Mamake Mama Sehemu ya Tano
MAISHA

Ep 05: Mama’ke Mama

Mama'ke Mama Sehemu ya Kwanza
Mama’ke Mama Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA

********************************************************************************

Simulizi: Mama’ke Mama

Sehemu ya Nne (5)

Yeye alikuwa anauza maji ya mifuko ambayo kwa jijini Dar yamezoeleka kama maji ya Kandoro. Maji ambayo hutumiwa zaidi na watu wa daraja la chini sana kimaisha, kutokana na unafuu wake katika bei.

Akaniuliza kama nina hela nikamwambia sina kitu.

Akafungua deli lake akatoa pakiti moja.

Lahaula! Maji yale yalifanana na damu, lakini yeye hata hakushtuka. Aliponipa niligoma kuyapokea nikimuuliza kulikoni maji yapo vile.

Akanitazama !

“Ngomeni ndugu yangu… usipokuwa makini njaa itakuua…” aliniambia na mara akaja mteja…. Alikuwa anahitaji maji. Huyu mtu amenijuaje? Nilijiuliza.

Nikasubiri amuhudumie yule mteja kwanza.

Yule kijana akafunua na kumpatia pakiti moja, akanywa kwa fujo akaongeza pakiti nyingine.

Nilikuwa nimeikunja sura yangu nikistaajabu yule mtu anayekunywa damu.

Na hajui kama ni damu!

Hapo sasa nikakumbuka kuwa kuna dawa Mariam alinipaka ya kuweza kuona mambo ambayo wengine wa macho ya kawaida hawawezi kuona.

Nikasikitika kuona wanadamu wanavyolishwa vitu vibaya bila wao kujua.

Yawezekana hata mimi nilikula sana vitu hivyo nikiwa na macho yangu ya kawaida.

“Ngomeni.. wewe ni mwenzetu lakini unavyojikimbiza utadhani utafanikiwa kutoroka mdogo wangu…. We bora utulie tu maana isingelikuwa kuandaliwa kumrithi bibi yako we ungeshakatwa ulimi zamani sana kwa tabia ulizoonyesha…. Wenzako wote waliojifanya wajuaji kama wewe waliishia kukatwa ndimi zao….” Aliniambia huku akiwa anatazama mbele.

Nilibaki kushangaa tu…. Akaendelea kuzungumza.

“Hapa utazunguka sana lakini kurudi nyumbani kirahisi, hiyo sahau kabisa…. Sikia kuwa mjinga nenda ukatulie upewe cheo chako uanze kula raha tu…..” alinieleza kana kwamba yale ni mambo ya kawaida kabisa aliyokuwa akisema.

Nilitaka kujibu kitu lakini maneno hayakuwa yamepangana sawa kichwani.

“Ngomeni… bibi yako anakupenda sana….. usije ukamkasilisha kwa kujifanya mjuaji… mi nakusihi sana kwa sababu nipo katika falme hizi mwaka wa sita sasa… ukiwa mpole wala hawana habari na wewe……” alimaliza… akawa ameitwa na mtu aliyekuwa anahitaji maji. Akaondoka na kuniacha pale nikiwa nimegwaya tu bila kujua ni kipi natakiwa kufanya kwa usahihi zaidi kulingana na hali ile.

Kuhusu kuwa mtawala wa falme za kichwawi sikuwa tayari hata kidogo.

Lakini kuhusu nini naweza kufanya kujitoa katika hali ile sikuwa najua pia.

Niliendelea kuwa eneo lile, hadi aliporejea yule kijana nikamsihi anisaidie niweze kupata chakula.

Alinitazama kwa masikitiko kisha, akaniambia nimsogelee. Akanishika macho yangu na kunipaka vitu nisivyovijua.

Alipoitoa mikono akanipa pesa niende kuata chakula. Sasa nilikuwa naonekana, watu akanisalimia na kuniuliza nini kimenisibu.

Nikijitazama, matope yalikuwa yamenitawala.

Niliwaongopea kuwa kuna mahali tunafanya ujenzi wa nyumba ya matope.

Baada ya kumaliza kula niligundua kuwa wateja wote wanaokula pale maji wanayokunywa ni kutoka kwa yule kijana ambaye nimegoma kunya maji yake ambayo ni damu na sio maji kama wanavyodhani.

Bado sikuweza kuyanywa yale maji japokuwa yalionekana kuwa safi kabisa tofauti na awali nilipoyaona kama damu.

Nilipomaliza kula nilirejea tena kwake akaniuliza ikiwa nataka kuendelea kubaki na hali ileile ama anirudishie macho yangu.

Nikawa najiulizauliza, hakunisubiri nimjibu akanigusa tena nikarejea katika ile hali.

Nilipogeuka kule kwenye chakula nilishuhudia mambo ya ajabu sana nikajaribu kujitapisha lakini haikuwezekana tayari nilikuwa nimemeza.

Hakika dunia hadaa, walimwengu shujaa!

Ndugu msomaji na msikilizaji wa simulizi hii, nilijifunza jambo kutokana na maswali yangu mengi.

Huyu kijana alinieleza kuwa nyama ya wanadamu ina tabia ya kuwa kama ulevi wa kudumu. Ukilishwa nyama ya mwanadamu utatamani tena na tena kuipata.

Wanapokuisha hautafahamu kama hii nd’o nyama ya mwanadamu.

Utaiona kwa jicho lako la kawaida, utaishika kwa mkono wako dhaifu, kisha bila shurti utaitia kinywani.

Utaitafuna, utaimeza! Kisha utabeua….

Yawezekana unapenda sana mishkaki, ama unapenda nyama ya mbuzi kupindukia, yawezekana u mlevi wa nyama ya ng’ombe. Wachawi hupitia humuhumu, anakulisha nyama ya mwanadamu katika mgahawa mmoja, unaondoka pale ukiisifia sana pasi na kujua kama ni nyama ya mwanadamu.

Utasema, mishkaki ya bwana yule mitamu sana.

Kesho utarejea tena, kisha utawaleta na rafiki zako. Wote wataisifia mishkaki.

Hata wasijue kuwa wapo katika kuila nyama ya mwanadamu!

Migawaha ya namna hii, muhusika akipoteza maisha. Hata ajitokeze mtu wa kupaendeleza kwa biashara ileile ya kuuza nyama hawezi kufanikiwa. Biashara itakufa!

Kwa sababu aliyeondoka alikuwa anauza nyama za wanadamu, anayemrithi anauza nyama za kawaida. Anauza mishkaki ya kawaida kabisa.

Wateja wataondoka huku wakilalamika kuwa marehemu kaondoka na utamu wake.

Jitafakari sana ndugu yangu!

Wewe ni mlevi wa nyama gani?

Nikiwa nimefumba macho vilevile mara nilishtuka nikimwagikiwa na majimaji ya moto, kisha nikasikia yowe kubwa likimtoka bibi.

Nikafumbua macho yangu na kujikuta damu ikiwa imenitapakaa sana, nilipagawa na kupiga mayowe.

Nilipomtazama bibi nilimuona akiwa anavuja damu katika bega lake, upanga ulikuwa umeanguka chini na alikuwa akipambana kukabiliana na damu ile.

“Washenzi nyie nitawachinja kama kuku…” alinikoromea huku akinitazama kwa jicho kali sana.

Nikiwa bado katika mshangao niliisikia sauti ikinisihi nikimbie, niliangaza huku na kule ni nani anaye nitazama lakini sikuona mtu yeyote Yule, sauti iliendelea kunisihi… nikajitoa katika yale matope. Sasa niliweza kutoka, nikawa narudi kinyumenyume bibi akinitisha kuwa nikiondoka ananiua.

Sikukubali kirahisi kumsogelea, nikarudi hadi nilipostuliwa na mlio mkubwa wa paka.

Nilipogeuka nikakutana na paka mweusi mwenye macho yenye rangi ya dhahabu, paka Yule alikuwa ananitazama akiwa ananikazia macho… niliogopa sana nikajaribu kumfukuza lakini badala aondoke akanyoosha mguu wake mmoja juu akawa ananifanyia ishara ambazo sikuwa nazielewa.

Ni kama naye alielewa wazi kuwa sizielewi zile ishara… akaanza kutoa miungurumo… sasa nikawa namuogopa.

Nilipomtazama vyema nikaona akitoa makucha yake, yalikuwa makucha marefu sana na kama angefikia hatua ya kunirarua lazima angenijeruhi vibaya mno.

Nikaanza kujiuliza, sasa nirudi makaburini kule kwa bibi ama nikabiliane na huyu paka.

Wanasema zimwi likujualo halikuli likakwisha… nami nikaona ni heri bibi anaweza kuwa na huruma na mjukuu wake japokuwa alionyesha waziwazi kutaka kuniua.. na sikuwa najua ni kitu gani kilitokea hadi akashindwa kutimiza azma yake.

Nilipoanza kurudi kinyume nyume mara ghafla yule paka aliunguruma kwa nguvu na hapohapo akanirukia kwa kasi ya ajabu kifuani makucha yake yakiwa yamechomoka vilevile.

Kumbuka sikuwa nimevaa shati hivyo yalijikita moja kwamoja katika kifua changu na kunisukuma kwa nguvu sana nikaanguka chini, ule muda nilipoanguka chini hapohapo nikaona kitu kama mkuki kikipita kwa kasi sana eneo lilelile nililokuwa nimesimama.

Yule paka alibaki akiwa juu yangu amenigandamiza, mimi nilikuwa natweta tu… kama ni kujikojolea nilikuwa nimejikojolea mpaka mkojo ukaisha.

Sasa nilikuwa mtu wa kupiga mayowe, na sauti nayo ilikuwa imekauka sikuweza kupiga mayowe kwa muda mrefu.

Nikiwa bado pale chini, paka yule akafanya mlio mkubwa sana ulionipagawisha, alifanya vile kama mara mbili. Na punde wakatokea fisi wawili, wale fisi walipofika walimnusanusa kisha akaondoka ikawa zamu ya wale fisi kunigandamiza pale chini.

Ilikuwa ni kama ndoto ya kutisha, ndoto inayongoja jua lichomoze, jogoo wawike nami niwaweke watu kitako kuwasimulia ndoto hii.

Lakini hii haikuwa!

Paka akaondoka kwa kasi sana, na baada ya sekunde kadhaa kutoka katika kile kichaka alitokea mtu na si paka tena, alikuwa hana nguo ya juu…. Na alikuwa msichana.

Alikuwa ni Bi. Mariam, alikuwa amejeruhiwa hapa na pale lakini alikuwa anatabasamu.

Nilishangaa sana kumuona kwa sababu hapo awali nilielezwa kuwa alikuwa amekatwa viungo vyake na kugeuzwa kuwa chakula.

“Bibi yako ni mtu mmoja hatari sana… lakini pambano ndo kwanza limeanza nitamnyoosha ama ataniua…” alizungumza bi Mariam. Mimi nikiwa nimepigwa butwaa tu.

“Ilikuwa akuue ule mkuki alioutuma ulikuwa umeelekezwa kwenye moyo… wewe nakwambia uiname unanitazama tu… sasa hivi ungekuwa umegongwa gari huko uraiani na ungezikwa…. Huko duniani sasa wanashangaa jinsi ulivyokoswakoswa na gari……” aliendelea kuzungumza.

Maelezo haya ya Mariam yalinikumbusha mambo kadhaa niliyowahi kuyasikia na mengine kuyashuhudia. Mtu anagongwa na gari, wanaenda kuzika kisha baadaye wanaingiwa mashaka wakifukua wanakutana na kinu ama chungu cha kupikia.

Ninakiri kuwa kama ni uhuru basi viumbe hawa walipewa uhuru mkubwa sana. Uhuru wa kufanya lolote dhidi ya imani dhaifu kabisa ya wanadamu.

Pasi na kuhitaji kuridhika, Mariam akasema sehemu ile si salama tuondoke, safari hii sikusubiri kufundishwa kumpanda fisi nilipanda mwenyewe, tukaondoka huku Mariam akinisimulia kilichojiri baada ya mimi kufanya makosa ya kukimbia na kisha kugundulika na wafuasi wa falme ile na kisha taarifa kumfikia bibi yangu kuwa kuna ujanja najaribu kuufanya ili kupingana na matakwa yake.

Akanieleza kuwa alikamatwa na kupewa adhabu kubwa kubwa lakini ikawa bahati yake pale ambapo mtu aliyepewa kumlinda alipomtamani kimapenzi na kujikuta akilegeza kamba alizomfunga.

“Ujue nisingeonyesha kumkubali basi wangenikata mikono na miguu.. na hadi sasa wanajua kuwa sina mikono wala miguu.. ndo maana bibi yako amepagawa nilipompiga skadi kwenye bega wakati anakaribia kuikata shingo yako… lakini ukweli ni kwamba sikukatwa kiungo chochote nilimkubalia yule bwana kuwa naye katika mapenzi akamkata mtu mwingine na kudanganya kuwa amenikata mimi… kosa alilofanya ni kuniamini na kunivujishia siri nyingi sana… alipolegeza kamba tu, nikamsubiri anisogelee nikaivunja shingo yake kwa mikono yangu mwenyewe kisha nikakizika kabisa kivuli chake asije akatoa ushahidi wowote na hapo nikatoroka na baadhi ya silaha.

Bila hivyo nisingeweza kukukomboa….” Alimaliza kunisimulia huku akiniacha na viulizo kibao….. hasahasa kile kitendo cha kubadilikana kuwa paka kiliniacha katika giza.

Tulifika eneo jingine ambalo alinieleza kuwa kidunia ni kama boda, kutoka mji huu wa kwanza kuelekea mji wa pili akanieleza kuwa baada ya boda hiyo kuna boda nyingine ambayo ndipo wanaofanikiwa kuivuka huweza kurejea duniani kama misukule iliyotoroka ama kutajwa kama watu waliofufuka.

Si kweli kuwa wanafufuka bali wanafanikiwa kuvuka boda kuu!!

Boda ya hatari kupita zote…..

Mariam hakusita kunieleza bayana kuwa si jambo jepesi kabisa kuivuka boda ile. Akanisihi sana nijitahidi kukubaliana na ukweli kuwa pale hatupo duniani bali tupo malimwengu ya giza.

Hivyo natakiwa kuishi kama itakiwavyo kule, nikijaribu kuyapeleka mambo kidunia basi yatanikuta mabaya sana.

Tulifika mahali tukashuka katika zile fisi akaziruhusu ziondoke, wakati zinaondoka akageuka kuzitazama na kisha akanyoosha mikono yake juu na alipoishusha niliona wale fisi wakiruka huku na kule kabla ya kutulia chini na kuwa wakimya.

Kabla hata sijamuuliza ni kitu gani kimetokea akanieleza kuwa amewanyamazisha fisi wale kwa sababu wakirudi kambini wanaweza kutoboa siri kwani kila tunachozungumza wanakisikia.

Baada ya hapo akawaendea wale fisi sijui alichofanya lakini alirejea akiwa amevaa shati la kiume.

“Ngomeni….” Akaniita. Nikaitika akanitazama na kunieleza jambo.

“Tunataka kuondoka katika ngome hii ya wachawi…. Sikufichi kuwa mimi ni mchawi ambaye nahitaji kutubu na kumrejea muumba wangu… amini usiamini huku wanamuogopa sana Mungu lakini ni ubishi tu… na hili la hawa watu kumuogopa Mungu ndo linanifanya na mimi nione haina haja ya kuendelea kuishi huku.

Lakini Ngomeni kabla hatujaondoka nahitaji nikueleze jambo ambalo ni wewe utafanya maamuzi juu yake. Unamjua Chausiku!!”

Nilimuuliza Chausiku yupi akanijibu.

“Yule aliyemchukua mama yako na baba yako….” Alinijibu kwa utulivu.

“Mama na baba yangu walikufa mbona muda mrefu sana umepita…..” nilimjibu huku nikiwakumbuka wazazi wangu na namna ya vifo vyao ilivyokuwa.

“Mh! Huko kwenu wamekufa lakini huku wanaishi…. Nasikitika kuwa watakufa ikiwa utafanikiwa kuivuka ngome hii…. Je upo tayari wafe sisi tuondoke zetu ama nini tunafanya…..” alinihoji kwa utulivu.

“Mariam ni nini unamaanisha?? Yaani wazazi wangu wapo hai?? Kivipi…”

“Huyo Chausiku ndiye alipewa jukumu la kuwaleta huku ili kujenga mazingira mazuri ya kumchukua mama na baba yako…… aah!! Kwani unakumbuka tarehe aliyokufa baba yako huko duniani…. Na mama yako je?” aliniuliza huku akitabasamu.

Nikafikiria kidogo nikakumbuka kuwa mama alikufa tarehe moja na baba lakini miezi tofauti.

Nikamuuliza hiyo ina maana gani.

“Tarehe sita.. hiyo ni siku yetu ya damu na kafara…. Wazazi wako wangekuwa wametolewa kafara zamani sana tatizo ulikuwa wewe… walitaka urithishwe kwanza ufalme ndipo wawaondoe,, lakini wameteseka sana….. ukiwaona hautawakumbuka kabisa…..” alizidi kunieleza.

Tukiwa bado tumesimama pale pale mara kwa mbali tuliwaona wanawake wawili wakitufuata, walikuwa wasichana warembo sana.

“Wakikusemesha usijibu hovyo bila kufikiria… ukiona huwezi kujibu nitawajibu mimi…. Sawa!!” Mariam alininong’oneza.

Wasichana wale wakatufikia…….

Mmoja akasimama pembeni yangu na mwingine pembeni ya Mariam.

Niliiona hofu machoni mwa Mariam.

Jambo hilo liliniogopesha sana. Kama Mariam ambaye ni mzoefu anaogopa, mimi nina kipi hadi niridhike?

Tulisubiri wazungumze hawakuzungumza walikuwa wanatutazama tu. Mariam naye hakuzungumza alibaki kuwatazama tu.

Mara ghafla….. ilikuwa ghafla sana si mimi wala Mariam aliyetegemea, wasichana wale ambao walikuwa wanazungumza kwa ishara zao wenyewe walifanya jambo la kustukiza mno.

Ghafla akina dada wale ambao walikuwa hawajasema neno lolote lile, walishikana mikono kisha wakapiga kelele sana. Wakati wanapiga kelele hizi kimbunga kikali kilivuma….

Kelele zao zilipokoma na kimbunga nacho kikawa kimeishia pale.

Lakini kulikuwa na maajabu mengine mapya, akina dada wale walitoweka na akatokea bibi yangu.

Mariam akanivuta na kuninong’oneza.

“Nenda kule makaburini, tafuta kaburi uulilozikwa hakikisha unalifukua mpaka ukipate kivuli chako. Mimi niache napambana na huyu kiumbe… najua ni hatari lakini usiogope lolote lile hakikisha unapambana…. ukifanikiwa kuingia kaburini jichane ili damu yako ikiite kivuli chako” alinisihi kisha mara moja akanisukuma.

Nikalazimika kukimbia huku nyuma nikiacha kivumbi kikali sana.

“Ngomeee…..” niliisikia sauti ya Mariam ikiniita, nilipogeuka nilimuona fisi mkubwa akinijia kwa kasi nikataka kukimbia lakini Mariam akanielekeza kuwa nipande katika mgongo wa yule fisi. Nikafanya vile upesi sana, sasa nilikuwa na ujasiri na nilikuwa nimeyasahau kwa muda mambo ya kidunia.

Fisi aliondoka kwa kasi sana na mimi nikiwa nimeshikilia.

Tulitumia muda kama dakika nne tu.. tayari tulikuwa makaburini, nikaongozana na yule fisi hadi nikayafikia makaburi, nikaanza kusoma majina katika makaburi, tulitafuta sana hatimaye tukalifikia kaburi lililokuwa na jina langu lile la Ngomeni.

Nikaanza kujaribu kuchimba lilikuwa gumu sana. Nikaanza kukata tamaa.

Ndugu msikilizaji umewahi kusikia kitu kinachoitwa fisi mtu. Kama unadhani ni hadithi tu basi fisi mtu wapo…

Huyu alikuwa fisi mtu, alipoona ninasota peke yangu akasogea hadi pale kaburini, akatanguliza miguu yake ya nyuma, kilichofuata ulikuwa ni mtafutano kati yangu na vumbi, fisi yule alifukua kwa kasi kubwa sana.

Baadaye vumbi lilitulia, nilimtazama yule fisi na kwa mara ya kwanza nikamuonea huruma kiumbe huyu wa ajabu, ulimi ulikuwa umemtoka nje na alikuwa akihema juu juu.

Nikawa najiuliza nini cha kufanya, yule fisi alikuwa amertulia akaniachia mimi ukumbi.

Nikalazimika kuingia pale kaburini huku nikiwa natetemeka. Bado nilikuwa siamini kuwa nilikuwa nimezikwa.

Nilianza kufukua zaidi, nikaanza kukutana na nguonguo zilizooza…

Hatimaye nikaanza kukutana na mbaombao…..

Nilivyofukua zaidi nikaliona jeneza…. jeneza lile halikufanania na la mtu aliyezikwa siku za karibuni bali aliyezikwa miaka mingi iliyopita.

Ile naendelea kufukua zaidi nikamsikia fisi yule akilia kwa sauti kuu.

Alilia sana huku akichungulia pale shimoni….. sikujua ni kitu gani kinaendelea nilikuwa nimebabaika tu.

Nikiwa sina hili wala lile mara ukasikika mshindo mkubwa sana, mchanga uliofukuliwa ukaanza kurudi ndani ya kaburi…

Kumbuka wakati huo sijatoka na tauyari shimo lilikuwa refu, nikawa natapatapa kupanda ili nitoke mchanga ukaniingilia machoni hapo sasa sikuiwa naona tena mbele. Nikawa natapatapa huku mchanga ukizidi kuingia mle shimoni.

Nikajiona nikizikwa angali nipo hai kabisa…. nilipatwa hofu ya kifo.

Mchanga ukazidi kuingia shimoni kwa kasi sana.

“Ngomeni…… rudishaaaaaa rudishaaaa jina kwake….. likatae jina…” niliisikia sauti ikinisihi ilikuwa sauti ya Mariam, baada ya sauti ile kusihi mchanga nao ukakoma kurudi shimoni bila shaka aliyekuwa anaurudisha alikuwa amesita… nikajaribu kupekecha macho yako, jicho moja likaweza kuona mbele.

Nilichokiona kilikuwa hakifai hata kukisimulia, alikuwa ni Mariam lakini sio Mariam yule… huyu alikuwa amelowa damu vibaya mno,. Japokuwa sikuwa naona vizuri lakini niliweza kutambua kuwa hakuwa na jicho lake moja.

Mkono mmoja pia haukuwepo…na alikuwa amefungwa kamba katika mti.

Mara nikamuona bibi yangu akijivuta kuelekea alipokuwa mariam, nikatapatapa niweze kujitoa katika ule mchanga lakini haikuwezekana tayari miguu yangu ilikuwa imenasa.

Sikuwa naelewa nalikataaje jina langu, je ni kwa kusema silitaki jina langu ama ni kwa kufanya nini.

Nikajaribu kusema kuwa silitaki jibna lile lakini sikuona mabadiliko……

Mariam akapaza sauti tena, akanisihi nijichane nitokwe damu iingie kaburini. Na hapo nikakumbuka jinsi alivyonieleza mwanzo

Aliposema vile nikaona bibi anaweweseka ni kama aliyekuwa anajiuliza aende kwa mariam ama aje kwangu.

Kuona vile na mimi nikaona niitumie nafasi ile ya mwisho kupambana na watu hawa wabaya.

Hamna kitu kigumu kama kujijeruhi wewe mwenyewe, ona tu katika filamu mtu anajichana na kisu…. lakini katika maisha ya kawaida kujijeruhi ni kazi ngumu.

Nikajaribu kujing’ata lakini sikutokwa damu zaidi ya kuumia na kuacha kufanya vile.

Bibi alinitazama kisha akacheka kwa sauti ya juu, bila shaka aligundua kuwa siwezi kufanya kile nilichokuwa najaribu kukifanya.

Nikiwa bado palepale, mara nilisikia kishindo, na mara nilikuwa nimebanana mle kaburini na yule fisi mtu.

Fisi hakupoteza muda licha ya mimi kupiga mayowe alinirukia na kunirarua mkono wangu kwa kutumia makucha yake…..

Hapohapo damu ikaanza kunitoka na kaburi nalo likaanza kutetemeka, fisi akaruka na kutoka nje.

Ilikuwa kweli kilichotokea, nikashangazwa kujisikia nikiwa imara sana, bibi aliporejea pale sikuwa namuogopa tena nilijiona mtu mpya kabisa nisiyekuwa na hofu dhidhi ya watu hawa wabaya.

Alifika na kutoa amri zake lakini sikudhurika…….

Nikawa natembea huku nikiwa nashangaa.

Mara akapiga miluzi mikali na baada ya muda kidogo kiza kikatanda.

Na kimya kikachukua nafasi yake hadi alivyopiga miluzi tena mwanga ukarejea.

Nikamuona bibi akiwa na upanga mkali sana. Na mbele yake kulikuwa kuna watu wawili wachafu sana.

“Ukijifanya mjuaji nawachinja watu hawa mbele yako….” alinisemesha huku akicheka.

Nikakumbuka maneno ya Mariam aliniambia kuwa baba na mama yangu wapo hai lakini wamezeeka na wameteseka sana.

Mungu!

Inakuwaje tangu awali sikukumbuka kuwa kuna Mungu?? nilistaajabu

Nikafumba macho yangu palepale ili nisiweze kushuhudia lile ambalo lilitakiwa kutokea. Wazazi wangu kuchinjwa…

Nilipofumba macho mara nikakumbuka nilipokuwa mdogo, siku ambayo mama yangu alikuwa amekumbwa na pigo la ajabu kijijini kwa babu kuna mganga aliniuliza kama ninamuamini Mungu. Nilipokubali akaniambia niwe mkimya niseme na Mungu nimwambie kuwa sitaki mama yangu afe katika mazingira yale.

Kweli baada ya kusema na Mungu kuna muujiza ulitokea lakini kutokana na ule utoto sikukumbuka kusema asante kwa Mungu kwa sababu nilikuwa siujui vyema utukufu wake.

Nikazungumza katika nafsi yangu, kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu nikasema na Mungu wangu, nikamwambia kuwa atende muujiza kwa sababu sisitahili kufa kwa amri ya watu wale wabaya.

Ajabu iliyoje hii…..

Alinisikia na leo hii naweza kusema hadharani kuwa hakuna chenye uwezo popote pale zaidi yake Mungu.

Niliposema naye tu mara bibi na wenzake wakaanza kutetemeka, mara wakimbie huku mara kule…

Nami nikajikuita natetemeka sana na kisha nikaanguka chini.

Sikujua kilichoendelea zaidi hadi pale niliporejewa na fahamu zangu, nikajikuta nipo maeneo ya makaburini.

Nilikuja kupatwa na fahamu zangu tena nikiwa nimelala chini nikiwa nimezingirwa na watu.

Kamera zikiwa zinanimurika na nilikuwa nipo eneo la makaburini, kitu cha kwanza kusikia nilisikia watu wakisema kuwa nimefufuka.

Wengine walisema nimetoroka kutoka katika misukule.

Nilisimama nikiwa dhaifu sana, nikajitazama jinsi nilivyo. Nilikuwa nimechafuka sana.

Nikanyanyua macho yangu, waandishi wa habari wakawa wananipiga picha.

Mwandishi mmoja akanisogelea na kuniuliza jina langu, aliponiuliza hivyo nikakumbuka juu ya jina la NGOMENI…. Sikujitambulisha vile.

“Naitwa Fredric naombeni maji ya kunywa nina kiu sana…..” nilimjibu, upesi wakanipatia maji nikanywa.

Wasamaria wema wakanichukua kwa ajili ya kunipatia maji ya kuoga.

Baada ya kuoga nikapewa chakula… hapo nikapata nguvu upya.

Na punde baada ya hayo yote nikakutana na mwandishi wa mkasa huu, akaanza kuniuliza swali moja baada ya jingine.

Naam! Chanzo cha hayo yote alikuwa ni mama yake mama…..

Lakini aliyenitoa katika suluba ile hakuwa mwingine bali mwenyezi Mungu muweza wa yote.

Nashukuru kuwa baada ya mkasa huu… wasamaria wema walijitolea michango yao…. Viongozi wa dini mbalimbali walichangisha michango ikanifikia.

Nikayaanza maisha yangu mapya nikiwa nimelikataa jina la Ngomeni nikaendelea kuishi kama Fredrick nikiwa sina tatizo na mtu. Sikuwqahi kujua hatma ya wazazi wangu kwa sababu miili yao haikuonekana tena, sikujua kuhusu Mariam lakini Jasmin nilionana naye akiwa yu salama bin salmini alinieleza kuwa ile mimba niliyompa ilitoka yenyewe akiwa amelala usiku

Nimesimulia mengi ila napenda kukusihi mzazi na mzazi mtarajiwa, usimpe mwanao jina kwa sababu tu unapenda jina hilo… kuna baadhi ya majina yanazunguka na balaa yanamsubiri atakayepewa jina hilo ili balaa litue juu yake.

IMEKWISHA!!!

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment