Zawadi ya Ushindi Sehemu ya Pili
IMEANDIKWA NA BEN R. MTOBWA
************************************************************************
Simulizi: Zawadi Ya Ushindi
Sehemu ya Pili (2)
na bosi wake Rusia alipotoka na Sikamona kuruhusiwa kuingia.
Aliingia shingo upande. Alipotoka aliaga kwa huzuni na kusindikizwa kwa tabasamu ambalo lilijijenga rohoni mwake, jengo imara ambalo lilimtia kiu ya kuendelea kuonana na Rusia na njaa ya kuliona tena tabasamu lake.
Bila shida maalumu, siku ya pili, Sikamona alijikuta amewasili tena katika ofisi hiyo. Ni siku hiyo ambapo alifanikiwa kumtaka wakutane jioni nje ya ofisi hiyo.
Walikutana. Wakaendelea kukutana.
Tabasamu la Rusia liliufanya kila mkutano ufane na kushawishi mwingine. Wakajikuta tayari wamefahamina tosha.
Rusia alimfahamu sikamona kuwa alikuwa mwana wa mkulima mmoja wa kahawa huko mkoani Iringa na kwamba alikuja hapa Dodoma miaka miwili iliyopita baada ya kuamishwa toka Songea alikokuwa akifanya kazi tangu alipomaliza kidato cha nne.
Naye Sikamona alifurahi kufahamu kuwa Rusia, mtoto pekee wa mzee Rashid alikuwa mzaliwa wa mkulima wa hapahapa Dodoma ingawa asili yao ni huko Tabora. Baba yake alikuwa amestaafu kazi ya ualimu baada ya kuifanya maisha yake yote. Sasa walikuwa wakiishi kwa kutegemea mashine yao ya kusaga nafaka pamoja na kimshahara cha
kima cha chini cha Rusia. Mama yake alikuwa amefariki miaka kadhaa iliyopita. Rusia aliishi na mama wa kambo
Naam, walijuana tosha. Wakazidi kupendana.
Katika moja ya mikutano hii Sikamona alimfichulia mwenzake siri ya roho yake. Kwamba hana hali wala afya kwa ajili yake.
“Sasa?” Rusia aliuliza
“Nakutaka uchumba. Nataka nikuoe.” Alimjibu Tamko hilo lilifanya Rusia aangue kicheko.
Alicheka kwa muda mrefu, kisha akamfahamisha kuwa tangu siku ile walipoonana ofisini kwa mara ya kwanza alikuwa amefahamu kuwa Sikamona alikua amezaliwa kwa ajili yake, na hivyo asijisumbue kusema mengi.
Tabasamu la Rusia likaendelea kuurutubisha uchumba wao kama maji katika bustani. Tabasamu ambalo lilimfanya Sikamona ajisikie afya na furaha kila alionapo. Si furaha tu, bali pamoja na kuwa na hakika ya uhai na kuyapenda maisha, kwani alijisikia kama tajiri mbele ya malkia mzuri kila awapo mbele ya msichana huyu.
Naam, siku zote isipokuwa leo tu ambapo Rusia alipoteza kabisa tabasamu na kusahau ule uchangamfu wake, hali ambayo ilimfanya Sikamona akose furaha na kuishuku afya yake.
“Unasema habari nzuri?” alihoji tena. “Mbona
waonekaana kama mwenye msiba?”
Rusia alijaribu kuatabasamu, tabasamu ambalo halikuwa kamili. “Kwani kuna mwenye furaha leo hii?”
Akauliza “Kwani kuna nini?” Badala ya kumjibu. “Naona huna habari.” Rusia alimwambia. “Habari ipi?”
“Ya kuvamiwa.” “Kuvamia!”
“Na Idd Amini. Hujasikia kuwa ameteka sehemu ya nchi yetu na kuangamiza mamia ya watu wasio na hatia?”
“Hee? Wacha!” alifoka kwa mshangao “Ametuchokoza. Ameanzisha vita…”
NAKUPENDA kusikia zaidi. Hakuwa tayari.
Vita kwake ilikuwa jambo la mwisho, jambo lenye kila aina ya mikosi, dhiki
na maafa. Ni fursa pekee ambayo, licha ya kusababisha uharibifu wa maisha ya watu wengi, wasio na hatia, hurejesha nyuma maendeleo ya jamii.
Hakupenda vita. Kwa ujumla alivichukia. Hivyo, alimchukia kila mtu ambaye huanzisha au kuwa kiini cha vita.
Ni kweli kuwa viko vita ambavyo huanzishwa na jamii kwa manufaa ya jamii, vita ambavyo hupiganwa na jamii nzima kutokomeza tawala dhalimu zinazoikandamiza. Haja ya vita hivi ni kuinua maisha ya wananchi ili waweze kufaidi matunda ya uraia wao. Vita vya Mau-Mau wa
Kenya, mapinduzi ya Zanzibar, Kyuba, China na Urusi ni mifano dhairi. Hivi kwake vilikuwa vita vitakatifu, vita ambavyo ingawa pia hakuvipenda bado ilikuwa lazima vipiganwe ili jamii hizo ziweze kuwa hapo zilipo. Vita hivyo aliviheshimu kwa kuwa vilitengeneza njia kwa vizazi vya baadaye. Hivyo, waliovianzisha na kuviongoza walikuwa na nafasi pekee katika moyo wake. Kila alipoyafikiria majina yao neno shujaa lilitangulia kila jina.
Lakini si vita kama vile vya Adolf Hitler, vita vya mtu mwenye njaa ya kupanua mipaka yake na kutapakaza jina lake, mtu mwenye kiu ya kumwaga damu, vita ambavyo vilisababisha majonzi makuu na kuyapotosha maendeleo ya dunia nzima.
Mtu kama huyu kwake alikuwa zaidi ya mkatili, mtu ambaye jina lake aliliona karibu zaidi na shetani, kwani ni mtu ambaye hufuraishwa na mateso ayapatayo mtu mwingine, huchekelea aonapo mtu akifa, hutabasamu aonapo mama akilia kwa uchungu wa kuwa mjane na kushangilia pale ambapo umati wa watu huanguka na kufa mbele ya risasi zake. Utu wa mtu kama huyu aliutilia mashaka.
Mtu kama Idd Amini! Kiongozi ambaye amejipa uongozi mwenyewe baada ya kuunyakua toka katika serikali halali iliyochaguliwa na wananchi kwa manufaa yao. Ni mtu ambaye alikuwa na sifa zote za ukatili na unyama. Vitendo vyake vya kinyama vilikuwa vingi kiasi cha kuwafanya watu washindwe kuamini kama ni vitendo vya kweli au
hadithi za kubuni.
Baadhi ya vitendo hivyo ni kile cha kumuua kila ambaye alimshuku kuwa ni mpinzani wa uongozi wake. Ukatili haukutokana na kuua tu bali pia mbinu alizozitumia katika mauaji. Aliua kwa namna ya kusikitisha sana, namna ambayo mtu yeyote asingefurahi kuona mwenzake akitendewa, yeyote, isipokuwa Amini pekee na wale ‘wateule’ wake wachache wenye roho ngumu kama yake.
Baaaadhi ya watu ambao dunia iliwafahamu, waliofanyiwa unyama huo na Amini ni marehemu Godfrey Kiggala ambaye alikuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje. Huyu alipigwa risasi na kung’olewa macho na ngozi yake kuchunwa. Alipopelekwa hospitali ilikuwa vigumu kumtambua.
Mwingine alikuwa Jemedari wake Brigedia Charles Arube. Huyu aliteswa na kuhangaishwa kupita kiasi. Yasemekana kuwa Amini hakuridhika na mateso hayo. Hivyo, aliifuata maiti hospitali ambako aliwafukuza madaktari na kujifungia peke yake na maiti hiyo chumbani kwa dakika kadhaa. Alichomfanya maiti ni siri yake.
Pamoja na hao, ni maelfu ya watu wengi, wote walipoteza maisha yao kwa namna ya kusikitisha ama kwa amri yake au kwa mkono wake, wengi mno, maaskofu, waumini, wasiojiweza n.k.
Sifa hizo si kwa mauaji tu, ilikuwa pamoja na yale mambo yake ya ajabuajabu. Mara atadai anataka kuikomboa Afrika Kusini, mara atatuma jeshi lake kuwatoa Waizrael katika sehemu
ya Waarabu inayokaliwa kwa mabavu, mara Uingereza ina haki kuzuia Afrika Kusini silaha nakadhalika. Mara mbili aliwahi kuutangazia ulimwengu akidai kuwa ameongea na Mungu, na ameambiwa hivi na vile. Sifa hizi ni pamoja na ile inayosemekana kwamba alijitapa sana kwa kula nyama pamoja na kunyonya damu za watu.
Sikamona hakujua amweke katika kundi lipi mtu kama huyu. Kumwita mkatili ni upendeleo mkubwa kwake, kichaa labda ni kumwonea, nduli ni kumsifu kupita kiasi na dikteta ni kumvimbisha kichwa. Hakujua amwite nani. Kwa kweli, hakujua.
Baada ya kuwafanyia unyama usio kadirika wananchi wa Uganda, sasa alikuwa amevuka mpaka na kuja Tanzania kupanua milki yake! Kuiweka sehemu ya nchi yetu chini ya kwato zake! Chini ya jinamizi!
“Tusi lililoje hili!” Sika aliropoka bila ya kufahamu.
Sauti yake ikamzindua yeye mwenyewe. Akaibuka toka katika dimbwi la mawazo. Ndio kwanza akagundua kuwa alikuwa kando ya mpenzi wake, chumbani. Akamtupia jicho ambalo lilikuwa na dhamira ambayo binafsi hakuifahamu. Kisha, aliinuka na kuondoka.
Usiku akiwa amelala chali kitandani, redio yake kaifungua kwa sauti kubwa kuliko alivyozoea, ndipo aliposikia yote aliyoyasikia kwa uhakika zaidi, kwamba jeshi la Idd Amini likiongozwa na
vifaru limeingia nchini kupitia Kagera na kuteka eneo la Tanzania, sehemu ile ambayo tangu aliponyakua madaraka alikuwa akidai kuwa ni eneo lake. Si kuteka tu, bali ilikuwa pamoja na kuwaua kinyama mamia ya wananchi wasio na hatia, kwamba, alikuwa amewashika wananchi, wake kwa waume, watoto kwa wazee na kuwalaza chini kisha akawasaga kwa vifaru pamoja na kubomoa majumba na madaraja, kuiba ng’ombe na kila walichokitamani, na kwamba sasa bendera yake ilikuwa ikipepea katika tarafa hiyo akidai ameikomboa kuondokana na ujamaa!
Sikamona akajigaragaza kitandani kwa uchungu uliochanganyika na hasira. “Aibu iliyoje… ukatili ulioje…” alifoka kwa sauti ndogo. “Na serikali yetu inafanya nini?” Alijiuliza. “Mtu aamue kutuvamia nchi ya amani na haki kama hii, tumtazame tu? Huyu anastahili kufunzwa adabu… serikali yetu inafanya nini?”
Kisha ilifuata ile hotuba ya Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ilikuwa hotuba kali yenye hasira ingawa Mwalimu alizungumza kwa sauti ambayo haikufaulu kuacha huzuni na uchungu hasa kwa kule kufahamu maafa ambayo yangefuatiwa.
“…Tumevamia… Mwendawazimu katuvamia… Katutangazia vita… Na sasa tutampiga… Uwezo wa kumpiga tunao. Nia ya kumpiga tunayo. Sababu ya kumpiga tunayo. Hivyo, tutampiga, wananchi tulieni, msibabaike, sikilizeni muone
vijana wetu watafanya nini…”
Moyo wa Sikamona ulifarijiwa na hotuba hii. Afya na ujana ukamrejea huku akihisi tabasamu katika roho yake. Huu ndio utu, vinginevyo isingekuwa taifa, kuacha ukatili ukineemeka katika ardhi yako! Ingekuwa sawa na mwumini aendaye msikitini bila kutawadha, aliwaza. Polepole usingizi ukamjia. Alafu, ile ndoto yake ya siku zote, kwamba yu pamoja na Rusia, wakizungumza na kucheka, ikamjia tena. Alipogeuka na kujaribu kumkumbatia, kama kawaida ndoto hiyo ilitoweka. Na ilifuatwa na kupaa kwa usingizi. Akabakia macho, akimwaza Rusia.
Mara akakumbuka kuwa alikuwa amesahau angalau kumdokeza ile haja iliyompeleka kwao. Haja ya kupanga siku kamili ya harusi yao.
Umesema haja yako ni kujitolea kwenda vitani kumwadhibu nduli aliyeivamia nchi yetu?” Kamanda huyu wa Jeshi la Wananchi, aliyevaa magwanda yenye tepe tatu begani, alimhoji tena huku kamkazia jicho ambalo alihisi lapenya mwili na roho yake hata kuiona roho na
fikra zake. “Ndio, afande.”
“Una hakika uamuzi huo ni wako mwenyewe? Au umeshawishiwa na mtu au kitu fulani?”
“Hapana, mzee,” alimjibu “Nimeamua mwenyewe.”
Unaweza kuniambia kwa nini umeamua hivyo?” Kamanda hakuchoka kuuliza.
Angeweza kutaja sababu nyingi zilizomtuma kuamua hivyo, nyingi mno, kwamba nchi ilikuwa imeonewa, nchi imedharauliwa, nchi imetukanwa,
nchi iko katika hatari ya kuangamia kwa ukatili wa mkatili mmoja. Hivyo, nchi inahitaj kurudisha hadhi yake. Kujikomboa na kumwadhibu mkatili huyu. Yeye kama mwananchi, yeye kama kijana ambaye taifa linamtegemea, angewezaje kuzibia masikio wito wa taifa? Angewezaje kujistarehesha katika mabaa na majumba yote ya starehe hali afya na ujana wake unahitajika na taifa kwa manufaa ya taifa?
Ni hayo, ambayo angeweza kumwambia Kamanda huyo. Lakini licha ya ukosefu wa muda, hakuwa mwepesi wa kuongea mawazo yake. Hivyo, alitamka kwa sauti nyembamba. “Nimeamua kwa kuwa nafahamu ni wajibu wangu kufanya hivyo.”
Kamanda alitabasamu kisha akamwandika jina lake katika ile orodha ya mamia ambao walikuwa wamekwishajiandikisha, “Taifa linawahitaji watu kama wewe. Na lina haki ya kujivunia watu wenye moyo kama wako,” alisema akimuaga.
Sikamona aliondoka katika ofisi hiyo ya CCM hali amefurahi na kuridhika kabisa. Akaelekea nyumbani kwake kufunga virago vyake pamoja na kuagana na rafiki zake.
“Hongera kwa uamuzi wako,” Luoga alimwambia huku wakiwa wameshikana mikono wakati wakitoka nje ya ofisi hiyo. Alikuwa amemwomba amsindikize. “Hata mimi ningeenda iwapo mama yangu angekuwa na mtoto wa pili. Lakini nipo peke yangu naye ni mjane.
“Sio lazima twende wote. Kuna mengi ya kufanya
huku nyuma. Sisi tutakuwa mstari wa mbele. Tutategemea sana juhudi zenu mlioko nyuma yetu,” alimjibu ingawa kiasi alimfikiria kama mwoga. Vipi kama kila mmoja angetoa ai hii au ile? Nani ambaye angeikomboa nchi kutokana na nduli mwenye kiu ya damu?
“Mungu akujalie baba…” walimtakia kheri majirani mara ilipofahamika kuwa yeye ni mmoja wa vijana waliokuwa wakijiandaa kufanya msafara huo.
“Nenda na urudi salama.”
“Na… utarudi tu mwanangu.” Zilimfanya Sikamona kiasi aingiwe na hofu.
“Mbona wote wanasema hali wana huzuni? Wanadhani nitakufa?” alijiuliza.
Vipi kama angekufa? Swali hili lilimtia hofu kidogo. Hata hivyo, aliishinda hofu hiyo kwa kujiuliza wangapi wamekwisha kufa kwa ajili ya taifa! Wako wapi wakina Mkwawa, Mirambo, Kinjekitile na askari wao? Wako wapi mashujaa wengi ambao majina yao hata hayakubahatika kuingia katika kurasa za historia? Kwanza hawakufa! Hawakufa kamwe. Majina na hadhi yao vinadumu na vitaendelea kudumu milele kwa ajili ya kujitoa kwao mhanga. Naye akifa jina lake litabaki katika orodha ya mashujaa. Ni bora mara elfu kufa vitani kuliko kukutwa na kifo kitandani au kilabuni.
Mawazo hayo yalimrudishia ushujaa na kumfanya aamue kupigana. Hakuwa na shaka na
uamuzi wake huo.
Sasa kulibaki wajibu mmoja tu, kuagana na Rusia. Asingekwenda bila ya kuonana naye. Kwani moja kati ya sababu ambazo zilimfanya aamue kwenda vitani, ambazo hakumtajia yule Kamanda alikuwa Rusia.
Tangu siku ile ambayo alimwendea kwa haja ya kupanga harusi yao lakini badala yake akaondoka na habari za kuvamiwa, alikuwa amemwendea zaidi ya mara tatu na kurejea bila mafanikio. Siku ya kwanza alimkuta Rusia akiosha vyombo. Akapewa kiti na kukaa kando yake. Kabla hajazungumza chochote Rusia alianza maongezi ya vita kwa sauti ya huzuni. “Ndugu zetu wanakufa bure. Sijui wana hali gani watoto wachanga, wajawazito, wazee, vilema na wote wasiojiweza…”
Sauti yake yenye huruma na majonzi ikamfanya Sikamona ajihisi mwenye hatia kuongelea harusi. Hivyo, aliondoka pasi ya kusema lolote. Safari ya pili walikutana njiani. Kama kawaida Rusia alianzisha maongezi yaleyale ambayo yalikuwa katika midomo ya watu siku zote hizo. Alimweleza Sikamona kuwa amesikia wapelelezi kadhaa wenye mabomu walikuwa wamekamatwa wakiwa katika hatua za kutega mabomu ili kubomoa majengo kadhaa mjini Arusha na hapo Dodoma. Habari hizo zilifuatiwa na nyingine kadha wa kadha zinazosikitisha na kuchukiza.
Sikamona alishindwa tena kutamka alichokusudia.
Wala si habari tu ambazo zilimfanya Sikamona ashindwe kutamka haja yake kwa Rusia, kwani nyingi kati ya alizoambiwa alikuwa amekwishazisikia kitambo. Wala si sauti yake yenye majonzi tu ambayo ilimzuia. Alikwishazisikia sauti nyingi zenye huzuni kuliko hiyo. Kilichomnyang’anya uwezo wa kutamka haja yake, hasa ilikuwa ile hali ya ukosefu wa tabasamu katika uso wa Rusia, tabasamu ambalo lilikuwa likimfariji awapo na huzuni, kumchangamsha achokapo, kumfurahisha hauzunikapo na hivyo kumfanya azungumze lolote analojisikia kulizungumza. Kwake lilikuwa kama nuru ambayo humtoa gizani. Hivyo, kukosekana kwa nuru hiyo ndiko kulikomfanya ayasahau maneno yote, pamoja na kuupoteza ulimi wake.
Hata hivyo, siku hiyo hakukubali kushindwa. Alikuwa amemfuata Rusia kazini kwa ajili hiyo. Rusia alimlaki kwa habari ambayo ilikuwa mpya kwake. “Nasikia serikali imewataka vijana kujitolea kwenda kupambana na hili joka. Mashujaa wengi wanajiandikisha…”
Sikamona hakumbuki kama alimjibu au la. Alichokumbuka ni jinsi alivyofanya haraka kutamka kilichomleta kabla hajashindwa nguvu. “Rusia nimekuja ili tupange lini tufunge ndoa.”
Pengine alisikia, pengine hakusikia. Lakini Sikamona alimsikia akiendelea kama anayezungumza peke yake. “Hadhi iliyoje kijana kujitolea kuilinda nchi yake. Ni mchango ambao hautasahauliwa na nchi hii kamwe. Kama
ningekuwa mtoto wa kiume…”
“Nijibu Rusia. Niambie lini unaona tufunge ndoa,” Sikamona alimkatiza na kusisitiza.
Ndipo Rusia alipomgeukia na kunong’ona kwa sauti ya wazi kabisa, “Sikia, twawezaje kuzungumzia harusi yetu wakati nchi nzima imo katika msiba?”
Maneno hayo kama hayakumkomesha Sikamona, basi yalimtosha. Alijihisi mwenye hatia kubwa kufikiria harusi hali ni kweli kabisa taifa lilikuwa katika msiba mkubwa. Watu wasio na hatia walikuwa wakifa na maiti zao kutupwa mapangoni, watoto wakitaabika kwa ukosefu wa wazazi, mali nyingi za thamani zikiharibika!
Aliyaepuka macho ya Rusia, kisha alianzisha maongezi mengine kwa kupoteza lengo, maongezi ambayo hayakupokelewa na Rusia kwani alionekana yuko maili nyingi nje ya chumba hicho.
Hayo na ule mwito wa taifa, hasa kwa vijana waliopitia jeshi la kujenga taifa, kwenda kujitolea kumwadhibu adui, kulimfanya ghafla asikie akipatwa na njaa ya kwenda huko. Maneno ya Rusia aliposema “Hadhi iliyoje kijana kujitolea… ni mchango usiosahaulika…” na… “twawezaje kuzungumzia harusi hali nchi imo katika msiba…” yalikua katika moyo wake kama kengele ambayo ilimwita kwenda vitani. Kengele hiyo ilizidiwa nguvu na lile tamko la Mwalimu Nyeyerere katika hotuba yake akisema… “Tulieni… Sikilizeni
muone vijana wetu watafanya nini…” vijana wanaotegemewa kama yeye si mmoja wao? Alijiuliza.
Ni hapo alipofikia uamuzi.
Alimkuta Rusia chumbani kwake, kainama akifanya jambo fulani katika sanduku lake la nguo. Sikamona aliingia kwa kumnyatia. Akamkaribia. Lakini kabla hajafanya chochote alichokusudia kufanya Rusia aligutuka na kumwona. Akalakiwa kwa lile tabasamu lake jipya, dhaifu lisilomsisimua.
“Vipi uko safarini?” “Kwa nini?”
“Naona unafungafunga”
“Ah! Niende wapi. Mimi ni mtu wa hapahapa tu.”
Walizungumza mengi wakibadilishana habari, matukio pamoja na kuambiana yote ambayo kila mmoja alidhani mwenzake angehitaji kujua.
Kisha…
“Wajua Rusia? Nimekuja kukuaga” Sikamona alisema baaadaye.
“Kuniaga! Waenda wapi?” “Uganda,”
“Uganda!”
“Vitani.” akasita. “Kesho naondoka kwenda Monduli kupigwa msasa kwa muda mfupi. Baada
ya hapo ndipo nitaelekea mpakani.”
Rusia aliduwaa kwa muda, akimtazama kana kwamba ndio kwanza anamwona maishani mwake.
Ukimya wake ulimtisha Sikamona hata akajikuta akifoka ghafla bila ya kujua anachokifanya.
“Rusia. Sio kosa langu. Ni wajibu ulionilazimisha kuufanya hivyo. Sitakusahau kamwe Rusia. Nitaendelea kukukumbuka daima. Hata kama nikienda kaburini…”
Kama jibu lake Rusia aliinuka na kumkumbatia kwa nguvu. Kwa sauti ya mnong’ono Sikamona alimsikia Rusia akisema, “Usijali mpenzi wangu. Nenda na utarudi salama. Na utakaporudi utanikuta. Na ndipo nitakapokukabidhi zawadi yako maalumu, zawadi ya ushindi.”
Sikamona angependa ainue uso wake. Lakini kwa bahati mbaya hakuuona. Ulikuwa umefunikwa katika kifua chake. Hivyo, alichoambulia ni lile joto la Rusia na mguso wake. Mguso ambao ulimfariji pamoja na kumfanya ajisikie ushujaa ambao alikuwa hajapata kuusikia hapo mbeleni.
ALIPOKUWA mtoto mdogo, kabla hata ya kuanza shule, alikuwa hodari katika michezo yote iliyokuwa ikichezwa na watoto enzi hizo, michezo kama vile ya kukimbizana, mieleka, kutupa mawe na ile miti ambayo waliita mikuki, kujificha porini na kutafutana. Si yeye tu aliyeipenda, bali karibu vijana wote. Michezo ilitawala enzi yao na ilioana na mazingira yao. Hivyo, yeyote kati yao, ambaye aliikwepa wenzake walimtenga na kumdharau wakimwita ‘msichana.’
Ule mchezo wa kujificha na kukimbizana porini ndio uliokuwa maarufu kwao wote. Kila jioni walikwenda msituni na kumteua mmoja wao kama ‘simba’ huyo aligeuka simbamtu na kukabiliwa na jukumu la kuwakamata wengine. Sikamona ilimtukia mara chache sana kukamatwa katika msitu huo ambao aliuzoea hata nao ukamzoea. Alizifahamu vizuri njia na
vitengo vya kila aina ambavyo vilimwezesha kumwepuka ‘simba’ kadhalika, alikuwa hodari wa kujificha katikati ya vichaka vinavyotisha, juu ya miti ambayo matawi yake yalimwezesha kupanda upesiupesi kama nyani ama katika makorongo na mapango yaliyotapakaa huko na huko. Shule ilikuwa imemtenga na michezo hiyo. Hata hivyo, mchakamchaka na gwaride la kila asubuhi ilikuwa badala yake, hivyo, akaipenda shule na kuithamini vilivyo, jambo ambalo lilimfanya achaguliwe kuwa kiranja mkuu akiwa darasa la tano tu na kiranja wa taaluma ya michezo huko sekondari. Kama si kumaliza shule basi ni umri ambao ulimfanya aachane na michezo hiyo kabisa. Akawa akiamka asubuhi na kujikokota kivivu hadi ofisini ambako alishinda kakaa kitini, mafaili yakimtazama kifuani siku zikaja na kwenda.
Halafu likaja Jeshi la Kujenga Taifa. Huko, kwa kiasi fulani, alirudia utoto wake, ingawa kwa njia ya kikubwa zaidi. Licha ya furaha ya kucheza maporini na milimani, alipata fursa ya kujifunza silaha, mbinu za kivita na ukakamavu ambao ulirandana na yale mafunzo ya kuwa ari ya ujenzi wa taifa kiuchumi.
Lakini hayo pia yalichukua muda mfupi tu. Mwaka mmoja baadaye alirejea tena katika maisha yaleyale, maisha ya kitanda na ofisi, maisha ambayo kukimbia mchakamchaka mitaani watu wangekwita mwendawazimu na kupiga gwaride uwani, jirani wangeishuku akili yake.
Leo alikuwemo tena katika michezo hiyo akijifunza na kujikumbusha yote yale ambayo aliyapitia jeshini na utotoni. Lakini safari hii haikuchezwa kwa ajili ya kujifurahisha, kulazimishwa na umri pamoja na mazingira wala kwa sababu ya kujiandaa tu. Ilikuwa maalumu kwa ajili ya hali halisi ambayo ilikuwa usoni mwa kila mwananchi, maalumu kwa ajili ya kuyaokoa maisha ya wananchi na kurejesha hadhi ya nchi. Hivyo, kama wengine, Sikamona alijifunza au kurudia mafunzo ya silaha na ukakamavu kwa juhudi zote.
Kama kawaida, penye wengi pana mengi. Hivyo, wazembe hawakukosekana ingawa walikuwa wachache mno. Hao, ama kwa ajili ya kutopitia michezo hiyo utotoni, au kwa ajili ya uzembe tu, walilazimika kutoroka ama kuombwa na viongozi warejee majumbani na kuwapisha wenye afya. Ilimshangaza sana Sikamona, mtu mzima kushindwa na jambo ambalo mtu mzima mwingine analitenda.
Ni katika kambi hii ambako Sikamona alikutana na Mdoe. Waliwahi kukutana zamani walipokuwa wanafunzi wa shule ya msingi. Baaada ya kumaliza shule hiyo kila mmoja alizama katika upande tofauti wa dunia, akifuata mkondo wa maisha ulikomwelekeza.
Kumbe mkondo wa Sikamona ulikuwa umemtiririsha hadi katika ukumbi wenye heri na matumaini kuliko mwenzake, elimu ya sekondari,
kazi na maisha mema ni baadhi ya heri hizo; si Mdoe ambaye mkondo huohuo ulimsukuma hadi kumdidimiza katika bahari yenye kila aina ya dhiki, majonzi na machungu yasiyo na dalili zozote kukatika.
Alifiwa na mama yake mwaka wa pili tu tangu alipomaliza masomo ya msingi. Halafu, akaangukia katika hifadhi ya mama wa kambo ambaye alikuwa na kila sifa ya u mama wa kambo. Akamlea kwa taabu na kumtunza kwa matusi, masimango na kutumikishwa kitumwa huku akila kwa taabu. Hata hivyo, Mdoe aliendelea kuvumilia kwa kujikumbusha methali inayodai eti, “Baada ya dhiki faraja.” Akawa akiisubiri kwa njaa kubwa siku hiyo, siku ambayo angefarijika na kuneemeka kama wengine.
Faraja aliyoiambulia ilikuwa ile ya kushuhudia kifo cha baba yake kikitokea kwa njia ya ajabuajabu. Alikufa usingizini. Jirani walidai amerogwa hali minong’ono ikisema aliuawa na mke wake ambaye alikusudia kuiba urithi, urithi ambao haukuwa wa haja machoni mwa Mdoe.
Baada ya hapo Mdoe akawa huru katika dunia huru, uhuru uliomtisha na kumbabaisha nusura umtie kichaa, hali ambayo ilimfanya hata adiriki kuutamani ule utumwa wa mama yake wa kambo zaidi ya uhuru huu ambao ulimlazimisha kujitegemea, si kwa chakula na mavazi tu, bali pamoja na mawazo pia.
Hali ambayo iliizeesha mwili na akili zake kabla ya wakati. Akajitoma katika mojawapo ya vijiji vya
kwao Sumbawanga ambako alijijengea kijumba chake na kujilimia mashamba ya chakula. Ni hapo ambapo mawazo yenye matumaini mapya yalianza kuchipua tena katika fikra zake, kwamba huenda angeneemeka na kuwa mtu kama watu wengine, mtu asiye na hofu ya uhuru wala mashaka ya kuishi.
Halafu likazuka hili janga la vita. Likafuatwa na ule mwito wa taifa wa kujitolea kwenda kumwadhibu adui, “Mwito usiopingika” kama alivyowahi kuuita mbele ya Sikamona. Akayaacha yote aliyokuwanayo mkononi na rohoni na kuja kujiunga katika kikosi hiki kilichokuwa kikijiandaa kuelekea katika uwanja wa mapambano.
Sikamona alikuwa amehiari kujitoa mhanga, lakini bado ilimshangaza sana kila alipowaza juu ya watu kama Mdoe na hatua zao za kujitoa. Mara kwa mara alijiuliza kwa nini watu kama hao waliamua hivyo wakati kila mmoja wao alifahamu dhahiri kuwa kitendo hicho ni cha kufa na kupona, kitendo ambacho ni cha kumtoa mtu katika tumaini halisi la maisha yake. Kwa nini? Ushujaa? Labda. Aliwaza. Lakini ushujaa ni nini? Na shujaa ni nani? Mdoe ni shujaa?
Hakupata majibu. Badala yake aligundua tu kiasi gani alikuwa hamwelewi rafiki yake Mdoe, pamoja na watu wengine. Pengine ni vigumu mwanadamu kuufahamu undani wa mwanadamu mwingine, kama ilivyokuwa kwake na Mdoe? Ingawa walikuwa wameishi pamoja miaka saba, wakisoma pamoja, kucheza pamoja, kushirikiana
na kugombana, kuchokozana na kupatana n.k lakini bado alikuwa hamwelewi hata kidogo. Hakuifahamu siri iliyofichika katika nafsi yake, siri ambayo ilikuwa imemnyang’anya hofu ya kifokiasi cha kumsukuma kuyanadi maisha yake.
Nyakati kama hizo ilimjia kujiwazia yeye binafsi pia. Ni kipi hasa kilichokuwa kimemtoa hofu ya kifo? Yeye ni shujaa? Ushujaa ni nini? Au inatosha kuwa aliamua kupambana kwa ajili ya uchungu na aibu ya kuvamiwa? Mbona walikuwepo wengi ambao hawakuwa tayari kujitolea? Wengi hata baadhi ya wale ambao wameshuhudia jamaa zao wakichinjwa kama mbuzi na kuzikwa kama mbwa! Yeye ni shujaa? Alijiuliza tena na tena kiasi kwamba si kwamba hakuelewa watu kama Mdoe tu, bali pia hakuwa hata na uwezo wa kujielewa yeye mwenyewe.
sasa alikuwa tayari uwanja wa mapambano. Tayari. Tayari kabisa. Tayari kwa lolote. Tayari kufa, tayari kuua.
Giza lilikuwa likikaribia kuimiliki nchi nzima. Nuru hafifu iliyobakia ilimwezesha kuona umbali wa mita chache tu toka katika handaki lake. Alikuwa amelala ndani ya handaki hilo, mtutu wa bunduki lake ukielekea upande ambao uliaminika adui alikuweko. Alikuwa ameipakata barabara silaha yake, tayari kuipa uhai wakati ambao amri ingetolewa. Mavazi yake ya mabaka na kofia yenye muundo wa kichaka vilimfanya awe kama kichaka cheusi kilichoota pangoni.
Aliendelea kutulia, ukimya mwingi ukiwa umetapakaa anga zima, ukimya huo wa kutisha pamoja na kimya kingi ambacho kilitanda huko na huko vilimfanya ajikumbushe jambo moja
ITAENDELEA
Zawadi ya Ushindi Sehemu ya Tatu
Also, read other stories from SIMULIZI;