Utata wa 9/12 Sehemu ya Tano
KIJASUSI

Ep 05: Utata wa 9/12

SIMULIZI Utata wa 9/12
Utata wa 9/12 Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA: HUSSEIN ISSA TUWA

*********************************************************************************

Simulizi: Utata Wa 9/12

Sehemu ya Tano (5)

“Sasa hali ya Dilunga ikoje huko hospitali?” Superintendent Tib Haggard alimuuliza Inspekta Brian Koba baada ya kupokea ripoti ya matukio ya siku ile mbaya kwa askari waliokuwa wakiendesha msako ule ulioshindwa.

“Sijaenda hospitali bado bosi…nikitoka hapa ndio nitaenda huko. Niliona hii taarifa ni muhimu sana kukufikishia.” Brian alimjibu bosi wake aliyechanganywa na taarifa ya kutoweka kwa John Smith.

Superintendent Tib Haggard aliguna kwa fadhaa, na kubaki kimya, Brian akisikia pumzi zake zikishuka na kupanda upande wa pili wa simu ile. Ukimya ulipozidi ilibidi aulize; “Afande…upo…?”

“Just how could a man disappear like that, jamani, eenh? How, my good lad…?” Superintendent Tib Haggard alifoka ghafla kwenye simu huku akigonga meza. Inspekta Brian Koba aliuma meno kwa hasira, na kufumba macho kwa kukosa la kufanya, kisha akameza funda kubwa la mate makavu, na kumjibu bosi wake.

“Ndiyo hivyo super…jamaa ametoweka…just like that!”

“Jeepers Creepers Brian! Yaani…pamoja na kuanguka korongoni, bado ameweza kuinuka, kutoka kwenye gari na kukimbia kiasi mpaka mnafika eneo lile awe amefika mbali kiasi cha kutoweza kuonekana? Hii si kawaida Brian…haiwezekani!” Tib Haggard alisema kwa mastaajabu makubwa, akiwa kilometa kadhaa kutoka pale alipokuwa Brian.

“Yule si mtu wa kawaida Super…amefanya mengi ya ajabu mpaka sasa, ingawa kwa hili hata mimi limeniacha hoi…”

“Sasa unadhani utachukua hatua gani baada ya kituko cha leo?”

“Msako utaendelea tu afande, lazima nimpate huyu mbwa, na nitampata tu. Nimemuwekea nadhiri kitambo, na sitatulia mpaka nimnase…!” Brian alijibu huku akijikung’uta vumbi kutoka kwenye shati lake la polisi. Alikuwa ofisini kwa Inspekta Dilunga, askari waliokuwa wakishiriki katika ule msako ulioshindwa walikuwa wamesharuhusiwa kurudi makwao. Jua lilikuwa limezama, huko nje kiza kilikuwa kimechukua nafasi yake, naye alikuwa amechoka vibaya sana.

“Nadhani nimekusikia ukisema kuwa yule si mtu wa kawaida…sasa unadhani utaweza vipi kumkamata wakati tayari ameshajionesha kuwa ana nguvu na uwezo usio wa kawaida?” Tib Haggard alimuuliza kijana wake.

“Sasa ulikuwa na ushauri mwingine zaidi ya huu wa kuendelea kumsaka afande? Unataka tuache kumsaka kwa sababu ana hizo nguvu za ajabu…?” Brian alimuliza bosi wake kwa mshangao kidogo. Tib Haggard aliguna kabla hajaongea tena.

“Brian, naamini kuwa kama kuna askari anayeweza kumtia mbaroni mtu yeyote anayesakwa kama huyo tumsakaye sasa hivi, basi askari huyo ni wewe, lakini hata mimi wakati nakuteua kwa kazi hii, sikujua kuwa nilikuwa nakupambanisha na kiumbe cha ajabu…kiumbe chenye nguvu za kichawi, hivyo nisingependa kupoteza nguvu-kazi muhimu kwenye vita ambayo ni ya kushindwa, ndio maana nakuuliza hivyo nikuulizavyo.” Tib Haggard alimuambia kijana wake kwa upole.

“Afande, mimi nitamtia mbaroni tu yule mjinga. Naamini hizo nguvu zake zinaelekea kupungua, na kama tungeendelea kumuweka mtu-kati kwa muda mrefu zaidi angesalimu amri tu. Si nimekusimulia kuwa sasa ameanza kutokwa damu kama binadamu wengine, wakati hapo awali alikuwa akitoa cheche za umeme tu…mwisho wake umefika bosi, na mimi ndiye nitakayemfikisha kwenye huo mwisho!” Brian alijibu kwa jazba.

Kimya kilitanda kwa muda, na Brian alitumia muda huo kuachia mwayo mrefu.

“Unadhani uchawi huwa unafikia wakati ukapungua, au kwisha kama unavyodai? Maana nyie ndio wenye mila hizi…” Tib Haggard alimuuliza.

“Yule sio mchawi afande, yule ni kitu kingine kabisa, kama ni uchawi basi sio wa kiafrika…” Brian alijibu na muda huo huo akajipiga kofi begani alipoumwa na mbu.

“What? Kwa nini unasema hivyo?”

“Ingekuwa ni uchawi asingetoa cheche na shoti za umeme afande. Angetoa moto tu wa kawaida, au angekuwa akifuka moshi na kutoa mijoka mikubwa mikubwa…au hata yeye mwenyewe angejigeuza nyoka au sokwe hapo ningekubali kuwa ni mchawi au anatumia uchawi, lakini umeme…? Hapana, hii ni kesi nyingine bosi, aweze kutoa umeme wakati watanganyika wanalalia vibatari na kandili huko? No way bosi wangu…this is something else altogether!” Brian alijibu kwa jazba, huku akili ikimtembea, alikuwa akiwaza huku akiongea, na yale maneno yalikuwa yakimtoka kadiri alivyokuwa akiendelea kulifikiria jambo lile. Na kwake ilileta maana zaidi kadiri alivyokuwa akilifikiria swala zima la yule mtu wa ajabu, John Smith.

“Na hicho kitu kingine kabisa unachokisema ndio kitu gani sasa Brian? Mi’ nataka majibu bwana na sio utata zaidi…” Superintendent Tib Haggard alimuambia kijana wake.

“Sijui ni kitu gani, lakini sio uchawi afande, kama ni uchawi basi sio wa hapa kwetu Tanganyika wala Afrika…”

“Mnh, Brian…unachosema kinaleta maana lakini ni kigumu sana kukithibitisha…kama si uchawi itakuwa kitu gani basi? Mbona bado unataka kuifanya hii kesi iwe kama Science Fiction Brian?”

“Sio mimi ninayeifanya hii kesi iwe hivi Super…na labda hicho ndicho hasa kilichopo, kuwa hiki ni kisa cha kisayansi, tofauti pekee ni kuwa sio cha kubuni bali ni kitu kinachotokea kweli!” Brian alijibu na kuachia mwayo mwingine mkubwa.

“Haileti maana hata moja. Nawe umechoka, matokeo yake unabaki ukipiga miayo tu. Nenda kapumzike, tutaongea kesho juu ya hili swala, ila kilicho wazi juu ya swala hili ni kwamba maamuzi lazima yafanyike, na lazima yafanyike haraka iwezekanavyo…”

“Samahani Bosi, maamuzi juu ya nini…”

“Juu ya muda gani msako huu uendelee Brian, hatuwezi kutumia nguvu ya askari wetu wachache kwenye kazi moja tu kwa muda mrefu zaidi…”

“Hah, kwa hiyo…”

“Kwa hiyo kama John Smith anapatikana, basi hakikisha anapatikana haraka, ili tuelekeze akili zetu kwenye mambo mengine!” Superintendent Tib Haggard alimjibu na kukata simu.

Brian Koba alibaki akiikodolea macho ile simu iliyokuwa mkononi mwake kwa mshangao, akili ikimtembea. Aliirejesha mahala pake ile simu, kisha akaiinua tena na kupiga namba nyingine ya simu.

“Bruno Mgimba…” Sauti iliyopokea simu ilisema kutoka upande wa pili.

“Bruno, Inspekta Brian Koba hapa. Nakuhitaji hapa ofisini kwa Inspekta Dilunga…”

“Okay, lini na saa ngapi…” Bruno alijibu na kusaili.

“Leo hii, na sasa hivi…”

“Hah…unajua ni saa ngapi sasa…?”

“Unakuja au huji bwana, mi’ nimechoka na sina muda wa kubembeleza waandishi wa habari saa hizi…”

“Nakuja…”

“Good man.” Alijibu na kukata ile simu. Muda huo huo akaiinua tena na kupiga namba ya hospitali ya wilaya.

“He…hellow…” Dokta Nigel Smith alipokea simu ile.

“Dokta, Inspekta Brian Koba hapa. Nipe hali ya Dilunga…”

“Still unconscious…” Dokta Nigel alijibu.

“Okay…sasa nahitaji nguo, magwanda yangu ya serikali yamechanika na hayatamaniki kwa vumbi. Naomba uniandalie nguo hata za hao wahudumu wako wa hapo hospitali, nizikute kwenye ile wodi ndogo niliyokuwa nimelazwa hapo awali, hiyo ndio itakuwa nyumba yangu ya kulala Kisarawe hii mpaka hapo nitakapopata uelekeo mwingine, upo?”

“Ah, eem…okay. Unatarajia kufika hapa baada ya muda gani?” Nigel aliuliza.

“Nadhani ndani ya nusu saa.” Brian alijibu na kukata simu.

Aliketi kwenye kiti na kuchukua karatasi iliyokuwa juu ya meza ile, kisha akachomoa kalamu iliyokuwa kwenye mfuko wa shati lake na kuanza kuandika.

Dakika kumi na tano baadaye Bruno Mgimba aliingia ofisini kwa Inspekta Dilunga huku akitweta.

“Haya niambie nisilolijua Brian, kwani habari kuwa John Smith amewatoka tena tayari ninazo…” Alimwambia, akilitilia msisitizo lile neno “tena”, huku akijiweka kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza ya Inpekta Dilunga.

Brian Koba, aliyekuwa ameketi nyuma ya meza ile, kwenye kiti cha Inspekta Dilunga, miguu yake mifupi ikiwa juu ya meza, alibaki akimtazama huku uso wake ukionesha kuwa na mawazo mengi. Mgimba akaongeza kauli nyingine, “Halafu umetapakaa vumbi mwili mzima Inspekta, kulikoni? Au ndio heka heka za John Smith…?”

Brian alizidi kumtazama kwa muda, asijue amjibu nini, kisha akavuta droo iliyokuwa kwenye ile meza ya Inspekta Dilunga na kuitoa ile picha ya mtu waliyemtambua kama John Smith iliyochorwa na wachoraji mahiri wa jeshi la polisi na kuitupia juu ya meza ile, mbele ya Bruno Mgimba.

“Nataka kuiona hiyo picha kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti lako kesho asubuhi, na kuwe na maelezo haya…” Alimuambia huku akimsogezea ile karatasi aliyokuwa akiandika juu yake muda mfupi kabla ya ujio wa yule mwandishi wa habari machachari.

Bruno Mgimba aliichukua ile picha na kuitazama kwa muda, kisha akaichukua ile karatasi aliyopewa na Inspekta Brian. Aliisoma kwa muda, kisha akainua macho yake na kumtazama yule askari kijana.

“Tangu lini ukanifundisha kazi Inspekta? Nitaiweka hii picha sawia, lakini juu ya maneno gani yaambatane na picha hii ni kazi yangu, huwezi kunifundisha maneno ya kuandika…”

“Ndio nimeshakufundisha hivyo Bruno, na hivyo ndivyo nitakavyoyaona maneno hayo kwenye gazeti lako kesho asubuhi. Sasa nahitajika hospitali ya wilaya, tutaonana kesho.” Brian alimjibu huku akiinuka na kwenda kusimama mlangoni, akimsubiri naye atoke nje ya ofisi ile.

Bruno Mgimba alipigwa na butwaa. Hakuamini alichokuwa akifanyiwa na yule askari kijana. Alifunua kinywa kutaka kuongea lakini akaghairi. Akabaki akimtazama yule askari kwa hasira.

“Bloody Fool Brian! Bloody, bloody fool…!” Alifoka na kupiga meza kwa ubavu wa ngumi yake, kisha akainuka na kutoka nje ya ofisi ile akiwa amefura kwa hasira…mkononi akiwa na ile picha ya John Smith, na ile karatasi aliyopewa na Brian Koba mbishi.

Brian alifunga mlango wa ile ofisi taratibu na kutoka kuelekea hospitali ya wilaya.


Aliingia kwenye wodi aliyolazwa swahiba na mkuu wake wa kazi pale Kisarawe, Gezza Dilunga.

Alikuwa ameoga pale pale hospitali na sasa alikuwa amevaa mavazi ya wahudumu wa hospitali, suruali ya kitambaa cha Khaki ya rangi ya kijani, pamoja na shati la mikono mifupi la kitambaa cha aina na rangi ile ile, miguuni alikuwa amevaa makubadhi aliyopewa na Dokta Nigel Smith, ambaye tayari alikuwa ameshamuaga kuwa anaenda nyumbani kwake kujipumzisha.

Chini ya shati lile la wahudumu wa hospitali alilovaa, alikuwa ameificha bastola yake iliyokuwa imesheheni risasi zile zenye kulipuka, tayari kutumika wakati wowote pindi itakapolazimu kuwa hivyo.

Inspekta Dilunga alikuwa amelala bila fahamu, kichwa chake kikiwa kimezongwa na mabandeji mengi, miguu yake miwili iliyovunjika ikiwa tayari imefungwa P.O.P., ilihali mkono wake mmoja ukiwa umefungwa bandeji kubwa.

Lah, hakika huyu bazazi John Smith ametutuia misukosuko mikubwa kabisa. Kwanza nusura anivunje mbavu, sasa amemfanya hivi Dilunga…!

Alimtazama yule askari mzoefu mtu mzima kwa muda mrefu bila ya kusema neno, akihisi ghadhabu zisizo kifani moyoni mwake, kisha akainua macho yake na kumtazama nesi aliyekuwa ameketi kimya kwenye kiti kilichokuwa kando ya kile kitanda alicholalia rafikiye.

“Nesi…unadhani ataendelea kuwa hivi kwa muda gani…” Alimuuliza. Yule nesi aliguna kwanza kabla ya kumjibu.

“Sina hakika…Dokta Nigel ndiye anayeweza kujibu swali hilo, mi’ niko hapa kumsubiria tu pale atakapoamka ili nitoe taarifa…”

“Unatoa taarifa kwa nani…Dokta Nigel ameshaondoka.”

“Nyumba yake iko ndani ya eneo hili hili la hospitali, na ameacha maagizo kuwa muda wowote Inspekta atakapoamka, aitwe mara moja…” Nesi alimjibu. Brian alimshukuru na kutoka nje ya wodi ile kuelekea “chumbani” kwake, kwenye ile wodi aliyofanya makazi yake pale hospitali. Hakuwa na lolote ambalo angeweza kufanya kwa wakati ule, naye alikuwa amechoka sana.


Picha kubwa sana ya wajihi wa yule mtu wa ajabu aliyebandikwa jina la John Smith ilikuwa kwenye ukurasa wa mbele ya gazeti la Ngurumo la siku iliyofuata, na maneno ANATAFUTWA NA POLISI yalienea sehemu yote ya uso wa gazeti lile, juu ya picha ile. Maelezo yaliyokuwa chini ya sura ile yalimuelezea mtu yule kuwa ni hatari sana kwa jamii nzima ya watanganyika. Kwamba mtu huyo amepewa jina la “John Smith” mpaka hapo jina lake halisi litakapotambulika, na kwamba anahusishwa na mauaji ya kutisha yaliyotokea wilayani Kisarawe siku kadhaa zilizopita, na kwamba mtu yeyote anatakaye muona atoe habari haraka sana kituo chochote cha polisi kitakachokuwa karibu yake. Raia walitahadharishwa kutomsogelea, wala kujaribu kumkamata “John Smith” pindi watakapomuona kwani kufanya hivyo itakuwa ni kuhatarisha maisha yao.

Aidha, habari ile iliwataka mtu yoyote wenye habari juu ya mtu yule hatari, aziwasilishe kituo chochote cha polisi kitakachokuwa karibu yake, au aziwasilishe moja kwa moja kwa Inspekta Brian Koba wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kisarawe. Kisha ikawekwa na namba ya simu ambayo Brian Koba anaweza kupatikana kwayo.

Baada ya maelezo hayo yalifuata maneno yafuatayo:

UJUMBE MAALUMU KWA MHALIFU “JOHN SMITH”:

Kwako John Smith uliyepotoka. Nakuahidi kuwa serikali itakusaka juu, na itakusaka chini; itakusaka kusini na itakusaka kaskazini. Itakusaka mashariki na magharibi. Itakusaka pande zote za nchi na dunia, na hatimaye itakutia mbaroni. Salama yako ni kujisalimisha, na nakushauri ujisalimishe haraka iwezekanavyo, kwani siku zako zimekwisha. Kama una hamu ya kuhatarisha maisha ya raia wema wa Tanganyika, basi nakushauri uanze na wale waliopewa jukumu la kuwalinda raia hao, ambao mimi ni mmoja wao. Anza na mimi John Smith, halafu, kama bado utakuwa hai, ndio uendelee na huo udhalimu au chochote ambacho wewe unaamini kuwa unakifanya.

Kwa mamlaka niliyopewa na serikali huru ya Tanganyika nakuamuru kwa mara nyingine John Smith, JISALIMISHE MARA MOJA!

Ni mimi, Inspekta Brian Koba.

Tangazo lile lilileta mtafaruku mkubwa.


“Jeepers Creepers Brian Koba! What the hell have you done now?” Superintendent Tib Haggard alifoka kwenye simu asubuhi ile, gazeti likiwa linatetemeka mkononi mwake.

“Sikuelewi afande…nimefanya nini cha kukufanya ufoke namna hiyo?” Brian alimuuliza mkuu wake wa kazi aliyekuwa upande wa pili wa simu ile. Ilikuwa ni saa moja asubuhi, naye tayari alikuwa kwenye magwanda mapya ya kiaskari aliyopata pale kituo cha polisi cha Wilaya ya Kisarawe, gazeti la Ngurumo la siku ile likiwa mbele yake, juu ya meza ya Inspekta Dilunga.

“Hujui…? Hili tangazo hapa gazetini…nani kakupa ruhusa ya kutoa tangazo namna hii gazetini? Wewe kama Inspekta Brian unajinadi gazetini kwa mamlaka uliyopewa na serikali huru…serikali gani hiyo iliyokutuma utoe hilo tangazo Brian…? Tena nataka…”

“Relax boss, relax…” Brian alimtuliza mkuu wake kwa upole. Tib Haggard alipandisha na kushusha pumzi ndefu mara tatu mfululizo, kisha akaongea kwa utulivu kidogo.

“Okay…ongea sasa Brian, nataka maelezo…”

“Afande, jana umenipa amri kuwa iwapo kuna uwezekano wa John Smith kupatikana, basi nihakikishe kuwa anapatikana haraka iwezekanavyo…sio?” Brian alimuambia na kumuacha na swali.

“Ndivyo…lakini sikukupa mamlaka ya kujinadi namna hiyo gazetini Brian…hilo tangazo la kuwa mtu huyo anatafutwa na polisi tu lingetosha, sasa hayo uliyoongezea hapo chini yanahusu nini Brian?”

“Super, naomba uniamini katika hili. Matangazo ya mtu kutafutwa na polisi huwa yanatolewa kila siku, watu wanayaona na kuendelea na hamsini zao, aidha wanageukia kwenye kurasa za michezo au za malenga na mambo mengine. Baada ya hapo hakuna tena anayejishughulisha na mtu huyo atafutwaye. Lakini kwa hivi nilivyofanya, hakika kila mtu atataka kujua zaidi juu ya huyu mtu aitwaye John Smith afande, na hilo ndilo tulitakalo…”

“Alaa…?”

“Ndio eenh, John Smith hatakuwa na mahala popote atakapoenda watu wasimjue au wasimtumbulie macho. Hivi niongeapo naamini kabisa baada ya tangazo hili kama lilivyotoka gazetini, sasa hivi hata wewe Super ukitoka mtaani watu watataka kukutazama mara mbili kujihakikishia iwapo wewe sio John Smith, na kila askari huko mitaani ataonekana ndiye Inspekta Brian Koba…”

“Ah, Brian matata sana wewe…unachosema kinaleta maana. Lakini hata hivyo bado huwezi kupita ukijinadi tu gazetini namna hiyo kama kwamba wewe ndiye mwanzo na mwisho wa jeshi la polisi, tangazo kama hilo anaweza kulitoa mkuu wa jeshi la polisi tu na si mwingine yeyote…”

“Afande jambo limesha fanyika. Na kwa hali tuliyo nayo sikuona namna nyingine ya kuweza kumnasa mtu huyu bila mimi mwenyewe kujinadi namna ile…”

“Kivipi Brian…iweje kujinadi kwako namna hii kuwe ndio njia ya kumnasa John Smith? Nijibu hilo, na labda nitalifumbia macho hili jambo na nitatoa maelezo yanayofaa ngazi za juu, kwani ni lazima hili swala litaulizwa.”

Upande wa pili wa ile simu uso wa Brian Koba ulichanua kwa tabasamu pana.

“Ni rahisi sana Afande.” Alisema na kutulia kwa muda, kisha akaendelea, “Kwa kufanya hivi, najaribu kumchokoza na kumkera John Smith. Kwa ujumbe huu, sasa ataelekeza ghadhabu zake moja kwa moja kwangu, na kusahau lengo lake, lolote liwalo. Na kwa kuwa atakuwa na hasira na mimi, lazima atakuja kwangu kutaka kunitia adabu. Na hapo ndipo tutakapomtia mbaroni…na safari hii hatochoropoka asilani! Huo ndio mpango wangu afande…”

Kimya kilitanda kwa muda, na Brian alianza kuhisi kuwa Superintendent Tib Haggard ameiacha ile simu huko aliko na kuondoka, wakati alipomsikia yule mkuu wake wa kazi mwingereza akisema kwa sauti ya mastaajabu.

“Ah, yaani unajifanya chambo Brian? John Smith ni mtu…kiumbe…hatari sana! Unajua huko ni kujitafutia madhara mwenyewe… ”

“Huko ni kujitolea kwa ajili ya taifa langu afande…nimedhamiria kumtia nguvuni huyu mtu, au kiumbe kama umuitavyo, na hivyo ndivyo itakavyokuwa.”

Kimya kingine kilichukua nafasi, kisha Tib Haggard akamuuliza, “Sasa…ni nini mkakati wako baada ya tangazo hili?”

“Nasubiri.”

“What…?”

“Nasubiri afande. Mi’ si nimeshamchokoza John Smith? Sasa nakaa kumsubiri ajibu uchokozi wangu, na hapo ndipo atakapojuta kuzaliwa…au kutotolewa…au vyovyote ilivyokuwa hata akatokea katika nchi hii…”

“Huo ni mpango kabambe na nakubaliana nawe moja kwa moja, ila naamini hutakuwa peke yako wakati John Smith anakufuata baada ya huu uchokozi wako kwake, sio?” Tib Haggard alimuuliza.

“Kabisa afande. Nitakuwa na walenga shabaha makini watatu muda wote, nao nimewapa maelekezo kuwa atakapotokea tu, popote pale, kila mmoja ahakikishe anamalizia risasi zote zilizokuwa kwenye bunduki yake miguuni mwa John Smith, hata kama hiyo miguu ikibidi kukatwa potelea mbali, alimuradi awe hai na aweze kuongea na sisi!” Brian alimjibu mkuu wake wa kazi.

“Okay Brian, endelea…na lazima nikuambie kuwa najivunia sana utendaji wako.”

“Ahsante afande…ndio maana ukaniteua kwa kazi hii afande.” Brian alimwambia.

“Yeah…na hakika sikukosea kukupa hii kazi Inspekta Brian. Hakikisha unanijulisha kila tukio jipya mara moja, sasa kesi hii inafuatiliwa kwa umakini mkubwa ngazi za juu.” Tib Haggard alisema na kukata simu.

Brian alibaki akiikodolea macho ile simu kwa muda mrefu.


Watu walijiuliza huyu Inspekta Brian Koba ni nani? Na ana uwezo gani wa kukabiliana na huyo “John Smith” ambaye ametajwa kuwa ni mtu hatari sana? Kuanzia Kisarawe hadi jijini Dar na nchi nzima, raia wote walijikuta wanakuwa makini ghafla, kila mtu akijaribu kumtafuta huyo “John Smith”, ambaye sura yake ilienea wazi wazi gazetini, wengine kwa woga tu ili wawahi kumtambua na kujisalimisha kabla hajawadhuru, na wengine kwa lengo la kumtambua na kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola, hasa kwa huyo Inspekta Brian Koba aliyetajwa gazetini na ambaye namba zake za simu ziliwekwa pale gazetini.

Askari mijini walikuwa makini sana kumsaka mtu yeyote aliyeelekea kufanana japo kidogo tu na John Smith.

Msako ambao hapo awali ulikuwa ukiendeshwa kimya kimya, sasa uliwekwa bayana, na kwa hakika ulikuwa na athaari kubwa sana kwa mhalifu yule majinuni.

Lakini John Smith, kwetu Jadu Mfaume, hakuonekana hata kidogo.

Yaani ilikuwa kama kwamba Brian Koba na jeshi la polisi kwa ujumla, alikuwa akimsaka katika ulimwengu wa viumbe hai, mtu aliyemuona kwenye ndoto zake tu usingizini.

Wananchi walikaa kwa mashaka makubwa, wakimhofia huyo “John Smith” anayetafutwa na serikali juu na chini, kusini na kaskazini, na pande zote za dunia.

Lakini hakuna yeyote aliyemuona mtu mwenye sura ile iliyooneshwa gazetini siku ile na siku mbili zilizofuatia. Na haikuwa mpaka siku ya tatu baada ya tangazo lile kutolewa gazetini, ndipo mtego na uchokozi ule wa Inspekta Brian Koba ulipozaa matunda…

Usiku wa siku ambayo tangazo la Brian Koba lilitoka gazetini kumtemea cheche Jadu Mfaume, Dokta Nigel Smith alimfuata Brian Koba aliyekuwa amejilaza kitandani kwenye ile wodi ndogo aliyoifanya makazi yake pale hospitali na kumuambia kuwa Inspekta Gezza Dilunga alikuwa amerejewa na fahamu.

“Yu hali gani?” Brian aliuliza huku akiinuka na kuvaa shati lake haraka haraka.

“Amevunjika miguu yote miwili Inspekta, unatarajia awe kwenye hali gani?”

“Natarajia awe kwenye hali mbaya…” Brian alijibu huku akitoka mle ndani, bastola yake ikiwa mfukoni mwake na mmoja wa wale walenga shabaha makini watatu waliokuwa nje ya wodi ile akimfuata nyuma ya Dokta Nigel.

“Na hivyo ndivyo alivyo…ana hali mbaya. Sio tu ya maumivu, bali pia ya kisaikolojia…anahisi kama kwamba ameshindwa kutimiza wajibu wake.”

“Aaah? Sasa hiyo inakuwaje? Yeye amefanya jambo la kishujaa kabisa bwana! Hatakiwi awe na mawazo kama hayo…” Brian alisema huku akiingia ndani ya ile wodi aliyolazwa Dilunga.

“Itachukua muda kuikubali hali hiyo…ni kawaida…” Dokta Nigel alimjibu kwa sauti ya chini.

“Heeeey, big boy! Ongea na mimi, vipi hali yako?” Brian Koba alimchangamsha kwa utani bosi wake.

“Ah, Brian…uko salama? Mara ya mwisho nilipokuona ulikuwa ukisambaratika korongoni kumkwepa John Smith…”

“Yeah…na we’ nilipokuona mara ya mwisho ulikuwa ukielea hewani kuangukia korongoni kando ya barabara, lakini sasa naona wote tuko salama.”

“Isipokuwa tu mi’ nd’o nimekuwa hivi…Dokta Nigel ameniambia juu ya madhila yaliyonikuta. Nimevunjika miguu yote miwili, Brian, na ananiambia mgongo wangu pia umepata mshtuko mkubwa, wanasubiri miguu iunge, ndipo waangalie juu ya hatima ya mgongo wangu…”

“Oh, una maumivu mgongoni…?”

“No…ni kama ganzi tu. Ila ameniambia kuna uwezekano nikaishia kwenye baiskeli ya viwete Brian…nisiweze kutembea tena iwapo mgongo wangu utaonekana kuwa na athari kubwa, ingawa ananipa moyo kuwa hiyo ni nafasi ndogo sana…”

Brian hakuwa na la kusema. Alimgeukia Dokta Nigel kwa macho ya kuuliza, na yule tabibu aliafiki maneno ya Dilunga kwa kichwa. Akamgeukia tena Dilunga.

“Ah…okay, natumai haitafikia hatua mbaya kama hiyo Inspekta…”

Dilunga aliitikia kwa kichwa na kutazama pembeni, na haraka Brian akaongezea, “…na umefanya jambo la kishujaa sana afande…”

Dilunga hakujibu na kimya kilitawala kwa muda mle wodini.

“Mmemtia mbaroni…?” Hatimaye Dilunga aliuliza ghafla.

“Ennh…?” Brian aliuliza kwa kutoelewa maana ya swali lile.

“John Smith…Mmemtia mbaroni?” Dilunga aliuliza tena, na uso wa Brian ukaingia fadhaa na kitu kama ghadhabu. Mara moja Dilunga akaelewa kuwa John Smith hakupatikana.

“Ame…amekufa…?”

Brian aliguna kwanza, kisha akamueleza kila kitu kama jinsi kilivyotokea.

Dilunga alichoka kabisa.

“Dah…sasa…huyu ni mtu gani lakini Brian, eeh?” Dilunga aliuliza kwa fadhaa.

“Si mtu…lakini tutamtia mbaroni tu, kwa namna moja au nyingine…”

“Nami nadhani sasa Inspekta anahitaji kupumzika…” Dokta Nigel alidakia.

“Okay…sawa kabisa…” Brian alisema na kumgeukia Dilunga, “…wewe pata pumziko afande…mimi niko humu humu hospitali, nitakuja kukuona tena kesho…”

“Ah, Okay…”


Siku ya tatu baada ya tangazo la Inspekta Brian Koba kutoka gazetini na bado hakukuwa na matokeo yoyote mapya juu ya mtukutu aliyetambulika kama John Smith, Inspekta Brian Koba na Superintendent Tib Haggard waliingia kwenye wodi aliyolazwa Inspekta Gezza Dilunga wakiongozwa na Dokta Nigel Smith.

Inspekta Dilunga alikuwa ameegemea mito iliyopangwa pale kitandani na kuegeshwa kwenye sehemu ya kichwa ya kitanda kile. Kando ya kitanda kile alikuwako mke wa Inspekta Dilunga aliyekuwa amejitanda khanga na mwenye uso uliojaa fadhaa.

Inspekta Dilunga aliinua uso wake na kuwatazama wale askari wawili walioingia mle ndani pamoja na yule tabibu mkongwe, na kujitahidi kuachia tabasamu la kuwakaribisha lakini hakufanikiwa kwani lile tabasamu liliishia kinywani tu na halikufika machoni.

“Jambo shujaa wangu?” Tib Haggard alimsalimia Dilunga huku akiachia tabasamu pana la kumtia moyo huku macho yake makali yakimtazama kwa makini, na mara moja yakiona kuwa bado hali ya Dilunga, kisaikologia ilikuwa mbaya.

“Jambo afande…karibuni…” Dilunga alijibu, sauti yake ilikwaruza kidogo.

Superintendent Tib Haggard alimgekia mke wa Dilunga na kumsalimu, wakati Brian akichukua muda huo kusalimiana na rafiki na mkuu wake wa kazi. “Yes Inspekta, pole sana…vipi hali yako leo?”

“Dah, hata sijui bwana lakini nadhani nitaishi, yule mujirima alitaka kutuangamiza…” Dilunga alimjibu.

“Yeah…lakini hakufanikiwa…hakika pale ulifanya kitendo cha kudiriki kikubwa kabisa afande. Umemchapa risasi mbili na kumuacha akitumbukia korongoni peke yake…” Brian alimjibu mwenzake huku akionyesha wazi kuwa alikuwa amevutiwa sana na kile kitendo cha yule mpelelezi mzoefu. Inspekta Dilunga alitabasamu kidogo.

“Lakini ingeleta maana kama angalau angetiwa mbaroni…sasa ametoweka tena. Amewezaje lakini mbwa yule…?” Alisema huku akimtazama Brian kwa makini.

“Mnh, Inspekta utata mbona bado uko pale pale? Hicho kinabaki kuwa kitendawili kikubwa…”

“Nimeona tangazo lako gezetini…that was very smart of you… yaani ulichofanya ni kumtia ghadhabu ili akurupuke…” Dilunga alisema huku akionekana kuwa mjadala ule ulianza kumtia bashasha.

“Ama! Kumbe ulielewa maana yangu katika lile tangazo, eenh…?” Brian alimuuliza kwa mastaajabu kidogo. Dilunga alitaka kuongea zaidi lakini muda huo Superintendent Tib Haggard akamgeukia Dilunga.

“Pole sana kamanda…” Alimwambia.

“Ah, n’shapoa afande…vipi kuna habari zozote mpya juu ya John Smith?” Dilunga alimjibu bosi wake na kumtupia swali, macho yake yakitembea baina ya Tib Haggard na Brian Koba.

“Ohooo, wewe sasa achana kabisa na mawazo ya John Smith, zingatia nafuu na afya yako Dilunga, sawa? John Smith sasa ni jukumu la jeshi lako la polisi, uliyoyafanya mpaka sasa yanatosha sana kukufanya utulie na kujiangalia afya yako….” Tib alimjibu kwa hamasa kidogo. Dilunga na Brian alitazamana na Brian akatazama pembeni.

“Eti…!Hata mimi namueleza hilo hilo lakini hanielewi…” Mama Sikudhani mke wa Inspekta Dilunga naye aliongezea.

“Ni sawa hayo usemayo afande…lakini mkumbuke kuwa huyo John Smith, laana za mwenyezi Mungu zimuangukie, ndiye aliyenifanya hivi jamani…hivyo nina haki ya angalau kutaka kujua iwapo amepatikana au la!”

Dilunga alijibu kwa sauti yenye mchanganyiko wa hisia, na hali mle wodini iliingia ubaridi wa nafsi kidogo.

Tib Haggard na Brian walitazamana, kisha Tib alikohoa kidogo na kumjibu.

“Okay, uko sahihi Inspekta…John Smith bado hajapatikana. Msako bado unaendelea, ingawa sasa tunategemea kuwa ni yeye ndiye atakayekuja kumsaka Brian hapa…na ndipo tunapotarajia kumnasa.Isikupe tabu sana kamanda…”

Dilunga hakujibu kitu ingawa uso wake ulionesha kuwa hiyo ilimpa taabu sana. Na muda huo mmoja wa wahudumu wa pale hospitali aliingia mle wodini.

“Kuna simu ya Inspekta Brian…” Aliarifu. Brian na Tib Haggard walitazamana, kisha Brian akamuuliza yule mhudumu

“Kutoka wapi?”

“Ni Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya…ofisini kwenu…” Mhudumu alijibu, na Brian alimgeukia mkuu wao wa kazi. Tib Haggard alimuashiria kwa kichwa kuwa aende kuongea na hiyo simu naye akatekeleza.

“Yes… Brian Koba hapa…”

“Afande unahitaji kuja kituoni…kuna habari za John Smith.” Askari wa zamu alimjibu na Brian hakusita.

“Nakuja!”


Inspekta Brian Koba na superintendent Tib Haggard waliingia ndani ya jengo la Makao Makuu ya polisi ya Wilaya ya Kisarawe na kupitiliza moja kwa moja hadi ofisini kwa Inspekta Dilunga. Tib Haggard aliketi kwenye kiti kilichokuwa nyuma ya meza ya Inspekta Dilunga, wakati Brian Koba akichukua kiti kilichokuwa mbele ya meza ile na kukivutia kando ya meza ile na kuketi. Aliinua simu iliyokuwa juu ya meza ile na kuongea.

“Walete…” Alisema na kuiweka tena mahala pake ile simu. Muda mfupi baadaye askari mmoja wa kike aliwaongoza mle ndani watu wawili, mzee mmoja wa makamu aliyekuwa amevaa kanzu na koti, kichwani akiwa na barghashia na mkononi akiwa na fimbo ya kutembelea, na mwanamke mmoja kijana akiwa amejitanda khanga mwilini.

Yule askari aliwaelekeza wale wageni wawili waketi kwenye viti vilivyokuwa mle ndani kisha naye alikwenda kuketi kwenye kona kabisa ya chumba kile, ambako kulikuwa kuna meza ndogo na kiti, juu ya meza ile kukiwa na mashine ya kupiga taipu. Alijiweka sawa nyuma ya ile mashine vidole vyake vikiwa tayari kuchapa kila kitakachoongelewa mle ndani. Hii ndio ilikuwa kazi yake.

Muda wote huu wale askari wawili walikuwa wakiwatazama wale watu wawili walioletwa mle ndani, na baada ya kuona kuwa yule askari wa kike ameshajiweka sawa nyuma ya ile mashine Brian Koba alianza kuongea na wale watu, akielekeza akauli yake kwa yule mzee.

“Ndio mzee, mimi ndio Inspekta Brian Koba… na huyu ni mkuu wetu wa kazi, Superintendent Tib Haggard. Nimeambiwa kuwa umekuja hapa kuonana nami kuhusiana na mhalifu John Smith…”

Yule mzee aliafiki kwa kichhwa, kabla ya kuongea

“Ahsante sana ma-Inspekta. Mimi naitwa Mzee Chopa natokea kijiji cha Shugubweni, wilaya ya Mkuranga, na huyu binti hapa anaitwa Mwajina Mfaume…mke wa Jadu Mfaume.”.

Tib Haggard na Brian Koba walitazamana.

“Jadu Mfaume?” Brian alimuuliza na yule mzee alitoa kipande cha gazeti kutoka kwenye mfuko wa koti lake, ambacho kilikuwa kimefinyangwa-finyangwa, na kukiweka juu ya meza.

“Huyu mtu ambaye mmetoa habari zake gazetini kuwa anatafutwa kwa kuhusika na vifo?” Mzee alisema huku akiwatazama wale askari kwa macho ya kuuliza.

“Anhaa…John Smith…?”

“Hapana, huyu ni Jadu Mfaume…ndio jina lake. Na huyu hapa umuonaye ndiye mkewe…tumekuja hapa baada ya kuona tangazo hili kwenye gazeti.” Ukimya ulitanda mle ndani wakati wale askari wakiichekecha ile taarifa vichwani mwao huku wakimtazama yule mzee.

“Na tumeonelea bora tuje tuongee nawe moja kwa moja Inspekta, kwani kama huyu mtu hapa ndio huyo Jadu Mfaume tuliyekuwa naye sisi huko Mkuranga, basi kuna haja ya kuwafahamisha zaidi khabari zake…” Mzee Chopa aliendelea baada ya kuona wale askari wamepiga kimya.

Tib Haggard na Brian Koba walitazamana. Hii ilikuwa habari muhimu sana kwao, na hawakuamini masikio yao.

“Una hakika kuwa huyu mtu ndiye mume wako bibie?” Tib Haggard alimuuliza yule mwanamke huku akiioneshea ile picha ya kuchorwa iliyokuwa pale juu meza.

“Ndi…ndiyo, kwa mujibu wa hiyo picha uliyochorwa gazetini, huyo ndiye hasa mume wangu na nimeshitushwa sana kuona ametolewa gazetini kuwa anatafutwa na polisi.”

“Okay, nadhani tungeanza kwa kusikia upande wenu wa maelezo kwanza… kwa nini mzee Chopa unasema kuwa kuna haja ya kutufahamisha zaidi juu habari za huyu mtu?” Brian Koba aliuliza wakati yule askari kwa kike akiendelea kuchapa mashine kila kilichokuwa kikiongelewa mle ndani.

Ndipo ndani ya saa mbili zilizofuata, Mzee Chopa alipowaelezea wale askari mambo yote yaliyotokea kule mkuranga siku ile kilipoonekana kitu cha ajabu kikianguka kutoka angani na kutumbukia baharini, kikimzamisha baharini Jadu Mfaume na wavuvi wenzake wawili kabla ya Jadu kuibuka kimaajabu na kurudi kijijini kwao, ambako aliacha maajabu makubwa zaidi kisha akatoweka.

Wale askari walibaki hoi.

Inspekta Brian Koba alikunja uso kwa tafakuri, kabla ya kumuuliza yule mzee.

“Mzee unasema tukio hilo la kitu kutumbukia baharini lilitokea siku gani?”

“Siku ya sherehe za uhuru…hilo nina uhakika nalo kabisa.”

“Ah!” Brian alimaka.

“What?” Tib alimuuliza huku akimtazama kwa uso uliojaa maswali mengi.

“Mnh, Afande…usiku ule nilikuwa kiwanjani wakati sherehe zinaendelea, na nilishuhudia kwa macho yangu kikianguka kitu kutoka angani kikitoa mwanga mkubwa na taa zote pale uwanjani zilizimika kwa muda, kisha kile kitu kikapoteaa tu!”.

“Ah, sasa…?”

“Inaniwia ngumu kuamini lakini hii inaniletea picha kuwa kile kitu tulichokiona pale uwanjani usiku ule, ndicho kilichoangukia baharini huko Mkuranga…”

“Na ndicho kilichomfanya Jadu awe hivyo alivyo sasa wazee…” Mzee Chopa alidakia, na kuendelea “…nimekuwa nikiwaambia wanakijiji wenzangu pamoja na Mwajina kuwa kile kitu kilichotumbukia baharini kinahusika sana na mambo yote haya, kuwa ni wazi kwamba Jadu Mfaume tuliyemtambua sisi alizama baharini na wavuvi wenzake siku ile, lakini aliyeibuka kutoka mle baharini, hakuwa Jadu tuliyemjua sisi, kilikuwa ni kiumbe tu cha ajabu kilichochukua wajihi na dongo la Jadu…”

“Ah, kwa hiyo, haya matukio mawili yanahusiana kwa namna fulani…” Superintendent Tib Haggard alisema kwa sauti ya chini.

“Yaani hilo ndilo wazo linalokuja akilini mwangu afande…” Brian alimjibu, na kimya kikatawala tena mle ndani, isipokuwa kwa ile sauti iliyotokana na yule askari wa kike kugonga mashine kwa nguvu na kasi.

“Je, kuna picha yoyote ya huyo Jadu, ambayo alipiga kabla ya kutoweka kwake huko kijijini…?” Tib alimuuliza Mwajina.

“Hapana afande…”

“Picha itoke wapi kijijini kule afande?” Mzee Chopa alidakia.

“Mna cheti cha ndoa labda, au…”

“Ndio.” Mwajina alijibu na kuchomoa bahasha iliyokunjwa mara kadhaa kutoka kwenye sidiria yake, na kutoa ndani yake cheti cha ndoa. Brian alikipokea na kukitazama kwa muda. Ni kweli kabisa jina la muoaji lililoonekana pale kwenye cheti lilikuwa ni Jadu Mfaume, kazi mvuvi. Kisha sehemu ya saini ya muoaji na muolewaji zote zilikuwa zimewekwa alama za dole gumba. Alimpa Tib Haggard kile cheti ili naye akitazame.

Baada ya kukitazama kile cheti, Tib aliamuru kitolewe nakala, na muda huo huo wakaitwa wale askari waliochukua alama za vidole vya yule mhalifu ambaye sasa waliambiwa kuwa alikuwa anaitwa Jadu Mfaume ili walinganishe ile alama ya dole gumba iliyokuwa kwenye kile cheti cha ndoa.

Jibu lilikuja dakika kumi baadaye.

Alama ya dole gumba la muoaji iliyokuwa kwenye kile cheti cha ndoa, na zile zilizokutwa kwenye lile gari alilokuwa akijaribu kutoroka nalo mhalifu aliyejulikana kama John Smith zilikuwa zinalingana kwa kila kitu.

Na hapo iliwafunukia wazi wale askari kuwa John Smith, alikuwa kwa hakika, ni Jadu Mfaume.


Kukiwa hakuna jipya zaidi ya yale waliyoyapata kutoka kwa Mzee Chopa na Mwajina Mfaume, Superintendent Tib Haggard aliinuka na kumpa mkono yule mzee kwa kumshukuru.

“Mzee Chopa, kwa niaba ya jeshi zima la polisi, nakushukuru sana wewe na Bi. Mwajina kwa uzalendo wenu wa kuja na taarifa hii muhimu sana kwa jeshi letu la polisi. Ahsanteni sana kwa kweli.”

Mzee Chopa aliupokea ule mkono huku naye akisimama

“Shukurani ni zetu sisi kwa kutupokea, kutusikiliza…na kutuamini, kwani taarifa za Jadu zinaonekana ngumu sana kuaminika…” Mzee Chopa alijibu.

“Sio kwa sisi tuliokutana na kupambana naye uso kwa uso, kwetu kila mlichotueleza kimekuwa na maana sana, na kimetuwezesha kumuelewa zaidi huyu mtu anayepita kwa jina la Jadu Mfaume.” Brian Koba alimjibu yule mzee na alijikuta akipeleka jicho kwa Mwajina pale alipotaja jina la yule Mhalifu. Na aliona kuwa yule mwanamke alikuwa akipata wakati mgumu kuukubali ukweli kuwa yule mtu aliyekuwa akimtambua kama mumewe, hakika hakuwa mumewe na badala yake ni kiumbe cha ajabu kilichochukua umbo na wajihi wa mumewe.

“Lakini Inspekta hakuna namna ya kuchunguza zaidi juu ya hilo? Hakuna uwezekano kuwa huyu…mtu…akawa mwingine tu na Jadu wangu akawa…” Mwajina aliuliza huku akiwatazama wale askari mmoja baada ya mwingine kwa wasiwasi, lakini kabla kauli yake haijaisha, Mzee Chopa akadakia huku akimtupia jicho la pembeni.

“Chini ya bahari…? Jadu tumjuaye Mwajina hayupo tena duniani! Hili lililopo ni kama jipepo tu lililouingia mwili wake kutoka huko baharini…we’ unadhani mambo aliyowafanya hawa maaskari mpaka kufikia kumnadi magazetini namna hii ni madogo? Wacha bwana! Tena nakuasa kwa mara nyingine mjukuu wangu, hata akikutokea tena usije ukampokea ukiamini ni mumeo…” Mzee Chopa alimng’akia Mwajina kwa jazba mbele ya wale askari.

Askari walitazamana. Mwajina alimtazama mzee Chopa kwa fadhaa, machozi yakimlenga.

“Sasa jamani Mzee Chopa…” Alianza kusema na Supentendent Tib Haggard alidakia.

“Mzee yuko sahihi kabisa bibie…sisi tutaendelea na msako wetu na tuna hakika kabisa tutakapo mpata, tutaweza kujua ukweli juu ya hayo mashaka yako.”

“Naam…” Brian alidakia, “…ila kwa sasa bibie, tunakuomba umchukulie huyo mumeo Jadu kuwa ni mhalifu mpaka hapo itakapo thibitishwa vinginevyo. Kwa hiyo ikitokea akakujia au akawasiliana nawe kwa namna yoyote ile, haraka sana wasiliana na uongozi wa kijiji…Sawa ?” Alimalizia kwa msisitizo.

Mwajina aliwatazama wale wanaume waliokuwa mle ndani huku akibubujika machozi .

Dakika tano baadaye, Mzee Chopa na Mwajina walipanda gari la polisi lililowarudisha Mkuranga, pamoja nao, walikuwako askari wawili waliopewa uhamisho wa papo kwa hapo kwenda Mkuranga ambako walitakiwa kuweka ofisi yao ya muda kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Jukumu lao lilikuwa ni kusubiri iwapo mhalifu Jadu Mfaume atatokea tena kule Shungubweni, au iwapo atajaribu kuwasiliana na Mwajina, wapokee taarifa hizo kutoka kwa Mwajina au yeyote atakayemuona Jadu kule Shungubweni, na kuziwasilisha kwa Inspekta Brian Koba.

Wakati Mwajina na Mzee Chopa wakirudishwa Mkuranga, huku nyuma mjadala mzito ulipita baina ya Brian Koba na Superintendent Tib Haggard.

Muda mfupi maadaye ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya mjadala ule, muandishi Bruno Mgimba aliingia akitweta pale ofisini. Alipewa maelezo juu ya habari za utambulisho rasmi wa yule mtu ambaye hapo awali alitambulika kama John Smith.

“Tunahitaji tangazo litoke tena gazetini likimnadi huyu mhalifu kwa jina lake halisi, Jadu Mfaume. Hii peke yake itawaonyesha wananchi kuwa jeshi la polisi linapiga hatua katika uchunguzi…” Tib haggard alimwambia Bruno na kuongeza, “…halafu na lile tangazo la Brian lirudiwe tena, ila safari hii utoe jina la John Smith na uweke Jadu Mfaume…”

“Okay Sir…” Bruno Mgimba aliafiki kwa bashasha, na kuongezea, “Je, hakuna habari zingine juu ya huyu mhalifu zaidi ya kujua hilo jina lake halisi…?”

“Ni hayo tu kwa sasa.” Tib Haggard alimjibu huku akimtazama kwa macho makali. Ukweli ni kwamba alikuwa na hasira naye sana kwa makala zake za mwanzo kwenye gazeti lake dhidi ya jeshi la polisi, lakini alikubaliana na wazo la Brian Koba la kumtumia kwa maslahi yao nasi vinginevyo.

Bruno alimtazama yule askari, kisha akamgeukia Brian, halafu akatoka bila ya kuongeza neno zaidi, akijua wazi kuwa kuna mengi ambayo wale askari walikuwa wakimficha.

Taarifa ya habari ya mchana wa siku ile ilitangaza rasmi juu ya kutafutwa na polisi kwa mtu aitwaye Jadu Mfaume, ambaye hapo awali alitambulika kama John Smith. Uhatari wa mtu huyo ulisisitizwa tena redioni na wananchi waliarifiwa kuwa jeshi la polisi lilikuwa linaendelea na msako dhidi ya mtu huyo hatari.

Asubuhi ya siku iliyofuata, gazeti la Ngurumo lilimnadi kwa mara nyingine yule mhalifu aliyetoweka, safari hii likiujulisha umma kuwa mhalifu yule alikuwa akiitwa Jadu Mfaume.

Na kama alivyoagiza Superintendent Tib Haggard, “uchokozi” wa Brian Koba kwa Jadu Mfaume, ulirudiwa tena gazetini.

Lakini Jadu Mfaume, zamani John Smith, hakuonekana asilani.


Wiki mbili baada ya ujio wa Mzee Chopa na mke wa Jadu Mfaume mvuvi, Dr Nigel Smith aliwaruhusu wazazi wa Chambuso Mwagala kumchukuwa mwana wao aliyerukwa akili na kurudi naye nyumbani. Akili yake ilikuwa imeathirika moja kwa moja, na hakukuwa na lolote ambalo wangeweza kulifanya pale hospitali kurekebisha hali ile.

Ilikuwa ni huzuni kubwa kwa wazazi wa kijana yule muungwana, lakini hakukuwa na namna. Kibaya na kichungu zaidi kwao kilikuwa ni kule kuondoka na kijana wao aliyeharibikiwa akili bila kujua ni kitu gani hasa kilichomsababishia hali ile.

Na bado hakukuwa na hata dalili ya Jadu Mfaume

Inspekta Brian Koba alichanganyikiwa! Vipi mtu huyu atoweke moja kwa moja namna ile?

Na kadiri siku zilivyozidi kwenda ndivyo uzito wa kesi yote ile ulivyozidi kupungua.

Watu walianza kusahau juu ya mauaji yaliyotokea katika ile barabara pweke ya Kazizumbwi, na wengine wakisahau kabisa juu ya habari za mtu hatari anayetafutwa na polisi aliyejulikana kwa jina la John Smith, na baadaye kwa jina la Jadu Mfaume.

“Uko wapi Jadu Mfaume wewe? Najua kuwa unanisikia huko uliko. Jitokeze basi japo mara moja tu tupambane kimburu wewe…!” Brian alijikuta akisema peke yake ofisini kwake wiki ya tatu ilipoingia bila ya mtu yule kuonekana wala kuibuka na kufanya kituko kingine tangu siku ile alipoonekana kwa mara ya mwisho akiporomokea korongoni.

Brian hakujua kuwa askari wenzake walikuwa wakimuona akiongea peke yake akiwa mle ofisini, jambo ambalo aliondokea kulifanya mara kwa mara baada ya hapo.

Sasa taarifa zilianza kuzagaa baina ya askari wa ngazi za chini pale Kisarawe kuwa Inspekta Brian Koba alikuwa anaelekea kupata wazimu kutokana na ile kesi ya Jadu Mfaume.

Ilipoingia wiki ya nne, Dokta Nigel alistaafu ile kazi ya utabibu pale Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, na kurudi kwao Uingereza, kumalizia siku zake zilizobakia hapa duniani, akiiacha Hospitali katika mikono ya Dokta Shabbir.

Inspekta Gezza Dilunga alitolewa hospitali akiwa kwenye kiti cha matairi. Ingawa aliambiwa kuwa ataweza kutembea tena, aliambiwa atahitaji kuwa kwenye kiti cha magurudumu kwa muda mrefu kidogo kabla hajarudia tena kusimama kwa miguu yake kama zamani.

Na Jadu Mfaume hakusikika tena.

Ndipo Inspekta Brian Koba, zikiwa zimebaki siku mbili tu kutimia wiki tano bila kuonekana wala kusikika kwa Jadu Mfaume popote pale nchini, alipopokea simu kutoka Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam.

“Inspekta Brian Koba…” Aliongea kwenye simu ile aliyoipokea akiwa ofisini kwa Inspekta Dilunga, ambako kufikia muda huu ilikuwa ndio ofisi yake.

“Inspekta…unahitajika makao makuu haraka sana…Superintendent Haggard anataka kukuona leo hii hii, mara moja!” Katibu muhtasi wa Superintendent Tib Haggard alimuambia kutokea upande wa pili wa simu ile.

“Kuhusu nini tena…? Mi’ bado niko na kesi ya Jadu Mfaume…”

“Na unaitwa huku kuhusiana na hiyo hiyo kesi ya Jadu Mfaume, Inspekta…”

“Kuna jipya? Na kama kuna jipya kwa nini Super asinipe habari kwenye simu kama ilivyokuwa hapo awali, na badala yake anitake nije huko?” Brian aliuliza, hisia zake zikiwa makini sana.

“Hivi tuongeavyo Superintendent Haggard yuko kwenye kikao kizito na wakuu wengine wa jeshi afande…alichofanya ni kuchomoka mara moja kutoka kwenye kikao hicho na kunipa maagizo kuwa nikupigie simu kukuita jijini…”

Mnh, nini tena…?

Brian alitaka kumsaili zaidi yule afande wa kike, lakini alijua kuwa atakuwa anamuonea bure tu.

“Okay…nakuja…” Alijibu na kukata simu.


Inspekta Brian alipitiliza moja kwa moja hadi ofisini kwa Superintendent Tib Haggard, na kumkuta yule katibu muhtasi wa Tib Haggard nje ya chumba ambacho kilikuwa ndio ofisi ya Tib Haggard.

“Ingia tu moja kwa moja afande…alikuwa akikuulizia sasa hivi!” Yule dada alimuambia, na Brian alizidi kujawa na udadisi juu ya hicho alichoitiwa ghafla na kwa uharaka namna ile kuhusiana na ile kesi ya mhalifu Jadu Mfaume.

Je, Jadu amejisalimisha…?Au mwili wake umekutwa sehemu akiwa amekufa? Ni nini hasa…?

Aligonga mlango kidogo, kisha akausukuma na kuingia ndani ya ile ofisi ya mkuu wake wa kazi, mkoloni Tib Haggard, ambaye alimkuta akiwa ameketi nyuma ya meza yake kubwa, akipitia faili moja lenye ukubwa wa wastani.

“Jambo afande…!” Brian alisaluti kumsalimu.

“Brian…!” Tib aliinua uso huku akilifunika lile faili lililokuwa mbele yake naye akiinuka na kumpa mkono yule Inspekta kijana.

Brian alipokea mkono wa bosi wake na wakati huo huo akiketi kufuata ishara aliyopewa na Tib Haggard. Mara moja macho ya Brian yalitua kwenye lile faili lililokuwa mbele ya Superintendent Tib Haggard, na hisia zake za udadisi zilizidi kusisimka baada ya kuona kilichoandikwa juu ya faili lile kwa hati kubwa kabisa.

UTATA.

Hicho tu basi…UTATA.

“Ndio afande, nimeitika wito wako…” Brian alimuambia bosi wake.

“Ndio Brian…nimekuita. Na sababu ya kukuita…” Tib alisema huku akisogeza faili jingine jembamba lililokuwa pale mezani na kuliweka juu ya lile faili la kwanza lililoandikwa UTATA, kisha akatoa karatasi moja kutoka kwenye lile faili la pili na kumkabidhi Brian, “…ni hii…”

Brian aliipokea ile karatasi huku akiitazama kwa udadisi mkubwa, wakati Tib Haggard akijiegemeza kwenye kiti chake na kumtazama kwa makini yule Inspekta kijana machachari. Brian aliitazama ile karatasi na kugundua kuwa ilikuwa ni barua ya kiofisi, aliyoandikiwa yeye.

Alianza kuisoma taratibu, na kadiri alivyokuwa akiisoma ndivyo alivyojikuta akishindwa kuamini alichokuwa akikisoma.

Ile barua ilikuwa ikimthibitisha kwenye cheo chake kipya cha u-Inspekta kuanzia tarehe ya barua ile. Aidha ilikuwa ikimpa majukumu mapya, kuanzia tarehe ya barua ile, kuwa mkuu wa kituo kidogo cha polisi cha Chilambo, kilichokuwa mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, huko Mtwara.

E bwana we!.Brian alipagawa si kidogo.

Aliinua uso wake na kumtazama Tib Haggard kwa mshangao uliochanganyika na hamaniko dhahiri.

“Khah…! Super…ni nini hii?” Alimuuliza akiwa ameiweka mezani ile barua na akiioneshea kidole.

“Hiyo ni barua yako ya kukuthibitisha kwenye wadhifa wako mpya Brian, na wakati huo huo kukuhamishia Chilambo kuwa mkuu wa kituo chetu kidogo kule…” Tib alimjibu huku akimtazama moja kwa moja machoni.

“Ah, lakini Super…bado kuna hii kesi ya Jadu ambayo…”

“Imekuwa ni wiki tano sasa na Jadu hajapatikana wala hakuna dalili za kupatikana Brian…”

“Sasa si ndio maana naona kuna haja ya kuendelea kumsaka mpaka apatikane Super…? Mimi ndio ninayeijua hii kesi kwa undani kuliko askari mwingine yoyote hapa nchini kwa sasa, kwa nini msiniache niimalize…”

“Lini Brian, eenh? Wiki tano nyingine? Miezi mitano mingine? Miaka mitano mingine…mpaka lini Brian? Unadhani wewe uliajiriwa na jeshi la polisi kwa ajili ya kuutafuta muujiza uitwao Jadu Mfaume…?” Tib Haggard alimuuliza kwa ukali na jazba.

Brian alipigwa butwaa.

“Sio hivyo Super…sidhani kama itachukua muda wote huo…na kwa nini umenibadilikia ghafla namna hii…?”

“Hapana, kwa kumbukumbu zangu ni wewe ndiye uliyenibadilikia. Nakumbuka nilipokuita hapa ofisini wiki tano zilizopita na kukutuma kazi ya kwenda Kisarawe hukuonekana kuifurahia kabisa, lakini sasa hiyo kazi ndiyo imekupa u-Inspekta, na sasa inakupa majukumu mengine makubwa zaidi ya Ukuu wa Kituo. Lakini kwa kukujibu swali lako ni kwamba nimekubadilikia, kama mwenyewe unavyodai, kutokana na maamuzi ya ngazi za juu kuhusiana na kesi hii Brian. Maamuzi yamepitishwa kuwa iwe hivyo inavyoelezwa kwenye hiyo barua.

“Wewe kama askari uliyekula kiapo cha utii wajibu wako ni kutekeleza na si kutoa hoja zinazoongozwa na matakwa binafsi!” Tib alimchachamalia Brian.

Brian aliona dunia ikimgonga kutokea kila upande.

“Sielewi afande…basi si angalau ningehamishiwa huko huko Kisarawe…?” Brian alisema huku akionekana wazi kuwa lile suala lilikuwa limemchanganya.

“Si juu yako kuchagua Brian…” Tib alimjibu huku akionekana wazi kuwa hakupenda kuwa katika mjadala ule na yule kijana muda ule, ila hakuwa na budi.

“Ah, kwani nini lakini?” Brian bado hakuelewa. Tib alimtazama kwa muda kisha akashusha pumzi ndefu na kujiweka sawa.

“Sikiliza Brian…wewe sasa una miaka ishirini na minne tu, kijana na hujaoa. Ni bahati kubwa kwako kupata wadhifa huu. Tekeleza unachotumwa na jeshi lako na usahau kabisa juu ya suala la Jadu Mfaume. Nenda Mtwara, tafuta mke, oa, tulia na mkeo…fanya kazi yako kwa ufanisi…kwisha!”

“Ah, Super…yaani nisahau kuhusu Jadu tena…?”

“Jadu Mfaume ni ligi isiyo daraja lako wala langu Brian…yeye alikuja kama radi tu na bila shaka ametoweka tena kama radi itowekavyo…” Wakati akisema hayo, Tib Haggard hakujua ni jinsi gani alivyokuwa karibu na ukweli juu ya namna Jadu alivyokuja hapa duniani.

“No Sir! Hili ni kosa kubwa sana. Vipi kuhusu familia ya akina Chambuso…na Uwesu, na Esmund, eenh? Vipi kuhusu Mzee Malambi na mkewe na yale yaliyomkuta binti yao Huba…? Huoni kuwa wote hawa wanastahili kujua juu ya nini hasa kilichowakuta wapendwa wao…?” Brian alimaka huku akiinuka kutoka kwenye kiti alichokuwa amekalia.

“Sit Down Brian!” Tib Haggard alimkemea, kisha akaendelea, “Hii kesi si yako tena, na hii ni kwa usalama wako mwenyewe…sasa umeanza kuongea peke yako Brian, unaelekea kwenye kuingiwa wazimu kwa kesi hii, ambayo haijulikani ni lini itatatuliwa…ni utata mtupu! Sasa kabla hujapata wazimu, bora uelekeze akili yako katika mambo mengine…”

“Akh, sina wazimu afande…mi’ naongea na Jadu Mfaume, kwani nina hakika kuwa ana uwezo wa kunisikia…huenda hata sasa ananisikia…anatusikia…”

“Na huo ndio mwanzo wa wazimu Brian, amini usiamini. Na ndio maana pamoja na barua hiyo niliyokupa mwanzo…” Tib alisema na kutoa barua nyingine kutoka kwenye lile faili la pili na kumkabidhi, “…nakupa na barua hii vile vile…”

Brian alishangaa huku akiipokea ile barua ya pili na kuisoma haraka haraka.

Ilikuwa ni barua iliyompa likizo ya mwezi mmoja kabla hajaripoti kwenye kituo chake kipya cha kazi. Likizo ile ilikuwa inaanzia siku ile ile aliyokuwa akiongea na Superintendent Tib Haggard.

Brian alichoka!

“Ah, sasa…sasa ni nani atakayeendelea na kesi ya Jadu, Super? Inspekta Dilunga hawezi kufanya lolote sasa hivi…”

“No one!” Tib Haggard alimjibu huku akimtazama usoni.

“Whaaaaaaatttt?” Brian alimaka huku akimuinamia mkuu wake wa kazi kwa mshangao usio kifani. Tib Haggard alibaki akimtazama bila ya kusema neno, akijua wazi kuwa Brian alikuwa amemsikia, ila alitaka tu kusikia tena jibu alilopewa.

“Kwa nini Super…mbona sikuelewi?” Hatimaye Brian aliuliza huku akiketi tena kwenye kiti. Tib Haggard alikohoa kidogo na kujiweka sawa kwenye kiti chake, kisha akamjibu.

“Kwa sababu kesi ya mauaji ya Kazimzumbwi, inayomuhusisha mtu aitwaye Jadu Mfaume imefungwa.”

“Eeenh?”

“The Case is closed Brian!” Tib alimsisitizia.

Brian alipumbaa kwa muda, hakuelewa hata kidogo.

“How come Super? Kesi itafungwaje afande wakati mhalifu hajakamatwa?”

“Swali zuri Brian…the case is indeed closed…” Tib alimwambia na kutulia kwa muda, macho yake yakiwa yamekamatana na yale ya yule askari kijana mwenye ari, kisha akamalizia taratibu; “…but unsolved!”

“Hah!”

“Ndiyo!”

Brian alifungua kinywa lakini akakosa la kusema. Akabaki akimkodolea macho yule mkoloni akiwa kinywa wazi.

Ama hakika duniani kuna mambo.

“Hayo ni maamuzi ya ngazi za juu kuhusu kesi hii Brian, nawe unatakiwa uyaheshimu ipasavyo…” Tib Haggard alimwambia huku akimtazama usoni kwa utulivu mkubwa.

E bwana we!

“Closed but unsolved..?” Brian Koba alijikuta akiyarudia yale maneno ya Tib Haggard bila ya kuamini.

Tib Haggard hakumjibu kitu, alibaki akimtazama huku akimpa muda ili yale maneno yamuingie vizuri kichwani yule askari.

Kimya kilitanda kwa muda mle ofisini, kisha Brian Koba aliinuka taratibu akiwa na zile barua zake mkononi, akasaluti kwa mkuu wake wa kazi, na kutoka nje ya ofisi ile kwa mwendo mkakamavu, ilhali uso wake ukiwa umefura kwa ghadhabu.


Gezza Dilunga alijua kuwa hali haikuwa sawa pindi alipomuona Inspekta Brian Koba akiingia ndani ya sebule yake

“Brian vipi…kuna nini…mbona hivyo?” Alikunja uso kwa mshangao na kumuuliza kwa kiherehere huku akisukuma kiti chake kwa matairi kumsogelea pale alipokuwa amesimama hatua chache ndani ya mlango wa sebule ile.

Inspekta Brian Koba alimtazama yule askari mzoefu ambaye alikuwa na hati-hati ya kuwa kilema kwa maisha yake yaliyobakia kutokana na kulitumikia jeshi la polisi la nchi yake huru, na roho ikazidi kumuuma.

Mama Sikudhani, mke wa Inspekta Dilunga aliinua uso wake na kumtazama yule askari kijana mara moja tu na kuona kuwa hali haikuwa salama kabisa. Inspekta Brian Koba alikuwa amebadilika kiasi cha kukosesha amani.

Macho yalikuwa yamemuiva, mishipa ya kichwa ikiwa imemtutumka na ghadhabu za wazi zilikuwa zikionekana usoni mwake.

“Heh, shemeji…kulikoni tena?” Aliuliza kwa mshangao wakati mumewe akiendelea kumtazama yule askari mwenzake kwa uso uliojaa maswali mengi.

Brian alibaki kimya kwa muda. Ukweli ni kwamba alitaka kusema kitu lakini ghadhabu ilikuwa kubwa sana kiasi kwamba kauli ilimkwama kooni. Badala yake aliingia ndani ya sebule ile na kujibweteka kwenye kochi lililokuwa karibu yake, akatoa kitambaa na kujifuta jasho usoni, kisha akakohoa kidogo kuweka koo lake sawa, kabla ya kuongea kwa sauti iliyokwaruza, kauli yake akielekeza kwa mke wa Dilunga.

“Shemeji naomba utupe nafasi kidogo nahitaji kuongea na Dilunga…”

“Bila samahani shemeji…” Mke wa Dilunga alisema huku akiinuka na kutoka, akiwaacha peke yao pale sebuleni.

“Nini lakini Brian? Ongea na mimi bwana, mbona hivi?” Inspekta Dilunga alimuuliza mwenzake kwa wahka.

Inspekta Brian Koba akamueleza kila kitu.

Gezza Dilunga alibaki hoi. Hakutaka kabisa kuamini alichokisikia kutoka kwa Brian.

“Khah…! Yaani, ina maana ndio jeshi limekiri kushindwa na huyu mtu kweli?” Aliuliza kwa mshangao huku akimtazama Brian kwa macho ya kutoamini.

“Tib amesema wazi afande, kuwa hii ligi siyo daraja letu…” Brian alisema kwa uchungu. Gezza Dilunga alighadhabika kuliko kiasi.

“Ah, Inspekta…sasa na mimi nime…nimelemaa namna hii bure tu…? Kweli…?” Alisema kwa uchungu huku akitikisa kichwa.

“Oh, pole sana Inspekta, nami pia nimeumizwa sana na maamuzi haya ya wakubwa wetu…ila sina la kufanya. Niliona tu nije nikupe taarifa hii na nikuage rasmi Inspekta.” Brian alimjibu kwa uchungu.

“Kwa hiyo katika kesi hii tumeshindwa Inspekta?” Dilunga aliuliza kwa kutoamini. Brian hakujibu kitu, aliuma meno kwa uchungu.

“Bidii zote tulizoweka kwenye kesi hii ziwe ni bure?” Dilunga alizidi kuuliza kwa fadhaa.

Brian aliinuka.

“Inspekta, yanipasa niondoke sasa. Sina tena sababu ya kuendelea kubaki hapa Kisarawe…lakini kama itakuwa ni liwazo, basi ni kwamba mimi naamini kuwa sisi…mimi na wewe…hatujashindwa hata kidogo katika kesi hii Inspekta.” Alimwambia

“Ah, Brian…kwangu mimi huku ni kushindwa bwana…nione hali yangu sasa…” Dilunga alisema huku macho yakimchonyota kwa machozi, kisha akaendelea, “…tumepewa kazi hatukuimaliza, nami nimeishia hali hii”.

“Ndio maana nakwambia kuwa kama kushindwa, basi limeshindwa jeshi la polisi, na sio sisi! Sisi ni mashujaa tuliokuwa tayari kuendelea na mapambano mpaka tone la mwisho la damu afande, ila jeshi la polisi limeshindwa kututumia ipasavyo.” Brian Koba alimjibu bosi wake kwa upole.

Dilunga alimtazama yule askari kijana huku chozi likimtiririka kwa uchungu na hasira, na liliendelea kumtiririka wakati akimshuhudia Inspekta Brian Koba akiingia kwenye gari lake na kuondoka kwa mwendo wa kasi kurudi jijini Dar, akiwa ameketi kwenye kiti chake cha matairi nje ya nyumba yake, mkewe akiwa amesimama nyuma yake tayari kumsukuma tena ndani kwa kiti kile…


Inspekta Brian Koba alifungua mlango wa chumba chake cha kupanga maeneo ya magomeni mapipa jijini Dar es Salaam na kuingia ndani ya chumba chake alichokikosa kwa muda mrefu. Baada ya kuagana na rafiki yake Dilunga kule kisarawe, alirejea makao makuu ya jeshi la polisi kuliacha lile gari la polisi alilokuwa akilitumia, akikabidhi ufunguo wa gari lile kwa afisa anayehusika na magari, kisha akaondoka kuelekea nyumbani kwake kwa kutumia usafiri wa basi.

Alikuwa amechoka na amefedheheka sana. Kila kitu kilikuwa kimeenda vibaya, tena kwa ghafla sana. Alitembeza macho yake mle ndani na kujutia jinsi alivyokuwa akilala kwenye kitanda kidogo cha chuma kule kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, katika mazingira magumu, wakati ana kitanda chake kikubwa tu na chenye kila aina ya raha. Eti kwa ajili ya kulitumikia jeshi la taifa lake huru (alisonya).

Alirudisha mlango ule na moja kwa moja alianza kutoa nguo zake za kiaskari, akiiweka bastola yake chini ya mto. Kisha akiwa amejifunga taulo, alichukua sabuni na kutoka nje ya chumba kile na kuelekea bafuni kuoga.

Muda wote aliokuwa akioga kule bafuni, akili yake ilikuwa ikirudia matukio mbalimbali aliyokutana nayo akiwa katika kesi ile ya ajabu na bado akili yake ilizidi kuvurugika.

Jadu Mfaume kapotelea wapi?

Kwa nini imebidi hii kesi ifungwe ghafla hivi…tena kabla ya kutatuliwa…?

Je, ni kweli kuwa alikuwa anaelekea kupata wazimu?

Brian Koba alikosa amani kabisa.

Dakika kumi baadaye alitoka bafuni na kurudi chumbani kwake, wazo pekee lililokuwa kichwani mwake ni kuuchapa usingizi mzito, baada ya hapo aelekee baa iliyo karibu achape mtindi…

Alimaliza kuonga na kurudi chumbani kwake, ambako alikwenda moja kwa moja hadi kwenye kabati lake la nguo, akilitupia kitandani taulo alilokuwa amejifunga kiunoni, akilini akiwa na lengo la kutoa bukta mle kabatini, aivae kisha ajitupe kitandani.

Hatua mbili kabla ya kulifikia kabati lile, akiwa kama alivyozaliwa, alisimama ghafla, macho yake yakinasa kwenye kioo kikubwa cha kujitazamia kilichokuwa kwenye uso wa kabati lile, moyo ukimlipuka.

Alihisi ubaridi mkali ukitembea kutokea utosini kwake, ukimtambaa nyuma ya kichwa chake, na kushuka taratibu sana kwenye uti wake wa mgongo, ubaridi ule ukiongezeka kadiri ulivyokuwa ukishuka mgongoni kwake na kutambaa hadi miguuni mwake.

Inspekta Brian Koba alipata mshtuko ambao hajawahi kuupata maishani mwake. Akili ilimsimama kwa muda na hakuamini alichokuwa akikiona pale kwenye kioo.

Aligeuka upesi kule alipotokea, uso ameukunja kwa taharuki na macho ameyatumbua kwa kutoamini, akitaka kuhakikisha kweli ile taswira aliyoiona ikiwa nyuma yake kupitia kwenye kile kioo cha kabati lake ilikuwamo mle ndani.

Naam, hakika kile kioo hakikuwa kikimdanganya, kwani alichokiona hasa kilikuwa ndicho. Na hapo mshtuko wake uliongezeka mara dufu, akabaki akikodolea macho kile alichokiona kupitia kwenye kioo, kikiwa hai kabisa mbele ya macho yake.

Jadu Mfaume alikuwa ameketi kwenye stuli ndogo kando ya mlango wa chumba kile, akimtazama kwa uso uliofanya tabasamu la kejeli kubwa.

E bwana we!

Wakati anatoka mle ndani kuelekea bafuni, ile stuli aliyokalia yule mtu wa ajabu ilikuwa katikati ya chumba kile.

Brian Koba alimtazama yule mtu kwa mshangao mkubwa, akili yake ikianza kujiweka sawa taratibu, ikijaribu kuielewa hali ile.

Jadu Mfaume! Chumbani mwangu! Jinsi gani hii..?

Jadu aliendelea kumtazama huku akitasabamu, akiifurahia ile hali ya mshtuko aliyoipata yule askari mbishi, na Brian Koba alijaribu kusema neno lakini sauti ilimkwama kooni, bado hakujua afanye nini.

Kilichotokea kilikuwa ni nje kabisa ya matarajio yake, na hakika hakuwa amejiandaa kwa hali ile. Alibaki akimkodolea macho yule mtu, sasa ikimjia wazi akilini mwake kuwa alikuwa amesimama mbele ya adui yake akiwa uchi wa mnyama.

Oh, Mungu wangu, hii ni nini sasa…

Jadu Mfaume alikuwa amevaa suruali ngumu aina ya “Lee West” ya rangi nyeusi, na fulana nyeupe yenye kola na mikono mifupi iliyomkaa vizuri sana, ikionesha misuli yake iliyotuna kijabali. Miguuni alikuwa amevaa viatu vya raba, na kichwani, nywele zake alikuwa amezinyoa katika mtindo uliomfanya aonekane tofauti kabisa na hapo awali. Kwenye sehemu vilipoishia vifungo vya ile fulana yake aliyoivaa, alikuwa amechomeka miwani myeusi ya jua, ambayo ilibaki ikining’nia kifuani mwake.

“Hey Brian, huoni haya kumsimamia mwanaume mwenzio bila nguo namna hiyo?” Hatimaye Jadu alimuuliza Brian huku akimtazama kwa kejeli.

“Jadu…! U…unataka nini kwangu?” Brian alimuuliza kwa sauti iliyokwaruza, huku akianza kuvuta hatua kusogelea kitandani kwake.

“What’s the problem Brian, hujafurahi kuniona? Si ndiye uliyekuwa ukinitafuta kwa hamu sana wewe, sasa tena unaniuliza ninataka nini kwako? Mbona sikuelewi?” Jadu alimuuliza taratibu, huku bado uso wake ukifanya tabasamu la kejeli.

Brian alizinduka.

Kwa hatua moja kubwa alijitupa kitandani kwake, akiupiga kofi mto uliofunika bastola yake pale kitandani kwa mkono mmoja huku kwa mkono mwingine akiikwapua ile bastola naye akipindukia upande wa pili wa kitanda na kubaki akiwa amepiga goti upande wa pili wa kitanda na wakati huo huo akiwa amemuelekezea bastola yake yule mhalifu kwa mikono yake yote miwili .

“Tulia hivyo hivyo Jadu! Uko chini ya ulinzi, na hii ni ile ile bastola yangu yenye…” Briani alianza kumfokea, lakini Jadu alimkata kauli kwa kebehi.

“Risasi za kulipuka?”

Brian alimtazama kwa mshangao kidogo, kisha akafunua kinywa chake kutaka kumkemea tena, lakini kauli yake iliishia kwenye mguno wa mshangao pale alipoona Jadu Mfaume akimfunulia kiganja cha mkono wake na kumuonesha risasi za bastola ile.

“Kama hizi Brian…? Au kuna nyingine?” Jadu Mfaume alimuuliza, bila kufikiri Brian alibonyeza kifyatulio cha ile bastola ikiwa bado imemuelekea Jadu.

Kwacha!

Patupu.

Ah!

Aliinua uso wake kumtazama yule mhalifu kwa mshangao. Kumbe Jadu alishazitoa risasi kutoka kwenye ile bastola, na kisha akaiacha pale pale ilipokuwa imefichwa hapo awali.

Brian alichanganyikiwa.

Jadu aliinuka kutoka pale kwenye ile stuli na wakati huo huo akizitupa sakafuni zile risasi, sasa uso wake ukiwa umefuta kabisa lile tabasamu lake la kejeli na kumsogelea Brian pale kitandani huku akitoa kipande cha gazeti kutoka kwenye mfuko wa nyuma wa suruali yake.

“Ulitaka nijisalimishe, au kama sitajisalimisha na nataka kuendelea na udhalimu wangu, basi nianze na wewe Brian…sasa ndio nimekuja, utafanyaje?” Jadu alimuuliza kwa hasira huku akikipungapunga kile kipande cha gazeti kilichokuwa na lile tangazo la pili na Brian Koba lililotoka gazetini wiki kadhaa zilizopita.

Brian alimtazama yule mtu kwa hasira.

“Sasa ndio umekuja kujisalimisha au…?”

“Nijisalimishe kwako mpumbavu wewe? Nimekuja kukuanzia wewe kama ulivyotaka kwenye gazeti lako…unajua huu ujumbe wako umenikera sana?” Jadu alimuambia kwa hasira.

Good, kumbe nilikuwa sahihi…

“Sasa ulikuwa wapi siku zote hizo, muoga mkubwa wewe?” Brian naye alimtemea maneno ya ghadhabu.

“Nilikuwa nasubiri siku inayofaa kuja kukutia adabu mjinga wewe, unasema nimekuja kufanya udhalimu hapa? Unajua ninachokifanya hapa mimi wewe?”

“Sasa kwa nini usinielimishe juu ya nini unachotaka kwa Chambuso Mwagala, na unahusika vipi na kisa chote cha mauaji ya Kazimzubwi? Huenda tukawa marafiki baada ya hapo…”

“Sasa nikuelimishe kama nani? Kesi imeshafungwa, na wewe umeshaondolewa kwenye hii kesi…”

“Hah…?”

“Ng’waa nini? Mimi ndio Jadu Mfaume bwana! We funga safari tu uende Mtwara huko ukaoe watoto wa kimakonde! Hii ligi si daraja lako…si ndivyo ulivyoambiwa na wakuu wak…”

“MWANAHARRAAAAMMM…!” Brian aliruka mzima mzima kutoka upande upande wa pili wa kile kitanda huku akimtupia tusi la ghadhabu yule mtu wa ajabu, na kumshindilia kichwa kwa nguvu usoni.

Jadu hakuwahi kumalizia kauli yake ya kebehi, na badala yake alishtukia akishindiliwa “ndosi” ya nguvu, mguno wa maumivu ukimtoka naye akisukumwa nyuma, Brian akiwa amemng’ang’ania mabegani.

Wote wawili walipiga mwereka upande mwingine wa kile kitanda na kubingirika sakafuni.

Jadu alijitupa wima na kusimama haraka, lakini Brian aliyepandwa ghadhabu alikuwa mwepesi zaidi.

Alimrukia na kumtandika teke la uso, na Jadu akayumba huku mguno mwingine ukimtoka. Haraka Brian alimtandika teke la pili lililokuwa limeukusudia uso wake kwa mara nyingine, lakini Jadu naye alikuwa amejiweka sawa sasa. Alimdaka ule mguu, na hapo hapo akimpiga kwa nguvu kwa kitako cha kiganja chake sehemu za siri.

Brian alipiga ukelele mzito, maumivu makali kuliko kawaida yakiutawala mwili wake wote huku akihisi kuwa ameshavunjwa kizazi. Pigo lile lilimtupa nyuma na kumpigiza tena kwenye upande wa kitanda chake kabla ya kuanguka tena sakafuni.

“Shezi taipu, unadhani utaniweza mimi wewe?” Jadu alimfokea kwa hasira.

Brian alijaribu kujiinua lakini alishindwa, akaanguka tena sakafuni. Akabaki akitambaa huku akitweta, akihisi kutapika na fahamu kumhama.

Lile pigo moja tu la Jadu Mfaume lilitosha kummaliza nguvu kabisa. Jadu alimuinamia na kumkamata koo, kisha akamuinua uso wake na kumtazama kwa karibu, uso wake ukiwa umejikunja kwa dhadhabu.

“Naweza kukua sasa hivi Brian, tena kwa mikono yangu tu,” alimwambia, Brian alibaki akimtazama kwa fadhaa.

“…lakini sitafanya hivyo kwa sababu wewe sio kusudio la mimi kuja hapa duniani kwenu…na pia nataka uendelee kuishi na uchungu wa kushindwa kunikamata na kunidhibiti. Najua hilo, kwa mwenye kupenda sifa na kiherehere kama wewe, ni bora kifo…” Alimwambia huku akiwa amembinya koo kiasi cha kumkosesha pumzi. Brian alijitutumua bila mafanikio, hadi pale Jadu alipomuachia koo na kusimama mbele yake.

Brian alitweta huku akijizoazoa pale chini.

“U…unataka ni..nini wewe lak…kini…?” Hatimaye alimuuliza kwa taabu.

Jadu Mfaume alimtazama kwa muda, kisha akaguna na kuketi tena kwenye stuli aliyokuwa amekalia hapo awali.

“Sasa umekwisha Brian…huna kitu tena. Hakuna atakayekuamini asilani. Mtu unakaa unasema peke yako, hata wakuu wako wa kazi hawana imani na wewe…mwenyewe unaamini kuwa unaniongelesha mimi, na kweli nimekuwa nikikusikia, lakini nani atakuamini? Kwa hiyo hata nikikujulisha nikitafutacho hapa duniani haitakuwa na faida yoyote kwako wala kwa kwa hao wakuu wako wa kazi wanaokuona kuwa tayari umesharukwa na akili kama Chambuso Mwagala na Mzee Malambi…”

“Niambie nijue tu…ni muhimu kwangu kujua…” Brian alimwambia kwa taabu, maumivu ya ajabu yakimtawala sehemu zake za siri. Alijivuta hadi kitandani kwake na kujifunika taulo.

“Nitakuambia kitu kimoja tu Brian Koba mjinga…kuwa hawa viumbe niwasakao mimi hapa duniani hakuna binadamu yeyote atakayewaweza isipokuwa mimi…au mtu mwingine kama mimi. Na kwa hakika ninyi mnatakiwa mnishukuru sana mimi kwa kuwawinda vuimbe hawa, na nitakapowapata na kuwaangamiza, nitakuwa nimeifanyia fadhila kubwa sana jamii yenu ya kibinadamu…”

“Sikuelewi…” Brian alisema huku akimtazama kwa taabu, akihisi macho yake yakipoteza nuru.

“Tangu lini mwendawazimu akaelewa kitu anachoambiwa Brian? Nina kazi ya kufanya, ila nilitaka tu kukuonesha kuwa bado nipo, na nitaendelea kuwepo mpaka kazi yangu itakapoisha hapa duniani. Kwa heri.” Jadu alimjibu huku akiinuka na kuweka miwani yake usoni.

“Noo! Usiondokeee…” Brian aliruka kutoka pale kitandani, bastola yake ikiwa mkononi.

Jadu Mfaume alifungua mlango taratibu na kutoka nje ya chumba kile.

Brian alijirusha hadi pale zilipokuwa zile risasi zake na kuzijaza kwenye ile bastola kwa mikono iliyojaa kitetemeshi, kisha alikurupuka mbio kutoka mle ndani bastola ikiwa mikononi mwake.

“Simama Jadu, ama nakupiga risa…”

“Mamaaaaaaa weeeeee….”

“Toba Yarabiiiiiii…!”

“Uuuwiii…!”

Brian alishtushwa na mayowe ya akina mama wapangaji wenzake waliokuwa pale uani wakipiga makelele, naye akabaki akiwa ameduwaa kwa muda, bastola mkononi.

Wale akina mama walikuwa wakimkodolea macho kwa mshangao na woga, wengine wakijifunika macho yao.

“Yuko wapi?” Brian alipiga kelele huku akiangaza huku na huko, asimuone Jadu wala dalili kuwa Jadu alikuwa pale muda ule.

Jadu hakuwepo kabisa eneo lile!

Akina mama walizidi kupiga mayowe ya mshangao na ndipo Brian alipogundua kuwa alikurupuka bila nguo mwilini, taulo alilojifunika nalo likiwa limeanguka chumbani kwake wakati akimkimbilia yule mtu.

Oh My God…

Brian alirudi mbio ndani kwake.

Sasa kila mtu ataamini kuwa hakika Inpekta Brian Koba amerukwa na akili.

Brian Koba alijikunyata chumbani kwake na kulia kwa uchungu mkubwa.

Jadu Mfaume alikuwa sahihi…bora ya kifo kuliko fadhaa hii…


“Ni mara ngapi napaswa niwaeleze kuwa mimi sina wazimu?” Inspekta Brian Koba aliuliza kwa jazba huku akijitahidi kudhibiti ghadhabu zilizokuwa zikimpanda kwa kasi kubwa. Walibaki wakimtazama tu bila ya kusema kitu, ingawa macho yao yalimuambia kuwa walikuwa hawamuamini hata kidogo.

Inspekta Brian Koba aliwatazama wakuu wake wa kazi na kujiuliza ni nini ingekuwa hatma yake baada ya kituko kile cha nyumbani kwake siku iliyopita.

Alikuwa amelala kitandani katika wodi maalumu ya Hospitali ya Princess Margareth, jijini Dar es Salaam. Alimtupia macho Superintendent Tib Haggard aliyekuwa amesimama kando ya kile kitanda alicholalia, kisha akamgeukia mkuu mwingine wa jeshi la polisi ambaye naye alikuwa mzungu. Aliona kuwa wote walikuwa wakimtazama kwa macho yaliyojaa masikitiko, kama jinsi watu wanavyoweza kumtazama mtu wanayeamini kuwa amepotea kabisa kimaadili au aliyepatwa na hasara kubwa.

Alihamishia macho yake kwa daktari aliyekuwa akimchunguza tangu siku iliyopita alipofikishwa pale hospitali, na kuona kuwa yule tabibu mwenye asili ya ki-giriki alionekana kuchanganyikiwa kuliko vinginevyo. Alimgeukia tena Tib Haggard.

“Hamniamini sio?” Alimuuliza kwa masikitiko.

Tib Haggard alimtazama Brian kwa huzuni na kutikisa kichwa.

“Brian, umetoka nje bila nguo…bastola mkononi, unapiga kelele ovyo kumuulizia mtu asiyekuwepo…unataka sisi tukufikiriaje?” Tib Haggard alimuuliza taratibu.

“Akh, lakini taulo lilinianguka bahati mbaya…sikuwa makini na hilo kwa wakati ule! Akili yangu ilikuwa kwa yule mhalifu tu…” Brian alijibu kwa hasira.

“Mhalifu ambaye ni wewe tu ndiye uliyemuona, watu wote waliokuwa pale nje wasimuone isipokuwa wewe tu Brian? Halafu unataka tukuamini?” Tib alimuambia kwa sauti iliyodhihirisha kuchanganywa na kusikitishwa kwake na hali ile.

“Khah, Jamani…! Jadu Mfaume alivamia chumbani mwangu, nami nika…”

“Nasikitika sana kuwa umeitia sana kichwani mwako kesi ya Jadu Mfaume, sasa inakuletea ubovu wa akili. Ingawa mwenyewe unaamini vinginevyo, lakini unapotoka nje bila nguo na silaha mkononi huku ukipiga mayowe ovyo, haimpi taabu hata mtoto mdogo kutambua kuwa kuna mgonjwa wa akili mbele ya macho yake, sembuse sisi watu wazima?” Tib Haggard alizidi kugongelea msumari wa moto kwenye kidonda.

“Nilikuwa namfukuza Jadu Mfaume afande! Mara ngapi niwaeleze jambo hilo?”

“Jadu Mfaume hakuwepo pale wala popote karibu na pale ulipokuwapo Brian!” Tib Haggard alimfokea kwa hasira.

“Hah, yaani…yaani unataka kuniambia kuwa hata wale akina mama waliokuwa pale nje hawakumuona? Haiwezekani bwana! Alitoka chumbani mwangu si zaidi ya dakika tatu ndipo nami nikatok…”

“Walichoona wale akina mama ni korodani zako tu na bastola mkononi mwako, si kingine Brian! Hakukuwa na Jadu Mfaume wala kivuli cha Jadu Mfaume pale!” Tib Haggard alimfokea.

Brian alijiinua na kumsogezea uso wake mkuu wake wa kazi.

“Sasa kama Jadu hakuwepo eneo lile unadhani ni nani aliyenifanya hivi afande?” Alimkemea huku akimuoneshea pale shingoni alipokabwa na Jadu. Alama za vidole zilionekana wazi wazi shingoni kwake.

Tib Haggard na yule askari mwenzake walitazamana, kisha wakamgeukia yule tabibu, ambaye alikohoa kidogo kabla ya kuongea.

“Swali zuri sana hilo afande…hii alama lazima itakuwa imesababishwa na mtu, na mtu huyo hawezi kuwa Brian mwenyewe…”

“Au niwaoneshe na sehemu nyingine wazee ili muamini kuwa ninajua ninachosema?” Brian aliwauliza huku akianza kujifunua shuka kuwaonesha sehemu zake za siri ambapo Jadu alimpiga kwa nguvu na kumuumiza vibaya. Sehemu ile ilikuwa imevimba vibaya sana, na yule daktari alikuwa amemchoma sindano maalumu ya kudhibiti maumivu na uvimbe.

“Haina haja Brian, daktari ameshatueleza juu ya hilo…” Yule askari mwingine aliyeambatana na Tib Haggard alidakia haraka.

“Na bado hamtaki kuamini ninayowaeleza…?” Brian aliuliza huku akitembeza macho yake baina ya Tib na yule askari mwingine. Yule askari aliyeambatana na Tib Haggard alishusha pumzi ndefu kabla ya kumuambia, “Brian, ukweli unabaki kuwa Jadu Mfaume hakuonekana kabisa eneo lote la nyumbani kwako siku ile, na sisi tumepigiwa simu na wapangaji wenzako kuwa umetoka mbio chumbani kwako bila nguo huku ukiwa na bastola mkononi…ukiuliza Jadu yuko wapi wakati wao wanakuona wewe tu…”

“Ah, sasa…”

“Sasa matokeo yake woga umeenea mtaa mzima, kuwa Inspekta Brian Koba kapata wazimu…wengine wanasema kuwa umerogwa baada ya kupewa cheo, wengine wakisema kuwa ni kutokana na kesi ya Jadu Mfaume, na sisi tunakuwa njia panda!” Tib alimjibu kwa kirefu.

Brian alichanganyikiwa.

“Kwa hiyo ndio kusema…”

“Ni kwamba hatujui ni kipi tuamini kuhusu wewe Brian, na hiyo inatufanya tuzidi kusisitiza msimamo wetu juu ya kufungwa kwa kesi hii ya utata usioisha…na wewe kukaa mbali na shughuli za kipolisi kwa muda.” Yule askari mwingine alimjibu.

“Kwa usalama wako…” Tib Haggard aliongezea huku akimpigapiga Brian begani.

Dah!

Brian aliwatazama wale wazungu akiwa mdomo wazi.

Hakika Jadu Mfaume alikuwa sahihi, hakuna yeyote anayeniamini sasa.


Jadu Mfaume alikuwa kwenye wakati mgumu. Amekuwa akijaribu kuingia akilini mwa yule kijana aliyetambulika kama Chambuso Mwagala kwa muda mrefu bila mafanikio. Kijana alikuwa amerukwa akili, na akili ya mwehu si ya kuingilika kabisa.

Ndio maana ilimlazimu amfikie yule kijana na aonane naye macho kwa macho…mano a mano…na labda, tena labda, ndipo angeweza kujua kilichokuwa kichwani mwa yule kijana, na hatimaye kujua kilichotokea kule barabarani Kazimzumbwi usiku ule.

Kutokana na jinsi alivyokuja kulielewa lile tukio la kule barabarani kupitia kwenye magazeti aliyokuwa akisoma, na hasa baada ya kuliona lile jeraha la ajabu lililokuwa kifuani kwa yule binti aliyeuawa usiku ule, ikiongezewa na mazungumzo mbali mbali aliyoyanasa kutoka kwa wale maaskari waliokuwa wakijaribu kuifuatilia kesi ile isiyo katika daraja lao kabisa, ilimfunukia mapema sana kuwa watu….viumbe…aliokuwa akiwasaka hapa duniani ndio waliohusika na tukio lile.

Kwa hiyo wapo hapa Tanganyika, na Chambuso Mwagala ndiye pekee aliyebaki hai katika wale vijana waliokumbana na mkasa ule. Sasa naye kawa mwehu! Kwa hali hiyo, ni lazima tena lazima, amuone yule kijana, tena amuone haraka, kwani tayari ameshapoteza muda mwingi.

Balaa gani hili sasa!

Alikumbuka jinsi alipojaribu kwenda kumuona yule kijana uso kwa uso kule Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, na kujikuta ametumbukia kwenye mtego kabambe wa Inspekta Brian Koba mshenzi.

“Nusura wanizime siku ile wale maaskari, pumbavu! Lakini sasa wote kwisha habari yao! Hasa Brian Koba, maana yule ndiye hasa alikuwa kipingamizi kikubwa kwenye harakati zangu.” Alikuwa amesimama upande mmoja wa barabara na kapu lake la karanga, na akiwa na mavazi yanayoendana hasa na kazi ile ya kuuza karanga. Kichwani akiwa amebandika barghashia iliyochakaa na ambayo aliilazia upande wa kushoto wa uso wake kiasi kwamba ile barghashia ilifunika kabisa nyusi ya jicho lake la kushoto. Mwilini mwake alikuwa amevaa kanzu iliyochakaa na miguuni alikuwa amechomeka makubadhi yaliyoenea vumbi.

Hakika Jadu Mfaume huyu alikuwa tofauti kabisa na yule aliyemuibukia Inspekta Brian Koba nyumbani kwake siku moja tu iliyopita. Kutokea upande wa pili wa barabara aliona kile alichokuwa akikisubiri, kwani baada ya kufanya uchunguzi kwa siku tatu mfululizo, alikuwa ameshapata taswira ya mwenendo wa taratibu za ile nyumba iliyokuwa upande wa pili wa barabara, nyumba ya Mzee Mwagala Kifyagi.

Asubuhi saa moja na nusu yule mzee hutoka na gari lake kuelekea kwenye biashara zake, akiwa na mwanae mdogo wa kike ambaye bila shaka huwa anampeleka shule. Saa tatu na nusu asubuhi, mama mmoja mtu mzima bila shaka ni mama wa mke wa yule mzee, hutoka nje na kuketi kwenye mkeka barazani na kuanza kusuka ukili. Muda huo huo, Chambuso naye hutolewa nje na wasaidizi wa kazi wa mle ndani na kuwekwa ubavuni kwa bibi yake. Yule kijana hujilaza pale mkekani, akijaza kichwa chake mapajani mwa bibi yake, na hukaa hivyo kwa muda mrefu, bila fujo wala purukushani, wakati bibi yake akiendelea kusuka ukili wake.

Jadu Mfaume amekuwa akiiona hali hii kwa siku tatu mfululizo, na kabla hajachukua hatua za kujaribu kumuingia akilini yule kijana mwehu lakini mtulivu, aliamua kwenda kumtia adabu Inspekta Brian Koba na kuondoa kabisa kipingamizi kikubwa katika harakati zake. Iwapo mpango wake huu wa kumfuata Chambuso hautafanikiwa, au kitu kitaenda kombo, basi hakutaka kabisa Brian Koba apate sababu ya kuendelea kumfuatilia zaidi. Na hilo limeshafanyika, kwani sasa ni nani anayemuamini Brian tena? Wakuu wake wa kazi wenyewe wanamuona mwehu, au anayeelekea kwenye wehu, jambo ambalo ni tosha kabisa kutomtilia maanani lolote atakalosema.

Na sasa, baada ya kutimiza hilo, ndipo alipoamua kuchukua nafasi yake ya kumkaribia Chambuso Mwagala, na labda kuelewa kilichotokea siku ile, ili angalau apate mwanga zaidi katika harakati zake zilizomleta hapa duniani. Aliwaona wale wasaidizi wakimtoa Chambuso Mwagala na kumkalisha kwenye ule mkeka kando ya bibi yake. Bibi alimuongelesha yule mjukuu wake kwa muda, na kutokea kule upande wa pili wa barabara, Jadu alimuona Chambuso akitikisa kichwa kuafiki alichoambiwa na bibi yake, kisha akamuona yule bibi akicheka na kumpapasa kichwa mjukuuu wake.

Chambuso alilaza kichwa chake mapajani mwa bibi yake huku akijinyoosha pale kwenye mkeka.

This is it!

Aliinua kapu lake lililojaa karanga na kuanza kutembea kuambaa ile barabara, bado akiwa upande ule ule wa barabara aliokuwako hapo awali.

“Hayyaa Karangaa! Hayyaa za hamuuuu! Hayaa karanga za hamuu…!” Alitupa jicho upande wa pili wa ile barabara, akaona yule bibi akigeuka kule alipokuwa baada ya kusikia kelele zeke.

“Hayaa Karangaa! Hayyaaa za hamuuuu! Hayaa karanga za hamuu…! Ni tamu kuliko wali wa karamu, wallahi haziishi hamu… Yuuu-Hhuuuu…!”

Upande wa pili wa barabara Jadu alimuona yule bibi akicheka huku akimtazama, bila shaka kutokana na yake maneno yake ya kuchombeza karanga zake na jinsi alivyokuwa akiyatoa kwa vina.

Alivuka ile barabara na kuelekea moja kwa moja hadi pale barazani kwa Mzee Mwagala Kifyagi.

“Karangaa! Bibi shikamoo…karanga bibi, senti kumi tu kipimo….” Alimwambia yule bibi huku akimchotea karanga kwa kijiko kikubwa kilichokuwa kwenye kapu lake na kumpa.

“Ah, baba yangu we, hiyo senti kumi nitaitoa wapi kikongwe miye, ninataka nizione tu hizo karanga zilizo tamu kuliko wali wa karamu…” Bibi alimjibu huku akicheka.

“Sasa ndio hizi bibi yangu, senti kumi tu…”

“Sina hiyo senti kumi baba…”

“Basi onja kidogo kwanza mzazi wangu, labda hapo utakumbuka kuwa una senti kumi pale mchagoni uliyoificha tangu juzi….” Jadu alimwambia yule bibi huku akimmininia karanga kwenye kiganja. Muda wote macho yake yalikuwa yakitembea kutoka kwa yule bibi kwenda kwa Chambuso, na kurudi kwa yule bibi. Chambuso Mwagala alijiinua taratibu kutoka mapajani kwa bibi yake na kuketi mkekani, akimtazama yule muuza karanga kwa udadisi na utulivu wa kiendawazimu.

Jadu alijaribu tena kuingia akilini mwake na kujua ni nini kilikuwa kikipita kichwani mwa yule kijana muda ule, lakini aliambulia kupata hisia ya wingu jeusi tu, hisia aliyokuwa akiipata siku zote alipokuwa akijaribu kufanya vile kwa yule kijana.

Hii ndio nafasi pekee ya kujaribu karata yangu ya mwisho…

Bibi alipokea karanga na kuzitupia kinywani, muda huo huo Jadu akamgeukia Chambuso.

“Na rafiki yangu hapa je? Rafiki, onja kidogo bwana…..”

“Ah, huyo mgonjwa…ana…”

“Haidhuru ati…kwani mgonjwa hajui utamu unapomtembelea bibi?” Jadu alisema huku akichota karanga kwa mkono wake, akiacha kutumia kijiko makusudi, na kumsogezea Chambuso mkono wake uliofumbata rundo la karanga.

Chambuso alimtazama kwa macho yasiyo na hisia yoyote, kisha taratibu alinyoosha mkono wake kupokea kile alichokuwa akipewa na yule mchuuzi wa karanga mcheshi. Jadu aliukamata mkono wa Chambuso kwa mkono wake wa kushoto ilihali kwa mkono wa kulia akimimina karanga taratibu sana kwenye kiganja cha yule kijana.

Na hapo alipata alichokuwa akikitaka.

Muda mkono wake na ule wa Chambuso ilipogusana tu, hisia na fahamu zilizokuwa kwa Chambuso zilipita moja kwa moja hadi kwenye mishipa yake ya fahamu. Na muda ile mikono yao ilipokuwa imeendelea kushikana, wakati yeye akimimina taratibu zile karanga kiganjani mwa Chambuso, macho yake yalikuwa yameyakamata moja kwa moja macho ya Chambuso, na kwa kasi ya umeme, matukio yaliyoshuhudiwa na yule kijana yalipita kichwani mwake haraka haraka, moja baada ya jingine, hadi yale matukio yaliyotokea barabara ya Kazimzubwi, na kuishia kwenye lile lile wingu jeusi.

Jadu alimuachia mkono yule kijana na kumuacha akiwa na karanga mkononi mwake.

Kazi ilikuwa imekwisha.

Alibaki akimtazama yule kijana kwa muda huku akihema kwa nguvu, yaliyokuwa kichwani na kwenye hisia za yule kijana sasa yalikuwa kichwani mwake, alikuwa na kazi ya kuyachuja.

“Sasa baba yangu…Sisi pesa ndio hatuna, na karanga kweli ni nzuri…” Jadu alishitushwa na kauli ya yule bibi, naye akarudisha hisia zake pale alipokuwapo.

“Ah, bibi…si haba, siku nyingine utanunua tu…si umeshaona jinsi zilivyo tamu?”

“Aaaah, sana tu babu, asante sana…..”

“Asante bibi…na kwa heri.” Jadu muuza karanga alimjibu, kisha akamgeukia Chambuso, “… kwa heri rafiki, eenh?” Alimsemesha huku akimpungia mkono. Chambuso Mwagala alibaki akimtazama kwa macho yasioonesha kujali iwapo alimuaga au alijiondokea tu bila kuaga, mkononi mwake akizifinyangafinyanga zile karanga, baadhi zikimwagika mkekani.

Jadu Mfaume aliondoka haraka sana eneo lile, huku akijilazimisha kupiga kelele kuzinadi karanga zake zilizo tamu kuliko wali wa karamu…


Wakati Jadu Mfaume akimuonjesha karanga yule bibi wa Chambuso, Superintendent Tib Haggard alikuwa akisoma barua iliyoandikwa na Inspekta Brian Koba akiwa kitandani, Hospitali ya Princess Margreth. Aliisoma ile barua kwa mara ya pili, na kwa mara ya pili alijikuta akitikisa kichwa kwa masikitiko na kutoamini.

Ilikuwa ni barua ya kuacha kazi kutoka kwa yule Inspekta aliyekuwa akimuamini sana hapo awali, kabla ya kumuingiza kwenye kesi ya mauaji ya kule Kazimzumbwi.

Oh, shit…nadhani nimekuwa mgumu sana kwa huyu kijana masikini. Lakini lazima aelewe kuwa hii kesi ingemharibu akili yake na nimefanya hivi kwa faida yake.

Tib Haggard aliwaza huku akiingia kwenye gari lake kuelekea hospitali, kuongea na Inspekta Brian Koba.

Lazima aelewe kuwa uamuzi wa kuifunga hii kesi ni wa ngazi za juu…! Hii kesi si ya kawaida…si yeye wala yeyote duniani ambaye anaweza kupambana na Alliens…hakuna ajuaye ni vipi namna ya kukabiliana navyo, na iwapo tutakosea kidogo tu tunaweza kujiingiza kwenye matatizo makubwa zaidi! Sasa Brian ataelewa hilo?

Alizidi kujiwazia wakati akiendesha gari kuelekea kule hospitali ambako Brian Koba alikuwa akipatiwa tiba kutokana na majeraha aliyoachiwa na yuke kiumbe wa ajabu.

Shit, itambidi aelewe sasa, ingawa hakutakiwa kuelezwa juu ya hili mpaka hapo tutakapopata uhakika juu ya namna ya kukabiliana na viumbe hivi…

Aliegesha gari nje ya ile hospitali na kuingia moja kwa moja hadi wodini alipolazwa Brian.

Kitanda kilikuwa kitupu!

Alitoka wodini na kumtafuta yule tabibu aliyekuwa akimtibia Brian. “Afande, tumekuwa tukikupigia simu ofisini kwako sasa hivi…” Tabibu alimwambia mara alipomuona.

“Huna haja ya kunitafuta kwa simu tena kwa sababu mwenyewe nimeshafika! Brian yuko wapi, mbona hayuko kitandani kwake?” Tib alimuuliza yule tabibu kwa jazba.

“Ndio maana tulikuwa tukikutafuta kwa simu afande…Brian Koba amejitoa hospitali…”

“Whaat…?”

“Ndiyo…alitaka tumruhusu atoke, nikamuambia kuwa bado hajawa mzima kiasi cha kutoka hospitali, hivyo akasema kuwa anajitoa mwenyewe…”

“Hah, na nyie mmemruhusu……?”

“Hatukumruhusu, amejitoa mwenyewe nakwambia, na akasema anayejiona rijali ajaribu kumzuia. Tukamuacha…” Tabibu alimjibu.

“Oh Shit…..!” Tib alilaani, “Sasa…” aliinua uso wake na kuanza kumuuliza yule tabibu ni wapi ameelekea, lakini akaamua kubadili mawazo, “…anyway acha tu.”

Alitoka na kutia gari moto hadi Magomeni, nyumbani kwa Brian Koba. “Afande Brian amehama asubuhi hii…” Mama mwenye nyumba alimjibu Tib alipoenda kumuulizia Brian pale nyumbani.

“Say whaat…?” Tib Haggard alimaka kwa mshangao.

“Sijui kizungu baba…Brian kahama na hatujui kahamia, wapi mambo ya aibu aliyoyafanya juzi hapa yamemtia aibu…akona ajiondekee…”

“Ah, kahama lini…yaani, saa ngapi?”

“Asubuhi hii ameingia na lori hapa. Kasomba vijana mtaani wampakilie vyombo vyake, kanilipa kodi yangu ya mwezi huu japo mwezi haujakamilika, akaondoka.” Mama mwenye nyumba alizidi kutanabahisha.

Tib Haggard alichoka kabisa.

Alimshukru yule mama na kurudi kwenye garini, akilini akijua kuwa tayari ameshampoteza askari mmoja makini na mwenye ari ya kazi yake.


Jadu Mfaume aliingia chumbani kwake alipopanga maeneo ya Manzese na kujifungia kwa ndani. Nguo za kuuzia karanga na kapu lake la karanga alishavitupa vichakani, na sasa alikuwa kwenye nguo zake za kawaida alizotoka nazo asubuhi ile, ambazo zilikuwa chini kabisa ya lile kapu la karanga alilokuwa amelibeba.

Alijilaza chali kitandani na kufumba macho, kisha akaanza kurudisha zile taswira zilizopita katika fahamu zake wakati akiwa ameshikana mkono na Chambuso Mwagala, ila safari hii zilikuwa zikipita taratibu mno.

Akiwa amefumba macho pale kitandani, Jadu Mfaume aliitazama historia nzima ya Chambuso Mwagala kutokea akilini mwake, kama jinsi mtu anavyoweza kuwa anatazama mkanda wa video. Na hapo aliliona tukio zima la kule Kazimzumbwi, kama jinsi Chambuso Mwagala alivyoliona usiku ule, na hatimaye alimuona yule kiumbe wa ajabu, kama jinsi alivyoonwa na Chambuso, akitoka mwilini mwa Huba binti Malambi, na kumgeukia Chambuso kwa muda, kisha akatoweka huku akiyeyuka.

Jadu Mfaume alifumbua macho ghafla, uso wake ukiwa umejikunja kwa hasira, kwani alimtambua yule kiumbe wa ajabu, na sasa akijua fika kuwa hakika wale aliokuja kuwasaka walikuwa Tanganyika.

Na alijua kuwa katika kile kiumbe kilichoonekana cha ajabu kilichotoka mwilini mwa yule binti, kulikuwa kuna mkusanyiko wa wale wote aliokuwa akiwasaka…kwa namna fulani wale vijana waliombaka yule binti walikuwa wameingilia kile walichokuwa wakikifanya, na hivyo kuwafanya wasiwe na nguvu kama walivyotakiwa. Na sasa ile alama waliyoacha pale kifuani kwa yule binti ilileta maana.

Jadu Mfaume mpya aliyaelewa haya kwa sababu na yeye ni kiumbe wa asili ya wale viumbe waliojijumuisha ndani ya ule mwili wa yule binti. “Sasa nimejua kuwa uko hapa Mxulu…na nakuahidi kuwa nitakuwinda wewe na vibaraka wako, na nitawaangamiza mmoja baada ya mwingine!” Jadu Mfaume mpya alisema kwa sauti ya kunong’ona huku uso wake ukiwa umejikunja kwa hasira.

Alitoka nje ya chumba kile na kuingia mitaani kuwasaka wabaya wake. Huo ulikuwa ni mwaka 1961.

Msako wake uliendelea kwa miaka mingi sana…


Wiki moja baadaye, Superintedent Tib Haggard aliweka simu chini, na kubaki akiwa amekunja uso kwa tafakuri nzito. Inspekta Brian Koba hakuwepo Kisarawe vilevile, ambako alitaraji labda angekuwa huko. Sasa itambidi aidhinishe ile barua ya kuacha kazi kwa yule askari shupavu, jambo ambalo hakutaka kabisa kulifanya hapo awali kabla ya kuongea na Brian na kumuelewesha zaidi sababu ya kesi ile ya ajabu kufungwa namna ile. Hakuwa na la kufanya tena.

Zilikua zimebaki saa chache kabla hajakabidhi ofisi kwa Mkuu Mpya wa Jeshi la Polisi mzalendo naye arejee kwao Uingereza, ikiwa ni matokeo ya kukoma kwa utawala wa Kiingereza nchini Tanganyika.

Naondoka Tanganyika nikiacha nyuma yangu kesi moja ambayo pamoja na kufungwa kwake, bado ina utata mkubwa…

Aliinuka taratibu na kumalizia kufungasha makabrasha yake pale ofisini, akili yake ikiwa imezongwa na mawazo mengi.

Saa mbili baadaye Tib Haggard aliinua uso wake na kumtazama yule Afisa Mpya wa Jeshi la Polisi ambaye kwake ndio alikabidhi madaraka yote aliyokuwa nayo hapo awali.

“Okay, kamanda, hayo ndiyo yote. Kazi yangu hapa Tanganyika sasa imekomea hapa, nawe utaendelea kutokea hapa. Kuna swali lolote zaidi?” Alimuuliza.

Kaimu Superintendent Magadula Mbuya alimtazama mkuu wake wa kazi wa muda mrefu na kutikisa kichwa kabla ya kujibu.

“Umegusa maeneo yote afande…sina la kuuliza…”

Tib Haggard alimtazama yule afisa wa polisi mzalendo mwenye umri wa miaka arobaini na minane kwa muda, kabla ya kuongea tena.

“Vizuri. Sasa…” Alisema na kutulia kwa muda, akimtazama kwa makini yule afisa aliyekabidhiwa madaraka ambayo hapo awali yalikuwa yake, huku akilini akitafakari juu ya lile jukumu la mwisho alilotaka kumkabidhi yule afisa, kisha akaendelea; “…limebaki swala ambalo ni nyeti mno, nalo ni…” Aliinuka na kuliendea kabati la chuma lililokuwa kwenye kona moja ya ukuta wa ofisi yake na kulifungua, Kaimu Superintendent Magadula Mbuya akigeuka kufuatilia kila kitendo alichokuwa akikifanya, kisha akarudi pale mezani akiwa na faili jembamba mkononi mwake, ambalo aliliweka pale mezani taratibu.

“…hili!” Alimalizia kauli yake huku akiketi tena nyuma ya ile meza yake, akimtazama Magadula kwa makini.

Kaimu Superintendent Magadula Mbuya alilitazama lile faili kwa muda, na kuona kuwa lilikuwa limeandikwa neno moja tu juu yake, tena kwa hati kubwa sana.

UTATA.

Aliinua uso wake na kumtazama yule mzungu anayemkabidhi madaraka mazito siku ile kwa uso uliojaa maswali.

“Utata afande…?” Aliuliza.

“Ndiyo Magadula, Utata. Hebu funua hilo faili, uone kilichoandikwa kwenye ukurasa wa kwanza wa faili hilo…” Tib Haggard alimwambia, na Magadula alisita kidogo kisha akatekeleza. Alisoma kilichoandikwa kwenye ule ukurasa wa kwanza wa lile faili, kisha uso wake ukiwa umejaa umakini, alimtazama tena yule mzungu aliyemkabidhi madaraka mazito kwenye jeshi jipya la Tanganyika huru.

“Closed but unsolved…?” Alitamka kile alichokisoma kwenye ule ukurasa wa mwanzo wa lile faili.

“Hasa! Na hilo ndilo linalofanya hili faili liwe nyeti sana…” Tib alimjibu huku akiendelea kumtazama. Magadula Mbuya alimtazama huku bado uso wake ukiwa na udadisi.

“Unakumbuka kuwa kulikuwa kuna kesi ya vijana watatu wa hapa mjini waliouawa katika mazingira ya ajabu sana huko Kisarawe?” Tib alimuuliza.

“Ndiyo, niliisikia juu juu tu, wakati huo mimi nikiwa nashughulikia kesi ya wahamiaji haramu kule kwenye mpaka wetu na Msumbiji…”

“Sawasawa! Sasa hiyo kesi ndiyo imekuja kubandikwa jina la Utata, kwani ni utata mtupu. Naomba unisikilize kwa makini, kwani kuanzia leo hili faili litakuwa kwenye himaya yako kwa muda wote utakaokuwa katika wadhifa huu, na mle…” Tib Haggard alioneshea kidole chake kwenye lile kabati la chuma alimolitoa lile faili, “…ndimo mahala pake!”

Kwa saa nzima iliyofuatia, Kaimu Superintendent Magadula Mbuya alipokea maelezo na maelekezo juu ya kesi na lile faili la UTATA.

Usiku wa siku ile, ikiwa ni mwanzoni mwa mwaka 1962, Tib Haggard, pamoja na askari wengine waingereza waliokuwa wakiongoza jeshi la polisi la Tanganyika, walipanda ndege kurudi kwao, Uingereza.

Ukoloni ulikuwa umekwisha, ilhali Utata bado ukiwa haujatatuka, na kesi ikiwa imefungwa…

MWISHO WA KITABU CHA KWANZA

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment