Fedheha Sehemu ya Pili
MAISHA

Ep 02: Fedheha

SIMULIZI Fedheha
Fedheha Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA

*********************************************************************************

Simulizi: Fedheha

Sehemu ya Pili (2)

Huyu bwana anaratibu mashindano ya urembo kisha….kisha… yaani amemratibu hadi mke wangu!!

Niliikunja ngumi yangu kwa nguvu sana nikijaribu kuidhibiti hasira yangu!!

Ilikuwa ngumu sana kudhibitika!!

Sikuwa nahitaji ushahidi wowote ule kuhakikisha kuwa mke wangu alikuwa na mahusiano na mwanaume mwingine wakati yu katika ndoa!!

Nikaivaa suruali yangu kisha nikatoka nje ili nikaukate mzizi wa fitina kwa namna yoyote ile!!

Ni aidha talaka ama vyovyote ilimradi tu tugawane maumivu!!

Nikatoka hadi nje, mara jirani yangu ambaye ni mwanamke akanikumbusha kuwa nilikuwa nimegeuza suruali yangu!!

Hakika nilikuwa nimechanganyikiwa!!

Nikarudi ndani!! Nikaivaa vyema suruali yangu!

Kabla sijatoka nikapigiwa simu!!

Ilikuwa ni namba mpya kabisa ambayo sikuwahi kuiona kabla nikaipokea huku nikiwa vilevile na ghadhabu!!

“Nazungumza na bwana Khalfani hapo” sauti ikaniuliza.

“Kwani we umempigia nani bwana?’” nikauliza kisharishari.

“Kama ni bwana Khalfani basi mkeo yupo kituo cha hospitali hapa Magomeni tafadhali fika upesi sana!!! Upesi Khalfani.” Ilitoa maelekezo sauti ile kisha simu ikakatwa.

Nilijaribu kupiga lakini haikupokelewa tena.

Nikazidi kuchanganyikiwa ni kitu gani kilikuwa kimemtokea mke wangu. Nilitoka mbiombio na kupanda taksi.

Nikamuamuru dereva aniwahishe sana hospitali. Sikuwa najua ni wodi gani na ni kitu gani kimemtokea mke wangu.

Kama ambavyo haikuonekana kuwa imetosha kunipagawisha mara nikapokea simu kutoka kwa mama yake Latipha.

“Khalfani si nilikwambia tangu zamani kuwa Latipha wangu sijawahi kumpiga tangu alipobalehe, ni kitu gani kimekutuma kumpiga mwananngu na kutaka kumuua.. Khalfani nasema hivi, mwanangu akipona naomba umpe talaka mara moja, hakuua nyumbani tunampenda sana yaani sana, lakini ole wako apate kilema chochote ndo utajua kwanini hakuna mabasi mengi yanayofanya safari za kwenda Sumbawanga. Utapajua vizuri nasema…..” alimaliza mama yule kisha akakata simu!!!

Na yeye nilipompigia hakupokea simu yangu!!!

Mimi Khalfani nimempiga latipha!!! Mbona hili ni balaa ambalo limeibuka kama filamu tena filamu isiyokuwa na mvuto.

Inakuwaje msichana ajiondokee kwenda chuo na ghafla naambiwa yupo hospitali na mara mama ananiambia nimempiga sana mwanaye.

Nikamwamuru dereva teksi asimamishe!

Lakini nikagundua kuwa hata akisimama sitakuwa na cha kufanya!!

Nikamwambia tena aendelee na safari!!!

Kupitia kwenye kioo nikamuona alivyoikunja sura yake!!!

NILIBAKI kama zezeta nisijue ni uamuzi gani sahihi ninaoweza kuufanya ili kuweka sawa jambo lile ambalo lilikuwa si jambo tena bali tatizo.

Kichwa changu kilikuwa aidha wazi ama kilikuwa kimejaa sana. Sikuweza kupata jambo jipya la kufanya.

Nilipofika hospitali ya Magomeni nilishuka nikamlipa Yule dereva haki yake na kisha nikajaribu kuipiga ile namba.

Nikiwa palepale simu ikiwa inaita tu bila kupokelewa mara nikaona kundi la vijana wapatao wanne likisogea upande ambao nilikuwa nimesimama.

Sikuwatilia maanani, zaidi niliwaza juu ya mke wangu. Ni kitu gani kilikuwa kimemtokea!!!

Na nilitaka kujua yupo wodi gani ili nikajue ni kipi kimemtokea mke wangu!!

Lile kundi lilinifikia mara nikawasikia wakiambizana.

“Ndiye huyu, ni huyu huyu!!” nikaitoa simu yangu sikioni na kuwatazama vyeama katika namna ya kuwaeleza kuwa walikuwa wamenifananisha!

Haikuwa rahisi kama nilivyodhani!!

Ghafla mmoja akanirukia na kunikaba koo, kisha akaanza kuniuliza eti nimetoa wapi ruhusa ya kumpiga dada yao. Sikuweza kutoa jibu kwa sababu ile kabali ilikuwa imeniingia haswa.

Mmoja kati yao akamwambia anilegezee ili nijibu!!

“Dada yenu gani jamani… sijapiga mtu mimi nilijaribu kujitetea”…..

Palepale Yule bwana akanikaba tena, mchana kweupe nilikuwa naumbuka mimi Khalfani. Nakabwa na watu nisiowajua na wananituhumu eti kwa nini nampiga dada yao!!

Ghafla akaniachia, wakati napambana kupata hewa nikashtukia natandikwa kichwa kikali katika mwamba wa pua yangu.

Ikafuata damu kunitoka puani huku kipigo kikali kutoka kwa wanaume nisiowajua kikifuatia nyuma yangu!!

Dah! Dar es salaam, ewe ambaye una mpango wa kuja huku kaa ukijua huku hakuna utu!! Nilipigwa huku raia wema wakiendelea na shughuli zao. Hawakujali kabisa.

Baada ya kunipiga watakavyo eti kisa nampiga dada yao waliondoka na kuniacha pale!!

Ajabu sasa!! Hawakuchukua simu wala pesa yangu.

Waliniachia kila kitu!!

Ni hapo ndipo wasamaria wema waliponifikia na kuniuliza ni kitu gani kimetokea.

Sikumjibu hata mmoja kati yao, maana maswali yao niliyaona kama dhihaka tu!!

Waliniona nimekabwa kisha nikapigwa vibaya sana, halafu wananiuliza kitu gani kimetokea.

Nilijiondokea bila kuzungumza na mtu yeyote, huku nyuma nikawasikia baadhi yao wakicheka.

Nilijisikia vibaya sana na mbaya zaidi sikuwa na uelekeo maalumu!!

Ni kitu gani hiki kinatokea katika maisha yangu!!

Nilijiuliza huku nikizidi kutembea bila kuwa na uelekeo maalumu.

Baadaye nikasimama na kujiuliza kuwa nilikuwa mpuuzi sana kutembea pasipo kuwa na uelekeo maalumu.

Nikamkumbuka mama yangu!!

“Ya nini sasa kuzurura huku na kule wakati mama Khalfani yupo?” nilijiuliza kisha nikasonya!!

Nikageuka na kuangaza huku na kule kisha nikaita taksi, nikaingia na kumwamrisha anipeleke nilipokuwa nahitaji!!

Nikamlipa kabisa pesa yake, na sikuzungumza kitu kingine hadi aliponifikisha nilipokuwa nahitaji!! Alikuwa akiniangalia kimashaka sana nd’o maana nikaona nimlipe kabisa pesa yake.

Na nilipoketi na kujikuta nikikitazama kile kioo cha mbele ndipo nilipogundua kuwa nilikuwa nimevimba jicho langu, na pua yangu ilikuwa imelowana damu.

Kujiona katika hali ile nikayahisi macho yangu yakichonyota. Na kimoyomoyo nikaanza kulalamika.

“Yaani wamenipiga bila sababu, yaani mimi sijawahi hata kumpiga mke wangu…” sikuweza kuendelea kuzungumza katika moyo wangu.

Nilijisikia uchungu sana, na hapo nikayasikia machozi yakichuruzika kutoka katika macho yangu!!

Nikatamani kufika kwa mama yangu tu! Ni huyo pekee ambaye angeweza kunifuta machozi yangu hakuna mwingine, ni huyo tu ambaye angetega sikio lake na kunisikiliza nitakaposema yangu ya moyoni.

Ni mama Khalfani pekee ambaye angeweza kuniamini katika hili!!

Naam! Hatimaye nikashuka garini na kutembea upesi upesi huku nikiwa naangaza mama yangu iwapo yupo katika kibanda chake ambacho alikuwa akiuza mbogamboga ambazo alikuwa akizilima katika bustani yake ndogo nyumbani.

Nilimuona mama kwa mbali, ni kama hisia zilivutana mama akageuka tukagonganisha macho.

Naam! Ule uchungu ukazidi nikajikuta nalia kwa sauti.

Ama kwa hakika mtoto hakui kwa mama!!!

Nililia sana, hadi mama anafika uso wangu ulikuwa umelowana haswa!!

Mama Khalfani akanikimbilia akiacha kila kitu alichokuwa anafanya!!

Akafika na kunikumbatia!!

“Mama wamenipiga bila makosa.. eti…eti nimepiga dada yao…” niliongea huku ninali, kwikwi ilinipa kipingamizi cha kuzungumza vizuri.

Mama hakusema neon lolote badala yake alinishika mkono na kuniongoza mpaka ndani.

Ni huko ambapo lilizuka jambo jipya kabisa!!

“Khalfani, mama Latipha alikuwa hapa. Amekufungulia jalada eti umempiga mwanaye. Khalfani mwanangu ni lini umeanza hii tabia….ni lini Khalfani. Na hao waliokupiga watakuwa ni kaka zake tu si wengine!!” mama alinieleza.

Nikapinga vikali kuwa sijafanya kitu kama kile.

“Khalfani, nilikwambia uende kumbembeleza mkeo na si kumpiga Khalfani…eeh!! Ukaenda kupeleka mahasira yako huko ona sasa…” mama aliendelea kunilaumu.

Nilijisikia fadhaa sana!

Mambo aliyokuwa akiongea mama ni uongo mtupu, sikuwa nimefanya lolote kwa mke wangu alikuja amevimba na hakuniambia nini tatizo!!

Sasa naambiwa eti mimi nimempiga!!

“Mama.. mama nisikie..” nilimkatisha mama.

“He! Khalfani ni lini umeanza kuniingilia nikiwa nazungumza, yaani umkoromee mkeo huko na mimi unataka kuniletea ubabe. Haya nipige na mimi, nipige Khalfani si umekuwa bondia nipige nasema” mama alinisimamia mbele yangu huku akiiweka kanga yake vizuri.

“Aha! Hautaki kunipiga sasa ngoja…” akaweka senti kadhaa alizokuwa amezishikilia mkononi, na mara akaninasa kofi kali usoni.

Yale maumivu yakaibuka upya.

“Ni kipi kimekufanya umpige mtoto wa watu??? Eeh!” aliniuliza.

Sasa nilikuwa nimepagawa haswa!

Mama Khalfani naye ananipa tuhuma nisizozijua!!

Akiwa anasubiri nimjibu na mimi nikiwa sina jibu, mara tulipata wageni pale ndani ghafla!!

Hawakusalimia badala yake walitamka maneno ambayo si mimi wala mama waliotegemea.

“Upo chini ya ulinzi Khalfani Masoud!!” walitamka kisha wakatoa vitambulisho vyao. Na bila kupoteza muda wakanitia pingu!!

Yule mama aliyekuwa ananipiga na kunikaripia sasa alianza kulia huku akijaribu kuwadhibiti wale askari wasiondoke na mimi!!

Mara askari mmoja akamsukuma mama akaanguka sakafuni!!

Sikuweza kuvumilia kufikia hapo!!

Nikamvamia Yule askari na kumtandika ngumi huku nikiwa nimefungwa pingu!!

Lakini kilichofuata baada ya hapo ni kipigo kikali kisha wakaondoka na mimi.

Sikuamini kilichokuwa kinaendelea katika maisha yangu!!

Lakini haikuwa ndoto ile ulikuwa ukweli mtupu!!

Nilipopatwa na fahamu nilikumbana na hali ambayo siwezi kuielezea kwa maelezo mengi, naweza kusema kwa maneno machache tu ilikuwa ni FEDHEHA!!

Nilikuja kupata fahamu zangu tena na kujikuta nikiwa gizani, nilipojaribu kuinuka nikajikuta namkanyaga mtu. Nikapokea tusi kali la nguoni huku nikisukumwa mbali.

Bado akili yangu ilikuwa haijakaa sawa. Nikataka kuuliza nikashangaa kinywa changu hakifunguki na hapo nikatambua kuwa mdomo wangu ulikuwa unauma sana.

Nikajaribu kujilamba na hapo nikakumbuka juu ya kile kipigo!!

Kumbe nilipigwa hadi kupoteza fahamu!!

Nikakumbuka kuwa nilikamatwa ghafla nikiwa nyumbani, sikumbuki kama hata walinitajia kosa langu!!

Nilijiweka kitako huku nikiwa nimetambua wazi kuwa kwa mara ya kwanza nilikuwa nimeingizwa mahabusu, na wale waliokuwa wamelala pale walikuwa ni mahabusu wenzangu!!

Nilijiuliza maswali mengi sana lakini sikupata jibu juu ya haya mauzauza, yaani nimehisi kuwa mke wangu ananisaliti, nikaamua kumsamehe ghafla Napata balaa kama hili. Eti nimempiga na kumjeruhi sana!!

Nikiwa nimekaa palepale nilijihisi kuonewa kwa hili ambalo nilikuwa napitia. Na mara machozi yakaanza kunitoka na mara kilio cha kwikwi!!

Hilo likawa kosa kubwa sana!!

Mahabusu mmoja akainuka na kunihoji ni kwa nini ninapiga kelele. Sikuwa natambua kuwa maeneo kama yale kuna watemi pia! Nikajifanya mjuaji tena ninayeonewa kuwa eneo lile!!

Nikamwambia kuwa aniache kama nilivyo!!

Ghafla akanikamata shingo yangu na kunigandamiza ukutani, sikuweza kuiona sura yake. Giza lilikuwa kali sana!!

“Umewahi kufa dogo?” aliniuliza huku akizidi kunikaba na kunigandamiza ukutani!!

Alikuwa na nguvu yule bwana na hakuonekana kuwa na masihara hata kwa mbali!! Sikuweza kujibu kwa sababu alikuwa amenikaba kwa nguvu sana!!

Baadaye aliniachia ghafla!!

Nikapumua kwa kasi huku nikikohoa!!

“Naitwa Geza Ulole yaani Iga uone!!” alijitambulisha kisha kama vile hakuna baya alilokuwa amenifanyia akajinyoosha tena ili aweze kulala.

“Ole wako utupigie kelele tena, nitakufundisha jinsi ya kulala bila kuamka.” Alimaliza na hakuzungumza tena.

Nilijinyoosha nami na kujaribu kuutafuta usingizi pale sakafuni. Nilihisi sitaweza kusinzia lakini hatimaye nilisinzia!!

Haikuwa asubuhi njema kama nilivyoweza kudhania. Niliamini kuna neno ambalo nitaambiwa ili niweze kujitetea lakini sikuambiwa jambo lolote, mahabusu wenzangu walitoka na kurejea huku wengine wakienda moja kwa moja.

Mimi sikuitwa na askari wala ndugu yeyote.

“Ina maana hata mama hajui kama nipo kituo cha polisi ama?” nilijiuliza baada ya kuona giza likiingia kwa mara ya pili.

Sikuwa nimetia kitu chochote mdomoni tangu asubuhi. Na sasa nilikuwa nikiisikia njaa waziwazi ikilishambulia tumbo langu.

Ningekula nini ikiwa ugali ulioletwa kwa ajili ya mahabusu ulichukuliwa na watemi na kuushambulia wajuavyo.

Hali ilikuwa mbaya sana na nilijiona nipo katika hatua za mwisho kabisa za kuendelea kuumiliki uhai niliokuwanao.

Nikiwa bado nimejikunyata nisijue ni kitu gani kilikuwa kinaendelea mara alikuja bwana mmoja mwembamba aliyekuwa amevaa kipensi kifupi sana. Hakuwa na shati wala fulani yoyote. Na alikuwa mwenye furaha sana kana kwamba alikuwa anapendezwa zaidi kuwa katika chumba kile kuliko kuwa nje.

“Dogo mbona mawazo sana” aliniuliza, na hapo nikatambua kuwa ile sauti ni ya Geza ulole yule bwana aliyenikaba koo usiku.

Kitendo cha kutambua kuwa yule ndiye adui yangu wa usiku ule kilinifanya nikaingiwa na uoga zaidi.

“Hapana kawaida tu wala siwazi kaka…” nilimjibu huku nikilazimisha kutabasamu.

“Dogo sikia humu sisi sote waarifu, iwe umefanya kweli ama umesingiziwa sasa hizo pigo unazoleta za kujifanya we ndo ustaadhi umeonewa sana tambua kuwa hapa sio msikitini sasa. Hapa ni Guantanamo… unapajua gwantanamo wewe?? Hapa nd’o nusu ya jela sasa. Usijiweke kinyongenyonge unatufanya na sisi tuanze kuwaza upya misala yetu… umesikia?” aliniuliza kwa shari kubwa.

Nikatikisa kichwa kukubaliana naye!!

“Haya sasa nini kimekuleta humu?” akaniuliza kiutulivu.,

“Nimesingiziwa……” kabla sijaendelea akanikatisha.

“Hayo majibu ya nimesingiziwa utawajibu wapelelezi huko sio mimi sawa!! Haya nini kimekuleta hapa?”

“Nimepiga mke wangu vibaya sana!!” nilijibu kwa ghadhabu kiasi fulani.

“Hah! Mbona we mwenyewe mnyonge sasa umeanzaje kumpiga mkeo?” akaniuliza.

“Ndo maana nikakwambia kuwa nimesingiziwa!!”

“Halafu kama niliwahi kukuona sehemu wewe… we unakaa sehemu gani hapa Mwanza?” aliniuliza.

Nikabaki kushangaa, Mwanza? Mwanza kivipi tena.

“Mi siishi Mwanza….” Nilijibu.

Akazidi kuniuliza ni wapi nilikuwa naishi ikiwa siishi Mwanza. Nikamweleza kuwa mimi naishi Dar es salaam!

“Hah! Dogo mbona unanichanganya sasa… mkeo umempiga ukiwa naye hapa Mwanza au?”

“Mwanza… Mwanza kivipi.. kwani hapa ni Mwanza..” nilimuuliza huku nikijaribu kuchungulia nje. Nilikuwa nimepagawa na sikuelewa kabisa ni kitu gani kilichokuwa kinatokea.

Eti nilikuwa Mwanza punde baada ya kukamatwa jijini Dar es salaam!!

Niliishiwa nguvu msikilizaji!!

Ni kwanini haya yalikuwa yanatokea kwangu!! Kuna jambo gani baya nilikuwa nimefanya. Ama kosa ni kumuoa Latipha!!

Niliendelea kuwa humo huku ukaribu wangu na Geza Ulole ukiwa umenisaidia sana kuwa Napata chakula na kupata nafasi ya kuoga!!!

Niliendelea kusubiri pale hadi zikapita siku nne ndipo nilipofanikiwa kuitwa kwa mara ya kwanza. Nilichofika na kuulizwa kilikuwa kitu cha ajabu sana, nikaulizwa ni kwanini naendesha gari huku nikiwa nimelewa.

Ndugu! Laiti kama ingekuwa ni maigizo ningechekeshwa na kile kipande kwa sababu anayeambiwa ameendesha gari huku akiwa amelewa hata gari hana sembuse kujua tu kuliendesha!!

Nilibaki kinywa wazi nikingoja maamuzi yao!! Kwa sababu mambo waliyokuwa wakiniambia sikuwa nikiyatambua kabisa!!

Wakaniuliza juu ya ndugu zangu walipo, nikasema kuwa mama yangu yupo Dar es salaam!

Hawakutka ndugu wa mbali wakahitaji ndugu wa palepale jijini Mwanza. Sikuwa na ndugu kabisa.

Wakazungumza maswali mengi kisha wakanikabidhi eti vitu ambavyo niliacha mapokezi kabla ya kuingizwa mahabusu.

Ilikuwa ni pochi na ndani yake zilikuwa ni pesa kadhaa!!

Hii filamu sikuielewa!!

Nikaachiwa huru kabisa jijini Mwanza.

Wanasema kuwa yawezekana hujui kusoma yaani hata picha pia huielewi!!

Nikajiongeza kuwa ile niliyorudishiwa ilikuwa ni nauli ya kurejea jijini Dar lakini sikuwa mwenyeji kabisa katika mji ule.

Lakini bado ilikuwa ni bora kutangatanga humo lakini si kuishi mahabusu!!!

Nilitembea hadi nikapata kibanda cha simu, namba za kwanza kabisaa katikla akili zangu zilikuwa zile za mama yangu!!

Niliomba sana namba ile iwe inapatikana.

Naam! Ilikuwa hivyo!!

Alipopokea nikajitambulisha, wala mama hakushtuka!!

Hii hali ilinifadhaisha sana.

“Kwa hiyo umeona heri aolewe sivyo?” aliniuliza.

“Mama sielewi unachonileza. Ni nini kinatokea….”

“KESHO HARUSI YA LATIPHA!!” Mama alinijibu na kisha akakata simu!!

Nilipagawa!!!

Nilishatambua wazi kuwa kuna hila ilikuwa imefanyika na inaendelea kufanyika dhidi yangu!!

No! sio dhidi yangu, ni dhidi ya ndoa yangu!! Mimi na Latipha wangu

Ni nani anayeleta hila hizo…..

Hili lilikuwa swali gumu ambalo kulitatua ulikuwa mtihani mgumu.

Sikuwa mpepelezi Khalfani mimi wala sikuwa mwandishi wa habari sasa ningeanza vipi kuingámua hila hiyo. Nilikuwa na kishahada changu tu cha uhasibu, sasa uhasibu na upelelezi wapi na wapi.

Usiku huo nililala nyumba ya kulala wageni. Japokuwa nilikuwa bado ninayo maumivu makali kutokana na kulala chini lakini bado sikuweza kusinzia upesi kwa kulalia lile godoro pale ndani.

Nilimkumbuka mke wangu, nilitamani kuonana naye tuongee na kuyajenga haya yanayotaka kutuporomosha lakini nilifadhaika sana kwa kugundua kuwa nilikuwa nimechelewa sana na sasa alikuwa anaolewa.

Ila? Anaolewa katika misingi gani jamani? Hatujapeana talaka wala kupigana!! Hapana Latipha ni wangu na si wa mtu mwingine.

Nilisinzia nikiwa nimesimamia msimamo huo!!

Asubuhi ilinikuta stendi, nikaingia mapema kabisa katika basi ambalo nilikuwa nimelipia.

Nikaichukua siti yangu ya dirishani!!

Majira ya saa kumi na mbili safari ya kuelekea Dar es salaam ikaanza.

Kuna muda nilidhani dereva anaendesha gari taratibu sana kwani nilikuwa ninahitaji kuwahi kabla hiyo ndoa haijafungwa niweze kuingilia kati na kuharibu mipango.

Na kuna muda niliona kuwa yule dereva anakimbiza sana gari sikuhitaji kuwahi maana kuwahi kwangu kufika ningeenda kuishuhudia fedheha kubwa kupita zote katika maisha yangu!!

Kushuhudia mke wangu akiolewa na mwanaume mwingine tena bila kutalikiana, ingenitesa sana kumbukumbu ile hasahasa kama ningeiona kwa macho yangu!!

Ni ya heri ningehadithiwa!!

Hali hizi mbili zikanifanya nikose msimamo kabisa, sikujua ni kitu gani ningeweza kufanya baada ya kulikuta tukio hili.

Hivi Latipha nilikuwa simpi kitu gani jama? Ni kweli sikuwa na mali nyingi sana lakini walau huduma zote za msingi alikuwa anazipata!!!

Au ni wakati wa faragha yetu…. sasa ina maana alivyokuwa anasema ameridhika huko chumbani alikuwa ananikejeli ama??

Kwa hiyo mimi alikuwa akinikejeli wakati huo kuna mwanaume wake mwingine ambaye alikuwa anamridhisha sivyo!!

Na kama ni mwanaume mwingine basi yule mratibu wa mashindano ya Miss Tanzania lazima kuna kitu alikuwa anatambua.

Ama la ni yeye mwenyewe ambaye alikuwa akimridhisha mke wangu!!

Kauli hizi zilizopita katika kichwa changu ziliniumiza sana kiasi kwamba niliusikia moyo ukipiga hodi kwa nguvu kifuani kama unaosisitiza kuwa unataka utoke nje kupunga upepo!!

Na kwanini alikuwa ananikumbatia kwa nguvu huku akilia na kuniambia kuwa ananipenda!!

Ina maana kuna mtu anamlazimisha tu ili ampende au?

Na ni kwanini sasa apelekeshwe!! Latipha sio wa kihivyo hata kidogo, hapelekeshwi!!

Nilisinzia na kuamka huku mawazo yakiwa hayohayo!!

Niliposinzia kwa mara ya tatu nilikuja kushtuswhwa na kelele tele za abiria kila mmoja akisema lake. Lakini kwa ujumla hofu ilikuwa imetanda

Nikapikicha macho yangu na kisha nikamuuliza mtu aliyekuwa pembeni yangu!! Hata yeye alikuwa ametaharuki sana, hakunijibu!!

Mara akaingia mwanaume akiwa na bunduki, akasisitiza kuwa sote tushuke chini!!

Ndugu msikilizaji tulikuwa tumetekwa!! Nilipagawa!!!

Sote tulishuka huku kila mmoja akimuomba muumba wake.

Niliwasikitikia sana abiria wenzangu, kwani niliamini kuwa ni mimi chanzo cha hayo yote. Nilijiona kama mtu ambaye sina bahati kabisa!! Hivyo nawaambukiza wenzangu mikosi!!!

Tuliposhuka yule mtekaji akaongezea kuwa ni wakati wa kila mmoja kuvua nguo aliyovaa kisha wataangalia ipi ni bora kuliko nyingine na kuchukua na zile zitakazobaki wataziweka kando kisha kuzitia moto.

Watekaji hawa walikuwa wamenuia kutuaibisha na kisha kutuibia!!!

Lakini niseme kuwa walichelewa sana.

Wakati wanatulazimisha kuvua nguo zetu mara ghafla abiria mmoja kati yetu akachomoka mbio mbio na kumvaa yule aliyekuwa ameshika Bunduki!!

Akamsukuma yule bwana mpaka chini na sekunde iliyofuata mlio mkubwa sana ukasikia.Na mara akasimama yuke abiria ambaye bado nilikuwa sijapata nafasi ya kumuoa vyema!!

Akarusha teke kali sana la kuzunguka akamtandika yule mtekaji aliyebaki wima upande wa kidevu akatokwa nay owe kubwa sana huku akitupwa chini.

Na hapo yule abiria mwenzetu alikuwa ameishikilia ile bunduki!!

Nikamtazama kwa makini sana, ni kama niliwahi kumuona mahali hapo kabla. Haikuwa mara ya kwanza kumuona!!!

Ama! Alikuwa ni Geza Ulole yule rafiki yangu wa mahabusu.

Naam! Nikakutana naye tena katika tukio hili.

Safari hii hakuwa katika kuwaonea na kuwanyanyasa watu badala yake alikuwa ametukomboa sisi na mali zetu!

Na hii haikuishia hapo bali kukutana huku tena kukaifanya safari mpya ya maisha yangu ianze!!!


CHUMBA kilikuwa kimya sana, ni matone ya maji yaliyokuwa yanadondoka bafuni pekee ndiyo yalifanya eneo lile lionekane kuwa na uhai walau kidogo!!

Niliutambua ukimya ule lakini sikuujutia bali niliona yale yalikuwa maisha yangu stahiki niliyotakiwa kuishi baada ya tukio lile la kiudhalilishaji kunikumba!!

Kwamba haikuwa ndoto tena Latipha alikuwa mke wa mtu mwingine. Na mimi nilikuwa nimechafuliwa vibaya sana mtaani, kiasi kwamba hata mama yangu hakuweza kuniamini tena. Na hata angeniamini kitendo cha mimi kuendelea kuonekana mtaani kungefanya tukio lile liendelee kuonekana jipya kila siku na mimi kuzidi kudhalilika.

Nikiwa bado nipo pale mara uliingia ujumbe katika simu yangu ambayo niliikuta nyumbani bila shaka ilibaki siku ile nilipokamatwa na polisi kwa kosa la kuzushiwa eti kumpiga mke wangu.

Nilipotazama ilikuwa namba ya mama.

Nikaufungua ule ujumbe na kuusoma.

“MWANANGU ALUFANI MIMI MAMA YAKO NIAMBIE UKWELI ULIFANYA AU UKUFANYA!!” ujumbe ule wa mama ukanifadhaisha sana. Yaani mama yangu haniamini kwa kiasi kile.

Nilijifikiria sana kuwa iwapo mama yangu hakuwa akinielewa katika jambo hili baada ya watu wabaya kuunda tukio ambalo lilikuwa na muunganiko wa kimataifa. Tukio ambalo lilinifanya mimi nionekane kuwa ni mjinga fulani tu ambaye nilikurupukia ndoa na hatimaye imenishinda na kujikuta nikitapatapa huku na kule.

Tukio hilo likanifanya nikose rafiki!!

Sasa nipo hotelini mwili wangu dhaifu kabisa nikiwa peke yangu!!

Nikawa naibofya bofya simu yangu, nikitazama majina ya watu bila kuwapigia simu!!

Hatimaye nikajikuta nimekutana na jina la Geza ulole. Namba ambayo alinipatia siku ya tukio la kutekwa ambapo ni yeye alituokoa!!

Sasa niliiona ina maana kubwa zaidi. Licha ya kwamba Geza alininyanyasa tulipokutana mahabusu hii haimaanishi kitu!! Mbona baadaye alinisaidia hata nikawa Napata nafasi ya kuingia bafuni kuoga na kupata chakula!!!

Huyu pekee ndiye naweza kumueleza matatizo yangu yote akanielewa na ikibidi kunishauri!! Na hata asiponishauri anaweza kunisaidia kujua namaliza vipi matatizo kama yale!!! Nikakata shauri nikabofya namba ya Geza Ulole.

Simu ikaita na hatimaye ikapokelewa alikuwa ni yeye!!

Nikajitambulisha na kisha kumsihi lakini haikuwa nyepesi!!

Alinisumbua sana akidhani. Mimi ni mtu wa usalama hivyo najaribu kumchimba. Haikuwa siku hiyo wala haikuwa siku ya pili, niliweza kuonana na Geza baada ya siku tatu.

Kukutana na Geza ulole kukabadili kila kitu maishani mwangu!!!

Amakweli Geza ulole kwa maana yake Kiswahili IGA UONE!!!

Baada ya muda mrefu wa kunikwepa na kunipa majibu ya kukatisha tamaa kutoka kwa Geza Ulole hatimaye akanikubalia kuonana nami!!!

HATIMAYE IKAFIKA SIKU YA KUKUTANA MTAANI!!!

Geza Ulole alikuwa ni mtu tofauti sana na yule ambaye niliweza kuonana naye mahabusu jijini Mwanza.

Huyu alikuwa ni nadhifu sana, na alikuwa makini sana kwa kila kauli ambayo alikuwa akiitoa na kubwa zaidi alikuwa akifikiria kabla ya kusema jambo lolote. Tabia zake zilinistaajabisha sana, wakati najidanganya kuwa Geza hamna kitu kichwani nilikuwa najidanganya tu!!

Siku ya kwanza kukutana, ilikuwa hotelini tukaketi nje ya ile bustani ya hapo hotelini kisha nikajieleza juu ya jambo ambalo lilikuwa linauponda moyo wangu.

Nilijielezea kuanzia siku ya kwanza nilipopata mashaka juu ya mke wangu kisha kuamua kufunga naye ndoa upesi na hatimaye kisa kimoja baada ya kingine pasi na kupeana nafasi hadi kujikuta matatani nikapoteza fahamu na kuzindukia Mwanza.

Geza alinitazama moja kwa moja machoni akiwa anaigida soda yake taratibu kabisa kisha akajikohoza kidogo ili kuweka koo sawa na hapo akaniuliza jambo la msingi sana. Ambalo sikuwahi kuwaza kulifuatilia!!

“Umesema kuwa mkeo alihitaji kushiriki masuala ya umiss mara ghafla akasema tena hashiriki, halafu umewahi kukutana na mratibu wa mashindano ya umiss akiwa anatokea kwa mkeo. Na kuna picha umewahi kuiona ndani ya chumba chako…..” akasita akanywa soda yake kisha akaendelea tena huku akiwa anatabasamu..

“Dogo…. Vizuri huliwa na wengi. Sijui mkeo ni mzuri kiasi gani hadi watu wazito kama hao waamue kumuoa kabisa. Ok! Mkeo alikuwa mzuri kiasi gani?” Geza aliniuliza swali zito.

Nikabaki kujiumauma! Hakutaka niendelee kuhangaika kutoa jibu la uongo!!

Dogo!! Aliniita kiutulivu sana kisha akaendelea kwa sauti ileile tulivu, “jichunge sana wasije wakakufanya mkimbizi kama walivyoweza kunifanya mimi!!”

“Mkimbizi? Mkimbizi kiaje? Nilimuhoji huku nikiwa katika mshangao.

“Yangu utayajua siku nyingine ngoja tuyamalize ya kwako kwanza….”, “Khalfani ukipendacho wewe kuna wengine kama mia moja na wao wanakitamani!!

Lakini kwa hii kesi yako wewe hapo hakuna cha tamaa wala mdogo wake tamaa kuna mchezo ambao una wachezaji wengi lakini walio makini sana.

Aisee! Yaani ukazimia Dar ukazindukia Mwanza!!

Aisee jamaa wapo vizuri!

“Jambo la msingi nakuomba achana kabisa na haya mambo tulia tu ufanye mambo yako, muda si mrefu mbona utapata mwanamke mwingine utamuoa na mtafanya maisha!!!” Geza alinipa ushauri ule katika namna ya utulivu sana.

Maneno yake hayakuniingia hata kidogo yaani mke wangu ameondoka nyumbani bila kuaga na baadaye ameolewa bila mimi kujua tatizo lolote. Achilia yale ya kukaa mahabusu na kuachiwa katika namna inayotia kero.

Nikiwa katika kufikiria kule. Geza ulole alinishika bega na kunieleza jambo huku akiwa anajikaza asitokwe na machozi.

“Nimewahi kuwa kama wewe dogo, nayajua maumivu ya mapenzi, najua jinsi tunavyoumizwa wanaume wengi ila tunajikaza lakini msichana mmoja tu akiumizwa anaitangazia dunia nzima ili tuonakane wanaume wote kuwa hatuna maana habisa, hatuna utu wala huruma. Tunaumizwa sana dogo….. nimeguswa sana na tatizo lililokukumba wewe kama kijana mwenzangu nami yaliwahi kunikuta na haya ndo yananifanya niishi katika duniani ya hapa si kwangu na pale si kwangu pia.

Mdogo wangu nayaona waziwazi mapenzi yakikuendesha na baada ya muda mrefu ukiyaendekeza basi yatakufanya uwe kiumbe kingine. Kiumbe ambaye hata wewe mwenyewe hautaweza kumuelezea ni wa aina gani.

Nilipanga kukushauri ulipuuzie jambo hili. Lakini hebu nipe siku mbili nitakuja kukupa majibu juu ya mawili matatu ambayo yanaweza kuwa ni chanzo cha mkeo kukusaliti na kisha kuolewa bila kuaga.

Alimaliza Geza huku akisimama!! Nikatamani kumrejesha aketi lakini nikasita.

Siku hiyo ikaisha hivyo!

Akaondoka bila kuaga!!


ITAENDELEA

Fedheha Sehemu ya Tatu

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment