Njama Sehemu ya Kwanza
NEW AUDIO

Ep 01: Njama

Njama Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA : ARISTABLUS ELVIS MUSIBA (A.E MUSIBA)


Simulizi : Njama

Sehemu Ya Kwanza (1)

NAONANA NA CHIFU

Ndege ilitua kwenye uwanja wa ndege wa mjini Dar es Salaam kiasi cha saa moja na nusu asubuhi. Nilipita harakaharaka katika sehemu za afya, uhamiaji na ushuru wa forodha, kisha nikachukua teksi iliyonipeleka moja kwa moja katika ofisi yangu ya ‘Afrika International Agencies’, iliyoko mtaa wa Independence karibu na ofisi kuu za shirika la Bima la Taifa.

“Hallo bosi, umerudi!”, Rose mfanyakazi wetu sehemu ya mapokezi alisema.

“Naam nimepata ujumbe wa teleksi kutoka kwa Marcelina kuwa mama anakufa”.

“Na kweli nenda ofisi kwako mwandishi wako mahususi alikuwa na wasi wasi maana huko juu wanakuulizia kila baada ya dakika kumi. Ama kweli huko juu kuna kitu kikubwa kinawawasha”.

Nilielekea ofisini kwangu, nilipofika nikafungua mlango wa mwandishi wangu mahsusi, Linda.

Oh, Mungu wangu, afadhali umefika, kidogo nipate wazimu maana huko juu hawanipi nafasi hata ya kupumua. Naulizwa kila wakati kwanini hujafika, utafikiri mimi ndiye nakufuga”.

“Poa sasa nimefika mwenyewe. Vipi shughuli hapa?”.

“Mambo shwali, isipokuwa toka juzi kuna jambo limeharibika, maana jana nzima ofisi inawaka moto. Chifu huko juu ametingwa na mambo. Na afadhali uende sasa hivi, mimi nawajulisha kuwa uko kwenye lifti unaelekea ofisini kwake”.

“Yaa fanya hivyo”.

Niliacha mzigo wangu kwa Linda, nikaelekea ofisini kwa Chifu ambaye ofisi yake ilikuwa orofa ya tatu, na sisi tulikuwa chini katika jengo hilo hilo.

Nilifungua mlango bila kubisha hodi. Nikaingia ndani ya ofisi ya mwandishi mahsusi wa Chifu.

“Ooh, Mungu wangu! Afadhali umekuja!”, Maselina alisema kwa moyo wa furaha.

“Hujambo lakini?”.

“Sijambo ila wasiwasi ni juu yako tu. Pole sana, nafikiri tumekukatishia likizo murua kabisa”.

“Wacha kusema. Tayari nilikuwa nimeshapata kipande cha msichana. Nilipopata ujumbe wako kidogo nipate ugonjwa wa moyo. Je kuna nini huku kinacholeta wasiwasi hivi?”.

“Atakueleza mwenyewe kinachompandisha damu yake. Nakwambia amekuwa anakuhitaji kwa haraka sana, hata hivi anaona umechelewa. hivi sasa nilikuwa nataka kutuma teleksi nyingine”.

“Mama yangu mzazi! mtafikiri nina roketi yangu mwenyewe!”.

“Ngoja nimwambie kwamba umefika. Akifungua mlango kisha atukute tunapga soga sijui atafanya nini. Huenda atapasuka!”.

“Mwache apasuke! Mnafikiri kunikatisha likizo yangu nilijisikiaje. Utadhani moyo wangu umetengenezwa kwa chuma, na wake kwa udongo”.

“Kamwambie mwenyewe hayo huko ndani”, Maselina alijibu akimwemwesa huku akiinua simu.

Huyu Maselina tumefanya kazi pamoja kwa muda mrefu kiasi ya kwamba uelewano wetu hauwezi kuelezeka kwa maneno. Huenda siku moja nitapata maneno ya kueleza, ila tu kwa leo naweza kusema ni rafiki yangu mkubwa.

“Chifu, namba moja yuko hapa”, Maselina alitamka katika simu.

Nambari moja, ndivyo nilikuwa najulikana kikazi. Katika kazi yetu sisi hutumia namba, mimi nilikuwa namba moja hivyo unaweza mwenyewe kuchekecha ukajuwa kwa nini. Mimi Willy si mtu wa majivuno. Watu wengi, hasa wakubwa wa serikali walinijua kwa hii namba yangu. Wengi walikuwa hawajui namba moja ni Willy Gamba, ila kwa watu wachache sana. Hii ilinipa fursa hata nyumbani Dar es Salaam nijulikane kama mfanyabiashara wa kawaida tu, na si Willy Gamba ambaye ni namba moja katika Idara ya Usalama, Tanzania.

Maselina aliweka simu chini.

“Nenda ndani mara moja”.

Nilifungua mlango, na nikamkuta Chifu akitembea toka kona moja ya chumba hadi kona nyingine. Kwa mtu ninayemfahamu nikajua hapo alipo alikuwa na matatizo makubwa sana yaliyomsakama rohoni mwake.

“Kaa chini namba moja’, Chifu aliamru.

Chifu anaponiita kwa namba yangu ya kazi ujue kuna jambo kubwa.

nilivuta kiti nikaa, yeye akazidi kutembea kona hadi kona nyingine, hatimaye akasimama nyuma ya kiti chake.

“Nashukuru kwa kufika kwako mapema, namba moja ndio sababu nakutegemea sana”.

“Asante”, nilijibu halafu nikaendelea.

“Mbona hivi, nini kinakuwasha?”.

Alichukuwa mtemba uliokuwa mezani, akafungua mkebe wa tumbaku akaijaza, kisha akawasha na kuanza kupuliza. Alipuliza mara mbili, halafu akazungusha kiti chake ambacho kinazunguka kwenye tendegu, akaketi.

“Kina jambo kubwa limetokea!”.

Aliweka mtemba wake mezani na kuweka mikono yake kwenye mezani.

Akaniangalia machoni, huku macho yake yakionesha ukali wake.

Akili yangu ikiwa tayari kusikiliza jambo hili huku moyo ukinidunda.

Utanisikiliza, utauliza maswali baadaye”.

Sawa”.

“Nafikiri nitaanza toka mwanzo. Ingawaje mambo mengine unayajua, nitayarudia tu kwa ajili ya umuhimu wa habari yenyewe ilivyo, unaonaje?”.

“Utakavyoona wewe Chifu”.

“Unajua nchi yetu inalea vyama vingi vya wapigania uhuru. Kama vile vyama vya wapigania uhuru toka Zimbabwe, Afrika Kusini n.k. Pamoja n a kulea vyama hivi tunawapatia vijana wao ya kijeshi. Kwa vile mafunzo mengi yanapatikana hapa na makao makuu ya vyama hivi yapo hapa, basi silaha zao vile vile zinapitia hapa na sisi tunazipokea toka nchi rafiki na kuwapa wanaohusika.

“Hapa tuna vyama viwili vya wapigania uhuru katika Afrika kusini. Vyama hivi ni ‘The Peoples liberetion Front, of South Afrika (PLF)” kinachoongozwa na Ndugu Cecil Chimalamo na South Afrika National Party (SANP) kinachoongozwa na Ndugu Ray Simbuche. Miezi sita iliyopita Ndugu Cecil Chimalamo wa PLF alikwenda Urusi ambako alioba msaada wa silaha na akaahidiwa kupewa silaha hizo ambazo zingepelekwa Dar es Salaam mnamo muda wa miezi sita.

“Wiki iliyopita Ubalozi wa Urusi wa hapa mjini ulipata karatasi za maelezo ya silaha hizi ambazo tayari zilikuwa zimeshapakiwa kwenye meli siku nyingi na zilikuwa njiani kuwasili Dar es Salaam. Na makaratasi haya yalisema meli hiyo itawasili mjini hapa mnamo wiki hii’.

“Basi yalipofika, ubalozi uliyashughulikia kikamilifu kwa upande wake, kisha ukayapitisha kwenye kamati ya ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), maana kamati hii ndiyo inashughulikia mambo haya kama unavyofahamu. Kamati nayo ilianza kuzishughulikia karatasi hizi mpaka zikawa tayari, wakawa sasa wanangoja meli kufika. Habari kutoka kwenye Wakala wa Meli zilieleza kuwa meli hiyo itaingia bandarini Dar es Salaam tarehe tatu mwezi huu ambayo ilikuwa juzi ile”.

“Baada ya kupata habari hizi kamati ilipanga pamoja na ofisi ya mambo ya silaha za wapigania uhuru pia na maofisa wa bandari wanaohusika kuwa mizigo hiyo ipakuliwe usiku wa tarehe nne yaani juzi kuamkia jana. Kwa sababu karatasi zote zilikuwa zimekamilika na sehemu zote zikiwa na habari kamili, pande zote zilikaa zikisubiri silaha hizo mnamo siku hiyo kama ulivyopangwa”.

Chifu alichukua mtemba wake tena akavuta kidogo kisha akauweka juu ya meza.

“Nafikiri umenielewa mpaka hapo?”.

“Wakati huo mpango hii yote ya kupakua mizigo hii, ofisi ya PLF ilikuwa ikishirikishwa?”, niliuliza.

“Ndio, kwa sababu huwa wanaelezwa mambo yote yanavyokwenda, hivyo huwa wana habari kamili ya mambo yote. Naweza kuendelea?”.

“Unaweza”.

“Sasa jambo la kushangaza likatokea juzi. Maofisa wa ofisi ya jshi la ulinzi inayoshughulikia silaha za wapigania uhuru walikwenda kwenye ofisi ya kamati ya ukombozi juzi mnamo saa nne ili kuchukua karatasi hizo za mizigo, wapate kijitayarisha kwa upakuaji wa mizigo hiyo wakati wa usiku. Walipofika kwenye ofisi hii wakakuta ofisa anayehusika hajafika kazini. Ikabidi wamwone ofisa wa juu katika ofisi hiyo kumweleza umuhimu uliopo wa kuandaa kupakua silaha hizo usiku.

“Huyu ofisa wa juu katika ofisi hii ya kamati naye alisema kuwa alikuwa ameshangazwa kwanini ofisa huyo alikuwa hajafika kazini. Hivyo wote kwa ujumla wakaondoka kuelekea nyumbani kwa ofisa huyo kuona kama anaumwa aweze kuwaelekeza wapi walipoziweka karatasi hizo. Huyu ofisa alikuwa akikaa sehemu za Upanga, Barabara ya Umoja wa mataifa, nyumba namba 1168”.

“Walipofika nyumbani kwa ofisa huyo walimkuta mfanyakazi wake akiwa nje. Walipomuuliza kama wenye nyumba wapo aliwajibu kuwa yeye hakai hapo ila huwa anakuja kila asubuhi lakini alipofika asubuhi hii alikuta milango yote ya kuingilia ndani ya nyumba imefungwa. Hivyo mpaka muda huo alikuwa anasubiri kwani alifikiri wametoka. Ofisa huyo alikuwa anakaa yeye pamoja na mke wake na walikuwa bado hawajapata watoto. Ofisa mmoja wa jeshi alikwenda kuangalia gereji akakuta gari la ofisa huyu lipo na lilikuwa bado halijatoka. Kitu hiki kilimtia mashaka akawaeleza wenzake na akashauri wajaribu kuingia ndani ya nyumba huenda walikuwa bado wamo ndani. Kwani kama kutoka wangekuwa wametoka na gari lao, walikubaliane wavunje mlango wa kuingilia ndani”.

Chifu alinyamaza kidogo akainua macho yake kuniangalia.

“Walishtushwa kwa kumkuta ofisa huyu amepigwa risasi amekufa sebuleni, huku akiwa amevalia vizuri kabisa kuonyesha kuwa alikuwa anatoka matembezini. Halafu ukumbini walimkuta mke wa ofisa huyo naye amepigwa risasi amekufa huku akiwa amevalia nguo za kulia. Haapo hapo wakanyanyua simu na kutoa ripoti ya vifo hivi kituo cha polisi Oysterbay ambacho hakikuchelewa kutuma maofisa wao kwenye nyumba hiyo. Baada ya polisi kufika, maofisa hao wa jeshi na ofisa kutoka kamati ya ukombozi ilibidi warudi upesi kwenye ofisi ya kamati, maana vifo hivi vilileta wasiwasi”.

Wakati wote huu akieleza, mimi nilikuwa kimya kabisa na akili yangu ilichemka niliposikia habari hizi za mauaji.

“Halafu ikawaje?”.

“Walirudi ofisi za kamati upesi upesi, na kuanza kutafuta makaratasi haya ya mizigo kila mahali ofisini hapa, lakini hawakuona kitu. Hapo ndipo jasho lilipowatoka. Jambo hili liliwapa wasiwasi zaidi ikabidi wakimbilie bandarini kutoa habari kwa maofisa wa bandari kuwa karatasi zimepotea”.

Chifu macho yake yaliwaka nikajua karibu anasema kitu cha kustua.

“Walipofika katika ofisi za bandari, ofisa anayehusika na habari hizi, walipomweleza kuwa makaratasi yamepotea, alishangaa sana, ndipo mwishoni akawaeleza kuwa silaha zilikuwa zimeisha chukuliwa usiku uliokuwa umepita na wanajeshi waliovalia nguo za jeshi la ulinzi na wakiwa na karatasi zote za kuchukulia silaha, zikiwa kamili kabisa. Walikuwa wamefika na magari ya jeshi la wananchi, hata akawatolea namba za magari. Kundi hili lililochukua silaha liliongozwa na mtui aliyevalia nguo za cheo cha meja. Kusikia hivi kundi lote lililofika kwenye ofisi ya bandari lilichoka kabisa.

“Lakini si walikuwa wamekubaliana na ofisi ya bandari kuwa watapakua usiku wa juzi kuamkia jana, ilikuwaje yeye akaruhusu mizigo ipakuliwe usiku wa juzi ile kuamkia juzi?”.

“Huko ndiko nakuja kufafanua. Ofisa wa bandari alieleza kuwa mnamo terehe tatu mwezi huu ambayo ni juzi ile kiasi cha saa kumi alipata simu toka ofisi ya Kamati ya Ukombozi. Simu hii ilikuwa inatoka kwa ofisa wa juu katika Kamati ya Ukombozi anayeshughulikia mambo ya silaha, Ndugu Jones Mantare. Ambaye ndiye aligundua maiti ya ofisa huyo wa kamati akiwa pamoja na wanajeshi. Yeye anasema sauti ya Jones Mantare anaifahamu maana ameshughulika naye siku nyingi, na sauti hii aliyoisikia kwenye simu ilikuwa kama ya Mantare hivyo akaamini kuwa anazungumza na Mantare”.

“Simu hiyo ilieleza kwamba, kwa ajili ya usalama ratiba ya upakuaji silaha imebadilika, kwa hiyo silaha zilikuwa zipakuliwe siku hiyo hiyo kuanzia saa mbili za usiku kwani silaha zilikuwa nyingi. Hivyo akasema amtegemee meja mmoja wa jeshi kwa jina la Paul Liboi, atakuja pamoja na askari wa jeshi la wananchi kutoka kwenye ofisi inayoshughulikia silaha za wapigania uhuru ambaye atashughulikia kazi hiyo. Kwa hiyo, anasema alimwomba aiweke hiyo meli tayari kwa kupakuliwa saa mbili usiku. Yeye alikubali bila masharti maana kazi ya silaha ni muhimu”.

“Na mnamo saa kumi na nusu wakati akishughulika na kutoa amri ya meli hiyo kupewa nafasi kwenye geti alipata mgeni mwingine. Mgeni huyu alijitambulisha kwa jina la Andrew Mwambina ofisa usalama toka kamati ya ukombozi ya OAU. Alitoa kitambulisho chake na ofisa huyu wa bandari alivyokiona kilionekana halali maana ameshawahi kuona vitambulisho vya watu hawa. Mtu huyu alimwuliza kama amepata habari kuwa upakuaji umebadilishwa na ilibidi silaha zipakuliwe usiku huo saa mbili. Yeye alikubali kuwa amepata ujumbe na muda huo alikuwa anashughulikia jambo hilo. Ofisa huyo wa usalama alimwaga na kumwambia yeye na wenzake watakuwepo kikazi kama kawaida, akaondoka”.

“Kwa taarifa yako. Namba moja maafisa watatu wa usalama wa Kamati ya Ukombozi ambao walipangiwa kufanya kazi bandarini tangu ilipofahamika kuwa meli hiyo inaingia walikuwa wameuawa na maiti zao zilikutwa sehemu ya Shimo la Udongo jana jioni”.

Chifu alitua kidogo kupuliza mtemba wake.

“Taarifa ya ofisa wa bandari iliendelea kusema kuwa ilipofika saa mbili kamili za usiku magari manne ya jeshi tani kumi na mbili kila moja yaliingia. Na mtu aliyejitambulisha kama Meja Paul Liboi alifika ofisini kwake akiwa amevalia kijeshi na cheo chake kwenye mabega. Yeye alisema amekuja kushughulikia upakuaji wa silaha na kwamba aliamini ameshapewa habari na kamati ya Ukombizi mapema, na akatoa karatasi za kupokelea mizigo ya silaha ambazo zilikuwa sawa”.

“Yeye alimjibu kwamba alishapata habari na mipango yote ilikuwa tayari, hivyo baada ya kumaliza shughuli za makaratasi alitoka na Meja huyu na kuwaelekeza meli ilipokuwa tayari kwa upakuzi. Aliendelea kueleza kuwa magari haya manne yalikuwa na askari wengi waliovalia kijeshi. Hivyo silaha zilianza kupakuliwa saa tatu na kufikia saa kumi alfajiri gari la mwisho liliondoka. Silaha zilikuwa nyingi sana za kisasa na za hali ya juu. Nafikiri umenielewa mpaka hapo”.

“Ndio nimekuelewa”.

“Sasa kitu cha kutia huzuni ni kwamba silaha hizi zimepotea hazijulikani zilipo. Na wala watu na magari yaliyochukuwa silaha hizi hayajulikani yalipo mpaka dakika hii tunapozungumza. Idara ya polisi imejaribu kutafuta lakini mpaka sasa hawana hata fununu. Huu ni wizi wa silaha uliopandwa barabara na kwa serikali yetu hii ni “KASHFA”, kwa taarifa yako habari hizi zimevunja na zimeshatangazwa na nchi za Magharibi pamoja na Afrika Kusini juu ya tukio hili. Na tayari nchi adui za Tanzania zimeanza kuropoka ovyo ili kulichafua jina la nchi hii”.

“Mimi ninadhani hizi ni hila na Njama za mabeberu, wapinga mapinduzi wa mapambano Kusini mwa Afrika. Nia yao ya kufanya hivi ni kutaka mambo matu. Nia yao ya kwanza ni kuhujumu, kuchukua silaha hizi kusudi zisiwafikie wapigania uhuru ambao mapambano yao huko Kusini mwa Afrika sasa yanapamba moto, maana silaha hizi zilikuwa za kisasa na zingalifika kwenye uwanja wa mapambano wanajua wangepata cha mtemakuni. Kwa hiyo hizi ni njama za kuhakikisha kuwa silaha hazifiki kwenye uwanja wa mapambano”.

“Pili, wanataka kulipaka matope jina la Tanzania kwa vile Tanzania imeamua kuongoza ukombozi kusini mwa Afrika sasa ina maadui wengi sana, na maadui hawa wameanza kulipaka matope jina la Tanzania na kusema kuwa Tanzania huzitumia hizi silaha kwa majeshi yake. Wendawazimu wengine wameendelea kusema eti Tanzania kwa muda mrefu imekuwa inatumia misaada inayotolewa kwa faida yake!”.

“Hivi hili jambo si geni. Nia yao ya tatu ni kutaka kuzikatisha tamaa nchi rafiki zinazotoa misaada kwa wapigania uhuru, zisizidi kufanya hivyo, kwa kufikilia kuwa wanapoteza mali zao kwa kufanya kazi ambazo wao hawakuzipangia. Kwa hiyo, namba moja unaona hali ya hatari nchi yetu ilimo”.

“Lo! ni hali mbaya sana. sasa sisi tunatakiwa kufanya nini?”.

“Jambo hili sasa linashughulikiwa na Idara ya polisi na ofisi ya usalama. Upelelezi wao bado unaendelea na ni mkali sana. Katika usiku wa kuamkia jana serikali imeamua sisi lazima tulishughulikie jambo hili. Maana inaamini wizi huu uliofanywa ni wa kimataifa, hivi polisi hawakuzoea kupambana na hali kama hii. Kwa hiyo ingawake wao wataendelea na shughuri zao, sisi itabidi tujishughulishe kikamilifu juu ya jambo hili maana ni kima chetu polisi wameagizwa kuleta nakala ya ripoti zao zote za upelelezi wanaoufanya. Hii itafanya kupata habari nyingine ambazo zitatusaidia sana”.

“Serikali inataka jambo hili litatuliwe haraka kusudi tuweze kuwafichua hao maadui zetu wanaotaka kutupaka matope, maana itabidi tuionyeshe jumuia ya ulimwengu jinsi maadui zetu wanavyojaribu kutupiga vita kwa ajili ya msimamo wetu thabiti katika ukombozi wa Afrika. Na hatuwezi kufichua ukweli wa jambo hili mpaka hapo tutakapowakamata hawa waliofanya kitendo hiki. Kwa hiyo kazi yetu sasa ni moja tu, nayo ni kuwakamata watu hawa. Na wewe namba moja umepewa jukumu hili kubwa la kulinda hadhi ya nchi yako, Tanzania. Una maswali?”.

“Nipe muda kidogo nifikiri”.

Nikasimama na muda huu kwa ajili ya mafikara niliyokuwa nayo nilianza kutembeatembea toka kona hadi kona ya chumba kama nilivyomkuta Chifu akifanya. Ilionekana Chifu alijisikia nafuu baada ya kutua mzigo huu kwangu ikawa zamu yangu kubanwa na mawazo ya tukio hili.

“Hizi habari zimevujaje?”.

Niliuliza hukU bado natembeatembea nimeinamisha kichwa chini.

“Naamini, maharamia hao hao ndio wamezitoa ili wafanikishe moja ya shabaha zao. Yaani kuivunjia Tanzania hadhi”.

Mara moja nikawakumbuka Sherrif na Veronika nikajuwa lazima habari hizi zilikuwa zimeshafika ofisi za gazeti la Afrika na Sherrif alikuwa anakuja Dar es Salaam ili kuja kuchunguza na kuandika juu ya tukio hili. Katika mipango yangu iliyokuwa inapita kichwani nilipata pointi moja ya kunisaidia.

“Huyu Jonas Mantare anasemaje juu ya tukio hili?”.

“Baada ya kupata maelezo ya ofisi ya bandari, mara moja polisi walimkamata Jonas Mantare kwa kusaidia polisi katika uchunguzi, yeye alipoulizwa kama yeye ndiye aliyepiga simu, alikataa kabisa, na kukataa kwake kumedhihilishwa na Mwenyekiti wa kamati ya ukombozi kuwa Mantare alikuwa ofisini mwake toka saa tisa mpaka saa kumi na moja siku hiyo wakifanyakazi pamoja na wala hawakutoka hata dakika moja katika muda wa masaa hayo mawili”.

“Kwa hiyo kutokana na usemi wa ofisa wa bandari, kuna mtu mwingine aliyeiga sauti ya Mantare. Hii ina maana mtu huyu amemzoea”.

Nikarudi na kuketi kwenye kiti kwani akili zilianza kufanya kazi. Kwa mara ya kwanza nilitoa paketi yangu ya sigara nilizokuwa nimenunua katika ndege, nikaanza kuvuta.

“Bila ya shaka”, Chifu alijibu.

“Ofisa huyo aliyeuawa anaitwa nani?”.

“Anaitwa Kamara Frank, yeye ni mwenyeji wa Sierra Leon”.

Unaona sasa mambo yanavyokuwa huyu mtu alikuwa rafiki ya Sherrif kama unakumbuka.

“Daktari anafikilia Frank na mkewe walikufa saa ngapi?”.

“Daktari anakadilia kuwa walikufa kati ya saa sita na saa nane usiku. Na inavyoonekana ni kuwa kuna wakati alikuwa amefungwa kamba, maana alama zinaonekana kwenye mikono na miguu”.

“Sasa Chifu kuna jambo moja ambalo lazima tuelewane. Tangu nimeanza kazi hii nimekuwa nikifanya kazi zangu nje ya Tanzania. Hapa nyumbani najulikana kama mfanyabiashara tu. Lakini kama nikianza shughuli hii lazima nitajulikana hasa mimi ndiye nani. Unasemaje?”.

“Nani anajali”, alifoka Chifu kwa sauti ya juu. “Kitu ninachotaka mimi ni kuona jambo hili linatekelezwa na washenzi hawa wamekamatwa. Kama itabidi ujulikane potelea mbali!”.

“Lakini Chifu…”

“Hamna cha lakini hii ni amri ya serikali na serikali inataka matokeo juu ya suala hili na mapema iwezekanavyo”.

Nilijuwa kuwa kweli iko kazi kama kweli Chifu kakubali mimi nitambulike kirahisi hivi nilikaa nikaanza kufiri jinsi ninavyoweza kufanya upelelezi wa tukio hili bila kutambuliwa maana mimi sikuwa nataka kabisa nijulikane kama mimi ni mpelelezi hapa nyumbani. Kwani watu wengi Tanzania wanajuwa wana mpelelezi mashuhuri, kiasi cha kujitapa mitaani lakini hawajui kuwa ni mimi Willy Gamba. Na hivi ndivyo nataka, vinginevyo kila nitakapokuwa napita nitakuwa nafuatwa na kundi la wapenzi.

“Najuwa waandishi wa habari toka nchi za nje watakuwa na shauku kubwa kuja kuandika habari hizi. Kuna msimamo gani?”.

“Haturuhusu waandishi wowote toka nje. wamezuiliwa mpaka hapo tutakapojuwa msimamo kamili wa jambo hili. La sivyo watakuja kuzidi kuchafua mambo hapa. hatutawaruhusu kabisa idara ya uhamiaji imeshaelezea na imeshatoa amri kwa vituo vyake, na jambo hili limeanza kutekelezwa. Asubuhi hii nchi za Magharibi zimelalamika kusikia haturuhusu waandishi wa habari toka nje.

Nilichukua nafasi hii kumweleza Chifu juu ya kukutana kwangu na Veronika Sherrif. Nikaendelea kumweleza kila kitu juu ya kuja kwao hapa.

“Hivyo nahisi gazeti la “Afrika” linawatuma waje kwa ajili ya tukio hili. Ni lazima wameishapata habari”.

“Hawataruhusiwa kuingia”.

“Mimi naomba hawa waruhusiwe kwa sababu nafikiria kuwatumia katika shughuri hii”.

“Haiwezekani, watakuja tifua mambo tu, sitaki kuona waandishi wa habari toka nje!”, Chifu alifoka huku akionyesha hasira.

“Sasa Chifu, ni lazima tuelewane, hili jukumu umenipa mimi. Na inabidi mimi mwenyewe nipange ninavyoona, jinsi nitakavyoweza kulitatua tatizo hili, na kama sasa hatuwezi kukubaliana, sijui shughuli itawezekanaje?”.

Chifu alinyamaza kwa muda mrefu.

“Hebu ni majina kamili ya watu hao”.

Nikampa. Akainua simu, akazungumza na Maselina.

“Hebu angalia kwenye mafaili ya waandishi wa habari hasa waandishi wa gazeti la “Afrika”, angalia kama kuna faili zozote za majina ya Veronika Hamadu na Ahmed Sherrif wote kutoka Sierra Leon”.

Akaweka simu chini, tukasubiri katika ukimya. Baada ya kitambo kidogo Maselina alifungua mlango akaingia na mafaili mawili, akampa Chifu. Chifu alipoinama kuyafungua kusoma,

Maselina alinikonyeza na kufua mlango, akatoka nje.

Chifu alisoma faili la kwanza, alipomaliza akanitupia. Lilikuwa faili ya Ahmed Sherrif. Na mimi nilianza kulipitia kwa makini sana nilipomaliza kulisoma Chifu alikuwa nae amemaliza kusoma faili la Veronika Hamadu, akanitupia. Nilisoma faili la Veronika kwa makini vile vile, lilikuwa na habari zilizonifanya nitabasamu mara kwa mara mpaka nilipomaliza. Nilikuta Chifu ameegemea kwenye kiti chake akaniangalia kwa makini.

“Oke, wataruhusiwa kuingia, inaonekana wanaweza kuwa wa manufaa kwako. Sijui unataka kuwatumiaje, kama hutajari kunieleza”.

Baada ya kuwa nimesoma mafaili ya watu nilikata shauri namna ya kushughulika nao. Hivyo nilionelea juu ya mipango yangu maana huyu mzee kichwa chake kinafanyakazi. Kama akiona kuna kitu chochote hakifai atanikosoa mara moja. Waliompa kazi hii ni dhahiri walichagua mtu hasa anayefaa. Sidhani kuna mtu wa uwezo kama wake katika kuongoza kazi hii katika nchi hii. Yeye hiki ni kipaji alichopewa na Mungu. Na maendeleo yote ya idara hii ya upelelezi yamefanikishwa na uongozi wake ulio thabiti na wa busara.

“Mimi bado nahitaji kufanya upelelezi katika tukio hili, kujulikana kuwa mimi ni mpelelezi kwa watu wengi. Hivyo nimepanga kuwa kampuni yetu Afrikan International Agencies itakuwa wakala wa gazeti la Afrika. Kwa kufanya hivyo kampuni hiyo itawapokea hawa waandishi wa gazeti hilo kama wageni wake kwa sababu mimi najulikana kama meneja mkuu wa kampuni hivyo nitaandamana nao katika kutafuta habari zao nikiwa kama mwenyeji wao na kwa vile nafahamika hapa Dar es Salaam, nitawaongoza na wakati huo huo nitakuwa nafanya upelelezi wangu. Kwa kufanya huvi nitaweza kushughulika bila kutambuliwa kuwa mimi ni nani na ninafanya nini. Mpango kamili nitapanga na nitakueleza”.

Alikaa kimya kutafakari mpango wangu.

“Vizuri sana, namba moja, akili yako inafanyakazi. Nimeishaona shughuli yote itakavyokuwa kwa urefu. Mpango wako ni mzuri, endelea nao. Unafikiri hawa waandishi watafika saa ngapi”.

“Si zaidi ya usiku wa leo”.

“Oke nitapeleka habari sasa hivi watu hawa waruhusiwe kuingia. Wewe nenda sasa ukapumzike maana najua haujalala tengeneza mpango wako wote wa upelelezi huo, na uniletee kesho asubuhi. Lakini kumbuka kazi hii ni kubwa na ya haraka, hivyo msaada wowote utakaoutaka utapewa. Ofisi yote imeweka kando kazi nyingine mpaka tutakapoona mwisho wa kazi hii. Mungu akusaidie kama amnavyo amekusaidia siku zote. Nina imani na wewe Willy. Najua utafanikiwa. Kwa heri Willy mpaka baadaye, kapumzike”.

Chifu anapoanza kuniita Willy ujuwe kuna kitu kimemfurahisha hasira na wasiwasi wake umepungua. Na anakuwa na imani kuwa kazi itafanyika.

“Asante”, nilijibu.

Niliangalia saa yangu. Ilikuwa saa saba za mchana mkutano huo ulikuwa umechukua muda mrefu sana. Nilimwaga Chifu nikamwahidi kumletea nakala ya mpango wangu wa operesheni hii asubuhi.

Nilifungua mlango nikaingia ofisini kwa Macelina.

“Kazi kubwa unayo, pole sana Willy”.

“Nitafanyaje Macelina, mimi mwenyewe nilikubali kazi hii sasa siwezi kurudi nyuma. Na vile vile kwa sababu tukio hili linahusu wapigania uhuru, niko tayari kabisa kwa lolote. Wewe mwenyewe unajuwa moyo wangu ulivyo juu ya ndugu zetu wanaoteswa huko Kusini mwa Afrika”.

“Naelewa Willy, naelewa sana roho yako ilivyo juu ya ukombozi wa Afrika Kusini. Vijana wote wa Kiafrika wangekuwa na roho kama yako sasa hivi kungekuwa hakuna ukoloni Afrika”.

“Asante kwa kunipa moyo”.

“Usiwe na wasiwasi, naamini mungu atakusaidia kama siku zote, maana wewe unatetea wanyonge wanaoonewa. Hata hivyo tukio hili n hatari kuliko mengine yote. Pole sana”.

“Asante tena Maselina. Vipi huendi kula mchana?. Twende nikakununulie chakula cha mchana”.

“Ngoja nimwage Chifu”.

Maselina aaliingia ndani, alipotoka akasema ameruhusiwa muda wa saa moja tu saa nane ilimbidi awe kazini.

“Yeye haendi kula?”.

“Ana vitafunio vyake humo ofisini, ndio hatoki tena. Huyu mzee kazi itamwua”.

“Shauri yake. Yeye ameshaula kidogo si kama sisi. Miaka sitini ni miaka mingi.

Maselina alichukua mkoba wake tukaondoka.

                   CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/     



                                   III

Niliingia ofisini kwangu mnamo saa nane baada ya kupata chakula kitamu na Maselina.

“Linda nipeleke Colt Motors nikachukue gari langu”.

“Hamna taabu bosi, twende zetu”, Linda alijibu huku akichukua mkoba wake. Gari langu ni aina ya Colt GallantCoupe hivyo kila nikisafiri huwa naliacha kwenye kampuni yao.

“Vipi bosi, naona umeitwa shauri ya wizi wa silaha wa majuzi”, Linda alinidadisi.

Huyu katibu wangu mahsusi alikuwa amefanya kazi nasi kwa muda wa miaka minne na mwaka huu alifikia kiasi cha kuaminika sana na kupewa nafasi ya kuwa katibu mahsusi wa Namba Moja.ambacho ni cheo cha juu sana. Kwa upande wa makatibu mahsusi yeye alikuwa amejipatia nafasi ya pili ya kuaminika baada ya Maselina. Alikuwa msichana mwenye akili nyingi, na alikuwa mzuri wa urubi. Alikuwa na kila sifa anazostahili katibu mahsusi kwa mpelelezi wa hali kama yangu. Nilimpenda kwa jitihada zake za kazi na nilimtegemea bila wasiwasi.

“Ndio Linda, matatizo kila wakati hutokea wakati niko katika kilelel cha maraha, sijui mkosi gani huu.

“Mimi huwa naamini huwa unapata raha fulani katika pilika pilika zako, maana kila ukimaliza shughuli fulani huwa nakuona katika hali ya furaha sana”.

“Hiyo inatokana na kumaliza kazi yangu katika hali ya kuridhisha”.

“Unafikiri watu hawa wameiba hizi silaha kusudi wazitumie kupindua serikali?”, Linda aliuliza.

“La hasha, wanajua hawawezi kabisa kupindua serikali, maana wananchi wote wa nchi hii wamejidhatiti katika ulinzi. Mimi nafikiri wana sababu nyingine, na sababu hii nitaipata katika muda si mrefu”.

Saa nane hii magari yalikuwa mengi maana watu wengi walikuwa wanarudi makazini. Hivyo barabara hii ya Pugu ilikuwa na msongamano wa magari. Linda alitumia ujuzi wake wote ili kujipenyezapenyeza tuweze kufika upesi.

“Lazima nikupeleke upesi bosi maana najua una bonge la usingizi”.

“Ndio sababu sikuchukii Linda, maana huwa ndiye mtu unayenionea huruma, wewe na Maselina, wengine wote wanafikiri mimi nimetengenezwa kwa chuma”.

“Hata mimi lazima niungame kuwa huwa vile vile nafikiri wewe si binadamu wa kawaida maana mambo unayofanya nashindwa hata kueleza”.

“Taa kwenye barabara hii zimezidi, hapa na pale taa, nadhani ndizo zinazosababisha msongamano wa magari”, Linda alilalamika wakati tukiwa tumesimamishwa kwenye taa za usalama barabarani za karibu na Shirika la Usagaji na ofisi za Tazara..

“Hata mimi nafikiri hivyo hivyo. Nafikiri barabara hii ingefanywa barabara muhimu, na magari yote yatakiwe kwenda kasi, tuseme si chini ya kilomita themanini kwa saa. Hii ingesaidia watu kufika kazini haraka au wasafri wanaosafiri kwa ndege wasingekuwa na wasiwasi wa kuchelewa kama ilivyo hivi sasa”.

Tulipoingia Colt Motors tulimkuta meneja ndio anarudi kipindi cha alasiri.

“Mbona umerudi haraka nawe ulisema utarudi baada ya wiki tatu?,” meneja wa karakana aliniuliza.

“Nilipata habari kuwa mama anaumwa ikabidi nirudi haraka sana”.

“Oh pole sana, kuna kitu chochote tunaweza kusaidia?”.

“Asante sana, nimemwona; anapata matibabu ya kutosha huko hospitali ya Muhimbili”.

“Kama utahitaji msaada wakati wowote usisite kusema”.

“Asante, nitakumbuka”, nilijibu.

Tulikuwa tumejenga uhusiano mzuri wa kibiashara na kampuni hii. Nilifuatana na Linda mpaka kwenye gari lake nikachukua mfuko wangu.

“Linda itabidi umwambie Godwin aweke watu wa kuaminika sana kwa usiku wa leo maana nategemea wageni. Akipata habari zozote anieleze moja kwa moja nyumbani, mimi sitakwenda mbali leo. Nitatoka kidogo saa mbili hivi na nitakuwa Palm Beach Hoteli kwa chakula cha jioni, lakini baada ya chakula nitarudi nyumbani.

“Usiwe na sahaka, yote yatatekelezwa kama ulivyotaka”.

Tuliagana mimi nikaingia ndani ya gari langu na kuelekea nyumbani kwangu Upanga.

                                      IV

Wakati nilipokuwa nimeondoka, kwa kujua kwamba nitakaa nje karibu mwezi mzima, nilikuwa nimemweleza mfanyakazi wangu naye achukue likizo. Alikuwa amekwenda Morogoro.

Nilipofika nyumbani kwangu, nyumba ambayo iko barabara ya Upanga karibu na Hoteli ya Plm Beach, nilimkuta mlinzi niliyekuwa nimemwajiri kwa muda kutoka kampuni ya ulinzi.

“Hapa salama”, niliuliza.

“Salama tu, Mzee”, alijibu.

“Nimerudi, hivyo sidhani kama nitakuhitaji tena. Nitawapigia simu ofisini kwako, hivyo unaweza kuondoka.

“Asante sana Mzee”, alijibu huku akiondoka.

Niliweka gari langu gereji, nikafungua mlango wa nyumba, nikaingia ndani. Nyumba ilikuwa shwali kabisa.

Nilipomaliza kuoga ilikuwa saa kumi kamili za mchana, nilijibwaga kitandani nikalala na kupata usingizi moja kwa moja. Nilipoamuka ilikuwa saa moja na nusu. Hivyo nilivaa nguo nikanawa uso na kuelekea Palm Beach Hoteli. Kwa sababu Palm Beach ni karibu na nyumbani kwangu nilitembea kwa miguu. Na nilipoingia Palm Beach niliagiza chakula nikaomba nipewe haraka kwa sababu mimi najulikana kwenye Hoteli hii, nilishughulikiwa haraka sana.

Nilikula chakula changu upesi upesi na kurudi nyumbani. Nilipofika nyumbani nilivaa nguo za kulalia na kuingia kitandani. Kwa vile nilikuwa na usingizi mzito nilikuwa nasikia uchovu tena nilijua huu ndio ulikuwa usiku wangu wa kulala, maana siku zifuatazo nilijua kulala kwangu kutakuwa haba kweli. Usingizi ulinichukua mara tu baada ya kujitupa kitandani.

Niliamswa na mlio wa kengere ya simu. Nilipoangalia saa yangu ilikuwa inasema yapata saa nane.

Niliinua simu.

“Hallo Gamba hapa”.

“Hallo bosi habari za kulala?”.

“Lo Linda vipi?, bado uko ofisini”.

“Nilijua kazi uliyoagiza inaweza kuwa ya maana hivyo nilionelea niishughulikie mwenyewe”.

“Oh, mtoto wewe, wacha kufanya hivyo wewe bado mdogo unahitaji usingizi wako, tuachie sisi mambo hayo”.

“Ni lazima nianze kujikomaza, vinginevyo sitaweza kulingana na shughuli zako, maana nimejifunza toka kwa Maselina ambaye anaweza kukaa siku mbili bila kulala kama kuna kazi inayobidi kufanyika kiasi hicho. Hivyo na mimi lazima nijizoeze muda huo ufikapo nisiuone mgumu”.

“Haya mama, nafikiri una sababu ya maana. Haya leta ujumbe, naamini hukunipigia kunielezea uko ofisini mpaka saa hizi”.

“La hasha, kuna wageni wako wawili wameingia hapa mjini wameniambie nikupashe habari zao. Ahmed Sherrif amefikia New Afrika Hoteli na Veronika Amadu amefikia Kilimanjaro Hoteli. wanasema kama inawezekana uwapigie simu sasa hivi”.

“Asante nitafanya hivyo. Sasa wewe nenda ukalale. Mpigie Juma aje aendelee na kazi maana nitakuhitaji kwa kazi kesho asubuhi”.

“Haya bosi nitafanya hivyo”.

“Kwa heri, kalale salama mtoto wewe”.

“Asante”, alijibu na kukata simu.

Niliinua simu tena na kupiga New Afrika.

“Hallo New Afrika Hoteli habari yako ndugu?”.

“Nzuri”.

“Nipe mapokezi”.

“Oke”.

“Hallo mapokezi hapa”.

“Nina mgeni wangu hapa ameingia usiku huu anaitwa Ahmed Sherrif naomba kuzungumza naye”.

“Subiri bado yuko hapa mapokezi”.

“Willy hapa habari ya safari?”.

“Ohoo Willy, ofisi yako inafanya kazi vizuri sana tayari umeshapata habari?”.

“Ndio, mmefika salama?”.

“Ndio salama, salimini”.

“Tulifikiri hatutaruhusiwa kuingia kama waandishi wengine wanavyorudishwa uwanja wa ndege wasiingie Tanzania. Lakini sisi tumeruhusiwa ni ajabu sana”.

“Usijali tutazungumza kesho”.

“Oke tuonane hapa Hotelini saa nne maana nina usingizi tele hapa niliposimama”.

“Oke, tutaonana saa hizo, lala salama”.

“Asante sana Willy”.

Nilikata simu kisha nikapiga Kilimanjaro Hoteli.

“Hallo Kilimanjaro hapa”.

“Habari yako ndugu?”.

Nilimsalimia Opareta.

“Nzuri”.

“Nina mgeni wangu amefikia Hotelini kwenu hapo nafikiri bado yuko mapokezi anaitwa Veronika Amadu”.

“Subiri amepelekwa sasa hivi chumbani kweke”.

“Hallo”, nilisikia sauti ya Veronika.

“Hallo binti hujambo?”.

“Hallo Willy, hujambo mpenzi?”.

“Sijambo mie, pole na safari”.

“Asante nimepoa”.

“Najua umechoka nilitaka kujua tu kama umfika salama”.

“Nimefika salama. Njoo unione saa tatu hivi kesho nitakuwa nimeisha amka”.

“Uko chumba gani?”.

“Niko orofa ya pili 208”.

“Oke binti, tutaonana asubuhi”.

“Ukifika gonga mara mbili haraka haraka, halafu ya tatu subiri kidogo halafu gonga nitajua ni wewe”.

“Asante nitafanya hivyo”.

“Kwa heri mpenzi, tutaonana asubuhi”.

“Asante, kwa heri”.

Niliweka simu chini nikalala ili nipumzike tayari kwa shughuli za asubuhi.

VERONIKA NA SHERRIFF

Asubuhi hii niliamka mapema, na baada ya kuoga na kuvaa vizuri niliamua nikastaftahi hapo Palm Beach Hoteli, kwani niliona uvivu kujipikia chai. Kama kuna kitu nachukua ni mambo ya kupikapika.

Nilikuwa mtu wa kwanza kufika Palm Beach Hoteli kwa ajili ya kusitaftahi. Kijana mmoja muuza magazeti alinifuata ndani ya chumba cha chakula na kuniuzia magazeti ya Daily News na Uhuru. Nilipitisha macho kwenye magazeti haya huku nikisubiri niletewe chemsha kinywa.

Magazeti haya yalijaa habari nyingi kama kawaida, lakini habari juu ya tukio lililokuwa limetokea katika wiki hii haikuwemo. Bila shaka ilikuwa imeachwa kwa ajili ya usalama. Nilipoletewa chemsha kinywa niliishambulia haraka haraka, nikalipa na kuondoka kuelekea ofinini. Wakati huo ilikuwa yapata saa moja na nusu.

Nilipokuwa napita karibu na nyumba yangu, mara akili ikanijia kuwa afadhali nichukua bastola yangu kwani nisingeweza kuamini tu kuwa hali ilikuwa ya usalama. Nilirudi nyumbani kwangu, nikachukua bastola moja aina ya 38mm ya kipolisi na kuiweka ndani ya shati langu kwa jinsi ambavyo isingeweza kuonekana kwa urahisi.

Nilichomeka shati vizuri, nikafunga mkanda wa suruali na kuifungia vizuri bastola chini kidogo ya kitovu. Kwa sababu kulikuwa na hali ya mawingu-mawingu nilivaa jaketi juu. Kisha nikaelekea ofisini.

Nilikuta ofisi imeshafunguliwa, nikapita nikawasalimia maofisa wangu wadogo, kisha nikaelekea ofisini kwangu. Linda alikuwa tayari ameshafika.

“Hallo bosi, umelalaje?”, Linda alinisalimia nilipofungua mlango na kuingia ndani.

“Safi kabisa, je wee?”.

“Mimi ndiye nimelala vizuri kabisa, hata sikuota leo ingawaje mimi ni muotaji”.

“Itabidi uwe unalala si chini ya masaa sita, bado mtoto mdogo wewe”.

“Sawa, lakini panapokuwa na shughuli maalum sina budi kukesha.

“Kama ndivyo hivyo naona kazi itafanyika”.

“Na usiwe na shaka, itafanyika”.

“Niitie Eddy aje ofisini kwangu”.

“Sawa bosi”.

Kwa sababu Namba mbili, tatu na namba nne walikuwa safarini huko Kusini mwa Afrika kwa shughuli maalum, ilibidi katika shughuli hii nishirikiane na kijana Eddy Kisanga, ambaye alijitokeza kuwa kijana shupavu sana katika kazi yetu hii.

Eddy alikuwa kijana mwenye umri wa miaka ishirini na mitatu, lakini alikuwa na akili za kuweza kumiliki matatizo na kujifunza mambo magumu katika kazi yetu hii kwa haraka sana.

Kitu cha kutufurahisha ni kwamba alikuwa mwanafunzi wangu mimi mwenyewe, hivyo matendo yake yalifanana na yangu, kiasi kuwa hapa ofisini aliitwa Willy mtoto.Na yeye alikuwa akifurahi sana kuitwa hivyo.Kwa hiyo nilipopeleka jina lake kwenye kamati ya upelelezi, nikawa nimeweka sifa zake kama mimi haikuwa ajabu kukuta amethibitishwa.

Baada ya kuthibitishwa ilibidi apewe kazi maaum ili kumpima na kuweza kumpa namba. Hivyo yeye na Sammy Rashid namba mbili walikuwa kwenye kazi maalum huko Johannesburg, Afrika Kusini. Kazi hiyo ilitekelezwa vizuri sana, na waliporudi namba mbili alitoa ripoti juu ya kazi hiyo na ikaonekana sehemu aliyofanya Eddy ilimshangaza hata Chifu, Eddy aipewa namba ya juu kuiko wote tuivyotegemea na kutokana na muda wake kazini; Kutoka kwenye kamati ya usalama alipewa namba ‘TANO’.

“Eddy yuko hapa”, Linda ainieleza kwa simu.

“Mwambie aingie”, nilimjibu.

Eddy aiingia ndani nikamuonesha kwa ishara ya mkono avute kiti aketi.

“Habari za leo bosi”, alisalimia Eddy.

“Nzuri, habari yako wewe?”.

“Ni nzuri”.

“Eddy natumaini umesikia jambo lililotokea hapa mjini siku chache zilizopita?”.

“Ndio, lakini nimezisikia kwenye radio za nje, na rafiki yangu mmoja polisi wa kituo cha kati, ndiye aiyenielezea kwa kirefu kidogo. Vile vile alinieleza kuwa wao ndio wanapeleleza tukio hili lakini kufikia sasa hawajafika popote. Wanasema mpaka sasa hawajaona au kupata kitu chochote kinachohusika na tukio hilo. Hata hivyo wanasema watajitahidi”.

“Kwa kutokana na hali ya namna hiyo serikali imeamua kutupa sisi jukumu hili, ingawa polisi wataendelea na upelelezi kamambe juu ya tukio hilo. Na ndio sababu nimeitwa kurudi mara moja toka likizo. Kwa hiyo toka sasa hivi ahirisha mambo yako mengine yote na tushughulikie tukio hili. Umenielewa?”.

“Bila shaka”.

Nilianza kumweleza jinsi nilivyoendesha mipango yangu yote nikiwatumia Sherriff na Veronika.

“Kwa hiyo Eddy, ninachotaka wewe ufanye, kwanza, nataka ukodishe magari manne kutoka kwenye kampuni mbali mbali zinazokodisha magari hapa mjini kama vile Co-cabs, Safari Toures Afrika Ltd., Takim’s Agancies, nk. Gari moja kati hizi liegeshe mahali pa kuegesha magari New Afrika Hoteli na lingine liegeshe Kilimanjaro Hoteli. Magari mawili yatakayobaki nataka wewe pamoja na kijana mwingine kati yetu mtufuate kila mahali tutakapokwenda leo. Lakini mtufuate kwa siri kabisa kiasi kwamba mtu yeyote asitambue kama mnatufuata sisi. Mimi nitatumia gari langu. Nia yangu nataka muwe macho kama kuna watu wengine watakaoweza kuwa wanafuata safari yetu kwa siku ya leo. Umeelewa?”.

“Nimeelewa vizuri kabisa bosi. Kazi itatekelezwa. Si ajabu hata wewe hutatuona.”

“Kazi ya namna hiyo ndio nataka”.

“Utapata, bosi.”

“Gari zile utakazoziegesha New Afrika na Kilimanjaro Hoteli, weka swich ya gari hizi chini ya zuria kwa upande anaotoka dereva.”

“Nitafanya hivyo.”

“Haya sasa nenda ukashughulike na kazi hii ili saa nne muwe tayari nje ya New Afrika Hoteli ambapo ndipo tutaanza safari yetu.”

“Tutakuwa hapo saa hizo, usiwe na wasiwasi”.

ILIKUWA saa tatu kamili niliposimama mbele ya chumba namba 208 katika ghorofa ya pili ya hoteli ya Kilimanjaro, niligonga mlango mara mbili haraka haraka, halafu nikatulia kidogo kisha nikagonga tena. Hivi ndivyo nilivyokuwa nimeelekezwa.

“Karibu”, nilisikia sauti kali ya juu ikitokea ndani ya nyufa za mlango. Nilifungua nikajikuta katika sebule ya chumba hiki ambamo Veronika alikuwa amevaa kaputula na sidiria tu akifanya mazoezi ya viungo. Alikuwa ameelekea upande mwingine na kunionesha mgongo na kuendelea na mazoezi yake kama kwamba hakuna mtu aliyeingia. Nilirudisha mlango, nikauegemea na kutazama jinsi binti huyu alivyokuwa akichukua mazoezi.

“Karibu Willy Gamba, kaa kwenye kiti upumzike”, alinielekeza bila kugeuka na huku akiendelea na mazoezi yake. Kisha akaanza kusema kana kwamba anajizungumzia yeye peke yake.

“Willy Gamba anayejiita mfanyabiashara huku ni mpelelezi mashuhuri wa Afrika. Afadhali ningejua mapema naamini ingekuwa furaha kubwa kuonana na mtu huyu mashuhuri nyumbani kwetu. Lakini nimekuja kujua mjini London katika ofisi za gazeti la ‘Afrika’, hasa ni hii teknolojia iliyoingia ulimwenguni maana tumeelekezwa na komputa ya pale ofisini. Sherriff aikuwa na mashaka kuwa amewahi kusikia jina la Willy Gamba mahali. Hivyo kufika tu London akailisha komputa hiyo jina la Willy Gamba. Maana komputa hiyo imeweka kwenye ubongo wake waandishi wote maarufu wa habari, wapelelezi wote maarufu ulimwenguni, wakubwa wote wa serikali mbali mbali na watu wote maarufu katika nyanja mbali mbali.

“Lo! alipoilisha jina hili ndipo ikatutolea maajabu. Ilionyesha kuwa Willy Gamba mwenye umri wa miaka ishirini na tisa, mwenye urefu wa futi tano na inchi kumi na mwenye umbo la kupendeza sana ni mpelelezi maarufu ulimwengu mzima. Iliendelea kusema kuwa Willy Gamba amehitimu katika chuo kikuu cha Dar es Salaam na kupata shahada katika sheria. Baada ya kutoka chuo kikuu moja kwa moja aliteuliwa kwenda kujifunza mambo ya upelelezi kwa kutokana na sifa zake alizoandikiwa na wakubwa wa Jeshi la Kujenga Taifa, wakati akiwa katika Jeshi hilo”.

“Komputa ilieleza kuwa Willy Gamba anasemekana amepata mafunzo katika nchi mbali mbali kama vile Uingereza, Cuba, Urusi, Marekani, China na Japan. Kutokana na mafunzo haya amejulikana kama mtu hatari katika kutumia aina yoyote ya silaha. Vile vile anajua karate na Kung-fu ya hali ya juu kwani wakati akiwa Japan aliwahi kushindana na Inoki na kutoka sare naye. Watu wanashangaa kwanini hakuendelea maana bila shaka sasa angekuwa bingwa wa dunia. Zaidi ya yote anaaminika kuwa amehitimu mafunzo ya kikomandoo. Komputa ilizidi kuonesha kuwa Willy Gamba ana I.Q ya hali ya juu sana, hivi sasa ni mtu anayeweza kusokoroa matatizo yaliyojisokota sana. Na iliendelea kuonyesha kuwa ameifanyia ‘OAU’ kazi nzuri sana hasa kuhusiana na Ukombozi wa Afrika Kusini”.

Alipofika hapa alinyamaza, kisha kama umeme alikatisha mazoezi yake na kunigeukia na kurukia kifuani pangu kwani bado nilikuwa nimesimama mlangoni nikisikiliza kwa makini.

“Kwanini usinieleze toka mwanzo Willy mpenzi, kwanini?”.

Nilimkumbatia kifuani kwangu na badaa ya kujibu swali lake nilisema. “Veronika Amadu”.

Aliinua macho akaniangalia usoni, mimi bila kusita niliendelea. “Mwandishi maarufu wa gazeti la “Afrika”, Veronika Amadu mwenye umri wa miaka ishirini na sita, mwenye urefu wa futi tano na inchi tano, mwenye macho na umbo la kupendeza la vipimo 38′-22′-36′. Alihitimu katika Chuo Kikuu cha Ibadani nchini Nigeria na kupata shahada katika uandishi, baada ya kuhitimu aiajiriwa na gazeti la ‘Newsweek’ la Marekani, akiwa mwandishi wao katika Afrika Magharibi. Kwa vile gazeti lilitaka kumtumia mwandishi huyu kupata habari zingine ambazo kuzipata kwake itabidi uhatarishe maisha yake, lililazimika kumpeleka Japan kujifunza namna ya kujikinga kwa mikono, hatari yoyote itokeapo, hivyo mwandishi huyu amehitimu katika Judo na Karate na kupata mkanda mweusi. Baada ya kuwa na gazeti hili kwa muda mrefu aliacha na kujiunga na gazeti a Afrika. Anajuikana kuwa msichana mwandishi jasiri sana, amewahi kusafiri na majeshi ya Chama cha wapigania uhuru wa Sahara Magharibi kiitwacho “The Popular Front for the Liberation of Saguiet el-Hamara na Rio de Oro” yaani “POLISARIO”, katika mapambano yao dhidi ya majeshi ya Morocco ambayo yameshika sehemu hiyo, inasemekana mwandishi huyu alikaa na majeshi haya na kuandamana nayo katika uwanja wa mapambano kwa muda wa miezi sita na kuwa mwandishi wa kwanza kuandika habari kamili za mapambano haya akiwa shahidi wa macho. Je unasemaje Veronika Amadu”.

“Sasa naamini kabisa wewe ndiye Willy Gamba, maana mimi nilifikiri tumekutangulia kumbe wewe ndiye umetutangulia zaidi. Naamini hata Sherriff sasa umamfahamu kama nyuma ya kiganja chako hebu nieleze”.

Nilimweleza. “Ahmed Sherriff mwandishi mashuhuri wa gazeri la Afrika hasa juu ya mapambano ya Kusini mwa Afrika. Ahmed Sherriff mwenye umri wa miaka thelathini na mbili, mwenye urefu wa futi tano na inchi kumi na moja na mwenye masharafa mengi, alihitimu katika Chuo kikuu cha Patrick Lumumba mjini Moscow, Urusi. Baada ya kuhitimu kwake alipotea isijulikane aliko kwa muda wa mwaka mmoja. Lakini habari za kuaminika zinasema kwamba alikuwa akichukua mafunzo ya kijeshi katika kambi za kijeshi za Wapalestina huko Mashariki ya Kati. Baada ya kuonekana alipatiwa kazi moja kwa moja na gazeti la Afrika ambalo linaaminika lilipata fununu juu ya mafunzo ya kijeshi ya Sherriff huko Mashariki ya Kati. Kwani baada ya kumwajiri tu alipelekwa moja kwa moja Kusini mwa Afrika ambako aliandamana na majeshi ya wapigania uhuru wa Frelimo, MPLA na siku hizi anaandamana na majeshi ya SWAPO katika uwanja wa mapambano huko Namibia.

“Vile vile kuna habari zinazosema kuwa alikuwepo katika mkasa uliotokea Soweto na ndiye aliyeandika habari za kuaminika juu ya tukio hilo. Hivyo ujasiri wake huu umemfanya kuwa mwandishi maarufu sana anayechukiwa sana nan tawala dhalimu za Afrika Kusini na Rhodesia na nchi zote zinazopinga mapinduzi ya Afrika na harakati zake za kujikomboa kutokana na ubeberu. Umeridhika sasa.”

“Sasa naamini ukiambiwa mtu ana I.Q ya hali ya juu, lazima utambue kuwa kwa kila jambo unalotaka kufanya yeye yuko hatua nyingi mbele yako”, Veronika alijibu na kuanza kunibusu huku midomo yake ikiwa ya chumvi chumvi sababu ya mazoezi.

“Ngoja nioge mara moja ili tukaonane na Sherriff tukaanze mazungumzo yetu ya kwanza.”

“Sawa”. Aliniacha na kwenda maliwatoni. Mimi nikabaki katika mawazo makali jinsi ya kuanza kulishambulia tatizo hili.

Niiegesha gari langu kwenye maegesho ya Hoteli ya New Afrika. Nikatelemka na kuzunguka ili nimfungulie Veronika. Tuliingia New Afrika Hoteli katika sehemu iitwayo duka la Kahawa tukatafuta meza tukaa.

“Ulishastafutahi?”, nilimuuliza Veronika.

“Kawaida yangu huwa ninastafutahi kabla ya kufanya mazoezi kila siku, ili kujiweka katika hali nzuri”.

“Ndio sababu umbo lako linapendeza namna hiyo”.

“Asante”.

Mtumishi wa hoteli alifika na kutuuliza mahitaji yetu.

“Mimi nitakunywa maji ya machungwa kama yapo”.Veronika alisema.

“Mimi niletee maji ya ndimu”. niliagiza.

Alipoondoka mtumishi huyo nilimweleza Veronika kuwa mimi nitakwenda mapokezi kumwita Sherriff, ambaye niliamini alikuwa bado chumbani.

“Habari za leo Tom?”, nilimsalimia kijana wa mapokezi ambaye tunafahamiana vizuri sana.

“Aha mzee, shikamoo”, alinisalimia.

“Marahaba”, nilimjibu.

“Sijui nikusaidie nini mzee?”.

“Kuna mgeni wangu hapa anaitwa Ahmed Sherriff, alifika usiku”.

“Ndio ndio, yuko yuko namba 406, unahitaji kwenda huko au nimpigie simu”.

“Mpigie simu nizungumze nae”.

Alimpigia simu na alipompata akanipa.

“Hallo Sherriff habari za leo?”.

“Ohoo, Willy salama?, nilikuwa ninakusubiri kwa hamu”.

“Oke, telemka chini. Tuko hapa duka la kahawa pamoja na Veronika”.

Oh, amekwisha wahi namna hii?”.

“Sana tena”.

“Oke nakuja sasa hivi”.

“Haya tunakusubiri”, nilimjibu na kukata simu.

“Oke Tom asante sana”, nilimwambia kijana wa mapokezi.

“Asante mzee karibu”, alijibu Tom.

“Asante niko hapa duka la kahawa”.

Niliporudi nilikuta vinywaji tayari.

“Yupo?”, aliuliza Veronika.

“Yupo, anakuja sasa hivi”, nilimjibu.

Haukupita muda Sherriff alitokea na kuja moja kwa moja mezani kwetu. Tulisalimiana akavuta

kiti na kuketi. Mtumishi aliyekuwa anatuhudumia alipomuona alikuja mara moja.

“Mzee nikusaidie nini?,” alimuuliza Sherriff.

“Kuna maji ya nanasi?”.

“Ndio, yapo”.

“Haya niletee hayo, lakini weka barafu nyingi, maana si joto hili”.

“Bila ya wasiwasi mzee”.

Mtumishi alipoondoka tulikaa kimya tunatazamana kwanza kila mtu anashindwa kuanza

mazungumzo. Veronika aipoona hivi akatabasamu kisha akasema. Sherriff wewe kidogo uko nyuma

ya habari, lakini nitakueleza kwa kifupi ili kukuweka pamoja nasi katika habari zinazotuhusu

wote”.

“Nitakushukuru”, alijibu Sherriff.

“Willy nimemweleza yote tunayojua juu yake, na jambo la kushangaza ni kwamba na yeye

anatufahamu sisi huenda kuliko tunavyojifahamu wenyewe”.

“Usitie chumvi”, nilimuasa.

“Ala!”, Sherriff alitamka kwa mshangao mkubwa. “Kama ni hivyo basi ni vizuri sana. Kwani

wote sasa tunafahamiana misimamo yetu. Unajua mimi nilishangaa sana usiku pale uwanja wa

ndege. Waandishi wote wengine wa magazeti mbali mbali ulimwenguni tuliokuja nao wamekataliwa

kuingia hapa nchini, na tumewaacha uwanja wa ndege wakilalamika vibaya sana wakiomba kuonana

na mabalozi wao, lakini sisi tumeruhusiwa kwa urahisi sana, kitu hiki kilinishangaza sana

nikahisi lazima huu utakuwa mpango wa Willy. Sasa nimeamini kabisa. Uongo au kweli”.

Sherriff aliuliza huku akiniangalia.

“Bila shaka niliwaahidi toka tukiwa Freetown kuwa mnakaribishwa kwa dhati Tanzania, sasa

nimetimiza ahadi yangu”.

“Asante sasa”, Sherriff alijibu.

“Mimi naamini unajua tumekuja kwa ajili gani, na vile vile naamini likizo yako imekatishwa

kwa ajili sababu hiyo hiyo tuliyoijia sisi”, Veronika aieleza huku macho yake yaking’aa

kuonesha kuwa sasa tulikuwa tunazungumza kikazi.

“Sawa, endelea”, nilimjibu.

“Mimi naonelea tungeliungana na wewe, kwani wewe ukiwa mwenyeji itakuwa kazi rahisi kwetu

kuweza kupata habari. Sijui wewe unaonaje?”.

“Kwa taarifa yenu lazima niwaeleze kuwa tukio hili lililotokea si la kawaida. Mnaweza kuwa

mmeshiriki katika mambo ya hatari sana kama vile mambo ya vita, lakini lazima

niwatahadharishe kuwa kutafuta habari za aina yoyote zinazoweza kufichua kundi lililofanya

ujahiri wa hari ya juu ni hatari sana kwa maisha yenu kuliko hatari yoyote mliyokwisaha

kuikabiri. Nadhani mmenielewa. Ningewaomba ili kuponya maisha yenu muwe watoto wazuri,

muachane kabisa na kuuliza uliza habari za tukio hili”.

“Kabla hatujatoka ofisini kwetu London, tumetahadharishwa kama unavyotutahadharisha sasa,

lakini tulikaa tukaamua kuwa tutaendelea; Lolote baya litakalotupata tutakuwa tumetoa damu

yetu kwa ajili ya ndugu zetu. Kwani sisi tunaamini watu waliofanya kitendo hiki si watu

wengine bali ni mabeberu wapinga ukomboni wa kusini mwa Afrika”, alijibu Sherriff kwa nia

moja.

“Kama uamuzi wenu ni huo basi tutashirikiana kwa kadiri tutakavyoweza”.

“Mlikuwa na nia ya kuanza kutafuta habari tokea lini?”.

“Tokea sasa hivi kama unaweza kutupa fununu tuanzie wapi!”, Sherriff alijibu.

Kwa vile katika mpango wangu wa upelelezi nilikuwa nimepanga kuwatumia ndugu hawa. niifurahi

sana kuona kuwa mambo yaikuwa yanakwenda kama nilivyopanga. Hivyo niliamua kuwaeleza kwa

kirefu maelezo aliyokuwa amenieleza Chifu.

“Ili kuwaweka sawasawa ninyi katika picha ya tukio hili mtakuwa wageni wa kampuni yangu. Kwa

hiyo mimi naona tangia sasa nitakuwa ni wakala wa gazeti lenu, kwa kufanya hivi nitapata

kisingizio cha kutembea na kupeleleza na nyinyi mkiwa kama wateja wangu; nafikiri

mmenielewa?”.

ITAENDELEA

Njama Sehemu ya Pili

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment