Utata wa 9/12 Sehemu ya Pili
KIJASUSI

Ep 02: Utata wa 9/12

SIMULIZI Utata wa 9/12
Utata wa 9/12 Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA: HUSSEIN ISSA TUWA

*********************************************************************************

Simulizi: Utata Wa 9/12

Sehemu ya Pili (2)

“Gari haliwaki bwana! Doh, balaa gani hili sasa…!”

Jibu la Uwesu lilimchanganya sana Esmund. Alifunua kinywa kwa fadhaa, kisha akakifumba pasi kusema neno. Nguvu zilimuisha. Akamgeukia Chambuso aliyejibweteka kama gunia kando yake pale kwenye kiti cha nyuma, na woga mkubwa ukamtawala. Aliweka kiganja cha mkono wake kifuani kwa yule mwenzao na kusikiliza kwa makini. Hakuhisi mapigo ya moyo hata kidogo.

“Mnh, we’ Uwesu we’…una hakika hujamuua huyu wewe?”

“Huyu nani tena na gari haliwaki huku weye?” Uwesu aliuliza kwa sauti iliyokereka, jasho likimvuja na moyo ukimwenda mbio, akihangaika kuliwasha lile gari bila mafanikio.

“Si huyu Chambu bwana…! Mi’ namuona kakauka kabisa huyu!”

“Hebu acha ujuha weye! Huyo mzima bwana. Badala ya kutilia maanani swala la gari kutowaka unaleta woga wa kibwege tu hapa!” Uwesu alimkemea.

“Sasa mtu hapumui hata kidogo! We’ unafikiri ni mchezo! Isije kuwa kafa huyu…? Kama kafa ujue ni mada kesi hii hivyo!” Esmund alimpayukia mwenzake kwa woga, akimaanisha kuwa iwapo yule mwenzao alikuwa amekufa basi itakuwa ni kesi ya mauaji.

“Mada na ubakaji! Usijitie kusahau makosa mengine hapa…na yote hayo na we’ umo!” Uwesu alimjibu kwa jeuri na hasira yule swahiba wake katika maovu huku akizidi kujishughulisha na lile gari akiwa pale nyuma ya usukani.

“Hoooooohhh…!” Esmund aligwaya kwa woga na kukata tamaa.

“Hajafa huyo bwana, si tulimcheki pale nje bwana? Mbona unataka kunichangaya saa hizi lakini weye?” Uwesu alifoka huku akimgeukia Esmund aliyekuwa na Chambuso kule nyuma, na akamuona jinsi alivyokuwa ameishiwa nguvu kabisa kwa woga.

“Sasa nini weye lakini, enh? Mbona unaleta ulofa sasa?” Alimkemea huku akimsukuma kichwa chake kwa kidole chake cha shahada.

“Oooooh…!” Esmund alizidi kulalama kwa kukata tamaa.

“Hebu acha ukhanithi weye, ama! Tunahitaji kufikiri namna ya kuondoka eneo hili na mwenzetu…hebu mtikise kwanza aamke hapo!” Uwesu alimkemea tena. Esmund alimgeukia tena Chambuso, na alipomuona jinsi alivyojibweteka kama mtu aliyekufa, akageuza uso wake na kuzidi kugumia kwa kukata tamaa.

“Ooooh-Hooooooo…!”

“Hebu niondolee kelele mimi huko weye, ebbo! Ulivyokuwa unananihii kule mbona hukuogopa? Hebu mtikise huko!” Uwesu alizidi kumkemea swahiba wake, na hapo Esmund aliachia ukelele mkubwa sana, kama kwamba hakusikia yale maneno makali ya mshirika wake, na kubaki akiendelea kupiga kelele kubwa huku akiwa ametumbua macho kuelekea kwenye uwazi wa kilipokuwa kioo cha mbele cha gari, ambako Uwesu alikuwa amepageuzia mgongo wake.

“ETIIII…!?” Uwesu alimaka kwa kihoro, akiona uelekeo wa macho ya Esmund, naye akajikurupusha na kugeukia kule alipokuwa akitazama mwenzake.

Hamadi!

Macho yalimtoka pima Uwesu, kinywa kikamuanguka pasina habari.

Taa za mbele za gari ambazo zilizima wakati lile gari ilipogoma kuwaka, sasa zilikuwa zikiwaka. Na katika mwanga ule walimuona yule binti waliyetoka kumbaka muda si mrefu uliopita, akilisogelea taratibu lile gari walilokuwamo.

Binti yule alikuwa akiliendea lile gari kwa hatua moja baada ya nyingine huku mkono wake mmoja akiwa amejishika chini ya tumbo lake, na ule mwingine.akiwa ameutanguliza mbele yake. Na hata pale alipokuwa akimkodolea macho binti yule kwa hamaniko lisilo kifani, Uwesu bin Shaame alielewa sababu ya rafiki yake kuachia yowe kubwa namna ile. Koo lilimkauka na alihisi kitu kama jongoo mwenye miguu ya baridi sana akimtambaa kwenye uti wake wa mgongo, na mwili ukamsisimka.

Mbele ya ule mwanga wa taa za gari, yule binti alionekana kuwa na vidole virefu kuliko kawaida ya binadamu, na macho yake yalikuwa yakitoa mng”aro mithili ya makaa ya moto. Na hata pale alipokuwa akiwasogelea, vijana wale walimshuhudia binti yule akionekama na kupotea kwa namna ya kutisha kweli kweli. Yaani sekunde moja wanamuona, sekunde ya pili haonekani, vinabakia vile vijinga viwili vya moto ambavyo ndio yale macho yake!

Hapo Uwesu naye aliishiwa ujasiri.

“WAAAAARGHHH!” Yowe kubwa lilimtoka huku akirukia kule nyuma alipokuwa Esmund, ambaye ndio aliongeza mayowe maradufu, na wote wakabaki wakiwa wamejikunyata kwenye kiti cha nyuma ndani ya ile gari wakimtazama yule binti aliyewabadilikia kwa namna ya ajabu akiisogelea ile gari. Sasa wote wawili walikuwa wakitetemeka vibaya sana.

“Oooh, Mu-mu-mungu wa-wa-nng-u! Huyu vipi te-te-te-tena Uwesu? Mbon-na vi-vi-vil-le?” Esmund alibwabwaja kwa kitetemeshi kikubwa huku akimng”ang”ania Uwesu mkono na akihisi kutaka kulimwaga kojo kwa kwa mara ya pili usiku ule.

Uwesu wala hakuweza kujibu kitu, badala yake alibaki akitetemeka huku akitoa sauti za woga uliokithiri.

Muda huo huo yule binti aliachia yowe kali sana la kuogopesha huku akiinua juu mikono yake na kuchanua vidole vyake vilivyorefuka, akiinua uso wake juu angani ilhali akiwa ametanua miguu yake. Misuli ya mwili wake ulioonekana mbichi muda mchache tu uliopita, sasa ilikuwa imechomoza na kumkakamaa vibaya sana.

Sasa binti alitisha kweli kweli.

“AAAAAH…Uwesu tumebaka jini…!” Esmund alibwabwaja kwa woga.

“HAH..!” Uwesu naye alianza kuropoka kitu, lakini hapo hapo walimuona yule binti akianguka chini kwa kishindo, kisha akafurukuta pale chini kwa muda kabla ya kutulia pale chini mbele ya ile gari, na zile taa za gari nazo zikififia na kutoa mwanga hafifu sana.

Kimya kilitanda ndani ya gari, kisha Esmund alikurupuka na kutoka mbio nje ya gari ile huku akipiga kelele kama mwehu akimuita mama yake mzazi, kuifuata ile barabara ya Pugu – Kazimzumbwi.

“Esmuuuund…!” Uwesu aliita kwa kihoro baada ya kuona mwenzake ameamua kutimua mbio kuelekea Dar kwa miguu, naye akijaribu kujikurupusha kutoka kwenye ile gari.

Kwa mara ya kwanza, Chambuso Mwagala alijitikisa kidogo akiwa mle ndani ya gari, akisikia sauti ndogo ikimnong”oneza sikioni, ikiita jina la Esmund…

Jadu Mfaume alikuwa akiwatazama wale wanakijiji walioitwa na yule mwanakijiji aliyekuwa akimsemesha muda mfupi uliopita, na alishangaa kuona kuwa wanakijiji wale walikuwa hawamuoni wakati yeye alikuwa amesimama pale pale akiwatazama.

Hawa watu hawanioni!

Alitaka kuwasemesha, lakini mara akahisi kinywa chake kimekuwa kizito sana. Hakuweza kuongea neno lolote. Lakini hata mimi mwenyewe sikutaka wanione…

Alitaka amsogelee mmoja wao na amguse bega aone itakuwaje, lakini mara na miguu yake ikawa kama iliyoshindiliwa zege pale alipokuwa amesimama.

Alibaki akiwatazama wale wanakijiji wakimhoji kwa jazba yule mtu juu ya Jadu Mfaume…juu ya yeye. Yule mtu alikuwa amehamanika vibaya sana.

“Jamani! Mi’ nimemuona hivi hivi…kwa macho yangu! Na…na…nimemgusa…ah! Nilivyomgus…oh!” Yule mtu alikuwa akijitetea, na kuishia katikati ya kauli.

“Nini? Ulivyomgusa halafu nini…?” Mmoja wa waliokusanyika pale alimuuliza kwa kiherehere, huku akionesha wazi kuwa alikuwa hamuamini hata kidogo. Ghafla wazo lilipita kichwani kwa Jadu Mfaume wakati akimtazama yule mtu aliyekuwa akijitahidi kuwathibitishia wenzake kuwa ni kweli amemuona Jadu Mfaume mvuvi.

Uzegeni. Jina lake Uzegeni. Anavuta bangi. Huyu mtu huwa anvuta bangi.

Ulikuwa ni ufahamu wa kweli uliopita kichwani mwake wakati akimtazama yule mtu, na ghafla akawa anajua kila kitu kuhusu yule mtu. Tangu jina lake, wazazi wake, na sehemu ambapo nyumba ya mama yake, ambako ndimo alikuwa akiishi, mpaka umri wake.

“We’ Uzegeni we’, yaani umemgusa kabisa Jadu hapa! Halafu ikawaje? Mbona ameduwaa tena…?” Yule mwanakijiji alizidi kumhoji kwa udaku yule mtu, huku akionesha wazi kuwa alikuwa na hamu ya kudhihirisha kuwa yule mtu aliyemwita kwa jina la Uzegeni alikuwa akisema uongo.

Uzegeni aliwatazama wale wanakijiji wenzake waliokuwa wakimkodolea macho ya kuuliza kama kwamba ndio anawaona kwa mara ya kwanza, kisha akajibu kwa sauti iliyojaa kitetemeshi kikubwa kabisa.

“Ni…nimemgusa, na mm…mwili wake uk…kanipiga shoti ya umeme!”

Kilichofuatia ni mgongano wa maneno kutoka kwa wale wanakijiji waliomzunguka, kila mmoja akitoa wazo lake bila kusubiri mwingine amalize.

“Mweee!” Mama mmoja alimaka.

“Haaah!” Mtu mwingine aliropoka huku akijishika kichwa kwa mshangao.

“Ee Uzegeni wee! Haya tangu lini mtu akatoa shoti ya umeme!?” Mama mwingine alimsogezea uso Uzegeni huku akiwa amemkaushia macho na amemshikia kiuno kwa pozi kali la msuto.

“Mmnh!(msonyo mkali) Jongo hili…! Tena jongo kweli kweli! Lishavuta mibangi yake “uko sa” linataka kutuchanganya “apa!” Jamaa mwingine alisema kwa hasira huku akitupa mikono yake hewani huku akigeuka na kuanza kurejea kule ufukweni ambako msako wa miili ya akina Jadu Mfaume mvuvi ulikuwa unaendelea.

“Ni kweli jamani! Jadu alikuwa amesimama hapa hapa mbele yangu…na nimemgusa…” Uzegeni alizidi kujitetea, lakini kabla hajaendelea na utetezi wake mwanakijiji mwingine akadakia.

“Halafu ukapigwa shoti ya umeme!”

Ilikuwa ni kauli ya kejeli iliyomaanisha msemaji alikuwa haamini kabisa juu ya jambo lile, kama jinsi ambavyo wewe utakavyoshindwa kuamini pale utakapoambiwa kuwa malkia wa Uingereza ni binamu yako wa karibu sana. Uzegeni alimtazama kwa macho yaliyojaa uwazi na imani juu ya kila neno alilotamka.

“Ndiyo, nikapigwa na shoti kubwa ya umeme!”

Wote walimtazama kama kwamba alikuwa amepatwa wazimu, kisha mmoja baada ya mwingine wakaanza kugeuka kurudi kule walipokuwa hapo awali, wakimuacha Uzegeni akiwa amesimama peke yake akitazama vidole vya mkono wake wa kulia kwa butwaa.

“Mibangi imemchanganya huyu!” Jadu Mfaume alimsikia mmoja wa wale wanakijiji akisema kwa hasira huku akiondoka, na akamtazama tena yule mtu aliyebaki akivikodolea macho vidole vyake kwa butwaa kama kwamba ndio kwanza alikuwa anagundua kwamba alikuwa na vidole mkononi mwake. Alikuwa amesikia kila kitu kilichosemwa pale, na hakuna hata kimoja kilichoonekana kumshitua zaidi Jadu Mfaume mpya kuliko kule kushindwa kwake kuwaongelesha wale watu na kunyanyua miguu yake pale alipotaka kuwasogelea.

Uzegeni alikuwa amesimama kama bwege kiasi cha hatua mbili tu kutoka pale alipokuwapo, akiumulika mkono wake wa kulia kwa tochi aliyoishika kwa mkono wake wa kushoto.

Na mara Jadu akahisi miguu yake ikiachiwa na kumuwia myepesi, na akajihisi anaweza kuongea tena. Lakini sasa wale wanakijiji aliotaka kuwasemesha hapo awali walikuwa wameshaondoka, wakimuacha Uzegeni pale pale walipomkuta.

Jadu aligeuka na kuondoka taratibu eneo lile, naye akimuacha Uzegeni mvuta bangi, ambaye kwa wakati ule akili yake haikuwa imechafuliwa na bangi hata kidogo, akikodolea macho malengelenge yaliyotokeza kwenye vidole vyake vilivyougusa mwili wa yule mtu aliyeamini kuwa ni Jadu Mfaume mvuvi.

Na wakati akiyakodolea macho kwa mshangao mkubwa yale malengelenge yaliyotokeza vidoleni mwake, Uzegeni alihisi koo likimkauka, na alijikuta akihitaji sana kuliko wakati mwingine wowote maishani mwake, kupata japo pafu mbili za bangi, vinginevyo hakika angepata wazimu.

Jadu Mfaume “mpya” alielekea usawa wa mahala ambako alihisi kuwa kijiji kile cha wavuvi kilikuwako. Akilini mwake alikuwa akisikia sauti za watu wakiongea kwa huzuni juu ya maendeleo ya kukatisha tamaa ya kuwatafuta wale wavuvi watatu waliopotelea baharini, na pia aliweza kusikia vilio vya akina mama na watoto kutokea kule pwani ambako msako ulikuwa ukiendelea, na wakati huo huo aliweza kusikia vilio vilivyokuwa vikitokea kule kijijini. Na alivisikia vilio hivi akiwa mbali sana na wale waliaji, kama kwamba waliaji walikuwa ndani ya kichwa chake. Na mmoja wa waliaji wale alikuwa akilia huku akilitaja jina lake, kwamba yeye ni mume wake…

Jadu Mfaume huyu mpya alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Yaani aliweza kuvuta hisia na kupata mawimbi ya vitu vilivyokuwa vikipita akilini mwa wanadamu. Jadu wanayemlilia hao wanadamu hakuwa na uwezo huo hata kidogo. Huu ni uwezo ambao hata huko anakotokea Jadu huyu mpya, ni viumbe wachache kutoka huko walikuwa nao.

Lakini kuanzia sasa yeye ni Jadu Mfaume mwanadamu, na ataendelea kuwa hivyo mpaka hapo atakapomaliza kazi iliyomleta kwenye hii sayari iitwayo dunia.

Sasa Jadu Mfaume mpya alibadili uelekeo na kuanza kufuata kule ilipokuwa ikitokea ile sauti ya mke wa Jadu Mfaume mvuvi, mwendo wake ukiwa wa taratibu sana, na jukumu lililomleta sehemu hii ya ulimwengu likiwa thabiti kabisa kichwani mwake.


Esmund alikuwa akitimua mbio huku akiwa amejikunja kutokea kiunoni, kiwiliwili chake kikiwa kimelalia mbele, huku akipunga mikono yake mithili ya mapangaboi, akipepesuka na akijitahidi asiangukie uso pale barabarani, akielekea kule kule ambako Huba binti Malambi alikuwa amejibwaga kama gogo.

Nyuma yake, Uwesu alijrusha nje ya gari ile huku akimuita rafikiye kwa sauti iliyojaa woga mkubwa, na alipojirusha namna ile, alimkumba Chambuso Mwagala aliyekuwa kwenye kiti cha nyuma ndani ya ile gari na kumdondosha chini ndani ya ile gari.

Akiwa nje ya gari Uwesu aliinuka na kuanza kumkimbilia Esmund.

“Eeeesssmuuunnnnddd…! Ngojaaaaa…” Aliita huku akimfuata mbio yule mwenzake, lakini jambo aliloliona mbele yake lilimfanya anyamaze ghafla na huku macho yakimtumbuka kwa woga usio kifani…

Kule ndani ya gari Chambuso Mwagala alifumbua macho ghafla na kutikisa kichwa.

“Esmund…?” Alitamka lile jina alilokuwa akilisikia kwa mbali likitamkwa kichwani mwake wakati fahamu zilipokuwa zikimrudia. Alihisi maumivu makali kisogoni kwake, na akapeleka mkono wake taratibu kujipapasa kisogoni huku akiguna kwa maumivu, na hapo hapo akishangaa imekuwaje hata akawa ndani ya gari. Mkono wake ukamjulisha kuwa alikuwa na uvimbe mkubwa kisogoni, na alipougusa uvimbe ule, maumivu makali yalimtambaa kichwa chote na kupeleka mwale mkali wa maumivu mpaka ndani kabisa ya moyo wake.

Aliguna tena kwa maumivu, akili yake ikiendelea kuamka taratibu sana.

“Oooh…ni…nini kimet…tokea…?” Alibwabwaja peke yake kwa sauti iliyokwaruza, huku akijiinua kutoka kwenye sakafu ya gari ile. Kwa mbali alirejewa na kumbukumbu ya makabiliano baina yake na Esmund aliyekuwa akijaribu kumbaka yule binti asiye nguo, na hapo alisikia yowe kubwa sana la kuogofya kutokea nje ya ile gari…

Esmund alikuwa akikimbia kwa nguvu huku akipiga kelele, mbele yake alimuona yule binti waliyembaka muda mfupi uliopita akiwa amelala chali kati kati ya barabara, akiwa aidha amekufa au hana fahamu. Alikuwa ameshainua mguu kuuruka mwili wa yule binti ili azidi kutokomea kwa kasi sana kutoka eneo lile, wakati kwa kihoro kikubwa sana alipoona yule binti akiinuka ghafla na kutoka pale alipokuwa amelala, na kuketi katikati ya ile barabara na kumgeuzia uso wake huku akimtazama kwa macho mekundu yaliyong”aa kama makaa ya moto, na ndipo hapo alipoachia lile yowe kubwa lililomshitua Chambuso kule ndani ya gari , na kumjaza woga Uwesu aliyekuwa nje ya gari akimkimbilia Esmund.

Uwesu aliona kile kitendo naye akaachia ukelele wa woga huku akijilazimisha kusimama na kubaki akitetemeka bila maamuzi.

Esmund naye alikuwa akipiga kelele huku akijilazimisha kusimama, lakini kasi aliyokuwa ametoka nayo ilikuwa kubwa kiasi kwamba alishindwa kusimama. Alimpamia kwa nguvu yule binti na wote wawili wakabiringika vibaya sana pale chini.

Esmund aliinuka huku akilia kwa woga, tayari akiwa amechubuka sehemu kadhaa za mwili wake, na kuanza kukimbia tena, lakini alijikuta akiwa amekabiliana uso kwa uso na yule binti, aliyekuwa amemsimamia mbele yake akimtazama kwa macho mekundu yaliyojaa ghadhabu kali huku akiunguruma kama simba, mikono yake akiwa ameitawanya kila upande, vidole vyake virefu vikiwa vimechanuliwa.

Macho yalimtoka pima Esmund, na akahisi miguu ikimuisha nguvu na matumbo yakimcheza. Uwesu alibaki akitazama tukio lile la kutisha wakati sauti nzito ya kuogofya ikitoka kinywani kwa yule binti.

“Mmefanya kosa kubwa sana wanadamu! Mmeingilia kazi isiyo yenu…kabla ya wakati wake…” Yule binti alisema kwa sauti isiyo yake huku akimtazama Esmund moja kwa moja usoni.

“Aaaarghh…Mamaaanguu wee!” Esmund alilia kwa woga huku akigeuka na kutimua mbio kurudi kule alipotokea, na hapo jambo la ajabu lilitokea.

Mkono wa yule binti ulichomoka haraka na kumdaka shati. Esmund aliachia yowe kubwa wakati akivutwa nyuma kwa nguvu na yule binti, na hata pale alipokuwa akipiga ukelele ule, alijikuta akigeuzwa na kuchapwa kofi kali sana la uso lililomtupa nyuma kwa msukumo mkubwa kabisa. Alijibwaga chini na kupigiza kichwa chake kwenye ile lami ngumu ya pale barabarani, ukelele wake wa woga ukibadilika na kuwa wa maumivu.

Uwesu aliachia mguno wa woga aliposhuhudia kitendo alichofanyiwa mwenzake na yule binti, na hapo akaona hana wa kumsubiri. Aligeuka ana kutimua mbio kurudi kule alipotokea. Binti aliunguruma kwa ghadhabu ya kutisha na kuruka kwa hatua tatu kubwa na kumfikia Uwesu pale alipokuwapo. Bila ya kujitambua Uwesu alimrushia ngumi nzito yule binti huku akimpigia kelele.

“Toka hukooo…!”

Binti aliupiga kwa nguvu mkono wa Uwesu kabla ile ngumi haijamfikia, na Uwesu alilia wakati maumivu makali yakimtambaa mkononi mwake, na hapo hapo binti alimshushia kwa nguvu mkono wake uliochanua vidole vyake virefu kuelekea usoni kwa Uwesu. Uwesu aliruka nyuma huku kilio cha shaka kikimtoka, na lile pigo likaukosa uso wake na kumpitia kifuani. Vidole virefu vya yule binti vilimchimba vibaya sana kifuani. Maumivu makali yaliukata mwili wake huku akishuhudia damu ikiruka kwa wingi kutoka mwilini mwake na kumtapakaa usoni yule binti aliyekenua meno kwa ghadhabu.

Uwesu alilia huku akiinamisha uso wake kujitazama kifuani, na akaingiwa ubaridi mkubwa alishuhudia michirizi minne ikiwa imemchimba vibaya sana kifuani, nyama zikining’inia kutoka kwenye majeraha yale marefu, damu nyingi ikimtambaa kutokea upande wa kulia wa kifua chake hadi chini ya tumbo lake.

Aliinua uso wake kumtazama yule binti kwa mshangao, na wakati huo huo akaona vidole virefu vya yule binti vikimshukia tena usoni, na akaachia yowe kubwa huku akivitazama vile vidole vikiushukia uso wake na akijaribu kuinua mikono yake kuukinga uso wake, lakini mikono ikawa kama iliyouhama mwili wake, kwani haikuinuka hata kidogo na badala yake ilibaki ikining”inia kila uande wa mwili wake.

“HYEEEEEKHHH…!”

Ukelele mwingine mkubwa ulisikika kutokea kule kwenye gari, na Huba binti Malambi akageukia kule ilipotokea ile sauti, mkono wake wa kulia ukabaki ukielea hewani usawa wa uso wa Uwesu ilhali kwa mkono wake wa kushoto akiwa amemkamata shati Uwesu.

Chambuso Mwagala alikuwa ametoka nje ya ile gari katika muda ule ambapo Huba binti Malambi aliyebadilika alipokuwa anataka kushusha pigo lake la pili kwa Uwesu, damu iliyomtapakaa usoni kwake ikionekana wazi wazi kutokana na mwanga hafifu wa taa za lile gari. Na ndipo alipoachia yowe lile kubwa la woga, yowe ambalo lilimuokoa Uwesu kutokana na kifo kibaya, angalau kwa wakati ule.

HMMMMMNNNNNHHHH…

Uwesu alikuwa akilia kwa fadhaa huku akiwa ameuma mdomo wake kwa woga, naye akimtazama Chambuso, nguvu za kujinasua kutoka kwenye himaya madhubuti ya yule binti ambaye sasa ilikuwa imemdhihirikia kabisa kuwa alikuwa jini, zilikuwa zimemhama kabisa. Miguu ilikuwa imemlegea na alibaki akining”inia kwenye mkono wa yule binti aliyepata nguvu za ajabu.

Huku nyuma Esmund alijiinua kwa taabu kutoka pale chini alipotupwa na pigo lile la kuumiza. Alihisi kizunguzungu na aliiona ile lami ikicheza cheza kama kwamba ilikuwa akielea juu ya maji. Alisimamia magoti na mikono yake pale barabarani kama jinsi ambavyo mbwa huwa wanasimama. Alihisi shavu likimchonyota pale ambapo alipigwa na yule binti, na akajipapasa shavuni kwa mkono wake na kushangaa kuhisisi unyevu na maumivu makali. Alipokitazama kiganja chake na kuona kikiwa kimetapakaa damu, alipiga ukelele wa mshituko na kukaa chini huku akikitazama kwa kihoro kiganja chake kilichotapakaa damu na akilia kama bwege.

Uwesu alisikia mayowe mapya ya Esmund na akazidi kuchanganyikiwa. Alirudisha macho yake yaliyokata tamaa kwa yule binti dahifu waliyetoka kumbaka muda mfupi tu uliopita, na sasa alikuwa na nguvu za ajabu, ambaye bado alikuwa akimshangaa Chambuso kama kwamba alikuwa ni kiumbe wa ajabu ambaye ndio anamuona kwa mara ya kwanza, huku bado akiwa amemning”iniza hewani kwa mkono wake mmoja tu, ncha za vidole vyake vilivyokuwa ndani ya viatu vyake zikiigusa kidogo tu ile lami waliyokuwa wamesimama juu yake.

Chambuso alikuwa akishuhudia tukio lile huku macho yakiwa yamemtumbuka na mdomo umem-mwagika kwa mshangao na woga mkubwa. Akili yake ilishindwa kabisa kuelewa au kuamini kile ambacho macho yake yalikuwa yakikiona. Mtoto wa kike akiwa uchi wa mnyama, ametapakaa damu usoni akiwa amemninginiza rafiki yake hewani kwa mkono mmoja, na kwa mkono mwingine akijiandaa kumshambulia kwa vidole virefu kuliko kawaida vilivyokuwa vikichuruzika damu…hakika ilikuwa ni taswira ya kutisha sana.

Na Chambuso alikuwa ametishika vibaya sana, muda wote alikuwa akipiga kelele huku macho yake yakishindwa kabisa kujinasua kutoka kwenye taswira ile ya kuogofya.

Huba binti Malambi alikuwa akimtazama Chambuso kwa macho yake makubwa yaliyoiva kwa ghadhabu, ngurumo za kutisha zikimtoka kooni mwake. Alimgeukia Chambuso aliyekuwa akipiga kelele za woga, na kufinya macho yake kwa namna ya kuongeza umakini, kisha akalaza kichwa chake upande mmoja huku bado akimtazama Chambuso kwa makini, kama kwamba alikuwa akijaribu kukumbuka ni wapi alipata kumuona yule kijana. Kwa muda alikuwa amemsahau Uwesu, na ndipo Uwesu alipozinduka na kujisukuma mbele kwa nguvu, akimkumba yule binti kwa nguvu zake zote zilizobakia huku akipiga kelele. Shati lake likachanika, kipande kikibakia mkononi mwa yule binti, naye akaanguka chini kwa kishindo.

Huba alitoa sauti ya ghadhabu na kumgeukia Uwesu huku akiwa ametanua mikono yake na amechanua vodole vyake. Nyuma yake, Esmund alikurupuka kutoka pale chini na kuanza kutimua mbio huku akilia kwa woga na fadhaa…

Uwesu alimrukia kwa nguvu miguuni yule binti kwa lengo la kumuangusha kisha akimbie, lakini kwa wepesi wa ajabu Huba binti Malambi aliruka juu huku akitanua miguu yake na Uwesu akaambulia patupu na kuangukia tumbo pale chini, akijichubua vibaya kwenye lami lile eneo ambalo tayari lilikuwa limejeruhiwa vibaya kwa kucha na vidole vigumu vya yule binti. Yowe kubwa la uchungu lilimtoka na alijigeuza akilalia mgongo na kuanza kujiinua kutoka pale chini wakati Huba alipomshukia na kumtandika kofi kali kwa mgongo wa kiganja chake. Uwesu alitupwa pembeni kama mzoga kwa msukumo wa kofi lile, meno na damu vikiruka kutoka kinywani mwake.

Chambuso alipiga ukelele wa woga aliposhuhudia tukio lile na kujisogeza hadi kando ya tairi la mbele la ile gari, miguu ikimuisha nguvu na kupiga magoti kando ya tairi la gari ile.

Huba binti Malambi alitoa sauti ya kutisha, na wakati Uwesu akitupwa pembeni na lile pigo alilomtupia, yeye aliruka mbele kwa kasi na kumuwahi Esmund aliyekuwa akikimbia huku akiwa amejishika shavu lake lililocharangwa kwa vidole virefu vya yule binti. Huba alimrukia kama jinsi chui anavyorukia windo, akiwa ametanguliza mikono yake mbele na vidole vyake akiwa amevichanua, muungurumo wa ghadhabu ukimtoka kooni mwake.

Akiwa amejikunyata kando ya tairi la gari lao, Chambuso Mwagala alimshuhudia Huba binti Malambi akimuangukia Esmund mgongoni na kumng’ang’ania kama luba kwa mikono yake yenye nguvu. Esmund alipiga ukelele wa woga na kupiga mwereka mzito huku Huba akiwa mgongoni mwake. Waligaragazana pale kwenye lami, Esmund akipiga mayowe ya woga uliokithiri, huku Huba akiunguruma kwa ghadhabu.

Walibiringishana kwa muda pale chini, na hatimaye Huba binti Malambi akamkalia tumboni Esmund aliyebaki akiwa amelala chali kati kati ya ile barabara, na hapo Chambuso alimshuhudia yule binti akishusha mapigo mazito mwilini mwa Esmund kwa mikono yake yote miwili. Pigo moja la nguvu baada ya jingine. Na kwa kila pigo, alisikia kilio cha uchungu kutoka kwa Esmund aliyekuwa akitupa tupa miguu na mikono yake huku na huko. Na kila mkono wa yule binti ulipoinuliwa juu kukusanya nguvu ya pigo jingine, Chambuso aliona mchirizi wa damu ukichuruzika kutoka kwenye ncha za vidole vya yule binti wa ajabu…

Jadu Mfaume alianza kuziona nyumba za kijiji kwa mbali, ilhali akilini mwake akiendelea kusikia zile sauti za akina mama waliokuwa wakilia, hususan yule aliyekuwa akimlilia Jadu Mfaume mvuvi. Na ni hii ndiyo sauti aliyokuwa akiifuata muda wote.

Hatimaye aliingia kijijini taratibu na bila woga. Kiza kilikuwa kimetanda pale kijijini, na ingawa njiani alikuwa akikutana na watu mara moja-moja, yeye hakujishughulisha nao na wala hakujishughulisha kujificha, kwani alijua kuwa walikuwa hawamuoni…kwa sababu hakutaka wamuone.

Kutokea kulia kwake alisikia vilio vya sauti na maombolezo, sasa zikiwa sawia na ile ya mke wa Jadu Mfaume mvuvi. Jadu Mfaume mpya alisimama na kusikiliza kwa muda, na kubaini kuwa sauti iliyokuwa ikilia kutokea nyumba iliyokuwa karibu naye haikuwa ile ya mke wa Jadu Mfaume mvuvi. Ilikuwa ni ya mwanamke anayemlilia mumewe aliyezama baharini, lakini si Jadu. Ni mvuvi mwingine miongoni mwa wale waliokuwa wakitafutwa. Sauti ya mwanamke aliyokuwa akiifuata ilikuwa ikitokea upande mwingine wa kijiji kile. Aliendelea na safari yake taratibu, akiifuata sauti ya mke wa Jadu Mfaume mvuvi.

Nahitaji nguo…chakula…

Sasa sauti ya mke wa Jadu Mfaume mvuvi ilikuwa ikisikika kwa ukaribu zaidi, kiasi kwamba alikuwa akiisikia akilini kwake na masikioni mwake pia.

Ipo karibu sasa…nyumba iko karibu…nimeshafika…

Alipita upenuni mwa nyumba moja ya matope iliyoezekwa kwa makuti kama nyumba nyingine za pale kijijini, na kutokea kwenye eneo lililokuwa wazi, likiwa na majaluba ya mpunga mdogo. Upande wa pili wa majaluba yale aliweza kuona nyumba kadhaa zikiwa zimejikusanya pamoja. Taa za vibatari zilikuwa zikiwaka kutokea kwenye baadhi ya nyumba zile, ambako huko ndiko vilio vya mke wa Jadu Mfaume mvuvi vilikuwa vikisikika wazi wazi. Nje ya nyumba zile kulikuwa kuna makundi madogo madogo ya watu waliojikusanya, wakiongelea kwa jazba juu ya yale yaliyosemekana kuwa yamewakuta wale wavuvi watatu.

Jadu Mfaume mpya alihisi akiingiwa wepesi wa mwili, na akaongeza kasi. Aliingia kwenye moja ya yale majaluba, akihisi ulaini wa matope kwenye nyayo zake na maji yaliyokuwa kwenye jaluba lile aliloingia yakimfikia kwenye kongo za miguu yake. Aliielekea nyumba alimokuwamo mke wa Jadu Mfaume mvuvi. Sasa alisikia vilio vikirindima kutokea kwenye nyumba nyingine jirani na ile aliyokuwa akiielekea.

Msiba. Kijiji kilikuwa kimekumbwa na msiba mkubwa…

Alisita. Alisimama kizani na kutazama kule kwenye nyumba ilimokuwa ikitokea sauti ya mke wa Jadu Mfaume mvuvi. Kundi dogo la wanakijiji lilikuwa limejikusanya baina ya nyumba zile mbili zilizokumbwa na msiba. Muda huo mbwa alianza kubweka kwa nguvu. Alikuwa akibweka huku akikimbilia pale ambapo Jadu Mfaume mpya alikuwa amesimama. Jadu alimtazma yule mbwa akimjia kwa kasi na jazba, naye akatulia kimya, akitazama kule kwenye ile nyumba.

Mbwa alimfikia hadi miguuni kwake kwa makeke na kuanza kubweka kwa fujo huku akitifua-tifua michanga karibu na miguu ya Jadu Mfaume, ambaye alikuwa ametulia tu akimtazama.

“Heh! Huyu mbwa wenu vipi? Ameona nini kule…?” Alisikia mtu mmoja akiuliza kutokea kule kwenye kundi la watu.

“Ah, sijui bwana…we’ popi! Popiiii…! Kuja…!” Ile sauti iliyomjibu mwenzie ilianza kumuita yule mbwa, lakini mbwa popi alizidi kumbwekea Jadu kama kwamba hakumsikia bwana wake akimuita. Jadu aliendelea kutulia pale pale alipokuwa amesimama, na mbwa yule mtaka sifa alipoona kuwa Jadu hamjali, alimrukia kwa hasira akiwa amekenua meno yake makali ili amng”ate mguuni.

Lahaula!

Alipougusa tu mguu wa Jadu, mbwa alipigwa shoti kubwa sana mithili ya ile ya umeme na kutupwa nyuma kwa nguvu. Aliviringishwa mchangani huku viyowe vya mfululizo vikimtoka, kisha mbwa yule aliinuka na kutimua mbio kwa kasi mno huku akibweka mfululizo, mkia wake akiwa ameufyata.

“Heh, huyu mbwa kawaje…?” Sauti iliuliza kwa mshangao kutokea kule kwenye kundi la watu, na hapo mwanga mkali wa tochi ukamulika kule alipokuwa amesimama Jadu Mfaume. Mwanga ukapita mara ya kwanza, Jadu akasikia mguno kutokea kule kwenye kundi la watu, na mwanga ule ukarudi kwa mara ya pili, safari hii ukimpitia usoni, na akasikia mguno mwingine. Kisha ule mwanga wa tochi ukasaidiwa na mwanga wa tochi nyingine, zote zikim-mulika usoni. Na hapo mayowe yakarindima eneo lote lile.

“Hah, si Jadu yule…?”

“Ndiye yule…ndiye…ndiyeeeee, jamani ndiyeee…!”

“Jamani Jaduuuu! Jaduuu huyuuuuu!”

“Heh, miujiza jamaniiiii! Jadu katokeaaaa…!”

“Ja…Jadu…? Ja…Mume wangu? Mume wanguuuuu…Oooohhh, Mume wangu jamaniii…mume wangu ameponaaa…Uuuwwwiiiii…!”


Huba Binti Malambi aliinuka taratibu na kusimama akiwa ametanua miguu yake, mwili wa Esmund ukiwa umelala chini katikati ya miguu ile. Esmund alikuwa akitikisa-tikisa miguu yake kwa udhaifu mkubwa.

“Uwes….su! Cha…cha…mbusssss….” Esmund alikuwa akigumia kwa taabu, mwili wote ukiwa umemtapakaa damu.

Huba binti Malambi aliinamisha kichwa chake na kumtazama kwa muda, kisha akawageukia Uwesu na Chambuso, macho yake yakitoa mng’ao wa kutisha, damu ikichuruzika kutoka kwenye ncha za vidole vyake virefu.

Muda wote ambao mwenzao alikuwa akishambuliwa na binti yule aliyebadilika ki-ajabu sana, Chambuso na Uwesu walishindwa kukimbia na badala yake walibaki wakigumia kwa fadhaa na woga uliopumbaza maungo yao yote.

Ingawa akilini walijua kabisa kuwa walitakiwa wakimbie kutoka eneo lile, hakuna hata mmoja aliyeinua mguu wake kutoka alipokuwa. Ilikuwa ni kama kwamba lile tukio lilikuwa limewakamata kwa namna ya ajabu kiasi kwamba hawakuweza kabisa kutekeleza kile ambacho akili zao zilikuwa zikiwasukuma kufanya.

Kibaya zaidi ni kwamba na pamoja na woga mkubwa uliowakumba kutokana na tukio lile, hawakuweza kabisa kuyang”oa macho yao kutoka kwenye kile yalicholazimika kukishuhudia.

Haiwezekani hii! Hii sivyo…! Sivyo kabisa…Ni ndoto tu hii…si kweli kabisa!

Mawazo haya yalipita kichwani kwa Chambuso Mwagala wakati akimshuhudia yule binti akimchana chana Esmund kwa vidole vyake kama kwamba alikuwa akichana chana vipande vya magazeti.

“Aaaah, Uwesu…! Mmemfanya nini huyu binti jamani…?” Alibwabwaja kwa fadhaa kubwa, kauli yake akiielekeza kwa Uwesu ilhali bado macho yake yakiwa kule kwenye tukio lile la kutisha.

Uwesu alibaki akilia na kugumia kwa woga, akibwabwaja jina la swahiba wake katika maasi. Naye hakuweza kabisa kuyang”oa macho yake kutoka kule ambako mwenzake yule alikuwa akichambuliwa kuliko karanga na yule binti, damu ikiruka huku na huko wakati vilio vya uchungu kutoka kwa Esmund vikimfikia wazi wazi pale alipokuwapo.

Vijana walikuwa kwenye wakati mgumu mno wa maisha yao, na kwa mara nyingine Chambuso Mwagala alijithibitishia kuwa alikuwa amekumbwa na nuksi kubwa…

Sasa yule binti alikuwa amewageukia wao, akimuacha Esmund akimalizia pumzi zake za mwisho pale chini.

Macho ya kutisha ya yule binti yalimfanya Uwesu alie kwa woga huku akijaribu kukimbia, na ndipo alipogundua kuwa alishaanguka chini kitambo, na maungo yake yaligoma kutii kila alichojaribu kuyaamuru. Na hapo akajua kuwa alikuwa amelala chini akisubiri kifo, tena kifo kibaya na cha kutisha. Kama cha Esmund…kwani hakuwa na shaka kabisa kuwa Esmund alikuwa anakufa…

Aaah, jamani! Ibilisi gani aliyetuma hata kule kufikiria tu kumbaka yule binti lakini…?

Majuto yalipita kichwani mwake, na akazidi kulia kwa simanzi.

Laiti tungemsikiliza Chambuso…!Oooh, Mungu wangu, nakufa sasa Uwesu mimi…nakufa mwana wa Shaame, Ooooh Mungu wangu, nisaidie tafadhali…!

Aliendelea kulia kwa kukata tamaa huku akimshuhudia yule binti ambaye sasa alikuwa amesimama huku akitembeza kichwa chake baina yake na Chambuso, akiwatazama kwa zamu kwa yale macho yake ya kutisha, ngurumo za ajabu zikimtoka. Uwesu alibaki akiwa amejishika matumbo yake yaliyochanwa kwa pigo moja tu la yule binti, damu ikimvuja kutoka kwenye jeraha lile na kuchuruzika kupitia kwenye nafasi baina ya vidole vyake…

Taratibu binti alianza kuwasogelea kule walipokuwako. Hapo kila mmoja wao alikurupuka kutokea upande wake, akili ikirudi kwenye hatima yao.

“Aaaah, Anakuja Chambu! Anak…Oooh My God, twafa sasa! Twafaaa…twafaaaaaaa!” Uwesu alipayuka na kujiinua kutoka pale chini kwa nguvu ambazo hakujua kuwa bado alikuwa nazo, lakini alipojaribu kukimbia miguu ikamsaliti na akarudi tena chini kwa kishindo.

“Aaah Chambu! Ananijia mimi Chambu…mimi! An…nifanye kkk-kama Esmund! Aaaarghhhh…!” Uwesu alipiga kelele huku kwa mara nyingine akijiinua kutoka pale chini ili aokoe sehemu iliyobakia ya maisha yake mabovu, na kwa mara nyingine alifanikiwa kuinuka nusu tu kabla magoti yake hayajagongana na kujikuta akipiga mwereka mwingine.

“Oooooh….ooooo…ho ho ho ho…..” Alilia kwa kukata tamaa huku akiinua uso wake kumtazama yule binti.

Chambuso naye alikuwa kwenye kipindi kigumu kama mwenzake. Alipomuona yule binti akianza kuwaelekea kule walipokuwa, naye alijikurupusha kwa pupa kutoka pale kando ya tairi la gari alipokuwa amejikunyata na kuinuka akiwa ameshijikilia kwenye boneti la gari, lakini kila alipojaribu kusimama miguu yake ilikuwa ikiteleza na kuserereka kurudi tena pale pale chini alipokuwa

Huba binti Malambi, akiwa na nguvu zilizofifia za viumbe sita wa ajabu ndani ya mwili wake, nguvu zilizojikusanya na kuwa kitu kimoja mwilini mwake baada ya wale vijana wawili wapumbavu kuingilia kati na kukatisha mfumo wa nguvu zile kujizatiti ndani ya mwili ule, alikuwa akiwasogelea wale vijana huku azma ya mauaji ikiwa dhahiri kabisa machoni mwake. Vidole vya mikono yake miwili vilikuwa vimetangulizwa mbele huku vimechanuliwa na kuwa kama machanuo makubwa ya chuma. Sasa upepo mkali ulikuwa ukivuma, miti ikipepea kwa nguvu, majani kutoka kwenye miti ile yakipeperushwa huku na huko, mvumo wa upepo ule ukitoa sauti ya mbinja nzito ya kuogopesha.

Huba alisimama hatua chache baina ya wale vijana wawili waliotishika pasina mfano, kisha moja kwa moja akamgeukia Uwesu na kumtazama kwa macho ya kutisha huku akiwa amekenua meno kwa ghadhabu, vidole vyake vilivyorefuka vikijikunja na kujikunjua taratibu.

Mkojo ukampita Uwesu, na ladha chungu ya nyongo ikamjaa kinywani.

“Aaaa….Aaaaaaah, nis…nisssamme-he bibie! Nisam…aaaah, mama yangu wee nafa leo mwanaooooooo…!” Alilia rijali yule huku akijisikuma nyuma kwa kusotea matako, mkono mmoja akiwa amejishika pale tumboni alipojeruhiwa, mwingine akiwa amemuinulia yule binti kwa ishara ya kumzuia asimsogelee zaidi.

“Mmemfany…mmemfanya nin…ni huyu binti Uwesu! Mmemfanya…nini…?” Chambuso naye alikuwa akibwabwaja huku akimtazama kwa kihoro yule binti mwenye azma ya maangamizi makubwa.

Bila kujali vilio na maombolezo vya yule bazazi mbakaji, Huba binti Malambi alijikunja na kutanua mikono yake, huku akikunja na kukunjua vidole vyake haraka haraka, muungurumo wa kuogofya ukimtoka kooni kwake mithili ya chui anayetaka kushambulia. Huba binti Malambi alikuwa akijiandaa kuua…

“Aaaa! Aaaahhh! Tok…kaah! To…to..tok…k…kaaa” Uwesu alikuwa akimfukuza yule binti kwa woga kutoka karibu yake huku akizidi kujisotesha nyuma, lakini kila alivyojisogeza nyuma ndivyo yule binti alivyozidi kumfuata.

Ah! Hivi kweli ndio nakufa kirahisi namna hii Uwesu miye…?

Kwa nguvu zote alizoweza kuzikusanya Uwesu alijikurupusha kutoka pale chini na kuanza kutimua mbio kwa taabu, na hapo hapo Huba binti Malambi aliachia ukelele mkubwa sana wa ghadhabu huku akiruka mbele kama chui, mikono yake akiwa ameitanguliza mbele na vidole amevichanua.

Chambuso Mwagala alipiga ukelele wa woga huku akifumba macho kwa hofu ya kile ambacho angekishuhudia, ukelele wa woga na uchungu kutoka kwa Uwesu ukimfikia waziwazi masikioni mwake, ukifuatiwa na kishindo kizito kilichomaanisha kuwa tayari yule binti alikuwa ameshamnasa Uwesu. Uwesu na yule binti walianguka na kuviringika hadi upande wa pili wa lile gari, na huku akilia kwa woga wa kile ambacho atakiona, Chambuso Mwagala alijivuta mbele, na kutokea kwenye ukingo wa lile tairi alilokuwa amejibanza kando yake, alichungulia kule walipoangukia wale mahasimu wawili. Na ndipo aliposhuhudia tukio jingine la kutisha sana maishani mwake. Tukio lililotosha kabisa kumtia mtu wazimu.


Kule Shungubweni wilayani Mkuranga, Jadu Mfaume alijikuta akizingirwa na kundi la watu, wanaume kwa wanawake, waliotoka mbio kwenye nyumba zao hadi pale alipokuwako.

Kaa kimya sasa! Usiseme kitu…wewe ni mtu uliyenusurika na kifo kwa namna ya ajabu…hujui kilichotokea…umepumbaa…

Alibaki akiwatazama kibwege wale watu waliomuwekea nusu-duara mbele yake. Vilio vya akina mama na watoto vikisikika kutokea kila kona.

“Jadu! Jadu mume wangu…! Oooh jamani Mungu mkubwa huyu! Mume wangu amerudi jamani…!” Mwanamke mnene na mweusi alijichomoza kutoka kwenye lile kundi la watu na kumkimbilia huku akiwa ameinua mikono yake tayari kumkumbatia. Lakini kabla hajamfikia, akina baba wawili walimdaka na kumzuia yule mama huku wakimtazama Jadu kwa mashaka, kama jinsi watu wote wengine waliokuwa pale walivyokuwa wakimtazama, wakiogopa kumsogelea.

“Niacheni! Niacheni jamani…nikampokee mume wangu! Niacheni…waaaaarghh!” Mke wa Jadu alipiga kelele kwa jazba huku akijikukurusha kwa lengo la kujinasua kutoka mikononi mwa wale watu waliomshika.

“Ngoja mwanamke…Tulia! Ngoja kwanza…!” Mmoja wa wale waliomshikilia alimuambia huku akizidi kumdhibiti.

“Ningoje nini? Ningoje nini nakuuliza? Jadu! Jadu m”me wangu! Njoo kwangu laazizi, njoo! Njoo uwatoe hawa watu…wanan”zuia…!” Mwanamama alipayuka kwa kiherehere kikubwa kabisa. Jadu Mfaume alibaki akitazama yale mambo kwa mastaajabu makubwa. Yaani sasa alikuwa bwege kabisa, kila kitu kikiwa ni cha kushangaza kwake, na hakuonekana kama alikuwa akimfahamu yule mwanamke aliyekuwa akijinadi kuwa ni mkewe.

“Suburi bibie! Hii ni miujiza mikubwa! Hatuna hakika kuwa huyu ni mumeo kweli…”

“Sasa kumbe mume wa nani kama si wangu, mwehu nini…?”

“Unajua ametokaje huko baharini…? Lazima tuite wenzetu…”

“Wenzenu gani, nipishe mie huko!”

“…wazee wa kijiji! Lazima tuite wazee wa kijiji hapa ili…”

“Hakuna hiyo! Huyu ni mume wangu! Jadu Mfaume huyu…mume wangu, sasa wazee ndio wafanyaje? Niachieni bwanaaaaaa!” Mwanamama alikuwa hashikiki wala haambiliki, alizidi kubisha na kujitutumua. Muda huo alitokea mwanamke mwingine aliyekuja mbio huku akilia, khanga alizojitanda zikimuanguka ilhali akina mama wengine wakimfuata nyuma huku wakiziokota zile khanga na kujaribu kumvika tena, yeye akiwa amebaki na gagulo na sidiria tu.

“Jadu! Jadu babaangu…! Wapi mume wangu Dilunga, Jadu, eenh? Yu wapi yeye? Mlitoka wote kwenda dagoni Jadu…yu wapi Dilunga sasa eenh?” Yule mwanamke alikuwa akimuuliza Jadu kwa jazba huku akilia.

Jadu alizidi kushangaa. Watu wengine walimkamata yule mwanamke ili asizidi kumsogelea Jadu.

“Niambie kuwa mume wangu Dilunga…Dilunga wangu…anakuja! Niambie hajafa, Jadu! Niambie hajazama kama…” Mwanamke alizidi kubwabwaja, huku akiwa ameshikwa na wanaume wengine wawili.

Muda huo akaletwa mzee mmoja mtu mzima sana, naye akasogea taratibu kutoka kwenye ule mpaka uliojiweka baina ya wanakijiji na yule mtu aliyeonekana kuwa ni Jadu Mfaume. Yule mzee alimtazama kwa makini yule mtu aliyeibuka kutoka baharini usiku ule huku akizidi kumsogelea. Sasa watu wote waliokuwepo pale walikuwa kimya kabisa, hata wale akina mama waliokuwa wakilia kwa kuomboleza. Wote walitaka kuona nini kitajiri baada ya ujio wa yule mzee wa kijiji.

Jadu Mfaume alishusha macho yake taratibu na kumtazama yule mzee kwa macho yaliyoonesha kutomtambua kabisa.

Natakiwa nionekane nimepumbaa…

“Jadu?” Yule mzee aliita taratibu huku akizidi kumsogelea. Jadu hakumuitikia wala kusema kitu, aliinua macho yake kumtazama yule mwanamke aliyekuwa akimlilia huku akijinadi kuwa ni mkewe, kisha akayashusha tena macho yake kwa yule mzee.

“We’ Jadu we’! Si nimekuita? Unanifahamu mimi…? Unamfahamu yeyote kati yetu hapa?” Yule mzee alimuuliza, na Jadu akazungusha macho yake kuwatazama kibwege watu waliojazana pale, ambao walikuwa wakimtazama kwa mashaka huku wakinong”onozena vitu kuhusiana na tukio lile.

Jadu alibaki kimya.

Mzee aliinua mkono wake kutaka kumshika bega ili amuulize zaidi.

“Wachaaa! Usimguse!” Sauti kali ilitokea nyuma yake, na yule mzee na wote waliokuwepo pale waligeuka kutazama kule sauti ilipotokea. Uzegeni alikuwa akilisogelea lile kundi kwa mwendo wa haraka huku akiwa amejishika kiganja chake kilichobabuliwa kwa shoti ya umeme pale alipojaribu kumshika yule mtu aliyeonekana kuwa ni Jadu Mfaume mvuvi.

Wote waliokuwepo walipigwa na butwaa.

“We’ Uzegeni! Nini tena…?” Mzee aliuliza kwa mshangao.

“Si mtu huyo! Siye Jadu Mfaume tumjuaye huyo! Ni muujiza mkubwa huyo…ni balaa!” Uzegeni alisema kwa sauti huku akimsogelea yule mzee.

Macho yalimgeukia Jadu.

“Njaa…!” Jadu alisema kwa sauti dhaifu, kisha akaanguka chini kwa kishindo.

“Jaduuuu…!” Mkewe alipiga kelele huku akikimbilia pale alipoangukia yule mtu aliyeonekana kuwa ni Jadu Mfaume mumewe.

Heka heka mpya ikaanza pale kijijini, watu wakimzonga Uzegeni wakitaka ufafanuzi juu ya ile kauli yake, wengine wakimsogelea kwa hofu kubwa Jadu Mfaume aliyepoteza fahamu.

“Kafa!”

“Hapana…amezimia…!”

Wanakijiji walimzunguka yule mtu aliyelala bila fahamu pale chini ilhali mke wa Jadu Mfaume mvuvi akizidi kumlilia mumewe huku akijikurupusha kutoka mikononi mwa watu waliokuwa wamemshika akitaka kumkimbilia mumewe.

Yule mzee mtu mzima alikuwa akimtazama Uzegeni kwa macho makali yaliyojaa udadisi, lakini Uzegeni hakuwa akimtazama. Badala yake alienda moja kwa moja hadi pale alipoangukia Jadu Mfaume mpya na kumuinamia, akimazama kwa karibu.

Akiwa pale alipokuwa amemuinamia Jadu, Uzegeni aliwageukia wale wanakijiji waliojazana eneo lile.

“Siyo Jadu huyu!” Alisema na kuanza kurudi nyuma taratibu huku akiendelea kumtazama yule mtu aliyelala pale chini kama kwamba alikuwa akihofia kuwa ataamka muda wowote na kuanza kutembeza maafa kwa wote waliokuwepo pale.

“We’ mzima kweli wewe?” Yule mzee alimuuliza kwa mashaka, na Uzegeni alitaka kusema kitu kwa ukali, akitaka kuwasisitizia wote pale kuwa yule sio Jadu wanayemdhania wao, lakini hapo hapo alielewa ni kwa nini yule mzee aliuliza swali lile. Alisita.

“Toka huko muongo mkubwa! Ulikuwa unataka mume wangu afe sio…?” Mke wa Jadu naye alikuwa akipiga kelele huku akizidi kujitutumua kutoka mikononi mwa wale watu waliomshika.

Bila kutilia maanani kelele za mke wa Jadu, Uzegeni alifinya macho na kutikisa kichwa, na kumtazama yule mzee.

“Mzee najua kuwa mnadhani nimevuta bangi…!” Alianza kuongea, lakini mke wa Jadu bado alikuwa hajamaliza kumpasha vipande vyake.

“Ili unioe wewe au vipi…?” Alizidi kumpasha, sasa akimuona Uzegeni kuwa ndio adui yake mkuu.

“…lakini sivyo jamani! Mimi nimeacha kabisa kuvuta bangi hii wiki ya pili sasa! Hapa n”na akili zangu timamu kabisa mzee…!” Uzegeni alizidi kumueleza yule mzee kwa msisitizo.

“Basi kwa taarifa yako hajafa babu, eenh? Hajafa! Huyo hapo…mzima huyo! Kazimia tu kwa njaa mume wangu!” Mke wa Jadu naye alizidi kumpayukia Uzegeni.

“Hebu kelele we’ mwanamke…alla!” Mmoja wa wanakijiji waliokuwepo pale alimkemea kwa hasira.

“Wandugu, huyu si Jadu tumjuaye huyu nawaambia! Siye kabisa huyu!” Uzegeni alimalizia maelezo yake kwa msisitizo.

“Sasa kama si Jadu ni nani kumbe?” Mwanakijiji mmoja alidakia, na kabla Uzegeni hajajibu, yule mzee alidakia kwa upole.

“Uzegeni unachosema ni kigumu sana kwetu kukielewa. Ni kweli tuna mashaka na mazingira ya huyu mtu kuwepo hapa…”

“Jadu! Huyo ni Jadu, siyo “huyu mtu”…ni Jadu mume wangu huyo!” Mke wa Jadu alimkatisha yule mzee huku akilia.

“Hebu kelele we’ mama! Hivi huoni tunajaribu kutatua tatizo hapa?” Mwanakijiji mwingine alimkemea yule mke wa Jadu.

“…lakini hilo unalosema ni zito.” Mzee alimalizia kauli yake kwa Uzegeni bila kujali kauli nyingi zilizopita katikati, kisha akaendelea, “Kwa nini unasema huyu si Jadu wakati si” tunamuona kuwa ni Jadu? Kwa nini unasema huyu ni muujiza? Una kitu unachojua juu yake ambacho sisi hatukijui?”

Kwa mara nyingine Uzegeni alitazama ule mkono wake uliobabuka kwa kugusana tu na yule mtu anayedaiwa kuwa ni Jadu Mfaume mvuvi.

“Ndiyo mzee! Kuna mambo nimeyashuhudia kutoka kwa huyu mtu ambayo…ambayo si…si ya kawaida kwa kweli! Niliwaambia hata wale waliokuwa wakiendesha msako kule pwani hawakuniamini. Sasa si huyu hapa! Kafikaje huku? Katokaje kule baharini? Hebu tazameni huu mkono wang…”

Ghafla mke wa Jadu aliwasukuma huku na huko wale watu waliokuwa wamemshika ambao walizubaa wakisikiliza maelezo marefu ya Uzegeni, na kutimua mbio kumkimbiia mume wake aliyelala pale chini.

“Hah! We’ mwanamke…!” Mmoja wa wale waliokua wamemshika aliropoka kwa mshituko.

“Heh! Wewww-weeeh!” Mwingine alipiga kelele huku akijaribu kumdaka, lakini mke wa Jadu alimkwepa na kuzidi kukimbia huku akitamka jina la mumewe. Miguno ya wasiwasi ilitawala eneo lile, Uzegeni aligeuka na kumuona yule mwanamke akikimbilia pale kwa Jadu asiye Jadu, na akili yake ikarudi kwenye ile hali ilimtokea yeye pale alipojaribu kumshika yule mtu.

“Hapanaaa! Mkamate!” Alipiga kelele huku naye akijaribu kumrukia yule mwanama, lakini akamkosa, na kwa kihoro kikubwa akamshuhudia yule mwanamke akijibwaga kando ya yule mtu, mikono yake akiwa ameiinua juu na akiangusha kiwiliwili chake juu ya yule mtu aliyelala chali pale chini.

“AYYYAAAAAH! ANAKUFAAAH…!” Uzegeni alipiga kelele wakati yule mke akijiangusha kifuani kwa mumewe, na bila kupenda Uzegeni alijiziba macho, akihofia kuona mlipuko wa shoti za umeme ambazo alijua kuwa zingetokea pindi yule mama atakapogusana na mwili wa yule mtu.

Watu waliokuwapo pale nao walipiga kelele za woga kutokana na zile kelele za Uzegeni, wengine wakikimbia kutoka eneo lile wakihofia kile ambacho Uzegeni alikuwa akikihofia.

Kimya. Hakuna mlipuko wala tafrani iliyotokana na mlipuko.

“Jadu! Jadu…amka mume wangu, amka! Amka ewe nuru ya maisha yangu…amka…!” Mke wa Jadu alikuwa akilia kwa nongwa huku akiwa amejilaza kifuani kwa “mumewe”, akimsukasuka huku na huko kwa namna ya kumuamsha.

Uzegeni alitoa mikono yake usoni na kugeuka pale yule mwanamke alipokuwa amemlalia kifuani Jadu Mfaume, na mdomo ukamuanguka.

“EH!” Macho yalimtubuka kwa mshangao uliokithiri, na hapo akaona macho ya wote waliokuwepo pale yakimtazama kwa dharau na shutuma. Uso ukamdondoka na akabaki akilikodolea macho lile tukio la yule mama kumshika na kumtikisa yule mtu bila kudhurika hata kidogo.

“Ana…ana…mshika! Anamshika…!” Alisema kwa hofu na mshangao huku akimuoneshea kidole yuke mwanamke pale chini, na akitembeza macho kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Hakuna aliyemtilia maanani tena.

“Hebu mnyanyueni huyu mtu mumpeleke nyumbani kwake…anahitaji tiba na chakula.” Yule mzee alisema, akimgeuzia mgongo Uzegeni mvuta bangi, aliyebaki akitembeza macho kwa aibu na mshangao mkubwa sana.

Au haya mambo yamo kichwani mwangu tu jamani…?

Uzegeni alijishika kichwa kwa mastaajabu huku akiwatazama watu wanne wakimnyanyua yule mtu ambaye yeye hakuamini kabisa kuwa ni Jadu Mfaume mvuvi, na kuondoka naye, wakiongozwa na mke wa Jadu aliyekuwa akiendelea kulia.

Yaani ndio kusema bangi imenitia wazimu…?

Aliutazama tena ule mkono wake uliobabuliwa na shoti za umeme kutoka mwilini kwa Jadu Mfaume mpya.

Uzegeni alianza kulia kama mtoto.

Muda huo, baadhi ya watu waliokuwa kule pwani walifika mbio eneo lile, macho yakiwa yamewatoka pima.

“Yu wapi huyo Jadu…? Yuko wapi…?”

Huku akilia, Uzegeni aliwaoneshea kwa kidole chake kule walipoelekea wale watu waliombeba Jadu, nyuma yao wakifuatiwa na kundi la wanakijiji waliokuwa wamejazana eneo lile na walioshuhudia kila kilichotokea.


Wakati Uzegeni anampigia kelele yule mwanamke asimguse Jadu Mfaume mpya, upande mwingine wa mkoa wa Pwani, Uwesu alipiga mwereka mzito, akihisi kucha kali na ngumu zikizama juu ya mabega yake na uzito mkubwa ukimuangukia mgongoni mwake. Alijipigiza chini huku yowe likimtoka, maumivu yakitambaa mwilini mwake, sauti za kuogofya za yule binti wa ajabu zikiwa karibu kabisa na sikio lake.

Huku akipiga kelele Uwesu alijigeuza haraka, akijaribu kujinasua kutoka kwa yule mwanadada hatari, na kujikuta uso kwa uso na yule msichana aliyekuwa amekenua meno kwa ghadhabu.

“Tokk-kkaaah…niacchhe-eeee!” Alipiga kelele kwa woga na hapo hapo alimsukumia teke zito la kifua yule binti. Binti alisukumwa nyuma na msukumo wa teke lile, na wakati huo huo Uwesu alijirusha nyuma na kuanza kukimbia tena, akijiweka mbali na kile kiumbe. Alipepesuka kwa kukosa nguvu na kuegemea kwenye boneti la gari lao. Aligeuka kumtazama yule binti mwenye nguvu za ajabu huku akitweta.

Huba binti Malambi alipiga ukelele mkubwa huku akijiinua kutoka pale alipoangukia na kumeundea kwa kasi huku akiwa ametanguliza mikono yake tayari kushambulia. Uwesu alimuinulia mkono wake kumtaka msamaha huku akitweta bila kujiweza. Kile kitendo cha kumsukuma kwa teke yule binti, na kujiinua hadi pale kwenye boneti la gari, kilikuwa kimemmaliza nguvu kabisa kiasi hakuweza kuendelea kujitetea zaidi.

Huba binti Malambi alizungusha kwa nguvu mkono wake wa kulia na kutupa pigo moja lililokuwa na msukumo wa hasira zote alizokuwa nazo dhidi ya yule kijana, na kumchimba vibaya Uwesu kutokea chini ya tumbo lake na kutambaa hadi kifuani kwake, ukelele wake wa ghadhabu ukioana na ule wa maumivu na woga kutoka kwa Uwesu.

Na ni katika hatua hii ndipo Chambuso Mwagala alipochungulia kutokea kwenye ukingo wa tairi la gari na kushuhudia jinsi vidole virefu na vigumu vya yule binti vikimchimba tumboni Uwesu na kutawanya damu kila upande, hadi juu ya boneti la lile gari.

“WAAAAAAARGGGHHH…!” Ukelele mkubwa wa woga ulimtoka Chambuso, na hata pale alipokuwa akipiga ukelele ule, alimshuhudia yule binti akishusha kwa nguvu mkono wake wa kushoto, vidole vikiwa vimechanuliwa, na kumparura tena Uwesu usoni, akiacha michirizi minne minene ya damu.

Uwesu alilia kwa maumivu, akipeleka mikono usoni kwake, miguu ikimlegea na alibaki akiyumba-yumba kama mlevi, miguu ikigongana magotini .

“Mamaaa…nakuffff…” Uwesu alikuwa akilia kwa maumivu na kukata tamaa huku akizidi kujitahidi asianguke.

“Umeingilia jambo usilo…” Sauti nzito ilitoka kinywani mwa Huba binti Malambi huku akitupa pigo jingine kwa mkono wake wa kulia na kumpangusa vibaya sana usoni yule kijana, akiisukumizia mbali mikono ya yule kijana mpumbavu, na kuacha michirizi mingine mitatu usoni pake, na mmoja mnene ukiwa nyuma ya kiganja cha mkono wa kushoto wa yule kijana.

“…usilolijua mwana…damu!” Sauti nzito kutoka kwa Huba binti Malambi ilimalizia kauli yake kwa pigo lile lililommaliza kabisa Uwesu.

“Yalllaaa-aaarrghh…!” Uwesu alilia huku akipepesuka na kuanguka chini kama mzigo.

“Uwesuuuuu…!” Chambuso Mwagala aliita kwa fadhaa huku akiwa amejishika kichwa kwa kutoamini yale aliyokuwa akiyaona.

“Hayo ndiyo malipo ya kuvamia mambo yasiyokuhusu mwanadamu!” Huba binti Malambi alisema kwa hasira huku akiwa amemuinamia Uwesu pale chini, sasa sauti yake ikiwa ya kike, lakini ya mwanamke mkubwa na aliyekomaa, si ya kisichana kama jinsi umri wake ulivyo.

Chambuso Mwagala alichanganyikiwa vibaya sana. Aliuma meno kuzuia yasiendelee kugongana kinywani mwake kutokana na kitetemeshi kilichomshika, na kushuhudia kwa woga mkubwa kabisa kile kilichofuatia.

Huba binti Malambi alimkalia tumboni Uwesu aliyekuwa amelala chali pale chini na kuanza kushusha mapigo ya mfululizo kwa mikono yake yenye nguvu, akitumia vidole vyake virefu vyenye kucha kali, ndefu na ngumu.

“Uweess…Uweeeesssuuuu….Uwesuuuu…!” Chambuso alikuwa akimlilia rafiki yake kwa kitetemeshi na hamaniko la hali ya juu kabisa.

Ah, Mungu wangu kwa nini unaniletea mambo yote haya…kosa langu nini mimi lakini…?

Uwesu alikuwa akilia kwa uchungu kwa kila pigo lililomshukia, na Huba binti Malambi alikuwa akiendelea kushusha mapigo, moja baada ya jingine, kwa nguvu na ghadhabu kubwa. Kila pigo lilionekana kuwa ni zito kuliko lililotangulia, na wakati huo huo, kila pigo lilipokewa na yowe dhaifu zaidi kutoka kwa Uwesu.

Huba hakuacha kushusha mapigo mpaka Uwesu aliponyamaza kabisa na kubaki akiwa amelala kama gogo pale chini.

Chambuso Mwagala alihisi kizunguzungu na mwili ukimfa ganzi. Alikuwa ameshuhudia rafiki zake wawili wakiuawa kinyama mbele ya macho yake usiku ule, na hilo lilikuwa ni zaidi ya ambavyo fahamu zake zingeweza kustahamili.

Huba binti Malambi aliinuka taratibu na kuutazama kwa dharau mwili usio roho wa Uwesu bin Shaame, kidume kilichombaka muda mfupi uliopita, ambacho sasa hakikuwa kidume tena. Alibaki akimtazama kwa muda mrefu huku akihema kwa nguvu, kote kukiwa kimya kabisa.

Akamgeukia Chambuso aliyekuwa amejikunyata hatua chache kutoka pale ilipokuwa ile Gari lao akitetemeka vibaya sana huku akiwa ameuma vidole vyake kwa meno yake huku akigumia kwa sauti ya chini.

Huba alimtazama kama kwamba ndio kwanza anamuona, na kuanza kumsogelea taratibu, vidole vya mikono yake vikiwa vimechanuka huku vikichuruzika damu.

Macho yalimtoka pima Chambuso Mwagala, na kufikia hapa mwili wake haukuwa ukitetemeka tena bali ulikuwa ukitikisika mfululizo. Midomo ilimcheza huku meno yakigongana kwa sauti kinywani mwake. Alijua kuwa kifo kilikuwa kimemkabili na safari yake ya ulaya haikuwepo tena, na badala yake alikuwa safarini kuelekea kuzimu.

“Mnnnhhh…mmmmnnnngnnn…Nim…nimeku…k…kosea ni…ni…mimi we…we binti…?” Alilia huku akiuliza kwa kitetemeshi na woga mkubwa.

Binti alizidi kumsogelea huku akikunja na kukunjua vidole vyake, akimtazama kwa macho yaliyojaa unyama mkubwa yule kijana aliyejaribu kumsaidia dhidi ya udhalimu wa wale wenzake wawili aliowaangamiza. Chambuso alibaki akimtazama yule binti kwa kukata tamaa huku akibubujikwa na machozi. Alijaribu kujiinua lakini kwa mara nyingine maungo yake yaligoma kabisa kutii maelekezo ya fahamu zake.

Eh, Mungu wangu…

Alianza kujisotesha nyuma kwa matako yake ili angalau acheleweshe muda wa kufa, lakini alifanikiwa kusota hatua mbili tu na kujikuta akigota kwenye ngao ya lile gari.

Ah, wema wangu wa kukwepa kumgonga sasa unaniletea umauti Chambuso mimi…!

Alitembeza macho yake huku na huko akijaribu kutafuta njia nyingine ya kujiokoa kutoka pale alipokuwa amezingirwa na umauti, na macho yake yakaangukia hatua kadhaa mbele yake, nyuma ya yule binti, na kuuona mwili wa aliyekuwa Esmund Bwaira ukiwa umekauka katikati dimbwi la damu juu ya ile barabara pweke.

“Oooooohhh!” Alilia kwa kukata tamaa huku akigeuza uso wake pembeni, akijitahidi kutomtazama yule binti aliyejua kuwa ndiye atakayeitoa roho yake usiku ule.

Macho yake yaliangukia kwa Uwesu aliyekuwa amejikunyata katika umauti wa uchungu.

Nguvu zilimuisha kabisa.

Alibaki akilia huku akiwa ameinamisha uso wake chini, akisubiri yule binti amfikie na amuangamize kama aliavyowaangamiza wenzake.

Lakini mimi sikumkosea kitu huyu binti jamani…sikumkosea chochote mimi maskini…!

Chambuso Mwagala, kijana mstaarabu na muadilifu, alikuwa ameinamisha kichwa akilia kwa uchungu katikati ya barabara pweke, ndani ya usiku usio na mbalamwezi, akisubiri kuraruriwa vipande vipande na binti mdogo asiye na nguo… na mwenye nguvu za ajabu.


Wakati Chambuso akilia kwa kukata tamaa akisubiri kuondolewa duniani na yule binti asiye na nguo kule Kazimzubwi, kule Mkuranga Jadu Mfaume alikuwa akipatiwa huduma ya awali kutokana na madhila yaliyosadikika kuwa yamemkuta huko baharini. Mkewe alikuwa ameacha kulia na sasa, baada ya mtima wake uliojaa wahka kutulia, akili yake ilianza kuyatafakari yale yaliyokuwa yakisemwa na wanakijiji wenzake waliojazana pale nyumbani kwake, hususan mle chumbani ambamo Jadu alikuwa akihudumiwa. Hakika kuibuka kwake kutoka kwenye ile dhoruba kubwa kule baharini kulionekana kuwa ni muujiza mkubwa, lakini yeye siku zote alikuwa akijua kuwa mume wake alikuwa ni muogeleaji mzuri. Kwake haikuwa ajabu kwa mumewe kuweza kuogelea na kujikomboa kutoka kwenye dhoruba iliyotokea kule baharini.

Lakini haya maneno kuwa anaonekana kwamba eti si yule Jadu waliyemzoea yanakujaje tena?

Alimtupia jicho mumewe aliyekuwa amelazwa kwenye kitanda cha kamba, na wavuvi wenzake wakimuosha kwa maji ya vuguvugu ili kumtoa baridi iliyougubika mwili wake na kujaribu kumrejeshea fahamu. Akina mama wenzake walikuwa wakimsaidia kupika uji ili wamnyweshe yule mumewe pindi atakapozinduka na kuikabili njaa aliyokuwa nayo.

Hali iliendelea vile kwa muda, kisha yule mzee mtu mzima alimgeukia mke wa Jadu na kutikisa kichwa.

“Ni nini babu…” Mke wa Jadu aliuliza kwa mashaka makubwa.

“Ni ajabu kubwa hii…ajabu kubwa sana…” Mzee alisema huku akiendelea kutikisa kichwa, na kabla yule mke mwenye wahka hajauliza ni kipi kilichokuwa cha ajabu sana, mzee akaendelea, “…mpaka sasa hajamka tu! Kuzimia gani huku? Halafu inasemekana kuwa Uzegeni alikutana naye huko msituni na alipomshika akapigwa na shoti ya umeme…yaani ni mambo ya ajabu sana!”

“Ah, Uzegeni si mvuta bangi tu yule mzee…?” Mmoja kati ya wanaume waliokuwamo mle ndani alisema.

“Kwanza ye’ Uzegeni umeme kaujulia wapi? Ni nani mwenye umeme hapa kijijini kwetu hata ye’ leo hii ajue kuwa hicho alichokipata au kukihisi kutoka kwa Jadu ni umeme?” Mke wa Jadu alidakia kwa jazba.

Ghafla, mtu mwingine aliingia mle ndani kwa pupa, macho yakiwa yamemtoka pima.

“Mzee Chopa! Mzee Chopa…balaa! Balaa kubwa! Jadu yuko wapi? Yu” wapi Jadu nauliza…?”

“Nini wewe…?” Yule mzee aliyetambuliwa kwa jina la Chopa pale kijijini aliinuka kutoka kwenye kigoda alichokuwa amekalia kando ya kile kitanda alicholazwa Jadu na kumkabili yule mtu. Watu wote waliokuwemo mle ndani nao walimgeukia yule mtu. Yule mtu alitembeza macho yaliyojaa woga na jazba huku akihema kwa nguvu. Alimtazama Jadu aliyelala bila fahamu pale kitandani, kisha akamtazama mke wa Jadu na kuyarudisha macho yake kwa yule mzee.

“Haya na wewe umepatwa na nini tena? Mbona unakuja kwa vishindo na tashtiti zisizo msingi hapa, eenh?” Mzee Chopa alimuuliza yule jamaa.

“Popi wangu bwana…mbwa wangu popi…!” Yule jamaa alisema kwa wahka mkubwa.

“Ebbo! Si’ tuna wasiwasi na maisha ya mtu, we’ unaongelea mbwa? Au una…” Mmoja wa wanaume waliokuwamo mle ndani alisema kwa jazba, na hapo mke wa Jadu alidakia, “Na Jadu anahusika vipi na huyo mbwa wako? Mbona mnataka kunieleleza miye leo hii ndugu zangu, eenh?”

“Mbwa wangu amekufa jamani! Amekufa…!”

“Khah! Sasa…”

“Jadu atakuwa amemfanya kitu mbwa wangu! Popi, mbwa wangu…ndiye aliyeanza kumuona…akamkimbilia huku akibweka kwa nguvu sana. Mara tukamsikia akitoa kilio cha woga na akatimua mbio huku mkia ameufyata. Tulipoenda kutazama kilichomshitua ndipo tulipomuona Jadu” Yule mtu alijieleza huku akihema haraka haraka na akitupa mikono yake huku na huko.

“Kweli bwana! Hivyo ndivyo iliyokuwa…!” Mtu mwingine aliyekuwapo wakati tukio lile likitokea aliunga mkono.

“Sasa mbwa kafa!” Mwenye mbwa alimaliza kwa kukata tamaa. Miguno ya mshangao, fadhaa na kuchanganyikiwa ilitawala mle ndani.

“We” bwana una hakika na unayoyasema?” Mzee Chopa alimuuliza yule mwenye mbwa.

“Mzee Chopa, mbwa yuko huko nje amekufa! Mbwa wangu kafa jamani, na Jadu…huyo mtu hapo kitandani…ndiye anayehusika na kifo chake…!” Jamaa alimjibu akiwa amehamanika kweli kweli. Mke wa Jadu alipigwa na butwaa.

“Sasa…unataka kusema kuwa…” Mzee Chopa alibabaika.

“Huyo si Jadu huyo! Ni muujiza tu miongoni mwa miujiza ya bahari, lakini hakika si Jadu Mfaume tumdhaniaye huyu. Ni balaa lililoingia kijijini kwetu!” Yule mtu alimkatisha mzee Chopa kwa wahka.

Kimya kilitanda mle ndani, watu wote wakimtazama yule mtu aliyelala pale kitandani, kisha mzee Chopa alimgeukia yule mwenye mbwa na kusema kwa sauti iliyokwaruza.

“Kwa…kwa hiyo aliyosema Uzegeni yanaweza kuwa kweli…?”

“Bila shaka mzee Chopa…bila shaka…inawezekana kabisa!”

Miguno na minong”ono vilitawala mle ndani sasa, kila mtu akimtazama Jadu Mfaume kwa fikra tofauti.

“Hebu tokeni humu ndani jamani…wote!” Mzee Chopa alisema kwa mashaka, na watu wote waliokuwemo mle ndani walikurupuka, kila mmoja akiuwahi mlango.

Na hapo ndipo mke wa Jadu alipozinduka.

“Hapana jamani!Hapana…!Haiwezekani! Ngojeni kwanza jamani…!” Alipiga kelele huku akilia, lakini hakuna aliyemsikiliza, wote walitimkia nje ya nyumba ile, wakimkimbia yule mtu aliyelala bila fahamu pale kitandani.

“Twende we” mama…toka humu ndani!” Mzee Chopa alimkemea huku akimvuta mkono atoke naye nje. Lakini mwanamke hakukubali.

“Hakuna! Simuachi mume wangu hata kidogo! Huyo mtu ni muongo, muongo mkubwa!”

Mzee Chopa hakutaka kubishana naye. Alitoka nje haraka kwenda kumshuhudia huyo mbwa aliyeuawa na Jadu, na kama ndiyvo, basi awe mbali na nyumba ile kabisa.

Mke wa Jadu alibaki akilia kwa uchungu mle ndani, akiwa amejibwaga hatua chache kutoka kwenye mlango wa chumba alichokuwamo Jadu.

Mambo gani tena haya jamani lakini…?

Nyuma yake, Jadu Mfaume alifumbua macho ghafla, na kubaki akilitazama dari la chumba kile, akimsikia yule “mkewe” akilia kwa uchungu. Akilini mwake, mazungumzo yote yaliyopitikana ndani ya chumba kile wakati yeye akiwa “hana fahamu” pale kitandani, yalijirudia kama jinsi mtu anavyoweza kurudia kusikiliza mazungumzo yaliyorekodiwa kwenye mkanda wa redio…


Dakika zilizidi kusogea na bado Chambuso Mwagala alikuwa hajauhisi mkono wa damu wa yule binti ukiugusa mwili wake. Alizidi kujikunyata chini ya ngao ya lile gari huku akilia na kutetemeka kwa woga mkubwa, akimhisi yule binti akiwa hatua chache sana kando yake.

Ooooh…nakufa sasa Chambu…!

Alizungusha macho yake kwa woga na kuuona mguu wa yule binti ukiwa karibu sana na mguu wake, kiasi kwamba kama angetaka kuugusa, basi angeugusa kwa urahisi sana.

Aliinua uso wake na kumtazama yule binti kwa majonzi na fadhaa kubwa, uso ukiwa umemsawajika, machozi yakimtiririka,na midomo ikimcheza.

Lakini alichokiona usoni kwa yule binti kilimfanya akunje uso na azubae kwa muda, kwani alimuona yule binti akimtazama kwa uso uliojaa mshangao mkubwa. Binti alikuwa kama mtu aliyetoka usingizini na kujikuta yuko sehemu ambayo hakujua alifikaje, na hapo hapo, alikuwa akimtazama Chambuso kwa macho yaliyojaa wasi wasi kama aliyekuwa akijaribu kukumbuka ni wapi alipata kuonana na yule kijana.

Walitazamana. Chambuso akiwa amejawa woga, binti akiwa amejawa mshangao na udadisi.

Hii ni nini sasa…?

Na hapo, muda ule ambapo swali lile lilipita haraka kichwani mwake, Chambuso Mwagala aliona macho ya yule binti yakitoa ule mng’ao wake wa mauaji, kama kwamba hatimaye binti alikuwa amekumbuka kuwa naye ni mmoja wa wabaya wake. Binti alitoa sauti ya kuogofya huku akichanua vidole vyake yatari kwa kushambulia.

“Nilekese…! Nilemaaa…!” Chambuso aliropoka kwa woga mkubwa na akimuinulia mkono wake yule binti, huku, kutokana na kuchanganywa na wazo la kuuawa kinyama kama wenzake, akitumia ile lugha ya kizaramo aliyoongeleshwa na yule binti hapo mwanzo.

Binti alisita.

Alilaza kichwa chake pembeni na kumtazama kwa udadisi zaidi akiwa amechutama kando ya Chambuso, mikono yake bado akiwa ameiinua juu na vidole vyake amevichanua. Chambuso alimtazama kwa woga huku akitetemeka na akibubujikwa machozi bila kujiweza.

Taratibu yule binti alishusha mikono yake na huku bado akimtazama Chambuso kwa makini, alimshika shavuni kwa upole sana kwa mkono wake uliotapakaa damu, akimpakaza damu ile Chambuso usoni.

Chambuso Mwagala alijihisi akipotelewa na fahamu kwa woga uliomgubika.

Huba Binti Malambi alifumbua kinywa chake kutaka kusema, lakini alishikwa na kwikwi kubwa ya kilio, na machozi yakaanza kumbubujika huku akimtazama Chambuso, nyuso zao zikiwa zimekaribiana sana.

Chambuso alihisi kuishiwa nguvu kabisa, alibaki akimkodolea macho yule binti kwa woga mkubwa. Muda wote midomo yake ikimtembea kwa namna ilivyotaka yenyewe bila ya kushirikiana na akili yake iliyokuwakama imekufa ganzi.

“Nilemaa…nilekese….nilemaa….nilekeseee….” Midomo ya Chambuso Mwagala ilikuwa ikirudia tena na tena maneno yale, lakini akili yake haikuwa na habari kabisa kuwa midomo yake ilikuwa ikifanya kazi ya kuokoa maisha yake wakati ule.Akili yake ilikuwa ikijaribu kuelewa ni nini kilikuwa kikitokea pale, kwani alikuwa na hakika kabisa kuwa yule binti alikuwa ameazimia kumuua naye alikuwa ameshakubaliana na hali ile, lakini sasa ghafla, yule binti alikuwa akimshika usoni na kumpakaza zile damu zilizotoka kwenye majeraha ya wale wenzake waliouawa na yule binti, huku akilia!

Na bado, bila akili yake kutambua au kupanga, midomo yake ilikuwa ikirudia tena na tena yale maneno aliyoamini kuwa ni ya mwisho kwake kuyatamka akiwa mtu hai.

Nilema…Nilekese…

Niachie…Sitaki…

Sasa Huba binti Malambi alikuwa akilia kwa kuchanganyikiwa huku akimtazama yule kijana kwa macho yaliyojaa machozi na hisia ya simanzi. Yale maneno yaliyokuwa yakitoka kinywani mwa yule kijana yakimkumbusha jinsi yule kijana anayetokwa machozi mbele yake alivyojaribu kumuongelesha kwa ile lugha ya kwao, lugha aliyoielewa kwa wepesi zaidi, muda mfupi kabla wale wenzake hawajaanza kumfanyia kitendo kile kibaya.

Alimnyooshea kidole kilichokuwa kikitemeka yule kijana na kujaribu kusema kitu lakini hakuna kitu kilichokuja kichwani wala kutoka kinywani mwake. Sasa alihisi kitu kikubwa kikiwa kimemkaa kooni, alitembeza macho yake kule huku na huko eneo lile huku akilia na akiurudisha mkono wake uliokuwa ukitetemeka kinywani mwake kama namna ya kujizuia asilie, na macho yake yakaangukia kwenye ule mwili wa yule kijana mkorofi aliyelala bila uhai hatua chache kutokapale walipokuwa, na akabaki akiukodolea kwa mshangoa na mshutuko mkubwa, kama kwamba ndio kwanza anauona ukiwa pale chini, na si yeye aliyeucharanga kwa vidole vyake na kuuacha ukiwakama ulioraruriwa na mnyama mkali wa porini.

“Hooooooo…..ooooooo…” Kilio kilimtoka yule binti huku akiitazama mikono yake iliyojaa damu, na kuutazama tena ule mwili wa mtu aliyekuwa akiitwa Uwesu Shaame, sasa marehemu Uwesu Shaame, kisha akamgeukia tena Chambuso aliyekuwa amejikunyata pale chini huku naye akimkodolea macho na midomo yake ikimtetemeka, sasa hakuna sauti yoyote iliyotoka kwenye kinywa kile.

“Sasa ina maana hajui kama yeye ndiye aliyefanya mauaji haya…?” Chambuso alijiuliza kwa mashaka huku akili yake ikianza kufanya kazi taratibu, lakini woga wake ukiongezeka maradufu, akijaribu kujisogeza nyuma zaidi na akijiinua kutoka pale alipokuwa amechutama, karibu kabisa na yule binti.

Hilo lilikuwa kosa!

Binti alimgeukia ghafla na kumkamata shati lake kwa nguvu, na yowe kubwa lilimtoka Chambuso na ubaridi mpya ukamtambaa kutokakichwani hadi vidole vya miguu yake nakurudi tena kichwani. Sasa akijua kuwa ndio alikuwa akiraruriwa vipande vipande kama wenzake na yule binti.

Lakini haikuwa!

Binti alikuwa amemng”ang”ania shati lake hukuakitoa sauti za woga na akiitazama ilemiili ya wale watu wawili aliotoka kuzirarua roho zao kutoka kwenye miili yao, akizidi kumtapakaza Chambuso damu zilizokuwa mikononi mwake kwenye shati, usoni na kifuani, harufu ya damu ile ikimletea maluweluwe Chambuso.

“Binti…! Binti…! Ni…nini…? Niachi…” Chambuso alibwabwaja kwa hofu, huku akijaribu kujichomoa kutoka kwenye himaya ya yule binti, huku akimtazama kwa mchanganyiko wa woga na mshangao, na akijaribu kujiinua, lakini asifanikiwe kutokana na uzito wa yule binti aliyemng’ang’ania kwa nguvu.

Hakika Chambuso alichanganyikiwa.

“Ni..ni…nini…! Kim…metokk..kea…?” Huba binti Malambi, binti aliyekuwa akiwararua marijali wawili kwa mikono yake hadi kuwatoa roho, alikuwa akimuuliza Chambuso kwa mshangao na woga huku akimtazama usoni kwa macho yalioonesha kila chembe ya woga na mshangao wake.

“Ooohh…! Mama yangu weeeee!” Chambuso alijikuta akilia kwa fadhaa na kuzidi kujaribu kujitoa mikononi mwa yule binti ambaye sasa aliamini kuwa ni mwehu au aliyeingiwa na mapepo mabaya ambayo yanaweza kumgeuka muda wowote na kumtuma yule binti aanze kumrarua na yeye kama jinsi alivyowararua wale wenzake halafu aanze tena kuuliza ni nini kilichotokea.

Lakini binti alikuwa amemkamata kwa nguvu sana na Chambuso alijikuta akibaki pale pale chini, akiwa amepiga goti moja chini, na yule binti, akiwa hana nguo hata moja, akiwa amepiga magoti mbele yake na akiwa amemkamata kwa nguvu shati lake kwa mkono mmoja, na kwa mkono mwingine akiwa amemkamata mkono wake, chini kidogo ya kinapoanzia kiganja chake.

Chambuso alizidi kuishiwa nguvu, na machozi yalizidi kumbubujika. Alimtazama yule binti kwa kukata tamaa, na alikuwa akitaka kufunua kinywa chake kusema kitu lakini binti alimuwahi.

“Wewe…! U…U-mtu…mzuri…”

Ilikuwa ni sauti hafifu iliyotoka kama ya mtoto mdogo aliyejaa woga mkubwa. Mdomo ulimuanguka Chambuso Mwagala. Hakumuelewa kabisa yule binti, na akabaki akimkodolea macho kwa mzubao usio mithali.

“Nis…Ni…Nisaidie tafadha…li…!”

“Khah…?” Chambuso alipigwa na butwaa.

Yaani mtu umetoka kuua watu sasa hivi na mi’ nakuona! Halafu ulitaka kuniua na mimi muda huu huu! Mara ghafla ukaniona kuwa ni-mtu mzuri…! Na sasa unataka usaidiwe? Tena mimi ndio nikusaidie…?

Ni maswali yaliyopita kichwani kwa Chambuso haraka haraka wakati akimkodolea macho Yule binti kwa mshangao, lakini maswali hayo yalibaki huko huko kichwani, katu hakuthubutu kuyatoa nje ya kichwa kilekupitia kinywani mwake ambako hata hivyo, hakukuwa na uwezo wa kusema au kufanya lolote zaidi ya kulegea kwa butwao lililozidi kiwango.

Na hata kabla hajajua afanye nini zaidi, alimshuhudia yule binti akijitupa nyuma kwa nguvu huku yowe kubwa la maumivu likimtoka kinywani mwake na bado akiwa amemkamata shati na mkono wake.

Chambuso alipiga ukelele wa woga huku naye akivutwa pamoja na yule binti hadi chini walipopiga mwereka, binti akipigiza kisogo chake kwa nguvu kwenye ile lami, Chambuso akimuangukia juu yake huku kelele za woga zikimtoka.

Binti alianza kujitupa huku na huko pale chini, akimuacha Chambuso aliyekuwa akigaagaa kando yake.

“Uuuuwwwi! Aaaarghhh….! Mam…..Mmaaaaa….!” Binti alikuwa akipiga kelele za uchungu na Chambuso alijiinua akiwa amekolewa na woga na hakutaka tena kuendelea kuwepo eneo lile. Aligeuka na kutaka kukimbia, lakini alimuona Yule binti akijishika kwa mikono yake yote miwili shingoni kwake kama anayejikaba, au kama kuna mtu asiyeonekana aliyekuwa akimkaba, na miguu ya Chambuso ikagoma kukimbia. Alibaki akimkodolea macho Yule binti kwa kihoro kikubwa. Binti alikuwa akilia na kutoa sauti za kukoroma huku akijishika shingoni, akitupa kichwa chake huku na huko, macho akiwa ameyafinya kwa uchungu, na akijitupa tupa mzima mzima pale chini.

“Binti! We’ binti! Ni nini…?” Chambuso alijikuta akimpigia kelele huku akimzunguka yule binti pale alipokuwa akihangaika kwa uchungu mkubwa.

“Aaaargghh! Nakufff…naku…ghaaaaaagh….nak…Uuuuuuuuuhhhh…!”

“Nini lakini…? We’ binti una nini tena…?” Chambuso alipiga kelele kwa woga huku akimtumbulia macho yule binti, akijaribu kumshika, lakini akiogopa na wakati huo huo akishindwa kufanya hivyo kutokana na yule binti kujitupa tupa huku na huko pale chini bila mpangilio maalumu.

“Haya mambo sasa yamenishinda…”

Chambuso aligeuka na kuanza kukimbia huku akiwa amefunua kinywa chake tayari kupiga kelele za woga, lakini hapo ghafla alihisi ukimya ukishuka kama guo kubwa na kufunika eneo lote lile; yule binti akawa kimya kabisa.

Alisimamana kugeuka haraka, na moyo ukamlipuka alipomuona yule binti akiwa amekauka kau pale chini.

Amekufa…? Ghafla tu? Nani kamuua, kwani ni wazi kuna kitu…mtu…nani…? aliyekuwa akimkaba na kumfanya apige kelele na kutapatapa namna ile.

Binti alikuwa ametulia kimya kabisa pale chini.

Chambuso Mwagala, pamoja na woga uliomkuba, alijikuta akirudi pole pole kando ya yule binti na kumtazama kwa karibu. Mwanga wa taa za gari lao bado ulikuwa ukimuwezesha kuona katika usiku ule, ingawa si kama ambavyo yeye angetaka. Alimuinamia yule binti na kumtazama kwa karibu zaidi. Bado ile hisia kuwa yule binti alikuwa amekufa ilizidi kushamiri kichwani mwake.

Eh! Sasa…miujiza gani tena hii jamani!

Chambuso alipiga goti kando ya yule binti, si kwa kupenda bali kwa miguu yake kuishiwa nguvu kutokana na woga uliokuwa umemuelemea. Taratibu, huku akitetemeka mwili mzima, upepo mkali uliokuwa ukivuma eneo lote lile ukitoa sauti za kuogofya, Chambuso Mwagala alinyoosha mkono wake kujaribu kumshika kifuani yule binti, kusikia kama moyo wake bado ulikuwa ukipiga, na ghafla macho ya yule binti yalifumbuka.

Ukelele mkubwa ulimtoka Chambuso na akajirusha nyuma ili atimue mbio lakini mkono wa yule binti ulichomoka haraka sana na kumkamata mguu. Chambuso alianguka chini, mguu wake ukiwa umeshikwa kwa nguvu na yule binti.

“Ni..saidie…!” Binti alimwambia huku akiwa amemshika mguu ule kwa nguvu. Chambuso alikuwa akipiga kelele mfululizo na akijaribu bila mafanikio kuuchomoa mguu wake kutoka mkononi mwa yule binti.

“Waambie…waambie siyo…miye…” Binti alizidi kumwambia Chambuso kwa uharaka ulioashiria kuwa alikuwa aidha anataka kumuachilia aende zake, au yeye alikuwa anataka kuondoka amuache Chambuso pale barabarani. Chambuso alibaki akimshangaa yule binti, yale maneno yakiingia vizuri sana masikioni mwake lakini yakikosa kabisa idara ya kufikia ndani ya ubongo wake. Hakuelewa hata kidogo alichokuwa akiambiwa na yule binti.

Binti alikuwa akimtazama moja kwa moja usoni, na uso wake ulionesha kuwa yule binti alikuwa kwenye maumivu makubwa kabisa. Jasho lilikuwa linamtoka na mishipa ua uso ilikuwa imemtutumka kama jinsi mtu anayekabwa anavyokuwa.

“Siyo mie…siyo mie…SIYO MIYEEEEEEEEEEEEE….!” Binti alisema kwa uchungu na kumalizia na ukelele mkubwa huku akijitupa tena chini na kuanza kugaagaa kwa pupa. Chambuso alikuwa akimtazama huku naye akipiga kelele za woga.

Pale chini, Huba binti Malambi alikuwa akijitupa huku na huko, akiwa amejishika sehemu ya kifuani. Na wakati Chambuso Mwagala akimtazama yule binti huku akipiga kelele, alishuhudia jambo lililokuja kuharibu kabisa maisha na akili yake. Lilikuwa ni jambo lisiloweza kufikirika hapa duniani hata siku moja, na jambo ambalo hatopata nafasi ya kuja kumuelezea mtu yeyote maishani mwake.

Alibaki akipiga kelele kwa sauti ya juu kabisa huku akilishuhudia jambo lile la ajabu, sauti yake ikiimeza hata ile ya yule binti aliyekuwa akilia kwa uchungu pale chini.

Pasina kuamini macho yake huku akiona wazi wazi kilichokuwa kikitokea, Chambuso Mwagala aliuona mwili wa yule binti ukichanika taratibu sehemu baina ya yale matiti yake madogo.

Mwili ulimsisimka upya na alihisi nywele zikimsimama. Kwa mara nyingine tena katika usiku ule, alihisi kama kwamba kulikuwa kuna buibui mwenye miguu ya baridi sana akimtambaa mgongoni, vipele vya baridi vikichomoza ghafla mikononi mwake ilhali sehemu ya ndani ya mapaja yake ikilowa kwa maji ya uvuguvugu.

Chambuso Mwagala sasa alijikojolea!

Lakini akili yake haikushughulika kabisa na hilo la kujikojolea, kwani ilikuwa imezongwa na kile kitu kilichokuwa kikitokea mbele ya macho yake ambayo hakutaka katu kuyaamini.

Lilikuwa ni jambo la kutisha kusiko mfano, na Chambuso Mwagala alijikuta akijibweteka kando ya yule binti huku akilia kwa kelele, macho yakimkodoka. Ngozi iliyokuwa katikati ya kifua cha yule binti ilikuwa ikichanika huku mchirizi mwembamba wa damu ukifuatisha mchaniko wa ngozi ile, na wakati ngozi ile ikichanika, yule binti alikuwa akilia kwa maumivu makali, lakini sasa ilikuwa kama kwamba mikono yake imeshikiliwa ardhini kwa nguvu za ajabu, na hivyo mikono ile ilibaki ikiwa imelazwa pale chini ikionekana wazi kuwa haikuweza kuinuka kujishika pale palipokuwa pakitokea maumivu yale makali.

Chambuso alijiona akiingiwa wazimu hivi hivi, na hakuwa na lolote aliloweza kufanya juu ya hilo. Alibaki akipiga kelele huku akiwa amejishika kichwa, macho yake yakiwa bado yameganda kwenye kituko kile cha kupagawisha.

Na hata pale alipokuwa akiutazama ule mwili wa yule binti ukijichana wenyewe, Chambuso aliona kuwa ile sehemu ya mwili iliyokuwa ikichanika, haikuwa ikichanika hivi hivi tu…… la hasha! Ilikuwa ukichanika kufanya kitu kama alama fulani hivi… mchoro wa namna fulani hivi… ambao ulikuwa ukijichana wenyewe mwilini mwa yule binti!

“Whaaah…….. Whaaaaah……… aah…….aaayyy……….!” Chambuso alikuwa akilia kama bwege sasa, na kila ule mchoro ulivyojisukuma mbele na kuacha mchirizi wa damu kufuatisha ile alama ya ajabu iliyokuwa ikijichora mwilini mwa yule binti, ndivyo naye alipoachia yowe jipya la kilio chake cha kupagawa, sambamba na kilio cha yule binti aliyekuwa akitapatapa bila kujiweza pale chini. Na wakati akiutazama ule mchoro ukijikunja na kufanya alama kama ya nusu duara lililofunukia chini, wazo jingine lilipita kichwani mwake na kuongezea woga juu ya ule ambao tayari ulikuwa umemgubika kuliko hata uwezo wake wa kustahamili.

Ilikuwa kama kwamba kuna mkono usioonekana ambao ulikuwa ukimchora kifuani yule binti kwa kitu chenye ncha kali sana, bila ya kujali maumivu aliyokuwa akiyapata wala zile kelele zake na zile za Chambuso Mwagala mjaa nuksi.

“Heeeeeeh……sasa ni nani anayefanya mambo haya jamani lakini …?” Chambuso alibwabwaja kwa woga mkubwa huku akilia peke yake katikati ya usiku ule usio na mbalamwezi. Mbele ya macho yake ule mkono usioonekana uliendele kuuchora mwili wa yule binti kwa kisu chake chenye ncha kali kisichoonekana, safari hii ukichora michoro miwili kama alama ya mkwaju haraka haraka, chini ya ule mchoro wa nusu duara lililofunukia chini, na Chambuso aliachia yowe jingine kubwa sana la woga. Alijaribu kutimua mbio lakini akashindwa, na badala yake akabaki akibwabwaja huku akilia ovyo, akishindwa kabisa kuondoa macho yake kutoka kwenye kifua cha yule binti. Na hata pale alipokuwa akiendelea kushuhudia kituko kile huku akipiga kelele, Chambuso alibaini kitu kingine kibaya zaidi, kitu ambacho bila shaka kilizidi kumzamisha kwenye lindi la taharuki.

Ule mchoro uliokuwa ukitokea kwenye mwili wa yule binti ulikuwa ukichorwa kutokea ndani ya mwili ule na sio nje.

Yaani Kama kweli kulikuwa kuna mkono usioonekana uliokuwa ukiuchana mwili ule kwa kisu chenye ncha kali kisichoonekana, basi mkono ule ulikuwa ndani ya mwili wa binti yule!

Na hapo kitu fulani kilifyatuka kichwani mwa Chambuso Mwagala. Akili yake haikuweza tena kustahimili yale mambo iliyokuwa ikilazimishwa kuyaelewa. Alipiga kelele huku akitupa tupa mikono yake hewani, na sasa alikuwa akilia na kucheka kwa wakati mmoja.

Huba binti Malambi alipiga ukelele wa mwisho huku sehemu ya juu ya kiwiliwili chake ikijiinua kutoka pale chini.

Kidonda cha ajabu kilichobakia kifuani mwake kikiwa ni mchoro mbaya wa damu uliofanya alama ya ajabu na isiyoeleweka kabisa sio tu machoni mwa Chambuso Mwagala aliyepagawa, bali pia kwa macho ya binadamu yoyote hapa duniani.

Huba binti Malambi alijibwaga tena chini kwa kishindo. Alifurukuta kidogo pale chini, kisha akamgeukia Chambuso Mwagala, uso ukiwa umemnyauka ghafla, mchirizi mzito wa damu ikichuruzika kutoka kwenye kona ya mdomo wake.

Pamoja na woga uliomgubika, Chambuso Mwagala alijikuta akinyamaza kimya na kubaki akimkodolea macho yule binti aliyekumbwa na madhila mazito. Alikuwa amepiga magoti kando ya yule binti huku amekalia visigino vyake, machozi yakifanya michirizi miwili juu ya mashavu yake, mikono yake ikiwa inaelea juu ya mwili wa yule binti kama kwamba alikuwa akitaka kumshika lakini akiogopa kufanya hivyo kwa sababu ambazo mpaka sasa wote tutakuwa tunazijua.

Mkono dhaifu wa Huba binti Malambi ulianguka juu ya paja lake na yowe la woga likamtoka Chambuso huku akimtazama yule binti aliye taabuni. Huba alimkamata kwa nguvu pajani na kuinua kichwa chake kutoka pale chini, akimtazama moja kwa moja machoni.

“Wa-aambie…si….sio…miy….ye! Sio…miye!”

“Sio wew…? Kina nani…?”

“Sio miye…!”

Kisha Huba binti Malambi akaangusha tena kichwa chake chini kwa kishindo, akihema na kutweta kwa taabu na wahka mkubwa. Chambuso alibaki akimkodolea macho kwa kuchanganyikiwa kukubwa kabisa. Alitaka kusema kitu akaishia kumung”unya midomo yake. Huba binti Malambi alitoa mguno mkubwa. Akafurukuta kidogo na kutoa pumzi ndefu, kisha akatulia moja kwa moja.

Alikata roho.

“Aaah……! Aaaah…….Aaarrghhh…!”

Chambuso alipiga kelele huku akijirudisha nyuma kujiweka mbali na mwili wa yule binti, kama kwamba yule binti alikuwa akiogopesha zaidi akiwa mfu kuliko alivyokuwa wakati alipokuwa hai.

Aliyoyaona yalikuwa yametosha kumtia wazimu na hakuwa na uwezo, nguvu, wala nia ya kuona vituko zaidi kwa usiku ule. Alitaka awe mbali na eneo lile kwa namna yoyote ile iliyowezekana.

Wazo lililopita kichwani mwake muda ule ni kwamba baada ya yote aliyoyaona usiku ule, hakukuwa na lolote jingine atakololiona hapa duniani ambalo litamtisha zaidi ya yale aliyoyashuhudia katika barabara ile pweke.

Laiti angejua lililokuwa likimsubiri mbele yake, hakika asingeruhusu kabisa wazo lile kupita kichwani mwake wakati ule. Alibaki akijisotesha nyuma huku akiendelea kupiga kelele kwa woga mkubwa…


“Njaa….” Jadu Mfaume alisema kwa sauti iliyokwaruza huku bado macho yake yakiwa yamekodolea kwenye dari la miti la chumba kile alichokuwamo. Mke wa Jadu Mfaume alishituka akiwa pale alipokuwa amejibweteka akilia kwa muhemko mkubwa, na kulaza kichwa chake upande mmoja, akisikiliza kwa makini kujihakikishia iwapo alikuwa amesikia vizuri kile alichodhani kuwa amekisikia.

Woga ulimjaa sasa, alikumbuka jinsi nyuso za wale wanaume waliokuwa mle ndani zilivyohamanika kwa woga baada ya kuletewa habari kuwa Jadu alikuwa amemfanya kitu cha ajabu mbwa wa jirani yao na sasa amekufa. Alikumbuka jinsi uso wa mzee Chopa ulivyojaa msisitizo na woga halisi pale alipomshika mkono na kumvuta ili watoke nje ya nyumba yao na wamuache Jadu…mtu waliyedhani kuwa si Jadu… mle ndani, naye akabisha.

Na sasa….

Alisikia kishindo nyuma yake na akageuka haraka kilio cha woga kikimtoka. Jadu Mfaume alikuwa amesimama kando ya kile kitanda alichokuwa amelalia hapo awali, ile shuka nyepesi iliyokuwa imeufunika mwili wake ilikuwa imeanguka sakafuni hivyo akabaki uchi.

Walitazamana, na kwenye macho yake aliona kuwa Jadu alikuwa kwenye maumivu au taabu fulani.

Hivi huyu ni Jadu mume wangu kweli au…? Lakini mbona anaonekana ni yeye tu…?

“Jadu …..?” Aliuliza kwa kitetemeshi huku akiinuka na kumtazama mumewe kwa makini zaidi usoni, machozi yakimtiririka, mikono yake akiwa ameitanguliza mbele yake kama kwamba alikuwa akitaka kumdaka asianguke.

“Mwajina…. Njaa………!”Jadu alimwambia mkewe kwa taabu na kujibwaga tena kitandani, safari hii akibaki ameketi kwenye kitanda kile.

Ah! Ameniita kwa jina langu! Ananitambua kama mimi ni mkewe! Ni Jadu jamani! Ni mume wangu Jadu…!

Mwajina, mke wa Jadu Mfaume mvuvi aliwaza kwa furaha. Alimuendea mumewe pale kitandani na kumkumbatia kwa upendo huku akibwabwaja, “Jadu! Jadu mume wangu… Oooh, Jadu wangu jamani! Jadu…!”

“Njaa….n’na njaa kali mke wangu…” Jadu alisema kwa taabu huku akiwa amemkumbatia mkewe kwa nguvu dhaifu, macho yake yaliyokuwa yakitazamana moja kwa moja ukutani nyuma ya yule mwanamke, hayakuonesha muhemko wowote wa mahaba kama jinsi ambavyo yangetakiwa yaoneshe katika mazingira kama yale. Jadu Mfaume mpya alikuwa na mawazo na malengo mengine kabisa kichwani mwake wakati ule.

“Pole sana Laazizi! Pole usingizi wangu…subiri hapo hapo mpenzi, nakuletea uji sasa hivi” Mwajina alisema huku akiinuka na kukimbilia jikoni ambako alikuwa na hakika wale akina mama wenzake walikuwa wameshampikia uji kabla hawajatimka mbio kumkimbia Jadu.

“Mnnhu! Watu bwana! Eti hooo, sijui kamfanya nini sijui mbwa wetu…mara hooo, huyo si Jadu tumjuaye…!” Mwajina alijisemesha peke yake, kisha akasonya kwa dharau huku akimimina uji kwenye bakuli kubwa.

“Watu wameshindwa kumlisha mbwa wao vizuri huko halafu wanasingizia eti Jadu kamfanya nini sijui…” Alisonya tena, huku akirudi haraka kule chumbani na bakuli lake la uji mkononi. Alimkuta Jadu akiwa ameshavaa suruali safi kutoka kwenye kapu la nguo safi lililokuwa kwenye kona moja ya chumba kile, na sasa alikuwa amejiinamia pale kitandani, akiwa amekishika kichwa kwa mikono yake yote miwili, viwiko vya mikono ile vikiwa vimeegemezwa juu ya mapaja yake.

Jadu aliufakamia uji kwa pupa. Hakika alikuwa na njaa, na wakati akiufakamia, Mwajina alikuwa akisimulia kila kitu kilichopitikana pale kijijini tangu alipoonekana hadi jinsi wale wanakijiji wenzao walipotimua mbio na kumuacha peke yake mle ndani wakiamani kuwa Jadu ni kiumbe wa ajabu aliyejileta pale kijijini kwa kutumia sura ya Jadu.

“Hah! Sijui ni wapi…

(kumbe binadamu wakati mwingine wana akili, eeh?)

…wametoa mawazo kama hayo mke wangu!” Jadu Mfaume alimwambia mkewe huku akiendelea kufakamia uji ule baada ya mkewe kumaliza maelezo yake, kichwani mwake, akikubaliana kabisa na mawazo ya wale wanakijiji wengine.

Mara zogo lilisikika nje ya nyumba yao. Sauti za watu wengi zilisikika zikipiga kelele kwa jazba. Mwajina na Jadu walitazamana, Jadu akiliweka chini taratibu bakuli tupu lililokuwa na uji hapo awali. Kabla yeyote kati yao hajasema lolote, walisikia mlango wa nyumba yao ndogo ukipigwa pigwa kwa nguvu.

“Mtoe huyo mtu humo ndani! Mtoe!” Sauti zenye jazba zilinadi kutokea nje ya nyumba yao. Mwajina aliinuka na kumtazama mumewe, au mtu aliyeamini kuwa ni mumewe, kwa woga.

“Jadu! Wana …..wanakijiji…wanataka…” Mwajina alianza kuongea kwa hofu kubwa.

“Go and check them out!” Jadu alimkatisha haraka, uso wake ukionesha umakini wa hali ya juu na mkewe akabaki akiwa ameduwaa.

“Jadu! Tangu lini umejua kusema kizungu?” Mwajina aliuliza kwa mshangao mkubwa. Jadu wake amjuaye yeye kuandika jina lake tu hajui, sasa huyu wa kumsemesha kizungu tena katokea wapi!

Mwajina alichanganyikiwa.

“Fungua mlango huo mwanamke!” Kelele kutoka nje zilisikika. Mwajina aligeukia kule mlangoni, kisha akamgeukia Jadu. Sasa Jadu alikuwa ameshavaa shati na alikuwa akivaa viatu vya makubadhi alivyovichomoa chini ya kitanda.

“Mtoe huyo mtu bibie…ama sivyo tunaingia sisi…..” Wanakijiji walizidi kumpigia kelele kutoka kule nje.

“Jadu….hivi ni wewe kweli mume wangu……? Mbona unanitisha…….?” Mwajina alimuuliza mumewe kwa mashaka. Jadu Mfaume alimtazama yule mwanamke huku akiwa makini sana. Akapeleka macho yake kule mlangoni, kisha akayarudisha tena kwa yule mwanamke aliyesimama mbele yake.

“Una wasiwasi na mimi mke wangu…? Hata wewe…?”

“Tunasema mtoe huyo mdudu humo ndani!” Kelele zilizidi kushamiri kule nje.

“Au na wewe unadhani kuwa mimi ni mdudu…?” Jadu alizidi kumuuliza kwa upole huku akimtazama moja kwa moja machoni, na sasa macho yake yalikuwa yakimtisha Mwajina.

“Si…sio hivyo Jadu, lakini….”

“Vizuri!Sasa nenda basi ukawasikilize wanataka nini, halafu uje uniambie…” Jadu alimkatisha kwa utulivu, na ule utulivu wake ulizidi kumtisha Mwajina. Sasa alikuwa akitetemeka mwili mzima. Alikuwa ametanzika vibaya sana. Hakujua iwapo aende kule nje alipoambiwa na Jadu aende, au abaki pale pale alipokuwa. Na kama akienda kule nje alipoambiwa na Jadu aende, aende kwa nia ya kuwasikiliza wale watu waliojaa jazba wanataka nini, au ndio akimbie moja kwa moja? Maana hakuwa na shaka kabisa sasa kuwa huyu si Jadu wake amjuaye yeye.

Lakini yawezekana vipi…?

“Ja….Jadu…! Umewezaje ku…kuongea …kizung….”

Kishindo kikubwa kilisikika kule nje, kama kwamba jiwe kubwa lilikuwa limevugumizwa kwenye ukuta wa nyumba ile na kumkata kauli Mwajina. Yowe la mshituko lilimtoka, na hapo hapo Jadu alimkemea.

“Hebu nenda ukawasikilize hao watu Mwajina! Wananiita mimi mdudu? Kwa nini…?”

Kwani we’ hujui…?

Swali lilikuja haraka kichwani kwa Mwajina lakini woga ulikuwa umemshika na badala yake akatoka mbio nje ya chumba kile kukimbilia kule zilipokuwa zikitokea kelele za wale wanakijiji.

Muda Mwajina alipotoka tu nje ya chumba kile, Jadu Mfaume alipiga hatua moja kubwa na kulifikia dirisha la chumba kile. Lilikuwa ni dirisha dogo, lilichongwa kwa luva za mbao na lililoweza kufunguka kwa nje. Alilisukuma dirisha lile na kuchungulia nje, uso wake ukiwa umejaa utulivu wa hali ya juu, pamoja na mayowe ya watu aliyokuwa akiyasikia huko nje.

Dirisha lile lilifungukia nyuma ya nyumba ile, ambako kulikuwa na migomba mingi, michungwa na minazi mifupi ya mbegu ya kitale. Mimea hii ilikuwa imepandwa karibu karibu sana na kufanya kichaka cha kutosha kabisa nyuma ya nyumba ile.

Aligeuka kule mlangoni alipopotelea Mwajina, na kuona kuwa bado alikuwa hajarudi…


Mwajina alitoka nje ya nyumba ile akiwa bado amechanganyikiwa na yale aliyoyashuhudia kutoka kwa mumewe, au mtu aliyeamini kuwa ni mumewe, Jadu Mfaume. Na alizidi kuchanganyikiwa baada ya kuona kundi la wanakijiji wenzake likiwa limeizonga nyumba yao.

Lilikuwa ni kundi la akina baba na vijana aliowajua fika pale kijijini, na wote walikuwa wameshika silaha za aina mbali mbali – mapanga, mishale, marungu, visu, fimbo, majembe, na hata magobore. Na wengine walikuwa wameshika mienge iliyokuwa ikitupa mwanga mkubwa eneo lote lile.

“Tunatamka huyo mtu humo ndani, tena sasa hivi!” Mmoja wa wale watu alimkemea kwa hasira, huku wenzake wakiwa wanashabikia kwa jazba.

“Sasa jamani ….” Mwajina alihamanika.

“Sikiliza wewe mama! Yule si Jadu! Hatujui ni jinsi gani, lakini bahari ina mambo mengi! Inawezekana kabisa aliyezama ni Jadu Mfaume ….mumeo, lakini aliyeibuka siye…..” Mzee Chopa alimwambia kwa hisia kali, na hata kabla Mwajina hajaweza kujibu au kusema kitu chochote, yule mzee aligeuka kulia kwake na kumuonesha kwa kidole chake, “Hebu ona mwenyewe!”

Mwajina aligeuza kichwa chake kama bwege kufuata kule kidole cha mzee Chopa kilipokuwa kikimuelekeza, nako akashuhudia kundi la akina mama wenzake waliojazana kando ya kundi lile la akina baba wenye hasira likisogea pembeni na kumuwezesha kuona mzoga wa mbwa aliyekufa. Mwajina alivuta pumzi fupi za ghafla kwa mshituko. Yule mbwa kweli alikuwa amekufa, na ingawa hakuwa na uhakika wowote wa kumjulisha kuwa yule ndiye mbwa anayedaiwa kuwa ameuawa kimaajabu na mtu ambaye kufikia sasa alikuwa anazidi kupoteza imani kwa kasi kubwa sana kuwa ni mumewe, kitu kimoja kilimjia waziwazi akilini mwake. Yule mbwa alikufa kifo cha machungu na maumivu makubwa sana! Alikuwa amekakamaa kama jiti, macho yamemtumbuka hadi kuchana kingo za macho yale na kutoa mboni za macho yake nje kabisa ya kichwa chake, na kinywa chake akiwa amekichanua katika mbweko wa mwisho wa uchungu, meno kadhaa yakiwa yameng’oka kutoka kwenye kinywa kile, na yale machache yaliyobaki yalikuwa meusi kama vijiti vya mkaa.

Mwajina hakujua iwapo meno yaliyong”oka yalifanya hivyo kabla au baada ya mbwa yule kufanyiwa hicho inachodaiwa kuwa alifanyiwa na Jadu. Mguno wa fadhaaa ulimtoka bila ya kupenda, na alijikuta akihamisha upesi macho yake kutoka kwenye kituko kile cha kutisha.

“Sasa hayo ndiyo mambo ya huyo mtu unayemng”ang”ania!” Bibi mmoja alimkemea kwa jazba. Na hapo makelele yalianza upya, kila mtu miongoni mwa wale waliojazana pale nje akiropoka la kwake, na Mwajina hakuelewa hata moja.

“Yumo humo ndani huyo mtu?” Mmoja wa wale akina baba alimuuliza kwa hasira, Mwajina hakujibu, alikuwa akilia tu.

“Yumo au hayumo we” mwanamke…?” Mwingine aliuliza kwa hasira.

Sasa Mwajina alikuwa akilia waziwazi, na bila ya kuinua uso wake alijibweteka kwenye kizingiti cha mlango wa nyumba yao, na kuwaoneshea kwa mkono wake kule ndani.

“Twendeni!”

“Hayaaaaa!”

“Uaaaaa……..! Zimwi hilooooo!” Kundi la wale wanakijiji lilimruka Mwajina pale kizingitini na kuingia ndani ya nyumba ile huku wakipiga kelele za jazba, silaha zao zikiwa juu mikononi mwao.

“Jamani tutamuweza lakini…?”

“Hebu acha woga wewe!”

“Uaaaaaaa…….!”

Waliingia kwa vishindo ndani ya chumba ambacho awali yule mtu aliyeonekana kuwa ni Jadu Mfaume alikuwa akipatiwa huduma ya kwanza baada ya kuibuka kutoka baharini.

Chumba kilikuwa kitupu!


Chambuso Mwagala aligota tena kwenye ngao ya gari lao lililokuwa likiendelea kuangaza eneo lile kwa taa zilizokuwa zikizidi kufifia. Bado alikuwa akibwabwaja ovyo kwa woga mkubwa, huku akiukodolea macho ule mwili wa yule binti aliyekata roho mbele yake sekunde chache zilizopita. Ile taswira ya jinsi mwili wa yule binti ulivyokuwa ukichanika wenyewe kwa namna ya kuogopesha na kuacha alama ya kidonda cha ajabu, ilikuwa hai kabisa akilini mwake.

Alitupa macho huku na huko kwa woga, akihisi kabisa kuwa kulikuwa kuna kitu…mtu…uwepo wa namna fulani…eneo lile. Lakini bado alikuwa ni yeye tu na zile maiti zilizomzunguka. “Ooooh…mama yangu! Mama’angu weeeee…!” Aligeuka kulia kwake na kumuona Uwesu akiwa amekakamaa katika ile hali ya umauti.

“Aaaah…aaaaaa…!” Alilia kwa fadhaa. Akatupa macho yake kule alipokuwa ameangukia Esmund, na kuona muinuko mweusi tu kutokana na kufifia kwa mwanga uliokuwa ukitoka kwenye taa za gari lao, ila alijua pale alikuwa amelala rafiki yake mwingine akiwa hana uhai tena.

“Hoooooo…ooooh…!” Chambuso alilia tena kwa simanzi na hamaniko. Alikumbuka jinsi Esmund alivyokuwa akiimba nyimbo za kihindi kwa sauti lake zito la kilevi na akatamani wangekuwa tena kwenye gari lao wakipigiana kelele kama hapo awali kuliko kuwa katika mazingira yale wakati ule. Alihamisha macho yake kutoka upande ule, akitamani atazame mahala pengine popote isipokuwa pale alipolala Esmund wakati ule, na hapo macho yake yakaangukia tena kwenye mwili wa yule binti.

Na ndipo alipoona jambo jingine lililoifyatua kabisa akili yake. Jambo lililofanya vituko vyote alivyoshuhudia usiku ule vionekane kama masikhara tu…

Mwanga hafifu wa taa za ile gari ulikuwa ukiumulika moja kwa moja mwili wa hayati Huba binti Malambi, na kutoka kwenye ule mwili usio na uhai, Chambuso Mwagala aliona kitu, au umbo la kiumbe kilifanana na binadamu, umbo lililoonekana kama moshi–moshi hivi, ambalo ukilitazama, macho yako yanaweza kuona hata upande wa pili wa umbo hilo, kama vile unatazama kupitia kwenye kioo. Kilikuwa kama moshi mwepesi sana usio na harufu…unajua upo lakini huna namna ya kuushika wala kuunusa. Kilikuwa ni kiumbe chenye umbo ambalo unaweza kuliona na wakati huo huo hulioni!

Yaani pale macho yake yalipotua juu ya mwili wa yule binti, ndipo kiumbe yule wa namna ya moshi–moshi alipokuwa akijiinua kutoka mwilini kwa yule binti…na kuketi kwa muda kifuani kwa yule binti.

Mwili wote ulimuingia baridi.

Mdomo ulimuanguka na macho yalimkodoka kwa mshangao na woga uliokithiri. Na hata pale alipokuwa akiukodolea macho ule utata uliokuwa mbele ya macho yake, kile kiumbe kiliinuka taratibu mno na kusimama wima, kikiuacha pale chini ule mwili usio uhai wa yule binti. Kilikuwa ni kiumbe chenye mwili mrefu na mwembamba, miguu, mikono na vidole vyake vyote vilikuwa virefu sana na vyembamba. Kichwa kikubwa cha kiumbe kile kilikuwa na umbo la yai na kilikuwa kimebebwa na shingo ndefu na nyembamba.

Lilikuwa ni jambo la kutisha sana kuliona, na wakati Chambuso Mwagala akikikodolea macho kiumbe kile cha kutisha, mwili wake ulipoteza kabisa mawasiliano na fahamu zake.

Kile kiumbe kirefu cha ajabu kiligeuza kichwa chake taratibu na kumtazama Chambuso Mwagala moja kwa moja machoni, na hapo Chambuso Mwagala alitoa sauti hafifu ya kugwaya na bila kujitambua alijikunyata chini zaidi ya ngao ya gari ile akiwa ametumbua macho mpaka ukomo wake wa mwisho kabisa kwa woga. Matobo mawili makubwa yalikuwa sehemu ambapo macho yalitakiwa yawepo kwenye kile kichwa kikubwa cha kiumbe kile cha ajabu, na wakati akitazamana na yule kiumbe, Chambuso Mwagala alikuwa akiona hadi upande wa pili wa kichwa cha kile kiumbe kupitia kwenye matobo yale yaliyotakiwa yawe macho. Walibaki wakitazamana namna ile kwa muda ulioonekana kuwa ni mrefu sana kwa Chambuso, na katika muda ule Chambuso aliona kuwa zaidi ya matobo yale mawili yaliyokuwa usoni kwa kiumbe kile, hakukuwa na kiungo kingine chochote…si pua, si mdomo, wala si masikio.

Kisha taratibu, kile kiumbe kiligeuka na kuanza kuondoka kwa hatua moja baada ya nyingine, shingo yake ndefu ikiwa imeonyooka wima juu ya mabega yake mapana, na kichwa chake kikubwa kikiwa kimetazama moja kwa moja kule alipokuwa akielekea.

Na hata pale alipokuwa akikitazama kile kiumbe kikiondoka eneo lile, Chambuso Mwagala aliuona mwili wa yule kiumbe wa ajabu ukiyeyuka mbele ya macho yake kama jinsi moshi unavyotoweka upulizwapo na upepo.

Chambuso Mwagala alizidi kujikunyata kama mtoto mchanga chini ya lile gari, akiwa ametumbua macho moja kwa moja mbele yake, eneo ambalo ule mwili ulikuwako sekunde kadhaa kabla ya kuyeyuka…


Kule Shungubweni, wilayani Mkuranga, wanakijiji wenye jazba nao walipigwa na butwaa baada ya kukuta chumba kikiwa kitupu.

“Hah…! Mbona hamna mtu…?” Waliulizana kwa mastaajabu, wengi wao wakimgeukia Mzee Chopa, ambaye alitembeza macho huku na huko mle ndani.

“Hayupo bwana…!” Mzee Chopa naye alirudia maneno yale kama kwamba wale wanakijiji wenzake walioja jazba hawakuwa wakilijua hilo.

“Kayeyuka huyo! Si niliwaambia mimi?” Uzegeni alisema kwa wasiwasi.

“Haiwezekani bwana! Katokea dirishani huyu, hebu oneni!” Mmoja wa wale wanakijiji alisema kwa jazba huku akiwaonesha lile dirisha lililokuwa wazi.

“Twendeni…!” Mwingine alipiga kelele huku akikimbilia pale dirishani na kuchungulia nje ya chumba kile, wakati wengine wakikimbilia kule nje na silaha zao huku wakipiga kelele. Akina mama waliokuwa kule nje waliuliza kulikoni.

“Katoweka bwana…! Hayumo mle ndani…katoweka!” Wale wanaume waliwajibu huku wakikimbilia nyuma ya nyumba ile na kulivamia lile shamba lililokuwa nyuma ya nyumba ile wakimsaka yule mtu wa ajabu kwa kelele za ghadhabu na jazba. Mwajina alikurupuka kutoka pale chini alipokuwa amejibweteka na kukimbilia ndani ya nyumba yao kuhakikisha iwapo ni kweli Jadu alikuwa ametoweka.

Aliingia mle chumbani ambamo muda mfupi tu uliopita alikuwa amesimama mbele ya Jadu, na akamsikia kwa masikio yake akimtakia maneno ya kizungu, na kukuta chumba kile kikiwa kitupu. Alisikia mayowe ya wanakijiji waliojawa jazba wakipiga kelele kumtafuta Jadu kwa lengo la kumuangamiza, mwanga uliotokana na mienge waliyoshika mikononi mwao ikitupa vivuli virefu hadi ndani ya chumba kile kupitia pale dirishani.

“Oooh, Jadu…!” Mwajina alihisi kuchanganyikiwa, na akajibwaga pale kitandani huku akibubujikwa na machozi, harufu ya mumewe bado ikiwa imezagaa pale kitandani.

Kule nje msako uliendelea usiku kucha, na mpaka kunapambazuka, si Jadu Mfaume wala miili ya wale wavuvi wawili waliozama baharini pamoja naye, aliyepatikana. Kijiji kiligubikwa na hofu kubwa. Hofu iliyotokana na utata wa kitu cha ajabu kilichoonekana kikitumbukia baharini kutokea angani, na kuzamisha wavuvi watatu pamoja nacho… na kuibuka kutoka baharini mle kwa mtu aliyetatanisha akiwa katika umbo la Jadu Mfaume.

Ni utata ambao utazungumziwa kwa miaka mingi itakayofuata pale kijijini.

Athari za lile tukio la kutisha katika ile barabara ya Kazimzumbwi zilionekana asubuhi ya siku iliyofuata na akina mama waliotoka asubuhi ile kutafuta kuni porini. Akina mama wawili waliokuwa wametokea upande mmoja wa barabara wakiwa katika harakati za kukatisha barabara ile kwenda upande wa pili ndio walioiona ile miili iliyozagaa ovyo barabarani. Kilichofuata ni mayowe na vilio huku wakikimbia mbio kurudi kijijini kwao kupeleka taarifa ile ya kutisha na kuogopesha.

Mara moja wanakijiji waliofika kwenye tukio walimtambua Huba binti Malambi kuwa ni binti wa kijiji cha jirani na kile kilichokuwa kando ya barabara ile pweke ya Kazimzumbwi, lakini wale vijana wengine wote walikuwa wageni machoni mwao. Akina mama walikuwa wamepigwa na butwaa, wakati wazee wa kijiji wakijadili nini la kufanya. Ile miili ilifunikwa kwa khanga ili kuisitiri na aibu ya umauti, na ni katika zoezi hili la kuifunika miili ile ndipo wanakijiji wale walipopigwa na butwaa pale mmoja wao alipougosegelea mwili wa kijana wa tatu aliyekuwa amejikunyata chini ya ngao ya ya gari iliyokuwa kando ya miili ile iliyouawa na mnyama asiyejulikana, na kuruka nyuma kwa woga.

“Mzima..! Huyu mzi…ma….!” Alibwata yule mzee aliyekuwa akiusogelea mwili wa Chambuso Mwagala kwa lengo la kuufunika akiamini naye alikuwa amekufa.

“Mtumee!” Mwingine alipayuka huku akijumuika na wanakijiji wengine kumtazama yule kijana aliyejikunyata pale chini huku akiwa ametumbua macho moja kwa moja mbele yake. Alikuwa kama aliyekufa isipokuwa kwa macho yake yaliyokuwa yakikodoa mbele lakini yasiyoona kitu chochote.

Alikuwa kama zoba, au bwege….au ndondocha. Na hili la mwisho ndilo lililogota kwenye akili ya kila mmoja wa wale wanakijiji waliojazana pale barabarani asubuhi ile. Walijaribu kumsemesha yule kijana kwa kiswahili na kizaramo, lakini hawakupata jibu la aina yoyote. Mara moja mjumbe alitumwa kijiji cha jirani kwenda kutoa taarifa kwa wazazi wa yule binti aliyekutwa akiwa amekufa bila nguo katikati ya wale vijana wageni, kilichohisiwa kuwa kilimtokea binti yule mikononi mwa wale vijana kabla ya kifo kile kikiwa wazi akilini mwa kila mtu mzima aliyekuwepo pale asubuhi ile, lakini kila mmoja alibaki na hisia zake moyoni mwake. Woga mkubwa uliwatawala wanakijiji wale, wakati wakisubiri kufika kwa viongozi wa kiserikali eneo lile, ambao walipelekewa taarifa sambamba na zile zilipolekewa kijiji cha pili kwa wazazi wa yule binti aliyeuawa kikatili.

Walibaki wakimkodolea macho ya mshangao yule kijana mgeni aliyejikunja kama mtoto mchanga pale chini ya gari, hakuna aliyejua afanye nini. Nusu saa baadaye mjumbe wa kijiji aliwasili eneo lile akiwa ameongozana na mama wa Huba binti Malambi. Yule mama alikuja akiwa tayari anabubujikwa machozi, kwani alishaelezwa kilichomtokea bintiye, na sasa alikuwa amekuja kuthibitisha tu.

“Yu wapi mwanangu….? Yu wapi mwanangu……?” Alilia huku akitembeza macho yake kutoka kwenye mwili mmoja uliofunikwa khanga pale chini hadi mwingine. Alipooneshwa mwili wa mwanake ulipokuwa, yule mama aliufunua kwa kiherehere na kutoa mguno mkubwa wa fadhaaa alipoona jinsi bintiye alivyokufa kinyama na kwa aibu. Aliufunika haraka ule mwili na kuulalia pale chini, akiukumbatia huku akilia kwa uchungu, akilitamka jina la mwanaye yule tena na tena. Akina mama wenzake walijaribu kumnyanyua kutoka kwenye mwili ule huku wakimbembeleza nao wakilia, lakini mama Huba hakukubali. Alibaki akilia kwa kuomboleza na kwa uchungu mkubwa huku akiwa ameukumbatia mwili wa binti yake pale chini.

Muda mfupi baadaye gari aina ya 404 Peugeot ilifika kwa kasi eneo lile na kusimama kwa vishindo. Mlango wa mbele upande wa abiria wa gari ile ulifunguliwa taratibu na mguu mmoja ulikuwa umevaa kiatu cheusi kilichokolea kiwi ulitokeza kutoka kwenye gari ile ukifuatiwa na mtu mmoja mrefu na mweusi kweli kweli aliyekuwa kwenye mavazi rasmi ya kiaskari, ambaye alibamiza mlango wa gari ile na kutembea kikakamavu kuelekea pale kwenye lile kundi la wanakijiji. Bila ya kuambiwa wanakijiji walimpisha njia yule mtu aliyekuwa akifuatiwa na askari wengine wawili walioteremka kutoka sehemu ya nyuma ya gari aliyokuja nayo, mmoja wa wale askari alikuwa amening”iniza kamera shingoni kwake.

Mjumbe wa kile kijiji alimsogelea yule askari mweusi na mrefu na kusalimiana naye, kisha akaanza kutoa maelezo ya hali iliyokuwapo pale, lakini yule askari alimuinulia mkono kumnyamazisha huku akitembeza macho yake madogo na makali eneo lile. Alisimama katikati ya barabara ile na kutazama pale ulipofunikwa mwili wa Esmund Bwaira, kisha akautupia macho mwili uliofunikwa wa Uwesu bin Shaame, na kuutupia macho ule mwili wa Huba Binti Malambi, ambao sasa ulikuwa umebaki peke yake pale chini ukiwa umefunikwa kwa khanga ile, wanakijiji wakiwa wamefanikiwa kumuondoa yule mama aliyekuwa amemkumbatia mwanaye pale chini huku akilia hapo awali.

Watu wote walikuwa kimya, macho yao yakiwa kwa yule askari mrefu mweusi aliyekuwa akilitazama lile eneo la tukio kwa umakini wa hali ya juu. Hatimaye macho ya Inspekta Gezza Dilunga yaliangukia kwa Chambuso Mwagala, na hapo wanakijiji walimshuhudia yule askari akirudisha nyuma kichwa chake ghafla kama aliyepigwa kofi la uso, na kufinya macho yake kwa umakini wakati akimtazama yule kijana aliyekuwa amejikunyata pale chini ya gari.

Alimsogelea taratibu na kupiga goti mbele yake , kisha akapitisha mkono wake mbele ya macho ya yule kijana, lakini Chambuso Mwagala hakukepua wala kupepesa macho. Inspekta Dilunga alimtikisha bega kwa muda, lakini Chambuso Mwagala hakushituka wala hakuonekana kuhisi kuwa kuna mtu aliyekuwa akimtikisa mwili wake. Inspekta Dilunga alibaki akimtazama kwa muda yule kijana huku maswali mengi yakimpita kichwani mwake.

Mafunzo yake ya upelelezi wa eneo lolote la uhalifu hasa mauaji yalimwambia kuwa alitakiwa alitathimini eneo yeye mwenyewe kwanza, na kupata mtazamo wa kwanza juu ya eneo la tukio kabla ya kupata maelezo ya mashahidi waliokuwapo katika eneo husika. Na amekuwa akiifuata kanuni hii aliyofundishwa na jeshi la polisi la mkoloni, na imekuwa ikimsaidia sana katika kutekeleza kazi zake za kupeleleza wa makosa ya jinai aliyokabiliana nayo. Lakini hili aliloliona hapa lilimfanya aanze kuitafakari upya kanuni ile. Ni nini atakielewa katika kituko hiki kilichokuwa mbele yake? Mtu kakodoa macho kama mfu wakati yu hai, na hata akitikiswa haoneshi kuhisi chochote!

Aliinuka na kuundea mwili wa Esmund Bwaira, akifuatwa na wale wasaidizi wake. Muda wote huu hakuwa ametamka hata neno moja, na wanakijiji wote walikuwa kimya kabisa wakifuatilia kila kitendo alichokuwa akikifanya, na wale wasaidizi wake wawili wakijiona ni watu muhimu sana kuwa na Inspekta Dilunga wakati ule, wakiwatumbulia macho ya mastaajabu wale wanakijiji.

Inspekta Dilunga alipiga goti kando ya mwili wa Esmund Bwaira na kuifunua ile khanga iliyokuwa imeufunika mwili, na hapo hapo uso ulimbadilika pale aliposhuhudia jinsi mwili ule ulivyoraruwa kwa namna ya ajabu, ghadhabu ya kiumbe kilichomfanya vile ikijionesha waziwazi kwenye majeraha yale. Alibaki akiutazama ule mwili kwa muda mrefu, kisha akainuka taratibu, akiitupia kando ile khanga na akimuashiria yule masaidizi wake mwenye kamera aupige picha mwili ule. Haraka Yule askari alianza kuupiga picha mwili ule kutokea katika pembe tofauti. Inspekta Dilunga aliuendea mwili wa Uwesu bin Shaame na kuufunua, na alichokiona pale hakikuwa tofauti na kile alichokiona kwenye ule mwili wa kwanza, lakini hapa aliona kuwa ghadhabu zilikuwa kubwa zaidi, na majeraha yalikuwa makubwa zaidi. Alikunja uso na kuuma meno kwa tafakuri, macho yake makini yakichukua kila kitu yalichokuwa yakikiona kwenye mwili wa kijana yule mgeni machoni mwake.

Nyuma yake alisikia vilio vya chini chini vya mwanamke aliyekuwa akijitahidi kujizuia kulia bila mafanikio. Na hata pale alipokuwa akiutazama mwili ule, Inspekta Dilunga alijua kuwa safari hii alikuwa amekabiliwa na kesi moja isiyo ya kawaida. Hakujua ni kwa nini, lakini siku zote amekuwa akiamini hisia zake za kiaskari, na sasa alipata hisia kuwa hii ilikuwa ni kesi moja ambayo haikuwa ya kawaida kabisa.

Aliinuka na kuuendea ule mwili wa mwisho uliokuwa umefunikwa kwa khanga pale barabarani huku akumuashiria yule askari wake achukue picha za ule mwili wa Uwesu. Alipiga goti kando ya ule mwili, na kabla hajaifunua ile khanga iliyoufunika mwili ule alikatishwa na ukelele mkali kutoka nyuma yake.

“Muache hivyo hivyo!”

Insepkta Dilunga aligeuka kule ilipotokea sauti ile akiwa amekunja uso, mkono wake ukiwa umeshika upande wa ile khanga iliyoufunika ule mwili na kumuona mwanamke mmoja wa makamu akiwa katika hatua ya kumkimbilia pale alipokuwa amepiga goti, lakini hapo hapo mmoja wa wale wasaidizi wake aliwahi kuruka mbele na kumzuia yule mwanamke.

“Muache mwanangu…muache! Huwezi kumfunua mbele ya kadamnasi namna hii…!” Mama Huba alikuwa akimfokea kwa jazba huku akitiririkwa na machozi.

“Mama hebu tulia! Hii ni serikali iko kazini…!” Yule askari alimkemea mama huku akizidi kumzuia asiende pale alipokuwapo Inspekta Dilunga.

“Hakuna! Hii ni idhilali kubwa! Leo hii mwanangu ndio amekuwa maonesho ya kupigwa picha akiwa…akiwa …yoooooh mama weee!” Mama hakuweza kumalizia kauli yake badala yake aliishia kuangua kilio kikubwa cha uchungu huku akijitupatupa huku na huko kwa jazba. Inspekta Dilunga alibaki akimtazama yule mama kwa muda, kisha bila ya kusema neno aliugeukia ule mwili uliokuwa umefunikwa pale chini na kuufunua.

Kama yule Inspekta wa jeshi la polisi alishituka alipomuona Chambuso Mwagala akiwa amejikunyata na ametumbua macho pale chini ya gari lililokutwa kwenye lile eneo la tukio, basi mshituko alioupata pindi alipouona ule mwili usio nguo wa yule binti ulikuwa ni mkubwa maradufu. Aliguna kwa sauti na kukunja uso huku akirudisha nyuma kichwa chake kama kwamba alikuwa akihofia kuwa yule binti atamshambulia akiwa amelala pale chini. Alichokiona kilikuwa ni nje kabisa ya matarajio yake. Hajapata kukutana na kitu kama kile katika miaka yake yote kumi na miwili ya kazi ya uaskari, tangu wakati akiwa konstebo mdogo tu katika jeshi la polisi la mkoloni hadi wakati ule akiwa Inspekta katika jeshi la polisi la taifa huru lililojitawala.

Aliutazama ule mwili uliochakaa wa yule binti, na bila ya kufikiri zaidi akijikuta akiirudisha ile khanga na kuufunika ule mwili wakati bado akiwa na hamu ya kuuchunguza zaidi. Akili ilimzunguka, na kwa mara nyingine asubuhi ile alijikuta akipata ile hisia kuwa safari hii alikuwa amekutana na kesi isiyo ya kawaida. Aliinuka taratibu kutoka pale chini na kubaki akiwa amesimama huku amejishika kiuno.

Duh! Lile jeraha pale kifuani …!

Mama Huba alikuwa akizidi kulia na vilio vyake vilianza kumkera Inspekta Dilunga. Muda huo ving”ora vya gari la kubebea wagonjwa vilisikika vikielekea eneo lile. Alitembeza macho yake kwa wanakijiji waliosongamana eneo lile, akijua kuwa ni wajibu afanye kazi yake ipasavyo, pamoja na ile hali isiyo muafaka ya mrundikano wa watu. Kuwafukuza kutoka eneo lile ilikuwa ni nje kabisa ya uwezekano, kwani huenda kuna ndugu na jamaa wa marehemu wale, mmoja wao akiwa yule mama aliyekuwa akilia kwa kero.

“Wewe…,wewe…na wewe!” Aliwaoneshea kwa kidole chake cha shahada vijana watatu waliokuwa miongoni mwa wale wanakijiji waliojazana eneo lile. Macho yaliwatumbuka kwa woga wale vijana na kabla hawajajua waseme au waulize nini, Inspekta Dilunga aliwaita kwa mkono wake, na kuthibitisha utashi wake huo kwa kuwaambia, “Hebu njooni hapa…”

Kinyume na umbo lake kubwa, sura yake ya kiaskari na weusi wake ulioongezea kuleta ile taswira ya askari anayepaswa kuogopwa, Inspekta Gezza Dilunga alikuwa na sauti nyembamba na nyororo, ambayo ingekuwa gumzo iwapo bwana yule angeamua kuwa muimba taarabu. Vijana walisogea mbele kwa woga huku macho yakiwatembea na minong”ono ikizizima miongoni mwa wanakijiji walikuwapo pale.

Inspekta Dilunga aliwaamrisha wale askari wake wawafunue wale marehemu wa kiume waliokuwa wamesitiriwa na guo zao, kisha akawaamrisha wale vijana watatu aliowateua kutoka kwenye lile kundi la washuhudiaji kushirikiana na yule askari wake mmoja kumkinga yule binti aliyelala pale chini kwa kutumia zile khanga, ambazo walizikunjua na kuzishika kuuzunguka mwili ule na hivyo kufanya ukuta wa muda. Akiwa ndani ya ule uzio wa khanga, yule mpiga picha wa polisi aliupiga picha mwili wa hayati Huba binti Malambi kutokea katika pembe mbalimbali, huku mwili ule ukisitirika na macho ya wanakijiji waliopigwa bumbuwazi na mauaji yale ya ajabu na kutisha.

Na wakati Inspekta Dilunga akisimamia upingwaji picha wa mwili ule, Gari la kubebea wagonjwa aina ya Volkswagon Combi ilifika eneo lile kwa vishindo na makeke, huku vingora vikirindima eneo lote lile na kuwafanya wanakijiji wazidi kudadisika huku wengine wakijiziba masikio kutokana na kelele za ving”ora vile. Inspekta Dilunga alimwambia yule mpiga picha wake ampige picha na Chambuso Mwagala aliyekuwa bado amejikunyata akiwa amekodoa macho vile vile kama alivyokuwa wakati Inspekta Dilunga alipofika eneo lile. Watu watatu waliokuwa wamevaa makoti marefu ya kitabibu waliteremka kutoka kwenye ile Volkwagon Combi na kuelekea mbio kwenye lile eneo lililokuwa limezungukwa na wanakijiji. Mmoja kati yao, ambaye alionekana kuwa ndio kiongozi wao, alikuwa na asili ya kihindi, na alienda moja kwa moja hadi kwa Inspekta Dilunga.

“What have we got here Dilunga?” Alimuuliza kwa kimombo, ikiwa wazi kuwa walikuwa wakifahamina vizuri.

“Mauaji….na wazimu. Vijana watatu wameuawa kwa namna ya ajabu kabisa, na mmoja bila shaka amerukwa akili…na wewe kama kawaida yako umekuwa wa mwisho kufika eneo la tukio!” Inspekta Dilunga alimjibu yule tabibu kwa Kiswahili.

Tabibu mwandamizi wa hospitali ya wilaya ya Kisarawe Shabbir Ramaiya alibetua mabega yake bila ya kujibu shutuma ile, na kuiendea ile miili mmoja baada ya mwingine. Aliitazama ile miili iliyouawa kikatili bila ya uso wake kuonesha hisia yoyote, kisha akamgeukia Inspekta Dilunga aliyekuwa akimuendea mjumbe wa kijijji ambaye hakutaka kuongea naye kabla hajalichunguza eneo la tukio.

“Naomba unikusanyie watu wa kwanza kuona tukio hili…walioleta habari juu ya tukio hili kijijini kwako…na ndugu na jamaa yoyote wa hawa marehemu ambaye yuko hapa sasa hivi. Nitahitaji kuongea nao baadaye, pamoja na wewe mwenyewe!” Alimwambia kwa kirefu.

“Sawa Afande…lakini,nadhani hawa vijana ni wageni kabisa eneo hili, ila huyu binti tunamfahamu….!” Mjumbe wa kijiji alisema.

“Uliza watu wako hata hivyo…huenda walikuja kumtembelea mmoja kati yao…” Yule Inspekta alimwambia, kisha akamuendea Dokta Shabbir aliyekuwa amechutama mbele ya Chambuso Mwagala, ambaye bado alikuwa amejikunyata vile vile akiwa ametumbua macho kama sanamu.

“Unasemaje Dokta?” Alimuuliza huku naye akichutama kando yake, mbele ya yule kijana. “Umemaliza na wale kule?” Dokta Shabbir alimuuliza huku akiashiria kule ilipokuwa miili ya akina Uwesu na yule binti kwa kidole chake cha gumba.

“Yeah…… kwa sasa!” Inspekta Dilunga alijibu, na kuendelea “Unaweza kuwaondoa, tena fanya haraka, kwani wamekaa sana hapa.”

Dokta Shabbir aliwageukia wale wahudumu aliokuja nao na kuwaashiria waichukue ile miili. Mara moja wale wahudumu walikimbilia machela kutoka kwenye gari lao na kuanza kuiingiza ile miili kwenye ile gari, mmoja baada ya mwingine. Inspekta Dilunga alimgeukia Dokta Shabbir

“Unadhani ni nini kimemkuta huyu kijana?” Alimuuliza. Dokta Shabbir hakumjibu mara moja. Alikuwa akimtazama yule kijana kwa makini, kisha akatoa tochi ndogo ya kitabibu kutoka kwenye mfuko wa kifuani wa lile koti lake jeupe, na kummulika machoni yule kijana. Mwonzi mwembamba wa mwanga kutoka kwenye tochi ile ulimpiga machoni yule kijana, lakini hakupepesa macho wala hakuonesha kuwa alikuwa anahisi kwamba alikuwa akimulikwa na mwanga machoni.

“Mnh…hii ni ngumu kusema bila ya uchunguzi wa kina…ni dalili ya shock…mshituko mkubwa kabisa…” Dokta Shabbir alijibu kwa sauti ya kunong’ona, uso wake ukiwa umejaa mastaajabu juu ya hali ile.

“Kwa hiyo atakuwa ameona kitu kilichomsababishia mshituko mkubwa kiasi cha kuwa hivi?”

“Possibly…”

“Unadhani uchunguzi wake utachukua saa ngapi?”

Dokta Shabbir alitikisa kichwa

“Hii iko nje ya uwezo wangu…hii mpaka mganga mkuu wa wilaya mwenyewe, lakini lazima nikwambie Inspekta, hii ni kesi kubwa na ya aina yake! Sijapata kukutana na kesi kama hii kabisa!”

Inspekta Dilunga alimtazama yule tabibu kwa muda, akili ikimzunguka. Alishajua kuwa hii itakuwa ni kesi ngumu kwake, lakini kumsikia yule tabibu naye akitamka mawazo yake kwa sauti namna ile, hakukumfanya ajisikie vizuri.

“Come on Shabbir, niambie kitu ambacho sikijui bwana! Mi najua kuwa hii ni kesi ngumu…nisichojua ni muda gani itawachukua kujua sababu ya huyu kijana kuwa hivi…na muhimu zaidi, iwapo ataweza kuongea…!” Dilunga alilalama. Dokta Shabbir alitikisa tena kichwa.

“Samahani Inspekta, lakini nasikitika siwezi kujibu lolote katika maswali yako hayo kwa sasa…labda Dokta Nigel mwenyewe ndiye anayeweza kukujibu, naye ni baada ya kumfanyia uchunguzi wa kina huyu kijana.”

“Sasa huo uchunguzi wa kina utachukua muda gani bwana?”

“Ah! Muda wowote utakaohitajika Inspekta! Uchunguzi wa kitabibu si sawa na kuchagua mchele bwana! Kuna vitu vingi vya kuzingatiwa, navyo huchukua muda!” Shabbir alimjia juu. Inspekta Dilunga aliuma meno kwa hasira na kuchanganyikiwa.

“Shabbir, inaelekea huyu kijana ndiye shahidi pekee wa lolote lililotokea hapa, hivyo ni muhimu wewe na huyo mkoloni wako wa kizungu…huyo Nigel vitu gani sijui huko, mkalitia hilo akilini!Nataka majibu, na nataka majibu fast!” Inspekta Dilunga alimkemea Dokta Shabbir kwa sauti ya chini, akichunga wanayozungumza yasisikiwe na wanakijiji waliojazana pale.

Dokta Shabbir alimtazama yule askari mweusi kwa macho yaliyoumia. Alitaka kusema kitu lakini akaghairi. Badala yake alishusha pumzi ndefu na kutazama kule lilipokuwa limeegeshwa gari lao la kubebea wagonjwa. Wale vijana wake walikuwa wameshaiingiza miili yote ndani ya lile gari, sasa walikuwa wakivutana na mama wa yule marehemu wa kike aliyekuwa aking’ang’ania kuingia ndani ya gari lile. Alimgeukia Dilunga na kumuambia huku akimuoneshea kidole Chambuso. “Itabidi tumfikishe hospitali haraka sana…!”

“Oke… mi” sina kazi naye yoyote huyo sasa hivi.” Dilunga alimjibu, na Dokta Shabbir aliwaongoza wale wahudumu wawili wa hospitali kumnyanyua Chambuso na kumlaza kwenye machela. Kisha walimbeba kwa machela ile hadi kwenye gari lao la kubebea wagonjwa. Katika zoezi lote lile la kunyanyuliwa kutoka pale chini, kuwekwa kwenye machela, na hadi kunyanyuliwa na kuingizwa kwenye gari, Chambuso Mwagala hakutikisika wala kushituka. Alibaki akiwa amekodoa macho vile vile!

Inspekta Dilunga alilitazama lile gari la hospitali likiondoka kutoka eneo lile huku ikipiga ving’ora. Wanakijiji walianza kutawanyika naye akageukia kule alipomuacha mjumbe wa kijiji na kuona alikuwa amesimama na akina mama na akina baba wachache, na hatua chache kando yake, akina mama wengine watatu walikuwa wamemuweka chini mama Huba aliyekuwa akiendelea kulia kwa uchungu. Aliwageukia wale askari wake wasaidizi.

“Chunguzeni hilo gari…muwe makini na alama zenu za vidole.” Aliwambia, kisha akawaendea wale watu waliokuwa wamesimama kwa mashaka pamoja na yule mjumbe wa kijiji ili kuanza uchunguzi wa kesi ngumu kuliko zote alizowahi kukutana nazo maishani mwake.

Aliwakusanya wale watu chini ya mti uliokuwa karibu na eneo lile, kisha akaanza kuwauliza maswali wale akinamama walioigundua ile miili. Hawakuwa na habari mpya zaidi ya kile ambacho tayari kufikia muda ule alikuwa akikifahamu. Walikuwa wametokea upande mmoja wa ile barabara kwa nia ya kuivuka kwenda upande wa pili ili kuokota kuni, ndipo walipoliona lile gari, na waliposogea karibu, wakaona ile miili ya wale vijana. Ndipo walipokimbia kijijini kutoa taarifa kwa mjumbe wao.

Mjumbe alithibitisha maelezo yale.

“Je, wakati mlipowaona hawa vijana kwa mara ya kwanza wakiwa wamelala hapa barabarani, mliweza kumtambua yeyote kati yao?” Inspekta Dilunga aliwauliza wale akina mama, macho yake madogo yakitembea kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine.

“Mn-Mhn. Hatukuwatambua…” Mmoja alijibu

“Tuliona watu tu, na madamu yamejaa kila upande tukakimbia…” Mwingine alimalizia. Inspekta Dilunga aliandika kwenye kijitabu chake kidogo.

“Kwa hiyo mliporudi na wanakijiji wengine ndipo mlipoweza kuwatazama kwa karibu?”

“Ndio. Ndipo tulipogundua kuwa yule msichana alikuwa ni Huba, mwali wa mzee Malambi”.

“Na wale vijana wa kiume je?”

“Hapana…wale hatujawahi kuwaona kabisa afande, bila shaka ni wageni tu walikuwa wakipita njia tu na gari lao”. Inspekta Dilunga alimgeukia mjumbe wa kijiji.

“Na wewe pia hujawahi kuwaona hawa vijana eneo hili kabla ya leo hii?”

“Ndio bwana. Kama nilivyokuambia hapo mwanzo, hawa ni wageni kabisa eneo hili.”

Inspekta Dilunga aliwageukia wake akina mama .

“Kina mama nawashukuru sana, Mnaweza kwenda, ila nitawahitaji tena, na pindi muda huo ukifika, nitawahitaji kituoni, sawa?”

Kina mama walionekana kusita kidogo.

“Ina maana utatukamata?” Mmoja wao aliuliza.

“Hapana, ila nitahitaji maelezo zaidi kituoni.Kwa sasa mnaweza kwenda.” Aliwajibu, na wale akina mama waliondoka haraka eneo lile. Aliongozana na yule mjumbe wa kijiji hadi pale mama Huba alipokuwa akibembelezwa na wenzake.

“Mama pole sana… naamini wewe ndiye mama wa yule binti tuliyemuondoa muda mfupi uliopita…”.Mama Huba aliafiki kwa kichwa huku akibubujikwa machozi.

“Sasa mimi nitakuuliza maswali machache tu kuhusiana na msiba huu mzito uliotukuta, naomba uwe mstahamilivu kidogo, sawa?” Alimwambia kwa upole. Mama huba aliafiki kwa kichwa, na Inspekta Dilunga alimtupia swali lililokuwa likizunguka kichwani mwake kwa muda mrefu.

“Unafahamu ni mazingira gani yaliyosababisha binti yako akawa eneo hili?”

“Oooh, baba yangu we! Sijui chochote! Sisi tulikuwa kwenye ngoma kijiji cha jirani, na Huba alibaki nyumbani, kisha baba yake akawahi kurudi ili awe naye pale nyumbani. Nnashangaa leo asubuhi nimefuatwa huko kwenye ngoma nilikokesha na kuambiwa kuwa Huba mwanangu amekutwa barabarani…” Mama hakumalizia, akaangua tena kilio.

Inspekta Dilunga alimtazama kwa macho makavu, akimsubiri amalize kulia amtupie swali jingine.

“Na baba yake…mumeo…alikuwa wapi muda huo, na yuko wapi hivi sasa?” Inspekta Dilunga alimuuliza baada ya yule mama kutulia kulia kidogo.

“Si…sijui afande! Nimefika nyumbani nikakuta nyumba iko wazi na dimbwi la damu likiwa nje ya nyumba yetu, lakini baba Huba hakuwepo, ndipo nikakimbilia huku nilipoambiwa kuwa Huba amekutwa…” Mama Huba alijibu katikati ya kilio, na kuishia kulia upya.

Jibu hili liligusa udadisi wa Dilunga.

“Umesema kulikuwa kuna dimbwi la damu nje ya nyumba yenu…?” Alimuuliza.

“Eeee babaangu!Sijui mkosi gani huu umeniangukia mimi binti Mrisho!” Mama Huba alijibu na kuangua kilio zaidi. Inspekta Dilunga aliinamisha kichwa kutafakari yale mambo, kisha akainuka taratibu na kumtazama yule mjumbe wa kijiji.

“Mpelekeni nyumbani…sitakuwa na kazi naye tena kwa sasa, ila nitakuja kuitembelea nyumba yake kwa uchunguzi zaidi. Damu iliyokuwa nje ya nyumba ile isifutwe mpaka nitakapofika!” Alimpa maelekezo, ambayo alikuwa na hakika kuwa na wale akina mama walikuwa wakiyasikia. Mjumbe wa kijiji, wale akina mama na akina baba wachache waliobakia eneo lile waliondoka taratibu kurejea kijijini kwao.

Inspekta Dilunga aliliendea gari la akina Chambuso, ambako wale wasaidizi wake walikuwa wakiendelea kulichunguza, wakijaribu kutafuta iwapo kulikuwa na kitu chochote cha kuwawezesha kutambua mazingira ya gari lile kuwa pale, na hasa juu ya wale waliosadikika kuwa ni wamiliki wa gari lile.

“Enheeh? Mmegundua nini kwenye hili gari Koplo?” Alimuuliza mmoja wa wale askari, ambaye muda ule alikuwa amepiga magoti akichungulia uvunguni mwa gari lile.

Yule koplo aliinuka na kujipangusa vumbi. Yule mwenzake aliyekuwa na kamera shingoni alikuja kutokea nyuma ya gari lile.

“Afande…inaelekea hili gari lilipata ajali na kugonga mti au kitu kigumu, tazama ngao ilivyobonyea, na kioo chake cha mbele kilivyopasuka… na kioo cha taa moja ya mbele.” Yule Koplo alisema na Inspekta Dilunga aliafiki maelezo yale kwa kichwa huku akilitazama lile gari kwa ukaribu zaidi.

“Pia ndani ya gari kuna vipande vichache vya vioo, ambavyo tunahisi vimetokana na kupasuka kwa kioo hiki cha mbele wakati wa ajali hiyo”. Yule askari mwingine naye aliongezea, na Inspekta Dilunga alitikisa kichwa kwa mara ya pili kukubaliana naye huku akichungulia ndani ya lile gari.

“Dalili yoyote ni wapi ajali hii itakuwa imetokea? Mti wowote jirani na hapa unaoonekana kuwa umegongwa na gari hili?” Inspekta Dilunga aliuliza.

“Hiyo ndio ajabu Inspekta, kwani hakuna mti wowote wenye dalili za kugongwa eneo hili, ila upande huu wa barabara kumechimbika-chimbika, kuonesha kuwa gari ilijikita kwenye upande wa barabara kabla ya kusimama…” Koplo wa kwanza alijibu.

“Okay sasa hii ni kesi ya usalama barabarani vile vile. Nenda kwenye gari ukawaarifu kitengo cha usalama barabarani waje hapa haraka!” Aliamuru, na yule Koplo aliondoka haraka kuelekea kwenye gari lao, ambalo lilikuwa na redio maalumuu ya mawasiliano ya kipolisi ndani yake.

Inspekta Dilunga alimgeukia yule askari aliyebaki. “Kutokana na namba zake, ni wazi kuwa hili gari limetokea au limesajiliwa Dar es salaam. Je, mmegundua chochote ndani ya gari hili kuhusu mmiliki wake…? Kadi ya gari…, au kitu kama hicho?”

“Ndio afande… kadi ya gari inaonesha kuwa hili ni gari la mtu aitwaye Mwagala Kifyagi” Yule askari alijibu huku akimkabidhi kadi ya gari aliyoitoa ndani ya lile gari. Inspekta Dilunga aliipokea ile kadi na kuitazama huku akiwa amekunja uso, akionekana wazi kuwa akili yake muda ule ilikuwa ikifanya kazi kwa kasi sana.

ITAENDELEA

Utata wa 9/12 Sehemu ya Tatu

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment