Mama’ke Mama Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA
********************************************************************************
Simulizi: Mama’ke Mama
Sehemu ya Nne (4)
Sasa maji yale mithiri ya damu yalikuwa yamenifikia magotini ndipo yule kikongwe akazungumza.
“Jitahidi sana uogelee kwa bidii zako, ukithubutu kuyameza haya maji utakuwa ni mwisho wako, utakufa kwa uchungu sana kwa sababu umeitwa kwa hiari yako unaleta ujanja ujanja….” alizungumza vile na kama kawaida yake aliendelea kunicheka.
Mvua ilizidi kuongezeka, nilikuwa nimeuziba mdomo wangu ili nisije kumeza yale maji kama alivyonionya yule kikongwe.
Hayawi hayawi hatimaye maji yalikuwa shingoni, sasa nikalazimika kuogelea katika lile dimbwi la maji, nilikata maji kwa kutapatapa lakini yule kikongwe yeye alikuwa amesimama tu.. yaani ni kama alikuwa anazidi kurefuka kadri maji yale yalivyokuwa yanaongezeka.
Nilipiga mbizi mpaka nikaisikia mikono ikiwa imeshika ganzi na hapo nikasalimu amri nikijisemea na liwalo na liwe.
Nikaacha kupiga mbizi nikasubiri kifo kama alivyokuwa ameniahidi. Kifo cha uchungu mkali.
Nilipoacha kupiga mbizi maji yale yakakauka na nikajikuta katika ardhi kavu kabisa isiyokuwa na hata dalili ya kulowana. Nikajiuliza ile mvua ilikuwa imetokea kweli ama nilikuwa naota, lakini nilipojigusa nguo zangu zilikuwa zimelowana sana.
Na nilihisi muwasho na harufu ya damu.
“Mkuu nimeufikisha ujumbe uliokuwa unauhitaji…” mara nikaisikia sauti nyuma yangu, ilikuwa sauti ya mwanamke.
Sikuwa na haja ya kugeuka kwa sababu nilishatambua kuwa alikuwa ni yule kikongwe, nikatazama ni nani anayeambiwa vile. Sikuona mtu yeyote yule zaidi ya kuisikia sauti ikinikaribisha katika ufalme aliouita ufalme wa pepo.
Wakati sauti ile ikinisifia na kunikarimu yule kikongwe aliinama na kuninong’oneza kuwa kila nitakaloulizwa nikubali, la si hivyo nitauwawa kifo kibaya sana.
Nilitishika sana lakini nililazimika kutii, kweli kila nilichoulizwa nilikubaliana nacho kwa kutikisa kichwa.
Sikujua nilikuwa najiingiza katika jambo zito nisilolijua.
Baada ya kukubali kila kitu nilishtuka kutoka katika usingizi, nilikuwa kitandani kwangu. Jasho likinitoka huku nikiwa natetemeka sana. Niliketi kitako na kujiuliza ile ilikuwa ndoto ya aina gani. Ndoto ya kutisha vibaya mno, nilijaribu kujipapasa huku na kule, kwa mbali niliihisi ile harufu ya majimaji yanayofanana na damu niliyoota nikiwa naogelea.
Nilikurupuka na kuwasha taa, nikatazama saa ilikuwa ni saa nane na nusu usiku, niliitafakari siku yangu nzima ilivyokuwa kuanzia asubuhi hadi inakwisha, kuna baadhi ya matukio ambayo sikuweza kuyakumbuka kwa ufasaha kabisa, ni kama kuna mambo yalitokea katika siku yangu na kisha yakafutika katika ubongo wangu.
Nilishindwa kulala kabisa usiku huo!! Nilijiuliza sana juu ya lolote lile lililotokea, nilijiaminisha kuwa nimeota ndoto ndefu sana inayohusisha ujio wa Jasmini nyumbani kwangu kisha ikawa maluweluwe ya kutokea mtu mwingine ambaye aliiharibu kabisa siku yangu.
Nikajaribu kulala, nikakumbuka tukio la mimi kwenda sokoni, nikajiuliza kama ile nayo ni ndoto basi sitakuta kitu chochote kinachohusisha manunuzi yale ya sokoni. Nikajitia ujasiri nikasimama tena nikaenda upande wa pili wa pazia yangu, nikajikuta nashusha pumzi zangu kwa nguvu sana. Hapakuwa na kitu chochote kilichonunuliwa kutoka sokoni hivyo basi hii ilimaanisha kuwa yote yaliyotokea ilikuwa ni ndoto tupu hapakuwa na uhalisia wowote.
Ghafla! Harufu ikakutana na pua zangu.
Harufu ya uozo.
Nikazinusa nguo zangu, harufu pekee ilikuwa harufu ya damu kwa mbali ambayo sasa nilianza kuipuuzia.
Uozo unatoka wapi?
Nikajaribu kupekua huku na kule. Huenda ni panya amefia sehemu fulani ndani ya nyumba yangu.
Harufu gani ya ghafla kiasi kile sikuweza kuibaini mchana kutwa? Nilijiulizaq huku nikiendelea na msako.
Nikauona mfuko wa plastiki. Nikaufunua…
Uozo!!
Nyanya, vitunguu, karoti, nyanya chungu pamoja na hoho. Vyote vimeoza.
“Jamani, hivi si nilinunua…” nikasita. Hapo sasa nikakumbuka kuwa safari ya sokoni haikuwa ndoto. Nilienda sokoni.
Nilinunua mahitaji kwa ajili ya kupikiwa na mchumba wangu Jasmin.
Nikiwa najiona dhahiri nikiupoteza ujasiri ndani ya chumba changu, nikalisogelea sufuria ambalo lilikuwa mkabala na kile kifuko kilichobeba uozo.
Nililifunua huku hofu ikizidisha makazi ya kudumu katika moyo wangu.
Ngomeni mimi nilikuwa nimepatikana.
Waaa! Likafunuka.
Harufu kali ikatapakaa na kuzifikia pua zangu.
Nyama ile ilikuwa imeoza kiasi kwamba ilikuwa inatoa wadudu aina ya funza.
Nilipagawa!
Nilie? Namlilia nani?
Nikimbie? Nakimbilia wapi?
Nilijaribu kujiweka sawa lakini wapi? Nilibaki kujiongopea tu. Nilikuwa natetemeka sana.
Nyama na viungo vyote vimeoza angali nilivinunua ndani ya masaa kadhaa yaliyopita.
Usingizi uligoma, kila kilichonigusa nilikuwa nashtuka. Sikuzima taa wala sikuweza kujifunika shuka.
Niliamini kuwa sitaweza kupata usingizi, na haikuwa nia yangu kusinzia.
Kwa raha na amani ipi katika moyo wangu?
Tofauti na matazamio. Nilisombwa na usingizi, sasa na dakika nisiyoikumbuka.
__
Siku iliyofuata asubuhi majira ya saa nne ndipo nilishtuka kutoka usingizini, nilihisi viungo vyangu vikiwa vinauma sana. Na nikatambua kuwa nilikuwa nimelala kwa muda mrefu kupita kawaida yangu ya kudamka mapema sana kufanya mazoezi ya viungo kisha kuingia katika harakati zangu za siku zote.
Ilikuwa imetimu saa nne asubuhi.
Upesi nikakurupuka na kufunua pazia linalotenganisha kitanda changu na pahali pa kuitwa jiko na sebule.
Labda nilikuwa naota?
Hiki ndicho nilichojiuliza huku nikilazimisha jibu liwe ndiyo.
Haikuwa!
Vile viungo na mboga yenyewe, hakika vilikuwa vimeoza na kunuka.
Funza wakifanya riaria ya hapa na pale ndani ya chumba changu.
Hofu ikaanza upya.
Nikiwa katika kutojiamini, nikaufungua mlango na kutoka nje. Nilikuwa nakiogopa chumba ambacho kilikuwa paradise yangu siku za nyuma.
Nini hiki?
Nikiwa bado katika tafakari ile, mara akapita jirani yangu mmoja tusiyekuwa na ukaribu sana zaidi ya ujirani, akanisalimia huku akiniuliza habari za kupotea.
Nilishangaa lakini nikahisi ni ulimi tu uliokosa mfupa ulikuwa umepitiwa nikamjibu kuwa ni njema ni tu.
“Anauliza habari za kupotea wakati nilikuwa nimeonana naye siku iliyopita tu. Au nd’o yale ya habari za jioni kuulizwa asubuhi kimakosa?”
Nikapuuzia salamu ile!!
Mwili wangu uliotota katika uchovu ulihitaji walau maji niweze kuupata uchangamfu.
Nilipata faraja kuwa bafu la chumba nilichopanga lilikuwa nje. Nikaingia upesi na kuchukua ndoo moja. Nikajikokota kuelekea kuchota maji. Mitaa miwili kutoka nilipokuwa nimepanga.
Huko napo, nikakutana na mwanadada mmoja ambaye alikuwa ni muuza vitumbua na mara kwa mara nilikuwa nikienda kununua vitumbua kwake ama la!, hunipitishia nyumbani kwangu. Na yeye akanisalimia huku akiniuliza habari za kuhadimika.
“Tuwe tunaangana kaka, si unajua tena haya maisha tunaweza kuwa tunalindiana hata nyumba.” Alizungumza kwa uchangamfu.
Huyu sasa nikapatwa na kigugumizi katika kumjibu. Isingewezekana watu wawili watumbukie katika kosa lilelile.
Tena huyu! Hata siku mbili hazikuwa zimekatika tangu ninunue vitumbua kwake.
Nimehadimikaje sasa! Nilijiuliza.
Nilijilazimisha kutabasamu huku nikiamini kuwa na huyu naye amepitiwa.
Nikachota maji na kuondoka zangu, nikamfikiria huyu dada na yule jirani yangu! Lakini katu sikusahau kufikiria juu ya kizaazaa cha uozo kilichokuwa ndani ya nyumba.
Hawa watu vipi? Nilijiuliza.
Nilipofika nyumbani nilikuta kuna ugeni, wageni wale walikuwa wageni kabisa machoni kwangu, alikuwa ni mwanamke mmoja na wanaume wawili.
Waliponiona kwa mbali niliona yule mwanamke akinyoosha kidole kunielekea mimi.
Nilijitoa hofu kuwa sikuwa na tatizo lolote na mtu…… hivyo nilijongea na ndoo yangu mkononi hadi nikawafikia.
“Karibuni jamani.. shkamooni!!” niliwakaribisha na kuwasalimia.
Mwanamke pekee ndiye aliyenijibu lakini wale wanaume wawili watu wazima hawakujibu. Ni kama watu waliokuwa wanaisubiri shari ilipuke washangilie.
“Samahani wewe ndiye Ngomeni?” aliniuliza mwanamke yule, nikakubali kuwa ni mimi hawajakosea. Sura ya muulizaji haikuwa ngeni sana, lakini sikukumbuka pahala tulipokutana.
Nilipokubali kuwa ujio wao haujapotea njia, wale wanaume wakaonyesha jazba yao waziwazi.
“Kaka eeh! Sikia, hii ni wiki ya tatu tunakuja hapa kukutafuta bila mafanikio…sasa leo tumekupata yaani..” alizungumza kisha akasita nikagundua kuwa anajaribu kukabiliana na hasira iliyokuwa inamtawala.
“Wiki? Mbona… mhh! Ujue sielewi.. mimi nipo hapa kila siku jamani..” niliwajibu huku nikikumbwa na mshangao. Na hapo kichwani kwangu zikarejea kumbukumbu za kuulizwa habari za siku nyingi na za kuhadimika.
Kikazuka kizaazaa!
Baadaye sana nilimuuliza Mariam hiyo inawezekana vipi, fisi kukimbia kwa kasi vile bila kusababisha ajali wakati kuna watu barabarani?
Mariam akanieleza wale wote ninaowaona ni aidha watu ambao wameshikwa kimadawa na wanatembezwa bila wao kujua ama ni wachawi wengine kazini. Nikakumbuka niliwahi kuzisikia simulizi za wale watu ambao huota ndoto usiku na kujikuta wanafungua mlango na kutoka nje wakiwa wamefumba macho.
Kumbe sio ndoto za kawaida, bali wanakuwa wameitwa kichawi.
“Ngomeni, sio kila mchawi anaweza kumuona mchawi… inategemea una nguvu kiasi gani…. Mfano bibi yako ni hatari sana…. Anaona mno! Ni ngumu kumlaghai yule, hata sisi tumeamua tu kujilipua.”
KILE Kitendo cha mimi kukimbia ni kama kilihalalisha viumbe wale kutambua kuwa mimi nina ugeni katika ile sayari yao hivyo wakaanza kunifuata kwa kasi nikiwa sijui ni lipi lengo lao. Sijui hata ni nani aliwaamuru!
Kwa jinsi walivyonifuata kwa wingi nilijikuta hata Mariam simuoni tena, nikayakumbuka maneno yake alisema kwamba nikifanya kosa mimi na yeye tutakufa, sasa sikujua kama tayari alikuwa ameuwawa ama vipi.
Nikabaki kujipigania mimi kama mimi katika ulimwengu wa kiza.
Nilizidi kukimbia nikivuka makaburi yenye misalaba na yasiyokuwa na misalaba mbele yangu, nilikuwa sijui ni wapi ninaelekea na wakati huo wale viumbe wakizidi kunikimbiza, huku wanaunguruma.
Walikuwa wanatisha sana kuwatazama, walikuwa ni wanadamu lakini ni kama akili zao zilikuwa zimewaruka tayari, walikuwa na nywele ndefu na miili yao ilikuwa michafu. Wachache wakiwa na viungo kamili, wengi wakikosa baadhi ya viungo hususani mikono na miguu.
Kadri nilivyozidi kukimbia nilizidi kwenda porini na mara ardhi ilianza kuwa na unyevu unyevu, sikuwa na uwezo wa kusimama ili kujiuliza niliendelea kukimbia, kiumbe mmoja aliyekuwa anakimbia kwa kasi kubwa sana hatimaye alinifikia akanirukia, ilikuwa bahati yangu nikawa nimemzidi hatua moja mbele.. akaishia kunidaka shati langu huku akianguka chini, shati likachanika nikabaki kifua wazi nikaendelea kukimbia kuelekea katika uelekeo nisioujua.
Nilikuwa nalia kama mtoto, nilikuwa naomba msamaha lakini hakuna nilichojibiwa.
Ardhi nayo, ikazidi kuwa matope, sasa uwezo wa kukimbia kwa kasi ukapungua nikawa nazama katika matope na kuibuka.
Hii sasa haikuwa ndoto!
Nikakiona kifo kikinimendea, kadri nilivyozidi kwenda mbele matope nayo yalizidi kuongezeka kina chake kuelekea chini.
Nilipogeuka nyuma wale viumbe walikuwa wametoweka… hakuwepo kiumbe hata mmoja… nilikuwa peke yangu katika eneo hili linalotisha sana.
Eneo likiwa na ukimya, zikisikika sauti za ndege na mivumo ya miti.
Hapo sasa nikaanza kurudi kinyume nyume ili nisiendelee kuzama katika tope, nilifanikiwa kunyayua mguu wangu wa kulia lakini nilipojaribu kunyanyua mguu wa kushoto haikuwezekana.
Mguu ulikuwa mzito.
Nilivuta kwa nguvu nikagundua kuwa nilikuwa nimenasa katika kitu yawezekana ni mzizi ama chochote kile, nikavuta kwa nguvu sana lakini mguu ulikuwa unanyanyuka kidogo kisha unarudishwa kwa kasi.
Wakati nafikiria kuhusu ule mguu mmoja ulionasa, nikahisi kitu. Nikalazimika kutulia ili nipate uhakika.
Kweli! Kulikuwa na kiumbe hai katika lile tope kikiupapasa mguu wangu mwingine.
Nikajaribu kutapatapa huku napiga kelele. Kile kiumbe hai ndani ya tope kikanishika vyema.
Safari hii miguu yote miwili ilikuwa imekamatwa, huku ikivutwa kwenda chini zaidi katika lile tope.
Najirusha huku na kule, kiumbe hakiniachii. Tope linanuka sana name nazidi kudidimizwa.
Tope likafika kiunoni, kelele hazitoki koo limekauka.
“Niachiee, Niachie.” Ni kama nilikuwa najisemesha.
Mikono miwili yenye nguvu inazidi kunizamisha chini.
Tope kifuani. Kile kiumbe kikajiimarisha, kikahamisha mikono kutoka katika miguu na kuipandisha katika mapaja.
Kama huwa kuna hisia za kufakufa, huenda hizo ndo nilizokuwa nazo kwa wakati ule.
Sikuweza kutulia zaidi, nikaingiza nami mikono yangu katika lile tope, liwalo na liwe.
Nikaanza kuitoa ile mikono iliyonishika mapaja, nikawa naifinya, naipigapiga.
Mmoja ukaachia, nikawa narusha miguu, natukana matusi, natoa vitisho, mara namuita Mungu!
Yote ni katika kuutimiza ule usemi wa mfa maji…
Kikaachia mkono wa pili, nikaanza kutapatapa nijitoe katika yale matope. Naanguka uso ukiyasalimia yale matope, napiga kelele naendelea kutapatapa.
Nikatoka katika lile tope.
Nikabai pembeni nikihema juu juu, nikaisikia michakato katika lile tope. Nguvu zikanijia tena, nikaanza kukimbia.
Hofu ilikuwa imenitanda!!!
Nililiona kwa mbali kundi la watu, ulikuwa ni kama mji. Nikaufuata kwa tahadhari kubwa.
Kadri nilivyozidi kuusogelea nikaanza kuutambua. Ulilikuwa ni eneo nililokuwa nalifahamu.
Eneo ambalo huwa inafanyika gulio la kijiji chetu.
Na palikuwa na gulio.
Nikajitazama, tope limeniganda.
Nikajaribu kujifuta ilimradi tu, nisingeweza kutakata.
Nikaanza kukutana na watu. Nikiwa nimejiandaa kutomjibu mtu yeyote ambaye ataniuliza juu ya masaibu yaliyonikuta.
Hapa sasa nikakiri kuwa kuna wanadamu wana uwezo wa ajabu sana… wapo kinyume na matakwa na Mungu lakini mambo wanayoyafanya ukihadithiwa unaweza kukataa. Mpaka siku yanakutokea, hautapata nafasi ya kuwaomba radhi wale uliowaletea ubishi walipokusimulia.
Mimi nakusimulia! Ni uamuzi wako, kuniamini leo, ama kusubiri yakutembelee uamini kivyako.
Nilikuwa nawafahamu watu wengi niliokuwa nakutana nao, lakini ajabu sasa kila nilipotaka kuwaita majina nilikuta nayasahau majina yao… waliendelea na shughuli zao kuingia na kutoka mimi nikiwatazama tu.
Wengine walinipita kwa karibu kabisa, najiandaa kuwasalimia. Hawajali wananiacha hapo.
Kuna mmoja niliamua kumzibia njia kabisa, aliponifikia akanigonga kama hanioni. Kisha akayumbayumba akaanguka chini.
Akageuka nyuma na kutazama chini, ni kama mtu aliyejikwaa bahati mbaya katika ubovu wa ardhi.
Ina maana hawanioni!!
Nilistaajabu.
Nilijiuliza kwenda nyumbani kwangu lakini mwili ukawa mzito. Akili inaniambia nenda,mwili umefungwa kamba, hakuna kwenda.
Hadi gulio linamalizika mimi nilikuwa nazurura na sikuwa na maamuzi.
Nikabaki tena peke yangu.
Taratibu eneo lile la gulio likaanza kuingiliwa na wakazi wapya. Wakitanguliwa na wanama mbalimbali, paka na fisi wakiongoza katika orodha.
Nikarejea tena katika maisha yamashaka.
Nimejificha nyuma ya mti natazama yanayoendelea. Nikaliona tukio lililonikumbusha enzi ninasoma shule ya msingi.
Mwalimu akituagiza kukusanya vifuniko vya soda kwa ajili ya kujifunza somo la hesabu. Wanafunzi tulikutana katika kumbi za starehe, kila mmoja akiwania kuokota vifuniko vya soda kwa wingi.
Hawa walikuwa ni watu wazima, wakiwania kuokota alama za unyayo katika ile ardhi.
Sijui hata waikuwa wanazibagua vipi, sikuelewa walihitaji nyayo za nani na zipi hawakuhitaji.
Kuna sehemu walifikia hatua ya kukwidana, kisa fulani aliwahi alama ya unyayo ambayo mwenzake aliiwahi pia.
Hatimaye na hawa wakaondoka, nikabaki peke yangu. Kiu na njaa vikanikumbuka……
Ningepata wapi chakula na maji hili lilikuwa swali gumu sana.
Ndugu msikilizaji usiombe akili yako ikashikwa na watu hawa wabaya wanakufanya watakavyo, wakati wewe unajiona ni mjanja sana wao wanakuona mpumbavu na unakuwa unawafurahisha…..
Nilianza kuzurura kutafuta maji, kiu na njaa vilikuwa vinanisumbua…..
Sikufanikiwa hadi mwanga uliporejea, nikatembea hadi katika ule mji tena niliokuwa naufahamu, lengo langu likiwa moja tu… kuhakikisha nakutana na mtu ambaye namfahamu na kumueleza kile kilichokuwa kinanikabili. Safari hii nilijiahidi nikimuona mtu ninayemfahamu hata kama sio kwa jina, namkaba kwa nguvu mpaka anisikilize.
Mwili wangu ulikuwa unawasha sana na kunuka…. Nilikuwa ninazo siku kadhaa bila kuoga. Lile tope bado likiendelea kuning’ang’ania.
Nilipoufikia mji ule hakuna aliyejishughulisha na mimi, kwa saa zima nilikuwa nashangaa tu, kila ninayemsemesha ananitazama bila kunijibu anaondoka zake.
Sijui walikuwa wanaonana nini?
Nilimfikia mtu mmoja, alikuwa makamo yangu huyu nilipomsemesha alinijibu.
Sikuamini, nikashukuru sana kuwa hatimaye shida zangu zitatatuliwa.
Nikamueleza kuwa nina kiu na njaa kali.
Akanitazama, kisha akainama na kufungua deli lililokuwa mbele yake.
ITAENDELEA
Mama’ke Mama Sehemu ya Tano
Also, read other stories from SIMULIZI;