Mpatanishi Sehemu ya Kwanza
RIWAYA: MPATANISHI
MTUNZI: RICHARD MWAMBE
SEHEMU YA KWANZA
Aprili 1984
UKUMBI WA RAILWAY GEREZANI
“Ina maana unafurahia kwa ushindi wake?”
“Of course yes! Jamaa anapiga ngumi za kilo nyingi, yaani kamtwanga Kibwana mpaka kamwacha na meno ishirini na nane…”
“Na uhai kamwondoa!”
“What? Unasemaje wewe?”
“Ndiyo maana nikakuuliza unafurahia ushindi wake?”
Badala ya kujibu swali lile Stella aliamua kuinuka na kutoka nje ya ukumbi huo uliosheheni watu waliokuwa wakishangilia kwa kelele na mbinja zenye kukera masikioni mwa wasiopenda. Ijapokuwa alipata upinzani mwingi katikati ya mashabiki hao wa mchezo wa ngumi, mwishowe alifanikiwa kutoka kabisa na kujikuta nje. Baada ya kujikuta nje akagundua kuwa hana pa kwenda zaidi ya kusimama na kushangaa magari yapitayo kutoka Kurasini kwenda Shule ya Uhuru.
“Stella! Stella!” Sauti ya kiume ikasikika nyuma yake ikiita kwa mbisho. Stella hakugeuka nyuma zaidi ya kuikusanya mikono yake kifuani mwake na kutulia kimya kabisa.
Mtu mzima, ambaye ngozi ya mashavu yake tayari ilianza kujikusanya na kufanya makunyanzi alisimama kando ya binti huyo. Hakuwa mtu mzima bali msichana mwenye kadiri ya miaka ishirini na tano hadi thelathini hivi.
“Sasa kilichokutoa nje ni nini?” Yule mtu mzima akauliza.
“Sasa si pambano limeisha, nikae nifanye nini?” Stella akajibu.
“Sidhani kama umetoka kwa sababu hiyo!” Yule mtu mzima akaonesha shaka.
“Mzee taksi, twende!” Dereva wa taksi alimwita mzee huyo kwa sauti kwa kuwa yeye alikuwa upande wa pili wa barabara ile. Gari lake aina ya Volvo ilikuwa bado inaunguruma.
“Tuondoke na hii…” Yule mtu mzima akamwambia Stella. Msichana huyo hakujibu zaidi ya kubetua mabega kuashiria hataki.
“Tunapanda UDA, sasa hivi litakuja…”
“Utapandaje UDA na mimi nipo? We ni malkia wangu watakiwa kutumia taksi mama kufika kwako…”
“SITAKI, EH!” Stella akajibu kwa sauti ya juu wakati huo tayari watu walikuwa wamezagaa kila upande nje ya ukumbi huo, wakitoka kushuhudia pambano la ngumi kati ya Joseph Marwa na Kibwana Mtwana. Pambano hilo lililokuwa gumzo katika kona za Jiji la Dar es salaam lilimalizika kwa raundi tatu tu baada ya Kibwana Mtwana kupigwa kwa K.O. Kila aliyetoka alikuwa akizungumzia mchezo huo. Dakika chache za ukimya zikamfanya Stella na yule bwana wajikute mbele ya basi kubwa jekundu lenye maandishi ‘UDA’ ubavuni mwake. Basi hili aina ya Leyland lilimeza watu wa kutosha akiwamo Stella na yule mtu mzima.
Safari nzima ilikuwa ni ya ukimya kati ya wawili hawa, zaidi ya mazungumzo ya abiria wengine walikuwa wakisikia mlio mkali wa basi hilo. Haikuchukua muda kufika katika kituo cha Shule ya Uhuru, wakateremka kwa kuwa safari ya basi hilo iliishia hapo.
“Tunaelekea wapi?” Yule mtu akamuuliza Stella.
“Ukitaka tuelewane nipeleke DDC Kariakoo nikacheze muziki wa NUTA,” Stella akamwambia mshikaji wake huku akiweka sawa nywele zake alizochoma mchana wa siku hiyo.
“DDC hakuna NUTA leo! Twende Mlimani Park tukaburudike,” akamwambia.
“Aaaaaa! sawa!” Stella akakubali, wakavuka barabara na kuingia katika taksi iliyokuwa mbele yao, nayo ikaondoka kwa kasi. Yule dereva akafungu droo katika dashboard ya gari hiyo na kuchomoa bahasha ya kaki, akampatia mtu huyo. Yule mtu mzima akashangaa kabla ya kuipokea.
“Yangu?” Akauliza.
“Ndiyo! Yako”.
Yule mtu mzima akaipokea na kuigeuza, upande wa juu ilikuwa imeandikwa ‘TANZANIA GOVERNMENT’ na pembeni yake karibu na kona ya kulia juu iligongwa mhuri wa rangi ya zambarau wenye neno moja tu la Kiingereza, ‘CONFIDENTIAL’.
Akaichukua na kuifutika ndani ya koti alilovaa, kisha akashusha pumzi ndefu na kujiegemeza katika kiti cha nyuma, akauinua mkono wa Stella na kuuweka juu ya paja lake.
“Bora umenilipa pesa zangu!” Yule mzee akamwambia dereva mara baada ya kuona Stella akitaka kumtwanga swali, akamkatisha na tayari akawa amempa jibu kwa swali lake.
“Mzee unafika wapi?”
“Mlimani Park!” akajibu.
“Unaonaje nikikupeleka Magomeni Lango la Jiji?”
“Kuna nini?”
“Kuna taarabu ya JKT inapiga pale…”
“Aaaaaaaa! Ewe njiwa, ewe njiwa, peleka salaamu…” Mtu mzima akamalizia.
Muda wote wa mazungumzo kati ya dereva huyo na yule mtu mzima, Stella alikuwa kimya kabisa huku mkono wake ukiwa juu ya paja la mzee huyo. Ile Peugeot ikasimama mbele ya mlango mkuu wa ukumbi huo maarufu katika jiji la Dar es salaam.
“Twende mrembo wangu,” akamwambia Stella.
“Mzee!” Yule dereva akaita na mtu mzima huyo akasogea karibu, akainama kidogo kwenye usawa wa kioo cha mbele upande wa abiria.
“Kaa meza ile ile ya siku zote!” akamnong’oneza kisha akaondoa gari kwa kasi na kumwacha mzee huyo akiwa kasimama palepale.
“Inaonekana unamjua vyema kijana huyu,” Stella akamwambia mzee huyo mara baada ya kufika pale aliposimama.
“Ah! Ni mdeni wangu,” akamdanganya kisha akamkamata kiuno na kuingia naye katika ukumbi huo uliofurika watu.
Ukumbi huo ‘ulitapika’, wasemavyo watoto wa mjini, taarabu ya JKT ilikuwa ikitumbuiza huku watu wakijipatia vinywaji na mishikaki. Stella aliketi katika moja ya viti vingi ndani ya ukumbi huo na kufuatiwa na mzee wake. Kidogo tu, mhudumu aliwafikia na kuwasikiliza na baada ya maagizo wakaletewa vinywaji. Huyu mtu mzima hakuwa na utulivu hata kidogo, macho yaliyofunikwa na kofia ya ‘Mungu Usinione’ yalikuwa yakiutalii ukumbi ule. Stella alikuwa akiburudika na muziki huo laini huku akinywa kinywaji chake taratibu na huku akifuatisha maneno matamu ya wimbo huo kila apumzikapo.
“Mbona hutulii?” Stella akamuuliza mtu mzima.
“Aaaa! nimebanwa kidogo…”
“Si uende chooni” Stella akashauri na yule bwana akashukuru moyoni kwani alitaka kufanya hivyo muda mrefu isipokuwa alikuwa akimwogopa msichana huyu mrembo.
Stella alikuwa msichana mbembe, alipenda wazee na watu wazima wenye pesa, penzi atakupa ilimradi tu umshikishe kibunda chake. Kwa mzee huyu alinasa, pesa iliyotakata aliipata, hakuwa na shida na mabwana mengine zaidi ya zee lake hili. Mapenzi aliyopewa mtu mzima huyu yalimfanya asahau shida na familia yake. Alibebwa, akaogeshwa, akapetipetiwa na kufanyiwa kila aina ya mahaba, akaridhika.
Mwanamke si ndiyo huyu! Akajisemea kila alipomtazama akiwa kama alivyozaliwa. Kutokana na haya yote, mtu mzima huyu hakuwa na kauli juu ya ratiba yake ya maisha, akiamuliwa hivi hufuata, akiamuliwa vile hutii. Mara hii alipewa bahasha ya kikazi, lakini alijikuta akishindwa hata kutafuta nafasi ya kuisoma kwa kumwogopa Stella. Mtu mzima akatabasamu na kuvuta hatua kuelekea choo cha wanaume. Ndani yake, akajifungia, akapachika mkono wake ndani ya koti na kuitoa ile bahasha, akaigeuzageuza na kuichana kisha akaisoma taratibu sana. Haikuwa na maandishi mengi isipokuwa machache ambayo yalichapwa kwa mashine ya kupigia taipu ya Oliveti. Alitambua hata upangaji wa maneno na kujua kuwa mwenye mtindo huu si mwingine zaidi ya Fatuma Beka ambaye alikuwa akifanya kazi katika ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
‘Ikukutapo bahasha hii, fika Lango la Jiji, meza ya kwenye kona kushoto mwa ukumbi, Ukitakiwa kusoma gazeti, sema ndiyo, kisha soma kurasa ya 11’
‘D’
Asante
Kijasho chembamba kikamtiririka, akaikunja ile karatasi na kuitia kinywani, akajiweka sawa na kuifutika bahasha katika mfuko wa nyuma wa suruali yake ya dengiriz kisha akatoka nje. Alipopiga jicho katika meza aliyomuacha Stella, hakumuona.
Kaenda wapi? Akajiuliza kisha akasonya na kupiga hatua nyingine kadhaa mpaka katika ile meza, alichokikuta ni chupa yenye bia nusu, basi. Tayari kwa kutoweka msichana huyo, mtu mzima akasahau majukumu ya kikazi, akaketi katika kile kiti na kutulia kimya kwa nukta kadhaa. Alipokumbuka barua ile imemwambia akakurupuka kama mbwa aliyefurumushwa sehemu, akaiendea ile meza na kuketi.
Dakika chache tu, mhudumu wa baa hiyo akamsogelea na kumsabahi.
“Karibu sana, kinywaji gani?” akauliza.
“Pilsner tafadhali…”
“Unapenda kusoma gazeti?”
“Yap,” akajibu na yule mhudumu akapotelea.
Mtu mzima Yule aliendelea kuzungusha macho yake huku na kule kama atamwona Stella, hakumwona, akasonya na kupiga ngumi mezani.
“Vipi kaka?” akashtushwa na sauti kutoka nyuma yake, kabla hata hajageuka mgeni huyo akajikaribisha mwenyewe na kuketi katika kiti kilichokuwa mbele yake, wakatazamana.
“We n’nani?” mtu mzima akauliza.
“Huna haja kujua, ila nilitaka kukujulisha tu kuwa kasichana kako nimekachukua na ninakwenda kukahifadhi mpaka utakapokaidi kazi utakayopewa,” yule kijana akamwambia mzee huyu. Macho makali ya mzee huyu yalimtazama yule kijana kwa nukta kadhaa.
“Unamjua unayemwambia maneno hayo na kujitamba mbele yake kuwa umemchukua msichana wake?” Akamuuliza.
“Sina haja ya kumjua!” Yule kijana akajibu.
“Sawa, basi nimesikia, mchukue huyo msichana… kwa taarifa yako, maisha yako hayana thamani kama msichana huyo…”
“Kwenda huko!” Yule kijana akang’aka na kuinuka, kisha akaanza kuondoka.
“Unasikia kijana, kama hujawahi kunisikia, mimi ndiyo Chameleon!” akamwambia, na wakati huo huo yule mhudumu akawa tayari amefika na kumwekea gazeti mezani. Chameleon akamtazama kijana yule akipotelea kwenye kundi la watu huku akielekea mlango mkubwa. Haraka akanyakua lile gazeti na kuelekea upande wa chooni huku akiacha kinywaji chake bila kukigusa.
* * *
Nje ya ukumbi ule kulikuwa na magari mengi sana yameegeshwa huku na huko, walevi na wanaouza miili yao walikuwapo pia. Yule kijana alipotoka tu ndani ya ukumbi ule akayapita magari kadhaa na kuingia ndani ya Volkswagen moja jeupe, Transporter. Katika kiti cha mbele, kushoto, akaketi, kisha akageuza uso wake nyuma na kutazama.
“We are going for honeymoon baby!” Akamwambia Stella.
Stella hakuweza kujibu chochote kutokana na gundi la plastiki lililobandikwa midomoni mwake, miguu yake na mikono ilifungwa kwa kamba katani. Hakuwa kwenye kiti, kwani gari hiyo ilikuwa na viti viwili tu, cha dereva na abiria wake mmoja. Kila alipojaribu kujikukurusha hakufanikiwa kwani mfungaji wa kamba zile aliijua vyema kazi yake.
“Let us go!” akamwambia dereva naye akaliondoa lile gari kwa kasi mpaka watu wa nje wakaanza kupiga kelele. Akiwa katika mwendo huo, kabla hajamaliza kuupita wigo wa ukumbi ule, Yule dereva akakanyaga breki na gari ikasimama ghafla.
“Vipi?” Yule kijana akamuuliza dereva.
“Kuna mtu mbele!” dereva akajibu ndipo yule kijana naye alipotazama vizuri, kweli, akaona mtu aliyesimama katikati ya barabara akiwa na koti refu la rangi ya chai ya maziwa akiwa amejishika kiuno, kichwani mwake alikuwa kavalia kofia ya Mungu Usinione.
“Mgonge!” akamwabia. Yule dereva akaliondoa tena lile gari kwa kasi kwa minajili kumpamia yule mtu lakini ghafla lile gari likayumba na kugonga nyumba iliyokuwa pembeni mwa barabara. Chameleon akashusha mkono wake wenye bastola kubwa aina ya Revolver. Kishindo kilichosikika kilifanya watu waanze kukimbilia eneo lile kujua kulikoni.
Ndani ya gari yule kijana akamtazama dereva wake na kumkuta akiwa na jeraha baya kabisa la risasi kisogoni mwake. Tayari watu walikwishajaa katika eneo lile, Chameleon alijichanganya na kufanikiwa kulifikia lile gari lakini zaidi ya mwili wa yule dereva hakuona mtu mwingine. Vurugu za watu zikamfanya atoke haraka eneo lile na kusimama kando akitazama huku na kule kama atamwona yule kijana au Stella.
Amenizidi akili! Akawaza kisha akavuta hatua na kuvuka barabara mpaka kwenye moja ya kibanda cha simu, akaingia na kuchukua lile gazeti, akalifungua ukurasa aliotakiwa kusoma. Hakukuwa na kipya zaidi ya makala ndefu iliyojaa upande huu mpaka ule. Makala ile ilikuwa ikizungumzia juu ya kilimo cha kisasa kilichoanzishwa na walowezi huko Zimbabwe. Akapitisha macho na kuhesabu maneno machache ambayo yalikuwa yamezungushiwa miduara kwa kalamu nyekundu. Kichwani mwake akayakusanya maneno yale ambayo yamezungushiwa miduara na kuyaunganisha kwa akili yake na kupata sentensi kamili.
Kamati ya mapatano itakutana jijini Harare kesho.
Fika bila kukosa katika Hoteli ya Zim maagizo utayakuta hapohapo.
Baada ya kuunganisha maneno yale, akapata ujumbe huo.
Zimbabwe! Akawaza.
Niende Zimbabwe au nimtafute Stella? Akajiuliza bila kupata jibu.
“Huna haja kujua, ila nilitaka kukujulisha tu kuwa kasichana kako nimekachukua na ninakwenda kukahifadhi mpaka utakapokaidi kazi utakayopewa,” alipoikumbuka kauli hii aliyoambiwa na yule kijana, akameza funda kubwa la mate.
Ina maana huyu kijana alikuwa anajua juu ya kazi hii kabla yangu? Akajiuliza.
Anachotaka nisiende Zimbabwe ndiyo anipe Stella wangu, huu mtihani! Akatia shaka moyoni. Alipoinua saa yake na kutazama, ilimwonesha kuwa ni saa nne za usiku. Na mara hiyohiyo ile simu pale kibandani ikaita. Si kawaida kwa simu za vibandani kuita, kawaida hutumika kwa kupiga tu. Chameleon, akageuka na kuitazama, kisha akainyakua na kuiweka sikioni bila kuongea lolote.
Usipokaidi namkata kichwa, na kitakachotokea Zimbabwe hutoamini, na serikai yako itapoteza matumaini na wewe!
Go or do not go… Is up to you!
Ile simu ikakatika na kumwacha mzee huyu akiwa kaduwaa hajui nini cha kufanya. Akatoka ndani ya kile kibanda cha Posta na Simu na kuingia mitaani. Mtaa kama wa tatu hivi akachukua taksi na kumtaka dereva amfikishe Kawe Mzimuni. Chameleon akamlipa dereva huyo kisha akasubiri aondoke, ile taksi ilipopotea kabisa, ikapita gari nyingine Ford Angria kwa mwendo wa taratibu kabisa na kwenda zake. Hatua chache zikamfikisha katika nyumba yake kubwa aliyoijenga miaka kadhaa nyuma. Ndani ya nyumba hiyo alimkuta mkewe akimsubiri sebuleni huku akisikiliza kipindi cha Lala Unono kutoka RTD.
“Karibu mume wangu!” akamkaribisha. Mzee huyo akajitupa kochini na kushusha pumzi ndefu.
“Vipi, nikuandalie maji uoge?”
“Hapana, muda umenitupa mkono, nahitaji kusafiri usiku huu kuelekea Zimbabwe, vipi umesikiliza kipindi cha ATC Hewani?” Chameleon akamuuliza mkewe.
“Eh! Mume wangu safari tena, si juzi tu ulikuwa Misri? Unakumbuka kuwa kesho kutwa ni kumbukumbu yetu ya ndoa?” Mkewe akamuuliza.
“Najua, lakini nitafanyaje nawe unajua kazi zangu! Nijibu basi…”
“Nimesikiliza, ndege ya nje ipo inayokwenda hapo hapo Zimbabwe!” Yule mama wa Kizigua akajibu.
Chameleon akaiendea simu mezani, akavuta kiti na kuketi, akiinua mkonga wa simu ile na kukoroga namba kadhaa kisha akaiweka sikioni. Simu ile ikapokelewa na opereta wa idara ya Posta na Simu.
“Naomba niunganishe Uwanja wa Ndege tafadhali…” akamwambia opareta yule.
“Subiri kidogo!” akajibiwa.
Sekunde kama thelathini hivi akasikia sauti ya kiume ikiita na kutambulisha kuwa hapo ni uwanja wa ndege.
“Nahitaji usafiri wa kufika Zimbabwe usiku huu…” akamwambia.
“Nafasi ipo, lakini ndege inaondoka dakika tisini zijazo…” mtu wa upande wa pili akajibu.
* * *
Dakika kumi kabla ya ndege ile kuondoka, Chameleon alikuwa mtu wa mwisho kuketi kitini, akafunga mkanda tayari kwa safari hiyo ya dharura. Mpaka dakika hiyo alikuwa akijua tu kuwa anakwenda kwa ajili ya mkutano wa kamati hizo. Ulikuwa mkutano muhimu sana kati ya Serikali ya Tanzania na Makaburu kutoka Afrika Kusini. Mkutano huu ulipangwa kufanyika katika Jiji la Harare nchini Zimbabwe na wajumbe wa pande zote mbili walitakiwa kufika siku hiyo.
Masikini Stella wangu! Akajiwazia wakati ndege ikiwa inakaa sawa angani.
Wacha nifanye kazi kwanza, na nikirudi watanikoma kama watakuwa wamemuua! Lakini wana uhusiano gani na kazi hii ninayoifanya na wamejuaje kama mimi ninatumwa huko? Maswali mengi yakampitia kichwani mwake asipate jibu. Muziki wa Kilwa Jazz ulikuwa ukitumbuiza kwa sauti ya chini, hakuna aliyekuwa anaongea, wengine walionekana kusinzia na wengine kusoma vitabu ili mradi tu kuifanya safari hiyo kuwa fupi.
****Mnh! Mambo juu ya mambo…Stella matatani, na safari ya Zimbabwe ndo imeiva. Ina maana Stella ndio basi tena??
Also, read other stories from SIMULIZI;