Najisikia Kuua Tena Sehemu ya Kwanza
NEW AUDIO

Ep 01: Najisikia Kuua Tena

Najisikia Kuua Tena Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA


Simulizi : Najisikia Kuua Tena

Sehemu Ya Kwanza (1)

POLISI…kikosi cha kumi na mbili…Inspekta Kombora anaongea. Nani mwenzangu?”

Kwa muda kukawa kimya. Kombora alisikiliza kupumua kwa dalili ya hofu katika chombo cha simu kutoka upande wa pili. “Nani mwenzangu?” akaongeza nguvu kidogo.

“Ni Kombora mwenyewe anayeongea?” iliuliza sauti hiyo yenye wasiwasi kutoka upande wa pili.

“Ni mimi, nani mwenzangu?”

“Ndiye! Mkuu wa kituo hicho sio?”

“Ndiye, tu…”

“Sikiliza Inspekta,” sauti ilidakia na kunong’ona harakaharaka, “Nina tatizo zito sana. Sijui kama utaweza kunisaidia.”

“Nadhani tunaweza. Tutajie tatizo lako na jina lako ili tujadiliane.”

“Jina sitaji,” iliongeza sauti hiyo, “Na tatizo lenyewe ni zito sana, siyo mzaha. Najisikia kuua mtu Inspekta. Najisikia kuua. Na ni lazima niue. Waweza kunisaidia Inspekta?”
“Kuua!” Kombora aliropoka. Katika matatizo yote, hilo kamwe hakulitegemea. Ni rahisi mtu kupiga simu polisi na kusema “mtu anataka kuniua.” Ni rahisi pia mtu kudai “nilimwona fulani akiua” lakini “nataka kuua” lilikuwa jipya kwa Inspekta Kombora.

Angeweza kulichukulia suala hilo kwa mzaha; kwamba ni chizi au mlevi mmoja ambaye ameamua kuwasisimua polisi lakini uchizi au ulevi haukuwemo kabisa katika sauti hiyo. Ilikuwa sauti dhaifu iliyojua kipi inasema. Kwa muda Kombora aliduwaa akiwa hajua lipi amjibu mtu huyo.

“Upo Inspekta?” ilihoji sauti.

“Nipo ndugu yangu,” Kombora alijibu kwa unyonge.

“Mbona kimya? Huna msaada wowote?”

“Ninao. Sikia rafiki yangu, njoo zako hapa mara moja ili tukae na kulijadili tatizo. Naamini tutakusaidia.”

“Hilo sifanyi Inspekta. Nikija huna uwezalo kufanya zaidi ya kunitia ndani, na mimi nauhitaji uhuru wangu. Kama huna msaada mwingine…”

“Ninao. Ni hivi, u nani jina lako?…Uko wapi?…Na unayetaka kumuua ni nani…Kwa nini?…Haloo!…Haloo!…”

Haikumchukua muda Kombora kung’amua kuwa alikuwa akizungumza katika simu iliyokatwa. Kwa muda aliendel;ea kuduwaa, simu mkononi, macho kayakodoa kutazama ukuta uliokuwa mbele yake, akiwaza mengi. Kisha alitua simu na kuinuka. Mara akakumbuka kuwa hakujua anakotaka kwenda. Akaketi na kutikisa kichwa kwa wingi wa mawazo mazito yaliyomjaa ghafla.


KITENGE alizinduka kutoka usingizini kwa kugutuka kidogo. Hakujua kilichomwamsha ghafla hivyo. Akatazama huku na huko kama anayejaribu kutafuta kitu hicho kilichomfanya auache usingizi wake ambao haukuwa na ndoto yoyote.

Mara mlango ukagongwa tena, ndipo alipokumbuka kuwa kilichomwamsha ni mlio wa mlngo huo. Kwa dalili za uchovu aliinuka kutoka kitandani na kuvuta taulo iliyokuwa juu ya kiti, akaitanda kiunoni, kisha aliuendea mlango na kuufungua.

Mlango huu ulimfikisha ukumbini ambapo alipita kuuendea mlango mkubwa, macho yake yakiipitia saa ya ukutani ambayo ilidai kuwa ni saa kumi na mbili kasoro dakika nne, jambo ambalo lilimshangaza mno, kuona ugeni wa alfajiri kama hiyo.

Alifungua mlango; aliyesimama hapo nje alikuwa ni mwanamke ambaye Kitenge, baada ya kumtazama kwa muda, alimkumbuka. Alikuwa ni Machozi Rashidi. Mwanamke ambaye alipokuwa msichana waliishi jirani na Kitenge wakihusiana kwa njia mbalimbali katika harakati za maisha baina ya wasichana na wavulana.

Kitenge hakujua kama ilimpasa kumkaribisha au la. Kwa kila hali huyu hakuwa yule Machozi ambaye Kitenge alimfahamu wakati ule. Huyu, wakati ulikuwa umemwathiri sana na kumtenga mno na Kitenge kiasi cha kumfanya aionee aibu kila dakika ambayo aliendelea kusimama naye hapo mlangoni.

Hakuwa mwanamke wa haja hata kidogo. Kama aliwahi kuwa mzuri, Kitenge hakuiona dalili yoyote ya uzuri iliyosalia katika sura hiyo. Sasa ilikuwa sura kavu, yenye mikwaruzo mingi, macho mekundu kwa athari ya kitu kama gongo au bangi, nywele nyekundu, kavu zenye dalili zote za kutoonja aina yoyote ya mafuta. na mwili mzima ulikuwa na mikwaruzo juu ya ngozi hiyo kavu na ilikuwa dhahiri kuwa mwanamke huyu aliishi kwenye mazingira yasiyofaa. Ngozi hiyo ilifunikwa na mavazi hafifu ambayo pamoja na kuwa dhaifu yalikuwa yamechanika hapa na pale.

“Haunikaribishi Boni?” aliuliza mwanamke huyo. Sauti yake pia ilikuwa tishio jingine, haikuwa ya mwanamke hata kidogo, wala haikumfaa mwanamume. Boni lilikuwa jina la utotoni la Kitenge ambalo sasa lilikuwa limetoweka kabisa baada ya majina mengine kuibuka, majina ambayo yalifungamana na hadhi yake mpya. Kwani sasa Boni alikuwa mwandishi maarufu wa vitabu.

Ghafla jina hilo likamkumbusha uhusiano wa kimapenzi aliokuwanao awali na kiumbe huyu.

“Ingia,” alimwambia.

Mwanamke huyo aliingia ndani na kufuata moja ya makochi sita yaliyopangwa kistaarabu katika ukumbi huo. Alitazama kila upande akihusudu hiki na kuvutiwa na kile. Kisha akamtupia Kitenge macho yake mabaya. “Hongera,” akakoroma kwa sauti hiyo ya kuchukiza.

“Kwa?”

“Vitabu vyako. Hukujua kuwa hata sisi washamba ambao hatukusoma tungeweza kuviona? Ulidhani kuwa tusingeona hata picha nyuma ya vitabu hivyo? Ama hujui kuwa hata redioni vinaongelewa? Pamoja na hayo, ningependa kukujulisha kuwa ingawa sikusoma sana, naweza kuelewa waandishi wanasema nini katika magazeti yao. Karibu wote wanakusifu. Hongera tena Boni.”

Kitenge hakujua kwamba ilimpasa kufurahi au kuchukia kwa sifa hizo. Kusifiwa halikuwa jambo geni kwake. Tangu alipotoa kitabu chake cha kwanza, MACHOZI YA DAMU, kupata sifa lilikuwa jambo la kawaida. Kitabu cha pili, KIFO USONI, kilimzidishia sifa kemkem, cha tatu na ambacho ni kama cha mwisho katika vitabu vilivyokwishatolewa; ALIKUFA ANACHEKA, kilifanya sifa zitapakae pembe zote kiasi cha kumtia katika mashaka ya kukosa nafasi ya kufikiria vitabu vingine.

Kila alikopita aliandamwa na ‘hongera’, yeyote aliyemfahamu alimtupia tabasamu. Waandishi wa habari walimtaka picha na mahojiano mara kwa mara. Katika baa moja aliwahi kuona maandishi yanayosema ‘Kondokondo Kitenge zaidi…’ na kadhalika. Hata katika basi ilikuwa ni jambo la kawaida kukuta kikundi cha watu kikizijadili sifa zake.

Naam, kusifiwa kwake sasa lilikuwa jambo la kawaida. Lakini sifa hizi za alfajiri, kutoka kwa mama huyu ‘aliyechoka’ kwa sauti yake ambayo licha ya kuchakaa, ilidhihirisha kitu kama kebehi, unafiki au uadui katika sifa hizo, zilimfanya ghafla ahisi jambo lisilo la kawaida katika nafsi yake. Wasiwasi ukamwingia rohoni. Wasiwasi ambao nafsi yake ilipokonywa na hasira, akajikaza kisabuni kumtazama mama huyo huku akisema, “ Nadhani hukuja asubuhi yote hii kwa ajili ya kunisifu. Niwie radhi, kama huna zaidi, nenda zako ili nijiandae kwenda zangu kazini.”
Machozi akacheka. Kicheko chake kilikuwa kitu kingine cha kutisha, na kilikuwa mbali kabisa na kicheko cha mwanamke, na karibu zaidi na kile cha shetani.

“Nilitegemea hutasema hayo,” alisema. “Najua umekuwa mtu mkubwa na tajiri sasa. Umetoa nakala elfu ngapi hadi sasa? Haikosi una akiba ya milioni benki. Mungu akujalie,” akacheka tena. Bila kusubiri jibu la Kitenge, aliongeza, “Ndiyo nimekuja kukusifu, kwani hukumbuki kuwa mimi ni mpenzi wako? Hukumbuki kuwa uliniahidi kuwa bila mimi usingeishi? Kwamba lazima tungeoana tu. Hukumbuki?”

Kitenge aliduwaa, hakujua mwanamke huyu anaelekea wapi katika maongezi hayo. Hivyo akaamua kunyamaza akimtazama.

Baada ya kicheko kingine Machozi aliongeza, “Nimekuja mpenzi, nimekuja kukukumbusha ahadi hiyo, kama umesahau. Nyumba yako hii nimeitafuta mwaka mzima, leo ndiyo nimeipata. Nimefika nyumbani, kwa hiyo wewe nenda zako kazini utanikuta mkeo nimekuandalia kila kitu. Au ulianza kusahau mapenzi yetu hadi ukaoa mke mwingine?”

Bado Kitenge aliamini Machozi alikuwa akimkebehi, hakuwa amesema alilokusudia. Hata hivyo tayari alianza kupandwa na hasira, huku akiificha hasira hiyo katika sauti yake alisema, “Sikia Machozi, mimi sina muda wa kupoteza. Kama umechanganyikiwa nenda mahala ukazungumze yote unayotaka kuzungumza. Hapa sipo kabisa. Sasa inuka utoke zako.”

“Kweli mpenzi tuseme umesahau ahadi zako zote?”

“Toka…”

“…. umesahau barua zako tamu…”

“…uende zako haraka!”

“….zenye kila neno la mapenzi na ahadi za kuishi pamoja?”

“Nasema toka!”

“Pamoja na jinsi nilivyokupenda nikajitoa kwako mwili na roho? Umesahau kweli mara hii? Siamini!”

Ana wazimu mwanamke huyu? Kitenge alijiuliza. Mapenzi!
Mapenzi gani hayo ambayo hakumbuki? Kwa kadri ya kumbukumbu zake, neno ‘nakupenda’ wakati huo lilikuwa moja ya michezo ya kawaida mongoni mwa watoto. Angeweza kumwambia yeyote wakati wowote ‘wewe ni wangu wa heri na shari,’ kadhalika angeweza kusikiliza jibu lolote la msichana yeyote na kumwamini.

Halikuwa jambo la ajabu mtu kumwambia mtu ‘nikila sishibi kwa ajili yako’ au ‘usiku silali’. Karibu kila mvulana alikuwa na faili kubwa la barua za mapenzi. Barua hizo zilikuwa zikiandikwa kwa ufundi au kunakiliwa kutoka vitabuni huku zikiwa zimenakshiwa kwa maua ya kuvutia pamoja na kupambwa kwa harufu ya poda. Machozi alikuwa na akili gani hadi leo hii kuendelea kuamini mambo kama hayo?

Mchezo wa mapenzi, vichakani na hata nyumbani ni jambo lililokuwa la kawaida pia. Ingawa Kitenge hakuwa mpenzi sana wa mchezo huo, lakini Machozi alikuwa mmoja tu katika orodha ndefu ya wasichana aliowahi kufanya nao mapenzi.

Yalitokea, yakatoweka. Yeye Kitenge baada ya kufaulu darasa la saba, akiwa mtoto pekee aliyetoka katika kijiji hicho cha Mayange, wilayani Kasulu, alijibidiisha zaidi katika masomo yake. Kila aliporudi likizo wasichana wote walimlaki kwa furaha na kuridhia lolote alilotaka; Machozi akiwa mmojawao.

Alipohitimu kidato cha sita na kupata kazi hapa Dar es Salaam, alikata mguu kijijini hapo. Hakuwa na muda wa kutosha kumfikisha huko mara kwa mara kutokana na shida ya usafiri. Huu ulikuwa mwaka wake wa sita tangu alipofika huko kwa mara ya mwisho. Likizo ya mwaka huu alikuwa akijiandaa au kutarajia kuwa angeenda. Katika mapya na mageni yote aliyotarajia kuyakuta huko nyumbani, hili hakulitarajia kabisa.

“Unatoka katika nyumba hii au hutoki?” aliuliza ghafla.

Machozi hakumjibu haraka. Alitazama huku na huko kisha akasema, “Nikisema sitoki nadhani utaniitia mgambo. Vizuri sana. Sasa nitasema dhamira ya safari yangu hii; ilikuwa ni kukupa hongera, ndiyo, lakini si hongera ya mafanikio ya kuandika kwako vitabu. Ni hongera kwa kufanikiwa kwako kuniharibia maisha yangu. Kwa kunidanganya hata nikadanganyika na kuamini kuwa ulikuwa wanipenda kumbe la. Haukuishia hapo, ukanijaza mimba na kisha ukaikana. Hongera sana Boni.”

Ndipo Kitenge alipokumbuka kuwa aliwahi kupata barua moja kutoka kwa baba au mmoja wa wadogo zake ambaye alidai kuwa amemtia mimba msichana mmoja. Ati aende akamuoe! Wakati huo, Kitenge alikuwa ndiyo kwanza anaanza kazi. Wazo la kuoa, na hasa kumuoa mtu kama huyo, lilikuwa nje ya ratiba yake a maisha. Hivyo suala hilo alilipuuza. Hakumbuki kuwa aliwahi kujibu barua hiyo. Kumbe ilikuwa kweli? Yaweza kuwa kweli? Alijiuliza.

“Nikikuruhusu kusema utaanza kuikana mimba hiyo. Waweza hata kudai kuwa hukuwahi kufanya nami mapenzi japo ni wewe uliyeniharibia ubikira. Napenda kukufahamisha kuwa mwanao alikuwa msichana. Nilimtupa katika mapipa ya takataka za hospitali ya Maweni. Kama walimwokota akiwa hai au maiti, sijui. Sikujali. Najua na wewe hujali wala usingejali.” Machozi akanyamaza akimtazama Kitenge kuona hadithi yake ilimwingia vyema.

Alipomwona akitoa macho ya mshangao aliongeza: “Usiseme unasikitika, najua una moyo wa jiwe kama mimi. Ingawa mimi sikuzaliwa na moyo huo, nimeupata ukubwani kwa haki kabisa ingawa nikiiambia hivyo jamii haitanielewa.”

Akasita kidogo na kuendelea, “Ninachotaka kueleza ni taabu niliyoipitia baada ya kumtupa mtoto huyo. Njaa ilinifanya niangukie mikononi mwa mwanamume mwingine. Huyu, tangu awali nilijua ananilaghai, lakini sikuwa na njia ya kumzuia asinitie mimba nyingine. Alipogundua nina mimba aliniepuka, ikabidi niteseke sana kutunza mimba hiyo bila mafanikio. Mwisho, niliamua kumeza dawa za kuitoa. Ilitoka kwa taabu, nami niliponea chupuchupu. Nilipopata nafuu zawadi yangu ilikuwa kifungo cha miaka mitatu.

“Majuzi tu ndiyo nimetoka jela. Maisha yangu yamekuwa mpira usio na thamani. Unaochezwa na kila mwanaume atakaye. Nadhalilishwa, naonewa na kufanywa kiumbe duni asiye na haki ya kuwa hai. Yote hayo ni kwa ajili yako Boni. Ni wewe uliyenivuta katika mkondo huu ukahakikisha siwezi kutoka.”

“Mimi!” Kitenge aliropoka akiwa hajui la kufanya.

“Wewe!” Machozi alijibu. Sauti yake haikuwa ya kebehi tena, wala haikujali kuweka furaha ya kinafiki. Ilikuwa wazi ikitangaza kulipiza kisasi na uadui.

“Wewe!” aliongeza, “Na nilichokuja kukuambia si kukuomba unioe au unipe pesa za kutumia, la. Nimekuja kukuambia kuwa nakuchukia. Ninakuchukia kama ninavyomchukia shetani. Sasa hivi, mimi ni kama maiti ambaye hajaanza kunuka tu. Sina mbele wala nyuma. Lakini kabla sijaoza nitahakikisha na wewe unalipa gharama za madhambi yako. Lazima twende wote ahera Mungu akatuamulie nani mwenye haki. Nitakuua Boni. Tena kwa mkono wangu huu!” Aliutikisa mkono huo huku akiinuka na kuanza kutoka.

Mlangoni aligeuka na kuanza kumtazama Kitenge. “Kwa heri,” alisema, Tutakapoonana tena, ujue ndiyo mwisho wa uhai wako.” Akatoka na kutoweka.
Kitenge alibaki akiduwaa juu ya kiti chake. Aliyemzindua ni mama mwenye nyumba, kikongwe ambaye huwa hapitwi na neno lolote humo au nyumba za jirani. Alibisha hodi na kusimama mlangoni.

“Baba, mwanamke huyo ni nani?” aliuliza.

“Simfahamu. Nadhani ni mwendawazimu,” Kitenge alilaghai akiinuka na kuelekea bafuni.
“Anasema anakufahamu…. jihadhari baba,” sauti ya Bi mkubwa huyo ilimfuata.

Hakujishughulisha kumjibu.


ASUBUHI hiyo, Kitenge alikuwa mtu wa kwanza kuwasili ofisini. Milango yote ilikuwa imefungwa. Akatumia funguo zake za akiba kufungua na kuingia hadi katika ofisi yake. Alikuwa na maandishi yaliyochorwa kisanii kabisa, juu ya kipande cha ubao kilichowekwa juu ya meza yake yaliyosema, KONDOKONDO KITENGE, MANAGING DIRECTOR-BLACK POWER PUBLISHERS. Zamani maandishi haya yalikuwa yakimvutia sana na aliyatazama mara kwa mara. Si sasa ambapo aliweza kushinda ofisini humo macho yake yalitazama na kuona kila kitu isipokuwa maandishi hayo.

Hii ilikuwa ofisi yake. Ofisi ya kampuni ambayo alikuwa ameianzisha miaka miwili iliyopita, kushughulikia vitabu vyake na vya wandishi wengine ambavyo vilionekana vyafaa. Wazo la kuanzisha kampuni hii lilikuwa limemjia baada ya kuona alivyowatajirisha wachapishaji wake wa awali, huku yeye akimegewa kidogo kutoka katika faida hiyo kubwa, wakati huohuo wakichelewesha uchapishaji wa vitabu vyake bila sababu ya kuridhisha.

Kitabu chake cha kwanza ambacho alikiandika akiwa shuleni kilikuwa kimesubiri miaka minne ndipo kikatolewa. Cha pili kiliwahi sana, miaka miwili! Tangu alipoanzisha kampuni hii mambo yalianza kumwendea vyema, ingawa yapo matatizo kadhaa yaliyomkwamisha hapa na pale. Alifurahi kupambana nayo mwenyewe badala ya mtu mwingine kumpigania.

Tatizo kubwa ambalo lilimtisha ni lile la kuona kama aliyeelekea kuishiwa na ule uwezo wake wa uandishi. Tangu alipobeba mzigo huo wa Ukurugenzi Utendaji, mtiririko wa mawazo yake ulipungua kasi. Na alipojikongoja hadi kumaliza kitabu washauri wake walidai kuwa hakifai kutolewa. Kwamba kingemvunjia hadhi yake. Ati mambo mengi yalikuwa marudio ya vitabu vya waandishi wengine, hasa wa magharibi.

Jambo hilo lilimtia hofu sana, kuona akielekea katika hatari ya kuishia vitabu vitatu tu ilhali alidhamiria kutoa vitabu vingi kama kina James Hadley Chase, Shabani Robert, Ngugi wa Thiong’o na wengi wengine. Aibu ilioje! Mara kadhaa alijiuliza kama alitumia busara kuamua kuwa mchapishaji badala ya kuacha wachapishaji wake waendelee kushughulikia miswada yake, yeye akishughulikia mawazo mapya.

Akiwaza hayo Kitenge alikuwa ameketi juu ya kiti chake, hafahamu wala hajaamua lipi aanze katika shughuli nyingi alizoacha jana. Kulikuwa na mengi ya kufanya. Kuna ule muswada wa kusoma, miswada miwili ya kusahihisha lugha, mmoja wa kumrudishia mtunzi afanye marekebisho, madai ya fedha katika maduka ya vitabu, kuwasukuma wachapaji waliokwamisha vitabu viwili vya hadithi za watoto na kadhalika. Mengi. Hakujua lipi aanze kushughulikia na lipi liahirishwe tena.

Mara, mawazo yake yakaikumbuka tena ziara ya alfajiri ya yule mwanamke, Machozi. Ana nini? Wazimu au upungufu wa akili? Madai yake yana ukweli kiasi gani? Na hata kama yana ukweli wowote, si yamhitaji mtu mwendawazimu sana kuyafuatilia madai ya aina hiyo! Ati ulinitia mimba miaka mingapi iliyopita, kwa hiyo tangu leo mimi mkeo! Ati nitakuua kwa kuwa ni wewe uliyeniharibia maisha yangu!

Wazimu ulioje! Kitenge akaangua kicheko. Hakujua kama alikuwa akimcheka Machozi alivyochakaa au madai yake yasiyokubalika.


KAMA kawaida Rusia alikuwa katika moja ya mavazi yake ya thamani zaidi ya mshahara wake, nywele kazitia mafuta au madawa yaliyozifanya zifanane na za Kizungu, kama si chotara. Ni sura yake tu ambayo Kitenge aliona hairidhishi. Hakumbuki kwa nini alimwajiri mtu mwenye sura kama hiyo kuwa karani wake mahususi. Kilichomshangaza ni wale watu wakubwa ambao huja mara kwa mara na magari yao kumchukua msichana huyu kwa chakula cha mchana.

Hakujua nini wanaona cha haja katika sura hii. Hawaioni kasoro yoyote? Wakati mwingine alijiona pengine ni yeye mwenye kasoro. Kwani hajawahi kumpenda msichana yeyote kwa dhati. Wote aliotembea nao, na anaotamani kutembea nao, huwatoa kasoro kemkem. Jambo ambalo limemfanya hadi leo hii kutokuwa na mke.

“Naona unaendelea kucheka, vipi? Au tayari umepata hadithi mpya kichwani? Najua wewe huridhishwi na chochote zaidi ya hadithi,” Rusia aliendelea.

Mara wazo likamwingia Kitenge; kweli! Tukio la leo asubuhi baina yake na Machozi ni hadithi nzuri sana! Hadithi ya mapenzi! Mapenzi ambayo yatageuka kuwa chuki. Hata jina la riwaya sasa lilielea kichwani mwake. Ataiita MAPENZI HUCHUJA. Naam, itakuwa hadithi nzuri. Mwisho? Akajiuliza. Uweje mwisho wake? Machozi alipendekeza mauaji, yeye ataangalia mwisho wa kuridhisha. Akacheka tena.

Safari hii kicheko kilimtia Rusia mashaka. “Mwenzangu! Nadhani tumwite daktari. Tangu nilipoingia husemi lolote, hufanyi lolote zaidi ya kucheka. Sema tumwite kama unaona mambo si ya kawaida,” alisisitiza bila mzaha wowote.

“Usiwe juha we mwanamke,” Kitenge alimjibu akiukunja uso wake. “Siku nikianza wazimu itakuwa ni kwa hasira si furaha. Na katika ofisi hii hatatoka mtu. Nitavunjavunja kila kitu na kila mtu, huyo daktari atakayenisogelea ataadhirika.”

Wote wakacheka.

“Basi tuombe Mungu isitokee.”

“Wala haitokei. Hata shetani ni mwoga, anaangalia wapi aelekeze pepo wake mchafu.”

Baada ya maongezi hayo walizama katika shughuli zao. Kitenge alikuwa hajafanya lolote mhudumu alipomtaka radhi ili afagie. Akaamua kutoka nje kabisa. Ofisi yao ambayo ilikuwa katika Mtaa wa Samora, haikuwa mbali sana na Hoteli ya Salamander. Kitenge alivuka huku akiendelea kuitayarisha hadithi yake mpya kichwani. Akataka kuiandika mara moja, lakini roho nyingine ikamzuia na kumshauri aitafiti vyema na kuipamba kabla hajaitia katika maandishi.
Aliporejea ofisini, Rusia alimtambulisha kwa mgeni ambaye hakuwa mgeni sana machoni mwa Kitenge.
“Bwana Bazile Ramadhani, mwenye ule muswada ambao bado tunautafuta. Nimemwambia aje kesho, lakini mwenyewe anadai anataka kuzungumza na wewe.”

Kitenge akaukumbuka muswada huo, ulikuwa mmoja kati ya ile miswada ambayo huwezi kuitilia maanani. Ulikusudiwa kuwa hadithi ya upelelezi, lakini ilivyoandikwa si hadithi ya upelelezi, isipokuwa mtiririko wa mauaji ya kikatili yanayotokea bila sababu za kuridhisha. Muswada huo ulimfanya Kitenge kumfikiria mwandishi kama mtu mwenye hasira dhidi ya ulimwengu wote, mtu atakayefurahi sana endapo lolote lingetukia kuharibvu dunia na vyote vilivyomo.

Ni kama mtu ambaye alidhani au kuamini maisha yanamwonea na binadamu wote wanamchukia, hivyo akaondokea kumchukia kila mtu ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe. Kwa kuwa hana silaha wala uwezo wa kuiangamiza dunia, ndipo akaandika kitabu hicho ambacho binadamu wanateketezwa ovyo na mhusika wake mkuu kujiua mwishoni. Sababu ya vifo vyao haionekani, sababu ya kujiua kwake haikutajwa. Nje ya hayo, muswada huo uliandikwa kwa mtindo usioleweka na lugha isiyotamanika. Kitenge hakumbuki alivyofaulu kuusoma mpaka mwisho.

Kitenge akamgeukia mwandishi huyo na kumtazama. Naam, uso wake ulidhihirisha yote, macho yake yalisema kila kitu. Ni mtu aliyetaabika akakata tamaa. Tazama uso ulivyojikunja! Tazama macho yanavyotangaza uadui! Tazama tabasamu lake lilivyoficha chuki! Kitenge akajikuta akimwogopa.

“Ndivyo, bwana Ramadhani,” alisema kwa jitihada. “Muswada wako kama alivyokwambia dada huyu, haujafikia kiwango. Unahitaji marekebisho mengi. Kwa kuwa hapa tunayo miswada mingi mno si rahisi kufahamu wapi uliwekwa. Pengine tumeutuma kwa wasomaji wa nje. Mpe muda aendelee kuutafuta.”

“Sina muda zaidi bwana Kitenge,” sauti yake ilikuwa na hasira kama macho yake. “Hujui taabu kiasi gani nilipata hata kuukamilisha. Bado huo ni wa nne, yote imo mikononi mwa wachapishaji. Na jibu ni hilohilo, ‘ngoja.’ Tafadhali leo hii nitoke na muswada wangu. Jana nilipiga simu nikiwaambia niukute, leo mnasema kesho. Nisipoupata leo kwa kweli utajilaumu Kitenge.”

Kitenge na Rusia wakatazamana. “Ya nini maneno yote hayo?” alihoji Kitenge baada ya kucheka kidogo. “Unadhani tuna haja gani ya kukaa na muswada wa aina ile? Mara tu utakapopatikana utapewa.”

“Nitapewa?” Ramadahani alidakia akiinuka, Kitenge akashangaa kuona alivyo mrefu mwenye mwili mkubwa. Fedha au chakula zaidi kingeweza kumfanya awe pande la mwanamume zaidi ya alivyokuwa.

“Nitapewa!” alinguruma tena. “Wadhani sifahamu kitu gani kinatokea? Usijidanganye bwana Kitenge, nafahamu vizuri sana kuwa muswada huo umeubadili jina na kufanya umeutunga wewe. Najua kuwa sasa hivi, uko KIUTA ambako unachapwa.”

“Nini?” Kitenge aliuliza kwa mshangao akimgeukia Rusia. Wakaangua kicheko.

“Chekeni, ndiyo. Lakini kaeni mkijua kuwa hicho ni kicheko chenu cha mwisho pamoja. Nisipoupata muswada wangu kesho nitahakikisha mmoja wenu anachekea kuzimu, naapa!” Akamgeukia Rusia na kuongeza, “Nakupa hadi saa nane niwe nimeupata, vinginevyo mtajilaumu.” Akageuka na kuanza kuondoka.

Kitenge akamwahi kumshika mkono, “Ngoja bwana Rama,” alimweleza, “Hivi unafahamu usemalo?”

“Nafahamu.”

“Kwamba nimeubadili muswada wako uonekane kuwa nimeutunga mimi?”

“Ndiyo.”

“Ni nani huyo aliyekupa wazo la kipumbavu kama hilo?”

Ramadhani hakujibu. Si kwamba hakutaka kujibu bali hakuwa na jibu halisi. Alijua na kuamini kuwa Kitenge aliubadili muswada huo. Alikuwa na hakika, hakika ambayo ilimtatanisha yeye binafsi kila alipojiuliza ni wapi alikoipata. Anachokumbuka vyema ni kitu kama maongezi ambayo aliyasikia baina ya watu wawili wafanyao kazi KIUTA wakisema wameletewa muswada wa mtu anayeitwa Bazile Ramadhani watayarishe na kubadili jina la mtunzi kuwa Kitenge.

Watu hao walisema kuwa muswada huo utamtajirisha sana Kitenge. Kwamba kama wangekuwa wao, wangeamua kuua kuliko kuacha Kitenge asifike na kujitajirisha kwa jasho lao. Ramadhani hakumbuki pia kama aliwajibu chochote watu hao, anachokumbuka vyema ni nadhiri aliyoweka ya kujiua au kumuua Kitenge endapo muswada huo usingepatikana. Hilo alilidhamiria akizingatia taabu alizokwishazipata katika harakati zake za uandishi wa vitabu.

Kama utunzi huwaletea watu wengine faraja, yeye ulimzalia simanzi. Kama wengine huwapa utajiri, kwake ulimfanya fukara zaidi. Alikuwa ameanza kutunga tangu akiwa shuleni, muda wake wote wa mapumziko aliutumia kuandika. Senti zake zote za matumizi ziliishia kununua kalamu, karatasi na stempu za kusafirishia. Akawa hana rafiki.

Wenzake wote walimdharau wakimwita mwendawazimu. La kusikitisha zaidi ni jinsi miswada yake ilivyorudishwa na wachapishaji wakidai ‘haieleweki’ wala hana ‘fununu’ juu ya mtunzi. Hakukata tamaa. Alipokuwa sekondari vitabu vilianza kutoa ‘picha’ ya kutamanika. Wachapishaji walianza kumtia moyo kwa kumwelekeza hapa na pale. Halafu miswada ikaanza kupotea. Kila alipotuma haukurudi. Barua za madai hazikusaidia. Ofisi za wachapishaji wengine hata hazikujulikana kama kweli zipo, alizitafuta bila mafanikio. Miswada mingi ikatoweka!

Huu aliompa Kitenge ulikuwa wa nne kati ya zile zilizokuwa mikononi mwa wachapishaji. Aliupenda na kuuthamini kuliko yote. Hakudiriki kuutuma kwa posta, bali aliupeleka kwa mkono baada ya kuitafuta ofisi hii kwa siku kadhaa. Matumaini yalikuwa yamezidi baada ya kumwona Kitenge, mtunzi mashuhuri, akitabasamu baada ya kusoma sehemu kadhaa siku ile alipouleta. Leo aambiwe hauonekani, wakati ana uhakika uko mitamboni! La asingevumilia, lazima huu uwe ama mwanzo wa faraja zake ama mwisho wa mateso yake!

“Nani alinipa wazo hilo?” alijibu Kitenge kwa swali jingine. “Sina haja ya kumtaja,” akalaghai. “Ninalokutaka uelewe ni kuwa njama zako ziko hadharni. Ukiendelea nazo utapoteza bure maisha yako. Saa nane nitarudi hapa. Tafadhali nikute muswada wangu, vinginevyo, kichwa chako halali yangu.”

Akatoka na kuufunga mlango kwa nguvu.

Rusia akajaribu kucheka kicheko ambacho alikikatiza ghafla baada ya kuhisi kuwa hakikuwa na ladha yoyote ya kicheko. Kadhalika macho ya Kitenge ambayo yalimtazama kwa namna ambayo hakupata kuiona huko mbeleni, ilikuwa sababu nyingine iliyomkatisha kicheko hicho.

“Usijali bosi, ana wazimu…”

“Labda,” Kitenge alidakia, “Suala ni watu wangapi wenye wazimu watakaonisumbua asubuhi ya leo? Nisipoangalia wataniambukiza wazimu wao.” Alipoona Rusia akipanua mdomo kuuliza swali, aliongeza harakaharaka, “Hatuhitaji watu wenye wazimu katika ofisi hii. Jitahidi kutafuta muswada wake umpatie. Usisahau kumwonya asilete kazi yake nyingine hapa.”

Baada ya maneno hayo alitoka nje.


HUKO nje Kitenge hakujua aende wapi. Moyo haukumpa kwenda kokote. Kurudi ofisini roho ilikataa vilevile. Kwa muda aliduwaa hapo nje ya ofisi yake akitazama pande zote. Mara, akajikuta akiifuata miguu ambayo ilianza safari bila idhini yake. Ilimwongoza hadi Coffee Bar, chini ya Telephone House.

Hapo aliwakuta baadhi ya rafiki zake ambao walimkaribisha kwa kahawa ambayo aliinywa japo hakushiriki katika maongezi. Baada ya kitambo, alijikuta kabaki peke yake. Miguu ikamchukua tena hadi British Library ambamo alishika kitabu hiki na kile na kukodolea macho maandishi, lakini akiwa haoni chochote.

Mawazo yake yalikuwa yakitatanishwa na siku kama ya leo kwake. Wazimu? Alikuwa akijiuliza. Ramadhani pia ana wazimu? Na vipi kisa chake, si kinatosha kuwa hadithi nzuri? Hadithi ya mtunzi aliyechanganyikiwa, ambaye baada ya kushindwa kuitumia vyema kalamu yake anatumia ulimi wake kwa vitisho. Naam, ni hdithi nzuri. Ataiunganisha na tukio la Machozi. Atawafanya wote wahusika wakuu. Mwisho wa hadithi? Swali hilo alilipuuza tena. Atapata mwisho wa kuridhisha baada ya hadithi kuanza.

Mara akasikia furaha ikimjia tele moyoni. Pengine alicheka kwa nguvu, kwani aliwaona watu kadhaa waliokuwa wakisoma kimya wakiinua macho kumtazama. Akatua mezani kitabu alichokuwa nacho mkononi na kutoka nje.

Akaifuata tena Barabara ya Samora hadi alipoifikia sanamu ya askari. Hapo alielekea baharini akiiendea hoteli ya New Africa. Hotelini hapo alipata kiti katika meza iliyokuwa imekaliwa na Wazungu watatu, mmoja akiwa mwanamke. Akaagiza bia nne aina ya Safari, akiwakaribisha wale Wazungu. Walipokataa alizinywa zote moja baada ya nyingine. Baada ya hizo aliagiza whisky. Jinsi alivyokunywa harakaharaka, haukupita muda akawa hajiwezi.

Mmoja kati ya Wazungu hao akamwinamia na kumnong’oneza: “Excuse me sir, i think you have taken too much. Can’t you switch off and go back home?”
Kitenge alimkosa kofi hafifu huku akisema, “Go to hell.”

Wazungu hao wakaondoka na kuhamia meza nyingine. Aliendelea kunywa. Kisha usingizi ukamchukua, akainamia meza na kujilaza kwa starehe.

Alipoinuka alijikongoja kuendea teksi. Dereva akamsaidia kuingia baada ya kuuliza anakoishi. Kitenge aliitazama kwa taabu saa yake ambayo ilisema ni saa mbili za usiku kasoro dakika kadhaa. “Magomeni Mapipa Mtaa wa Kiyumba namba kumi na mbili,” alijibu kilevi huku akilala tena.

Kilichomzindua tena ni dereva ambaye alimsukasuka kumwamsha. Walikuwa wamewasili. Akajikongoja kuingia ndani, nusura amgonge mama mwenye nyumba ambaye alikuwa kasimama mlangoni akimtazama kwa mshangao kwani alikuwa hajawahi kumwona Kitenge akilewa kiasi hicho. Kitenge alifungua mlango kwa shida, alipoingia hadi chumbani hakujishughulisha kuwasha taa wala kuvua viatu. Alijibwaga kitandani na kuanza kukoroma.

Ilikuwa usiku wa manane alipokurupuka ghafla kwa maumivu makali ambayo yalipenya kifuani mwake. Mkono wenye nguvu ulimkandamiza asiweze kuinuka kutoka kitandani hapo. Mkono wa pili ulimziba mdomo hata akashindwa kutoa sauti. Pigo la pili lilipenya hadi moyoni, Kitenge akahisi maumivu yakipungua na badala yake akimezwa na usingizi mzito wenye kiza cha kutisha. Usingizi ambao ulimfanya asisikie chochote kisu kilipopenya kwa mara ya tatu katika kifua chake.


“SEMA kama mwanamume, sajini Abdala!” InspeKta Kombora alifoka, macho kayatoa. “Zungumza lugha ya kiaskari; amekufa au ameuawa?”

“Ameuawa afande,”Abdalla alisema akitua faili lililokuwa kwapani mwake. “Taarifa kamili ya kifo na mauaji yake utaipata katika faili hilo.”

Kombora alipokea faili na kulitupia jicho la haraka haraka. Kisha alitazama saa yake ambayo mshale wa dakika ulikuwa juu ya kumi na mbili, wa saa ukiwa juu ya nane. Ghafla, aliinua uso wake na kumtazama sajini Abdala. Macho yake yalitulia kwa muda juu ya uso huo wenye macho maangavu, yakateleza hadi juu ya kifua chake kipana na kiwiliwili kirefu ambacho kilitoa picha ya ukakamavu.

Ingawa alimtazama kijana huyo ni macho tu yalikuwa yakimwona. Kifikra alikuwa mbali akifikiria kifo hiki na kujaribu kulinganisha na simu ile aliyoipokea jana kutoka kwa mtu asiyejulikana. Mtu ambaye alidai anajisikia kuua mtu. Sauti hiyo ikiwa haina chembe yoyote ya mzaha ilikuwa imemfanya Kombora ashinde kutwa nzima ya jana akiwa na hofu ya kupokea habari mbaya.

Usiku ulipoingia hofu hiyo ilimzidi, kwani mara nyingi ni usiku ambapo waovu hutenda maovu yao. Hakupata usingizi kikamilifu, kila dakika alitegemea simu ambayo ingemfahamisha maafa. Hivyo kulipopambazuka bila habari hiyo kumfikia, alianza kufarijika akidhani kuwa pengine aliipa uzito usiostahili ile sauti; yawezekana ni mlevi au mpungufu wa akili na hata mtu mzima kabisa ambaye alikuwa na muda wa kuchezea akaamua kuutumia kwa kuwasisimua polisi, lakini mawazo hayo yalimtoka Kombora mara alipopokea simu ya kumjulisha kifo hicho alipokuwa akijiandaa kuja kazini.

“Nani aliyeuawa?” alinguruma katika chombo cha simu.

“Kitenge.”

“Kitenge! Tuna vitenge madukani sajini?”

“Kondokondo Kitenge afande. Yule mtunzi mashuhuri wa hadithi za ujambazi na upelelezi.”

“Alaa!”

Alifahamishwa kwa ufupi maafa hayo yalivyotokea. Ndipo akaharakisha kuja ofisini ambako alikabidhiwa faili la mkasa huo ambalo bado alikuwa kaduwaa nalo kabla hajaanza kulisoma.

“Ungelisoma haraka mzee,” sajini Abdalla alimzindua, “Kuna mengi ambayo hayajaanza kutekelezwa, yanayoisubiri idhini yako. Kwa maoni yangu, muuaji hayuko mbali, tutamtia mikononi mara moja.”

Kombora akayateremsha macho yake mezani na kuanza kupekua faili hilo. Hakujishughulisha kuipokea saluti ya Abdala, alipokuwa akiondoka. Badala yake, kama kwa kumtupia aliongeza, “Usiende mbali. Nitakuona mara baada ya hii,” alisema.

Aliisoma kwa makini. Hakukuwa na mengi zaidi ya aliyokwisha simuliwa. Marehemu alikuwa ameuawa kwa kisu baina ya saa nne na saa nane usiku. Maiti yake ilikutwa chali juu ya kitanda. Kwa mujibu wa daktari, marehemu alikuwa amelewa sana kabla ya kufa, hivyo hakufanya vurugu yoyote kabla ya kukata roho.

Ripoti ya wataalamu wa vidole inadai haimo alama yoyote ya vidole zaidi ya zile za marehemu mwenyewe. Jambo ambalo linaonyesha kuwa muuaji au wauaji walivaa glovu maalumu kwenye mikono yao kabla ya kugusa kitu chochote humo ndani. Silaha iliyotumiwa haikuonekana. Taarifa iliongeza kwamba, aliyearifu polisi ni mmoja wa wapangaji ambaye aliarifiwa na bi kizee mwenye nyumba aliyeigundua maiti alfajiri.

Kilichomsisimua Kombora katika ripoti hiyo ni madai ya bi kizee huyo kwa makachero kwamba anamfahamu muuaji, ati ni mwanamke ambaye alidai kwa sauti na kuapa kuwa angemuua Kitenge. Hilo Kombora hakulitegemea.

Kwanza hakutegemea ufumbuzi uje kwa urahisi namna hiyo; pili hakudhani kuwa muuaji angetukia kuwa mwanamke. Sauti iliyompigia simu ilikuwa ya kiume. Aliamini kuwa ni mwenye sauti hiyo ambaye alielekea kuwa muuaji. Hivyo aliinua simu yake na kumtaka opereta amwitie sajini Abdala.

“Afande.”

“Sajini. Unaonaje kesi hii, waweza kuyaamini maneno ya huyu mama?”

“Hadi dakika tano zilizopita nilikuwa nikiyaamini afande…”

“Sikia Abdala,” Kombora akamkatiza kwa ukali, “Hatuna muda wala nafasi ya kuzungumza kwa mafumbo. Katika ripoti yako mwenyewe unadai kuwa silaha ya mauaji haikupatikana. Hilo peke yake linatosha kukufahamisha kuwa muuaji bado ana nia au uwezo wa kufanya unyama mwingine kwa silaha ileile au nyingine, wakati wowote. Hatutaki jambo hili litokee. Sasa, haya mambo ya kuamini ripoti yako mwenyewe dakika tano zilizopita yanaingiaje katika swali langu?”
Sajini Abdala, akiwa mtu anayemfahamu vyema ofisa wake, hasa katika masuala ya aina hii, kuwa hapendi mzaha wala maneno mengi, alitabasamu kwa uficho, kisha akamjibu mara moja.

“Nilichotaka kusema ni hivi afande, taarifa hiyo ya mama mwenye nyumba alinipa mimi mwenyewe asubuhi ya leo. Alikuwa na hakika na kile anachosema. Nikaelekea kumwamini, hasa baada ya kusema kuwa mama huyo anayeshukiwa anayo kila dalili ya ulevi wa gongo na bangi. Mlevi wa vitu hivyo anaweza kufanya lolote afande, hasa anapoondokea kuamini kuwa ni wewe uliyemfanya yeye aishie kuwa mlevi hali wewe unainuka kimaisha.”

“Sawa,” Kombora alijibu. “Na baada ya dakika hizo tano?”

“Baada ya dakika tano, siyo kwamba simwamini kabisa, ila nimechanganyikiwa tu. Nilikuwa nikipiga simu katika ofisi ya marehemu kuwafahamisha maafa haya. Katibu wake mahsusi akaropoka kuwa, alitegemea jambo hilo. Nilipomuuliza kwa vipi, akaniambia kuwa anamfahamu hata muuaji kwa jina na sura. Nilipomuuliza kama mtu huyo ni mwanamke, alikanusha na kudai kuwa ni mwanamume, mtunzi wa vitabu. Kwamba mtu huyo alifika ofisini hapo na kuahidi kumuua Kitenge. Unaona ilivyo vigumu mzee? Wauaji wawili, marehemu mmoja! Kila shahidi ana imani na ushahidi wake.”

“Kweli inatatiza,” lilikuwa jibu la Kombora baada ya kuwaza sana. Kisha akaongeza, “Nitapenda kuonana na hawa mashahidi mara moja. Andaa gari twende kwanza huko nyumbani kwake halafu tutamwona huyo karani wake ofisini.”

“Timamu afande.”

Dakika chache baadaye walikuwa ndani ya Land Rover wakielekea Magomeni Mapipa. Walipoufikia Mtaa wa Kiyungi hawakuhangaika kuipata nyumba waliyoihitaji. Nje kulikuwa na watu wengi waliozungumza hili na lile.

Kombora na Abdala waliupenya umati huo kwa urahisi, kwani watu wenyewe walijitenga kuwapisha. Ndani walikuta umati mwingine ambao ulimzunguka mama mwenye nyumba aliyekuwa akiendelea kueleza kwa sauti yenye shauku kubwa. Kombora aliwataka radhi majirani hao na kumchukua mama katika chumba cha marehemu.

“Sijisikii kabisa kuingia chumba hiki baba, kinatisha,” alisema bibi huyo huku akiingia.

“Usijali mama. Hamna litakalotokea,” Kombora alijibu bila kumtazama. Macho yake yalikuwa yakitazama kila upande. Kama ilivyosema taarifa, haikuonekana dalili yoyote ya kuashiria mauaji katika chumba hicho. Kila kitu kilikuwa katika hali inayostahili. Ni shuka moja tu yenye damu iliyosaliti siri hiyo. Shuka nyingine bila shaka zilikuwa zimechukuliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi. Kisha Kombora aliyarejesha macho yake kumtazama kizee ambaye alikuwa akisema.

“Wamekuja hapa wenzako baba. Wanauliza mengi ambayo hayana maana. Muuaji najua ni yule mwanamke tu. Sauti yake inaonyesha wazi alikuwa akisema kweli. Kama angekuwa mwingine, lazima angeiba kitu chochote humu ndani. Yule hakuwa na nia ya chochote bali kumuua tu.”

“Kweli mama,” alijibu Kombora. “Unaweza kumfahamu iwapo utamwona tena?”

“Bila shaka. Hata wewe baba, ukimwona japo hujawahi kumwona utamjua tu. Ana sura ya kutisha sana.”

“Unadhani tunaweza kumpata wapi bibi?” aliongeza Abdala.

“Mjukuu wangu, usiniambie hujui wanakopatikana walevi wa gongo. Darisalama hii ni kubwa, ndiyo, lakini nyie mnajua wapi na wapi mnaweza kumpata mwanamke yule.”

Kombora alitabasamu kwa haya kidogo kabla hajajibu, “Kweli mama, tutampata hivi karibuni. Unasema ulisikia marehemu akimwita Machozi sio?”

“Ndiyo baba, nitafurahi mkimkamata. Aweza kuua tena yule.”

“Tutamkamata bibi.”

Yakafuata maswali mengine ya kawaida. Ilimshangaza Kombora kuona bibi huyo alivyokuwa hodari wa kujibu maswali ambayo yangeweza kuwatatanisha wasomi na vijana. Walipotosheka walimshukuru na kumuaga. Wakatia moto gari na kurudi mjini.


OFISI ya BLACK POWER PUBLISHERS ilikuwa kimya kupindukia Kombora na Abdala walipoingia. Waliwakuta vijana wawili wa kiume wameinamia meza zao, na msichana ambaye mikono yake ililalia mashine ya chapa. Kombora aliyaona machozi yakimlengalenga msichana huyo pindi alipoinua uso kumtazama.
“Karibuni,” mmoja kati ya vijana wale alitamka polepole.

“Asante,” maofisa hao walijibu wakijiketisha juu ya viti vilivyokuwa wazi.

Yalifuata maongezi mafupi, Kombora akihoji juu ya hili na kutaka kujua juu ya lile. Mengi yalimsaidia ingawa ni machache yaliyopata nafasi katika daftari lake. Mengi yalikuwa yaleyale ambayo alikwishaambiwa kabla. Aliporidhika, alimgeukia msichana huyo ambaye alikuwa akijibu kwa nadra sana na kumwita, “Tafadhali bibie. Bibi Rusia kwa jina sio?”

“Ndiyo.”

“Nadhani ni wewe mwenye ufunguo juu ya suala hili. Nina maana kuwa, ni ushahidi wako ambao utatuwezesha kumtia mkononi huyu muuaji mapema zaidi. Unasema una uhakika kuwa huyu kijana anayeitwa Bazile Ramadhani ndiye aliyemuua bwana Kitenge?”

“Naamini hakuna mwingine,” alijibu bila kuwatazama.

“Kwa nini?”

“Mwenyewe alisema hivyo. Zaidi ya kusema anaonyesha kuwa ni mtu katili. Aliporudi mara ya pili nilipomjulisha kuwa muswada wake bado ulikuwa haujapatikana alitoa macho na kukimbilia katika chumba cha marehemu. Kama angemkuta naamini angemuua papohapo. Kwa bahati nzuri hakuwepo. Hata hivyo…” akasita na kufuta machozi yaliyomtoka ghafla.

“Pole dada,” alitamka Abdala.

“Ulikuwa unahusu nini huo muswada wake?” Kombora alihoji.

“Mauaji tu, yaelekea ni mtu anayependa sana mauaji?”

“Na unafikiri umekwenda wapi?”

“Muswada huo sio? Kwa kweli hata mimi nashangaa. Iko hapa miswada iliyoletwa miaka miwili iliyopita. Huo wake hatujakaa nao miezi minne, hauonekani. Kama ungekuwa wa kuvutia, tungesema mwenzetu mmoja kauchukua nyumbani kwake akausome. Kila aliyejaribu kuusoma alikata tamaa.”

Kombora akamshukuru na kuongeza, “Waweza kutusaidia vipi kumpata mtu huyu, Rusia?”

“Sidhani kama…”

“Huna barua yake yoyote yenye anuani yake?”
“Zipo nyingi. Alikuwa akiandika kila mara. Barua nyingine hata tulichoka kuzisoma. Nakumbuka iko moja ambayo aliiambatanisha na picha yake. Eti iwekwe nyuma ya kitabu.”

“Itafute tafadhali.”

Baada ya upekuzi mfupi katika majalada, Rusia alimkabidhi Inspekta Kombora barua tatu, moja ikiwa na picha. Kombora aliitazama picha hiyo kwa makini.

Akiwa mtu mzoefu wa kusoma picha za wahalifu alimwona Bazile vilivyo: kijana mwenye ndevu changa, umri baina ya miaka ishirini na mbili hadi ishirini na sita, sura yenye busara ingawa ilibeba macho yaliyokuwa yakitangaza mengi na hayakuwa na ladha ya maisha wala uangavu wowote, na ni kama ambayo yalikuwa yakinong’oneza kwa huzuni: “nimeonewa jamani.”

“Ndiyo, huyu anaweza kuwa muuaji,” aliwaza Kombora, huku akimpa Abdala picha hiyo. Akafunua barua kusoma anuani. Ilikuwa rahisi kuliko alivyotarajia. Anuani zote zilitaja sanduku la kazini pale TEGRY. Kiwanda cha kutengenezea vifaa vya plastiki.

“Tunashukuru sana dada,”Kombora aliaga ghafla akiinuka. “Nadhani sasa tuondoke tukawahi shughuli nyingine.”

“Asante mzee,” alijibu msichana huyo akiinuka kuwatazama kikamilifu kwa mara ya kwanza. Macho yake hayakuchelewa sana juu ya umbo la makamo la Inspekta Kombora, ambalo nywele zilianza kumezwa na mvi, uso ukiingiliwa na mikunjo. Lakini macho hayo yalikawia katika umbo lenye kiasi kikubwa cha ujana la Sajini Abdala. Sura ikiwa nzuri na umbo la mwanamichezo, Sajini Abdala alipendeza vyema katika magwanda yake ya kipolisi machoni mwa Rusia.

“Karibuni tena.”

“Asante bibie,” Abdala alijibu.

Walipofika katika ofisi yao walianza maongezi yenye lengo la majadiliano. Kila mmoja alitaka wazo la mwenziwe.

“Nadhani mwenye nafasi nzuri ya kuua ni huyu mwanamke Inspekta. Yeye ndiye aliyefika nyumbani kwa marehemu. Pia bado anaongozwa na nguvu za bangi na gongo. Simwamini mtu yeyote anayetumia vileo hivyo.”

“Kwa hiyo?”

“ Kwa hiyo, napendekeza uturuhusu tumsake huyu mama. Tukiwatuma vijana huko katika mageto ya Luhanga, Buguruni, Kigamboni, Kawe, Tandale na kote nadhani atapatikana tu. Sidhani kama yuko nje ya jiji hili mara hii.”

Kombora hakujibu mara moja. Yeye alimshakia zaidi huyu mtunzi, Bazile. Sauti katika simu ile haikuwa ya kike. Wala hakuona kama mwanamke huyu mlevi wa gongo angekuwa na haja ya kumwandaa na kumpigia simu polisi kama hadithi ile ya Simu ya Kifo.

Hata hivyo, bado aliona umuhimu wa kuwapata wote wawili mapema iwezekanavyo. Yawezekana kuwa mtunzi yule hahusiki. Yawezekana vilevile kuwa yeyote kati yao hahusiki! Aliwaza ghafla kwa hofu. Jambo ambalo litaongeza uzito katika jukumu hili.

*HAYA, INSPEKTA KOMBORA YUKO KAZINI AKIMSAKA MUUAJI HUKU AKISHIRIKIANA NA SAJINI ABDALA. NI KIPI KITAKACHOFUATA? FUATILIA RIWAYA HII KALI
ITAENDELEA

Najisikia Kuua Tena Sehemu ya Pili

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment