Isabel Ndani ya Mpango Hasi ya Tatu
IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE
Simulizi : Isabel Ndani Ya Mpango Hasi
Sehemu ya Tatu (3)
Kutoka ndani ya kichaka kile vijana wale wavuta bangi walitulia tu, kwa mbali waliiona treni ile ikija kwa kasi sana usiku ule.
“Oya jiandaeni sasa hivi kitu kinaitika, we Nyau washa jeep hiyo tayari tayari” kiongozi wao aliwapanga vijana wake, na wote wakakaa tayari.
“Kwa hiyo hatpekui kidogo?” mwingine aliuliza huku akivuta pafu la mwisho na kukitupa kipisi kile cha bangi porini.
Kitu wasichokitegemea kilitokea, kishindo kikubwa kilitokea, injini ya treni ile ilijipiga kwenye mawe na mchanga na kutoka nje ya reli na kusimama porini ikifuka moshi mweusi, behewa moja liliokuwapamoja na injini hiyo lilinyanyuka na kujikunja vibaya kasha likajipiga ubavuni mwa injini ile na kubondeka vibaya. Jomse na Ton walirushwa mbali na kudondoka mchangani.
Kutoroka porini vijana wale walipigwa na butwaa maana wameona kipisi tu ambacho kimekuja lakini treni iliyobaki hawajaiona kabisa. Walimuona Jomse na Ton wakigalagala mchangani waliwakimbilia na kwaokota moja kwa moja waliwapakia katika jeep
“Mbona mpo wawili?” yule kiongozi wa wale vijana aliwauliza
“Hata hatuji mwingine yuko wapi, nyie twendeni hayo tutayacheki kesho” Jomse aliwajibu na wote wakapanda katika jeep moja na kutokomea porini.
“Mandi mjinga sana, na yule ndiye atakaye ttia matatizoni kwa ujinga wake” Ton alimueleza Jomse wakati jeep ile ikikata mapori kuelekea kusikojulikana.
“Na mi nilishalijua hilo, sasa sijui bwana twende tutulie kwanza tutajua la kufanya” Jomse alimjibu Ton.
Mabehewa yasiyo na kichwa yaliendelea kwenda kwa kasi lakini yalionekana kukosa nguvu hasa yalipopambana na miinuko, muinuko wa mwisho ulikuwa mkubwa zaidi yalipanda mpaka katikati yakasimama kasha yakaanza kurudi nyuma, abiria wote walitulia kimya kabisa wakisubiri mwisho wake, mchezo huo uliendelea na mwisho mabehewa yale yakasimama bila kuleta shida yoyote, abiria walipiga kelele za furaha kwa kupona dhidi ya kifo ambacho hawakukitarajia, wengi waliamini sala zao zimewaokoa, waliokuwa mbele kabisa, polisi na Amata waliamini ujanja wao umewaokoa. Amata alikumbatiana na polisi wale kwa shangwe hawakuyaamini macho yao kile wanachokiona. Abiria walianza kuteremka kwa furaha japokuwa trenin ile ilisimama porini sana na ilikuwa tayari usiku mwingi, wote hawakuamini kama wamepona walianza kuimba na kucheza kwa furaha. Amata aliwatazama wananchi wale machozi yakaanza kumtoka
“wengi wangekuwa marehemu, wengine wangekuwa yatima na walemavu, asante Mungu, Asante Isabel” Amata aliyasema hayo bila kujijua akiwa kasimama kando ya mabehewa hayo akitazama wananchi wale wakicheza na kuimba
“Tumesalimika, tunaomba msaada wa usafiri kutoka hapa tulipo, ova” Polisi mmoja alikuwa akiongea katika redio call kutoa taarifa makao makuu ya polisi Tabora.
“Tumekupata na tunafanyia kazi, ova” sauti ya upande wa pili ilijibu “Nimekusoma” alijibu.
Furaha ililipuka katika viwanja vya stesheni ya Tabora, hakuna aliyeamini walipopokea taarifa hiyo kutoka kwenye chumba cha mawasiliano. Mkuu wa polisi mkoa wa Tabora aliruka kwa shangwe haikujalisha kama alikuwa na kitambi kilichomzidi uzito, alimkumbatia stesheni masta na kupongezana kwa furaha.
“Thank God, watu wetu wamepona” alisikika stesheni masta akipiga kelele kwa furaha sana.
Madam S, IGP na waziri wa ulinzi hawakuamini wanachosikia baada ya simu iliyopigwa na Amata kumfikia Madam S kabla hajaondoka katika eneo hilo la makao makuu ya JKT. Kila mmoja alifurahi kwa furaha ya aina yake
“Well done Kamanda Amata” Madam S alisikika akiyatamka hayo maneno.
“Ok, tunamshukuru Mungu, sasa kesho asubuhi wote tukutane tuelekee Tabora kwa ndege ya kukodi” waziri alimaliza na wote wakaagana kuelekea walikotoka.
Gari za jeshi ziliondoka kutoka kambi ya Kaliua KJ 320B kuelekea eneo la tukio ili kuwasaidia abiria wale kuwafikisha mjini, usiku kwa usiku amri ilitolewa na kiongozi wa kambi hiyo na kazi
ilianza mara moja bila hata kchelewa.
Watu walikuwa ni wengi sana kiasi kwamba ilipelekea wengine kubaki ili gari zingine zije kuwasaidia, vijana wa jeshi la wananchi wa Tanzania walifanya kazi yao vizuri sana na kwa moyo wa kizalendo kuwasaidia abiria wale japo kuwasogeza karibu na stesheni au kuwafikisha kabisa. Steshen masta wa Tabora aliamuru vibelenge kadhaa kufuatana ili kuona hali ilivyo na ndani ya kimojawapo mlikuwa na mkuu wa polisi wa Tabora, stesheni masta mwenyewe na viongozi wachache wa chama na serikali, wote walitaka kwenda kujionea wenyewe kile kilichotokea.
Wakiwa bado njiani kwa mwendo wa taratibu, kwa mbali waliweza kuona kitu kikubwa kimezuia reli, operetta aliongeza mwanga wa taa yake kubwa na kupiga honi nyingi lakini hakuona dalili ya kitu hicho kuondoka mahali pale, alipunguza mwendo na walipokaribia walikuta ni injini ya treni iliyokuwa ikitoka Kigoma kuja Tabora
“Oh my God!” stesheni masta alisikika akisema kwa sauti. Operetta alisimamisha chombo chake na wote wakashuka kuangalia hali hiyo, walikuta injini ile ikiwa imeacha reli na kusimama kando katika mawe wakati lile behewa lilikuwa limeanguka na kuharibika vibaya. Waliteremka, kwa kusaidiwa na kurunzi walizonazo waliweza kulikagua behewa lile na injini ile, hawakukuta madhara katika injini ile ila tu behewa lilikuwa limeharibika vibaya. Baadhi ya polisi waliingia ndani ya injini hiyo kuangalia hiki na kile wakisaidiana na mafundi, katika chumba kimojawapo ndani ya injini hiyo ndimo waligundua mwili wa mzee kasimu usio na uhai, waliutoa na kuuhifadhi vizuri kasha kuupeleka katika kibelenge kile
“Alikuwa operetta wetu mahili sana” stesheni masta alijikuta akisema mwenyewe huku akiuangalia mwili ule, machozi yalimlenga
“Kwa vyovyote atakuwa kafa kishujaa, kwani mwili wake unaoneka umepigwa sana” aliongezea mkuu wa polisi mkoa.
Waliupakia mwili ule katika kibelenge lakini hawakuweza kuendelea na safari kwa kuwa reli ilikuwa imeharibika vibaya. Kwa uchunguzi wa haraka walioufanya waligundua kuwa reli ile ilikuwa imefunguliwa
“Washenzi hawa walifungua reli!” mmoja wa mafundi alisema kwa sauti
“Ha! Hawa walidhamilia, mpaka wamefungua reli, no hii ni hujuma” Mkuu wa polisi alizungumza hayo huku mkononi mwake akiwa ameshika moja ya nati kubwa zinazotumika kufungia reli hiyo ya kijerumani.
“Tungewapata hawa jamaa leo wangejuta kuzaliwa” mkuu wa polisi alisema kwa hasira “Unafikiri bado watakuwa kwenye treni iliyobaki?” Stesheni masta aliuliza
“Sio rahisi, hii ni hujuma kabisa lazima walifanya hivi ili kuwaokoa wenzao, lakini dunia ni ndogo tutawatia mkononi” mkuu wa polisi alimjibu stesheni masta. Vijana wa polisi walijaribu kuangalia huku na kule japokuwa ilikuwa ni giza lakini mwanga wa taa kutoka katika kibelenge kile uliwawezesha kuona vizuri, polisi mmoja alipiga hatua chache pale mbele akaona kitu kama karatasi ndogo iliyokuwa ikisukwasukwa na upepo mdogo uliokuwa ukivuma eneo hilo, akakitazama akataka kukiokota lakini akaona ni upuuzi akaamua kuondoka zake. Walirudi katika kibelenge kile lakini askari wane walibaki kwa ajili ya ulinzi lakini pia walijua wahujumu wale wangeweza kurudi hasa kufuata mafuta.
Amata ga Imba, alisimama pembeni akiliangalia zoezi zima linavyoendelea la kuwahamisha abiria wale kwa kutumia magari ya jeshi,
“Kamanda, asante kwa kazi, wewe waweza kwenda sisi tutamalizia, na ulinzi tutaimarisha” polisi mmoja alimwambia Amata.
“Hamna shida, lakini nasikitika kuwakosa wale washenzi japokuwa mmoja wao kajiua mwenyewe, sasa hatujui walikuwa wangapi” Amata alimjibu yule polisi
“Hawa jamaa hata mi sijui walikuwa wangapi, nahisi ni yuleyule mmoja” yule polisi alitoa jibu na hisia zake
“Kama ni yule peke yake basi! Lakini sidhani, lazima wako wengine au lazima ana mtandao
mkubwa, usijali afande” Amata alimaliza na kuondoka eneo lile mpaka kwenye gari mojawapo la kijeshi aina ya MAN ililokuwa limeegesha hapo likipakia baadhi ya abiria.
Kichwa kilimzunguka Amata, hakutaka kukubaliana na wazo lake kuwa mle ndani kulikuwa na jambazi mmoja tu, kwake kama mzoefu wa kazi ile alijuwa wazi lazima watakua kikundi ama ndaniya treni ile au nje yake, alimfikiria sana Isabel ambaye muda huo alikimbizwa hospitali ili kuokoa maisha yake kwa kuwa alijua wazi kuwa ni yeye pekee anayeweza kutoa mwanga wa tukio zima. Amata alitoa karanga zake na kuanza kurushia mojamoja kinywani mwake huku akiwaza ili na lile, moyoni akiomba na kusali Isabel apone ili azungumze naye machache ‘watakuwa washapata ile memory card?’alijiuliza, mara kwa mara alipofikiria juu ya Isabel alishtuka kwa kuwa hakuwa na uhakika kama atamkuta mzima alijua wazi kuwa kama wale majambazi wana mtandao mkubwa haitakuwa kazi kugundu Isabel alipo ‘lakini wamfuate wa nini wakati washapata wanachotaka’ alijiwazia ‘mh naomba asife’ alijiomba mwenyewe na hapo alijikuta anaingiwa na shauku ya kumuona Isabel japo asikie neno moja kutoka kwake labda lintampa muelekeo wa nini cha kufanya. “Walikuwa watatu bwana we hukuwaona vizuri” baadhi ya vijana abiria walikuwa wakibishana, Amata alijiunga nao katika mazungumzo yao.
“Yule tall sura yake sio ngeni kabisa, kama namuonaona madukani pale Mwanga sokoni au itakuwa namfananisha labda” mwingine aliongezea. Amata alivutiwa na mazungumzo hayo alitulia kimya akijifanya kuchocheachochea vikuni kwenye ule moto uliokuwa ukiwaka taratibu ili kuwapa joto usiku ule.
Baada ya mazungumzo yale marefu Amata alikuwa amehifadhi vitu fulanifulani kichwani mwake ili labda itakapobidi vitamsaidia katika upelelezi wake. Kufumba na kufumbua abiria wote walikuwa wameondoshwa eneo lile, askari wachache walibaki kulinda mabehewa yale na mizigo ya watu. Amata alitazama saa yake tayari ilikuwa inakaribia saa kumi na moja alfajiri, kichwa chake bado kilikuwa kinawazua mengi kikitoa hili na kuweka lile, moyo wake haukuridhika hasa alipomkumbuka Mandi jinsi alivyojiua kwa mbinu ya kijinga namna ile, alijua wazo kuwa wapo wenzake lakini aliumiza kichwa jinsi gain ya kupata ukweli ‘mpango hasi’ alikumbuka neno hili alilotumiwa na Isabel kupitia facebook, Amata alipenda ajue hasa undani wa mpango huo ni nini.
Alitamani kama ni upelelezi basi akabidhiwe yeye hilo faili kwani alitaka kulipa kisasi cha kuumizwa Isabel.
Mwili wa Koplo Kibona ulikuwa umehifadhiwa vizuri kabisa katika sanduku la kisasa liliofunikwa kwa bendera ya polisi, maafisa wa jeshi hilo waliovalia nadhifu kabisa walikuwa wamesimama kwa mstari ulionyooka vizuri na upande mwingine kulikuwa na waombolezaji wengine. Kasisi alipomaliza ibada ya marehemu, vijana sita waliovaria nadhifu vazi la kipolisi walisoge karibu na sanduku lile kwa ukakamavu wa hali ya juu mara ilipigwa buluji maalumu ya kazi hiyo kabla ya kushusha sanduku lile kaburini. Jeshi la polisi liliamua kumzika kiheshima kwa sababu amekufa akiwa katika harakati za kulilinda taifa, baada ya buluji ile kumalizika zilipigwa risasi kadhaa hewani kisha sanduku lile lilishushwa taratibu kaburini.
Amata alisimama kwa mbali akiwa ndani ya suti yake nyeusi iliyomkaa vizuri, pembeni yake alikuwa na Madam S wakifuatilia kwa karibu kabisa matukio yote ya mazishi hayo.
Muda si mrefu shughuli ilikamilika na watu kuanza kutawanyika wengine wakienda kumpa pole mjane wa marehemu.
Isabel alihifadhiwa katika chumba maalum chenye mitambo tiba ya hali ya juu iliyomsaidia kupumua na mingine ikisoma mapigo ya moyo wake jinsi yanavyoendelea, Isabel alilala kimya katika kitanda kile chenye shuka safi lenye maandishi ya buluu yaliyosomeka MSD, hakuwa hata anatikisa mkono wla kupepesa macho alitulia kabisa, mara kwa mara muuguzi alikuja kumuona maendeleo yake huku akiandika vitu fulanifulani katika faili lililopo karibu kabisa na kitanda hicho “Mgonjwa anaendeleaje?”sauti ilimuuliza kutoka nyuma ya kichwa chake, yule muuguzi alistuka sana alijua labda ni mzuka. Amata ga Imba alitabasamu hasa alipogundua kuwa muuguzi yule
kapata mshtuko kwa hilo.
“Anaendelea vizuri, ila bado hajarudiwa na fahamu” Muuguzi alijibu kwa utulivu. Amata alilisogelea faili na kulisoma harakaharaka japokuwa watu huamini kuwa muandiko wa daktari ni mgumu kusoma lakini kwa Amata haikuwa hivyo. Alielewa moja kwa moja yaliyoandikwa, Isabel alivunjika mbavu nne za kulia inaonekana alipigwa sana kwa mateke na kitu kigumu sehemu za mbavu, amekutikana na majeraha ya kichwani, fuvu lake limepata shida kidogo kadiri ya uchunguzi imeoneka Isabel alijigonga vibaya kwa paji lake la uso hivyo kusababisha majeraha eneo hilo, damu nyingi imepotea hasa kutokana na majereha aliyoyapata, mkono wake wa kulia umevunjika hivyo alikuwa tayari amefungwa muogo ‘POP’.
Amata alimwangalia Isabel kwa uchungu sana machozi yalitaka kumtoka lakini hakuruhusu hali hiyo itokee. Mitambo mingi ya kidijitali iliyomzunguka Isabel ilikuwa ikitoa ushirikiano wa hali ya juu kuhakikisha mambo hayataharibika, aliporidhika alimuaga yule muuguzi na kuondoka zake.
Siku 3 nyuma NYUMBANI
KWA KINA ISABEL
Mama na Baba wa Isabel walikuwa shambani kwao huko Kasulu wakiendelea kulima ili kuhakikisha watoto wao hawalali njaa katika msimu wote wa mwaka, redio ya mbao aina ya National ilikuwa chini ya mchikichi ikiendelea kuwaburudisha. Wazee hawa ambao bado walishikilia falsafa za Mwalimu Nyerere kuwa kilimo ni uti wa mgongo hawakuchoka na kilimo japokuwa bado walikuwa wakitumi dhana duni ‘jembe la mkono’ lakini hawakukata tama kwani walikumbuka ‘mkitaka mali mtaipita shambani’.
“Mama Isabel! Aaaah mama mi nimechoka bwana napumzika” Baba wa Isabel alimwambia mkewe huku akitupa jembe pembeni na kuiendea redio ile ambayo ilikuwa imetulia hapo bila ya wasiwasi. “Ah Baba Isabel, unanitia uvivu mwenzio, na mi naacha” Mama Isabel naye alitupia jembe pembeni na kwenda chini ya migomba alipoficha viazi vyake ili kutafuna atulize njaa ambayo wakati huo ilikuwa ikimtafuna kwelikweli.
Ngoma maarufu iliyopigwa na marehemu Moriss Nyunyusa ilirindima ndani ya redio ile kushiri taarifa ya habari ilikuwa mbioni kuwa hewani, baba wa Isabel alitazama saa yake ilikuwa saa saba mchana.
‘Tabora,
Watu wawili wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi na wengine wawili kujeruhiwa katika treni iliyokuwa ikitoka Kigoma kuelekea Dar es salaam jana usiku, dulu za kiusalama zimesema treni hiyo ilivamiwa na majambazi ambao hawajajulikana idadi yao na kusababisha vifo hivyo. Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora amethibitisha kutokea tukio hilo na amesema waliouawa ni askari polisi Koplo Kibona na operetta wa treni hiyo mzee Kasimu, eitha mkuu wa polisi huyo amethibitisha majeruhi wawili walioumizwa vibaya na kukimbizwa Muhimbili kwa matibabu kuwa ni askari polisi konstebo Kirama na msichana mmoja mwanafunzi aliyetambulika kwa jina moja tu Isabel, mpaka sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na polisi na uchunguzi unaendelea…’
Taarifa ile ilimshtua baba wa Isabel, alianza kuhema kwa haraka haraka akamuita mkewe, hali
haikuwa nzuri, kilimo kilisitishwa, mama wa Isabel akaanza kuagua kilio kilichowafanya majirani waanze kukusanyika uko huko shambani.
“Mwanangu Isabel, jamani nifanyeje mimi, Oh Mungu we …” kilio kilitawala mama wa Isabel hakuweza kujizuia kulia, alilia sana hata kupelekea kuzimia mara kwa mara.
“Mama nyamaza, si wamesema yupo hospitali…” dada mkubwa wa Isabel alimbembeleza mama yake
“Wanatudanganya, mwanagu mimi atakuwa ameshakufa, nimlilie nani mimi” Mama wa Isabel hakuweza kutulia kwa haraka, muda mfupi nyumba ilikuwa imejaa watu kujua kulikoni, Baba wa Isabel alishafikishwa katika hospitali ya mission Kabanga maana BP ilipanda ghafla.
Taarifa za treni hiyo zilisambaa sana na kwa haraka, watu wengi walisikitishwa kwa tukio hilo “Yaani hawa ni wakutia moto tu!” mmoja wa vijana aliyaongea maneno hayo kwa sauti akionesha jinsi ambavyo angependa majambazi hao waadhibiwe.
Gari ya polisi aina ya Land Cruiser pick up ilisimama mbele ya nyumba ya akina Isabel, askari wawili walishuka mmoja kiwa na redio mkononi mwake alionekana mara nyingi akiongea ongea katika chombo hicho. Walisalimiana na watu wachache waliokuwa hapo nje, kila mmoja lionekana akiwa na uso wa huzuni juu ya tukio lile na wengi kati yao waliamini kuwa taarifa zilizosikika redioni hazikuwa za kweli, kila mtu aliongea anachokijua yeye. Polisi wale waliingia ndani na kukutana na mama Isabel ambaye alikuwa analia sana mpaka kukosa nguvu kabisa. Ndugu waliwakaribisha ndani na moja kwa moja waliketi sebuleni, baada ya kuwaondoa watu waliokuwa humo ndani walibaki na mama na ndugu wa familia ya Isabel.
“Mama pole sana kwa taarifa ulizozipata! Sisi ni wana usalama kama utuonavyo. Ujio wetu hapa kwako ni kukuletea taarifa ya binti yako ambaye kwa sasa amelazwa hospitali ya Taifa Muhimbili” polisi mmoja aliyeonekana ndiyo kiongozi wa msafara huo alizungumza hayo.
“Niambiyeni mimi kama mwanangu amekufa” Mama wa Isabel aliendelea kulia kwa uchungu “Hapana mama, binti yako hajafa ila ameumia na anaendelea vizuri yuko pale Dar es salaam” yule polisi alimfariji mama wa Isabel kwa kumbembeleza sana hata mama yule akatulia, akachukua kanga yake kujifuta machozi.
“Sasa lengo letu la kuja hapa ni kuongea mawili matatu na ndugu wa familia” aliendelea yule Polisi “Ndiyo Baba tunakusikiliza” mama alijibu
“Mnaweza kutueleza kwa kifupi mpangilio wa safari ya Isabel ilikuwa ni ya wapi nay a vipi?” yule polisi aliuliza.
Kaka mkubwa wa Isabel akazungumza kwa niaba ya familia
“Isabel alikuwa anakwenda Dar es salaam likizo kwa rafiki yake, mara tu baada ya kufunga shule ndipo alipopanga safari hiyo, ilikuwa aondoke kwa basi lakini alitutumia meseji ya simu kuwa amekosa basi hivyo kaenda stesheni kapanda treni.”
“Labda nikukatishe kidogo, kwenye safari hiyo alikuwa peke yake au alikuwa na wenzake?” Polisi yule aliuliza
“Alikuwa peke yake kabisa na ni mara nyingi huwa anakwenda kwa huyo rafiki yake” kaka aliongeza.
“Ok, sasa Isabel yupo Hospitali na anahitajika mtu wa karibu wa kumwangalia, kama angepatikana ndugu wa kike basi tungeondoka naye ili jioni hii ya leo aweze kuwa Dar es salaam” Polisi yule aliwaeleza wanafamilia, nao kwa haraka haraka wakamchagua dada yake aliyemtangulia kuzaliwa ili aende akafuatilie hali ya mdogo wake huko Muhimbli.
Amata ga Imba aliketi kwa utulivu kabisa juu ya kiti chake cha kunesanesa akishikashika magazeti ya siku hiyo ili aone chochote kilichandikwa, kila gazeti liliandika habari hiyo kwa manjonjo kweli kweli ili mradi kuvutia wasomaji ‘Majambazi yavamia Treni’ mojawapo liliandika, ‘Polisi auawa ndani ya Treni’ lingine liliandika hivo ‘Treni yatekwa, wawili wauawa akiwemo Polisi’. Amata alipitia yote hayo na hakuona jipya lililokuwemo zaidi ya habari za kubuni.
“Boss!” sauti ya kike ilimstua Amata akiwa amezama katika moja yha magazeti hayo. Alikuwa ni Gina aliyesimama kaegemea mlango wa kuingia ofisini kwa Amata
“Unatamani kama ungekuwepo eti!?” Gina alimtupia swali Amata. Amata alimuangalia na kutoa tabasamu pana kisha akazama tena katika gazeti hilo.
“Boss!” Gina aliita tena
“Nimekwambia mara nyingi usiniite Boss, we husikii” Amata alimwambia Gina katibu muhtasi wake
“Oh nilisahau, samahani Mr Amata” Gina alijisahihisha na kusogea karibu na meza ile huku akiwa na faili mkononi mwake, Amata alikunja gazeti lile na kuliweka pembeni.
“Nipe ripoti mrembo” Amata alimwambia Gina. Gina akiwa antazama dokumenti fulanifulani katika faili lile alikuwa akimueleza Amata taarifa mbalimbali za kazi alizomuachia lakini wakati huo Amata mawazo yote yalikuwa hayapo hapo alifikiri tu kama angekuwa ‘Mungu’ angemponya Isabel ili ajue nini kilitokea katika mkasa ule wa jana usiku.
“Mr Amata, inaonekana haupo kabisa hapa kimawazo, au hiyo habari imeshakutia kiwewe, tayari unatamani kuanza fujo zako” Gina aliongea kwa hamaki kidogo.
“Ah Gina, unajuaje? Kama waniletee mzigo niufaulishe” alimueleza Gina huku akiwa anacheka kiutani, akatoa karanga zake mfukoni na kula moja moja. Amata ga Imba alipenda sana kutembea na karanga mfukoni tangu utoto wake alipokuwa shule ya msingi Ukonga mpaka ukubwani, tabia hii imepigiwa kelele na watu wengi akiwemo marehemu mama yake lakini alishindwa kuiacha.
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
Kikao cha watu wanne kiliendelea katika moja ya ofisi za jengo la wizara ya mambo ya ndani karibu kabisa na barabara ya Ohio, makubaliano yalikuwa ni magumu kwa jinsi kila mtu alivyofikiri juu ya tukio hilo.
“Hii ni kazi ya polisi tuwaachie wenyewe” IGP Makabayo, alilieleza jopo hilo
“Hatukatai usemalo lakini linavyoonekana tatizo lenyewe unafikiri polisi wataliweza kadiri ya mipaka yao ya kazi?” Madam S aling’aka kwa kuwa yeye anahusika na usalama wa Taifa moja kwa moja.
“Tuna kitengo cha CID, kazi haiwezi kutushinda hata kidogo” IGP aliongeza
“Ok! Nafikiri hii ni kazi yetu sote, kulinda usalama wa nchi vinatuhusu sisi sote. Haina haja ya kugombana. Tuwaachie jukumu hilo vijana wetu wa polisi walishughulikie, wakishindwa tutaona kwa pamoja tufanye nini” Waziri wa mambo ya ndani alipitisha uamuzi wake.
“Sikatai unalosema mheshimiwa lakini tangalie tunachokifanya tusije kulaumiana baadae” Madam S aliliambia jopo huku akiwa amesimama. Madam S alishaliona swala lile kuwa polisi kama wao peke yao hawaliwezi kwa jinsi lilivyo katika mapana yake, na alishangazwa jinsi ambavyo IGP alivyolitaka swala lile libaki mikononi mwa polisi, Madam S alikubali kwa shingo upande lakini atafanyeje, hakuna jinsi. Kikao kiliendelea na kuona mipango ya hapa na pale.
Maagizo yalitolewa kwa pande zote mbili jinsi ya kufanya kazi hiyo.
“Ok sasa baada ya hapo, nitaomba mambo yafuatayo yafuatwe, moja, hakikisheni yule binti anawekwa chini ya ulinzi asiruhusiwe mtu awaye yote kumuona kwa sasa bila kibali cha polisi, pili, Madam S mueleze Kamanda Amata juu ya hili na mueleze kwa sasa asijihusishe kabisa na swala hili mpaka atakapopata taarifa tofauti. Nafikiri tumeelewana, jinsi ya kufanya kazi IGP unajua kuwapanga watu wako. Asanteni.” Waziri alimaliza na kuagana na wajumbe.
Madam S alibeba faili lake na kutoka nje bila kuaga, hakupenda wala kufurahia juu ya uamuzi uliotolewa na wizara, kwake hakuingia hakilini kabisa.
Kamanda Amata alipata taarifa yote ya kikao kutoka kwa Madam S, hakuwa na la kufanya isipokuwa ni kukubaliana na utaratibu uliotolewa lakini moyoni mwake alikuwa na shauku sana ya kutaka kujua hasa kiini na mpango mzima wa mkasa huu. Alitulia juu ya kiti kile huku
akimwangalia Madam S kama mtu ambaye hajawahi kumuona katika maisha yake
“Hii ndiyo shida ya polisi” Amata alimwambia Madam S, ambaye wakati huo alikuwa anaperuzi mambo Fulani katika kompyuta yake pale mezani, sauti hiyo ya Amata ilimgutusha kidogo maana alishasahau kama ofisini mle hakuwa pekeyake.
“Usijali Kamanda, kwa kuwa mambo yenyewe ndiyo yanaanza wakizidiwa watatutafuta” Madam S alijibu huku akicheka kwa kebehi.
“Nina wasiwasi sana juu ya hili, na usalama wa yule binti” Amata aliongeza huku akitikisa kichwa chake na kupepesa macho kuzunguka ukuta uliopambwa kwa kalenda nzuri na picha moja kubwa ya Madam S alipokuwa chuoni huko Canbella. Alipiga picha hiyo na wasichana wenzake kutoka nchi mbalimbali, Amata aliiendea na kuitoa pale ukutani
“Kamanda! Nini sasa unatoa picha za watu ukutani bila kuomba?” Madam S aliongea huku akinyanyuka na kumfuata Amata.
“Subiri bibi” Amata alipenda kumuita Madam S bibi, kwa kuwa umri wake ulikuwa umekwenda sana lakini bidii yake kazini iliishawishi serikali kumuongezea muda kabla ya kustahafu.
“Hii picha imekaa vibaya au wewe hujagundua?” Amata alimwambia madam S huku akikimbili upande wa pili wa ofisi hiyo kubwa, kitu kidogo mfano wa kifungo kikaanguka kutoka katika picha hiyo, Amata alisimama na kukiangali kidubwasha hiko, Madam S alikitazama na kushika kichwa, akakiokota, kilikuwa ni kinasa sauti, kifaa kilichona sauti na kupeleka sehemu Fulani wasiyoijua, Madam S alirudi na kuketi katika kiti chake akitazamana na Amata, hakuna aliyemsemesha mwenzake, Amata akairudisha ile picha pale ukutani na kumpa madam S kile kidubwasha. Madam S akakichukua na kukivunjavunja, kisha akajitupia kwenye kiti chake, akamwangalia Amata na kumuona kuwa ni mtu wa ajabu sana, alijiuliza kidubwasha hiko kimekaa pale kwa muda gani, hakupata jibu, kama waliweka ili kupata siri za ofisi je; hapo alichanganyikiwa kabisa.
“Umejuaje kuwa hiyo picha ilikaa vibaya” Madam S alimtupia swali Amata
“Nilipokuja wiki ikiyopita hii picha haikuwa hivi, leo nimeona imeyumba kidogo” Amata alijibu “Jesus!” Madam S alinong’ona, kwa jibu la Amata aligundua kuwa kidubwasha hiko kilipachikwa karibu wiki moja nzima hapo ukutani.
“Haya! Nambie kilichokuleta, nilishakwambia usije hapa bila kuniambia” Madam S alimueleza Amata kwa utani wa mtu na mtoto wake
“Mama nina njaa nimekuja unipe lunch” Amata alijibu kwa kudeka “Gina yuko wapi?” Madam S alimuuliza Amata
“Nimempa kazi moja hivi ofisini, kuna mzigo wa kuufaulisha kutoka bandari kavu ndiyo anatengeneza mazingira” Amata alijibu.
Baada ya mazungumzo mafupi waliteremka ngazi na kuliendea gari la Madam S, walipolikaribia Amata alimshika mkono Madam S kama ishara ya kutofungua mlango wa gari hiyo. Walitoka na kuchukua tax mpaka mgahawa wa Steers na kuketi, juice mbili zikawa mezani na sambusa kadhaa. Mara wateja walokuwa hapo walinyanyuka mmoja mmoja na kuingia ndani ya mgahawa huo wote walisimama mbele ya luninga kubwa wakitazama habari fulani, Madam S na Amata walibaki palepale lakini hawakujua kwa nini watu wale wamevutiwa na habari hiyo, Amata alitaka kunyanyuka kuelekea huko ili ajue kilichojiri, Madam S akamvuta mkono na kumrudisha kitini. “Tumia akili, sio unakurupuka tu!” alimwambia Amata ambaye wakati huo alikuwa akitoa kicheko cha kitoto. Madam S alitoa simu yake kubwa mkobani na kuiwasha simu ile ilikuwa na uwezo wa kukamata matangazo ya televisheni ya kidigitali bila chenga, akabofya vitufe fulani fulani kisha akatulia kuangalia
“What!? Jesus!!” Madam S alipata mshtuko na kumpa simu ile Amata, wote walihamanika na taarifa ile
“IGP?! Ameuawa!!” walijikuta wote wakinyanyuka kwa pamoja na kuacha juice zao, lakini baada ya hatua mbili tatu, Amata akarudi mezani na kupiga tarumbeta juice zote mbili na kisha kuondoka eneo lile.
Mwili wa IGP, Bw Makabayo, mkuu wa jeshi la polisi Tanzania ulikuwa umelala juu ya machela ukiwa umefunikwa na kitambaa cheupe mpaka kifuani na kuruhusu sehemu ya juu kuonekana.
Madam S akiwa anafuta machozi alishikwa bega na Kamanda Amata na kumuegemeza kwake akimbembeleza. Viongozi mbali mbali walifika mchana huo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya rufaa ya Muhimbili kushuhudia walichokisikia, hawakuamini lakini ukweli ulikuwa ndiyo huo.
HALI ILIVYOKUWA
IGP alikuwa katika safari ya kikazi akitoka makao makuu ya jeshi la polisi, jingo la wizara ya mambo ya ndani na kuelekea Lumo Kigilagila kufungua kituo kidogo cha polisi katika mtaa huo, msafara wake ulikuwa na gari mbili tu, mbele ilitangulia golf na yeye mwenyewe alikuwa katika Toyota Prado iliyokuja nyuma, walipoiacha barabra ya Nyerere na kuingia barabara ya Jet, kwa mwendo wa kawaida walivipita viwanda eneo hilo kuuzunguka uwanja wa ndege, wakiwa katika kona ya mwisho walipishana na gari nyingine ailiyokuwa ikiyumba njia nzima kiasi kwamba ilibidi gari zingine zisimame. Msafara wa IGP haukusimama bali ulipikwa upande wa kulia hapondipo iliposhuhudiwa kioo cha Prado kikitawanyika nakumwagika kama chumvi, gari iliacha njia na kuingia kwenye mtaro wa maji uliojengwa pembeni mwa barabara hiyo. Polisi waliokuwa kwenye golf walishuka haraka na bunduki mkononi walipofika hapo tayari walikuta IGP hana uhai tena, bila kuchelewa waliwabeba katika golf na kurudi mjini.
Majambazi watatu waliokuwa katika Land Rover 110 waliifanya kazi yao kwa umakini na kasi kama walivyoelekezwa, kwa kutumia bastola maalum ya kizamani PSS silent pistol, bastola ya kirussia iliyotengenezwa 1983, inaonekana mtumiaji alifuzu mafunzo maalum ya kuitumia bastola hiyo inayofanya kazi yake kwa ukimya wa hali ya juu.
Hakuna aliyeamini kilichotokea kila mmoja alijiuliza kwa nini IGP Makabayo kukumbwa na umauti katika jinsi ile, kama ilivyo ada kwa jeshi la polisi, mara moja walianza kufanya uchunguzi wa tukio lile, walifuatilia nyendo za gari lile ambalo si mpita njia wala aliye dukani aliiona namba yake kwa jinsi lilivyokuwa mwendo wa kasi, walijaribu kulifukuzia lakini walichoambulia ni kulikuta Tazara karibu na kampuni ya Azam likiwa limeegeshwa pembeni na hakuna mtu ndani yake. Baada ya kufanya yote ambayo kanuni zao zinawataka walilivuta na kulipeleka kituo cha polisi kati na msako wa kuwasaka wauaji ulianza.
Walijaribu kuangalia gari ile ni mali ya nani baada ya kuwasiliana na wakala husika wa magari hayo CMC, jibu walilolipata liliwaridhisha kidogo, lilikuwa ni mali ya mburushi mmoja aliyekuwa akiishi huko Mbalali kwenye mashamba ya mpunga, lakini jambo moja likawachanganya, katika kadi kivuli ya gari hiyo kulikuwa na jina la mtu mwingine kabisa, walipowasiliana na TRA wakapata jibu kuwa hilo gari lilishauzwa na mmiliki alishabadilishwa katika kadi, kadi ilionesha gari ni ya Bw. Costantino Chawala. Baada ya kuchunguza kwa kina hata huyo Costantino Chawala alishafariki siku nyingi nyuma.
Bujumbura – Burundi
Kikao cha watu wachache kilifanyika katika moja ya vyumba maalum ndani ya mgahawa wa Amahoro (Amahoro Cafe), uliopo katikati ya viunga vya jiji la Bujumbura. Maelewano yalikuwa tete. Msemaji mkuu wa kikao hicho, Madam Rose alionekana wazi kukasirishwa na yaliyotokea
katika mission yao hiyo, Mpango Hasi.
“Kweli kabisa, niliwaamini sana lakini inaonekana mna uzembe wa hali ya juu sana” Madam Rose aliongea kwa hasira huku akipigapiga meza yake, akawatazama vijana wale waliokaa viti vya mbele tu ya meza yake, “Hamjui kazi? Au uzembe tu?” aliwatupia maswali ya haraka haraka. Wote walionekana kushindwa maswali hayo machache lakini yenye fedheha kwao.
“Jomse!” Madam aliita “Hata wewe ninayekuamini na kukuweka mstari wa mbele, leo umeniangusha namna hii!”
“Hapana Madam Rose” Jomse alisema
“Hapana nini; wakati hali yenyewe inajidhihirisha?” Madam Rose aliendelea kuongea kwa hasira. Ukumbi wote ulikuwa kimya kabisa, hamna aliyethubutu kufungua kinywa chake maana walijua moto utakaomuwakia kutoka kwa Madam Rose.
“Tupo hapa, hata hatujui Mandi yuko wapi, kama kakamatwa; na kupata mateso si atatoa siri yote! Hilo la kwanza, la pili, Memory Card, wanaume wapumbavu nyie” Madam Rose aliongea huku akitembea kutoka kona moja kwenda nyingine “Mmepoteza siri yote, eti msichana! Msichana mdogo, anawashinda piga risasi moja ya kichwa mengine yatafuata” alinyamaza kidogo na kuinua bilauri yake iliyojaa maji na kuoiga mafunda kadhaa kisha akaitua mezani. Frank Sabatie akamwangalia mwanamke yule jasiri mwenye maamuzi yasiyopingwa jinsi alivyotingwa kwa mawazo na hofu, mwanamke mwanajeshi aliyekuwa kiongozi wa battalion moja ya katika vita vya msituni, alivuta faili lake na kulifungua kurasa kadhaa.
“Ok! Madama tulia kitini,” alimweleza Madama Rose ambaye alionekana kutokujua nini champasa kutenda katika hili.
“Tuna wasiwasi kuwa siri yetu imeshavuja katika serikali ya Tanzania” Frank alizungumza kwa upole huku akiwa kaikutanisha mikono yake pamoja na kuiegemeza juu ya meza hiyo “ Tuko matatani, Watanzania hawana mchezo hata siku moja, kila raia anailinda nchi yake, kutokana na hili kutukia tunapaswa kutumia nguvu kurekebisha makosa.” Jomse na Tonton walikuwa wameketi kimya wakiwasikiliza mabosi wao, hakuna aliyeongea lolote.
“Sasa hivi, plan B, maandalizi ya mpango hasi yameshaanza matekelezo, kwa kuwa ninyi mlivyoleta uzembe tuliunda kikosi kazi kingine cha watu wanne kutoka nchi za Magharibi, kazi ya kwanza tayari imekamilika siku nne zilizopita, na ya pili si muda mrefu itakuwa tayari. Sasa ninyi tunawageuzia kibao, lazima muende Tanzania mkahakikishe yule msichana anauawa kabla hajatamka chochote, fanyeni kila hila, sistoshe hakikisheni mnarudi hapa na ile memory card hapa” Frank aliongea kwa msisitizo swala hilo. Tonton na Jomse walibaki kumwangalia tu wakisubiri amri kutoka kwa wakuu hao, wakuu wa kikosi kazi.
Kila mtu alikuwa kachanganyikiwa kwa jinsi yake, Madam Rose alitakiwa kupeleka taarifa ya mission yote baada ya siku chache kwenye kikao cha matop, huko Geneva alishindwa afanyeje baada ya vijana hao kuvuruga katika utendaji, missing in action!.
Jomse aliishusha sigara yake kutoka kinywani na kuikandamiza katika kidubwasha maalumu kwa kazi hiyo kilichowekwa mezani hapo, akachukua bilauri yake iliyojaa pombe aina ya Primus na kujimiminia tumboni kabla hajashusha bilauri ile kwa nguvu hata kupasua kitako chake na kufuatiwa na sonyo kali ambalo lilimfanya kila mtu kati mgahawa huo kugeuka. Alinyanyuka na kuchukua suitcase yake, kisha taratibu aliivuta kuelekea barabarani ambako alichukua tax na kupotelea mjini.
Dakika kadhaa, Jomse alikuwa ameingia katika uwanja wa ndege wa kimataifa Bujumbura, tayari kwa safari yake ya kuelekea kunako Bandari salama ‘Dar es salaam’. Safari hii walijua kabisa kuwa wanaweza kushtukiwa hivyo Frank aliwapanga kuondoka kila mmoja kwa staili yake na kuingia Dar es salaam kwa staili yake ili wasijulikane. Walishapewa tahadhari kuwa wawe makini na makachero wa Tanzania na Watanzania wenyewe ‘trust no one’, mara kwa mara sentensi hii ilijirudia kinywani mwa Jomse. Jomse alikuwa na uchungu uliochanganyika na hasira hasa kwa
kulaumiwa na Madam Rose juu ya makosa waliyoyafanya, lakini kilichomuumiza kichwa zaidi ni kuhusu Mandi na Isabel, hakujua kabisa kuwa swahiba wao Mandi alikwishakuwa marehemu.
Akiwa ameketi sawia na kujifunga mkanda katika ndege hiyo ya shirika la ndege la Afrika ya Kusini ‘SA Airline’, alikuwa akijisomea gazeti la Daily Mail alilolikuta kwenye kijimeza kidogo karibu yake, ‘Tanzania’s Inspector General of Police died on car accident’ , habari iliyokuwa juu katika kurasa ya habari za kimataifa, Jomse aliisoma kwa umakini mkubwa sana na akaelewa kuwa kazi imeanza.
Masaa sita baadae Dar es salaam
‘Valley View Hotel, chumba namba 407’, Tonton aliikunja karatasi ile mara baada ya kuisoma, kisha kuitia mfukoni. Aliishusa miwani yake myeusi na kuifuta vumbi kidogo, kisha akairudisha tena usoni pake. Mtu mmoja alipita nyuma yake na kumpiga kibega kisha kumuomba samahani kwa tukio lile, Tonton alinyanyua briefcase yake na kuelekea kule alikoelekea yule kijana. Ilikuwa ni trick ya utambulisho kati yao.
“Kila kitu kipo katika mstari” Kijana mmoja alimueleza Ton wakiwa ndani ya Tax, Ton hakujibu kitu alinyamaza tu.
Tax ailifika mitaa ya Jangwani, Ton alilipia Tax hiyo na kuisogelea hotel iliyokuwa akitazamana nayo, juu ya lango kuu kwenye canopy kulikuwa na maandishi makubwa yaliyosomaeka Valley View Hotel, alipiga hatua chache na kuifikia meza ya mapokezi.
“Tonton, bila shaka!” mdada wa mapokezi alimwambia Ton. Ton alitikisa kichwa kuonesha ishara ya kukubali. Alipewa funguo zake, na msaidizi akamsaidia suitcase yake kuelekea chumbani. Ton aliweka vitu vyake sawa chumbani humo, akajimwagia maji na kujilaza akisubiri muda ufike ili awasiliane na swahiba wake tayri kuanza kazi waliyotumwa.
Polisi katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere walikuwa makini kuchunguza kila ashukae na kuingia nchini, ukaguzi wa kina ulifanyika hasa baada ya kupata tetesi ya mpango hasi uliopangwa na vikundi vya waasi kutoka nchi jirani. Waliamuriwa kumkamata yeyote atakayedhaniwa ili kumhoji kwa kina, haikuwa kazi rahisi maana watu wengi kutoka nchi mbalimbali walifikia uwanja huo.
Majira ya saa kumi na moja na nusu jioni ndege ya shirika la ndege la Tanzania iliikanyaga ardhi yake ya Dar es salaam na kujiegesha sawia kabisa katika ngazi za kuteremkia abiria. Watu walianza kuteremka mmoja baada ya mwingine, vyombo vya usalama vilikuwa makini kuangalia wote washukao katika ndege hiyo. Dakika chache walikuwa wamekwisha na ndipo aliposhuka mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI Salila, akiwa na katibu wake pamoja na watu watatu waliomsindikiza, waliteremka ngazi za ndege hiyo kwa umakini, alipoikanyaga ardhi tu kitu kisichotegemewa kilitokea, DCI Salila alionekana kujishika kifua kwa mikono yake miwili na kuanguka chini, wasaidizi wake walimuwahi kumdaka lakini walichelewa. Walipomuinua tayari alikuwa marehemu Salila, risasi iliyopita upande wa kushoto wa kifua chake iliutoa uhai wake kwa wepesi sana. Damu ilichafua suti yake hasa upande wa pili ilipotokea risasi hiyo. Gari ya wagonjwa iliingia haraka uwanjani hapo na kutoa huduma iliyostahili. Tafrani kubwa ilizuka uwanjani hapo, polisi walitanda haraka eneo la uwanja wa ndege kuhakikisha wanamtia nguvuni aliyetenda hayo.
Lakini uwingi wa watu haikuwa rahisi kufanikisha hilo.
Joseph Msengiyumva au ‘Jomse’ kwa jina bandia, akiwa ndani ya mavazi ya shirika la Dahaco alisitazama tukio zima baada ya kuanguka kwa DCI Salila, huku bastola yake maalum ya kijasusi akiwa ameifutika vizuri uvunguni mwa gari maalumu ya kuvutia ngazi ambazo hutumika kwa kushukia abiria katika ndege kubwa kama ile, bastola tulivu isiyotoa kelele, ndogo inayotosha
kukaa kwenye kiganja cha mkono. Hakuna aliyemdhania, kama ni yeye aliyetekeleza mauaji yale. Alisimama mara moja kutoka pale alipojifanya anaangalia kitu Fulani kwenye gurudumu ya gari hiyo na kwa muda huo ndipo alipotekeleza kazi hiyo kwa ufundi wa hali ya juu kabisa. Alitoka pale alipo na kusogea jirani na tukio kwa ajili ya kutoa msaada.
“Kijana, tunaomba msaada wa haraka.” Wasaidizi wa Salila waliomba msaada kutoka kwa vijana wa Dahaco akiwemo Jomse, baada ya kumaliza kutoa msaada huo na kuhakikisha kuwa mtu yule tayari ni marehemu alirudi na kuchukua kale kagari akaondoka na kuelekea upande wa pili, balaa!
Inspekta Simbeye alijikuna kichwa chake kana kwamba kulikuwa na chawa anayemsumbua. Lakini la, ni katika kuchanganyikiwa tu na mambo yanayomzunguka katika siku hizo. Taarifa juu ya kifo cha DCI Salila, kilizidi kumzeesha kitini hapo, alijikuta akiongea mwenyewe ofisini huku kaishika bastola yake akiitazama tazama. Hakujua hasa ni kitu gani anataka kufanya. Wakati bado machungu ya kifo cha IGP Makabayo hayajafutika katika mioyo ya watu, sasa wanapokea kifo kingine cha mtu wa juu katika medani ya usalama hapa nchini. ‘Lazima kuna mchezo unaofanyika’ alijiwazia huku akiwa kasimama dirishani na kuangalia nje, kijasho chembamba kilimvuja makwapani na kumfanya kutota kiasi Fulani.
Aliinua simu iliyopo mezani hapo na kuzungusha namba fulanifulani kisha kuweka sikioni kidubwasha hiko cha kusikilizia.
“Nini kinaendelea hapo?” aliuliza
“hatujafanikiwa kumkamata muuaji, lakini watu kadhaa tunao kwa mahojiano” sauti ya upande wa pili ilijibu.
“Muwe makini na kazi yenu, msipoangalia huyo muuaji atawatoroka na ninyi mkiwa hapo hapo” Simbeye alitoa maagizo.
“Sawa mkuu, tumekupata” ilijibu sauti ya upande wa pili.
Inspekta Simbeye alishusha pumzi na kutoka nje ya ofisi yake, shughuli za watu ziliendelea kama kawaida kana kwamba hakuna lolote lililotokea la kuhatarisha amani ya nchi. Akiwa na karatasi mkononi lililomtaka kwa muda mfupi awe amefika katika makao makuu ya polisi pale jingo la wizara ya mambo ya ndani, Simbeye alijikuta anzidi kupata wakati mgumu, ukizingatia dhamana ya ulinzi wa mji huu ipo mikononi mwake. Alirudi ofini na baada ya muda mfupi alielekea kuitikia wito.
ITAENDELEA
Isabel Ndani ya Mpango Hasi Sehemu ya Nne
Also, read other stories from SIMULIZI;