It’s Happening Sehemu ya Pili
IMEANDIKWA NA: HUSSEIN O. MOLITO
*********************************************************************************
Simulizi: It’s Happening
Sehemu ya Pili (2)
Aliongea hayo Mariamu na kumuangalia Hussein ambaye alikuwa kwenye dimbwi la mawazo.
“hata mimi sikupenga kwenda huko. Tatizo mama ndio kangang
ania.” Aliongea Hussein na kumuangalia Mariamu ambaye wakati huo alikua akimsikiliza kwa umakini mkubwa.
“usiwe na akili za kushikiwa. We mueleze kuwa, kama kweli ni mama yako na ana nia na wewe, basi angekutafuta. Huo ndio ukweli wenyewe.” Aliongea Mariamu na kuonyesha wazi kuwa hakua tayari mpenzi wake kwenda mjini.
“sijawahi kumkosea heshima mama yangu. Hivyo nitafuata alichoniambia. Nitakutafuta tena kwa ajili ya kukuaga. Niombee dua.”
Aliongea Hussein na kumfanya Mariamu ageukie upande wa pili. Alipomgusa, Mariamu aliinama na kuanza kulia.
“usifanye hivyo mpenzi wangu, mi nakupenda na nakuahidi kuwa nitarudi hata kama nikishindwa kuonana na mama yangu. Na ikitokea kuwa mama yangu kanikubali basi tutaishi wote maisha mazuri zaidi ya haya ya mateso tunayoishi.”
Aliongea Hussein na kumnyua kichwa Mariamu ambaye wakati huo machozi yalishalowanisha mashavu yake. Alimnyanyua na kukilaza kichwa cha mpenzi wake kifuani.
“nakupenda Hussein. Kwanini unaniacha peke yangu. Huko mjini kuna wasichana wazuri na wenye kujipamba. Kuna urembo wa kila aina ambao huwafanya watu wawe wazuri zaidi ya uhalisia wao… najua kuondoka kwako utakua mwisho wa mapenzi yetu kitu ambacho sitaki kitokee.”
Aliongea mariamu na kuzidi kulia kwa uchungu akililia penzi lake kwa Hussein ambaye anampenda kupita kiasi.
“safari sio kifo mamaa, kifo ndio kinaweza kututenganisha. Uzuri wao utanifanya nione wivu wa kukupendezesha na wewe. Mbona hapa kijijini hutumii chochote na unawakimbiza. Unafikiri nikiwa nakutumia mapambo na nguo za mjini si watakuloga mwaka huu… acha kulia mpenzi wangu. Wivu weka kando na angalia mustakabali wa mapenzi yetu.”
Maneno ya Hussein yalifananishwa na msamaha wa mtu aliyehukumiwa kunyongwa na tayari kitanzi kilishawekwa shingoni. Tabasamu la matumaini lilianza kuchomoza na kumfanya Mariamu kunyanyua uso wake uliolowa kwa machozi lakini sura yake ikiwa na hali ya kutabasamu. Alinyanyuka na kumkumbatia Hussein.
“naomba tuwe waaminifu. Na popote ulipo uwe na kumbu kumbu ya kuwa umemuacha mtu anakusubiria wewe kwa shida na raha.” Aliongea maneno hayo Mariamu na kumfanya Hussein kutabasamu.
“ndio maana nakuambia kuwa akili na mawazo uliyonayo ni sawa na almasi iliyokuwa juu ya mchanga. Sema tu walowezi hawajaishtukia. Maana ningekuwa sina changu hapa.” Aliongea Hussein na wote wakacheka huku wakiendelea kuliwazana na mabusu pamoja na maneno matamu ya mapenzi.
Ni siku ya jumamosi tulivu isiyokuwa na dalili zozote za kunyesha mvua, Hussein alijiandaa na kutoka akiwa amependeza kiasi. Alichukua begi lake na kutoka nje.
“mama. Nitemee mate ili safari yangu iwe yenye Baraka .” aliongea Hussein na mama yake akamtemea mate.
“safari njema mwanangu.” Aliongea mama yake Hussein.
Hussein alianza kuchanja mbuga na kulekea kwa kina Mariamu kwanza kabla hajaondoka.
“ndio hivyo mpenzi wangu, nisindikize basi.”
Aliongea Hussein na Mariamu akaanza safari ya kumsindikiza Hussein kituoni.
“chukua picha yangu. Nahisi tutakuwa tunawasiliana kupitia hizi picha. Utakuwa unanikumbuka kama mimi nitakavyoanza kulala na picha yako kuanzia leo.” Aliongea Mariamu na kumkabidhi Hussein.
“ahsante sana mpenzi wangu.” Aliongea Hussein na kuichukua ile picha na kuiingiza kwenye begi lake.
Walifika kituoni ambapo kulikua na watu wachache waliokuwa wakisubitri huo usafiri wa kuwafikisha kituo kikubwa cha mabasi yaendayo mikoa mbali mbali.
“acha niwahi gari, mungu akipenda tutaonana. Niombee dua nifike salama.” Aliongea Hussein na kumuangalia mpenzi wake ambaye alionyesha wazi kuhuzunika kuondoka kwake.
“nakutakia safari njema.” Aliongea Mariamu huku machozi yakianza kujenga vifereji kwenye mashavu yake.
Hussein alikimbilia gari na kupanda. Gari lilipoanza kuondika alimpungia mkono mpenzi wake kama ishara ya kumuaga. Mariamu aliunyanyua mkono wake kivivu na kumuaga Hussein huku machozi yakimtiririka kama maji.
Gari lilianza safari salama usalimini na kufika kituo kikuu ambacho walipanda mabasi yaendayo mikoa waliyotaka kwenda siku hiyo. Hussein alifanikiwa kupata tiketi na kupanda basi ambalo linaelekea Dar-es-salaam
Aliinama na kuomba dua sana kwa Mwenyezi Mungu aiwezeshe safari yao wafike salama. Basi lilianza safari muda mfupi baada ya wasafiri wote kuingia ndani ya basi.
Kwanza ilikuwa ni mara ya kwanza kusafiri kwa basi, pia aendapo ni mara ya kwanza pia kufika kama watafika salama.
Hussein alionekana mtulivu huku akiwa kwenye msongo wa mawazo.
Kutokana na gari walilolipanda lilikua chakavu, walikwama mara kadhaa njiani na kufanikiwa kuingia kwenye kituo kikuu cha mabasi yatokayo mikoani Ubungo mida ya saa tatu usiku.
Watu wengi walishuka na kupokelewa na ndugu zao. Hussein hakuwa na wa kumpokea. Zaidi alikua anashangaa tu mataa yaliyokuwa yakimulika eneo hilo. Kutokana na kutojua wapi pa kuanzia, aliamua usiku huo kulala hapo hapo ubungo baada ya kuwashuhudia watu kadhaa wakilala.
Asubuhi palikucha salama na yeye alidamka na kutoka nje. Hela alizompa mama yake zilibaki kiasi cha shilingi elfu thelathini. Hela hizo walizipata baada ya kuvuna na kuuza mahindi yaliyostawi vizuri kwenye shamba lao.
“magomeni kariakoo…. Manzese,magomeni kariakoo bado watu wawili tuondoke.”
Hussein alizisikia kelele za makonda na wapiga debe wakinadi gari zao zilizokuwa nyingi pembeni kidogo tu mwa kituo cha mabasi makubwa.
“kariakoo..kariakoo nilishawahi kupasikia.”
Aliwaza mwenyewe kwenye kichwa chake kutokana na eneo hilo kuwa maarufu na lilitajwa mara kwa mara kwenye taarifa za habari huko kwao.
Alipanda hilo gari na kuelekea kariakoo. Purukushani za watu zilimfanya Hussein aamini kuwa alishafika mjini. Alitembea huku akiyaangalia magorofa ambayo alikuwa anayaona kwenye tv tu. Baada ya kutembea muda mrefu, njaa ilianza kumuuma na kuingia kwenye mgahawa wa mama ntilie na kunywa chai. Aliposhiba, alitoka na kuanza kuitalii kariakoo kila pande. Alitokea mtaa wa congo na kuvutiwa na watoto wenye rika lake wakiwa wanafanya kazi mbali mbali. Alimfuata mtoto mmoja aliyekuwa kashika mifuko mikononi na kumfuata.
“mimi ni mgeni hapa, eti kama na mimi nataka kufanya biashara nitapataje malighafi ?” aliuliza Hussein na kumuangalia yule dogo ambaye kiumri alikuwa mdogo kwake lakini alionekana dhahiri kuwa ni mjanja sana.
“kwani wewe una shilingi ngapi?” aliuliza yule dogo baada ya kumuangalia Hussein ambaye alikuwa na begi lake la nguo.
“elfu ishirini na tano ndugu yangu.” Aliongea Hussein na kumuangalia yule dogo.
“zilete nikakulatee mzigo wa maana” aliongea yule dogo na kuendelea kumsoma Hussein.
“mi ntakuamini vipi wakati ndio kwanza leo tunaonana?” aliongea Hussein huku akihofia kutapeliwa hela zake.
“siwezi kukimbia na elfu ishirini wakati hapa nazipata kwa siku tu, kama hutaki nikusaidie basi tambaa.” Aliongea yule dogo maneno ya kishujaa.
“sio kwamba sitaki, ila mwenzio ndio nazitegemea hizo.” Aliongea Hussein huku akionyesha wazi kuhofia kudhulumiwa.
“we zilete hizo hela, nakupa mzigo wangu nikirudi nakupa wako na wewe unanipa wangu.” Aliongea yule dogo na Hussein akakubali na kumuhesabia yule dogo elfu ishirini na tano na kumkabidhi.
“we nisubiri hapa, dakika sifuri nitakuwa nisharudi.” Aliongea yule dogo na kumuachia mifuko yake Hussein na yeye kuondoka na zile hela.
Masaa yalizidi kukatika bila dalili zozote za yule dogo kurudi. Alisubiri mpaka jioni, hapo aliamini kuwa tayari alishatapelewa. Machozi yalianza kumtoka na hakujua afanye nini. Maana njaa ilikua inamuuma na mfukoni alibakiwa na shilingi elfu mbili tu.
Akiwa peke yake kajiinamia baada ya kulia muda mrefu, anashtushwa na mtu aliyemgusa bega. Alinyanyua shingo na kumuangalia, alikua mvulana mmoja aliyekuwa mchafu kidogo akiwa na maboksi akiwa ameyakumbatia.
“vipi mdogo wangu, nimekuona umejiinamia muda mrefu,.. umepatwa na nini?” aliuliza yule mtu na kukaa karibu na Hussein.
“we acha tu kaka, mimi ni mgeni hapa Dar, nimeingia jana usiku kutokea huko Tanga. Hivi leo nilikuwa na akiba yangu ambayo nilikuwa naitegemea kuanzisha biashara yoyote hapa mjini. Nimetapeliwa na sijui nitaishi vipi.” Aliongea Hussein huku akiwa na dalili zote za kutaka kulia.
“wewe mwanaume, unatakiwa ujikaze na upigane kiume…. Umekula?” aliuliza yule jamaa.
“bado sijala” alijibu Hussein.
Yule mvulana alinyanyuka bila kuongea kitu na kwenda kwa mama ntilie wa jirani ambaye alikuwa amemaliza kuuza na kununua mabaki ya chakula. Baada ya hapo alirudi kwa Hussein na kumletea kwenye mfuko kile chakula.
“hicho kinaitwa buti, ndio chakula bei chee kwetu.” Aliongea yule mtu baada ya kumkabidhi makoko Hussein
“nashukuru sana.” Aliongea Hussein baada ya kumaliza kula.
“nenda pale kachukue maboksi yatakayo kutosha. Hicho ndio kitanda chetu. Kesho tutaangalia michakato ya kukutafutia mishe, usiwaze sana dogo.” Aliongea yule jamaa na kuanza kutandika maboksi yake na kujilaza.
Hussein hakua na jinsi, alienda kuchukua maboksi na kujiunga na watu wengi wasiokuwa na makazi na kulala huku amejifunika ngumi mpaka asubuhi.
Saa kumi alfajiri, Hussein aliamshwa na yule jamaa na kwenda naye kwa mzee mmoja mnene mwnye ndevy nyingi ambaye aliikuwa mmiliki wa mikokoteni na matoroli.
“mzee Ndevu, kijana wangu huyu, mpe mkokoteni.” Aliongea yule jamaa baana ya yeye kuchukua toroli kubwa kwa mzee huyo ambaye walimlipa hela yake ya kukodisha baada ya masaa kadhaa.
“ataweza kazi huyu??” aliuliza mzee Ndevu kiutani.
“hili jembe mzee, naliaminia.” Aliongea yule jamaa huku anacheka.
“poa, kamtolee lile dogo.”
Aliruhusu mzee Ndevu na yule jamaa akachukua funguo na kumtolea Hussein mkokoteni.
Alienda nae kijiweni kwao na kumuelekeza jinsi ya kumfuata mteja atakayekuwa na mzigo na kuongea nae bei kutokana na uzito au ukubwa wa mzigo wenyewe.
Alijitahidi kufanya kazi kwa bidii, mpaka jioni alikuwa na shilingi elfu tano. Alirudisha mkokoteni na kulipia shilingi elfu moja kama kiwango ambacho watu wate walikuwa wanamlipa mzee Ndevu ambaye alikuwa na matoroli yapatayo themanini.
Maisha hayo mapya alianza kuyazoea taratibu na kujikuta anaanza kufahamiana na watu wengi kila kukicha. Alijiua jinsi ya kumtongoza mtu mpaka akavutiwa na kitu anachomtangazia.
Baada ya miezi miwili, aliamua kubadilisha biashara baada ya kupata fedha kidogo zilizomuwezesha kumiliki meza ya viatu kariakoo. Mungu aliendelea kumsaidia hadi kufikia uamuzi wa kupanga chumba yeye na rafiki yake mpya waliokuwa karibu hapo wanapouzia viatu vyao.
Zilipita siku tatu rafiki yake hakuonekana nyumbani walipopanga wala pale kazini. Hussein hakuwa na taarifa zozote juu ya rafiki yake huyo kutorudi nyumbani.
Siku hiyo mida ya saa kumi na mbili akiwa anarudi nyumbani, alimshuhudia kibaka akimpora dada mmoja mkoba wake na kukimbilia upande wake. Alimsubiri na alipomkaribia alimpiga ngumi nzito iliyompeleka yule kibaka chini na kuachia ule mkoba alioiba ukiwa upande wake.
Kwa haraka yule kibaka alinyanyuka na kuondoka. Hussein aliufuata ule mkoba na kuuokota. Alimfuata yule dada aliyeporwa ule mkoba na kumkabidhi.
“ahsante sana kaka yangu, yaani nakushukuru sana” aliongea yule binti aliyekuwa amevalia mavazi ya kileo na kuwa na muonekano mzuri tena wa hali ya juu.
“usijali.”
Hussein alimkabidhi yule dada mkoba wake , bila kusubiri chochote kutokwa kwa yule dada. Hussein aliondoka. Kabla hajafika mbali, deffender ilisimama na maaskari kadhaa walishuka na kumkamata Hussein.
Si Hussein tu aliyekuwa kwenye bumbuwazi juu ya kukamatwa kwake, bali hata watu waliomjua Hussein walishangaa pia. Hakuna aliyejua sababu ya kukamatwa kwa Hussein
“dereva naomba ifuatilie ile deffender.”
Aliongea yule dada aliyesaidiwa na Hussein akimwambia dereva wake na bila hiyana, Dereva alichoma mafuta kuifuatilia ile Deffender inapoelekea.
Defender hiyo ilienda kusimama kwenye kituo kikubwa cha polisi msimbazi na kumshusha Hussein na kuingia naye ndani. Huku nyuma gari iliyokuwa ikiwafatilia wale polisi ilipaki pembeni na yule dada akashuka na kwenda pale kituoni.
“huyo kaka aliyekamatwa hapo mimi ni ndugu yangu. Amefanya kosa gani mpaka mume mkamata?” aliongea yule dada baada ya kufika pale polisi akitaka maelezo juu ya kukamatwa kwa Hussein
“ tumemkamata kwa kosa la kupigana hadharani, maana hawa wamezidi kujifanya wana ugomvi kumbe ndio njia zao za kuwaibia watu.. hii operation ya kuwakamata wenye tabia hizi ndio tumeianza leo.” Aliongea mmoja wa maaskari waliokuwepo kwenye ile Deffender.
“nimekuelewa afande, lakini huyu sio kama alikuwa anapigana kwa nia ya kuiba. Yule aliyempiga ndio kibaka aliyenipora mimi na huyu kaka wa watu ni msamaria mwema tu ameamua kunisaidia.” Aliongea yule dada huku akionyesha wazi kumuhurumia Hussein.
Huku na huku ilitakiwa atoe elfu kumi ili wamuachie, bila hiyana yule dada alifugua pochi yake na kutoa noti moja kati ya noti nyingi nyekundu alizokuwa nazo.
“pole sana kaka.” Aliongea yule dada baada ya Hussein kuruhusiwa.
“ahsante sana, hawana lolote hawa. Njaa tu zinawasumbua.” Aliongea Hussein huku akionyesha wazi kukasirishwa na kile kitendo.
“usijali, pia nakushukuru sana kwa wema ulionitendea. Maana bila wewe nisingeupata huu mkoba wangu pia bila ya kunisaidia mimi usingekamatwa.” Aliongea yule dada huku akitabasamu.
“tuko pamoja.” Alijibu Hussein na kumlipizia tabasamu lake.
“unaelekea wapi muda huu?” aliuliza yule dada baada ya kuona giza limeanza kutawala.
“kigogo.” Alijibu Hussein
“ingia basi kwenye gari nikusogeze.” Aliongea yule dada na Hussein alitii na kuingia kwenye gari.
“milima haikutani ila binaadamu tunakutana. Ni vizuri kama tukijuana hata majina ili ikitokea siku tukaonana tena basi iwe ni sababu ya kukumbukana zaidi.” Aliongea yulee dada huku akionyesha kufurahi uwepo wa Hussein siku ile.
“naitwa Hussein.” Alijitambulisha Hussein
“mimi naitwa Belinda.” Alijitambulisha yule msichana.
Baada ya kupiga story mbili tatu hatimaye walifika kigogo na Hussein alishuka kwenye lile gari.
Baada ya siku mbili toka Hussein alipokutana na Belinda, ndipo rafiki yake alipokuja baada ya kutoonekana siku tano pale magetoni kwao.
“ulikuwa wapi mwana siku zote bila taarifa wala nini?” aliuliza Hussein baada ya kumuona rafiki yake.
“sorry rafiki yangu, nilikuwa location na shoot movie. Si unajua natafuta tobo mwenzako.” Aliongea yule rafiki yake maneno yaliyomfanya Hussein akae vizuri.
“habari njema hizo mwanangu. Hata mimi nazi feel sana hizo ishu.” Aliongea Hussein huku akikaa vizuri kumsikiliza rafiki yake huyo.
“poa, zikitokea nyingine nitakushtua.” Aliongea rafiki yake huyo bila kujua lengo la Hussein kuja pale mjini.
Wiki mbili baadae, matangazo yalirushwa kwenye vituo mbali mbali vya habari na matangazo mengine yalibandikwa kila sehemu juu ya muigizaji mkubwa Tanzania na Afrika nzima kuandaa Audition ya kutafuta wasanii wachanga watakao shiriki kwenye movie yake mpya.
Tangazo hilo alilipata Hussein na kuchekelea sana kwakua aliamini ndio nafasi pekee ya kuonana na mama yake.
Alifanya mazoezi kwa bidii akishirikiana na rafiki yake kwenye vikundi mbali mbali vya sanaa hiyo ya maigizo.
ITAENDELEA
It’s Happening Sehemu ya Tatu
Also, read other stories from SIMULIZI;