Pasipoti Ya Gaidi Double Agent Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE
Simulizi : Pasipoti Ya Gaidi ‘Double Agent’
Sehemu Ya Nne (4)
Kamanda Amata aliingia katika Jiji la Beira, jiji la pili kwa ukubwa huko Mozambique. Usiku huo, watu wachache walikuwa uwanjani kuwapokea ndugu na jamaa zao. Akaelekea kwenye maegesho ili kupata huduma ya usafiri.
“Tax hii hapa mzee!” sauti ya kijana mmoja ikamwambia kutoka nyuma, akasimama na kumtazama, alikuwa amevaa sare maalumu ya dereva tax pale Beira. Kwa jicho la haraka akamtazama na hakuuona uovu wowote machoni pake. Wakaongozana mpaka kwenye moja ya taxi zilizojipanga hapo nje wakaingi na kuondoka zao.
“Tivoli Hotel tafadhali…” Amata akamwambia yule kijana huku akijiweka vyema katika kiti cha nyuma.
“Ok. Ni mara ya kwanza kufika Beira?” akauliza yule dereva.
“Ndiyo, hapa sijui lolote kuhusu Beira itamkuta mwenyeji wangu pale,” Amata akajibu.
“Karibu sana Beira, jiji la raha zote, wanawake wazuri na watamu utawakuta na kila aina ya starehe watakupa…”
“Beira mnapenda sana Starehe eeenh! Kazi hamtaki kufanya,”
“Tunafanya, si ndio kama hivi,” akadakia kujibu yule dereva.
Yule dereva akaicha barabara ya Uwanja wa ndege na kukamata ile ya Masano Di Amori iliyomfikisha katika hoteli hiyo ndani ya dakika kumi tu. Akalipa dola kadhaa kwa safri hiyo na kuiacha ile tax iende zake.
Hoteli Tivoli katika jiji la Beira, pembezoni mwa barabara ndogo ya Bagamoyo, kilomita kumi na moja kutoka uwanja wa ndege.
“Bem-vindo Trivoli Hotel…” sauti ya kike ilimkaribisha Amata katika hoteli hiyo.
“Muito obrigado,” aliitikia kwa Kireno safi akimaanisha ‘asante sana’. Mbele ya kaunta alijaza fomu kwa jina la Mr. Spark na namba za Pasipoti yake zikanukuliwa.
“Quarto trinta e cinco!” kijana wa mapokezi alimwambia mwenzake kuwa ampeleke chumba namba thelathini na tano, naye akamwongoza. Amata aliitazama saa yake ilikuwa ikikaribia alfajiri, akaingia maliwato na kuoga kisha akautafuta usingizi kwa dakika kadhaa. Majira kama ya saa nne hivi asubuhi, aliamka na kujiweka sawa tayari kwa kuanza kumtafuta huyo mtu aliyetumwa kwake. Akaipachika sawia bastola yake kiunoni na kuteremsha fulani yake ndefu ya maikono mirefu. Jinzi yake iliyomkaa vyema ikionesha ni jinsi gani kijana huyo alikuwa ana misuli ya kimazoezi. Akateremka na kuingia mgahawani kupata kifungua kinywa. Juice na Mihogo ya kuchemsha vilimkuta mezani, chakula cha kwetu akawaza na kutabasamu moyoni.
Ndani ya mgahawa huo alikuwa peke yake, baada ya kumaliza kupata kifungua kinywa alitoka taratibu nje ya hoteli hiyo, miwani ya jua ikawekwa usoni na kofia kubwa, pama, ikatua kichwani na kijana huyo akapata mwonekano mpya.
“Nasikia jamaa katuma mtu wa kunimaliza!” Hernandez akawaambia vijana wake, “Na huyu mtu ametua hapa jana usiku kutoka Maputo, nasikia amemkodi kutoka Congo DR,” akaongeza.
“Lakini kiongozi, tumekaa Airport mpaka abiria wa ile ndege wamekwisha, hatukuweza kumwona, tumetega pale hotelini Trivoli hatujaona mtu wa sura hii,” mmoja wa vijana wake akamwambia.
“Sina uhakika kama hajaja, kwani Forbess kanihakikishia kuwa mtu huyo kapanda ndege hiyo niliyokwambia, anaitwa Moya Mampasi raia wa Congo,” akazidi kudadavua.
“Mh!” mmoja akaguna, “Mkuu, sasa hii ni hatari kubwa kama kaingia tu hatujamwona unafikiri hatoweza kufika hapa bila kuonekana?” akauliza.
“Hilo ndili nililotaka kulisema, nataka muhakikishe ulinzi kila kona ya hii nyumba, asiingie mgeni yeyote humu ndani mpaka ruhusa yangu, tena baada ya ukaguzi wa hali ya juu,” Hernandez akawaambia kisha akanyanyuka na kuingia ndani ya ofisi yake ndogo na kufuatwa na kijana mmoja mwenye mwili mkubwa, wakajifungia ndani.
“Sikiliza Versil…. Nahitaji kuondoka, kuna sherehe ya kuzaliwa mtoto wa La Peruz kule kisiwani, hakikisha usalama wa hapa kuanzia kesho saa saba mchana sintokuwepo,” akaacha maagizo.
“Sawa mkuu, nakuhakikishi hakuna litakaloharibika,” akajibu na kutoka nje huku akimwacha Hernandez peke yake.
Kama kawaida, wageni mbalimbali walikuwa wakifika katika himaya ya tajiri huyo, Hernandez mwenye asili ya Ureno, lakini walishangaa kwa jinsi kulivyokuwa na upekuzi wa hali ya juu sana tofauti na siku nyingine zote.
“Kwani leo mbona mwatukagua sana?” aliuliza kijana mmoja mtu wa Pemba.
“Vita dhidi ya ugaidi,” akajibiwa.
Kamanda Amata aliegesha gari gari yake katika barabara ambayo makazi ya tajiri huyo yalikuwapo. Mtaa wa Krusse Gomes kitalu namba 129, ndipo liliposimama hekalu la tajiri huyo, hakushuka garini bali aliangalia kutoka mbali watu wakiingia na kutoka katika jumba lile. Ana biashara ileile au? Akajiuliza pasi na jibu lolote. Akiwa katika mawazo hayo, akamwona binti wa kadiri miaka ishirini na tano mpaka thelathini hivi, yule binti alitoka kwenye geti la ile nyumba na kuvuka barabara kisha akaingia katika gari yake na kuondoka. Amata naye akawasha gari na kumfuata.
Gari ya yule binti ikaingia ndani ya wigo wa Chuo Kikuu cha Katoliki pale Beira, haikuwa mbali na ile Hoteli ya Tivoli, naye akaingia taratibu akaegesha gari mahali fulani, akateremka na kufunga mlango. Yule binti moja kwa moja kwanza akaingia katika duka la vitabu.
“Bingo” akajisemea kwa sauti ndogo kisha akavuka ujia mmoja na kuingia ndani ya duka lile. Katika shelfu kubwa zilizojaa vitabu, Amata alisimama nyuma kidogo ya msichana yule akiangaliza vitabu kwa uongo na kweli.
Akamtazama akichagua kitabu, alipouliza bei ikawa juu sana kiasi kwamba binti huyo hakuweza kumuadu kwa muda huo.
“Basi nitakuja kununua kesho, usikiuze tafadhali,” yule binti akamwambia muuzaji.
“Usaijali nitakuwekea,” akajibiwa. Amata akarefusha mkono na kukichomoa pale kilipo, yule binti alipoona hivo akageuka na kugongana macho na kijana huyo, akashusha pumzi na kumtazama.
“Kaka usikinunue nimekiweka oda!” akalalamika.
“Sikinunui bali nakununulia,” Amata akajibu na kumfanya mrembo yule kutabasamu. Akachomoa noti kadhaa za Kimarekani na kukabidhi kaunta huku akiwa ameshika kitabu kile, alipolipia akamrudia yule mwanadada.
“Asante sana kaka, una roho nzuri sana ubarikiwe!” akamwambia Amata.
“Usijali, warembo kama ninyi inabidi mtunzwe,” kanyosha mkono na kuuvuta mkoba wa huyo msichana akamwekea kile kitabu kisha akamuaga na kumwacha msichana huyo akimkodolea macho huku akiuma kidole cha shahada cha mkono wa kulia.
Moja kwa moja aliingia ndani ya gari yake na kuondoka mpaka hotelini kwake, mbele ya hoteli hiyo, alipita taratibu sana akitazama waliopo nje na maegeshoni, nyele zake zikamsimama na mwili ukamsisimka, hakuna usalama akawaza na kupitiliza.
Beira Bay Café
Ndani ya mgahawa huo, Kamanda Amata aliketi katika moja ya kona akitazama pande zote na kuona kila aingiaye na atokaye. Akiwa anapata kinywaji alimuona mzee mmoja akiingia ndani ya mgahawa huo. Yule mzee alitembea kwa mwendo wake wa kizee na kuifikia meza aliyokuwa ameketi Amata, akavuta kiti naye akaketi.
“Koh! Koh! Koh! Mwanzo mzuri Kamanda!” yule mzee akamwambia. Amata akashtuka kusikia jina lake likitamkwa na mtu huyo tena kwa ufasaha kabisa, “Usishtuke, tulikutana Arusha na sasa tumekutana Beira, nilijua utafika Beira, kwani ufumbuzi wa swala lako upo hapa, uwe mwangalifu, epuka sana wanawake, adui yako anatumia wanawake kukusanya habari,” akazungumza yule mtu huku akinyanyuka na kuondoka. Amata hakumsemesha bali alimtazama tu akiishia.
Alipoinua saa yake muda ulikuwa umekwenda sana, akatoka na kuwasha gari na hapo nje hakumwona yule mzee. Akaondoka zake na kurudi kulekule katika mtaa wa Krusse Gomes, mara hii akaegesha gari upande mwingine na kubaki ndani yake. Hakuruhusu jicho lake kusinzia ili aone anayeingia na kutoka katika nyumba ile ya Hernandes. Baada ya saa kama nne hivi, aliiona ile gari ya yule msichana ikiwasili na kufunguliwa geti kabla ya kumezwa na jumba hilo la kifahari. Akajiweka sawa, akachomoa simu yake kubwa na kuwasha program fulani kisha akiweka vifaa vya masikioni.
Kupitia kifaa hicho aliweza kusikia mazungumzo mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea ndani ya jumba hilo, alisikia mipango anuai iliyopangwa na Hernandez na vijana wake.
“Ko! ko! Ko!” sauti ya kugongwa kioo cha gari ikasikika. Amata akageuka na kukutana uso kwa uso na walinzi wa eneo hilo waliokuwa na mbwa.
“Unafanya nini hapa?” mmoja akamwuliza.
“Nimechoka tu afande nikaona niegeshe gari nilale kidogo,” akajibu huku akitazama saa yake ambayo ilimwonesha saa kumi na mbili jioni ikielekea saa moja. Akawasha gari na kuiondoa mahali pale, alipofika umbali wa mita hamsini ile sigino yake ikaanza kuwa dhaifu na mwisho kupotea kabisa. Hakuweza kusikia tena mazungumzo yale.
Kamanda Amata alitegesha kifaa kidogo sana ndani ya mkoba wa yule binti baada ya kukitumbukiza kile kitabu katika mkoba wake. Alipiga ngumi kichakani kwa tendo hilo kwani hakutegemea sana kuwa binti huyo angerudi pale lakini aliona potelea pote, ngumi yake haikuwa tupu kwani binti yule alikuwa ni mmoja wa wanafamilia wa Hernandez.
Nilichokipata kinatosha sana tu, akawaza huku akiendesha gari yake kuelekea hotelini. Akaegesha gari na kuteremka, harakaharaka akaelekea chumbani kwake. Kabla hajafungua mlango alitulia kwanza na kuangalia katika tundu la ufunguo, akagundua ndani kuna mtu au alikuwapo mtu, kwa maana alama aliyoiweka ya kutengeneza kifundo cha uzi na kukipachika katika tundu hilo ingemjulisha kama kuna mtu aliyeingia au la. Akasita kidogo, akainua bastola yake na kuiweka sawa kisha akapachika ufunguo wake na kufungua mlango, akausuikama ndani lakini yeye hakuingia akasubiri kidogo kama sekunde kadhaa hivi, akiwa masikio walu, akasikia kamlio ka bastola inayoondolewa usalama, akajua mtu huyo kwa vyovyote yuko upande wa kushoto, akaingia ghafla na kuruka sarakasi ya mtambaa panya alipotua alimimina risasi upande ule aliofikiria, hakukosea, jamaa mmoja aliyejibanza kwenye kona ya ukuta nyuma ya ua alianguka na ua lake huku damu zikimvuja kifuani. Amata akajiinua kumtazama yule marehemu lakini alijikuta akipigwa na kitu kama gongo miguuni mwake, mkono ulioshika gongo hilo ulijitokeza kutokea uvunguni.
Kumbe hayuko mmoja, akawaza. Nukta yiyohiyo akajikuta akifungwa kamba miguuni, kamba zile zilikuwa zikizunguka kwa ustadi sana, akajaribu kujinasua lakini alijikuta anachelewa, zikavutwa na yeye akaanguka chini, akajaribu tena kujinasua, bastola yake ikapigwa na kuanguka kando, alipojaribu kuirukia alishindwa kwa kuwa miguu ilikuwa imefungwa kwa kamba madhubuti. Vijana wawili wakajitokeza kutoka uvunguni, wamevalia nguo nyeusi na kuficha sura zao, wakiwa wamebakisha macho tu kuonekana. Ninja, akawaza haraka.
“Aaaaa ha ha ha ha !!! umepatikana Moya Mampasi, hata kama ulijaribu kujificha kwa jina na muonekano, umepatikana,” mmoja wa wale maninja akatoa kauli hiyo ambayo Amata aliona wazi kuwa bado hawajamgundua.
Wakamchukua na kutoka naye nje kwa kupitia dirishani, wakateremka naye kitaalamu kwa kamba mpaka chini na kumtupia garini kisha wakaondoka zao. Hakuna mtu aliyegundua tukio hilo.
Kamanda Amata alitupwa ndani ya chumba chenye giza nene ambalo hakuweza hata kuona umbali wa sentimeta hamsini, akafungiwa humo akiwa na kamba zake. Baada ya kama nusu saa hivi mlango ulifunguka na watu kadhaa wakaingia lakini hakuweza kumwona hata mmoja. Taa kali ikawashwa na moja kwa moja ikammulika usoni na kumpa usumbufu mkubwa. Kutokana na mikono yake kufungwa kwa kamba hakuweza kabisa kujizuia zaidi ya kufumba macho tu.
“Mr. Moya Mampasi….” Aliita kwa upole mtu mmoja aliyeonekana kuwa ni mtu mzima, mustachi uliotulia juu ya mdomo wa juu ulimea vizuri na kuionesha afya ya mtu huyo bila kuhoji, “najua umetumwa kwa kazi gani hapa Beira, lakini swali ni nani kakutuma nataka unambie ukweli,” akauliza huku akitembea huku na kule ilhali vijana wake wane walioshiba miosuli wakiwa kando wameifumbata mikono yao vifuani.
“Nimetumwa na adui yako, Mr. Bocca! Wewe kwa nini umemfanyi mabaya namna hiyo ilhali yule bwana ni swahiba wako?” Amata akajibu na kurusha swali.
“You are foolish! So foolish!” Hernandez alitamka akimaanisha Amata ni mpumbavu kwa hayo anayoyasema.
“Hakuna mtu aliyewahi kuzuia juhudi hizi, ugomvi wangu mimi na Bocca huwezi wewe kuumaua, mbona nimekukamata kama kinyonga akamatavyo mdudu mdogo?” akauliza kwa dharau. Amata muda wote huo hakuonesha ulegevu au uoga alijua mafunzo yao hasa katika Art of War inayosema, onesha una nguvu pale unapohisi huna nguvu.
“Nimetumwa kukuua wewe na La Peruz….”
“Ha! ha! ha! ha! Muoneni mjinga huyu, nimekufunga kamba halafu unasema utaniua…”
“Tena nitakuua kwa kisu,” Amata akamalizia.
“Hebu mtieni adabu halafu mpelekeni bandarini niondoke naye kesho tukamkate kichwa La Peruz,” Hernandez akawaagiza vijana wake nao wakaanza kumsulubu huku bado akiwa amefungwa kamba. Vipigo vya nguvu vilishuka mwilini mwa Amata mpaka akalegea kabisa na kuwa hoi pale chini.
“Safi sana, mpelekeni bandarini, mfungieni mahali pazuri ili kesho mapema niondoke naye kama nilivyosema,” alipomaliza kusema hayo, akaondoka mle ndani na Amata akainuliwa juu juu mpaka katika buti ya gari na wale vijana wakaingia garini na kuondoka naye.
Simu ya Bocca ikaita kwa fujo, akiaendea na kuinyakuwa, akili yake ilimpanga kusikia habari nzuri lakini haikuwa hivyo.
“Ugonvi wangu na wewe hauwezi kutatuliwa na mtu mwingine yeyote, nimemkamata kibaraka wako, Moya Mampasi, na nitahakikisha anakufa kifo kibaya kuliko vyote vilivyowahi kutokea hapa Mozambique…” kisha akatulia. Bocca akashusha pumzi ndefu huku sura yake ikiwa imejaa jasho.
“Umekwisha, mbinu zako zote tunazijua…” Hernandez akamalizia na kukata simu. Bocca akajitupa juu ya kochi huku sura yake ikiwa imesawajika kwa mawazo.
“Vipi boss?” mlinzi wake akamuuliza.
“Moya yuko mikononi mwa Hernandez,” akajibu huku akitokwa jasho, akajilaza juu ya kochi hilo, yule mlinzi akabonyeza kengele ya dharula na dakika hiyohiyo waliingia wauguzi wawili kumsaidia, presha ilikuwa inashuka.
“HUmu ndani tuna mole?” yule mlinzi aliwaambia wenzake baada ya kuwaita pembeni, “Kwa sababu haiwezekani kila mission ikipangwa dhidi ya wale nyau inashindikana, na kwa jinsi inavyoshindikana sasa Napata wasiwasi kuna mtu anatoa siri huku anapeleka kule. Nakuambieni akijulikana lazima akatwe kichwa na nyama yake tuitalisha mbwa!” akamalizia na kuondoka eneo lile moja kwa moja mpaka chumba alichohifadhiwa Bocca.
“Carlos!” Bocca akaita kwa sauti ya upole.
“Yes Boss!”
“Hawa jamaa kwa nini wanatuzidi akili kila wakati?”
“Boss, kwenye himaya yako lazima kuna mamluki, kwa vyovyote kuna watu au mtu sio wetu na ndiye apelekaye taarifa hizi,” Carlos akaeleza.
“Mbona mambo haya nayafanya kwa akili na siri sana?” Bocca akaonesha wasiwasi.
“Boss hata huyo mtu atakuwa anadukua taarifa zako kwa siri na kwa akili hivyohivyo,” Carlos alieleza.
“Mtafute na ukimpata hakikisha unaniletea hapa!” akamwambia. Carlos akatoka ndani ya kile chumba na kumwacha Bocca na wale wauguzi walioingia punde tu baada ya kijana huyo kutoka.
SIKU ILIYOFUATA
Kisiwani – La Peruz
BOTI YA KIFAHARI ILIKUWA MAJINI ikikikaribia kisiwa hicho, mabaharia na wafanyakazi walikuwa wamesimama nje wakikitazama kwa mbali jinsi kinavyopendeza. Lakini ndani ya chumba fulani katika upande wa chini wa boti yiyo hiyo mtu mmoja alikuwa amefungwa kwa kamba na kutupwa katika sakafu. Chumba kidogo kilichotawaliwa na giza kila kona. Kamanda Amata kutoka pale alipokuwapo akaisikia komeo la mlango wa chumba hicho likifunguliwa, akajilaza kimya kwani mwili wake ulikuwa na maumivu makali kutokana na kile kipigo cha usiku uliotangulia.
“Hey! We mpumbavu! Tumefika kisiwani, elewa kwamba kaburi lako ndiyo lipo huku, ndugu zako wa Congo watatafuta mabaki ya mwili wako na wasiyapate, mtoeni nje,” vijana wa kazi wakamnyanyua Amata na kumtoa nje ya boti ile.
Nje kwenye deki, akalazwa chini kwani hakuwa na uwezo wa kusimama, Hernandez na binti yake wakafika eneo hilo, kinywani akiwa na cigga linalofuka moshi. Mshtuko mkubwa ulimpata yule binti alipogongana macho na Amata.
“Dad! Huyu mtu kufanya nini?” yule binti akauliza.
“Huyu, huyu nataka kumuua sasa, muda umefika!” Hernandez akamwambia yule binti.
“Oh no! Dad huyu ni rafiki yangu, ndiye niliyekwambia kuwa aliniongezea pesa kununua kile kitabu,” akaeleza.
“Ndiyo huyu? Aaaaaaaa!” Hernandez akang’aka….
Kila mmoja akapigwa na butwaa, akawaangalia vijana wake na kisha akamtazama binti yake kwa jicho kali.
“Paaaaaaa!!” kofi kjali lilitua shavuni mwa yule binti, akaanguka kando.
“Nilishakwambia, na nikwambie mara ngapi kuwa sitaki uhusiano wowote kati yako na mwanaume?” akaongeza kwa ukali, “Kwa nini unaniletea matatizo katika nyumba na kazi zangu we msichana?” akaongeza swali. Yule binti akabaki analia huku akiinuka kwa kujizoazoa.
“Lete kile kitabu!” akamwambia mmoja wa vijana wake, kile kitabu kikubwa kikaletwa.
“Ulishindwa nini kunambia baba yako kuwa umepungukiwa na pesa? Ukakubali kuongwa na mwanaume huyu! Huyu ametumwa kuniua baba yako, tazama alichokufanyia…”
Hernandez akafungua kile kitabu na katika kurasa fulani kulikuwa na kidubwasha kidogo cha kunasa sauti, kila mmoja akashangaa,
“Unaona! Unaniletea nini ndani mwangu, pumbavu sana wewe, siri na mambo yote tuliyoongea huyu jamaa akayasikiliza. Toka hapa, potea!” akamfukuza yule binti, naye akakimbilia ndani ya boti hiyo.
Muda mfupi tu kile chombo kikaegeshwa katika gati ndogo ya kile kisiwa, Drotone La Peruz, Tajiri mkubwa sana rafiki wa Hernades alikuwa tayari kumpokea.
“Karibu sana komredi,” akamkaribisha huku tayari mhudumu keshafika na chano yake yenye bilauri kadhaa za pombe kali.
“Asante sana,” wakakumbatiana, “Nimekuja na surplies”.
“Surplies! Ha! ha! ha! ha!” Drotone akacheka huku akimpigapiga mgongoni rafiki yake Hernandes.
“Hey! Mleteni huyo!” akawaambia vijana wake. Kamanda Amata akatolewa ndani akiwa anaburuzwa huku zile kamba bado zikiwa mwilini mwake.
“Huyu ni nani?” Drotone akauliza.
Hernandes akapunga mkonoi wake kumwita pembeni, “Sikia, huyo jamaa katumwa na Bocca kuja kuniua na nilivyomhoji kanambia kuwa katumwa pia kukuua wewe!” akaeleza.
“Bocca! Huyu Bocca anadiriki kufanya hivi, mara ngapi nimemuonya? Hajakoma, sasa naitoa roho yake baada ya kumkata huyu marehemu,” akamtazama Amata pale chini alipotupwa kama furushi.
“Draco! Besta! Compli…”
“Yes. Sir!” vijana hao wakaitikia.
“Mchukueni huyu firauni, mpelekeni shimoni, mumtie disprin nakuja hukohuko kukata koo lake kwa mkono wangu,” akatoa amri. Amata akaburuzwa kama awali kupelekwa ndani huku wengine wakitazama akiwemo yule binti wa Hernandes.
“Hana ujanja, mfungue kamba ili tumchape vizuri,” kiongozi wao mwenye tambio kubwa akawaambia, wale vijana wakamfungua kamba na kumsukumiza ndani ya chumba kipana chenye kila aina ya mateso kwa mwonekano.
“Aaaaa ha! ha! ha! Na sasa ni show time,” yule kiongozi akawaruhusu wale vijana waanze kazi yao. Wakamvamia Amata aliyekuwa pale chini, mara hii akiwa hana kamba mwilini mwake. Kitendo bila kutegemea, Amata alinyanyuka haraka na kuruka sarakasi miguu yake ikatua vifuani mwa wale jamaa wakaanguka chini na Amata akasimama wima. Waliponyanyuka wakamkuta TSA 1 yupo ngangali, konde moja zito likatua kwa mmoja wao akarudi chini, konde la pili likatua kwa mwingine yeye hakuanguka, akatuma konde zito, likadakwa na Amata, kwa haraka akageuka na ule mkono na kuuvunja, kisha akamnyanyu a na kumbwaga chini huyo mjinga. Yule kiongozi wao akachomo bastola na kufyatua risasi lakini Amata alikuwa amekwishahama eneo lile na zile risasi zikachimba ukuta. Amata akainuka na kupiga mguu wake chini, kisu kikali kikafyatuka na kuzama upande wa moyo wa yule kiongozi, akapiga yowe la uchungu na kuanguka chini kama mzigo. Amata akaruka kiufundi na kuinyakuwa bastola, akabingirisha na kupiga goti moja risasi mbili ziliwaondoa uhai wale vijana, pumzi zikawatoka.
Nje ya jumba lile, mlio wa hatari ukasikika, mmoja wa wale vijana kabla ya kufa aliminya swichi ya hatari iliyo ukutani mwa chumba hicho.
“What the hell is this?” akang’aka Drotone na kuinua simu yake ya upepo, akawapa taarifa walinzi wake waingie ndani haraka kuona kuna nini na wao wakafuatia nyuma.
“Acha ujinga wako jisalimishe, hapamupo kisiwani huwezi kukimbilia popote!” sauti hiyo ilimfikia Amata ndani ya kile chumba, akatoka na kufika kwenye korido, mbele yake kulikuwa na kijana mmoja mwenye bunduki, akainua bastola na kufyatu lakini haikuwa na kitu.
“Ha! ha! ha! ha! Umekwisha!” yule kijana akamwambia Amata na kujiweka sawa tayari kumllipua lakini alishangaa kwa kitendo kilichofanyika mbele yake. Amata alimrushia ile bastola ikampiga usoni na wakati huo, akakanyaga ukuta upande huu na kujikuma upande mwingine tayari akawa juu akitembea mithili ya buibui. Yule jamaa alifyatua risasi lakini zote zilipotea akajikuta akipokea pigo moja zito la shingo lililompeleka chini kimya. Akatua na kuichukua ile bunduki, sekunde hiyohiyo walitokea vijana wenye silaha na Amata akatumia SMG iliyokuwa mikononi mwake kuwasambaratisha kwa risasi huku akipita na kujificha upande mwingine.
Mmoja wa vijana wale alipoanguka, bomu la mkono likamtoka mkononi mwake na kubingirika sakafuni.
“Shiiit!” Amata akang’aka na kulinyakuwa, akalirusha kwenye chuma kingine kilicho wazi, lakini hakujua kama ndani ya chumba kile kulikuwa na mitungi ya gesi. Mlipuko mzito ukatokea ukafumua fumua lile jengo, Amata alifanikiwa kuruka katika moja ya dirisha na kutoka nalo nje lakini nyuma yake moto na moshi mzito vilifuata.
Kwa kishindo, akadondoka juu ya barabara akfuatiwa na vipande vya matofali, akabiringika na kujitupa kando, mlipuko mwingine ukatokea na kufumua sehemu kubwa ya ardhi. Amata akainuka na kukimbilia upande wa mbele huku akiwatafuta walengwa wake. Mlio wa boti ukamshtua, akarudi haraka upende ule alikosikia mlio ule na kuiona ile boti ikipondoka pale gatini. Wanatoroka! Akawaza, “Siwaachi,” akasema huku akiuma meno. Akatazama huku na kule kulikuwa na Speed Motorboat iliyotengenezwa kwa muundo wa pikipik, akachumpa majini na kuogela mpaka ilipo mashine hiyo, akakaa juu yake, akabonyeza swichi nayo ikaitika, akakunja kona na kuanza kuifuata ile boti kubwa kwa nyuma.
Drotone na Heranandes walikuwa ndani ya boti wakiondoka, pamoja nao alikuwapo binti wa Hernandes na vijana wengine waliokuwa wakifanya kazi katika boti hiyo. Wote wawili walikuwa kimya kabisa, Drotone aliona kwa mbali kisiwa chake kikiteketea kwa moto, pesa, utajiri na ndoto zake zilikuwa zikiteketea kwa moto na kubebwa ka moshi mzito uliokuwa ukiishia mawinguni. Donge la gadhabu na hasira lilimkaa katika kolomeo lake, alishindwa kulimeza, mwili ulimtetemeka. Mara mlango wa kuingia katika chumba hicho walichoketi ukafunguliwa na kijana mmoja aliyekuwa akihema akasimama mbele yao.
“Boss, jamaa anakuja!” akasema.
“What! Ina maana hajafa?” Hernandes akang’aka, kisha akasimama pamoja na Drotone La Peruz wkaenda kwenye chumba maalum kilicho juu ya boti hiyo na kuweza kumuona kijana huyo akiwa jirani tu. Heranandes akainua simu iliyofungwa ndani ya boti hiyo na ubofya namba fulani.
“Mlipueni kwa nini mnamwachia?” akawauliza wahusika.
“Sasa boss…”
“Sasa nini, fanya kazi,” akang’aka.
Nahodha wa ile boti hakuwa na ujanja ilimbidi aigeuze ile boti kwani mitutu yake ya ilikuwa mbele hivyo hakukuwa na ujanja zaidi ya kuigeuza na kumkabili Amata. Muda huo aliokuwa akiigeuza tayari Amata alikuwa amewafikia, akaigongesha ile Speed Motor Boat, akarushwa na kudondokea ndani ya boti hiyo. Hakutulia palepale, alibingirika na kuingia kwenye kiupenyo fulani na risasi zikatua hata kutoboa bati gumu lililojenga sakafu hiyo. Akajiweka sawa, akajitokeza ghafla na kumimina risasi akamuua yule kijana, kisha akakwea ngazi na kuelekea juu huku akitawanya risasi huku na kule na kuwapoteza watu kadhaa.
Chumba alichokuwako Hernandes na Drotone kilifungwa. Alipiga risasi lakini vioo vyake havikuingiza risasi. Ndani ya chumba hicho wale matajieri walikuwa wakicheka tu. Amata akatupa jicho na kuliona bomba la moshi akajua kwa vyovyote tanki la mafuta haliko mbali, kwa kutumi ile SMG mikononi mwake, akapiga risasi mfululizo eneo lile na mara mlipuko mwingine wa maana ukatoke, akajirusha na kutua ndani ya maji huku akishuhudia ile boti ikipasuka vibaya. Pande kubwa la chuma lilikuwa likimjia pale alipo, akapiga mbizi na kuogelea kwa ustadi sana na kuibuka umbali kama wa mita mia moja hivi.
MAPUTO
KIJANA MMOJA akaingia katika chumba cha Bocca na kuketi, akachukua rimoti na kuwasha luninga kubwa iliyokuwa imezimwa.
“Boss, tazama habari hiyo!” akamwambia Bocca, anaye akainuaka kutoka pale alipolala, akaeti, kilichoonekana katika luninga hiyo kilimpa faraja.
“Eeee! Moya Mapasi!” alijikuta akipiga kelele. Habari ya dharula ilikuwa ikirushwa kupitia Televisheni ya Msumbiji ikionesha tukio la kile kisiwa kulipuka na mali kuteketea vibaya, hawakusema nini chanzo cha moto huo ila walihisi tu inaweza kuwa gesi.
“La Peruz has fallen! Finally,” Bocca akasema kwa sauti ya taratibu hukuakiangalia kila tukio.
“Lakini Moya hapatikani kwenye simu,” yule kijana akamwambia.
“Hata kama atakuwa amekufa shauri zake, mimi tu nimefuarahi kwa kazi hiyo, na sasa mimi ni Mfalme,” akajisifu huku akionesha kutojali kama mtu aliyemtuma kafa au mzima.
“Twendeni, tukafurahie maisha,” akawaambia vijana wake.
“Lakini Boss wewe bado unaumwa!”
“Ugonjwa wangu umepona,” akajibu na kunyanyuka. Bocca aliwapigia simu rafiki zake na kuwaalika hapo Quiety Corner kwa ajili ya tafrija ya ushindi, nusu saa baadaye tayari watu kadhaa wa kadhaa walikusanyika kula na kunywa kando tu mwa Bahari ya Hindi na Ulinzi mkali ukiwa umewekwa.
7
UWANJA WA NDEGE MAVALANE
MAPUTO
NDEGE YA SHIRIKA LA AFRIKA KUSINI, iliegeshwa na kuzima injini zake, kisha mlango ukafunguliwa mara tu baada gari ya ngazi kufika na kuiweka ngazi hiyo mahali pake. Abiria wakatelemka na kati yao, mwanamke mmoja mfupi aliyevalia suti safi ya suruali, miwani nyeusi iliyoyaficha macho yake ilimfanya aonekane mrembo haswa. Akamaliza ngazi na taratibu akalifuata jengo la uwanja huo. Hakuonekana kuongea wala kuwa na uhusiano wa mtu yeyote, baada ya ukaguzi na kumaliza itifaki za mahali hapo, aliondoka na kutoka nje ya uwanja huo, akaelekea katika maegesho ya tax. Akiwa bado anaangazaangaza macho tax gani achukue, akajikuta akipigwa na kitu kizito kisogoni, akayumba na kuanguka chini. Akatapatapa na kujipindua chali, macho yake yakaona vivuli vya watu ambao hakujua idadi yao, watu wale walikuwa wakififia ndani ya giza la usiku, akapigana nalo lakini wapi akajikuta usingizini.
Wale jamaa wakamchukua yule mwanamke na kumtia kwenye buti la gari waliokuja nayo nakuondoka zao.
“Ana pasipoti nne sasa hatujuai ipi ni halali, hii ni ya Afrika Kusini anaitwa Sebeth Sebutwa na ndiyo aliyoingilia sasa hapa Mozambique. Hapa kuna nyingine, hii ni ya Congo DR inamtambulisha kama Mirabel Zubi Kabasele. Kuna hii ya U.S.A anaitwa Jenitrose McLaren…”
“Na ya mwisho…”
“Ya mwisho ni ya Kenya, inamtambulisha kama Magdalene Wanjiku,” kijana mmoja alimweleza bosi wake aliyekuwa ameketi huku miguu ikiwa juu ya meza na pombe kali ikiwa pembeni. Akashusha miguu chini na kupiga funda moja kubwa kisha akapiga pafu moja la cigar iliyokuwa kinywani mwake.
“Zote hizo nne hakuna hata moja ya ukweli,” akawaambia
“Atawadanganya wote lakini sio mimi Banginyana, mimi ni Kanali wa jeshi najua uongo wa aina hii, lakini maadam tumempata huyu anajua nani anayefanya naye kazi hapa,” akiwa katika kuongea simu yake ikaita, akaitazama, Bocca, akaiweka sikioni.
“Ndiyo komredi…”
“Fika hapa Quiety Corner kuna tafrija ya dharula, tumefanikiwa kuiangusha ngome ya La Peruz,” akamwambia kwa simu.
“Ok, ok, nakuja na pia tumemkamata nyoka mmoja alijificha uraia wake, huyu ni mmoja wa watu ninaowatafuta,” Banginyana akaeleza.
“Mleteni huku, kuna pango la wanyang’anyi tutamuhifadhi na atatupa siri zote,” Bocca akamwambia yule Kanali.
“Hey! Haya tia huyo mateka kwenye gari twende Quiety Corner,” akawaamuru na wale vijana wakamchukua yule mwanamke na kumtia garini akiwa bado yupo kwenye mzimio mzito.
Haikuwachukua muda kufika eneo hilo, wakamteremsha mzobemzobe yule mwanamke na kuelekezwa mahali pa kumweka.
“Hili ndilo pango la wanyang’anyi,” mmoja wa vijana wa Bocca aliwaambia wale watu waliomleta yule mwanamke. Bocca na Banginyana nao wakafika eneo hilo na kuhakikisha kuwa amehifadhiwa vyema, wakaacha vijana wawili wa kulinda eneo hilo wakati wao wakija tena nje kuungana na wageni wengine.
Katikati ya sherehe, Bocca alisimama…
“Mabibi na Mabwana, Bocca The Don kama kawaida yangu nimewaalika hapa kuungana nami katika sherehe hii ya dharula. Uzuri ni kwamba ninyi ni kama mimi ndiyo maana nikawaita kwani nitakalowaambia hata ninyi mtalifurahia. Leo kama mlitazama Televisheni ya Taifa mtakuwa mmepata habari juu ya lile lililotokea La Peruz…”
Aliposema hayo minong’ono ikatawala kila mmoja akiongea lake kumwambia huyu, Bocca akanyosha mkono juu na wote wakanyamaza.
“La Peruz has fallen!” akatamka na kuinua bilauri yake juu huku akishangiliwa na wageni waliohudhuria hafla hiyo, “Nyote mnajua ni jinsi gani tumekandamizwa na Drotone La Peruz lakini sasa zama zake zimepita, nilipata mtu ambaye ameweza kuinyanyasa ngome ile na kuisambaratisha kuliko matarajio yangu, sijui kama yeye amepona au la lakini hilo kwangu halina maana, ila nitakachosema tu ni Long live Moya Mampasi,” wakashangilia na kugonga bilauri zao huku wakiendelea kunywa na kutawanyika huku na huko. Banginyana akamvuta pembeni Bocca na kuteta naye jambo.
“Ndiyo!”
“Sasa huyu jamaa uliyemtuma huko unafikiri anaweza kuwa msaada kwetu?” akauliza.
“Kwa nini unauliza?”
“Sikia Bocca, unajua ngome yetu imesambaratishwa vibaya na hawa Watanzania na niko hapa kwa sababu namsaka huyo nyoka wao niliyekwambia…”
“Nikukatishe, una uhakika yupo hapa?”
“Bila shaka, kwa kuwa ananusa kama mbwa, kwa vyovyote anaweza kuwa hapa kwa kificho akimsaka Benzilahagi, lakini jambo zuri ni kuwa hajui kama niko hapa, na ninataka kumfundisha adabu, Mkuu wa wakuu anaihitaji roho yake. Sasa basi, huyu anaweza kuwa msaada katika mission yetu ya pili na tukamlipa pesa iliyotakata,” banginyana akaeleza.
“Ni kweli, kwa kuwa kazi yangu kamaliza, kama yuko hai lazima atafika hapa kwani sijakamilisha malipo yake,”
“Nitamsubiri nionane naye, lakini sasa ngoja nimwamshe huyu mwanamke,” akamaliza kusema na kujimiminia kinywani kile kinywaji chote kisha akaondoka na kuingia ndani ya lile jengo akifuatiwanna Bocca. Walipofika katika kile chumba wakapigwa na butwaa wote wawili, wakabaki vinywa wazi, wakatazamana. Mbele ya ule mlango kulikuwa na miili miwili ya wale vijana waliokuwa wakilinda pale. Banginyana akakimbilia mlangoni, akausukuma, uko wazi, mwanamke hayupo. Kwa hasira akapiga ngumi ukutani huku kauma meno, akamtazama Bocca.
“Ulitaka nimlete huku huyu mwanamke ili atoroke?” akamwuliza.
“Hapana walinzi wako wameshindwa kumlinda, we inawezekanaje mwanamke akawatoroka watu shupavu kama hawa?” Bocca naye akaja juu.
“Nitamsaka popote alipo!” akatoka ndani ya ile nyumba na kuchukua vijana wake, wakaingia garini na kuondoka.
Bocca alibakia akimtazama jamaa huyo akipotea kutoka katika lile jumba la kifahari ambalo nje yake kuna hoteli kubwa na nzuri yenye utulivu. Akarudi nje ambako bado watu walikuwa wakiendelea kuburudika, akawaita vijana wake wa ulinzi na kuwahoji kama wamemwona mwanamke huyo akitoka lakini hakuna aliyebahatika kwa hilo.
BEIRA
KAMANDA AMATA aliibuka katika pwani ya Beira Bay, baada ya kuogelea kilomita chache kutoka pale chombo chake kilipoishiwa mafuta baada ya lile sekeseke la baharini. Kwa hatua za taratibu alijivuta na kutulia katika moja ya majengo chakavu yaliyo kando kabisa ya eneo hilo, alijua kwa vyovyote mji huo haukumfaa tena kuishi na kichwani mwake alijua kwa kazi hiyo lazima atakuwa amemfurahisha Bocca na hapo atakuwa kajisogeza zaidi kwa wale anaowatafuta.
Aliinuka kutoka pale alipokuwa amejilaza kwa uchovu, akavuta hatua kuzunguka ukuta wa gofu hilo na alipokaribia kwenye kona akasikia sauti za watu waliokuwa wakiongea ndani ya jengo hilo, akasita ma kustulia kusikiliza. Lugha waliyotumia alishindwa kuielewa kwani iliuwa ni Kireno lakini cha kihuni zaidi. Kwa haraka haraka alijua kuwa hao walikuwa ni vijana wahuni tu, akazunguka na kuwaona wakicheza kamari na wengine wakijidunga sindano za dawa za kulevya. Akapita eneo hilo na mbele akakuta barabara kubwa yenye magari machache, akaifuata bila kujali kuwa amelowa au la. Hoteli aliyofikia haikuwa mbali na baharini hivyo aliweza kutembea mpaka hotelini.
Saa moja baadae hakuwa yule, ndani ya mavazi mengine, begi lake mgongoni aliamua kuuacha mji huo bila kuchelewa. Akitembea kwa hadhari kubwa barabarani maana alijua kama si polisi basi adui zake wangeweza kumkamata na kumfanya kitu kibaya na hilo hakutaka litokee wakati kazi yake bado haijakamilika. Akiwa njiani saa yake ikampa ishara kuwa kuna ujumbe unaingia, akauruhusu na kusimama kando ya nguzo moja barabarani hapo.
“Sina taarifa yoyote kutoka kwako, bado upo na roho yako?” ule ujumbe uliuliza. Moja kwa moja alijuwa kuwa ujumbe huo si wa mwingine bali Madam S. hakujisumbua kuujibu bali akaendelea na safari yake mpaka akafika Uwanja wa Ndege kwa kutembea kwa miguu tu kwa maana aliona ni salama zaidi kwake kufanya hivyo kuliko usafiri mwingine wowote. Haikumchukua muda kupata ndege ndogo ya kukodi ambayo ingemrudisha Maputo jioni hiyo. Macho yak eyalikuwa kwenye luninga iliyotundikwa ukutani katika jengo hilo la Uwanja wa ndege na habari iliyotawala ni shambulizi katika kisiwa cha La Peruz huku vyombo vya usalama vya Beira vikilitaja kuwa ni shambulizi la kigaidi na serikali imeahidi kufanya msako dhidi ya watu hao. Akainua mkono wake wenye saa na kuiangalia, saa kumi na moja kasoro robo. Nusu saa baadaye aliondoka Beira kwa ndege ndogo kurudi Maputo, hakutaka kuwasiliana na Bocca bali alitoka kusika moja kwa moja katika kasri la tajiri huyo, na kuhakikisha anafahamiana na maswahida zake ili afanikishe azma yake.
DAR ES SALAAM
MADAM S ALITULIA kimya ofisini mwake, kichwa chake kilionekana kusawajika kwa mawazo. Hakuwa na utulivu hata kidogo, mara alikaa mara alisimama. Kutokana na kazi nyingi zilizoikabili ofisi yake siku hizo alijikuta anapitisha siku mbili au tatu bila kupata lepe la usingizi. Akiwa katika lindi la mawazo kengele ndogo ya mezani kwake ikatoa mlio fulani naye moja kwa moja akajua anayegonga mlango huo ni mmoja wa vijana wake, akauruhusu ufunguke, hakukosea, Chiba wa Chiba aliingia katika ofisi hiyo ndogoliyopo jirani kabisa na ofisi za Hazina katikati ya Jiji la Dar es salaam.
“Karibu sana Chiba!” akamkaribisha huku akimpa mkono.
“Asante Madam, nimerudi,” akajiu na kuketi kitini.
“Pole na kazi na pole na safari,”
“Asante sana, nashukuru kazi imekwenda sawa na kama ulivyopata majibu,” Chiba akajibu.
“Ndiyo majibu yote nimeridhika nayo na tayari yamefika panapohusika. Nashukuru sana kwa hilo lakini kabla hujatulia wala kupumzika, kuna kazi nyeti sana nataka nikupe uifanye,” Madam akamwambia Chiba.
“Ndiyo wajibu wangu Mkuu!”
“Vyema!”
“Hakikisha unampata Kamanda Amata, nataka nijue yuko wapi kwani tangu ameondoka sijapata taarifa sahihi,”
“Lakini si amekwenda kwenye operesheni kule Maputo?”
“Ndiyo, sasa umtrace na ujue yuko kona zipi na anaendeleaje ikiwezekane apatiwe msaada wa kibinadamu,” Madam akamwambia na Chiba akakubali kazi hiyo mpya na kuianza mara moja.
Ndani ya chumba chake kidogo kilicho katika ofisi hiyo ya Madam S palikuwapo kompyuta moja aliyopenda kuitumia. Akaiwasha na kuanza kumtafuta Amata p[opote alipo kwa kutumia GPS kwa kuwa alikuwa ameunganishwa kwa kudungwa kidubwasha ambchi huweza kusafirisha taarifa zozote zile kuifikia ofisi yake. Baada ya kompyuta hiyo kufunguka, moja kwa moja aliliita bara la Afrika, akaitafuta nchi ta Msumbiji na kuingiza namba fulani katika sehemu maalumu ya kazi hiyo kisha akasubiri. Zile tarakimua zikajizungusha takribani sekunde thelethini hivi na zilipotulia zilitengeneza uwiano ambao Chiba aliuelewa nini maana yake.
Chini ya zile tarakimu kulikuwa na maneno mawili, GO na CANCEL, akabofya kwenye lile la kwanza na kuiruhusu kompyuta hiyo ifanye kazi yake. Ishara mbili zikaonekana zikiwakawaka, moja kwa moja akelewa, gari aliyokuwa akiitumia Amata ipo Maputo na yeye mwenyewe yupo Beira, akaandika pembeni na kunza kujaribu kumuunganisha kwa mawasiliano lakini bado ilikuwa ngumu. Akasubiri wakati mzuri ambao angeweza kumuunganisha, kumbe wakati ambao alijaribu kumuunganisha, Amata alikuwa tayari ndani ya ndege kwa kuondoka hivyo ikawa ngumu kwa mawasiliano maana alitakiwa kuzima kila kifaa cha mawasiliano kuepusha muingiliano na mawasiliano yale ya ndani ya ndege hiyo.
Madam S bado alikuwa ameketi katika kiti chake, akivuta faili hili na kulisogeza lile, akifunua lile na kulifunika hili ilimradi tu alikuwa ametingwa mezani kwake. Chiba alifika na kuketi meza ya mbele yake.
“Vipi?” Madam akauliza.
“Yuko Beira, lakini nashindwa kumpata kwa mawasiliano,”
“Yupo sawa au kuna shida?”
“Nafikiri yupo sawa lakini nitakuwa na uhakika zaidi baada ya kumpata kwa zile njia zetu,” Chiba akasema.
“Ok, kwa sababu kama vipi tumwongezee nguvu, nilifikiri labda Dr. Jasmine aache ile operesheni yake kwa muda asogee pale kwa lolote linaloweza kuudhuru mwili wake, maana nimeona kuwa kundi analopambana nalo si la kuchezea na kwa maelezo yake ya awali alinambia kuwa ili kumpata adui lazima aingie ndani ya mtandao unaomlinda…”
“Yaani awe Ndumilakuwili?” Chiba akamkatiza.
“Yap!”
“Aaaa lakini namwamini Kamanda hawezi kukosea na huwa hakosei, kama kaupanga mpango namna hiyo naamini mpaka sasa atakuwa tayari ni mmoja wao,” Chiba akaeleza.
“Sawa basi naomba nifaye hivi, wewe uende Maputo, ukahakikishe unazijua nyendo zako na kunipa taarifa zote bila yeye kujua kama upo hapo,” Madam S akamweleza Chiba.
“Madam! Sasa mi nitajua kava sura gani huko aliko?”
“Unajua Chiba usitake kuniuzi, ina maana hujui jinsi ya kumfuatilia mtu? Haya nimemaliza, nikiweka nukta mwisho wa kauli hii, ujue tayari upo Maputo na si vinginevyo”.
Chiba hakuwa na la kusema, alinyanyuka na kusimama kando, madam S akasimama wima na kumwangalia kijana huyo ambaye hata begi lake lililkuwa haijashushwa garini.
“Wewe ni TSA 2 na hii ni kazi yako, nenda na unipe ripoti zote hakikisha nyendo zako hazijulikani na yoyote yule,” akamaliza.
“Sawa Mkuu, Im in!”
“Haya, ondoa mkia wako hapa!”
Chiba alirudi garini na kuondoka zake, kwanza kabisa alielekea nyumbani kwake eneo la Msasani kwa Mwalimu kubadilisha baadhi ya mavazi na vitu vingine. Jumba lilikuwa kimya hakukuwa na mtoto wa kuchezacheza wala mwanamke wa kutandika kitanda, isipokuwa tu mfanyakazi wa ndani wa kike na yule wa nje anayetunza bustani ambao walikuwa wakiishi hapohapo lakini katika nyumba ya watumishi iliyopo nyuma ya nyumba hiyo.
Saa moja usiku wa siku hiyo, Kamanda Amata aliwasili Hoteli Trivoli, mahali ambapo alifikia, hakurudisha chumba hivyo moja kwa moja alifikia kaunta ambako alikabidhiwa funguo yake.
“Hakuna ujumbe wowote?” akamwuliza mhudumu wa kaunta.
“Hakuna!” akajibu na kisha akaendelea na kazi zake.
Kamanda Amata moja kwa moja akaelekea chumbani kwake na kukifungua kisha akasukuma mlango na kuuacha wazi kabla ya yeye kuingia. Katika eneo hilo hakukuwa na mtu yeyote isipokuwa yeye tu, akaingia kwa hadhari na bastola yake mkononi, kimya. Alipohakikisha chumba kipo sawa ndipo alipoitupa bastola ile kitandani na kuingia maliwato kujimwagia maji kala ya kazi nyingine yoyote.
Nusu saa baadae alikuwa mbele ya kioo akiondoa vishina vya ndevu vilivyoanza kujichomoza kujitokeza kidevuni mwake. Shati jeupe safi kabisa na suruali nyeusi vilikaa sawia mwilini mwake, kiatu kilichopigwa kiwi kiling’aa mguuni mwake, kiatu hicho spesho kwa kazi yake alikivaa mara hii akiviacha vile vyenye visu ndani yake. Hiki kilikuwa na mlipuko ndani ya kisigino chake. Akatazama simu yake kubwa ikamwambia kuwa ni saa mbili usiku. Muda mzuri, akawaza na kujitupia koti lake juu huku akipachika bastola zake vizuri, miwani moja yenye uwezo wa kuona gizani akaipachika katika mfuko wa koti ulio upande wa ndani kisha akatoka zake na moja kwa moja akaelekea alikokukusudia.
UWANJA WA NDEGE MAVALANE
CHIBA WA CHIBA aliingia mjini Maputo majira yayo hayo ambayo mlengwa wake alikuwa akienda kwenye nyapo zake. Akatoka ndani ya uwanja huo na moja kwa moja akachukua tax na kuomba imfikishe Hoteli Polana Selena, iliyo kando tu ya Bahari ya Hindi na si mbali kutoka hoteli ile aliyofikia Kamanda Amata. Baada ya itifaki zote aliingia katika chumba alichokabidhiwa na kupanga mambo yake sawa. Lakini kabla ya yote, akiwa ndani ya chumba hicho akafungua kitasa cha mlango kwa upande wa ndani, akakiweka mezani na kufungua mashine yake inayoruhusu funguo kufungua au kufunga. Akatazama jinsi yale meno yalivyopangiliwa, akayageuza kwa namna anayojua yeye ambayo itaruhusu funguo yake alivyokuja nayo kuweza kucheza na mlango ule, akiweka mchezo huo wa kuiruhusu kama akifunga kwa funguo yake, mtu mwingine asiweze kufungua kwa funguo nyingine na akifunga kwa funguo ile ya hoteli basi mtu mwingine pia aweze kufungua kwa funguo hiyo.
Alipohakikisha kuwa kila kitu kipo sawa, akafungua kompyuta yake ndogo na kuiweka mezani, akabofya hapa na pale na kuingia katika mtandao wao wa usalama na kuingiza namba maalumu za kumtambulisha Amata kiofisi, zilipopokelewa na ule mtandao ukamwuliza anataka kufanya nini na namba hiyo, akaiamuru kumtafuta wapi alipo, nayo ikamwambia huruhusiwi kufanya hilo kama si mhusika. Kisha ikamtaka kungiza namba za kumtambulisha yeye mwenyewe, akafanya hivyo na baada ya sekunde chache ikamtaka kuingiza nywila yake, alipoingiza tu, kitufe fulani kikazunguka kwenye kioo cha kompyuta hiyo kwa takribani dakika moja hivi kisha kikaleta maelezo fulani. Chiba akayasoma na kuyaelewa akabofya ‘ENTER’ kwenye kichakata cha kompyuta hiyo na ramani kubwa ya Mozambique ikaonekana kisha aikajizungusha na kuleta karibu jiji la Maputo.
Mwanga mdogo mwekundu ulikuwa ukiwakawaka mahal fulani na mwingine wa kijana ulikuwa ukiwakawaka kuionesha pale kwenye Hoteli ya Polana Selena. Chiba akajiridhisha, akachukua simu yake na kuiunganisha kitaalamu kabisa na ile kompyuta, kisha akaiweka ile kompyuta kabatini bila kuizima ili iweze kufanya kazi moja kwa moja na simu yake, vilevile kila maelezo yatakayonaswa iwek wa sauti au kwa maandishi yaweze kusafiri moja kwa moja kwenye kompyuta hiyo na kila baada ya nusu saa yatumwe automatiki kwenye mtambo wao mkubwa wa mawasilino uliopo Dar es salaam.
Chiba aliona Amata yupo Quiety Corner muda huo, akatoka na kukodi gari katika kampuni iliyoweka ofisi zake katika hoteli hiyo, kisha akaondoka kuelekea Quiety Corner.
Kamanda Amata aliegesha gari yake ya kisasa nje ya nyumba hiyo ya wageni, ambayo daima huwa na wageni maalum tu na si kila mmoja anaweza kupanga hapo. Aliteremka na kujiweka sawa, kisha akavuta hatua na kuifikia kaunta, mara hii akuomba kuoneshwa wapi anakwenda bali alipita moja kwamoja na kuchukua njia inayoelekea nyuma kabisa kwenye eneo lililozungukwa na kichaka cha minazi na miti mingine. Nje ya mlango mkubwa vijana wawili waliokuwa kwenye Ulinzi hawakumpa shida yoyote walimruhusu kupita naye akaingia ndani na kuketi kwenye kochi kubwa, akachukua gazeti na kutazama vichwa vya habari.
Ndani ya ofisi ya Bocca kulikuwapo watu wawili tu, Bocca mwenyewe pamoja na swahiba wake wa karibu Colonha wakijadilia hili na lile hasa sakata la jinsi gani ya kuwasaidia akina Banginyana kumaliza kazi yao.
Ijapokuwa alikuwa ni mtu maalumu sana kwa Bocca lakini aliombwa kusubiri hapo kwani boss alikuwa na mgeni nyeti ofisini. Amata akachomoa vifaa vya kusikiliza masikioni na kupachika kwenye simu yake kisha akiweka masikioni na kupekuwa faili la muziki, akichambua taratibu na kuupata muziki anaoutaka, Mwanameka. Kwa kuubofya wimbo huo upige aliruhusu kifaa cahke cha kunasa sauti alichokitega chini ya meza ya Bocca pasi na yeye kujua kianze kumsafirishia mazungumzo yote ya wawili hao, akaitumbukiza simu hiyo mfukoni mwa shati na kuendelea kusoma gazeti.
“Sikiliza Colonha, mimi nilifikiri huyu jamaa tumpe Moya amsaidie katika kazi yake ya kuwasaka hao watu wake…”
“Hapana Bocca, unajua ile ni kazi spesho, isitoshe ni ya siri sana ambayo inaweza kuziweka nchi fulani katika matatizo ya kidiplomasia, hivyo tusithubutu kusema eti tumpe mtu wa kumsaidia, sisi ndiyo tumsaidie kumbuka biashara zetu tunazifanya kwa raha tu kule Nduruta sasa tusiharibu,” Colonha alieleza.
“Sawa nimeelewa, Banginyana kanambia kuwa anwataka watu wawili ambao ndiyo haswa anajua wapo katika msako wa Ludovique…”
“Ndiyo, kuna huyu anaitwa Kamanda Amata wa Idara ya usalama ya Tanzania, ana wasiwasi kuwa anaweza kuwa hapa Maputo kumsaka Ludovique kwa sababu baada ya kumuua Abiseilim (Kubrah) kule Arusha, macho yetu hayamwoni tena! Hivyo Kanali ana wasi wasi kuwa huenda yuko hapa Maputo,” Colonha akadakia, “Ila amechukizwa sana na kitendo cha yule mwanamke kutoroka mikononi mwako…”
“Mikononi mwangu au mikononi mwake mwenyewe?” Bocca akauliza.
“Mi sijui, ila alichosema ni kurahisishiwa kazi ili aikamilishe kwa wakati, sasa leo usiku saa saba inabidi tukutane nao kule chimbo ili tuyaweke sawa,” Colonha akamwambia Bocca kisha kikao hicho kikavunjwa.
Kamanda Amata aliketi palepale na alipojua kuwa kikao kimevunjwa, mpaka saa saba huko Chimbo, akatoa simu yake na kujifanya akibadilisha muziki kumbe alikuwa akiweka kamera yake tayari, mara Colonha akajitokeza akifustiwa na Bocca, akachukua picha zao kila mmoja peke yake na kuziingiza katika mtandao maalumu wa utambuzi wa haraka haraka. Colonha akaondoka kwa kupitia njia tofauti kidogo na wanazotumia wengine.
“Boss, kuna mgeni hapa!” mmoja wa vijana wake alimwambia na wakati huo Amata akashusha gazeti lake na kukutana uso kwa uso na Bocca.
“Oooooh Moya!” Bocca hakuamini alipomwona kijana huyo, akamkumbatia kwa bashasha kubwa na kumwita ofisini kwake. Wakaketi wao wawiili tu, saa ya Amata ikawa ‘On’ ikirekodi mazungumzo yote.
“Moya Mampasi! Ha! Ha! Ha! Ha! Wewe ni Intelligent kabisa, umefanikisha kazi iliyoshindikana miaka na miaka…”
“Ndiyo hivyo, kazi imekwisha…”
“Na ngome imeanguka!” Bocca akamalizia, “Kwa kweli Moya umefanya kazi nzito, unastahili kulipwa malipo yako stahiki kwa kazi hiyo, pia usiku huu inabisi uishi kama uko peponi vile, upate msichana mrembo atakayekufanya ujisikie na wewe mwanaume kabisa leo. Nakuandikia cheki yako hapa, unataka ulipwe kwa Dola za Kimarekani, Paundi za Kiingereza, au…”
“Paundi za Kiingereza!” akajibu na Bocca akamwamndikia malipo yake yote na kumkabidhi ile cheki.
“Sasa hilo limekwisha, kuna kazi nyingine ya dharula hapa imejitokeza, nahitaji unisaidie kwa siri sana,” Bocca akamwambia Amata.
“Kazi gani, nitaifanya tu…”
9
“Njoo huku…” Bocca akamwita na kufungua mlango mwingine uliokuwa nyuma tu ya kiti chake, lakini kwa jinsi ulivyo hakuna mtu angeweza kujua kuwa hapo kuna mlango. Lilikuwa ni kabati kubwa la vitabu, akalishika upande mmoja na kulisukuma kisha wakaingia wote na lile kabati likajifunga….
“Ok, sasa unataka nifanye nini?” akauliza.
“Nataka umsake kwa gharama yoyote ile umlete akiwa hai hapa kwangu ili niwakabidhi wenyewe,” Bocca akampa maagizo.
“Sawa, hamna tabu na nitaanzia hapahapa tulipo, kwanza yukoje huyo mwanamke, yaani anaonekanaje machoni?” akauliza. Bocca akaeleza wajihi wa mwanamke yule vizuri sana. Muda wote huo Amata alikuwa akirekodi kwa kutumia saa yake maelezo yote hayo. Baada ya kujiridhisha nayo akamwangalia tena Bocca. Akavuta hatua na kukikagua kile chumba, inaonekana kulikuwa na pambano zito humu ndani, akawaza baada ya kuona alama za damu ukutani na sakafuni.
“Sasa we nenda kaendelee na kazi yako, mi niache na huyu kijana hapa!” Amata akamwambia Bocca naye kibopa huyo akaondoka zake. Uchunguzi ukaendelea na katika kona moja ya kile chumba aliona kitu kinachong’aa ng’aa, akakifuata na kukiokota.
“Nini hicho?” yule kijana aliyebaki akauliza.
“Ah, heleni tu hii, tazama” akampa. Lakini sekunde chache tu akamrudishia kwani hakuelewa kabisa. Amata akaiangalia kwa makini ile heleni akagundua kuwa si heleni ya kawaida, akaitia mfukoni na kutoka kwa mlango mkubwa kisha akamwuliza yule kijana ni wapi ambapo wahnahisi mwanamke yule alipitia, akaoneshwa. Kilikuwa kichaka cha miti midogodogo na minazi iliyodumaa, Amata akaifuata njia hiyo kwa msaada wa tochi ili aweze kuona vitu alivyovihitaji katika vichaka hivyo. Hatua mbili tatu zikamfikisha katikati ya kichaka na huko akaona uwazi mkubwa ambao alihisi kuwa huenda mtu huyo alipita eneo hilo. Hakuona cha maana alipojishika katika mfuko wa shati lake akaigusa ile heleni, hii itanisaidia akajisemea kwa sauti ya moyoni kisha akatoka. Lakini kabla hajamaliza kile kichaka macho yake yakavutwa na kitu kama chip ya simu, ndogo, nyeupe. Akainama na kuiokota, akaitia mfukoni bila hata kujiuliza kisha akatoka kichakanai na kulikabili kasri la Bocca.
“Vipi?” Bocca alimuuliza mara tu baada ya kuketi kitini.
“Yeah, itamsaka, na nina uhakika wa kumtia mkononi ndani ya saa kumi tu,” akajibu.
“Lazima uwe mchawi ili ufanikishe hilo,”
“Sio uchawi ni akili tu, nipe muda, nitarudi nikiwa naye mkononi,” akamweleza.
Chiba akatabasamu, maana akiwa ndani ya gari yake aliweza kudukua mazungumzo yote aliyokuwa Amata akiyafanya na Bocca, akawasha gari na kuondoka taratibu eneo lile la ile nyumba ya wageni. Mbele kidogo akasimama na kutoa kichwa akinunua korosho kwa kijana mmoja aliyekuwa akifanya biashara hiyo. Kwenye kioo cha ndani cha dereva aliweza kuiona ile gari ya Amata, Kilimanjaro, ikipita kwa kasi. Akaingia barabarni na kuifuata kwa mbali mpaka alipoona pale ilipoingia katika ile hoteli ya Trivoli. Chiba akapitiliza moja kwa moja akaingia hotelini kwake na haraka akawasha kompyuta yake na kuingia katika mtandao alioutengeneza kwa maswala ya utambuzi. Akasikiliza maelezo ya Bocca alivyokuwa akieleza juu ya wajihi wa huyo mwanamke kisha yeye akawa anaingiza katika kompyuta sifa hizo, baada ya dakika kumi akawa tayari na picha ya kuchora inayoonesha uhalisia wa mtu huyo.
Akaitazama ile picha vizuri, hakuijua wala kuitambua sura hiyo, akaikopi na kuipesti sehemu nyingine ndani ya mtandao kisha akaifanyia crossmatch ili kuona ni nani mtu huyo kama yupo kati ya watu wanaotafutwa au walioko kwenye Blacklist. Picha mbalimbali zikazunguka hapa na pale kwa kasi ya ajabu kisha picha mbili zikasimama pamoja, upande huu ile aliyotengeneza kwenye kompyuta na upande mwingine ile picha halisi iliyokuja kutoka mtandaoni.
“Shiiiit!” akang’aka kwa sauti kisha akaruhusu maelezo juu ya mtu huyo kuendelea kumiminika.
Maelezo hayo yalimweleza mwanamke huyo kwa jina la Jebeleth Isaac, zaidi ya hapo yalimweleza umri wake, bado alikuwa mbichi miaka thelathini na tano tu, mwajiriwa wa shirika la kijasusi la Namibia NIS, chini kabisa kukafuata maelezo mengi sana juu yake ambayo yalimfanya Chiba kuwa na hamu ya kumwona kwa macho. Hakuamini kama yuko sawa kadiri ya mchoro wake ulioonekana kwenye kioo cha kompyuta, alipojaribu tena na tena bado jibu lilikuwa lilelile. Akaiprinti ile picha akaiweka kando na kutafuta mawasiliano na bosi wake.
“Yes Chiba!” Madam S alipokea simu ile upande wa pili.
“TSA 1 yuko salama salimini na kazi inaendelea vyema,” akafikisha ujumbe.
“Sawa, hakikisha unafuata kila nyendo anayofanya, na unipe ripoti, over and out!” simu ikakatika. Akanyanyuka kutoka pale alipokuwepo na kuteremka chini, nje ya hoteli hiyo, akaingia garini na kuondoka kuelekea hoteli ya Trivoli ambapo Amata amefikia.
Kamanda Amata, mara tu baada ya kufika chumbani mwake, aliitoa ile heleni mfukoni mwake na na kuipachua katikati ya lile ua, akachomoa chip ndogo sana ya kunasa sauti iliyokuwa ndani yake. Katika mkoba wake ndani ya kabati akachomoa kifaa maalumu cha kuweza kuisoma chip hiyo, akaipachika na kuunganisha na kompyuta yake. Ndani ya kifaa hicho alisikia mazungumzo mbalimbali ya mwanamke huyo hasa alipokuwa akitekwa pale uwanja wa ndege. Ijapokuwa yeye alizimia lakini heleni ile ilikuwa ikirekodi kila jambo. Amata akasikia mazungumzo ya wale watekaji, maelekezo ya wapi walitakiwa kumpeleka.
“Ana pasipoti nne sasa hatujuai ipi ni halali, hii ni ya Afrika Kusini anaitwa Sebeth Sebutwa na ndiyo aliyoingilia sasa hapa Mozambique. Hapa kuna nyingine, hii ni ya Congo DR inamtambulisha kama Mirabel Zubi Kabasele. Kuna hii ya U.S.A anaitwa Jenitrose McLaren…”
“Na ya mwisho…”
“Ya mwisho ni ya Kenya, inamtambulisha kama Mgdalene Wanjiku,”
Mazungumzo hayo yalimvutia zaidi Amata, akili yake ikafikiri mara mbili, kwa nini awe na pasipoti nne? Akajiuliza. Kisha akakusanya yale majina yote na kuyaingiza mtandaoni lakini hakuweza kupata uwiano na mtu yoyote.
Jebeth Sebutwa, huyu ilielezwa kuwa ni marehemu, bibi wa siku nyingi wa huko Afrika ya Kusini, hii ilimfanya Amata acheke. Akatazama jina la pili, Mirabel Zubi Kabasele, hakupata kabisa uwiano wowote wa jina hilo, akaliweka pembeni, akaingiza la tatu, Jenitrose Mc Laren, akapata kujua kuwa alikuwa dereva wa kujaribisha magari mapya huko USA katika tawi la kampuni ya Mc Laren.
Alipogundua zote ni za uongo, akachukua ile SIM aliyoiokota kule kichakani, akaipachika kwenye simu yake ya akiba na kuiwasha japo kwa sekunde ishirini, hakuna chochote kilichosikika. Akiinua ile simu na kuipekuwa katika box la ujumbe, kulikuwa na ujumbe mmoja tu.
…Postana Rovuma…
Alisoma na kurudia rudia ujumbe huo lakini hakuuelewa, akaandika maneno hayo kwenye kijikaratasi kidogo. Postana Rovuma, akarudia kulitamka kwa sauti yake mwenyewe. Akaingia maliwato na kupata maji ya kuoga kisha akabadili nguo na kuamua kutumia saa mbili nyingine kuzunguka mjini japo kuona mandhari ambayo kwayo labda angepata lolote.
Aliifikia gari yake na kufungua mlango, kisha akaketi kitini, ndipo macho yake yalipogongana na bahasha moja nyeupe.
“Mh!” akaguna. Mwili wake ukamsisimka, akakumbuka kisa cha rafiki yake mmoja aliyewahi kutumiwa sumu katika bahasha ya mtindo huo, akafungua droo ya dashboard ya gari hiyo na kutoa barakoa, akaivaa usoni kuzuia pua na kinywa kisha akiwa na gloves maalum huku gari ikiwa milango wazi, akafungua taratibu, lakini badala yake ni karatasi moja ilijitokeza. Akatoa ile barakoa na kuikamata vyem,a ile karatasi. Akaikunjua na kukutana na sura ya mwanamke wa makamo. Moyo wake ukapiga kwa nguvu, akahisi damu kukimbia kwa kasi.
Sura ile haikuwa ngeni kabisa, alimkumbuka mwanamke yule, walikutana Arusha katika chumba cha marehemu Hamadou pale Hoteli ya Mount Meru, akamfanyia hila na kumtoroka, mara ya pili alikuta amekamatwa na yuko chini ya himaya ya Abiseilim, yaani Kubrah ambaye mpaka hapo naye pia alikuwa ni marehemu. Amata akatikisa kichwa.
“Ni nani mwanamke huyu?” akauliza kwa sauti ya chini, alipomaliza kuitazama ile picha akaikunja na kuitia mfukoni mwake huku akihema kwa nguvu.
Ina maana kama wanamtaka huyu mwanamke kwa jinsi alivyonieleza Bocca basi huyu ni nyoka, ndiyo ni nyoka, lazima nimpate, na nimjue ni nani, akawaza kisha akasonya na kuwasha gari huku akiwa kabana meno yake na kuiondoa kwa kasi eneo lile la Trivoli kuelekea mjini. Hakwenda mbali bali alivutiwa na kilabu kimoja cha usiku kilichopambwa kwa maandishi Africa Bar katika pembezoni mwa barabara ya Carl Marx, akaegesha gari na kukaribishwa na wadada warembo waliokuwa nje ya baa hiyo. Kwa jicho la haraka haraka walikuwa makahaba wanaojiuza.
“Oh! você tem um bom carro!” mmoja wa wanawake wale alisikika akilisifia gari hilo zuri kwa Kireno. Amata akashusha kioo na kuwatazama wanadada wale, akamwita mmoja aliyemwona ana umri mdogo kati ya wote, akamfungulia mlango akaingia upande wa pili, kisha akaondoa ile gari na kupotelea mtaani, mpaka katika baa ya Copacabana Discotech, akaegesha gari na kulizima. Yule mwanadada akaketi vizuri katika kiti chake na kukunja nne iliyofanya paja lote libaki wazi. Kamanda Amata akameza mate ya uchu kwa mvuto wa paja lile lakini moyoni akapigana na Ibilisi aliyemolazimisha kulitazama.
“Unajua Postana Rovuma?” akamwuliza. Yule mwanamke akamtazama kwa mshangao.
“Postana Rovuma?”
“Ndiyo!”
“Hiyo ni hoteli iko huko mtaa wa saba! Ndio wataka tukafanyie mambo yetu huko?”
“Hapana sikukuchukua pale kwa kufanya hayo ila nilitaka unielekeze ilipo,”
Yule mwanamke akamsonya na kutikisa kichwa, “Go fish!” akatoka na kuufunga mlango kisha akapotelea kwenye maua makubwa yaliyojazana nje ya ukumbi huo. Amata kwenye mtandao na kuipata ile hoteli, kwanza alijua ni jina la mtu lakini jibu la huyo mwanamke lilimpa mwanga kuwa ni hoteli. Bila shaka kafikia pale akajisemea na kuondoka polepole. Haikumchukua muda akaifikia hoteli ile, akaegesha gari na kuteremka kisha kuongoza mpaka kwenye meza kubwa ya mapokezi. Hakutaka kupoteza muda wake, alisalimiana na wahudumu wawili waliokuwa hapo na kuwaonesha kitambulisho cha polisi kikimtambulisha kuwa yeye ni afisa wa polisi kisha akawaonesha ile picha.
Wale wahudumu waliitazama, kisha wakatazamana wao kwa wao.
“Tunamjua, amefika hapa jana!” mmoja wao akajibu huku akionekana kuwa na woga usoni mwake.
“Chumba namba ngapi?”
“520” akajibiwa na dakika hiyohiyo akaelekea kwenye lifti na kupanda mpaka ghorofa ya tano, akakitafuta chumba namba ishirini, haikumsumbua kukipata. Taratibu aliukaribia mlango huo na kutega sikio kwa makini ili kusikia kama kuna lolote linaloendelea ndani ya chumba hicho. Kwa mbali alisikia maji yakimwagika, akjua kwa vyovyote mwenye chumba hicho atakuwa bafuni. Akanyonga kitasa na kuutikisa mlango, umefungwa. Akachukua funguo yake inayoweza kufungua vitasa zaidi ya thelethini vya mtindo huo, akacheza nacho mara mbili tatu tu nacho kikatii amri, mlango ukafunguka. Akausukuma taratibu na ile sauti ya maji yanayomwagika ikazidi masikioni mwake, kengele ya hatari ikalia kichwani mwake. Kwa mwendo wa mnyato akajitoma ndani ya chumba hicho….
ITAENDELEA
Pasipoti Ya Gaidi Double Agent Sehemu ya Tano
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;