It’s Happening Sehemu ya Kwanza
IMEANDIKWA NA: HUSSEIN O. MOLITO
*********************************************************************************
Simulizi: It’s Happening
Sehemu ya Kwanza (1)
Ni asubuhi tulivu iliyokuwa na kila dalili za siku hiyo kuwa nzuri. Ndege angani walionekana kulifurahia anga kwa kuwa halikuwa na dalili zozote za mvua.
Alfajiri ya siku hiyo HUSSEIN aliamka kama kawaida yake na kuanza kufanya kazi za kusafisha nyumba yao
Huo ndio ilikuwa utaratibu wake kila siku. Baada ya kumaliza usafi wa ndani na nje ya nyumba yao. Akaenda kisimani ambapo ni mbali kidogo na kwao na kuchota ndoo kadhaa za maji.
Alipomaliza kuchota maji, tayari mama yake alikua ameshaamka. Alimsalimia na kuingia jikoni ambapo alienda kupika chai. Alichemsha mihogo na kwenda kuandaa tayari kwa kupata kifungua kinywa.
“mama chai tayari, ni vizuri tunywe chai kwanza ndio tuendelee na kazi nyingine.” Aliongea Hussein na mama yake akaacha kufua nguo na kuungana naye kunywa chai kwa pamoja.
Walipomaliza kunywa chai, walisaidiana kufua nguo na baadae Hussein aliondoka nyumbani baada ya kuhakikisha amemaliza kazi zote za nyumbani.
Mama yake alifarijika sana kuwa na mtoto mwema ambaye alikua mfano wa kuigwa kwa majirani zake. Kila mtu alitamani Hussein angekuwa mtoto wake kwa jinsi alivyokuwa mtiifu kwa mama yake. Alizifanya kazi hata ambazo watu walisema za kike.
Hussein alienda kijiweni kukutana na wenzake ili kujua ratiba za mechi kwakua alikua mchezaji pia katika timu ya kijiji chao.
Alipofika alikutana na marafiki zake waliokuwa wanasoma gazeti la ijumaa. Aliwasubiri wamalize kusoma na yeye akaomba apitishe macho yake kwenye gazeti hilo.
“kama vipi njoo nalo mazoezini baadae, maana sisi tunaondoka sasa hivi.” Aliongea mmiliki wa gazeti hilo.
Hussein alivutiwa zaidi na kurasa ya kwanza baada ya kuandika habari za mwanadada Super star anayemkubali kutoka moyoni kutokana na kazi zake.
Ilitokea picha kubwa ya JAQUELINE WOLPER huku maandishi ya kichwa cha habari yakiripoti juu ya msanii huyo kutwaa tuzo ya oscar huko marekani kama muigizaji bora wa kike Afrika. Taarifa hizo zilimfurahisha sana kwakua alikua anaamini kuwa alikua anastahili.
Baada ya kumaliza kusoma lile gazeti, alirudi nalo nyumbani na kuliweka mezani na yeye kuingia chumbani kwake na kuchukua daftari lake na kuendelea na utunzi.
Mbali na kucheza mpira. Ndoto kubwa ya Hussein ni kuwa super star katika fani ya uigizaji kama marehemu Kanumba na wengineo. Kila siku alikua anaandika story za filamu hiku akiamini kuwa kuna siku atapata nafasi ya kuonyesha kipaji chake kwenye jamii.
Wakati akiendelea kuandika stori hiyo, kwa mbali alisikia sauti ya mama yake akiwa analia. Aliacha kuandika na kutoka chumbani kwake haraka na kumkuta mama yake sebuleni akiwa ameshika lile gazeti huku machozi yanmtoka.
“mama. Kuna nini kimetokea?” aliuliza Hussein kwa wasi wasi mkubwa.
“hamna kitu. Nimewakumbuka tu wazazi wangu.” Aliongea mama yake Hussein na kuendelea kulia.
“pole mama, ukilia unaniumiza na mimi kwakua siijui hata sura ya baba. Natamani na mimi angalau niseme kitu hiki nimenunuliwa na baba yangu kama watoto wengine wanaojivunia baba zao.” Aliongea Hussein na kumfanya mama yake kumkumbatia na kumuomba anyamaze kwa kua kauli ile iliendelea kumuumiza zaidi.
Hussein alijitahidi kumbembeleza mama yake na baadae mama yake akawa sawa tena. Baada ya kula chakula cha mchana na kupumzika kidogo. Hussein alienda mazoezini kama kawaida yake kila ifikapo jioni.
Kocha wao alitangaza kuwa mechi imeghairishwa mpaka kesho yake mida kama ile. Ila wanatakiwa kuendelea na mazoezi.
Ilipotimia saa kumi na mbili na nusu. Walimaliza mazoezi yao na Hussein akarudi nyumbani kwao. Alichukua maji na kwenda kuoga. Alipomaliza aliingia ndani na kubadilisha nguo.
Aliamua kumfuata mama yake aliyekuwa amekaa nje huku akionyesha wazi kuwa hakuwa na furaha kama siku zote.
“mama, kama nimekukwaza ni vizuri kuniambia kuliko kuwa katika hali kama hiyo.” Aliongea Hussein baada ya kumuona mama yake akiwa katika hali ya kukosa furaha.
“nipo sawa tu mwanangu.” Aliongea mama yake hussein.
“hapana mama, mimi nakujua ukiwa kawaida au ukiwa una huzuni. Leo ni wazi una huzuni au hasira na kitu Fulani.” Aliongea Hussein na kumfanya mama yake amgeukie na kumuangalia usoni.
“kweli mwanangu sipo sawa. Nawaza haya maisha magumu tunayoishi mimi na wewe yataisha lini?.” Aliongea mama yake Hussein huku akionyesha wazi kuwa kitu kile kilimtatiza.
“turidhike tu mama. Si unajua kuwa mungu anagawa kwa foleni. Ipo siku tutapata na sisi hata kama foleni yetu ipo nyuma sana.” Aliongea Hussein huku akimshika mama yake uso kumuondioa makunyanzi yaliyojitokeza usoni kutokana na huzuni aliyokuwa nayo.
“hasa nikikuangalia wewe ndio machungu yanazidi halafu nikiangalia watu wengine wanazidi kufanikiwa na wanatumia hela nyingi sana kwa siku. Roho huwa inaniuma sana.” Aliongea yule mama kwa uchungu.
“ndio hivyo mama. Mungu ameweka matabaka kwa walionazo na sisi wengine tusio nazo. Unafikiri wote tungekuwa sawa ni nani angemtuma mwenzake?” aliongea Hussein huku akiendelea kumfariji mama yake.
“una maneno mazuri sana na kila siku huwa nafurahi unaponiita mama. Hata siku moja sikutamani wewe ujue ukweli nilionao moyoni kwa miaka mingi. Ila wakati mwengine roho inanisuta kwakua mimi ni mwanadamu. Ipo siku nitakufa ghafla bila ya wewe kuujua ukweli wa maisha yako. Leo nimeumia sana kumuona msanii mkubwa kwenye gazeti ulilokuja nalo kupata mafanikio makubwa zaidi. Najua itakuwa ngumu kuamini. Ila amini haya maneno niyatamkayo leo hii………. Mimi sio mama yako mzazi.”
Aliongea mama yake Hussein huku machozi yanamtoka. Alilia na kumtazama Hussein ambaye alionyesha wazi kutoamini alichokisikia kutoka kwake.
“wewe ndio mama yangu. Na sihitaji mama mwingine zaidi yako wewe. Kwanini uanikataa mama. Kama kuna makosa makubwa nimekugfanyia ni bora uniweke wazi ili nikuombe msamaha kuliko kuninyima haki ya kukuita mama. Ni adhabu kubwa sana kwangu.” Aliongea Hussein huku machozi yakianza kutiririka kwenye mashavu yake.
“nakupenda sana Hussein. Na kwakua nakupenda ndio maana sikuwa tayari kukuambia ukweli mapaka hivi sasa. Ila roho inaniuma kukuona unapata tabu kukaa na mimi wakati mama yako anakula raha huko Dar-es-salaam. “ aliongea mama yake Hussein kwa uchungu.
“mama yangu halisi ni nani?” hatimaye Hussein aliuliza swali lile.
“ninachokuambia ndio ukweli halisi. Mama yako mzazi ndio huyo super star aliyetokea kwenye gazeti ulilokuja nalo. Mama yako ni JAQUILINE WOLPER”
Mama yake Hussein aliongea maneno hayo na kumuangalia Hussein aliyepigwa na bumbuwazi baada ya kusikia taarifa zile.
“Nakataa mama, hawezi kuwa mama yangu.” Aliongea Hussein huku machozi yanamtoka.
Kilio hicho kilikua cha dhahiri kwakua hata mama yake alikua analia pia.
“mama yako alikua ni rafiki yangu tu toka enzi tulizokuwa tunasoma shule.” Aliongea mama yake Hussein na kumuangalia mwanaye huku anafuta machozi yake ili amuhadithie stori nzima kuanzia mwanzo mpaka pale walipo.
Hadithi aliyohadithiwa Hussein kuhusu mama yake mzazi ilimtoa machozi. Hakuamini kuwa mama yake angewaza kumtelekeza pale kwa rafiki yake na yeye kukimbilia mjini.
“sawa mama nimekuelewa. Ila mimi sihitaji hata kumuona kwa alichoamua kunitendea. Siwezi kumuita mama mie.” Aliongea Hussein huku machozi yanamtoka.
“mama ni mama Hussein. Haijalishi kuwa amekutelekeza au amekutendea vitu vibaya. Angekuwa hakupendi basi usingekuwa hai mpaka sasa hivi.” Aliongea yule mama yake wa hiyari huku akijaribu kumbembeleza.
“kama kweli anamapenzi na mimi, kwanini hanitafuti?..kwanini hakupi msaada kwa kazi kubwa ya kumlelea mwanaye? Kwanini sikusoma shule nzuri kama watoto wengine wa mastaa???..kwanini hanitangazi na anatangaza kuwa ana mtoto mmoja aliyezaa na tajiri maarufu?….hawezi kuwa mama yangu japokuwa amenizaa. Wewe ndio mama yangu tosha.”
Aliongea Hussein kwa hasira na kunyanyuka na kuondoka eneo lile huku analia.
“Hussein…Hussein….”
Aliita mama yake Hussein bila mafanikio. Tayari Hussein alishakimbia na kwenda kukaa peke yake kijiweni jioni ile.
Mawazo yalimrudisha mbali sana. Aliwaza vile mama yake huyo wa kufikia alivyokuwa anajivunia kuwa naye na kumpa sifa kwa majirani zake kuwa na mtoto mtiifu.
Mara kadhaa mama yake huyo wa hiyari alikua analia kila akimuangalia jambo ambalo mwanzoni hakutambua ilikua kwa sababu gani. Kuna wakati alijisahau na kumwambia kuwa ana kipaji kama mama yake na alipomuuliza alizuga kuwa hata yeye alikua muigizaji mzuri alipokuwa shuleni.
Mawazo hayo na mengine mengi ndio yalimfanya kuamini kabisa kuwa alikua na mama mwingine tofauti na huyu anayeishi naye.
Aliwaza juu ya kumkubali mama yake wa ukweli lakini moyo wake ulikataa katu katu kwakua alionekana dhahiri mama yake kutokuwa na nia nae.
Aliwaza sana na kulia kupita kiasi. Baada ya muda kuna mtu alimshika bega, alipogeuka alimkuta mama yake wa hiyari alikua amemfuata.
“usiwaze sana mwanangu, turudi nyumbani.” Aliongea mama yake huyo kwa sauti iliyojaa huruma na mapenzi juu yake. Alinyanyuka Hussein na kumkumbatia.
Alikubali kurudi nyumbani. Chakula cha usiku hakikupita kabisa kooni mwa Hussein. Alinyanyuka na kuingia chumbani kwake.
Usingizi uligoma kabisa na mawazo juu ya kile alichoambiwa siku hiyo ndio yalichukua nafasi kwa muda huo.
Asubuhi aliamka na kufanya usafi kama kawaida yake. Wakati anakunywa chai, mama yake alimuhitaji waongee baada ya kupata kifungua kinywa hicho.
“mwanangu. Mungu kakuumba wewe mwanaume ili upambane na kila jambo. Zuri au baya, zito au jepesi. Nilikua naombi. Ni vizuri ujiandae wiki hii ili wiki ijayo uenda Dar-es-salaam ili ukamtafute mama yako.”
Aliongea yule mama na kumuangalia Hussein ambaye alionekana kukosa furaha toka jana yake.
“mama, mimi nishamkubali kuwa ndio mama yangu, ila swala la kumtafuta itakuwa ngumu sana. Kama kweli atakua ananihitaji basi atanitafuta. “ aliongea Hussein huku akionyesha wazi kutokubaliana na mawazo ya mama yake huyo.
“unajua kuwa kuna uweezekano mkubwa sana kuwa mama yako anaamini wewe umeshakufa kutokana na hali aliyokuacha nayo. Hivyo si ajabu ukawa faraja yake na wewe ikawa sababu ya kutimiza ndoto yako. Hustahili haya maisha ya kutatapa wakati mama yako mzazi anabadilisha magari kila siku.” Aliongea mama yake huyo wa hiyari na kumuonyeshea umuhimu wa yeye kumtafuta mama yake.
“mama, mimi nayafurahia sana haya maisha ya amani na upendo ambayo naishi na wewe. Hayo magari ni yake na mimi hayanihusu hata kidogo.”
Hussein aliendelea kumgomea mama yake huyo swala la yeye kwenda mjini kumtafuta mama yake. Baada ya mama yake huyo kumbembeleza sana, alikubali kwa shingo upande kwenda Huko Dar ambapo hajawahi kufika toka azaliwe. Alipasikia tu kwenye Radio na kupaona kwenye taarifa ya habari.
Baada ya kula chakula cha mchana. Alienda kwenye mechi ambayo timu yake ilikuwa inacheza siku hiyo na timu kutoka kijiji cha pili.
Kiwango chake uwanjani kilikuwa kibovu kutokana na mawazo aliyokuwa nayo. Hata kocha alimshangaa na kusababisha kumkaripia mara kwa mara.
Alimchezea mtu rafu mbaya iliyomsababishia kadi nyekundu. Alitoka uwanjani bila kuongea na mtu na kushika njia ya kuelekea kwao.
“nilikua naelekea kwenye mechi kukuangalia mpenzi wangu, nimechelewa nini?”
Aliuliza msichana mmoja aliyekutana naye njiani alipokuwa anarudi nyumbani.
Hussein hakumjibu kitu yule msichana na kuendelea na safari yake.
“
“Jamani Hussein, si nakuuliza lakini?” aliongea yule msichana baada ya kumfata na kumzuia Hussein.
“achana na mimi Mariamu, huwezi jua jinsi nilivyochanganyikiwa hivi sasa.” Aliongea Hussein huku akimuangalia Mariamu aliyekuwa katika hali ya sinto fahamu.
“nini faida ya kuwa na mpenzi?,,, si kuliwazana katika shida na matatizo na kupongezana katika furaha au?…kama huoni msaada wangu kwa hilo basi. Ukiona umuhimu wangu utanitafuta.” Aliongea Mariamu na kumuacha Hussein na kuondoka zake.
Hussein alifikiria kwa muda maneno ya mariamu na kujikuta hakumtendea haki mpenzi wake.
“Mariamu,…Mamu subiri basi.”
Aliongea Hussein huku akimkimbilia mpenzi wake ambaye alikua anaendelea na safari yake.hakutaka kumsikiliza kwakua alikua amekasirika kwa kitendo chake cha kutomshirikisha kwenye mambo yanayomsibu.
“nakuomba nisikile Mamu. Sio mimi ambaye napenda hali kama hii itokee. Ila nina tatizo tu lililonikuta ndio maana najihisi nimechanganyikiwa.”
Alijitetea Hussein huku akimfuata mpenzi wake ambaye alikua anazidi kuongeza mwendo na kutotaka kumsikiliza.
Baada ya kuona hasikilizwi, Hussein alimfuata na kumshika mkono.
“sio kwamba sihitaji msaada wako mpenzi wangu. Nahitaji faraja kwa hili. Nimechanganyikiwa mwenzio.” Aliongea Hussein kwa sauti ya upole.
Mariamu hakujibu kitu zaidi ya kwenda kwenye gogo ambalo halikua mbali na hapo ili amsikilize mpenzi wake yapi yaliyomkuta.
“mama ameniambia kitu ambacho kama angeniambia mtu mwengine tofauti na yeye basi nisinge muamini hata aape kiapo gani.” Aliongea hayo na kumuangalia mpenzi wake ambaye alikua njia panda mpaka hapo.
“jambo gani hilo.” Aliuliza Mariamu na kumuangalia Hussein bila kupepesa macho.
“anadai yeye sio mama yangu mzazi.” Aliongea Hussein huku akiangalia chini.
Alipoinua kichwa kumuangalia mpenzi wake ambaye alikua na hamu ya kumjua mama yake halisi baada ya huyo wanaye amini siku zote kuwa ndio mama yake.
“nilibisha sana, ila baada ya kunielezea historia yao ndio nikaamini kuwa mama yangu mzazi ni JAQUELINE WOLPER”
Aliongea Hussein na kumfanya Mariamu kupigwa na butwaa. Hakuamini mara moja yale maneno aliyoambiwa na mpenzi wake. Ila baada ya kudokezwa story ya mama yake halisi na huyu mama yake wa hiyari anayeishi naye. Mariamu aliamini.
“kwahiyo umechukua hatua gani baada ya kuujua ukweli?” aluliza Mariamu huku akimsikitikia mpenzi wake huyo kutokana na maswahibu yaliyomkuta.
“mama ameniambia kuwa wiki ijayo niende Dar-es-salaam kumtafuta mama yangu halisi.”aliomgea Hussein na kumuangalia mpenzi wake ambaye alikuwa na sura ya huruma juu yake.
“hivi unawajua ma super star wewe au unawasikia tu. Kwanza kuonana nae shughuri nzito. Kuna watu wamezaliwa Dar na kukulia huko lakini hawajawahi kumuona hata Kinyambe katika maisha yao. Itakuwa wewe ambaye unataka kuonana na Jaqueline Wolper bila mawasiliano yake…. Sikushauri hata kidogo kwenda huko.”
ITAENDELEA
It’s Happening Sehemu ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;