Mama’ke Mama Sehemu ya Kwanza
IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA
********************************************************************************
Simulizi: Mama’ke Mama
Sehemu ya Kwanza (1)
Laiti kama leo ingekuwa ni miaka ishirini iliyopita basi ningewekewa dau la dola milioni moja na kuambiwa nikifanikiwa kuandika simulizi yoyote ile basi zile dolali ni halali yangu basi kila mmoja angeweza kunicheka kwa sababu hakuna ambacho ningeweza kushinda. Bali ningekuwa upande wa kushindwa!!! Sikudhani kama ipo siku nitakuwa na simulizi ya kuandika hasahasa miaka ishirini iliyopita…..
Ama laiti kama asingekuwa mama yake mama, nd’o kabisaa nisingekuwa na simulizi ya kusisimua na yenye kuelimisha na kuonya kizazi mpaka kizazi…..
******
Angali nikiwa na miaka tisa, siku moja mama alikuwa mwenye furaha sana na alikuwa akitusimulia mambo kadha wa kadha kuhusu enzi zao, mengi yalikuwa ya kuchekesha sana kwa sababu laiti kama yangefanyika enzi hizi za utandawazi kingekuwa ni kituko. Alielezea ubaguzi wa vyakula jinsi wasichana walivyozuiwa kula mayai na mapaja ya kuku pamoja firigisi. Akaelezea pia juu ya utamaduni wa wanaume kuchaguliwa wanawake wa kuwaoa.
Hapa tulicheka sana, alitueleza kuwa zama zile hapakuwa na mambo ya kujichagulia mume….. kasha akanong’ona kuwa hata yeye alikutana na baba siku ya ndoa yao ya kimila tu….
Hakika ilifurahisha!!
Hatimaye akafikia suala la majina, alieleza kuwa kizazi cha sasa mzazi anajisikia tu jina lolote anamuita mtoto wake, lakini zamani mtoto angeweza kukaa mwezi mzima pasipo kuwa na jina rasmi hadi pale linapopatikana jina lililobeba maana kubwa ndani yake. Sio jina ilimradi jina unalojisikia kuita.
Mama akataja baadhi ya majina, yalikuwa magumu sana kutamka kila alivyotamka sisi tulikuwa tunacheka tu.
Baadaye mdogo wangu akamuuliza mama kuhusu sisi majina yetu, mama akamjibu kuwa kwa sababu tulizaliwa kijijini na sisi tulipewa majina yenye maana.
“Tena kama wewe Fred ulibadilishwa majina mara tatu.” akanigeukia mimi, hapo sasa mada ikageuka mdogo wangu, mpwa pamoja na dada yangu mkubwa wote wakataka kujua kuhusu mimi. Huu ulikuwa utaratibu wa utotoni ilimradi wapate tu cha kunitania kutokana na hiyo simulizi atakayotoa mama. Nilitamani mama asisimulie lakini nisingeweza kumzuia.
Mama akawatuliza kisha akasimulia kuwa jina langu la kwanza kabisa ambalo yeye na marehemu baba walinipa lilikuwa TABULO lakini baada ya kupewa jina lile nilianza kulia sana bila kukoma, wakadai kuwa huenda lile jina lina urithi mbaya, akaja babu kizaa baba na yeye akanibatiza jina jingine akaniita KIRENGE….. kuanzia siku nilipopewa jina lile kila usiku nilikuwa nashtuka na nikishashtuka silali tena, wakalazimika kunipeleka kwa mganga wa kienyeji baada ya siku sita za jina lile, mganga akashauri kuwa nibadilishwe jina lile jina halinifai hata kidogo na ni hatari sana kwa afya yangu, basi ikawa zamu ya mama kunichagulia jina akaniita Ngomeni, idhini hii alipewa na baba yangu!!
Jina lile likawa kama baraka likanituliza nikawa na amani tele na mwenye furaha.
Kilichobaki haikuwa simulizi kutoka kwa mama tena bali ni mimi nakusimulieni kilichojiri katika maisha yangu. Sina miaka tisa tena ni mtu mzima sasa….
Tafadhali makinika ili ujifunze.
Nilidumu na jina lile kwa mwaka mmoja kabla ya kupata ubatizo kanisani ambapo baba alinipa jina la ubatizo FREDI.
Naam! kwa sababu ubatizo ule niliupata wakati huo tukiwa tumehamia mjini tayari basi nikazoeleka kama FREDI na hatimaye lile jina NGOMENI ama kwa kifupi NGOME likapotea.
Nikaanza shule ya awali kwa majina FREDI Boniphace.
Mara moja moja sana mama yangu alikuwa akiniita jina NGOMENI na hapa ni pale anapokuwa anazungumza kikabila ama akiwa amekumbuka enzi hizo.
Basi ataniita na kunisemesha kikabila angali nilikuwa naambulia maneno machache tu.
Nikamaliza shule ya awali na hatimaye shule ya msingi nikijulikana kama Fred Boniphace.
Mdogo wangu pamoja na dada yangu wote wakalisahau lile jina Ngomeni, na walipokuwa wakiniita jina lile nilikuiwa napatwa na hasira sana kwa sababu niliona kama halifai jina lile hasahasa pale mjini.
Nilisoma hadi darasa la tano, upeo wangu darasani ulikuwa mkubwa kiasi kwamba mkuu wa shule akamshauri mama kama inawezekana anitafutie nafasi kidato cha kwanza nivushwe darasa.
Mama akafanyia kazi lile wazo na hatimaye siku moja akaja nyumbani na taarifa ya kufurahisha akanieleza kuwa amepata nafasi shule moja ya serikali kuna kijana aliyechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza lakini hajaweza kuripoti shuleni hivyo nafasi ile ipo wazi, hiyo pekee haikuwa habari ya kufurahisha lakini habari kubwa ni kwamba jina la kijana yule lilikuwa sawa na jina langu la ukoo. Yaani Ngomeni!!
Ni kweli jina lile lilikuwa linanichukiza lakini kwa sababu ilikuwa nafasi ya kwenda kidato cha kwanza bila kumaliza darasa la saba ilikuwa habari njema sana kwangu.
Ikawa habari na kisha ikahamia kwenye matendo, nikaingia kidato cha kwanza huku nikiitwa Ngomeni Paulo, jina lisilokuwa langu.
Nilikuwa na mwili mdogo sana kiasi kwamba kwa pale darasani nilionekana kwa kila aliyeingia kwa urahisi sana.
Mdogo na ninakaa nafasi za mbele.
Lakini ule udogo haukuwa upande wa akili, nilikuwa naelewa upesi na nilifanikiwa kuwashawishi waalimu upesi kunitazama kwa jicho la tatu.
Wanafunzi waliokuwa wakubwa kwa miili na umri. Kila nilipowazidi darasani, wqaalimu walkinitumia kama mfano ili kuwadhalilisha.
Mimi sikuwa najali sana kuhusu hayo… niliitazama elimu na kuipa kipaumbele.
Huku jina Ngomeni likiwa sio tatizo tena kwangu.
Amakweli wakati mwingine nyakati mbaya huanza kwa dalili kuwa nzuri sana.
Ulikuwa ni mwezi wa tano wakati tukiwa katika maandalizi ya mtihani wa kufunga shule kwa ajili ya likizo ndefu ya mwezi mmoja. Nilikuwa nimeupania sana mtihani na nilijiona kuwa nipo tayari hata kama wataleta mtihani mgumu kiasi gani.
Siku tatu kabla ya mtihani kuanza, niliamka asubuhi kama ilivyokuwa kawaida yangu kwa ajili ya kusoma na kujiandaa na shule, lakini siku hii niliamka shingo ikiwa inauma sana. Nikapuuzia na kuona ni hali ya kawaida kuwa huenda nimeilalia vibaya, nikajaribu kujinyoosha wakati ninanawa uso lakini hapakuwa na nafuu.
Shingo ikazidi kukakamaa huku maumivu yakizidi na ikinilazimu kuigeuzia upande wangu wa kulia ili kupunguza yale maumivu.
Hilo likawa kosa la jinai, nilipogeuzia upande ule ikawa shughuli pevu kuirudisha upande wa kushoto ili niweze kutazama mbele.
Wanafunzi wakubwa kiumbo na umri walikuwa wakinipenda sana kutokana na ule udogo wangu akili darasani na pia nilikuwa mpole hivyo nashukuru kuwa hawakuwahi kunionea.
Hata nilipokumbwa na hali ile na kuanza kuangua kilio walinijali haraka sana. Wakajaribu kunichua lakini hali ilikuwa tasa isiyozaa matunda. Hapo wakaamua kunipeleka kwa kiongozi wa bweni ambaye alichukua dhamana ya kunipeleka kwa mwalimu wa zamu.
Mwalimu akaniingiza katika orodha ya wanafunzi wagonjwa, nikapakiwa garini na kupelekwa nje ya shule ambapo palikuwa na zahanati iliyokuwa inatuhudumia.
Nilipewa kipaumbele cha kwanza kabisa, nilipokewa na wauguzi wakinibeba mgongoni kama mtoto wao wakanipeleka kwa daktari.
Daktari alinitazama na kunigonga gonga kisha akanichoma sindano na kunisihi nitulie kwa muda na nisiiilazimishe shingo yangu kugeuka.
Kweli baada ya takribani nusu saa shingo yangu ilirejea katika hali ya kawaida nikawa ninao uwezo wa kupeleka kushoto na kulia.
Baada ya wenzangu kuhudumiwa tukarejea shuleni.
Mwalimu wa zamu alinisihi nijipumzishe kwa siku hiyo kwa sababu ulikuwa utaratibu waliopewa na daktari.
Kweli nikapumzika huku mara kwa mara wanafunzi wenzangu wakifika kunitania na kunipa pole.
Siku ile ikapita na siku za kuufikia mtihani zikazidi kujongea, bado nilijihisi kuwa nipo tayari kuliko mwanafunzi yeyote yule katika kuukabili mtihani wangu huo mkubwa wa kwanza kwa shule ya sekondari.
Nakumbuka ulikuwa usiku wa jumapili, siku hiyo kabla haijawa usiku mvua ilinyesha kwa wastani wake na kuleta kiubaridi. Ilikuwa ni kama mvua ya kuukaribisha mtihani uliotakiwa kufanyika siku ya jumatatu.
Wanafunzi katika vitanda vyao walikesha wakikariri tayari kwa kujibu mtihani. Mimi nililala mapema sana, hadi pale nilipokuja kushtuka giza likiwa nene sana.
Lakini sikuwa katika hali ya kawaida.
Mwili wa mwanadamu ni wa ajabu sana jamani, usiombe ukajeruhiwa inaweza kuwa kitu kidogo tu lakini madhara yake mwili mzima ukauma.
Hii ilikuwa upande wangu, awali nilidhani ni muwasho wa kawaida tu nikaingiza kidole sikioni na kujikuna. Hilo likawa kosa, nilipofanya vile sasa kwa akili zangu kabisa nikasikia kitu ambacho kipo hai kikiwa ndani kabisa ya sikio langu kikitembea.
Nikajaribu kwa uoga kujikuna tena. Sasa kile kiumbe hai ndani ya sikio langu nacho kikawa kama kinapambana aidha kwenda ndani zaidi ama kutoka nje……….
Balaa likaanzia hapo, nikapiga mayowe nikiita jina la mama huku nikiwa nimelishika sikio langu.
Yule kiumbe hai naye akazidi kutapatapa, kila alipokuwa anatapatapa na mimi nazidi kupata maumivu!!
Awali nilidhani ni muwasho wa kawaida tu nikaingiza kidole sikioni na kujikuna. Hilo likawa kosa, nilipofanya vile sasa kwa akili zangu kabisa nikasikia kitu ambacho kipo hai kikiwa ndani kabisa ya sikio langu kikitembea.
Nikajaribu kwa uoga kujikuna tena. Sasa kile kiumbe hai ndani ya sikio langu nacho kikawa kama kinapambana aidha kwenda ndani zaidi ama kutoka nje. Ikawa kama tunapambana
Balaa likaanzia hapo, nikapiga mayowe nikiita jina la mama huku nikiwa nimelishika sikio langu.
Yule kiumbe hai naye akazidi kutapatapa, kila alipokuwa anatapatapa na mimi nazidi kupata maumivu makali sana ndani ya sikio!!!!
ENDELEA
Nilipiga mayowe makubwa sana kiasi kwamba bweni zima hakuna ambaye hakuamka na hapo upesi taarifa zikatolewa jenereta likawashwa mwanga ukapatikana, zikaanza harakati za kunituliza.
Haikuwa rahisi hata kidogo!!
Haikuwa rahisi kwa sababu ile karaha na maumivu nilikuwa napata mimi na si wao. Hivyo niliwazuia wasiutoe mkono wangu katika sikio langu kwani ile nd’o njia pekee niliyoona ni sahihi kabisa ya kupunguza maumivu yale.
Mwalimu wa zamu tayari alikuwa amefika eneo lile akiwa na waalimu wengine kadhaa waliokuwa wakiishi katika nyumba za waalimu pale shuleni, upesi waliwasiliana na dereva aliyekuwa na jukumu la kuendesha gari la shule. Lakini dereva hakupokea simu bila shaka alikuwa amelala hoi usiku ule ama la alikuwa yu mbali na simu yake.
Mwalimu wa zamu alivyoona hali inazidi kuwa mbaya alilazimika kuendesha gari yeye mwenyewe akaamuru wanafunzi kadhaa wenye ubavu zaidi yangu wanikamate kwa nguvu kabisa. Maana nilikuwa sina utulivu hata kidogo na kila jambo lililokuwa linafanywa kwa ajili yangu nililitazama katika namna ya kwamba sio jambo sahihi. Ajabu sikujua lipi linaweza kuwa sahihi kwa muda ule.
Walifanikiwa kunidhibiti japokuwa nakumbuka nilijaribu kutapatapa huku nikifanikiwa kumng’ata mmoja wapo mkononi.
Ndugu yangu unayesikiliza ama kuusoma mkasa huu, hali ile niliweza na ninaweza mimi tu kuisimulia na usiombe ikakukuta wewe. Nilihisi nanyanyaswa, nanyimwa haki zangu za msingi.
Nilifikishwa hospitalini kama mgonjwa wa akili anavyokuwa, nilifungwa kamba kikamilifu wakati napelekwa chumba cha daktari ambaye kama bahati tulimkuta usiku ule…. alishangazwa na hali ile nilimshuhudia alivyokuwa na hofu, sijui ni kutokana na muonekano wangu ama ni vile nilivyokuwa nimefungwa kamba.
Upesi wakamuelezea kama kilio changu kilivyokuwa kikijieleza.
Daktari akanifikia kisha akawaita vijana wawili wanafunzi wale waliofanikisha zoezi la mimi kufungwa kamba.. akawaambia wanigandamize kichwa ili aweze kunimulika sikioni atazame kunani.
Walinigandamiza kwa nguvu sana kiasi kwamba hata ningefanya nini nisingeweza kuwaponyoka. Ni mdomo tu uliobaki kupiga mayowe kuwa naumiaaa naumiaaaa! Lakini sikuweza kujitikisa sehemu nyingine tena.
Ndugu zanguni, nilijua wazi kuwa ile ingeweza kuwa siku yangu ya mwisho kuishi ulimwenguni kwa hali ile nilivyokuwa najisikia. Nilihisi kama kichwa kitapasuka muda wowote, niliamini hapatakuwa na lolote la kuiweka tena sawa hali yangu ile.
Nilimsikia daktari akiwaeleza kuwa haoni kitu chochote sikioni mwangu.
Alipoyasema hayo nilistaajabu kwa sababu nilikuwa nikisikia kabisa mdudu ananitembea ndani kabisa ya sikio.
“Daktari yumo mdudu yumo ananitembelea.. ananiumiza daktari naumiaaaa naumiaa” nilimweleza huku nikimkazia macho kumaanisha nilichokuwa nasema.
Daktari aliwaambia kuwa amenitazama kwa makini na hakuna kitu chochote kile.
Majibu yale ya daktari yalifanya niingiwe na hofu mpya!
Nilimsihi sana daktari kuwa mdudu yule anazidi kuniumiza.
Daktari akasema aniwekee dawa kama mdudu yumo basi atakufa lakini yeye hajaona kitu chochote kile. Na akasisitiza kuwa kifaa alichokitumia kimemuweza kuona ndani kabisa ya sikio.
Daktari alimwita nesi na kumuagiza dawa iliyokuwa katika mfumo wa kimiminika akawaita wale wanafunzi walioniinamisha na kunigandamiza tena, daktari akanimiminia matone kadhaa sikioni.
Mungu wangu weee! Bora asingeniwekea dawa ile maana nilikuwa kama niliyechokoza vita, sasa haikuwa mitambao ya kawaida bali muungurumo mkubwa iliyoambatana na mitikikisiko, nilipiga kelele sana hadi nikawa najisikia mimi mwenyewe tu. Sikusikia yeyote katika eneo lile.
Kama ile haitoshi mara nikasikia sauti nyingi sana zikiniita jina langu la shuleni ‘Ngomeni’ zilikuwa sauti za kike nikajiuliza wale manesi wamejuaje jina langu na mbona wananiita kwa sauti ya juu vile.
Nilizidi kupagawa nikigeuka huku na kule sasa hakuna aliyekuwa anajihangaisha na mimi katika kunishika pale kitandani ni kamba zilikuwa zinanidhibiti.
“Tunatoka tukitaka tunatoka na tutarudi tena tukitaka kurudi!!!” nilizisikia sauti zile zile za kike zikiniambia vile. Nikajiuliza hawa manesi wananiambia kitu gani hiki nisichokielewa asilani, na palepale nikajikuta nikiwa nakumbwa na nguvu za ajabu sana. Nikajikakamua na kisha nilivyofyatuka nikakatakata zile kamba nikatoka mbio sana nisijue mbele yupo nani. Nikajikuta namkumba mwalimu wangu wa zamu. Ilikuwa bahati mbaya sana kwake kwani alikumbana na kichwa changu katika mdomo wake. Nilianguka chini na yeye akaanguka chini lakini hakuishia kuanguka tu, aliacha meno mawili palepale.
Nilitulia kwa muda huku nikihema juu juu… sikupata kuisikia tena ile mitapotapo ya yule mdudu katikia sikio langu.
Sikio lilikuwa linauma tu lakini hapakuwa na mdudu.
Wanafunzi wenzangu walikuwa wananishangaa na ni kama walikuwa na hofu ya waziwazi juu ya kile kilichokuwa kimetokea.
Kitendo cha kijana mdogo kama mimi kukata kamba ngumu kama zile kiliwaacha midomo wazi.
Hata mimi nilipoziona kamba zile nilishangazwa mno, niliwezaje kuzikata kamba zile. Lakini lile halikuwa na nafasi ya kujadiliwa badala yake mwalimu alikuwa anapata tiba ya kwanza baada ya dhahama ile.
Tukio lile ukawa mwanzo wa kila kitu kisichopendeza katika maisha yangu.
Tulirejea shuleni majira ya mchana.
Nikapitwa na mitihani mitatu ya siku hiyo.
Mtihani wa hisabati, Kiswahili na historia…. mojawapo kati ya masomo niliyokuwa nayapenda sana. Sikuumizwa sana na kuikosa mitihani hii, nilibaki kushangazwa na kile kilichonisibu.
Lile tukio liligoma kufutika kichwani kwangu upesi, na kikuu kilichonisumbua ni sauti za wale manesi wengi walioniambia maneno yale kuwa watatoka wakitaka, na baada ya hapo kitendo cha kuzikata zile kamba pale kitandani, kamba ngumu kabisa ambazo hata uwe na nguvu kiasi gani inakuwa shughuli pevu kuzikata.
Eti mimi na kimwili changu hiki nikaweza kuzikata.
Wakati huo nilikuwa ninayo miaka kumi na mbili tu!!
Siku iliyofuata niliamka nikiwa mzima wa afya kabisa nikafanya mitihani yangu vyema hadi siku ya kumaliza. Lakini kutokana na kukosa kufanya mitihani ya awali nikajikuta nakuwa mwanafunzi wa sitini kati ya wanafunzi mia moja.
Niliumia sana kutokana na matokeo yale mpenzi msikilizaji na wewe unayeusoma mkasa huu.
Waalimu walinifariji sana na kuniambia kuwa laiti kama ningefanya masomo yale ningekuwa wa kwanza lakini haikuniingia akilini kabisa. Utoto ulikuwa bado pamoja nami…
Naam! Shule ikafungwa, sasa sikuwaza tena juu ya mdudu sikioni mwangu badala yake nilifikiria juu ya kuangukia nafasi mbaya kabisa darasani.
_____________________
Kitendo cha kukuta sijajaziwa masomo matatu kikamfanya mama anihoji ni kwanini sikufanya mitihani yangu, nilimweleza kuwa sikufanya mitihani ya masomo matatu, mama alistaajabu sana na hakulilazia jambo lile damu. Kumbe kimya kimya bila kunieleza alienda shuleni kuulizia kuwa ilikuwaje nikakosa kufanya masomo yale. Uzuri wakati anauliza alikuwepo yule mwalimu wa zamu, akamuelezea kila kilichojiri.
Mama aliporejea nyumbani aliniuliza ni nini kilitokea nikamueleza kuanzia habari ya shingo kugoma kugeuka na kisha mdudu katika sikio langu!!!
Mama alishangaa sana ni kama kuna kitu alitaka kusema lakini akashindwa kusema kwa sababu alizokuwa akizijua yeye mwenyewe.
“Mama yule mdudu sikioni alikuwa anaongea!!” nilimwambia mama baada ya kimya cha muda. Mama alitabasamu kisha akanichukua na kunikumbatia.
Nikiwa nayasimulia haya na utu uzima huu hata mimi mtoto wa miaka kumi na mbili akinieleza jambo la kustaajabisha kama lile ni vigumu sana kumuamini zaidi nitahisi ni akili za kitoto.
Bila shaka hata mama yangu alihisi kuwa zile ni akili za kitoto tu!! Mdudu anaanzaje kuongea katika sikio langu!
Mzaha mzaha jipu hutunga usaha!
Mama naye hakutilia maanani hata kidogo. Hili yawezekana lilikuwa mojawapo ya kosa lililokomaza tatizo.
Nilipokuwa nyumbani kipindi cha ile likizo nikiwa nasoma masomo ya ziada hakuna kilichokuwa kinaenda vibaya kila kitu kilienda sawa sawia.
Hatimaye nikasahau yale yote kuhusiana na mdudu aliyeongea katika sikio langu. Nikajiwekea dhana yawezekana nilikuwa naota angali nimefumbua macho.
Siku zikahesabika na hatimaye tukafungua tena shule.
Niliendelea kufanya vizuri hatimaye hata wanafunzi na waalimu wakasahau juu ya yule mdudu na kama kunikumbushia walifanya kama utani tu. Nikacheka na wao wakacheka, maisha ya shule yakaendelea.
Kama kawaida ya shule kipimo cha mwanafunzi ni mitihani.
Ikafikia tena wakati wa mitihani, hapo ikiwa imebaki kama siku siku nane kabla ya kufanya mtihani. Hii ya sasa ilikuwa ile ya kumaliza mwaka wa masomo.
Nilikuwa si mtu wa michezo sana kwa sababu nilikuwa naogopa sana kuteguka, hivyo kwenye michezo mimi nilikuwa mtu wa kushuhudia tu wenzangu. Hofu yangu kuu ilikuwa kuumia mkono na kisha kushindwa kuandika vyema.
Safari hii sikuwa tayari litokee jambo lolote lile la kunizuia kufanya mitihani yangu vizuri.
Lakini waneni wanasema kuna mambo hayakwepeki na hata ukijaribu kuyakwepa kumbe wajipeleka kwenye njia yao mbadala.
Siku moja nilichelewa kuamka, haikuwa kawaida yangu na hata hii niliihesabu kama ajali tu.
Kuchelewa huku kuamka nikachelewa kuhesabu namba, wachache walioenda shuleni hata wewe hapo msikilizaji najua wajua kero za kuhesabu namba!
Basi siku hiyo sikuhesabu namba, na sikuwaza sana kwa sababu nilijua kuwa kwa sababu ni kawaida yangu kuhesabu namba kila siku basi siku hiyo hata nikiomba msamaha mwepesi tunaweza kusamehewa.
Kumbe siku hiyo watu wengi sana walipuuzia hawakuhesabu namba!
Jambo hili likawa kero kubwa sana kwa mwalimu wa zamu, ule muda wa kuwa mstarini akaagiza wote waliohesabu namba wapite mbele.
Hapo sasa mapigo ya moyo yakaongeza kasi yake nikiamini kuwa na kile kiubaridi cha asubuhi nikichapwa bakora nitaumia sana. Nikafikiria cha kujitetea.
Kweli wakatoka mbele wakahakiki namba zao na kisha wakaruhusiwa kwenda darasani.
Wengi tuliosalia tukaambiwa tupige magoti chini, mwalimu akawaomba waalimu wenzake wamsaidie kutuchapa bakora tatu tatu kila mmoja. Wanawaume tuchapwe makalio na wasichana wachapwe mikono.
Kweli waalimu wakaanza kutushambulia, nilikuwa naogopa kila mwalimu naona anachapa kwa nguvu sana.
“Ngomeniii!” hatimaye nilisikia sauti ya mwalimu ikiniita, alikuwa mwanamke na ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona bila shaka alikuwa mgeni.
Sikujiuliza sana amelijua vipi jina langu kwa sababu ule umri wangu mdogo ulikuwa umaarufu tosha achana na uchapakazi wangu lilipokuja suala la masomo.
Nilinyanyuka kinyonge kwenda kwa yule mwalimu.
“Kwanini haujahesabu namba leo” aliniuliza kiupole sana huku akinishika shika mashavu yangu.
Katika umri ule sikujiuliza juu ya kauli yake lakini katika umri huu najiuliza aliposema sikuhesabu namba leo anamaanisha siku zilizopita alijuaje kama nilikuwa nahesabu namba wakati mimi namuona ni mgeni kabisa kwangu?
“Madam… leo nimepitiwa tu nisamehe!!” nikamjibu kinyonge katika hali ya kumshawishi asinichape.
“Kukusamehe kwangu nakuchapa kamoja tu sikuchapi tatu.. ili kesho ukumbuke kuamka mapema na ninakuchapa mkononi….haya tega mkono.” akaniambia huku akiiandaa fimbo yake ndogo.
Niliiona ahueni kuadhibiwa na mwalimu huyu, tena kiboko kimoja.. nikautega mkono wangu wa kulia ili anichape.
Ndugu zanguni mnaofuatilia mkasa huu, Yule mwanamke hata hakuunyanyua mkono wake juu sana, hilo likanipa ujasiri sana. Nikaamini hakuwa na nia ya kuniadhibu bali alifanya geresha kasha aniache.
Akaishusha fimbo yake, ni kama nilivyodhania awali kuwa sitapata maumivu sana.
Ilikuwa hivyo sikuumia sana, akaniruhusu niende darasani.
Nikakimbia upesi kuelekea darasani.
Nilipofika darasani nikachukua siti yangu na kufungua madaftari kwa ajili ya kuanza siku hiyo…. punde akaingia mwanafunzi mwingine ambaye naye hakuhesabu namba moja kwa moja akanifuata huku akicheka.
“Dogo mjanja wewe umetimua mbio haujachapawa daah! halafu kidogo ticha Haule akuone ungekoma leo…..” alinieleza yule mwanafunzi huku akionyesha uhakika kabisa machoni pake.
Nilimweleza kuwa nimechapwa akakataa katakata nikanyoosha mkono wangu ili aone kuwa ni kweli nimechapwa.
Mama yangu!! Mkono wangu ulikuwa umevimba na kuna mchirizi wa damu iliyovilia ilionekana ndani kwa ndani.
Sio mimi tu niliyeshtuka hata yule mwanafunzi alishtuka, kushtuka kwake kukawashtua na watu wengine, watu waliponizunguka kwa akili ya utoto nikaona lililonikuta ni balaa nikaanza kulia. Wakanipooza.
Sasa yakaanza maumivu kunitambaa.
Nikajaribu kuyazoea lakini haikuwezekana, nilipojaribu kushika kalamu sikuweza kabisa, mkono ulikuwa unauma sana.
Mwalimu wa hisabati alipoingia darasani na kuanza kuandika ubaoni mimi sikuweza kabisa kuandika, alipogeuka nilinyoosha mkono akanifuata, nikamweleza mkono unaniuma sana siwezi kuandika.
“Wewe Ngomeni wewe mbona unakuwa kahuni wakati bado kadogo, si ulitoroka wewe hata haujachapwa nikakuona nikajikausha tu.. sasa nini kinakuuma tena…..” mwalimu alisema huku akicheka na kusababisha darasa liangue kicheko.
Kasoro mimi tu ambaye kwa macho yangu nilishuhudia nikichapwa. Nilichapwa na mwalimu mgeni tena ni mwanamke na alinichapa mkononi.
Nikamkatalia mwalimu na kumweleza kuwa kuna mwalimu mgeni alinichapa ila alinichapa bakora moja tu mkononi.
“Ona sasa huyu naye, waalimu wote hakuna hata mmoja aliyemchapa mtoto wa kiume mkononi we Ngomeni wewe uongo sio mzuri sawa mwanangu!! Kwanza hakuna mwalimu mgeni hapa shulenikwetu” alinieleza kiupole. Akionekana kabisa kuwa katika kunisihi.
“Mwalimu nimechapwa na madam mgeni, mimi sio muongo hata kidogo…naapa mwalimu” nilimkatalia.
“Haya baada ya kipindi utanifuata ofisini!!” alinieleza kisha akaendelea kufundisha.
ITAENDELEA
Mama’ke Mama Sehemu ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;