Shindikana Sehemu ya Tano
LIFESTYLE

Ep 05: Shindikana

SIMULIZI Shindikana
Shindikana Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA: UNKNOWN

**************************************

Chombezo: Shindikana

Sehemu ya Tano (5)

“Kwa nini wasema hivyo mpenzi?”. Jasmine aliuliza huku akinitazama usoni.

“Unajua malaria mimi naifahamu sana. Dalili zake ni kama hizohizo ambazo umezitaja. Itakubidi uende hospitali ukapime ili uanze dozi mapema?”. Nilongea huku nikimfariji Jasmine.

“Basi jana niliamua kwenda hospitali kwa lengo la kupima. Baada ya vipimo, niligundulika kwamba nina ujauzito wa mwezi mmoja”.

.

“Unasemaje weweeeee?”. Niliuliza kwa taharuki utadhani ya kwamba nilikuwa sijakisikia kile ambacho Jasmine alikuwa amekiongea.

“Nina ujauzito wa mwezi mmoja mpenzi”. Jasmine alirudia kuongea tena kwa mkazo.

“Hapana haiwezekani!”. Niliongea huku ubongo wangu ukiwa kama umeacha kufanya kwa sekunde kadhaa.

“Sasa haiwezekani nini?”. Jasmine alihoji kwa mshangao.

“Sasa wewe unafikiri tutafanyaje?”. Nami nilimjibu kwa kumkandika swali.

“Tutafanyaje kivipi?”. Naye alinijibu kwa kunirushia swali lilelile.

“Hivi wewe huoni kama hili ni tatizo kubwa?”. Nilimwambia.

“Sasa kuna tatizo gani hapo wakati wewe ulisema wanipenda na wataka kuanza maisha na mimi”. Jasmine aliongea.

“Sawa, lakini vipi mama Careen akiligundua hili? Huoni kwamba patachimbika?”. Nilijaribu kutoa tahadhari.

“Hilo utajua wewe maana tangu mwanzo mimi nilikwambia kuhusu hili. Je, wewe ulinijibuje? Si ulisema nikuachie wewe ya kwamba utajua namna ya kufanya!”. Jasmine aliongea huku sasa akionekana kukasirika kidogo usoni.

“Sawa la … la … lakini ….”. Kigugumizi cha ghafla kilinijia.

“Lakini nini?”. Jasminie aliuliza.

“Tena ulisema wewe ndiye mwanaume wa nyumba na unaamua nini ukifanye na nini usikifanye. Hebu acha kunichanganya bwana”. Moto wa Jasmine sasa ulizidi kupanda.

“Ok, mama wala usijali. Mimi nitajua namna ya kufanya. Nakupenda sana Jasmine”. Niliamua kumuweka sana ili kuisafisha hali ya hewa ambayo niliona inaanza kuchafuka taratibu.

.

“Hayo ndiyo maneno. Siyo unakuwa unaleta ngonjera zako hapa ambazo hazieleweki kama siyo mwanaume bwana!”. Jasmine aliongea huku akionesha wazi kwamba alikuwa na furaha kutokana na maneno yangu.


Ujauzito wa Jasmine ukazidi kuyaimarisha mapenzi yetu. Mimi nikampenda sana Jasmine na yeye pia akanipenda sana. Tulithaminiana na kuheshimiana. Tuliweka ahadi na mipango mingi na kabambe katika kuliimarisha penzi letu.

Ujauzito wake ukazidi kukua kwa kasi. Miezi ikazidi kukatika. Kichwa changu kikawa na mawazo mengi sana ambayo yalikuwa yakizidi kuongezeka kila uchao.

Nilikuwa nikiwaza ni namna gani nitaweza kukabiliana na varangati la mama Careen pindi ambapo atakuja kuyagundua mahusiano yangu ya kimapenzi na Jasmine.

Hilo lilikuwa ni dogo kati ya yale ambayo nilikuwa nikiyawaza. Jambo kubwa ambalo ndilo liliniumiza kichwa hasa ni suala la ujauzito wa Jasmine. Suala la mimi kutembea na Jasmine niliona ningeweza kulizima endapo moto wa mama Careen ungewaka lakini suala la ujauzito mh!

Hili lilikuwa kubwa na nilishindwa kulibeba kabisa. Nilikuwa nikiliona kabisa jahazi likienda mrama na mimi kama nahodha nilikuwa sina uwezo wa kulinusuru jahazi hili katika gharika hili kubwa.

“Lakini haya yote ameyataka yeye mwenyewe mama Careen. Mwanamke ni mshari balaa. Hajui hata kuibembeleza na kuitunza ndoa. Kila siku ni ugomvi tu ambao hauna hata sababu ya msingi”. Niliwaza siku moja nikiwa chumbani wakati mama Careen akiwa nje uwanjani akicheza na Careen.

“Furaha ya ndoa yetu ilipotea miaka mingi nyuma. Siku za mwanzo za ndoa yetu ndipo nilipolifurahia penzi langu na mama Careen lakini baada ya hapo, ndoa yetu ilibadilika na kuwa chungu kabisa”. Niliendelea kuumizwa na mawazo kichwani mwangu.

“Na kila nikijaribu kumsogeza jirani mke wangu ili tuitengeneze ndoa yetu, yeye alikuwa mbali nami zaidi ya kuzidisha ushari wake. Hajali kabisa ustawi wa ndoa yake”. Nilizidi kutiririkwa na mawazo lukuki mengine yakiwa ni maswali ambayo yalikosa majibu.

Hatimaye taratibu machozi ya uchungu yakaanza kuniporomoka. Niliumia kwa sababu mimi na mke wangu tulikuwa tumeshindwa kuitengeneza ndoa yetu na hatimaye ilikuwa ikielekea katika misukosuko.

.

Baadaye usingizi ukanipitia na kunisahaulisha yale yote ambayo yalikuwa yakiniliza. Nilianza kuota ndoto nzuri na tamutamu juu yangu na Jasmine. Niliota tukiyafurahia maisha pamoja.


Siku moja mama Careen akawa amepata mgeni. Mgeni huyu alikuwa ni mwanamke. Mwanamke huyu alikuwa ni mzuri na mrembo sana.

“Mh! Mdogo wangu wewe una mambo makubwa sana”. Mama Careen aliongea pindi walipokuwa wamekaa sebuleni.

“Kwa nini waongea hivyo dada?”. Mgeni aliuliza.

“Yaani tumepoteana miaka mingi sana hatuonani. Halafu jambo la kushangaza eti sote twaishi katika jiji hilihili la Kano”. Mama Careen aliongea.

“Nisamehe dada yangu. Ni maisha tu ndiyo yamesababisha yote haya”. Mgeni aliongea.

“Wala hata usiyasingizie maisha. Maisha ndiyo yakufanye ushindwe hata kunijulia hali nduguyo?”. Mama Careen aliendelea kuongea kwa kutoa lawama kwa mgeni ambaye alikuwa ni mdogo wake.

“Halafu naona mambo yako si mabaya. Yaani safari hii umeamua kabisa kutundikwa mpaka mimba. Mbona siyaamini macho yangu!”. Mama Careen aliongea kwa mshangao huku akilitazama tumbo la mdogo wake ambalo kwa sasa lilikuwa kubwa.

“Dada yangu. Mimi safari hii ninataka kuolewa. Nimepata mchumba ambaye ananijali na yuko tayari kabisa kunioa”. Mgeni aliongea.

“Ha ha ha ha haaaaaaaa! Yaani Jasmine wewe leo hii unataka kuolewa?. Mh! Haya bwana. Je, na biashara yako ya ukahaba unamwachia nani?”. Mama Careen aliuliza.

“Ile biashara nilikwishaiacha dada. Huyu mchumba wangu ndiye ambaye amenibadilisha na kunifanya niiache biashara hii kabisa. Nimeamua kubadilika kabisa na kuanza maisha mapya dada yangu”. Mgeni aliongea huku machozi yakimlengalenga.

“Yaani leo ndiyo unatambua kwamba biashara uliyokuwa ukiifanya ilikuwa ni mbaya. Je, wakati mimi nakukanya juu ya biashara ile mbona hata ulikuwa hunisikilizi?”. Mama Careen aliongea.

“Nisamehe dada yangu. Na ndiyo maana leo hii waniona niko hapa mbele yako nikiwa nimebadilika kabisa. Mimi si yule Jasmine wa zamani, kahaba. Mimi ni Jasmine mpya. Naomba unisamehe kwa yote ambayo nilikukosea dada yangu mpenzi”. Jasmine aliongea huku akiporomokwa na machozi.

“Haya nimekusamehe mdogo wangu”. Mama Careen aliongea huku akimkumbatia Jasmine.

Ghafla simu ya Jasmine iliita.

“Hallo! Baby”. Jasmine aliongea mara baada ya kubonya kitufe cha kupokelea simu.

“Uko wapi? Mbona nimefika hapa kwako sijakuona?”. Upande wa pili wa simu uliongea.

“Nisamehe mpenzi wangu. Leo nimeenda kumtembelea dada yangu yule ambaye nilikwambia”. Jasmine aliongea.

“Sasa mbona hukunitaarifu?”. Upande wa pili wa simu uliongea.

“Naomba unisamehe mume wangu. Mimi nilifikiri kwamba hutakuja nyumbani kwa wakati huu ndiyo maana sikukutaarifu. Nisamehe sana mpenzi wangu”. Jasmine aliongea.

“Ok, nimekusamehe”. Upande wa pili wa simu uliongea.

“Halafu mpenzi, nilipenda jioni ya leo twende pamoja huku kwa dada yangu ili nikutambulishe kwani dada ana hamu kubwa sana ya kukuona”.

“Ooooh! Hilo wala usijali. Nitajaribu kuziweka sawa ratiba zangu ili kusiwe na usumbufu wowote”. Upande wa pili wa simu uliongea.

“Ahsante sana mpenzi”. Jasmine alishukuru.

“Ok, usijali”. Upande wa pili wa simu uliongea.

Baada ya Jasmine kuongea na ile simu, basi maongezi yake na mama Careen yakaendelea. Wakaendelea kupeana michapo ya hapa na pale ambayo iliwaletea furaha tele katika nyoyo zao.

“Ndiyo hivyo dada. Hakika utampenda kwani ni mwanaume mzuri, mtanashati, anayejali na ambaye anajua nini maana ya pendo la dhati”. Jasmine aliongea.

“Mh! Haya bwana. Waswahili walisema mtu chake. Tutaona hiyo jioni kama hizo sifa unazompamba kweli anazo?”. Mama Careen aliongea huku akicheka.

CHANZO CHA TATIZO MAMA CAREEN NADHANI UMEPATA PICHA.

Hapa hii inaitwa Ndoige ya Mandonga hahaha.. Dada MTU laiti akijuwa Wanashea Mme itakuwejeee????

Mbaya zaidi Mdogo MTU Mjamzito loooh… Hapo nani MBAYAA????

Waswahili Husema Nyumba Ikosapo furaha lazima kuna kuteleza nje kupata furaha au Amani ya moyo hii inaambatana na Majuto Mjukuu,unakuja kuelewa tatizo its too late kama ilivyo Kwa mama Careen.

“Hodi humu ndani!”. Nilipiga hodi mara baada ya kufika nyumbani na kubaini kwamba mlango ulikuwa umefungwa.

Kwa upande wa wakati ilikuwa ni majira ya mchana. Nilikuwa nimerudi nyumbani mapema ili nipate kujiandaa kwa ajili ya safari yangu na Jasmine kwenda kwa dada yake kwa ajili ya kunitambulisha.

Sikutaka kabisa kumwangusha mpenzi wangu Jasmine.

Mlango ulifunguliwa na mama Careen ambaye leo alinishangaza sana. Uso wake ulikuwa na furaha kubwa sana tofauti na siku zote katika maisha yetu ya ndoa. Hakika sijawahi kumshuhudia mke wangu akiwa katika hali hii ya furaha katika maisha yetu ya ndoa.

Furaha ile iliufanya uso wake uchanue na kuuruhusu uzuri wake uonekane dhahiri. Hakika mke wangu alikuwa ni mwanamke mzuri sana ila uzuri wake siku zote ulikuwa ukifunikwa na ukali wake.

Roho yangu sasa ilianza kuniuma. Nikaanza kujilaumu ni kwa nini nilikuwa nikimsaliti mwanamke huyu ambaye mwenyezi Mungu alikuwa amenipatia.

Ikafika kipindi mpaka nikataka nighairi safari yangu ya kwenda kwa Jasmine lakini nikaamua kukaza kwamba kwani nilimfahamu sana huyu mwanamke. Alikuwa ni mwanamke ambaye alikuwa hatabiriki.

“Leo tuna mgeni mume wangu”. Mama Careen aliongea kwa furaha.

“Mgeni?”. Niliuliza kwa staajabu.

“Ndiyo mume wangu”. Mama Careen alijibu.

“Mgeni gani?”. Name nikauliza.

“Mdogo wangu, yule ambaye nilikuwa nikikupa habari zake kila siku”. Mama Careen akaongea.

“Anhaaaaaa! Basi hamna tatizo”. Nilimjibu mama Careen mara baada ya kukumbuka kwamba amekuwa akinieleza mara kwa mara kwamba ana mdogo wake ambaye anaishi katika jiji hili la Kano.

Mama Careen akatangulia mbele kuelekea sebuleni akaniacha mimi pale mlangoni huku nikijiweka sawa mavazi yangu kwa lengo la kwenda kukutana na mgeni ambaye nilikuwa sijawahi kukutana naye hata siku moja.

Nilipoingia ndani moyo wangu ulitaka kupasuka kwa mshutuko mkubwa sana ambao uliupata. Macho yangu hayakuamini kile ambacho yalikuwa yakikishuhudia. Ubongo wangu ndiyo uligoma kabisa kukubaliana na picha nzima ambayo ilikuwa ikionekana pale sebuleni.

“He! Mayanja vipi? Umekujuaje huku?”. Jasmine aliuliza swali ambalo lilileta utata kwa mama Careen.

Mimi nikaiona hali ya hewa imeanza kuchafuka kabisa pale sebuleni. Nikakosa kabisa nmana ya kuweza kulinusuru lile balaa ambalo harufu yake ilianza kusikika.

“Vipi Jasmine, kwani mnafahamiana?”. Mama Careen aliuliza kwa mshangao.

“Huyu ndiye yule mchumba wangu ambaye nilikuwa nikikueleza hivi punde kwamba anataraji kunioa. Mayanja huyu ni dada yangu mpendwa anaitwa mama Careen”.

Masikini Jasmine alikuwa akiyaongea haya yote asijue ni siri gani ilikuwa nyuma ya pazia. Hakujua kabisa kwamba aliyekuwa akimkaribisha alikuwa ni mwenyeji wa nyumba ile na ndiye ambaye alipaswa kumkaribisha yeye.

Mama Careen hakukiamini kile ambacho alikuwa akikisikia. Alibaki amesimama akiwa ameduwaa huku macho akiwa ameyatoa mithili ya mjusi ambaye alikuwa amebanwa na mlango.

Ghafla mama Careen alianguka chini na kuzimia. Kitendo kile kilizua tafrani kubwa mle sebuleni na kufanya kila mtu ataharuki.

“Kwani ni nini kinaendelea Mayanja? Mbona sielewi?”. Jasmine alihoji wakati huo mimi nikiwa ninampepea mama Careen.

“Fanya utaratibu tumuwahishe hospitali Jasmine. Huyu ndiye mke wangu niliyekuwa nakueleza siku zote”. Nilimweleza Jasmine.

“Oooooooh! Mamaaaaaaa! Jamani Mayanja. Ni kwa nini umenitenda hivi. Mbona umenitia aibu ambayo nitashindwa kuibeba. Nitaiweka wapi sura yangu jamani?”. Jasmine naye alikaa chini na kuanza kulia.

Mimi nikaona hapa nikifanya uzembe nitampoteza mama Careen. Nikachomoka mbio kutoka mle sebuleni na kuelekea nje ambako nilitafuta taksi.

Tulimpakia mama Careen na kumuwahisha hospitali. Na kwa wakati wote huo Jasmine alikuwa amempakata Careen huku akilia kwa uchungu.

Tulipofika hospitali, tulimshusha mama Careen na manesi wakampokea na kumpeleka kwa lengo la kupatiwa huduma. Hali yake haikuwa nzuri hata kidogo.

Mimi na Jasimine tulikaa katika dawati la kupumzikia huku tukimwomba mwenyezi Mungu atende muujiza wa kuyanusuru maisha ya mama Careen.

Baada ya dakika kama ishirini hivi kupita, daktari alitoka na kutujia pale ambapo tulikuwa tumekaa.

“Ok, wewe ndiye mume wa mgonjwa?”. Daktari aliuliza hilo kwa kuzingatia maelekezo ambayo tulikuwa tumeyaandikisha kwa nesi awali pindi tukimfikisha mgonjwa pale hospitalini.

“Ndiyo dokta. Mgonjwa wangu anaendeleaje?”. Nilimwuliza daktari kwa bashasha ya kutaka kujua hali ya mama Careen.

Daktari hakunijibu bali alinivuta na kunisogeza mbali kidogo na Jasmine. Moyo wangu ulikuwa una hofu kubwa sana kwa wakati ule.

“Wewe ni mwanaume hivyo unapaswa kujikaza kiume kwa taarifa hii nitakayokupa”. Dakatari alianza kuongea huku akinigongagonga bega.

“Unataka kusema nini dokta?’ Nilimwuliza daktari huku nikiwa nimemtolea macho.

“Kwa bahati mbaya, mkeo tumempoteza. Amefariki dunia”. Maneno yale yaligota katika ubongo wangu na kuniletea kizunguzungu ambacho kinilinifanya nile mweleka na kuanguka chini.

Baada ya hapo nikazirai.


Mazishi ya mama Careen yalifanyika nyumbani kijijini kwetu. Ulikuwa ni msiba mkubwa sana ambao ulinipa uchungu mkubwa. Msiba huu ulikuwa umekitikisa kijiji chetu kutokana na umaarufu wangu.

Jasmine kwa wakati wote huo alikuwa akilia asijue ni nini cha kufanya. Kifo cha dada yake kilikuwa kimemchanganya kabisa.

Baada ya mazishi ya mama Careen tulikaa matanga.

Msiba ulipokwisha, mimi na Jasmine tulirejea jijini Kano huku Careen tukiwa tumemwacha kijijini na bibi yake.

Maisha yetu jijini Kano hayakuwa ya furaha hata kidogo. Ile furaha ambayo mimi na Jasmine tulikuwa nayo ilikuwa sasa imeyeyuka.

Baada ya wiki mbili toka mimi na Jasmine tutoke kijijini, kuna tukio moja kubwa sana lilitokea. Tukio hili lilizidisha ule uchungu ambao mimi nilikuwa nao.

Jasmine alikutwa akiwa amekufa kwa kunywa sumu huku akiwa ameacha ujumbe wa kunituhumu mimi kuwa ndiye msababishaji wa madhila hayo yote.

Polisi walinikamata na kunifungulia mashtaka ya kusababisha vifo vya watu wawili ambao ni mama Careen na Jasmine. Kesi hii ilikuwa nzito na ililalia upande wangu.

Hatimaye nikapatikana na hatia na nikahukumiwa kifungo cha miaka ishirini gerezani.

FUNZO

Katika mahusiano ya ndoa yatupasa tuepuke tamaa. Turidhike na ndoa zetu. Siku zote tuishi katika kuzijenga ndoa zetu na si kuzibomoa. Tuepuke kufanya maamuzi ambayo baadaye huja kutugharimu

MWISHO*

MWISHOOOO

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment