Tufaa Jekundu Sehemu ya Kwanza
NEW AUDIO

Ep 01: Tufaa Jekundu

Tufaa Jekundu Sehemu ya Pili
Tufaa Jekundu Sehemu ya Kwanza

TUFAA JEKUNDU

SEHEMU – 1

KIJICHI SPICES – ZANZIBAR

NASRA AMRY mfanyakazi wa usafi katika hoteli ya Kjichi Beach Resort alitimua mbio akipiga kelele za hofu na woga huku akiacha maji katika chombo chake cha usafi yakimwagika baada ya kukikwaa na kuanguka chini.

“Mamaaaaaa! Maamaaaa! Uuuwiiiiiiii mieee!”.

Meneja wa hoteli hiyo Bwana Jecha akaiacha ofisi yake na kutoka kuangalia kuna nini, alipofika karibu na mapokezi alisimama ghafla, hakuamini anachokishuhudia, aliweka mikono kichwani akitokwa na macho mithili ya mjusi aliyebanwa na mlango.

Binti huyo aliyekuwa akikimbia huku akiteremka ngazi alianguka vibaya na kuvingirika kwenye zile ngazi mpaka sakafuni na kunyamaza kimya huku pumzi zake zikishuka taratibu kabla ya kupotea kabisa.

“Muwahisheni hospitali haraka,” Jecha akapiga kelele mara tu akili yake ilipomrudia, wakambeba na kumpakia kwenye gari. Ilikuwa ni hali ya sintofahamu kwa kila mtu. Si wafanyakazi tu bali hata wageni walitoka vyumbani mwao na kuja kutazama nini kinaendelea.

“Asma, mwenzako kapatwa na nini?” Jecha akauliza kwa ukali huku akizungukazunguka.

“Sijui boss! alikuwa kaenda kufanya usafi chumba namba 110, akarudi akiwa katika hali hiyo,” Asma akaeleza anachokijua huku kifua chake kikipanda na kushuka kuonesha jinsi alivyoingiwa na hofu, hofu isiyo ya kawaida. Jecha hakuuliza, akapanda ngazi kuelekea huko juu akajionee mwenyewe kilichopo, huku nyuma akifuatiwa na kundi la wafanyakazi na wateja.

Chumba namba 110 kilikuwa ghorofa ya kwanza, Jecha alipofika alikikuta wazi alichokishuhudia ni pazia lililokuwa likitikiswa na upepo kutoka baharini. Akasita kabla hajaingia, akavuta hatua fupi fupi za mtu anayeogopa huku nyuma yake waliomfuata wakifanya vivyo hivyo. Akaufikia mlango na kuchungulia ndani, akahisi mwili wote ukiingia baridi na nywele zikimsimama kwa kile alichokiona kitandani, akaegemea ukuta akiwatazama waliomfuata huku akihema kwa nguvu.

“Kuna nini boss?” wakauliza kwa sekunde tofauti na kusababisha mgongano wa sentensi hiyo masikioni mwa Jecha. Hakuwajibu, akawapa ishara tu ‘jioneeni wenyewe’.

“Mama yangu!” mmoja wa vijana waliofuatana na Jecha akapiga kelele huku akijishika kichwa na kurudi nyuma na kuwapisha wengine kujionea. Kila aliyechungulia alirudi ama kajiziba kinywa au analia kwa sauti. Hii ikapelekea wengine hata wasichungulie kabisa kuona kuna nini.

Juu ya kitanda kikubwa chumbani humo, mwili wa mwanamke ulikuwa umelala juu yake. Kamba ya manila ikiwa shingoni mwake, ulimi nje na macho yamekodoka, chali kitandani, bila nguo, chini ya kichwa chake kulikuwa na damu nzito iliyotapakaa na kufanya kitu kama ‘taji la malkia’.

“Batuli!” Mmoja wa wafanyakazi wa kiume alisikika akisema baada ya kuuangalia mwili ule. Vilio vikatawala ndani ya hoteli ile, wafanyakazi walichanganyikiwa kwa kifo cha kikatili cha mfanyakazi mwenzao.

***

Inspekta wa polisi kutoka kituo cha Bububu bwana Ally Shakur alikuwa akizunguka huku na huko katika chumba kile kidogo.

“Afande, huyu mwanamke hajanyongwa,” sauti ya kijana wake ikamshtua kutoka katika lindi la mawazo. Akamtazama yule kijana aliyevalia gloves mikononi mwake na mavazi ya kipolisi alipokuwa akieleza uchunguzi huo wa awali. Akamjibu kwa kutikisa kichwa, kisha akamtazama Jecha, meneja wa ile hoteli.

“Mnapangisha majambazi siku hizi?” akamwuliza kwa sauti ya upole.

“Hapana afande, ni vigumu kumjua mteja unayempangisha,” akajibu huku kamasi jembamba lilimtiririka naye akijaribu kushindana nalo kulirudisha litokako japo mashindano hayo hayakupata mshindi.

“Marehemu huyu mnamjua?” akauliza tena Yule inspekta.

“Ndiyo, ni mfanyakazi wetu,” Jecha akajibu mara baada ya kufuta machozi kwa kitambaa chake.

“Kitengo gani?”

“Mapokezi,” Jecha akaendelea kujibu maswali ya inspekta huyo aliyeonekana kuwa mtu makini sana katika kazi yake.

“Sawa! Haya ni mauaji, na hii ni kesi, inabidi utoe ushirikiano wa hali ya juu katika hili ili muuaji atiwe mbaroni. Kumbuka aliyekufa ni mtu wenu wa karibu,” Inspekta akaongea huku akiteremka ngazi kuelekea mapokezi ya hoteli hiyo. Katika dirisha hilo la mapokezi kulikuwa na mwanadada mweupe aliyejitanda hijab kichwani mwake, macho yake yalikuwa mekundu kwa kilio, huku bado akiwa anatokwa na kamasi jembamba akamkaribisha inspekta huyo.

“Pole sana, (akaitikiwa) naomba unipe kitabu cha wageni,” akamwambia huku tayari mkono wake ukiwa wazi ukisubiri kukipokea. Akakabidhiwa na kuipekuwa tarehe za nyuma kidogo. Chumba namba 110 kilipangishwa na Bw. Swebe Kayinda kutoka Dar es salaam. Akaandika kwenye kijitabu chake kisha akachukua na namba ya simu ya mteja huyo. Baada ya kuchunguza sana akagundua kuwa upangishwaji wa chumba hicho umefanyika mara mbili kwa jina lile lile.

“Swebe Kayinda alifika hapa lini?” Akamwuliza yule mhudumu.

“Alifika hapa wiki moja iliyopita, juzi aka-check out, lakini kwa taarifa nilizopewa ni

kuwa, huyu mteja alirudi tena hapa juzi yiyohiyo, akidai kuwa ameomba kupumzika siku nne zaidi,” yule mhudumu akaeleza.

“Alikuwa na uhusiano na marehemu?”

“Kwa kweli hapo sijui kwa kuwa alipenda kucheka na kila mtu hapa, na alikuwa mcheshi

sana,” Asma aliendelea kumjibu inspekta huyo aliyekuwa akiuliza maswali kana kwamba ameyaandaa.

“Kwa maelezo yako nikikwambia kuwa Swebe Kayinda ndiyo muuaji, utakubali au

utakataa?” Inspekta akarusha swali gumu zaidi kwa mwanadada huyo aliyebaki kimya huku akitikisa kichwa chake kushoto na kulia.

“Asante sana, husisite kunipa ushirikiano wako pindi nikiuhitaji,” akamwambia na kuondoka pale kaunta.

“Bwana Jecha, kama huyu mteja wako atarudi naomba unipe taarifa ya haraka, lakini nasi tunatafuta mbinu ya kumkamata,” akamwambia na kuaga huku mwili ule wa Batuli ukiwa tayari uneondolewa chumbani mle na kupelekwa hospitalini kuhifadhiwa. Wakati huo huo Nasra Amry naye alipumzishwa katika hospitali ya wilaya kwa matibabu ili arudiwe na fahamu zake zilizopotea mara tu baada ya anguko lile.

Haikuwa kawaida ya hoteli hii kuwa katika hali ya majonzi lakini asubuhi hii ilikuwa hivyo, wafanyakazi makundi makundi walisimama huku wageni nao wakionesha hofu ya hapa na pale ilhali wengine wenye moyo mwepesi wakisaini kitabu kuondoka huku wakiacha pesa zao zilizokuwa bado zikiwahitaji kulala zaidi na zaidi katika hoteli hiyo.

“Is difficult to know who will be the next one, I am sorry” (Ni vigumu kujua nani atayefuatia) aliongea mmoja wa mabinti wa Kizungu huku akikokota sanduku lake kutoka nje ya hoteli hiyo.

SAJINI CHUBI aliitwa ofisini na Inspekta wake mchana wa siku hiyo ya tukio. Kwa ukakamavu wa hali ya juu alisimama mbele ya inspekta huyo na kutoa saluti kwake.

“Keti chini,” inspekta akamwambia huku na yeye akijiweka sawa.

“Sajini, nimekuita, najua wazi, na siku zote kuwa wewe ndiye unayeweza kutatua

migogoro mizito kama hii.” Akakohoa kidogo na kisha akaendelea kusema, “Kuna haya mauaji yaliyotokea pale hotelini, Kijichi Beach Resort, nahitaji ufuatilie, ikiwezekana tumtie mkononi muuaji, mpaka sasa mtuhumiwa wa kwanza anaitwa Swebe Kayinda, na namba yake ya simu hii hapa.” Akamkabidhi ile namba. Chubi akaitazama ile kwa makini, kisha akaiweka katika simu yake na kile kitabu akamrudishia mkuu wake wa kazi.

“Sawa afande ninekuelewa vyema, nitaianza kazi hii saa zizi hizi,” Chubi akajibu na kusimama, akatoa saluti kisha akageuka na kushika kitasa cha mlango kuondoka.

“Chubi!” inspekta akaita, “nakuamini, fanya kazi, popote penye ugumu niambie mimi na si mtu mwingine,” Inspekta akatoa rai na kumwacha aende zake.

Chubi Maduhu, kijana wa Kinyamwezi, aliyezaliwa Unguja baada ya wazazi wake kulowea huko tangu enzi na enzi alikuwa afisa wa polisi mwenye cheo cha Sajini katika kituo cha Bububu. Aliondokea kujenga jina kubwa kwa wakubwa wake kutokana na juhudi, umakini, ukakamavu awapo kazini. Alishatatua kesi nzito na ngumu ndani na nje ya Zanzibar hata nyingine zikahatarisha maisha yake. Siku hii alipewa kesi nyingine nzito na mkuu wake wa kitengo aliyotakiwa kuipatia ufumbuzi, ikiwezekana mtuhumiwa atiwe nguvuni. Na hii ndiyo kazi ya polisi.

Akiwa ndani ya gari yake ndogo aliwaza jinsi atakavyoitatua kesi hiyo, kila wakati alihisi damu kuchemka, mikono kumwasha na ari ya mapambano ikimjia kwa fujo, alifyonza, akameza mate, akatikisa kichwa na kisha kupigapiga usukani wa gari kwa ubavu wa ngumi yake. Aliwasili katika hoteli hiyo dakika chache tu kwani barabara hazikuwa na foleni ya kumpotezea muda. Alipokelewa na hali ya huzuni iliyomfanya hata yeye kuhuzunika kabla hajaingia mapokezi ya hoteli hiyo.

“Habari dada?” Alimsabahi mhudumu wa mapokezi. Akajibiwa na kuomba kuonana na meneja wa hoteli hiyo.

Jecha Hamisi alikuwa ametulia tuli kwenye kiti chake cha kuzunguka, huku meza yake ikiwa tupu bila kabrasha lolote juu yake.

“Karibu, karibu sana,” akamkaribisha mgeni huyo.

“Bila shaka naongea na Jecha Hamisi. Mimi ni Sajini Chubi, kutoka kituo cha polisi

Bububu,” akajitambulisha na kumuonesha kitambulisho chake cha kazi.

“Karibu sana, nakusikiliza,” Jecha akajiweka sawa kitini ili kumsikiliza mgeni huyo.

“Poleni sana na msiba, lakini nilikuja kujua machache tu, hivi marehemu alikuwa na

mahusiano na Swebe Kayinda?” Akaanzia hapo. Jecha akatulia kwa nukta kadhaa kisha akakohoa kidogo na kusema, “Unasikia afande kiukweli kabisa, mi sifahamu ila labda hawa wahudumu ambao daima wanakuwa na wateja, ninachojua mimi Batuli alikuwa na mchumba wake na walitegemea kufunga ndoa miezi mitatu ijayo”.

“Asante kwa jibu zuri, na huyu mchumba wake naweza kumpata vipi?”

“Kiukweli afande sijui utampataje, labda nikuelekeze nyumbani kwao huko watakujuza,” Jecha akajibu. Ukimya uliopita katikati ya watu hawa wawili ukaleta maswali na majibu kwa kila mmoja wao.

“Bwana Jecha, sisi kama polisi tunataka kumkamata muuaji ili kukomesha kabisa unyama huu, ninapenda unipe ushirikiano wa karibu sana katika hili ili kuiondoa nuksi hii katika hoteli yako.”

“Nimekuelewa afande”.

“Ok, Batuli alikuwa anafanya kazi kitengo gani?” Chubi akauliza.

“Kitengo cha Mapokezi”.

“Na mara ya mwisho alikuwa kazini lini?”

“Alikuwa kazini juzi na ana mapumziko ya siku 3, ina maana alitakiwa aje kazini kesho kutwa,” Jecha akaeleza kwa ufasaha. Chubi aliandika vitu fulani katika kijitabu chake na kukifungua kurasa inayofuatia.

“Naweza kuonana na mtu wa kwanza kuiona maiti pale chumbani?” Chubi akauliza.

Jecha akatulia kidogo kisha akafungua kinywa kujibu swali.

“Huyu mtu amezimia na sijui kama ameamka, yuko hospitali ya wilaya wodi nne,” akamaliza.

“Ok asante sana.” Akashukuru na kunyanyuka wakapeana mikono na kuahidi kurudi muda wowote kama atahitajika kufanya hivyo. Alipopita dirisha la mapokezi akasita akiwa hatua tano mbele, akageuka na kurudi pale dirishani na kumsabahi kwa mara nyingine mwanadada aliyekuwa hapo.

“Samahani mimi ni afisa wa polisi, kama hutojali nikuulize swali moja tu,”

“Uliza,” yule mwanadada akajibu.

“Unamjua mpenzi wa marehemu Batuli?”

“Ninayemjua walikwishaachana labda kama alikuwa na mwingine,” yule mwanadada akajibu.

“Sio kwamba walikuwa na ahadi ya ndoa miezi mitatu ijayo?” akauliza huku mshangao wa wazi ukiwa juu ya uso wake.

“Walishaachana kwa kuwa walikuwa na ugomvi kati yao,” Asma akajibu huku akimtazama Chubi aliyekuwa akijiuliza maswali na kujitengenezea majibu, kuna kitu hakiko sawa hapa, akawaza huku akijikuna kidevu chake.

“Sawa, huyo waliyeachana naweza kumpata wapi?” akauliza na Asma akamjibu kwa kumpa maelekezo ya labda wapi angeweza kumpata kisha wakaagana na Chubi akaondoka zake eneo lile. Akiwa njiani kurudi ofisini akapokea ujmbe mfupi wa simu ukimtaka kuelekea hospitali ya Mnazi Mmoja kuchukua taarifa ya uchunguzi wa mwili wa Batuli.

***

Katika hospitali ya Mnazi Mmoja, Chubi alikutana na Daktari Zaytun ofisini mwake. Baada ya kutambulishana na kuoneshana vitambulisho vya kazi mazungumzo yalianza kati yao.

“Ndiyo dokta…” Chubi alianza.

“Sasa mimi nimefanya uchunguzi wangu nimekamilisha na ripoti yake ndiyo hii,” akampa karatasi ya ukubwa wa A4 iliyoandikwa kwa mashine na sehemu nyingne kwa mkono mwandiko ambao ulipaswa utulie ili uuelewe.

“Huyu marehemu amepigwa na kitu kizito kisogoni, anaoneka aliburuzwa kwa kushikwa mikononi ama kabla au baada ya kuuawa kutokana na michubuko kwenye vidole vyake vya miguu, hajanyongwa ijapokuwa mwili wake ulikuwa na kamba shingoni,”

Muda wote Chubi alikuwa akisikiliza kwa makini na kuandika vitu vichache katika kijitabu chake kidogo.

“Hakutenzwa kwa nguvu?” Chubi aliuliza.

“Hapana, hakutenzwa, muuaji hakuwa na haja ya penzi la nguvu wala ugomvi bali alikuwa na kiu ya kuua tu,” yule daktari akajibu kwa ufasaha. Kila mara alitamani aseme jambo ambalo lilimtatanisha hata yeye kama daktari lakini alijikuta akikinzana na nafsi yake.

Itaendelea….

Tufaa Jekundu Sehemu ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment