Fedheha Sehemu ya Kwanza
MAISHA

Ep 01: Fedheha

SIMULIZI Fedheha
Fedheha Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Simulizi: Fedheha

Sehemu ya Kwanza (1)

Mbanano mkubwa katika daladala niliyokuwa nimepanda kutokea Kariakoo kuelekea Mbezi ya kimara kwa mama yangu mdogo ulinizuia hata kugeuka nyuma japo nilitamani sana kugeuka ili niweze kushuhudia jambo fulani lililokuwa linatokea karibu yangu, akili yangu yote ambayo awali ilikuwa imeelekezwa katika mkoba niliokuwa nimeshikilia kwa usalama wa mali chache zilizomo sasa ilikuwa imehama.

Mlio wa simu niliousikia ndani ya daladala ulinishtua sana, tofauti na mchumba wangu Latipha niliamini hakuwepo mwanadamu yeyote aliyekuwa nao kwenye simu yake kwani nilikuwa nimeubuni mwenyewe kiujanja ujanja japo haukuwa na mvuto sana ila nilimpa huyo mchumba wangu kama zawadi katika maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa. Tangu siku hiyo akaufanya kuwa muito katika simu yake.

“Ina maana Latipha yupo ndani ya gari hili au kuna mtu ameiazima simu yake!!!!” nilijiuliza mimi Khalfani bila kupata jibu lolote lile, jasho lililokuwa linanitoka kwa sababu ya mbanano mkubwa ndani ya gari sasa liliongezeka maradufu kutokana na hisia mbaya zilizonijia kichwani mwangu. Hisia kali za wivu na hasahasa kusalitiwa.

“Lakini amekuja kufanya nini sasa huku wakati ameniambia anaumwa sana na leo hatatoka???” niliendelea kujiuliza huku nikikumbuka mawasiliano yangu ya mwisho na Latipha!!

“Au Latipha amemuonga simu mwanaume wake mwingine maana hata jana alikataa kata kata kuamka kutoka kitandani eti kisa amechoka sasa nini hicho kimemchosha?? ” nilijiuliza kwa mara nyingine, hakika nilikuwa na hasira sana kwani nilimpenda sana Latipha na niliamini siku moja atakuwa mke wangu. Hivyo sikutaka mwanaume yeyote yule ajiweke karibu naye.

Wivu wangu ulikuwa unaniteketeza.

Nilitamani ile simu iendelee kuita mpaka tutakaposhuka niweze kujua ni nani anayo huenda hata ninamfahamu ili aweze kunipa ufumbuzi wa mawazo yangu hayo, lakini haikuwa hivyo mlio haukuendelea tena baada ya simu ile kutopokelewa na mwenye simu na baada ya pale haikuita tena hadi tuliposhuka.

Nikakosa ushahidi wowote wa kumtuhumu Latipha nikabaki kuumia peke yangu. Niliumia kwa sababu nilikuwa nampenda vilivyo

“Mapenzi yananipeleka puta mimi Khalfani” nilijiwazia wakati nakaribia kufika kituo cha Temboni ambapo ndio ulikuwa mwisho wa safari yangu.

Nilijipa moyo kwamba huenda mlio ule niliufananisha, nilifanya hivyo ili kupunguza machungu yaliyokuwa yanaivizia nafsi yangu wivu ulikuwa umechukua nafasi yake kwa kiasi kikubwa sana katika moyo wangu wa nyama.

Niliamini Latipha aliumbwa kwa ajili yangu pekee.

Latipha hakuumbwa kwa ajili ya mtu mwingine duniani.

Mawazo haya nd’o yaliyozidi kuufanya moyo wangu uwew unaumia hata kwa hisia zisizokuwa sahihi.


Majira ya saa tatu usiku nilikuwa njiani kurudi Kurasini chuo cha uhasibu ambapo nilikuwa nasoma, nilirudi kwa sababu moja tu kuna nguo zangu niliziacha nje baada ya kuzifua na katabia ka wizi kalikuwa kameibuka ghafla pale chuoni, sikuona haja ya kuwasumbua wenzangu ninaoishi nao chumba kimoja kunianulia kwani niliamini Jamestafanya kama ninavyotaka mimi.

Hasahasa siku za mwisho wa juma kama hivi wao hupendelea kwenda kujirusha katika kumbi za starehe. Jambo hilo Khalfani mimi sikujaaliwa kuvutiwa nalo katika umri wangu huo, japo zamani nilikuwa mpenzi wa masuala hayo. Lakini nilipogundua hakuna manufaa ninayoyapata nikaamua kujiweka kando.

Wote waliamini kuwa sitarejea siku hiyo kwa sababu ilikuwa kawaida yangu kuanzia ijumaa hadi jumapili kutoweka eneo la chuo na kuelekea kwa mchumba wangu Latipha halafu baadae kwa mama mdogo Mbezi ya Kimara maeneo ya Temboni.

Kwa sababu funguo za chumba nilijua ni wapi huwa zinahifadhiwa sikuhangaika kumpigia mtu yeyote simu, nilirejea kimya kimya.

Saa nne usiku nilikuwa mbele ya chumba chetu, kama nilivyodhania ni kweli hapakuwa na mtu yeyote nikachukua funguo kutoka chini ya tambala la kujifutia miguu mbele ya mlango kisha nikafungua na kuingia ndani.

Harufu iliyonipokea pale iliupasua moyo wangu upya kwa hofu, hofu ambayo tayari ilikuwa imejificha baada ya kusikia mlio wa simu ya Latipha kwenye daladala niliyokuwa nimepanda, sasa kilikuwa kitu kingine, yalikuwa ni marashi yaliyonukia kama ya Latipha mchumba wangu yaliyotawala pale ndani, yalikuwa marashi yanayoitwa ‘one million’ hakuna hata mmoja pale chumbani kwangu aliyekuwa anayatumia wala wapenzi wao na ilikuwa nadra sana kuyapata kwani yalikuwa aghali sana. Niliyanunua kwa gharama kubwa bila kujutia kwa sababu ya kumfurahisha Latipha.

Kwa sababu ya kupalilia shamba la mapenzi kati yetu!!

“Amekuja kufanya nini wakati nimemuaga kwamba mimi naenda nyumbani na sitegemei kurudi hadi jumapili???….halafu si anaumwa yule amekuja kumuona nani huku, na mbona Jamesjaniambia sasa kama amekuja??” nilijiuliza maswali mengi huku harufu ile ikiendelea kuzisumbua pua zangu kwa fujo.

Hakuwepo wa kunijibu!!!

Nilitamani atokee mtu mbele yangu nimuulize kama Latipha alipita hapo lakini hakuwepo, chumba kizima nilikuwa peke yangu. Hakika niliumizwa na hisia.

Hata kilichonipeleka pale chuoni nilikisahau, chumba nilikiona kichungu ghafla, sikukumbuka kwenda kuanua nguo tena hadi majira ya saa nane na nusu usiku ndipo nilikumbuka kuwa nguo ziko nje bado.

Kutokana na uwepo wa mwanga wa umeme palionekana bado mchana pale chuoni pia kelele za midundo ya muziki katika madarasa kadhaa ilizidi kunipa ujasiri wa kutoka nje, hivyo bila wasiwasi nilijongea hadi mahali nilipozianika nguo zangu na kuzianua moja baada ya nyingine kisha hatua kwa hatua nikaanza kurejea tena chumbani. Nilipofika mlangoni nilisita kidogo, sikumbuki awali kama niliacha mlango wa chumba wazi, kumbukumbu zangu zinadai kwamba nilifunga tena vyema kabisa kulikoni upo wazi, nilidhani nimefananisha chumba lakini kilikuwa kilekile chumba namba kumi na nane (22) nilichoishi pamoja na wenzangu watatu.

Nikiwa nazidi kukaribia mlangoni nilisikia sauti za watu mle ndani, mara moja niligundua walikuwa ni James pamoja na Michael sauti zao nilikuwa nimezikariri sana kwani hao ndio walikuwa ndugu na rafiki zangu wa karibu pale chuoni.

Walikuwa wanaongea kwa sauti zao za kilevilevi, lakini walikuwa wakizungumzia juu ya mtu waliyemuita shemeji yao, lakini mambo waliyoyazungumza yalionekana wazi kuwa kuna kitu kibaya kinaendelea hapo katikati.

Walikuwa wanazungumzia kuhusu mziki huku wakikisifia kiuno chake, na hapo wakaenda mbali zaidi na kusema kuwa hawajui ameondoka na nani lakini lazima atakuwa ameondoka na mtu!!

Nilikuwa natetemeka huku nikiomba maongezi hayo yasiwe juu ya mtu ninayemuhisi mimi yaani Latipha maana huyo pia alikuwa shemeji yao. Na mbaya zaidi niliyasikia yale marashi yake chumbani pale.

Wakati huo nilikuwa nimeangusha baadhi ya nguo bila kujua, mara nikasikia Michael anavaa viatu ndipo nikagutuka na kuamua nini cha kufanya. Nikiwa bado sijielewi mara mlango ukafunguliwa.

“Haa!!! Khalfani ni wewe….mh!! umerudi saa ngapi jamaa….” Alinihoji Michael huku dhahiri akionyesha kushtushwa na uwepo wangu eneo lile, nilimjibu kwa tabasamu hafifu, na kisha nikamweleza kwa nini nipo pale hadi wakati ule huku nikijilazimisha kutabasamu.

“Hee!! Khalfani nawe, yaani ukaona tabu kutupigia simu tukuanulie ona sasa eti umeona ni heri kulipa nauli sijui elfu mbili nzima kuliko kupiga simu….hee!! sikuwezi ndugu” alisema Michael huku akiondoka kuelekea msalani.

Niliokota nguo nilizokuwa nimeangusha kisha nikaingia ndani, cha ajabu na kuduwaza James huyu huyu niliyemsikia kwa masikio yangu akipeana habari na Michael nilimkuta amelala hoi kabisa, na aliongezea na kukoroma juu. Sikutaka kuamini kwamba nilichosikia kwa masikio yangu hakikuwa kweli. Hapana sikuiruhusu akili yangu kunidanganya, sikumsemesha kitu James nilijidai sijui lolote nikapanda kitandani kwangu na kuanza kukunja nguo zangu moja baada ya nyingine kwa utaratibu mbovu ambao sijawahi kuutumia hii ni kwasababu sikuwa hata najua ni nini nafanya, kisha nikazipanga katika kabati lililokuwa hapo chumbani kisha nikaingia kulala.

Nilijaribu kuulazimisha usingizi.

Kuepusha usumbufu wowote na mimi nikajidai nimesinzia hoi lakini ukweli ni kwamba sikuwa hata na lepe la usingizi, mawazo yangu yalikuwa yanavutana huku na huku, sikujua lipi ni sahihi na lipi sio sahihi.

Hakika niliteseka sana usiku ule, nilijigeuza huku na kule bila mafanikio yoyote ya kuupata usingizi. Nilijiuliza kama kweli huyu Latipha ambaye hadi kaka na dada zangu wanamfahamu anaweza kunifanyia kitendo kama kile tena kwa rafiki zangu wa karibu kiasi kile, jibu la haraka haraka lilikuwa HAPANA haiwezekani alinipenda sana.

Nilijichagulia jibu lile ili kuufariji moyo wangu!!

Sikujua kuwa kujikaza kule ni kuendelea kulitunza bomu ambalo muda wowote ule linaweza kulipuka na kuleta madhara makubwa!!!

Aah! Sikujua Khalfani mimi!!

Kitendo cha kuanza kuhisi kuwa kuna mchezo ambao yawezekana nilikuwa nikichezewa na Latipha kilinisumbua sana kichwa na kunifanya niishi kwa tahadhari kubwa sana. Niliamini fika kuwa moyoni nilikuwa nampenda kwa dhati binti yule na sikutaka aguswe na mwanaume mwingine.

Nikajaribu kuikumbuka sauti yake tulivu yenye madaha ya kike ikininongóneza kuniambia kuwa ananipenda.

Macho yake hayakuficha kitu chochote Latipha alikuwa akinipenda kwa dhati.

Nikaamua kulifukia lile jambo nikafanya kitendo cha Kiswahili kiitwacho ‘funika kombe mwanaharamu apite!!!

Siku iliyofuata nilipokea jumbe za kawaida kutoka kwa Latipha akielezea kuukosa uwepo wangu jirani yake.

Nikayafumba macho yangu na kufikiria mambo chungu nzima ambayo huwa nayafanya na Latipha tukiwa katika faragha yetu.

Nikajiuliza itakuwa vipi siku nikitambua kuwa mambo yaleyale anayafanya na mwanaume mwingine.

Hakika nilitetemeka!!

Siku zikazidi kusonga na tukio lile la kunusa harufu ya marashi ya Latipha chumbani kwetu baada ya kurejea ghafla likiwa linaendelea kunishambulia.

Hatimaye nikaamua kuupunguza mzigo ule nikaamua kuzungumza na mwalimu wangu pale chuoni, mwalimu ambaye tulitokea kuelewana naye sana.

Nilimueleza hisia zangu kali juu ya Latipha na hatimaye nikamwelezea juu ya mashaka yangu juu ya nuaminifu alionao Latipha juu yangu.

Mwalimu yule aliyekuwa ameamua kunipa masaa mawili kwa ajili ya kujadili jambo lile alinieleza kwa kina juu ya mahusiano na kisha akanieleza tabu wanazozipata hata wao walio katika ndoa.

Lakini akanieleza kuwa ikiwa uwezo wangu utaruhusu basi nikimaliza chuo tu nimuoe Latipha awe mke wangu halali kabisa ambaye jamii inatambua na baada ya hapo nitakuwa na amri juu yake.

Alipokuwa akizungumza hata akaniuliza iwapo nimewahi kumwel;eza Latipha juu ya ndoa, nikatikisa kichwa ishara ya kukataa.

Akanisihi nianze kuzungumza nayer mambo hayo kwa sababu ndoa ni kitu cha thamani kuliko haya mapenzi ya kuambiana nakupenda kila kukicha!!!

Wazo la mkufunzi likanikaa kichwani, nikaamini ule usemi usemao kuwa mtu mzima dawa.

Miezi minne si mingi sana!!!

Nikaamua kulivalia njuga suala lile la ndoa.

Nilisahau usemi usemao akili za kushikiwa changanya na za kwako!!!

Nikaamini ndoa itakuwa tiba ya wivu wangu juu ya Latipha!!!


Hayawi hayawi hatimaye yakawa.

Nikamuoa Latipha akawa mke wangu rasmi. Mke ambaye jamii ilimtambua, kwao nikakubalika na yeye kwetu akikubalika.

Huu ukawa mwanzo wa kupona lile jeraha ambalo lilikuwa likinisumbua kabla Latipha hajawa mke wangu rasmi.

Nilimuoa Latipha wakati yu likizoni nami nikiwa nimemaliza masomo yangu ya chuo kikuu.

Tukadumu katika nyumba moja kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu tu. Mke wangu Latipha akarejea shuleni.

Ama hakika umbali hunyausga mapenzi na kuchipua penzi jipya kwa wanandoa wengi.

Ni hili jambo ambalo lilinitokea mimi Khalfani.

Nilijaribu kumtembelea mke wangu mara kwa mara chuoni kwake. Awali alikuwa akinitambulisha mbele ya marafiki zake wachache pale chuoni lakini baadaye utambulisho huu ukanyauka.

Tukaanza kuishi kimazoea, hilo la kuishi kimazoea halikunipa shida, baadaye akadai kuwa kuonana nami mara kwa mara namsababishia ashindwe kabisa kufanya vyema katika mambo yake ya chuoni.

Nikastaajabu sana, wakati nipo chuo ni kama tulikuwa tumeoana tu maana kwa juma moja tuliweza kuonana hata mara tano hadi sita na kulala pamoja. Sasa naenda mara tatu ama mbili kwa juma moja anadai namvuruga!!

Nikafunika kombe tena!!

“Mtoto wa watu asije kufeli akasema chanzo ni mimi” nikajisemea kisha nikapunguza safari zangu za kwenda chuoni kwao.

Hakika maisha ya kuishi mwenyewe nyumbani yalinipa upweke wa hali ya juu sana. Ni upweke ule ambao ulinifanya nizidi kuamini kuwa nampenda Latipha.

Siku zikazidi kwenda huku tukionana mara chache sana na mke wangu wa ndoa.

Niliamua kufanya atakalo yeye ilimradi tu asikwazike.

Sikujua kuwa kuna bomu nazidi kulitikisa kwa kumkubalia binti yule kila kitu.

Naam! Najua ni ile hali ya kumsikiliza ilimfanya apitilize na kunijaribu kwa kila kitu.

Siku moja nilivamia bila taarifa na kwenda chuoni kwao. Sikupanga lakini ni katika mihangaiko yangu nikajikuta jirani na chuo chao nikaona si mbaya ikiwa nitamsalimia mke wangu.

Nikaingia pale chuoni, nilifahamu darasa alilokuwa akisomea na pia kama hayupo hapo bila shaka nitamkuta nyumbani kwake, ambapo alikuwa akiishi yeye na rafiki yake.

Kweli, sikumkuta shuleni nikaamua kucheza pata potea na kujikongoja kuelekea nyumbani kwake.

Kwanza nikampigia simu Mariam binti ambaye alikuwa akiishi nma mke wangu, nikazungumza naye akanieleza kuwa yupo darasani wakati huo. Nikamuulizia Latipha, akanieleza kuwa alimuacha nyumbani lakini kwa uhakika zaidi nimpigie simu.

Nikamweleza kuwa nahitaji kum’surprise’ sitaki kumpigia simu.

Hapohapo simu ikakatwa, nikajiongeza kuwa huenda binti yule yupo katika dikasheni na wenzake hivyo anawakosesha wenzake utulivu.

Nikaondoka na kuendelea kujongea katika njia ya kuelekea nyumbani kwa Latipha, nilikuwa nimemnunulia zawadi kadhaa nilizokutana nazo barabarani.

Nilipokuwa nakaribia nyumbani kwake nilikutana na mwanaume ambaye alikuwa mwenye haraka sana, na hakunisalimia akanipita kwa kasi tu.

Sikumjali hata kidogo nilikuwa nikiwaza juu ya Latipha tu!!

Nikaikaribia nyumba aliyokuwa akiishi Latipha.

Ile naufikia mlango na yeye akatoka.

Akatabasamu kidogo kisha akanikumbatia.

“Mungu! Wangu…. Latipha alikuwa akinukia marashi mapya kabisa ambayo hayakuwa mageni hata kidogo katika pua zanguu”

“Marashi gani tena haya nimeyapenda sana…” nilimsanifu, akajichekesha kifedhuli kabla hajanijibu kuwa aliazima kwa rafiki yake ila si yak wake.

Sikutaka kuzungumza sana juu ya hayo marashi nikaingiza mada nyingine hasahasa za kumfanya atabasamu.

Naam! Akatabasamu lakini sio lile tabasamu kutoka moyoni nililokuwa nalitambua kutoka kwa Latipha. Kuna namna fulani za mashaka zilihesabika usoni mwake.

Mashaka ya nini sasa? Nilijiulliza….

Hapakuwa na mtu wa kunijibu!!

Nikamkabidhi zawadi zile nilizomnunulia na kuaga kuwa nilikuwa napita tu.

Latipha akanihoji kwa nini nilienda nyumbani kwake pasipo na taarifa!

Nilibaki kinywa wazi nikilishangaa swali lile. Inakuwaje mke wangu ananipangia namna ya kufika nyumbani kwake.

“Üsinielewe vibaya mume wangu, nimeuliza tu nahitaji kujua, ama ni vibaya kuuliza. Basi kama ni vibaya iam sorry..” alizidi kunishangaza mke wangu.

Na bila kunipa nafasi ya kuzungumza akazungumza tena.

“Ehee halafu kuna jambo nahitaji tuzungumze kidogo kama dakika tatu hivi..”

“Jambo gani..” nikamuuliza, badala ya kunijibu akanivuta mkono nikaketi chini.

Akanitazama kwa tuo usoni, kisha akainama na baada ya hapo akainuka tena.

“Ninahitaji kushiriki Miss chuo, hivyo nahitaji ruhusa yako babaa!!” alizungumza Latipha.

Moyo wangu ukapiga kwa nguvu sana, yaani jambo zito kiasi kile eti anasema tulizungumze kwa dakika tatu ama mbili.

Niliusikia mchirizi wa jasho ukitiririka katika mgongo wangu!!

Latipha alikuwa amenishtua sana!!!

“Mbona unakodoa macho Khalfani, jisikie fahari mkeo nimeonekana mrembo mbele ya macho ya watu…” alizungumza tena huku akijiamini.

“Latipha mke wangu una wazimu…..” nikamuuliza huku nikimtazama usoni.

“Nini? Nini Khalfani umeniambia nina nini, nakuuliza Khalfani umesema nina nini?” akauliza mara mbilimbili na hapo ikazuka tafrani!!

Sikutegemea kama yule kweli ni Latipha mke wangu!!!!

“Latipha mke wangu una wazimu…..” nikamuuliza huku nikimtazama usoni.

“Nini? Nini Khalfani umeniambia nina nini, nakuuliza Khalfani umesema nina nini?” akauliza mara mbilimbili na hapo ikazuka tafrani!!

Sikutegemea kama yule kweli ni Latipha mke wangu!!!!

Nilibaki kumtazama na vitisho vyake vilivyonistaajabisha sana. Huyu alikuwa ni Latipha katika sura ya nje lakini kwa ndani hakuwa Latipha yule mke wangu!!

Niliamini kuwa nikiendelea kukaa na kiumbe huyu basi kwa mara ya pili katika maisha yangu naweza kujikuta napiga mwanamke.

Sikutaka hili jambo litokee.

Nikalikumbuka lile onyo la mama yangu alilokuwa akinisihi tangu nikiwa mtoto mdogo.

“USIZUNGUMZE NENO LOLOTE UKIWA NA HASIRA!!”

Nikasimama bila kuaga nikiwa mnyonge kabisa huku nikipambana na hasira yangu.

Nilidhani Latipha atanifuata kwa nyuma na kuniomba msamaha huku akinisihi nisiondoke.

Nilisubiri hilo tukio na halikutokea badala yake niliusikia mlango ukibamizwa kwa nguvu nyuma yangu!!

Nikajikaza sikugeuka!!

Nilipopiga hatua takribani kumi na tano, mara nikajikuta naganda ghafla!! Kuna kitu kilikuwa kimenijia akilini mwangu, eneo nililokuwa nimesimama ni eneo ambalo nilipishana na yule mwanaume mwenye haraka sana ambaye hakunisalimia.

Ni eneo lile lile kwa mara ya kwanza niliweza kukutana na harufu ya marashi, marashi yaleyale ambayo mke wangu alikuwa ananukia siku ile.

Mungu wangu!! Inamaana yule bwana alitoka chumbani kwa Latipha, na ikiwa alitoka kule ndani basi iwe isiwe lazima alimkumbatia ndo maana akamuachia harufu ile kali.

Nilifumba macho nikauma meno yangu kisha nikaitazama mikono yangu jinsi ilivyoshindana katika kutokwa jasho!!

Wakati naitazama mikono nikangámua kitu kingine kipya.

Nilikuwa nina pete kidoleni lakini mke wangu hakuwa na pete!!

Sikuendelea mbele nikaamua kurejea kule chumbani na liwalo huko liwe hivyohivyo.

Nilikuwa tayari kwa heri ama kwa shari!! Latipha alikuwa amenifanyia namna fulani ya usaliti. Nilihitaji majibu, yule alikuwa ni mke wangu wa ndoa tena mke pekee bila msaidizi.

Nilirejea hadi mlangoni, nikagonga bila kuzungumza neno lolote.

Kimya!!

Nikajaribu kuugonga tena, safari hii kwa nguvu zaidi. Bado pakawa kimya!!

Anajifanya amelala eeh!! Ngoja!! Nikajisemea kisha nikazunguka upande wa dirishani, kitanda kilikuwa wazi hapakuwa na mtu juu yake. Nikajaribu kutazama kwa makini bado sikuona mtu.

Nikatega sikio huenda yu bafuni anaoga lakini sikusikia mchakato wowote ule.

Hapo sasa nikaingiwa na hofu.

Asijekuwa ameenda kujinyonga huyu mtoto ohoo!! Nikazungumza mwenyewe kwa sauti ya chini huku nikianza kuchachawa.

“Latipha mama yangu, usitafsiri vibaya mke wangu. Sijaondoka kwa mabaya haya njoo basi mke wangu.. njoo tujadili sasa mikakati juu ya hili jambo njoo mpenzi wangu..” nilijikuta nikiongea mambo ambayo kwa lugha nyepesi tunasema ni kuropoka.

Mikakati! Mikakati gani ikiwa hata mambo hayo ya umiss sijui lolote lile. Na nilivyokuwa nayachukia hayo mambo basi ilichangia zaidi kutoyatilia maanani!!!

Leo hii mke wangu anataka kushiriki namuita tufanye mikakati!!

Khalfani nilikuwa nimechanganyikiwa!!

Licha ya hayo yote bado sikumsikia binti yule akijibu jambo lolote.

Nikaona isiwe tabu nikaamua kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani ikiwa watakuwepo waje kunisaidia.

Hapakuwa na mtu yeyote!!

Nikahangaika huku na kule!!!

Nilipogeuka nikakutana na mke wangu akiwa ameufungua mlango na kusimama mbele yake huku akiwa ameshika kiuno chake.

“Ni kitu gani kimekurejesha we mwanaume usiyependa maendeleo ya mke wako, usiyefurahia kuona mkeo anapata mafanikio. Ondoka uniache, yaani wakati mwingine hadi najuta mimi…..” alilalamika kwa sauti ya juu. Nikaona kuwa si vyema kuendelea kuzungumza tukiwa katika hali ile, nikamsihi mke wangu tuketi ndani na kuyazungumza mambo yale.

Kweli akaachia upenyo nikapita na kuketi katika kiti kimoja cha plastiki kilichokuwa pale ndani.

Yeye akarejea na kuichukua simu yake kisha akatoka nje bila kuaga. Nikatambua kuwa anarejea ndani ya muda mfupi ujao.

Haikuwa dakika moja wala dakika mbili. Ni hadi pale nilipokuja kuupokea ujumbe wake saa moja baadaye.

“Ukimaliza kilichokuleta utaufunga huo mlango kisha funguo utauweka hapo chini upande wa kushoto!!!

Nilihamanika ndugu msikilizaji baada ya kuipata meseji ile kutoka kwa mke wangu.

Nilijaribu kumpigia simu hakuwa akipatikana.

Nikaituliza akili yangu kwa kiasi fulani, nikatambua kuwa kuna jambo kubwa linaendelea katika maisha ya mke wangu na hataki kuniweka wazi.

Ni jambo gani sasa?

Nilijiuliza huku nikiwa nimeshika simu yangu nikitafakari ni nani wa kumshirikisha katika jambo hili. Nilibofya namba ya mama yake Latipha kisha upesi nikaachana nayo. Lile halikuwa tatizo la kufikisha ukweni, nikabofya namba ya Hamis rafiki yangu. Hii nayo nikaachana nayo angenishauri nini wakati hata alikuwa hajaoa.

Nikaifikia namba ya mama Khalfan!!

Naam huyu ndiye mtu pekee ambaye sikuwa na kipingamizi linapokuja suala la kumpelekea matatizo yangu. Liwe kubwa ama dogo mi nililipeleka tu, na kitu ambacho sikutaka kujali ni umri!!

Eti umri wangu umesogea sana basi niogope kuomba ushauri!!

Huyu sikumpigia simu badala yake nilienda nyumbani moja kwa moja.

Nikamvuta kando tukaketi katika mkeka na kumweleza juu ya lile jambo ambalo lilikuwa limetokea katika maisha yangu ya ndoa changa. Lakini suala la Latipha kutaka kugombea umiss sikuligusia kabisa.

Mama alitikisa kichwa chake ishara ya masikitiko nami nikamuunga mkono nikiamini kuwa anamsikitikia Latipha na hiyo tabia yake mpya!!

“Khalfani mwanangu, mwanamke anapenda sana kubembelezwa. Yaani wewe hata siku mbili hazijapita unakimbilia kwa wazazi kuomba ushauri. Nenda kazungumze na mkeo hayo ni mambo madogo sana mwanangu….” Mama alinijibu katika namna ya kushushua. Nikabaki kinywa wazi nisiamini kuwa mama naye hakuwa upande wangu siku hiyo!!

Nilipomaliza soda aliyokuwa ameninunulia niliaga na kuondoka huku nikiamini fika kuwa nitamkuta Latipha nyumbani kwani ilikuwa ni kawaida siku ya ijumaa hadi jumapili jioni Latipha kuja nyumbani kunisaidia kufua na kupika!!

Ikawa tofauti tena, sikumkuta Latipha nyumbani!!

Nikajaribu kupiga simu yake, bado ilikuwa haipatikani.

Nikakata shauri kuwa siwezi kuendelea kujiumiza kichwa kwa mtu ambaye anazo akili zake timamu na anajijua kuwa ni mke wa mtu kihalali!!

Nikatulia nikijisahaulisha juu ya Latipha lakini ikaja picha nyingine kichwani, Latipha kugombea umiss.

Nikajikuta natabasamu nilipoitazama picha ya Latipha pale ukutani.

Hakuwa mrefu na hakuwa mwembamba. Alikuwa mnene mfupi.

Sasa urembo gani na umbo hili jamani!!! Au ndó ananitania kweli kama mama anavyosema.

Sijui ni kitu gani kilinituma kupekua begi la Latipha ambalo huwa anawekea vifaa vyake vya shuleni.

Nikiwa katika upekuzi usiokuwa na mantiki nikakutana na picha katika daftari lake.

Picha ya mwanaume!!!

Mwanaume huyu alikuwa anatabasamu.

Sura ngeni kabisa machoni pangu, nikaipuuzia na kujisemea kuwa iwapo angekuwa pale jirani mke wangu ningemuuliza yule mwanaume ni nani??

Lazima angenijibu!!!

Majira ya saa tano usiku nikiwa nimepitiwa na usingizi pale kwenye kochi. Mara nikashtushwa na mikono ikitembea katika shavu langu!!

Nikafumbua macho upesi.l nikakutana na sura ya mke wangu ikiwa katika tabasamu la kujilazimisha na alionekana yu mchovu sana.

Lakini mbaya zaidi alikuwa amevimba jicho lake la kulia!!

Alinikumbatia kwa nguvu sana bila kusema neno lolote.

Kisha akazungumza huku akitokwa na kilio cha kwikwi.

“Sitashiriki tena mashindano ya urembo mume wangu kipenzi tafadhali naomba unisamehe sana kwa lolote baya nililokufanyia siku hii ya leo….” Alilia sana Latipha hadi nikajisikia vibaya na kuanza kumbembeleza huku nikizuga kuwa mimi nilimsamehe zamani sana hata kabla hajaomba msamaha.

Kilio cha mke wangu na mwonekano wake vikaniweka katika jitimai ya nafsi!!!

JIFUNZE: Katika maisha yoyote yale, mwanadamu lazima ajigawanye nakuishi maisha ya aina tatu. Maisha ya kujichanganya na watu, maisha binafsi na maisha ya siri.

Epuke kuyafanya maisha yako ya siri kujulikana kwa kila mtu!!!

Usiku ule ulikuwa mrefu sana, nilijiuliza maswali nisipate wa kunipa jibu. Nikajaribu kuulazimisha usingizi lakini ukagoma katukatu!!

Nikajaribu kumkumbatia mke wangu lakini badala ya kulipata lile joto nikahisi yu wa baridi sana.

Na baada ya muda akaanza kukoroma!!

Hii ilikuwa mara ya kwanza kabisa kumsikia mke wangu akikoroma!!

Nini kimemsibu mtoto wa watu!!

Ni wapi alikuwa hadi amevimba namna hii!!

Niliendelea kujiuliza kisha nikaizima taa na kujaribu tena kulala. Ndugu msikilizaji ilikuwa ngumu sana kulala na mtoto wa watu akiwa katika hali ile. Nikaona isiwe tabu kwanza yule ni mke wangu ninammiliki kwa asilimia zote.

Nikaamua kumuamsha, nikamtikisa hadi nikafanikiwa kumuamsha. Alikuwa kama aliyekunywa pombe nyingi na zimekizidi uzito kichwa chake.

“Latipha mke wangu umekuwaje…” nilimuhoji.

Badala ya kujibu akaniangukia mapajani na kuendelea kuuchapa usingizi.

Sikuwa na namna zaidi ya kumuacha aendelee kulala, zaidi nilimuweka vyema kisha nikamfunika shuka.

Mimi nilishindwa kulala kabisa, nikanyanyuka na kwenda kuketi sebuleni.

Nikawasha luninga lakini sikutilia maanani katika kuiangalia. Nikawa najiuliza iwapo il ndoa ilikuwa yaelekea kunishinda, ama umri wangu wa miaka 24 haukuwa sahihi kuingia katika ndoa??

Eti mama ananiambia haya ni mapenzi tu nimbembeleze…

Amakweli mama Khalfani anazeeka vibaya!!

Nilijisemea huku nikijilazimisha kutabasamu.

Na hapo nikakumbuka tena juu ya ile picha ya mwanaume nisiyemjua ambayo niliikuta katika madaftari ya mke wangu!

Ni nani mtu yule!! Nilitamani kumuamsha tena Latipha ili nimuulize lakini nilijua ni yaleyale ya kutwanga maji kwenye kinu!!

Nikamuacha aendelee kulala.

Bila kujua usingizi ulinipitia nikiwa palepale kwenye kochi.

(Achia nafasi ya biti)

Nikiwa palepale kwenye kochi mara alikuja msichana nisiyemfahamu alikuwa ameongozana na Latipha mke wangu, nilijaribu kumpa tabasamu Latipha lakini hakunipa tabasamu kama malipo badala yake aliniangalia kwa jicho lililoonyesha mashaka, na sekunde iliyofuata yule dada aliyeongozana na Latipha alitoa kisu kikali sana na kisha akaanza kunisogelea huku Latipha akimsisitiza afanye upesi. Nilianza kutetemeka huku nikimuuliza Latipha ni kosa gani nilikuwa nimefanya hadi anamsisitiza yule dada anichome kisu.

Hatimaye yule dada alinifikia anauleta kwa kasi mkono wake ili anichome kose… nikajikuta natokwa nay owe kali huku nikijaribu kumsukuma mbali.”

“Khalfani mume wangu ni nini kinatokea eeh kitu gani kinatokea….” Niliisikia sauti ya Latipha mke wangu. Nikayapikicha macho yangu, palikuwa ni asubuhi tayari.

Na ile ndoto mbaya ndiyo iliyokuwa imeniamsha!!

Nilibaki kutweta bila kujibu lolote. Latipha akanisogelea akanivutia upande wake kisha akanikumbatia na kuanza kulia huku akinisisitiza kuwa ananipenda sana!!

Ni kama sikuyasikia maneno ya mke wangu, nilikuwa nawaza juu ya ile ndoto, mwanamke mwenye kisu anasisitizwa na mke wangu eti aniue upesi!!

“Kwani yule uliyekuja naye alikuwa ni nani?” nilijikuta nauliza swali ambalo Latipha hakulielewa nami nikakumbuka kuwa namuuliza Laty vitu ambavyo niliviona katika njozi.

Baada ya kuniandalia maji ya kuoga kisha stafutahi. Latipha alijiandaa na kuniaga kuwa anaenda chuoni na akirejea tutapata muda mzuri wa kuzungumza!!

Nikamgomea ombi lake!!

Nikamwambia ni lazima tuzungumze kwanza.

“Khalfani hivi uliponitolea mahari ulimaanisha kuninunua ama? Kwanini wanaume mnakuwa hivyo.. yaani hadi wewe Khalfani unakuwa kati yao. Nawe hautofautiani nao Khalfani…” Latipha hakuweza kuendelea kuzungumza, chozi likaanza kumchuruzika.

Maneno ya Latipha na ile sauti yake ya kike yakanifadhaisha!! Yalikuwa na ukweli ndani yake, nikajisikia aibu. Lakini sikutaka kujishusha, nikageuka kulelekea chumbani kisha nikazungumza kwa sauti ya kukoroma ‘haya tutaongea baadaye’.

Nikaingia chumbani Latipha akatoweka!!

Kwa mara nyingine tena nikajiuliza juu ya kuzidiwa na ndoa ilea ma ni utoto unanisumbua!!

Baada ya Latipha kuondoka pepo la wivu likaniongoza kuzidi kupekua makorokoro yake. Nikagusa huku na kule kwa pupa lakini sikuambulia kitu chochote kile kilicholeta mashaka.

Hali hii ikasababisha hata niipuuzie ile picha ya mtu nisiyemjua niliyoikuta pale ndani.

Mwisho nikampangia vitu vyake lakini nikiwa nimekamata kijarida kidogo ambacho nilipanga kukisoma kama namna ya kupoteza muda pale ndani.

Naam! Nikajilaza kitandani na kuanza kuchambua kurasa mojamoja. Sikuwa nikisoma kwa kumaanisha sana lakini walau nilifanikiwa kupoteza muda. Nilihitaji ufike ule muda wa kwenda msikitini kwa ajili ya swala ya magharibi.

Ukurasa wa katikati ulikuwa umeambatanishwa picha za rangi, nikajaribu kusoma kilichoandikwa. Hakikuwa na maana kwangu, habari za michezo na burudani?

Sikuwa mpenzi wa mpira wa miguu wala hizo burudani!!

Wakati nataka kufunua ukurasa unaofuata, niliiona picha. Mwanaume akiwa amezungukwa na wasichana.

Picha ile ikanifanya nisiendelee kujilaza bali kukaa kitako na kuitazama vyema. Niliwahi kuiona mahali sura ile.

Nikajiuliza sana ni wapi nilipoiona sura ile hapo kabla!!!

Yees!! Ni yule mwanaume nilipishana naye akiwa na haraka sana kisha akawa ananukia marashi ambayo nilimkuta mke wangu naye akiwa ananukia!

Nikaamua kukituliza kichwa changu, nikasoma maelezo pale chini ya picha.

“MRATIBU WA MASHINDANO YA MISS TANZANIA LEODGARD KILEO”

Nikasimama na kukizunguka chumba changu bila kukimaliza, nilishika hiki nikaachia nikashika kile na kuachia. Nilikuwa nimepagawa!!

ITAENDELEA

Fedheha Sehemu ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment