Utata wa 9/12 Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA: HUSSEIN ISSA TUWA
*********************************************************************************
Simulizi: Utata Wa 9/12
Sehemu ya Tatu (3)
Jijini Dar es salaam:
Wakati Inspekta Dilunga akiwa anawakabili wale akina mama walioigundua ile miili iliyokutwa katikati ya ile barabara pweke ya Pugu–Kazimzumbwi, katikati ya jiji la Dar es salaam, usingizi mzito wa Konstebo wa polisi Brian Koba ulikuwa ukiingiliwa na vishindo vya mlango wake uliokuwa ukigongwa kwa nguvu na mfululizo. Aliguna kivivu na kugeukia upande wa pili, akijifunika kichwa chake kwa mto aliokuwa ameulalia, lakini ile sauti ilizidi kumfikia masikioni mwake.
Ngon…!Ngon…!Ngon…!
“Aaah! nani…?” Alibwabwaja huku akizidi kushindilia kichwa chake chini ya ule mto.
“Konstebo Brian….! (Ngo, Ngo, Ngo!) Konstebo Brian!” Sasa vishindo vya kugongwa ule mlango wa chumba chake cha kupanga kilichokuwa maeneo ya Magomeni mapipa, vilikuwa vikishadidiwa na sauti ya mtu akiita jina lake.
“Nini…?” Kosntebo Brian alibwabwaja tena huku bado akiwa amefumba macho yake, usingizi mzito bado ukimuelemea. Alikuwa amekesha usiku wote uliopita kwenye shamrashamra zilizokuwa zikifanyika kwenye uwanja wa michezo jijini, kuadhimisha tukio kubwa kabisa katika taifa hili ambalo sasa lilikuwa huru, na alipewa muda wa kupumzika kabla hajaingia tena kazini jioni ya siku ile. Sasa huyu anayekuja kunigongea asubuhi hii ni nani tena?
“Konstebo Brian!”
Ngo, Ngo, Ngo!
“Konstebo Brian…”
NGO, NGO, NGO…
“NINI LAKINIII?” Konstebo Brian alikurupuka kutoka kitandani kwake huku akifoka kwa hasira, akitupa pembeni mto aliokuwa amejifunika nao.
“Ah, Konstebo!”
Konstebo Brian Koba alitazama saa aliyokuwa ameivaa na kulala nayo. Ilikuwa ni saa kumi na mbili na robo za asubuhi. Alisonya kwa hasira na kuutazama ule mlango uliokuwa ukigongwa kutokea nje.
“Brian!”
Ngo, Ngon, Ngoooo!!
Akiwa na bukta tu ilihali kifua chake kikiwa wazi, Konstebo Brian Koba alifungua mlango wa chumba chake na kukutana uso kwa uso na askari mwenzake ambaye alikuwa ni karani kwenye kituo chao cha kazi.
“Jambo Afande!” Private Juma Gombo, ambaye hakuwa na muda mrefu tangu ajiunge na jeshi lile la polisi, alisalimu huku akisaluti.
“Jambo mwenyewe! Sema shida yako upesi Private… nataka kwenda kulala m’mi saa hizi!” Konstebo Brian Koba alimjibu kwa hasira yule askari, ambaye alimtumbulia macho kwa mshangao na woga, kisha akameza mate na kumpasha habari.
“Unahitajika Ofisini haraka sana….kuna dharura, na mkuu ameagiza uende haraka iwezekanavyo!”
Brian alitamani kum-meza yule askari.
“Mkuu” alikuwa ni mkuu wao wa kituo, ambaye alikuwa raia wa kiingereza, mabaki ya ukoloni wa mwingereza uliokoma rasmi siku ile, na Konstebo Brian Koba hakuficha kukereka kwake.
“Lakini si inajulikana kuwa mimi leo niko off mpaka jioni? Nimekuwa wima usiku kucha! Sasa tena….” Alilalamika, lakini akaona kuwa anamuonea bure yule karani aliyefikisha ule ujumbe.
“Oke… nitakuwa huko muda si mrefu!” Alimwambia huku akipiga mwayo.
Nusu saa baadaye, Konstebo Brian Koba alikuwa ofisini kwa Superintendent Tibbedeux “Tib” Haggard, au “mkuu”, kama wote walivyozoea kumwita.
“Tuna kesi ya kutoweka kwa vijana watatu… mmoja wao alitakiwa asafiri alfajiri ya leo hii. Ilipotimia saa tatu usiku wa jana na kijana hajaonekana wazazi wake wakapatwa na wasiwasi na kuleta ripoti hapa kituoni. Inasemekana alionekana akiwa na vijana wengine wawili, wakiwa wenye Gari la baba wa huyo kijana aliyetakiwa kusafiri leo.” Tib Haggard alimueleza kwa kirefu na kwa kiswahili fasaha kabisa. Brian aliendelea kumsikiliza bila kutia neno, na Tib akaendelea, “Sasa kama ujuavyo, kutokana na shamrashamra za jana, hakukuwa na askari yeyote aliyeweza kuifuatilia kesi hii. Mpaka muda huu hao vijana hawajaonekana na hawajulikani waliko. Ndugu na jamaa wanalia ovyo huko. Nataka usimamie kesi hii Brian, na nataka matokeo haraka sana…. sitaki niondoke Tanganyika nikiwa nimeacha kesi ambayo haijatatuliwa…”
“Sasa … ninaanzia wapi afande…” Brian aliuliza huku akijiuliza inakuwaje jeshi la polisi linakosa askari wa kufuatilia jambo kama lile usiku kucha hadi siku ifuatayo, eti kwa kuwa kulikuwa kuna shamrashamra usiku kucha. Akilini alijua wazi kuwa kama aliyepotea usiku ule angekuwa ni mtoto wa kizungu au wa kihindi, hakika angetafutwa usiku ule ule, hata kama kungekuwa na shamrashamra gani. Bora hata huo utawala wao ulivyokoma… wakoloni wakubwa! Labda sasa na sisi wengine tutapandishwa vyeo!
Brian alijiwazia wakati akimtazama yule mkuu wake wa kazi akivuta droo na kutoa faili jembamba, ambalo aliliweka taratibu pale mezani.
“Maelezo yote ya awali yamo ndani ya faili hili…taarifa juu ya hao vijana waliotoweka, wazazi wao, na kadhalika. Lakini hasa ni juu ya huyo aliyetakiwa asafiri, ambaye wazazi wake ndio walioleta taarifa hii hapa kituoni. Kama utahitaji msaada wowote utasema, lakini sioni kama hiyo ni kesi ya kuhitaji msaada…” Superintendent Haggard alimwambia.
Konstebo Brian Koba alilichukua lile faili kisha akainuka na kusaluti kikamavu kabla ya kutoka nje ya chumba kile akiwa amefura kwa hasira.
Nusu saa baadaye aliegesha tena baiskeli yake nje ya ofisi yao, na kuiendea moja kwa moja simu iliyokuwa mezani kwake. Aliinua simu ile na kupiga namba za kitengo cha usalama barabarani. Alimpatia askari aliyepokea simu yake namba ya gari iliyosadikika kuwa waliondoka nayo wale vijana, na kuulizia iwapo kuna ripoti yoyote ya ajali iliyohusisha gari lile. Yule askari wa kitengo cha usalama barabarani aliahidi kumjulisha pindi zitakapopatikana habari zozote kuhusiana na gari lenye namba za usajili DSM 14, Ford Anglia.
Alirejesha simu ile mahala pake na kuweka miguu yake mifupi juu ya meza yake na kutoa kijitabu kidogo kilichokuwa mfukoni mwake na kuanza kusoma vitu alivyoandika kwenye kijitabu chake kidogo baada ya kutembelea familia zote tatu za wale vijana watatu waliotoweka, na kuanza kutathmini uelewa wake wa kesi ile ambayo mkuu wao wa kazi, mkoloni Tib Haggard, aliiona kuwa haihitaji msaada wowote zaidi.
Alianzia nyumbani kwa mzee Mwagala Kifyagi, ambako huko alichogundua ni kuwa kijana aitwaye Chambuso Mwagala alikuwa amepatiwa nafasi ya masomo nchini Uingereza na baba yake, Mzee Mwagala, ambaye alikuwa ni miongoni mwa wazalendo wachache wenye uwezo nchini. Siku ya tukio Chambuso na wenzake wawili, Uwesu bin Shaame na Esmund Bwaira, walichukua gari la mzee Mwagala aina ya Ford Anglia, lenye namba za usajili DSM 14 kwa lengo la kwenda kuaga jamaa na marafiki kabla ya safari yake ya Uingereza. Muda ulikuwa ni kiasi cha saa nane za mchana Chambuso hakufafanua jamaa na marafiki hao ni akina nani na wako wapi, na tangu wakati huo hakuonekana tena.
Nyumbani kwa akina Uwesu bin Shaame, alimkuta baba wa huyo kijana akiwa amehamanika vibaya mno. Huko akagundua kuwa Uwesu alimuachia dada yake duka lao la vitu vya rejareja kwa mealezo kuwa alikuwa akiendea kumuaga rafiki yake Chambuso aliyekuwa akitarajia kwenda masomoni Uingereza siku iliyofuata. Muda huo ulikuwa ni saa sita za mchana, na hakuonekana tena tangu wakati huo.
Kwa akina Esmund Bwaira nako maelezo hayakuwa tofauti na yale aliyokuta kwa akina Uwesu. Alifinya midomo yake na kukunja sura kwa tafakuri.
“Sasa hawa vijana watakuwa wamekwenda wapi?” Alijiuliza kwa sauti huku akiinuka na kwenda jikoni, ndani ya lile jengo la polisi, na kuanza kujichemshia chai kwa kutumia birika la umeme.
“Hakika Chambuso asingekubali kuikosa safari ya kwenda ulaya hivi hivi tu, lazima kutakuwa na jambo zito lililosababisha hali hii…” Alizidi kujisemea mwenyewe wakati akisubiri maji yachemke pale jikoni.
Dakika tano baadaye alirudi kwenye kiti chake nyuma ya meza yae pale ofisini na kupandisha tena miguu yake juu meza na kuanza kunywa chai yake pole pole.
Sasa ni jambo gani hilo?
Alizidi kujiuliza, na hata pale swali lile lilipopita kichwani mwake, jibu kuwa vijana wale watakuwa wamepata ajali lilikuwa la kwanza kichwani mwake, na ndio maana akapiga simu kitengo cha usalama barabarani.
Huenda pia vijana wale wakawa katika moja kati ya Hospitali za jijini muda ule, aidha majeruhi au marehemu, lakini hiyo pia ni kutokana na ajali, hivyo bado taarifa kutoka kitengo cha usalama barabarani ilikuwa muhimu.
Alizidi kuwaza.
Nini kingine…?
Aliteremsha miguu yake na kuanza kuandika sababu mbalimbali zilizomjia kichwani mwake ambazo zingeweza kusababisha wale vijana watoweke namna ile, hasa katika siku muhimu kwa mwenzao kama ile. Aliandika “Pombe”, kwenye kijidaftari chake na kubaki akilitazama lile neno huku akitafakari. Inaweekana kuwa wameenda kunywa pombe na kulewa hadi wakajisahau….na kupitiliza mpaka leo….?
Aliguna na kutikisha kichwa. Hiyo ilikuwa ngumu kuingia kichwani mwake. Akaandika tena kwenye kitabu chake.
Wanawake.
“Yes! Kama mimi nd’o ningekuwa nasafiri kwenda ulaya, hakika ningetaka kuwa na mpenzi wangu siku ya mwisho kabla ya kuondoka!” Alijisemea.
Lakini ndio kweli mwanamke anifanye niahirishe safari muhimu kama hii…?
Alitikisa kichwa. “Haiwezekani…kutakuwa na jambo zito zaidi ya hilo…”
Mnh! Lakini Al-junuuni funuuni… wazimu uko wa namna nyingi bwana, inawezekana vile vile. Aliinua tena simu na kupiga namba ya nyumbani kwa Mzee Mwagala, na mara moja mzee Mwagala aliipokea simu ile.
“Ndio afande… kuna habari gani juu ya mwanangu?” Mzee Mwagala aliuliza kwa kiherehere, sauti yake ikiwa imejaa hofu kubwa.
“Hapana mzee, nilikuwa nataka nikuulize vitu viwili kuhusu Chambuso….”
“Oh!”
“Ndio…kwanza nilitaka kujua iwapo alikuwa anakunywa pombe…”
“Hapana. Mwanangu hanywi kabisa!”
“Okay…na…je, alikuwa na mpenzi yeyote wa kike ambaye labda mnaweza kuwa mnamfahamu?”
Mzee Mwaga aliguna kwa sauti kwa swali hili, kama kwamba yule askari alikuwa amemuuliza swali la nguoni kabisa, kisha akajibu.
“Hapana… yaani, sijui kama kuna mtu wa aina hiyo, hebu subiri kidogo afande…” Konstebo Brian alimsikia yule mzee akimuuliza mtu mwingine mle ndani swali lile, bila shaka mama au dada wa Chambuso, kisha alirudi tena kwenye simu.
“Hapana afande…hakuna yeyote mwenye kujua juu ya hilo hapa nyumbani…ila inawezekana. Lakini hata kama ni hivyo, Chambuso hawezi kupoteza nafasi muhimu kama hii kwa ajili ya mwanamke! Hilo nakukatalia afande!”“Nakubaliana na wewe…ni vile tu ni lazima tuchunguze kila liwezekanalo…”
“Sawa…kwa hiyo?”
“Kwa sasa ni hayo tu mzee…nitakupigia tena iwapo nitahitaji chochote, au iwapo nitapata taarifa yoyote mpya…”
“Ina maana mpaka sasa bado hakijajulikana kitu chochote kipya?” Mzee Mwagala aliuliza kwa kiherehere.
“Nasikitika bado mzee, lakini tunalifanyia kazi kwa nguvu sana hili suala…”
Ukimya ulitanda upande wa pili, na Konstebo Brian Koba alitaka kufunua tena kinywa kumuuliza yule mzee iwapo alikuwa amemsikia, wakati Mzee Mwagala alipokata ile simu. Alirejesha mkono wa ile simu mahala pake huku akitikisa kichwa kwa masikitiko, na mara alishtushwa tena na mlio wa ile simu.
Aliinua na kuiweka sikioni mwake.
“Konsebo Brian Koba!” Alijitambulisha kwenye ile simu, na kusikiliza maelezo ya upande wa pili huku sura yake ikijikunja kwa umakini.
“Naelekea huko sasa hivi!” Alisema kwa bashasha na kuirudisha tena mahala pake ile simu, huku akiinuka na kutoka mbio kuelekea nje ya ofisi yake.
Gari lenye namba za usajili DSM 14, Ford Anglia, lilikuwa limeonekana likiwa kwenye mazingira ya ajali katika barabara ya Pugu–Kazimzumbwi, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani.
Dakika tano baadaye, Konstebo Brian Koba alikuwa nyuma ya usukani wa Gari la polisi aina ya 504 Peugeot, akiendesha kwa mwendo wa kasi sana kuelekea Kisarawe.
Kazimzumbwi:
Wakati yule konstebo mfupi na mwenye mwili uliokakamaa Brian Koba akizidi kubadili gia za gari lake kuelekea Kisarawe, Inspekta Gezza Dilunga alikuwa akiinua uso wake na kumtazama yule koplo aliyemkabidhi ile kadi ya gari lililokuwa katika lile eneo la maafa na kumwambia, “Nadhani hii itakuwa ni njia mojawapo ya kumtambua mmiliki wa gari hii…tatizo hizi kadi haziandikwi namba za simu…ni sanduku la barua tu!”
Kisha aligeuka na kumuendea yule askari aliyemtuma kwenda kufanya mawasiliano na kitengo cha usalama barabarani.
“Umefanikiwa?” Alimtupia swali kabla hajamfikia.
“Ndio afande…wako njiani…”
“Good…! Sasa nataka mchunguze eneo lote kutoka hapa kwenda kule ambapo inaelekea hili gari lilikuwa likitokea …tazameni kando ya barabara, nina hakika mtakuta sehemu ambapo hili gari lilipata ajali…” Alifungua mlango wa dereva wa lile gari lao na kuketi nyuma ya usukani, yule koplo alibaki akishangaa na kupigwa na butwaa. Inspekta Dilunga alijua ni nini kilichokuwa kikimshangaza na wala hakujali.
“Mtakaa kulinda hilo gari mpaka askari wa usalama barabarani watakapofika. Mtaliacha hilo gari mikononi mwao, kisha mtaendelea na uchunguzi wa mahala ambapo hilo gari lilipata ajali…askari wa usalama barabarani watakuwa na msaada mzuri kwenu katika hilo, mpo?” Alimwambia, akiishia kumtupia swali.
“Ndio afande….kwa hiyo wewe…?”
“Mimi naelekea kule kijijini kufuatilia habari za yule binti aliyeuawa hapa. Nitataraji ripoti yenu ofisini kabla ya saa sita mchana, sawa?” Alizidi kumpa maelezo. Koplo alimeza mate na kusaluti.
“Ndio afande!”
“Good!”
Inspekta Diliunga alitia gari moto na kuondoka kwa kasi eneo lile, akiwaacha wale wasaidizi wake wakiwa wameduwaa, kwani wao walitarajia kuwa wangekuwa wote katika kila hatua ya uchunguzi ule, lakini Inspekta Dilunga alikuwa na utaratibu tofauti wa kukabiliana na kesi ile isiyo ya kawaida.
Na wakati akiendesha kwa kasi lile gari la serikali, ile picha ya lile kovu la ajabu aliloliona kifuani kwa yule binti aliyekutwa akiwa ameuawa baina ya wale marijali wawili ilimjia tena kichwani mwake.
Oh, My God! Ni kitu gani kile…?
Akili yake ilirudi kwa yule kijana aliyekutwa akiwa ametumbua macho tu pale chini ya lile gari, na alihisi mwili ukimsisimka.
Mnh! Balaa kubwa hili…
Alipofika eneo la kijiji ambapo ile familia ya yule binti aliyeuawa ilikuwa ikiishi, alienda moja kwa moja hadi kwenye nyumba ya mjumbe wa kijiji ili apelekwe nyumbani kwa yule binti. Lakini kabla hajaifikia nyumba ile, aliona kundi la watu likiwa limejaa nje ya nyumba moja pale kijijini. Aliegesha Gari lake nje ya nyumba ile, na kuteremka haraka, akilini mwake akihisi kuwa ile ndio ile nyumba aliyokuwa akiikusudia. Akina mama kadhaa walikuwa wakilia nje ya nyumba ile, ilhali akina baba kadhaa wakiwa wameketi kwenye majamvi.
Alipofika tu karibu na ile nyumba mtu aliinuka na kumkaribisha huku akimpa mkono.
“Karibu afande….karibu!”
“Ahsante …ni kitu gani kimetokea hapa?”
“Msiba afande…bibi yetu bwana amefariki ghafla tu…”
Eh, Bibi tena…?
“Bibi…! Ni yupi huyo?” Inspekta Dilunga aliuliza huku akiona kuwa wanakijiji waliorundikana nje ya nyumba ile ya matope na makuti wakimkodolea macho kwa mastaajabu, kama kwamba alikuwa mtu wa ajabu sana, kama kawaida yao.
“Bibi yetu hapa nyumbani…Binti Beho….”
“Oh? Aam…alikuwa akiumwa au…?
“Hapana, alikuwa amelala tu. Amekufa kwa amani kabisa maskini. Amekufa usingizini bwana…”
Inspekta Dilunga alipumua.
Mambo aliyokuwa nayo mpaka kufikia pale yalikuwa mazito ya kutosha, hakika hakuhitaji kifo kingine cha kutatanisha. Bora ya huyu aliyejifia kiistaarabu.
Laiti angejua kilichotokea kwa yule marehemu aliyelala mle ndani wakati ule, hakika angezidi kukiri kuwa ya safari hii ilikuwa sio tu kali, bali ilikuwa ni kali ya mwaka.
“Poleni sana bwana…sasa nilikuwa nahitaji kufika nyumbani kwa Mzee Malambi…” Alimwambia yule mtu.
“Oh! Na huo ni msiba mwingine leo hii hapa kijijini kwetu, tena msiba wa ajabu kabisa!” Yule mtu alimwambia, na Inspekta Dilunga aliafiki kwa kichwa bila ya kuongezea neno lolote.
Dakika tano baadaye alikuwa tena ndani ya gari akielekea nyumbani kwa Mzee Malambi akiwa na kijana mmoja aliyepewa na yule mtu ili amfikishe nyumbani pale.
Alipofika akakuta kisanga kingine!
Kundi la watu lilikuwa limejaa nje ya nyumba ya mzee Malambi, ilhali vilio vya sauti vikisikika kutokea ndani ya nyumba ile, sauti ya mama Huba ikiwa juu kuliko nyingine zote. Aliisogelea ile nyumba na kumkamata bega kijana mmoja aliyekuwa pale nje na kutaka kumuuliza kulikoni, maana ilionekana wazi kwamba kulikuwa kuna kitu zaidi ya ule msiba wa Huba binti Malambi. Lakini kabla hajauliza alimuona mjumbe wa kijiji akiwa anatoka ndani ya nyumba ile.
“Ah, Inspekta! Nilikuwa nataka kukutumia ujumbe sasa hivi…kuna mambo ya ajabu sana hapa!” Mjumbe wa kijiji alimwambia huku akimfuata pale alipokuwapo.
“Ni kitu gani kilichotokea hapa mzee?” Dilunga alimuuliza.
Yule mjumbe wa kijiji alimkamata mkono na kumuongoza kurudi ndani ya nyumba ile.
“Mzee Malambi ameonekana!” Alimwambia.
“Na hilo ndilo la ajabu…?” Dilunga aliuliza huku akiuchomoa mkono wake kutoka kwenye himaya ya yule mjumbe. Hakupenda kukamatwa mkono namna ile.
“Hapana afande …ila mazingira yenyewe ndiyo ya ajabu shekhe …”
Sasa nimeshakuwa shekhe …!
Walipita kwenye korido nyembamba iliyojaa watu na kuingia ndani ya chumba kilichoonekana kuwa ni sebule ya nyumba ile, ambamo vilio vyote vilikuwa vikitokea, na hapo bila hata ya kuambiwa Inspekta Dilunga aliona ni nini alichokuwa akimaanisha yule mjumbe pale aliposema kuwa Mzee Malambi alikuwa ameonekana katika mazingira ya ajabu.
Mtu wa makamu aliyekuwa ametapakaa damu kifuani, alikuwa ameketi sakafuni huku akiwa amenyoosha miguu yake mbele na kichwani alikuwa ana jeraha baya lililogandia damu na kuzingirwa na uvimbe mkubwa. Yule mtu, ambaye mara moja Inspekta Dilunga alibaini kuwa ni Mzee Malambi, alikuwa amekumbatia kwa nguvu bunduki aina ya gobore kifuani mwake, huku macho yake akiwa ameyatumbua moja kwa moja mbele yake. Na hata pale alipokuwa akimtazama yule mtu, Inspekta Dilunga alibaini kuwa mzee Malambi alikuwa hajui lolote lililokuwa likiendelea pale. Yaani alikuwa kama mtu aliyewashangaa wale watu waliojazana mle ndani, hususan yule mama, ambaye ni mkewe, aliyekuwa akilia kwa uchungu mwingi.
Inspekta Dilunga alibaki akimtazama yule mzee kwa kutoamini, wakati mjumbe wa kijiji pamoja na watu waliokuwamo mle ndani walikuwa wakimtazama yeye, wakitaka kuona atachukua hatua gani baada ya kujionea hali ile.
Huyu mtu amepumbaa kama…kama…Hapana, hii haiwezekani…! Inspekta Dilunga alimsogelea yule mzee na kuchutama mbele yake, akiwa makini sana na lile gobore lililokuwa mikononi mwake. Alimtazama usoni huku vilio vya yule mama vikizidi kumchanganya kichwani mwake. Mama alikuwa akilia kwa nongwa na tashtiti nyingi, akijitupa huku na huko, akiropoka maneno mengi ya kulaani bahati mbaya iliyomuandama, akichanganya kiswahili na kizaramo…kama kwamba alikuwa akiisubiri kwa hamu siku kama ile itokee ili aoneshe umahiri wake wa kulia, na hali hii ilikuwa ikimkera sana Inspekta Dilunga.
Alijitahidi kudharau kelele za yule mama na kumtazama kwa makini yule mzee, ambaye naye alimgeuzia macho yake na kumtazama bila ya hisia au ufahamu wowote. Na katika macho ya yule mzee, Inspekta Dilunga aliona wazimu wa wazi ukiwa umeshamiri vilivyo.
Oh, my God…what the hell is this…?
“Mzee Malambi…” Aliita, na yule mzee aligeuza kichwa chake pembeni huku akizidi kulikumbatia kwa nguvu gobore lake. Yule mzee alikuwa amerukwa na akili kabisa!
Inspekta Dilunga alimgeukia yule mjumbe wa kijiji na kuanza kumuuliza, “Amefikaje ha…”
“Mume wangu jamanii…! Mwanangu Huba….mbona mnaniacha hivi mwenzenu lakini yoooooooooo…” Mama Huba alikuwa akilia kwa sauti, na swali la Inspekta Dilunga halikuweza kusikika. Mjumbe wa kijiji alimsogelea Inspekta ili amsikilize vizuri.
“Nauliza huyu mzee amefik…”
“…nimekosa nini kwa Mungu lakini mimi jamanieeeeeeeee…” Mama alizidi kupayuka kwa kelele, na kwa mara ya pili Inspekta Dilunga alilazimika kukatisha swali lake ili mama atulie kidogo, naye akazidi kukereka.
Mjumbe wa kijiji alisogea zaidi. “Unasemaje Inspekta?”
“Nataka kujua ni jinsi gani huyu…”
“Walimwengu nisaidieni mwenzenu, woooo…!”
“SHUT–THE SHIT-UP, WOMAN!” Inspekta Dilunga alimkemea yule mama kwa hasira huku akimnyooshea kidole, macho yakiwa yamemuiva, na kichwa kikimzunguka. Mambo aliyokuwa akiyaona siku ile yalikuwa mazito, na mama alikuwa anazidi kuyachanganya. Miguno ilitawala mle ndani, na mara moja mama Huba alinyamanza, macho yakimtoka kwa woga na mshangao.
“Hebu mtoeni humu ndani sasa hivi! Tunataka kufanya kazi hapa, ebbo…!” Dilunga aliamrisha kwa ukali, na mara moja akina mama wenzake walimchukua yule mama aliyeanza kulia tena na kumtoa nje ya sebule ile.
Ndipo mjumbe wa kijiji alipomjulisha Dilunga kuwa muda mfupi baada ya wanakijiji kutoka kule kwenye eneo la lile tukio la kutisha kule barabarani, kundi la wanakijiji cha jirani lilimleta yule mzee pale nyumbani, wakidai kuwa wamemkuta akizurura peke yake porini akiwa ametapakaa damu huku amekumbatia lile gobore lake, na alipoulizwa kulikoni, hakuweza kujibu lolote zaidi ya kuduwaa tu. Sasa kwa kuwa walijua kuwa mzee Malambi anatokea kijiji kile, walichukua jukumu la kumfikisha pale kijijini.
Na tangu amefika pale nyumbani yule mzee amekuwa katika hali ile, haongei, halii, hajibu swali lolote, na wala haoneshi kutambua mtu yeyote mle ndani, hata mkewe.
Inspekta Dilunga alichanganyikiwa si kidogo.
Ni wazi kabisa kuwa lililotokea kwa yule mzee ni sawa kabisa na lile aliloliona kwa yule kijana aliyekutwa chini ya lile gari lililohusika na tukio lile la kutisha kule barabarani…
Kuna uhusiano gani kati ya mambo yote haya?
Dakika ishirini baadaye, Inspekta Dilunga aliondoka eneo lile akiifuata ile Volkswagon Combi ya hospitali ya wilaya, ikiwa imembeba yule mzee aliyepagawa kiajabu kuelekea hospitali ambako tayari Chambuso Mwagala na wale marehemu waliokutwa kule barabarani walikuwa wamepelekwa. Alikuwa akiendesha gari lake kulifuata lile la hospitali huku akilini mwake akiwa na mawazo tele.
“Hakika hii ni kesi moja ngumu na ya ajabu kuliko zote nilizopata kukutana nazo maishani mwangu…..” Dilunga alijisemea peke yake ndani ya gari, na muda huo huo redio iliyokuwa ndani ya gari lake ilianza kuita.
“Now whaaaat?” Aliamka kwa hasira huku akifyatua kifungo maalumuu kilichowezesha mawasiliano kufanyika baina ya yeyote aliyekuwa ndani ya lile gari na aliyekuwa upande wa pili wa kifaa kile, akilini mwake akitarajia mashaka zaidi kuliko kitu kingine chochote ndani ya siku ile muhimu kwa wananchi wote wengine katika taifa hili jipya, isipokuwa yeye tu.
“Gezza!” Alijinadi kwa sauti huku akiendelea kulifuata lile gari la kubebea wagonjwa liliyokuwa mbele yake. Sauti za mkoromo zilisikika kutoka kwenye ile redio maalumu ya mawasiliano, kisha sauti ya mmoja wa wasaidizi wake aliowaacha kule barabarani ilisikika.
“Afande…!”
“Unawasiliana kwa kutumia redio gani koplo?” Dilunga aliuliza.
“Natumia redio ya gari la wana usalama barabarani!”
“Oh, Good, niambie kitu koplo!”
“Tumeliona eneo la ajali afande…ndio tuko kwenye eneo husika sasa.”
“Great! Nipe hali halisi…”
“Inaelekea hawa jamaa waligonga mti, lakini ni nje kabisa ya barabara. Kuna alama za matairi kuchimba vichaka kando ya barabara hadi pale lilipogonga mti!”
Gari la wagonjwa mbele yake liliashiria kukata kulia, na Inspekta naye akaashiria kukata kulia. Walikuwa wanaingia ndani ya eneo la hospitali sasa.
“Ni umbali gani kutoka pale tulipolikuta lile gari?” Dilunga aliuliza huku akiegesha Gari lake kando ya lile gari la kubebea wagonjwa mbele ya jengo la hospitali ya Wilaya ya Kisarawe.
“Kama nusu kilometa hivi.”
“Okay. Nataka mlichambue eneo lote hilo hatua kwa hatua, sentimeta kwa sentimeta. Msiache kitu! Nahitaji full report ofisini kwangu saa sita juu ya alama!”
“Ndio afande!”
“Over and out!” Inspekta Dilunga alimaliza mjadala ule na kuzima kile kifaa cha mawasiliano. Aliteremka kutoka kwenye lile gari na kuangaza huku na huko, akishangaa kuona kuwa kundi la watu likiwa limekusanyika nje ya jengo lile la hospitali. Alimuita nesi mmoja aliyekuwa akipita mbele yake na kumuuliza kulikoni kuna kundi la watu nje ya hospitali ile.
“Wamekuja kuwaangalia hao watu waliouawa huko barabarani… hasa huyo aliyebaki akitumbua macho!” Nesi alimjibu na Inspekta Dilunga akabaki kinywa wazi.
“Hah, yaani habari ndio zimezagaa namna hii?” Alisema kwa mastajaabu, lakini yule nesi alikuwa ameshapita na hakumsikia. Alitikisa kichwa na kuanza kupanda ngazi fupi na pana zilizokuwa mbele ya lango kuu la hospitali ile, ambamo majeruhi na maiti wote waliotokana na tukio lile la ajabu walikuwamo. Alikuwa na hamu kubwa ya kusikia ni nini Dokta Shabbir na mtaalamu wake Dokta Nigel Smith, mganga wa serikali ya mkoloni, watamwambia juu ya hali ya yule kijana aliyekutwa akitumbua macho katikati ya barabara ile, na pia juu ya yule mzee aliyeingizwa mle ndani muda mfupi uliopita.
“Inspekta Dilunga! Inspekta Dilunga! Inspekta…” Dilunga aligeuka taratibu kuelekeza kule ilipotokea ile sauti iliyokuwa ikiita jina lake kwa wahka. Mtu mmoja aliyepata kiasi cha miaka thelathini na mitano au na minane hivi, alikuwa akimkimbilia huku begani kwake akiwa ameninginiza mkoba mweusi.Alikuwa amevaa barghashia nyeupe, na usoni alikuwa amevaa miwani ya macho iliyokuwa na fremu nene nyeusi.
Inspekta Dilunga alikunja uso na kufinya macho yake kumtazama yule mtu, na kwa mara nyingine akajihakikishia akilini mwake kuwa hakuwa amepata kumuona mtu yule kabla, na udadisi ukamjaa, hasa katika mazingira ya kesi ile ya ajabu.
“Inspekta afadhali nimekuona! Habari za asubuhi kwanza…”
“Sijui zikoje kwa kweli.Wewe ni nani bwana, na una shida gani nami?” Inspekta Dilunga alimjibu na kumuuliza yule mtu huku akimtaza kwa makini.
Yule mtu alimnyooshea Inspekta Dilunga mkono wake kwa nia ya kusalimiana naye huku akijitambulisha, uso wake ukichanua kwa tabasamu pana.
“Ah, Inspekta unanijua sana, ila hujapata kuniona tu”. Alimwambia huku akizidi kumpa ule mkono wake ili wasalimiane kwa kushikana mikono. Inspekta Dilunga hakufanya bidii yoyote ya kuupokea ule mkono, na badala yake akamkoromea.
“Sasa kwa nini usiniambie wewe ni nani badala ya kunitolea mafumbo bwana? Nitakujuaje halafu niwe sijakuona?”
“Bruno Mgimba! Gazeti la Gurumo!” Yule mtu alijitambulisha kwa kujiamini huku akizidi kupanua tabasamu lililokuwa usoni kwake, na Inspekta Dilunga alijikuta akiinua uso wake juu na kuzungusha macho yake kwa fadhaa.
Bruno Mgimba!
Hakika alimjua yule mtu, na hakika hakuwa amepata kumuona kabla ya pale. Alikuwa ni mwandishi wa habari wa gazeti la Gurumo, na alikuwa amepata kusoma makala zake mara nyingi sana.
“Oh, kumbe ni wewe. Samahani sina taarifa yoyote kwa sasa, na…” Inspekta Dilunga alianza kuongea lakini yule mwandishi wa habari alimkatisha kwa swali huku akitoa kijitabu kidogo kutoka kwenye mkoba wake, na akichomoa kalamu kutoka kwenye mfuko wake wa shati.
“Inspekta Dilunga, inasemekana kuwa tukio zima lililotokea pale barabarani linahusiana na nguvu za kichawi. Je, ukiwa kama mpelelezi mzoefu, ni kweli hali hiyo inaweza kuwa hivyo inavyosemekana?”
“Siwezi kusema lolote juu ya hilo, na naomba uniache niendelee na uchunguzi wangu”.
“Pia kuna tetesi kuwa yule binti aliyekutwa akiwa amekufa pamoja na wale vijana pale barabarani alikuwa amebakwa. Una kauli gani juu ya hilo?” Bruno alizidi kuuliza, kama kwamba yule askari alikuwa ameletwa hapa duniani kujibu maswali yake tu.
Inspekta Dilunga alimtazama kwa ghadhabu, kisha bila ya kuongea neno zaidi aligeuka na kuingia ndani ya ile hospitali, akimuacha yule mwandishi wa habari mdaku akiwa amesimama nje ya jengo lile.
Gari kubwa aina ya Bedford lililokuwa katika muundo wa lori, lilikuwa likisafiri kwa mwendo mdogo, na makelele mengi likiwa limesheheni mzigo wake wa thamani kwa watumiaji waliokuwa wakipelekewa shehena ile huko mjini. Sehemu ya mbele ya gari lile dereva na utingo wake mmoja walikuwa wakiendelea na safari yao wakiwa kimya kabisa.
Ilikuwa ni saa moja ya asubuhi nao walikuwa na hamu ya kurudi jijini walikokuwa wakiishi, na kuachana na yale maisha yaliyodorora ya kule kijijini walipokuwa wakisafiri kutoka kijiji kimoja hadi kingine kukusanya magunia ya mikaa hadi kufikia kiasi cha kujaza lori lao, na hatimaye kulazimika kupitisha usiku uliopita kando ya barabara katika moja ya vijiji vya wilaya ile ya Mkuranga wakisubiri kupambazuke kutokana na gari lao lililochoka kutokuwa na taa.
Uchovu ulikuwa umetawala na akili zao zilikuwa zinafikiria kule walipokuwa wakielekea, bila ya kujua kuwa pamoja na shehena yao ile ya mikaa, walikuwa wamebeba abiria mwingine aliyedandia gari lao usiku uliopita wakati wao wakiwa wamelala sehemu ya mbele ya lile gari huku wakiwa wamefunga vioo vyote vya madirisha kwa hofu ya kuvamiwa na wanyama wakali.
Jadu Mfaume alikuwa amejikunyata kimya sehemu ya nyuma ya lori lile lililokuwa likielekea sehemu ambayo alikuwa na hakika kwamba ndiko angeweza kuwapata watu aliokuja kuwasaka hapa duniani.
Aliwafikiria wale wanakijiji wajinga aliowaacha wakipiga mayowe ovyo porini usiku kucha kumsamka yeye eti ili wamuangamize!
Alitikisa kichwa na kuchungulia nje ya lori lile kupitia kwenye uwazi wa mbao za sehemu ya nyuma ya lori lile na kuona miti tu.
Kutokana na mazungumzo ya wale watu waliokuwa kule mbele, alijua kuwa walikuwa wakielekea sehemu iitwayo Dar es Salaam, na ilielekea kuwa hiyo ilikuwa ni sehemu ya mji mkubwa kama miji mingine mikubwa aliyowahi kuipitia katika msako wake huu ambao bado haukuwa umezaa matunda yoyote tangu auanze. Na alijua kuwa hawezi kurudi huko alikotoka mpaka awapate aliokuja kuwasaka.
Aliegemeza kichwa chake kwenye ukingo wa lori, lile, na kufumba macho, akivuta hisia zake kujaribu kusikiliza iwapo atasikia kitu cha kumuwezesha kujua ni wapi walikuwa wale aliokuja kuwasaka.
Kichwani mwake alisikia mchanganyiko wa sauti nyingi zisizoeleweka hata kidogo, kama jinsi mtu unavyoweza kusikia idhaa nyingi za redio kwa wakati mmoja. Lakini hili halikumpa taabu, kwani alijua kuwa kuna sehemu tu itafika ambapo atasikia anachotaka kukisikia.
Safari iliendelea kwa mwendo wa pole huku lile lori likipiga kelele nyingi.
Inspekta Gezza Dilunga aliingia ndani ya hospitali ile na kumfuata mhudumu aliyekuwa nyuma ya dawati la mapokezi.
“Nahitaji kutumia simu!” Alimwambia huku akipeleka mkono wake kwenye simu iliyokuwa pale juu ya dawati.
Yule binti alimtamaza mara moja na kuona serikali ikiwa imetanda mwili mzima wa yule mtu mrefu na mweusi aliyesimama mbele yake na kumsogezea ile simu bila neno.
“Nataka askari watatu hapa hospitali ya wilaya haraka. Panahitaji ulinzi mkali…na marufuku kwa askari yoyote kuongea na waandishi wa habari kuhusiana na tukio zima la leo asubuhi!” Aliongea kwenye kile chombo na kuirejesha ile simu mahala pake bila ya kusibiri maelezo zaidi kutoka upande wa pili. Akamgeukia yule dada wa pale mapokezi.
“Nahitaji kuonana na Dokta Shabbir” Alimwambia.
“Sawa afande…subiri kidogo.” Binti alijibu na kuinua ile simu. Inspekta Gezza alimskia akimwambia mtu wa upande wa pili kuwa anahitajika aje pale mapokezi kumchukua mgeni wa Dokta Shabbir.
Dakika tatu baadaye, mhudumu mwingine wa kiume alikuja na kumuongoza Inspekta Dilunga hadi sehemu ambapo Dokta Shabbir alikuwa akiwahudumia wale majeruhi, na ile miili ya wale mareheumu ilikuwa ikifanyiwa uchunguzi wa awali.
Na huko, Inspekta Gezza Dilunga alikuta mambo mengine mazito na yenye kuchanganya zaidi.
Wakati Inspekta Gezza Dilunga akisubiri kupelekwa kwa Dokta Shabbir, Konstebo Brian Koba alikuwa akisimamisha gari lake kwenye njia panda baina ya njia iendayo Kisarawe mjini na ile barabara pweke ya Pugu¬Kazimzubwi.
Alifikiria achukuea uelekeo gani, kwani alijua kuwa vyovyote iwavyo, taarifa kamili za kipolisi juu ya lile gari lililokutwa katika mazingira ya ajali, na hatima ya waliokuwa wakiliendesha gari hilo, zitapatikana kwenye makao makuu ya polisi ya wilaya ile.
Lakini pia alifikiri kwamba kwa vile lile gari lilionekana katika barabara ya Kazimzumbwi, basi huko ndiko hasa kulikuwa eneo la tukio. Alikunja kushoto na kuchukua uelekeo wa ile barabara ya Pugu¬Kazimzubwi
Mwendo mfupi mbele yake aliona basi la abiria lililokuwa likitokea vijiji vya Mzenga, Mfyoza, Banda, Chakenge na Kazimzumbwi yenyewe. Brian aliliwashia taa zake za mbele lile basi kisha akabonyeza kitufe cha honi ya kipolisi, na king’ora cha tahadhari ya polisi kutoka kwenye gari lake kilianza kuvuma kwa sauti. Alitoa mkono wake nje ya dirisha na kumuashiria dereva wa lile basi asimame.
Dereva alitii amri ile Brian Koba aliteremka na kumuendea yule dereva wa lile basi, ambaye naye aliteremka kutoka kwenye basi lake, abiria waliokuwa kwenye lile basi walichungulia madirishani kwa udadisi mkubwa.
Yule dereva mnene mwenye tumbo kubwa alipandisha juu suruali yake huku akijioonyesha na kumuendea Konstebo Brian.
“Jambo afande…!” Dereva alisalimia, na Brian alimjibu huku akimuinulia mkono. “Jambo…jambo…!”
Kisha akamhoji iwapo huko walipotokea walikuta ajali yoyote, au dalili kuwa kulikuwa kumetokea ajali.
“Ah, afande! Dalili? Ni ajali hasa bwana! Damu zimetapakaa barabara yote. Kuna gari moja ndilo nahisi lililopata ajali, na gari nyingine ya polisi wa usalama barabarani….na huko nyuma zaidi kuna askari wengine wakipekua vichaka sijui wanatafuta nini…”
“Je, mliona miili au majeruhi wowote hapo kwenye eneo la ajali?”
“Mnh…mnh! Miili haikuwepo…nadhani itakuwa imeshaondolewa…”
“Okay…ahsante sana mzee, safari njema.” Konstebo Brian alimshukuru yule dereva na kila mmoja akarudi kwenye gari lake.
Dakika kumi baadaye Konstebo Brian Koba alikuwa kwenye eneo la tukio ambapo yale mauaji ya kikatili yalitokea. Hapo aliwakuta askari wawili wa usalama barabarani waliokuwa wameegesha gari maalumuu la kukokotea magari mabovu au yaliyopata ajali kando ya lile gari lililohusika na ajali ile.
Aliwasalimu na kujitambulisha, kisha akaliendea lile gari na mara moja alizibaini zile namba za usajili za lile gari. DSM 14, Ford Anglia. Alichungulia kwa makini ndani ya lile gari, akiwa makini sana kutoshika hata sehemu moja ili asiache alama za vidole vyake kwenye gari lile, na kuona jinsi ndani mwa gari kulivyosimulia misukosuko iliyowakuta wale waliokuwamo ndani yake.
Alirudi na kuichunguza kwa nje, na kuona jinsi ilivyobonyea upande mmoja wa ngao yake, jinsi taa yake moja ya mbele ilivyopasuka, na jinsi kioo kikubwa cha mbele ilivyopasuka na kujithibithishia kuwa hakika lile gari lilikuwa limekutwa na msukosuko mkubwa.
Alihisi kuwa lilikuwa amegonga kitu kigumu, kwa mazingira yale, bila shaka itakuwa ni mti. Aliangaza eneo lile na kujaribu kutafuta iwapo kuna mti uliogongwa, na aliona kuwa hilo halikuwezekana, kwani pale lilipokuwa lilikuwa ndani zaidi ya barabara kuliko nje ya barabara ile, ambako ndiko kwenye miti.
Alikumbuka maelezo ya yule dereva wa basi aliyemhoji kabla ya kufika eneo lile.
…na huko nyuma zaidi kuna askari wengine wakipekua vichaka sijui wanatafuta nini…
“Dalili ni kwamba hawa jamaa walipata ajali huko nyuma, na walipofika hapa…” Alijisemea peke yake na kuishia hewani, kwani hakujua ni nini kilikuwa kimetokea pale, na akaanza kupata hisia kuwa ile haikuwa kesi nyepesi kama ilivyotaka kuonekana…au kama mkoloni Superintendent Tib Haggard alivyoiona. Alitazama damu iliyokaukia pale barabarani kwa muda mrefu, na ile hisia ikazidi kujizaliti kichwani mwake.
“Kilichotokea hapa ni zaidi ya ajali…” Hatimaye alijisemea peke yake, huku akiwatatazama wale askari wa usalama barabarani wakianza kulifunga lile gari la mzee Mwagala kwenye lile gari lao maalumuu la kuvutia magari tayari kwa kulipeleka wilayani.
“…yumkini hawa vijana, kama ndio wao, watakuwa waliharibikiwa na gari, na wakati wakijaribu kulitengeneza, wakashambuliwa na mnyama mkali….simba au chui….hii damu ni nyingi sana, si ya kusababishiwa na mtu kugongwa na gari au kugongana gari kwa gari…” Alizidi kuwaza huku akivua kofia na kujifuta jasho kwa leso yake.
“….na hapa swala la kugongana na gari nyingine halipo! Gari lililopata ajali hapa ni moja tu…” Alizidi kujiwazia yule konstebo kutoka mjini, na kadiri alivyowaza ndivyo alivyojikuta akizidi kujiongezea idadi ya maswali kuliko majibu.
Mungu wangu, ni kitu gani kilichotokea hapa lakini…?
Alimfikiria mzee Mwagala na mkewe na moyo ukamtumbukia nyongo.
“Yaani ndio niende kuwaambia mtoto wao aliyekuwa anatarajia kupaa kuelekea Uingereza ameshambuliwa na simba huku porini…!” Alitikisa kichwa na kusonya. Alimkumbuka mzee Shaame, baba wa Uwesu, na mama Esmund Bwaira, na moyo ukazidi kumnyong”onyea.
Sasa hawa vijana walikuja kutafuta ni nini huku lakini…?
“Ohaa…afande, sisi inatubidi tulipeleke hili gari kituoni sasa!” Mmoja wa wale askari wa usalama barabarani alimpigia kelele, na Konstebo Brian Koba aliwageukia, akikatisha mawazo yaliyomgonga.
“Ah…okay…si kuna askari wengine pamoja nanyi…?” Brian aliwauliza huku akioneshea kule lilipokuwa lile gari walilokuwa tayari kulikokota.
“Oh…wale…? Wako huko msituni…kiasi cha kama nusu kilometa tu kutoka hapa, wakichunguza sehemu ambapo tunahisi kuwa hili gari lilianza kugonga mti kabla ya kufika hapa..” Yule askari alimjibu.
Brian aliwashukuru na kuingia kwenye gari lake kuelekea kule alipoelekezwa kuwa wale askari wengine walikuwa wakiendelea na uchunguzi, sehemu ambapo ile Ford Anglia yenye namba za usajili DSM 14, ilikuwa imetokea kabla ya kufika pale ilipokutwa.
Mwendo mfupi baadaye aliwakuta wale askari wawili wakitembea kwa miguu kuelekea kule alipokuwa akitokea, naye akaegesha gari kando ya barabara na kuwaendea. Alijitambulisha kwao na kuwapa sababu ya kuwepo kwake pale.
“Nami ningependa kuliona hilo eneo la tukio. Mnaweza kunipeleka? Aliwauliza, na wale askari walitazama.
“Itabidi tumwambie Inspekta Dilunga kwanza…” Mmoja alisema huku akimtupia jicho mwenzake.
“Naye yuko wapi?” Konstebo Brian aliuliza na aliwashangaaa wale askari walipomjibu kuwa Dilunga atakuwa ofisini kwake huko wilayani.
“Khah! Yaani tuende wilayani tukamtaarifu halafu ndio tuje kuliona hilo eneo…?”
“Nadhani huo ndio utaratibu afande!”
Konstebo Brian alitaka kumuuliza swali jingine kali, lakini akaghairi. Aliwatazama wale askari mmoja baada ya mwingine.
“Oke…isiwe taabu, nitaenda mwenyewe…” Aliwaambia na kurudi kwenye gari lake, akiwaacha wale askari wakiwa wemepigwa na butwaa.
Mwendo wa dakika tano baadaye alilifikia lile eneo, ambapo alimkuta mkulima mmoja akiwa ameketi ki-hasara hasara kando ya barabara. Aliegesha gari na kumsogelea yule mzee kabla ya kuanza kumuuliza juu ya eneo ambalo gari ilikuwa imegonga mti jirani na pale.
“Ndio hapa bwana…sasa hivi wenzako wameondoka hapa kwani nyie huwa hampeani habari jamani?” Mzee alimjibu na kumtupia swali lililoonesha kuwa alikuwa amechoka kuulizwa maswali na wana-usalama.
Brian Koba aliamua kudharau yale maneno yake mengine na kuchagua yale yaliyokuwa na faida na kilichompeleka pale asubuhi ile.
“Una maana gani kuwa ndio hapa mzee…?”
Mzee alimtamza kwa hasira kidogo.
“Si shamba langu hili! Hilo gari limeparamia shamba langu na kutifua viazi huku na huko! Nawauliza hao askari wenzako nani atanilipa wananipa siasa za ujamaa na kujitegemea …kisha haoooo, wanaenda zao! Sasa na wewe sijui umekuja kuniambia nini?” Mzee alimpayukia huku akitupa mikono yake kuelekea kule kwenye lile shamba, na bila ya kujibu shutuma za yule mzee, Konstebo Brian Koba alienda moja kwa moja pale shambani na kuanza kulichunguza lile eneo.
Eneo lote lilikuwa limezagaa alama za matairi ya gari, na kama alivyosema yule mzee, viazi vilikuwa vimetifuliwa na kuzagaa huku na huko. Alama za tairi za lile gari ziliishia kwenye shina la mkorosho mkubwa, na gome la mti ule lilikuwa limebanjuka vibaya na kuuathiri ule mti kwa kiasi kikubwa. Ni wazi kuwa lile gari liliugonga mti ule, tena liliugonga kwa kishindo kikubwa sana.
Vipande vya kioo vilikuwa vimetapakaa chini ya shina la mti ule na mara moja Konstebo Brian alijua kuwa hapa ndipo lile gari alilolikuta kule barabarani lilipovunjikia kile koo chake cha mbele.
Sasa kidogo mambo yalianza kuleta maana kichwani mwake, kwani hakuwa na shaka kabisa kwamba gari lililougonga ule mti ndio lile la mzee Mwagala, ambalo ndilo lile aliloacha likikokotwa kupelekwa kituo cha polisi cha wilaya ya kisarawe muda mfupi uliopita.
Alijaribu kulichunguza lile eneo kwa muda kidogo, lakini hakuona kitu chochote kipya zaidi ya ule ushahidi kuwa lile gari liliacha njia na kuparamia shamba la viazi la yule mzee aliyekuwa akidai polisi imlipe kwa hasara ile, na kuishia kujibamiza kwenye ule mti mkubwa. Hata hivyo, hakutegemeaa kukuta kitu chochote cha kumsaidia katika eneo lile, hasa baada ya wale askari wa wilaya ya Kisarawe kulipitia eneo lile.
Aligeuka na kuanza kurudi kwenye gari lake.
“Sasa na we’ nd’o unaniambiaje kijana? Shamba langu ndio kama hivi…” Yule mzee alimuuliza.
“Kama hivi vipi?” Brian alimuuliza huku akifungua mlango wa gari lake.
“Si limevamiwa na kutifuliwa namna hivi..!”
Brian Koba aliingia kwenye gari lake na kutia moto.
“Mzee mimi nadhani we’ ungeshukuru tu kwa kuvuniwa shamba lako bure, au sivyo…?” Alimjibu na kuondoka eneo lile kwa kasi, akimuacha yule mzee akiwa kinywa wazi.
Mwendo mfupi mbele aliwakuta wale askari wawili wakiendelea kutembea kwa miguu kufuata barabara. Aliwapigia honi, na walianza kutabasamu na kumpungia mikono kwa ishara ya kumsimamisha ili awepe lifti.
Konstebo Brian Koba alibadili gea na kuongeza kasi huku akiwapungia mkono kwa dirishani, akiwaacha wale askari wakiwa wameduwaa barabarani.
Inspekta Gezza Dilunga aliingizwa kwenye chumba kidogo na kuambiwa asubiri hapo, wakati yule mhudumu wa kiume aliyeongozana naye akifungua mlango mwingine mzito uliokuwa ndani ya chumba kile na kupotelea ndani ya chumba kingine. Akiwa peke yake kwenye kile chumba, Dilunga aliliendea dirisha lililokuwa upande mmoja wa chumba kile na kuchungulia nje, ambapo aliona kuwa lile kundi la watu lilikuwa kubwa zaidi, na Bruno Mgimba akiongea na nesi mmoja wa pale hospitali.
“Oh, Shiit!” Aliilaani hali ile na muda huo mlango wa kile chumba kingine ulifunguliwa na Dokta Shabbir alitoka akifuatana na yule mhudumu wa pale hospitali.
“Dokta…wakataze manesi wako kuongea na waandishi wa habari juu ya habari ya vifo hivi…uchunguzi bado unaendelea na tusingependa wananchi waanze kusoma habari za kubahatisha kwenye magazeti na kutuletea matatizo zaidi!” Alimwambia huku akioneshea kule nje ya dirisha. Dokta Shabbir alichungulia pale dirishani na kumuona Bruno Mgimba akiongea na yule nesi. Alimgeukia yule mhudumu wa kiume na kumuashiria kwa kichwa aende kumtoa yule nesi pale kwa yule mwandishi wa habari, na yule mhudumu alitoka haraka kwenye chumba kile. Shabbir akamgeukia Inspekta Dilunga.
“Yes Inspekta…hali si nzuri sana bwana…” Alimwambia, na Inspekta Dilunga aliuma meno kwa kutopendezwa na taarifa ile.
“Una maana gani hali si nzuri?” Alimuuliza.
“Ah! Hali ya yule kijana ni ngumu sana…Dokta Nigel bado anaendelea na uchunguzi na nasikitika leo hatuwezi kujua lolote mpaka kesho. Amemdunga sindano ya usingizi ili atulie huku akiipa dawa aliyompatia ifanye kazi ipaswavyo…”
“Kwa hiyo hakuna mabadiliko yoyote…?”
“Hakuna…na sasa Dokta Nigel anamshughulikia huyu mzee aliyeletwa sasa hivi, bila shaka naye kesi yake itakuwa kama ya yule kijana tu…ni nini kinatokea Inspekta? Ni mambo gani haya?” Dokta Shabbir alimwambia na kuishia kumuuliza kwa wasiwasi, na katika macho yake, Inspekta Dilunga aliona hofu ya wazi.
“Kwa nini unasema hivyo Dokta…?” Alimuuliza huku udadisi wake ukiwa juu kabisa.
Badala ya kumjibu Dokta Shabbir alimuongoza hadi ndani ya kile chumba alichokuwamo kabla Inspekta hajafika, ambamo ile miili ya wale vijana watatu waliokutwa wamekufa kule barabarani ilikuwa imelazwa juu ya meza tatu kubwa za chuma, na kumpeleka hadi pale ulipokuwa umelala ule mwili wa hayati Huba binti Malambi.
“Hebu tazama hili jeraha Inspekata…”
Kwa mara nyingine Inspekta Dilunga alijikuta akilitazama lile jeraha la ajabu lililokuwa kifuani kwa yule binti. Na wakati akilitazama, aliona kama kuna kitu hakikuwa sawa katika jereha lile, ila hakuweza kugundua ni kitu gani. Akili ilimzunguka.
“Hilo jereha limetokea ndani kuja nje Inspekta!” Dokta Shabbir alimwambia.
“WHAAAT…?” Inspekta Dilunga alimaka huku akiliinamia zaidi lile jeraha, na hata pale alipobwatuka mshituko ule, alielewa ni kitu gani ambacho hakikuwa sawa katika lile jeraha, na alizidi kuchanganyinikiwa
Eeeeh, Mungu! Vitu gani hivi unavyotuletea sasa…?
Inspekta Dilunga alimtazama yule Dokta kwa macho yaliyojaa maswali, akageukia tena ule mwili wa hayati Huba binti Malambi uliolala bila uhai pale mbele yake, na kwa mara nyingine akajithibitishia kichwani mwake kuwa hakika safari hii alikuwa amekutana na kesi isiyo ya kawaida.
Alilitazama lile jeraha lililokuwa pale kifuani kwa yule binti, na hakika aliona kuwa kingo za jeraha lile la ajabu zilikuwa zimefunukia nje ya mwili ule, ikileta picha kuwa yeyote aliyesababisha jeraha lile, alikuwa akiuachana ule mwili wa yule binti kutokea ndani!
“Lakini hii haiwezekani! Ni nani anayeweza kufanya mambo haya…?” Inspekta alijisemea mwenyewe kwa mshangao mkubwa.
“Inspekta hata mimi nataka kusema hivyo hivyo, lakini ukweli uko wazi mbele ya macho yetu Dilunga…hilo jeraha limetokea ndani, kama ni kisu, basi kilikuwa ndani ya huo mwili na ku…” Dokta Shabbir alimwambia, na hapo hapo Inspekta alimkatisha.
“Lakini hilo linawezekana Dokta…! Wewe ndiye daktari hapa, nataka ushauri wako wa kitabibu, linawezekana hili?”
Dokta Shabbir alitikisa kichwa kwa nguvu.
“Haliwezekani na sijawahi kuona…ndio maana nikakuuliza wewe, ni nini kinachotokea hapa? Wewe ndiye mpelelezi hapa, nami nataka kujua ni vipi hali kama hii inakuwa…!” Shabbir alimtupia mpira Dilunga. Inspekta Dilunga alijishika kiuno na kulitazama tena lile jeraha.
“Hili jereha si la bahati mbaya Dokta…ni kitu kama alama fulani ya ajabu ajabu tu kwenye macho ya kawaida, lakini mimi inanipa picha kuwa hii ni alama yenye maana fulani kwa huyo aliyeliweka kwa ukatili wa hali ya juu kwenye huu mwili wa huyu mtoto maskini…!”
“Sasa ni nani huyo aliyefanya jambo la ajabu kama hili…?” Dokta Shabbir aliuliza tena kwa wasiwasi. Inspekta Dilunga alimtazama kwa muda huku ubongo ukimchemka.
“Ndio maana nikasisitiza sana kuwa ni lazima niongee na yule kijana aliyekutwa katika eneo la tukio! Nahisi yeye ndiye atakayeweza kutuambia ni nini kilichotokea pale…”Alimjibu yule tabibu na kunyamaza kwa muda akifikiri kwa makini, kisha akaongezea kwa sauti ya chini kidogo “…kama ataweza kufanya hivyo…”
Dokta Shabbir alimtazama Inspekta Dilunga kisha akatikisa kichwa .
“Inspekta hapa bado kuna mambo mengi ya ajabu na yanayoacha maswali mengi na hisia zisizokubalika kisanyansi….” Alisema, na Inspekta Dilunga alimgeukia akiwa makini sana.
“Una maana gani Dokta?”
Badala ya kumjibu, Dokta Shabbir aliukamata mkono mmoja wa yule binti kwa mkono wake uliovikwa glovu maalumuu za kitabibu na kumuonesha kucha za yule binti zilizokuwa zimegandiwa damu na mabaki ya ngozi za binadamu ndani yake.
“Inspekta…hii ni ngozi ya binadamu iliyoganda chini ya kucha za huyu binti…na hii unayoona kuwa limegandia kwenye vidole na mikono yake ni damu ya binadamu…”
Inspekta Dilunga alitazama yale aliyokuwa akioneshwa kwa udadisi na umakini mkubwa, moyo ukimuenda mbio kwani alihisi kuwa alichokuwa anaelekea kuambiwa na yule Dokta kilikuwa kitu kingine cha kuzidi kumchanganya.
“Sasa hebu njoo hapa….” Dokta Shabbir alimwambia huku akielekea kule ilipokuwa ile miili ya wale marehemu wawili wa kiume, na kusimama kando ya meza ambapo mwili wa marehemu Uwesu bin Shaame ulikuwa umelazwa chali, majeraha marefu na mazito yakiwa yameurarua mwili wake.
Inspekta alisogea hadi pale kando ya ile meza, tayari hisia zake zote za kiaskari zikiwa makini. Alikuwa amejiandaa kupokea habari nyingine ya kuchanganya.
“Inspekta…nina kila sababu za kuamini kuwa haya majeraha yamesababishwa na mikono ya yule binti aliyelala pale!” Dokta Shabbir alisema huku akioneshea kwa kidole chake cha gumba kule ulipolala mwili wa Huba binti Malambi.
Inspekta Dilunga alibung’aa.
“Atii…?” Ndio neno pekee lililotoka kinywani mwake huku akiwa amekodoa macho.
“Yes!” Dokta Shabbir alithibitisha kauli yake ile kwa msisitizo, na macho madogo ya Inspekta Dilunga yaliongezeka ukubwa kwa mduwao uliozidi viwango.
Ukimya ulitanda wakati Inspekta Dilunga akiyakodolea macho yale majeraha mabaya yalikokuwa mwilini mwa yule marehemu asiye jina kwake, na kujikuta akipuliza upepo nje ya kinywa chake kama mtu anayejaribu kuzima moto kwa pumzi, na kujishika kichwa, labda kwa kujaribu kukipoza kisichemke zaidi, au ndio kuchanganikiwa kwenyewe…na kwa kufanya hivyo akaipangusa na ile kofia yake ya polisi iliyokuwa kichwani kwake, ambayo ilianguka sakafuni.
“Oh Shiit…!” Alilaani hali ile huku akiinama kuiokota ile kofia, na mara mlango wa mle ndani ulivamiwa kwa kishindo, huku zikisikika sauti za mabishano.
Haraka sana Inspekta Dilunga, ambaye tayari hisia zake zote zilikuwa wima kutokana na hali aliyokuwa akikutana nayo wakati ule, alijigeuza huku akichomoa bastola yake, wakati huo huo akipiga goti moja pale sakafuni, bastola ikiwa tayari imeelekea kule mlangoni kilipotokea kile kishindo.
“Tulia wewe…! Polisi…! Alibwata huku akiwa tayari kushambulia na wakati huo huo Dokta Shabbir naye akigeukia kule mlangoni huku akiropoka neno la mshtuko.
“Heeeyy…yyy! Amani! Amani… Ni mimi tu jamani!” Konstebo Brian Koba alisema haraka haraka huku akiwa ameinua mikono yake juu, akifuatiwa na askari mmoja wa jeshi la polisi aliyekuwa nje ya mlango wa ile hospitali na wahudumu wawili wa pale hospitali.
“Afande, tulimshauri asubiri tuje kukutaarifu lakini yeye akaamua kuja moja kwa moja…” Yule askari wa jeshi la polisi alimwambia Inspekta Dilunga kwa jazba huku akimtazama yule askari kutoka mjini kwa jicho la pembeni.
Hasira ilikuwa wazi usoni mwa Inspekta Dilunga wakati akiinuka kutoka pale chini huku akiirudisha bastola yake kwenye mkoba maalumu uliokuwa kiunoni kwake na akiiweka ile kofia yake ya polisi kichwani.
Alimtazama yule afisa wa polisi aliyeingia kwa vishindo ndani ya chumba kile cha uchunguzi wa kitabibu na macho yake yalizidi kuwa madogo kwa ghadhabu.
“Wewe ni nani…na vipi unaingia kwa vurugu namna hii humu ndani ningeweza kuku-shoot bure!” Alimuuliza huku akimsogelea.
Konstebo Brian Koba alimtazama yule Inspekta mtu mzima, na kusaluti.
“Konstebo Brian Koba afande! Kutoka makao makuu ya polisi Dar es Salaam. Nafuatilia kesi hii hii unayoishughulikia na ninadhani nina taarifa za kusaidia sana katika suala hili…nami pia nahitaji msaada kutoka kwako juu ya hili…cha ajabu hawa wenzangu wananizuia kuja kukuona kwa sababu ambazo kwangu hazina msingi!” Brian Koba alijieeleza kwa kirefu na kujiamini sana mbele ya yule Inspekta.
Inspekta Dilunga alimtazama yule askari mfupi na hakummaliza. Alitaka amtamkie maneno mengi makali yaliyomjia kichwani wakati ule, lakini aliwahi kujizuia, na hatimaye akamuuliza.
“Kwa hiyo ukaamua kuingia kwa nguvu?”
Lakini macho ya Koba yalikuwa yamenasa kwenye ule mwili wa yule binti aliyelala juu ya ile meza ya bati iliyokuwa jirani na pale alipokuwa amesimama.
“Oh, My God! Ni nani huyu….?” Aliuliza huku akilitazama lile jeraha la ajabu lililokuwa kifuani kwa yule marehemu.
“Konstebo!” Inspekta Dilunga alimkemea, na mara moja Brian Koba akawa makini na kumgeukia yule Inspekta, lakini tayari uso wake ulikuwa umeshapata ile taswira ya mashaka inayomvaa kila anayeliona lile jeraha la ajabu pale kifuani kwa yule binti.
“Samahani afande…lakini…hii hali ya hapa…” Brian Koba alisema huku bado macho yake yakirudi tena na tena kwenye ule mwili wa yule binti.
Inspekta Dilunga aliwageukia wale wahudumu pamoja na yule askari aliyekuwa akijaribu kumzuia Brian.
“Okay…mnaweza kwenda afande…huyu nitamalizana naye mimi!” Aliwaambia, na wale wahudumu pamoja na yule askari walitoka nje ya chumba kile.
Muda wote huu Dokta Shabbiri alikuwa kimya akimtazama kwa makini yule konstebo toka mjini, na wakati huo huo akionesha kuvutiwa na tabia ile ya uchakaramu wa yule askari kijana.
Inspekta Dilunga alimgeukia Brian Koba.
“Naweza kuona kitambulisho chako cha kazi afande?” Alimuuliza, na Brian alimshangaa.
“Khah, afande… kitambulisho…?” Aliuliza huku akijitazama zile nguo zake za kiaskari alizovaa, na kumtazama tena yule Inspekta kwa macho ya kuuliza.
“Hizo ni nguo tu umevaa kijana, toa kitambulisho au nakuweka chini ya ulinzi sasa hivi!”
Brian Koba alimtazama yule Inspekta kwa muda, kisha taratibu, bila ya kuondoa macho yake usoni kwa yule Inspekta, alitoa kitambulisho chake na kumkabidhi. Inspekta Dilunga alikitazama kile kitambulisho na kujidhihirishia kuwa kilikuwa halali. Alikirejesha huku akimwambia, “Umevuka mipaka Konstebo…hili ni eneo langu na unapofika hapa ni wajibu kuripoti kwangu kwanza kama jinsi ulivyokuwa ukishauriwa na wenzakko huko nje. Lakini tuliache hilo… ni kipi kilichokuleta hapa, na ni kesi ipi hiyo unayodai kuwa sote tunaishughulikia?”
“Kesi ya Chambuso na wenzake!” Brian alijibu huku akimtazama moja kwa moja machoni yule Inspekta, akijua kuwa lile jibu huenda likamchanganya yule askari, na kweli.
“Chambuso na wenzake…? Ongea zaidi askari, sikuelewi!” Dilunga alimuuliza akiwa makini sana.
Badala ya kujibu, Konstebo Brian Koba alimtazama Dokta Shabbir, kisha akamgeukia yule Inspekta, na Inspekta Dilunga alielewa.
“Ongea tu, Dokta Shabbir ni daktari wa polisi, na anaelewa mambo mengi tu kuhusiana na umuhimu wa kutunza siri za kikazi…” Alimwambia.
“Nimekuja kumtafuta kijana aitwaye Chambuso Mwagala, na wenzake wawili waliokuwa wakisafiri kwa kutumia gari aina ya Ford Anglia lenye namba za usajili DSM 14…gari ambalo nimepigiwa simu na askari wa usalama barabarani wakinitaarifu kuwa limepatwa na ajali kwenye barabara ya Pugu-Kazimzumbwi…”
Brian alimjibu kwa kirefu, na hapo aliona kuwa alikuwa amekamata udadadisi wa yule Inspekta.
Inspekta Dilunga alimakinika mara dufu pale aliposikia jina la Mwagala likitajwa na yule askari machachari kutoka mjini, kwani alikumbuka kuwa kadi ya gari iliyopatikana ndani ya lile gari lililopata ajali ilionesha kuwa mmiliki wa lile gari alikuwa ni mtu aitwaye Mwagala Kifyagi.
“Nadhani mimi na wewe tunahitaji kuketi na kuongea kwa kirefu juu ya hili suala, kisha tutarudi kwa Dokta Shabbir kwa maelezo mengine kuhusiana na kesi hii ya iana yake…” Inspekta Dilunga alimwambia Brian huku akimtoa nje ya chumba kile na kwenda kuketi naye kwenye kile chumba cha pili pale hospitali.
Ndani ya nusu saa iliyofuata, wale askari wawili waliokutana katika mazingira yasiyo ya kirafiki sana, walibadalishana taarifa walizokuwa nazo juu ya kesi ile. Baada ya hapo, kila mmoja kati yao alikuwa amepata mwanga mpya juu ya kesi ile, lakini wote bado walibaki wakiwa wamechanganyikiwa, ila safari hii, ni Brian Koba ndiye aliyechanganyikiwa zaidi, kwani aliyoelezwa na Inspekta Dilunga juu ya yaliyowakuta wale vijana watatu waliokuwa wakiendesha lile gari lenye namba za usajili DSM 14, yalikuwa ni nje kabisa ya mafikirio yake.
“Duh, Inspekta! Hakika hii ni kesi moja ya ajabu sana. Yani ina maswali mengi kuliko majibu…!” Brian Koba alimwambia Inspekta Dilunga mara baada ya kupeana mustakabali wa suala lile la gari namba DSM 14 pamoja na watu waliokuwa ndani yake. Inspekta Dilunga alitikisa kichwa kwa masikitiko kabla ya kuongea.
“Hiyo ni sahihi konstebo…lakini kwa upande wangu lazima niseme kuwa sasa nina mwanga angalau kidogo juu ya hawa vijana waliokuwa kwenye hilo gari ingawa bado kuna mambo mengi sana hayajawa wazi.”
“Kama ndio wao, maana bado sijawaona na hata mimi sikuwa nimepata kuwaona kabla”.
“Ni kweli, lakini bado kuna mwanga kidogo sasa…na maswali mengi pia.”
“Ndiyo…mojawapo likiwa ni nini kilichowaleta huku hawa vijana…” Brian alijibu.
“Na ilikuwaje hata wakakutana na yule binti pale barabarani …au yule binti alifikaje pale barabarani…” Dilunga aliongezea.
“Na nini kilichomfanya huyo kijana mwingine abaki akikodoa macho mfululizo kama…kama…oh, Mungu wangu….kama kitu gani tu sijui!” Brian aliongezea. Sasa walikuwa wakiongea kwa namna ya kuchanganywa na ule mzigo wa maswali uliowaelemea. “Sasa siyo huyo kijana tu, bali na baba wa yule binti naye yuko kwenye hali hiyo hiyo bwana…” Dilunga alisema kwa fadhaa iliyochanyika na hamaniko.
“Eti bwana! Hivi ni nini lakini kilichotokea hapa Ispekta…?” Inspekta Dilunga alimtazama yule konstebo kijana kwa muda, na badala ya kumjibu alitupa mikono yake hewani na kubaki akitikisa kichwa tu.
“Nadhani hilo ni swali lenye thamani ya paundi milioni mia moja Konstebo…na tukiweza kulijibu hilo swali basi utata wote huu utakuwa umetoweka…” Hatimaye alimjibu.
Konstebo Brian Koba alimtazama kwa makini, kisha akasema taratibu sana, “Neno muafaka hilo Inspekta…”
“Nini…?” Inspekta Dilunga alimuuliza, wazi kuwa hakumuelewa.
“Utata…nadhani hilo ni neno muafaka kwa kesi hii…utata…” Alifafanua.
“Yeah…” Dilunga aliafikiana naye huku akitikisa kichwa, na kuendelea huku akionekana kuzidi kulitafakari neno lile, “…utata…utata mkubwa…”
Kimya kilitawala kwa muda, kisha Dilunga akaongea tena huku bado akionekana kulitafakari neno lile, “Na kibaya zaidi…inawezekana kweli yale majeraha yawe yamefanywa na yule binti?”
“Aaah ….ila hapo nadhani itabidi turudi tena kwa Dokta Shabbir….kwani naona ni jambo lisilowezekana…” Brian alimwambia na mara moja Inspekta Dilunga aliinuka na kuongoza kwenye kile chumba kingine ambamo walimuacha Dokta Shabbir akiendelea na uchunguzi zaidi wa ile miili.
Konstebo Brian Koba alimfuata yule Inspekta mrefu, mweusi, mtu mzima, na kwa mara nyingine alipata fursa ya kuutazama tena ule mwili wa yule binti mwenye jeraha la ajabu kifuani mwake.
Dokta Shabbir alirudia tena maelezo aliyokuwa akimpa Inspekta Dilunga kabla Brian Koba hajavamia mle ndani, kwamba alikuwa ana kila sababu za kuamini kuwa yale majeraha yaliyokuwa kwenye ile miili ya wale marehemu wawili wa kiume yalikuwa yamefanywa kwa mikono ya yule binti.
“Dokta…yawezekana vipi lakini hiyo..?” Brian Koba aliuliza kwa mshangao.
“Mabaki ya ngozi na damu katika mikono ya huyu binti…chini ya kucha zake…vinashabihiana sana na damu na ngozi…kitaalamu tunaita Tissue sample…za hawa marehemu. Kwangu mimi kama mtaalamu wa miili ya binadamu hiyo inaniambia kuwa ni huyu binti ndiye aliyesababisha majeraha haya.!” Dokta Shabbir alizidi kuthibitisha.
Askari wawili walibaki hoi. Brian Koba aliitaza ile mikono ya yule binti na kuona zile damu na vipande vya ngozi na nyama vikiwa vimegandia kwenye vungu za kucha za yule binti. Aliuendea ule mwili wa mtu aliyekuwa akijulikana kama Uwesu bin Shaame na kuutazama kwa karibu kwa mara ya kwanza, sasa Inspekta Dilunga alikuwa akimtazama Brian kwa makini, akitaka kuona iwapo ataweza kumtambua yule kijana.
“Mungu wangu, Inspekta!” Brian alimaka huku akimgeukia Inspekta Dilunga na kusema, “Huyu mtu lazima atakuwa ameraruriwa na mnyama mkali na mwenye nguvu sana! Sio…sio yule binti…haiwezekani!”
Dokta Shabbir na Inspekta Dilunga walimtazama bila ya kusema neno. Dokta Shabbir alishaeleza alichokiana kutokana na utaalamu wake, na Inspekta Dilunga alishapitia mshituko kama ule hapo awali, na hakuwa na kingine cha kumshangaza zaidi kwenye jambo lile isipokuwa kuzidi kumchanganya tu.
Brian aliwatazama wale watu kwa mshangao uliokithiri, kisha akaondoka hadi kwenye mwili wa aliyekuwa Esmund Bwaira na kuyakodolea macho yake majeraha, na kilichomjia kichwani mwake kilikuwa ni kile kile; kuwa haikuwezekana kabisa yale majeraha yawe yamefanywa na yule binti dhaifu.
Lakini Dokta Shabbir anasema hivyo ndivyo ilivyo! Na sababu anazotoa kitaalamu zinaleta maana.
Hakika Konstebo Brian Koba alichanganyikiwa, tena alichanganyikwa vibaya sana. Alipeleka macho yake usoni kwa yule kijana aliyelala pale juu ya ile meza na mara moja sura ya mke wa Mzee Bwaira ikamjia. Muda wote Inspekta Dilunga alikuwa akimtazama na akaona kuwa ameweza kumtambua yule kijana.
“Unamtambua huyo kijana afande?” Alimuuliza kama njia ya kutaka kuthibitisha hisia zake. Brian Koba alimgeukia.
“Mmnh! Sijapata kumuona hata siku moja huyu kijana, lakini kutokana na sura yake, nahisi huyu atakuwa ni Esmund Bwaira, mmoja wa wa vijana walioondoka na Chambuso Mwagala…sura yake inshabihiana sana na mama yake, mke wa mzee Bwaira…” Alisema. Inspekta Dilunga aliafiki kwa kichwa na kumuuliza juu ya ule mwili wa kwanza. Brian Koba alirudi tena hadi kwenye mwili wa Uwesu na kumtazama kwa muda yule kijana, kisha akatikisa kichwa.
“Hapana…hapa sioni mshabihiano wowote na aidha mzee Shaame au mzee Mwagala, ingawa huyu kijana anaonekana wazi kuwa alikuwa na asili ya ki-unguja au ki-pemba.”
“Hivyo inawezekana huyo akawa ndiye Uwesu Shaame…?” Dilunga aliuliza, na Brian aliafiki kwa kichwa, na kuongezea, “Lakini nitakuwa na hakika zaidi iwapo nitamuona huyo kijana wa tatu ambaye mnasema amebaki akikodoa macho tu…huenda huyo ndiye akawa Chambuso mwenyewe…”
Dokta Shabbir aliwaongoza wale askari hadi kwenye wodi ambamo kijana Chambuso Mwagala alikuwa amelazwa akiwa amelala usingizi mzito wa madawa. Brian Koba na Inspekta waliusogelea ule mwili na aliutazama uso wa yule kijana Brian hakuhitaji kujiuliza mara ya pili. Alikuwa ni mzee Mwagala mtupu!
“This is my man Inspekta… huyu ndiye Chambuso Mwagala huyu!” Konstebo Brian Koba alisema huku akimtazama yule kijana mwenye bahati mbaya kabisa hapa duniani.
“Una hakika…?” Dilunga aliuliza.
“Kab-bisa Inspekta…yaani amefanana kabisa na Mzee Mwagala Kifyagi, baba yake!”
“Basi yule pale anaweza kuwa Uwesu Shaame…” Dokta Shabbir alisema na Inspekta Dilunga aliafiki kwa kichwa huku akiwa ameuma midomo yake na uso ameukunja kwa mawazo. Na muda huo mhudumu mwingine wa kiume wa hospitali aliingia mle ndani na kumkabidhi Dokta Shabbir faili dogo jembamba na kutoka. Shabbir alilifunua lile faili na kuanza kulisoma akiwa amesimama, na kadiri alivyokuwa akizidi kulisoma, ndivyo uso wake ulivyozidi kuonekana kubadilika na kujaa mchangayiko wa hisia.
“What is it Shabbir…?” Inspekta Dilunga alimuuliza huku akimtazama kwa makini. Dokta Shabbir aliinua uso wake kumtazama yule askari na kurudia tena kulisoma lile faili pasina kufanya bidii yoyote ya kumjibu.
“It does’nt make sense…” Alisema peke yake huku akitoka haraka mle ndani akiwaacha wale askari wakiwa wamepigwa butwaa.
“What is it that doesn’t make sense now Doctor…?” Inspekta Dilunga alimpigia kelele huku akimfuata, Brian Koba akiwa nyuma yake huku akili ikimzunguka.
Walimkuta akiwa ameketi nyuma ya meza iliyokuwa kwenye kona moja ya kile chumba kingine, nje ya kile ambamo ndani yake kulikuwa kuna ile miili ya wale vijana waliouawa kule barabarani. Mikononi mwake alikuwa ameshika karatasi moja wakati macho yake yakiwa kwenye lile faili alilokabidhiwa na yule mhudumu muda mfupi uliopita, sasa hivi likiwa wazi juu ya meza iliyokuwa mbele yake.
“Shabbir! Hebu ongea na mimi Dokta…ni nini hicho ambacho unasema kuwa haki…” Inspekta Dilunga alianza kumkemea yule tabibu, lakini muda huo Dokta Shabbir alimuinulia mkono kumnyamazisha huku bado akiwa amekunja uso akisoma zile karatasi zilizokuwa mkononi mwake, akijaribu kulinganisha kilichoandikwa kwenye zile karatasi na ile taarifa iliyokuwa kwenye lile faili lililokuwa mbele yake juu ya ile meza.
Inspekta Dilunga na Konstebo Brian walitazamana, na Konstebo Brian alibetua mabega na midomo yake huku akiketi kwenye kiti kilichokuwa mbele ya ile meza.
Inspekta Dilunga alienda kusimama kwa muda nyuma ya dirisha la chumba kile, kisha akarudi tena pale mezani na kuweka mikono yake juu ya ile meza huku akimuinamia yule daktari wa polisi. “Ongea na mimi Dokta, tena ongea na mimi sasa hivi!” Alimkemea yule Dokta, na taratibu Dokta Shabbir aliinua uso wake na kumtazama yule askari, uso wake ukiwa umehamanika, na hivyo kuzidi kumjaza wahka Inspekta Dilunga.
“Ni nini unachoona hapo na kinahusiana vipi na kesi hii? Leo moja hii tu tumeshapata vitendawili kibao mpaka sasa katika kesi hii, na hatutaki vitendawili zaidi kutoka kwako Dokta…what the hell is that?” Dilunga alimkoromea yule tabibu huku akiwa ametumbua macho na akitomasa kidole chake kuelekea pale kwenye lile faili lililokuwa mbele ya Dokta Shabbir. Brian Koba alikuwa akitazama kisanga kile kwa makini.
Dokta Shabbir alikohoa kidogo kisha akashusha macho yake hadi kwenye lile faili, na kuzitazama zile karatasi zilizokuwa mkononi mwake, na kumtazama tena Inspekta Dilunga aliyekuwa amemuinamia na akihema kwa nguvu, pua zikimtanuka na kumsinyaa haraka haraka.
“Samahani Inspekta, hii ripoti kidogo imenichanganya kwani…muda wa vifo hauoni!” Dokta Shabbir alisema huku akionekana wazi kuwa alikuwa amechanganyikiwa.
“Fafanua Dokta tafadhali…sijakuelewa, una maana gani muda wa vifo hauoni?” Dilunga aliuliza.
“Yeah, hapo inabidi ufafanue mzee…” Konstebo Brian naye alidakia. Dokta Shabbir aliwatazama wale askari wawili, kisha akaongea kwa upole sana, kama kwamba akitaka kuyapa muda maneno yake yazame vichwani mwa wale watu waliokuwa mbele yake.
“Hii ni ripoti ya muda ambao vifo vya wale vijana vilitokea…na inaonesha kuwa kuna tofauti ya saa nzima baina ya vifo hivi.”
“Sasa hilo ni tatizo Dokta…?” Brian aliuliza.
“Lisingekuwa tatizo kama isingeonesha kuwa Huba binti Malambi alianza kufa saa moja kabla ya hawa vijana wawili!” Dokta Shabbir alisema, na wale askari bado walibaki wamkitazama kama kwamba hawakuwa wameelewa maana ya kauli ile, na kisha taratibu uzito wa kauli ile ukazama vichwani mwao.
“Ah! Itawezekana vipi…?” Brian Koba alisema kwa mshangao.
“Sasa …kama alianza kufa, vipi tena iwe yeye ndiye aliye wajeruhi wale vijana na hatimaye kusababisha vifo vyao?” Inspekta Dilunga aliuliza huku naye akionesha kuwa ameshachanganywa na taarifa ile ya Dokta Shabbir.
“Na hicho ndicho hasa ninachokiona kuwa hakileti maana Inspekta!” Dokta Shabbir alisema kwa hisia kali.
Ukimya ulitanda mle ndani, kila mmoja akiwaza vyake, wote wakiwa wamechanganyikiwa.
“Sina nia ya kuonesha kuwa siamini uwezo wako wa kitatibu Dokta, lakini hivi vipimo vyenu viko sahihi kweli…?” Brian aliuliza. Dokta Shabbir alisisitiza usahihi wa vipimo vile, na kwamba alikuwa amevichukua yeye mwenyewe na kuvikabidhi kwa vijana wa maabara kutoa ripoti yake.
“Basi aidha ripoti kuwa Huba ndiye aliyewaua hawa vijana si sahihi… ” Brian alisema, na hapo hapo Dokta Shabbir alimkatisha.
“Hiyo sina shaka nayo hata kidogo! Tissue sample zinakubaliana kabisa”
“….au hii ripoti yako ya pili ina makosa.” Brian alimalizia. “Hapana kijana. Hii ripoti iko sahihi, mimi ndiye ninayejua! Ingawa haileti maana, ripoti iko sahihi…Huba binti Malambi amefariki saa moja kabla ya hawa vijana wawili mabwanwa! Sasa ni juu yenu kuutatua utata huu, lakini ripoti hii ndiyvo inavyosema…na imesainiwa na Dokta Nigel Smith mwenyewe….!” Dokta Shabbir alisisitiza, na wale askari walichoka.
“Kwa hiyo alikufa kwanza halafu akaja kuwashambulia na kuwasabibishia vifo hawa vijana…halafu akafa tena…au…?” Brian Koba alijaribu kupata maana ya maneno ya Dokta Shabbir, lakini akaishia njiani, hakupata maana. Alimgeukia Inspekta Dilunga.
“Hii imeshakuwa kesi ya kipekee kijana, yatupasa kuwaarifu wakuu haraka sana!” Inspekta Dilunga alisema.
Ndani ya nusu saa iliyofuata simu baina ya Kisarawe na Dar es Salaam zilipigwa. Taarifa za mkasa uliowakuta vijana watatu kutoka mjini waliokuwa wakiendesha gari namba DSM 14 zilifika makao makuu, na hatimaye kwa wazazi wa watoto wale.
Ilikuwa ni heka heka kubwa.
Wakati vilio vikishamiri nyumbani kwa familia walizotokea wale vijana, ving’ora vya gari mbili za polisi kutoka Dar es Salaam vilikuwa vikirindima njia nzima kuelekea Kisarawe, moja ikiwa imembeba Superintendent Tib Haggard, na nyingine ikiwa imewabeba wazazi wa kiume wa wale vijana watatu kutoka mjini kwenda kuitambua miili ya vijana wao, na mwingine kwenda kumtambua mwanaye aliyebaki amekodoa macho mfululizo hadi alipopigwa sindano ya usingizi.
Na katika saa mbili zilizofuatia, mji wa Kisarawe ulizizima kwa pilika pilika za huku na huko, wakati wana usalama wakihangaika kuwadhibiti wananchi waliojaa udadisi, na mwandishi Bruno Mgimba akiwa makini na kila kilichokuwa kikiendelea pale mjini, hasa eneo la ile hospitali ya wilaya ambapo msafara kutoka Dar ulifikia.
Baada ya wazazi wale kuwatambua watoto wao, Superintendent Tib Haggard aliitisha kikao cha dharura na watendaji wake wakuu wa wilaya ya Kisarawe, na ndani ya kikao kile, ile kesi ilikabidhiwa rasmi kwa Inspekta Dilunga na Inspekta mpya katika jeshi la Polisi, Brian Koba.
Tib Haggard alimpandisha cheo Brian Koba siku ile ile. Ilikuwa ni siku ambayo yule Inspekta mpya kijana hatoisahau maishani mwake.
Ilikuwa ni tarehe 9 Disemba, mwaka 1961…
Superintendent Tib Haggard aliafikiana na watendaji wake kuwa ile kesi ilikuwa ni kubwa na iliyohitaji afisa mwenye hadhi iliyoendana na uzito wa kesi ile. Aidha, wote walikubaliana kuwa kwa vile kesi ilitokea wilaya ya Kisarawe na ilihusisha kifo cha mkazi wa wilaya ile, ni vyema ikasimamiwa na afisa kutoka wilaya ile, na moja kwa moja Inspekta Dilunga ndiye aliyekabidhiwa jukumu hilo.
Lakini kwa kuwa pia kesi ile ilihusisha vifo vya wale vijana wawili kutoka jijini Dar es Salaam, na ugonjwa usiojulikana wa kijana wa tatu kutoka huko huko jijini, iliamuliwa kuwa apatikane afisa mwingine kutoka mjini ambaye atashirikiana na mpelelezi mwenyeji kuendesha uchunguzi na hatimaye ufumbuzi wa kesi ile iliyoumiza vichwa vya watendaji wa jeshi la polisi waliohudhuria kikao kile cha dharura.
Ndipo badala ya kuleta afisa mwingine kutoka mjini, Superintendent Tib Haggard alipitisha uamuzi wa kumpandisha cheo Konstebo Brian ili awe na mamlaka yanayohitajika katika kuendesha upepelelezi wa kesi ile, na kumhamishia Kisarawe kwa muda wote ambao uchunguzi wa kesi ile utakuwa unaendelea.
Brian Koba hakuamini.
“Nimefanya kazi kwa muda mrefu na Brian Koba, hivyo najua fika kuwa utendaji wake ni mzuri na unahitaji kupewa nafasi ya kubeba majukumu makubwa…” Superintendent Tib Haggard aliwaambia watendaji wake wa wilaya, na kutembeza macho yake ya bluu kwenye nyuso zao mmoja baada ya mwingine. Macho yalitembea mle ndani, na baadhi ya maafisa wa juu katika jeshi la polisi pale wilayani walianza kumtazama Brian Koba kwa mtazamo mpya, wakati Brian mwenyewe alibaki akitazama mbele moja kwa moja bila kutikisika wala kupepesa macho, moyo ukimpiga kwa nguvu.
“…na pamoja ya kuwa tayari nilikuwa nimeikabdihi hii kesi mikononi mwake kabla ya kujua uzito wake, bado naamini kuwa iwapo kuna afisa yeyote atakayeweza kusaidiana kikamilifu na Inspekta Gezza kwa moyo, ujasiri na ikibidi ukorofi unaohitajika, (hapa Tib haggard alicheka kidogo huku akimtazama Brian kwa jicho la kujua), basi mtu huyo ni Brian…” Superintendent Haggard aliwaambia watendaji wake na Konstebo Brian alihishi kichwa kikimtanuka.
“Ndio maana kwa kutilia maanani uzito wa kesi hii, napenda kuchukua mamlaka yaliyowekwa juu yangu kumpandisha cheo Konstebo Brian Koba na kuwa Inspekta kuanzia leo hii…”
“Hah!” Brian Koba aliropoka kwa mshtuko, sambamba na sauti nyingine za mishangao mle ndani, macho yakimtumbuka kwa kutoamini alichokuwa amekisikia.
“Ndio!” Tib Haggard alidakia kwa msisitizo, na kuendelea, “…kwa hivyo sasa nina ma-Inspekta wawili watakao ishughulikia kesi hii, na nitahisi kuwa nimeangushwa na nimefedheheshwa vibaya sana iwapo kesi hii itashindwa kutatuliwa haraka iwezekanavyo!” Tib Haggard alisema na vichwa vilitikiswa mle ndani kuunga mkono kauli ile.
Inspekta Dilunga alitikisa kichwa kwa masikitiko wakati akisikia maneno yale na wakati huo huo akikumbuka yale aliyoyaona na aliyoyasikia tangu taarifa ya vile vifo ilivyofikishwa ofisini kwake asubuhi ya siku ile.
Oh, my God…Tib Haggard anatutakia balaa huyu… hii sio kesi ya kawaida…!
“Na kwako Inspekta Brian …” Tib Haggard aliendelea kuongea, sasa akiwa amemkazia macho yake yaliyoonekana kupenya moja kwa moja hadi ndani kabisa ya moyo wa yanayemtazama, na kuendelea, “…nakukpa cheo hiki na jukumu zito nyuma yake. Utakuwa Inspekta under probation…kwa majaribio…na kipimo cha majaribio hayo ni utendaji na ushirikiano wako na Inspekta Dilunga. Na utatuzi wa kesi hii ndio utakao kuthibitisha katika wadhifa wako huu mpya, unanielewa Inspekta?”
Brian alihisi msisimko wa ajabu mwilini mwake kwa vile kusikia akiitwa kwa kile cheo cha “Inspekta” .
“Ndio afande!” Brian alijibu.
“Vizuri!” Tib Haggard aliafiki.
Inspekta Dilunga na Inspekta mpya Brian Koba walitazamana, na Inspekta Dilunga aliona mng’ao wa ari kwenye macho ya yule askari kijana, na hapo alijua kuwa Tib Haggard alikuwa amepatia sana kwa uamuzi wake ule. Yule kijana atafanya kazi kama punda kuhakikisha kuwa kile cheo alichopewa kinaendelea kubaki kwake.
“Sasa sina haja ya kusisitiza tena juu ya umuhimu wa kesi hii…na hivyo ni wajibu wenu nyote hapa kutoa ushirikiano wa kila hali kwa Inspekta Dilunga na Inspekta Koba….hawa wanabeba jukumu kubwa, lakini sisi tuna jukumu kubwa zaidi…la kuhakikisha kuwa wanapta kila wanachohitaji katika kumaliza tatizo hili moja kwa moja!” Tib Haggard alimalizia maelezo yake na maafisa wote wa polisi waliohudhuria kikao kile waliinuka huku wakipiga makofi .
Tib Haggard alipeana mikono na wale ma-Inspekta wake wawili waliokabidhiwa kesi ile ngumu, alitoka nje ya ukumbi wa kikao kile, na kuingia kwenye gari lake.
Aliwapungia mkono watendaji wake waliojipanga nje ya jengo la makao makuu ya polisi ya wilaya, ambao walisaluti kwa heshima, kisha akampa ishara dereva wake na gari ikaondoka taratibu eneo lile.
Tib Haggard, aliondoka Kisarawe akijua wazi kuwa alikuwa ameiacha ile kesi mikononi mwa askari wawili wenye ari na jukumu lililokuwa mbele yao.
Inspekta Dilunga na Inspekta Brian Koba walienda ofisini kwa Inspekta Dilunga kujadili muelekeo wa kesi ile ngumu.
“Hongera Inspekta…ingawa sasa hili jukumu limeachwa rasmi mikononi mwetu!” Inspekta Dilunga alimwambia Inspekta Brian Koba wakati wakiwa ndani ya gri kuelekea ofisini kwake.
“Yeah…na sasa muuaji au yeyote mwenye siri ya mauaji haya akae chonjo…n’na ari mpya sasa!” Inspekta Koba alisema kwa hamasa.
Inspekta Dilunga alimtazama yule kijana na mdomo wake ukafanya tabasamu dogo. Aliona jinsi yule kijana alivyojaa furaha na ari.
“Umefurahi sana leo, eenh?”
“Saa–nnaa! Hakika hii ni siku muhimu sana kwangu Inspekta…na lazima nidhihirishe kuwa ninastahili cheo hiki nilichopewa leo hii… lazima niiivunje kesi hii!”
Inspekta Gezza Dilunga alitikisa kichwa kwa namna ya kusikitika. “Unadhani unaweza kuitatua kesi hii Inspekta?”
Inspekta Brian Koba alimtupia jicho la pembeni.
“Sio ninaweza Inspekta…tunaweza! Mimi na wewe…!”
“Kwa sababu tu-ma Inspekta…?” Dilunga alimuuliza.
“Oh, come on Inspekta…sote tunajua kuwa hii kesi ni ngumu, lakini haina maana kuwa haiwezekani…! Au unataka kuniharibia siku yangu Inspekta…?”
Inspekta Dilunga aliguna tu, na hakuongea neno jingine hadi mwisho wa safari yao.
Kitu ambacho Inspekta mpya Brian Koba hakukijua wakati ule ni kwamba ingawa yeye aliiona siku ile ya tarehe 9 Disemba 1961 kuwa ni siku muhimu sana kwake, ni kwamba atakuja kuikumbuka kwa majuto makubwa sana siku ile kutokana na mambo yaliyokuwa yakimsubiri mbele yake.
Kwani hakika ile ilikuwa ni siku ambayo, kutokana na ari yake ya kutaka kuthibitishwa katika cheo chake kile kipya cha u-Inspekta alichokuwa akikitamani kwa muda mrefu, alijikuta akijiingiza rasmi historia ya jeshi la polisi hapa nchini.
Utata wa 9/12…
Ripoti kutoka wale ma-koplo waliokuwa wakilichunguza eneo la tukio kule barabarani haikuwa na kipya cha kuwawezesha kuleta japo mwanga mpya kati kesi ile ya aina yake.
Hivyo wale ma-Inspekta waliamua kurudi kule hospitali kuonana na Dokta Nigel Smith. Waliingia kwenye gari la Inspekta Dilunga na kuelekea kule hospitali.
Wale ma-koplo waliomnyima Brian ushirikiano hapo nyuma kule barabarani walibaki wakitazama kwa kutoamini.
“Yaani mara hii jamaa kawa Inspekta!” Mmoja wao alisema kwa mshangao. Mwingine alibaki akitikisa kichwa asiwe na la kusema. Dokta Nigel Smith alikuwa ni mtu mwembamba na mrefu, mwenye hali iliyokaribia kuwa kibyongo. Alipata kiasi cha kama miaka sitini na sita hivi na alionekana kuwa amechoka sana. Brian hakujua iwapo alikuwa katika hali ile ya uchovu kwa uzee, au naye alikuwa amechoshwa na kile kitendawwili cha vile vifo ambayo muuaji wake alionekana kuwa alikufa kabla ya watu aliowaua.
Lakini baada ya kuongea naye kwa muda mfupi, mara moja Brian alijua kuwa Dokta Nigel Smith alikuwa amechoshwa na ile kesi na si uzee.
“Si…Sijawahi kuzaliwa tangu kuona hali kama huyu!” Alisema mwingireza yule kwa sauti iliyotetema, na Inspekata Dilunga alimkodolea macho
“Eti…?”
“Ndio! Hii ni extraordinary!”
Brian alitabasamu kidogo, na kutikisa kichwa kuafiki kuwa kweli yule mzee alikuwa amechanganywa na hali ile.
“Una maana hujawahi kuona tangu kuzaliwa Dokta…sio kuzaliwa tangu kuona…” Alimsahihisha, na yule mzungu alimtazama kama kwamba alichokisema hakikuwa na maana hata kidogo.
“Nakwambia hii ni nguvu nyeusi hii…! Hii ya kwenu Africans tu…” Dokta Nigel alimtumbulia macho, na wale askari wakabaki midomo wazi.
“Yaani uchawi…?”
“What else…?” Dokta Nigel aliuliza huku macho yakiwa yememtoka pima. Wale askari walitazamana
“Hata wewe Dokta unaamini habari kama hizi…?” Dilunga alimuuliza .
“Sasa hii itaelezeka vipi kisanyansi? Huyu binti kweli alikufa one hour before hao vijana wengine …na kweli inaonekana kuwa ni yeye ndiye aliyesababisha haya majerahaa kwa hao vijana…na hao vijana wamekufa kutokana na yale majeraha…”
“Sasa huo ndio uchawi dokata….?” Brian aliuliza, akiwa makini sana.
“Sio hilo tu …ni vipi utafafanua lile jeraha la ajabu kifuani kwa yule binti?” Dokta Nigel aliwauliza, na wale askari wakaona kuna ukweli kwenye lile swali.
“Na wale watu wawili waliobaki wakitumbua macho kama bundi…?” Dokta Nigel alizidi kuwaambia huku akiwa ametumbua macho kwa jazba huku uso ukiwa umemuiva.
“Na hilo ndilo hasa lililotuleta hapa kwako Dokta…kupata maelezo ya kitalaamu juu ya hali ile, na iwapo yeyote kati ya wale watu wawili anaweza kuongea na labda kutupa habari juu ya kitu au mambo aliyoona kabla ya kukutwa na hali ile…?” Inspekta Dilunga alisema.
Dokta Nigel alitikisa kichwa na kujifuta uso wake kwa mikono yake. Brian hakuona alikuwa akijifuta kitu gani, lakini aliona kuwa yule Dokta alikuwa amechanganyikiwa kweli kweli.
“Saa ishirini na nne zijazo ndizo zitakuwa muhimu sana kwa watu hao wawili…iwapo wataamka kutoka kwenye usingizi wa dawa nilozowapa kwa sasa, huenda kukawa na matumaini… lakini kwa mimi sikuona kitu chochote kwao. Kila kitu kinaonekana kiko sawa katika mifumo yao ya mwili na fahamu… isipokuwa kule kukodoa macho na kutoongea kitu tu…!”
“Hata fahamu zao ziko sawa…ubongo haujaathirika…?”
Dokta Nigel alitikisa kichwa kwa masikitiko, na kukaa kimya kwa muda.
“Ndio maana nawaambia hii ni kesi ya mambo mengine ya ajabu-ajabu. Vipimo vyote vya awali vinaonesha kuwa bongo zao hazijaathirika kwa lolote!”
Askari walitazamana.
“Kwa hiyo wanaweza kuongea..?” Brian aliuliza.
“Wataweza kuongea alright …lakini, dalili ni kwamba wanaweza wasikumbuke chochote kilichotokea kabla ya wao kuwa katika hali ile…!”
“WHAAAT…?” Dilunga aliropoka huku akimtumbulia macho yule tabibu.
“Ndio…lakini the next twenty four hours ndizo zitakazoamua juu ya hilo!”
“Basi nami sitakuwa mbali na hospitali kwa saa ishirini na nne zijazo Dokta!” Inspekta Brian Koba alisema. Aliazimia kupitisha usiku wa siku ile akiwa pale hospitali, ndani ya chumba ambamo Chumbuso Mwagala alikuwa amelazwa.
Lakini Inspekta Dilunga alikuwa na mawazo mengine juu ya kadhia ile iliyo jaa utata.
Kabla Brian Koba hajatimiza azma yake ya kupitisha usiku ule wodini kwa Chambuso Mwangala kwa lengo la kuwa jirani na yule kijana pindi atakapozinduka kutoka katika ule usingizi wa madawa, Inspekta Gezza Dilunga alipitisha rai nyingine katika hatua za kujaribu kulipatia ufumbuzi suala lile lililojaa mtungo wa maswali. Alimwita pembeni Inspekta mpya Brian Koba na kumwambia, “Kijana…itabidi tuongee na Superintendent Tib Haggard haraka sana!”
“Halafu tunamwambia nini tukiongea naye haraka sana Inspekta?” Brian Koba alimuuliza.
“Tunamwambia kuwa tunahitaji liitishwe jopo la madaktari kuchunguza upya vifo hivi…na hali za wale watu wawili waliobaki kukitumbua macho kama mijusi iliyobanwa na mlango! Haya maelezo ya Dokta Nigel hayaniingii akilini hata kidogo”
Brian koba alimtazama kwa muda yule Inspekta mzoefu, kisha akatikisa kichwa taratibu kuafikiana na wazo lile.
“Yeah…wazo zuri sana Inspekta, ingawa naamini kuwa Dokta Nigel alisema aliyoyasema kwa kukosa maelezo ya kisayansi juu ya hali iliyojitokeza katika uchunguzi wa miili ile na wale watu wawili waliokumbwa na ule ugonjwa wa kuduwaa mfululizo.”
“Jambo linaloonyesha ni jinsi gani hii kesi ilivyokuwa ngumu…” Dilunga alisisitiza hoja yake.
“Hakika! Kwa sababu bado naamini kuwa walichokiona Dokta Nigel na Dokta Shabbir ndicho kilichopo… wale ni matabibu waliobobea…” Brian alimwambia
“Sawa…sasa tuone ni nini jopo la madaktari nalo litagudua kwenye uchunguzi huu, tena haraka iwezekanavyo, kwani tayari ndugu wa marehemu Uwesu Shaame wameshaanza kudai mwili wa marehemu wao wakazike…”
“Uko sahihi Inspekta, kwani kama kuna mtu anayeweza kuitisha jopo la madaktari kwa uharaka unaohitajika, basi mtu huyo ni Superintendent Haggard”
“Basi sasa na lifanyike litakiwalo, tusizidi kupoteza muda”
Inspekta Brian Koba aliingia ofisini kwa Dokta Shabbir na kutumia simu iliyokuwa mle ndani kuwasiliana na ofisi ya makao makuu ya polisi jijini Dar es salaam.
Huko aliambiwa Superintendent Tib Haggard alikuwa hajafika jijini kutokea kisarawe. Akaacha maagizo kuwa pindi akifika awasiliane naye, akiacha namba ya ofisini kwa Dokta Shabbir na ile ya ofisini kwa Inspekta Dilunga. Kisha akamgeukia Inspekta Dilunga.
“Hilo limefanyika …nini kifuatacho Inspekta?”
“Tukaongee na mzee Mwagala Kifyagi…nadhani sasa atakuwa ametulia kiasi cha kuweza kuongea nasi kwa kituo.” Inspekta Dilunga alielekeza, na wakaelekea sehemu ya kupumzikia ndugu na jamaa wanaopeleka wagonjwa wao pale hospitali ambako walimkuta mzee Mwagala akiwa amejiinamia kwenye moja ya makochi yaliyokuwa sehemu ile.
Yule mzee alipowaona wale askari wawili wakimuendea, aliinuka haraka kutoka alipokuwa ameketi na kuwatazama kwa wasiwasi mkubwa.
“Ku…kuna lolote? Chambuso ameamka?” Yule mzee aliwauliza huku akitembeza macho kutoka kwa Brian kwenda kwa Dilunga na kuyarudisha tena kwa Brian.
“Hapana hali ya Chambuso bado ni ile ile ya usingizi kwa sasa, ila sisi tulikuwa tunataka kuongea nawe kidogo” Brian alimwambia.
“Maswali mengine…” Mzee mwagala alisema kwa huzuni.
“Ndio mzee…” Brian alimwambia.
“Wakati mwanangu anaendelea kulala bila kujijua huko?” Mzee Mwagala aliuliza kwa hasira.
“Hakuna lolote linaloweza kufanyika kwake kwa sasa mzee… tunaomba ushirikiano wako, labda kwa kufanya hivyo tutajua ni kwa nini saa hizi Chambuso yuko huko amelala bila kujijua.” Inspekta Dilunga alimwambia na Mzee Mwagala alionekana kuelewa na kutulia.
“Okey…mnataka kuongea nami juu ya nini sasa?”
Na ni kutokana na mahojiano baina yao na mzee Mwagala pale hospitali, ndipo Brian Koba alipopata jibu la swali kubwa alilokuwa akijiuliza hapo awali, juu ya ni nini kilichowapelekea wale vijana kule walipokutwa na madhila yale ya ajabu siku ile.
“Kwa eneo ambalo mmesema gari lilikutwa, nahisi Chambuso alikuwa akitokea kwa bibi yake…kijiji cha Mzenga.” Mzee Mwagala aliwaeleza
“Je, waweza kutupeleka huko mzee?” Brian aliuliza. Mzee Mwagala alisita, na muda huo Dokta Shabbir alifika pale walipokuwapo.
“Tib Haggard yuko kwenye simu…” Aliwaambia, na wale askari walimtaka radhi mzee Mwagala na kwenda kule ilipokuwa ile simu.
Superintendent Tib Haggard aliafiki ombi la Inspekta Dilunga moja kwa moja, na mara moja, akiwa kule jijini Dar es salaam alipiga simu hospitali ya taifa ya Princess Margareth, na kuongea na mganga mkuu wa hospitali ile.
Baada ya kueleza nia yake alielekezwa kuwa alitakiwa aongee na waziri wa afya, naye hakufanya ajizi.
Alikata simu na kuiinua tena, safari hii akiongea na mkuu wake wa kazi na kufikisha habari ile. Mkuu wake wa kazi, Inspekta Jenerali wa polisi mwingereza Brown Chamberlain, aliwasiliana na waziri wa afya, ambaye baada ya kuongea na mkuu mwenzake, aliinua simu na kuongea na mganga mkuu wa hospitali ya taifa ya Princess Margareth.
Nusu saa baadaye, jopo la madaktari lilikuwa likiundwa kuanza kazi ya dharura huko Kisarawe, na Inspekta Dilunga na mzee Mwagala Kifyagi walikuwa barabarani wakielekea kijiji cha Mzenga, kwa bibi yake Mwagala.
Inspekta Brian Koba alibaki pale hospitali kando ya kitanda alicholalia Chambuso Mwagala. Ilikuwa ni saa tisa alasiri.
Saa mbili baadaye Mzee Mwagala, Inspekta Dilunga na bibi mmoja mzee waliingia ndani ya wodi aliyolazwa Chambuso na kumkuta Inspekta Brian Koba akiwa kando ya kitanda alicholalia yule kijana aliyekutwa na madhila usiku uliopita.
“Kuna mabadiliko yeyote?” Mzee Mwagala aliuliza, na Brian alitikisa kichwa kuwa hakukuwa na mabadiliko yetyote.
“Huyu ni bi Mkiwa, bibi yake Chambuso. Yeye amethibitisha kuwa Chambuso na wenzake walifika kwake huko kijijini Mzega, na kumuaga kuwa alikuwa akienda Ulaya, masomoni.” Inspekta Dilunga alimwambia mwenzake.
“Sasa Ulaya yenyewe ndiyo imekuwa hii mjukuu wangu tena jamani!” Bi Mkiwa alisema kwa kulalama huku akitokwa machozi. Alimsogelea mjukuu wake na kumtazama kwa karibu
Inspekta Dilunga na Brian Koba walitoka nje ya wodi ile ndogo na kwenda ofisini kwa Dokta Shabbir, ambako sasa ilikuwa kama ndio ofisi yao ya muda pale hospitali. Brian aliagiza nesi mmoja abaki na Mzee Mwagala na mama yake ndani ya ile wodi.
“Kwa mujibu wa maelezo ya Bi Mkiwa, Uwesu bin Shaame na Esmund Bwaira walikunywa pombe ya kienyeji pale kwake kabla hawajaondoka, ni yeye mwenyewe ndiye aliyewakaribisha pombe hiyo” Dilunga alimtaarifu mwenzake. Brian Koba aliinua nyusi kwa taarifa ile, na Inspekta Dilunga alithibitisha kwa kichwa.
“Chambuso?”
“Chambuso hakunywa… huwa hanywi pombe kabisa, na kibaya zaidi ni kwamba walipoondoka pale kwa bibi yake, ni Uwesu ndiye aliyekuwa akiendesha ile gari, Chambuso alikuwa sehemu ya nyuma ya gari ile, wakati Esmund alikuwa kwenye kiti cha mbele kando ya Uwesu”
“Alaa! kwa hiyo hii inaelezea juu ya ile ajali ya kule kwenye shamba la viazi kando ya barabra kabla hawajafika pale tulipolikuta lile gari… na wale vijana wakiwa wameuawa huku Chambuso akiwa katika ile hali ya kushangaza…” .
“Yeah…”
“Lah! Jamaa walikuwa wakiendesha gari huku wamelewa… pumbavu!”
“Na walipotoka huko ndio wakaja kuishia pale katikati ya ile barabara ya Pugu-Kazimzumbwi…” Inspekta Dilunga aliongezea.
Kimya kilichukua nafasi kwa muda.
“Sasa ni nini hasa kilichotokea pale barabarani…?” Inspekta Brian Koba aliuliza, zaidi akiwa kama akijiwazia kwa sauti kuliko kumuuliza Dilunga, uso wake ukiwa umejikunja kwa kuvuta tafakuri. Dilunga aliguna kabla ya kuongea.
“Ninapata hisia kuwa huenda tusijue kabisa kilichotokea pale barabarani usiku ule Inspekta…”
Brian Koba alimtazama bila ya kusema neno. Hakuwa na la kusema.
Muda mfupi baadaye Mzee Mwagala na mama yake walitoka kule alipokuwa Chambuso. Inspekta Dilunga na Mzee Mwagala walimrudisha yule bibi kijijini kwake, na Brian Koba alirudi tena kwenye ile wodi alimolazwa Chambuso Mwagala, na kuketi kwenye kiti kilichokuwa kando ya kitanda kile.
Alikuwa amedhamiria kuwepo na kushuhudia chochote kitakachotokea pindi Chambuso atakapozinduka. Aliagiza aletewe chakula mle mle wodini, na kunyoosha miguu yake mifupi huku akipiga miayo.
Ilikuwa ni siku yake ya kwanza akiwa Inspekta wa jeshi la polisi, na bado alihisi msisimko wa kushiriki katika kesi ile kubwa na aliyokuwa na hakika kuwa kufikia wakati ule itakuwa inafuatiliwa kwa karibu sana na wakuu wa jeshi la polisi nchini.
Usiku ulipita bila ya tukio lolote Chambuso Mwagala aliendelea kulala kama alivyokuwa hapo awali.
MAUAJI YA AJABU YAITIKISA KISARAWE
Kichwa cha habari ukurasa wa kwanza katika gazeti la Ngurumo kililinadi tukio lile la Kazimzubwi, na kwa maandishi madogo chini ya kichwa kile cha habari yalifuata maelezo.
Watatu wauawa kitalii, wawili wabaki wakitumbua macho mfululizo… imani za kichawi, ubakaji vyahusika.
“HOLY SHIIT” Inspekta Dilunga alimaka kwa mshangao na kutoamini alipoiona habari ile huku akiusogeza uso wake karibu kabisa na gazeti lile lililokuwa mikononi mwake asubuhi ile, na kwa kufanya vile alikigonga kikombe cha chai kilichokuwa kando yake juu ya meza ambacho kilianguka sakafuni na kuvunjika kwa kelele.
“Nini wewe bwana!?” Mkewe alimkemea kwa wahka huku akiingia mbio pale sebuleni akitokea jikoni
“Mjinga sana huyu…Pumbavu kabisa!” Inspekta Dilunga alifoka huku bado akilikodolea macho lile gazeti.
“Nani mjinga sasa baba Sikudhani…?Huyo wa kwenye gazeti au wewe unayetuvunjia vikombe ovyo humu ndani?” Mkewe alimkemea kwa jazba, kwake matatizo ya kikazi ya mumewe hayakuwa sababu ya kuhalalisha kuvunjiwa vikombe vyake. Gezza Dilunga alimtazama mkewe kwa jicho la hasira na bila kujibu aliinuka na kutoka hadi barazani, nje ya nyumba yake, na kuanza kuisoma habari ile.
Chini ya vichwa vile vya habari, Bruno Mgimba alielezea tukio lile kwa kirefu, akitaja majina ya wale vijana waliokutwa wakiwa wamekufa katika tukio lile, na pia jinsi Chambuso Mwagala na baba wa Huba, binti aliyeuawa na kusadikika kuwa alibakwa kabla ya kifo chake, walivyokumbwa na ugonjwa wa ajabu na kuduwaa mfululizo.
Kibaya zaidi, Bruno Mgimba aliendelea hadi kuelezea juu ya jeraha lililosadikika kuwa ni la ajabu sana lililokuwa kifuani kwa yule mwanadada aliyeuawa kikatili.
Mgimba alielezea kuwa ile habari ni ya kutisha sana, na kuwaweka wananchi kwenye hali ya tahadhari dhidi ya mashambulizi mengine kama yale, akiwaasa kutotembea usiku na kutoongea na watu wasio wajua.
Mwisho alilaani tabia ya vyombo vya dola, hasa jeshi la polisi, ya kutotoa ushirikiano na waandishi wa habari kwa kisingizio cha kuwa uchunguzi bado unaendelea.
Je, itakuwaje iwapo wananchi zaidi wataendela kuuawa namna hii wakati bado uchunguzi wa jeshi letu hili la polisi unaendelea?
Bruno Mgimba alimalizia habari yake ile kwa swali.
“Bloody fool, Mgimba…bloody, bloody fool!” Inspekta Dilunga alijisemea mwenyewe kwa hasira
Alitoka akiwa na gazeti lake mkononi, uso ameukunja vibaya sana na kuingia kwenye gari lake kuelekea ofisini.
Saa moja kabla Inspekta Dilunga hajaliona lile gazeti lililokuwa na zile habari za tukio lile la mauaji ya Kisarawe, jijini Dar es Salaam Jadu Mfaume mpya alikuwa akilisoma lile gazeti, na ile habari iliyoandikwa na Bruno Mgimba ilimvutia sana.
Mara moja alijitia ndani ya basi la Kisarawe, mfukoni akiwa na kitita cha pesa alichomuibia mchuuzi wa viazi vitamu pale kituo cha basi bila ya hata yule mchuuzi kubaini.
Akiwa ndani ya basi, alihisi msisimko wa ajabu mwilini mwake, na hilo lilimpa hisia kuwa sasa alikuwa karibu sana na aliokuwa akiwasaka…
Dokta Shabbir aliingia ofisini kwake mapema sana, sababu kubwa ikiwa ni kutaka kuona iwapo kulikuwa na maendeleo yoyote katika hali ya Chambuso Mwagala aliyemuacha katika usingizi mzito wa madawa siku iliyopita.
Alienda moja kwa moja hadi kwenye wodi aliyolazwa yule kijana, ambamo pia alikuwamo Inspekta Brian Koba. Alimkuta Brian Koba akiwa ameketi kwenye kile kiti kilichokuwa kando ya kitanda cha Chambuso. Alikuwa amevaa bukta na fulana mchinjo, nguo zake za kiaskari zikiwa zimetundikwa kwenye misumari maalumuu nyuma ya mlango wa wodi ile.
“Vipi Inspekta, ina maana ndio umeketi hapo kwenye kiti usiku kucha?” Alimuuliza kwa mshtuko huku macho yake yakienda kwa Chambuso Mwagala., ambaye bado alikuwa amelala vilevile alivyomuacha.
Inspekta Koba alijinyoosha na kupiga mwayo mrefu, kisha akamuoneshea yule tatibu kwa kidole chake cha shahada kwenye kitanda kingine cha hospitali kilichokuwa kwenye kona moja ya wodi ile ndogo.
“Ah…nililala kwenye hicho kitanda …japo ndio huo usingizi wa mang’amung’amu tu” Alimwambia.
“Na hakukuwa na badiliko lolote katika hali ya Chambuso…?”
“Hakuna…jamaa amelala moja kwa moja…tena fofo…hata kukoroma hakuna! Sasa sijui kama hivyo ndivyo ilivyotakiwa iwe au vipi…”
Dokta Shabbir alimsogelea Chambuso na kumtazama kwa karibu. Alimgusa shavu kwa mgongo wa kiganja chake kama aliyekuwa akipima joto la mwili wake, kisha akamfunua jicho lake na kutazama mboni za jicho lile.
Alichoona hakikuwa cha kutia moyo sana, kwani alitikisa kichwa na kumuacha, lile jicho alilolifunua likijifunga tena na Chambuso akabaki akiwa amelala kama alivyokuwa hapo awali.
“Sio kawaida hii….ingawa bado kuna muda wa ziada wa dawa kuendelea kufanya kazi. Labda kutakuwa na badiliko muda wowote kutoka sasa.”
“Labda…sio hakika?”.
“Hakuna cha uhakika tena katika suala hili afande! Tusubiri uchunguzi wa jopo linaloundwa, huenda kukawa na ufumbuzi tofauti…”
Inspekta Brian aliishia kuguna tu.Hakuwa na la kusema tena.
Dokta Shabbir alimuaga na kuelekea moja kwa moja hadi kwenye kile chumba kingine ambamo ile miili ya wale vijana waliouawa kwenye lile tukio la ajabu ilikuwa imehifadhiwa kwenye majokofu maalumu. Aliingia mle ndani na moja kwa moja alianza kuiandaa ile miili kwa ajili ya uchunguzi wa jopo la madaktari wane wazoefu, akiwemo Dokta Nigel Smith kama mwenyeji wao.
Taarifa zilishaletwa tangu jioni kabisa ya siku iliyopita kuwa matabibu wale bingwa watafika Kisarawe siku ile muda wa saa tatu za asubuhi, na kulikuwa na uwezekano mkubwa wa ile miili kuhamishiwa kwenye hospitali ya taifa Princess Margareth, pindi ikionekana kuna haja ya kufanya hivyo.
Alikuwa katika hatua ya kuuvuta nje ya jokofu mwili wa hayati Esmund Bwaira wakati alipohisi kishindo hafifu sana cha mlango wa chumba kile alichokuwamo, kama kwamba ulikuwa umefunguliwa na sasa ukifungwa.
Alishtuka, kwani yeye tayari alikuwa ameufunga mlango ule japo si kwa ufunguo. Aligeuka taratibu na hapo hapo mwili ulimfa ganzi, kwani aliona mtu ambaye hajawahi kumuona hata siku moja akiwa amesimama ndani ya chumba kile, akiutazama mwili wa yule binti aliyeuawa kikatili katika lile tukio la ajabu la siku iliyopita, Huba binti Malambi.
“Hey! Nani wewe? Umefikaje hapa? Umepotea njia, naomba utoke tafadhali, hiki ni chumba cha uchunguzi na si cha kutembelea wagonjwa…”. Alimwambia yule mtu, akiamini kuwa ni mmoja wa ndugu aliyekuja kutembelea mgonjwa wake aliyelazwa pale hospitali, kisha akaongezea, “…kwanza saa hizi ni mapema mno kutembelea wagonjwa, umepitaje huko mapokezi?”
Jadu Mfaume alimtazama yule Dokta kidogo tu, kisha bila hata ya kujali kauli ya yule Dokta, alipiga hatua za haraka hadi pale ulipolala ule mwili ambao tayari alishasoma habari zake kwenye makala ya gazeti iliyoandikwa na Bruno Mgimba.
“Hey…HEEEY…!” Dokta Shabbir alimkemea yule mtu wakati akiusogelea ule mwili, lakini Jadu Mfaume wala hakutetereka katika alilokusudia kulifanya. Aliufikia ule mwili uliokua umefunikwa kwa shuka maalumu ya nailoni hadi kifuani, na kuitupia pembeni ile shuka.
Macho yake yalitua kwenye lile jeraha la ajabu na akaanza kulitazama kwa makini. Dokta Shabbir alimuendea kwa lengo la kumuondoa kutoka pale alipokuwa, sasa akiamini kuwa alikuwa ni mmoja wa waandishi wa habari aliyetaka kuja kuhakikisha vilivyoandikwa kwenye gazeti la siku ile juu ya jereha la ajabu la yule binti.
“Nakuambia toka humu ndani haraka kabla sijakuitia polisi…” Alimfokea huku akimnyooshea mkono kumkamata bega. Kitendo kilichofuatia kilikuwa cha haraka sana na kilimuacha Dokta Shabbir akiwa ameduwaa.
Jadu Mfaume aligeuka haraka na kumpiga kifuani kwa nguvu sana kwa kiganja chake kilichofunuliwa. Dokta Shabbir alihisi maumivu mazito na akatupwa nyuma hadi kwenye moja ya meza zilizokuwamo mle ndani, ambayo juu yake kulikuwa kuna mwili wa hayati Uwesu Bin Shaame, na kupinduka na meza ile hadi sakafuni kwa kishindo kikubwa.
Muda huo huo Jadu Mfaume aliruka kwa hatua kubwa hadi mlangoni na kuubana kwa loki mlango ule, kisha akamgeukia tena yule Dokta.
Dokta Shabbir alihisi kama amewekewa tofali kubwa na zito kifuani. Alibaki akimkodolea macho ya mshangao yule mtu huku akihisi maumivu ya ajabu kifuani kwake, mwili wa Uwesu ukiwa hatua chache kutoka pale alipoangukia.
Sasa aliingiwa na woga mkubwa.
Alitaka kupiga kelele za kuomba msaada lakini hata kinywa chake kilikuwa kama kilichobebeshwa gunia, na hata pale alipokuwa akimuona yule mtu mwenye nguvu za ajabu akimsogelea taratibu huku macho yake yakionyesha ghadhabu za hali ya juu, Dokta Shabbir alianza kujisukuma nyuma kwa taabu huku akimuinulia mkono yule mtu kama ishara ya kumzuia asimsogelee.
Huyu ndiye aliyewaua hawa vijana Yarabi…sasa ananiua na mimi…! Dokta Shabbir alianza kulia kwa fadhaa.
Jadu Mfaume aliona kuwa yule tabibu alikuwa amesambaratika kiasi cha kutoweza kumbughudhi tena. Aliachana naye na kuuendea tena ule mwili wa yule binti na kuendelea kulitazama lile jeraha la ajabu kwa binadamu wa kawaida, ambalo kwake halikuwa la ajabu hata kidogo. Mara moja aliielewa ile alama iliyofanya jeraha lile, ila bado lilimchanganya, kwa sababu ingawa alielewa kile kitu kilichoandikwa kwenye ule mwili wa yule binti, hakuelewa ni kwa nini kilikuwa kimeandikwa pale, au kilikuwa kimewekwa pale kwa lengo gani.
Lakini kitu kikubwa zaidi ni kwamba lile jeraha lilimthibitishia kuwa aliokuwa akiwasaka walikuwa eneo lile…au angalau walikuwa eneo alilokuwako yule binti wakati akipatwa na madhila ya jeraha lile. Lakini sasa wako wapi?
Kwa mara ya kwanza Jadu Mfaume mpya alionekana kuchanganyikiwa.
“Shit…shit…shit!” Alifoka kwa hasira na kumuendea Dokta Shabbir aliyekuwa akitapatapa pale sakafuni.
Inspekta Brian Koba alisikia kishindo kikubwa kutokea upande ule wa ofisi ya Dokta Shabbir, na mara moja aliruka kutoka kwenye kiti alichokuwa amekalia kando ya kitanda cha Chambuso, alijirusha kwenye kitanda alichokuwa amelalia usiku uliopita na kuchomoa bastola yake iliyokuwa chini ya mto. Bila kujishughulisha kuvaa nguo zake za kiaskari alitoka mbio nje ya chumba kile, bastola ikiwa wazi mkononi mwake, kuelekea kule alipohisi kuwa kishindo kilikuwa kimetokea.
Nje ya wodi ya Chambuso alimkuta nesi wa zamu na kumpigia kelele.
“Kaite askari kule mlangoni…aje aweke ulinzi hapa!”
Nesi aliruka huku akiachia yowe la mshtuko, na kubaki akiwa amezubaa, wazi hakuelewa kilichokuwa kikiendelea.
“Upesi wewe!” Brian alimfokea, na yule nesi akatimua mbio kuelekea lango kuu la hospitali ambako kulikuwa kuna askari kama ilivyoagizwa na Inspekta Dilunga siku iliyopita.
Brian alivamia ofisi ya Dokta Shabbir, akiwa makini sana huku bastola yake ameitanguliza mbele tayari kwa lolote.
Hakuna mtu.
Alitupa macho kule kwenye mlango wa kuingilia kwenye kile chumba ambamo miili ya wale marehemu wa tukio lile la kutisha ilikuwa imehifadhiwa, na hata pale alipotupia macho mle ndani alimsikia Dokta Shabbir akipiga ukelele wa woga.
Bloody shit…!
Brian aliruka na kupigiza bega lake kwenye ule mlango, bastola yake akiwa ameishika kwa mikono yake yote miwili, tayari kujiviringisha ndani ya chumba kile kukabiliana na kilichokuwa kikitokea nyuma ya mlango ule
Akadunda.
Mlango ulitikisika tu lakini haukufunguka, na yowe jingine kubwa likasikika likitokea nyuma ya mlango ule.
“Polisi…!” Brian alipiga kelele akiwa nje ya mlango ule na kurudi nyuma hatua mbili, sasa ilikuwa ni hekaheka ndani ya jengo lile, manesi na matabibu wengine walishajua kuwa kuna kitu kisicho sawa kilikuwa kikiendelea, hivyo walikuwa wakikimbia ovyo huku na huko, wakipigiana kelele bila mpangilio.
Brian aliruka na kuushindilia teke kwa nguvu ule mlango, ambao safari hii ulitawanyika vibaya sana naye akajitupa ndani ya chumba kile bastola yake ikiwa mkononi.
Alijiviringisha sakafuni na kupiga goti katikati ya chumba kile, bastola yake aina ya Smith & Wesson Police Special ikiwa imeelekezwa mbele kwa mikono yake yote miwili, akitembeza macho yake haraka ndani ya chumba kile, na kuyatuliza kwenye kona moja ya chumba kile. Akili ilimzunguka kwa kasi, akijaribu kuliweka sawa akilini mwake lile jambo lililokuwa mbele ya macho yake, hisia zake zote zikiwa wima.
Jadu Mfaume alikuwa amesimama kwenye ile kona ya chumba kile akiwa amempiga kabali kali sana Dokta Shabbir, aliyemuweka mbele yake kama ngao.
Kwa jinsi Dokta Shabbir alivyokuwa amesimama mbele ya yule mtu, Brian Koba alijua kuwa alikuwa ameishiwa nguvu kabisa, kwani ingawa alionekana kuwa amesimama mbele ya yule mtu, miguu yake ilikuwa imelegea kabisa kutokea magotini, na mkono wake mmoja ulikuwa ukining”inia bila nguvu yoyote kando yake, ilhali mwingine ukiwa umekujiwa mgongoni kwake na yule mtu aliyemkaba kutokea nyuma.
“What the…shiit!” Brian alimaka huku akilikodolea lile tukio lililokuwa mbele yake, na hakupata neno la zaidi, akili yake sasa ikimgongea kengele nyingi za tahadhari na umakini.
Dokta Shabbir alibaki akimtazama Brian kwa macho yaliyojaa woga na uchungu wa maumivu, mishipa ya kichwa ikiwa imemtutumka kwa kukabwa, mdomo ukiwa umemtanuka kwa kutafuta hewa.
Brian Koba aliinua macho yake hadi usoni kwa yule mtu aliyemkaba Dokta Shabbir, bastola yake ikiwa imelenga kati kati ya paji la uso la yule mtu.
Walitazamana.
Jamaa alikuwa akimtazama kwa makini sana, tena moja kwa moja machoni. Hakuonesha woga, wasiwasi, wala ghadhabu yoyote, badala yake Brian Koba aliona udadisi wa ajabu kwenye macho ya yule mtu. Udadisi ulioelekezwa kwake yeye.
Ni nini sasa hii..?
“Mwachie huyo mtu sasa hivi!!” Brian alimfokea kwa sauti kali ya kipolisi huku bado akiwa amemuelekezea bastola, na uso wake akiwa ameukunja kwa hasira. Jadu Mfaume hakumjibu wala hakutetereka. Alizidi kumtazama tu.
“Naongea na wewe…na nataka utekeleze nikuambialo mara moja, la sivyo…”
“Utanipiga risasi ya paji la uso?” Jadu Mfaume alimuuliza kwa sauti ya upole, huku bado akimtazama machoni kwa makini, akilitamka wazo lililokuwa kichwani mwa Brian muda wote, na Brian akashituka kidogo.
Amejuaje…?
Jadu Mfaume alitabasamu.
“Nimejuaje?” Alimuuliza tena swali lile lililopita kichwani mwake muda ule ule, na Brian alizidi kuchanganyikiwa. Aliinuka kutoka pale chini alipokuwa amepiga goti ilhali bado akiwa amemlengeshea bastola yule mtu. Sasa akili yake ilikuwa ikifanya kazi katika ile kasi ya ziada.
“Wewe ni nani…? Na unataka nini? Umefikaje humu…” Alimuuliza huku akimtazama kwa makini kwa lengo la kuiweka akilini mwake sura ya yule mtu aliyekuwa akizidi kumshangaza kadiri muda ulivyozidi kusogea wakiwa mle ndani. Jadu hakumjibu. Dokta Shabbir alianza kutoa sauti za kulalama, machozi yakimbubujika na akimtazama Brian kwa macho ya kuomboleza.
“Hebu muachie huyo mtu basi…mimi na wewe tunaweza kuongea kirafiki tu, na ukanieleza shida yako…” Brian aliamua kubadili mbinu, akijaribu kuvuta muda mpaka msaada wa askari wengine utakapofika.
“Sina shida na yeyote kati yenu…ila naomba msiniingilie kwenye ninalotaka kulifanya, kwani haliwahusu. Na hata mkijitia kujihusisha nalo hamtaliweza kamwe!” Jadu alimjibu.
“Mimi naona kuwa ni wewe ndiye uliyeingilia tunalofanya sisi…na…una maana gani kuwa…” Brian alimjibu na kuanza kumtupia swali, lakini kabla hajamaliza Jadu alimshtukiza kwa kumsukuma kwa nguvu sana Dokta Shabbir kuelekea pale alipokuwa amesimama. Dokta Shabbir alipiga kelele huku akielekea kumkumba Brian, na wakati huo huo Jadu Mfaume alijirusha pembeni kwa wepesi wa ajabu. Brian alilishtukia tendo lile akiwa ameshachelewa.
“Aaaaahkkkhhh…!” Alipiga kelele kwa hamaniko huku akijirusha pembeni kumkwepa yule tabibu, ilhali akijaribu kuielekeza tena bastola yake kwa yule mvamizi. Lakini tayari Jadu Mfaume mpya alikuwa ameshajiandaa kwa kitendo kile, na aliipiga teke ile bastola kutoka mkononi kwa Brian, na ile bastola ikatupwa pembeni. Huku nyuma, Dokta Shabbir alijipigiza ukutani na kusambaratika sakafuni kama gunia tupu.
Brian alimaka kwa hasira na hapo hapo aligeuka na konde zito lililokuwa linaelekea usoni kwa Jadu, lakini Jadu Mfaume mpya alijiyumbisha kwa wepesi wa kushangaza na lile konde likamkosa. Brian akapoteza muelekeo, na kabla hajajiweka sawa, Jadu alimshindilia ngumi nzito sana ya mbavu iliyomsukuma hadi chini ya ile meza iliyokuwa na mwili wa Huba binti Malambi, maumivu ya ajabu yakiutawala mwili wake.
Jadu alimtazama kwa macho makali wakati akijizoazoa kwa taabu kutoka pale chini, akiwa amechanganyikiwa na maumivu yaliyotakana na ngumi ile.
Huyu si mtu wa kawaida huyu…si wa kawaida kabisa…!
Alibaki akimtazama kwa mastaajabu huku akiwa amejishikilia kwenye ile meza, akijaribu kujiinua bila mafanikio, akihisi mbavu zake kadhaa zitakuwa zimevunjika. Alitembeza macho kutafauta mahala bastola yake ilipoangukia, lakini hakuiona kabisa.
“Tulia hapo hapo na hutadhurika…na kama umeshajua kuwa mimi si mtu wa kawaida, basi utajua kuwa hutakiwi kabisa kunijaribu kwani hujui uwezo wangu!” Jadu alimwambia kwa ukali, na Brian aliishiwa nguvu, alibaki kinywa wazi huku akimkodolea macho kwa mshangao yule mtu.
Bila kujali mayowe na tafrani zilizokuwa zikisikika nje ya chuba kile, Jadu Mfaume alimuendea Dokta Shabbir na kumnyanyua kwa nguvu kutoka pale sakafuni kwa kutumia kola za koti lake la utabibu.
“Umegundua nini kwenye uchunguzi wa miili hii wewe, eeenh?” Alimuuliza kwa ukali. Dokta Shabbir alitikisa kichwa kwa woga, akimaanisha kuwa hakuna alichogundua, huku mikono ikimtetema na machozi yakimbubujika.
Jadu alimtazama kwa hasira, lakini aliona kuwa hakuna kitu anachoweza kupata kutoka kwa yule tabibu, na ghadhabu zikazidi kumpanda, si dhidi ya yule tabibu bali dhidi ya wale watu aliokuwa akiwasaka ambao aliamini kuwa ndio waliofanya mauaji yale na kuacha ile alama juu ya kifua cha yule binti.
“Shit…!Shit…!Shit…!” Jadu alifoka huku akimtikisa yule tabibu, kisha akamuacha akijibwaga tena sakafuni huku akilia kama mtoto naye akageuka kutoka nje ya chumba kile kwa mwendo wa haraka.
Alikutana uso kwa uso na Brian Koba aliyekuwa amesimama huku akiwa ameegemeza mkono mmoja kwenye ile meza iliyokuwa na mwili wa Huba binti Malambi, na kwa mkono mwingine akiwa amemuelekezea bastola yake aliyofanikiwa kuiona na kuiokota tena.
“Tulia hapo hapo wewe!” Brian alimkemea kwa sauti iliyojaa maumivu.
Jadu Mfaume aliendelea na safari yake bila kusita, na alipomfikia karibu alimtupia jicho na kumwambia, “Usijaribu hata kidogo…ama sivyo hutakuwa na uhai tena wa kukuwezesha kujutia kitendo hicho!”
Brian alibaki akimshangaa, hakuamini alichokuwa akikisikia, huku akilini mwake akijiuliza kipi ambacho yule mtu alikuwa akijiamini kwacho.
“Simama nasema, ama sivyo na-shoot!” Alifoka tena kwa ukali zaidi, na hapo hapo akaanza kukohoa, mbavu zikimuuma vibaya sana na akihisi kifua kikimbana.
Oh, My God…
“Just go ahead and try” Jadu alimjiu huku akiendelea na mwendo wake bila kusita wala kujali. Brian alibaki akiutazama mgongo wa yule mtu kwa hamaniko, asijue la kuamua.
Ni-shoot au…ni nini kitatokea…?
“Simama nasema! Nitahesabu mpaka tatu!” Alimkemea yule mtu, na alipoona jamaa hamtilii maanani akaanza kuhesabu, “Moja!”
Jadu hakutetereka, alizidi kwenda.
“Mbili…!” Aliita tena, akihisi maumivu yakizidi kumtawala mbavuni. Jadu hakumjali. Brian aliachia kitunza usalama cha bastola yake, tayari kumfyatulia risasi yule mtu jeuri.
“Ta…”
Jadu Mfaume aliufikia mlango wa kutoka mle ndani na kumgeukia, kisha akamnyooshea kidole cha shahada kama namna ya kumkanya, na bila kuongea neno zaidi aligeuka na kutimua mbio huku akipiga kelele.
“MOTOOO…MOTOOO…MOTOOOOO….!”
Brian Koba alifyatua risasi, mlipuko wa bastola ile ukitawala jengo zima, naye akishuhudia risasi ikipiga nyuma ya bega la yule mtu, na hapo hapo kihoro kikimpanda pale alipoona yule mtu akizidi kutimua mbio, na mtawanyiko mkubwa wa cheche kama za umeme ukitoka pale ambapo risasi iliupiga mwili wa yule mtu. Na hata pale alipokuwa akishuhudia kituko kile, mlipuko mwingine mkubwa ulifuata, kama wa shoti kubwa sana ya umeme, na nguvu ya mlipuko ule ilimtupa kwa nguvu na kumbabatiza ukutani kwa kishindo. Yowe kubwa lilimtoka huku akahisi mwanga mkubwa ukipasuka mbele ya macho yake.
Jadu Mfaume alitoka mbio nje ya chumba kile huku akiendelea kupiga kelele za moto, na wakati huo huo ile milipuko miwili mikubwa iliyosikika kote pale hospitali iliwachanganya vibaya sana watu waliokuwamo ndani ya jengo lile. Watu waliokuwamo mle ndani walianza kukimbia ovyo mle ndani huku nao wakipiga kelele za moto pasina kujua ni wapi hasa moto ule ulikuwa unatokea.
Ilikuwa ni kizaazaa cha aina yake, na ndani ya kizaazaa kile, Jadu Mfaume alijichanganya na kutoka mbio kuliendea lango la kutokea nje ya jengo lile. Nyuma yake, Brian Koba alitoka nje ya chumba kile kwa kuchechemea huku akipiga kelele hafifu na akimuoneshea Jadu kidole.
“Kamata! Kamata huh…huyooo! Hakuna Moto…! Muuaji huyyyooo…!”
Lakini sasa watu wote waliokuwepo mle ndani walikuwa wamechanganyikiwa na hakuna aliyemuelewa wala kumtilia maanani. Alimuona Jadu akijichanganya kwenye tafrani ile kuelekea nje ya jengo na moyo ukamnyong’onyea. Alijitahidi kumkimbiza, lakini alikuwa akiyumba sana, mbavu zilikuwa zikimuuma na watu walikuwa wakimpiga vikumbo kila upande.
Ah! Dilunga uko wapi sasa…? Bloody Hell…!
Adui yake alizidi kutokomea mbele ya macho yake naye hakuwa na la kufanya.
Jadu Mfaume alizidi kutimua mabio huku akiwasukuma na kuwapiga vikumbo watu walioingilia njia yake, na hatua chache kabla ya kuufikia mlango wa kutokea nje ya jengo lile, alimshuhudia Inspekta Dilunga akiingia mbio mle ndani, bastola ikiwa wazi mkononi mwake, macho yakimtembea huku na huko, askari wengine watatu wakimfuata nyuma yake.
“Nini pale….?” Inspekta Dilunga alimaka, akikutana macho kwa macho na Jadu Mfaume mpya, na mara moja Jadu Mfaume alijua cha kufanya.
“MOTOO! Motooooo….YAAAAAAARGHHH….” Alipayuka kwa kelele huku akitupa mikono hewani na akiwa ametumbua macho pima, nyuma yake kundi kubwa la wahudumu wa hospitali na raia wengine likija mbio kwa kelele zile zile za moto.
“Oh…Shiiiiit….!” Dilunga alilaani huku akipishana na wale watu waliokuwa wakikimbilia nje ya jengo lile naye akizidi kuingia mle ndani, akili yake ikiwa kwenye ile miili iliyotakiwa kufanyiwa uchunguzi mpya na jopo la matabibu, Chambuso Mwagala na kwa Mzee Malambi.
Inspekta Dilunga alikimbia ndani ya korido ndefu ndani ya hospitali ile akitafuta ni wapi moto ulipokuwa ukitokea, huku akilini mwake akijiuliza maswali mengi sana. Nyuma yake wale askari aliowakuta pale nje ya jengo lile walikuwa wakimfuata mbio, naye akijitahidi kupishana na wahudumu na madaktari wengine walikuwa wakikimbia ovyo huku na huko.
Hatua chache mbele yake alimuona Inspekta mpya Brian Koba akiwa ameanguka chini kando ya korido ile na akijitahidi kujiinua kwa taabu, huku akitembeza uso wake huku na huko, akijaribu kuaomba msaada kwa watu waliokuwa wakikimbia na kumpita bila ya kumjali.
“Brian…! Brian….what happened….!” Alimkimbilia pale alipokuwa huku akimuuliza huku akiwa makini sana.
“Mkamate…mkamate….ah! Atakuwa ametoweka sasa…” Brian alimuambia kwa taabu, maumivu makali yakiutawala ubavu wake kuanzia lile eneo ambalo alipigwa ile ngumi nzito na yule mtu wa ajabu.
“Nani…ni nini unaongelea….?” Dilunga alimuuliza, kisha akamgeukia mmoja wa wale askari aliokuja nao na kumpigia kelele, “…hebu chunguza sehemu moto unapotokea wewe….na wewe, piga simu kituo cha zima moto….”
“Hakuna moto Inspekta…ni uongo…!” Brian alisema kwa taabu huku akijishika mbavu.
“Whaat…?”
“Sio moto…ni yule mtu aliyetoroka…amezua mtafaruku kusudi ili atoroke…AAUUUCHH…!” Brian alisema na kuishia kutoa yowe la maumivu huku akijishika mbavu. Inspekta Dilunga alimtazama yule askari kijana na kuona kuwa yuko kwenye maumivu, na alijua kuwa kuna mengi yalikuwa yametokea.
“Una hakika Inspekta…?”
“Kabisa…! Mi” si nimepambana naye hapa? Kanishinda bwana…kakimbilia nje ya jengo, bila shaka utakuwa umepishana naye…”
Mara moja akili ya Dilunga ilirudi kwa yule mtu aliyekutana naye pale mlangoni wakati akiingia ndani ya jengo lile.
“Oh, Shiiit…” Alilaani na hapo hapo alimgeukia yule askari aliyebaki na kumpigia kelele, “…hakuna moto…mkimbilie mwenzio muambie asipige simu kituo cha kuzima moto…waambie watu watulie, ni tahadhari ya uongo hii…hakuna moto…!”
Mara moja yule askari alikimbia kule alipoelekea yule mwenzake huku akipiga kelele kwa watu wote waliokuwa wakihaha ovyo mle ndani.
“HAKUNA MOTO…HAKUNA MOTO…NI TAARIFA YA MAKOSA JAMANI, HAKUNA MOTO…TULIENIII…!”
Watu walianza kubabaika sasa. Walisimama kwa mashaka huku wakiangaza huku na huko, na wengine ikiwaingia akilini mwao kuwa kweli hakuna moto, kwani muda wote ule tangu wasikie kuwa kuna moto mle ndani hawakuona moshi wala kunusa harufu ya moshi….
Inspekta Dilunga alimsaidia Brian Koba kuinuka kutoka pale chini alipokuwa ameanguka na kuanza kumkokotea kule kulipokuwa na ile wodi ya Chambuso Mwagala.
“Dokta Shabbir…naye anahitaji msaada…” Brian alisema kwa taabu.
“Yuko wapi…?”
“Ofisini kwake…kwenye chumba cha uchunguzi…”
“Dammit…” Inspekta Dilunga alilaani kwa mara nyingine. Aliangaza huku na huko na akaona wahudumu wawili wakikimbia kwenye ile korido na mara moja aliwaita.
“Nendeni mkatoe huduma kwa Dokta Shabbir…yuko ofisini kwake…haraka!” Wale wahudumu walitimua mbio kuelekea ofisini kwa Dokta Shabbir.
Inspekta Dilunga alimkokota Brian hadi kwenye wodi ya Chambuso, ambako alikuta askari mmoja akiwa ameweka ulinzi nje ya mlango ule. Alimkamata nesi mmoja na pamoja walisaidiana kumlaza Brian pale kwenye kitanda alichokuwa amelalia usiku uliopita, kisha akamtupia macho Chambuso Mwagala.
Alikuwa amelala kama alivyomuacha siku iliyopita!
Kichwa kikimzunguka, alimuacha yule nesi akimhudumia Brian naye akaenda moja kwa moja hadi ofisini kwa Dokta Shabbir, na kukutana na wale manesi wakitoka huku wakimsukuma Dokta Shabbir aliyekuwa amelala bila ya fahamu juu ya kitanda cha magurudumu.
“Mnampeleka wapi sasa?” Aliwauliza.
“Wodi namba mbili…”
“Okay…nitakuja huko baadaye…”
Aliiendea simu iliyokuwa mezani kwa Dokta Shabbir na kuongea na ofisi yake, akitoa maelezo ya kuanza kwa msako mkali dhidi ya yule mtu aliyeanzisha vurugu pale hospitali asubuhi ile na kumtaja mtu huyo kuwa ni hatari sana.
Kwa kuwa hakuwa na maelezo rasmi ya wajihi na maumbile ya mtu huyo zaidi ya kumbukumbu hafifu iliyokuwa kichwani mwake, na ambaye hata hivyo hakuwa na hakika iwapo ndiye huyo hasa Brian aliyekuwa akimkusudia, alitoa maagizo kuwa polisi wakamate mtu yeyote anayeonekana kuwa mgeni na mwenye kuleta mashaka ya aina yoyote ile.
Kisha alipiga simu moja kwa moja makao makuu ya jeshi la polisi Dar es Salaam na kumpasha habari Superintendent Tib Haggard juu ya tukio zima la asubuhi ile, na kushauri kuwa zoezi zima la jopo la matabibu kuichunguza upya ile miili ya ajali ile ya kutisha lisitishwe kwa siku ile mpaka hapo atakapokuwa ameiweka hali kwenye mustakbali utakiwao.
“Say whaat…?” Tib Haggard alimaka, na kumwambi kwa jazba, “Jopo limeshaondoka mjini kuelekea huko asubuhi hii…”
“Basi na lirejeshwe huko huko…huku bado hapajawa salama kwa sasa, na pindi tutakapopata picha kamili ya wajihi wa huyu mtuhumiwa wetu, tutaleta taarifa huko ili msako uendelee mpaka huko na ikiwezekana nchi nzima!” Dilunga alisema kwa msisitizo.
“Brian yu hali gani…?”
“Yu-taabani kitandani…”
“Na yote hiyo kutokana na huyo huyo mtu anayeshukiwa kuhusika na vurugu ya hapo hospitali?”
“Kwa sasa hivyo ndivyo niaminivyo…mpaka nitakapoongea kwa kituo na Brian…”
Kimya kilitanda kidogo.
“Hivi ni nini hasa kinachotokea huko Inspekta…?” Tib Haggard aliuliza kwa namna ya kuchanganyikiwa baada ya kimya kile kifupi.
“Sijui afande…lakini ukweli unabaki pale pale, kuwa hii ni kesi moja ngumu na ya ajabu sana…”
“Nadhani nakubaliana na wewe Inspekta…okay, nitafanya mawasiliano ya redio na msafara wa matabibu. Nitataraji ripoti kamili mara ukishaongea na Brian!”
“Yes Sir!”
Aliweka simu chini na kuingia mle ndani ilipokuwa imehifadhiwa ile miili ya wale watu na kubaki akiwa mdomo wazi baada ya kuona hali ya mle ndani. Meza zilikuwa zimeanguka na mwili wa marehemu Uwesu ukiwa sakafuni, ilhali ule wa Huba binti Malambi ukiwa juu ya meza lakini ukiwa unakaribia kuanguka.
“La Haula! Ni mtu gani huyu aliyekuja humu ndani…? Na alikuwa anataka nini…?” Alijikuta akisema peke yake huku akitikisa kichwa.
Aliwaita vijana wa alama za vidole, na kuwaagiza kuchukua alama zote za vidole zilizokuwa mle ndani, kisha kwa robo saa iliyofuata alisimamia wahudumu wa ile hospitali kuisitiri miili ya wale marehemu. Kisha alitoka na kwenda moja kwa moja hadi kwa Dokta Nigel kupata taarifa ya hali za Dokta Shabbir na Brian Koba. Huko aliambiwa kuwa Dokta Shabbir hataweza kuongea kwa muda wa saa zipatazo kumi na mbili, akiwa amepatwa na mshituko mkubwa kabisa, ila hali yake itakuwa nzuri tu baada ya muda huo.
“Kwa hiyo siwezi kujua kilichomtokea mpaka baada ya saa kumi na mbili?” Alimuuliza yule mganga mkuu wa hospitali ile, ambaye aliafiki kwa kichwa.
“Oh Come on Dokta, hatuna muda kiasi hicho…!”
“Kwa hiyo unataka nifanye nini sasa…?”
Dilunga hakuwa na la kusema, alimtazama kwa ghadhabu, kisha akamtupia swali jingine.
“Na Brian je?”
“Brian ameumia sana kwenye mbavu, mbavu moja imetoa ufa, nusura ivunjike, sijui amepigwa na nini…na yuko kwenye maumivu makali, lakini nadhani ataweza kuongea, japo kwa taabu…”
“Kwa hiyo naweza kwenda kuongea naye?”
“Ningependa apumzike kwa muda wa angalau saa tatu hivi kabla hajaanza kuong…”
Mara mlango ulivamiwa kwa ghafla na wote wawili wakageukia kule mlangoni, na kumuona nesi mmoja akiingia mle ndani huku ametumbua macho.
“Chambuso Mwagala kaamka…!”
Wote wawili walitimua mbio kuelekea kule ilipokuwa wodi aliyolazwa Chambuso Mwagala.
ITAENDELEA
Utata wa 9/12 Sehemu ya Nne
Also, read other stories from SIMULIZI;