Fedheha Sehemu ya Tano
IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA
*********************************************************************************
Simulizi: Fedheha
Sehemu ya Tano (5)
“Kwa hiyo kumbe dogo unamuonea huruma huyu mama wakati anajua kila kitu kuhusu mkeo alipo eeh!” Geza alinifokea kisha hakuendelea kuleta vurugu. Akaenda katika kiti akaketi na kuanza kulia kwa kwikwi huku akinilaumu sana eti nilishirikiana na Baisar njama za kumfanya mke wangu aingizwe katika shughuli mbaya ya kusafirisha madawa ya kulevya!!!
“Sasa nitawaonyesha mimi ni nani yaani mpaka mtasema Latipha yupo wapi, wewe dogo, we mwanamke pamoja na huyo bosi wenu Baisar!! Na mtaniambia mnalipwa shilingi ngapi…” Geza alikoroma alikoroma huku akitupa mikono huku na kule!!
Baadaye alipitiwa na usingizi!!
Mimi nilibaki macho kwa muda kwa sababu nisingeweza kulala wakati yule mwanamke alikuwa yu macho na hakuwa amedhibitiwa kwa namna yoyote.
Ama hakika dhaifu ni dhaifu tu!!
Baada ya muda kidogo nikaanza kusinzia nikajaribu kuidhibiti hali ile. Na nilipogundua kuwa kuna uwezekano wa hali ile kunizidia na kujikuta nikisinzia, nikaufunga mlango kisha nikahifadhi ule ufunguo. Nikarejea katika kochi, usingizi ukaniandama tena. Sasa nikajidanganya eti ngoja nilale kidogo nitashtuka kila baada ya dakika mbili kumtazama yule mama!!
Hakika nilijidanganya!!
Nikasinzia na kunogewa!!
Nilikuja kushtuka ghafla nikajaribu kupiga kelele lakini sauti haikutoka!!
Macho yangu yalifunguka na kumuona yule mwanamke akiwa juu yangu, alikuwa amenikaba shingo yangu!!!
Nilijaribu kuruka huku na kule lakini alikuwa amenidhibiti ipasavyo!!!
“Taka funguo!!!” alininong’oneza!!
Mbaya zaidi hakunipa kabisa nafasi ya kuzungumza!!
Na hapo akaanza kunipekua mifukoni. Nilitamani kumuita Geza lakini nikawa naisikia tu sauti yake ya kukoroma.
Hakika nilikuwa nimepatikana!! Nikajutia zile nguvu nilizotumia kumdhibiti Geza asimdhuru yule mama!!
Yule mama alikuwa na nguvu ya ajabu sana sikutegemea kama mwanamke anaweza kuwa na nguvu zile!!
Alininyanyua na kusogea nami mlangoni, akiwa amenidhibiti vilevile!! Akaingiza funguo katika kitasa akaufungua mlango!! Akauvuta upesi kisha kwa nguvu akanisukuma nje, nikaangukia tumbo ile natafuta hewa tayari akanifikia na kunikaba tena.
“Piga kelele hata kidogo nakuua!!! Nataka kitu moja tu…. Taka njia… njia wapi??” aliniuliza kwa kunong’oneza lakini alikuwa anatisha!!
Wakati najiuliza nitamjibu nini mara sauti ikasaidia kujibu lile swali.
“Taka njiaa eeh!!” ilikuwa sauti ya bwana Geza!!
Yule mama akasimama aweze kutimua mbio, ila hakupiga hata hatua tatu zaidi, akatua chini baada ya Geza kumnasa miguu!!
“Dogo, kati ya siku umefanya ujinga basi ni leo ila nafurahi kuwa umepata somo. Sikia dogo hata siku moja usimwamini mwanadamu anaweza kulia ukadhani ana machungu kumbe mwenzako amepewa tu kipaji yaani ukimsifia analia, ukimkera analia, ukimpiga analia…. Sasa we jidanganye kuwa kila chozi linakuwa likimaanisha uchungu. Ok! Endelea kumtetea sasa!! Na angekuua huyu, ile kabali nimeiona ilivyokutoa macho.” Geza alinieleza huku akiwa amemnyanyua yule mwanamke ambaye nilitegemea kuwa atapokea kipigo kikali sana kutoka kwa Geza!! Ajabu hakupigwa hata kidogo!!
Geza akamrejesha hadi ndani!!
Akamfungia katika chumba ambacho alikuwa anahifadhiwa kila siku!!
Usiku ule ukapita nikiwa mpole kabisa Geza akawa mtawala maongezi!!!!
Niliongozana na Geza siku iliyofuata tena. Siku ambayo alikuwa amepanga kuendelea kumhenyesha Baisar!!
Siku hiyo ilikuwa ya aina yake tena. Geza alikuwa na akili nakiri kwa mara nyingine na kwa yote niliyopitia nachelea kusema kuwa Geza amekuwa muhimili mkubwa sana!!!
Tulitumia usafiri wa Bajaji kama kawaida…
Siku hii tulishuka maeneo ya Magomeni Geza akiwa na kipara chake tuliyapita magazeti ambayo yalikuwa yameandika na kuchora picha yake iliyotokana na waliomshuhudia kumchora!!
Geza hakujali hata kidogo siku hii alikuwa na jambo jingine kabisa!! Na hapa nikakiri kuwa huyu mtu alikuwa sio tu na akili kubwa ila na roho yake ilikuwa ya aina yake!!!
Aliniacha nje akaingia katika jingo fulani akaniambia kuwa atatoka humo baada ya dakika 30 tu!!!
Kweli baada ya dakika thelathini alirejea na tukaondoka kuelekea Posta!!! Tulipofika posta akaanza kunisimulia kilichotokea alipoingia katika jingo lile.
GEZA ANASIMULIA!!
Dogo maisha ni ya ajabu sana na hakuna kitu kibaya kama maisha ya kukariri!! Wabongo wengi tunaishi maisha ya kukariri, yaani ukiandikia 9 na mwalimu akakueleza kuwa ile ni TISA basi hata ikigeuzwa bado kuna wajinga wajinga watasema ni TISA. Wajanja wachache sana watatambua kuwa sio tisa tena bali ni SITA!!
Ndo kilichotokea huko, nimeingia nikiwa najiamini kabisa. Lile ghorofa kuna ofisi ya huyu boya Baisar. Kwa nilivyomvuruga jana kwa ule mkwara nilijua tu lazima ataweka ulinzi mkubwa sana ofisini kwake ili asije kudhurika.
Alivyo mjinga sasa kama wajinga wengine amewapatia walinzi picha iliyochorwa gazetini. Dah! Yaani nimepita kiulaini kweli hadi nikaifikia ofisi yake.
Katibu muhtasi wake ni mwanamama hivi mrembo. Nikamfikia na kumsalimia kisha nikajifanya kuwa ninazo taarifa za msingi sana za kumweleza Baisar!! Aligoma sana na kuniambia kuwa jamaa amesema hataki wageni siku hiyo!!! Nikamwambia ampigie simu!!
Kweli alivyopiga jamaa akatia ngumu hataki kuonana na mtu!!
Nikafurahi sana kwa sababu kwa kawaida kabisa ninapoingia katika harakati zangu huwa najiandaa kwa majibu ya aina mbili!!
Nikautazama mlango wa yule katibu muhtasi ulikuwa wazi, nikafanya jaribio moja!!
Nikajifanya mimi kiburi na iwe isiwe lazima niende kuonana na Baisar!!
Kweli yule mama akajifanya kunifuata. Aisee nimemzimisha kofi moja kali hadi najisikia vibaya yaani!!
Sekunde moja kaanguka chini, sekunde inayofuata nikasukuma mwili wake akawa katika ofisi yake!!
Na palepale nikachukua simu na kubofya namba 1 ambayo ndo aliibofya na kuongea na Baisar!!
Simu ikaita kisha ikapokelewa!!
“Nimesema staki usumbufu wowote dada!!” alifoka. Upesi nikawahi kumjibu.
“Mimi ni yule jamaa tuliongea jana. Naomba nije ofisini kwako nikuue au unaonaje!!!” nikaongea vile kisha nikaiacha ile simu hewani nikashuka mbiombio! Ndo hapa nipo na wewe, aisee yule bwana asipojiua sijui!!!
Nilibaki kinywa wazi kwa ile simulizi ya Geza ulole. Yaani ni kama alikuwa akisimulia tu filamu ambayo mwisho wake itabaki kuwa filamu tu bila uhalisia wowote ule….
Lakini Yule bwana hakuwa na masihara hata kidogo!!
Alikuwa anamaanisha!!
Maeneo ya posta hatukwenda kwa sababu ya kushangaa maghorofa!!
Geza hakuwa mtu wa kupoteza muda hata kidogo bila sababu za msingi!!
Tulipofika posta Geza akaniongoza moja kwa moja hadi katika shule ya ya msingi ya kimataifa!!
Akaitazama saa yake kisha akaniambia ‘wamekaribia kutoka!!’ sikuelewa alichojaribu kumaanisha!!
Akanivuta karibu zaidi na kuniambia alichokuwa anataka tufanye!!
“Dogo nenda hadi kwa yule dereva pale hivi mfuatilie kwa ukaribu kabisa na watoto wakifika hakikisha kuwa unafanya lolote la kumchelewesha. Haya nenda!!” akanisukumua!! Nikaenda hadi nikawa jirani na eneo lile nikazuga natafuta kitu ambacho sina uhakika nao.
Naam! Wakafika watoto wawili wa kiarabu, nikamwita Yule bwana wakati huo watoto wakiwa wameingia garini tayari.
Nikazuga kuuliza jingo fulani ambalo halikuwa kabisa jirani na pale. Mswahili mwenzangu asiyejua nini hasara za kupoteza muda, akaanza kunielekeza!!
Mara Geza naye akafika!! Alipofika ni kama alikuwa hanijui kabisa akafika na kumkaribia Yule dereva kuna vitu alimnong’oneza hata sikusikia. Badala yake nikamuona dereva akiingia katika gari na Geza naye akaingia!!!
Ni hapo ndipo nilipoiona bunduki!!
Ileee ya Yule mama isiyokuwa na risasi!!!
Mimi nikakaa kiti cha nyuma pamoja na watoto!!
Gari ikaendeshwa hadi nyumbani kwa Geza!! Ile nyumba nyingine tofauti na ile ya siku ya kwanza.
Watoto wakaingizwa chumba kingine na dereva naye chumba kingine!!!
Kisha Geza akaondoka peke yake!!!
Alichokifanya Geza nikakiri kweli ile ilikuwa ni fedheha kubwa kwa Baisar na iwe isiwe lazima tu atafuata anachotaka Geza!!!
Geza akaiendesha ile gari hadi katika fukwe za koko beach akaitelekeza huko lakini si hivyo tu. Alichukua mabegi ya shule ya wale watoto akayaweka garini na kuyatelekeza huko!!!
Kisha akarejea nyumbani, huku alikuwa na masweta ya shule ya wale watoto.
Sasa alikuwa ana kwa ana na Yule mama wa kiarabu pamoja na mimi!!
“Mama jana niliahidi kuwa nitakuua… lakini nikaona kuwa si vizuri mama kuzikwa na watoto wake nikaona nianzie watoto ili walau na wewe ujisikie vizuri kuwazika watoto wako.. aahm! Sio kuwazika walau kusikia kuwa walikufa!! Hivi ngoja kwanza lipi jambo jema mama kumzika mtoto ama mtoto kumzika mama….. au! Tuachane na hilo. Nd’o nshaua mtoto mmoja Yule wa pili bado. Hebu otea ni nani nimemuua!!” Geza alimtupia swali Yule mama!! Huku akitabasamu
Aisee Yule mama macho yalimtoka pima!! Alikuwa anatetemeka kisha akaanza kulia.
“Ooh! Nimepata jibu kumbe watoto ndo wanatakiwa kumzika mama, ila bado hatujachelewa kesho nitakuua halafu Yule mtoto mmoja aliyebaki ndiye atakuzika hapo vipi? Imekaaje hiyo kwa mtazamo wako mama!!” Geza akaendelea kuuliza maswali ya karaha!!
Na kisha akachukua simu yake na kuiwasha kisha akazungumza tena.
“Nakupa hii simu uongee na muuaji mwenzako. Mwambie kila kitu kama ambavyo umekiona….”
Akabofya namba simu ikaanza kuita..
“Ndugu niambie kiasi chochote cha pesa unachotaka nakusihi usiiue familia yangu!!” sauti ya Baiasar ikasikika.
“Baisar Baisar Please…peana na huyu mtu atakacho.. peana naye aache toto moja akiua yote na mimi kufa Baisar… Baisar Please!!” mwanamama alisihi kwenye simu!!
Bila shaka ni hiki Geza alikuwa anahitaji na alikuwa amefanikiwa!!
Baisar alisikika kwenye simu akitokwa na kilio kama mtoto mdogo!!
Geza akatabasamu!!!
“Nakupa hii simu uongee na muuaji mwenzako. Mwambie kila kitu kama ambavyo umekiona….”
Akabofya namba simu ikaanza kuita..
“Ndugu niambie kiasi chochote cha pesa unachotaka nakusihi usiiue familia yangu!!” sauti ya Baisar ikasikika.
“Baisar Baisar Please…peana na huyu mtu atakacho.. peana naye aache toto moja akiua yote na mimi kufa Baisar… Baisar Please!!” mwanamama alisihi kwenye simu!!
Bila shaka ni hiki Geza alikuwa anahitaji na alikuwa amefanikiwa!!
Baisar alisikika kwenye simu akitokwa na kilio kama mtoto mdogo!!
Geza akatabasamu!!!
Kisha akaikwapua ile simu na kuzungumza.
“Baisar yaani hadi wewe kaka mkubwa… yaani na mindevu yote hiyo kweli na wewe unalia kama mtoto mdogo dah! Kweli dunia kitu kingine… anyway mambo vipi Baisar. Ndo nshajichinjia katoto kako, vipi bado hautaki kujisalimisha.
Halafu ni lini mimi nimesema kuwa nahitaji unipatie pesa. Acha basi mambo yako ndugu yangu!!! Pesa zako nilikuwa nikizihitaji zamani wakati nilipokuwa navamia na kuvunja maduka yako sio sasa Baisar.
Sihitaji hata shilingi kumi kutoka kwako. Ninachotaka ni kitu kimoja uondoke nchini bila kuaga ama la uwe tayari kujisalimisha mbele ya serikali na kutaja biashara zako zote haramu unazozifanya. Au tuseme basi mimi ndo serikali niambie ni kwa nini natakiwa kukuacha huru wewe na familia yako?” Geza akatupa swali!!!
“Kaka aah! Kaka… nisamehe nipo chini ya miguu yako!!” Baisar alijiumauma. Nilijisikia fahari sana kumsikia katika hali ile.
“Haya kuna mwanaserikali mwingine hapa IGP mkuu wa majeshi ya ardhini na ya majini hapa luteni kanari mstaafu!! Anaitwa DOGO…. Kuna maswali anataka kukuuliza… huyu hapa!!!” Geza alizungumza vile kwa majigambo kisha akanipatia simu huku akicheka .
“Baisar Latipha yupo wapi…….” Nilimuuliza kwa ukali. Na hapo nikatambua kuwa hali yangu ya kujiamini ilikuwa inaongezeka tofauti na ilivyokuwa awali.
“Jamani naomba niwe muwazi na ninaomba mnisamehe…. Latipha yupo China.. Kule Hong Kong!!! Naomba msamaha jamani nakiri nimekosea” alijibu!!
“Ameenda kufanya nini?” hilo likawa swali la pili.
“Kuna biashara amee… ameenda kuchukua huko!!” alijibu katika hali ya kigugumizi!!
“Biashara gani? Jieleze na usitake kila kitu nikuongoze kwa maswali wewe bwege sawa” nikatia mkwara, Geza akatupa ngumi juu kuashiria kufurahia mkwara ule.
“Aaah! Naomba mnisamehe…. Nisameheni jamani.”
Geza akaikwapua simu…
“Yaani wewe Luteni anakuuliza swali badala ujibu swali we una yaani unaanza habari za kuomba msamaha… nasema hivi ukifanya kosa kama hilo tena naenda kukata sikio ya katoto kalikobakia!!! Na kama kawaida yangu nakata sikio bila ganzi, sina huruma nadhani wanijua..” Geza akakoroma…
Kisha akanirudishia simu!!
“Nimekuuliza ni biashara gani?” nikarejea katika swali langu.
“Ni madawa ya kulevya naomba niwe wazi kabisa. Nisameheni jama nimekosea sana, lakini ni mzima wa afya!!! Na nipo tayari kulipia gharama yoyote ile ndugu zangu” alijibu huku yale maneno yakionekana kukiumiza kinywa chake mwenyewe.
“Ooh! Unaonaje kama na sisi tukimpasua mkeo kisha tuweke nazi kama nane hivi zile kubwakubwa kutoka Pemba na Unguja, tunataka kuzisafirisha kutoka Pemba kupeleka nje ya nchi!!!” nilimuuliza swali ambalo sijui hata lilitoka wapi. Geza alicheka sana!! Eti wakati anacheka akaona furaha yake haiwezi kuishia hapo akamtandika ngumi ya mgongo ghafla yule mama, kwa jinsi alivyoshtuka yule mama hakika ilifaa tu kucheka. Geza akaendelea kucheka huku akikimbia huku na kule.
Alicheka hadi machozi yakamtoka!!!
Yule mama kusikia kuhusu kupasuliwa tumbo alipagawa!! Jasho likawa linamtoka.
Baisar upande wa pili alikuwa analia tu huku akiomba msamaha!!
Geza akachukua simu akaikata!!
Ikawa ni kucheka tu, kasoro yule mwanamke wa kiarabu!!!
“Dogo! Tuko pazuri sana!!! Ngoja niumalize mchezo sasa.” Aliniambia Geza kisha akamchukua yule mama na kumpeleka chumba chake, hapo alikuwa amempatia chakula tayari kisha watoto nao akawapatia chakula!!!
Usiku ukapita na kuamsha siku nyingine tena!!!
Geza kwa kutambua fika kuwa simu anayozungumza na Baisar inaweza kuwa inarekodiwa na kufahamu inatumika kutoka wapi.
Akiwa analiamini sana jengo lile akawahamishia wote sehemu tofauti tofauti kisha akafanya kitu kilichonishangaza tena!!
Geza alimchukua yule dereva na kisha kumlisha chakula kilichokuwa na dawa kali ya usingizi baada ya hapo kwa kutumia gari yake ikiwa na namba za usajili nyingine kabisa alimpakia yule kijana na mimi nikapanda.
Tukaondoka nisijue ni wapi tunaenda!!
Tulisafiri hadi tukafika Morogoro ndani ndani kabisa.
Ilikuwa majira ya saa nane mchana akaniagiza nikachukue chumba katika gesti ya kawaida kabisa!! Nikafanya alivyohitaji!!
Baada ya hapo ikawa ni kuzunguka mara huku mara kule!!! Hadi kigiza kikaingia!!! Dereva akiwa bado hajapatwa na fahamu.
Ni hapo Geza akafanya alichokuwa amepanga!!
Akamwingiza yule bwana kwa siri kabisa katika chumba kile akamlaza kitandani!!
Kisha tukatoweka kurejea jijini Dar!! Jamani Geza alikuwa na akili ya ziada!!
Aisee!! Kesho yake Morogoro ilikuwa haikaliki!!
Taarifa za habari zikawa zinatangaza kuwa mtekaji yupo Moro..
Wakati haya yanaendelea nilikuwa nimeketi sebuleni na Geza tukisaidiana kucheka!!!
“Huyu jamaa anajuana na watu wakubwa serikalini itafikia wakati nitafanya kwa vitendo na si vitisho tena!!! Ngoja usiku wa leo nitakacho muamrisha akikataa tu atajuta kuzaliwa!!!” Geza alizungumza kwa hasira!!
Mimi nikawa sina cha kumshauri. Ningemshauri nini?
Ilikuwa yapata majira ya saa nne usiku, Geza akaingia pale sebuleni akiwa yu pamoja na yule mwanamke mateka wetu.!!!
Nilipomuona nilishtuka sana!! Kwa sababu alikuwa anavuja damu vibaya mno kutoka katika mkono wake!!
Geza sura ilikuwa imemuiva sana!!
“Leta kamera dogo masihara yamezidi naona… yaani huyu mwanamke ananing’ata eti akiamini anaweza kutoroka!!! Mpuuzi sana huyu sasa leo sihitaji ushauri na ninasema hivi na hili likishindikana basi nasalimu amri mimi badala ya yeye Baisar kusalimu amri!!! Yaani anadhani mimi ni wewe kizembezembe tu akakukaba, sasa ngoja nimuonyeshe kuwa kule jela nilipigana mara sitini na mara hamsini nilishinda yaani huko jela ushindi kama huo ni sawa sawa na bingwa wa dunia tu kwa huku uraiani. Yaani bingwa wa dunia nije kupigwa na mwanamke masihara haya… leta kamera!!!”
Nilienda kuichukua kamera upesi!!
Na nikaanza kupiga picha!!!
“Bofya pa kurekodi!!” alinipa maelekezo!!
Na hapo akakiweka kisu kikali sana katika shingo ya yule mama.
Jieleze kwa kirefu kabisa juu ya biashara zako wewe na Baisar bila kukosea hata kidogo, bila kusitasita!!! Upesii!!” aliamrisha Geza na kweli alikuwa hatanii wakati huu. Nilitetemeka sana kulitazama jambo hilo. Sikuwa tayari kurekodi tukio la mtu kuondolewa uhai.
Yule mwanamke alijieleza huku akitetemeka haswa.
Na hapo Geza akampigia simu Baisar!!!
“Ndani ya dakika tano zijazo mkeo anakufa kwa kukatwa shingo yake….. sitanii kwa sababu unaoleta sasa ni ujinga. Yaani Baisar unakuwa kama mjinga fulani hivi familia yako imetekwa wewe unawashirikisha polisi. Aisee haya msaada wa mwisho kabisa kwako wakati huu….. ili kuepusha fedheha hii ya kukutana na shingo za familia yako. Nahitaji uniambie ni wapi yupo Latipha!!”
“Baisar hatunaye!!” sauti kutoka upande wa pili ilijibu na haikuwa sauti ya Baisar!!
“Ameenda wapi usitake kunilaghai eti amejiua!!!”
“Naam! Amejiua!! Na ameacha ujumbe… tafadhali usiwadhuru watoto wala mke wake tafadhali. Kituo cha polisi Msimbazi hapa nsdo simu hii inazungumza.” Sauti iliendelea kujibu!!!
“Sasa amejiua ili iweje kwani?” Geza akauliza swali lile la kukera!!
Kabla hajajibiwa swali lake mara ghafla mlango ukagongwa kwa nguvu na bila kusubiri mshindo uliofuata ukauvunja kabisa.
Wanaume wawili wakiwa wamezificha nyuso zao wakatukabili ana kwa ana wakiwa na bunduki mikononi.
Acha nisimulie nilichokiona jama!
Kwanza Geza hakushtuka hata kidogo, wakaamuru tunyooshe mikono juu. Geza akawa wa kwanza kufanya vile. Akakitupa kisu chake chini
Wakamchukua yule mwanamke, na hapo mmoja akajifunua ile sura yake.
“Naitwa Baisar kubwa la maadui!! Siulizi swali mara mbili, ninauliza kwa mdomo usipojibu nakuuliza kwa risasi. Sijui kubutua pengine zaidi ya kichwa!!!” alitia mkwara bwana yule huku akitabasamu!!
Hah!! Walikuwa wanafanana tabia!!! Wote wazee wa mikwara!!
Geza hakuwa na papara!! Hakujibu lolote.
“We boya watoto wangu wapo wapi najua hawajafa!!” alisema sasa.
“Sijui!!” Geza alijibu kwa kiburi.
Baisar akamrukia na kumtandika teke la kifuani. Geza akarushwa mbali sana. Mbabe kapata mbabe mwenzake.
Alipotua hakupiga kelele za maumivu badala yake alitabasamu!!
Nikiwa natetemeka huku nikiamini kuwa iwe isiwe ile ilikuwa siku ya mwisho kuishi duniani nilimshangaa sana Geza!!
“Wewe… wewe si ndiye Khalfani…. Kwa hiyo huyu fala ndo alikwambia atakusaidia umpate mkeo ama??” baisar aliniuliza sikumjibu mdomo ulikuwa mzioto haswa!!
Akaachana na mimi akasogea kwenda mahali alipokuwa Geza.
“Unajibu swali langu ama la!!” Baisar alihoji kwa ghadhabu!!
Geza akatabasamu kisha akasema, “Nakujibu kaka mkubwa!!”
Dah! Jibu lile likanifanya niamini kuwa kwa mara ya kwanza Geza alikuwa amesalimu amri mbele ya adui!!
“Watoto wangu wapo wapi?”
“Usiniuee mkuu, Miguuni miguuni..Miguuni!!!” akajibu kwa sauti ya juu sana.
Baisar akashangaa na kujitazama miguu yake kama kweli kuna watoto.
Naam! Kikatokea kisichosahaulika na kinachonifanya nisimulie kila siku. Kila mtu na maisha yake hapa duniani, kama umejaliwa elimu shikilia hiyo hiyo usiige maisha yaw engine, hasahasa Geza!! Yaani aliposema miguuni kwa sauti ya juu kumbe kuna watu alikuwa anawasiliana nao mle ndani!!
Mlio haukusikika lakini ndani ya sekunde tatu ama nne. Baisar alikuwa akitapatapa chini, na wenzake wawili vilevile. Bunduki zikiwa zimewatoka huku wakilia kwa maumivu makali sana.
Geza akasimama hatimaye!!! Akacheka kwa nguvu sana!!
“Kazi nzuri vijana wangu!!! Mnaweza kushuka sasa ili tufurahi pamoja!!!” akamaliza kuzungumza na hapo wakatokea vijana wanne wakiwa wameziziba nyuso zao.
Yaani kumbe siku zote mle ndani wakati mi naamini tupo na Geza kuna watu walikuwa wanatutazama tu tayari kwa lolote litakalotokea!!
Naam! Walikuwa wameifyatua ile miguu ya maadui!!
“Naitwa Baisar…. Siulizi swali mara mbili……” Geza akamuigiza Baisar ambaye alikuwa haamini kinachotokea!!!
“Ok! Baisar Latipha yupo wapi” Geza akauliza kwa utulivu. Kisha bila kusubiri jibu lolote akamrukia baisar na kuukanyaga mguu wake sehemu ileile aliyopigwa risasi.
Yowe likamtoka Baisar huku akitoa jibu kuwa Latipha alikuwa yupo nje ndani ya gari!!!
Hakuuliza swali akawaagiza wale vijana wa kazi!!
Ndani ya dakika mbili tu waliingia pale ndani wakiwa na latipha!!
Latipha mke wangu alikuwa amekonda sana, na hakuwa na furaha!! Ni kama alikuwa anaumwa!!!
Nikajikuta nimesimama wima.
Ana kwa ana na Latipha!!
“Khalfani mume wangu, nisamehe mume wangu kwa kila kitu. Sikujua nililokuwa nafanya nisamehe sana Khalfani!!!” alizungumza huku akilia mke wangu!!
Geza aliwafunga kamba wale wavamizi watatu kisha akawapiga picha na kurekodi mipango yao yote.
Kisha akawaambia kuwa anawasamehe lakini ukweli wote anautuma serikalini na kwenye vyombo vya habari.
Kauli ile ya kuhusu msamaha ikamfanya Latipha azungumze.
“Hastahili kuishi hata kidogo…” alisita kisha akaendelea!!
Na hapa akasimulia tukio ba ya sana lililotokea akiwa katika nyumba ya Baisar.
Yaani kumbe Baisar ndiye aliyemsomesha Latipha hadi chuo kikuu, wakati akifanya haya alikuwa ni hawara wa mama yake mzazi Latipha. Na hii ni kwa sababu za umaskini.
Latipha hakuwahi kujua kama mama yake alikuwa katika mahusiano na Baisar.
Japokuwa alikuwa akimuona mara kwa mara pale nyumbani ama wakitoka naye ….
Na alimzoea kwa jina la Anko Baisar!!!
Hakujua kitu kingine kabisa!!
Baadaye huyo Baisar akaanza kumtaka kimapenzi, kwa kuhofia kuwa mama yake atajisikia vibaya Latipha akaificha siri ile.
Lakini mambo yakawa mabaya baada ya kuamua kuwa na Khalfani katika mapenzi. Na ikawa hatari baada ya kuamua kuolewa kabisa!!
Hapo ndipo Baisar alimfuata mama Latipha na kumweleza kuwa hataki Latipha aolewe. Jambo hili likazua kizaazaa baada ya mama Latipha kupingana na Baisar!!
Latipha akaelezea kuwa Baisar alimtishia mama yake kuwa atamuua. Mama latipha akalazimika kumshawishi mwanae kuwa amkubali tu Baisar kwa sababu ni mtu ambaye anaweza kufanya lolote ambalo anataka.
Latipha alikosa namna ya kunieleza mimi juu ya hilo jambo, akajaribu kutafuta visa ili tuachane na bado visa vyenyewe havikufanya kazi.
Mara anitishie kuwa anataka kushiriki umiss!!
Hatimaye Baisar akaingilia kati akishirikiana na mama Latipha wakaamua kunichafua vibaya mno!!
Hatimaye Latipha akaolewa!! Latipha alisimulia mengi hadi akanieleza kuwa rafiki yangu mmoja enzi hizo chuoni alikuwa ni rafiki wa Baisar na alikuwa akimleta Baisar pale chuonbi mimi nisipokuwepo na kuna muda pia alimchukua na kumpeleka kwa Baisar, ilifikia hatua Baisar akawa anaichukua simu yake kilazima na kushinda nayo siku nzima. Ilimradi tu kumvuruga akili!!
Naam!! Maelezo ya Latipha wangu yakanifungua akili juu ya mafumbo mengi yaliyokuwa mbele yangu.
“Khalfani, nimenyanyaswa sana na hasa nilipoguindua kuwa Baisar aliwahi kuwa na mapenzi na mama yangu. Hili jambo linanitesa hadi sasa Khalfani. Najiona sistahili kuishi hata kidogo, ni heri nife tu ijulikane moja. Nitamtazama vipi mama yangu unadhani…… ok! Hata nikiishi huyu bwana amenipasua mara mbili…” akasita na kulifunua tumbo lake!! Lilitisha!!
Dah! Sijui nilitoa wapi zile hasira nilichomoka mbio kisha nikajirusha miguu yote miwili na kutua katika kifua cha baisar huku nikitukana matusi yote!!!
Akajibamiza kichwa ukutani na kutulia tuli!!
Kufikia hapo hapakuwa na maongezi tena!!! Mara Geza akatabasamu kisha akapiga makofi mara tatu kunipongeza.
Tukatoweka pale usiku uleule!!! Baada ya kuondoka simu ikapigwa polisi!!
Kilichofuata tulikitazama katika runinga tu!!
Baisar na wenzake walihukumiwa kwenda jela maisha yote.
Ushahidi wa latipha ukaniweka huru, Geza kama kawaida yake hakuonekana mahakamani wala wapi. Bali alikuwa akiwasiliana nami katika namna alizotaka yeye. Alijua kuwa kuonekana kwake ataishia gerezani tu kwa sababu hata hapo alipokuwa mtaani alikuwa ametoroka mikononi mwa polisi baada ya kuwekewa dhamana!!
Sasa akawa ananitembelea, Mara saa nane usiku, mara apige simu kila siku namba mpya, mara awe kimya miezi sita na zaidi!!
Hakika Msaada wa Geza ulikuwa mkubwa nikafanikiwa kumuona Latipha tena lakini hakuwa na afya yake.
Latipha alikuwa muathirika wa gonjwa la Ukimwi aliloambukizwa na Baisar!!
Ulikuwa mwisho mbaya lakini walau ukweli ulikuwa wazi kabisa!!!
Ile fedheha niliyopata mtaani ikapotea na kugeuka kuwa heshima!!!
Mke wa Baisar alifungwa kama mumewe lakini watoto walichukuliwa na ndugu zao huko uarabuni!!
Jifunze!! Unapoamua kupigania ukipendacho tafadhali usichoke!!
Tafadhali, unapoitafuta heshima hakuna njia zaidi ya kufanya kazi kwa bidii.
Tafadhali, fanya yote ufanyayo lakini tambua kuwa siku moja UKWELI UTASIMAMA WIMA!!!!
Mimi sina la ziada katika FEDHEHA ukomo wangu wa kupanga visa umeishia hapa na sina budi kusema asante kwa kunifuatilia kwa mfululizo huu wa siku ishirini bila kuchoka…
SASA TOA MAONI YAKO!!!
NIPO HAPA KUJIBU KILA COMMENT….
MWISHO!!!
Also, read other stories from SIMULIZI;