Mama’ke Mama Sehemu ya Pili
IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA
********************************************************************************
Simulizi: Mama’ke Mama
Sehemu ya Pili (2)
Baada ya kipindi nikaondoka naye nikimbebea boksi la chaki.
Tulifika hadi ofisi ya waalimu akanisimamisha katikati.
“Huyu mtoto ameshindwa kuandika leo darasani anadai kuna mwalimu wa kike amemchapa kiboko kimoja sasa mkono umevilia damu na unamuuma sana… haya Ngomeni ni mwalimu gani kati yetu hapa….nikigundua unanidanganya nitakupa adhabu kali sana. Sitaki kabisa watotyo kuwa waongo” Mwalimu wa hisabati alizungumza na kunitupia mpira.
Niliangaza huku na kule kama nitamuona yule mwalimu lakini ajabu sikumuona wala kumfananisha kati ya wale waliokuwa pale.
“Ni mwalimu mgeni kabisa, aliniita akanichapa kiboko kimoja!!” nilizungumza huku nikishangaa.
“Ngomeni mwanangu, hapa hatunaye mwalimu mgeni hata mmoja mbona. Hebu sema ukweli huo mkono umeufanya nini… sema kama uliruka sarakasi ukastuka au umejichoma na mwiba….” alizidi kunisihi.
Nikajikuta nalia nikishindwa kuongea kabisa, mwalimu mmoja wa kike akafika na kunikumbatia begani… akauchukua mkono wangu na kuutazama.
“Jamani waalimu hii ni fimbo aliyochapwa huyu mtoto wala sio mwimba au mkono kuteguka hebu njooni muone… aliwaita ambao walikuwa hawajaniona akawaonyesha na wao wakakiri kweli ni fimbo.
“Sasa kama hayupo aliyemchapa hii bakora ina maana amechapwa na shetani au?” Mwalimu mmoja wa kiume alihoji huku akiwa katika mshangao.
Maumivu ya mkono nayo yalizidi kunisumbua. Mwalimu mmoja akaingia katika ofisi nyingine na kuchukua dawa ya kuchukua akanichua, lakini sikuipata nafuu yoyote.
Mkono ulikuwa unauma, maumivu ya mkono yakaanza kusambaa hadi kichwani, kichwa kikaanza kuuma sana, na hatimaye yakawa maumivu ya mwili mzima…..
Ikawa ni homa!!!
Siku zikazidi kwenda mbele, siwezi kuandika na mwili unauma, hadi ikafikia siku ya kufanya mtihani nikaishia kuuona hivihivi mtihani. Mkono haushiki kalamu kabisa kama ni hospitali walikuwa wamenipeleka lakini hakuna kilichosaidia kabisa.
Mitihani mitatu ya kwanza ikapita…. mitihani ya siku ya pili ikapita nikiwa mtu wa kulala tu na kulia.
Siku ya tatu na ya mwisho ya kufanya mitihani nikaamka nikiwa ninayo alama ya damu kuvilia lakini mkono wangu ukiwa na nguvu sana na imara!
Niliweza kushika kalamu na kufanya lolote lile ambalo nilikuwa siwezi kufanya siku za nyuma.
Nikafanya mitihani ya siku hiyo!!
Mwalimu mkuu msaidizi ambaye alikuwa mwanamke baada ya hali yangu kuwa njema aliniita na kuniambia kuwa napewa ruhusa ya kurejea nyumbani na huko niende nikamueleze mama yangu kila kitu juu ya kila kilichonitokea shuleni.
Hakuongeza neno katika kauli zake badala yake alinisihi sana nisimfiche kitu chochote kile!!
Sikuelewa kwanini alinisisitiza sana juu ya kumweleza mama kila kitu.
Huu ukawa mwanzo wa kumchanganya mama yangu mzazi!!
Lakini ningefanya nini kwa sababu ilibidi tu nifanye hivyo!!
Mwalimu mkuu msaidizi ambaye alikuwa mwanamke baada ya hali yangu kuwa njema aliniita na kuniambia kuwa napewa ruhusa ya kurejea nyumbani na huko niende nikamueleze mama yangu kila kitu juu ya kila kilichonitokea shuleni.
Hakuongeza neno katika kauli zake badala yake alinisihi sabna nisimfiche kitu chochote kile!!
Huu ukawa mwanzo wa kumchanganya mama yangu mzazi!!
Lakini ningefanya nini kwa sababu ilibidi tu nifanye hivyo!!
Mwalimu alinipatia wanafunzi wawili waliokuwa kidato kimoja juu yangu na hata kiumri walikuwa wakinizidi mbali. Hawa walipewa jukumu la kunifikisha nyumbani salama. Utaratibu huu wa mwanafunzi kusindikizwa nyumbani ulikuwa ni utaratibu maalumu kabisa pale shuleni pindi mwanafunzi mmoja anapokuwa katika matatizo.
Kweli walinifikisha nyumbani na kunikabidhi kwa mama yangu mzazi niliyemkuta akiwa anafua nguo!
Mama alistaajabu kuniona nyumbani wakati ule lakini wale vijana walizungumza naye na kumtoa hofu, kisha wakaaga na kuondoka.
Kitu cha kwanza mama aliniuliza nini kimetokea na mimi kama nilivyoelezwa na yule mwalimu mkuu msaidizi. Nikalazimika kuelezea kwa tuo.
Ujue akili ya utoto safi sana ulichoagizwa unakieleza kama kilivyo, nikamueleza mama kuanzia kuchelewa namba. Kuchapwa na mwalimu hadi mauzauza yote ya mkononi yaliyojitokeza.
Tofauti na awali nilipomueleza mama juu ya kuingiwa na mdudu sikioni, siku hii mama alitilia maanani zaidi.
Na kile kitendo cha kuagizwa kumueleza kila kilichonitokea kilileta uzito zaidi.
Mama akaniambia nipumzike kwanza ndani tutazungumza baadaye, lakini nikiwa na akili zangu nilipatwa hofu kwa mambo yaliyoendelea, mama aliacha kufua ghafla. Na hakuwa na utulivu kabisa. Namjua vyema mama yangu, akiwa sawa najua akivurugwa najua vyema.
Nikiwa naingia ndani akaniita tena.
“Umesema huyo mwalimu aliyekuchapa alikuwa amevaaje?” aliniuliza huku akionekana kutetemeka waziwazi.
“Alikuwa amevaa sketi nyekundu na blauzi kama nyeupe hivi na kichwani ana nywele fupi tu……” nilimjibu.
“Je viatu unaweza kuvikumbuka……” mama akaniuliza.
Hapo sasa mapigo yangu ya moyo yakapiga maradufu, kuna kitu nilikiona na kukipuuzia na kisha akili yangu ikasahau. Hata nilipokuwa nawasimulia waalimu juu ya kilichojiri sikukumbuka kipande kile.
Mwalimu yule alikuwa peku!
“Ngomeni… we Ngomeni,… niambie alikuwa amevaaje miguuni!!” mama alikazia baada ya kuona nimeshtushwa na hata nisiseme lolote.
Nilimjibu kuwa yule mwalimu hakuwa na viatu miguuni.
Hapo sasa mama akaifungua kanga yake na kujifunga upya kiunoni. Nilimsikia akilalamika kikabila sikuambulia maana ya maneno aliyokuwa anasema lakini nilijua analalamika. Hapo awali nilikueleza kuwa nilizaliwa mjini hivyo sikuwa naelewa sana kabila langu.
Nakusihi nawe unayenisikiliza jitahidi kujua walau kwa asilimia hamsini tu juu ya kabila lako. Ipo siku utaujua umuhimu wa kulijua kabila lako.
Aliondoka bila kuniaga sikujua alipoenda, na hakurejea siku hiyo hadi aliporudi siku iliyofuata na taarifa kuwa baba yetu mzazi alikufa akiwa safarini huko Dodoma amekutwa ametupwa mtaroni. Hana jeraha lolote lile.
Ilikuwa taarifa nzito sana hakika, ikabidi msiba ukae pale nyumbani.
Kuna baadhi ya ndugu walikuwa wanaishi Dodoma wakashauri baba azikwe huko. Hali ya uchumi haikuwa nzuri sana nyumbani ikalazimika mama na kaka yangu waende msibani mimi na mdogo wangu tukabaki pamoja na mama yetu mdogo.
Japokuwa nilikuwa mdogo nilikuwa naielewa vyema maana ya msiba.
Niliumia sana.
Ni kweli baba yetu hakuwa mtu anayeijali sana familia yake. Lakini hii haibadili hata nukta ya yeye kuwa baba pekee wa familia ile kwa uhalali.
Baada ya siku takribani kumi mama alirejea nyumbani akiwa amenyoa nywele zake ishara ya ujane. Alikuwa yu mpole sana na hapo mi nikiwa najiuliza mama alikuwa ana maana gani kuniulizia juu ya yule mwalimu, ina maana alikuwa amewahi kumuona ama?
Mama alituita familia nzima kwa ujumla na kutuelezea kuwa kifo cha baba yetu ni mipango ya Mungu tu na tusimsikilize na kumuamini mtu atakayetwambia vinginevyo. Alijaribu kurejea vifungu kadhaa vya maandiko matakatifu kwa ajili ya kutuimarisha katika imani.
Neno la mama likawa neno lililoaminika zaidi.
Mama amesema!!
Na baada ya hapo akatupatia picha kadhaa walizopigwa huko Dodoma msibani ikiwa ni pamoja na santuli (CD) ya siku ya maziko.
Tulizitazama zile picha zote kwa utulivu, picha zilizoleta msiba upya pale nyumbani. Kuwaona akina mama wadogo, shangazi na wengineo wakiweka shada za maua juu ya kaburi alilozikwa baba. Ilitonesha sana.
Hapakuwa na namna ya kubadilisha maana ya kile kilichotokea!
Mama naye alituruhusu tulie kwa uchungu ili kuzipa ahueni nafsi zetu.
Nakumbuka siku kama nne baada ya mama kurejea nikiwa na mdogo wangu sebuleni niliikumbuka CD aliyokuja nayo mama, nikaiweka katika deki tukaanza kuitazama mimi na mdogo wangu, haikutuumiza sana kuona jeneza lililombeba baba ujue utoto nawe ushawahi kuwa mtoto nadhani unaelewa!! Tulishalia mara moja siku ya kuziona picha. Sasa hatukulia tena.
Wakati tukiendelea kutazama ile CD mara ukafika wakati wa kuaga mwili wa marehemu.
Ni hapo ambapo nilikutana na kisanga cha kutisha.
Alianza mdogo wangu tukawa tunashindana kumtafuta mama atakayekuwa wa kwanza kumuona anamfinya mwenzake, hivyo kila mmoja alikuwa makini kutazama katika luninga. Naukumbuka utoto kuna muda nautamani tena. Lakini kamwe hautarudi!
Nikiwa makini kabisa kuwatazama watu wanaoaga mara ghafla macho yangu yakakutana na mtu niliyewahi kumuona hapo awali, alikuwa amevaa nguo zilezile juu hadi chini.
Alikuwa katika msafara wa watu wanaoenda kuaga mwili wa marehemu baba yangu.
Alikuwa ni nani yule? Nilijiuliza hata nisipate jibu upesi.
Shangazi? Hapana
Ma’mdogo Samira? Hapana.
Ma’mkubwa Suzy? Siye?
Paaah! Moyo ukapiga kwa nguvu sana. Nilikuwa nimemkumbuka.
Alikuwa ni mwalimu aliyenichapa siku ile na kunizulia balaa katika mkono wangu.
Balaa lililosababisha nikashindwa kufanya mitiahani yangu. Sasa nipo nyumbani.
Nilijikuta napiga kelele kubwa sana za hofu, kelele zilizomfikia mama chumbani nikamsikia akituonya kuwa tukacheze nje lakini mimi niliendelea kupiga mayowe.
Hatimaye mama alikuja akiwa mwenye hasira, alipokuja nilimkimbilia na kumkumbatia kwa nguvu, hapo sasa ghadhabu zikamwisha akaingia katika uoga akiniuliza nimekumbwa na nini.
Nikamweleza mama kuwa nimemuona yule mwalimu akiwa anaenda kuaga mwili wa baba….
Mama alikataa katakata, nikamsisitiza kuwa nimemuona katika ile CD aliyoileta.
Mama akaketi pamoja na mimi kuitazama ile CD kwa umakini ili na yeye awe shuhuda wa kile nilichokuwa nakisema.
Ndugu msikilizaji kama hujawahi kukutana na maluweluwe basi omba sana yasije yakakosea njia yakakutana na wewe.
Ninachokusimulia ndicho kilichojiri.
CD ilionyesha vizuri kabisa kuanzia mwanzo, ajabu sasa ilipofikia sehemu ya kuaga ilisikika sauti tu hakuna picha iliyoonekana hadi watu wanamaliza kuaga.
Mama akaanza kutokwa jasho!!
“Mwanangu huyo mwalimu ndiye aliyemuua baba yenu. Ni huyooo” mama aliniambia huku akiwa anatetemeka sana. Kauli ya mama iliniacha hoi lakini mama akatulia na kunisimulia,
Alinieleza kuwa baba akiwa Dodoma alimpigia simu na kumueleza kuwa amekaa siti moja na dada mmoja ananukia marashi makali ambayo yamemsababisha kichwa kimuume sana. Akaelezea muonekano wa huyo dada na muonekano huo ni sawa kabisa na muonekano wa mwalimu wa maajabu aliyenichapa na kuniletea hitilafu kubwa katika mwili wangu.
Mama akakamilisha simulizi yake kwa kunieleza kuwa mwanadada huyo hakuwa na viatu miguuni, sasa inakuwaje wafanane kila kitu?
Bila shaka huyu ni mtu mmoja……
Anataka nini sasa katika familia yetu??
Hili lilikuwa swali la muhimu sana mbalo jibu lake halikuwa hadharani!!!
Mama akaniambia kuwa yatupasa tusafiri hadi kijijini tukamueleze babu yangu ambaye ni baba yake marehemu baba juu ya huu utata. Kwa sababu yeye ni mtu mzima basi anaweza kujua ni kitu gani cha kutushauri ama kutusaidia!!!
Ndugu msikilizaji ile ikawa mwanzo wa safari yangu ya misukosuko isiyokuwa na ahueni hata kidogo!!!
Siku iliyofuata alfajiri kabisa mama aliniamsha akaniandalia nguo za kuvaa na kisha safari ikafuatia.
Tulianza kutembea kwa miguu kwa mwendo kama wa dakika tano tukaifikia barabara. Tukasubiri gari kwa takribani nusu saa. Gari lilifika likiwa limejaa, mama akashauri tupande hivyohivyo, tukapanda na kujiunga na abiria wengine waliokuwa katika mbanano ule.
Njia ilikuwa mbaya sana kiasi kwamba nilikuwa namuonea huruma mama kila gari lilipokuwa linayumba alienda huku na kule hadi jasho likawa linamtoka.
Ndugu zanguni, sitaki kusema kuwa baba zetu hawana upendo kwetu lakini acha akinamama wapewe heshima yao kwa upana wa hali ya juu. Wanafanya mambo mengi sana kwa ajili yetu sisi watoto wao. Wanafanya hata ambayo hayajawahi kuwa katika ndoto zao.
Mama alikuwa anafanya yote haya kwa ajili yangu!
Ilikuwa safari ya masaa matano hadi kufikia kijijini, mama alikuwa yu hoi sana.
Tuliposhuka ilikuwa yapata saa sita za mchana, jua lilikuwa kali sana mama akaniuliza iwapo nilikuwa na njaa. Kweli nilikuwa nina njaa kali lakini nilisema kuwa sina njaa.
“We Ngomeni kuna kamwendo kwenda kwa babu yako, kama una njaa ni heri useme ule kabisa….” alinisihi mama yangu.
Nikakataa kwa mara nyingine. Safari ikaanza tena, mama alikuwa amechoka sana lakini hakutaka nijue, jasho lilikuwa linamtoka kwa wingi na nilimsikia akihema juu juu. Lakini hakunyanyua kinywa chake kulalamika kuwa amechoka.
Mungu wabariki akinamama hawa!
Wakati ule sikuwa na chuki kali juu ya wanadamu lakini ninapoyasimulia haya nikimkumbuka na mama yangu nawachukia sana wanadamu wa dunia ya giza, dunia ya kujifanya wao ni miungu watu!!
Tuliendelea kutembea hadi tulipouona mji wa babu, mama akanieleza kuwa hatimaye tumekaribia kufika.
Tulipiga hatua kama kumi hivi mama akalalamika kuwa kuna kimwiba kimemchoma, nakumbuka alisema kimwiba akimaanisha kidogo tu!
Akainama aweze kukitoa, alijaribu akiwa ameinama ikawa ngumu. Akasema ngoja atembee mbele zaidi akifika kwa babu atakitoa hicho kimwiba. Mimi nikawa mtazamaji tu na zaidi nikimpa pole.
Lakini hakuweza kupiga hata hatua tano, akadai anajisikia uchungu sana ngoja tu akae aweze kukitoa kile kimwiba ili aweze kuwa sawa. Mama akaketi, akatoa pini katika pindo la nguo yake, akaanza kujichokonoa ili aweze kujitoa hicho kimwiba.
“Ngomeni ujue nilisikia ni kimwiba kidogo ila naumia kweli, halafu naona weusi tu nakitoa hakitoki!!” mama alilalamika huku akitabasamu kumaanisha kuwa hata yeye anaona tukio lile kama ni mzaha tu.
Ikawa dakika mbili lakini hadi zinafika kumi mama hakuwa amefanikiwa kukitoa kimwiba kile.
“Ngomeni, kabla sijalalalmika huu mwiba hamna kitu chochote umesikia?” aliniuliza, sasa alikuwa ameacha kujishughulisha tena kuutoa ule mwiba. Na uso wake haukuwa na tabasamu tena.
Jasho lilikuwa likimtiririka mama yangu.
Nilifikiria kwa muda kidogo sikupata muafaka kabisa wa kitu gani cha tofauti nilikuwa nimekisikia.
“Hebu fikiria, fikiria kitu gani umekisikia mwanangu, huu sio mwiba hata sio mwiba huu… nakataa hakuna mwiba hapa mwanangu.” alisema mama, sasa hofu ilikuwa wazi katika macho yake.
Mama aliponisihi kuwa mtulivu nikatulia kweli na hapo nikakiri kweli kuna kitu cha tofauti nilikuwa nimekihisi.
“Mama nilisikia jotooo!!” nilimwambia.
Mama akapiga mayowe makubwa sana kabla hajanieleza kuwa kuna mtu anawaroga na anataka kuiangamiza familia yetu wote. Na lile joto nililohisi sio bahati mbaya, bali nilikuwa nimepishana na mchawi.
Nilikuwa mdogo lakini kuhusu wachawi nilikuwa nafahamu fika, haya mambo ya kishirikina hata shuleni tulikuwa tukihadithiana na kuna nyakati yalikuwa yakiwatokea baadhi ya wanafunzi.
Sasa nilikuwa nashuhudia kwangu.
“Ngomeni kimbia nenda kwa babu yako, nyumba ilee yenye bati ulizia mzee Uwele, mwambie upesi aje hapa siwezi kusimama Ngomeni mguu unawaka moto. Kimbia mwanangu kimbia na njia nzima mwambie Mungu awe na sisi mwambie Mungu hatutaki kufa kwa dhamira ya mwanadamu…mkatalie kabisa Mungu mwambie hatutakufa kwa hila zao.” mama alinisihi. Nikakimbia sana huku nikikumbuka kusema kama alivyonisihi. Nilimwambia Mungu awe na sisi.
Nilifika katika ile nyumba na kuulizia kwa mzee Uwele, aliyenipokea akanieleza ni kijiji cha mbele nikimbie kuelekea mbele zaidi nitakutana na nyumba nyingine ya bati.
Kwa sababu ya kupagawa niligeuka na kutaka kukimbia kama alivyioniagiza, lakini mara nikajisikia mwili wangu wote ukisisimka vibaya mno. Kuna kitu akili yangu ilikuwa imekitambua, nikajaribu kukimbia mwili ukawa mzito na hapo nikaamua kugeuka kama mwili ulivyotaka.
Naam! Ilikuwa kama akili yangu ilivyohisi, yule aliyenielekeza hakuwepo tena eneo lile, na nina uhakika kwa sababu nilimuona hapo awali na kumsikia.
Nikamkumbuka!
Aliyenipokea na kunielekeza ni yule mwalimu aliyenichapa kiboko mkono ukalemaa kwa juma zima, ni yule mwanamke ambaye baba alisema kuwa walikaa naye garini na hatimaye akapoteza maisha na ni yuleyule niliyemuona akiwa katika msafara wa kuaga mwili wa baba.
Hatimaye nakutana naye tena huku kijijini!!
Nilibaki nikiwa nimesimama wima nisijue ni kitu gani cha kufanya. Nikiwa nimesimama vilevile damu ikinichemka sana, akatoka ndani mtoto wa kike, akaniuliza ninatafuta nini pale. Huyu ndiye aliyenirejesha katika ulimwengu wa kawaida tena, nikamuulizia mzee Uwele akaniambia yupo ndani amelala.
Nikamueleza kuwa mimi naitwa Ngomeni na nimetumwa na mama upesi sana, yule mtoto akaendelea kuniuliza maswali mengimengi nikaona ananipotezea muda nikaita kwa sauti ya juu. Babuuuuuu!
Babu akatoka nje, kumbe hata hakuwa amelala. Aliponiona tu akanitambua japokuwa sio kwa jina lakini alijua tayari damu iliyopo pale inamuhusu.
Akaniuliza mimi ni nani nikajieleza.
Na sikusubiri aulize nini kilichonipeleka hapo ama nimefika na nani.
Nikajieleza kila kitu kuhusu mama upesiupesi.
Mimi nilikuwa bado kijana na ningeweza kukimbia zaidi ya babu lakini ajabu babu alitoka mbio kali, akielekea huko nilipomuelekeza mama.
Alifika na mimi nikafika.
Mama yangu alikuwa sio mweupe sana lakini ungeweza kumuita mweupe katika kundi la weusi, basi ilikuwa ni kazi rahisi sana kuuona mguu wake jinsi ulivyokuwa mwekundu!!
Mama alikuwa anatokwa jasho na alikuwa ameuma meno yake sana kumaanisha kuwa alikuwa anaumia. Babu alipiga mayowe kwa nguvu sana, alikuwa amepagawa pia, kelele zake ziliwavuta wanakijiji.
Acha bwana! Kijijini kuna ushirikiano mjini unafiki ndo umetanda. Watu hawakulazimishwa walifika eneo lile kumshuhudia mama, wakambeba mama yangu huku akilia kilio na machozi na kamasi vyote vikimtoka kama mtoto mdogo.
Ukimuona mtu mzima katika hali hii tambua kuwa anaumia sana.
Kilio cha mama kikanifanya na mimi niungane naye katika kulia, nililia sana kwa sababu licha ya utoto nilitambua kuwa kuna jambo lisilokuwa la kawaida lilikuwa linatokea kwa mama yangu.
Mama alipelekwa kwa bibi mmoja ambaye alikuwa hajiwezi hata kusimama bila kutumia mkongojo wake, bibi yule alimminyaminya mama mguu wake kisha akautazama na kuanza kuongea kikabila.
Sijui hata alichokuwa anasema ila ni babu alikuja kunieleza katika siku za usoni kuwamama alikuwa amewekewa tego la kuua!
Na kama isingekuwa kuwahishwa kwa yule bibi ilitakiwa afie palepale akiwa ameketi chini.
Tiba iliendelea kwa masaa mengine manne zaidi hali ya mama ilikuwa mbaya, hatimaye yule bibi naye akasalimu amri akasema alipofanya ndio mwisho wa utaalamu wake.
Mama akabebwa na kupelekwa kwa mtaalamu mwingine, kila muda mama alikuwa akiniita na kuninong’oneza kuwa nimuombe sana Mungu amwokoe kwani anajiona hana namna yoyote ile ya kuiona kesho.
Mara nyingine aliniita na kunieleza kuwa nisome sana kwa bidii pia niikusanye familia yangu iendelee kuwa moja siku zote.
Maneno haya ya mama niliyafananisha maneno ya kwenye filamu pindi muhusika anayeigiza kuumwa anapokaribia kukata roho.
Nililia sana hakika kwa sababu niliiona waziwazi hali ya hatari.
Tulipofika kwa mtaalamu wa pili, huyu alimchanja mama ili amuwekee dawa.
Ajabu damu ya kijani ikamtoka mama, mtaalamu yule akaruka kando na kuongea lugha zisizoeleweka na hapo akataja kitu kama skadi ama vinginevyo, ila nakumbuka alisema skadi!!
Hakuendelea tena kumwekea mama dawa.
Badala yake aliuliza ikiwa katika umati ule yupo mtoto wa mgonjwa, babu akanishika mkono na kumwonyesha yule bwana tabibu wa kijijini katika sekta ya tiba asilia.
Yule tabibu akaniita na kwenda kusimama nami kando, akaniuliza swali moja huku akitetemeka.
“Unamuamini Mungu! nikakiri kuwa ninamuamini.
“Wewe ni mtoto mdogo, wewe ni sawa na malaika tu japokuwa sio katika kiwango cha mtoto mchanga….. sogea pembeni pale kaa kimya mwambie Mungu hautaki mama yako afe katika namna hii ya mkono wa mtu… mwambie Mungu hautaki kuwa yatima. Nenda sasa!!” akanisogeza kando.
Ndugu zanguni, hii sio simulizi ya dhahania. Yalinitokea haya……
Nikafanya kama alivyoniagiza nikafumba macho, nikasema maneno yale kama mara nne hivi…… wakati nasema maneno yale nikasikia zile sauti zilizosema katika sikio langu siku ile shuleni. Sauti hizi zilifoka sana na kusema kuwa zinatoka kwa muda tu lakini zitarejea.
Nikapatwa na fahamu zangu sauti zile zikiwa zimepotea… nikageuka na kuukuta ule umati ukiwa umemzunguka mama.
Sijui kuna jambo gani lilikuwa linatokea lakini nilipatwa hofu kwa jinsi walivyokuwa wakihangaika huku na kule huku wamemzunguka mama.
Nilihisi jambo baya ambalo sikutaka litokee lilikuwa limetokea.
Nilihisi mama yangu alikuwa ameaga dunia!!!
JIFUNZE!!
Nakusihi tena, wapo wanaoishi wakisema hawana dini wala imani yoyote na hawa wanajiita wapagani.
Naam! Si tatizo hata kidogo kuinama chini huku ukijitazama miguu yako na kisha kufungua kinywa chako na kusema HAUNA DINI.
Lakini tafadhali usije ukajipa ujasiri wa kukinyanyua kichwa chako juu na kisha kusema HAKUNA MUNGU!!
Nakusihi!!!
ITAENDELEA
Mama’ke Mama Sehemu ya Tatu
Also, read other stories from SIMULIZI;