huku!” Chambuso Mwagala aliwakemea wenzake huku akijipenyeza baina ya vile viti viwili vya mbele na kunyoosha mkono wake kuizima ile redio.

“Aaah! ‘asa we’ alokukataza usinywe pombe nani bwana? Mbo’ un’tukera bure wenzio weyee? Hhih!” Uwesu alilalama kilevi kwa lafudhi yake ya ki-Pemba na hapo hapo akaangua kicheko kikubwa. Chambuso hakuwa kwenye ari ya kucheka kabisa.

“Nyie mnajua kuwa mimi si mlevi kama nyie! Na mnajua kuwa mwenzenu nina safari ndefu… mnataka kunitilia nuksi kwenye safari yangu bwana!” Alimkemea Uwesu huku akiielekeza kauli yake kwa Esmund pia, ambaye bado alikuwa akitumbuiza kwa kelele na ule wimbo wake wa kihindi.

“Aaah! Chambu’ weeee! Si we’ mwenyewe nd’o uliyetaka tukulete kwenu kabla hujapanda ndege kwenda huko ulaya! Sasa… tena imekuwa tunakutilia nuksi…?” Esmund alidakia huku akimgeukia Chambuso kule alipokuwa.

“Ndiyo eenh! Sasa kama si kutiana nuksi kitu gani huku! Watu mmeenda kubugia mipombe huko halafu mnaendesha gari kwa fujo na mikelele usiku kama huu? Hujui unawakera akina nani saa hizi ati! Huku vijijini bwana! Watu wamelala saa hizi…!” Chambuso alimjibu kwa jazba, na alikuwa anataka kuendelea kumjibu, lakini Uwesu alimkatisha. “Halafu ni bibi yako mwenyewe… tena bibi mzaa baba, ndiye aliyekukarisha hivyo vijipombe ili na si’ tuonje japo kidogo, sasa tena weye …”Alimwambia huku akigeuka nyuma kumtazama, tena akisisitiza kauli zake kwa mikono yake yote miwili, akisahau kuwa alikuwa akiendesha gari. Gari lilianza kuacha njia na kuingia porini. “Hebu tazama mbele wewe!” Chambuso alimpigia kelele Uwesu baada ya kuona gari lilikuwa likiacha barabara. Uwesu aliachia yowe kubwa la woga huku akigeuka kuangalia mbele, tayari gari lilikuwa limeshaacha njia, naye akawa akihangaika kuliweka sawa na kulirudisha barabarani. Esmund alipiga kelele huku akitupwatupwa huku na huko wakati gari likiparamia matuta ya viazi yaliyokuwa kando ya barabara. Chambuso, aliyekuwa kwenye kiti cha nyuma alikuwa ameng”ang”ania migongo ya viti viwili vya mbele vya gari huku akisukwasukwa na kutupwa tupwa na mitikisiko ya gari ile, matusi yakimtoka mfululizo kulaani hali ile kwa hasira.

“Nil-llise-ee-mma mi-mim! Nili-se-m-mma mii-mii…!” Alikuwa kipiga kelele akiwa ameng”ang”ania migongo ya viti vya mbele vya gari. Gari lilijipiga kwenye tuta moja na kutupwa hewani, kwa sekunde chache sana lilibaki likielea huko, ila wale vijana waliona kama kwamba lilikuwa likielekea hewani milele.

“Yeeeee! Tunakufa! Uwesu unatu-uaaaaaa!” Esmund Bwaira alipiga kelele, akitupwa juu na kupigiza utosi kwenye paa mle ndani ya gari na kubwagwa tena kwenye kiti, na kuserereka hadi kwenye sakafu ya gari.

“Ndiyo nuksi zenn-yewe hiiz-ziii…Aaaakh…!” Chambuso alilalama kwa hasira.

Uwesu alikuwa akihangaika na usukani huku akibwabwaja maneno yasiyoeleweka asilani, ingawa akilini mwake alikuwa akiamini kuwa alikuwa akimtaja mungu na kumtaka msaada. Muda huo Chambuso aliinua uso na kutazama mbele yake akiwa ametumbua macho, na kupitia kwenye kioo cha mbele cha gari aliona mwanga mkali wa taa za gari lile ukimulika mkorosho mkubwa uliokuwa mbele yao. Na hata alipokuwa akiukodolea macho mti ule, aliuona ukiwajia kwa kasi na akilini mwake akajua kuwa sasa hakika nuksi aliyokuwa akiihofia ilikuwa imetimia.

Gari lilikuwa linaenda kuugonga ule mti kwa kishindo kikubwa, na bila kutaka, yowe kubwa la woga lilimtoka, wakati huohuo akimsikia na Uwesu naye akipiga kelele kwa sauti iliyosheheni woga mkubwa kwani naye alikuwa akiliona gari lao likielekea kuubamiza ule mti, na hakuwa na lolote aliloweza kulifanya kuokoa maisha yao.

“Mama Weeeeeeeeeeeee!” Uwesu alilia kwa kihoro, hapana shaka pombe zikiwa zimetoka na sasa alikuwa akisubiri na roho tu imtoke. Bila kufikiri alijikuta akiachia usukani na kujikinga kichwa chake kwa mikono yake.

“HAH! Unaachia usukani tena!” Chambuso alipiga kelele huku akiuona ule mti ukizidi kuwakaribia kwa kasi. Esmund alikuwa akilia kama mjinga akiwa chini ya kiti cha mbele cha ile gari huku akihangaika kufungua mlango ili aruke nje, lakini kila akijaribu kufungua mlango ulikuwa haufunguki! Pasina kujua, alikuwa akijaribu kufungua mlango ule kwa kutumia kishikio cha kushushia kioo badala ya kile cha kufungulia mlango.

Ilikuwa ni kimuhe-muhe kweli kweli!

Gari lilizidi kuuendea ule mti kwa kasi, na huku mayowe yakiendelea kumtoka, Chambuso Mwagala alijitupa chini nyuma ya vile viti viwili vya mbele, kwenye uwazi uliokuwa baina ya vile viti na kile cha nyuma alichokuwa amekalia, na kujikinga kichwa chake kwa mikono yake. Akilini mwake alikuwa akisubili tu kishindo wakati ile gari ikijibamiza kwenye ule mti na mti na akiijutia nafsi yake kwa kutaka safari ya kwenda kijijini kwao Mzenga kumuaga bibi yake kabla ya kupanda ndege alfajiri ya siku iliyofuata kuelekea Uingereza.

Na sasa naelekea kupanda jeneza kuelekea kuzimu…

Ndilo wazo lililopita kichwani mwake kabla kishindo kikubwa hakijalitikisa lile gari, kikiambatana na yowe kubwa na refu kutoka kwa Uwesu Shaame, sawia na yowe dhaifu na la kuogofya kutoka kwa Esmund Bwaira.

Kioo cha mbele kilipasuka kwa kishindo kikubwa, na vipande vya vioo vikiwamwagikia kama mvua ndani ya ile gari, ilhali michanga kutoka nje ikitupwa hewani na kuwamwagikia wote waliokuwamo ndani ya gari pamoja na vile vipande vya vioo.

Chambuso Mwagala alijishuhudia akiinuliwa mzima mzima kutoka kwenye sakafu ya ile gari alipokuwa amejikunja na kutupwa juu kwa nguvu, mgongo na kisogo chake vikipigizwa vibaya kwenye paa la gari kwa ndani, kabla ya kubwagwa tena kwa nguvu kwenye kiti cha nyuma, ambako alidunda kama mpira na kupigiza tena mgongo wake kwenye mgongo wa kiti cha dereva na kuanguka tena pale kwenye ule uwazi baina ya viti vya mbele na kile cha nyuma, kichwa chake kikipigiza kwenye bati gumu lililofanya sakafu ya lile gari. Kisha taratibu akahisi macho yake yakipoteza nuru, na sauti zote zilizokuwa zikisikika masikioni mwake – vishindo vya lile gari, sauti yake mwenyewe wakati akilalama hovyo huku akitupwatupwa mle garini, na yale mayowe ya wenzake- zote zikififia taratibu na kuwa kimya kabisa.

Kisha, kwa utaratibu ule ule, aliuhisi mwili wake ukiwa kama pande moja kubwa na zito la nyama, lisilo na mfupa hata mmoja. Oh Mungu wangu… nd’o n’nakufa hivi…!

* * *

Ndani ya pango lililokuwa chini ya mlima Kazimzumbwi, kijijini Kazimzumbwi, wilayani Kisarawe, wale wazee saba waliendelea kusubiri kwa ukimya ulioficha hisia zao za hofu juu ya siku ile muhimu na ya hatari sana kwao iwapo jambo moja tu kati ya yale waliyotakiwa kuyatekeleza siku ile halitakwenda itakiwavyo. Walikuwa wamekaa nusu duara, miguu yao ikiwa imekujwa kama wanaosubiri mlo, migongo yao ikiwa imenyooka wima na mikono yao wakiwa wameilaza juu ya magoti yao, viganja vyao vilivyofunuliwa vikiwa vimeelekezwa juu.

Kiasi cha hatua kumi hivi za mtu mzima mbele yao kulikuwa kuna jiwe moja kubwa na refu, ambalo uso wake bapa ulikuwa umeelekea kwenye paa la pango lile.Jiwe lile lilikuwa limelala juu ya mawe mengine makubwa mawili, na moja kwa moja kuleta taswira ya meza kubwa ya jiwe iliyokuwa na urefu uliopata futi saba na upana uliopata futi nne. Ni jinsi gani hata jiwe lile likawa na hali iliyofanana na meza hakuna binadamu anayeweza kufahamu, ila wengi miongoni mwa binadamu wangeweza kuamini kuwa ile ilikuwa ni moja kati ya kazi au miujiza ya Mwenyezi Mungu…

Kuizunguka meza ile kulikuwa kuna vibuyu vikubwa vilivyokuwa na shingo ndefu na nyembamba. Kwenye ncha ya kila shingo ya vibuyu vile kulikuwa kunawaka moto ulioleta mwanga ndani ya pango lile lililojaa matando ya buibui na wadudu wengi wa hatari kwa binadamu. Vile vibuyu vilikuwa ni mishumaa mikubwa iliyotoa mwanga wa kutosha ndani ya pango lile. Mwanga uliotokana na mishumaa ile ya aina yake, ulitupa vivuli vya kutisha kwenye kuta za pango lile ambalo hakuna binadamu yeyote aliyewahi kuliingia tangu miaka mingi sana iliyopita, huku ukifanya sura zilizokunjamana za wale wazee wa ajabu zionekane kuwa ni za kutisha zaidi.

Baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu, wote wakiwa wamefumba macho yao na wamekunja nyuso zao kama waliokuwa mwenye mawazo mazito au wakijaribu kusikiliza sauti fulani kutokea mbali, hatimaye moja wa wale vikongwe watatu wanawake alifumbua macho yake mekundu na ya kutisha na kuwatazama wenzake mmoja baada ya mwingine, kisha macho yake yakatulia kwa mzee wa kiume aliyekuwa ameketi mbele kidogo ya wenzake, naye akiwa ameelekeza uso wake kule ilipokuwa ile meza kubwa ya jiwe.

Mxulu…mbona mwenzetu yuko kimya? Muda unakwenda!

Alimuuliza kwa sauti iliyotetema kwa uzee, lakini bila shaka pia ni kutokana na hofu iliyomdhibiti, huku macho yake yakionesha wahka mkubwa.Ajabu ni kwamba sauti le ilisikika kichwani kwa yule aliyembiwa tu, na vichwani mwa wale wengine waliokuwa ndani ya pango lile usiku ule. Yaani yule bi kizee alitamka maneno yale bila kufumbua kinywa chake hata kidogo, na bado wale wenzake wote mle pangoni walimsikia vizuri sana. Wale watu, kama utaweza kuwaita watu, walikuwa wakiongea kwa kutumiana ujumbe kwa njia ya mawazo na sio kwa midomo!

Na hapo sauti za wale wengine nazo zilisikika zikiongea kukubaliana na hoja ya yule msemaji wa kwanza.

Ni kweli…!

Hata mimi nimekuwa nikimsemesha kwa muda mrefu…kimya tu!

Sasa itakuwaje jamani…?

Lakini wote walikuwa wameketi kama walivyokuwa, miguu yao wameikunja, midomo yao imefumbwa, na macho yamefumbwa, wakionekana kuwa kimya kabisa!

Yule kikongwe aliyeitwa kwa jina la Mxulu aligeuza kichwa chake taratibu kumuelekea yule msemaji wa kwanza, kisha akafumbua macho yake taratibu na kumtazama moja kwa moja usoni. Iwapo ingetokea mtu yeyote ambaye si miongoni mwao kuwepo katika eneo lile muda ule, kwa hakika angetishika vibaya sana, kwani walileta taswira moja ya kuogopesha sana, kwa sababu kitu ambacho angekuwa akikiona wakati ule ni jinsi yule bibi kizee alivyofumbua macho yake ya kutisha na kumgeukia yule kikongwe wa kiume, akimtazama kwa macho yaliyojaa wahka bila ya kusema neno. Kisha angemuona yule kikongwe wa kiume akigeuza uso wake taratibu na kufumbua macho yake kumtazama yule bi kizee moja kwa moja usoni. Pasina na yeyote kati yao kuonekana akisema lolote.

Na wakiwa uchi wa nyama…kama walivyozaliwa…iwapo walizaliwa!

Ni kweli…nami nimekuwa nikimuita kwa muda mrefu bila majibu…

Mxulu alijibu huku bado akimtazama yule bibi kizee wa kwanza, kinywa chake, kama wenzanke, kikiwa kimetulia kama cha mtu aliyelala usingizi.

Sasa…?

Bibi kizee mwingine alidakia kwa mashaka makubwa.

Atakuwa amekumbwa na tatizo kubwa…akili yake haijatulia, na ndio maana tunashindwa kuungana na mawazo yake huko aliko!

Mxulu aliwaeleza wenzake jambo ambalo alifahamu kuwa wanalijua fika, ila tu woga ulikuwa unawafanya watafute matumaini kutoka kwake, kiongozi wao.

Kwa hiyo sasa ndio tunaangamia, Mxulu!

Mwingine aliongea, mashaka yakijidhihirisha wazi katika sauti yake.

Hapana…atakuja tu. Hata kama amekumbwa na tatizo zito namna gani, ni lazima aje…kwani anajua kwamba akishindwa katika hili ni kwamba sio tu anatuangaiza sisi sote, bali na yeye mwenyewe pia!

Lakini muda sasa Mxulu…!

Tuwe na subira! Tumevuka vikwazo vingapi mpaka kufikia hapa, eeenh?

Sasa Mxulu alikuwa mkali, na wote wakagwaya. Hakuna aliyetaka kukabiliana na Mxulu akiwa katika hali ya ghadhabu hata kidogo, na kimya kikatawala ndani ya pango lile la kutisha. Safari hii kilikuwa ni kimya halisi.

Nje ya pango lile upepo mkali ulivuma, na kwa mbali ilisikika sauti mbaya ya fisi akilia na wakati huo huo akisikika kama kwamba alikuwa akicheka…

Wakati huo huo, katika ule uwanja mkubwa wa michezo katikati ya jiji, sherehe na shamrashamra ziliendelea. Wahudhuriaji walikuwa wakisubiri wakati muafaka ili waadhimishe lile lililowafikisha uwanjani pale usiku ule kwa maelfu na maelfu, na kushuhudia historia mpya ikiandikwa nchini. Ingawa kwao ile ilikuwa ni siku muhimu sana, lakini ule muda waliokuwa wakiusubiri, ile saa iliyokusudiwa, ndio ulikuwa na umuhimu kuliko kitu kingine chochote ndani ya usiku ule. Kwani ile itakuwa ni saa ambayo itakumbukwa nao, na vizazi vyao vyote vitakavyofuatia baada yao…

Ghafla bila tahadhari yoyote, mlipuko mkubwa sana ulisikika na uwanja wote ukalipuka kwa vilio na kelele za woga na fadhaa. Kwa namna fulani watu wote walijikuta wakiinua nyuso zao kutazama juu angani ambako ndiko ule mlipuko uliposikika ukitokea. Na ndipo kwa kihoro kikubwa sana, watu wote waliohudhuria uwanjani pale usiku ule, waliposhuhudia mwanga mkali na mkubwa ukiwashukia kwa kasi sana kutokea kule angani huku ukitupa miale mirefu ya moto na cheche ambazo kwa hakika hazikuwa zikitokana na fataki ya aina yoyote hapa duniani. Kilikuwa ni kitu kama kimwondo kikubwa kilichokuwa kikianguka ardhini kwa kasi huku kelele na mvumo kubwa zikiambatana na muanguko ule.

Shamra shamra zilibadilika na kuwa tafrani. Wananchi walikimbia hovyo huku na huko, wakikanyagana huku wakipiga mayowe kuliko walivyowahi kupiga maishani mwao, baadhi yao wakimlaani ibilisi aliyewapanda na kuwashawishi kwenda pale uwanjani usiku ule. Na hata wakati wakikimbia huku na huko, hakuna aliyejua kuwa kile alichokuwa akikikimbia kilikuwa ni kitu gani na kilikuwa kinaelekea kuangukia wapi hasa.

Ghafla, kama jinsi ulivyotokea, ule mwanga, au kile kitu kilichokuwa kikishuka kwa kasi kutoka angani huku kikitupa mwanga mkali uumizao macho, kilipotea! Yaani kiliyeyuka ghafla tu. Kiza kikatawala pale uwanjani kwa muda mfupi sana, na kisha taa zote za pale uwanjani zilimwemwesa-mwemwesa kwa muda na kurudia tena kuwaka kama hapo awali.

Kama kungekuwa na mtu yeyote ambaye angekuwa akizingatia muda ambao tukio lile lilidumu uwanjani pale usiku ule, angegundua kuwa lilikuwa limedumu kwa muda wa sekunde zisizozidi thelathini.

Nusu dakika tu!

Mayowe ya fadhaa yalibadilika na kuwa vifijo vya furaha, huku wengi wa waliokuwapo pale wakijiuliza ni nini hasa kile kilichotokea. Wengine walipitisha uamuzi kuwa ile ilikuwa ni hitilafu mbaya ya umeme, lakini imerekebishwa haraka sana, na hivyo kuendelea na shamrashamra zao. Wengine wakiamini kuwa ile ilikuwa ni moja kati ya fataki zilizokuwa zikilipuliwa sehemu mbali mbali jijini wakati ule, ambayo ilikuwa imelipuka vibaya na kuleta tafrani na wasiwasi ndani ya nyoyo za watu.

Lakini wengine, hasa wale ambao walipoteza uwezo wao wa kuona siku ile kutokana na mboni zao kuunguzwa vibaya na mwanga ule wa ajabu, waliamini kuwa kile kitu, chochote kiwacho, kilikuwa ni kitu kibaya na cha hatari sana. Hakika kwao, lile halikuwa tukio la kawaida hata kidogo.

Vikundi vya ngoma na muziki vilivyokuwa vikitumbuiza vilijipanga upya na kuanza kuendelea tena kutumbuiza na kuwavuta tena watu kwenye majukwaa yao. Mtangazaji aliyekuwa akitoa mwenendo wa matukio pale uwanjani alisikika kutoka kwenye kipaza sauti akiwataka wananchi watulie na waendelee na shamrashamra zao kama kawaida, huku akiwataka radhi kwa hitilafu ndogo ya umeme iliyojitokeza na kuwaahidi kuwa hali hiyo sasa ilikuwa imedhibitiwa na haitatokea tena.

Hakika alikuwa hajui asemalo hata kidogo!

Uwanja uliripuka tena kwa shangwe na vigelegele. Burudani ziliendelea kama hapo awali, wakati bila ya wale waliokuwa wakirudia kusherehekea kujua, baadhi ya watu waliokuwa kwenye maumivu makubwa, walikimbizwa nje ya uwanja ule na jamaa zao kuelekea hosptali wakiwa wamepofuliwa na mwanga ule mbaya.

Kadiri shamrashamra zilivyozidi kurudia hali yake, ndivyo tukio lile lilivyozidi kusahaulika pale uwanjani wakati muda uliokuwa ukisubiriwa ili kuadhimisha shamrashamra zile ukizidi kukaribia.

* * *

Na ni katika muda ule ule ambapo kilometa kadhaa nje ya jiji, ile gari aina ya Ford Anglia ilipojikita kwa kishindo kikubwa kwenye tuta kubwa la viazi hatua mbili tu kutoka kwenye shina la ule mti mkubwa wa mkorosho, na kusota kwa msukumo wa kasi iliyotoka nayo kule barabarani huku ikitimua michanga na udongo kutoka kwenye matuta yaliyokuwa eneo lile, ikizidi kuserereka kwa nguvu, kabla ya kuubamiza vibaya ule mti na kupasua kioo cha mbele cha lile gari. Kimya kilitanda ndani ya gari ile wakati wale vijana waliokuwa ndani yake wakiwa wamepigwa na mshituko mkubwa. Kwa muda wote walikuwa kama waliopoteza fahamu, kisha Uwesu Shaame aliyekuwa akiendesha, aliinua uso wake taratibu kutoka kwenye usukani wa gari ile aliokuwa ameulalia na kutazama mbele yake, vipande vya vioo vikipukutika kutoka kichwani na mabegani mwake. Damu ilikuwa ikimchuruzika kutoka kwenye jeraha katika paji lake la uso baada ya kupigiza kichwa chake kwenye usukani wa gari pale ilipojikita kwenye ule mti.

Aliona nyota nyingi zikiwa zimetanda mbele ya mti ule, na kizunguzungu kikimkabili. Alikohoa kwa nguvu na kutema rundo la michanga, hata hajui ilifikaje kinywani mwake muda ule, lakini angalau alijiona kuwa alikuwa mzima.

Na ndipo alipowakumbuka wenzake.

“Ah! Esmund! Chambu…! Chamb…oooh Mungu wangu! Nimeua! Nime-oooh, Mama yangu!” Alibwabaja kwa hofu huku akiangua kilio na kufungua mlango wa gari ile na kutoka nje. Alipiga mwereka nje ya mlango wa gari ile na kubingirika kwenye matuta mawili yaliyokuwa karibu yake, akizidi kujitapakaza michanga. Kisha aliinuka na kuliendea lile gari kwa mwendo wa kuyumba-yumba, macho yakiwa yamemtoka pima na pombe zote zikiwa zimemyeyuka kichwani.

Na hata kabla hajaufikia mlango wa nyuma wa ile gari, aliuona ule mlango ukisukumwa kwa nguvu na kufunguka, na kwa mshangao mkubwa alimuona Chambuso akitambaa kutoka ndani ya ile gari huku akikohoa na kutema mate ambayo kama kungekuwa kuna mwanga wa kutosha, angeona kuwa yalikuwa yamechanganyika na damu.

“Chambu! Chambu! U-mzima rafiki yangu?” Uwesu alimkodolea macho Chambuso huku akijaribu kumkimbilia, na kujikwaa kwenye tuta jingine la viazi na kupiga mwereka mwingine mzito.

Chambuso Mwagala aliinuka kwa taabu na kusimama huku akiyumbayumba nje ya ile gari. Alimsikia na alimuona Uwesu akipayuka hovyo na kupiga mwereka, lakini akili yake haikuwa ikimtilia maanani kabisa. Alikuwa akijiuliza iwapo alikuwa ameshakufa na sasa ile ilikuwa ni roho yake tu ikimlaghai kuwa bado hajafa. Kichwa kilikuwa kikimgonga vibaya sana na alipeleka mkono wake kupapasa upande wa kichwa chake yalipokuwa yakitokea maumivu makali zaidi, na kugundua kuwa kulikuwa kumeota nundu kubwa, bila shaka ni pale alipopigiza kichwa chake kwenye sakafu ya bati gumu la gari ile.

“Chambu! Umeumia? Ume…” Uwesu alikuwa akimsemesha kwa kiherehere huku akimshika mabega, na hapo akili yake ilianza kurudi taratibu. Alimtazama kidogo bila kusema kitu, kisha akamkumbuka Esmund.

“Ahh…Esmund! Hebu mcheki Esmund…!” Alimwambia Uwesu kwa wasiwasi, kisha akaona Uwesu atachelewa, akaanza kuita huku akikimbia kwa taabu kuelekea upande wa pili wa gari lile, ambako mlango wa kule alikokuwa ameketi Esmund ulikuwako.

“Esmund! Esmuuund…!”

Na Uwesu naye alianza kumfuata nyuma huku akiita jina la rafiki yao kwa hofu kubwa.

Upande wa pili wa ile gari walikuta mlango wa abiria kule mbele ukiwa wazi, Esmund akiwa amelala chali nje ya mlango ule ilhali miguu yake bado ikiwa ndani ya gari ile. Walimkimbilia na kujibwaga kando yake huku wakiita jina lake kwa woga na wasii wasi mkubwa.

Lakini Esmunda alikuwa kimya.

Chambuso alimtazama kwa makini na kuweka sikio lake kifuani kwa Esmund, kusikiliza iwapo moyo wake ulikuwa ukipiga, wakati huo Uwesu alikuwa akizidi kuita huku akilia kijinga.

“Esmund! Eeeh, Esmund, eee…hebu itika basi raf”ki yangu, eenh?” Uwesu alimwita huku akimtikisha kwa nguvu.

Chambuso alisikia moyo wa Esmund ukipiga kama kawaida. Aliinua kichwa chake na kumwambia Uwesu.

“Hebu acha mikelele yako huko! Au ndio mipombe yako inavyokutuma? Moyo wake unapiga, hebu tumuinue…”

Uwesu alikurupuka na pamoja walimuinua mwenzao na kumkalisha. Mara Esmund alianza kukohoa kwa nguvu, mate yakiwa yamempalia.

Ilikuwa ni furaha kubwa kumuona mwenzao akiwa mzima. Walianza kumpigapiga mgongoni kumpoza huku wakimpa pole.

“Duh! Tumepona? Hatimaye Esmund aliuliza kwa mashaka huku akiwatazama wenzake.

“OOOH Mungu ashukuriwe! Tumepona bwana! Yaani pale nilijua kuwa sa” si” nd”o basi tena! Aaah, Mungu”uuyu!” Uwesu alisema kwa sauti huku akiinua mikono juu kwa ishara ya kushukuru. Chambuso alimtazama kwa hasira huku akiinuka. “Unashukuru kinafiki sio? Ulitakiwa umkumbuke Mungu kabla hujaanza kubugia hiyo mipombe yako! Ona sasa!Hii si ndio nuksi niliyokuwa nikiisema hii?(akasonya).Sasa sijui hata kama hii gari itatembea tena!” Alisema huku akiizungukia mbele ile gari na kuitazama kwa karibu baada ya kuona kuwa wote walikuwa salama…angalau kwa wakati ule. Uwesu aliinuka na kumfuata huku akijikwaa kwenye matuta yaliyokuwapo eneo lile.

“Bakhti mbaya tu Chambu…zilikuwa ni pombe tu rafiki yangu, lakini sasa…”

“Lakini sasa ujinga tu Uwesu…ujinga tu!” Chambuso alimkatisha kwa hasira na kusonya huku akitupa mikono yake hewani. Esmund aliinuka kwa taabu huku akigumia kwa maumivu na akijishika kisogoni alipopigiza kichwa chake wakati gari ile ilipojibamiza kwenye mti. Chambuso alikuwa akitazama madhara ya ajali ile ya kijinga kwenye gari lao. Sehemu ya mbele ya ile gari ilikuwa imebonyea vibaya, boneti likiwa limefunuka na moshi mwepesi ukitoka chini ya boneti lile. Taa za mbele zilikuwa zikiendelea kuwaka, ingawa kioo cha taa ya kulia kilikuwa kimepasuka, na ile gari ikitoa mvumo hafifu.

Chambuso alikuwa akiitazama ile gari huku akiwa amejishika kiuno, akili yake ikienda kwenye safari yake ya alfajiri ya siku iliyofuata. Ile gari ilijikita kwenye tuta moja la viazi lililokuwa kiasi cha kama mita tatu hivi kutoka kwenye ule mti mkubwa. Na ni lile tuta ndilo lililopunguza kasi ya lile gari na kupooza kwa kiasi kikubwa sana nguvu ya kishindo cha ile gari wakati lile gari lilipojipigiza kwenye ule mti. Mita zote tatu kutokea pale lile gari lilipojikita kwenye lile tuta hadi lilipoenda kugota kwa kishindo kwenye ule mti, zilikuwa ni kama kwamba zimetifuliwa kwa tingatinga la kuchonga barabara. Viazi vitamu vilikuwa vimetawanyika kila upande, na bila shaka kama si kwa lile tuta hakuna ambaye angetoka salama kwenye ile ajali. Ghadhabu zilimpanda Chambuso na alimgeukia Uwesu kwa jazba.

“Unajua ungetuua bure wewe? Sasa kama uliona ulikuwa umelewa sana si ungesema tu? Yaani kumbe nilikuwa nimefanya kosa sana kuwaomba mnisindikize huku, eenh?”

Uwesu alikuwa kwenye wakati mgumu. Alimtazama Chambuso kwa fadhaa iliyochanganyika na aibu na wasiwasi.

“Ah, Chambu…sikufanya kusudi bwana! Ni pombe tu…na…hata mimi sikujua kuwa ile pombe ilikuwa imenilewesha kiasi kile! Ilikuwa kali sana ile…we’ mwenyewe si uliona kuwa nilikunywa kidogo tu?”

“Bull shit, Uwesu, Bull Shit! Hebu ona sasa…!” Chambuso alimaka huku akilioneshea lile gari kwa mikono yake yote miwili, kisha akaendelea, “…usiku kama huu…! Unakuja kutukwamisha porini namna hii!”

“Aaah, gari inaonekana kama haijaharibika sana, Chambu…”

“Akhhh! Haikutakiwa iwe hivi kabisa Uwesu! Sasa unafikiri tukikwama huku usiku huu tutapata msaada kutoka wapi na huku tuko katikati ya zama za mwanzo za ujima! Si ndio mmenikosesha safari hivi hivi jamani!” Chambuso alizidi kulalama.

Uwesu alifunua zaidi boneti la gari na kupeleka mkoo ndani yake, akijaribu kuchunguza iwapo kuna athari yoyote kubwa kwa kutumia ule mwanga hafifu wa taa za lile gari. “Hebu ngoja basi tuitazame kwanza Chambuso…si ajabu we” una wasiwasi wa bure tu. Badala ya kushukuru tumesalimika na ajali we” walalama tu!” Alisema kwa sauti iliyooonesha wazi kuwa hata yeye mwenyewe hakuwa akiamini kile alichokuwa akikisema. Chambuso alitaka kumjibu kwa jazba, lakini muda huo Esmund naye alifika pale walipokuwapo akiwa amejishika kisogo. Taa za gari zilimmulika na Chambuso aliona baka kubwa jeusi la duara likiwa sehemu ya mbele ya suruali yake ya khaki, na kubaki akiikodolea macho sehemu ile kwa mshangao. Esmund aliona jicho la Chambuso lilipoelekea, naye aliinamisha kichwa chake kujitazama sehemu ile ya suruali yake iliyolowa kwa mkojo.

“Haya sasa! Mtazame mwenzio kajikojolea huku…ujinga-ujinga tu!” Chambuso alimuambia Uwesu kwa hasira iliyochanganyika na dharau.

“E bwana we!” Uwesu aliropoka huku akigeukia kule alipokuwako Esmund na kumtazama usoni kwa muda, kisha akateremsha macho yake pale kwenye ile sehemu ya suruali iliyolowa mkojo, na kumtazama tena usoni kwa mshangao.

“Ama! “asa na we” nd”o umeenda kujikojolea moja kwa moja?” Alimuuliza kwa mshangao kama vile Esmund alipenda mkojo umpite wakati alipokuwa akihangaika kufungua mlango wa gari ile kwa woga huku akijua kuwa walikuwa wakikiendea kifo, tena kwa kasi sana. Esmund aligwaya kwa aibu na kubaki akiwa amesimama kibwege huku akijipapasa kisogo chake. Chambuso alijikuta akiachia kicheko cha dharau huku akitikisa kichwa.

“Jamani pombe hizi…”

“Achana na hayo basi Chambu! Hebu njoo tusaidiane kuitoa hapa hii gari!” Uwesu alimuambia. Walirudia kuishughulikia ile gari. Baada ya kushika shika ndani ya ile boneti kwa muda na kuona kuwa hakukuwa na kitu chochote muhimu kilichovunjika au kuchomoka kutokana na ajali ile, Chambuso aliingia nyuma ya usukani na kujaribu kupiga stati. Hakuna kilichotokea.

Alijaribu tena, na safari hii gari ilikoroma kwa muda kisha ikazima.

Shit!

Akajaribu tena, mambo yakawa yale yale.

Pumm-baavu!

Akajaribu tena, safari hii gari ikakoroma kwa muda kasha ikawaka. Esmund na Uwesu walishangilia kwa furaha wakiwa nje ya ile gari, naye akapiga resi mara moja, ya pili, ya tatu, na gari ikazima tena.

Bloody Shit Uwesu!

“Itawaka hiyo Chambu…jaribu tena!” Esmund alimuambia kupitia dirishani, na Chambuso alimtukana tusi zito la nguoni kimoyo moyo. Akapiga tena stati, na safari hii gari ikawaka ipaswavyo. Wakati Esmund na Uwesu wakikumbatiana huku wakiruka ruka kwa furaha kule nje, Chambuso aliingiza gia na kuanza kurudi nyuma ili kutoka pale chini ya mti na kuirudisha gari barabarani, lakini gari ilirudi kidogo tu na kukwama kwenye michanga na matuta ya eneo lile.

“Haya walevi…tumekwama sasa. Itabidi mnisukume turudishe gari barabarani.” Chambuso aliwaambia.

“Mlevi bibi yako aliyetupikia pombe kali mpaka…” Uwesu alimjibu kwa hasira huku akianza kuliendea lile gari, na kabla hajamaliza kauli yake Chambuso akamkatisha.

“Mpaka mnajikojolea! Hebu sukumeni gari huko!”

Huku wakilalamika kwa kuitwa walevi, Esmund na Uwesu walianza kuisukuma ile gari kuirudisha barabarani. Dakika kumi baadaye, walifanikiwa kuirudisha ile gari barabarani. Chambuso alitoa kifyagio kutoka kwenye buti la gari ile na kwa msaada wa taa ya ndani ya gari alianza kufagia haraka haraka michanga na vipande vya vioo kutoka ndani ya gari, wakati wenzake wakiwa wameketi katikati ya barabara wakimsubiri huku wakitweta baada ya kusukuma ile gari, na wakizidi kulalamika kwa kuitwa walevi.

“Halafu nyie mnanishangaza sana. Yaani mnafakamia mipombe ya kienyeji huko hadi mnajikojolea, halafu mnataka muitwe waswalihina na watakatifu?” Chambuso aliwaambia na kuwauliza kwa kejeli wale wenzake huku akiendelea kufagia. Wale jamaa walizidi kukosa raha kwa kauli ile, lakini Chambuso hakujali. Kote kulikuwa kimya, na kiza kilikuwa kizito sana.

Dakika tano baadaye, Ford Anglia ilikuwa tena barabarani kuelekea jijini Dar, safari hii ikiwa haina kioo cha mbele, kioo cha taa moja ya mbele kikiwa kimepasuka, sehemu yake yote ya mbele ikiwa imebonyea vibaya sana, na Chambuso Mwagala akiwa peke yake kule mbele, nyuma ya usukani. Uwesu na mlevi mwenzake Esmund walikuwa wamenuna kwenye kiti cha nyuma cha gari ile. Nje ya gari ile, upepo mkali ulianza kuvuma, na kwa mbali sana, ulisikika mlio wa fisi uliosisimua miili ya wale vijana kutoka mjini.

* * *

Kimya kilichokuwa kimeligubika lile pango lililojaa hofu na nia mbaya kilivunjika ghafla pale sauti ya mwanamke aliyekuwa akiongea huku akihema kwa taabu sana, iliposikika vichwani mwa wale wazee waliokuwa mle ndani.

Niko njiani…! Nakuja…

Wote waliokuwamo mle ndani waliinua vichwa vyao na kufumbua macho yao. Waligeukiana taratibu na kutazamana, wakionekana kuwa kimya kabisa, lakini akili zao zikifanya kazi haraka haraka sana.

Uko wapi…mbona umechelewa hivi? Tumekuwa tukikuongelesha lakini…

Mxulu alimjibu kwa swali yule mwanamke aliyewasemesha kutokea mbali.

Ni hadithi ndefu Mxulu …mambo yaliharibika jamani…!

Wote waliokuwa mle pangoni walitazamana tena huku baadhi yao wakitoa miguno ya hofu kwa sauti, si kwa mawazo tena kama hapo awali. Mxulu alikuja juu.

Sasa tuambie kitu kinachoeleweka! Mambo yaliharibika ndio maana yake unatuambia nini?

Kimya.

Hivi unajua kuwa uhai wetu sote hapa, pamoja na wewe mwenyewe huko uliko, unategemea wewe kutimiza jukumu lako?

Mxulu aliendelea kufoka pasina kufungua kinywa, ilhali macho yake mekundu yaliyosheheni ghadhabu yakitembea huku na huko ndani ya pango lile.

Kimya tena.

Wee binti Beho! Hebu nijibu…mbona kimya?

Mxulu alizidi kubwata kwa wahka, na hapo mmoja wa wale vikongwe wa kiume aliyekuwamo mle ndani alidakia kwa kiherehere.

Anafifia Mxulu! Anafifia…Najaribu kuingia akilini mwake huko aliko, lakini…lakini anafifia!

Wote mle ndani walitazamana kwa muda, hofu ikijidhihirisha katika nyuso zao, kwani walielewa ni nini maana ya hali ile ingawa walishindwa kuamini; kwani hali ya mawazo ya yule mwenzao waliyemtambua kama binti Beho kufifia kila walipojaribu kuungana naye kimawazo, ilimaanisha kuwa mwenzao yule alikuwa kwenye maumivu makali sana. Maumivu yaliyomfanya akaribie kupoteza fahamu zake, na hivyo kushindwa kuungana naye kimawazo huko aliko na kuongea naye.

Binti Beho!

Mxulu aliita tena akili mwake.

…ku…ja…

Binti Beho alisikika kwa mbali sana, kama jinsi ambavyo unavyoweza kumsikia mtu unayeongea naye kwa simu ya kiganjani ilhali uko kwenye sehemu ambayo mtandao wa simu uko chini sana. Kimya cha butwaa kilitanda ndani ya pango lile.

Na ni wakati huu ndipo ambapo upande mwingine wa mkoa ule ule, kiasi cha kilometa kumi na tano hivi kutoka kwenye ule mlima wa Kazimzumbwi, ambapo chini yake ndipo lilikuwapo lile pango lililohifadhi wale wazee wa ajabu, lile gari aina ya Ford Anglia lilipoparamia tuta kubwa la viazi na kusota kwa kasi kabla ya kujibamiza kwa kishindo kwenye ule mkorosho mkubwa…

Ukimya uliotanda ndani ya lile pango ulikuwa ukinuka hofu na mashaka mazito kabisa, na kabla ya yeyote kati ya vikongwe waliokuwamo mle ndani hajaongea lolote, kishindo kizito kilisikika kutokea kule kwenye lango la kuingilia mle pangoni, na wote waliokuwemo mle ndani waligeukia kule kilipotokea kishindo kile.

Watu, au labda kwa usahihi zaidi, viumbe, watatu waliingia mle ndani na kuiendea moja kwa moja ile meza ya mawe iliyokuwa mbele ya wale vikongwe wasio na nguo waliokuwa wameketi kwa mfumo wa nusu duara kuielekea ile meza kubwa ya ajabu. Kati ya wale watatu walioingia, alikuwako kikongwe mmoja wa kike aliyezeeka sana kiasi kwamba mgongo wake ulikuwa umepinda kiasi kwamba alikuwa akitembea ilhali akiwa ameinama mithili ya mtu anayeingia ndani ya nyumba yenye mlango mfupi sana. Alikuwa akitembelea mkongojo alioukamata kwa mkono wake wa kulia, ilhali kwa mkono wake wa kushoto alikuwa amejishika kiuno, juu kidogo ya makalio yake yaliyonywea kwa uzee. Nyuma yake walifuatia vijana wawili wa kiume ambao walikuwa wamebeba mkatale baina yao, yaani mti mmoja mithili ya mchi wa kutwangia mabegani mwao, mmoja akiwa mbele na mwingine akiwa nyuma. Vijana hawa walikuwa wamejifunga kaniki kwa mtindo wa lubega. Umbali baina yao ukiwekwa sawa na urefu wa ule mkatale walioubeba mabegani mwao.

Kwenye ule mti uliokuwa mabegani mwa wale vijana, kigori aliyepata umri wa miaka kumi na mitano au na sita hivi, lakini hakika hakuzidi miaka kumi na saba, alikuwa amening’inizwa kama jinsi ambavyo mzoga wa swala aliyeuawa na wawindaji unavyobebwa. Miguu yake ilikuwa imefungwa kwa kamba ngumu sehemu juu kidogo ya visigino vyake, na mikono yake ikiwa imefungwa namna ile ile chini kidogo ya viganja vyake. Kisha ule mkatale ukapitishwa katikati ya miguu yake iliyofungwa pamoja, na kupitiliza kati kati ya mikono yake iliyofungwa pamoja, na ule mti ukawekwa mabegani kwa wale vijana.

Hakika ilikuwa ni hali ya kuumiza sana kwa mtu yeyote, lakini yule msichana alionekana kuwa kimya kabisa, aliweza kuwa amekufa, au amepoteza fahamu. Alikuwa akining’inia kwenye ule mkatale uliokuwa baina ya wale vijana wawili, kichwa chake kikining”inia hewani bila fahamu, uso wake ukiwa umeelekezwa kwa yule kijana aliyekuwa nyuma.

Yule bi kizee kikongwe alipiga hatua nyingine mbili zaidi kwa taabu kumuendea Mxulu, huku wote waliokuwa ndani ya lile pango wakimtazama kwa mshangao na butwaa, kisha akashindwa kuendelea zaidi. Aliyumba kidogo na kupiga mwereka mzito, mkongojo ukimtoka mkononi mwake huku akiachia mguno hafifu wa maumivu.

Binti Beho!

Mxulu na wale wenzake walipayuka kwa pamoja, lakini hakuna hata mmoja aliyeinuka kutoka pale alipokuwa ameketi.

Hawakuweza kufanya hivyo mpaka yule binti aliyebebwa na wale vijana wawili, ambao mmoja wao ndiye alitakiwa amuingilie kimwili yule binti siku saba baada ya wao kuuingia mwili wake kama itakiwavyo, awekwe juu ya ile meza kubwa ya jiwe. Mxulu alimtazama kwa kihoro yule kizee aliyeanguka hatua chache mbele yake.

“Mxulu…nime…umia…! Naku…f…fa…binadamu…ameniu…ameniua…!”

Binti Beho alisema kwa taabu huku akijitahidi kujigeuza pale chini, kaniki aliyokuwa amejifunga mwilini mwake ikimfunuka, ikiacha wazi kifua na matiti yake yaliyotepeta, na ndipo kwa kihoro kikubwa wale “wazawa” wenzake walipolishuhudia jeraha kubwa lililokuwa shingoni kwake, pembeni kidogo ya koo lake. Damu nyingi ilikuwa imemvuja na kukaukia mwilini mwake, na alikuwa akitweta kwa maumivu. Sasa Binti Beho alikuwa akiongea moja kwa moja kwa sauti na midomo yake, kwani kuongea kwa akili na mawazo kama jinsi wenzake walivyokuwa wakimuongelesha hapo awali kulihitaji utulivu mkubwa wa akili, na hali aliyokuwa nayo haikuruhusu kabisa utulivu wa akili. Mxulu aliinua uso wake na kuwatazama wale vijana walioongozana na Binti Beho, na kuwaona wakimlaza chali yule binti waliyekuja naye pale juu ya ile meza kubwa ya jiwe. Wale vijana walianza kumfungua zile kamba za miguuni na mikononi yule binti.

Fanyeni haraka! Itabidi tuanze zoezi letu mara moja…na tutaanza na Binti Beho ili tuokoe maisha yake. Hili jeraha ni baya…limekaa mahala pabaya sana.

Ni nini kimetokea huko?

Mmoja wa wale vikongwe waliokuwamo mle ndani aliwauliza wale vijana kwa mshangao.

Tulifanikiwa kumchukua huyu binti akiwa usingizini bila ya taabu wazee…lakini wakati tunatoka baba yake akatushtukiza. Binti Beho akawa anapambana naye wakati sisi tukikimbia na huyu binti…mara tukasikia mlipuko mkubwa nyuma yetu…yule baba alimpiga binti Beho kwa gobore…

Mmoja wa wale vijana alitoa maelezo haraka haraka huku akiendelea kumfungua kamba yule binti. Miguno ya mshangao ilisikika ndani ya pango lile.

Ah! Lakini… kwa mujibu wa Binti Beho mwenyewe, huyu binti alitakiwa awe peke yake nyumbani kwao usiku huu, wazazi wake walikuwa wanakesha kwenye ngoma kijiji cha jirani!

Mxulu alisema kwa kuchanganyikiwa.

Ndivyo haswa ilivyotakiwa iwe…lakini yule mzee alirudi ghafla tu, na Binti Beho aliamini kuwa angeweza kukabiliana naye…akatuambia tutangulie na huyu binti.

Kijana alimjibu, na alipoona wale wazee wanazidi kumkodolea macho kwa butwaa, akaendelea; Lakini tuliposikia ule mlio wa gobore tukajua mambo yameharibika. Ikabidi turudi kuona kulikoni…ndipo tukamkuta Binti Beho akiwa chini huku akivujwa damu…

Mxulu alitoa sauti mbaya ya ghadhabu.

Na vipi ilikuwa hata huyu binadamu akampiga risasi eneo hilo, na si mahala pengine mwilini mwake…?

Kikongwe mwingine wa kike aliuliza kwa woga mzito.

Hilo hakika ni utata mzito, kwani hata sisi tulishindwa kuelewa…lakini nahisi ilikuwa ni bahati mbaya tu!

Yule kijana aliyekuwa kimya muda wote alidakia, na miguno ya fadhaa ilizidi kusikika mle pangoni.

Mxulu alitoa tena sauti mbaya ya ghadhabu, na kufoka kwa sauti yake halisi huku akitumia midomo yake kama jinsi binadamu anavyotakiwa aongee.

“Sasa…sasa…huyo binadamu aliyemfanya hivi mzawa mwenzetu mmemuachaje?”

“Tumemdhibiti Mxulu…hayupo tena duniani.Tulifanikiwa kumuangamiza kwa ile ile bunduki yake.” Kijana alijibu.

“Sasa kwa nini nanyi msitupashe habari muda wote huo?” Kikongwe mwingine aliuliza kwa kulaumu. Sasa wote walikuwa wakiongea kwa sauti kama jinsi binadamu wanavyoongea.

“Si kosa letu…tulikuwa tukijaribu sana kuwasiliana nanyi, lakini nyie mlikuwa hamtujibu!”

Wazee waliokuwa wakisubiri pangoni walitazamana, na katika kutazamana kwao, walisema mengi, kwani walielewa kuwa muda wao ulikuwa unazidi kuisha.

“Sasa hilo, ukichanganya na kuwa Binti Beho alikwa amepoeza fahamu kwa muda mrefu, na kelele za wanakijiji waliotoka baada ya kusikia ile milipuko ya gobore, ilitufanya tuzidi kuhamanika na kuchanganyikiwa!” Kijana aliongezea.

“Heh! Haya mambo makubwa sasa…yaani imefikia hatua mpaka binadamu anaweza kutushinda sisi namna hii?” Mmoja wa wale vikongwe alisema kwa uchungu.

“Ah, katika hali ya kawaida, hata kama wangekuwa kumi wasingemuweza yeyote kati yetu…” Mwingine alidakia kwa hasira.

Na ndio maana inatubidi tutekeleze zoezi hili haraka sana, kwani kadiri muda unavyozidi kwenda, ndivyo tunavyozidi kupoteza nguvu na uwezo wetu!

Mxulu alisema kwa utulivu, sasa akirudia tena kuongea kwa akili na si kwa midomo tena, akiwa amerudisha utulivu wake wa akili. Kwisha kusema hivyo aliinuka na kuiendea ile meza kubwa ya jiwe, ambapo juu yake yule msichana bikira alikuwa amelazwa chali, akiwa uchi kama alivyozaliwa.

* * *

Kule mjini mgeni rasmi katika shamrashamra zile za usiku aliinuka na kuanza kutoa hotuba yake kwa umma wa wananchi waliojazana uwanjani pale. Kile kituko cha ule mwanga mkali uliokuwa ukianguka kwa kasi kutoka angani tayari kilikuwa kimeshasahauliwa kwa kuaminika kuwa ilikuwa ni hitilafu mbaya ya umeme iliyotokea wakati mmoja na fataki iliyolipuka vibaya na kufanya kishindo kikubwa kabisa.

Bila ya wale waliokuwa pale uwanjani kujua, lile donge la mwanga lililoonekana likiporomoka kutoka angani na kupotea ghafla hewani, halikupotea kama ilivyoaminika.

Wavuvi watatu waliokuwa katikati ya bahari huko Shungubweni, wilaya ya Mkuranga, walilishuhudia kwa mshangao mkubwa lile donge la mwanga lililokuwa likianguka kutoka angani, likipungua ukubwa kadiri lilivyokuwa likiikaribia dunia. Walizidi kuuangalia kwa mshangao mwanga ule, macho yao yakiumia vibaya sana, na wakati huo huo wakishindwa kujizuia kuukodolea macho mwanga ule wa ajabu. Kwa kihoro kikubwa walilishuhudia donge lile la mwanga likitumbukia baharini kiasi cha kilometa moja hivi kutoka pale ulipokuwa mtumbwi wao. Kishindo kikubwa kilisikika baharini, kikifuatiwa na mawimbi makubwa kabisa, mawimbi ambayo yaliusuka-suka na kuupasua vibaya sana mtumbwi wao, nao wakitupwa baharini huku wakiwa wamepofuliwa macho yao na mwanga ule mkali. Mayowe waliyokuwa wakipiga wakati wakitapatapa bila kuona mle baharini hayakuwa na msaada wowote kwao. Wale wavuvi walizama moja kwa moja baharini usiku ule, na wawili kati yao hawakuonekana tena.

********

Mxulu alimuinamia yule binti aliyelazwa chali pale juu ya ile meza kubwa ya jiwe, ambaye alikuwa amefumba macho na akipumua kwa taabu sana. Mxulu aliinua uso wake na kumtazama yule kijana wa pili aliyekuja na Binti Beho kutoka huko walikokuwa.

Una hakika kuwa huyu ndiye mliyetakiwa mje naye? Maana Binti Beho hajitambui!

Ni hakika kabisa Mxulu…Binti Beho mwenyewe alikuwepo wakati tunamchukua, na akathibitisha kuwa huyu ndiye binti aliyekuwa amemuandaa kwa shughuli hii tangu muda mrefu…ni bikra huyu Mxulu!

Bila ya kuongea neno zaidi, yule kikongwe aliyetambulika kama Mxulu aliinama na kumtazama kwa karibu zaidi yule binti. Hakika alikuwa ni binti aliyeumbika. Matiti yake madogo yalikuwa yamesimama imara kifuani kwake. Na hata pale alipomuinamia, yule binti alibwabwaja neno lisilotambulika na kugeuza uso wake pembeni huku akitikisa miguu yake, kama kwamba alijua kuwa ile sura mbaya ya kile kizee ilikuwa imemuinamia.

Haya, shughuli na ianze.

Hatimaye Mxulu alisema na kuwageukia wale wenzake aliokuwa nao mle pangoni. Wale wenzake wote waliinuka na kuisogelea ile meza taratibu. Ilikuwa ni picha moja ya kuogofya sana. Vikongwe saba wakiwa uchi wa mnyama wakijikongoja kuisogelea ile meza ambayo juu yake alikuwa amelazwa msichana mbichi, naye akiwa hana nguo hata moja mwilini. Mwanga uliotokana na ile mishumaa ya aina yake ulitupa vivuli vya kutisha kwenye kuta za pango lile. Na kibaya zaidi, ni kwamba wote walikuwa kimya kabisa.

Yaani si taswira ambayo ungeweza kuifananisha na tukio la kichawi wala uwangaji, kwani katika matukio kama hayo ungetarajia usikie wale wahusika wakiimba nyimbo fulani za ajabu-ajabu au angalau wangekuwa wakitoa sauti fulani-fulani za kuogofya na kushangaza au kutisha.

Sasa hawa walikuwa kimya kabisa.

Mmoja wa wale vikongwe aliweka kibuyu kingine juu ya ile meza, ambacho kilikuwa na shingo pana kuliko vile vibuyu vilivyokuwa vikitumika kama mishumaa. Mxulu alikichukua kile kibuyu na kwenda nacho hadi pale alipokuwa amelala Binti Beho. Wale wenzake wote walibaki wakiwa wameinamisha vichwa vyao huku macho yao wakiwa wameyaelekeza kwa yule binti aliyelala juu ya ile meza kubwa.

Mxulu alimuinamia Binti Beho na kumtikisa-tikisa kwa muda. Binti Beho alitoa mguno hafifu, na hapo sura ya Mxulu ilifanya kitu kama tabasamu la faraja. Kisha taratibu sana aliweka ncha ya kidole chake cha shahada shingoni kwa Binti Beho, chini kidogo ya koromeo lake, na kukididimiza kidole kile kwa nguvu shingoni pale. Shingo ile ilitoboka na damu nzito na nyeusi ilianza kutiririka kutoka kwenye jeraha lile. Haikuwa damu nyekundu kama ilivyo kwa binadamu wa kawaida, lakini labda ndiyo hiyo iitwayo damu ya mzee. Binti Beho hakutikisika wala kuguna. Alibaki akiwa ametula tuli wakati Mxulu akiikingia kwenye kile kibuyu ile damu iliyokuwa ikichuruzika kwa wingi kutoka kwenye lile jeraha. Aliikinga kwa muda mrefu kidogo, huku akitazama kwa makini sana wakati ile damu ikimiminika ndani ya kile kibuyu, kama kwamba kuna kitu maalumuu alikuwa akikisubiri kitoke kwenye mwili ule mkongwe pamoja na damu ile.

Hatimaye alikiona alichokuwa akikisubiri kwani pamoja na damu ile, kilitoka kitu kama kipande cha ukucha hivi, kilichopata ukubwa wa ukucha mzima wa dole gumba la mkononi la mtu mzima. Hapo Mxulu alikiweka pembeni kile kibuyu kwa tahadhari kubwa, kisha alibaki akimuangalia yule kizee aliyelala pale chini. Na wakati akiuangalia ule mwili wa yule kizee aliyelala pale chini, yale majeraha yote yaliyokuwa kwenye mwili ule yalianza kujiziba taratibu na kuwa kama hapo awali kabla ya kujeruhiwa!

“Ewe dongo lililobeba nafsi ya mwanadamu ajulikanaye kwa jina la Binti Beho! Sasa uko huru…nafsi ya mzawa mwenzetu iliyokuwa ikiutumia mwili wako kwa sehemu kubwa ya umri wako hapa duniani sasa haipo tena mwilini mwako. Nawe utaondoka hapa na kurudi nyumbani kwako, ambako utamalizia muda wako mfupi uliobaki hapa duniani kwa salama na amani.” Mxulu aliuambia ule mwili wa Binti Beho halisi, baada ya kumtoa yule mwenzao aliyekuwa akiutumia mwili ule. Kisha aliinuka na kurudi pale kwenye ile meza. Akiwa pale kando ya ile meza, alianza kufanya lile tendo alilomfanyia Binti Beho kwa kila mmoja wa wale wenzake, na kila aliyemaliza kutolewa kiasi cha ile damu na kile kitu kinachofanana na ukucha wa dole gumba la mtu mzima shingoni kwake, alibaki akiwa amelala usingizi mzito.

Hatimaye alibaki yeye na mmoja wa wale vijana wawili waliokuja na yule binti aliyelazwa pale juu ya ile meza ya jiwe. Kile kibuyu kilichokuwa kimejaa mchanganyiko wa damu za wale viumbe wenzao wa ajabu, pamoja na vile vijipande vya vitu kama ukucha ndani yake, kikiwa katikati yao. Mxulu na yule kijana walitazamana. Alikuwa ni kijana mrefu na aliyeshiba, muda huu naye akiwa ametupa pembeni ile kaniki aliyokuwa amejifunga hapo awali. Mxulu alikiweka kile kibuyu kando ya ule mwili wa yule binti pale juu ya meza.

Sasa tumebaki mimi na wewe, na kabla sijaondoka nataka nikukumbushe wajibu wako…

Naelewa kila kitu Mxulu…

Tulia! Mimi ndiye ninayejua wajibu wa kila mmoja wetu hapa duniani mpaka hapo muda wa kurudi nyumbani utakapofika. Hili ni tukio muhimu sana kwetu na sitaki kuwe na kosa hata kidogo!

Mxulu alimfokea huku akimtolea macho makali yule kijana.

Ndio Mxulu…samahani Mxulu…!

Kijana alijibu kwa hofu kubwa.

Mxulu alimtazama kwa muda bila ya kumjibu, na katika muda huo yule kijana alijikuta akitazamana uso kwa uso na yule kiongozi wao aogopwaye sio tu na wale wazawa wenzake waliokuwa nao mle pangoni muda mfupi tu uliopita, bali pia hata huko nyumbani kwao walipotokea. Nyumbani ambako hawakuweza kurudi mpaka muda muafaka utakapofika. Kijana alijaribu kuyashusha macho yake chini ili asiendelee kutazamana na yule mzee mwenye ghadhabu, lakini hakuweza, kwani kwa namna fulani, Mxulu alikuwa ameyakamata macho ya yule kijana kwa macho yake, na kijana hakuweza kushusha macho yake mpaka pale Mxulu atakapotaka iwe hivyo. Mxulu aliendelea kuyakamata macho ya yule kijana, wakitazamana moja kwa moja machoni, akitaka kumuonesha kijana kuwa alikuwa hataki mzaha kabisa katika swala lile, na alitaka kijana alione hilo katika macho yake.

Vizuri. Naamini sasa nimepata usikivu wako…

Hatimaye Mxulu alimuambia yule kijana ilhali bado akiwa ameuma meno yake kwa hasira.

Hakika Mxulu…hakika…!

Vizuri. Sasa…Mimi na wewe tutaungana pamoja kabla sijaondoka. Wewe ndiye utakayeuaga mwili wa huyu binadamu niliyekuwa nikiutumia dongo lake kwa muda wote huu…

Mxulu aliongea kwa ufasaha, sasa akiwa ameyaachia macho ya yule kijana.

Ndiyo Mxulu…

Na baada ya mimi kuondoka….kufa…kwa muda, wewe utabaki na huyu binti mpaka ule muda wa siku saba za kibinadamu utimie, ndipo utamuingilia…sawasawa?

Sawasawa kabisa Mxulu.

Narudia tena. Hutamuingilia kimwili huyu binti mpaka baada ya siku saba za kibinadamu zikamilike, tumeelewana?

Kabisa Mxulu!

Na utakapofika hapa, tukirejea tena na kwenye uhai, ndipo tutakapokabidhiana majukumu mapya…tukiwa watu wapya. Sawa?

Sawa Mxulu.

Alipokwisha kutoa maelekezo yale, Mxulu alimtoboa kidogo sana yule kijana shingoni, na kuikinga ile damu iliyochuruzika kutoka kwenye jeraha lile kwa kutumia kile kibuyu chao,ila hakusubiri mpaka kile kijikucha kitoke. Kisha na yule kijana akamtoboa Mxulu shingoni kwa namna ile ile, na kuikinga damu mpaka pale kilipotoka kile kitu kama ukucha. Baada ya hapo wote wawili walimuinamia yule binti aliyelala chali pale juu ya ile meza, kijana akimkamata kichwa kwa nguvu na kumbana pua, wakati Mxulu akimnywesha ule mchanganyiko wa damu zao na zile za wazawa wenzao, pamoja na vile vijipande vya vitu kama vikucha.

Binti alifumbua macho ghafla na kuanza kujikukurusha bila mafanikio huku akijaribu kupiga kelele. Lakini alikuwa amezibwa pua, na alipojaribu kuvuta pumzi kwa kutumia mdomo wake tu ile damu ilipita kinywani mwake, ikibaki kidogo tu kwenye kile kibuyu. Binti alitumbua macho kwa woga na taharuki. Alijitupa huku na huko, akitoa miguno ya kila aina huku bado akiwa amebanwa pua, lakini mikono iliyomkamata ilikuwa mikubwa na yenye nguvu.

Mbane vizuri…nguvu zinaniishia…sitaweza kudumu kwa muda mrefu zaidi…!

Mxulu alisema kwa taabu. Kijana alizidi kumbana pua yule binti huku kwa mkono wake mwingine akimbana taya yule binti na kuutanua zaidi mdomo wake, kama jinsi mtu anavyombana mtoto mdogo anayegoma kunywa dawa. Yule binti alifungua kinywa bila kupenda, na Mxulu alim-miminia damu yote iliyobakia kwenye kile kibuyu.

Hapo Mxulu alianguka chini, akiwa anaelekea kupoteza fahamu. Kijana mzawa alimuacha binti kwa muda na kubaki akimkodolea macho Mxulu, ilhali yule binti alibaki akiwa ameduwaa, michirizi ya damu ikimchuruzika kila upande wa mdomo wake. Alikuwa amepigwa bumbuwazi.

Na hapo kilisikika kishindo kutokea kwenye mlango wa pango lile. Kijana aligeuka kwa mshituko kule kilipotokea kile kishindo, na hakuamini kabisa kile alichokiona. Aliachia muungurumo wa ghadhabu.

Akiwa pale chini, Mxulu aligeuza macho yake kufuata uelekeo wa macho ya yule kijana na mdomo ukamuanguka kwa butwaa, kisha akavuta nyuma midomo yake kwa ghadhabu na kukenua meno yake yaliyochoka huku akimgeukia tena yule kijana. Lakini sasa alikuwa ameshakabidhi nguvu zake mwilini mwa yule binti bikira kama wenzake, na ilikuwa ni kwa ugumu wa nia yake tu ndio uliomuwezesha kuongea tena.

Ni nini hii…we’ si ulisema…

Sauti ya Mxulu ilisikika huku ikififia kwa mbali sana kichwani kwa yule kijana, lakini yule kijana hakuwa akimsikiliza. Aliruka mbele kwa hatua moja kubwa huku akiendelea kutoa muungurumo wa ghadhabu kuelekea kule kwenye lango la lile pango ambalo halijapata kuingiwa na binadamu yeyote kwa miaka mingi sana kabla ya siku ile…

* * *

Muda huo huo upande mwingine wa sehemu ile ya Tanganyika, Chambuso Mwagala alikuwa akibadili gia ya Gari lao iliyokuwa ikienda kwa kujikongoja, kutoka namba nne kuingia namba tano, huku bado ukimya ukiwa umetanda baina ya wote waliokuwa ndani ya gari ile. Alipiga mwayo mrefu na macho yalimregea kwa usingizi na uchovu. Lakini alijipa moyo kuwa angalau atalala akiwa ndani ya ndege alfajiri ya siku itakayofuata, hatimaye akikata anga kuelekea nchini Uingereza ambako alikuwa anaenda kusomea shahada ya kwanza ya ualimu, akiwa miongoni mwa wananchi wachache sana nchini kupata fursa ile adhimu baada ya kufaulu vizuri masomo yake ya awali hapa nchini aliyoipatia katika shule ya Minaki; na hususan akiwa miongoni mwa wazaramo wachache zaidi hapa nchini kupata nafasi ile.

Mwayo mwingine mrefu zaidi ulimtoka, na akaumalizia kwa msonyo hafifu ambao ulitokana si na kukerwa na lolote, bali mazoea tu ambayo wengi wetu huwa tunajikuta tukifanya hivyo bila ya sababu yoyote ya kueleweka. Tena bila hata ya yeye mwenyewe kujua au kufahamu kuwa amesonya.

“Ohoo! Sasa Chambuso unataka makubwa. Yaani umeona kutuita walevi haitoshi, umeamua kuanza kutusonya sasa!” Uwesu alimkoromea kutokea kule nyuma na Chambuso akapigwa na butwaa.

“Jama! Nimewasonya…? Saa ngapi?” Aliuliza kwa mshangao, kwani akilini mwake wala hakukuwa na japo lile wazo kuwa alisonya.

“Ah! Eti Esmund hujamsikia akitusonya hapa?” Uwesu alimgeukia sahibu yake kutafuta ushahidi, lakini kabla Esmund hajajibu, Chambuso aliingilia kauli ile.

“Hebu nipisheni huko nyie! Msitake kuleta kisirani cha kitoto hapa bwana! We” Uwesu umefanya jambo la kijinga lililokaribia kututoa roho hapa, halafu hutaki kukubali kosa na matokeo yake unatafuta vijisababu! Sasa kwani uongo kuwa nyie ni walevi? Acheni ujinga bwana!” Chambuso aliwajia juu wote wawili, na alipomaliza kusema hivyo ndipo alipoachia msonyo mkali na mrefu uliotokana na hasira za mazungumzo yale ya kijinga.

“Ah! Si unasikia sasa bwana! Si unamsikia Esmund?” Uwesu alimaka, kisha akamgeuki tena Chambuso kule mbele alipokuwa akiendesha, “Chambuso tutakorofishana huku huku porini ujue!”.

“Sasa ndio nimesonya Uwesu, na nimesonya kutokana na upuuzi wako unaotaka kuniletea saa hizi!”

“Hebu acheni kupigizana kelele jamani! Mi”hata sioni cha kupigishiana kelele hapo…” Esmund aliingilia kati.

“Akh! Si huyu mwenzako huyu… ujinga ujinga tu!” Chambuso alisema, wazi akiwa amekereka kabisa.

“Ah! Sawa bwana…lakini ujue tukifika mjini nalianzisha tena hili Chambuso!, ujue kabisa hiyo!” Uwesu alimwambia kwa hasira huku akipiga-piga ngumi nyuma ya kiti cha dereva, ambacho Chambuso alikuwa amekikalia.

“Hata sasa ukitaka tuteremke tulianzishe, we lofa nini?” Chambuso naye alikuja juu.

“Hebu nitoleeni wazimu hapa nyie, mmesikia? Watu tumenusurika na kifo kibaya sana huko, sasa mnataka kuuana kwa sababu za kijinga tu? Twendeni huko!” Esmund aliingilia kati kwa ukali.

“Potelea mbali! Bora hata tungekufa tu kwenye ile ajali, tuzikwe, udhia uishe…huyu bwana kupata hiyo nafasi ya kwenda ulaya ndio keshajiona ana mamlaka ya kutuita walevi na kutusonya…” Uwesu alibwata kwa hasira.

“Aaakh! Sio hivyo Uwesu, and you know it Goddamn it!” Chambuso alimjibu kwa hamasa, na hapo hapo Esmund naye akaingilia kati.

“Aaaah? Sasa huko uendako siko bwana…! Kwani si ni kweli tulikunywa pombe Uwesu? Acha wahka bwana”

Sasa hivi ni Uwesu ndiye aliachia msonyo mkali na mrefu.

Chambuso aliamua kunyamaza. Safari yao iliyokuwa imeanza kwa furaha na amani ilikuwa inaishia kwenye kero na ugomvi. Kimya kikatawala upya ndani ya gari, huku safari ikiendelea.

Lakini laiti wangejua kilichokuwa kikiwasubiri kule walipokuwa wakielekea, hakika wangemuunga mkono Uwesu kwa ile kauli yake kuwa ni bora tu wangekufa kwenye ile ajali ya gari waliyonusurika kwayo muda mfupi uliopita. Lakini usilolijua siku zote huwa ni usiku wa kiza.

Na hakika, ule ulikuwa ni usiku wa kiza kizito sana…ulioambatana na mambo mengi ya kiza…

* * *

Wakati akina Uwesu wanabishana, wakiwa katika ile barabara itokayo Kazimzumbwi, kule mjini mgeni rasmi alimaliza hotuba yake na uwanja uliripuka kwa makofi hoi hoi na nderemo. Bendi ya “Brass” ya polisi ilianza kupiga mipigo yake iliyoendana na muennendo wa gwaride wakati vikosi mbali mbali vya majeshi ya ulinzi na usalama vikipita mbele ya mgeni rasmi na kwenda kujipanga katika mfumo mzuri na wa kupendeza kabisa uliotokana na nidhamu ya kijeshi ambayo kila askari katika vikosi vile alikuwa amefundishwa na ikaeleweka vizuri sana kichwani mwake.

Wananchi walikuwa wakishangilia jinsi vikosi vile vilivyokuwa vikipita mbele ya mgeni rasmi na wale wageni wengine waalikwa kutoka mataifa mbali mbali, pamoja na wale viongozi wengine wa kitaifa, na wake zao.

Na sehemu nyingine, ambayo iliunganishwa na tukio lile la pale uwanjani na ule mwanga mkali ulioporoka kwa kasi kubwa kutoka angani, mambo yalikuwa yakitokea.

Wanakijiji wa eneo lile la Shungubweni nao walikiona kile kitu kilichokuwa kikitupa mwanga mkali na kuangukia baharini. Baadhi ya wavuvi waliokuwa baharini wakati ule walihamanika na vyombo vyao vilitupwa huku na huko baharini na kupinduka au kupasuka, lakini katika wale waliokuwa baharini wakati ule, ni wale wavuvi watatu tu ndio waliokuwa karibu zaidi na eneo kilipoagukia kile kitu, na ndio waliopata madhara makubwa zaidi.

Wavuvi waliokuwa baharini walitupwa nje ya bahari na kukimbia kijijini kutoa taarifa, wakati huo huo, wanakijiji waliokishuhudia kile kitu nao walikuwa wakikimbilia kule baharini, kushuhudia kulikoni.

Kilikuwa ni kizaazaa kwa muda, wakati wale wavuvi wachache walionusurika wakitoa maelezo ya mambo waliyoyaona, na jinsi wale wenzao watatu walivyozama baharini na kutoibuka tena.

Muda kidogo ulipita kabla juhudi za kusaka miili yao baharini hazijaanza, lakini hata wale waliokuwa wakiisaka miili ile mle baharini usiku ule walijua kuwa walikuwa wanatimiza wajibu tu. Kwani kwa jinsi walivyoona mabaki ya mtumbwi waliokuwa wakiutumia wale wavuvi waliopotea, mategemeo ya kuwapata wakiwa hai yalikuwa madogo sana….

Huku mjini, kwenye ule uwanja mkubwa wa michezo ambako shughuli ndio zilikuwa zinakaribia ukingoni, askari wawili wakakamavu walikuwa wanapiga gwaride kishupavu kabisa kuelekea kwenye milingoti miwili ya bendera iliyokuwa mbele ya uwanja ule, na watu wote pale kiwanjani walikuwa kimya kabisa, wakiwa wamesimama wima, macho yao yakiwafuata wale askari wawili waliokuwa wakiiendea ile milingoti huku mioyo yao ikiwaenda mbio, na wengine wakishindwa kujizuia na kubaki wakitiririkwa na machozi ya furaha isiyo kifani.

Hakika lile lilikuwa ni tukio la kihistoria ambalo ni kwa majaaliwa ya mwenyezi Mungu tu ndio wao walikuwa pale usiku ule kulishuhudia. Wakiwa ni miongoni mwa wale waliokuwepo wakati historia ile ikiwekwa.

Lakini pia walikuwa ni miongoni mwa watu ambao walikuwako wakati mtiririko wa matukio matatu yaliyogubikwa utata mkubwa yakijikusanya taratibu, hatua kwa hatua, kila moja kutokea upande wake, bila ya wao wenyewe kujua…

* * *

Kwa sekunde moja kabla hajazimika kabisa, Mxulu alimuona mtu mmoja wa makamu akiwa amesimama ndani kidogo ya mlango wa pango lile, huku akiyumbayumba na mkononi akiwa ameshika gobore kubwa.

Yule mtu alitembeza macho mle ndani na kwa muda alipigwa na butwaa. Hakuamini kuwa macho yake yalikuwa yakimuonesha kile alichokuwa akikiona mle ndani, na akili yake ya kibinadamu ilimtuma moja kwa moja kuwa hapa kilichokuwa kikifanyika ni uchawi tu na si kingine.

Angejuaje undani wa mambo yale?

Yule mtu alikuwa amevaa mkwiju mkubwa kiunoni mwake, na juu alikuwa amevaa shati la khaki jeupe ambalo lilikuwa limetapakaa damu sehemu yote ya mbele, damu iliyotokana na jeraha la risasi kutoka kwenye lile lile gobore lake wakati akipambana na vijana wawili aliomini kuwa ni wa kichawi, baada ya yeye kumpiga risasi kikongwe aliyemtambua kwa jina la Binti Beho ambaye alikuwa akiishi pale pale kijijini kwao. Risasi iliuingia mwili wake kupitia kwenye tundu iliyolitoboa juu kidogo ya ziwa lake la kulia. Alikuwa amejifunga upande wa khanga kifuani pale juu ya lile jeraha, khanga ambayo ilipita chini ya kwapa lake la kulia na kuzunguka kifuani na mgongoni kwake na kuja kufungwa upande wa kushoto wa shingo yake, juu ya bega lake la kushoto.

Ile khanga nayo ilikuwa imelowa damu.

Juu ya bega lake la kulia alikuwa amening”iniza shuka kubwa ya kulalia, nayo kidogo ilikuwa imeingia damu kutoka kwenye lile shati lake.

Kwa sekunde kama tano hivi yule mtu alijisahau, akitembeza macho yake mle ndani na akiwaona wale watu waliolala kwenye sakafu ya pango lile bila nguo, na alizidi kuchanganyikiwa.

Baadhi ya wale wazee vikongwe waliolala mle ndani walikuwa ni watu anaowafahamu fika! Wanakijiji wenzake kabisa! Kama Binti Beho…

Na alipomuona yule binti akiwa amekaa juu ya ile meza bila nguo, akiwa amezubaa kama aliyeamshwa kutoka usingizini, alishindwa kujizuia.

“Huba! Huba mwanangu! Binti Malambi…!“ Alimuita yule binti kwa sauti iliyojaa hofu na mashaka makubwa…upendo wa dhati.

Yule binti aliyeitwa kwa jina Huba binti Malambi aliwatazama wale watu wawili na kuwa kama anayewaona kwa mara ya kwanza maishani mwake. Alitoa mbwewe kubwa na kujifuta mchirizi wa damu aliyonyweshwa kutoka kwenye upande wa mdomo wake kwa kutumia mgongo wa kiganja chake na kujikunyata juu ya ile meza kwa woga.

Kisha alianza kutetemeka mwili mzima.

Bila ya kujijua, yule mzee alianza kuiendea ile meza aliyokuwa ameikalia yule binti huku akiiweka sawa ile shuka iliyokuwa juu ya bega lake la kushoto kwa nia ya kumfunika huku machozi yakimchonyota machoni, na ndipo aliposikia vishindo vya yule kijana.

Aliinua uso wake kukabiliana na yule kijana aliyekuwa akimwendea kwa haraka akiwa na sura iliyodhamiria kumdhuru, tena kumdhuru vibaya sana.

Hapo hapo yule mtu mzima aliyevaa mkwiju aliiweka sawa bunduki yake na kumuelekezea yule kijana.

“Hapo hapo! Simama hapo hapo au nakulipua kama nilivyomlipua mchawi mwenzenu, wadondozi wakubwa nyie!“ Alifoka huku akimtolea macho yule kijana ambaye alisimama ghafla hatua zisizozidi tano mbele yake.

Walitazama, yule mtu akimchungulia kwa makini yule kijana ili aweze kumuona vizuri kutokana na ule mwanga wa ile mishumaa ya ajabu iliyokuwamo ndani ya lile pango. Alihisi kizunguzungu kikimjia tena na akadhani alikuwa anakaribia kupoteza fahamu. Jeraha lililokuwa kifuani kwake lilikuwa likimuuma vibaya sana, lakini hakukubali kushindwa.

“Wewe! Umefikaje huku! ” Yule kijana alimuuliza kwa mshangao mkubwa uliochanganyika na ghadhabu pevu.

“Mnhu! Mimi ni mwindaji mzuri sana hapa kijijini, na kama ninaweza kufuatilia nyayo za kuku na nikampata, sembuse nyayo zenu, tena…tena…mlikuwa mkipita mkivuja damu njia nzima na kuvunja hovyo matawi ya miti porini? ” Yule mtu alimjibu, kisha akaendelea, “…na tena mmeangusha na shuka ya mwanangu huko nje…. ” Akamalizia kwa hasira, akimaanisha kuwa na ile shuka nayo ilimuwezesha kujua kuwa walikuwa pale kwa urahisi zaidi.

Yule kijana alimtazama kwa macho madogo yaliyojaa chuki na kutikisa kichwa kwa masikitiko.

“Umefanya kosa kubwa sana ambalo nasikitika kuwa hutakuwa na uhai zaidi wa kukufanya ujutie jambo hili baada ya hapa, kwa sababu utakufa hapa hapa! Tena sasa hivi…! ” Yule kijana alimkemea yule mtu aliyepata kiasi cha miaka hamsini na tano hivi huku akiwa ametanua mikono yake kila upande kama mtu anayetaka kupaa.

“Kelele! Mlidhani mmeniua sio? Bado sijafa wachawi wakubwa nyie! Mnataka kumfanya mwanangu msukule…? Basi labda niwe… ” Yule mtu alisema kwa hasira, lakini hapo tena wimbi la kizunguzungu likamkumba na akayumba kidogo, akafinya macho na kuhema kwa nguvu huku akijitahidi kumtazama yule kijana kwa makini, na kumalizia kauli yake, “labda niwe nimekufa…!”

Yule kijana alitazama kwa hasira kali, na kusema kwa sauti ya chini sana, lakini iliyofika vizuri sana masikioni mwa yule mzee.

“Tayari wewe ni mfu mzee, umeingilia kitu ambacho hukijui uzito wala madhara yake kwako na kwa jamii inayokuzunguka…. ”

“Basi utakufa wewe na hao wachawi wenzako! Mi” siogopi uchawi bwana, Mimi ndiyo mzee Malambi bwana! Na nitaipigania familia yangu mpaka damu ya… ”

Mzee Malambi hakumaliza, kwani hapo yule kijana alimrukia kwa ghafla. Yowe lilimtoka yule mtu aliyejinadi kuwa ni mzee Malambi na hapo hapo gobore liliachia mlipuko mkubwa ndani ya pango lile.

Risasi ilimpata kijana katikati ya kifua, na ilimtupa nyuma hadi kwenye ile meza, ambako alipigiza kiuno chake kwenye upande wa meza ile, na kuserereka hadi chini ya meza ile, akalala chali pale chini huku akitokwa damu kifuani.

Yule binti aliachia yowe kubwa la mshituko kutokana na mlipuko ule. Mzee Malambi alitoa risasi nyingine kutoka kwenye mfuko wa mkwiju wake mkubwa aliouvaa na kuanza kuweka risasi nyingine kwenye lile gobore lake haraka haraka huku akibwabwaja kwa kwa sauti iliyokuwa ikitoka kwa shida huku akihema kwa taabu

“Usiwe…na wasi…wasi mwanagu! Baba yako ni…po! Nime…kuja kukuok…”

“Baba…?” Yule binti aliuliza huku akimtazama kwa makini yule mzee.

“Ndi-” Mzee Malambi alianza kumjibu, lakini hapo hapo yule msichana alimkatisha.

“Nini maana yake hii? Si mlisema kuwa mmemdhibiti huyu binadamu na hataweza kuishi tena?”

Mzee Malambi alibaki kinywa wazi na akahisi mwili ukimwingia baridi kali. Alibaki akiwa ameishikilia ile bunduki yake kwa mikono miwili huku akimkodolea macho yule binti aliyekuwa pale juu ya ile meza.

“Eti…?” Ndilo neno pekee lililotoka kinywani mwake. Kioja alichokuwa akikishuhudia pale kilikuwa ni cha mwaka.

Kwani ingawa yale maneno yalitamkwa na yule binti yake aliyekuja kumuokoa kutoka katika mikono ya wale watu alioamini kuwa ni wachawi, lakini sauti iliyoyatamka maneno yale ilikuwa ni nzito, iliyojaa ghadhabu kubwa…na ya kiume.

Ilikuwa ni sauti ya Mxulu.

Mdomo ulimuanguka Mzee Malambi, na sasa ujasiri wake ukafunikwa na woga mkubwa kabisa. Woga ambao ulitokea chini kabisa ya pachupachu za moyo wake, na kutambaa taratibu katika mishipa yake ya damu na kuutia mwili wake baridi kali, pamoja na kwamba ndani ya lile pango lisilo na madirisha kulikuwa kukifukuta joto lililotokana na ile mishumaa mikubwa.

“Mungu wangu! Hii ni nini jamani…Huba kawaje tena mwanangu? Ameingizwa mashetani, au…?”

Na hata wakati wazo hilo likipita kichwani mwake, alisikia purukushani nyingine na mitikisiko ya miili mle ndani. Akageuka kutazama kule purukushani zile zilipotokea.

Mlipuko wa ile bunduki yake uliwagutusha wale wazee waliokuwa wamelala shaghala baghala mle ndani,kutoka kwenye ile hali waliyokuwa nayo hapo awali,ambayo mzee Malambi hakujua iwapo ilikuwa ni usingizi au kitu nyingine, na kwa kihoro kikubwa aliwashuhudia wale watu wakiinuka taratibu, kila mmoja kutokea mahala alipokuwako. Sauti ya mguno iliyokuwa nusu kilio-nusu mshangao ilimtoka pale alipomuona Binti Beho, ambaye hapo awali alimtwanga risasi, naye akiinuka miongoni mwa wale wenzake na kujikongoja kuelekea kwenye kona moja ya lile pango. Wote walikuwa kama watu waliokuwa wakitembea huku wakiwa usingizini, na walionekana kabisa kuwa hawakujua walikuwa wapi na wala hawakuonekana kutambua kuwa mle ndani kulikuwa kuna viumbe wengine. Yaani ilikuwa kama kwamba kila mmoja kaamka na kajikuta yuko peke yake, na hakushangazwa na hali ile. Wote walikuwa wakitembea huku wametanguliza mikono yao mbele ilhali macho wakiwa wameyakodoa moja kwa moja mbele yao, pasina kupepesa wala kugeuza vichwa vyao pembeni…na kibaya zaidi, Mzee Malambi alimuona Binti Beho akipita hatua chache sana mbele yake na wala hakuonesha kuwa alikuwa amemuona!

“We…wewe…! We bibi we…we Bbi…Bi…Binti Beh…Beho!” Alijikuta akiita kwa kitetemeshi kikubwa, macho yamemtoka pima. Binti Beho hakuitika wala kutetereka. Aliendelea kutembea vile vile akiwa ametanguliza mikono yake mbele kama mtu atembeaye akiwa usingizini…sleep walking…

Mzee Malambi alishangaa pasina maelezo, kwani alihakikisha kabisa kuwa alishampiga risasi yule kikongwe. Na ingawa wale wenzake walifanikiwa kumnyang”anya ile bunduki na kumpiga risasi kabla hawajakimbia na yule kikongwe wao mchawi, alijua kabisa kuwa yule kikongwe hangeishi. Tangu lini uchawi ukaishinda risasi? Mbona hata Kinjeketile alishindwa kuigeuza risasi ya mkoloni na kuwa maji kama alivyotaka?

Lakini hapa alikuwa akimuona yule kikongwe akitembea kindondocha mbele yake! Macho yake yalienda mpaka kifuani kwa yule kikongwe aliye uchi kabisa, ambapo alijua kuwa ndipo alipompiga risasi.

Binti Beho hakuwa na jeraha wala kovu!

Aaaaah…Mungu wangu…!

Aliwageuzia macho wale wengine, na wote waliendelea kuwa vile vile kama Binti Beho. Walikuwa kama madubwana tu ambayo tayari yameshapangiwa nini cha kufanya pindi ufikapo muda fulani. Lile liliuwa ni tukio la kutisha sana kulishuhudia, na hakika Mzee Malambi alitishika vibaya sana. Mikono ilimuisha nguvu nusura aangushe lile gobore lake, lakini alizidi kuling”ang”ania.

Na kabla hata hajatanabahi juu ya kile alichokuwa akikishuhudia, sauti nyingine ikamshitua na akageukia kule ilpotokea, na huko alimuona binti yake akiwa uchi kabisa, amesimama kando ya ile meza kubwa ya jiwe akiwa ameuma meno kama kwamba aliyekuwa kwenye maumivu makali, huku amejishika kichwa kwa mikono yote miwili ilhali akiwa amefinya macho yake kwa nguvu.

“Hu…Huba…?”“ Mzee Malambi aliita huku akianza kumsogelea bintiye kwa taabu, woga uliokithiri ukimtambaa mwili mzima. Huba binti Malambi alikuwa akisikia sauti za wale viumbe waliokuwa mwilini mwake wakati ule, zikipiga kelele bila mpangilio kichwani mwake.

Ah, Mungu wangu…ni nini kinanitokea mimi…? Nimefikaje hapa…!

Na mara sauti zilizokuwa kichwani mwake zikazidi kumzonga. Hakuweza kuelewa lolote kutoka kwenye sauti zile isipokuwa kelele tu zilizomzuia kufikiri vizuri. Yaani ilikuwa kama kwamba kuna msiba, na waombolezaji wa msiba huo waliamua kutumia kichwa chake…ndani ya kichwa chake…kuwa ndiyo sehemu ya kuombolezea, tena kwa makelele makubwa.

“AAAAAARRGHHH….!”“ Huba binti Malambi alipiga kelele kutokana na kushindwa kustahimili kelele zile, huku akiinama akiwa amejishika kichwa chake.

“Hubaaa! Ah, Huba mwanangu…idhilali gani hii inayotukuta…?”“ Mzee Malambi alimpigia kelele bintiye huku akijaribu kumfuata pale alipokuwapo, lakini alijikuta akisimama ghafla na kubaki akiwa ameduwaa, mwili ukimuingia ubaridi mpya kabisa. Yule binti aliinua uso wake ghafla pale alipomsikia akilitaja jina lake na kubaki akimtazama kwa macho ambayo Mzee Malambi hakuyaelewa kabisa kwani hayakuwa macho ya bintiye Huba binti Malambi aliyemzoea.

Yale macho yalikuwa kama…kama…

Walitazamana.

Mara macho ya yule binti yalirudi kwenye hali yake ya kawaida. Yaliyojaa woga, mshangao na…yanayohitaji msaada.

“Ah! Huba mwanangu…wamekufanya nini hawa? Wamekuharibu usichana wako kwa nguvu…?”“ Mzee Malambi alimuuliza bintiye huku akianza tena kumsogelea kwa mwendo wa kuyumba yumba huku akiwa ametanguliza ile shuka aliyokuja nayo ili amfunike. Kelele zilipungua kichwani mwake, na Huba alimtambua baba yake. Roho ilimuuma kuonana na baba yake akiwa katika hali ile, na alifunua kinywa chake kumuita, kumtaka msaada.

(Oh…Baba! Baba…nimefikaje huku…? Nisaidie baba…) Lakini maneno yalikuwa akilini mwake tu, kwani kitu kilichotoka kinywani mwake, na ambacho Mzee Malambi alikisikia, kilikuwa tofauti kabisa.

“Toka hapa, ewe mwanadamu mwenye kuangamia, toka! Ondoka mbele ya uso wangu! Ondoka! Ondoka! ONDOKAAAA…!”“

Mzee Malambi alipiga yowe kubwa na kumtazama bintiye kwa woga uliokithiri, kwani maneno yale yaliyotoka kinywani kwa mwanaye, yaliwasilishwa masikioni mwake kwa sauti ya Binti Beho!

E bwana we!

Pasina kujielewa alijikuta akigeukia kule alipokuwako Binti Beho, na kumuona kikongwe yule pamoja na wale wenzake wakiokota kaniki na vikoi vyao vilivyokuwa kwenye kona moja ya pango lile.

“Ha! Hah! Hhaaaaah….!” Mzee Malambi alibwabwaja kwa mshangao na woga huku akirudi nyuma, akiwakodolea macho Binti Beho na wenzake wakijifunga vile vikoi na kaniki zao wakiwa kimya kabisa, kama kwamba hakuna kilichokuwa kikitokea mahala pale muda ule. Na hata pale alipokuwa akiwatazama watu wale, aliwaona wakigeuka na kuanza kutoka nje ya pango lile wakiwa kimya kabisa.

Hapa Mzee Malambi aliamua kutimua mbio. Hakuweza kabisa kuendelea kushuhudia mauza-uza yale kwa hata sekunde moja zaidi bila ya kurukwa na akili. Lakini pia hawezi kumuacha binti yake aliyekuja kumuokoa, na ambaye alijua kuwa tayari “alisharogwa” na wale watu ambao yeye aliamini kuwa ni wachawi.

“Huba twende mwananguuu….Twendeeeee!” Alipiga kelele huku akimkimbilia mwanaye na kumtupia ile shuka. Alimkamata mkono na kuanza kukimbia naye kuelekea nje ya pango lile, akiwa na nia ya kuwahi kutoka mle ndani kabla ya wale vikongwe.

Huba alikubali kuongozwa na baba yake kwa muda, lakini mara alisimama ghafla na kuushikilia mkono wa babaye kwa nguvu. Mzee Malambi alimgeukia bintiye.

“Twende Hub…”

“Huu ndio mwisho

(Baba mbona siwezi kwenda…?)

Mwanadamu!” Sauti ya Mxulu ilimkemea Mzee Malambi kupitia kinywa cha Huba, na wakati huo huo Huba akishangaa kuwa hawezi tena kutembea, pasina kujua kuwa kile alichokuwa akimuambia baba yake kiliishia kichwani mwake tu, na akiona baba yake akimtumbulia macho ya mshangao badala ya kumsaidia.

Huba alichanganyikiwa. Mzee Malambi alihamanika vibaya sana, kwani hapo ilimfunukia wazi kuwa yule mwanaye si mwanaye tena.

“Oooh, samahani Huba mwanangu…!” Alisema kwa uchungu huku akiuachia mkono wa mwanaye ili atimue mbio kivyake. Lakini Huba alizidi kumng’ang’ania mkono wake kwa nguvu, akimzuia asiondoke.

“Unakwenda wapi…

(Baba usiniache tafadhali…)

Mwanadamu?” Sauti ya Mxulu ilimuuliza tena Mzee Malambi kwa kejeli kupitia kinywa cha Huba, na hapo Mzee Malambi akajua kuwa kweli mwisho wake ulikuwa umefika. Aligeuka nyuma huku akiuvuta kwa nguvu mkono wake kutoka kwenye himaya ya mwanaye ambaye si mwanaye tena, na hapo alijikuta akiachia mguno wa fadhaa na kukata tamaa, mdomo ukimuanguka na macho yakimtoka pima.

Yule kijana aliyempiga risasi muda mfupi uliopita alikuwa amesimama mbele yake huku akitabasamu kwa kejeli, macho yake yakimtazama kwa faraja ya ki-endawazimu uliodhihiri. Mzee Malambi alipeleka macho yake yaliyokodoka kwenye lile eneo ambalo alijua kuwa alimpiga risasi yule kijana, na hapo ndipo aliposhuhudia lile eneo ambapo risasi iliuingia mwili wa yule kijana likijikusanya na kusinyaa taratibu, kisha lile jeraha likapotea hivi hivi mbele ya macho yake.

Mzee Malambi alipagawa.

Ukelele mkubwa wa woga usiosemekana ulimtoka, na hapo hapo alimshuhudia yule kijana akimshushia pigo kwa mkono wake wa kulia, ukiwa umeshika rungu au jiwe refu mithili ya rungu, naye hapo hapo aliinua ile bunduki yake na kufyatua risasi yake ya mwisho.

Hakuusikia mlipuko wa bunduki ile, badala yake alihisi maumivu makali wakati pigo zito lilipokishukia kichwa chake. Mwanga mkali ulilipuka mbele ya macho yake, kisha kote kukawa kiza.

Huba/Mxulu alimuona yule kijana mzawa akimpiga kichwani kwa rungu Mzee Malambi, na hapo hapo alimuona yule kijana akitupwa nyuma huku upande mzima wa kichwa chake ukimeguka na kutupa damu na ubongo kila upande, sambamba na mlipuko mkubwa wa bunduki ya Mzee Malambi.

Yowe kubwa lilimtoka yule binti na kutimua mbio kuelekea nje ya pango lile, akiwapiga kikumbo vikongwe wawili wa mwisho waliokuwa wakiliendea lango la pango lile kwa mwendo wa ki-ndondocha.

* * *

Sasa kutokea kwenye redio ya ile Ford Anglia alikuwa akitumbuiza Gloria Gaynor na wimbo wake wa “I will Survive”, na Chambuso alikuwa akiufuatisha wimbo ule kwa mbinja nyororo, huku kule nyuma Esmund na Uwesu wakiwa kimya.

“Haloo, vipi nyie, mmelala huko?” Chambuso aliuliza huku akiendelea kuendesha.

“Kwani we’ shidayo nini?” Uwesu alimuuliza kwa kisirani, na Chambuso alitabasamu peke yake kule mbele.

“Eeeh, bado hayajaisha tu mwinyi?” Alimuuliza kwa maskhara, akijaribu kuizima ile hali ya jazba iliyopita baina yao.

“Kwani we’ wataka yaishe?” Uwesu aliuliza kwa kisirani kile kile kutokea kule nyuma.

“Haswa! Nataka yaishe kabisa shekhe wangu…”

“Basi nipishe niendeshe miye…” Uwesu alisema, na Esmund aliachia mguno mkubwa.

“Ddih! Bora tununiane tu mpaka huko mjini bwana, lakini kupewa wewe tena uendeshe! Hata siku moja!” Alisema kwa msisitizo. Chambuso alicheka kwa sauti kule mbele, na mara Uwesu naye akaungana naye katika kicheko kile. Kabla hawajamaliza, Esmund naye akaungana nao.

Ikawa ni cheko gari nzima.

“Ama! Kumbe watu bado hatujasahau namna ya kucheka eenh?” Chambuso alisema huku akiendelea kucheka, na kuibua mlipuko mpya wa vicheko ndani ya ile gari, na mtu asiye na nguo hata moja mwilini alichomoza mbio barabarani kutokea kwenye msitu uliokuwa kando ya barabara ile pweke huku akipiga kelele na akitupa mikono yake hovyo hewani.

“PUMMMMMMMBBAAAVVVVV….!” Chambuso alipiga ukelele huku akikanyaga breki kwa nguvu, ilhali akijua kuwa alikuwa anaelekea kumgonga yule mtu. Gari ilisota kwa kelele kumuendea yule mwanamke aliyeingia ghafla barabarani bila nguo usiku ule, na kule nyuma akina Uwesu walikuwa wakipiga kelele bila ya kujua ni nini kilichokuwa kikitokea kule mbele.

“CHAMBUSO UNATUUAAAAA!”

Mbele ya gari ile Chambuso alimuona yule mwanamama asiye na nguo mwilini akijikunja katikati ya barabara huku akijikinga kichwa chake kwa mikono yake wakati ile gari ikizidi kumsotea kwa kasi, sauti kali zikisikika wakati tairi zikisuguana na lami…

Kwa nukta moja ya sekunde Chambuso aliliona wazi wazi lile tukio la dakika kadhaa tu zilizopita, wakati Gari lao ilipokuwa ikiuendea ule mkorosho kwa kasi kubwa, likijirudia tena, na moyo ulimfa ganzi huku akimuona yule mwanamke asiye nguo akiwa amemulikwa na taa za lile gari katikati ya barabara, na gari likieleka kumgonga.

Gari halikuwa likienda kwa kasi sana, lakini yule mwanamke alichomokea karibu sana, na kwa umbali ule, ukichanganya na udhaifu wa gari ile baada ya ajali, haikuwa ajabu kabisa kwa breki kushindwa kufanya kazi kama zilivyotakiwa.

Huku naye akipiga kelele kwa woga na wahka, macho yakiwa yamemtoka pima, Chambuso alikandamiza mguu wake kwenye kikanyagio cha breki za gari ile kwa nguvu zake zote, lakini bado ile gari ikizidi kumsotea yule mwanamama.

“AYYYAAAAHHHHHH NAUAAAAAAAA…” Alipayuka huku akizidi kwa mbali akisikia sauti za woga na hofu kubwa kutoka kwa yule mwanadada aliyekuwa amejikunja katikati ya barabara, na kutokea kwenye kiti cha nyuma, mayowe ya Esmund na Uwesu yalizizima masikioni mwake.

Aaaah…! Nuksi…Nuksi…Nuksiiii…

Yote haya yalipita kichwani mwake haraka haraka sana, kabla hajapata akili ya kufanya kitu cha kukabiliana na hali ile. Ghafla, tena katika sekunde ya mwisho kabisa, aliupindisha usukani kwa nguvu, na kwa mara ya pili lile gari likaacha njia na kuingia porini, likimkosa kwa sentimeta chache sana yule mwanamke aliyekuwa akipiga kelele bila nguo katikati ya barabara.

Gari lilijikita kando ya barabara, upande mmoja ukiwa kwenye majani kando ya barabara wakati upande mmoja ukibaki barabarani, likiwa limelalia ule upande wa kando ya barabara. Kishindo cha lile gari kujikita kando ya barabara kiliwabwaga wote waliokuwa mle ndani, kila mmoja akiangukia upande wake mle ndani. Chambuso alibamiza kichwa chake kwenye dirisha la gari na alihisi maumivu makali mwilini mwake.

Kimya kilitanda ndani ya gari kwa sekunde kadhaa. Chambuso alibaki akiwa ameung’ang’ania usukani wa ile gari kwa nguvu huku moyo ukimpiga kwa woga usio kifani, akilini akijiuliza iwapo ni kweli aliona mwanamke asiye nguo akipepesukia ghafla barabarani, au yalikuwa ni mawazo yake tu. Ilikuwa ni maluweluwe tu…? Inawezekana kweli…?

Au alikuwa amesinzia huku akiendesha gari na akaota…?

Ee Mungu wangu, mambo gani tena haya…?

Alijaribu kuuachia ule usukani ili ateremke kwenda kuchunguza kile alichokiona, au alichodhani kuwa amekiona, lakini mikono yake ilikuwa ikimtetemeka vibaya sana, na ilikuwa imelowa jasho ghafla. Alizidi kuukamata kwa nguvu ule usukani kuzuia mikono yake isitetemeke hadi akahisi vidole vyake vikimuuma. Donge kubwa lilimkaba kooni na akajitahidi kujizuia asiangue kilio kwa taharuki.

Mungu wangu! Ee Mungu wangu…nuksi kubwa hii…!

Na hapo Uwesu alizinduka, akiparamia kiti cha dereva kutokea kule nyuma huku akimsuka-suka kwa hasira.

“Nini weye! Wataka kutuua yakhe? Huangalii uendako bwana? Au na we’ tuseme umelewa…?”

“Chambuso! Nini tena hii Chambuso…?” Esmund naye alimuuliza kwa wahka huku akijizoazoa kwa taabu kutoka kwenye sakafu ya gari.

Chambuso alibaki akiwa ameduwaa, macho yamemtumbuka pima, akitetemeka.

“We’ vipi bwana? Mbona umekuwa hivyo…? Unataka kutuua hivi hivi tu bwana? Tena uko peke yako barabarani na wala hujalewa?” Uwesu alizidi kumjia juu huku akimtomasa-tomasa kichwa chake kwa ncha za vidole vyake vya mkono, kama jinsi wengi tuwafanyavyo watu tuwaonao kuwa ni mabwege au waliofanya jambo la kibwege.

“Au ulikuwa unalala wewe…?” Esmund alimuuliza kwa ghadhabu.

“In…ina maana ham…kumuona…?” Chambuso aliuliza kwa kitetemeshi, huku bado akiwa amekodoa macho kule mbele, bumbuwazi ikiwa imemtawala.

Esmund na Uwesu walitazamana, kisha wakamgeukia taratibu.

“Nani?” Walijikuta wakimuuliza kwa pamoja, na Chambuso alifumba macho kwa kukata tamaa huku akimeza funda kubwa la mate.

Oh, Mungu wangu, nilikuwa naota…nilisinzia!

“In…na maana hamkumsikia…?” Aliuliza tena kwa kitetemeshi dhahiri.

“Nani bwana? Mbona unatuvuruga akili weye?” Uwesu alimjia juu huku akizidi kumpiga masingi. Chambuso aliwageukia taratibu wale wenzake, na kuwatazama kwa macho yaliyojaa woga mkubwa, midomo ikimtetemeka.

“Mwa-mwa-mwanam…ke!” Alijikuta akishindwa kabisa kuongea, akili ikiwa imemhama, ile taswira ya yule mwanamke asiye na nguo bado ikiwa wazi kichwani mwake.

“Khah?” Uwesu aliguna huku akimtazama kama kwamba alikuwa amerukwa na akili. Esmund naye aliachia mguno wa mshangao kwa namna yake baada ya kusikia yale maneno ya yule rafiki yao.

“A-alikuwa ka-ka-katik…kati ya bb-barab…bara!” Chambuso alisema huku akijaribu kujiaminisha kile alichokiona.

“Ayyaaah, twana lilikuwa limelala huku laendesha hili, hhih! Sa’ si nd’o tungekufa kijinga kuliko ile mara ya kwanza…walala hadi waota yakhe?” Uwesu alisema huku akimtazama kwa mastaajabu yaliyokithiri.

“Jamani! Kulikuwa kuna mtu…mwanamke…! Yuko u…u…ucch…uchh-i!” Chambuso aliwaambia kwa kitetemeshi kikubwa kabisa.

“Eti nini?” Esmund alimaka, kisha akamgeukia Uwesu,“jamaa yako kawehuka huyu! Hebu tuteremke tuiangalie hii gari kama itaweza…”

Vitu vitatu vilitokea kwa wakati mmoja.

Kwanza walisikia kishindo cha ghafla ubavuni mwa gari lao, kama kwamba kuna mtu kalipiga kwa nguvu gari lile kwa viganja vya mikono yake; pili, wote walisikia sauti ya kike ikigumia kwa woga; na tatu wote waliruka kwa mshituko huku kila mmoja akitoa sauti za woga na wakigeukia upande kilipotokea kile kishindo.

Kwanza waliona kiza tu, kisha, kabla hawajasema au kufanya lolote, waliona sura ya msichana ikijiinua kutoka ubavuni kwa gari lile, ambapo aliangukia wakati akijaribu kuikimbilia gari ile na mikono yake ikajipigiza kwenye ubavu wa gari ile wakati alipojaribu bila mafanikio kujishika kwenye mlango wa dereva ili asianguke. Yule msichana alichungulia ndani ya gari kupitia kwenye dirisha la dereva huku akilia na akiwasemesha kwa lugha ambayo kwanza hakuna yeyote kati yao aliyeielewa.

Si kizaazaa hicho!

Uwesu na Esmund walipiga kelele huku wakiparamiana kule nyuma, wote wakijaribu kuuwahi mlango wa upande wa pili wa gari ili watoke nje, na kuishia kuanguka tu mle ndani.

“Aaaaaakh! Kumbe kwel—li bwanaa-aaaa!” Uwesu aliropoka huku akifanikiwa kushika kifungulio cha mlango, na hapo Esmund alimparamia mgongoni na kujitupa nje pamoja naye huku akimtaja mama yake, akimtaka aende kumsaidia kutoka huko aliko.

Chambuso, aliyekutana uso kwa uso na yule binti, ambaye hapo awali alimuona kama mwanamke, na sasa alimuona kuwa kumbe alikuwa ni binti mdogo tu, alitumbua macho na kupiga yowe kubwa la woga huku akirukia kwenye kiti cha abiria kule mbele, lakini kwa namna fulani, mguu wake ukanasa kwenye usukani wa lile gari na akajikuta akirudi tena pale pale kwenye kiti cha dereva. Muda huo huo yule binti aliingiza mkono wake dirishani na kujaribu kumshika huku kwa mara nyingine akisema neno ambalo hakuwa na muda wa kulielewa, kwani ukelele mwingine mkubwa ulimtoka na akajikurupusha kwa nguvu kutoka kwenye kile kiti na kuangukia kwenye kiti cha pili.

Ilikuwa ni tafrani si kidogo!

“Toka Chambuso! Jini hilooo…!” Esmund alimpigia kelele akiwa nje ya gari ilhali amemfungulia ule mlango wa abiria wa upande wa pili wa gari. Chambuso alijitupa nje ya gari na kujibiringisha kwenye majani na michanga huku akibwabwaja vitu kuhusiana na nuksi zilizomuandama usiku ule.

Sasa wote watatu walikuwa nje ya gari, upande wa msituni, wakati yule binti akiwa upande wa barabarani, lile gari ikiwa katikati yao. Kuona hivyo, binti alikimbia kulizunguka lile gari akijaribu kuwafuata wale vijana watatu waliobaki wakiwa wamesimama pamoja, macho yamewatoka kwa woga na mastaajabu makubwa. Na pale yule binti alipozungukia mbele ya lile gari, taa za lile gari ziliumulika mwili wake mbichi usiokuwa na nguo.

“E bwana wee!” Uwesu aliropoka huku mdomo ukimuanguka, akiukodolea macho yasiyoamini ule mwili wa kike uliochongeka vizuri kabisa, wakati Esmund na Chambuso walijikuta wakisogeleana na kushikana mikono kwa woga, wakimtumbulia macho yule binti.

Sasa yule binti alikuwa amesimama mbele ya lile gari akilia huku akitetemeka na akitikisa kiganja cha mkono wake mmoja kama jinsi wanawake wengi wafanyavyo pindi wakiwa wameshikwa na woga mkubwa.

“Ji…jini hili jamani!” Kwa mara ya pili Esmund alijiropokea huku akitetemeka.

“Wayangu! Wayangu munisaidie…(Jamani! Jamani…nisaidieni)!” Yule binti aliwalilia huku akiwa anawatazama kwa macho ya kuomboleza, machozi yakimtiririka, na Chambuso alishtuka kidogo pale ile lugha aliyokuwa akiitumia yule binti ilipomuingia kichwani.

“Ngoja! Sio jini huyu…ni…ni…mtu…! Lakini…lakini…” Alianza kuwaambia wenzake.

“Nie myago nolonda…nolonda munisai-die…nofaaa(…naomba…naomba mnisaidie…nakufaaa)!” Binti alizidi kuwasemesha kwa masononeko mazito huku akilia na kuwasogelea kwa hatua za kubahatisha, bila ya kujali kuwa hakuwa na nguo hata moja mwilini mwake.

Yeye mwenyewe alikuwa amepagawishwa na mambo aliyokutana nayo huko alipokuwa, lakini wale vijana hawakujua hilo.

Wangejuaje?

Hakika ulikuwa ni mtihani mkubwa kila upande. Bila ya kupenda, Esmund na Uwesu walirudi nyuma na kumuacha Chambuso akiwa amesimama pale pale alipokuwa, akimtazama yule binti.

“Anasema nini huyo…?” Uwesu alibwata huku akirudi nyuma.

“Subiri…! Mi’ nadhani namuelewa!” Chambuso alisema huku akimtazama kwa makini yule binti, na kuongeza huku naye akimsogelea yule binti, “Anaongea kizaramo huyu…anaonekana ana matatizo.”

“Shauri yake bwana, tuondokeni hapa jamani…upesi tena!” Esmund alisema kutokea nyuma yake. Lakini sasa Chambuso alikuwa ameshatulia, na akili yake ilikuwa imeshaanza kufanya kazi itakiwavyo. Aliona kuwa yule binti alikuwa kwenye matatizo mazito kuliko wao.

“Huyu anahitaji msaada jamani…” Aliwaambia wenzake.

“We’ una wazimu nini? Yeye ndio tatizo lenyewe! We’ mtoto wa kike unatembea uchi katikati ya usiku namna hii? Tuondokeni jamani, tena tuondokeni upesi sana…bila shaka ni kachawi hako!” Uwesu alimaka kwa kitetemeshi.

Yule binti aliwatazama wale vijana watatu, na mara moja akaona kuwa ni Chambuso ndiye aliyeelekea kuwa mkombozi wake, hivyo kauli yake iliyofuata aliielekeza moja kwa moja kwake.

“Wanhu…wanhu…(watu…watu…)”

“Kulongadhe…(Unasemaje)?” Chambuso alimuuliza kwa lugha ile aliyokuwa akiitumia yule binti huku akimsogelea.

“We’ Chambu we’! Bila shaka hako ni ka-kibwengo ujue! Hebu achana nako bwana…!” Esmund alimuambia kwa mashaka mazito.

“Hebu toka huko! Kibwengo unamjua wewe? Huyu mtu yuko taabuni huyu….labda kuna watu walitaka kumbaka huko atokako…?” Chambuso alimbishia.

“Wanhu…wahawi…(Watu…wachawi…)!” Binti alikuwa akisema huku akili, na akizidi kumsogelea Chambuso, na alipofanya hivyo, alijiweka moja kwa moja mbele ya taa za lile gari.

Macho yalimtoka pima Uwesu. Yakapanda moja kwa moja hadi usoni kwa yule binti. Binti hakuwa mbaya masikini…alikuwa na sura ya kuvutia tu…

Uwesu akashusha macho yake hadi kifuani kwa yule binti na kuona jinsi matiti yake madogo yalivyochachamaa kifuani pale, na moyo ukaanza kumuenda mbio, pumzi zikimtoka kwa mbinja nyepesi, na wakati huo huo akihisi mzizimo maridhawa kutokea sehemu iliyo katikati ya miguu yake miwili. Akashusha macho yake chini zaidi na kutazama ile sehemu ambayo miguu miwili ya binti yule ilikuwa ikikutana, chini kidogo ya tumbo lake bapa, na kuyazungusha macho yale kwenye kiuno chembamba cha binti yule, na kuyatembeza kwenye mapaja yaliyonona ya binti yule wa kizaramo, na koo likamkauka.

Alimtupia jicho la pembeni Esmund, na kuona jinsi naye alivyokuwa amekamatika na umbile la binti yule mbichi. Alitamzama Chambuso aliyekuwa hatua chache mbele yao, kisha akamgeukia tena Esmund. Walitazamana, mawazo ya ajabu yakipita vichwani mwao na wakielewana bila hata ya kuongea.

“Eeem, Cha-Chambu…una hakika huyo sio jini huyo…?” Uwesu aliuliza kwa mashaka.

“Huyu binadamu jamani, sio jini wala nini…ni mtu kama sisi, na anahitaji msaada!” Chambuso alimjibu, kisha akamsogelea taratibu yule binti na kumuuliza kwa upole.“Eeee binti, unaweza kuongea kiswahili? Mimi sijui sana kizaramo, lakini tunataka kukusaidia…jina lako nani?”

Binti alimtazama kwa matumaini,.“Ndiyo…naongea kiswahili…nisaidieni!” Sasa Chambuso na yule binti walikuwa wamekaribiana sana. Nyuma yao, Uwesu na Esmund walianza kuwasogelea taratibu, ilhali mioyo yao ikiwaenda mbio, mawazo ya ngono yakichuka nafasi ya busara haba walizokuwa nazo.

“Sawa, tutakusaidia…” Chambuso alimhakikishia yule binti huku akimtazama kwa makini, na kumtupia swali, “…kwani we” ni nani, na inakuwaje uko hapa saa hizi…katika hali kama hiyo?”

Badala ya kumjibu, yule binti alianza kusikia tena yale makelele kichwani mwake, na akajishika kichwa huku akifunua kinywa na kufinya macho yake kwa uchungu, bila ya kutoa sauti yoyote. Chambuso alimsogelea haraka, uso wake ukiwa na wasiwasi mkubwa.

“Ni nini binti…unaumwa kichwa?”

Binti hakumjibu, bali alizidi kujishika kichwa namna ile huku akijikunja hata akawa amepiga goti mbele ya Chambuso, sasa sauti nyembamba ya kuugulia maumivu ikimtoka. Haraka haraka Chambuso alivua shati lake kubwa na kumuinamia yule binti pale chini.

“Hebu jifunike na hili shati kwanza…” Alimuambia huku akimuwekea lile shati mabegani. Binti aliinua uso wake uliojifinya kwa maumivu aliyokuwa akiyahisi kutokana na kelele zilizokuwa kichwani mwake. Alilipokea lile shati na kulifunga haraka kiunoni na kuusitiri kidogo utupu wake mbele ya wale marijali watatu wenye mitazamo tofauti juu yake.

Chambuso alimuinua kutoka pale chini na kumuuliza tena jina lake na kutaka kujua iwapo alikuwa anaumwa. Binti alianza kusema kitu, lakini ghafla akahihisi akili yake ikiwa tupu. Hakujua aseme nini. Alianza kulia.

Muda huo Uwesu na Esmund walimzonga yule binti kutoka kila upande, na Chambuso, aliyekuwa amebaki na fulana mchinjo tu, aliwatazama wale wenzake.

“Jamani huyu binti anahitaji msaada…naona tumchukue na tutafute nyumba yoyote hapa jira…” Alianza kuongea, lakini alipoona jinsi wale wenzake walivyokuwa wakimtazama yule binti kwa uroho ulio wazi kabisa, akakatisha kauli yake na kuwauliza haraka, “Nyie vipi…?”

“Sikiliza we’ lofa…huyu binti sisi hatuendi naye popote! Tunachofanya ni kumalizana naye hapa hapa, kisha twenda zetu! Alomtuma kutembea peke yake usiku kama huu, tena bila nguo nani? An’taa kutufanya sie makhanithi bure hapa!” Uwesu alisema kwa jazba huku akimkamata mkono kwa nguvu yule binti.

Chambuso alimtazama kwa mshangao usio kifani, kwani hakika hakuamini kile alichokuwa akikisikia na kukishuhudia. Alimgeukia Esmund kwa mshangao kutaka kuona ni jinsi gani naye atakuwa ameshangazwa na ile tabia ya Uwesu.

“Ndiyo! Kama we’ huwezi mambo haya kwa sababu unaenda ulaya basi tuachie sisi tumalize mchezo huu!” Esmund naye alimuunga mkono Uwesu kwa ushabiki.

Loh!

“Khah! Ama kweli nyie maluuni! Yaani…hivi mnajua kuwa mi’ siwaelewi! Kwa hiyo…nd’o kusema mnataka kumfanyaje?” Aliwauliza huku akimtazama mmoja baada ya mwingine, sasa akiwa amemzungushia mkono wake mabegani yule binti ili asiangukie mikononi mwa Uwesu aliyepandwa na mzuka wa kutenda dhambi iliyokemewa sana na muumba.

“Chambuso usiwe mjinga! Yaani mtoto mbichi namna hii tumuachie? We’ juha nini? Leo lazima tule ngoma hii, ala!” Uwesu alimchachamalia kwa jazba, macho yamemtoka pima. Binti aliachia ukelele mkubwa wa woga, na kuzidi kumng’ang’ania Chambuso.

“Say Whaaaat?? Are you out of your bloody minds?” Chambuso aliwajia juu kwa mshangao huku akimficha yule binti mgongoni kwake.

“Hebu tupishe sisi weye!” Uwesu alimvimbia huku akimsukuma. Chambuso alipepesuka lakini hakumuachia yule binti, ambaye alizidi kupiga kelele za woga.

“Aaakh! We’ vipi? Hebu…” Chambuso alilalama, lakini kabla hajamaliza Esmund alimvuta kwa nguvu yule binti, na hapo hapo Uwesu alijiweka mbele ya Chambuso kumzuia asimsogelee Esmund, ambaye sasa alikuwa amemshika yule binti.

Chambuso akabaki akitazamana na Uwesu, wote wakitweta kama majogoo yanayotaka kupambana. Huku kwa Esmund, binti alikuwa akijikukurusha kwa nguvu, na Esmund alikuwa akihangaika kumdhibiti, na katika purukushani zile, lile shati la Chambuso ambalo yule binti alikuwa amejisitiri nalo likamuanguka na akabakia utupu kama hapo awali.

“Uwesu hebu acheni ujinga bwana!” Chambuso alimkemea mwenzake kwa ukali huku akimuoneshea kidole. Uwesu hakumjibu kitu, bali alibaki akimtazama kwa macho ya kuogofya, pua zikimtanuka na kumsinyaa.

“Nyie si ndio mliokuwa mkisema kuwa huyu binti ni jini au kibwengo? Sasa tena mnataka kum…kumbaka…kibwengo…? Hebu mlaanini shetani jamani! Acheni! Msifanye hivyo…” Chambuso alizidi kumsihi Uwesu, na hapo wote wawili walishtushwa na ukelele mkubwa wa uchungu kutoka kwa Esmund, na walipogeuka, walimuona Esmund akiwa amejishika sehemu ya uume wake huku akizidi kugumia. Yule binti alikuwa amejishika kichwa kwa woga huku akimtazama yule rijali aliyejikunja kwa uchungu mbele yake baada ya kumpiga kwa goti katikati ya miguu yake.

“BINTI KIMBIAAA…!!” Chambuso alimpigia kelele yule binti, na bila ya kujishauri zaidi binti alitimua mbio huku akipiga mayowe.

“AH! Pumbaaavu!” Uwesu alilaani, na hapo hapo alitoka mbio kumfuata yule binti. Esmund naye alijizoa zoa na kuanza kumfuata Uwesu, naye akimkimbiza yule binti. Lakini hapo Chambuso akazinduka. Alimrushia teke zito la mbavu, na Esmund aliachia yowe la uchungu huku akienda chini kwa kishindo.

“Washenzi wakubwa nyie!” Chambuso alimkemea huku akitimua mbio kumfuata Uwesu aliyekuwa akimkimbiza yule binti asiye nguo.

Usiku ule ule, kule Shungubweni wilayani Mkuranga, msako wa kuwasaka wale wavuvi watatu ulikuwa ukiendelea bila mafanikio.

Wanakijiji walikuwa wamerundikana vikundi-vikundi ukingoni mwa bahari ile, wakisubiri kwa hofu kubwa matokeo ya msako ule. Ndugu na jamaa za wavuvi wale walikuwa wakilia kwa uchungu na maombolezo mazito, kwani kila dakika iliyokuwa ikipita bila ya badiliko lolote katika hali iliyokuwako, ilizidi kugongelea ule msumari wa ithibati kuwa wale jamaa zao walikuwa wamekufa. Samaki wengi walikuwa wakielea baharini na kutupwa ufukweni wakiwa wamekufa, bila shaka ni kutokana na tukio lile lile lililosababisha wale wavuvi watatu wapotee, na hali ile ilizidi kuwakatisha tamaa ya kuwapata wenzao wakiwa hai,.wanakijiji wale.

Sasa walichokuwa wakikiombea ni kuipata ile miili ya wale wapendwa wao tu, ili angalau wapate kuwazika ipasavyo badala ya miili yao kupotelea baharini na kuwa chakula cha samaki.

Lakini upande mwingine wa pwani ile, kiasi cha kama kilomita moja hivi kutoka pale ambapo wale wanakijiji walikuwa wamejikunyata kwa hofu, mashaka na baridi, mwili mmoja uliibuka kutoka baharini na kuelea ukiwa umelala kifudi fudi miongoni mwa rundo la samaki waliokufa, kuelekea ufukweni mwa bahari ile. Ulikuwa ni mwili wa mwanaume mrefu mwenye misuli iliyoshiba.

Mwili ule uliokuwa na kaputura kipande tu bila ya nguo nyingine yoyote, ulikuwa ukisukumwa taratibu na mawimbi ya bahari ile kuelekea eneo pweke sana katika pwani ile ya Shungubweni. Eneo lililozongwa na mikoko na msitu mdogo usiokaliwa wala kutembelewa na watu.

Ule mwili ulitupwa ufukweni na kubaki ukiwa umelalia tumbo pale mchangani, ilhali sehemu ya chini ya mwili ule bado ikiwa kwenye maji.

Si ule mwili uliokuwa umelala pale ufukweni wala wale watu waliokuwa wakiendesha msako wa miili ya wale wavuvi watatu waliozama baharini usiku ule, aliyejua ni nini kingefuatia baada ya kuibuka kwa mwili ule kutoka kule baharini katika usiku ule uliojaa matukio tata. Na hiyo ilitokana na ukweli kwamba ingawa ule mwili ulioibuka ulikuwa ni wa mmoja wa wale wavuvi watatu waliokuwa wakisakwa usiku ule aliyejulikana kama Jadu Mfaume, lakini kiumbe kilichokuwa ndani ya mwili ule kilikuwa ni tofauti kabisa na Jadu Mfaume mvuvi, ambaye hata wakati ule bado wanakijiji wenzake walikuwa wakiendelea kumsaka. Yeye pamoja na wale wenzake wawili…

* * *

Binti alikuwa akikaribia kuivuka ile barabara na kukimbilia kwenye kichaka kilichokuwa upande wa pili wa barabara ile huku akipiga kelele. Uwesu Shaame alijirusha mzima mzima na kumdaka kiuno, kisha wote wawili wakapiga mwereka mzito, wakibiringishana kwenye majani. Binti alikuwa akipiga kelele za hamaniko, na Uwesu alikuwa akigumia huku bado akiwa amemkamata kwa nguvu kiunoni.

Nyuma yao, Chambuso Mwagala alikuwa akiwakimbilia kwa kasi, uso ameukunja kwa hasira, moyo ukimuenda mbio kwa jazba, na akili ikimzunguka kwa jinsi ambavyo mambo yalivyokuwa yakigeuka kwa kasi ya ajabu baina yake na wale wenzake. Nyuma yake alisikia vishindo vya Esmund aliyekuwa akimkimbiza huku akimvurumushia matusi, lakini hakuwa na la kufanya. Akili yake ilikuwa kwa yule binti na Uwesu kule mbele yake.

Ni lazima amsaidie yule binti…hata iweje! Hawezi kuangalia udhalimu kama ule ukifanyika mbele ya macho yake.

Sasa Uwesu alikuwa amembana chini yule binti aliyekuwa amelalia tumbo pale kwenye majani huku akihangaika kwa nguvu zake zote kujinasua kutoka kwenye himaya ya yule baradhuli mwenye nia mbaya.

Chambuso aliruka mzima mzima na kumkumba Uwesu kutoka pale kwa yule binti na kuanguka naye pembeni.

“Aaaarghh! We’ Chambu…!” Uwesu alimaka, lakini kabla hajaendelea kulalama zaidi, Chambuso alikuwa ameshainuka na kumtandika teke kali la uso. Uwesu alitupwa nyuma kwa teke lile huku yowe la maumivu likimtoka.

Huku nyuma, binti alianza kujiinua kutoka pale chini lakini muda huo huo Esmund alimrukia na kumpeleka tena chini, ambako alimgandamiza kwa nguvu.

Binti alipigana kwa fujo huku akipiga kelele, akimparua Esmund usoni kwa kucha zake. Ukelele wa ghadhabu ukamtoka Esmund, na hapo hapo akamtamdika kofi kali sana la uso yule binti. Yowe la uchungu na mshituko lilimtoka yule binti, na kabla hajatanabahi Esmund alimbana vizuri zaidi pale chini, akimkalia na kukibana kiwiliwili cha yule binti, ambaye sasa alikuwa chali, katikati ya mapaja yake.

Binti alijikurupusha kwa nguvu, lakini hakuwa na namna ya kujinasua kutoka pale alipobanwa, na ndipo kwa mara ya kwanza Esmund alimposikia yule binti akitoa sauti zisizo za kawaida, lakini yeye wala hakuzitilia maanani, mzuka wa ngono ulikuwa umeshamkolea.

Akiamini kuwa ameshammaliza Uwesu, Chambuso aligeukia kule kwa Esmund, na alipoona jinsi Esmund alivyombana yule binti, ghadhabu zaidi zikampanda.

“ESMUUUND!” Aliita kwa hasira huku akikimbilia pale walipokuwako Esmund na yule binti.

Kosa! Uwesu aliinuka upesi kutoka pale alipoangukia akiwa na jiwe kubwa mkononi, na wakati Chambuso anageuka na kuanza kumkimbilia Esmund, yeye alimkimbilia kwa kasi, huku akiwa ameuinua juu kabisa ule mkono ulikuwa na lile jiwe, na kuushusha kwa nguvu kichwani kwa Chambuso, jiwe lililokuwa mkononi kwake likikutana kwa kishindo cha kutisha na kisogo cha yule mwenzao. Yowe hafifu lilimtoka Chambuso wakati maumivu makali yalipotawala kichwa chake na kumtambaa mwilini kote, mwanga mkali ukilipuka ghafla mbele ya macho yake, miguu ikaacha kumbeba na magoti yakagongana. Mboni zake zikatumbukia ndani kabisa ya macho yake, kisha kote kukawa kiza totoro.

Akapoteza fahamu.

Ukimya uliotanda kichwani kwa Chambuso baada ya kile kiza kizito kutanda mbele ya macho yake kabla ya kupoteza fahamu, haukuwa tofauti kabisa na ule ukimya uliotawala kwenye ule uwanja wa michezo, katika muda ule ule, kilomita kadhaa kutoka pale kwenye ile barabara ya Pugu-Kazimzumbwi.

Uwanja wote ulikuwa kimya kabisa, macho yote ya waliokuwepo yakiendelea kuwakodolea wale askari wawili waliosimama mbele ya ile milingoti miwili ya bendera, ambao walikuwa wamekakamaa kama ile milingoti iliyokuwa mbele yao, nyuso zao zikiwa zimeinuliwa moja kwa moja mbele yao. Wakihema kwa nguvu. Wakisubiri.

Sekunde zilizidi kusogea, muda uliokuwa ukisubiriwa ulikuwa ukiwadia kwa kasi sana, na kila aliyekuwepo pale uwanjani hakutaka kupiga kelele hata kidogo wakati tukio walilokuwa wakilisubiri kwa muda mrefu lilipokuwa likikaribia.

Wote walitaka kushuhudia kila hatua ya tukio lile adhimu, na kadiri dakika zilivyozidi kukaribia ndivyo ukimya ulivyozidi kutawala. Na sasa ukimya ule ndio ulikuwa umefikia kilele…

* * *

Uwesu alitupa pembeni lile jiwe na kukimbilia pale Esmund alipokuwa akikukurushana na yule binti. Esmund alikuwa akipata taabu kumdhibiti yule binti, kwani kila alipokuwa akimbana ili aweze kufanya lile alilolikusudia, yule binti alikuwa akijiinua na akijitupa tupa huku na huko.

“Tulia! Malaya mkubwa, tulia!”

“Sitakiii!! Yeeeekkhhh…!” Binti alipiga kelele. Esmund alimzaba kofi kali usoni, na kwa mara nyingine binti aliachia yowe la uchungu. Uwesu alimuendea na kumsukuma Esmund pembeni kwa nguvu,.“Hebu sogea huko weye!” Alimuambia. Esmund alianguka pembeni naye akamrukia yule binti na kumkalia. “Yaani huyu ndiyo ana…” Alisema kwa hasira, na hapo hapo alimtandika kofi kali sana la uso yule binti, ambaye alipiga kiyowe kikali na kubaki akiwa ameduwaa kwa mshituko, na Uwesu akamalizia sentesi yake, “…kupa taabu kiasi hiki?”

Hapo hapo alimbana koo yule binti kwa mkono wake wa kushoto huku kwa mkono wake wa kulia akifungua kwa pupa mkanda wa suruali yake, bila ya kujali purukushani za yule binti aliyembana baina ya mapaja yake pale chini. Binti alikuwa akitupa mikono yake kwa fujo, akijaribu kumparura usoni kwa kucha zake, na akitupa tupa miguu yake huku na huko. Lakini Uwesu alikuwa amejituliza sawia katikati ya miguu ya yule binti asiye na nguo, na akirudisha nyuma uso wake kiasi ile mikono ya yule binti ikashindwa kufanya madhara yoyote usoni kwake.

Lakini mkanda ukawa haufunguki kama jinsi alivyotaka.

“Sheeeiiittt…Huu mkanda vipi huu?” Uwesu alilalama kwa hasira huku akiendelea kuuvuta ule mkanda ilhali bado amembana yule binti pale chini. Alimgeukia Esmund kwa hasira.

“Hebu mkamate huyu Malaya weye! Unanishangaa tena?”

Esmund aliruka haraka na kumbana mikono yule binti. Uwesu akafungua ule mkanda kwa mikono yake yote miwili na kuteremsha suruali yake kwa pupa.

Macho yalimtoka yule binti, na hapo akajua kuwa alikuwa amepatikana. Alikuwa amebanwa vizuri sana na wale watu wawili, naye hakuwa na ujanja tena.

Zile kelele za ajabu zilizidi kuzizima kichwani mwake na kumpotezea kabisa uwezo wa kufikiri. Alifunua kinywa apige kelele, lakini kilichotoka kinywani mwake kilikuwa ni kitu tofauti, tena kwa sauti isiyo yake.

“Hapana! Bado! Bado…badooo! Mpaka baada ya siku saba za kibinadamu! Siku saba! Siku sabaaa….siku sabaaaaa! Msi-aaaargh, siyo nyieeee…SIO NYIEEEEE!!”

Kwa muda Uwesu na Esmund walipigwa na butwaa. Hawakuelewa ni nini yule binti alikuwa akisema, na walishangaa jinsi sauti yake ilivyobadilika ghafla na kuwa ya kiume.

Laiti wangejua, hapa ndio palikuwa mahala pa kumuacha yule binti na kutimua mbio. Lakini tayari ibilisi alikuwa ameshawapanda…

“Ish! Huyu demu vipi huyu…? Anaongea vitu gani?” Esmund aliuliza kwa mashaka. Walitazamana, Uwesu tayari akiwa ameshaishusha kabisa ile suruali yake na hata ile nguo yake ya ndani. Binti alimkodolea macho kwa kihoro kikubwa yule kijana aliyekuwa na dhamira mbaya juu yake. Alifunua tena kinywa chake kujaribu kuwaomba wale vijana wamuachie huku akibubujkwa na machozi.

“Niacheni jamaniii

(mwenzenu nimeshachumbiwa ndugu zangu…mtaniharibia maisha yangu bure)

mtafanya kosa kubwa sanaaaa…mtajutaaa!”

Esmund na Uwesu walizidi kutazamana, kisha Uwesu alitoa tusi zito na kuanza kulazimisha kumuingilia kwa nguvu yule binti mbichi, huku Esmund akiwa amemshika yule binti.

Binti alipiga kelele kubwa sana huku akijitutumua kwa nguvu zake zote kupingana na kitendo kile. Ilikuwa ni purukushani nzito iliyodumu kwa kama dakika tano hivi, Uwesu akilazimisha kumuingilia yule binti, kijasho kikimvuja, macho yakiwa yamemuwiva huku mishipa ya kichwa, shingo na mikono ikiwa imemtutumka. Lakini kila alivyojaribu, binti alikuwa akijitupa huku naye anashindwa. Akijaribu tena, binti anajitupa huko, naye anashidwa. Muda wote huo Esmund naye alikuwa anajitahidi kumbana yule binti, lakini ilikuwa ni kama kwamba ghafla tu yule binti aliingiwa na nguvu za ajabu za kuwadhibiti wale marijali wawili.

“Tulia weweee! Tulia!” Uwesu alimfokea kwa hasira na hapo hapo akambabatiza kofi zito la uso, binti akalia kwa uchungu, na hapo hapo Esmund naye akambamiza ngumi nzito iliyotua chini kidogo ya jicho la yule binti.

Binti alilia kwa uchungu na pasina kupenda, alipeleka mkono wake pale kwenye jicho lake lililojeruhiwa. Na hapo alijisahau kabisa, akili yake ikahamia kwenye maumivu yaliyotawala kichwa na jicho lake, na Uwesu akatumia nafasi hiyo kutimiza lengo lake.

Binti alihisi maumivu mengine makubwa sana na akapiga kelele. Uwesu akazidi kujisukumiza zaidi kwa yule binti mbichi huku akibwabwaja kwa ulimbukeni uliothibiti.

“Aaaaahh! Kumbe…mtoto…” Alizidi kupayuka huku akizidi kujisukuma kwa nguvu, na binti akizidi kulia kwa uchungu na maumivu makali kabisa aliyokuwa akiyahisi.

“…bik…bikkrr….bikkra bwana!” Uwesu alimalizia kauli yake huku akihisi mlipuko wa faraja ya haramu kifuani kwake.

“E bwana we!” Esmund alibwatuka kishabiki, huku akiwa ametumbua macho, udenda ukimbubujika bila kujitambua.

“Yalaaa! Mama weee! Nilekeseee! Naumiaa…mamaangu weee naumiaaaa!” Binti alizidi kulia.

“Kelele wewe!” Esmund alimfokea huku bado akiwa amemshikilia pale chini wakati mwenzake akiendelea kumfanyia ule unyama usiosemekana yule binti, naye akisubiri zamu yake ya kumfanyia jambo lile baya na ambalo bila ya wao kujua, lilikuwa na madhara makubwa sana kwao na kwa walimwengu wengine wengi tu…tena kwa miaka mingi ambayo ingefuatia.

Kwani pasina ya wale marijali wawili wajinga kujua, wakati ule walikuwa wakiingilia kati kitu kilichoanzishwa na viumbe wenye uwezo mkubwa na wa ajabu sana.

Maumivu makali yalizidi kumtawala yule binti, na Uwesu akazidi kujisukuma ndani yake, safari hii akifika pale alipokuwa anapataka.

Uwesu aligumia kwa faraja pale lile tendo alilokuwa akimfanyia yule binti lilipomfikisha kileleni, bila ya kujali vilio vya maumivu na maombolezo kutoka kwa yule binti asiye na hatia.

Na baada ya Uwesu kumaliza haja zake kwa yule binti, Esmund Bwaira naye alianza…

* * *

Sehemu moja katikati ya jiji saa kubwa iliyokuwa kwenye mnara mrefu iligonga saa sita kamili za usiku, na kule uwanjani ambako sherehe zilikuwa zikiendelea, bendi ya polisi ilipiga wimbo wa taifa kwa mara ya kwanza. Wananchi walisimama, wote wakiwa kimya kabisa kwa heshima. Mara wimbo ule ulipokwisha, uwanja ulilipuka kwa shangwe na vifijo, huku wananchi walioshuhudia tukio lile adhimu usiku ule, wakipongezana kwa kila namna, wakati bendera moja ikipepea juu kabisa ya mmoja kati ya ile milingoti miwili iliyokuwapo pale uwanjani.

Historia ya taifa jipya na huru ilikuwa imethibiti, na waliokuwepo pale uwanjani usiku ule walikuwa na hilo tu vichwani mwao. Hakuna hata mmoja aliyekumbuka tena juu ya kile kitu kilichoonekana kikishuka kwa kasi kutoka angani na kusababisha kiza kizito kwa sekunde chache pale uwanjani. Badala yake, hoi hoi, nderemo na vifijo vilitanda kila upande, na hata pale wakuu wapya wa nchi walipoanza kutoka pale uwanjani kurejea majumbani kwao, wananchi waliokuwa pale uwanjani waliendelea kusherehekea kwa ngoma, nyimbo, ngonjera, na kila jambo ambalo kwao lilileta hisia ya sherehe.

Walilokuwa wakilisubiri kwa muda mrefu sasa lilikuwa limetimia, na wao walikuwa wamelishuhudia. Siku mpya ilikuwa imeanza, ukurasa mpya ulikuwa umefunuliwa mbele ya macho yao, na kila aliyekuwa akitoka pale uwanjani hakuweza kujizuia kuitupia macho ya heshima ile bendera iliyokuwa ikipepea kwa majivuno kabisa kwenye ule mlingoti.

Hakika lililokuwa likionekana kama haliwezekani sasa lilikuwa limetimia. Si yeyote kati yao aliyekuwa na hata chembe ya wazo juu ya nini kilikuwa kikitokea, katika muda ule ule, kule kwenye ile barabara ya Pugu-Kazimzumbwi, na kule kwenye pwani ya Shungubweni, Wilayani Mkuranga.

* * *

Muda ile saa ilipogonga saa sita kamili za usiku kule mjini, kule pwani ya Shungubweni wilayani Mkuranga, mvuvi aliyejulikana kama Jadu Mfaume alifumbua macho yake ghafla, kama aliyeshtushwa na kitu fulani, na kubaki akiwa amelala kifudi fudi kando ya ile bahari kwa dakika kadhaa huku akitembeza macho yake huku na huko, akijaribu kuyasoma yale mazingira aliyokuwako. Kote kulikuwa kimya kabisa, isipokuwa kwa sauti hafifu za mawimbi yaliyokuwa yakijibwaga bwaga kivivu kwenye ufukwe ule alioibukia baada ya…baada ya…

Hakukumbuka alikuwa akifanya nini kabla ya kujikuta akiwa amelalia tumbo pale ufukweni. Wazo hilo lilipita kidogo sana kichwani mwake kisha likapoteza umuhimu, na badala yake kichwa chake kikaanza kufikiria mambo tofauti kabisa. Mambo ambayo Jadu Mfaume asilia asingeweza kuyafikiria hata siku moja maishani mwake.

Nina jukumu la kufanya…nina jukumu kubwa la kufanya…

Huku mawazo hayo yakipita kichwani mwake, alianza kujiinua taratibu kutoka pale mchangani.

Natumai hapa nilipokuja nitafanikiwa kuwaona ninaowatafuta…

Aliangaza kulia na kushoto, na kuona kuwa kote kulikuwa ni kiza kitupu. Mbele yake aliona msitu mdogo. Alianza kuhisi baridi mwilini mwake na akatetemeka kidogo

Nahitaji nguo…kivazi…na chakula…

Alianza kuuendea ule msitu kwa mwendo wa kuyumba na kujiburura, miguu yake akiihisi mizito sana, na maungo yote yakimuuma.

Sina muda wa kupoteza…yanipasa nianze kazi mara moja…

Aliwaza huku akiuingia ule msitu.

Alikuwa amefika kwenye sayari nyingine katika msako wake wa ulimwengu. Msako ambao umemchukua muda mwingi sana, na uliomfikisha Masi, Neptune, Satani, na sayari nyingine kadhaa, bila ya mafanikio yoyote.

Labda katika nchi hii ngeni iliyoko katika sayari ya dunia atafanikiwa kuwapata anaowatafuta na kuwaangamiza …kabla muda haujaisha.

Bila ya kujali kiza alizidi kusonga mbele, akikatisha katikati ya msitu ule bila woga. Aogope nini wakati yeye hakuwa yule Jadu Mfaume mvuvi, aliyezama baharini muda mfupi uliopita?

Kama wale wanakijiji waliokuwa wakiwatafuta Jadu na wenzake kule baharini wangemuona kwa muda ule, basi wangemtambua kwa sura yake tu, lakini hakika wangemshangaa mno kwa vitendo vyake.

Akiwa anaendelea na safari yake, alijikuta akikabiliana na mkanganyiko wa mawazo, mara akiwaza kama Jadu Mfaume mvuvi, mara akiwaza kama kiumbe tofauti kilichokuwa ndani ya mwili wa Jadu Mfaume mvuvi. Na kila alipokuwa akiwaza kama kiumbe tofauti alijikuta akipandwa na hasira kali. Hasira dhidi ya watu aliokuja kuwasaka…hasira ambayo ingeisha pale tu atakapofanikiwa kuwaangamiza wabaya wake aliokuja kuwasaka katika nchi hii ngeni, ya viumbe wa ajabu lakini dhalili kwake…

Nahitaji nguo…na chakula…kisha nifanye kazi….

Njaa ilikuwa ikimuuma sana, naye hakuwa na jinsi zaidi ya kuendelea kusonga mbele tu. Baada ya mwendo wa saa moja alikwa ameumaliza ule msitu. Akiwa kwenye kingo ya msitu ule, aliweza kuona vibanda vya wavuvi kwa mbali. Pia aliweza kuziona nyumba za wanakijiji kile cha Shungubweni. Alisita kidogo, asijue aende wapi kati ya kule kwenye vibanda vya wavuvi, au kule kwenye makazi ya wanakijiji.

Njaa…kula kwanza…kisha kazi…

Alianza kupiga hatua, safari hii zikiwa za haraka, kuelekea kule kwenye makazi ya wanakijiji. Mara aliona mtu akielekea kule alipokuwapo, kutokea kule kwenye makazi ya wanakijiji akielekea kule baharini kujiunga na wenzake kwenye msako wa wale wavuvi waliopotea. Jadu alisita.

Simama. Usimsemeshe.

Akasimama. Yule mtu aliyekuwa akitembea haraka haraka, hakuwa amemuona Jadu, ingawa alikuwa ameshika tochi yenye mwanga mkali iliyokuwa ikimulika huku na huko wakati akitembea. Ghafla yule mtu alimuona Jadu na akaruka kwa mshituko huku akimmulika kwa tochi yake usoni. Haraka Jadu alijikinga macho yake kutokana na mwanga wa tochi ile kwa kiganja cha mkono wake. Lakini yule mtu aliwahi kuyaona macho yake kabla hajajiziba uso wake.

Yalikuwa mekundu kama vijinga vya moto!

“Ah, Jadu…!” Yule bwana alibwata kwa mshangao mkubwa kabisa. Jadu hakujibu. Alibaki akiwa amesimama huku amejikinga uso wake kwa kiganja chake.

“Pole sana…pole sana ndugu yangu…lah, ama hakika mungu mkubwa, umeokokaje huko wewe? Na vipi wenzio, nao wamepona…?” Yule mtu alimuuliza kwa wahka mkubwa. Jadu hakumjibu, ingawa sasa alikuwa ameacha kujiziba uso baada ya yule mtu kuacha kummulika kwa tochi yake. Jamaa akapigwa na butwaa.

“We’ Jadu…! Vipi mbona hunijibu? Hebu…twende huku pwani basi, wanakijiji wakuone…utuelezee yaliyokukuteni.”

Kimya.

Jamaa akahisi kuwa Jadu bado alikuwa amechanganyikiwa baada ya kupata ile ajali ya kuzama baharini. Aliamua kumshika mkono ili amuongoze kule walipokuwa wanakijiji wenzao, lakini Jadu alikwepesha mkono wake.

“Usiwe na wasi Jadu…twende kule kwa wenzetu…” Mwanakijiji yule alimuambia huku akinyoosha mkono wake kumshika bega.

La Haula!

Alipougusa tu mwili wa Jadu alipigwa na kitu kama shoti kubwa ya umeme, naye akapiga yowe la woga na maumivu huku akisukumwa nyuma kwa nguvu.

Jamaa aliinua uso wake kumtazama Jadu kwa mshangao huku akimmulika tena usoni kwa tochi yake. Akayaona tena yale macho mekundu yanayowaka kama vijinga vya moto.

Ni Jadu huyu au mauzauza? Alijiuliza, woga mzito ukimgubika.

“Ja…Jadu…?”

Jadu hakumjibu kitu. Badala yake lile wazo lililokuwa kichwani mwake hapo awali lilijirudia tena kichwani mwake. Nahitaji nguo…nataka kula…

Yule mwanakijiji akaanza kurudi nyuma kwa hofu huku akimtazama yule Jadu ambaye si Jadu kwa woga mkubwa.

Hapana…huyu si Jadu kabisa! Labda kakumbwa na kitu huko baharini… Yule bwana aliwaza, na hapo aligeukia kule baharini na kuanza kuwapigia mayowe wale wanakijiji waliokuwa kule pwani. Wanakijiji wenzake walimsikia nao wakaanza kumpigia kelele kuuliza kulikoni.

“Jadu huyu hukuuu! Njooniiiii! Njoooniiii…Jamaniii!” Alipiga kelele, na kugeuka kuona iwapo Jadu atamsemesha kitu, na mdomo ukamuanguka kwa mshangao mzito.

Jadu Mfaume hakuwepo!

Jamaa alichaganyikiwa vibaya sana. Aliangaza huku na huko, akitupa mwanga wa tochi yake kila upande.

“Jadu…we” Jadu…?” Aliita kwa mshangao mzito, lakini Jadu hakuwepo kabisa eneo lile.

Baadhi ya wanakijiji waliokuwa kule ufukweni walikuja mbio pale alipokuwapo, na kumkuta akihaha na tochi yake huku akiita jina la Jadu kama aliyepagawa.

Walimshangaa pasina mfano…

* * *

Kule barabara ya Pugu-Kazimzumbwi, Chambuso Mwagala bado alikuwa amepoteza fahamu na akina Esmund walikuwa wameshakidhi haja zao kwa yule binti waliyembaka kwa zamu.

“Mmefanya kosa kubwa! Sio nyieee…sio nyie! Mtajuta! Mtajuta…mtajuta wanaadamu!” Sauti ya kutisha ilitoka kinywani kwa yule binti. Safari hii, baada ya kuwa wameshamaliza haja zao, Uwesu na Esmund waliisikia barabara sauti ile ya ghadhabu masikioni mwao, na wakagundua kuwa ilikuwa ni sauti tofauti kabisa na ile ya yule binti. Walitazamana, nyuso zao zikidhihirisha hofu kubwa.

“Mnh! Hebu twenzetu yakhe…!” Uwesu alisema huku akimtazama yule binti aliyekuwa akijizoa zoa huku akilia kwa uchungu wa kupokonywa usichana wake kinyama namna ile, na pia kwa maumivu aliyoyahisi mwilini mwake. Esmund alimtupia jicho Chambuso aliyekuwa amelala bila fahamu hatua chache kutoka pale walipokuwapo, na kumtazama Uwesu, kisha akarudisha tena jicho lake kwa Chambuso.

Kwa mara ya kwanza tangu amalize udhalimu wake, Uwesu alimtupia jicho Chambuso, akifuata uelekeo wa jicho la Esmund, na ndipo alipojua kuwa ametenda kosa kubwa sana kumpiga Chambuso kwa jiwe nama ile. Moyo ulimuingia woga mpya.

“Kafa?” Esmund alimuuliza swahiba wake katika maasi, na Uwesu alimeza funda kubwa la mate kisha akabetua mabega yake. Esmund alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu, kisha akamuuliza.

“Sasa…?”

Uwesu hakumjibu. Alimuendea Chambuso na kumsikiliza mapigo yake ya moyo, na kugundua kuwa bado moyo wake ulikuwa unadunda, ingawa kwa mbali. Alimuita Esmund, na pamoja walimbeba rafiki yao waliyemsaliti na kumuingiza ndani ya gari. Esmund alikaa na Chambuso kwenye kiti cha nyuma, wakati Uwesu aliingia nyuma ya usukani tayari kwa ajili ya kuanza safari ya kuelekea jijini Dar.

Tayari alishamtoa kabisa yule binti akilini mwake, na sasa alikuwa akimfikiria Chambuso na hatma ya safari yao tu. Kule kwenye kiti cha nyuma, Esmund alibaki akiwa ameduwaa kama sanamu. Hakuamini kama wameweza kufanya lile walilolifanya kwa yule rafiki yao, na kwa yule binti pia. Lakini maji ndio yalishamwagika…hayazoleki.

Wakati yule binti naye akisimama kwa taabu na kuanza kujipangusa michanga na majani kutoka mwilini mwake, Uwesu alipiga stati lile gari, akakanyaga klachi na kuweka gia ya kurudi nyuma ili alitoe pale kando ya barabara, na gari likazima. Alirudia tena, hali ikawa ile ile. Alijaribu kama mara tatu zaidi bila mafanikio. Gari liligoma kuwaka kabisa.

“Vipi tena…?” Esmund aliuliza kwa woga kutokea kule nyuma, na Uwesu alijaribu tena kupiga stati huku akimjibu…

* * *

Huba binti Malambi alijitahidi kadiri ya uwezo wake kupambana na wale wabakaji, lakini walikuwa wamemzidi nguvu kwa kila hali. Uchungu mkubwa aliokuwa nao wakati ule ulikuwa ukimjia na kuondoka kutokana na mambo ya ajabu aliyokuwa akiyahisi kichwani mwake.

Unajua unachotakiwa kufanya sasa…!

Sauti moja ilisikika ndani ya kichwa chake, na ilikuwa kama inamuambia yeye. Mara sauti nyingine ikadakia.

Hivi sivyo…! Sivyo ilivyotakiwa iwe. Muda haukuwa muafaka…haikuwa wakati wake. Hatuwezi tena sasa…siwezi!

Kichwa kilikuwa kikimgonga kwa nguvu sana Huba binti Malambi, wakati zile sauti zikizidi kubishana kichwani mwake.

Hakuna jinsi sasa! Hao hao waliofanya kitendo hiki ndio watumike kututoa sasa!

Aaah, hiyo itawezekanaje jamani? Wale sio wazawa…!

Hakuna namna nyingine sasa!

Huba aligumia kwa maumivu huku akitikisa kichwa kwa nguvu na akifinya macho. Zile sauti ndani ya kichwa chake, na yale maumivu mazito ya kichwa, vilikuwa ni zaidi ya ambavyo angeweza kuhimili.

Lakini…lakini si tutakuwa bado hatuja…

Tutakuwa tumekufa! Yaani hapa ni aidha tunatoka sasa hivi, au hatutoki kabisa wazawa! TUNAKUFA, mnanielewa wandugu? Tunakufa! Huyu mwanadamu akifa nasi tunakufa ndani yake!

Huba alilia!

Hah, Mxulu! Sasa tukitoka wakati huu…kabla ya muda…ndio itakuwaje?

Huba aliyumba na kutaka kuanguka, akajishika kwenye mti uliokuwa jirani yake.

Tutaendelea kuishi tu, lakini hatutadumu kwa muda mrefu kama zamani…itabidi tupate bikra mwingine baada ya muda mfupi sana…

Ooh come on, kama si hivyo…?

Kama si hivyo tunakufa tena!

Aaaaaahhh…Mxulu!

Huba alihisi kichefu chefu. Alijipinda akiwa ameushikilia ule mti na kufunua kinywa chake ili atapike, lakini hakuna kilichotoka.

Ndiyo! Itabidi iwe hivyo hivyo…kila itakapofika siku kama hii katika miaka ya kibinadamu…!

Kwikwi zilimbana Huba binti Malambi sasa, na alijihisi akipata taabu kupumua.

Hivi hivi Mxulu…?

Ndiyo wazawa…ndiyo. Kama tunataka kuendelea kuishi, BASI ITABIDI IWE HIVYO KWA SIKU ZOTE ZILIZOBAKIAAAAAAA…..!!

Huba alipiga ukelele wa woga na kihoro huku akianguka chini kando ya ule mti. Zile sauti zilizokuwa zikimzonga akilini mwake zilizidi kumuumiza, kwikwi zikizidi kumbana, pumzi zikimkauka, na akihisi kupoteza fahamu. Roho ilimuuma sana kwa madhila yaliyomkuta usiku ule.

Kwanza yale mambo aliyokuwa akiyakumbuka kama nusu ndoto tu yaliyomtokea kule pangoni, na sasa haya ya kubakwa na wale vijana wachafu…

“Ooh Mungu wangu, kwa nini umeniacha nifikwe na yote haya?” Alibwabwaja kwa uchungu huku akilia. “Nimejitahidi kujiokoa lakini nimeshindwa Huba miye…sasa hata mchumba wangu hatotaka kunioa tena…” Alizidi kuijutia bahati yake mbaya kwa sauti. Alijaribu kujiinua kutoka pale chini, lakini mwili ulimuwia mzito sana. Alibaki akilia pale chini, akilini mwake ile taswira ya jinsi alivyokuwa akibakwa kwa zamu na wale vijana wawili ikijirudia tena na tena.

Uchungu uliomkaba haukuwa na mfano. Moyo ulimuuma kama kidonda. Kichwa kikamgonga, na gadhabu za ajabu zikamtawala. Kisha kiza kikatanda mbele ya macho yake…

Lazima walipe kwa walilolifanya…lazima walipe! Hawastahili kuitwa binadamu hata kidogo! Hawastahili! Hawastahili! HAWASTAHILIIII!

Huba binti Malambi alifumbua macho yake ghafla, kisha akajiinua kwa taabu, maumivu makali yakimtawala sehemu ya uke wake. Alijikamata kwenye ule mti na kubaki akitweta. Alisikia sauti za wale vijana zikitokea sehemu upande wa pili wa ile barabara.

Alianza kujivuta taratibu kuelekea kule zilipokuwa zikitokea zile sauti, huku akiijihisi kama kwamba alikuwa akitembezwa na mtu mwingine, au akitembea kwa kutumia nguvu zisizokuwa zake…

* * *

ITAENDELEA

Utata wa 9/12 Sehemu ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment