SIMULIZI YA MASHIMO YA MFALME SULEMANI SEHEMU YA TATU
NEW AUDIO

Mashimo ya Mfalme Sulemani Sehemu ya Tatu

Simulizi Ya Mashimo ya Mfalme Sulemani
Simulizi Ya Mashimo ya Mfalme Sulemani Sehemu ya Tatu

IMEANDIKWA NA: HENRY RIDER HAGGARD

Simulizi: Mashimo Ya Mfalme Sulemani

Sehemu ya Tatu (3)

SURA YA TATU UMBOPA AMEINGIA KAZINI

Kutoka Capetown mpaka Durban ni mwendo wa siku nne au tano kwa kadiri ya mwendo wa meli ulivyo, na hali ya baharini na upepo ilivyo. Pengine meli inacheleweshwa East London muda wa saa ishirini na nne ikiwa mawimbi ni makubwa na bahari imechafuka. Lakini safari hii hatukuwekwa kwa sababu mawimbi yalikuwa si makubwa ila ya kadiri tu, na matishari yaliletwa mara moja kuja kuteremsha shehena. Basi kwa muda huo wote tuliokuwa tukisafiri kwenda Natal nilikuwa nikifikiri sana maneno ya Bwana Henry. Hatukupata kuongea juu ya safari muda wa siku mbili tatu, ingawa nilimsimulia visa vingi vya safari zangu za kuwinda, na hivyo vyote vilikuwa vya kweli kabisa.

Basi siku moja jioni katika mwezi wa January, tulipita bara ya Natal, tukitarajia kuingia bandari ya Durban kabla ya kuchwa. Lakini tulikuwa hatukupima wakati vizuri, maana jua lilikuwa limeshuka kabisa wakati tulipotia nanga nje ya rasi, tukasikia mzinga wa kuonya watu wa Durban kuwa meli ya Kiingereza imekwishafika. Tulichelewa kuingia bandarini usiku ule, kwa hivi baada ya kuteremsha mifuko ya barua katika mashua, tulikaa mezani tukala kwa raha bila ghasia. Tulipopanda tena juu sitahani, mwezi ulikuwa umetoka na kung’aa vizuri juu ya bahari kadiri ya kufanya taa ya mnara kama si kitu. Kutoka pwani upepo ulileta, harufu nzuri ya matunda iliyonitia hamu ya kuimba nyimbo za dini kwa jinsi zilivyokuwa nzuri, na huko katika madirisha ya nyumba za pwani, taa kwa mamia zilitoa mwangaza.

Tukasikia sauti za mabaharia waliokuwa katika meli nyingine wakijitayarisha kung’oa nanga ili wawe tayari kushika majira yao. Sisi watatu, yaani Bwana Henry Curtis na Bwana Good na mimi tulikwenda karibu na usukani tukakaa kimya kwa muda, Na badae kidogo, bwana Henry akasema, ‘Je, Bwana Quatermain umekwisha yafikiri maneno yangu?’ Na Bwana Good akasema, ‘Ndiyo, waonaje Bwana Quatermain? Natumai kuwa utapenda kusafiri pamoja nasi mpaka Mashimo ya Sulemani, au popote alipofika Yule mtu jina lake Neville.

Nikaondoka nikagonga kiko changu ili kukikongoa tumbako. Nalikuwa bado sijakata shauri, mradi nikataka nafasi ya dakika moja nipate kukata shauri kabisa. Basi dakika ile ilinitosha, nikakaa tena nikasema, ‘Vema nitakwenda, na kama mkinipa ruhusa nitawaambia sababu zangu za kwenda, na vile vile nitawaambia kwa mapatano gani. Kwanza mapatano ni haya:

Utalipa gharama zote, na pembe za ndovu zozote na vitu vya thamani vyovyote vingine tutakavyo pata vitakuwa shirika kati ya Bwana Good na mimi, Yapili, unipe pauni mia tano mshahara wangu kabla ya kuanza safari, nami nitaahidi kukutumikiavema mpaka siku utakapoazimu kuacha safari, au mpaka tutakapofaulu, au mpaka tutakapofikwa na ajali.

Ya tatu, kabla ya kuanza safari utaandika hati ya kuahidi kumpa mtoto wangu anaeelimishwa katika hospitali ya London, pauni mia mbili mwaka kwa muda wa miaka mitano, wakati huo ndipo atakapoweza kufanya kazi mwenyewe, akiwa ana akili zake timamu. Basi ni haya tu, na labda utaona ninataka mengi.’

Bwana Henry akajibu, ‘Sidhani kuwa unataka mengi, nami nakubali kwa furaha hayo yote. Mimi nimekaza nia kwenda safari hiyo, nami nilikuwa tayari kukulipa zaidi, ili nipate msaada wako, maana maarifa uliyonayo wewe si ya kawaida, watu wengine hawana.’basi nikasema, ‘Wanifanya kusikitika kwa kuwa sikutaka zaidi! Lakini haidhuru, mimi siwezi kuvunja ahadi yangu.

Na sasa tumekwisha patana, nitakwambia kwa nini nimekubali kwenda. Kwanza, siku hizi zilizopita nilikuwa nikiwatizama sana nyinyi watu wawili, na ikiwa hamtaudhika, nitasema kuwa ninawapenda na tena nadhani kuwa tutapatana vema pamoja. Tena kupatana huku si jambo dogo katika safari ya siku nyingi kama hii tunayokusudia kufanya.

Na sasa kuhusu safari yenyewe, nasema waziwazi kuwa naona hatutarudi salama, yaani, kama tukijaribu kuvuka milima ya Sulemani. Kumbukeni yaliyompata mzee Silvestre miaka mia tatu nyuma, tena yaliyompata Yule mtu mmoja wa ukoo wake miaka ishirini iliyopita! Na sasa yapi yaliyompata ndugu yako? Nitakwambieni waziwazi kuwa mimi nadhani ajali yao itakuwa ndiyo yetu.’

Kisha nikawatazama kuona nini watakayoyafikiri wakisikia maneno yangu. Bwana Good akageuka uso kidogo, lakini Bwana Henry akawa imara kabisa, akasema, ‘Liwalo na liwe, lazima tubahatishe.’Mimi nikaendelea kusema, ‘ Labda utaona ajabu ya kuwa mimi ingawa nimesema maneno hayo, lakini nimekubali kwenda safari hii? Lakini nina sababu mbili. Kwanza, mimi ninaamini ya kuwa mwanadamu hana hiari, yalioandikwa yameandikwa. Ikiwa ajali yangu imefika itakuwa tu bila shaka. Ikiwa nilazima niende safari ya milima ya Sulemani na kuuawa, basi nitakwenda na kuuawa. Haikosi, Mungu mwenyewe anajua nia yake juu yangu, nami sina haja ya kushughulika juu yake.

Na sababu ya pili, ni kuwa mimi si tajiri. Yapata miaka arubaini nimefanya biashara na kuwinda bila kupata kitu isipokuwa riziki tu. Nyinyi mnajua ya kuwa watu huhesabu maisha ya mwindaji ndovu kuwa miaka minne, au mitano tu. Hivyo nimeishi vizazi saba vya watu wanaoshika kazi ninayofanya, nami naona kuwa wakati wangu wa kufariki hauwezi kuwa mbali sasa. Na sasa namna ninavyoishi, ikiwa nitapatwa na ajali yoyote, sina kitu chochote cha kumwachia mwanangu arithi. Lakini tokea sasa atatazamwa kwa muda wa miaka mitano. Basi hizo ndizo sababu zinazonivuta niende.’

Bwana Henry alisikiliza sana maneno yangu, kisha akajibu, ‘Bwana Quatermain, zile sababu ‘ulizotaja za kukubali safari hii, ingawa unafikiri kuwa mwisho wake ni kufa, zaonyesha kuwa wewe ni mtu thabiti kabisa. Kama yale unayoyafikiri yatatokea kuwa kweli itaonekana baadae. Lakini ikiwa yatatokea kuwa kweli au si kweli, mimi nimenuia kuendelea mpaka nione mwisho wake, ukiwa mtamu au ukiwa uchungu. Ikiwa ndiyo tutakufa, basi mimi naona ni afadhali na tupate furaha ya kuwinda kwanza, sivyo Bwana Good? Bwana Good akajibu, ‘Ndivyo, ndivyo. Sisi sote watu watatu tumezoea tangu zamani kuingia katika hatari za namna nyingi na kustahamili mashaka makuu.’

Basi tukashuka chini tukalala. Siku ya pili tulishuka kwenda pwani nikamchukua Bwana Henry na Bwana Good mpaka nyumba yangu ndogo niliyokuwa nimejenga huko Durban zamani. Yule mtu aliyekuwa akitunza nyumba na bustani ni mtumishi aitwae Jack. Alikuwa mtu wangu wa zamani. Aliwahi kuvunjwa paja na nyati katika nchi ya Sikukuni tulipokwenda kuwinda, nae hawezi kuwinda tena. Lakini anaweza kufanya kazi kidogo kidogo katika bustani.

Bwana Henry na Bwana Good walilala katika hema katika bustani yangu kwa sababu hapakuwa na nafasi ndaniya nyumba. Lakini lazima niendelee kusimulia hadithi yangu usije ukachoka. Mara niliponuia kwenda safari hiyo nilianza kutengeneza kila kitu tayari. Kwanza niliandikisha hati ile ya mapatano ili mwanangu apate haki yake ikiwa nitapatwa na ajali. Kisha nikapata zile pauni mia tano. Kisha nikafanya hivi, nikanunua gari na ng’ombe wa kulivuta. Gari lilikuwa refu sana, lina namna ya hema iliyofunika nusu ile ya gari iliyo nyuma, na mbele nafasi ilikuwapo ya kuwekea mizigo yetu. Katika hema ile palikuwa na kitanda kikubwa likichotosha watu wawili, na tena mahali pa kuwekea bunduki na vitu vingine. Kisha nilinunua ng’ombe wa Kizulu ishirini waliokwisha zoea magonjwa ya humo. Kwa kawaida kumi na sita wanatosha, lakini nilichukua wane zaidi kwa tahadhari ikiwa wengine wata kufa.

Kisha kufanya hivi ilikuwa kazi ya kufikiri namna ya chakula na dawa za kuchukua katika safari. Kwa bahati Bwana Good alikuwa amekwisha elimishwa kidogo katika elimu ya utabibu, nae alikuwa na kasha lake la dawa za kila namna. Kisha, tulitengeneza mipango ya bunduki na risasi za kufaa safarini, tukazichagua kwa uangalifu sana, maana kila mwindaji anajua kuwa bunduki na risasi ni jambo muhimu sana. Sasa tukaanza kuchagua watu watakaofuatana nasi katika safari yetu, na baada ya mashauri mengi tukachagua watano, mtu mmoja wa kuchunga ng’ombe, kiongozi mmoja, na watumishi watatu. Yule mchungaji na kiongozi tukawapata upesi, walikuwa Wazulu wawili, na majina yao yalikuwa Goza na Tom; lakini kupata watumishi ilikuwa taabu kidogo. Ilikuwa lazima kuwachagua watu waaminifu na hodari, maana pengine labda maisha yetu yatategemea walivyo.

Mwisho tulichagua wawili, mmoja alikuwa kabila la Hottentot jina lake Ventvogel, maana yake ‘Ndege wa upepo,’ na Yule wa pili alikuwa Mzulu mdogo aliyeitwa Khiva, naye alijua Kiingereza sana. Nilimjua Ventvogel, tangu zamani, alikuwa mtu hodari wa kusaka wanyama, akiweza kufuata nyayo zao kwa namna ya ajabu kabisa, tena alikuwa hachoki kabisa. Sasa tulikuwa tumekwisha chagua wawili, lakini wa tatu hatukuweza kumpata, tukanuia kuanza safari yetu na kujaribu kutafuta mwingine njiani.

Lakini siku moja kabla ya kuondoka, wakati wa jioni, Yule Mzulu Khiva aliniambia kuwa yupo mtu mmoja anataka kuonana nami. Basi tulipokwisha kula, nilimwambia Khiva amlete. Baadae kidogo mtu jamili mwenye umri wa kama miaka thelathini aliingia. Alikuwa mwekundu kuliko Wazulu walivyo. Aliingia akaniamkia kwa kuinua rungu lake, akakaa kitako katika pembe ya chumba.

Niliona ya kuwa alikuwa mtu mwenye cheo, maana kichwani alivaa methali ya taji iliyong’aa, ambayo inavaliwa na Wazulu wakiisha kupata umri fulani, au cheo Fulani. Tena nikaona kama ninamtambua sura yake. Baada ya kitambo, nilimuuliza, ‘Je, jina lako nani? Akajibu, ‘Umbopa.’ Na sauti yake ilikuwa nene na alitamka polepole. Nikasema, ‘Nadhani tumekwisha onana mahali zamani.’ Akajibu, ‘Ndiyo, umeniona katika mahali paitwapo ‘Isandhlwana’ (maana yake ni ‘Mkono mdogo’) siku ile iliyotangulia vita.’

Ndipo nilipomkumbuka.

Mimi nilikuwa mmoja wa viongozi wa Jemedari mmoja katika vita vya Wazulu, na yeye alikuwa mkubwa katika kikosi kidogo cha wenyeji, na siku moja aliniambia ya kuwa alifikiri kuwa kambi letu lina hatari. Mimi nikaona uchungu kidogo, nikamwambia afadhali na uwaachie mashauri kama hayo wakubwa wenye akili kupita zake; lakini baadae niliona kuwa maneno yake yalikuwa ya kweli. Basi nilimwambia, ‘Ndiyo, sasa nakukumbuka. Je, unataka nini?’ Akajibu, ‘Ni hivi Makumazahn (hilo ndilo jina walilonipa wenyeji, na maana yake ni ‘ Akeshaye usiku’. Nasikia ya kuwa unasafiri kaskazini pamoja na mabwana hawa waliotoka Ulaya. Je, ni kweli?’ Nikamwambia, ‘Ni kweli.’ Akasema, ‘Nimesikia ya kuwa utapita mto wa Lukanga ulio safari ya mwezi mmoja kupita nchi ya Manika. Ni kweli, Makumazahn?’

Nikaona ajabu, maana habari za safari yetu tulifanya kuwa ni siri, nikamuuliza, ‘Kwa nini unauliza habari za safari yetu?’ Akajibu, ‘Kwa sababu hata na mimi nataka kufuatana nanyi.

Jina langu ni Umbopa. Mimi ni Mzulu lakini si Mzulu. Ukoo wangu unatoka katika nchi ya kaskazini kabisa. Wametoka huko zamani, miaka elfu nyuma. Wazulu walipokuja hapa, zamani sana kabla ya kutawala Chaka. Mimi sina nyumba. Nimetembeatembea kwa muda wa miaka mingi. Nilikuwa mtu wa Setewayo katika kikosi cha Nkomabakosi, nilikuwa chini ya Umslopogaas (maana yake, ‘Mwenye shoka’) naye ndiye aliyenifundisha kupigana. Baadae nilikimbia kutoka nchi ya Wazulu kwa sababu nilitaka kuona mambo ya watu weupe. Kisha nilimpigania Setewayo katika vita. Na tangu wakati ule nimefanya kazi katika Natal na sasa nimechoka, nataka kurudi kaskazini tena. Hapa si kwangu. Sitaki mshahara , lakini mimi ni mtu hodari nami nadhani ninastahili kupewa nafasi katika safari yako.’ Kwa namna alivyosema nilitambua kuwa anasema kweli. Lakini nilikuwa na shaka kidogo kwa kuwa alitaka kuja bila ya kupata mshahara. Basi nikawaeleza Bwana Henry na Bwana Good, nikawataka wakate shauri.

Bwana Henry akamwambia asimame. Umbopa akasimama akavua koti kubwa alilokuwa kavaa, akasimama amevaa ngozi kiunoni tu na makucha ya simba shingoni. Hakika alikuwa mtu aliyeumbika kabisa wala sijaona mtu aliyependeza kupita yeye. Urefu wake ulikuwa futi sita na inchi tatu, nae alikuwa mpana kwa kadiri ya urefu wake. Alikuwa mwekundu wala si mweusi sana, isipokuwa alikuwa na makovu ya majeraha aliyopata katika vita. Bwana Henry akasimama karibu nae akamtazama usoni, akasema kwa Kiingereza, ‘Napenda watu walio kama wewe Umbopa, utakuwa mtumishi wangu.’ Umbopa akafahamu maneno yale, akasema, ‘Vema.’ Akamtazama namna alivyokuwa mkubwa na mpana, akasema, ‘Sisi ni wanaume, wewe na mimi.’

Si nia yangu kueleza habari zote za safari yetu mpaka kufika mji wa Sitanda ulio karibu na mahali inapoungana mto Lukanga na mto Kalukwe. Maana ni safari ya zaidi ya maili elfu moja kutoka Durban, na sehemu ya mwisho wa safari, yaani mwendo wa maili mia tatu hivi tulikwenda kwa miguu kwa kuwa chafuo wengi wapo na ng’ombe wakiumwa nao hufa.

Tulitoka Durban mwisho wa mwezi wa Januari, na tulipofika Sitanda na kupiga kambi yetu, ilikuwa katikati ya mwezi wa Mei. Mambo yaliotokea ni kama yale yanayotokea katika kila safari katika nchi hii ya Afrika, ila jambo moja, na hilo nitaeleza baadaye. Tulipofika Inyati, ulio mji wa mwisho wa biashara katika nchi ya Matabele inayotawaliwa na Lobengula, tuliacha gari letu bila ya kutaka. Katika wale ng’ombe ishirini tulionunua, kumi na mbili tu walibaki. Mmoja aliumwa na nyoka, watatu walikufa kwa njaa na kiu: mmoja alitembeatembea akapotea, na watatu wengine walikufa kwa kula majani yenye sumu. Watano wengine waliugua kwa kula majani hayo hayo lakini tuliweza kuwaponya.

Basi tuliacha gari letu katika mikono ya Goza na Tom, yaani mchungaji na kiongozi, tukamwomba mtu wa Mission aliyekaa karibu aende kuwaangalia mara kwa mara, tukaanza safari yetu ya hatari pamoja na Umbopa, na Khiva, na Ventvogel na wapagazi sita tuliowaandika pale pale. Nakumbuka ya kuwa sote tulikuwa kimya kabisa tulipoanza safari hiyo. Nadhani sote tulikuwa tukifikiri labda hatutaliona gari lile tena; na mimi kwa hakika sikutumai kuliona tena. Kwa muda kidogo tulitembea kimya kabisa mpaka Umbopa aliyekuwa katangulia kidogo alianza kuimba wimbo wa Kizulu kuhusu watu hodari waliokuwa wamechoka kukaa hivi hivi tu, wakaanza safari ili watafute mambo mapya. Na kumbe, walipokuwa wamesafiri mbali sana katika jangwa waliona kuwa si jangwa ila ni mahali pazuri mno penye wanawali wazuri na ng’ombe walionona , na wanyama wa kuwinda porini, na adui wa kupigana nao. Basi sote tulianza kucheka tukaifanya kuwa ni njozi njema.

Umbopa alikuwa mcheshi na wakati mwingine alikaa akijisemea tu mwenyewe, nae aliweza kutuchangamsha sana kwa fikira zake. Sote tulimpenda sana. Na sasa lazima nisimulie habari za jambo nililotaja. Baada ya kupita juma mbili kutoka Inyati tulifika mahali pazuri katika mwitu. Miti mingi ya namna nyingi ilikuwa ikiota juu ya vilima, na miti mingi ilikuwa ikizaa matunda wanayopenda sana ndovu. Tukaona alama ya kuwa kweli wapo ndovu, maana wengine wameng’oa kabisa miti wapate kula matunda yake ndovu ni mlaji mharibifu sana.

Jioni moja, baada ya kufanya safari ndefu, tulitokea mahali pazuri chini ya kilima penye mto wa maji matamu kabisa. Mara tulipoingia katika mto tukaona kundi la twiga wakitoka: mbio’ kwa mwendo wao wa kuchekesha, na mikia yao imeinuka juu. Walikuwa mbali, hatua mia nne hivi na kwa hivyo ilikuwa mbali kuweza kuwapiga bunduki, lakini Bwana Good aliyekuwa katangulia hakuweza kujizuia, akaona lazima ajaribu kuwapiga.

Akaelekeza bunduki yake na kwa bahati alimpiga mmoja aliyekuwa nyuma kidogo. Risasi ikampiga shingoni akaanguka kichwa chini, kama sungura tu. Basi ustadi wa Bwana Good ulihakikishwa tokea siku ile, lakini kwa kweli alikuwa hana shabaha hata kidogo. Ikawa baadae kila mara alipomkosa mnyama, tulimsamehe kwa sababu ya kumpiga Yule twiga. Basi tukawatuma wapagazi watengeneze riyama ya Yule twiga, nasi tukaanza kutengeneza kambi yetu. Kambi yenyewe ilikuwa boma la miiba, na katikati tulitandaza majani makavu ya kulalia, tukakoka moto mwingi wa kuzunguka kambi.

Basi tulipokuwa tumekwisha tengeneza kambi, mwezi ukatoka na chakula chetu cha nyama ya twiga na mafuta ya mifupa yake kilikuwa tayari. Tulifurahi sana kula mafuta yale ya twiga, lakini ilikuwa kazi kuivunja jinsi ilivyokuwa migumu. Nadhani hapana chakula kitamu kama mafuta ya mifupa ya twiga, ila labda moyo wa ndovu.

Tulikula chakula chetu kwa mwangaza wa mbalamwezi, na mara kwa mara tulimsifu Bwana Good kwa shabaha yake; kisha tukakaa tukavuta tumbako na kusimuliana hadithi. Ungalituona ungalistaajabu tulivyokaa. Mimi nywele zangu zaanza kuwa na mvi, na Bwana Henry zake zilizo na rangi ya kimanjano zaanza kuwa ndefu na hatukufanana hata kidogo. Maana yeye ni mrefu, mweupe mpana, na mzito; lakini mimi ni mfupi, mweusi, mwembamba na mwepesi. Lakini labda aliyekuwa mcheshi zaidi ni Bwana Good. Alikaa juu ya mfuko wa ngozi kama ndiyo kwanza amerudi kutoka safari ya kuwinda kwao Ulaya, maana alikuwa maridadi sana, safi kabisa; nae amevaa vizuri. Alikuwa amevaa nguo za kizungu, na kofia vile vile iliyopatana na nguo zake, tena amenyoa vizuri na amevaa miwani yake ya jicho moja.

Basi tulikaa sisi watatu tukizungumza huku tukiwatazama watu wetu waliokuwa wamekaa karibu wakivuta tumbako yao, hata wakaanza mmoja mmoja kujifunika blanketi na kulala penye moto, ila Umbopa aliyekaa mbali kidogo peke yake kashika tama anafikiri. Niliona kuwa hachanganyiki kabisa na wenzake. Baadae kidogo kwa nyuma yetu tulisikia sauti, ‘Woof, Woof!’ Nikasema kuwa huyu ni simba, tukakaa tunasikiliza na mara kutoka mahali penye mto tulisikia sauti ya ndovu. ‘Unkungunklovo! Ndovu!’ Kikasisikia watu wetu wakinong’ozana, ‘Ndovu! Na baadae kidogo tukamwona wameandamana kama vivuli vikubwa wakitoka penye maji wanakwenda mwituni. Mara moja Bwana Good aliruka akataka kuwafuata. Nadhani labda alifikiri kuwa kumpiga ndovu ni sawasawa na kupiga twiga, lakini nilimshika mkono nikamwambia, ‘Waache waende zao.’ Basi Bwana Henry akasema, ‘Naona ni pahali pazuri hapa pa kuwinda wanyama, ni afadhali na tukae siku mbili tatu tuwinde.’ Nikasema, ‘ Vema, nadhani tunataka kujiburudisha kidogo, lakini sasa na tulale tuamke asubuhi na mapema na labda tutawaona wale ndovu kabla hawajaenda mbali.’

Tukajifunika na mablanketi yetu, tukalala. Mara nilisikia kishindo, nikashtuka na sote tuliruka na kutazama kwenye moto. Tukasikia kelele nyingi na mingurumo mingi sana kama nyama wanavutana. Tulijua kuwa hapana ila simba anayeweza kunguruma hivyo, tukazidi kutazama. Macho yalipozoea giza, mara tuliona mchanganyiko wa vivuli vyeusi na vya kimanjano vinatujia. Tukashika bunduki zetu tukavaa viatu vyetu tukatoka kambini kutazama kunanini. Sasa mchanganyiko wa vivuli ulianguka chini ukagalagala na tulipofika pale ulilala kimya.

Sasa tuliweza kuona ni kitu gani. Pale chini tuliona kulungu amekufa kabisa, na juu ya pembe zake amechomeka simba dume mkubwa naye vile vile amekwisha kufa. Nadhani yaliyotokea ni hivi: Yule kulungu alikuja kunywa maji, na Yule simba alikuwa pale akimvizia, akamrukia na akanaswa na pembe zake. Sasa Yule simba hakuweza kujitoa, lakini akageuka na kumuuma Yule kulungu mgongoni na shingoni, naye kulungu alikimbia mbio mpaka akaanguka na kufa.

Tulipokwisha tazama, tuliwaita watu wetu wawavute wanyama wale mpaka kambini, tukalala tena mpaka asubuhi. Kulipopambazuka tu! Tuliondoka tukafunga safari kwenda kuwinda. Tulichukua bunduki kubwa tatu na risasi nyingi, tukaweka chai baridi katika viriba vyetu vya maji. Baada ya kufungua kinywa kwa haraka, tuliondoka tukafuatana na Umbopa na Khiva na Ventvogel.

Tuliwaacha watu wengine kambini kuchuna ngozi ya Yule simba na kukatakata nyama ya Yule kulungu. Hatukuona shida kufuata nyayo za ndovu, na Ventvogel alikisia kuwa walikuwa ndovu ishirini au thelathini katika kundi lile, na wengi ni dume wakubwa. Tulikwenda mbali sana, na ilipopata karibu na saa tatu tulikuwa tumelowa jasho, lakini tulijua kuwa sasa hawako mbali. Tulifahamu hivyo kwa sababu ya miti iliyovunjika na kwa sababu mavi yao yalikuwa bado moto.

Baadae tukaliona kundi, tukaona kuwa kweli wapo ishirini au thelathini, nao wamesimama katika bonde wamekwisha kula, wanapunga masikio yao makubwa. Ilikuwa shani kubwa kuwaona, maana walikuwa karibu, kadiri ya hatua mia mbili na hamsini tu. Nikainama nikatwaa majani makavu kidogo nikayatupa juu hewani ili nipate kujua upepo unatoka upande upi; maana nilijua kuwa wakisikia harufu yetu watakimbia nasi hatutapata nafasi kuwapiga.

Basi nikaona kuwa upepo unatoka kwao, tukatambaa chini na kwa kuwa majani yalikuwa marefu tuliweza kuwakaribia mpaka kufika kiasi hatua hamsini hivi. Pale mbele yetu ndovu wakubwa dume wenye pembe kubwa sana walikuwa wamesimama. Nikanong’ona kumwambia Bwana Henry amlenge ‘yule wa upande wa kushoto, na Bwana Good achague Yule wa upande wa kulia, na mimi nikamlenga Yule wa katikati.

Nikasema , ‘Piga.’ Na mara bunduki zote tatu zikalia pamoja, na ndovu wa Bwana Henry alianguka amekufa, risasi imempenya moyo. Ndovu wangu aliangukia magoti, nikafikiria kama anakufa, lakini mara akasimama tena akaja mbio akanipita kabisa, lakini alipokuwa akinipita, nilimpiga risasi ya mbavu akaanguka. Basi nilimkaribia nikampiga ya kichwa kummaliza kabisa na kukomesha maumivu yake. Kisha niligeuka nimtazame Bwana Good, maana nilipokuwa nikimpiga ndovu wangu nilisikia ndovu akilia kwa hasira na maumivu. Nilipomfikia Bwana Good nilimwona ameingiwa na wasi wasi kabisa. Ikaonekana kuwa mara alipopiga ndovu wake ndovu huyo akaja mbio kumtafuta, nae Bwana Good alikuwa na shida ya kujiokoa. Kisha ndovu alikwenda mbio akifuata njia ya kwendea kambi yetu. Huku nyuma kundi zima lilikimbilia porini.

Kwa muda kidogo tulifikiri, tufuate kundi au tumfuate Yule aliyejeruhiwa, ndipo tulipokata shauri kufuata kundi, tukafikiri kuwa hatutamwona tena Yule ndovu mkubwa. Na toka siku ile ninatamani laiti kwamba tusingalimwona tena. Ilikuwa kazi nyepesi kufuata kundi, maana njia walimopita ilikuwa wazi kabisa kwa jinsi walivyokimbia.

Lakini kuwafikia tena ilikuwa kazi, tukafanya kazi ngumu kwa muda wa saa mbili kabla ya kuwafikia tena. Wote walikuwa wamesimama pamoja ila dume mmoja, nao kwa namna walivyoinua mikonga yao mara kwa mara kunusa nikajua kuwa wamefahamu kuwa hatari ipo karibu. Yule dume alikuwa amesimama yapata hatua hamsini kutoka kundi na hatua sitini kutoka sisi tulipo, akawa amesimama kama analinda zamu.

Nikadhani labda tukikaribia zaidi atasikia harufu yetu,. Basi nikawaambia wenzangu afadhali sote tumpige pamoja. Tukapiga na mara moja akaanguka amekwisha kufa. Basi lile kundi likashtuka likakimbia, lakini walifuata njia iliyowaongoza katika bonde, na mwinuko wa upande wa pili ulikuwa umekwenda juu sana. Basi tulipofika karibu tukawakuta wameshangaa kabisa na kusukumana na kupigana na kupiga kelele wakitafuta njia ya kuokoka.

Basi sasa tulipata wasaa; tukawapiga tukawaua watano. Kisha wakatoka kwa njia nyingine nasi kwa kuwa tumekwisha choka hatukuwafuata tena, maana ndovu wanane kwa siku moja walitosha kabisa. Baada ya kupumzika kidogo, watu wetu waliwakata ndovu wawili wakachukua mioyo yao kuwa chakula cha jioni, tukarudi kambini tukifurahiya kazi za mchana, na tukakusudia kupeleka watu kutoa pembe zote asubuhi. Tulipopita mahali pale tulipopiga wale ndovu wa kwanza, tuliona kundi la wanyama wengine, lakini hatukuwapiga, maana nyama tuliyokuwa nayo ilitosha kabisa. Lakini Bwana Good alitaka kuwakaribia ili awatazame vizuri maana alikuwa bado hajaona namana yao, akampa Umbopa bunduki yake, naye alifuatana na Khiva akaingia mwituni na sisi tulikaa tukiwangoja.

Jua lilikuwa linaanza kutua, likawa jekundu kabisa na Bwana Henry na mimi tukakaa tukitazama uzuri wake, na mara tulisikia ndovu analia, tukamwona anakuja mbio kabisa, mkonga na mkia juu hewani. Tena tukaona jambo jingine, tukaona Bwana Good na Khiva wanakuja mbio na Yule ndovu anawafuata. Tukaona kumbe ni Yule mkubwa aliyejeruhiwa na Bwana Good.

Kwa muda tulishangaa, maana hatukuweza kupiga bunduki kwa kuogopa kuwapiga Bwana Good na Khiva. Hapo jambo la kutisha sana likatokea, Bwana Good aliteleza akaanguka pale pale mbele ya miguu ya Yule ndovu.

Roho zilikuwa si zetu kwa hofu, tukamkimbilia tulivyoweza. Katika muda wa nukta tatu, mambo yangalikuwa yamekwisha, lakini hayakutokea kama tulivyodhania. Maana, Khiva mara alipoona kuwa Bwana Good ameanguka akageuka akatupa mkuki wake usoni pa ndovu, ukampiga mkonga.

Yule ndovu akalia kwa maumivu, akamshika Khiva akamtupa chini, akaweka mguu mmoja juu yake, akamzungushia mkonga wake akamvunja sehemu mbili. Sisi tulishikwa kama na wazimu kwa chuki, Yule ndovu tukampiga bunduki tena na tena, na mwishowe akamwangukia Yule mtu aliye muua. Bwana Good akaondoka akatikisa mikono yake juu ya Yule mtu hodari aliyemwokoa kwa kujitolea maisha yake, na hata mimi niliyezoea sana mambo ya hatari niliona kwikwi ikinipanda kooni. Umbopa akasimama akatazama maiti ya ndovu mkubwa na vipande vya maiti ya maskini Khiva, na baadae kidogo akasema, ‘Amekufa, lakini amekufa kiume!’

SAFARI YETU YA JANGWANI

Tulikuwa tumeua ndovu tisa, ikachukua kazi ya siku mbili kutoa pembe zao. Tulipokwisha kuzitoa tulizileta kambini tukachimba shimo chini ya mti mkubwa tukaziweka humo tukafukia shimo. Pembe zilikuwa nzuri kabisa, nadhani sijaona namna yake, maana zile za Yule mkubwa aliyemuua Khiva zilikuwa yapata ratili mia na sabini, kadiri tulivyoweza kukisia. Na marehemu Khiva tulimzika katika kaburi pamoja na sagai lake kama ilivyo desturi, yaani apate kujitetea katika safari yake ndefu kwenda ahera. Siku ya tatu tuliondoka tukafunga safari yetu tukitumaini kuwa tutarudi salama na kuchimbua pembe zetu. Baada ya safari ndefu ya kuchosha tulifika mji wa Sitanda karibu na mto wa Lukanga, na hapo kwa kweli ni mwanzo wa safari yetu. Nakumbuka sana siku ile tuliyofika huko.

Kwa upande wa kulia zilikuwa nyumba chache zimetawanyika pamoja na mazizi ya ng’ombe, na karibu na mto yalikuwapo mashamba ya wenyeji. Kupita mashamba hayo ni mwitu wenye majani marefu umejaa wanyama wa porini. Upande wa kushoto palikuwa jangwa lile kubwa. Hapo paonekana kwamba ni mwisho wa ardhi inayofaa kuoteshwa vitu, siwezi kujua kwa sababu gani, lakini ndivyo ilivyo.

Upande wa chini ya kambi yetu maji yalitiririka katika mto mdogo, na ng’ambo yamto palikuwa mteremko wenye mawe mengi. Huu ndio ulikuwa mteremko ule ule nilipomwona Yule Silvestre akitambaa kwa mikono na magoti miaka ishirini nyuma, yaani aliporudi katika safari yake ya kutafuta Mashimo ya Sulemani. Na kupita mteremko huo ni jangwa lile lisilo na maji, jangwa la ukiwa kabisa.

Tulipo piga kambi yetu ilikuwa ni jioni, na jua lilikuwa likizama, mfano wa mpira mkubwa mwekundu. Mishale ya nuru ya rangi mbali mbali ilitoka ikaenea jangwani. Bwana Henry na mimi tulimwacha Bwana Good atengeneze kambi, nasi tulipanda mteremko ule tukasimama tukitazama jangwa.

Mbingu zilikuwa nyeupe kabisa, na mbali sana tuliweza kuona milima ya Sulemani kama vivuli vikubwa, na wakati mwingine kuona theluji juu ya vilele vyake. Basi nikasema, ‘Kule ndipo upo ukuta unaozunguka Mashimo ya Sulemani, lakini anaejua kama tutaweza kuupita ni Mungu tu.’ Bwana Henry akasema, ‘Nadhani ndugu yangu yupo, na ikiwa yupo basi tutaonana, lazima.’ Nikasema, ‘InshaIlah.’

Tukageuka turudi kambini, nikaona kuwa sisi hatupo pekee yetu, maana nilimwona Umbopa amesimama nyuma yetu na macho yake ameyakodolea milima ile ya mbali. Umbopa alipoona tumemwona, akamwambia Bwana Henry, ‘Je, Inkubu, ile ndiyo nchi unayotaka kufika?’ (na jina la Inkubu ndilo jina walilomwita wenyeji, nadhani maana yake ni ‘ndovu’).

Basi Bwana Henry, akajibu, ‘Ndiyo ile nchi ninayokwenda.’ Umbopa akasema , ‘Inkubu, jangwa ni pan asana, tena hapana maji kabisa, milima ni mirefu sana na vilele vyake vimefunikwa na theluji, na mwanadamu hawezi kukisia kuna nini pale nyuma pale linaposhukia jua; utafika huko kwa njia gani, na kwa nini unataka kwenda?’

Basi nilimtafsiria maneno yale yote, na Bwana Henry akasema, Mwambie ya kuwa na kwenda kumtafuta ndugu yangu aliyenitangulia.’ Umbopa akasema, ‘Inkubu, ni kweli: maana njiani nilikutana na mtu mmoja kabila lake Hottentot akaniambia kuwa miaka miwili nyuma Mzungu mmoja alianza kuvuka jangwa amefuatana na mtumishi mmoja, nao hawakurudi.’ Bwana Henry akamuuliza, ‘Je, waona ya kuwa huyo ni ndugu yangu?’

Umbopa akajibu, ‘La, bwana sijui, ila nilipomuuliza Yule mtu yu wanamna gani, akajibu kuwa ana macho kama yako, lakini ndevu zake ni nyeusi, na tena amefuatana na mtumishi mmoja Mbechuana jina lake Jim.’

Basi nilipotafsiri maneno haya nikasema, ‘ Ndhani ‘ndiye bila shaka, maana mimi namjua Jim tangu zamani.’ Basi Bwana Henry akatikisa kichwa akasema, ‘Mimi nilijua hakika, maana ndugu yangu akitia nia yake kutenda jambo atalitenda. Ikiwa alitaka kuvuka milima ya Sulemani basi amekwisha kuivuka isipokuwa amezuiwa na jambo.

Na kwa hivi lazima tumtafute upande wa pili.’ Umbopa alifahamu Kiingereza ingawa hakukisema ila mara chache, akasema, ‘Inkubu, ni safari ndefu.’ Bwana Henry akajibu, ‘Ndiyo ni mbali, lakini hakuna jambo duniani asiloweza kufanya ‘mwanadamu ikiwa amedhamiria kulifanya.

Umbopa, ikiwa mapenzi yanamvuta mtu naye yu tayari kukosa maisha yake kama kwamba si kitu, hakuna jambo asiloweza kulitenda, hakuna milima asiyoweza kuipanda, hakuna jangwa asiloweza kulivuka, ila mlima mmoja na jangwa moja ambalo wewe hulijui.’ Nilipoyatafsiri maneno hayo , Umbopa alijibu, ‘Maneno makubwa, baba yangu, maneno yanapovuma kweli yanayostahili kusemwa na mwanaume. Umesema kweli, Inkubu baba yangu.

Sikiliza! Maisha ni kitu gani? Ni unyoya, ni mbegu ya majani, ikipeperushwa huko na huko, pengine huzaa na kujizidisha na ikisha kufanya hivyo hufa, pengine huchukuliwa mawinguni. Lakini ikiwa mbegu ni njema na nzito, huenda itasafiri kidogo katika njia ambayo inataka. Ni vizuri kujaribu kusafiri katika njia yako na kushindana na ajali. Kila mtu ameandikiwa kufa. Kama mambo yamezidi, basi hufa upesi kidogo zaidi tu. Baba yangu, nitafuatana nawe kuvuka jangwa na milima mpaka nitakapozuiwa na ajali njiani.’

Hapo alinyamaza kimya kidogo, na baadae akaendelea kutoa hotuba yake kama ilivyo desturi ya Wazulu. ‘Maisha ni kitu gani? Niambieni, Ee Wazungu, nyinyi wenye busara, nyinyi mjuao siri za dunia, na dunia ya nyota, na dunia iliyo juu na kuzunguka nyota; nyinyi mpelekao maneno yenu mbali bila kutumia sauti; niambieni, Ee nyinyi Wazungu, siri ya maisha yetu ni nini huenda wapi, hutoka wapi? Hamwezi kunipa jawabu; hamjui! Sikilizeni, nitawaambia. Maisha ni mkono tunaotumia kukinga mauti.

Ni kimulimuli kinachong’aa wakati wa usiku; ni kama pumzi nyeupe za ng’ombe zinazoonekana wakati wa baridi; ni kivuli kidogo kile kinachokimbia katika majani na kupotea katika jua hapo linaposhuka.’

Bwana Henry akasema, ‘Wewe Umbopa ni mtu wa ajabu.’ Umbopa akacheka kidogo akasema, ‘Huoni kuwa wewe na mimi tumefanana sana. Huenda hata na mimi nakwenda kuvuka milima ile ili kumtafuta ndugu yangu!; Nikamtazama sana nikamuuliza, ‘Je, maneno gani hayo, maana yake ni nini? Wewe unajua habari gani ya ile milima? Akajibu, ‘Kidogotu, kidogo sana.

Ni nchi ngeni kabisa, nchi ya uchawi na vitu vizuri; nchi ya watu hodari na miti na vilele vya theluji na njia nyeupe kubwa. Nimesikia habari zake, lakini iko faida gani kusema.? Sasa giza linashuka. Wale watakaoishi kuona wataiona.’ Nikamtazama tena, maana ilinibainika kuwa anajua habari zaidi. Alifahamu ninayoyafikiri, akasema, ‘Usiniogope, Makumazahn, mimi sitegi mitego upate kutegwa.

Mimi sifanyi hila. Ikiwa tutajaaliwa kuvuka milima ile iliyo nyuma ya jua, nitakwambia yote ninayoyajua. Lakini mauti yamekaa juu ya milima ile. Uwe na busara, urudi nyuma, nendeni mkawinde ndovu, mabwana. Nimesema.’

Na bila kusema neon jingine, aliinua sagai lake kutuaga akageuka akarudi kambini, na baadaye tulimkuta huko anasafisha bunduki kama wale watu wengine, Bwana Henry akasema, ‘Mtu huyu wa ajabu sana.’ Nikasema, ‘Ndiyo, nampenda kama simpendi.

Ajua neno lakini hataki kulisema. Lakini ya nini kugombana naye! Safari yetu ni ya ajabu na Mzulu wa ajabu hawezi kuzidisha ajabu yake.’ Siku ya pili tulifanya vitu vyote tayari kuanza safari yetu. Hatukuweza kuchukua bunduki nzito tukaziacha pamoja na vitu vingine kwa wapagazi wetu, tukafanya shauri kuwaacha katika nyumba ya mtu mmoja aliyekaa karibu.

Sikupenda kabisa kuviacha vitu hivyo, maana Yule mtu alivitazama kwa macho ya uroho sana, lakini nilifanya hila. Kwanza nilishindilia bunduki zote, nikaziweka tayari kupigwa, nikamwambia kuwa akizigusa hata kidogo, basi zitalia.

Yeye hakusadiki, na mara ile akashika moja, na kama nilivyomwonya, ikalia, na risasi ikampiga ng’ombe wake mmoja, na vile vile kishindo chake kikamwangusha chini. Akainuka upesi ameshtuka kabisa tena anaona uchungu kwa kupata hasara ya ng’ombe wake, akataka nimlipe, lakini hakutaka kabisa kugusa tena bunduki.

Akasema, ‘Weka shetani wale katika majani ya paa la nyumba au zitatuua sote.’ Nikamwambia kuwa tutakaporudi nikiona kuwa moja imepotea nitamuua yeye na watu wake wote kwa uchawi; na ikiwa haturudi naye akijaribu kuiba bunduki, basi vivuli vyetu vitakuja kumfuata na kuwatia wazimu ng’ombe wake, na kuharibu maziwa yao kabisa, mpaka maisha yake yatakuwa na udhia mtupu! baada ya hayo, akaapa kuwa atazitunza awezavyo.

Basi tukisha kuweka vitu vyetu salama, tulifunga mizigo midogo, tukawachagua Umbopa na Ventvogel wafuatane nasi, tukawa watano, yaani, Bwana Henry, Bwana Good, mimi na Umbopa na Ventvogel. Hatukuchukua vitu vingi, tulipunguza mzigo kadiri tulivyoweza. Tulichukua bunduki tano na bastola tatu, na viriba vya maji vitano, na mablanketi matano, na nyama kavu na shanga za kutoa zawadi, na dawa.

Tena tukachukua visu vyetu na vitu vidogo vidogo kama vile dira na vibiriti na tumbako. Basi vitu hivyo pamoja na nguo tulizokuwa tukivaa ndivyo tulivyo chukua, basi, Siku ya pili hatukufanya kitu, tulipumzika tu, na jua liliposhuka tuliamka tukala, tukafunga vitu vyote tayari, tukalala tena kungojea mbalamwezi.

Yapata saa tatu mwezi ukatoka ukaangaza nchi nzima na mbele yetu tukaona lile jangwa kubwa la kutisha sana. Tukaondoka, na baada ya dakika chache tukawa tayari, lakini hata sasa tulisita kidogo kama ilivyo desturi, ya kibinadamu ikiwa anaanza safari ya hatari. Sisi watu watatu tulisimama pamoja.

Umbopa akasimama mbele kidogo ameshika sagai lake mkononi na bunduki ameweka begani analitazama sana jangwa; na Ventvogel na watu watatu waliokubali kufuatana nasi kuchukua vibuyu vya maji kwa safari ya siku ya kwanza wakasimama pamoja nyuma yetu.

Basi Bwana Henry akasema, ‘Rafiki zangu, sasa tu tayari kuanza safari yetu ya ajabu. Labda hatutafaulu. Lakini sisi ni watu watatu, nasi tutashirikiana katika mambo mema na maovu mpaka mwisho, Na sasa kabla hatujaanza, na tumwombe Mungu anayeumba na kuandika ajali za wanadamu, ambaye tangu zamani amekwisha amuru njia zetu, atuongoze miguu yetu kama apendavyo.’

Akavua kofia yake na Bwana Good pia akavua yake, wakasimama kimya kwa muda. Mimi si mtu wa kuomba, nadhani wawindaji wachache sana huwa wa namna hiyo; wala sijamsikia Bwana Henry akisema namna hiyo lakini nadhani katika moyo wake ni mtu wa dini. Bwana Good vile vile ni mtu wa dini. Lakini siwezi kukumbuka hata siku moja niliyoomba kama nilivyoomba siku ile. Na lazima nikiri kuwa niliona faraja kwa kuomba hivyo.

Maana yaliyo mbele yetu hatukuyajua, na siku zote mambo yanayotisha na yasiyojulikana huvuta wanadamu wamkaribie Muumba wao. Kisha Bwana Henry akasema, ‘ Haya twendeni!’ Tukaanza safari yetu.

Hatukuwa na kiongozi ila milima ya mbali na ile ramani aliyoandika mzee Jose da Silvestre, na kwa kuwa iliandikwa na mtu aliyekuwa akifa juu ya kipande cha kitambaa miaka mia tatu iliyopita, haikuwa kiongozi cha kutia moyo sana.

Lakini hii ndiyo iliyokuwa tama yetu kufaulu. Tukikosa kuliona ziwa lile la maji machafu ambayo alama yake ilionyesha kuwa ni katikati ya jangwa, basi haikosi tutakufa kwa kiu.

Na nilifikiri kuwa bahati ya kuliona haiwezi kutumainiwa sana.

Na hata ikiwa Yule mzee da Silvestre alipima sawasawa na kufanya alama barabara katika ramani, je, baada ya miaka hii yote iliyopita sip engine limekauka,au labda wanyama wa porini wamekwisha kuyakanyaga maji mpaka yamekwisha, au labda yamekwisha kufunikwa na mchanga uliyopeperushwa na upepo? Basi tukaenda, tukaenda, usiku tukikanyaga mchanga na majani yale yaliyosokotana sokotana yalitunasa miguuni, na mchanga uliingia katika viatu vyetu ikawa mara kwa mara kusimama tupate kuutoa.

Basi hivi hivi tulisafiri, na Bwana Good alijaribu kututia moyo kwa kupiga mbinja, lakini sauti yake ilizidi kututia huzuni tu, akaacha. Baadae kidogo jambo lilitokea lililotushtua sana kwanza, lakini kisha lilituchekesha mno. Tulikuwa tukifuatana mmoja mmoja na Bwana Good ametangulia, mara nilisikia sauti yake inafifia kabisa, na tena tukasikia kelele na ghasia, na mkoromo na mguno na vishindo vya miguu. Katika giza tuliweza kuona kama vivuli vinakimbia vimefichwa kidogo kwa mavumbi ya mchanga.

Bwana Henry na mimi tulisimama tumeshangaa; na mshangao wetu ulizidi tulipoona Bwana Good anakwenda mbio kuelekea milima, juu ya kitu tulichodhani kuwa ni kama farasi, akipiga makelele moja kwa moja. Mara tulimwona ametupa mikono juu, tukamsikia akianguka chini kwa kishindo. Ndipo nilipotambua kuna nini; tulikuwa tumetokea kwenye kundi la punda milia waliokuwa wamelala, na Bwana Good alianguka juu ya mgongo wa mmoja ambaye aliamka akamchukua mgongoni mwake.

Nikawaambia watu wetu wasiogope, nikamkimbilia Bwana Good nikichelea kuwa labda ameumia, lakini nilifurahi nilipoona kuwa amekaa kitako juu, ya mchanga ameshangaa na kuogopa sana. Lakini hakuumia, Baada ya hayo tulikwenda bila ya kupatwa na jambo jingine mpaka saa saba hivi, tukapumzika kidogo tukanywa maji kidogo na baada ya kupumzika kwa muda wa nusu, ambaye mpaka sasa alikuwa akituchekesha mara kwa mara alinyamaza tu.

Basi ilipopata saa nane, tukafika kwenye kile kilima kidogo, tumechoka kabisa, na hapo tulikaa na kwa sababu kiu kilituzidi, tulimaliza maji yote. Tena hayakutosha . Basi tukalala, Nilipokuwa katika kusinzia, nilisikia Umbopa akisema peke yake, ‘Kama hatupati maji kesho kabla mwezi haujapanda mawinguni, basi tutakuwa maiti.’ Joto lilikuwa jingi sana, lakini hata hivyo nilitetemeka kama mtu aliyeshikwa na baridi. Maana kutarajia mauti si vizuri, na hasa mauti ya namna ile. Lakini hata fikira za mauti hazikuweza kunizuia nisipatwe na usingizi, nikalala.

Ilipopata saa kumi za usiku niliamka baada ya kulala kwa muda wa saa mbili tu, na sasa haja ya kwanza ya mwili, yaani kupumzika, imetimizwa. Maumivu yale mengine ya kiu yalianza kuniudhi, nami sikuweza kupata usingizi tena.

Kabla ya kuamka nilikuwa nikiota ndoto ya kuwa ninaoga katika mto wa maji mazuri yanayopita, na kando ya mto miti mizuri inaota, Kumbe! Niliamka kujiona katika jangwa la ukiwa, kavu kabisa, nakumbuka yale maneno aliyosema Umbopa kuwa kama hatupati maji leo tutakufa kifo kibaya. Hapana mwanadamu aliyeweza kuishi katika nchi ya joto kama lile jangwa bila maji ya kunywa.

Nilikaa nikasugua uso wangu uliokuwa mchafu kwa mikono yangu iliyokuwa mikavu kabisa. Midomo na kope zangu zilikuwa zimegandamana kabisa, nikaweza kuyafumbua macho kwa shida. Mapambazuko yalikuwa karibu, lakini baridi ile tunayozoea kuona asubuhi haikuwapo kabisa, na hewa ilikuwa nzito na nene jinsi nisivyoweza kueleza.

Wenzangu walikuwa wamelala.

Baadaye kukaanza kupambazuka, na ili nipate kusahau kiu yangu, nilitoa kitabu kidogo nilichozoea kuchukua mfukoni mwangu, nikaanza kusoma, na kwa bahati maneno niliyosoma yalikuwa haya: ‘Kijana mzuri ajabu alishika kombe la nakshi, Limejaa maji matamu na safi..’ Niliposoma maneno yale nilimeza mate au kwa kweli nilijaribu kumeza. Hata kufikiri maji kulitaka kunifanya niwe na wazimu.

Hapo nadhani nilishikwa na kichaa kidogo, maana nilianza kucheka, na sauti yangu iliwaamsha wenzangu, na wao wakaanza kusugua nyuso zao chafu, na kufungua midomo na kope zao zilizogandamana.

Mara tulipoamka kabisa tukianza kuzungumza juu ya shida yetu. Hapana hata tone la maji. Tulipindua viriba vyetu tukalamba kingoni, lakini wapi! Vikavu kabisa. Bwana Henry akasema ‘Tusipopata maji tutakufa.’ Nikasema, ‘Kama ile ramani ya Yule mzee ni sahihi, maji yapo karibu tulipo sasa.’ Lakini maneno yangu hayakufariji mtu, maana ilikuwa dhahiri kuwa hatuwezi kuitumai sana ile ramani.

Sasa ikaanza kuwa kweupe kidogo kidogo, tukakaa tunatazamana tu, nikamwona Ventvogel, Yule Hottentot, akiondoka na kuanza kwenda macho chini, na mara akafanya sauti kama ya kukoroma, akaonyesha chini katika mchanga.

Tukashtuka tukasema, ‘Nini, nini? Tukaondoka sote tukamwendea tukitazama chini. Akasema, ‘Wako wanyama wengi kama paa hapa. Tazameni nyayo zao.’ Nikamuuliza, ‘Je, hata kama paa ni wengi hapa hilo linatufaa nini? ‘ Akajibu, ‘Paa hawatembei mbali na maji.’

Nikasema, ‘Kweli, nilisahau, Alhamdulilahi.’ Basi jambo hilo lilitutia uzima tena; ni ajabu sana ya kuwa ‘kama watu wamo katika shida tama ya faraja hata ndogo huwafurahisha. Maana katika usiku wa giza hata nyota moja ni bora kuliko kutokuwa na nyota kabisa.

ITAENDELEA

Simulizi ya Mashimo ya Mfalme Sulemani Sehemu ya Nne

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment