My Repentance (Kutubu Kwangu) Sehemu ya Kwanza
IMEANDIKWA NA: AZIZ HASHIM
*********************************************************************************
Simulizi: My Repentance (Kutubu Kwangu)
Sehemu ya Kwanza (1)
Naitwa Flaviana Joel, mwanamke mwenye umri wa miaka ishirini na nane. Nilibahatika kuolewa miaka kumi iliyopita, nikiwa bado msichana mbichi katika umri wa miaka kumi na nane tu.
Niliolewa na mume wangu kipenzi, Ibrahim au Ibra kama mwenyewe nilivyozoea kumuita ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye benki moja maarufu ambayo sitaitaja jina kwa sababu maalum, iliyopo hapa jijini Dar es Salaam.
Kabla Ibra hajanioa, tulidumu kwenye uchumba kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja, kipindi hicho nikiwa nasoma chuo kimoja cha uhasibu kilichopo Posta, katikati ya Jiji la Dar es Salaam, nikiwa ndiyo kwanza nimeanza mwaka wa kwanza.
Baada ya ndoa, mimi na Ibra tulihamia Mbezi Beach kwenye nyumba yetu ambako tuliishi pamoja mpaka tulipokuja kutengana kwa sababu ambazo ndizo hasa zilizonifanya nitafute nafasi hii ya kutubu hadharani na kukiri kwa kinywa changu yote niliyowahi kuyafanya.
Nimesukumwa kuja kusimulia mkasa wangu huu kwa sababu nataka watu wajifunze kupitia maisha yangu na Ibra. Najisikia aibu sana, najikaza tu kwa sababu nataka wanawake wenzangu waelewe kilichonitokea na kamwe wasifuate njia kama ambazo mimi nilipita. Pia iwe funzo kwa wanaume, hasa wale ambao wapo ndani ya ndoa.
Nasikitika kwamba nimekuwa kikwazo kikubwa katika maisha ya Ibra, mwanaume niliyetokea kumpenda kwa moyo wangu wote lakini kwa sababu ya mapungufu ya kibinadamu ambayo nitayaelezea, nikageuka na kuwa mwiba mkali kwenye maisha yake.
Nilisema tangu awali na nitaendelea kusema kwamba sijawahi kutokea kumpenda mwanaume kama nilivyompenda Ibra ila hata sielewi ni kitu gani kilichosababisha haya yote yatokee.
Najisikia uchungu sana ndani ya moyo wangu hasa nikiwatazama wanangu Joel, James na Mahiza ambao bado walikuwa wakihitaji malezi ya baba na mama lakini kwa kukosa akili kwa mama yao (mimi) leo wanateseka mno.
Siwezi kumlaumu Ibra kwa sababu alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kufanya yale ambayo mwanaume anapaswa kuyafanya katika ndoa yake ingawa pia alikuwa na udhaifu mkubwa ambao ndiyo uliosababisha leo hii nipate nguvu ya kuja kutubu hadharani na kuwa sauti ya wengine ambao waume zao wana matatizo kama aliyokuwa nayo mume wangu Ibra lakini hawana pa kusemea.
Naamini kutubu kwangu na kueleza ukweli wa kila kitu kwenye maisha yangu, kutakuwa chachu ya mabadiliko katika nyumba nyingi na utaokoa ndoa nyingi.
Ukimya unaua, naamini kuna wanawake wengi sana ambao wanakufa taratibu kwa sababu hawataki kuyasema matatizo ya ndoa zao hadharani, matokeo yake wanazalisha matatizo mengine kwa waume zao ambayo mwisho wake ni kama huu ulionitokea.
Kama kujiua isingekuwa dhambi, hakika ningeyakatisha maisha yangu lakini naogopa nitakachokutana nacho siku ya kiyama. Naamini kwa kuyasimulia haya, angalau kidogo nitapunguza mzigo unaonielemea ndani ya nafsi yangu.
Nawaomba radhi wote mlioumizwa na matendo yangu na mtakaoumizwa na ushuhuda huu, hasa kipenzi changu Ibra, watu wote wanaotufahamu na kubwa zaidi kwa mama yangu ambaye matendo yangu yamemfanya adharaulike na kila mtu kwani inaonekana alishindwa kunilea katika maadili mema.
Pia naomba Mungu wangu anisamehe na nitaendelea kumlilia kila siku kama nilivyofundishwa na mtumishi wa Mungu, Mchungaji Mwakatobe ambaye ndiye aliyeniongoza katika sala ya toba.
April 8, 2003
Dar es Salaam.
Ilikuwa ni asubuhi yenye mvua kubwa ambayo ilisababisha hali ya taharuki kwa wakazi wengi wa Jiji la Dar ambao tulikuwa tukitegemea usafiri wa daladala. Nakumbuka vizuri ilikuwa ni tarehe 8 ya mwezi wa nne, mwaka 2003. Naikumbuka vizuri tarehe hii kwa sababu ambayo baadaye nitaielezea.
Nilikuwa nimebeba begi langu begani na kujikunyata pembeni ya kituo cha daladala cha Morocco, kwenye makutano ya Barabara za Ali Hassan Mwinyi na Old Bagamoyo Road (hivi sasa inaitwa Mwai Kibaki Road), nikisubiri usafiri wa kuelekea chuoni, Posta.
Daladala siku hiyo zilikuwa za taabu sana kwa sababu ya hali ya hewa iliyosababisha foleni kubwa karibu kwenye barabara zote za Jiji la Dar es Salaam. Kama ujuavyo Jiji la Dar mvua ikinyesha kidogo tu basi barabarani hakupitiki kutokana na foleni.
Ilikuja daladala ya kwanza iliyokuwa inaelekea Posta lakini ilikuwa imejaza mno kiasi cha watu wengine kuwa wananing’inia mpaka mlangoni. Nikashindwa kupanda. Ikaja ya pili nayo ikiwa katika hali hiyohiyo, ikanibidi niendelee kusubiri.
Mvua nayo ilikuwa inaendelea kunyesha, safari hii ikiambatana na upepo uliosababisha wote tuliokuwa tumejibanza pale kituoni kuanza kulowa. Nilitamani kurudi nyumbani kwani ukiachilia mbali kero ya mvua, muda nao ulikuwa umeenda sana.
Nikiwa najishauri cha kufanya, gari dogo aina ya Toyota Carina lilikuja na kusimama pale kituoni, jirani kabisa na pale nilipokuwa nimesimama. Kioo cha upande wa kushoto kikashushwa kisha tukamsikia dereva akituambia kuwa kama kuna wanaoenda Posta, anataka kuwabeba watu wanne tu kwa sababu daladala zinasumbua.
Mimi nilikuwa wa kwanza kulifikia gari hilo dogo lakini zuri, nikawahi kufungua mlango wa mbele na kujitoma ndani. Abiria wengine wengi wakafuata na kuanza kugombania lakini kwa sababu gari lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria wanne tu, watatu nyuma na mmoja mbele, ilibidi wengine wabaki.
Nilijiona kuwa na bahati kubwa, nikamgeukia dereva na kumsabahi huku nikimshukuru kwa msaada wake. Abiria wengine nao walifanya hivyohivyo, akaondoa gari na safari ya kuelekea Posta ikaanza. Kwa kuwa sote tulikuwa tumelowa, hakuna aliyekuwa na stori na mwenzake, kila mmoja akawa anajifuta maji.
Safari iliendelea taratibu kutokana na foleni na baada ya muda mrefu, hatimaye tulifika Posta. Kila mmoja alifungua nauli na kutaka kumpa dereva lakini mwenyewe alikataa na kutuambia kuwa ametusaidia tu kwa hiyo tusimlipe.
Tulimshukuru sana, sote tukashuka na kila mmoja akaendelea na hamsini zake. Baada ya lile gari kuondoka, nilikumbuka kuwa nilikuwa nimesahau begi langu lenye madaftari, vitabu na vifaa vyangu vingine vya kusomea. Nilijikuta nikichanganyikiwa ghafla, nikawa najilaumu kwa uzembe nilioufanya.
Ilibidi nianze kulifukuzia lile gari kwa nyuma lakini tayari nilikuwa nimechelewa, lilishajichanganya na magari mengine, hali iliyonipa wakati mgumu kulitambua kwani kulikuwa na magari mengi aina ya Carina Posta, tena yote yakiwa yanafanana.
Nilitoa simu yangu mfukoni lakini nilishindwa kuitumia kwa sababu sikuwa nikizijua namba za dereva. Nikajikuta nikiishiwa nguvu kabisa. Safari yangu yote haikuwa na maana tena kwa sababu nisingeweza kwenda chuo nikiwa sina vifaa vya kusomea.
Kwa kuwa bado mvua ilikuwa ikimwagika, nilisogea kwenye korido ndefu za Posta Mpya na kujibanza hapo pamoja na watu wengine wengi waliokuwa wamejisitiri mvua. Nikiwa bado najiuliza cha kufanya, simu yangu ilianza kuita. Nilipotazama namba ya mpigaji, ilikuwa ngeni kwangu.
Sina kawaida ya kupokea namba za simu nisizozijua lakini siku hiyo niliipokea haraka ilipoita mara moja tu.
“Halloo!”
“Haloo, nani mwenzangu.”
“Samahani, unamfahamu Flaviana Joel?”
“Ndiyo namfahamu, kwani vipi?”
“Kuna watu niliwapa lifti kwenye gari langu muda mfupi uliopita sasa kuna mmoja amesahau begi lake la vitabu, nilipopekua ndiyo nikaikuta hii namba imeandikwa nyuma ya kitabu kimoja. Naomba umpe namba yangu mwambie anitafute au nipe yake nijue namna ya kumfikishia mzigo wake,” alisema dereva wa ile Carina kwa sauti ya kiungwana mno.
Nilishusha pumzi ndefu na kuachia tabasamu, nikamwambia kwamba mimi ndiyo Flaviana, nikamsikia akicheka kidogo kisha akaniuliza nipo wapi kwa wakati huo. Nilipomuelekeza, aliniambia nimsubiri hapohapo anakuja.
Kweli baada ya kama dakika tano hivi, ile Carina ilipaki upande wa pili wa barabara, akanipigia simu na kuniuliza kama nilikuwa naliona gari. Nikatoka mbiombio na kukimbia kuvuka barabara. Kwa kuwa bado mvua ilikuwa inanyesha, nilipolifikia gari lake, alinifungulia mlango, nikaingia na kukaa kwenye siti ileile niliyokuwa nimekaa awali, nikamgeukia, na yeye akanitazama, macho yetu yakagongana.
“Pole kwa usumbufu,” aliniambia kwa sauti ya kiungwana, nikaachia tabasamu hafifu huku nikiendelea kujifuta maji ya mvua, nikwamwambia mimi ndiyo napaswa kumpa yeye pole kwani licha ya kunipa lifti bure, nilimpa kazi nyingine ya kunitafuta.
Alinipa begi langu na kuniuliza nilikokuwa nakwenda.
“Naenda chuo, pale jirani na mnara wa askari.”
“Unasomea nini?”
“Nasomea uhasibu.”
“Ooh! Safi sana, mimi pia nilisomea uhasibu pale IFM sasa hivi nafanya kazi benki,” alisema yule dereva huku na yeye akiachia tabasamu, akaniomba kama sitajali anisindikize jirani na chuo ili nisiendelee kulowa.
Nilikubali haraka na kumshukuru sana. Akawasha gari na kwenda mpaka mbele kidogo, akageuza gari na kurudi barabarani, akawa anaendesha gari taratibu huku tukipiga stori za kawaida.
Ndani ya kipindi kifupi tu nilichokaa naye, niligundua kuwa yule kaka alikuwa mtu mmoja mstaarabu sana, asiye na maneno mengi, anayejiheshimu na anayeheshimu watu wengine pia bila kujali umri, jinsia au hali ya kiuchumi.
Alinisogeza mpaka jirani na chuoni kwetu, akalitoa gari barabarani na kupaki pembeni huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha. Nilitaka kushuka lakini akaniambia nisubiri mvua ipungue kidogo kwani yeye hakuwa na haraka sana kwani ofisi anayofanyia kazi ni jirani na pale.
Tofauti na wanaume wengi niliokuwa nakutana nao kila siku katika pilikapilika zangu, yeye wala hakuonesha papara ya kuniomba namba yangu ya simu wala hakuonesha kabisa nia ya kutaka kunitongoza hasa ukizingatia kwamba licha ya umri wangu mdogo, nilikuwa nimejaliwa uzuri wa kipekee kuanzia sura mpaka umbo.
Mvua ilipungua na hatimaye ikaisha kabisa, nikarudia tena kumshukuru yule kaka ambaye mpaka muda huo wala sikuwa nikilijua jina lake. Tukaagana, nikashuka kwenye gari lake na kuanza kutembea harakaharaka kuelekea chuoni bila hata kugeuka nyuma.
Japokuwa nilikuwa nimechelewa, nilipoingia darasani, nilikuta wanafunzi wachache tu wakiwa wameshafika, nikajua ni kwa sababu ya hali ile ya hewa. Kwa kuwa jana yake sikumaliza kazi tuliyopewa chuo, sikutaka kupoteza muda, nikakaa kwenye kompyuta yangu na kuendelea na kazi.
Bado kumbukumbu za yule kaka zilikuwa zikiendelea kuja na kupotea kwenye kichwa changu. Sijui ni kwa sababu gani lakini nahisi ni kwa sababu ya uungwana alionionesha. Ndani ya muda mfupi tu niliokaa naye, nilijikuta nikianza kumzoea na kutamani kama niendelee kumuona au kuisikia sauti yake nzuri.
Haikuwa kawaida yangu kuvutiwa kirahisi namna hiyo na mwanaume, katika historia ya maisha yangu, wanaume ndiyo walikuwa wakinipapatikia kutokana na uzuri wangu, wala mimi sikuwahi kufanya hivyo hata mara moja, nikabaki najishangaa.
Nilijitahidi kujitoa kwenye mawazo hayo bila mafanikio, kila nilipofumba macho, sura ya yule kaka ilinijia akili mwangu na kujikuta nikitabasamu.
Kibaya zaidi, wala hakunipa namba yake ya simu na sikuwa nikijua anafanya kazi wapi zaidi ya kuniambia kuwa ofisi yao ilikuwa jirani na chuo chetu. Ghafla nilikumbuka kitu kilichonifanya nitabasamu. Nilikumbuka kwamba yeye ndiye aliyenipigia simu wakati niliposahau mkoba wangu kwenye gari lake.
Harakaharaka nikatoa simu yangu na kuanza kuangalia kwenye namba zilizoingia. Macho yangu yalitua kwenye namba yake, nikaitazama kwa muda kisha nikaiandika pembeni ya kitabu changu cha Financing. Nikafanya kama najaribu kumtumia hela kwa njia ya mtandao wa simu ili nione jina gani litatokea.
Baada ya kubonyezabonyeza namba fulani, likatokea jina la Ibrahim Mnasy, nikatabasamu tena na kushusha pumzi ndefu.
“Kumbe anaitwa Ibrahim!” nilijisemea huku nikiisevu namba yake. Kama kuna mtu angekuwa ananifuatilia ninachokifanya, angeweza kudhani nataka kurukwa na akili. Angalau sasa roho yangu ilitulia kwani nilijua naweza kumpata endapo nikihitaji kuwasiliana naye.
Mvua ilikuwa imekatika kabisa, wanachuo wengi wakawa wanakuja darasani na baadaye kidogo, walimu waliwasili, tukaanza masomo japo kwa kuchelewa. Masomo yaliendelea mpaka saa nane mchana, tukatoka kwa ajili ya chakula cha mchana kisha tukarejea tena darasani mpaka saa kumi ambapo kwa kawaida ndiyo ulikuwa mwisho wa vipindi.
Tukatawanyika na mimi kuongoza mpaka kwenye kituo cha daladala cha Posta ambacho kila siku huwa napandia magari ya kurudi kwetu, Kinondoni. Kama ilivyokuwa asubuhi, usafiri ulikuwa wa shida sana jioni hiyo. Hatimaye nilipanda daladala ingawa ilikuwa ni kwa kugombania sana, safari ya kurudi nyumbani ikaanza.
Njiani bado kumbukumbu juu ya Ibrahim ziliendelea kunisumbua, nikajiapiza kuwa jioni nikimaliza kazi zangu zote, lazima nimpigie simu japo nisikie sauti yake. Baada ya kusota kwa muda mrefu kwenye foleni, hatimaye tuliwasili Morocco, nikashuka na kuvuka barabara, nikatembea kidogo kuelekea nyumbani kwani hatukuwa tukiishi mbali sana na kitu hicho.
Nilipofika nyumbani, siku hiyo sikutaka stori na mtu, nilipitiliza chumbani kwangu, baada ya kupumzika kidogo nikaenda kuoga na kurudi sebuleni kusubiri chakula cha usiku kwani tulikuwa na desturi ya kukusanyika familia nzima kila jioni.
Tulipomaliza kula, harakaharaka nilirudi chumbani kwangu na kujifungia, nikachukua simu na kujitupa kitandani, nikatafuta namba ya Ibrahim na kumpigia huku nikiwa nimeshajiandaa nini cha kuongea.
Simu ilipoita kidogo tu, ilipokelewa, nikajikuta nikisisimka mno baada ya kuisikia sauti ya Ibrahim, mapigo ya moyo wangu yakawa yananienda mbio mno.
“Haloo!”
“Haloo kaka Ibrahim.”
“Naam! Naongea na nani?” Ibrahim alizungumza kwa sauti iliyotulia mno, nikazidi kuchanganyikiwa mtoto wa kike. Nilishusha pumzi ndefu na kujitambulisha, nilipomkumbusha tu mazingira tuliyokutania, alinikumbuka na kunichangamkia.
“Umelijuaje jina langu?”
“Si ulinitajia mwenyewe, au umesahau,” nilidanganya, nikamsikia akiguna kama anayekumbuka kitu kisha tukaendelea na mazungumzo. Nilimwambia nimempigia simu ili kumshukuru kwa wema wote alionifanyia siku hiyo, akafurahi na kuniambia nisijali.
Tuliendelea kuzungumza mambo ya hapa na pale, mimi nikiwa ndiyo mzungumzaji sana, nilichokuwa nakitaka ilikuwa ni ukaribu wake na kumzoea, jambo ambalo lilishaanza kuonekana kuwa litafanikiwa kwa jinsi alivyokuwa ananichangamkia.
Baadaye mazungumzo yaliisha, nikamtakia usiku mwema kisha nikakata simu. Nilishusha pumzi ndefu na kuanza kushangilia moyoni, sijui kwa nini nilifurahi sana kuongea na Ibrahim.
Kama hiyo haitoshi, nilimtumia ujumbe mfupi mzuri wa kumtakia usiku mwema, naye akanijibu ndani ya muda mfupi tu, nikalala na kuukumbatia mto wangu huku joto tamu likiendelea kuzunguka kwenye mwili wangu.
Niseme tu wazi kwamba nilishampenda sana Ibrahim tangu nilipomuona kwa mara ya kwanza tu, na sasa nilikuwa tayari kufanya chochote, hata ikibidi kujitongozesha ilimradi awe mpenzi wangu. Naomba watu wasinielewe vibaya kwa sababu najua kwa mila za Kitanzania, ni vigumu sana mwanamke kueleza hisia zake za kimapenzi, tumezoea kwamba sisi ni watu wa kutongozwa tu. Wapo wengi tu ambao walikuwa wakiwapenda watu fulani ila kwa sababu ya kukosa ujasiri, wakajikuta wakiolewa na watu ambao wala hawakuwahi kuwafikiria kwenye maisha yao.
Niliamua kujitoa mhanga mtoto wa kike, nikajiapiza kuwa lazima nimpate Ibrahim. Wala kilichonizuzua halikuwa gari lake au kusikia kwamba anafanya kazi benki, walaa! Ni mapenzi ya dhati ndiyo yaliyonisukuma mpaka kupata ujasiri wa namna ile.
Niliendelea kumfikiria Ibrahim mpaka usingizi uliponipitia, kesho yake asubuhi nikawahi kuamka kama kawaida yangu na kujiandaa kwa ajili ya kwenda chuo. Nilipomaliza kuvaa, niliwaaga baba na mama kama ilivyo kawaida yangu kila siku kisha nikatoka na kuanza kutembea kuelekea kituo cha daladala.
Siku hiyo hakukuwa na mvua kama jana yake ingawa kila kona kulikuwa na matope. Kumbukumbu juu ya Ibrahim zikanijia na kujikuta nikitabasamu mwenyewe. Nilitoa simu yangu kwenye mkoba na kutafuta namba yake, nikampigia.
Muda mfupi baadaye alipokea, nikamsalimia kwa adabu na kumuuliza kama ameamka salama. Alinijibu kwamba yupo poa na kwa muda huo anajiandaa kwenda kazini.
“Mi mwenyewe naelekea Morocco kupanda daladala.”
“Ahaa! Sasa kwa nini usinisubiri nikupe lifti?”
“Hutachelewa sana,” nilijibaraguza ili asinione najirahisisha sana kwake, akaniambia kuwa wala hatachelewa, baada ya dakika kumi tu atakuwa ameshafika. Tuliagana, nikakata simu huku nikiwa na furaha ya ajabu ndani ya moyo wangu.
Nilitembea harakaharaka mpaka kituoni, nikatafuta sehemu tulivu na kukaa huku macho yote yakiwa upande ule Ibrahim alikotokea jana yake. Nilitoa kioo changu kidogo ninachotembea nacho kwenye mkoba na kujikagua usoni, nikajiweka sawa na kuendelea kumsubiri.
Kweli dakika kumi baadaye, gari la Ibrahim lilifika pale kituoni, akapunguza mwendo na kusimama huku akishusha kioo. Kwa kuwa tayari nilishamuona, niliinuka harakaharaka na kumfuata, akanifungulia mlango wa mbele, nikaingia na kukaa.
“Mambo!” Ibrahim alinisabahi huku tabasamu pana likiwa limeupamba uso wake. Ibrahim alikuwa na mvuto wa kipekee machoni pa mtu yeyote. Nikajihisi mkondo kama wa umeme ukipita mwilini mwangu na kusambaa kwenye kila kiungo.
Nilimjibu huku na mimi nikiachia tabasamu pana, akaondoa gari na safari ya kuelekea Posta ikaanza. Mazungumzo ya kawaida yaliendelea huku mara kwa mara nikigeuka na kumtazama Ibrahim usoni.
Kila macho yetu yalipogongana, moyo wangu ulikuwa ukinilipuka mno mpaka nikawa najishtukia. Kwa kuwa siku hiyo hakukuwa na foleni kubwa, baada ya dakika kadhaa tayari tulikuwa Posta. Akanipeleka mpaka jirani na chuoni kwetu, tukaagana kisha akaondoa gari kwenda kazini kwake.
Nilimsindikiza kwa macho mpaka alipopotea kwenye upeo wa macho yangu, nikatembea harakaharaka kuingia chuoni huku moyo wangu ukiwa na furaha ya ajabu. Siku hiyo hata akili zangu hazikuwepo kwenye masomo kabisa, nilikuwa nikiwaza jinsi ya kumuingiza Ibrahim kwenye kumi na nane zangu! Moyo wangu ulishampenda.
Muda wa lanchi ulipofika, nilimtumia meseji Ibrahim na kumwambia kama ana nafasi aje tule wote mi nitamlipia, akanijibu kwamba alikuwa na kazi nyingi hivyo isingekuwa rahisi kuonana.
“Kwani kazini unatoka saa ngapi?”
“Saa kumi na moja.”
“Kuna mahali nataka unisindikize, utakuwa na nafasi?”
“Yaa, nikitoka kazini huwa naenda nyumbani moja kwa moja kwa hiyo usijali nitakusindikiza,” alisema Ibrahim bila hata kuhoji ni wapi nilipokuwa nataka anisindikize. Wala sikuwa na safari yoyote, nilitaka tu ukaribu wake.
Kichwani nikapata akili kwamba nitamwambia anisindikize ufukweni kuchukua mchanga kidogo wa bahari kwa ajili ya kumpelekea mama. Nilipanga kwamba tukifika ufukweni, nitamfanyia vituko mpaka mwenyewe achanganyikiwe na mimi. Muda wa lanchi ulipopita, nilirudi darasani, nikawa naona kama saa haziendi haraka.
Hatimaye muda wa kutoka ulifika, nikakusanya kila kitu changu na kutoka, nikampigia simu Ibrahim kwamba atanikuta namsubiri palepale aliponishusha asubuhi. Kwa kuwa mimi niliwahi kidogo kutoka chuo, ilinibidi nimsubiri Ibrahim kwa zaidi ya dakika arobaini. Kwangu hiyo wala haikuwa kazi kubwa, hatimaye nikaliona gari lake likija taratibu pale nilipokuwa nimekaa, akashusha kioo na macho yetu yakagongana, wote tukatabasamu. Harakaharaka niliingia kwenye gari na kukaa pembeni ya Ibrahim, nikamgeukia, na yeye akanigeukia, tukawa tunatazamana.
“Mambo!” alivunja ukimya, nikamjibu huku nikiachia tabasamu pana, na yeye akatabasamu na kuyafanya meno yake meupe yaonekane vizuri. Siyo siri nilijikuta nikimpenda sana Ibrahim.
Nilimwambia kuwa nataka anisindikize baharini nikachukue mchanga mama kaniagiza, wala hakuwa na kipingamizi chochote. Akawasha gari na kuanza kuendesha taratibu, tukawa tunaelekea baharini, upande wa Hospitali ya Ocean Road. Njiani tulikuwa tukipiga stori za hapa na pale, akawa ananiuliza kuhusu masomo yangu na kunisisitiza kuwa nikazane kwani elimu ndiyo ukombozi wetu.
Tulifika baharini, akatafuta sehemu nzuri na kupaki gari, pembeni ya barabara kisha tukashuka. Nikaona huo ndiyo muda muafaka wa kufanya nilichokuwa nakitaka.
“Samahani, nikitaka kuogelea kidogo utanisubiri?”
“Wala usiwe na wasiwasi, kwani huwa unapenda kuogelea?”
“Napenda sana,” nilisema huku moyoni nikifurahi kwani nilichokuwa nakitaka kilikaribia kutimia. Ibrahim alinisindikiza, tukashuka kwenye ngazi za ukingo wa bahari mpaka chini ambako haikuwa rahisi kwa wapita njia kutuona.
“Geukia kule nibadilishe nguo,” nilisema huku nikijichekeshachekesha, kweli Ibrahim akageuka na kunipa mgongo, nikavua suruali niliyokuwa nimevaa na kubaki na taiti, juu nikavua blauzi na kubaki na sidiria tu kisha nikachukua mtandio mwepesi na kujifunga juu kidogo ya kifua.
Nilifanya vile kwa makusudi kwani nilijua nitakapoingia kwenye maji na ule mtandio, utanichora mwilini na kulifanya umbo langu zuri la kuvutia lionekane vizuri. Nikaanza kutembea taratibu kumfuata Ibrahim ambaye bado alikuwa amenipa mgongo.
“Tayari,” nilisema huku nikimgusa begani, akageuka na kunitazama. Mshtuko alioupata haukuweza kujificha, alinitazama kuanzia juu mpaka chini kama ndiyo kwanza anakutana na mimi kwa mara ya kwanza, nikajua ameshaingia kwenye mtego.
“Vipi mbona umeduwaa,” nilimuuliza lakini hakuwa na jibu zaidi ya kutabasamu. Nikageuka na kuanza kutembea kwa maringo kuelekea kwenye maji, huku nikijitingisha kwa makusudi. Ibrahim akazidi kupagawa.
Nilipoingia kwenye maji, nilianza kuogelea kihasarahasara huku nikimuita Ibrahim naye aje tuogelee naye lakini alikataa, bado akawa anaendelea kunitazama kwa macho yaliyokuwa yamebeba ujumbe mzito.
Sikuogelea sana, nikachukua mchanga kidogo na kuuweka kwenye mfuko kama geresha tu kisha nikatoka kwenye maji. Kwa kuwa nilikua nimevaa taiti na sidiria tu huku juu nikiwa nimejifunga mtandio mwepesi, umbo langu lilionekana vizuri kabisa, uzalendo ukamshinda Ibrahim, akanitamkia:
“Kumbe umeumbika hivi? Loh, mpenzi wako anafaidi.” Nikacheka sana kwa furaha kwani nilichokuwa nakitaka, kilikuwa kimetimia. Tayari Ibrahim alishaanza kuonesha dalili za kunitaka kimapenzi.
Unajua sisi wanawake wengi huwa tunapenda sana kusifiwa, na mtu akishaanza kukusifia, basi ukijirahisisha kwake, lazima mwisho muishie kuwa wapenzi. Baadhi ya wanaume wanaujua udhaifu wetu huu na wamekuwa wakipitia humohumo kukidhi haja za miili yao.
Basi nikazidi kuringa mtoto wa kike, nikamtoa wasiwasi kwamba hakuna mtu yeyote anayenimiliki, nipo ‘singo’.
“Unasema kweli upo singo?”
“Ndiyo, kwa nini huamini?”
“Unajua wanawake wazuri kama wewe mara nyingi huwa hawawezi kuwa singo, tena wengine wanakuwa na mpenzi zaidi ya mmoja.”
“Wala mimi sipo hivyo, wazazi wangu wakali sana na hawapendi kabisa nijihusishe na mambo hayo ndiyo maana nimeamua kuweka nguvu zangu zote kwenye masomo,” nilisema huku nikiyarembua macho yangu mazuri, kauli ambayo ilionesha kumfurahisha sana Ibrahim.
Kwa kuwa sikuwa na nguo nyingine za akiba, ilibidi nivae nguo zangu juu ya zile zilizoloana, tukatoka na Ibrahim na kuanza kutembea kuelekea kwenye gari. Tayari akili za Ibrahim zilishabadilika kabisa kwa sababu hata wakati tukitembea, alikuwa anataka nitangulie mbele kidogo halafu akawa ananitazama kwa nyuma kwa kuibia. Nililijua hilo, nikazidisha vituko.
Basi tulifika kwenye gari, tukaingia na safari ya kurudi nyumbani ikaanza, mazungumzo kati yangu na Ibrahim yalianza kubadilika taratibu, akawa ananiuliza mambo mbalimbali kuhusu maisha yangu kuanzia vitu ninavyovipenda, nisivyovipenda, ratiba yangu ya maisha ya kila siku na mambo mbalimbali kuhusu maisha yangu.
Nilimjibu kila kitu alichotaka kukijua, hatimaye tukafika Morocco. Akasimamisha gari kituoni kisha tukaagana, nilipotaka kushuka, aliniita jina langu, nikageuka na kumtazama.
“Kuna jambo nitakwambia baadaye kwenye simu, tafadhali usikatae,” alisema huku akiwa amevaa uso uliokuwa na ujumbe mzito kwangu, nilitabasamu na kumtoa wasiwasi, nikashuka.
“Chukua hizi zitakusaidia matumizi yako madogomadogo,” alisema Ibrahim huku akinipa noti kadhaa za shilingi elfu kumikumi. Nilizipokea na kumshukuru, nikabeba furushi langu la mchanga na kuanza kuondoka kuelekea nyumbani. Naye aliwasha gari lake na kuondoka.
Kwa kuwa ule mchanga wala sikuwa na kazi nao, nilipofika mbele kidogo niligeuka na kumuangalia Ibrahim, nilipoona ameshaondoka, niliutupa ule mchanga na kuanza kuchekelea ujanja nilioutumia mpaka kumuingiza Ibrahim kwenye mtego.
Nilipofika nyumbani, nilipitiliza bafuni kuoga kisha nikabadilisha nguo na kutulia chumbani kwangu, nikiendelea kumuwaza Ibrahim. Mara simu yangu iliita, nilipotazama namba ya mpigaji, alikuwa ni Ibrahim, nikatabasamu na kuipokea nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kumsikia anachotaka kuniambia.
Alianza kwa kunisalimia, ila safari hii alikuwa akizungumza kwa sauti tulivu iliyobeba hisia nzito ndani yake. Nikamchangamkia kama kawaida yangu, akaniuliza kama nimeshalala, nikamjibu bado nasubiri nile chakula cha usiku kisha nifanye kazi niliyopewa chuoni.
“Ooh! Napenda sana mtu anayejali masomo, kazania elimu si unajua ndiyo urithi wetu?” alisema Ibrahim kisha tukaendelea na mazungumzo ya hapa na pale, bado shauku yangu ya kutaka kusikia anataka kuniambia nini ikiwa kubwa.
Cha ajabu, mpaka ananiaga, wala hakuniambia kitu ambacho aliniahidi jioni ile wakati akinishusha kwenye gari kwamba ataniambia na akanisihi nisimkatalie. Mtoto wa kike uvumilivu ukanishinda, ikabidi nimuulize. Maskini Ibra! Alibabaika sana na kuishia kuchekacheka mpaka alipokata simu.
Nilichokigundua ni kwamba Ibrahim alinipenda na alikuwa akitaka kunitongoza lakini aibu zilimjaa mkaka wa watu. Inavyoonekana hakuwa fundi wa kutongoza kama walivyo wanaume wengine. Hata hivyo kwa kuwa mimi ndiyo nilikuwa nyota wa mchezo, nilijiapiza kumfanya aweze kutongoza ili azma yangu itimie.
Alipokata simu, nilianza kumchokoza kwa meseji, nikamwambia kama ameshindwa kuniambia basi anitumie meseji. Akanijibu kwamba jambo lenyewe ni la kawaida wala nisiwe na wasiwasi. Bado sikukubali, nikaendelea kumganda kama ruba.
Wakati mwingine nilianza kuhisi kwamba Ibrahim hakuwa mwanaume wa kawaida kwa kile alichokuwa amekifanya. Mategemeo yangu yote nilidhani kwamba Ibrahim angenitongoza lakini matokeo yake, mwisho wa siku akakata simu bila kunitongoza na hata tulipokuwa tukichati hakutaka kufanya hivyo.
Mwanamke mimi, wakati mwingine nilijishtukia, nilitamani kukutana naye na kumwanzishia mazungumzo ya kimapenzi, sikupenda kabisa kila tunapokutana au kuongea simuni, alikuwa akisisitizia sana suala la elimu.
Nilimpenda Ibrahim na kila siku niliamini kwamba hata yeye mwenyewe alinipenda japokuwa hakutaka kuweka wazi. Hisia kali za mapenzi bado ziliendelea kuuchoma moyo wangu, nilikuwa nikimtamani Ibrahim leo kesho aniambie maneno ya kimapenzi na mwisho wa siku tuwe wapenzi, tupendane kama walivyokuwa wapenzi wengine.
“Ibrahim, mbona unanifanyia hivi? Mbona hautaki kuniambia ukweli kila siku unanirusha roho tu jamani?” nilijiuliza kana kwamba Ibrahim alisimama mbele yangu.
Sikujua kitu gani kilichomfanya Ibrahim kuchukua muda mrefu kabla ya kuniambia ukweli juu ya hisia alizokuwa nazo juu yangu. Si kwamba Ibrahim hakuwa akinipenda, hapana, alinipenda sana kwani hata macho yake yalikuwa yakidhihirisha hilo.
“Sasa anataka kuniambia nini?” nilijiuliza.
Wakati mwingine sikutaka Ibrahim anitongoze kwa sababu sisi wanawake unapomfanyia mwanaume mambo mengi ya kimapenzi huku ukimuoneshea ishara zote za kimahaba, hatakiwa kukutongoza bali anatakiwa kufanya mambo yote kama wapenzi, yaani leo kukushika kiuno na kesho kukubusu mdomoni.
Hiyo ndiyo hulka yetu. Kama unapata nafasi ya kumuoneshea mwanaume kila kitu halafu baadaye akaja na kukutogoza, huwa tunashangaa kwa sababu kitu ambacho huwa tunakitarajia ni kuona akianza kuonyesha mapenzi kwa vitendo, yaani kutushika hapa na pale na mambo mengine mengi ya kimahaba.
Mpaka kufikia hapo, tayari nilimuoneshea Ibra ishara zote, aliishia kunisifia tu. Japokuwa nilizifurahia sifa zake lakini bado nilitaka atamke maneno ya kimapenzi, ajaribu kunitongoza na mimi kumkubalia tu.
Ibrahim hakutaka kufanya hivyo, kitu ambacho kilikuwa kikinikera zaidi ni pale tunapokutana au kuongea halafu kuniuliza kuhusu masomo yangu tu.
Ibrahim hakutakiwa kufanya hivyo, alitakiwa kunioneshea kwamba yeye ni mwanaume anayejiamini, alitakiwa kuniambia maneno ya kimapenzi kwa sababu hicho ndicho kilikuwa kitu pekee nilichokuwa nikikitarajia kutoka kwake.
“Au hanitaki? Lakini haiwezekani, mbona kila nikimwambia twende sehemu tunakwenda? Mbona kila nikimwambia fanya hiki anafanya? Sasa kwa nini hataki kunitongoza? Au nimekuwa mbaya?” nilijiuliza maswali mengi lakini sikupata jibu.
Kuna kipindi nilikuwa nikiinuka kutoka kitandani na kukifuata kioo changu, ninapokifikia ninaanza kujiangalia huku nikiwa na nguo na mwisho wa siku navua nguo zote.
Umbo langu bado lilikuwa bora, sura yangu bado ilikuwa ikivutia na nilikuwa na uhakika wa kumteka mwanaume yeyote ambaye alikuwa akiniona kwa mara ya kwanza.
Sasa kwa haya yote, sura yangu na umbo langu bado tu Ibrahim hakuona kwamba ninatakiwa kuwa msichana wake, anipende na kunithamini? Bado Ibrahim hakuona kwamba nilikuwa msichana ninayestahili kutongozwa na mtu kama yeye?
Bado kichwa changu kilikuwa na maswali mengi yasiyokuwa na majibu, niliendelea kumfikiria huyu Ibrahim ambaye kila siku alinifanya kuwa na presha kubwa lakini hakuonekana kujali.
Kioo kilinitia moyo, ni kweli nilikuwa mrembo haswa lakini ukimya wa Ibrahim wa kutotaka kunitongoza ulinifanya nimshangae kila siku.
Wakati mwingine nilijitahidi sana kusoma makala mbalimbali za mapenzi ili kuona ni kwa jinsi gani unaweza kumtongoza mwanaume ambaye ulikuwa ukimpenda lakini yeye hakukwambia kitu japokuwa macho yake yalionesha kila kitu.
“Au nimtongoze mimi? Lakini yeye si ameshindwa bwana, kama vipi nimtongoze mimi mwenyewe,” nilijisemea.
Sikutaka kushindwa, inawezekana kabisa vitendo vyangu nilivyokuwa nikimfanyia havikutosha kumfanya anitongoze, nilichokuwa nikikifikiria ni kwamba niongeze zaidi ujuzi wangu wa kumtega huku nikijipa matumaini kwamba kuna siku atanitongoza tu.
“Ngoja niendelee naye, kesho nitahakikisha ananitongoza, nitamwambia tuonane halafu ataona,” nilijisemea na kurudi kitandani kulala huku nikiisubiria kesho.
Usingizi ulikuwa mgumu sana kupatikana, niliendelea kujigeuzageuza pale kitandani kama chatu aliyemeza mbuzi, baadaye nikapitiwa na usingizi, muda ukiwa umeshaenda sana. Kesho yake asubuhi nilipoamka tu, kitu cha kwanza ilikuwa ni kuchukua simu yangu na kuanza kumuandikia meseji Ibra.
Nikamsalimu na kumuuliza kama ameamka salama. Muda mfupi tu baada ya mimi kumtumia meseji, alinijibu kisha akanipigia kabisa. Tukasalimiana tena na kuanza kusimuliana ndoto za kila mmoja.
Japokuwa sikuota ndoto yoyote, nilimdanganya Ibra kwamba nimeota nimelala naye kitanda kimoja, akacheka sana mpaka simu ikakatika. Nikaendelea kumchokoza kwa meseji kwamba natamani ndoto yangu iwe kweli, naye akaniambia kuwa eti ameota ananivisha pete ya uchumba.
Baadaye aliniambia kuwa anikute pale kituoni Morocco ili anipe lifti, harakaharaka nikaamka na kwenda kujiandaa. Tofauti na siku nyingine, nilitumia muda mrefu nyuma ya kioo, nikijipodoa na kujipulizia manukato mazuri ili kuzidi kumtega Ibrahim. Nilipomaliza, nilitoka na kuanza kutembea taratibu kuelekea kituoni.
“Nimeshafika,” nilimtumia Ibra meseji, naye akanijibu kwamba yupo njiani nimsubiri kwa dakika chache. Kweli muda mfupi baadaye, gari lake, Carina lilipaki pale kituoni, harakaharaka mtoto wa kike nikalikimbilia huku nikijitingisha, Ibra akanifungulia mlango, nikaingia na kukaa pembeni yake.
Tofauti na siku zote, niliamua kumfanyia Ibra vituko kwa makusudi, nikamsalimu kwa kumbusu mdomoni. Hakukitegemea kitendo hicho, akabaki ameduwaa kwa sekunde kadhaa kisha akatabasamu na kunitazama usoni.
“Mbona umeshtuka sana?”
“Sijazoea,” Ibra alisema huku akijichekesha kwa aibu, nikamwambia nitamfanya azoee, akazidi kucheka. Kwa jinsi nilivyokuwa nimependeza, Ibra alijikuta akivutiwa kuendelea kunitazama tena na tena huku akiendelea kuchekacheka, na mimi nikawa namrembulia macho yangu mazuri, akazidi kudata.
“Yaani leo mwenzako sina mudi ya kusoma kabisa, natamani kama na wewe ungekuwa na nafasi tuende sehemu tukatulie wawili tu mpaka jioni,” nilimchokoza Ibrahim nikitaka kumsikia atasema nini. Kama kawaida yake, akacheka sana na kuniambia kuwa hajazoea kutegea kazi.
“Kwani wewe hakuna siku ambazo huwa unaumwa? Kawaambie kazini kwako kwamba unaumwa unaenda hospitali, wakikubali tunatafuta sehemu nzuri na kwenda kupumzika, we kila siku kazi tu huchoki.”
“Umetoa wazo, unajua mpaka nahisi macho yameanza kupoteza uwezo wake wa kuona, kila siku mimi na kompyuta tu, ngoja nikajaribu kudanganya kwamba naumwa ili wanipe ruhusa ya kwenda hospitali,” alisema Ibra, kauli ambayo ilinifurahisha mno, nikamsogelea na kumbusu tena, akazidi kupagawa.
Kweli tulienda mpaka kazini kwa Ibra, mimi akaniacha ndani ya gari kisha akateremka na kuingia ndani ya benki hiyo aliyokuwa akifanyia kazi. Baada ya takribani dakika tatu, nilimuona akitoka, mkononi akiwa na karatasi. Akaja mpaka kwenye gari na kuniambia kuwa amepewa ruhusa ya kwenda hospitalini, sote tukafurahi na kugongesheana mikono.
“Tunaenda wapi sasa kupumzika.”
“Twende Beach Comber, kwanza kule kumetulia hakuna kelele kama huku Posta, we mwenyewe utafurahi,” nilimwambia Ibra kwa manjonjo, akashindwa hata kukataa. Tukaianza safari ya kuelekea Mbezi huku njia nzima nikiendelea kumfanyia Ibra vituko kisawasawa.
Tulifika Beach Comber, tukalipia na kuingia mpaka ndani, tukaenda kukaa sehemu tulivu huku tukipigwa na upepo mwanana wa bahari. Kwa kuwa bado ilikuwa ni asubuhi, tulipata kifungua kinywa kisha tukaendelea kupiga stori za hapa na pale.
Baadaye nikamuomba Ibra nikaogelee kwenye ‘swimming pool’ iliyokuwa ndani ya hoteli hiyo ya kisasa. Alikubali ila nikawa namng’ang’aniza na yeye akubali tukaogelee pamoja, jambo ambalo hakulikubali kirahisi.
“Kama unaona aibu kubadilisha nguo hapa twende tukalipie chumba tukabadilishe nguo tuje tufurahi pamoja, tukichoka tutaenda kupumzika, au we hujafurahi kuwa na mimi leo?” nilisema huku nikizidi kumtega Ibra, akawa anakubali kila kitu kama kondoo anayepelekwa machinjioni.
Tukarudi mapokezi ambapo Ibra alilipia chumba, tukapanda ngazi na kuelekea kwenye chumba hicho tulichoelekezwa na mhudumu. Nilijiapiza kuwa siku hiyo lazima nipate ninachokitaka kutoka kwa Ibra.
Chumba kilikuwa kizuri, kitanda kikiwa kimetandikwa mashuka nadhifu na kupambwa kwa nakshi mbalimbali. Mimi ndiyo nilitangulia kujitupa kitandani, harakaharaka nikavua blauzi niliyokuwa nimeivaa na kubaki na sidiria tu, nikamuona Ibra akikikodolea macho kifua changu ambacho kilikuwa kimejaa vizuri mno.
“Na wewe vua tukaogelee, leo tutaogelea mpaka jioni, tukichoka tunakuja kupumzika,” nilijisemesha huku nikiendelea kujilegeza mbele ya Ibra. Nilipoona anakuwa mzito, nilivua na sketi yangu niliyokuwa nimeivaa, nikabaki na taiti tu, umbo langu zuri likazidi kumfanya kaka wa watu apagawe. Sijisifii lakini mwenzenu nimejaaliwa mambo flani, mwanaume yeyote aliyekamilika akiniona nikiwa kama nilivyokuwa siku hiyo, lazima atokwe na mate ya uchu.
Nikamsogelea Ibra ambaye bado alikuwa ameduwaa palepale alipokuwa amesimama, nikamfungua vifungo vya shati na kulivua, nikamfungua na suruali, akabaki na bukta huku wasiwasi wake ukionekana dhahiri machoni mwake.
Japokuwa Ibra kiumri hakuwa mtoto mdogo, inaonekana hakuwa mjuzi kabisa kwenye mambo ya kikubwa kwani alikuwa akiogopa kila kitu, hata kunigusa. Nadhani ni kwa sababu ya malezi aliyolelewa.
“Ibra! Nakupenda mwenzio, nimeshindwa kujizuia, nipunguzie mateso haya ndani ya mtima wangu, nataka uwe mume wangu,” nilijitoa fahamu na kuzungumza kwa sauti iliyokuwa inatokea puani, nikamkumbatia Ibra kwa nguvu na kumvutia kitandani, tukaanguka pwaaa, mimi nikiwa chini na Ibra akanifuata kwa juu.
Nikaanza vituko mtoto wa kike, kwa kuwa nilishamuona mwenzangu ni mgeni kabisa katika mambo hayo, niliamua kumuongoza. Taratibu akaanza kuwa vile nilivyokuwa nataka, nikaongeza mbwembwe mtoto wa kike, dakika chache baadaye, wote tulikuwa kama tulivyokuwa siku tunaletwa duniani kwa mara ya kwanza, Ibra akawa anatweta kama ametoka kukimbia mbio ndefu za marathon. Tuliendelea kupasha misuli moto kwa dakika kadhaa, hatimaye kipyenga kikapulizwa kuashiria kuanza kwa pambano la kirafiki, lisilo na jezi wala refa.
Kilichonishangaza ni kwamba licha ya kwamba tayari mimi nilishakanyaga mafuta na kilichobakia ilikuwa ni kuingiza gia tu ili gari lianze safari, mwenzangu alionekana bado kabisa. Nilishangaa sana kwani sikutegemea kwa muda wote huo tuliokuwa tukipasha misuli, mwenzangu anaweza kuwa bado hajapashika.
Ilibidi nianze kazi nyingine ya kuhakikisha gari lake linapiga ‘starter’ ili safari ya huba ianze. Licha ya kutumia uzoefu wangu wote, bado mwenzangu alikuwa vilevile, hali iliyoanza kunipa wasiwasi kuhusu uanaume wake.
“Ibra vipi mpenzi wangu?”
“Hata mimi nashangaa, sijui kwa nini leo nimekuwa hivi wakati kila siku asubuhi nikitoka kuamka mambo huwa yanakuwa mazuri,” alijitetea huku akionesha wazi jinsi alivyojisikia aibu. Maskini Ibra, alishindwa kabisa kuudhirisha uanaume wake mbele ya mrembo mimi.
Kuna muda nilijishtukia kuwa huenda sikuwa na vigezo vya kulifanya gari la Ibra lipige ‘starter’ lakini nikagundua kuwa haikuwa kweli kwani tangu nianze kuijua michezo ya kikubwa, hakuna mwanaume ambaye amewahi kutokewa na hali kama iliyomtokea Ibra siku hiyo.
Nikakumbuka kitu nilichowahi kukisoma kwenye kitabu kimoja kiitwacho Simulizi za Majonzi na Saikolojia kwamba hofu anayoipata mwanaume hasa anapokutana na mwanamke mrembo kwa mara ya kwanza, inaweza kumfanya akakosa nguvu na kushindwa kuonesha uanaume wake.
Niliamini hiyo inaweza kuwa ndiyo sababu kubwa kwa sababu tangu naingia na Ibra ndani ya chumba hicho, mwenzangu alionesha kuwa na wasiwasi mkubwa ambao hakuweza hata kuuficha, nikajikuta nikimuonea huruma.
“Basi usijali mpenzi wangu, nimetokea kukupenda na kamwe sitakuacha kwa hali yoyote, ngoja tupumzike kidogo kisha tukaogelee na tukimaliza tutarudi tena kujaribu,” nilimfariji Ibra huku nikimpapasa sehemu mbalimbali za mwili wake. Tukaendelea kujilaza pale kitandani huku nikijaribu kumdadisi Ibra maswali mbalimbali ili kumfanya arudi kwenye hali yake ya kawaida kwani kilichotokea kilionesha kumuathiri sana kiakili. Nilijitahidi kadiri ya uwezo wangu wote kumfanya aone kila kitu kuwa ni cha kawaida. Nikamuuliza kuhusu historia yake ya kimapenzi. Ibra alinishangaza sana aliposema kuwa tangu abalehe, hajawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke yeyote na kwamba mimi ndiyo nilikuwa wa kwanza.
Japokuwa sikuamini haraka, baadaye nilianza kuamini kwa sababu kweli Ibra alikuwa mgeni wa kila kitu. Tuliendelea kuzungumza mambo mbalimbali, akaniambia kuwa wazazi wake walimlea katika misingi ya kidini na kumuaminisha kwamba kukutana kimwili kabla ya kuoana, ni dhambi kubwa mbele za Mungu.
Akaniambia kuwa tangu akiwa kidato cha kwanza, alisoma shule za seminari, tena za wavulana watupu, jambo ambalo lilifanya iwe vigumu kukutana au kuzoeana na wasichana mpaka alipohitimu kidato cha sita. Tuliendelea kuzungumza mambo mbalimbali huku nikiendelea kumfanyia vituko mbalimbali vya kimahaba.
Kwa mbali nikaanza kumuona akisisimka na kadiri nilivyoongeza mbwembwe ndivyo alivyozidi kuimarika kama mwanaume aliyekamilika anavyotakiwa kuwa. Hali hiyo ilinifurahisha mno kwani sasa nilikuwa na uhakika kwamba ataikata kiu kali ya penzi lake niliyokuwa nayo.
Mtoto wa kike nilizidi kujituma, kweli Ibra akafikia kiwango nilichokuwa nakihitaji ingawa mapigo yake ya moyo yalikuwa yakimuenda mbio mno. Sikujali, nikaendeleza utundu na hatimaye gari lake likapiga ‘starter’ na kuwaka, mambo yakawa mazuri.
Sikutaka kupoteza muda, harakaharaka mtoto wa kike nikajiweka sawa kwa safari, nikamsaidia kuingiza gia ili gari lianze safari lakini ndani ya sekunde chache tu, tayari Ibra alinitangazia kufika mwisho wa safari yake, jambo ambalo lilinikasirisha mno.
Nilichokipata wala sikukipata kama nilivyotegemea zaidi ya kuambulia mateso makali mno, nikawa namlaumu Ibra kwa nini aliamua kuniacha njiani peke yangu katika safari ile niliyokuwa naisubiri kwa hamu lakini hakuwa na jibu zaidi ya kujiinamia kwa aibu.
Ni hapo ndipo nilipogundua kuwa kumbe Ibra alikuwa na tatizo kubwa la upungufu wa nguvu kiasi cha kukosa kabisa uwezo wa kukidhi kile nilichokitaka. Japokuwa aliniudhi lakini kwa upande mwingine nilimuonea sana huruma na kujiapiza kuwa lazima nimsaidie.
ITAENDELEA
My Repentance (Kutubu Kwangu) Sehemu ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;