Hofu Sehemu ya Pili
IMEANDIKWA NA : ARISTABLUS ELVIS MUSIBA (A.E MUSIBA)
Simulizi : Hofu
Sehemu Ya Kwanza (2)
Kijana huyu alitabasamu kisha akawaashiria wanyamaze na yeye akaendelea kusema. “Azimio la Arusha lilitangazwa mnamo mwaka 1967. Kutokana na tangazo hilo, makampuni makubwa ya binafsi yalitaifishwa. Hatu hiyo ilifanya siasa ya ujamaa ianze kuonekana. Lakini utaona kwamba tangu kutaifishwa kwa makampuni hayo uchumi wa nchi uliendelea kukua kwa kiwango kilichoridhisha. Uchumi ulikua kwa asilimia tano kila mwaka, hadi mwaka 1977. Tulikuwa na fedha za kigeni kiasi cha kutuwezesha kuagiza bidhaa za kukidhi mahitaji ya taifa kwa muda wa miezi mitano. Wakati huo wote sisi tulikuwa hatupati msaada wa fedha kutoka benki ya dunia wala shirika la fedha la kimataifa”.
“Hao wenzetu mnaowasema, uchumi wao wakati huo ulikuwa ukikuwa kwa asilimia mbili tu kwa mwaka. Na kukuwa kwa uchumi wao huo kulitokana tu na misaada ya fedha kutoka benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa. La sivyo hali yao ingekuwa mbaya zaidi kuliko sisi. Kwa muda wa miaka kumi ya kwanza ya siasa ya ujamaa, uchumi ulikuwa vizuri sana. Ni muhimu kukumbuka kuwa mnamo miaka ya 1973 – 1976 bei ya mafuta ilipanda. Vile vile kulitokea ukame. Lakini uchumi wa nchi uliendelea vizuri hii inaonyesha wazi kuwa siasa ya ujamaa haikuwa chanzo cha kuanguka kwa uchumi wa taifa letu”.
“Ngoja nikukate kilimi”, Sammy alimkatiza yule kijana.
“Sasa unafikiri nini kimetokea kama kweli sababu zako ni sawa sawa?”.
“Nilikuwa naelekea huko”, yule kijana aliendelea kusema.
“Kuanzia mwaka 1978 mambo yalikwenda mrama. Na mambo yote yalitokana na chanzo kilizho nje ya siasa ya aina yoyote. Kwanza Jumuia ya Afrika Mashariki ilivunjika. nyinyi mnajuwa kuwa hiyo ilitifanya tukose vitu kadhaa pamoja na huduma kutoka nchi wanachama wa jumuia hiyo. Bei ya mafuta iliongezeka sana kiasi cha kuathiri uwezo wetu utokanao na fedha za kigeni. Ukame pia uliathiri uchumi wetu. Zaidi ya hayo kulitokea vita kati yetu na majeshi ya uvamizi ya Nduli Iddy Amin. Mambo hayo ndiyo yalifanya uchumi wetu kuyumba. Na mbali na hayo, kumetokea hali fulani ndani kwa ndani. Ari ya mfanyakazi imedhorota”.
“Hali ngumu ya maisha imewafanya maafisa wa ngazi za juu kuendekeza rushwa. Ni dhahiri kuwa kuna maamuzi yanafanywa na maafisa wa serikali bila kujali maslahi ya umma. Si ajabu kuona vibari vinatolewa kuhusu matumizi ya fedha za kigeni kwa shughuri ambazo siyo muhimu. Wakati ule ule sekta za uzalishaji kama kilimo na viwanda zinanyimwa fedha za kigeni za kununulia pembejeo na kadharika siyo sahihi, kwa kweli, kusema kwa njia ya mkato kwamba mambo haya yamesababishwa na siasa ya ujamaa. Na kama nilivyokuwa nimesema hapo awali, shirika la fedha la kimataifa na benki ya dunia havikutupatia hata senti tano. Wakati huo huo wenzetu walipewa mamilioni ya fedha za kigeni”.
“Nia ya vyombo hivi ilikuwa kuhakikisha kuwa uchumi wetu unaanguka kwani vilichukia siasa ya ujamaa ambayo ni ya kimapinduzi. Walikataa kutusaidia huku wakifahamu fika kuwa matatizo yetu hayakutokana na siasa ya ujamaa. Lakini iliwafaa kutusingizia. Sasa pia na nyinyi mmejiunga na mabepari katika kulaumu badala ya kujiimarisha…”.
“Mara muhudumu mmoja wa hoteli hiyo alifika hapo mezani na kuuliza, “Wewe si ndiye Willy Gamba?”.
“Ndio”, yule kijana alimjibu haraka muhudumu.
“Kuna simu yako mapokezi”.
“Ahsante. Hebu nikasikilize simu halafu nitakuja tuendelee”.
Yule kijana aliondoka na kuwaacha wameduwaa kutokana na maelezo yake mazito na yenye msingi.
Pale mapokezi alimkuta muhudumu wa kike.
“Wewe mwanamume, hapo ulipokaa una bibi na bado unatafutwa na bibi mwingine”, muhudumu wa kike alimtania yule kijana. “Hutosheni mwenzetu?”.
“Nifanye nini, bibie, na wakati ndio huu! lazima niutumie ujana wangu, sitaki kuujutia nikishazeeka”, Willy alijibu, kisha akauchukua mkono wa simu na kuupachika kwenye sikio lake.
“Unauchapa tu mwenzetu”, sauti ya Maselina ilisikika waziwazi sikioni mwa Willy Gamba.
“Unataka kuja?”, Willy aliuliza.
“Unataka huyo bibi yako anikate masikio?” Sina haja ya kuharibiwa sura mwenzako.
“Sasa unasemaje?”.
“Nasema hivi: niko ofisini pamoja na Chifu. Unatakiwa kama ulifikili mambo yamekunyookea na huyo msichana uliyenae, basi ulie tu. Unatakiwa sasa hivi. Umenielewa?”, Maselina alisema kwa kebehi.
“Hamniachii angalau sikukuu hii nikala raha kidogo?”.
“Njoo umweleze mwenyewe maneno hayo huyu babu yako, kwani mimi hiyo raha siitaki? Au kwa kuwa umenizoea unafikiri mabwana hawanitaki. Hata mimi nimechomolewa kutoka kwenye raha na pilika pilika safi za Iddy El Fitri.
“Wacha utani; nakuja sasa hivi”.
Willy aliyakata mazungumzo, kisha akaiweka simu chini.
“Vipi huyo mkeo?”, yule msichana wa mapokezi alimuuliza Willy mara alipokata simu.
“Afadhali ningekuwa na mke”, alijibu Willy huku akielekea kwa wenzake.
Alipofika mezani ilibidi anywe pombe yake haraka ili aweze kuondoka. Jambo zuri ni kwamba vijana wote walikuwa wanafanyakazi ofisi moja na Willy ndiye alikuwa mkubwa wao wa kazi.
“Samahani”, Willy aliwataka radhi vijana wenzake. “Imenilazimu nikitoe. Kuna mZee wangu ameshikwa na ugonjwa wa ngiri. Lazima nimpeleke hospitali”.
Wale vijana wenzake walielewa ana maana gani ila wale wasichana masikini walidhani maneno ya Willy yalikuwa ya kweli.
“Oh pole sana,” Rukia na Esther walisema kwa pamoja.
“Ahsante. Mwana, tunakwenda au unabaki? Willy alimwuliza mpenzi wake.
“Nibaki vipi?” Mwana alihamaki, “huoni kitu mtu hapa? Je, ukiniacha halafu wenzangu wakaamua kuchukua vyumba vya kulala, mimi nitafanyaje?”
“Kwangu wawili ni saizi,” Sammy alitania” usiwe na wasiwasi”.
“Rukia mwenzetu, mbona unayo shida.”
“Maneno tu. Atawahi? kila siku jasho linamtoka,” Rukia alijibu huku Mwana na Willy wakiinuka kuondoka.
Willy Gamba alikuwa ni mpelelezi maarufu aliyekuwa akifanya kazi katika idara ya upelele ya Tanzania. Sifa zake zilitapakaa katika Bara zima la Afrika. Kutokana na ujasiri wake, watu wengi walifikiri mtu huyu alikuwa wa kubuniwa tu maanaa watu walifikiri kuwa vitendo vya Willy Gamba vilikuwa kama mchezo wa sinema.
Lakini ukweli ni kwamba huyu mtu yupo na vitendo vyake ni vya kweli tupu. Kijana huyu alikuwa amefanyakazi kubwa sana katika kusaidia harakati zinazoendeshwa na umoja wa nchi huru za Afrika. Kwa sababu hiyo yeye alijulikana katika Afrika nzima. Watu wengi waliohusika na kazi yake na wale waliobaki waliishia kusoma na kusikia habari zake bila kuamini.
Wakati akiendesha gari lake kuelekea mjini, Willy alikuwa na mawazo mengi. Maswali mengi yalimjia kichwani. Kwanini, kwa mfano, Chifu alikuwa anamhitaji wakati wa sikukuu kama hii?, lakini alihisi kulikuwako na kazi muhimu, kwani haikuwa kawaida ya Chifu kumbugudhi wakati wa mapumziko kama hayo. Chifu, kama alivyoitwa, ndiye alikuwa mkubwa wake wa kazi. Alikuwa Mkurugenzi wa upelelezi nchini Tanzania. Alikuwa Mzee wa miaka mingi katika kazi hiyo na sifa zake zilitapakaa mahali pengi, hasa kwa kumtoa kijana shupavu kama Willy.
Willy alipofika njia panda kati ya New na Old Bagamoyo ndipo mawazo yake yaliporudi kwa huyu msichana ambaye alikuwa pamoja nae kwenye gari. Msichana huyu alikuwa ameanza kusinzia. Mwana alikuwa anaishi sehemu za Mwenge, sehemu iliyo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
“Mwana”, Willy alisema. “Nitakupeleka nyumbani kwako halafu mimi nitaendelea na safari”.
“Aka, babu, twende wote”, Mwana alilalamika.
“Kwani huyo Mzee wako mimi siwezi kumpeleka Hospitali?”.
“Wewe unajuwa Mzee anayeumwa ngili anakuwaje?, unataka kukosa radhi kwa kuangalia vitu vya wazee, nini?”, Willy alimwasa huku akipinda kona kuingia barabara ya New Bagamoyo.
“Hukosi sababu wewe. si ajabu ni mwanamke mwingine unayemfuata huku ukinidanganya, maana wewe umezidi”, Mwana alijibu huku machozi yanamlengalenga.
“Wacha wivu usiokuwa na msingi mama, haukusaidii kitu. Kama ningekuwa na bibi mwingine kwanini nikuchukue wewe tangu asubuhi?, na huyo bibi ana nini mpaka nikurudishe na kumfuata yeye wakati wewe kwangu ndio mipango inanyooka?”, Willy aliuliza huku akicheka.
“Eh, huenda mipango yake ni zaidi. Nitajuaje mie?”, MWana alisema kwa kejeli.
“Afadhali ningekuwa na bibi kama huyo. Lakini hawajaanza kuzaliwa. Nasikia wataanza kuzaliwa mwaka Elfu mbili”, Willy alijibu.
“Wacha maneno mengi, utarudi?”.
“Usiwe na wasiwasi. Nikimaliza shughuri na mzee nitarudi”.
“Au ukaniache nyumbani kwako”, Mwana aliomba kwa sauti nyororo.
“Mimi nitakuja kwako, si mzee yuko nyumbani au hunielewi?”.
“Si mimi nitampikia?”.
“Asante, lakini bado sijakutambulisha rasmi. Subiri mpaka nifanye hivyo kwani wazee hawa wana nyadhifa zao”, Willy alisema huku akikata kona kuelekea nyumbani kwa Mwana. Walipofika Mwana alimvuta Willy na kumpa busu kali kisha kumwachia huku akisema, “Usiporudi usishangae kusikia kuwa nimekula kulolokwini kumi, wala usinilaumu”.
“Nitarudi”, Willy aliahidi.
Baada ya Mwana kutelemka, Willy aliondoa gari, moyoni alikuwa anashangaa jinsi wasichana walivyo. Hii ilikuwa miadi ya pili tu kati yake na Mwana. Hata hivyo msichana huyu alikuwa amekufa hasa kwa Willy. Willy aliendesha moja kwa moja hadi ofisini kwake katika mtaa wa Samora, katikati ya Jijini. Baada ta kuegesha gari alipanda ngazi. Aliongoza moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya Chifu. Alipofungua mlango kuingia kwa Katibu Muhtasi wa Chifu, alimkuta Maselina ameng’ang’ana na simu.
“Pole mwenzangu, nakwambia kazi hii itakuja kutuua siku moja”, Maselina alimkebehi Willy.
“Inatufaa lakini. Yupo?”, Willy aliuliza.
“Aende wapi!, leo kawa mzee ile mbaya, sijui nini kinamtia homa mzee wako”, Maselina alimwalifu.
“Basi ukiona hivyo ujuwe mambo ni yale yale. Asipostaafu huyu mzee atakuja kutufia humo ofisini kutokana na ugonjwa wa moyo”.
“Afe kwa ugonjwa wa moyo?, kwa ugonjwa huo utakufa wewe kabla yake. Mzima kweli huyo”, Maselina alisema.
“Umeshajaribu kutingisha kiberiti na kujua ziko njiti ngapi nini?”, Willy alitania.
Maselina alichukua rula na kutaka kumpga nayo. Willy aliepa huku akikimbilia mlango wa ofisi ya Chifu.
“Muhuni mkubwa, we!”, hayo ndio maneno aliyoyasikia Willy yakitoka kinywani mwa Maselina.
Watu hawa wawili walikuwa wamefanyakazi pamoja kwa muda mrefu. walikuwa wakielewana kiasi kwamba walikuwa kama kaka na dada mtu au hata mpenzi.
Willy alipofungua mlango wa kuingia ndani alimkuta Chifu anasoma gazeti la Daily News.
“Shikamoo mzee”, Willy alisalimia.
Chifu aliinua kichwa na kumtazama usoni.
“Marahaba. Imebidi nikuite maana nimepata habari ambazo zinahitaji sisi kuzishughulikia mara moja”, Chifu alieleza.
“Nimepata habari kutoka Lusaka kuwa kumefanyika mkutano kati ya wakurugenzi wa upelelezi wa Zambia, Zimbabwe, Angola, Msumbiji na Botswana, pamoja na wakuu wa upelelezi wa wapigania uhuru. Sisi hatukuweza kuwakilishwa kutokana na sababu ambazo hazikuweza kuzuilika. Mazungumzo yao yalihusu mkutano wa wapigania uhuru ambao utafanyika kesho kutwa huko Arusha. Nafikiri unazo habari”.
“Ndio ninazo”.
“Kuna habari za kuaminika kwamba makaburu wana nia ya kuleta maafa makubwa na kuvuruga mkutano huo. Habari hizi ni za kipelelezi. Sasa sisi tunaombwa tuwe macho. Ingawa idara ya Polisi ilishajidhatiti kwa ulinzi huko Arusha, ni lazima na sisi tushughulikie suala hili kikamilifu. Hii ni kwamba kama kweli makaburu wamenuia kutenda kitendo hicho, bila shaka watatumia majasusi wa hali ya juu ambao wana uwezo mkubwa. Tayari wapigania uhuru wameshatuma mpelelezi wao maarufu Bon Sipele. Serikali ya Zimbabwe nayo imetuma mpelelezi wake mashuhuri Rocky Malele. Hao watawasili hapa leo jioni wakiwa njiani kuelekea Arusha…”.
“Kwa hiyo hatuna budi kuungana nao leo hii ili kuimalisha usalama wa mkutano huu. Wakuu wa nchi wamekwisha julishwa. Vile vile Kamati ya ukombozi wa nchi huru za Afrika pamoja na wapigania uhuru wameaziimia mkutano huo lazima ufanyike. La sivyo, litakuwa pigo kubwa kwa wapigania uhuru na Afrika nzima na ushindi kwa makaburu. Kwa hiyo Willy hatuna uhakika makaburu watatumia mbinu gani. Ni dhahiri kuwa makaburu hawatatumia Jeshi ingawa Jeshi letu tayari limewekwa katika hali ya tahadhari tunahisi makaburu watatumia majasusi ili kuhujumu mkutano na ikibidi kuua wajumbe wengi kadiri inavyowezekana…”.
“Kazi yako wewe na wenzako ni kuhakikisha kwamba jambo hili halitokei na mkutano utafanyika kama ulivyopangwa. Huo ndio utakuwa ushindi kwa Bara la Afrika na vile vile kuwatia hamasa wapigania uhuru. Baada ya mkutano huo wapigania uhuru watakuwa na nguvu mpya. Hivyo makaburu watakiona cha mtema kuni. Nafikiri umenielewa”, alimalizia Chifu.
“Hatua gani za tahadhari zimechukuliwa awali, kwani inawezekana majasusi na makaburu wameshaingia nchini tayari”, Willy aliasa.
“Walinzi wote kwenye mipata wameshatahadhalishwa na jeshi la polisi linafanya kazi yao. Viwanja vya Ndege vya Dar es Salaam na Kilimanjaro viko kwenye hali ya tahadhari. Wana usalama wanapekuwa vikali kila mtu anayeingia na kutoka. Wote wako macho. Kama ni kuingia nchini Majasusi hawawezi kuingia nchini mapema kwa kuogopa kugutukiwa”, alijibu Chifu.
“Je wajumbe wameshawasili?”, Willy aliuliza.
“Kufuatana na ripoti ya Polisi baadhi ya wajumbe wameshaanza kuingia. Wengine wako Arusha tayari. Ndio sababu lazima nyinyi muondoke leo. Tuketi yako iko tayari kwani Maselina kaishaandaa kila kitu kwa ajili ya safari yako”, Chifu alimwambia Willy.
“Ni nani tutashughulika nae huko Arusha?”.
“Hatutaki Polisi huko Arusha wajuwe kuwa nyinyi mnakwenda huko. Wakijuwa hivyo wanaweza kuridhika kuwa usalama upo halafu wasifanye kazi yao barabara. Hata hivyo Afisa Usalama wa mkoa anayo habari. Hivyo huyo ndiye mtu wa kumuona. Ndiye mtu wa kumwamini”.
“Ni sawa kabisa, Hamisi ni mtu wa kuaminika. Lakini mbali na Hamisi, nisingependa mtu mwingine ajuwe kwani mimi nafahamu majasusi wa makaburu wanavyofanya kazi yao”, Willy aliongezea.
“Sasa nenda ukajitayarishe. Vile vile nataka ripoti kutoka kwako kila wakati unapogundua kuna kitu kipya. Kama utahitaji msaada wa vijana wako uko huru kufanya hivyo, kwani watakaa hapa ofisini katika hali ya tahadhali”, alisema Chifu.
“Ahsante, tuombe Mungu”, Willy alijibu.
Alipofika karibu na mlango Chifu alimwita tena.
“Willy, chunga sana kwani makaburu siyo watu wa kawaida”, Chifu alionya.
“Nitajihidi na Mungu atatusaidia”. Willy alijibu na kutokea kwenye ofisi ya Katibu Muhtasi.
“Kwanini ukunibonyeza kwamba ninasafiri na wewe ndiye uliyekata tiketi, una visa wewe”, Willy alimwambia Maselina.
“Nikwambie nini, mimi ndiye niliyekuajiri?. Mimi siyo mmbeya, bwana wewe”, Maselina alisema.
“Najua unafurahi rohoni kwa kuwa mimi nasafiri. Wacha roho mbaya”.
“Wewe Willy, wacha kuniumiza roho. Unajuwa jinsi gani ninavyojisikia ovyo unaposafiri. Mimi siyo kama hao wahuni wako, leo ukienda usirudi kesho wanao wengine. mimi kwangu wewe ni rafiki ambaye hana kifani na siwezi hata kufikiri ninaweza kuishi vipi bila wewe”, Maselina alieleza kwa masikitiko makubwa.
“Niombee na Mola atanisaidia”, Willy alijibu.
“Nakuombea kila siku”, alimwambia Willy huku akimpa tiketi yake, “Chunga sana”.
“Ahsante Maselina, nitajitahidi”, Willy alijibu akainama akambusu kwenye shavu halafu akaondoka.
Wakati Willy alipokuwa anaelekea kwake alianza kuwafikiria akina Bon na Rocky. Kule kuwafikiria kulimfanya apate nguvu rohoni mwake. Hii ilitokana na kwamba Willy aliwafahamu fika hao wenzake na zaidi ya hayo aliwaamini. Alifikiri sana juu ya kazi iliyokuwa mbele yake. Ni kweli kwamba kazi hiyo ilikuwa imewekewa uzito wa hali ya juu kama ilibidi kuwatuma watu wote hawa watatu katika operesheni moja. Mchukue Bon. Kwa mara kwanza Bon kufahamiana na Willy ilikuwa huko Japan ambako wote wawili walikuwa wanachukua mafunzo ya Ninja. Willy alikuwa amehitimu mapema na kumwacha Bon ambaye alikuwa amejiunga na chuo hicho nyuma yake. Willy alikuwa amemsaidia sana Bon katika masomo yake na alijuwa fika kwamba Bon nae angehitimu tu.
Bon alimchukulia Willy kama kaka yake na wote wawili walipendana sana. Baada ya mafunzo yake Bon alirudi Zimbabwe ambako alikuwa anakaa. Wakati huo Kamati ya Ukombozi ya nchi huru za Afrika iliwatuma kazi muhimu ambayo waliifanya kwa mafanikio makubwa. Kazi hiyo ilifanyika ndani ya Afrika Kusini na mpaka leo makaburu hawaamini kwamba kazi hiyo ilifanyika na watu wawili. Kisa hiki kukieleza kingechukua siku nzima, hivyo naachia hapa. Bali tu niseme kuwa safari yao huko Afrika Kusini iliwafanya wafahamiane vizuri na kila mmoja kudhibiti ujuzi na uwezo wa mwenzake. Kwa hiyo Willy, alipojuwa kuwa angekuwa na Bon katika kufanya kazi hii, basi wasiwasi ulitoka.
“Ninja wawili kutumwa Arusha. Kwani huko kuna nini?, labda makaburu watume jeshi zima”, Willy alijisemea kimoyomoyo. Alimfikiria Rocky pia. Ingawa ni mara yake ya kwanza kufanyakazi nae, umaarufu wake ulijulikana Afrika kote. Walikuwa wameonana mara mbili. Lakini ilijulikana Rocky alishatumwa kazi ambazo zilifanana sana na kujituma mikononi mwa kifo. Pamoja na hali hiyo, Rocky alikuwa amefanyakazi hizo na kurudi salama. Kuweza kufanyakazi kama hizo kulimdhihilishia Willy kuwa Rocky alikuwa mtu jasiri sana. Willy aliamini kuwa yeye na vijana hao wawili walikuwa na uwezo wa kuwazuia makaburu kusababisha maafa katika mkutano huo muhimu wa wapigania uhuru.
Kulikuwapo habari za kipelelezi kuwa baada ya mkutano huo, mapambano ya kupigania uhuru yangeahamia ndani ya Afrika Kusini. Kwa hiyo kama makaburu walikuwa na fununu juu ya habari hizi, ilikuwa ni dhahiri kwamba wangejitahidi kuvuruga mkutano huo, kinyume cha kufanya hivyo ilikuwa kufungua mlango ili wapigania uhuru waiangishe serikali ya makaburu. Makaburu walijuwa fika kuwa mkutano huo ulikuwa hatua ya kwanza muhimu katika safari ya kuuangusha utawala wao bila kujali safari hiyo ilikuwa ndefu kiasi gani. Kuzuia hatua hiyo ilikuwa lazima kwao.
Alipofika nyumbani Willy alikwenda bafuni na kuoga. baadae alifungua sanduku lake ambamo alikuwa anatunza zana zake muhimu za kufanyia kazi. Alizichukua na kuziweka kwenye mkoba wake, alipiga simu kwa Sammy ambaye alimwarifu kuwa alikuwa anasafiri kwenda Arusha na kuwa habari zaidi angezipata ofisini. Vile vile aliomba atumwe mtu uwanja wa ndege kwa ajili ya kurudisha gari lake. Sammy alikuwa chini ya Willy kikazi lakini walikuwa marafiki wakubwa sana na mara nyingi walifanyakazi pamoja. Baada ya kupiga simu aliondoka kuelekea Mwenge ili kumwaga Mwana.
Alifika nyumbani kwa Mwana mnamo saa moja usiku. Tiketi yake ilikuwa inaonyesha kuwa safari yake ilikuwa saa tatu na nusu usiku. Hivyo Willy alikuwa bado na muda kuzungumza machache na mpenzi wake. Alipofika alibisha hodi na kufunguliwa mlango. Alikaribishwa ndani. Mwana alikuwa amejinyoosha na huku amejifunga kanga tu.
“Afadhali umekuja, nilikuwa na wasiwasi! vua ulale”, Mwana alimwambia Willy.
“Nimekuja kukuaga”, alijibu Willy.
Mwana aliinuka na kanga aliyokuwa amejifunga ikadondoka. Willy alitupa macho yake na kuona mwili wa mtoto huyu ambaye ubichi wake ulisisimua na kuchangamsha roho. Matiti yalisimama kwenye kifua chake kilichokuwa kinatweta utafikiri ni mapera yaliyoiba. Mwana alimrukia Willy aliyekuwa amekaa kwenye tendegu la kitanda na kumkumbatia. Joto la msichana huyu lilimwingia willy kama kisu kinavyotoka na kuingia ndani ya siagi. Ilihitaji mtu mwenye roho ngumu kama Willy kushinda jaribu hili.
“Mwana tafadhari niache niende”, Willy alimsihi.
Mwana ambaye sasa alikuwa anatokwa na machozi alisema kwa uchungu, “Willy, kwanini unanitesa? kama hunitani si heri unieleze tu. Kama huna hamu na mimi kwanini ulinidanganya tangu siku ya kwanza. Kwanini usingeniambia ukweli kuliko kunitesa hivi, ooh! mungu wangu nimekosa nini mie”.
Mara Mwana alijitupa kitandani na kuanza kulia; machozi yakimtililika kama mtoto mdogo.
“Mwana tafadhali, kuna kazi imetokea ghafra. Nilipotoka tu hospitali kumpeleka mzee nilikuta tiketi na ujumbe kutoka kwa mkubwa wetu wa kazi kuwa lazima niende Arusha. Kama ujuavyo sisi wafanyabiashara safari zetu ni za ghafra ghafra tu. Wewe unafikiri ni kijana gani ambaye anaweza kumwacha msichana mbichi kama wewe kwa siku na saa kama hii, na hasa baada ya raha ya leo mchana? Huyo huenda siyo mwanaume kamili”, Willy alijibu kwa uchungu pia kwani hata yeye alikuwa amesisimka.
“Basi lala angalau kidogo. Dakika tano tu”, Mwana alimwomba Willy.
“Mwana mambo haya hayaendi namna hiyo. mimi nitarudi baada ya siku mbili au tatu. Baada ya hapo wewe mwenyewe utajua kuwa nina hamu kiasi gani mimi na wewe,” Willy alijibu.
“Haya nenda. Nakuruhusu,” MWana alisema kwa uchungu.
Willy aliinama na kumbusu. Alisikia lile joto tena. Bila kusita aliinuka, akafunga mlango nyuma yake na kwa maudhi alijisemea, “Kwa kweli kazi nyingine……!”.
Alipoingia ndani ya gari aliweka nyuma mawazo kuhusu Mwana. Wakati akiendesha gari, alifikiria safari iliyokuwa mbele yake.
Alifika uwanja wa ndege saa mbili usiku. Aliweka gari lake kwenye maegesho. Kisha alitoa swichi kwenye funguo zake na kuiweka mahali pa hifadhi ya swichi za magari. Hivyo ingemwezesha kijana ambaye angekuja kurudisha gari lake kuichukua hapo. Alifunga milango mitatu na kuacha mmoja umerudishiwa. Kisha kuchukua mkoba wake na kuelekea kwenye jengo la uwanja wa ndege.
“Tiketi yake tafadhari”, aliomba Afisa Usalama hapo uwanjani.
Wakati anatoa tiketi yake alikuwa akiangaza huku na kule katika jengo zima.
“Haya endelea”, alisema Afisa Usalama huku akimrudishia Willy tiketi yake.
Alielekea ndani. Kwenye kaunta alimkuta msichana aliyemfahamu.
“Willy, safari tena?”, msichana aliuliza.
“Ndio”, alijibu Willy.
“Wapi”.
“Arusha”.
“ZIko ndege mbili usiku huu. Wameongeza nyingine kwa sababu wageni wengi wanakwenda Arusha kwenye mkutano”, msichana yule alimweleza Willy.
“Alaaa, sasa mimi niko ndege ipi?”, Willy aliuliza.
“Chaguo lako. Sema unataka ipi. Iko ya saa tatu na nusu na pia ile ya saa nne na nusu”, mischana alijibu.
“Subiri kwanza, ile ndege kutoka Harare imefika?”.
“Ndio. Imefika saa moja”.
“Kulikuwamo wageni wangu wanaopitiliza kwenda Arusha”, Willy alisema.
“Majina yao tafadhari”, msichana aliomba huku akimsogeza Willy pembeni ili watu wengine wasiweze kusikia. Halafu alimtaka aendelee.
“Sipele na Malele”.
Msichana yule aliangalia kwenye orodha ya majina ya wasafiri kisha akainuka.
“Ya, wote wapo. Sasa hivi wanakula kwenye mghahawa hapo juu. Wataondoka kwa ndege ya saa nne na nusu”, msichana alieleza.
“Oke, mimi niweke kwenye ndege ya saa tatu na nusu”, Willy alisema.
Jina lake liliwekwa katika orodha.
Halafu alisema, “Hebu nikawaangalie hapo juu”.
Alipopanda kwenye baa na mghahawa alikuta watu wamejaa ndii. Huku akisalimiana na watu huku na pale, Willy alijipenyeza kupita kwenye baa mpaka kwenye mghahawa. Mara aliwaona Bon na Rocky wamekaa kwenye kona wakila na kuzungumza. Aliwaendea polepole na Rocky ndiye alikuwa wa kwanza kumuona Willy.
“Bon, Willy yule”.
“Aaaa mzee!”, Bon alisema kwa furaha huku akiinuka na kumkumbatia Willy.
“Usinipakazia uzee, Bon, au huoni humu ndani kuna watoto. Unataka kuniharibia soko, vipi?”, Willy alisema kwa mzaha.
“Hujaacha matani yako tu?”, Bon aliuliza huku wakipeana mikono.
“Keti, bwana”, Rocky alimvutia kiti.
“Ehee, leteni habari”, Willy alisema.
“Mambo safi”, Rocky alijibu.
“Safari, je”.
“Safi kabisa”, alijibu tena Rocky.
“Tulipata habari kuwa tungeungana hapa”, alisema.
“Mimi nimeambiwa leo mchana”, Willy alijibu.
“Kila mara huyo mzee wako anapenda kukushtusha”, Bon alitania.
“Wazee wengine kama ujuavyo…”, alisema Willy.
“Chakula vipi”, Rocky alimuuliza willy.
“Mimi ndiye napaswa kuwauliza swali hilo kwa kuwa mko nyumbani kwangu”, alisema Willy.
“Tumwisha jikaribisha”, Bon alijibu.
“Vipi mzee wako kakupasha kidogo?”, Rocky alimuuliza Willy kwa sauti ya chini.
“Kanipasha”, Willy alijibu.
“Je, tutasafiri katika ndege moja”.
“Hapana, mimi sina budi nitangulie na ile ya tatu na nusu, kama ujuavyo wote hatuwezi kusafiri katika ndege moja, ikianguka, je”, aliuliza Willy.
“Willy hubadiliki”, Rocky aliuliza.
“Siku nikibadilika ndio siku nitakapoacha kazi hii”, Willy alijibu.
“Ni kweli, maana waati huo itakuwa ni hatari kwa maisha yako”, Bon aliongeza.
Waliendelea kuzungumza huku wakiangalia kwa chati; kila kona ili kuona kama kuna watu waliowatia maanani. Lakini kufuatana na hali ya mambo ilionekana kila mtu alikuwa anashughulika na mambo yake.
“Tukutane hotelini kwangu mnamo saa sana usiku”, Rocky alieleza.
“Wewe uko hoteli gani?”, Willy aliuliza.
“Mimi niko Equator Hoteli kwa leo halafu nitahamia Maunt Meru hapo kesho, Bon alitaka Safari Hoteli”, Rocky alimjibu.
“Basi mimi naona tukutane kesho asubuhi, mpate kupumzika leo kwani huenda kukawa na kazi kali baadaye. Mimi nitafikia New Arusha Hoteli”, Willy alieleza.
“Mimi nafikiri maneno yako ni sahihi Willy”, Bon alijibu.
“Oke, tuonane wapi na saa ngapi”.
“Njooni hotelini kwangu saa tatu asubuhi”, alijibu Willy.
“Oke, ahadi……..”, Rocky alijibu.
Mara walisikia tangazo;
Shirika la ndege Tanzania: Ndege namba 1001 iendayo Arusha, niko tarari kuondoka, abiria wote wanaosafiri na ndege hii wanaombwa kuelekea kwenye ndege hiyo sasa hivi.
“Jamani eeh, kwaherini. Tutaonana kesho”, Willy aliwaaga wenzake na kukimbia akitelemka chini.
Alipofika kwenye kaunta alimkuta tena yule msichana.
“Siku nyingine utaachwa wewe”.
“Niko macho”, Willy alijibu.
“Utaniletea nini ukirudi?”.
“Vitunguu”.
“Nitafurahi sana. Haya safiri salama”, yule msichana alimwaga.
“Ndipo Willy alikumbuka kuwa alikuwa hajakata tiketi ya malipo ya kiwanja. Hivyo alifanya karaka na kukata tiketi hiyo. Halafu alirudi na kwenda kwenye chumba cha kuondokea. Hapo chumbani Willy alikuta msururu bado mrefu sana.
“Lo! Leo pana jua nini iko. Watu hapana panda”, Mhindi mmoja alilalamika.
Huenda kuna mtu anayo bastola. Labda wanaogopa kutekwa nyara maana hapo ndani wanakagua sana”, Kijana mmoja alijibu.
Msururu huo ulikwenda pole pole, lakini hatimaye wote walipekuliwa. Kisha waliruhusiwa kuingia ndani ya ndege. Willy alikuwa ameridhishwa na upekuzi ule kwani ulikuwa upekuzi kweli kweli.
Willy alikaa nyuma kiti cha mwisho kama kawaida yake. Alifunga mkanda na kisha na kisha akakaa akisubiri matangazo ambayo alishayasikia mara elfu kidogo. Hayo yalikuwa matangazo ya IATA yahusuyo usalama wa usafiri wa anga. Baada ya matangazo hayo, ndege yao aina ya Boing 737 ilirushwa na vijana hawa wa Kitanzania.
Willy aliinamisha kiti chake kikakaa sawa. Akaanza kufikiri juu ya yale yote aliyokuwa akiambiwa na Chifu. Alichambua kipengele kimoja baada ya kingine na namna ya utekelezaji wa kazi nzima.
“Patakuwa na kazi”, Willy alisema moyoni kwake.
Ilikuwa sikukuu ya Idd. Siku ile Willy na Chifu walipozungumzia mipango kujidhatiti kiulinzi ili kuzuia uwezekano wa majasusi wa makaburu kuingia nchini bila kujulikana na kuvuruga mkutano wa wapigania uhuru. Wakati huo huo majasusi tayari wameshaingia mjini Arusha na tayari walikuwa wanapumzika nyumbani kwa F.K wakiwa tayari kuanza kazi. Hiyo ilikuwa na maana kwamba usiku wa jana yake F.K na Tondo kwa upande wa Tanzania na Peter kwa upande wa Kenya walikuwa wameweza kuwaingiza nchini kwa siri. Zaidi ya hayo, majasusi wa Makaburu walikuwa wameingiza mizigo yao yote. Asilimia mia tisini ya mizigo hiyo zilikuwa ni silaha za aina mbali mbali na vyombo vya kisasa vya kufanyia ujasusi.
Kwa kuwa gari la F.K lilikuwa halipekuliwi, safari yao kutoka mpakani hadi Arusha haikuwa na kisanga chochote. Pamoja na ulinzi mkali uliowekwa kwenye vizuizi njiani, watu hao waliweza kupita. Kila alipofika kwenye kizuizi F.K alitoa kichwa chake nje tu na maafisa wa polisi kimzaha walimpigia saluti na kumwashilia aendelee. Hivyo sifa za kinafiki za F.K ziliweza kusaidia majasusi wa makaburi wa Afrika Kusini kuingia Tanzania tayari kutoa kipigo dhidi ya wapigania uhuru wa Afrika huru kwa ujumla.
Baada ya kuvuka mpakani, Peter alirudi Nairobi akiwa ameridhika kuwa nusu ya kazi yake ilikuwa imefanyika tayari.
Mchana wote wakati majasusi walipokuwa nyumbani kwa F.K walikuwa wanajitayarisha walisafisha silaha zao, na wale Ninja wawili walifanya mazoezi madogo madogo. F.K alikuwa amewapeleka likizo wafanyakazi wake wote hivyo aliacha nyumba yake nzima itumike na majasusi. Walikuwa wakijipikia na kujifanyia mambo kadhaa. Kama nilivyoeleza hapo awali, nyumba ya F.K ilikuwa imejengwa kwa madhumuni kama hayo. Hata mtu angefika kwa F.K asingeweza kugundua kuwepo kwa majasusi kwani walikuwa wanatumia vyumba vya siri.
Ilikuwa yapata saa za jioni wakati F.K alipowakusanya majasusi ili kuwapasha habari.
“Sasa hivi nimepata habari kupitia kwenye chombo cha kupashana habari kilicho chumbani kwangu”, F.K alisema “Wakubwa wetu wamepata habari kuwa mpelelezi mashuhuri wa wapigania uhuru, Bon Sipele na mpelelezi mwingine mashuhuri kutoka Zimbabwe, Rocky Malele, wameondoka leo mchana mjini Harare na Ndege ya shirika la ndege la Tanzania wakiwa njiani kuelekea Arusha. Taarifa niliyonayo inasema kwamba watu hawa ni hatari sana. Hivyo ni lazima wauawe, la sivyo watatia dosari katika mipango yetu. Vile vile nimeelezwa kuwa Paul na Fouche wanawafahamu watu hawa”.
Nyumbani kwa F.K kulikuwa na chombo kupashana habari cha hali ya juu sana. Chombo hicho kilikuwa kinapokea habari kutoka kwenye Setelaiti. Setelaiti hiyo iliwekwa angani na Makaburu wa Afrika Kusini wakisaidiwa na Marekani. Kazi yake kubwa ilikuwa kupashana habari za kijasusi. Hivyo mawasiliano kati ya F.K na mabwana zake yalikuwa hayapitii njia za kawaida. Ndiyo sababu aliweza kupashana habari na hao bwana zake bila kugunduliwa na vyombo vya upelelezi vya Tanzania.
“Ndio, tunawafahamu vizuri sana”, Paul alijibu.
“Kama kweli hawa watu wanakuja”, Fouche alieleza “ni lazima kujiweka tayari. Hao mimi nawajuwa siyo mchezo. Kama maagizo yanasema wauawe mara moja ni sahihi kabisa. Wakisha fahamu na kuwa na wasiwasi wanaweza kufanya kazi yetu iwe ngumu. Ujuzi na uwezo wao ni mkubwa. Mimi naamini kuwa hata kama wanatutilia wasiwasi, bado hawajui kama tayari tumeingia. Wao wanatarajia sisi tuingie kwa ndege. Hivyo watajishughulisha na kuchunga viwanja vya ndege vya Dar es Salaam na Kilimanjaro”.
“Kama wameweza kutuma wapelelezi mashuhuri kama hao”, John aliasa “Ina maana hata serikali hizi zinahisi kitu”.
“Lazima. Lazima mjue nchi hizi sasa hivi siyo mchezo”, F.K alionya “nchi hizi zina uwezo mkubwa wa kipelelezi. Hivyo mfahamu kuwa mmekuja kupambana na watu wenye ujuzi kama wenu hivyo msifanye mchezo”.
“Watafika saa ngapi watu hawa”, Geoger aliuliza. Yeye ndiye alikuwa mkubwa wa kikosi hiki na pia mmoja wa wale ninja wawili. Yeye na Dave walikuwa na uwezo mkubwa kuliko wale wenzao.
“Ndege hiyo inatarajiwa kufika hapa saa tatu na nusu”, F.K alieleza “Lakini nimepata habari sasa hivi kutoka kwa watu wangu walioko uwanja wa ndege kwamba kutokana na wingi wa wageni kutakuwa na ndege mbili. Kama mnavyojuwa mpaka sasa wageni wengi wameshaingia. Hadi kufikia kesho kila mjumbe anatakiwa awe hapa kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano hapo kesho kutwa. Hii ina maana kwamba lazima tufunge kazi takatifu mnamo muda wa masaa sabini na mbili yajayo”.
“Hiyo kazi itafungwa katika muda huo wala usiwe na shaka”, George alijibu.
“Sasa umeamua nini juu ya watu hawa wawili Dave, ambaye wenzake wanamwita Devil, yaani shetani, aliuliza.
“Watu hawa lazima wauawe usiku huu huu”. George alijibu “Kitendo hicho kitawafanya adui wapagawe. na hivyo kutupa sisi nafasi nzuri zaidi kufanya kazi yetu”.
“Hali ya ulinzi huko uwanja wa ndege ikoje”, aliuliza.
“Ilinzi mkali sana”, F.K alijibu. “Na siyo tu kwenye uwanja wa ndege, hali katika mji mzima, wameletwa askari polisi wageni kabisa kutoka mikoa mingine kulinda mkutano. Hivyo ulinzi ni mkali sana.
“Waacheni waonge ulinzi. Jambo hilo lisiwafanye tumbo moto. Ikiwezekana F.K uiambie serikali ya Tanzania ilete jeshi lake zima hapa Arusha na bado cha mtema kuni watakiona tu”, Dave alijigamba.
“Paul na Fouche, hiyo ni kazi yenu sitaki Bon na Rocky walione jua litakalochomoza kesho. Mipango yote mnaijua ni kama kawaida”, George alisema.
“Hesabu kwamba hiyo kazi imefanyika”, Paul alijibu.
“F.K. Nataka unipatie majina ya viongozi wote wa vyama vya wapigania uhuru ambao wameshaingia. Vile vile nataka unipatie majina ya hoteli na vyumba wanakolala. Habari hizi nazitaka leo hii”, George alimwagiza F.K.
“Utapata bila matatizo”, alijibu F.K.
“Wengine mliobaki nitawaeleza baadaye nini cha kufanya kwa usiku wa leo”, George alisema huku akigeuka upande mwingine. Na nyie Paul, Fouche na F.K nataka utekelezaji sahihi kutoka kwenu.
Siku hiyo ilikuwa sikukuu ya Idd-elftri. Mjini Nairobi mchana ule Mike alikuwa ofisini akipokea ripoti kutoka kwa Mwaura.
“Tangu jana mimi na vijana ulionipa tulikuwa tunachunga nyumba hii kwa zamu”, Mwaura alisema. “Hata hivyo, hatujagundua kitu chochote. Hakuna mtu hata mmoja ambaye ametoka nje ya nyumba ile. Ila kuna kitu kimoja kinashangaza. Ni kwamba jioni hatumwona Peter akirudi nyumbani. Na Onyango ameniletea habari kuwa amemwona akirudi sasa hivi tunahisi kwamba Peter hakulala nyumbani”.
“Unayo hakika hakurudi na kutoka?”, Mike aliuliza.
“Labda hiyo iwe wakati tulipokuwa hatujaanza doria wakati wa mchana”.
“Hivyo una maana wale watu bado wako ndani?”.
“Bila shaka. Labda tu ule muda ambao nilikuja hapa kuwasiliana nawe. Maana kama nilivyokwambia jana, kwa muda ule wa masaa manne hapakuwa na ulinzi”, Mwaura alijibu.
“Mike Maina alifikiri sana na kisha akasema. “Sidhani, lakini lazima tuwe na uhakika mtu anaweza kufanya hivyo kama amehisi kuwa tunamfuata”.
“Sidhani kama alikuwa ameniona”, Mwaura alieleza, “Mimi naelewa kuwa mtu ambaye huchukua tahadhari na mwenye ujuzi kama Peter hawezi kuwa katika hali ile kama alihisi kufuatwa na watu. Bali Onyango aliniambia alipokuwa anarudi leo mchana alionekana kama mtu mwenye wasiwasi kuwa anafuatwa”.
“Ndio. Hapa kuna kitu kinanitia wasiwasi sijui ni nini! Mwaura jiweke tayari mnamo saa sita usiku nipitie nyumbani kwangu. Tutakwenda kwa Peter kwani lazima tuhakikishe kuwa mambo gani yanaendelea ndani ya nyumba yake. Waache wale vijana waendelee kufanya kazi”, Mike aliagiza.
“Sawa mzee”, Mwaura alijibu.
Mnamo saa nne na nusu ndege namba TC 1001 iliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro. Willy Gamba alikuwa mmoja wa abiria walioteremka. Alijichanganya na kundi la abiria wenzake mpaka akafaulu kutoka nje ya uwanja bila mtu yeyote kumtambua. F.K, Paul na Fouche walikuwa kwenye kundi la wapokeaji wakichunguza watu kwa makini. F.K hakuweza kumtambua Willy. Mawazo ya Paul na Fouche yalikuwa juu ya Bon na Rocky na hata chembe hawakumfikiria Willy, mbali ya kumtambua.
Alipofika nje ya jumba, Willy alikuta madereva taksi wakigombania abiria. Ingawa taksi za kawaida huwa haziruhusiwi uwanjani hapo, siku ile zilijaa tele. Ziliruhusiwa kwa vibali maalum kutokana na haja ya kuhudumia wageni ambao walikuwa ni wengi sana.
“Oh, mzee njoo huku”, teksi dereva mmoja aliyemfahamu Willy alimwita huku madereva wengine wakimwandama na kumsihi apande magari yao.
“Oh, Omari, habari za siku nyingia?”, Willy alimsalimia.
“Nzuri tu, mzee, ila wewe tu umepotea”, Omari alijibu huku akipokea mkoba wa Willy na kuelekea kwenye gari.
“Sababu ya biashara, bwana. Siku hizi imekuwa ngumu”, Willy alijibu.
Wakati walipokuwa karibu kuondoka Willy alisita kidogo.
“Hebu subiri kidogo, kuna kitu nimekumbuka”, Willy alisema.
Omari ambaye alikuwa ameliwasha, gari alilizima.
Ilikuwa jambo la kawaida kwa Willy kulitumia gari la Omari. Mara nyingine Omari alimwachia gari Willy aendelee yeye mwenyewe kwa malipo fulani.
Baada ya kupanga na kupangana Willy aliamua kuwangojea wenzake ambao wangekuja kwa ndege ya pili.
“Omari, samahani nitakusumbua, kuna mahali ambapo nataka niende lakini nataka niende peke yangu. Je, sijui kama utaniachia gari yako ili nifanye shughuli yangu? wewe unaweza kupanda gari nyingine”, Willy alisema “Mambo mengine kama kawaida yetu”.
Bila kusita Omari alikubali ombi la Willy, alijua fika kwamba Willy alikuwa kizito na kila alipochukua gari lake kwa shughuli zake kwa muda mfupi, aliweza kulipwa kiasi ambacho angeweza kukifanyia kazi kwa zaidi ya mwezi mzima.
“Bila shaka”, Omari alijibu kwa furaha, Petrol imejaa mzee na gari kama kawaida halina matatizo. Ukisha maliza kazi utanipigia simu kunijulisha hata kama ni baada ya juma zima.
“Ahsante”, Willy alijibu huku akichukua swichi ya gari.
Omari alimwaga Willy na kuambaa zake.
Omari aliachana na Willy kwenye maegesho ya magari uwanja wa ndege. Katika gari la sita katika safu kutoka alipokuwa Willy. F.K. pamoja na wenzake walikuwa wamekaa ndani. Walifanya hivyo ili kusubiri maadui zao ambao wangefika kwa ndege ya pili.
“Mimi nafikiri niwaache maana hakuna usalama tukionekana pamoja. Nisingependa mambo yetu yagundulike kabla hata kazi yetu hatujaianza”, F.K. aliwashauri wenzake.
“Wewe nenda, kazi hii sisi ni saizi yetu, mambo yote tuliyotaka umefanya. Kazi yako umemaliza”, Paul alimruhusu.
“Nawatakia bahati njema”, F.K aliwaambia huku akiondoka kuelekea kwenye gari lake jingine ambamo Tondo alikuwa anamsubiri.
“Ahsante”, PAul alijibu.
Bila kujua, Willy. Paul na Fouche walikuwa wakisubiri wageni wale wale, lakini kwa nia na madhumuni tofauti.
Ndege iliwasili mapema kuliko ilivyotarajiwa. Ilifika saa tano kasoro dakika kumi.
“Ndege hii imewahi kuondoka Dar”, Willy alijisemea moyoni huku akiwa tayari kwenda kuwapokea wenzake.
Paul na Fouche walitoka kwenya gari lao mara moja na kwenda kujichanganya tena na wapokeaji wengine waliofika kuwalaki wenzao.
Ndege ilisimama na abiria wakatelemka kama kawaida.
Willy aalikuwa tayari amejigeuza kimawazo na kimazingira kutokana na ujuzi pamoja na uzoefu wa muda mrefu katika kazi hii. Alijibanza katikati ya nguzo moja kama asiyekuwa na hili wala lile. Hata hivyo aliweza kumwona kila mtu aliyetoka nje ya jumba la uwanja kutoka pale aliposimama. Paul na Fouche pia, wakitumia ujuzi wao walijitosa kwenye vurugu la wapokeaji kiasi kwamba hakuna mtu ambaye angewahisi chochote. Hii ilitokana na kwamba wao hawakuwa wazungu peke yao hapo uwanjani. Watu waliotoka kwanza ni wale waliokuwa wanasafiri bila mzigo mikubwa.
Hatmaye Rocky Malele alitokea. Paul alimgonga Fouche begani na wote wakamtambua Rocky. Willy nae alimwona Rocky lakini akaendelea kubana. Rocky aliangaza huku na kule kisha akaamua kupanda Kombi ya shirika la Taifa la Huduma za Kitalii.
“Wakati kama huu wa usiku ni vizuri kupanda gari la watu wengi kwa tahadhari na usalama”, Rocky alijisemea.
Kulikuwa na watu wengine ndani ya gari hili lakini lilikuwa bado kujaa. Hivyo iliwabidi kusubiri abiria wengine zaidi. Paul, Fouche na Willy Gamba walimwona Rocky akipanda gari hilo. Ingawa Paul na Fouche hawakujuana na Willy. Wote waliendelea kumsubiri Bon atokee.
Lakini jambo la kushangaza ni kwamba Bon hakutokea. Pande zote mbili zilitarajia kuwa angefika kwa ndege hii. Lakini kwa mshangao mkubwa Bon hakuonekana kamwe.
Willy ambaye alikuwa anachunguza nyendo za hapa kwa makini, aliona wazungu hawa wawili wanaondoka na kuelekea kwenye gari lao. Katika akili yake Willy alifikiri kitu fulani kilichojitokeza kama hakieleweki. Ilikuwa kwamba Willy aliwaona wakati anafika. Na sasa alikuwa amewaona tena Wazungu wale wale. Ilionekana kama kwamba nao pia walikuwa wanasubiri mgeni ambaye hakuwasili kwani wao pia walikuwa wa mwisho.
Pamoja na hayo, Willy alijisemea, “Lakini inawezekana walikuwa wamekuja kuwapokea wageni wao halafu wakakuta hawakuwasili. Hii inawezekana na haina ubaya wowote”.
Hata hivyo Willy aliamua kufuatilia nyendo za Wazungu hao. Aliwaangalia wakiingia kwenye gari naye pia aliamua kuingia ndani ya gari lake. Mara gari alilokuwemo Rocky liliondoka.
“Tulifuate gari hilo”, Paul alimwambia Fouche ambaye alikuwa anaendesha.
“Itakuwa vigumu kulishambulia gari hili; ingekuwa vizuri kama angekuwa amechukua teksi yeye peke yake”, Fouche alieleza.
“Kuna wakati atabaki peke yake. Usiwe na wasiwasi kwani tunayo siku nzima ya kufanya kazi hii”, Paul alijibu.
Gari la akina Rocky lilifuatwa na gari moja, halafu lilifuatwa na gari la akina Paul na Fouche. Willy alisubiri gari lingine lifuate ndio naye aweze kujiunga na msafara. Alipotaka kuondoka aligundua kuwa tairi mbili za nyuma hazina upepo!
“Shenzi”, Willy alilaani.
Wakati F.K anawaaga Paul na Fouche ili aende kwenye gari alilokuwa ameegesha Chris Tondo, Chris Tondo alikuwa amemwona Willy Gamba akitoka nje ya uwanja na kumtambua. Vile vile wakati Chris Tondo alipokuwa ofisa wa polisi aliwahi kumfahamu Willy kikazi na kimaisha. Kwa upande mwingine, Willy hakumweka Chris Tondo maanani. Hivyo alikuwa hawezi kumkumbuka.
“Nimemwona Willy Gamba”, Tondo alimwambia F.K.
Aliposikia hivyo F.K alishituka kwani alimfahamu Willy kutokana na umaarufu wake kama nilivyokwisha kusimulia.
“Oh, yuko wapi?”, liuliza F.K kwa mshangao mkubwa.
“Namwona anangojea ndani ya teksi ile”.
“Basi, bila shaka na yeye anawasubiri”, F.K alisema.
“Anawasubiri akina nani?”, Tondo aliuliza.
Pamoja na mambo yote ambayo Tondo alikuwa anayafanya kwa wizi nzima, F.K alikuwa hajamweleza kinagaubaga operesheni hii ilikuwa ya namna gani. Baada ya kufikiri kwa muda aliona ni vyena amweleze habari zote kwani kumficha Tondo kungeweza kusababisha makosa ambayo yangeweza kuleta hatari kubwa, hasa kwa wakati kama huu.
“Unajua Tondo, wewe nakuchukulia kama ndugu yangu. Ni mtu ambaye nakuamini katika maisha yangu. Hivyo wakati umefika na mimi kukueleza kinaganaga juu ya shughuli yote hii”, F.K alimwambia Tondo na kisha akamweleza juu ya operesheni hii kuanzia mwanzo mpaka mwisho, kisha alisema. “Hivyo umefika wakati wa kulipa kisasi dhidi ya serikali ya Tanzania kama ulivyowahi kuahidi. Bila shaka utakuwa upande wetu”.
“F.K wewe ni ndugu yangu. Mimi niko pamoja nawe. Naahidi kuwa nitatumia ujuzi wangu wa kipolisi kikamilifu ili nilipize kisasi changu cha kunionea na kunifedhehesha “, Tondo aliahidi.
Hivyo F.K na Tondo walibaki ndani ya gari lao wakimchunguza Willy alikuwa anafanya nini. Wakati ndege ilipwasili na Willy akatoka kuelekea mahali alipojibanza ili kuwaangalia akina Riocky. Tondo aliteleza gizani mpaka kwenye gari la Willy. Hapo hapo alitoa upepo kwenye matairi mawili ya nyuma.
“Nimemweza”, Tondo alijigamba huku akirudi kwenye gari.
“Kazi hii itakuwa kubwa”, F.K alisema. “Itakuwa ni vita vya kutafutana. Vita kwa akili na ujuzi kwani wapelelezi mashuhuri wa Afrika naona wako hapa. Heri sisi tutangulie tuwape habari wenzetu halafu tujitayaruishe kwa ajili ya mapambano makali. Hapa tulipo hatuna hata silaha yoyote. Kama tunapenda kuiona kesho tumkwepe Willy. Kazi tuliyofanya inatosha kwa leo. Willy anaweza kusubiri mpaka kesho. Waache Paul na Fouche nao wafanye kazi yao. Kesho tutakuwa tayari kumumaliza Willy. Hata yeye mwenyewe ataingiwa na woga baada ya kusikia wenzake wameuawa”.
“Nafikiri tungoje tuone kama Willy alikuwa anawasubiri wenzake”, Tondo alisema. “Ikiwa ni hivyo itakuwa rahisi kwa Paul na Fouche kuwamaliza wote kwa wakati mmoja”.
“Sidhani, hawawezi kusafiri wote pamoja, Tondo”, F.K alipinga usemi. “Mimi ni jasusi na mchezo huu naufahamu. Paul na Fouche wanajua sana mchezo huu pia. Hivyo wao waachie, wewe ni mchezaji wa ridhaa. Katika shughuli hii ya kijasusi vizuri kuwaachia wajuzi. Achana na Willy huyo atakuwa nyama yetu kesho”.
Tondo aliwasha gari na kujipenyeza kwenye msururu na kuondoka.
Wakati Tondo anatoa upepo kwenye tairi za nyuma za gari la Willy. Lyimo alikuwa sehemu ile. Lyimoa alikuwa mwizi mkubwa. Wizi wake alifanya wa kuvunja magari yaliyoegeshwa na kuiba vitu vilivyomo ndani. Siku ile alikuwa katika pilika zake hapo uwanja wa ndege wa Kilimanjaro, baada ya kusikia magari mengi yangekuwa hapo. Wakati huo Lyimo alikuwa hajabahatisha kitu chochote. Alikuwa amejibanza kwenye gari karibu na lile la Willy. Ndani ya gari lile Lyimoa alikuwa ameona mkoba ambao alikuwa anaunyemelea. Alikuwa anajaribu kufungua mlango wa nyuma. Mara alisikia mtu anasogea karibu na gari lililokuwa jirani. Aliinuka kidogo na kuchungulia. Alimwona mtu anakuja kwa kunyata. Kwanza kabisa Lyimo alifikiri yule alikuwa mwizi mwenzie. Lakini sura yake pamoja na jinsi alivyokuwa ilionyesha kinyume. Aliona huyo mtu anatoa upepo kwenye gari halafu kunyata na kuondoka.
Lyimo aligundua kwamba gari lile lilikuwa teksi ya Omari ambaye anamfahamu sana. Ili kuchunguza vizuri kisa hiki Lyimo alimfuatilia yule mtu na kuona gari alimoingia. Alichukua kalamu yake na kuandika namba za gari hilo kwenye kiganja chake cha mkono. Akitarajia kumweleza Omari kana angetokea. Mara nyingine Omari alikuwa akimsaidia. Safari hii aliona amepata nafasi ya kulipa ukarimu wake angalau kwa ishara hiyo ndogo.
“Mimi ni mwizi”, Lyimo alijisemea moyoni. “Ninaiba ili nipate fedha za kunifanya niishi. Lakini watu wengine ni waharibifu tu. Kwa mfano mtu huyu amemsumbua mwenzake bure. Afadhali mara mia angekuwa na nia ya kuiba kitu”.
Mshangao wake ulizidi alipoona lile gari linaondoka kuelekea mjini.
Wakati Willy alipokuwa anaangalia matairi, Lyimo alitokea.”Habari gani, mzee”, Lyimo alimsalimia Willy kwa heshima.
“Nzuri”, Willy alijibu huku akimwangalia Lyimo kwa makini. Kisha aliendelea, “Ngoja kidogo”.
Willy alisogea mbele na kuandika namba za gari la Wazungu lililokuwa linapita mbele yake halafu akarudi.
“Eh, unasemaje?”, Willy alimsaili Lyimo.”Mwenye gari hii ni rafiki yangu. Siyo gati la Omarui hili”, Lyimo aliuliza.
“Ndio, na mimi ni rafiki yangu. Ameniachia gari hili. Lakini ajabu nimekuta limepata pancha mbili sasa hivi”, Willy alijibu.
“Nimeona mtu anatoa upepo ndani ya matairi haya”, Lyimo alieleza.
Mara Willy alisikia kengele zinalia kichwani mwake.
“Eh, mtu wa namna gani?”, Willy aliuliza kwa shauku kubwa.
“Mtu mmoja nadhifu sana. Mwanzo nilifikiri ni mwizi. Lakini hakuonyesha dalili ya wizi. Aliinama, akatoa upepo na kuondoka. Aliingia kwenye gari ambalo lilikuwa na mtu mwingine ndani halafu wakaondoka zao. Hata hivyo, mimi nilichukua nambari za gari hilo ambayo ni ARKK 567”, Lyimo alimwambia Willy huku akisoma kwenye kiganja chake.
Willy alikariri nambari hiyo na kushangaa, kwa kujiona alikuwa na bahati iliyoje.
“Wewe unaitwa nani?”, Willy aliuliza
“Naitwa Lyimo”.
“Na wewe ni dereva wa teksi?”.
“Hapana, mimi ni shanta”.
“Shanta maana yake nini?”.
“Mimi huwa nawasaidia madereva kama wanao usingizi. Huwa naendesha halafu wao huwa wananilipa chochote”, Lyimo aliongopa.
Wakati huo akili ya Willy ilikuwa inafanya kazi haraka haraka. Mara alipata jawabu.
“Ninaweza kupata gari nyingine hapa?”.
“Subiri niangalie”, Lyimo alijibu na kuondoka.
Punde si punde Lyimo alirudi na kijana mmoja.
“Huyu anaitwa Tarimo, ni rafiki yangu vile vile, hata Omari ni rafiki yake pia”, Lyimo aliwajulisha.
“Aah, mimi naitwa Willy. Omari ni rafiki yangu. Kiniachia gari lakini nimepata mkasa”.
“Sasa unataka tukusaidie vipi?”, Tarimo aliuliza.
“Unayo pampu?”.
“Ndio”, Tarimo alijibu.
“Nafikiri kama utakubali utanipatia gari lako, mimi nitakulipa shilingi elfu tatu. Weka upepo kwenye gari la Omari halafu tuonane kesho asubuhi huko New Arusha Hoteli. Gari lako utalikuta hapo”.
Bila kuchelewa Willy alianza kutoa fedha na kumhesabia Tarimo. Tarimo aliona kama ameangukiwa na ngekewa. Alichukua fedha na huku Lyimo akibeba mizigo ya Willy, wakielekea kwenye gari.
“Lyimo umenisaidia sana. Chukua hizi shilingi tano ukanywe angalau bia moja”, Willy alimwambia Lyimo.
“Lo! ahsante sana. Leo siku nzima nilikuwa sijapata kitu. Mungu akuongezee.
“Amina”, Willy alijibu huku akifikiria namna Lyimo alivyokuwa amemsaidia bila kujua.
“Kesho asubuhi”, Tarimo alisema.
“Kesho asubuhi”, Willy alijibu na kuondoka.
“Sasa ni lazima niyakamate yale magari”, Willy alijisemea moyoni.
Gari la Tarimo lilikuwa aina ya Peugeot 404 lenye umri kidogo. Lakini lilikuwa na nguvu ya kutosha. Tangu yale magari yaondoke ilishapita muda wa dakika kumi na tano. Willy alilipamba moto na kuendesha kwa mwendo mkali sana. Wakati akiendesha Willy alifikiri mambo yote haya. Na ajabu zaidi, Willy alimfikilia Bon Sipele ambaye alikuwa hakuonekana hapo uwanja wa ndege.
Karibu na mpakani, katikati ya sehemu ya Tengeru, nje ya mji wa Arusha. Willy aliyafikia magari yaliyokuwa yametangulia. Alilipita gari moja ndipo akaliona lile lililokuwa linaendeshwa na wazungu. Vile vile aliona ile Kombi iliyombeba Rocky. Hivyo aliamua kubana nyuma ya magari hayo.
Kituo cha kwanza cha ile kombi kilikuwa Saba Saba Hoteli. Rocky alikuwa amemwambia Willy kuwa angefikia Equator Hoteli. Alipofika Sabasaba Hoteli na kuona ile kombi pamoja na gari la wazungu vikiongoza kwenda hoteli hiyo, yeye Willy aliamua kwenda moja kwa moja akabane Equator Hoteli. Alifanya hivyo ili akaone kama alivyofikiri ilikuwa kweli. Akiliwa ameegesha gari katikati ya magari mengine karibu na Safari Hoteli, aliona ile kombi inasimama pale Equator Hoteli. Watu watatu wakiwa na mizigo walitelemka. Rocky alikuwa mmoja wapo punde si punde, Willy aliona gari lile la wazungu linaegeshwa karibu na Hoteli hiyo hiyo. Lakini kwa upande mwingine wa barabara.
Mzungu mmoja aliondoka na kuelekea huko Hotelini. Willy alisubiri. Baada ya kama dakika kumi hivi, yule Mzungu alirudi na kuingia ndani ya gari. Willy aliendelea kusubiri. Alipoangalia saa yake ilisema saa sita usiku.
ITAENDELEA
Hofu Sehemu ya Tatu
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;