Tufaa Jekundu Sehemu ya Tatu
TUFAA JEKUNDU
SEHEMU YA 3
“Oh! Nimekuelewa, na vijana wanafanya vyema,” Nyota njema akaongeza kusema huku akipukuta jivu la sigara yake kwenye kibweta cha kazi hiyo kilichotulia tuli mezani.
“Hatuna budi kufanya kila kitu kwa ufasaha, huu ni mwaka wa neema, na neema hiyo lazima ifunuliwe; unaweza kuifunua kwa mkono, kisu, panga, shoka na hata bunduki inapobidi. Sio mara ya kwanza kufanya haya na kila tulipofanya yalifanikiwa,” ile sauti ya kukwaruza iliendelea.
“Ndiyo Bwana Bloodman, nami nayajua mafanikio yenu na kazi zenu,” Nyotanjema akamuunga mkono.
***
Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha nje ya nyumba hiyo iliyokosa matunzo na kujikuta katikati ya vichaka. Gari moja ndogo iliegeshwa nje yake na mtu mmoja akateremka akiwa katika mavazi meusi yaliyomkaa vema, akafyatua mwamvuli ulio mkononi mwake na kujikinga dhidi ya matone hayo ya mvua yenye hasira kali. Kwa mbali ungeweza kusema ni mwanamitindo fulani kwa jinsi vazi lile lilivyokubaliana na mwili wake, hakika alikuwa shababi, ambaye angesababisha ugomvi muda wowote endapo angesalimiana na wasichana wawili tofauti kwa wakati unaofanana.
Akaiacha ile gari ya kifahari aina ya Audi na kupotelea ndani ya jengo lile. Baada ya kuufunga mlango nyuma yake, akasimama kama sekunde kumi huku uso wake ukiwa umeinamishwa chini, alipounyanyua, akavua viatu vyake na kuvikamata kwa mkono wa kushoto huku ule wa kulia ukiwa bado umeshikilia ule mwamvuli ambao sasa ulikuwa umekunjwa, akatembea hatua chache na kulifikia kabati.
Ukimya uliotawala jumba lile haukuwa kikwazo kwa kijana huyo, hata lipotembea nyayo zake hazikufanya ukelele wowote ule, labda kwa sababu ya zuria zito la manyoya ya ngamia lililofunika kabisa sakafu yote. Akavuta milango ya kabati hilo na kuweka viatu kwenye saraka ya chini kabisa, kisha akatwaa joho kubwa jeusi na kulivaa juu ya yale mavazi, alipohakikisha yuko sawa, akachukua kinyago na kukipachika usoni mwake.
Hatua kumi na mbili nyingine zikamfikisha kwenye mlango wa chumba fulani, akaingia. Na huko akateremka ngazi kuelekea chini ya ardhi mpaka kwenye mlango wa chuma, akasimama na kubofya vitufe vyenye tarakimu kadhaa lakini mlango ule haukufunguka. Alipoangalia saa, ilimwonesha saa nane na dakika hamsini na nane.
Bado dakika mbili, akawaza na kutulia pale pale. Dakika mbili baadae ule mlango ukafunguka wenyewe, akaingia ndani. Akakanyaga ngazi iliyoanza kuteremka chini kadiri alivyosonga mbele, alipoiacha akaufikia mlango wenye nakshi safi na za kuvutia na akabisha hodi kwa namna anayojua yeye.
***
Mr Bloodman alibofya kitufe lilicho chini ya meza aliyokalia na ule mlango ukafunguka kwa kuachana katikati, kipande kikaenda kushoto na kingine kulia.
“Kiti chako, Bw. Mauti,” Bloodman akamkaribisha na yule kijana akaketi kwenye kiti cha tatu na kukiacha cha nne, “Nimeiona kazi yako,” akamwambia
“Mimi ndiye Israel malaika wa giza, bwana wa mauti, utembeapo na mimi basi uju eumetembea kwenye uvuli wa mauti,” akasema yule kijana. Mwanga hafifu wa taa bado ulikuwa ukikimulika chumba hicho na kuendelea kuwafanya wale jamaa wasionane vizuri, ukizingatia nyuso zao zilikuwa na vinyago, hii nayo iliwafanya wasijuane kabisa.
Utaratibu wao wa kuingia ndani ya jumba hilo ulitofautiana kwa dakika thelathini alikadhalika na utokaji wao ulikuwa vivyo hivyo.
“Mshtuko uliowapata leo nafikiri watahaha sana, watakuwa kama vichaa” Mauti akawaambia wajumbe wengine.
“Ndiyo!” Bloodman akaitikia na kutikisa kichwa
“Kabla hawajatulia inabidi wapate mshtuko mwingine na mwingine, wakati wao wanahaha kutafuta mchawi nani sisi tunatimiza azma yetu. Kumbukeni tuna mwezi tu ili tuisimike ngome yetu, na hapa patakuwa ndiyo kituo kikuu cha biashara zetu katika nchi za Maziwa Makuu”.
“Mkulu kila kitu kiko sawa?” Nyotanjema akauliza.
“Bila shaka, kila kitu kiko sawa. Unajua kila mtu ana idara yake, mwenye idara hiyo atatupa habari pindi tu atakapokuja,” Bloodman akatoa ufafanuzi.
Ukimya ukapita kwa mara nyingine na kuruhusu moshi ule wa sigara kukatiza anga la chumba hicho kwa maringo kana kwamba utaishi milele. Saa kumi na nusu mlango ukagongwa kwa mtindo mwingine kabisa na mtu mmoja akaingia mara tu baada ya Bloodman kuufungua kwa ile swichi yake iliyo chini ya meza.
“Kiti chako ni chako Bwana Axe,” Bloodman alimkaribisha na yule jamaa akaketi kwenye kiti kilicho pembeni kabisa, naye alikuwa kavaa kama wengine; vazi jeusi na kinyago usoni.
“Vipi ameitika?” Bloodman akauliza.
“Hawezi kuitika haraka namna hiyo, ataitika pale tukiita kwa fujo,” Mr. Axe akajibu.
“Tuhakikishe ameitika kabla ya saa sabini na mbili,” Nyotanjema akaongeza.
“Bila shaka,” Axe akajibu. Wanne hao wakaendelea kujadiliana mambo mbalimbali ya mpango wao huo, wakipeana mbinu za hapa na pale ili kumaliza kazi yao. Ijapokuwa kulikuwa na mabishano ya hapa na pale lakini mwisho walifikia muafaka.
“Hakuna muafaka bila mabishano. Ninafurahi kwa kuwa nimeona na kusikia jinsi ambavyo mmejipanga, na mi kama balozi wa kazi sina budi kuhakikisha inakwenda sawa ili katika saa hizo nilizowaambia tuanze kazi yetu kule Kigoma,” Bloodman akaeleza huku wajumbe wote wakiwa kimya kabisa kusikiliza.
“Kwa nini Kigoma?” Nyotanjema akauliza kwa bashasha.
“Kwa sababu ni karibu na ngome yetu ya Kongo, isitoshe ni kisiwa kidogo tulichokijenga kwa siri sana, hakuna anayejua mahala hapo,” Bloodman akamjibu huku akikohoa kidogo na kisha kujiweka sawa.
“Katika wiki tatu zijazo, sote tutatakiwa kukutana Kigoma mtapewa maelekezo mahali pa kukutania kwani kutakuwa na shughuli maalumu ya kukitabaruku kituo hicho”. Baada ya mazungumzo hao, Bwana Axe ambaye alikuwa wa mwisho kuingia akainuka na kutoka bila kuaga si kwa utovu wa nidhamu bali ndivyo ulivyo mpango wao kwani yeye katika kikao hicho alitakiwa akae si zaidi ya dakika sitini. Hivyo baada ya yeye kutoka, yakaendelea mazungumzo ambayo hakutakiwa kuyasikia kisha na Bwana Mauti naye akaondoka saa moja baadaye na kumwacha Bloodman na Nyotanjema.
“Itakapobidi nitakutumia, kwa kuwa hiyo ni moja ya kazi yako na wewe ni silaha yetu ya mwisho kabisa katika kazi hii,” Bloodman akamwambia Nyotanjema.
“Bila shaka, kwa kuwa ni moja ya kazi yangu nami nitafanya hivyo,” Nyotanjema akajibu huku akinyanyuka na kutoka ndani ya chumba kile na kumwacha Bloodman peke yake: kwa kuwa yeye alikuwa wa kwanza kuingia ilibisi awe wa mwisho kutoka.
MWANZA
NDEGE WA ANGANI walijifuta matongotongo kuashiria pambazuko jipya la siku hiyo. Jua la Mashariki lilianza kupasua anga kwa miale yake dhoofu iliyoleta burudani tamu kwa wana wa Adamu.
Bado watu wengi walikuwa wakijigeuza upande wa pili juu ya vitanda vyao, wakilelewa na kaubaridi ka muda huo. Ni wavuvi tu waliyokuwa wakirudi kutoka kwenye ‘vuvi’ zao alfajiri hiyo, mitumbwi inayoendeshwa kwa mashine ilikuwa ikisogea taratibu katika soko la samaki la bandarini hapo.
Kundi la wavuvi na wadau wengine wa biashara hiyo hasa akina mama lilikuwa limesimama kando kidogo ya ziwa. Katikati yao kulikuwa na msichana wa makamo kama ya miaka ishirini na nane au thelathini hivi, ulalaji wake pale chini haukuonesha dalili yoyote ya uhai.
“Watu wabaya, wamemuua bila huruma, jamani!” Alisikika mama mmoja aliyebeba ndoo yake kwa mkono wa kushoto. Kila mmoja alionesha sura ya masikitiko kwa ajili ya msichana huyo. Hakuna aliyemtambua mwanadada huyo si kwa sura wala kwa jina.
“Ngoja mi niondoke sitaki ushahidi,” alisikika mtu mwingine huku akiliacha kundi lile likizidi kuwa kubwa na nuru ya jua ikizidi kutawala anga la jiji la hilo. Gari ya polisi ilisimama upande wa bandarini na vijana wanne wenye machela mikononi mwao wakitembea kwa mwendo wa nusu kukimbia na nusu kutembea huku nyuma yao wakifuatiwa na na wengine wawili; mmoja mwanamke aliyekuwa na radio call mkononi na mwanaume aliyeambatana naye, hakuwa na chochote. Walipofika kwenye lile kundi wakapenya na kufika kwenye ule mwili.
Yule mwanamke mwenye, akavaa gloves na kuutazama ule mwili akiugeuza huku na kule. Nyuma ya kisogo cha mwili ule kulikuwa na jeraha kubwa na damu iliyoganda, macho yake yalikuwa yakitazama kama aliyekuwa akiangalia kitu kwa makini. Wale polisi wakafanya wanayotakiwa kufanya, wakapiga picha mwili ule na kisha kuuweka machelani wakisaidiana na wananchi. Wakachukua maelezo ya hapa na pale kwa waliowakuta kisha wakaubeba mpaka kwenye gari na kuondoka nao. Breki za gari hiyo zilisimamaisha tairi pembezoni mwa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya serikali katika jiji hilo, Sekou Toure.
Taarifa za kuokotwa kwa mwili huo zilitapakaa upesi sana kama upepo wa kimbunga. Vituo vya redio binafsi zilitangaza na kutaka yeyote aliyepotelewa na binti, mke, mpenzi au mchumba akautambue mwili huo.
HOSPITALI YA SEKOU TOURE
NDANI YA CHUMBA cha kuhifadhia maiti kulikuwa na daktari mmoja mzee aliyekuwa ametingwa kwa shughuli ya uchunguzi wa maiti hiyo huku pembeni kukiwa na askari polisi wa kike aliyekuwa akifuatilia zoezi hilo mwanzo mpaka mwisho.
Baada ya ukimya wa muda mrefu uliokuwa umesababishwa na kazi ngumu kwa Yule daktari, aliinua kichwa na kumtazama huyo polisi wa kike.
“Huyu marehemu hakufa majini, pale alitupwa tu,” sauti ya daktari ilimstua WP Melina aliyekuwa kwenye kina kirefu cha mawazo.
“Dokta unasemaje?” Melina aliuliza kwa kukurupuka kama mtu anayetoka usingizini.
“Nasema hivi huyu marehemu hajafa kwa maji ila pale ametupwa tu. Tazama jeraha hili la kisogoni, maji hayafanyi hivi. Kitu kingine cha ajabu kabisa afande njoo uone,” yule daktari akamwita yule WP. Kwa kutumia vifaa tiba alivyonavyo alikifungua kinywa cha marehemu na kubana kitu kama kipande cha chuma kisha akakitoa nje taratibu. Yule afande alibaki kakodoa macho kama aliyepigwa na shoku ya umeme, akiufuatisha kwa macho ule mkono wa daktari uliyokuwa ukikitua kile kitu katika kijibeseni jidogo cha chuma.
“Nini hicho?” Akauliza.
“Bado sijakijua, lakini nahisi ni risasi,” akajibu yule daktari. Baada ya kusogea karibu zaidi, yule afande akakiona kile kitu kwa uzuri na wakati huo tayari kilikuwa kimesafishwa vizuri. Akaiangalia na kuigeuzageuza.
“Hii ni risasi, inaonekana ndiyo iliyompiga kisogoni ikakwama kinywani.” Akaendelea kuingalia vizuri.
“TSA 1,” akasoma herufi hizo tatu zilizofuatiwa na tarakimu hiyo, akaduwaa na kufikiri kidogo. Aina gani ya bunduki hii? TSA 1, akawaza bila kupata jibu. Baada ya saa moja shughuli ile ilikamilika na yule afande akaondoka na kivuli cha ile taarifa kurudisha kwa mkuu wake wa kazi.
Taarifa ile ilipitiwa kwa kina na mkuu wa kitengo cha upelelezi akidukua hiki na kile alichoona kina utata kisha akamteua mwanadada huyo, Melina kuifuatilia kesi hiyo mpaka mwisho wake. Jambo la kwanza alilokuwa akilisubiri ni kama kuna taarifa yoyote ya upotevu wa binadamu tena wa kike, lakini haikutokea kabisa.
“Melina, hauna budi kuanza kazi hii, chanzo utakikuta hukohuko mbele ya safari,” Mkuu wa upelelezi alimwambia Melina.
“Sawa!” Melina akajibu kwa ukakamavu kama askari.
“Kwa maana hatujui marehemu alikuwa mhudumu wa baa, mwanafunzi wa chuo, kahaba, eenh! Hatujui, kwa hiyo jaribu kunusa maeneo hayo yote labda utaokota kitu, usisite kunipa taarifa yoyote unapohitaji msaada,” Mkuu wa upelelezi akamwambia Melina.
ITAENDELEA…
Tufaa Jekundu Sehemu ya Nne
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;